Quantcast
Channel: MPEKUZI
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live

Rais Magufuli amteua Waziri Mkuu mstaafu Mizengo Pinda kuwa Mkuu wa Chuo Kikuu Huria (OUT)

$
0
0
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Waziri Mkuu Mstaafu Mheshimiwa Mizengo Peter Pinda kuwa Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT).

Mheshimiwa Mizengo Peter Pinda anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Balozi Dkt. Asha-Rose Mtengeti Migiro ambaye ameteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Uingereza.

Taarifa iliyotolewa leo tarehe 25 Mei, 2016 na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi imeeleza kuwa uteuzi wa Mheshimiwa Pinda unaanza mara moja.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam

25 Mei, 2016

Dk Shein Amuwakilisha Rais Magufuli nchini Comoro

$
0
0
Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein anaondoka leo jioni kwenda Muungano wa Visiwa vya Comoro kwa ziara ya siku mbili.

Akiwa nchini humo Dk Shein atamuwakilisha Rais Dk John Magufuli katika sherehe za kuapishwa kwa Rais mteule wa nchi hiyo, Azali Assoumani Boinakher.

Kuapishwa kwa Boinakher kunafuatia ushindi wake alioupata katika uchaguzi mkuu wa nchi hiyo uliofanyika tarehe 10 Aprili 2016 na ule wa marudio katika kisiwa cha Anjouan uliofanyika tarehe 11 Mei, 2016.

Sherehe hizo za kuapishwa Rais huyo mteule zitafanyika kesho katika kiwanja cha Mpira cha mjini Moroni na zinatarajiwa kuhudhuriwa  na viongozi mbalimbali kutoka nje ya nchi hiyo.

Katika ziara hiyo Dk Shein amefuatana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Bora , Issa Haji Ussi Gavu na Mshauri wa Rais Uhusiano wa Kimataifa, Uchumi na Uwekezaji Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa.

Rais Magufuli Avunja Bodi ya TCU kwa kupitisha Majina 489 ya Wanafunzi Wasio na sifa......Katibu Mtendaji wa TCU Naye Kasimamishwa Kazi

$
0
0

RAIS John Magufuli amevunja Kamisheni  ya Tume  ya Vyuo Vikuu (TCU) na kuwasimamisha kazi watendaji wakuu wa tume hiyo baada ya kubainika kudahili wanafunzi wasio na sifa na kuwapa mikopo.

Pia serikali imetangaza kufanyika kwa udahili upya Vyuo Vikuu vyote nchi nzima ili kuwaondoa vyuoni wanafunzi wote wasio na sifa sambamba na kutangaza vita kali kwa wanafunzi hewa wanaopata mikopo ya elimu ya juu.

Hayo yamebainishwa leo na Prof. Joyce Ndalichako Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia alipozungumza na waandishi wa habali juu ya kuvunjwa kwa Kamishina ya TCU.
 
Amesema, kwa idhini aliyopewa na rais anawasimamisha kazi mara moja watendaji hao wa Kamisheni ya Tume ya Vyuo Vikuu.
 
Prof. Ndalichako amewataja waliosimamishwa kazi kuwa ni Prof. Yunus Mgaya, Katibu Mtendaji wa TCU kwa kushindwa kusimamia kazi za TCU akiwa kama mtendaji mkuu wa taasisi hiyo.
 
Pia, Dk. Savius Maronga, Mkurugenzi wa Udhibiti na Ubora kwa kushindwa kutekeleza wajibu wake wa kusimamia ubora na ithibati ya Vyuo Vikuu.
 
Amesema Rose Kiishweko, Mkurugenzi wa Udahili amesimamishwa kwa kushindwa kusimamia udahili wa wanafunzi na kupelekea kudahiliwa wanafunzi wasio na sifa, na mwingine aliyesimamishwa ni Kimboka Istambuli  ambaye alikuwa Kaimu Mkurugenzi wa  Udahili na Nyaraka.
 
Mbali na hilo Prof. Ndalichako amesema, ili shughuli za TCU ziendelee, Prof. Eliuter Mwageni ameteuliwa kukaimu nafasi ya katibu mtendaji  na kabla ya uteuzi wa kukaimu nahfasi hiyo Prof. Mwageni alikuwa Naibu Makamu Mkuu (Utawala na Fedha) wa Chuo Kikuu cha Ardhi.
 
 Aidha ameteuliwa Dk. Kokubelwa Mollel ambaye atakaimu nafasi ya ukurugenzi wa udahili na nyaraka na kabla ya uteuzi  wa kukaimu nafasi hiyo Dk. Kokubelwa  alikuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
 
Amesema kwa muda mrefu kumekuwa na taarifa za wanafunzi wa Chuo Kikuu cha St. Joseph wanaodahiliwa kutokuwa na sifa.
 
Waziri amesema, kutokana na hilo serikali imeamua kutoa tamko baada ya ukaguzi kufanyika katika chuo hicho katika kampasi za Arusha na Songea na kubaini kuwepo kwa upungufu mkubwa katika utoaji wa elimu isiyokuwa na kiwango.
 
Amesema, walibaini kuwepo kwa wanafunzi 489 ambao wapo katika vyuo hivyo ambao hawakidhi viwango na hawana sifa za kusoma Chuo Kikuu.
 
Amesema kibaya zaidi ni kuwepo kwa wanafunzi ambao ni wa kidato cha nne waliofaulu Daraja la Nne huku wengine wakiwa na pointi 32 lakini wakidahiliwa kusomea shahada ya kwanza .
 
“Mwanafunzi wa Kidato cha Nne anasoma digrii ya Sayansi, huku mtu huyo akiwa sekondari kasoma mkondo wa biashara lakini kadahiliwa asomee Sayansi na analipiwa mkopo na TCU.
 
“Si tu hana sifa ya kusoma Chuo Kikuu, hana hata sifa ya kuwa na cheti cha ualimu kwa maana hiyo mtu wa aina hiyo  hafai hata kuwa na cheti cha ualimu hatuwezi kukubali mtu wa jinsi hiyo akasomee digrii,” amesema.
 
Prof. Ndalichako amesema rais amekuwa akihangaika kutafuta fedha kwa ajili ya mikopo ya elimu ya juu lakini cha kusikitisha kuna wanafunzi waliofaulu vizuri Kidato cha Sita wanakosa mikopo ila wale waliofeli wanapata mikopo hiyo.
 
“Divisheni four pointi 34 yuko Chuo Kikuu hata ualimu simkubali mtu wa namna hiyo,” amesema.
 
Amesema, baada ya serikali kufunga chuo hicho wanafunzi hao walihamishiwa vyuo vingine lakini hata huko walikopelekwa uwezo wao umeonekana kuwa ni mdogo hali iliyolazimu kuwarudisha madarasa ya nyuma.
 
‘Wanafunzi waliotoka St. Joseph na kupelekwa Chuo Kikuu cha Dodoma uwezo wao umeonekana kuwa ni mdogo, ambapo wanafunzi wa mwaka wa pili na wa kwanza wamerudishwa nyuma muhula moja huku wale wa mwaka wa tatu wamerudishwa nyuma mwaka moja” amesema.
 
 Amesema, wale wa St. Joseph Tawi la Songea waliopelekwa Chuo Kikuu cha Kilimo Morogoro (SUA) waliokuwa wakisoma mwaka wa nne wamerudishwa mwaka wa tatu na wametengewa vipindi vya ziada ili kurekebisha upungufu huo, na hata wale waliopelekwa vyuo vingine vya Ruaha, Mkwawa wameonekana kuwa na upungufu pia.
 
“Kibaya zaidi hao wanafunzi walikuwa wanapata mikopo, Division four anapata mkopo haki iko wapi, tulipoona jambo hili si sawa, tulichukua hatua tukaieleza bodi ya TCU kusimamisha kazi waliohusika lakini hilo halikufanyika,” amesema.
 
Kufuatia kuwepo kwa matatizo hayo Prof. Ndalichako ametangaza vita kwa vyuo mbalimbali ambavyo vina watu ambao wanadahili wanafunzi wasio na sifa.
 
Kuhusu wanafunzi ambao hawakuwa na sifa lakini walikuwa wakisoma chuo kikuu hicho amesema licha ya kuwa wamepoteza muda wao mwingi lakini watalazimika kurejesha mikopo hiyo.
 
“Wale wote ambao walipata mikopo bila kuwa na sifa watarejesha mikopo hiyo na hakuna njia yoyote ya kuwasaidia bali wanatakiwa kuendelea kuangalia ni jinsi gani ya kujiendeleza,” amesema.

Mbunge Riziki Mngwali Ataka Mjusi Wao Urejeshwe Lindi

$
0
0

Mbunge wa Viti Maalumu (CUF), Riziki Mngwali amehoji Bungeni kwa nini serikali isirudishe mjusi ambaye alichukuliwa mkoani Lindi miaka ya 1900's katika kijiji cha Tandeguru kata ya Mipingo mkoani Lindi na kupelekwa ujerumani ambapo amehifadhiwa.

''Mkoa wa Lindi unaongoza kuwa na rasilimali kubwa tumepiga kelele ya mjusi, mjusi yupo ujerumani wao wanafaidika na mjusi wetu wapanata dola bilioni 3 kila mwaka sisi hatupati kitu''-Amesema Mbunge Riziki.

Mbunge huyo amebainisha kwamba kama mabaki ya mjusi huyo yangerejeshwa kwa kuwa ni kivutio kwa ukubwa wake angeweza kuhifadhiwa kwenye makumbusho nakusaidia ujenzi wa barabara na shule.

Aidha Mbunge huyo amemtaka waziri wa maliasili na utalii aeleze kwa nini tozo inayopatikana huko ujerumani haiwafaidishi wananchi wa eneo husika.

Hata hivyo mjusi huyo mara kadhaa amekuwa akiuliziwa bungeni na serikali kuahidi kulifanyia kazi jambo hilo kwa manufaa ya wananchi.

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Alhamisi ya May 26

Silaa adai wafuasi wa Chadema walitishia kuchoma nyumba

$
0
0

ALIYEKUWA mgombea ubunge wa Ukonga, Jerry Silaa (CCM) amedai kuwa wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) walimtishia kuchoma moto nyumba yake wakati wa Uchaguzi Mkuu uliofanyika mwaka jana.

Silaa alieleza hayo jana katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, wakati akitoa ushahidi wa kesi ya kupinga matokeo yaliyompa ushindi mbunge wa jimbo hilo, Mwita Waitara (Chadema).

Alitoa ushahidi huo kwa njia ya kiapo baada ya Jaji Fatuma Msengi kutupilia mbali pingamizi la upande wa walalamikiwa waliokuwa wanapinga kupokewa kwa kiapo hicho kwa kuwa kina mapungufu kisheria.

Katika kiapo hicho, Silaa anaeleza kuwa, Oktoba 27 mwaka jana katika kituo cha kujumlishia kura cha Pugu Sekondari, kulikuwa na idadi kubwa ya wapiga kura wa Chadema wakiwa wamesimama mita 20 kutokea usawa wa kituo hicho.

Alidai kuwa wafuasi hao walianza kuwatishia Mawakala na Msimamizi wa Kituo, jambo lililosababisha Polisi washindwe kufanya kitu zaidi ya kuwaonya, ndipo mjibu maombi wa pili na wenzake wakasema hawatopokea matokeo na watachoma moto nyumba yake pamoja na kituo hicho.

Silaa ambaye aliwahi kuwa, Meya wa Manispaa ya Ilala, alidai hadi Oktoba 27, baadhi ya vituo vilikuwa havijakusanya matokeo jambo lililosababisha aandike barua kwenda kwa Msimamizi wa Kituo kuomba mchakato wa kuhesabu kura urudiwe.

Rais Magufuli Mgeni Rasmi Mkutano Wa CRB

$
0
0
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli atakuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa Mkutano wa mashauriano wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi Nchini (CRB) leo tarehe 26 Mei, 2016 katika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo wa mwaka wa mashauriano na wadau wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi unatarajiwa kuhudhuriwa na  zaidi ya Makandarasi na wadau wa Sekta ya Ujenzi wapatao 1000 na utafanyika kwa siku mbili kuanzia tarehe 26 Mei, 2016 hadi tarehe 27 Mei 20l6.

Kaulimbiu ya mwaka huu ni ‘Juhudi za Makusudi za Kukuza Uwezo wa Makandarasi Wazalendo kwa Maendeleo Endelevu ya Kiuchumi; Changamoto na Mustakabali Wake’.

Lengo la mkutano huu ni kuwakutanisha wadau wa Bodi ya Usajili Makandarasi na Sekta ya Ujenzi ili kujadili changamoto zinazowakabili na kuweka mikakati ya kuwajengea uwezo Makandarasi Wazalendo.

Imetolewa; 
Eng. Joseph M. Nyamhanga
Katibu Mkuu (Ujenzi)
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Wema Sepetu: Ipo Siku na Mimi Nitaitwa Mama

$
0
0

Msanii wa filamu nchini Wema Sepetu ambaye siku za karibuni ilisemekana alipata ujauzito na kisha baadaye ujauzito huo kuharibika amefunguka na kuonyesha bado hajakata tamaa na anaamini ipo siku na yeye atapata mtoto kama watu wengine wanavyopata

Kupitia Account yake ya Instagram Wema Sepetu alipost picha akiwa na mama yake mzazi na kuweka maneno yalisomeka kuwa 'iko siku na mimi nitaitwa Mama', jambo ambalo liliibua hisia za mashabiki zake na wengine kuanza kumfariji kuwa Mungu yupo na anasikia kilio chake na wengine wakiendelea kumtia moyo kuwa asijali kweli upo wakati na yeye atakuwa mama na kupata mtoto.

"Muombe Mungu Wema Sepetu hata sisi wanawake wenzako tunaumia sana kuona unatukanwa kisa mtoto, tunakuombea Mungu akujualie mtoto wako usisemezane nao hao watu wanakuongelea vibaya" Lovenes France
A photo posted by wemasepetu (@wemasepetu) on

CCM Waituhumu Chadema Arusha Kugawa Miradi Kwa Kupendelea Maeneo Waliyoshinda

$
0
0
CCM Mkoa wa Arusha, imeziomba halmashauri tano kati ya saba zinazoongozwa na Chadema, kugawa miradi ya maendeleo kwa usawa katika maeneo yao ili kuunga mkono msimamo wa Rais John Magufuli wa kuhudumia wananchi bila ubaguzi wa itikadi za vyama.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Michael Laizer alitoa kauli hiyo jana katika mkutano na viongozi wa chama hicho na Serikali katika kata za Lolksale na Lemoot wilayani Monduli, wakati wa ziara yake ya kuhamasisha utekelezaji wa ilani ya CCM na kukiimarisha chama hicho. 

Alisema katika halmashauri zinazoongozwa na upinzani alikopita amegundua kuwapo kwa utoaji wa miradi usio na uwiano, kwa kubagua baadhi ya kata zinazoongozwa na madiwani wa chama tawala, hali inayoweza kuzua malumbano.

Hata hivyo, Katibu wa Chadema Mkoa wa Arusha, Calist Lazaro alisema malalamiko hayo ya CCM hayana msingi kwa kuwa madiwani wa chama hicho katika halmashauri zote wanajua wajibu wao na hakuna upendeleo wowote.

Lazaro ambaye pia ni Meya wa Jiji la Arusha, alisema CCM haitengwi kwani haina uongozi katika kata nyingi. Alisema kati ya kata 24 CCM imeshinda moja, hivyo wanapoona kazi zinafanyika kwenye kata hizo wanadhani ni upendeleo.

Madai ya Laizer 
Mwenyekiti huyo wa CCM alisema viongozi wa Chadema wanaoendekeza siasa hadi sasa baada ya uchaguzi kumalizika, hawatendi haki kwa kuwa kuchagua au kuchaguliwa ni hiari ya kila mtu na kamwe mwananchi hapaswi kuhukumiwa kwa uamuzi aliofanya kidemokrasia.

“Kwa nini wao viongozi wa chini wanaendekeza ubaguzi wakati kiongozi mkuu wa nchi ambaye ni Rais anaendelea kusisitiza kutoa huduma kwa wananchi pasipo na ubaguzi?” alihoji na kuongeza:

“Kama Rais Magufuli angeamua kuzinyima fedha baadhi ya halmashauri zinazoongozwa na vyama vya upinzani, kungekuwa na madhara makubwa hivyo wapinzani wajirekebishe.”

Laizer aliwataka wananchi wa kata na halmashauri hizo zinazokabiliwa na matatizo hayo, kutokuwa wanyonge kwa kuwa wanaye baba ambaye ndiye Rais anayeonyesha hana ubaguzi na wala si muumini wa masuala ya vyama vya siasa, baada ya yeye kuchaguliwa kushika wadhifa huo.

Mwenyekiti huyo anaendelea na ziara wilayani Monduli ikiwa ni wilaya yake ya nne, baada ya kupita katika wilaya za Meru, Arumeru na Karatu kwa kazi hiyo ya uhamasishaji wa utekelezaji wa ilani ya chama chake.

Rufani ya Jamhuri Dhidi ya Bosi wa Zamani wa TRA na Wezake Kusikilzwa Jumanne ya Wiki Ijayo

$
0
0

Mahakama ya Rufani imepanga kusikiliza rufaa dhidi ya Mwenyekiti wa kampuni inayoshughulikia uwekezaji wa mitaji na dhamana (Egma), Harry Kitilya na wenzake, Shose Sinare na Sioi Solomon juma lijalo.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Mahakama ya Rufani, rufaa hiyo imepangwa kusikilizwa Jumanne Mei 31 na chini ya majaji watatu Bernard Luanda, Salum Masatti na Semistocles Kaijage.

Rufaa hiyo ilifunguliwa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), akipinga uamuzi wa Mahakama Kuu iliyotupa rufaa yake ya kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu kuwafutia washtakiwa hao shtaka la kutakatisha fedha.

Kitilya na wenzake walikuwa wakikabiliwa na mashtaka manane ya kughushi, kuwasilisha nyaraka za uongo kwa mamlaka za Serikali, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu na kutakatisha Dola za Marekani 6 milioni.

Hata hivyo, baadaye Mahakama ya Kisutu iliwafutia shtaka la kutakatisha fedha, baada ya mawakili wa washtakiwa hao kupinga uhalali wa shtaka hilo, uamuzi huo ulipingwa na DPP na kukata rufaa Mahakama Kuu akipinga uamuzi wa Mahakama ya Kisutu, lakini mawakili wa washtakiwa hao waliweka pingamizi wakidai kuwa uamuzi wa Mahakama ya Kisutu hauwezi kukatiwa rufaa kwa kuwa ni uamuzi mdogo ambao haumalizi kesi.

Mahakama Kuu katika uamuzi wake uliotolewa na Jaji Moses Mzuna, ilikubaliana na pingamizi la mawakili wa washtakiwa hao na ikaitupa rufaa hiyo na kuelekeza DPP arudi Mahakama Kisutu aombe kufanya marekebisho katika hati ya mashtaka ili kurekebisha shtaka la kutatakisha fedha lililofutwa.

DPP hakuridhishwa na uamuzi huo wa Mahakama Kuu ndipo akaamua kusonga mbele na kukata rufaa nyingine Mahakama ya Rufani.

Kitilya na wenzake wanadaiwa kutenda makosa hayo katika tarehe tofauti kati ya Machi 2013 na Septemba 2015 wakati wa mchakato wa mkopo wa Dola za Marekani 550 milioni kwa Serikali ya Tanzania kutoka Benki ya Standard ya Uingereza.

Katika hatua nyingine, Mahakama ya Rufani imefufua kesi ya uchaguzi dhidi ya Mbunge wa Mbarali mkoani Mbeya, Haroun Mullah iliyokuwa imetupwa na Mahakama Kuu na kuamuru isikilizwe upya.

Mahakama ya Rufani imeamuru kesi hiyo isikilizwe upya katika uamuzi wake wa rufaa iliyofunguliwa na aliyekuwa mpinzani wake wa karibu katika kinyang’anyiro Uchaguzi Mkuu 2015, Liberatus Laurent Mwang’ombe. 

Mwang’ombe alikata rufaa hiyo baada ya kesi yake ya msingi ya kupinga matokeo yaliyompa ushindi Mullah kutupwa na Mahakama Kuu, kutokana na kutokuwasilisha baadhi ya vielelezo vya ushahidi wa kesi yake.

Mahakama Kuu katika uamuzi wake uliotolewa na Jaji Atuganile Ngwale, ilisema kutokana na kutokuwapo vielelezo hivyo ambavyo ni fomu ya matokeo na kadi ya gari la mdaiwa (Mbunge Mullah) kunaifanya kesi hiyo kukosa msingi wa sababu za madai.

Hata hivyo, Mahakama ya Rufani ilisema kuwa Mahakama Kuu ilikosea kuitupa kesi hiyo, kwani ilikuwa bado katika hatua za awali na ilikuwa haijaanza kusikilizwa, hivyo mdai alikuwa na nafasi ya kuwasilisha vielelezo hivyo.

Hivyo, Mahakama ya Rufani katika uamuzi wake uliotolewa juzi na majaji watatu Engela Kileo, Katherine Oriyo na Semistocles Kaijage, iliamua kesi hiyo isikilizwe upya.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Asema Hakuna UGAIDI Jijini Humo.......Adai Mauji Msikitini ni Tukio ya Uhalifu wa Kawaida Kama Yalivyo Mengine

$
0
0
Wakati Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza likiwashikilia watu 14 kwa tuhuma za mauaji ya watu watatu katika Msikiti wa Rahman uliopo Ibanda, Kata ya Mkolani mjini Mwanza, Mkuu wa mkoa huo, John Mongella amesema mauaji hayo hayana sura ya ugaidi.

Mongella amesema mauaji hayo hayafanani na vitendo vya aina hiyo, hivyo ni vigumu kuyahusisha na ugaidi bali ni uhalifu kama ulivyo mwingine.

Bila kufafanua, alisema mauaji mengine yanasababishwa na ndugu na jamaa za marehemu. Kadhalika, aliwataka viongozi wa mtaa huo kuimarisha vikundi vya ulinzi shirikishi vitakavyoweza kukabiliana na uhalifu wa aina hiyo.

Mauaji hayo yalitokea Mei 18, saa mbili usiku wakati waumini hao wakiwa msikitini wanaswali.

Waliouawa katika tukio hilo ni Imamu wa msikiti huo, Feruz Ismail, Mbwana Rajabu na Khamis Mponda, wakazi wa Ibanda na kumjeruhi Ismail Ghati.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alisema watuhumiwa hao walikamatwa katika msako dhid ya wahalifu unaoendelea maeneo mbalimbali mkoani humo.

Hata hivyo, alisema bado hawajamkamata mtuhumiwa aliyempiga risasi Mwenyekiti wa Mtaa wa Bulale, Kata ya Buhongwa jirani na ya Mkolani. 

Mwenyekiti huyo Alphonce Nyinzi (48), alipigwa risasi Mei 22, saa moja usiku muda mfupi baada ya kumaliza kuongoza kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mtaa huo.

Kamanda Msangi aliwataka wananchi kutoa ushirikiano ili kuwabaini watu wanaoendeleza uhalifu katika mkoa huo.

“Nawaomba wananchi watupatie ushirikiano maana sisi wenyewe hatuwezi kufanya kazi bila ya kupata ushirikiano wao kwa sababu jamii yenyewe ndiyo inayoishi na watu hao, tuleteeni taarifa za uhalifu tutazifanyia kazi,” alisema.

Kwa kipindi cha wiki mbili mkoani Mwanza, watu 12 wameuawa kwa kukatwa mapanga na shoka, mmoja kwa kupigwa risasi na watu wasiofahamika.

Ester Bulaya Achafua Hali ya Hewa Bungeni Baada ya Kumfananisha Waziri Maghembe na TISHU

$
0
0

Mbunge wa Bunda Mjini (Chadema), Ester Bulaya jana alichafua hali ya hewa bungeni baada ya kusema kwamba Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe ni mzigo na mwepesi kama ‘tishu’ kwa sababu hana uwezo wa kusimamia mambo mazito yaliyopo katika wizara hiyo, kama vile migogoro ya wananchi na hifadhi za Taifa.

“Huyu waziri ni mzigo kama alivyowahi kusema (Abdulrahman) Kinana. Mimi nasema yeye ni mwepesi kama tishu, hawezi kuisaidia wizara hii nyeti,” alisema mbunge huyo jana wakati akichangia hotuba ya Wizara ya Maliasili na Utalii.

Hata hivyo, Waziri wa Nchi, Sera, Uratibu na Bunge, Jenista Mhagama alisimama na kuomba mwongozo wa mwenyekiti juu ya mbunge huyo kutumia maneno ya kuudhi ambao uliungwa mkono na Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge aliyemtaka Bulaya kufuta neno mwepesi kisha aendelee na hotuba yake. Hata hivyo, Bulaya alikataa kufuta neno hilo na kusema wabunge hawaamuliwi maneno ya kutumia.

Chenge aliendelea kumsihi mbunge huyo kufuta neno hilo na katika mabishano hayo yaliyodumu kwa dakika tatu, baadaye, Bulaya alikubali kuondoa neno ‘tishu’ na kuliacha neno mwepesi na kuruhusiwa kuendelea kuchangia.

“Mwenyekiti sitafuta neno mwepesi, kama neno ‘tishu’ linawakera basi naliondoa libaki mwepesi,” alisema Bulaya.

Katika mchango wake, Bulaya alisema wananchi wanaoishi katika hifadhi zilizopo jimboni mwake wananyanyaswa na askari wanyamapori wakati Serikali imeshindwa kuwatengenezea mazingira mazuri ya kuishi.

Alimtaka waziri huyo kushughulikia kero zote zinazowakabili wananchi wa Bunda akisema Serikali haiendeshwi kwa maneno matupu, bali vitendo na dhamira ya dhati ya kuwahudumia wananchi.

“Tatua matatizo jimboni kwangu ili niweze kukupima kama wewe ni mzito au mwepesi,” alisema mbunge huyo akimwambia Profesa Maghembe.

Baada ya Bulaya kumaliza muda wake, mbunge aliyefuatia alikuwa Abdallah Ulega wa Mkuranga (CCM) ambaye alisema kuna haja ya wabunge kupimwa kama wamelewa getini ili kujua akili zao.

“Kijana aliyefunzwa vizuri hawezi kumtukana mzee kama yule (Maghembe). Kama suala ni uwaziri basi aangalie hata umri wake kabla ya kuzungumza... Naungana na aliyesema wabunge tupimwe vilevi kabla hatujaingia humu ndani. Unaweza kujenga hoja yako bila kutukana, huhitaji kutukana ili waziri atekeleze madai yako,” alisema mbunge huyo.

Lowassa Ajisafisha Tuhuma za Kukwapua ardhi Ya Wananchi na Kujimilikisha

$
0
0

Siku chache  baada ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi kulieleza Bunge kuwa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa alijimilikisha shamba la Makuyuni Wilayani Monduli mkoani Arusha, Mbunge wa Monduli, Julius Kalanga amejitokeza kutoa ufafanuzi unaomsafisha.

Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Dodoma, Kalanga alisema kuwa Lowassa hamiliki shamba hilo la Makuyuni kwakuwa tangu Rais wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa alipofuta hati ya umiliki wa shamba hilo kutoka kwa raia wa Kigeni aliyemtaja kwa jina la Stein, bado halijamilikishwa rasmi kwa wananchi na ndio ilikuwa hoja yake.

Alisema kuwa maelezo ya Lukuvi hayakuwa na ukweli  na kwamba alichanganya kati ya shamba hilo la Mkuyuni na shamba la Manyara Ranchi ambalo hati yake ilifutwa tangu mwaka 2000 na kukagawiwa kwa wananchi wa Monduli ambapo Lowassa alisaini hati miliki yake kama muwakilishi wa wananchi wa Wilaya hiyo kwakuwa wakati huo alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya udhamini ya Ardhi (Tanzania Land Trustee (TLCT).

“Jambo la kushangaza ni pale Waziri alipochanganya shamba hilo na lile la Manyara Ranchi ambalo hati yake ilifutwa tangu mwaka 2000 na kugawiwa kwa wananchi. Hati miliki ya shamba hilo la Manyara Ranchi ilisainiwa na Lowassa ambaye wakati huo alikuwa mwenyekiti wa Bodi ya Tanzania Land Trustee(TLCT),” alisema

Awali, Waziri Lukuvi alieleza kuwa Shamba hilo la Mkuyuni linapaswa kumilikishwa kwa wananchi lakini nyaraka zinaonesha kuwa hati yake imesainiwa na Lowassa na kwamba Serikali itamnyang’anya na kulirejesha kwa wananchi.

Juzi, Lowassa aliahidi kuwasiliana na Mbunge huyo ili kufuatilia kauli aliyoitoa Waziri Lukuvi dhidi yake kuhusu kujimilikisha shamba hilo ili aweze kutoa ufafanuzi kwani hakuna ardhi anayoimiliki kinyume cha taratibu.

Waziri Mkuu: Vita Dhidi ya Rushwa Si Nguvu ya Soda

$
0
0

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema vita inayoendeshwa na Serikali ya awamu ya tano dhidi ya wala rushwa na wale wanaofanya ufisadi siyo nguvu ya soda kama wengi wanavyofikiri.

“Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kupambana na wala rushwa na mafisadi. Wala hatutanii. Hawa tutacheza nao na wala wasidhani vita hii ni nguvu ya soda. Tutaendelea kuwasaka hadi tufike mwisho,” alisema Waziri Mkuu wakati akizungumza na Watanzania waishio Zambia katika mkutano uliofanyika kwenye Ubalozi wa Tanzania jijini Lusaka, Zambia juzi jioni (Jumanne, Mei 24, 2016).

“Hatutaki tabia iliyokuwepo ya mwananchi anakuja ofisini kutaka huduma lakini hasikilizwi hadi atoe chochote, sisi hiyo tabia hatutaki kuisikia kabisa. Tumedhamiria kurudisha heshima kwenye utumishi wa umma na nimeanza kupata faraja kwani sasa hivi (nimeambiwa) katika baadhi ya taasisi unasikia mtu akiulizwa una shida gani, nenda pale, jambo ambalo zamani halikuwepo,” alisema.

Alisema Serikali imeamua kupigia debe dhana ya utumishi wenye uadilifu kwa sababu huo ni utamaduni mpya. “Ni kipindi kigumu kidogo cha mabadiliko lakini tumesimamia mabadiliko haya na ndiyo maana watumishi wote tumewasisitizia kuwa suala la uaminifu, uadilifu na uwajibikaji ni muhimu,” alisema na kuongeza:

“Hatutamvumilia mtumishi yeyote ambaye hatakuwa tayari kuwatumikia Watanzania au atakayeendekeza uzembe lakini pia hatutamuonea mtu yeyote. Hapa tunasisitiza usawa na hatutaki kutengeneza gap kati ya mwananchi mtumishi na wa mwananchi wa kawaida, tunataka kila mwananchi aione Tanzania ni nchi yake na kila kinachozalishwa ni sehemu yake. Tukifika hapo, tunaamini kila mmoja ataweza kuisemea nchi yake.”

Akizungumzia kuhusu ubadhirifu wa fedha za umma, Waziri Mkuu alionya kwamba Serikali imelipa kipaumbele suala la uaminifu na uadilifu kwenye fedha za Serikali na kwamba haitakuwa tayari kuona fedha hizo zikifujwa.

“Hivi sasa Serikali imetenga fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya maendeleo na fedha hizo zitaenda vijijini. Tunataka zikafanye kazi iliyokusudiwa, na wale wadokozi wajue kuwa wamekalia kaa la moto,” alisema huku akishangiliwa.

Alisema watumishi wa umma wana wajibu wa kusimamia kazi zilizopangwa na kuhakikisha miradi iliyolengwa inakamilika. “Kama fedha zimeletwa kujenga zahanati simamia zahanati ijengwe na ni lazima zahanati hiyo ionekane,” alisema.

Alisema bajeti ya mwaka huu imeongezeka kutoka sh. trilioni 21 hadi trilioni 29 lengo kuu likiwa ni kuleta maendeleo kwa wananchi. “Ndiyo maana tumepandisha bajeti ya maendeleo kutoka asilimia 27 hadi asilimia 40. Ole wake atakayepokea fedha hizi halafu zisifanye kazi yake, ukiipoteza wewe utafute njia ya kwenda,” alisema huku akishangiliwa.

Akifafanua zaidi, Waziri Mkuu alisema vita inayoendeshwa imelenga kuifanya Tanzania ibadilike na itoke kwenye uchumi wa chini na kuingia uchumi wa kati. “Swali la msingi ni je tunafikaje hapo? Jibu ni kupitia uzalishaji wa bidhaa viwandani,” alisema.

“Nyote ni  mashahidi wa jinsi ambavyo shilingi yetu imekuwa ikishuka thamani kulinganisha na dola ya Marekani. Tulitoka sh. 1,600/-, tukapanda hadi sh. 1,900/- na sasa tumefikia sh. 2,180/-. Hii ni kwa sababu tunaagiza zaidi bidhaa kutoka nje ya nchi badala ya kuzalisha, hatuwezi kuendelea hivi na ndiyo maana tumeamua kuwa nchi ya viwanda. Leteni mitaji nyumbani muwekeze,” alisisitiza.

Akijibu swali kuhusu Serikali kutafuta njia ya kutoa mikopo kwa Watanzania waishio nje ya nchi, Waziri Mkuu alisema mkopo ni mkataba kati ya taasisi ya kifedha na mkopaji kwa hiyo Serikali haiwezi kubeba dhamana hiyo. “Benki wanataka ijue taarifa zako mkopaji, wanataka wajua dhamana zako ni zipi, wajiridhishe na shughuli unazofanya. Je panakopesheka hapo?,” alihoji.

Hata hivyo, aliwaeleza kwamba wakitaka kuwekeza nyumbani wanaweza kupata mikopo kutoka benki ya maendeleo ya kilimo (TADB), Benki ya Rasilmali (TIB Corporate na TIB Development). “Hizi benki ni za wakulima na wajasiriamali, na zina masharti yake, kwa hiyo ni lazima wakakague eneo lako au mahali unapofanyia biashara au wakague leseni yako na ukweli wa maombi uliyopelekea. Sasa ukiwa Zambia watawezaje kukukopesha? Kwa hiyo ukitaka fedha uwe nyumbani,” alisema.

Akijibu swali ni vipi Serikali itawasaidia wanadiaspora kupiga kura kwenye uchaguzi mkuu wakiwa nje ya nchi, Waziri Mkuu alisema Serikali haijawahi kujaribu jambo hilo licha ya kuwa ilikwishapokea mapendekezo kadhaa kutoka nchi mbalimbali lakini kwa vile wameliuliza, yeye analibeba na kwenda kulifanyia kazi.

Bajeti Ya Wizara Ya Maliasili Na Utalii Yapitishwa, Usafirishaji Wa Wanyama Hai Nje Ya Tanzania Wapigwa Marufuku Kwa Miaka 3.

$
0
0
Na. Aron Msigwa – MAELEZO.
Serikali imesimamisha utoaji wa vibali na uuzaji wa wanyama hai kutoka katika hifadhi za Taifa kwenda nje ya Tanzania kwa kipindi cha miaka 3 mpaka hapo itakapotangazwa tena.

Waziri wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe ametoa agizo hilo bungeni mjini Dodoma wakati akijibu hoja na michango mbalimbali ya wabunge iliyoelekezwa kwenye wizara hiyo wakati wa Majumuisho ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka 2016/2017 ambayo imetengewa kiasi cha  shilingi bilioni 135.7.

Prof. Maghembe ameiagiza Idara ya Wanyamapori ipange na kuweka utaratibu mpya utakaotumika kusimamia biashara hiyo pindi itakaporejeshwa tena baada ya kumalizika kwa muda wa zuio la Serikali la miaka 3 ikizingatia  mazingira ya uhifadhi wa wanyama hao.

USAFIRISHAJI WA WANYAMA HAI NJE YA NCHI.
Amesema kumekuwa na taarifa za baadhi ya watanzania wasio waaminifu ambao wamekua wakijihusisha na vitendo vya kusafirisha wanyama hai waliokatazwa kinyume cha utaratibu jambo ambalo limeisababishia Serikali ipoteze mapato kutokana na wanyama hao.

Kuhusu wanyama wanaoruhusiwa kusafirishwa kama nyani, Kenge,ndege, kobe, wadudu na tumbili amesema kuwa wamekuwa wakisafirishwa  kinyume na utaratibu na baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu kwa ajili ya kutumiwa na makampuni ya kimataifa kwenye shughuli za utafiti wa kisayansi wa tiba na chanjo.

Amesema makampuni hayo yamekuwa yakinufaika binafsi kwa kupata fedha nyingi pindi yanapofanikiwa kupata chanjo au tiba husika huku maeneo waliokotoka yakipata fedha kidogo jambo ambalo serikali ya awamu ya tano imeamua kulifanyia kazi.

 UTALII KUSINI MWA TANZANIA NA MAENEO MENGINE.
Amesema Serikali itatekeleza miradi mbalimbali ya uboreshaji wa Utalii wa Kusini ili kuweka mazingira wezeshi na kuondoa vikwazo vilivyokuwa vikisababisha watalii kushindwa kufika katika maeneo ya hifadhi za Taifa eneo la ukanda wa kusini  mwa Tanzania.

 Baadhi ya maeneo yatakayoshughulikiwa ni gharama ya usafiri wa ndege  kwenda na kurudi katika maeneo hayo kuwa kubwa hadi kufikia Dola za kimarekani 1800 jambo ambalo limekuwa kikwazo kwa watalii hao.

Amesema Serikali itaanzisha vituo vya kuwekea mafuta ya ndege mahali vilipo vivutio vya utalii ili kuziwezesha ndege ndogo kufika kwa urahisi na kupata huduma ya kuongeza mafuta ili kupunguza gharama kwa wasafiri wanaotembelea hifadhi za eneo hilo.

Aidha amesema katika mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali itanunua  ndege ndogo abiria ili kuwezeha watalii kufika kwa urahisi katika maeneo ya hifadhiza Taifa.

UTAMBUZI WA MAENEO MAPYA YA UTALII.
Serikali kwa kushirikiana na Wakuu wa wilaya, mikoa na Wabunge itaanzisha mpango mpya kuviorodhesha vivutio vyote vya utalii vilivyo katika maeneo yao ili viweze kutangazwa ipasavyo na kuongeza kuwa mara baada ya kukamilika kwa mpango huo itaandaliwa orodha ya vivutio hivyo ili vianzwe kutangazwa rasmi.

Katika kuimarisha shughuli za utalii nchini serikali itaweka mkazo katika uimarishaji wa utalii wa utamaduni, uimarishaji wa maeneo ya historia na Malikale ili kuwezesha eneo hilo kuchangia zaidi katika pato la taifa.

ULINZI NA USALAMA WA HIFADHI ZA TAIFA.
 Prof. Maghembe ameeleza kuwa suala la ulinzi na usalama wa hifadhi zote za Taifa liko kwa mujibu wa sheria na kubainisha kuwa serikali imeanzisha Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania(TAWA) litakalochukua mbuga zote zilizokuwa na uongozi ambazo ziko nje ya TANAPA.

 Jeshi hilo litapambana kikamilifu na ujangili, kuimarisha maadili na nidhamu ya askari wa ulinzi wa hifadhi za taifa pamoja na kushughulikia maslahi yao na kuondoa migogoro kati ya askari na wananchi.

Amesisitiza kuwa mara baada ya Bunge la Bajeti, Wizara itakutana na wahifadhi wakuu wote ili kuweka vigezo vya kuzingatia katika majukumu yao na kusisitiza kuwa wahifadhi wote watakaoshindwa kwenda na kasi ya vigezo vilivyowekwa hawatajumuishwa kwenye jeshi hilo.

Aidha, amekemea vikali vitendo vinavyofanywa na baadhi ya askari wa hifadhi kupiga raia na kuchoma nyumba za wananchi kuwa havikubaliki na ni kinyume cha majukumu yao.

” Nimesikiliza kwa makini michango ya wabunge na nimesikia wafanyakazi katika hifadhi zetu wanapiga raia wanaua mifugo na kuchoma nyumba za wananchi jambo ambalo halikubaliki, hatukuwatuma kufanya hivyo” Amesisitiza Prof.Maghembe.

MIGOGORO YA MIPAKA MAENEO YA HIFADHI.
Serikali imesema mpaka sasa kuna migogoro ya ardhi 281, kati ya hiyo 35 ambayo ni sawa na asilimia 12.5 ni migogoro ya hifadhi na kuita  Mikoa yenye migogoro hiyo kuwa ni pamoja na Mara , Tanga na Kagera inachukua jumla ya asilimia 50.

Aidha, amesema kuwa mkoa wa Tabora unaongoza kwa kuwa na eneo kubwa la ardhi na unaongoza kwa kuwa na migogoro mingi ya hifadhi kwa asilimia 40.

Katika kuishughulikia migogoro hiyo Serikali imeziagiza wizara za Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Maji na Umwagiliaji, TAMISEMI, Nishati na Madini, Ofisi ya Makamu wa Rais – Mazingira pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii kushirikiana pamoja katika kutatua migogoro yote ya ardhi nchini.

UBORESHAJI WA MAENEO YA HIFADHI NA MAMLAKA ZA UHIFADHI.
 Amesema katika mwaka wa fedha wa 2016/2017 kiasi cha shilingi bilioni 1 kimetengwa kushughulikia usafi wa mazingira na ujenzi wa vyoo vya kisasa  katika hifadhi ya mlima Kilimanjaro vitakavyokuwa na uwezo wa kugeuza maji taka kuwa poda ili kuweka mazingira yote ya mlima huo kuwa safi.

Aidha,amesema kuwa Mamlaka za hifadhi za Taifa zimeendelea kuchangia katika maendeleo ya wananchi katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo ujenzi wa madarasa, miundombinu ya barabara, utoaji wa madawati katika halmashauri mbalimbali nchini.

TAMISEMI yaziagiza Halmashauri zote kukamilisha agizo la Rais Magufuli Ifikapo Mwezi Juni.

$
0
0

Na Daudi Manongi- MAELEZO
HALMASHAURI za Miji na Wilaya nchini zimekumbushwa kukamilisha zoezi la upatikanaji wa madawati kwa shule za msingi na sekondari ifikapo juni 30 mwaka huu ili kutekeleza agizo lililotolewa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli.

Rai hiyo imetolewa  leo  na Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano Serikalini katika Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Rebecca Kwandu wakati wa mahojiano na mwandishi wa habari hizi kuhusu uchakavu wa madarasa na ukosefu wa madawati unaozikabili shule za kinesi A na B zilizopo wilaya ya Rorya mkoani Mara.

“Suala la upungufu wa madawati na uchakavu wa madarasa ni changamoto ya kitaifa na kwamba lilishatolewa agizo na mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli kuhusu halmashauri zote nchini kuhakikisha ifikapo Juni 30 mwaka huu kila mwanafunzi anaketi kwenye Dawati” Alisema  Kwandu.

Kwa mujibu wa Gwandu alisema Serikali ya awamu ya tano imepania kuinua kiwango na ubora wa elimu nchini kupitia mikakati na sera ya elimu bure nchini kote.

Aliongeza kuwa hatua hiyo imeibua changamoto kubwa kwa wanafunzi wengi kujitokeza kwa asilimia kubwa na hivyo ni wajibu wa halmshauri hizo kukidhi mahitaji ya madawati ili wasome katika mazingira mazuri.

“Mpaka sasa Serikali imeendelea kutoa pesa kwa ajili ya elimu bure nchini kote na kumekuwepo kwa changamoto mbalimbali kama upungufu wa walimu,madawati na madarasa ambapo serikali inafanya jitihada za kila namna ili kutatua changamoto hiyo”

Akifafanua zaidi Gwandu alisema Serikali inaandaa harambee mbalimbali na kuongeza wigo wa utoaji wa vibali vya kuchangia maendeleo ya elimu kwa hiari ili kutoa  nafasi kwa wadau mbalimbali wenye nia ya kufanya.

Rais Magufuli Akemea Vitendo vya Rushwa kwa Wakandarasi Wazawa.. .....Awataka Watangulize Mbele Maslahi ya Taifa

$
0
0

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewataka wakandarasi kote nchini kufanya kazi kwa kutanguliza maslai ya taifa, badala ya kutaka kupata faida kubwa kupita kiasi kutoka kwenye zabuni za miradi ya ujenzi wanayopata kutoka serikalini.

Dkt. Magufuli amesema hayo leo tarehe 26 Mei, 2016 alipokuwa akifungua mkutano wa mashauriano wa bodi ya usajili wa wakandarasi kwa mwaka 2016 unaofanyika kwa siku mbili katika ukumbi wa Diamond Jubilee Jijini Dar es salaam.

Rais Magufuli amesema serikali yake ipo tayari kuwapa kipaumbele wakandarasi wa Tanzania pale inapotangaza zabuni za miradi ya ujenzi, lakini amewataka kujirekebisha kwa kupanga viwango vinavyostahili vya gharama za ujenzi wa miradi hiyo ambavyo serikali itaridhika.

“Nawatolea mfano, idara ya mahakama imetangaza kujenga mahakama za mwanzo na za wilaya, kwenye bajeti wana shilingi bilioni 24, makadirio ya kitaalamu yanaonesha kila jengo lisizidi shilingi milioni 200, wakandarasi wazalendo walipoomba katika nyaraka zao wametaka jengo moja lijengwwe kwa shilingi bilioni 1 na milioni 400, sasa nakuuliza Mheshimiwa Mwenyekiti na ndugu wakandarasi, hata kama una upendeleo, upendeleo huo utapasua moyo.

“Hata kama utakuwa na upendeleo kiasi gani kwa wazalendo utashindwa, sasa mimi niwaombe ndugu zangu wakandarasi, pamoja na nia nzuri ya serikali kuwasaidia wakandarasi wazalendo ni lazima na ninyi muwe na nia nzuri ya kuisadia nchi” Amesema Rais Magufuli

Pamoja na hilo, Rais Magufuli ametaka wakandarasi hao kuacha kutoa rushwa kwa watendaji wa serikali pale wanapoomba zabuni za ujenzi na badala yake amewataka kutoa taarifa kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (TAKUKURU) ili watendaji hao wakamatwe na kuchukuliwa hatua za kisheria.

“Mimi niwaombe wakandarasi, msikubali kutoa rushwa, na muwafichue watendaji wanaoomba rushwa, atakapokuomba wewe rushwa hujui amewaomba wangapi, na utakapotoa rushwa huna hakika kama ile tenda utaipata, wengine wameishia kutoa rushwa hapa, rushwa hapa, rushwa hapa mpaka anafilisika, kazi huipati na rushwa umeitoa” Amesisitiza Dkt. Magufuli.

Aidha, Rais Magufuli ametoa wito kwa wakandarasi hao kujipanga ipasavyo ili waweze kupata zabuni katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya ujenzi itakayofanywa hapa nchini ikiwemo ujenzi wa bomba la mafuta la kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga hapa Tanzania, Ujenzi wa Reli ya Kati na Ujenzi wa Viwanda.

“Sina uhakika kwamba mmejipangaje wakandarasi wa Tanzania katika kuhakikisha hiyo kazi mnaipata ya kujenga bomba kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga.

“Nitasikitika sana kilometa zote 1,410 pasiwepo mkandarasi hata mmoja wa kutoka Tanzania, wenzetu wanajipanga, na ninavyoona wakandarasi wa Tanzania wameendelea sana, lakini nashindwa kuelewa kuna tatizo gani linatufanya kutojua changamoto zinazotukabili, tumejipanga kujenga reli ya kati (Standard Gauge) kwenye bajeti ya mwaka huu tunaanza na kilometa 100, lakini kuna fedha nyingine zitatolewa na serikali ya China, tutajenga zaidi ya kilometa 1,200 (Standard Gauge, Central Corridor) itakayounganisha Mwanza, Kigoma, Burundi na Rwanda. Wakandarasi wa Tanzania mmejipangaje? " ameuliza Rais Magufuli.

Mkutano huo pia umehudhuriwa na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Kamishna Valentino Mlowola ambaye amesema Taasisi hiyo ipo tayari kukabiliana na rushwa iliyopo katika sekta ya ujenzi ambayo ni miongoni mwa sekta zenye rushwa kubwa na ametaka wakandarasi watoe ushirikiano kukomesha tatizo hilo.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam

26 Mei, 2016

Makandarasi 4572 Wafutiwa Leseni Nchini

$
0
0

Bodi ya Usajili wa Makandarasi imefuta usajili wa jumla ya makandarasi 4572 kwa kushindwa kutimiza matakwa ya Sheria ya Usajili wa Makandarasi ya mwaka 1997.

Hayo yamebainishwa na Kaimu Msajili wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), Bw. Rhoben Nkhori wakati wa Mkutano wa Mashauriano wa CRB uliofanyika jijini Dar es Salaam na kufunguliwa na Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Bw. Nkhori amesema kuwa katika jukumu la kuratibu mwenendo wa kazi za makandarasi, Bodi ilikagua miradi 2735. Katika miradi hiyo iliyokaguliwa, miradi 1873 sawa na asilimia 68.5 haikuwa na kasoro.

Ameongeza kuwa miradi mingine ilikuwa na kasoro za kutofanywa na makandarasi waliosajiliwa, kutozingatia usalama wa wafanyakazi, kutokuwa na bango wala uzio na miradi kutosajiliwa. Kwa mujibu wa Bw. Nkhori miradi yote iliyopatikana na upungufu wahusika walichukuliwa hatua mbali mbali kwa mujibu wa sheria.

Aidha, Bwana Nkhori amesema kuwa kwa mwaka jana, Bodi ilisajili miradi 3,172 yenye thamani ya shilingi trilioni4.23. Katika miradi hii asilimia 44.4 ilifanywa na Makandarasi wazawa na asilimia 55.6 ilifanywa na makandarasi wa kigeni.

Licha ya mafanikio hayo CRD ilikumbana changamoto kadhaa ikiwemo kuwasilisha nyaraka za kugushi wakati wa usajili hususani kadi za magari na mitambo, vyeti vya wataalam, kutumia majina ya makandarasi kwa udanganyifu kwa kuuza vibao, waendelezaji kutotoa taarifa sahihi za umiliki kwa Bodi na baadhi ya makandarasi kushindwa kuwalipa wafanyakazi na vifaa vya ujenzi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi, Bi Consolata Ngimbwa amemwomba Mhe. Rais John Pombe Magufuli kuwapa kipaumbele Makandarasi wa humu nchini ili kuwawezesha kiuchumi. “Mhe. Rais tunaomba utupe kipaumbele kwani sisi tukipata hiyo miradi tutawekeza hapa nchi na kuongeza soko la ajira,”alisema Bi Ngimbwa.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesema serikali yake itawapa kipaumbele makandarasi wazawa lakini akawataka wajipange na kufanya kazi kwa weledi na kuzingatia maadili ikiwemo kujiepusha na vitendo vya rushwa.

Mkutano huu pamoja na mamabo mengine utajadili jinsi ya kuwajengea uwezo makandarasi nchini. Kauli mbiu ya Mkutano huo ni “Juhudi za Makusudi za kukuza uwezo wa makandarasi wazawa, changamoto na mustakhabali.”

Mamia Wajitokeza Kumuaga Mwanahabari Makongoro Oging’ Kuzikwa Mkoani Mara Kesho Kutwa.

$
0
0
 Picha ya Mwanahabari Makongoro Oging’ enzi za uhai wake.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Global Publishers alikokuwa akifanyia kazi Makongoro Oging’, Eric Shigongo akitoa heshima za mwisho mbele ya jeneza lenye lenye mwili wa marehemu Oging’ wakati wa kuagwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ilala ya Amana Dar es Salaam mchana wa leo.
 Mmiliki wa Blog ya Michuzi, Issa Michuzi akitoa heshima za kwa mwili wa marehemu.
Mhariri wa Habari wa Gazeti la Champion, Salehe Ali akitoa heshima za mwisho kwa marehemu.
 Waombolezaji wakiwa na huzuni wakati wa kuaga mwili wa mpendwa wao Makongoro.
Mtangazaji wa Kituo cha Televisheni cha ITV. Samu Mahela akitoa heshima za mwisho.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri wa Habari Tanzania (TEF), Absalom Kibanda akiwa kwenye shughuli hiyo ya kumuaga Makongoro Oging’

Mrema Alaani Hatua ya Katibu Mkuu CUF Maalim Seif Kutangaza Kumwondoa Rais wa Zanzibar, Dr Shein Madarakani kabla ya 2020

$
0
0
Mwenyekiti wa Taifa wa chama cha Tanzania Labour Party  ( TLP), Augustino Mrema amelaani hatua ya Katibu Mkuu wa  CUF Maalim Seif kutangaza kumwondoa Rais wa  Zanzibar, Dr Shein  madarakani kabla ya 2020 huku akiwataka wazanzibar kutoyumbishwa na kauli za mwanasiasa huyo.

Mrema amezungumza hayo leo jijini Dar es salaam mbele ya waandishi wa habari na kusema kwamba amani ya Zanzibar ni muhimu kuliko maslahi binafsi hivyo ni vyema kuzitafakari kauli ambazo zinaweza kuleta machafuko.

Amesema hakuna mtu aliye  juu  ya sheria hivyo kuwepo kwa watu wanaochochea  vurugu  ni kama waahini pia ni  vyema  hatua zichukuliwe dhidi yao katika kuhakikisha  wananchi wanakuwa salama

Aidha Mrema amesema kwamba amani ya Zanzibar ikiharibika hata bara haiwezi kuwa salama hivyo ni vyema kauli za kuvuruga amani zizingatiwe ili kulinda maslahi ya wananchi wa pande zote mbili.

Amesema Zanzibar ina historia ya kuuawa watu mwaka 2001 kutokana na vurugu za kisiasa hivyo lazma  kwa  sasa suala la ki uchochezi liangaliwe kwa macho mawili dhidi ya watu wanaotaka kuvuruga amani katika mazingira hayo.

Mrema amesisitiza hakuna chama cha siasa ambacho  kinajengwa kwa kususia uchaguzi bali kwa kufanya hivyo ni  kuwanyima wapiga kura haki pia ni hatari na  kunaweza kusababisha chama kusambaratika kama kulivyotokea kwa baadhi ya vyama mfano, UPC cha Uganda na vinginevyo.

Pamoja na hayo mrema amefafanua kwamba mahakama ya ICC haingalii tu viongozi wa serikali bali hata viongozi wa kisiasa ambao wamesababisha mauaji kutokana na kauli wanazozitoa.

Pia mwenyekiti huyo wa TLP amewataka wahisani kutoingilia mambo ya ndani ya nchi kwani kusitisha misaada kwa hoja ya kufutwa uchaguzi wa Zanzibar na sheria ya mitandao ni kuingilia uhuru wa watanzania.
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live




Latest Images

<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>
<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596344.js" async> </script>