Quantcast
Channel: MPEKUZI
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live

Lowassa Afunguka Kuhusu Mgogoro Unaoendelea Ndani ya Chama cha CUF

$
0
0
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amevunja ukimya kuhusu mgogoro wa uhalali wa Uenyekiti wa Profesa Ibrahim Lipumba anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa unaoendelea ndani ya Chama Cha Wananchi (CUF) ambao umekuwa ukihusishwa naye tangu awali.

Lowassa ambaye alitajwa na Profesa Lipumba kuwa chanzo cha yeye kujiuzulu kabla ya kurejea tena miezi 9 baadae kutengua uamuzi wake, amesema kuwa shida za chama hicho ni shida za vyama vyote vinavyounda Ukawa.

Mwanasiasa huyo mkongwe na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, ametumia ukurasa wake wa Facebook kueleza jinsi ambavyo Ukawa inalibeba tatizo la mgogoro wa CUF.

“CUF ni wenzetu katika Ukawa. Shida zao ni shida zetu, vita vyao ni vita vyetu, kushindwa kwao ni kushindwa kwetu, ushindi wao ni ushindi wetu,” aliandika Lowassa.

Kauli hiyo ya Lowassa imekuja miezi michache baada viongozi wa Ukawa kueleza msimamo wao kuwa hawamtambui Profesa Ibrahim Lipumba kama Mwenyekiti wa CUF na kwamba wataendelea kushirikiana na Katibu Mkuu wa Chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad.

Naye Profesa Lipumba amekuwa akieleza kuwa hayuko tayari kuona Chadema au Lowassa wanakinunua chama hicho.

Hivi karibuni, Ukawa wameweka msimamo wao kuwa watawasimamisha wagombea wa pamoja katika uchaguzi mdogo utakaofanyika mwakani.

Hata hivyo, kumekuwa na changamoto baada ya pande mbili zinazovutana ndani ya CUF kila mmoja kutangaza kuwasimamisha wagombea wake huku Tume ya Taifa ya Uchaguzi ikiweka msimamo kuwa ili iwatambue wagombea wa chama hicho ni lazima fomu zao zisainiwe na pande mbili zinazovutana.

Miezi michache kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, Profesa Lipumba alionekana akimtambulisha Lowassa mbele ya waandishi wabari na kujibu maswali mengi yaliyoelekezwa kwake lakini siku chache baadae alitangaza kujiuzulu akida moyo wake unamsuta hawezi kumuunga mkono mwanasiasa huyo.

UVCCM Wamlipua Kigogo CUF Aliyehoji Uhalali wa CCM Kufanyia Vikao Ikulu

$
0
0
Chama cha Wananchi (CUF), kimetakiwa kuacha kufuatilia na kuhoji uhalali wa kikao cha Kamati Kuu (CC) ya Chama cha Mapinduzi( CCM) kufanya vikao vyake Ikulu kwa madai kuwa kufanya hivyo ni kutumia rasilimali za umma kwa maslahi ya chama.

Aidha taarifa iliyotolewa na Kaimu Katibu Mkuu  wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Shaka Hamdu Shaka ,kwa vyombo vya habari  jijini Dar es salaam, imesema hoja hiyo iliyotolewa na kiongozi wa CUF, Mbarara Maharagande kushutumu hatua hiyo haina mashiko.

“UVCCM tunamwambia mwanasiasa huyo, amekwenda kombo, hajui kulinganisha wala kutofautisha mambo, alichokisema ni porojo tu na hiyo taarifa aliyoiandika kwa umma haina mantiki, haikuwa na kichwa wala miguu,kiufupi haikueleweka na kufahamika alichokusudia kukisema”amesema Shaka.

Shaka amesema kuwa Viongozi mbalimbali wa Upinzani wamekuwa wakialikwa Ikulu na kutumia rasilimia hizo ikiwemo kuandaliwa chakula na vinywaji.

Aidha, amemtaka Maharagande kutumia muda na rasilimali za CUF kutatua mgogoro  uliokigubika chama chao na kuwafanya viongozi wao kutokaa meza moja.

Serikali ya China kujenga kiwanja cha kisasa Chalinze

$
0
0
Serikali ya China imetoa ufadhili wa ujenzi wa uwanja wa Michezo kwa shule ya msingi Msoga iliyopo halmashauri ya wilaya ya Chalinze….

Akizungumza katika hafla ya kuoneshwa eneo patakapojengwa uwanja huo  Rais mstaafu wa awamu ya nne Dkt Jakaya Kikwete  ameishukuru serikali ya China kwa msaada huo kwakuwa Michezo ni Kitu muhimu kwa watoto huku akitoa rai kwa halmashauri ya chalinze kulinda eneo hilo.

Kwaupande wake mwakilishi wa balozi wa China amesema kuwa China inajivunia uhusiano mwema uliopo kati ya China na Tanzania,na watahakikisha wanajenga uwanja huo kwa wakati ili kuwapa fursa watoto kufurahia michezo.

Nae Mbunge wa Chalinze Ridhiwani Kikwete ametoa rai kwa wananchi wake kuhakikisha eneo lililotengwa linalindwa ili dhamira ya china kujenga uwanja huo itimie

Ufadhili wa ujenzi wa uwanja huo wa michezo kwa watoto wa Msoga ni muendelezo wa ufadhili wa China katika kijiji cha Msoga baada ya kujenga shule ya msingi Msoga.

Rais Magufuli Amteua Ngusa Dismas Kuwa Mnikulu Ofisi Ya Rais, Ikulu

Mwenyekiti wa CCM, Dkt Magufuli ataja mambo 10 atakayoanza nayo ndani ya CCM

$
0
0
Leo Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Dkt John Pombe Magufuli ameongoza Kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) kilichofanyika katika ukumbi wa Ikulu jijini Dar es Salaam.

Kikao hiki kilikuwa ni kikao chake cha kwanza tangu alipokabidhiwa mikoba ya kukiongoza cha hicho baada ya mwenyekiti aliyekuwepo Dkt Jakaya Mrisho Kikwete kuomba kung’atuka kabla ya muda wake kuisha.

Akizungumza na wajumbe wa NEC leo, Dkt Magufuli ametaja mambo 10 ambayo anaanza nayo kama mwenyekiti wa CCM. Mambo hayo na haya yafuatayo;-
 
1. Rushwa
Mwenyekiti wa CCM Dkt Magufuli alisema kuwa chama hicho ni miongoni mwa taasisi zinazotuhumiwa sana kwa uwepo wa mianya ya rushwa hasa kipindi cha uchaguzi ndani ya chama au serikali. Amesema katika kipindi chake cha uongozi atahakikisha hakuna kiongozi atakayechaguliwa kwa kutoa rushwa.
 
2. Uimarishaji wa chama
Jambo la pili alilosema wakati akizungumza na wajumbe wa NEC zaidi ya 370 alisema kuwa ni kujenga chama imara kitakachoweza kuwatetea wananchi na kulinda rasilimali zao. Dkt Magufuli alisema wao wamechaguliwa na wananchi kupitia chama hivyo hawapaswi kuwa sehemu ya walalamikaji.
 
3. Wanachama
Chama ni wanachama, ndivyo alivyosema akielezea kuwa ni lazima chama kihakikishe kinaongeza udadi ya wanachama wake hasa vijana. Aidha, ametahadharisha kuwa wanachama hao wasiwe wananchama hewa, bali wawe ni wanachama wakukitumikia chama na watakaolipa ada.
 
4. Chama kujitegemea kiuchumi
CCM ina vitega uchumi vingi sana, lakini kila mara tunakuwa ni ombaomba hasa kipindi cha uchaguzi. Katika kipindi changu cha uongozi hili sitaki kuliona. Ni lazima tuhakikishe mali za chama zinakinufaisha chama na tuweze kujitegemea bila kuwa tegemezi kwa mtu yeyote, alisema mwenyekiti Dkt Magufuli.
 
5. Wasaliti na makundi
Kumekuwepo wanachama ambao si waaminifu ndani ya chama, hawa ni hatari ni lazima tuhakikishe tunakuwa na wanachama wakweli. Pia akizungumzia suala la makundi Dkt Magufuli alisema kuwa makundi ndani ya chama hasa wakati wa uchaguzi yamezidi kushamiri, na wengi huendeleza makundi hata baada ya uchaguzi, ni wakati wa kujenga CCM mmoja.
 
6. Chama Imara kuanzia chini
Hapa alieleza kuwa chama imara ni kile chenye mizizi kuanzia ngazi za chini. Ni lazima tuwe na chama imara kuanzia ngazi za shina, tawi, kata, wilaya, mkoa hadi taifa. Hili litafanukiwa kwa sisi tulipo huku juu kushuka hadi chini katika jitihada za kueleza sera zetu kwa wananchi.
 
7. Nafasi za uongozi
Mwenyekiti wa CCM amesema kuwa wakati wa mtu kuvaa kofia nyingi ndani ya chama ufike mwisho na kuwa sasa ni wakati wa nafasi moja ya uongozi kushikwa na mtu mmoja. Akifafanua hili alisema kuwa litasaidia kutoa nafasi kwa watu wengine pia kukitumikia chama.
 
8. Kufutwa vyeo
Akielezea katiba ya CCM, Dkt Magufuli alisema kuwa katika awamu yake ya uongozi anataka vyeo ambavyo havujatajwa kwenye katiba ya chama visiwepo. Akitoa mfano wa vyeo hivyo alisema ni pamoja na Jumuita ya Wazazi, Chipukizi.
 
9. Uwajibikaji
Alisema kuwa chama kina wajibu wa kuwatumikia wanachama wote bila ubaguzi. Alisisitiza kuwa katika awamu yake ya uongozi hatokubali kuona watu wachache wa vyeo vya juu wananufaika na chama na mamia ya wanachama wa chini wakiteseka.
 
10.  Nguvu ya chama
Jambo hili ambalo alilisema kwa msisitizo na hata kulirudia mara mbilia ni kuwa, anataka chama kinachoongoza wananchama na si wananchama au mwananchama anyeongoza chama. Akitilia mkazo hapa alisema mwanachama ndiye anapaswa kukifuata chama na si chama kumfuata mwanachama au wanachama wachache.

PICHA: Mwenyekiti Wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais Dkt. Magufuli Alivyofungua Kikao Cha Halmashauri Kuu Ya Taifa Nec Jijini Dar Es Salaam

$
0
0
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Rais Dkt. John Pombe Magufuli akiwahutubia Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa NEC kabla ya kufungua rasmi Kikao hicho jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Rais Dkt. John Pombe Magufuli akiwahutubia Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa NEC kabla ya kufungua rasmi Kikao hicho jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Rais Dkt. John Pombe Magufuli akipiga makofi pamoja na Makamu Mwenyekiti wa (CCM Zanzibar) Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein, Katibu Mkuu Abdulrahman Kinana pamoja na Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara Philip Mangula kabla ya kuanza kikao hicho jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya Wajumbe waliohudhuria kikao hicho cha NEC wakifatilia kwa makini Hotuba iliyokuwa ikitolewa na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Rais Dkt. John Pombe Magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa CCM Taifa Abdulrahman Kinana akitoa hotuba yake kabla ya kuanza kwa kikao hicho cha NEC jijini Dar es Salaam. PICHA NA IKULU

Umuhimu Wa Kuwa Na Barua Pepe Ya Biashara

$
0
0
Unakumbuka lile sakata la mmoja wa wagombea kiti cha Urais nchini Marekani kukumbwa na kashfa ya kutumia anwani ya barua pepe binafsi kufanya shughuli za Serikali?

Au umeshawahi kuona barua pepe (Pengine unayo unaitumia) ikiwa na mchanganyiko wa herufi na namba, mfano, wateja wako watajali kweli ukiwa na barua pepe brian255@yahoo.co.tz au brian.mbunde@kampuniyako.co.tz? 

Sasa Extreme Web Technologies ni mshirika rasmi wa Microsoft kwa upande wa Tanzania na wanakufahamisha kwamba katika hii ulimwengu tunaoenda nao wa digitali unapokuwa na professional business email unajenga uaminifu katika biashara yako na unaonekana uko smart sana. 
 
Pengine bado unajiuliza “Professional Email” ni nini, ukiangalia mfano hapo juu wa barua pepe ya brian.mbunde@kampuniyako.co.tz inaonesha jina kamili la mhusika na kuna domain ya kampuni. 

Hii inamaanisha kwamba hauwafanyi watu waone jina lingine tofauti na jina lako halisi hivyo kuwapa mitazamo tofauti linapokuja suala la biashara (Uaminifu) na hapo ndipo Microsoft O365 inakuletea kile unachohitaji mahali unapokuwa.
Unapataje Barua pepe ya Biashara?
Jinsi ya kupata ni rahisi sana, unachotakiwa kufanya ni kuwa tu na email na kisha kuwa na “domain” ambayo imehifadhiwa mahali (server). Baada ya hapo utapewa uhifadhi kumbukumbu unaofikia 1 TB, kuwekewa Microsoft Office kwenye kompyuta mpakato yako na kwenye simu yako pia. Huduma nyingine zinahusisha “HD Video Conferencing”.
 
Kama bado huna uhakika na umuhimu wa “Professional Email” hizi hapa sababu tano za msingi za kwanini unatakiwa kuwa na barua pepe maalum kwa ajili ya biashara yako.
 
1.    Kuonesha Uweledi; “Professional Email” inaonesha kwamba biashara yako imeimarika na inaendeshwa kwa uweledi wa hali ya juu, lakini pia inaonesha uko makini na biashara yako na itakuwepo siku zote. Ukiwa na barua pepe ya kawaida unawapa mashaka wateja kama kweli biashara ni halali na una uzoefu.

2.     Kujenga Picha Kubwa; Barua pepe ya kawaida inaweza kuonesha kwamba biashara yako ni mpya au ndogo. Ukiwa na barua pepe maalum inaleta picha ya kwamba biashara yako ni kubwa na kuipa muonekano wa kampuni haswa. Pia kutengeneza barua pepe kwa ajili ya makundi mbalimbali katika biashara yako mfano finance@kampuniyako.co.tz, info@kampuniyako.co.tz, strategy@kampuniyako.co.tz itaimarisha biashara yako.

3.     Kujenga uaminifu na Imani; Miaka ya karibuni kumekuwa na ongezeko la wizi wa mtandaoni, hivyo wateja wengi huru kutuma taarifa binafsi kwenye barua pepe kama brian@yahoo.com, lakini unapokuwa na barua pepe maalum kwa ajili ya biashara yako unampa mteja hali ya kujisikia salama na uhakika kwa wateja kuwa biashara yako ni halali.

4.    Haina Gharama...Ni Rahisi; Unaweza kuwa na barua pepe maalum kwa jitihada ndogo tu kupitia mtoa huduma za domain au tovuti bure au kwa gharama ndogo sana. Faida kubwa ya kuwa na kusajili domain yako ni kwamba itakuwa pamoja na biashara yako.

5.    Kukuza Biashara Yako; Faida nyingine ya kutumia barua pepe maalum ni kwamba kila wakati unapowasiliana na mtu/mteja unakuza biashara yako. Hivyo kama ulikuwa unafikiria barua pepe maalum ni kwa makampuni makubwa tu, usifikirie hivyo tena.

Kwa Maelezo na taarifa zaidi tafadhali tembeleahttp://bit.ly/baruapepeyabiashara au piga simu namba 0784 987363 / 0715 247365 / 022-2127641 au tuma barua pepe kwenda sales@extremewebtechnologies.com




VIDEO: Tazama Hapa Kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM -NEC Kilivyofanyika pamoja na Maneno yaliyozungumzwa na Rais Maguful

$
0
0

Kikao cha halmashauri kuu ya Taifa ‘NEC’ ya chama cha mapinduzi ‘CCM’ kimekutana leo December 13 2016 ikulu jijini Dar es salaam ikiwa ni kikao cha kwanza kuongozwa na Rais Magufuli tangu achaguliwe kukiongoza chama hicho tawala July mwaka huu. 

Hii ni video nzima  jinsi kikao hicho kilivyokuwa

Mwanzilishi wa tovuti ya JamiiForums, Maxence Melo akamatwa na Polisi

$
0
0
Mwanzilishi wa tovuti ya JamiiForums, Maxence Melo amekamatwa na Polisi jijini Dar es Salaam kwa kukataa kutoa taarifa za watumiaji wa mtandao huo.

Taarifa kutoka kwenye tovuti hiyo zinaeleza kuwa Melo amenyimwa dhamana hivyo atalazimika kukaa rumande mpaka kesho atakapofikishwa mahakamani.

Jeshi la Polisi linadai kuwa Melo amekataa kuonyesha ushirikiano kwa Jeshi hilo ambapo walikuwa wakihitaji majina ya baadhi ya watumiaji wa mtandao huo.

JamiiForums wameeleza kuwa kiongozi huyo (Maxence) alikataa kutoa taarifa hizo kwa kile alichoeleza kuwa kufanya hivyo ni uvunjwaji wa Sheria na Haki za wananchi.

Polepole Ateuliwa Kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM Kuchukua Nafasi ya Nape Nnauye

$
0
0
Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Humphrey PolePole ameteuliwa na Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kuwa Katibu wa Halmashauri Kuu Itikadi na Uenezikuchukua  nafasi ya  Nape Nnauye

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na chama hicho kupitia ukurasa wake wa Twitter zinaeleza kuwa kikao chaHalmashauri Kuu ya Taifa kimemteua Polepole kushika wadhifa huo.

Kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM kimefanyika leo ambapo miongoni mwa mambo mengi yatakayojadiliwa ni pamoja na tathmini ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Halmashauri Kuu ya CCM Yamteua Rodrick Mpogolo kuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM upande wa Bara

$
0
0
Halmashauri Kuu ya CCM imemteua aliyewahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Chato na baadaye mshauri wa Rais masuala ya siasa, Bwana Rodrick Mpogolo kuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho upande wa Bara, akichukua nafasi ya Rajab Luhwavi aliyeteuliwa kuwa Balozi

Haya Ndiyo Maamuzi Ya Halmashauri Kuu Ya Taifa Ya CCM Baada Ya Kikao Chake Cha Siku Moja

$
0
0
Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM imekutana leo tarehe 13/12/2016 jijini Dar es salaam kwa kikao cha siku moja cha kawaida. Kikao hicho kimeongozwa na Mwenyekiti wa Taifa wa CCM Dkt. John Pombe Magufuli.

Pamoja na mambo mengine, Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM imepokea taarifa ya Tathimini ya Uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, baada ya kuitafakari taarifa hiyo, Halmashauri Kuu imeamua yafuatayo;-

1. Kupunguza idadi ya wajumbe wa vikao na idadi ya vikao vya Chama katika ngazi mbalimbali ili kuongeza ufanisi wa utendaji wa Chama na kuongeza muda wa viongozi wa Chama kufanya kazi za Chama kwa Umma badala ya kutumia muda mwingi vikaoni.

Ili kuwa  na vikao vya Chama vyenye tija imeamuliwa kama ifuatavyo:-

a). Halmashauri Kuu ya Taifa kwa sasa ina jumla ya wajumbe 388 idadi ambayo ni kubwa sana, hivyo imeamuliwa idadi hii ipunguzwe na kuwa wajumbe 158 kama  ifuatavyo:-

Wenyeviti wa Mikoa
Mikoa ya Bara           26x1    =      26
Mikoa ya Zanzibar      6x1   =          6

Wajumbe wa NEC wa Mikoa
 Mikoa ya Bara    26x1         =        26
 Mikoa ya Zanzibar   6x4         =        24
Wajumbe wa NEC wa Taifa
 Kutoka  Bara    =               15
 Kutoka  Zanzibar     =               15

Nafasi za Mwenyekiti   =                7

Wajumbe wa NEC wa Jumuiya
        UVCCM     =        5
        UWT   =        5
        WAZAZI    =        5
Wajumbe wa NEC kutoka Bungeni     =        5

Katibu wa Kamati ya Wabunge wa CCM      =       1

Wajumbe wa  NEC kutoka BLW   =       3

Katibu wa Kamati ya Wawakilishi =       1

Wajumbe wa NEC – wanaotokana na Nyadhifa zao
- Mwenyekiti wa CCM                  =       1
- Makamu Mwenyekiti (B)         =       1
-Makamu Mwenyekiti (Z)           =       1
- Makamu wa Rais                        =       1
-  Waziri Mkuu                               =       1
- Makamu wa Pili wa Rais (Z)   =       1
- Spika wa Bunge                          =       1
- Spika  wa  BLW                           =       1
- Mwenyekiti wa UWT                =       1
- Mwenyekiti wa WAZAZI          =       1
-Mwenyekiti wa UVCCM             =       1
- Katibu Mkuu – WAZAZI            =       1
- Katibu Mkuu – UWT                   =       1
- Katibu Mkuu – UVCCM              =       1
                                              Jumla:      158
#. Vikao vya kawaida vya Halmashauri Kuu ya Taifa vifanyike kila baada ya miezi sita badala ya miezi minne kama ilivyo sasa isipokuwa vinaweza kufanyika vikao maalum inapohitajika.

b). Kwa upande wa sasa imeamuliwa wajumbe wa Kamati Kuu wawe 24 badala ya 34 kama ifuatavyo:-

Mwenyekiti wa CCM.
Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara)
Makamu Mwenyekiti wa CCM        (Zanzibar)
Makamu wa  Rais
Katibu Mkuu wa CCM
Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara)
Naibu Katibu Mkuu wa CCM  (Zanzibar)
Waziri Mkuu
Makamu wa Pili wa Rais (Z)
Spika wa Bunge la Tanzania
Spika  wa BWL
Mwenyekiti  wa WAZAZI
Mwenyekiti  wa UWT
Mwenyekiti  wa UVCCM
Katibu wa   wa Halmashauri Kuu ya Taifa wa  Organaizesheni
Katibu wa   wa Halmashauri Kuu ya Taifa wa  Itikadi na Uenezi
Katibu wa   wa Halmashauri Kuu ya Taifa wa  Uchumi na Fedha
Katibu wa   wa Halmashauri Kuu ya Taifa wa  Mambo ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa
Wajumbe  watatu (3)  wa kuchaguliwa  na Halmashauri Kuu kutoka Tanzania

Wajumbe watatu  (3) wa kuchaguliwa  na Halmashauri Kuu kutoka Zanzibar.

#. Vikao vya kawaida vya Kamati Kuu vipunguzwe ili vifanyike kila baada  ya miezi minne badala ya miezi miwili isipokuwa vinaweza kufanyika vikao maalum inapohitajika.

c). Kwa ngazi ya mkoa, Wajumbe wa Kamati za Siasa za Mikoa wapunguzwe kwa kuondoa wajumbe  watatu ambao ni:-
Katibu wa Uchumi na Fedha wa Mkoa         -       1
Wajumbe wa kuchaguliwa na H/Mkoa        -       2

#. Vikao  vya kawaida vya Kamati ya Siasa ya Mkoa vifanyike kila baada ya miezi mitatu badala ya kila  mwezi kama ilivyo sasa isipokuwa vinaweza kufanyika vikao maalum inapohitajika.

d). Kwa upande wa Wilaya Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilaya wapunguzwe kwa kuwoandoa:-
 Katibu wa Uchumi na Fedha wa Wilaya    -       1
 Katibu wa Kamati ya Madiwani                   -       1
 Wajumbe wa kuchaguliwa na H/Kuu ya (W)-  2
  Jumla:  4

#.Vikao  vya kawaida  vya Kamati ya Siasa ya Wilaya  vifanyike kila baada ya miezi mitatu badala ya kila  mwezi isipokuwa vinaweza kufanyika vikao maalum inapohitajika.

#. Muundo wa Wilaya za Chama uendane na muundo wa sasa wa Serikali.

Kata,Tawi na Shina
Idadi ya kuanzisha Shina iwe wanachama 50  hadi 300.

Idadi ya kuanzisha Tawi iwe wanachama kuanzia 301 hadi 1,000.
Hata hivyo idadi hii izingatie eneo la kijiografia na wingi wa wanachama katika eneo hilo.

Vikao vya kawaida vya  Kamati za Siasa  za  ngazi hizi viwe vinafanyika mara moja kila baada ya miezi mitatu, isipokuwa vinaweza kufanyika vikao maalum inapohitajika.

#. Nafasi za Uongozi
Mwanachama anatakiwa kuwa na nafasi  moja tu ya uongozi wa kazi za muda wote kama ilivyoainishwa kwenye Kanuni za uchaguzi wa Chama Toleo la 2012 kifungu cha 22 na 23 ambazo zimetajwa kuwa ni:-
Mwenyekiti wa Tawi,Kijiji au Mitaa.
Mwenyekiti wa Kata/Wadi.
Mwenyekiti wa Jimbo, Wilaya na Mkoa.
Makatibu wa Halmashauri Kuu wa ngazi zote zinazohusika.
Mbunge, Mwakilishi na Diwani.

#. Viongozi wa kuchaguliwa waepuke kuwa watendaji badala yake waongoze na kusimamia shughuli za Chama kwa kuzingatia Katiba na Kanuni.

#.Vyeo ambavyo haviko kwenye Katiba
Vyeo  ambavyo havijatamkwa kwenye Katiba ya CCM haviruhusiwi katika Chama au Jumuiya zake mfano Umoja wa makundi mbalimbali kama Wenyeviti wa ngazi mbalimbali (mfano: Mwenyekiti wa Wenyeviti wa CCM n.k), Makamanda (UVCCM), Washauri (UWT) na Walezi (WAZAZI) katika ngazi zote.

#. Uhakiki wa Wanachama wa CCM
Halmashauri Kuu imeona ipo haja ya kufanya uhakiki wa wanachama wa CCM  na Jumuiya zake ili kujua idadi sahihi ya wanachama wetu kwa wakati huu.   Uhakiki huu uendane na kutoa kadi mpya za uanachama za kielektroniki ili kuwa na udhibiti wa usahihi wa wanachama na kuondoa wanachama HEWA. Aidha, Kadi za UWT, WAZAZI na UVCCM zifutwe ili tubaki na kadi za CCM tu.

#. Jumuiya za Chama Cha Mapinduzi
Jumuiya za CCM  zimetakiwa kufanya kazi zake kwa kuzingatia matakwa ya Katiba ya CCM na Kanuni za Jumuiya husika, kanuni za Jumuiya ziendane na  matakwa ya Katiba ya CCM.

#.Uaendeshaji  wa shughuli zote za Jumuiya za Chama na mali zake uwe chini ya usimamizi wa Chama Cha Mapinduzi. (Baraza la Wadhamini la Chama Cha Mapinduzi).
Makatibu Wakuu wa Jumuiya watakuwa wanateuliwa na Kamati Kuu  na  Manaibu Katibu Wakuu watateuliwa na Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa.

#. Wakati tukiendelea kubaki  na Bendera yenye rangi ya kijani na njano  na  alama ya jembe na nyundo, Halmashauri Kuu imeona ipo haja ya kuzifanya rangi hizo kuwa na muenekano wa kuvutia zaidi.

#. Utumishi  katika  Chama na Jumuiya zake. Katibu Mkuu wa CCM na Sekretarieti ipewe majukumu ya kusimamia ajira za Watumishi wa Chama na Jumuiya zake.

Nafasi za Makatibu Wasaidizi wa Mikoa na Wilaya zitaondolewa na badala yake kazi zao zitatekelezwa na Makatibu wa Jumuiya  za Chama wa Mikoa na Wilaya kwa utaratibu utakaopangwa.  Utaratibu huu utakipunguzia Chama Cha Mapinduzi gharama na kujenga umoja wa utendaji kazi wa Chama na Jumuiya zake katika Mikoa na Wilaya.

#. Tathimini ya hali ya Kisiasa na  Uchaguzi wa    Zanzibar .
Halmashauri Kuu ya Taifa imeagiza kuundwa kwa Kamati maalum ya kufanya tathimini ya kina kuhusu hali ya kisiasa Zanzibar kwa ujumla na masuala yanayohusu uchaguzi wa Zanzibar 2015.

# Mwenyekiti wa Kamati ya udhibiti na nidhamu ametakiwa akamilishe kazi ya taarifa ya udhibiti kwa wanachama waliokiuka mienendo ya kiuanachama kabla ya kuanza uchaguzi Mkuu wa Chama mwezi Februari 2017, Mikoa na Wilaya ambazo hazijaleta taarifa zao za kiudhibiti ziwe zimefikisha taarifa zao kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Udhibiti na Nidhamu kabla ya tarehe 30/01/2017.

#. Uhakiki wa Mali za Chama uendelee kufanyika kwa kina na uchambuzi zaidi ukikamilika Taarifa yake iwasilishwe kwa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa mapema iwezekanavyo.

#. Maamuzi na mapendekezo haya yatapelekea kufanyika kwa mabadiliko ya Katiba ya Chama na Kanuni za Jumuiya  za Chama.

#. Kwa mambo yale ambayo yatahitaji mabadiliko ya Katiba, Mkutano Mkuu utaandaliwa mapema mwakani na kutafakari na kupitisha mabadiliko hayo ya Katiba.

Mwenyekiti wa CCM Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ameteua wafuatao kujaza nafasi mbalimbali ndani ya sekretarieti ambazo zimekuwa wazi kutokana na waliokuwa wakizishikilia kupewa majukumu mengine ya kiserikali.

#.Ndg. Rodrick Mpogolo anakuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Ndg. Rajabu Luhwavi ambaye ameteuliwa kuwa balozi.
#. Col. Ngemela Eslom Lubinga- Kuwa Katibu NEC Siasa na Uhusiano wa Kimataifa kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Dr. Asha-Rose Migiro aliyeteuliwa kuwa Balozi
#. Humphrey Polepole kuwa Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Ndg. Nape Nnauye aliyeteuliwa kuwa Waziri.
#. Wajumbe wengine watabaki kama walivyo sasa.

Imetolewa na:-

NAPE NNAUYE
IDARA YA ITIKADI NA UENEZI
13/12/2016

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Jumatano ya Disemba 14

Rais Dkt Magufuli ateua Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango.

$
0
0
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, jana tarehe 13 Desemba, 2016 amemteua Dkt. Khatib M. Kazungu kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango.

Dkt. Khatib M. Kazungu anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Bw. Doto James ambaye aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango.

Kabla ya Uteuzi huo Dkt. Khatib M. Kazungu alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, iliyopo katika Mkoa wa Mtwara.

Uteuzi huu unaanza mara moja.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Watumishi TRA Wafikishwa Mahakamani kwa Rushwa ya Milioni 66

$
0
0
Maofisa waandamizi wa kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Tawi la Kariakoo, Dar es Salaam na mfanyakazi mmoja, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala, wakikabiliwa na makosa ya kujipatia Sh milioni 66 kwa njia ya rushwa.

Maofisa hao ni Liberatus Rugumisa (30), Keneth Mawere (29) na mfanyakazi mmoja Nassoro Nassoro (42) wote wakazi wa Kigamboni, Dar es Salaam.

Mwendesha Mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Lupyana Mwakatobe alidai jana mbele ya Hakimu Mkazi, Adelf Sachore kuwa washitakiwa hao walitenda makosa hayo kwa madai ya kumpunguzia kodi mfanyabiashara Humphrey Lema kinyume na sheria zao.

Katika mashitaka ya kwanza, Mwakatobe alidai kuwa Novemba 18 mwaka huu, maeneo ya ofisi za TRA Kariakoo wilayani Ilala, Rugumisa na Mawere wakiwa waajiriwa wa mamlaka hiyo, walijipatia rushwa ya Sh milioni 50 kutoka kwa Lema kwamba wangempunguzia Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).

Pia, alidai kuwa Novemba 23 mwaka huu, katika duka la kubadilishia fedha la Cate lililopo kati ya mtaa wa Nyamwezi na Donge, Kariakoo wilayani Ilala, walijipatia Sh milioni 10 kutoka kwa mfanyabiashara huyo kwa madai watampunguzia VAT.

Katika mashitaka ya tatu ambayo yanawakabili washitakiwa wote, inadaiwa washitakiwa walijipatia rushwa ya dola za Marekani 2,744 sawa na Sh milioni sita kutoka kwa Lema kwamba wangeweza kumpunguzia VAT, kinyume na maadili ya kazi hiyo.

Washitakiwa walikana mashitaka hayo na kurudishwa rumande kwa kushindwa masharti ya dhamana. Hakimu Sachore alitaja masharti hayo kuwa ni wadhamini wawili kutoka taasisi inayotambulika, watakaosaini bondi ya Sh milioni mbili. Hata hivyo, aliahirisha kesi hiyo hadi Desemba 27 mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa.

Hashim Rungwe kumtetea ‘Ndama mtoto wa ng’ombe’....Kesi yake Yaahirishwa Hadi Disemba 27

$
0
0

Wakili wa kujitegemea, Hashimu Rungwe amejitokeza kumtetea mfanyabiashara maarufu jijini Dar es Salaam, Ndama Shabani Hussein maarufu kama ‘Pedeshee Ndama mtoto wa Ng’ombe’. 

Rungwe aliyekuwa mgombea urais kupitia Chaumma katika Uchaguzi Mkuu uliopita, alijitokeza jana na kujitambulisha mahakamani kuwa ndiye atamtetea mshitakiwa huyo. 

Ndama mtoto wa ng’ombe (44) anakabiliwa na mashtaka ya kughushi, kutakatisha fedha na kujipatia dola za Marekani 540,390 kwa njia ya udanganyifu. 

Baada ya kujitambulisha mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Victoria Nongwa, Wakili wa Serikali, Christopher Msigwa alisema kesi hiyo imepangwa kutajwa, upelelezi bado haujakamilika na akaomba ipangiwe tarehe nyingine. Hakimu Nongwa aliiahirisha kesi hiyo hadi Desemba 27,2016. 

Mshtakiwa huyo alipelekwa rumande kwa sababu miongoni mwa mashtaka yanayomkabili limo shtaka la kutakatisha fedha ambalo halina dhamana. 

Katika kesi hiyo, Ndama anadaiwa kuwa Februari 20,2014 jijini Dar es Salaam, alighushi kibali cha kusafirisha madini kuonyesha kuwa kampuni ya Muru Platnum Tanzania Investment Company Limited iliruhusiwa kusafirisha kilo 207 za dhahabu yenye thamani ya Dola za Marekani 8,280,000 kwenda Australia wakati akijua si kweli. 

Mshtakiwa huyo anadaiwa kuwa Machi 6, 2014 jijini Dar es Salaam alitengeneza kibali cha Umoja wa Mataifa ofisi ya Dar es Salaam akijaribu kuonyesha dhahabu hiyo kutoka Congo inatarajiwa kusafirishwa kwenda Australia. 

Mshtakiwa huyo anadaiwa kuwa kati ya Februari 26 na Machi 2014 katika jiji la Dar es Salaam alitakatisha fedha kwa kufanya muhamala wa dola za Marekani 540,390 kwa kuelekeza ziwekwe katika akaunti namba 9120000085152 iliyopo katika benki ya Stanbic yenye jina la Muru Platnum Tanzania Investment Company Limited na kuanza kuzitoa taslimu wakati akijua fedha hizo zinatokana na zao la uhalifu.

Lowassa adai T.B Joshua ameitabiria Chadema ushindi

$
0
0

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa amesema ataingia Ikulu baada ya miaka minne ijayo na rafiki yake T.B Joshua amemtabiria kuwa Serikali ijayo itaongozwa na Chadema. 

Lowassa, ambaye alishika nafasi ya pili katika kinyang’anyiro cha urais mwaka jana, ameshaonyesha nia ya kuingia tena kwenye mpambano huo wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020. 

Akizungumza na viongozi na wanachama wa Chadema mkoani Tabora, waziri huyo mkuu wa zamani alisema ana uhakika wa kuingia Ikulu bila ya umwagaji wa damu. 

Huku akishangiliwa, Lowassa ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, aliwashukuru wana Tabora na Watanzania kwa ujumla kwa kura walizompa katika uchaguzi mkuu uliopita. 

Lowassa aliwaeleza wanachama na viongozi wa chama hicho kuhusu utabiri wa T.B.Joshua na angalizo alilompa. 

Alisema muhubiri huyo maarufu barani Afrika anayefanya shughuli zake nchini Nigeria na ambaye alikuja nchini mara baada ya Uchaguzi Mkuu uliopita, alimpa angalizo kuwa ili washinde ni lazima wawe wamoja, washikamane na kuwa majasiri.

 “Najua waandishi wa habari wataandika, lakini sijali rafiki yangu Joshua ametabiri Serikali ijayo ya Tanzania itaongozwa na Chadema,” alisema. 

Lowassa amekuwa akienda Lagos, Nigeria kuhudhuria ibada za T.B Joshua anayeongoza kanisa la The Synagogue Church of All Nations na ambaye amekuwa akitabiri matukio makubwa kutokea sehemu mbalimbali duniani. 

Katika kudhihirisha urafiki wake na T.B Joshua, Lowassa alisema katika mahafali ya wanafunzi wa vyuo vikuu ambao ni wanachama wa Chadema yaliyofanyika jijini Dar es Salaam katikati ya mwaka, kuwa CCM ilimuita nabii huyo nchini baada ya uchaguzi ili amshawishi akubali matokeo. 

Lowassa aliwaambia wanafunzi hao kuwa alimweleza T.B Joshua matukio yote yaliyotokea wakati wa uchaguzi na hivyo kumfanya nabii huyo aamue kutohudhuria sherehe za kuapishwa.

 Hata hivyo mwenyewe T.B Joshua hajathibitisha kauli hiyo ya Lowassa. Kuhusu Tabora, Lowassa alisema ni mkoa wa kihistoria na ndio kitovu cha siasa nchini kwa kuwa ndiko kulikoanza vuguvugu la mapambano ya kudai uhuru na kwamba una heshima yake kisiasa. 

Aliwataka viongozi na wanachama wa Chadema kuhakikisha wanalinda heshima hiyo kwa kuifanya Chadema kuongoza nchi. 

Lowassa, ambaye aliwahi kuwa Waziri Mkuu, aliwaeleza wanachama na viongozi kuwa ruzuku ni fimbo ya kuwagombanisha wanachama katika vyama vya siasa. 

Aliwataka wanachama na viongozi kuhakikisha hawagawanywi na ruzuku na kwamba waulinde Ukawa na wakatae kuvurugwa. 

“Vyama vingi nchi za Afrika hugawanywa kwa fedha za Serikali zilizopo madarakani, jambo ambalo sisi tulikatae,” alisema. 

Aliwaleza wanachama hao ruzuku inatolewa ili wanachama wabaki wakigombana na kushindwa kufanya mambo ya msingi. 

Akiizungumzia elimu, Lowassa alisema CCM inapata ushindi katika maeneo ambayo yapo nyuma kielimu na kuitaja mikoa ya Singida, Mtwara, Lindi, Dodoma na Tabora. 

Alieleza kuwa mikoa iliyo nyuma kielimu ndio ngome ya chama tawala na kwamba ndio maana anaposisitiza elimu itolewe bure, anajua anachomaanisha. 

Mbunge huyo wa zamani wa Monduli aliambatana na mjumbe mwingine wa Kamati Kuu ya Chadema, Mwita Waitara, ambaye katika hotuba yake alisisitizia suala la tume huru ya uchaguzi. 

Waitara, ambaye ni mbunge wa Jimbo la Ukonga aliwataka wanachama wa Chadema kusimama imara kudai tume huru. 

Awali, mratibu wa Chadema wa Kanda ya Magharibi, General Kaduma alisema watu watakaojaribu kuwagawa wanachama, watawekwa pembeni ili wawaache wengine waendelee kuongoza chama. 

Alisema madhumuni ya mikutano ya ndani ya chama hicho inayoendelea nchi nzima ni kupanga mambo yanayohusu ujenzi wa chama chao na kuwakumbusha viongozi mambo ya msingi ya chama.

Serikali Yamwaga Ajira za Walimu wa Sayansi na Hisabati

$
0
0
SERIKALI imetangaza kuajiri walimu wa masomo ya sayansi na hisabati katika shule za sekondari ambao wametakiwa kupeleka nakala za vyeti vyao vya elimu ya sekondari, vya taaluma ya ualimu (stashahada na shahada) kwa ajili ya uhakiki.

Tangazo kwa Umma lililotolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Maimuna Tarish lilisema vyeti vya sekondari vinavyotakiwa kuhakikiwa ni vya kidato cha sita.

Alisema ajira hizo ni kwa walimu wa Stashahada na Shahada za Mafunzo ya Ualimu wa Masomo ya Hisabati na Sayansi waliohitimu mwaka 2015.

Alisema nakala hizo ziwasilishwe kupitia barua pepe ya wizara kuanzia jana hadi Ijumaa ya Desemba 16 mwaka huu na yeyote ambaye vyeti vyake havitahakikiwa hatafikiriwa katika uajiri.

Kamanda Sirro: Aliyetishwa na kauli ya Mzee wa Upako afungue kesi

$
0
0
Polisi  Kanda Maalumu ya Dar es Salaam imemtaka yeyote anayeona kuwa kauli iliyotolewa na Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Maombezi (GRC), Anthony Lusekelo maarufu Mzee wa Upako imetishia maisha yake, afungue kesi.

Kamanda wa kanda hiyo, Simon Sirro aliyasema hayo jana Dar es Salaam wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari waliotaka kujua hatua polisi waliyoichukua kutokana na kauli aliyoitoa Mchungaji huyo kwamba waandishi waliomwandika vibaya watakufa kabla ya Machi mwakani.

“Kama kuna mtu anaona katishika na kauli hiyo aje afungue kesi milango iko wazi. Kama kuna mwandishi yeyote anayeona ametishika na kauli hiyo aje, kesi ikifunguliwa tutaifanyia kazi kwa sababu hadi sasa hakuna aliyelalamika,” alisema.

Kauli ya Mzee wa Upako aliitoa katika mahubiri yake ya Jumapili ikiwa ni mwendelezo wa majibu yake kutokana na tuhuma zilizoandikwa kwenye baadhi ya vyombo vya habari kwamba alimfanyia fujo jirani yake.

Wakati huo huo, Sirro alisema kuwa wanaendelea na uchunguzi wa madai ya kupotea kwa Bernard Saanane ambaye ni kiongozi wa Chadema. Kiongozi huyo anadaiwa kupotea tangu Novemba 18.

“Kuna watu wanasema wanataka ile miili ichunguzwe… lile ni tukio la Pwani na mwenye wasiwasi anaruhusiwa kuwasiliana na uongozi wa kule kwa sababu ule ni mkoa mwingine,” alisema. 

Hata hivyo, alipoulizwa kuhusu kukamatwa kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Jamii Forum, Maxence Melo alisema atazungumzia suala hilo Ijumaa.

Polisi Dar yawatia mbaroni watu 22 kwa kosa la uporaji katika magari

$
0
0
Kikosi  maalumu cha kupambana na wizi wa kutumia silaha na wizi wa kutumia nguvu cha Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, kimewakamata watuhumiwa 22 kwa makosa ya kuwapora wenye magari na wapitanjia kwenye mataa ya kuongozea magari.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Simon Sirro alisema watuhumiwa hao, wamekuwa wakijiunda kwenye vikundi na kuwanyang’anya watu wenye magari na watembea kwa miguu mali zao kama simu za mikononi, kompyuta, saa na fedha.

Alisema ufuatiliaji ulifanyika na kuwakamata watuhumiwa hao kwa nyakati tofauti, ambapo Desemba 11 mwaka huu huko Temeke maeneo ya Keko Magurumbasi na mataa ya Veta na Chang’ombe walikamatwa watuhumiwa 10 kwa makosa ya wizi kutoka maungoni na wizi kutoka kwenye magari.

Aliwataja baadhi ya watuhumiwa hao kuwa ni Ayubu Amiri (19), mkazi wa Mtoni Mtongani, Shabani Fadhili(18) mkazi wa Keko, Herman Francis (26), mkazi wa Keko Magurumbasi na wenzao saba.

“Katika mahojiano watuhumiwa wamekiri kujihusisha na makosa mbalimbali yakiwemo unyang’anyi wa kutumia silaha na kutumia nguvu,” alisema.

Aidha alisema uchunguzi wa awali umebaini mtuhumiwa Herman Francis anakabiliwa na tuhuma za mauaji, ambapo Machi 20 mwaka huu alimchoma mtu kisu na kutoroka kusikojulikana. 

Wakati huo huo, Desemba 12 mwaka huu askari waliwakamata watuhumiwa wengine 12 kwa makosa ya wizi kutoka kwenye magari.

Watuhumiwa hao wametajwa kuwa ni Sande Kassim (18), mkazi wa Keko, Emmanuel Abeli (21), Paulo Abeli(18), Jafari Nyerere (22), Hamis Salum (22), Hemed Idrisa(22) wote wakazi wa Keko na wenzao sita.

Katika tukio lingine, polisi wamewakamata watuhumiwa wanne wanaojihusisha na wizi kwa kuwarubuni watu kwa kukodi magari yao na baadaye hutumia nguvu  kuwapora.

Watuhumiwa hao wametajwa kuwa ni Juma Kajeni (35), mkazi wa Tabata, Hamadi Kaganda (38), mkazi wa Mbagala, Mashaka Ally(62), mkazi wa Yombo na Mshamu Ally (32), mkazi wa Mtongani. 

Alisema watuhumiwa wote wanaendelea kuhojiwa na upelelezi utakapokamilika watapelekwa mahakamani kujibu mashtaka yanayowakabili.

Pia aliwatahadharisha wananchi na wamiliki wa magari kuwa makini kwa watu hao ambao huja kwa nia ya kuwalipa fedha nyingi au kukodi gari kwa kiwango kikubwa na kisha wanatokomea na gari.

Wakati huo huo, polisi Kanda Maalum Dar es Salaam kupitia kikosi kazi chake cha kupambana na wizi wa magari kimekamata magari matatu ya wizi katika mikoa mbalimbali. 

Sirro alilitaja gari lenye namba T 386 CGY aina ya Verosa rangi nyeusi, mali ya Abraham Robert wa jijini Dar es Salaam na gari hilo lilikamatwa mkoani Mbeya likiwa limetelekezwa.

Gari jingine ni lenye namba T 946 DGH aina ya IST rangi ya fedha ikiwa inaendeshwa na mtuhumiwa aitwaye Hamadi Saidi (27) mkazi wa Kimara Dar es Salaam ambalo lilikamatwa huko mkoani Morogoro, gari hilo liliibiwa maeneo ya Kawe Beach jijini Dar es Salaam.

Alilitaja gari lingine kuwa ni Mitsubishi Canter lenye namba T 753 CVZ ambazo ni namba bandia huku namba zake halisi zikiwa ni T.815 DJF mali ya Magreth iliibiwa maeneo ya Kimara Suka jijini Dar es Salaam.

Alisema mtuhumiwa mmoja aliyekamatwa anaendelea kuhojiwa na upelelezi utakapokamilika atapelekwa mahakamani. 

Pia alisema  watuhumiwa wengine waliohusika na wizi wa magari hayo wanaendelea kutafutwa ili kubaini mtandao mzima wa wizi wa magari na watuhumiwa wengine wanaotafutwa kwa wizi wa magari hapo nyuma ambao walikimbia.
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live




Latest Images