Quantcast
Channel: MPEKUZI
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Jumatatu ya May 30


Naibu Waziri Wa Mambo Ya Ndani Ya Nchi Afanya Ziara Gereza la Msalato – Dodoma

$
0
0


Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni amesema Serikali imejipanga kulitumia Jeshi la Magereza kuhakikisha Tanzania inaingia kwenye uchumi wa viwanda.

Lengo hilo ni mkakati wa wizara kutaka kuendana na kauli ya Rais John Magufuli ambaye amekuwa akisisitiza kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda kuelekea kwenye uchumi wa kati ifikapo 2025.

Masauni aliyasema hayo jana alipotembelea mradi wa kiwanda cha kokoto cha Gereza la Msalato kilichopo Dodoma. Alisema Magereza ina rasilimali nyingi ambazo zikitumika kikamilifu zinaweza kuifanya nchi kupiga hatua.

 Alisema kuna fursa nyingi ambazo jeshi hilo linaweza kuzitumia kufikia azma hiyo, ikiwamo kuanzisha kiwanda cha viatu kwa ajili ya askari wa majeshi mbalimbali.

 “Inashangaza kuona majeshi yetu yananunua viatu kutoka nje wakati vinaweza kutengenezwa na Magereza.Lazima tujipange na ninaamini Jeshi la Magereza linaweza kuifanya kazi hiyo,” alisema Masauni. 

Akizungumzia mradi wa kokoto wa gereza hilo, alisema zinahitajika Sh2.5 bilioni kwa ajili ya uwekezaji katika mradi huo.

 Alisema kiwanda hicho kikianza kazi kitakuwa na uwezo wa kukusanya mapato ya Sh6.8 bilioni kwa mwaka. Alisema kuna namna mbalimbali jeshi hilo linaweza kupata mtaji huo ikiwa ni pamoja na kuomba mkopo kwenye benki za nchini, kuingia ubia na mwekezaji au kupata ruzuku kutoka serikalini.

“Nataka Magereza watafute namna ya kupata fedha hizo bila kusubiri ruzuku kutoka serikalini. Najua watapata fedha hiyo kwa sababu mradi huu ni mkubwa na utalifanya jeshi hili kuongeza mapato,” alisema.

 Masauni aliongeza kuwa anataka kuona siku moja jeshi hilo linajiendesha kwa kujitegemea kuanzia kwenye chakula cha wafungwa mpaka miundombinu yake.

Alisema hilo litawezekana kama watawekeza kwenye viwanda. Mrakibu Msaidizi wa Magereza, Patrick Nasola alisema mradi huo utaendeshwa na jeshi hilo na kuwa watakuwa tayari kumuuzia mtu yoyote kokoto watakazozalisha.

Alisema mradi huo ukianza kazi utakuwa na uwezo wa kuzalisha tani 15 za kokoto kwa siku. Alisema changamoto wanayokabiliana nayo ni uhaba wa fedha kwa ajili ya kutengeneza mtambo wao ambao sasa umeharibika.

“Walikuja wataalamu katika eneo hili la Msalato kupima wakabaini kuna madini mawe mengi na sasa tuna leseni 15 kwa ajili ya madini mawe. Mawe yaliyopo hapa ni kama yale yanayotumika kutengeneza tiles,” alifafanua.

Nasola aliongeza kuwa wataweza kuzalisha fedha nyingi kutokana na mradi huo kwa sababu ni eneo kubwa ambalo kwa ujumla wake lina madini mawe ya kutosha. Alisema wanatarajia kuuza zaidi kokoto ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Msalato utakapoanza.

Kwa upande wake, Mkuu wa Gereza la Msalato, Steven Mwihambi alisema kokoto ni moja ya miradi inayofanyika katika gereza hilo.

Alitaja miradi mingine kuwa ni ufugaji, kilimo na utengenezaji wa samani. “Tutaanzisha viwanda vidogo vidogo kwa ajili ya mazao tunayozalisha kama vile alizeti. Changamoto kubwa ni uhaba wa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mipango yetu,” alisema kiongozi huyo wa gereza.

Serikali Yapiga Marufuku Pombe Ya Viroba ya Kwenye Mifuko Ya Plastiki

$
0
0

Mifuko ya plastiki inayofungasha pombe maarufu kama ‘viroba’ imepigwa marufuku na Serikali kuanzia mwakani. 

Sambamba na hilo Serikali pia, imepiga marufuku moja kwa moja utengenezaji, usambazaji, uingizaji nchini wa mifuko ya plastiki kuanzia mwaka huo.

Waziri wa Nchi , Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba aliwaambia wanahabari jana sehemu kubwa ya mifuko hiyo inayotolewa bure imekuwa ikichangia uchafuzi wa mazingira kwa kiasi kikubwa.

Wakati Makamba akiyasema hayo, Februari mwaka huu Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Luhaga Mpina aliondoa zuio la matumizi ya mifuko ya plastiki akisema kuwa itaziweka rehani ajira za Watanzania wanaofanya kazi kwenye viwanda vinavyotengeneza mifuko hiyo.

Pia, Mpina alisema itapunguza kasi ya uwekezaji wa viwanda vilivyowekeza katika bidhaa hiyo.

Akizungumza katika siku ya Mazingira Afrika, Mkurugenzi wa Mazingira, Dk Julius Ningu alisema maamuzi hayo yamelenga kulinda viwanda vilivyoajiri mamia ya Watanzania, tofauti na nchi nyingine zinazotegemea wazalishaji wa nje ya nchi.

Makamba akizungumzia uamuzi mpya wa kuzuia mifuko ya plastiki, alisema matumizi ya mifuko inayofungashia vileo na inayotumika katika matumizi mengine husambaa na kuchafua mazingira. Alisema mifuko ya plastiki inatajwa kuziba mifereji na kusababisha mafuriko na athari nyingine za mazingira.

“Leo (Jana), tumeamua kutangaza ili kuwaanda wahusika wasiendelee kuwekeza katika mifuko hii badala yake wasubiri utaratibu mwingine utakaowekwa na Serikali,” alisema Makamba na kuongeza kuwa:

 “Asilimia kubwa ya uchafu kwenye nyanzo vya maji, mito, maziwa na fukwe za bahari ni mifuko ya plastiki.” 

Makamba ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli, alisema Serikali inakamilisha majadiliano ya ndani na baadaye itawahusisha wadau kuhusu dhamira ya kupiga marufuku ya moja kwa moja mifuko hiyo.

Alifafanua kwamba Serikali itatoa muda kwa walioajiriwa, kujiajiri na kuwekeza kwenye biashara ya mifuko hiyo ili kujiandaa kuacha shughuli hizo na badala yake itawezesha mazingira ya utengenezaji na upatikanaji wa vifungashio mbadala.

“Kwa wanaotengeza mifuko hii na kuiuza katika soko la nje hatuna tatizo nao waendelee. Ila kwa soko la ndani hawataruhusiwa kufanya hivyo.Zuio hili litakuwa la kisheria siyo kwa maneno,” alisisitiza Makamba. 

Aliongeza kuwa katika kuonyesha Serikali imedhamiria kupambana na hali hiyo wizara yake imeamua kutuma timu ya watu watano kwenda Rwanda kujifunza namna bora ya kudhibiti matumizi na kuzuia mifuko hiyo tangu mwaka 2008.

Waziri huyo alitoa wito kwa watengenezaji, wasambazaji na waagizaji wa mifuko hiyo kujiandaa na zuio hilo na katika siku zijazo Serikali itatoa utaratibu na maelekezo ya tarehe ya kuanza zuio huku taratibu nyingine za kina zikifuata ili kuondoa mkanganyiko.

 Katika hatua nyingine, Makamba alisema maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Mazingira Duniani ambayo hufanyika Juni 5 kila mwaka hayatafanyika kitaifa badala yake wizara imewaelekeza wakuu wa mikoa kufanya maadhimisho katika maeneo yao.

 “Tumewapa miongozo kuhusu utekezezaji wa shughuli hizo za maadhimisho zinazolenga kutoa hamasa ya hifadhi ya mazingira hususan nyanzo ya maji amabayo ni muhimu kwa viumbe hai,” alisema Makamba.

Kwa mujibu wa Makamba, kauli mbiu ya mwaka huu kitaifa juu ya maadhimisho hayo ni ‘ tuhifadhi vyanzo vya maji kwa uhai wa taifa letu’aliwashauri na kuwataka Watanzania kutumia siku hiyo kupanda miti, kudhibiti uchomaji wa misitu 

Ofisa Mwandamizi Mazingira wa Nemc, Arnold Kisagala alisema nusu ya mifuko ya plastiki nchini inazalishwa na kuingizwa kutoka nchi jirani ya Kenya.

Alisema agizo la Waziri Makamba litawezekana, lakini linahitaji ushirikiano kutoka kwenye sekta zingine kwa kuwa viwanda vingi vya mifuko ya plastiki vipo Kenya.

"NEMC tayari tulishaanza mazungumzo na wazalishaji kuhusu mifuko ya plastiki,” alisema. 

Bunge Laahirishwa Baada ya Wabunge wa Upinzani Kumgomea Naibu Spika Kwa Kukataa Hoja ya Wanafunzi 7000 Waliofukuzwa UDOM

$
0
0

Naibu Spika wa Bunge ameahirisha Bunge kabla ya muda wake baada ya wabunge kutaka kujadiliwa suala la wanafunzi wa Udom kufukuzwa chuoni wakati hawana kosa.

Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari aliomba mwongozo na kutaka sakata la wanafunzi hao lijadiliwe lakini Naibu Spika, Tulia Ackson alisema jambo hilo haliwezi kusitisha shughuli za Bunge hivyo haliwezi kujadiliwa kwa wakati huo.

Kauli hiyo iliwanyanyua wabunge wa upinzani na baadhi ya wa CCM wakipinga kauli hiyo huku wakiwa wamesimama jambo ambalo lilisababisha kuaihirishwa kwa Bunge hadi saa 10:00 jioni huku akiagiza kukutana kwa kamati ya uongozi ya Bunge

Rais Magufuli amteua Mama Makinda kuwa Mwenyekiti Bodi ya NHIF, Jaji Lila kuwa jaji Mahakama ya Rufani

$
0
0

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Mhe. Jaji Shabani Ally Lila kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani.

Kabla ya uteuzi huo Mhe. Jaji Shabani Lila alikuwa Jaji Kiongozi. Uteuzi huu umeanza leo tarehe 30 Mei, 2016.

Wakati huo huo, Rais Dkt. Magufuli amemteua Mhe. Anne Semamba Makinda kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF). Uteuzi wa Mhe. Anne Semamba Makinda ambaye ni Spika Mstaafu wa Bunge Ia Jamhuri ya Muungano wa Tanzania umeanza tarehe 25 Mei, 2016.

Mhe. Anne Semamba Makinda anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Balozi Ali Mchumo. Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amemteua Prof. Apollinaria Elikana Pereka kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Teknolojia Dar es salaam (Dar es salaam Institute of Technology -DIT).

Prof. Apollinaria Elikana Pereka ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) Morogoro. Prof. Pereka anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Prof. Fredrick Mwanuzi ambaye amemaliza muda wake. Uteuzi huu umeanza leo tarehe 30 Mei, 2016.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Awasili Jijini Arusha

$
0
0

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe (kulia) na Mkuu wa mkoa wa Arusha, Felix  (katikati)  baada ya kuwasili kwenye uwanja wa ndege wa Arusha May 30, 2016 ambako May 31, 2016 anatarajiwa kufungua mkutano wa  Kimataifa wa ‘Africa  World Heritage’ kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha -AICC. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Mgambo Jela miaka 3 kwa kuomba na kupokea rushwa wilayani chato mkoani Geita

$
0
0

Mahakama ya Wilaya ya Chato Mkoani Geita imemtia hatiani Mgambo wa Mahakama ya mwanzo Buseresere Bw. Majaliwa Revelian Gwakilala kwa makosa ya kuomba na kupokea Rushwa kinyume na kifungu cha 15 (1 na 2) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.
 
Kwa Mujibu wa Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kesi dhidi ya Mtuhumiwa huyo ilifunguliwa mnamo tarehe 14/1/2016. 
 
Akisoma hukumu mbele ya mwendesha mashitaka wa TAKUKURU Augustino Mtaki, Hakimu Hakimu Mfawidhi wa Wilaya hiyo Mh. Mh. Jovith Kato alisema kuwa ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo na upande wa mwendesha Mashitaka umethibitisha pasipo shaka yoyote kuwa Mtuhumiwa alitenda kosa hilo. 
 
Ilisisitiza Sehemu ya Taarifa hiyo kuwa kwa mujibu wa ushahidi Mtuhumiwa aliomba kiasi cha Tshs. 300,000/= na kupokea kiasi cha Tshs. 100,000/- kutoka kwa Bw. Reuben Francis Ndimila ili asimkamate mtuhumiwa aliyeruka dhamana. 
 
Taarifa hiyo imeongeza kuwa Mahakama ilimtia hatiani Mtuhumiwa katika makosa hayo mawili ya kuomba na kupokea hongo. 
 
Aidha Mh. Kato akitoa adhabu kwa Mshitakiwa alisema, Mshitakiwa anatakiwa kutumikia kifungo cha miaka Mitatu (3) jela au kulipa faini ya Tshs. 600,000/= kwa kila kosa. Mshitakiwa amepelekwa jela kuanza kutumikia adhabu hizo kama zilivyotolewa. Kesi hiyo ilisajiliwa mahakamani hapo kama kesi ya Jinai Na. 18/2016 na kusikilizwa na Hakimu Mfawidhi wa Wilaya hiyo. 
 
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa GEITA Bw. Thobias Ndaro ametoa wito kwa wananchi wa Wilaya ya Chato kutoa taarifa mbalimbali za vitendo vya Rushwa na ubadhilifu katika miradi mbalimbali ya maendeleo na maeneo mengineyo ili watuhumiwa waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.

Kudai Ajira Kwawaponza Wahitimu Wa JKT

$
0
0

WAHITIMU sita wa mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), wamepandishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka matatu ikiwemo kufanya mkusanyiko usio halali na kushawishi wenzao kuandamana kwenda Ikulu kudai ajira, anaandika Faki Sosi.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni George Mgoba, mwenyekiti wao; Parali Kiwango, makamu mwenyekiti; Linus Steven, katibu  wa umoja wa wahitimu hao na wahitimu wengine, Emmanuel Mwasyembe, Ridhiwani Ngowi na Jacob Mang’wita.

Akiwasomea mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi, Respicius Mwijage, Wakili Mwandamizi wa Serikali, Benard Kongola amesema, washitakiwa hao wanadaiwa kwamba 15 Februari 2014 katika eneo la Msimbazi Centre, Ilala Dar es Salaam walipanga njama za kutenda makosa hayo.

Katika shitaka lingine watuhumiwa hao wanadaiwa kufanya mkusanyiko usio halali kwa lengo la kuandamana kwenda kwa Rais kulazimisha kupewa ajira katika utumishi wa umma, jambo ambalo ni kinyume cha sheria na kwamba, hatua hiyo ingesababisha uvunjifu wa amani.

Kwa upande wa mshitakiwa Mgoba, Kiwango na Steven, wanadaiwa siku hiyo katika eneo hilo, walishawishi wahitimu wenzao wa mafunzo ya JKT, kufanya maandamano kwenda kwa Rais kulazimisha wapewe ajira katika utumishi wa umma jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Washtakiwa hao wamepandishwa kizimbani ikiwa ni siku chache baada ya kesi dhidi yao kufutwa na kuachiwa Mei 26, mwaka huu kisha kukamatwa tena na leo kupandishwa mahakamani kwa mashtaka hayohayo.

Katika kesi ya awali iliyokuwa ikisikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi, Emilius Mchauru, tayari mashahidi saba walikuwa wameshatoa ushahidi mahakamani hapo huku akiwa amebakia shahidi mmoja tu ili kufunga ushahidi ndipo kesi hiyo ilipofutwa na watuhumiwa hao kukamatwa tena na kusomewa mashtaka hayo.

Watuhumiwa hao wamerudishwa rumande hadi kesi hiyo itakapotajwa tena Juni 9 Mwaka huu.

Breaking News: Bunge Lawasimamisha Wabunge 7 Kwa Kufanya Vurugu Bungeni

$
0
0

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge limepitisha azimio la  kuwasimamisha kuhudhuria vikao vya Bunge baadhi ya wabunge wa Kambi ya Upinzani waliohusika katika kufanya vitendo vya vurugu ndani ya ukumbi na kudharau Mamlaka ya Spika Januari, 27, 2016.

Wabunge waliosimamishwa kuhudhuria vikao hivyo ni Mhe.Kabwe Zubeiri Ruyangwa Kabwe, Mhe.John Heche, Mhe.Halima Mdee,Mhe.Tundu Lissu, Mhe.Halima Mdee, Mhe.Pauline Gekul  na Mhe. Ester Bulaya.
 
 Azimio la adhabu kwa wabunge hao limetolewa na Bunge chini ya Kifungu cha 30A (1) cha sheria ya Haki Kinga na Madaraka ya Bunge Sura ya 296 na kanuni ya 74 (4) na (6).

Akisoma adhabu hizo Mwenyekiti wa kamati hiyo yenye wajumbe 15 Mhe.George Huruma Mkuchika amesema kuwa uchunguzi uliofanywa na Kamati hiyo kwa kuwaita na kuwahoji wahusika ulibaini kuwa wabunge hao walitenda kosa kwa kukiuka kanuni zinazoliongoza bunge hilo.
 
 Imebainishwa kuwa Mhe.Zitto Kabwe alivunja masharti ya Kifungu cha 24(c), (d) na (e) cha Sheria ya Haki na Kinga na Madaraka ya Bunge Sura ya 296 na Kanuni ya 60(2) na (12) , 74(1) na (b) kwa kusimama na kuzungumza bila kufuata utaratibu na kudharau mamlaka ya Spika.

Kamati hiyo ilibaini kuwa Mhe.Godbless Lema, Mbunge wa Arusha alivunja Masharti ya kifungu cha 24 (c),(d) na (e) cha Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge Sura ya 296 pamoja na Kanuni ya 74(1) (a) na (b) ya kanun hiyo Kudharau Mamlaka ya Spika.

Kwa upande wa Mhe.John Heche alivunja kanuni ya 72 (1) na 68(10) ya kanuni za Bunge kwa kuendelea kusimama na kuomba mwongozo kwa jambo ambalo limekwishatolewa mwongozo na kuongeza kuwa vitendo hivyo vilivuruga shughuli za Bunge.

Kwa mujibu wa maelezo ya kamati hiyo Mhe.Halima Mdee, Mhe.Tundu Lissu,Mhe Pauline Gekul  na Mhe.Ester Bulaya walivunja masharti ya kifungu cha 24 (c), (d) na (e) cha sheria ya Haki,Kinga na Madaraka ya Bunge Sura ya 296 na Kanuni ya 72 (1)68 (10), 60(2) na 12 na 74(1) (a) na (b) kwa kusimama na kuendelea kuomba mwongozo kwa jambo ambalo limekwishatolewa uamuzi, kuzungumza bila kufuata utaratibu na kudharau Mamlaka ya Spika.

Kufuatia uchunguzi huo Bunge kupitia kamati hiyo limeazimia kuwa Mhe. Ester Bulaya na Mhe.Tundu Lisu wasihudhurie vikao vyote vya mkutano wa tatu wa Bunge la Kumi na Moja vilivyobaki kuanzia tarehe 30 Mei , 2016 pamoja na vikao vyote vya Mkutano wa Nne wa Bunge la Kumi na Moja kwa kuwa walipatikana na makosa ya ukiukwaji wa Kanuni na kuonyesha dharau kubwa kwa mamlaka ya Spika.

Aidha, Bunge limeazimia kuwa Mhe. Pauline Gekul, Mhe.Godbless Lema, Mhe.Zitto Kabwe na Mhe Halima Mdee wasihudhurie vikao vyote vya mkutano wa tatu wa Bunge kuanzia tarehe 30 Mei 2016.

Aidha  Bunge limeazimia Mhe.John Heche asihudhurie vikao kumi mfululizo vya Mkutano wa Tatu wa Bunge hilo kuanzia Mei, 30, 2016 kwa kuwa alipatikana na kosa moja na pia kwa kuwa alitoa ushirikiano kwa kamati kwa kufika na kujibu maswali yote kama alivyoulizwa pamoja na kuheshimu vikao vya kamati na Mwenyekiti aliyeongoza vikao hivyo.

Pamoja na adhabu hizo Kamati hiyo imetoa maoni na mapendekezo kuwa Bunge liandae mafunzo ya kutosha kwa wabunge wote kuhusu matumizi ya uzingatiaji sahihi wa kanuni sahihi wa kanuni za Kudumu za Bunge hasa kanuni za majadiliano ndani ya Bungeni.

Aidha, Kamati hiyo imesema kuwa ipo haja ya kutungwa kwa kanuni za maadili kwa wabunge wote kama kifungu cha 12 A Cha Sheria ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge kinavyoelekeza ili kuweza kudhibiti nidhamu kwa wabunge kwa kuhakikisha heshima na hadhi ya Bunge inadumishwa.

Kwa upande wao baadhi ya wabunge wakichangia kwa nyakati tofauti kuhusu suala hilo wamesema kuwa ipo haja ya Bunge kurudisha heshima yake kwa wabunge wote kuheshimiana na kutoa michango yenye staha kwa kuzingatia nafasi walizonazo katika jamii.

Wamesema kuwa michango wanayoitoa ndani ya Bunge hilo lazima ijikite katika masuala yanayowahusu wananchi wanaowawakilisha badala ya mambo yanayochochea vurugu na kulifanya Bunge lipoteze heshima yake katika jamii.

Aidha, wabunge hao wamekubali kwa kauli moja kuanza upya kuzingatia kanuni zinazoendesha vikao vya Bunge huku wakimtaka Spika wa Bunge au Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kutosita kuchukua hatua za haraka kwa mbunge yeyote atakayekiuka utaratibu na kanuni zilizowekwa.

Sakata la Lugumi Laizindua Serikali

$
0
0

SAKATA la Kampuni ya Lugumi limesababisha Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, kuagiza kupitiwa upya mikataba yote.
 
Kauli hiyo imetolewa leo na Hamad Masauni, Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi wakati akizungumza na waandishi wa habari pamoja na wakuu na waandamizi wa vyombo vya usalama vilivyopo chini ya wizara hiyo.

Kampuni ya Lugumi iliyoingia mkataba wa Sh 37 bilioni na Jeshi la Polisi kwa ajili ya kufunga mashine za kielektroniki za kuchukua alama za vidole nchi nzima, haikutimiza matakwa ya mkataba wake baada ya kufunga mashine 14 tu kati ya 108 ilizotakiwa kufunga licha ya kulipwa  asilimia 99 ya fedha kwa mujibu wa mkataba.

Masauni amesema, kutokana na kuwepo kwa utata wa mikataba, wizara imeagiza mikataba yote kupitiwa upya na ile ambayo itabainika kuwa na kasoro, itavunjwa.

“Mikataba yote ambayo majeshi haya yameingia ihakikiwe na ipitiwe upya ili iweze kurekebishwa na kazi hiyo iende haraka sana ili kuleta tija kwa wananchi wetu,” amesema Masauni.

Mbali na hilo ameiagiza Idara ya Uhamiaji nchini kuhakikisha inawachukulia hatua kali wale wote ambao wanaonekana kufanya kazi kinyume na misingi ya jeshi hilo.

“Kuanzia kesho naagiza kuhakikisha wanachukuliwa hatua wale wote ambao hawaendani na kasi yetu ya utendaji wa kazi na kuwaleta vijana vijana ambao wanaendana na kasi yetu ya hapa ni kazi tu.

“Kumekuwepo na shida kubwa katika maofisa wetu wa Idara ya Uhamiaji wanaohusika na mambo ya uchunguzi ambao wamekuwa wakienda katika baadhi ya makampuni kufanya uchunguzi kama kuna watu ambao ni wahamiaji haramu lakini hawafanyi kile ambacho wanatakiwa kukifanya.

“Changamoto kubwa ipo katika Jiji la Dar es Salaam na kwa maana hiyo nimeagiza watu hao waondolewe mara moja na hatua za kinidhamu na kisheria zichukuliwe haraka iwezekanavyo na (kesho) leo zoezi hilo liwe limekamilika” amesema Masauni.

Aidha ameiagiza Idara ya Uhamihaji kuhakikisha inaimarisha ulinzi mipakani ili kutibu tatizo la wahamihaji haramu wanaoingia kutoka nchi za jirani na kukamatiwa katika maeneo ambayo siyo ya mipakani.

Masauni amesema, licha ya kuwa kwa sasa nchi ipo shwari kalini jeshi la polisi linakazi kubwa ya kuhakikisha linaimarisha ulinzi, na kufanya upelelezi wa kina na kwa haraka pale yanapotokea mauaji au uharifu wa aina yoyote.

Kuhusu masuala ya ajira ndani ya wizara hiyo ambazo serikali ilitangaza kuzisitisha, Masauni amesema, kwa sasa baada ya wakuu wa idara zote viongozi waandamizi kukaa, wamekubaliana kurejesha ajira hizo katika Idara ya Uhamiaji na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.

“Kwa sasa idara ya uhamiaji ina nafasi za ajira 702 ambazo zinahitaji kujazwa huku Jeshi la Zima moto na uhokoaji zinahitaji ajira 522.

“Kutokana na hali hiyo na kwa kuzingatia kwamba idara hizo zilikuwa hazijakamilisha ajira hizo wakati wa kipindi cha mwaka wa fedha 2015/16 zilikuwa hazijajazwa na hivyo kama ajira zingeendelea kusitishwa vijana wengi wangekosa haki yao nab ado kuna upungufu.

“Vijana wenye sifa sasa wanaweza kuanza kujiandaa kwa ajili ya kufanya maombi pale ambapo nafasi hizo zitaanza kutangazwa katika vyombo vya habari” amesema Masauni.

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Jumanne ya May 31

Mbunge Amtaja Kikwete Sakata la EPA

$
0
0
Mbunge wa Konde Khatibu Said Haji (Cuf), jana aliibua sakata la Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) bungeni akimtaja Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete kwamba alikiuka Katiba kwa kutoa msamaha kwa watu waliotuhumiwa.

Hata hivyo, Serikali kupitia kwa Waziri wa Katiba na Sheria Dk Harrion Mwakyembe ilikanusha madai hayo na kusema Rais alikuwa sahihi kwa kuwa viko vifungu ambavyo vinampa nafasi hiyo.

Katika swali la nyongeza, mbunge huyo alihoji ni kwa nini Kikwete alitoa msamaha kwa watu hao kabla hawajahukumiwa na Mahakama kama Katiba inavyosema.

 “Kama hivyo ndivyo, basi naomba ukubali kuwa Kikwete (Rais mstaafu) alivunja Katiba ya nchi kwa kuwapa msamaha watuhumiwa wa EPA ambao walikuwa hawajahukumiwa bado, naomba majibu,” alihoji Haji.

Katika swali la msingi Mbunge huyo alitaka kujua iwapo Rais kwa mujibu wa Ibara ya 45 (1) A hadi D anayo mamlaka ya kutoa msamaha kwa watuhumiwa wa uhalifu wa aina yoyote ambao mashauri yake yapo katika vyombo vya dola kwenye hatua za uchunguzi/upelelezi au mahakamani.

Waziri alisema ibara hiyo ni kweli inampa mamlaka Rais ya kutoa msamaha kwa mtu yeyote aliyepatikana na hatia mbele ya Mahakama kupitia kifungu cha kwanza (1).

Dk Mwakyembe alisema kifungu (ii) kinampa Rais Mamlaka ya kumwachia kabisa au kwa muda maalumu mtu yeyote aliyehukumiwa kuadhibiwa kwa kosa lolote.

“Katika kifungu cha (iii) Rais anaweza kubadilisha adhabu yoyote aliyopewa mtu kwa kosa lolote iwe adhabu tahafifu na kifungu cha (iv) anaweza kufuta adhabu yoyote au sehemu ya adhabu,” alisema Dk Mwakyembe.

Alisema kwa kuzingatia masharti ya Katiba, msamaha wa Rais unatolewa kwa mtu aliyetiwa hatiani na kupewa adhabu na Mahakama lakini watuhimiwa wa uhalifu ambao mashauri yao yako hatua za upelelezi au uendeshaji mahakamani hawaguswi na masharti ya ibara hiyo.

Alisema Rais hawezi kutoa msamaha kwa watuhumiwa wa uhalifu wa aina yoyote ambao mashauri yao yapo katika vyombo vya dola kwani hatima ya watuhumiwa hao inakuwa bado ipo katika mamlaka za uchunguzi, mashtaka na Mahakama.

Symbion Yaionya TANESCO.....Yasema Maneno ya Kizushi na Ukiukwaji wa Mkataba Wanaoufanya Utaligharimu Taifa

$
0
0

Kampuni ya kufua umeme ya Symbion imesema maneno ya uzushi na ukiukwaji wa mikataba unaofanywa na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) utaligharimu Taifa na kulitaka shirika hilo kusema ukweli kuhusu makubaliano yao.

Kampuni hiyo pia imeeleza kuwa mwishoni mwa mwaka jana, kigogo mmoja wa Tanesco (ametajwa jina lakini tunalilisitiri jina lake kwa sababu hakupatikana jana) alisaini mkataba na Symbion wa kuliuzia umeme shirika hilo la umma kwa miaka 15.

Taarifa iliyoletwa jana kwa vyombo vya habari na mshauri wa Symbion, Julius Foster inaeleza kuwa taarifa zote zinazotolewa na Tanesco kuhusu uhusiano wao wa kimkataba ni za uongo na zimewashtua kwa kuwa shirika hilo la Serikali halijawahi kuieleza Symbion kuhusu tuhuma hizo.

“Kama itatokea suala hili likaleta mgogoro wa kitaifa, tunataka Tanesco na Serikali na yeyote yule kufafanua masuala haya kwa kiapo na mbele ya mahakimu na tutaujulisha umma kila kitu,” inasema taarifa hiyo.

“Zaidi ya barua ambayo walitaka kusitisha majadiliano na Symbion, hajawahi kujadili na sisi jambo lolote ambalo (kigogo huyo wa Tanesco), analizungumza sasa kwenye vyombo vya habari huko Tanzania.”

Hivi karibuni, iliripotiwa kuwa Tanesco imepanga kufungua kesi ili kusitisha mkataba na Symbion kutokana na wingi wa kesi dhidi ya kampuni hiyo ya Kimarekani.

Miongoni mwa kesi hizo ni ile iliyofunguliwa Mahakama ya Biashara na East African Cables dhidi ya Symbion Tanzania Ltd kutokana na deni la Sh6.372 bilioni. Tanesco ina hisa kwenye kampuni ya East African Cables.

Kadhalika, taarifa hizo zinaeleza kuwa Tanesco imeamua kusitisha mkataba huo kutokana na Symbion kudaiwa Sh6 bilioni na kampuni ya Oilcom, yakiwa ni malimbikizo ya malipo ya usambazaji wa mafuta kwa miaka mitatu.

Hivi karibuni, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alisema mikataba yote ya Tanesco na kampuni za kufua umeme si mizuri na haina manufaa yoyote kwa Taifa.

Akijibu swali bungeni, Profesa Muhongo alikiri kwamba deni la Tanesco ni kubwa na limesababishwa na uongozi dhaifu, rushwa, wizi na mikataba mibovu ambayo Tanesco imeingia. Alisisitiza kwamba hakuna mkataba unaolinufaisha Taifa.

Taarifa ya Symbion inaeleza kuwa wakati Tanesco inataka kusitisha mkataba huo, imeshindwa kulipa kiasi cha kati ya dola 25 milioni za Marekani na dola 80 milioni katika kipindi cha miaka mitano.

“Pamoja na deni hilo katika kipindi cha miaka mitano, hatukuwahi kuzima umeme, tukaendelea kuzalisha umeme na kujenga vituo vya dharura vya kufua umeme kwa kuwa kama si hivyo, Tanzania ingeingia gizani kwa sababu kiwango cha maji cha Mtera, Kihansi na Kidatu kilikuwa chini,” inasema taarifa hiyo.

“Kwa kuwa sasa mabwawa yamejaa ndiyo mnataka kuvunja mkataba?

“Tukifanya hivyo, wanaoathirika ni Watanzania. Tuna uhakika baadhi ya vigogo wa Tanesco hawaathiriki kwa sababu wana jenereta, ni wananchi ndiyo wanaoathirika.”

Taarifa hiyo inasema pamoja na kauli ambazo imeziita za uzushi zinazotolewa na shirika hilo, bado Symbion inasubiri majibu ya barua ambayo iliituma kwa Serikali wiki tatu zilizopita kuhusu mkataba huo.

14 Mbaroni kwa Tuhuma za Ujambazi

$
0
0
JESHI la Polisi mkoani Kilimanjaro linawashikilia watu 14 wakiwamo wanawake wawili na mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule ya sekondari Mwika wilayani Moshi, kwa tuhuma za ujambazi wa kutumia silaha.

Miongoni mwa watuhumiwa hao wapo wanaodaiwa kuwa majambazi sugu 10, waganga wa kienyeji wawili ambao walikuwa wakitumika kwa ajili ya kuwapa dawa watuhumiwa hao ili wasikamatwe na polisi na kuzindika silaha zilizokuwa zikitumika katika ujambazi na wanawake wapishi wa watuhumiwa hao wakiwa mafichoni.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Wilbrod Mtafungwa alisema jana kuwa watuhumiwa hao walikamatwa kwa nyakati tofauti katika mikoa ya Tanga na Kilimanjaro kufuatia msako mkali wa askari uliotokana na taarifa za siri.

Mtafungwa alisema mwanafunzi wa sekondari ya Mwika, Kelvin Shayo (17) miongoni mwa matukio anayotuhumiwa kushiriki ni pamoja na la kumpora bastola yenye namba YP0466 Tz Car aina ya brown, askari mstaafu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Elibariki Urio (67).

Kamanda alisema silaha hiyo iliporwa Februari 25 mwaka huu baada ya majambazi kumvamia nyumbani kwake na kupora mali pamoja na silaha hiyo kisha kwenda kuificha nyumbani kwa Eleutery Nguma (62) mkazi wa Makami Chini, Tarafa ya Vunjo ikiwa imefukiwa ardhini kwenye mfuko wa plastiki.

Aidha, Mtafungwa alisema kwa mujibu wa kumbukumbu za polisi mtuhumiwa huyo (Nguma) ilidhaniwa kuwa ameacha vitendo vya ujambazi lakini amebainika kuwa ni mpangaji wa njama za ujambazi, kuficha mali za wizi pamoja na kuficha silaha zinazotumika katika uhalifu.

China Wammwagia Sifa Rais Magufuli....Wasema Kaipaisha Tanzania Kimataifa

$
0
0
SERIKALI ya China imeiunga mkono serikali katika mkakati wake wa kutoa elimu bure, ikisisitiza kuwa chini ya uongozi wa Rais John Magufuli, Tanzania inasifika duniani.

Katika kuunga mkono elimu bure, ubalozi wa nchi hiyo nchini umetoa msaada wa madawati 400 yenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 28 kwa shule mbalimbali za msingi katika wilaya ya Iramba mkoani Singida.

Balozi wa China hapa nchini, Dk Lu Youq’ng alisema msaada huo ni moja ya juhudi za nchi yake kuiunga mkono Serikali ya Tanzania katika kutoa elimu bure. 

“Wakati mimi nimechangia madawati 300, Kampuni inayochimba madini hapa ya Sun Shine Group imechangia madawati 100 ili kuniunga mkono,” alifafanua.

Akikabidhi madawati hayo katika mikutano mitatu tofauti kwenye mji wa Kiomboi, Shelui na Misigiri, Balozi Youq’ng alisisitiza umuhimu wa Tanzania kuwekeza kwenye elimu kuwaletea wananchi wake maendeleo ya kweli.

“Hata kama nchi ni maskini kiasi gani, lazima elimu itiliwe mkazo; tena iwe ni elimu bora na elimu bora haiwezi kuja kwa wanafunzi kukaa chini. “Madawati ni moja ya mambo ambayo yanamjengea mwanafunzi mazingira mazuri ya kujifunzia,” alisema.

Aliongeza,“kutokana na umuhimu huo, ndio maana mbunge wenu aliponijia na kuniomba msaada wa madawati, sikusita hata kidogo. Nilijua anafanya hivyo ili kuisaidia jamii yake kuboresha elimu”. Aliyeomba msaada huo ni Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba.

Aidha, balozi huyo amewapongeza wakazi wa mkoa wa Singida kwa kumchagua Dk Magufuli kuwa Rais na kuongeza kusema kuwa chini ya uongozi wake sasa Tanzania inasifika duniani kote. “Nitahakikisha nchi yangu inaendelea kusaidia maendeleo ya nchi hii kwa kuwa urafiki wetu ni wa enzi na enzi,” alisema.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mathew Mtigumwe alisema kuwa mkoa unathamini msaada huo kwa kuwa umepunguza kwa kiasi kikubwa upungufu wa madawati 4,016 ambayo wilaya hiyo ilikuwa nao.

Diwani wa Mtibwa Ashikiliwa kwa Tuhuma za Ubakaji

$
0
0
Diwani wa Mtibwa wilayani Mvomero, Lucas Edward (38) maarufu Mwakambaya anashikiliwa na Polisi Mkoa wa Morogoro kwa tuhuma za kumbaka binti wa miaka 14, mkazi wa Turiani kwenye nyumba ya kulala wageni.

Kamanda wa Polisi mkoani Morogoro, Ulrich Matei alisema kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa Mei 29 saa 12 jioni kwenye nyumba hiyo iliyopo Mtaa wa Sultan, Manispaa ya Morogoro.

Matei alisema polisi walipata taarifa kutoka kwa msiri wao kwamba katika nyumba hiyo, kuna mtu ameonekana akiwa na binti mdogo, hivyo askari walifuatilia nyendo zake na kumkamata.

Alisema askari baada ya kufika kwenye nyumba hiyo, walimkuta mtuhumiwa huyo akiwa na binti huyo chumba namba 108.

Alisema uchunguzi wa kitabibu unaendelea kuthibitisha tuhuma hizo.

Akizungumza kwa simu, Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Wilaya ya Mvomero, Mrisho Ramadhan alithibitisha kukamatwa kwa diwani huyo na kwamba mpaka sasa hajafahamu ni kwa tuhuma gani.

Ramadhan alisema kwa sasa wao kama viongozi wa chama wanafuatilia kujua tuhuma na ameomba uongozi wa Chadema Mkoa kufuatilia zaidi na kwamba, atatoa taarifa baada ya kufahamu kwa undani.

“Ni kweli nimesikia mheshimiwa kakamatwa huko mjini Morogoro, sijajua kosa nimewaomba viongozi wa Mkoa Chadema kufuatilia nitatoa maelezo baadaye,” alisema Ramadhan.

Alisema baada ya kupata undani wa tukio hilo, atatoa taarifa ili kujulisha umma kilichotokea.

Mwalimu Atiwa Mbaroni Kwa Tuhuma za Kumkuwadia Mwanafunzi Wake

$
0
0

Mwalimu wa Shule ya Msingi Nyaigabo iliyopo Kijiji cha Musati wilayani Serengeti, Mkoa wa Mara anatuhumiwa kumkuwadia kijana anayemuuzia duka kwa kumpelekea mwanafunzi na kusababisha apate ujauzito.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Ramadhani Ng’hazi alisema mwalimu huyo, Agness Matiko amekamatwa na kuhojiwa kwa tuhuma hizo.

Ng’hanzi alisema binti huyo mwenye umri wa miaka 16 alimaliza darasa la saba mwaka jana kwenye shule anayofundisha mwalimu huyo.

Alisema mwalimu huyo alikuwa akimtoa darasani mwanafunzi na kumpeleka nyumbani kwake na kumkutanisha na kijana wake huyo kwa ajili ya kufanya naye ngono.

Binti huyo alikuwa anasoma kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Ikorongo kabla ya kufukuzwa baada ya kubainika kuwa na mimba ya miezi sita.

“Mwaka jana nikiwa darasa la saba mwalimu alinipeleka nyumbani kwake ili nikamsaidie kukamua ng’ombe maziwa, siku ya pili wakati wa mapumziko alinichukua nikamuoshee vyombo tulimkuta huyo kijana baadaye mwalimu alinisihi nibaki naye ndani,” alidai.

Alidai licha ya kukataa kufanya naye ngono, lakini mwalimu alimwambia: “Mimi ni mwalimu wako, kama lingekuwa jambo baya nisingekushauri, hivyo wewe kubali, akatufungia kwa nje. Huyo kijana akanipeleka chumbani kwake akanilaza kitandani na kuniingilia.”

Kwa mujibu wa mwanafunzi huyo baadaye mwalimu huyo alikwenda kufungua mlango na kumchukua na kumpeleka darasani na huo ukawa mwendelezo wa kumkutanisha na kijana huyo.

Alidai kila mara alimpeleka nyumbani kwake na kuwakutanisha huku akimwambia anataka waoane.

“Baada ya kubainika nina ujauzito walimtorosha huyo kijana na kudai kuwa walimfukuza kwa madai aliwatia hasara dukani,” alidai.

Akizungumza baada ya kupata dhamana, licha ya kukiri kukamatwa kwa tuhuma hizo, mwalimu Matiko alisema hajawahi kumfanyia ukuwadi mwanafunzi huyo.

Alisema kijana aliyekuwa akiishi kwake walimpata kijijini hapa akiwa anatafuta kazi. “Ndipo tulimpatia kazi ya kuuza duka tangu Aprili hadi Oktoba 2015 nilipomfukuza kwa kunisababishia hasara na alisema kwao ni Mabatini mkoani Mwanza,” alisema.

Baba wa binti huyo, Marwa Nchama (53) alisema baada ya kubaini ana mimba alifuatilia na kubaini mwanaye alikuwa akifanyiwa vitendo vya unyanyasaji na kijana huyo.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Turuka Samwel alikana kulifahamu tukio hilo likiwamo suala la walimu kuwafanyisha kazi wanafunzi majumbani mwao.

Mkuu wa Wilaya hiyo, Maftah Ally, alisema watumishi wanaohusishwa na tuhuma za kuwapa mimba wanafunzi licha ya kufikishwa mahakamani, watawachukulia hatua za kinidhamu.

Maalim Seif Kikaangoni LEO.....Polisi Wamtaka Aripoti Makao Makuu ya Polisi Kwa Ajili ya Kuhojiwa

$
0
0
Baada ya Jeshi la Polisi Zanzibar kuahirisha kumhoji Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, hatimaye hatua hiyo sasa imeelekea kutekelezwa.

Taarifa rasmi ya jeshi hilo visiwani Zanzibar, imemtaka Maalim Seif afike katika Ofisi za Makao Makuu ya Polisi, Ziwani mjini hapa leo saa 4.00 asubuhi.

Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Uhusiano kwa Umma wa CUF, Salim Bimani alithibitisha Maalim Seif kupokea barua hiyo jana wakati akiwa njiani kuelekea Dunga, Wilaya ya Kati Unguja, akiendelea na ziara yake katika majimbo ya Unguja.

“Ni kweli Maalim amepokea taarifa hiyo na ametakiwa afike Ziwani (mjini hapa) kesho (leo) saa nne asubuhi,” alisema Bimani 

Bimani aliongeza kuwa hatua hiyo ya sasa imekuja baada ya jeshi hilo kuahirisha hatua ya wito wa kumhoji Maalim Seif, Ijumaa iliyopita.

Barua hiyo ya kuahirisha iliyosainiwa  na Msangi kwa niaba ya Kamishna wa Polisi Zanzibar Mei 26, yenye kumbukumbu namba PHQ/ Z/C.5/4/4/TEMP/34 kwenda kwa Maalim Seif ilikuwa na kichwa cha habari ‘Kuahirisha mahojiano’.

“Tafadhali rejea barua yangu PHQ/Z/C.5/4/4/TEMP 26 ya tarehe 22/5/2016 ambapo tulikuita hapa Makao Makuu ya Polisi Zanzibar kwa mahojiano maalumu ya masuala mbalimbali yanayohusiana na Ulinzi na Usalama wa Visiwa hivi,” ilisomeka sehemu ya barua hiyo ya Msangi.

Kadhalika, barua hiyo ya kuahirisha mahojiano hayo ilisema:

“Tutakujulisha mapema siku ile iliyosainiwa na DCP Salum ya mahojiano itakayofuata mara baada ya kukamilisha taratibu.”

Msangi alithibitisha wito huo wa leo baada ya hatua ya awali, kumtaka kiongozi huyo awasili mbele yao kwa mahojiano kama ambavyo walimuahidi awali.

Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) Profesa Tunus Mgaya Aliyesimamishwa Kazi na Waziri wa Elimu Afunguka Mambo Mazito

$
0
0
ALIYEKUWA Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu (TCU), Profesa Tunus Mgaya amesema amesikitishwa na taarifa zilizoandikwa katika vyombo vya habari za kukosoa maamuzi ya serikali ya kuwasimamisha kazi kuwa hayakuzingatia sheria na kanuni zilizowekwa.

Mgaya ambaye hakuwa tayari kueleza kama taratibu za kusimamishwa kwao zilifuata utaratibu au la, amewataka waandishi wa habari kuwa na vyanzo vya uhakika katika habari zao.

“Mimi nikiwa miongoni mwa watendaji waliopumzishwa kazi, napenda kueleza kuwa sihusiki na taarifa hizo, suala hili limeshapita na kutolewa uamuzi na serikali na tuiache Tume iendelee kufanya kazi,” alisema Profesa Mgaya alipozungumza na waandishi wa habari jana mara baada ya kukabidhi ofisi.

Aidha, Profesa Mgaya aliweka wazi kuwa, anaunga mkono jitihada za Rais John Magufuli katika kuhakikisha kuwa watanzania wengi zaidi wanapata elimu ya msingi bure na kutolewa kwa elimu inayokidhi viwango stahiki kitaifa na kimataifa na kusema jambo hilo ni jema na linapaswa kuungwa mkono kwa nguvu zote.

Katika hatua nyingine, alimtaka Waziri wa Elimu, Sayansi,Teknolojia na Ufundi , Profesa Joyce Ndalichako kuendeleza jitihada za kuinua ubora wa elimu katika ngazi zote ili kuwa na taifa lenye watu walioelimika vizuri na lenye mchango mkubwa katika kuendeleza taifa.

Mke wa Trafiki Kinyogori Adaiwa Kukiri Kumuua Mumewe

$
0
0

MKE wa askari polisi wa kikosi cha usalama barabarani (trafiki), Sajenti Ally Salum (Kinyogori) aliyeuawa hivi karibuni, inadaiwa amekiri kuhusika kwenye mauaji hayo, akidai ilitokana na mumewe kumuacha na kuoa mke mwingine.

Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa mwanamke huyo anashikiliwa na polisi kwa mauaji hayo yaliyofanyika nyumbani kwa Kinyogori, Mkuranga mkoani Pwani.

Wakati huo huo, Kamanda Sirro amezungumzia pia mauaji ya Anathe Msuya yaliyofanyika hivi karibuni Kigamboni na kusema polisi inaendelea kumtafuta msichana wa kazi za nyumbani aliyetoroka siku moja kabla ya kifo cha mwanamke huyo.

Anayetuhumiwa kuua mumewe 
Akizungumza na waandishi wa habari jana kuhusu matukio mbalimbali ya uhalifu yaliyojitokeza jijini Dar es Salaam, Sirro alisema katika mahojiano ya awali mke wa Kinyogori amekiri kuhusika.

Kwa mujibu wa kamanda, mwanamke huyo ambaye hata hivyo hakutaja jina lake kwa sababu za kipelelezi, aliamua kumtuma mtu kutekeleza mauaji hayo baada ya mumewe kumwacha na kuoa mke mwingine.

“Ni jambo la kusikitisha kuona mtu anatoa uhai wa mtu sababu ya kuachwa. Tunawasihi wananchi kuepuka kujihusisha na matukio kama haya, eti sababu tu ya kuachwa wanawake wapo wengi na wanaume wapo wengi unaweza kuachwa na ukaolewa na ukaoa kuliko kuondoa uhai wa mtu,” alisisitiza Sirro.

Hata hivyo, Sirro alisema wanaendelea kuwahoji watuhumiwa hao ili waweze kuwataja watu wengine walioshirikiana nao kutekeleza tukio hilo baada ya kuonekana kuwepo kwa wahusika wengine.

‘Hausigeli’ asakwa 
Kuhusu mauaji ya Anathe aliyechinjwa nyumbani kwake Kibada, Kigamboni, Kamanda Sirro alisema wanaendelea na jitihada za kumtafuta msichana huyo ahojiwe kuhusu tukio hilo.

Aidha alisema mtu mmoja anashikiliwa akituhumiwa kuhusika na tukio hilo huku polisi ikiwa imeandaa timu ya upelelezi itakayoshughulikia tukio hilo kufanikisha kuwakamata wote waliohusika na tukio hilo.

Sirro alisema msichana huyo aliondoka siku moja kabla ya tukio hilo la mauaji hivyo kupatikana kwake, kunaweza kusaidia polisi kujua kama kuondoka kwake kulikuwa salama au kuna kitu kimejificha.

“Msichana huyu tunaendelea kumsaka tujue kama aliondoka salama na kumhoji zaidi juu ya kuondoka kwake siku moja tu, tukio linatokea nina imani tutafanikiwa kumpata na wote waliohusika na kukomesha matukio haya,” alisema Sirro.

Mamia wajitokeza msibani 
Vilio na simanzi jana vilitawala wakati mamia ya wakazi wa Kibada Kigamboni na Salasala walipokuwa wakiuaga mwili wa marehemu Anathe Msuya (30), aliyeuawa Mei 25 nyumbani kwake kwa kuchinjwa na watu wasiojulikana.

Mwili ulichukuliwa jana asubuhi kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili na kupelekwa nyumbani kwake Kibada, kwa ajili ya kuagwa na majirani zake kabla ya kusafirishwa kwenda kuzikwa mkoani Arusha leo.

Akizungumza baada ya mamia kumuaga nyumbani kwa marehemu, mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Nyakwale Kibada, Said Pazi alisema kuwa wao kama majirani waliomba familia wapate fursa ya kumuaga jirani yao ambaye tangu ahamie ana muda wa miezi sita.

“Baada ya kuambiwa msiba upo Salasala tuliomba kama majirani na sisi tupatiwe fursa ya kuuaga mwili wa ndugu yetu ambaye alihamia mwaka jana… kwa kweli msiba wake umetusikitisha sana” alisema.

Akizungumzia tukio hilo alisema kuwa mtoto wa marehemu huyo, Allan Kimario (4) aliwataarifu majirani kuwa mama yake haamki na ndipo walipofika wakakuta ameuawa.

Mwenyekiti huyo alitoa pole na kusema atahakikisha wanaimarisha ulinzi na kuhimiza wenye viwanja ambavyo havijajengwa, wavifanyie usafi ili kuondoa vichaka ambavyo ni hatari kwa usalama.

Viewing all 45270 articles
Browse latest View live




Latest Images

<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>
<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596344.js" async> </script>