Quantcast
Channel: MPEKUZI
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live

Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Ijumaa ya May 27


Spika Job Ndugai (Mb) Afanya Mabadiliko Mengine ya baadhi ya Wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge.

$
0
0
Spika wa Bunge Mhe. Job Ndugai (Mb) amefanya mabadiliko mengine ya baadhi ya Wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge ili kuzingatia maombi ya baadhi ya Wabunge pamoja na mahitaji mapya yaliyojitokeza wakati wa utekelezaji wa shughuli za Kamati za Bunge.

Kwa mujibu wa taarifa yake, mabadiliko hayo yamefanywa kwa mujibu wa Kanuni ya 116(3) na (5) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Aprili 2016 ambapo yamehusisha maeneo manne ikiwemo; Kuhamishwa kwa baadhi ya wajumbe wa Kamati, Kualikwa kwa baadhi ya wajumbe katika Kamati ya Bajeti, Baadhi ya Wajumbe wa kamati ya Haki, Maadili, na Madaraka ya Bunge kuondolewa pamoja na Uteuzi wa wajumbe wapya katika kamati ya Haki, Maadili, na Madaraka ya Bunge.
 
Mabadiliko hayo ya wajumbe kwenye kamati yanaanza mara moja ambapo orodha ya wajumbe waliobadilishwa kamati na nafasi zao ni kama ifuatavyo; Wajumbe wanaohamishwa Kamati ni pamoja na Mhe. Ezekiel Magoyo Maige, (Mb) ambaye alikuwa katika Kamati ya Nishati na Madini na kwa sasa anahamia Kamati ya PAC, Mhe. Allan Joseph Kiula (Mb) ambaye alikuwa katika Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama na kwa sasa anahamia Kamati ya PAC, Mhe. Omary Tebweta Mgumba (Mb) ambaye alikuwa katika Kamati ya Sheria Ndigi na kwa sasa anahamia Kamati ya PAC, Mhe. Rhoda Rdward Kunchela (Mb) ambaye alikuwa katika Kamati ya Masuala ya UKIMWI na kwa sasa anahamia Kamati ya PAC.

Wengine ni Mhe. Joseph George Kakunda (Mb) ambaye alikuwa katika Kamati ya PIC na kwa sasa anahamia Kamati ya PAC, Mhe. Ahmed Ally Salum (Mb) ambaye alikuwa katika Kamati ya PAC na kwa sasa anahamia Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Mhe. Neema William Mgaya (Mb) ambaye alikuwa katika Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii na kwa sasa anahamia Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii pamoja na Mhe. Salma Mohamed Mwassa (Mb) ambaye alikuwa katika Kamati ya Bajeti na kwa sasa anahamia Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii.

Taarifa inaeleza kuwa, Wajumbe waalikwa katika Kamati ni pamoja na Mhe. Andrew John Chenge (Mb) ambaye yupo katika Kamati ya Sheria Ndogo, Mhe. Joseph Roman Selasini (Mb) ambaye yupo katika Kamati ya LAAC, Mhe. Dkt. Dalali Peter Kafumu (Mb) ambaye yupo katika Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira, Mhe. Japhet Ngalilonga Hasunga (Mb) ambaye yupo katika Kamati ya PAC, Mhe. Albert Obama Ntabaliba (Mb) ambaye yupo katika Kamati ya PIC pamoja na Mhe. Mussa Azzan Zungu (Mb) ambaye yupo katika Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii.

Aidha, Walioondolewa katika Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ni pamoja na Mhe. Dkt. Haji Hussein Mponda (Mb) pamoja na Mhe. Najma Murtaza Giga, (Mb).

Wanaoteuliwa kuwa Wajumbe wa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka Ya Bunge ni pamoja na Mhe. Asha Abdalla Juma (Mb). Mhe. Emmanuel Mwakasaka (Mb) pamoja na Mhe. Augustino Manyanda Masele (Mb).

Katibu Mkuu Kiongozi Afanya Ziara Hospitali Ya Rufaa Ya Mkoa Wa Kinondoni Mwananyamala Dar Es Salaam

$
0
0
SERIKALI imesema itaanza kutumia mbinu mpya kuwadhibiti madaktari na wauguzi wanaoiba dawa za serikali na kisha kuziuza kwenye maduka ya watu binafsi.

Tamko hilo lilitolewa jana na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Mhandisi John Kijazi alipoenda kukabidhi magodoro 50 katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Dar es Salaam Mwananyala yaliyotolewa na umoja wa makanisa ya Kipentekoste nchini.

Kijazi alisema mbinu hiyo itasaidia kuwabaini kiurahisi watumishi hao kwani itaendeshwa kwa siri ambapo kila kitengo katika wizara ya afya kutakuwa na mwakilishi atakayesaidia kutoa taarifa pindi atakapoona jambo hilo.

“Mimi niwatake wenye tamaa waache mara moja haiwezekani dawa serikali inunue kwaajili ya kuwapatia wananchi bure mtu mmoja kwa manufaa yake azipeleke kwa wafanyabiasha kuuza wananchi wakose dawa na kuanza kuhangaika”alisema Kijazi.

Pia amewataka wauguzi kuhakikisha kwamba malalamiko yanayotolewa na wananchi yanafanyiwa kazi mara moja na kuongeza serikali haitasita kumchukulia hatua mtu yeyote atakayebainika kumnyanyasa mgonjwa.

Alisema wagonjwa wamekuwa wakitoa malalamiko mengi juu ya huduma zinazotolewa katika hospitali ya Mwananyamala hivyo amewataka watendaji kubadilika ili kuepuka malalamiko yasiyo ya msingi.

Alisema ni lazima watoa huduma za afya wakazingatia nidhamu na weledi katika utendaji wa kazi kwani hawakulazimishwa kusomea taaluma hiyo na kuongeza kuwa fani zipo nyingi hivyo ambaye anaona hawezi kufanya yanayotakiwa aachie wengine.

Pamoja na hayo amezitaka hospitali zote kuanzisha dawati la malalamiko ili wanaohudumiwa wapate pakusemea pindi wanapofanyiwa vitendo vya unyanyasaji ikiwa ni pamoja na kucheleweshewa huduma au kuombwa fedha ili kuwahishiwa huduma ili hali ikiwa ni haki yao.

Hata hivyo ametaka madawati hayo kuwa wazi masaa 24 ili wananchi wapate muda mwingi wakujieleza na sio kusubiri kuelezea hisia zao pale wanapoona viongozi wakitembelea vituo hivyo.

Kijazi alitembelea wodi mbalimbali hospitalini hapo ikiwamo wodi ya wazazi, Wanaume, Watoto, Wanawake na watoto njiti ambapo alipata kujionea baadhi ya wagonjwa wakilala zaidi ya mmoja kwenye kitanda kimoja kutokana na kukosekana kwa vitanda.

Naye Mganga mkuu msaidizi katika hospitali hiyo Delila Moshi alieleza matatizo yanayoikabili hospitali hiyo kuwa ni pamoja na madeni ambapo inadaiwa stahiki za watumishi Sh. milioni 500 ambazo ni fedha za likizo kwa wafanyakazi, Sare za kazi, Nyumba na posho za masaa ya ziada.

Moshi alisema hospitali hiyo pia ina ukosefu wa vifaa vya kisasa kama CT Scan hali inayosababisha wagonjwa kupewa rufaa ya kwenda muhimbili kwaajili ya vipimo zaidi, Ukosefu wa chumba cha uangalizi wa wagonjwa mahututi (ICU) na Daktari bingwa wa mifupa na wagonjwa wa dharura.

Tatizo lingine ni wingi wa wagonjwa wa msamaha ambapo kwa kuanzia januari hadi desemba mwaka jana zaidi ya bilioni 2 zilitumika huku kwa mwezi wakitoa matibabu ya zaidi ya milioni 100 bure.

Sekondari Kongwe za Umma Kurejeshewa Makali Yake

$
0
0
Serikali imeeleza mkakati wa kuzirudisha shule 33 maarufu katika ubora wake ili ziweze kufanya vizuri kama ilivyokuwa zamani.

Mkakati huo ulielezwa jana na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako alipokuwa akiwasilisha hotuba ya bajeti yake bungeni. 

Alisema shule hizo zilipokuwa nzuri zikitoa elimu bora, zilizalisha vipaji vingi, akiwamo yeye aliyesoma katika mojawapo.Alisema katika awamu ya kwanza, shule 33 zitakarabatiwa.

Alizitaja shule hizo kuwa ni Ihungo, Ilboru, Kilakala, Mwenge, Msalato, Mzumbe, Ngaza, Pugu, Same, Tabora Boys na Tabora Girls.

Nyingine ni Azania, Jangwani, Kantalamba, Mpwapwa, Tosamaganga, Malangali, Milambo, Nangwa, Kibiti, Minaki, Ifakara, Songea Boys, Ndanda, Kigoma, Kibaha na shule za ufundi za Bwiru Boys, Ifunda, Iyunga, Moshi, Mtwara, Musoma na Tanga.

Rais Magufuli Atoa Mchango wa Milioni 10 Kusaidia Matibabu ya Mwafunzi Aliyepata Upofu

$
0
0
Rais John Magufuli ametoa mchango wa Sh. milioni 10 kwa ajili kusaidia matibabu ya mwanafunzi Bernadetha Msigwa aliyepata upofu hivi karibuni.

Msichana huyo anayesoma mwaka wa tatu katika Chuo Kikuu cha Mzumbe, ni miongoni wa wasichana ambao tatizo lake limeibuliwa kupitia kampeni ya Kipepeo, iliyoanzishwa na kampuni ya Clouds Media, Mei Mosi mwaka huu.

Kupitia matangazo yanayorushwa na kampuni hiyo, Rais Magufuli baada ya kusikia tatizo la Msigwa, ambaye pia picha yake imekuwa ikisambaa kwenye mitandao ya kijamii, akiwaomba Watanzania wamsaidie mchango wa fedha ili aweze kutibiwa. aliguswa na kuamua kutoa mchango huo.

Meneja wa kipindi cha 360 kinachorushwa kila siku za wiki asubuhi na televisheni ya Clouds, Hudson Kamoga alisema baada ya Rais kuona tangazo hilo, lililorushwa muda mfupi kabla ya kuanza uchambuzi wa magazeti, alimpigia simu.

“… Alisema ameguswa na stori ya Bernadetha, hivyo yeye na familia yake watachangia Sh10 milioni ili kumsadia,” alisema Kamoga.

Kamoga ambaye aliwahi kupigiwa simu na Rais Magufuli akiwa katika ya kipindi hicho na kuwasifu yeye na wenzake wanaokiendesha, alisema baada ya muda mfupi, Rais alimwagiza msaidizi wake apaleke mchango huo.

“Zilipita kama dakika 30 hivi au 45, akawa amemtuma mtu alete zile hela,” alisema Kamoga.
Mbali na Rais Magufuli, Kamoga alisema viongozi wengine walioguswa na tatizo la Msigwa ni Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi ambaye alikuwa mgeni kwenye kipindi cha 360 jana asubuhi, alichangia Sh2 milioni. 

Pia, Manaibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu), Anthony Mavunde Dk Abdallah Posi kila mmoja alichangia Sh1 milioni na Mkurugenzi wa Kampuni ya TSN, Farough Baghozah alichangia Sh3 milioni.

Kamoga alisema mwitikio wa Watanzania umekuwa mkubwa na hadi jana, michango iliyokuwa imetolewa ilikuwa zaidi ya Sh30 milioni anazohitaji Msigwa kwa ajili ya matibabu.

Kamoga alieleza kuwa msichana huyo alianza kupata maumivu makali ya kichwa mwaka huu na baada ya muda, alipoteza uwezo wa kuona.

“Hakuzaliwa kipofu. Amepata tatizo mwaka huu, wakiwa chuo mwaka wa tatu,” alisema Kamoga.

Alisema aliomba msaada kwao hivyo kupitia kampeni ya kipepeo, tatizo lake limefahamika na wengi na Watanzania wamemchangia ili aweze kutibiwa na kuona tena.

Dada wa Bilionea Msuya Auawa Kinyama Dar

$
0
0


Dada  wa marehemu Erasto Msuya aliyetambulika kwa jina la Anathe Msuya ambaye alikuwa ni Mtumishi wa Wizara ya Fedha, ameuawa kwa kuchinjwa na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia jana Dar es Salaam.

Anathe aliuawa nyumbani kwake eneo la Kibada block 16, Kigamboni, ambako inaelezwa wauaji hao hawakuchukua kitu chochote ndani ya nyumba yake.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro, alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo na kuahidi kutoa taarifa kamili leo.

Habari nyingine kutoka Wizara ya Fedha, ziliwakariri baadhi ya watumishi wakisema wamepata taarifa za msiba huo, lakini hawajapewa taarifa rasmi.

“Tuna taarifa tunazisikia sikia kuwa ameauawa, lakini jana (juzi) tulikuwa naye kazini ila leo (jana) ndiyo tunasikia amechinjwa na watu wasiojulikana. Imetusikitisha sana,” alisema mmoja wa watumishi hao ambaye hakutaja jina kwa kuwa si msemaji

Anathe ni dada wa marehemu Erasto Msuya ambaye alikuwa mfanyabiashara wa madini ya Tanzanite aliyeuawa kwa kufyatuliwa risasi.

Msuya aliuawa Julai 7, mwaka 2013 katika eneo la Mijohoroni,  kando ya barabara ya Arusha – Moshi wilayani Hai mkoani Kilimanjaro, akiwa ameitika wito wa kwenda kununua madini ya Tanzanite baada ya kupigiwa simu na vijana wawili  waliomtaka wakutane maeneo hayo.

Inaelezwa kuwa alifika katika eneo hilo akiwa na gari lake aina ya Range Rover T 800 CKF na kuwakuta vijana hao wakimsubiri.

Baada ya kuteremka,  Msuya aliekea kumsalimia mmoja wa vijana hao, hata hivyo kabla hajamfikia kijana huyo aliitoa bunduki ya SMG namba KJ 10520 aliyokuwa ameificha kwenye koti na kumfyatulia risasi takribani 22 mwilini.

Bilionea huyo aliyekuwa akimiliki vitega uchumi mbalimbali jijini Dar es Salaam na maeneo mengine nchini aliuawa saa 6:30 mchana.

Taarifa za polisi zilisema katika eneo la tukio ilikutwa  bastola  namba GLS 417T2 CAR 83271, mali ya Msuya na vitu vingine, ambavyo ni simu ya Samsung S5, iPhone na koti la mmoja wa watuhumiwa likiwa limetelekezwa mita chache kutoka eneo la tukio.

Polisi waliweza kuwakamata watuhumiwa wa mauaji hayo na kuwafikisha mahakamani mjini Moshi ambako kesi hiyo inaendelea kusikilizwa.

Nywele za Wema Sepetu kwa wiki hutumia Sh milioni 1.2

$
0
0

Miss Tanzania 2006, Wema Isaack Sepetu, ameweka wazi kwamba hutumia shilingi milioni 1.2 kwa ajili ya kutengeneza nywele zake kwa wiki moja.
 
Pia hutumia Sh 30,000 ya chakula kwa siku na kama atanunua na chakula cha mbwa wake huwa anatumia Sh 50,000 kwa siku.
 
Hata hivyo, Wema amesema si kila wakati hutumia kiasi hicho cha fedha, bali hutegemeana na aina ya nywele anazotengeneza.
 
Alifafanua zaidi kwamba gharama hizo pia zinatokana na kutumia ‘weaving original’ lakini wakati mwingine hutumia hadi laki moja na nusu kwa nywele za kawaida kama rasta.
 
“Huwa nabadilisha nywele kila baada ya wiki ambapo siku nyingine natumia milioni moja, siku nyingine laki saba au tano kwa sababu sipendi kukaa na nywele muda mrefu na nywele zangu ni ‘orijino’,” alisema.
 
Wema aliongeza kwamba anachopenda zaidi kwake ni kuwa na muonekano mzuri wa urembo kwa kuwa urembo upo kwenye damu yake.

Waziri Mbarawa Asema Wazee Hawatakiwi Tena katika Kampuni ya Simu ya TTCL

$
0
0

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amesema wakati umefika kwa wazee wanaofanya kazi katika Kampuni ya Simu ya TTCL, kuwaachia vijana kwa kuwa sekta ya mawasiliano hivi sasa ina ushindani mkubwa.

Akizindua nembo mpya ya kampuni hiyo na mtandao unaotumia teknolojia ya 4G LTE jana, Profesa Mbarawa alisema wazee wamekuwa watu wa kuzungumza zaidi ofisini, kuliko kufanya kazi na kubuni mbinu mpya zenye kuhimili ushindani.

Mbarawa alisema uzinduzi wa nembo mpya katika kampuni hiyo, hautakuwa na maana ikiwa wafanyakazi wa kampuni hiyo hawatabadilika na kutoa huduma zitakazowavutia wateja.

Aliishauri menejimenti kutoajiri watumishi kwa kujuana, bali watoe fursa kwa vijana wenye uwezo wa kuhimili ushindani unaotokana na mabadiliko ya teknolojia ya mawasiliano.

Aidha, aliwataka vijana kutumia fursa hiyo kwa kuchapa kazi ili TTCL yenye sura mpya ifike mbali kimaendeleo na kuwa kati ya kampuni bora zaidi za mawasiliano nchini.

Aliongeza kuwa serikali itaendelea kuchukua hatua thabiti za kuboresha na kuongeza kasi ya ukuaji wa sekta ya mawasiliano nchini na kusimamia vyema huduma za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) ili zisaidie katika jitihada za nchi kujiletea maendeleo.

Alisema sekta ya habari na mawasiliano inagusa shughuli nyingi za maisha yetu ya kila siku, kijamii, kiuchumi na kimaendeleo na kuongeza kuwa hivi sasa huduma hizi sio tena jambo la ziada katika maisha ya kila siku bali ni huduma za msingi zenye kipaumbele cha juu katika maisha.

Akizungumzia maombi ya wananchi ya kutaka kusogezwa mbele kwa siku ya kuzima simu feki, waziri alisema Serikali haitasogeza mbele siku hiyo.

“Siku ya Juni 16, mwezi ujao Serikali itazima simu na vifaa vingine vya mawasiliano feki bila kuongeza muda, huu ni muda wa watu kujiandaa,” alisema.

Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Bodi wa kampuni hiyo, Edwina Lupembe alisema TTCL wakati wowote kuanzia sasa itaanzisha huduma ya usafirishaji wa fedha kama zilivyo kampuni nyingine za mkononi.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Dk Kamugisha Kazaura alisema mabadiliko ya nembo hiyo yametokana na kampuni hiyo kuongeza huduma zinazotolewa kwa wateja.

Magufuli Kujaza Vijana Serikalini....Adai Wazee Ndo Wameihairibu Hii Nchi

$
0
0
Kuanzia sasa wateule wengi wa Rais John Magufuli serikalini watakuwa vijana kwa kuwa amegundua wengi hawapendi rushwa, amesema.

Aidha, Rais Magufuli amesema anafahamu kwamba vijana hawapendwi lakini amegundua ndio wachapakazi ambao watasaidia kulipeleka taifa katika maendeleo anayoyatamani.
 
Rais Magufuli alisema hayo jana wakati wa ufunguzi wa mkutano wa makandarasi wa mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya na Dodoma, jijini.
 
“Nimegundua vijana wengi hawapendi rushwa, hivyo nitaongeza vijana kila nikiteua kwa kuwa niliowaweka naona matunda ya kazi zao," alisema na kuongeza kuwa: “Najua watu wanawachukia sana ila nitawaongeza.
 
“Palipo na vijana nimeona mambo yanaenda na kuna mabadiliko. Wazee ndio tumelifikisha taifa hili hapa. Hakuna asiyejua kuwa Tanzania ilichakaa kila mahala.”
 
Tangu aingie Ikulu Novemba 5, mwaka jana, Rais Magufuli amejipambanua kama mwenye kupiga vita wizi, rushwa, ufisadi, ukwepaji kodi, uzembe na ukosefu wa maadili wa watumishi wa umma.
 
Aidha, Rais Magufuli alisema idadi ya watumishi hewa imefikia 10,292 huku vijana wengi wenye ujuzi wanamaliza vyuo vikuu na kukosa ajira. Alisema kama si tatizo la uwapo wa watumishi hewa, ajira zipo kwa wingi.
 
“Nataka vijana ili twende kwa kasi, ndiyo njia pekee ya kufikia maendeleo tunayoyatarajia,” alisemna. 
 
Rais pia alizungumzia uamuzi wake wa juzi wa kuvunja Bodi ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) na kutengua uteuzi wa aliyekuwa mwenyekiti wake, Profesa Awadhi Mawenya.
 
Rais Magufuli alisema zaidi ya Sh. bilioni 87 zililipa mikopo hewa kwa wanafunzi 480 wenye daraja la nne kidato cha nne, huku ikiaminika mikopo ni kwa ajili ya watoto wa masikini.
 
“Unashangaa anayesimamia kitengo ni Profesa. Hapa ndiko nchi ilikofikia,” alisema.
 
Rais Magufuli alitoa mfano mwingine wa Meli kubwa 65 za makontena zilizotia nanga katika Bandari ya Dar es Salaam bila kuandikwa, ambazo alisema “hazijulikani zilielekea wapi na hazikulipwa.”
 
Baada ya Rais Magufuli kumaliza hotuba yake, alimkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda (34) kuwasalimia wajumbe wa mkutano huo.
 
Makonda alisema alipokuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, aliunda kamati ndogo ya kufuatilia barabara na kubaini zaidi ya Sh. bilioni 2.2 zilitumika kujenga barabara ambazo mvua ikinyesha hazipitiki.
 
Alisema pia walibaini barabara zilizokuwa zikarabatiwe kwa Sh. milioni 200, zilitengewa Sh. bilioni moja kwa kila barabara na baadaye ziliombwa zaidi ya Sh. bilioni 5.9 na zilikuwa katika mchakato wa kulipwa lakini alizizuia.
 
“Manispaa ya Kinondoni ni tatizo kubwa...unakuta wananchi wanalia shida, wao wanalia kwa uongo kwa kuwa wanajua kuna fedha wanapata kama hizo.
 
“Nashukuru Mfuko wa Barabara umewanyima fedha na wameambiwa watengeneze barabara za awali hadi zikamilike kwa kutumia mapato yao ya ndani,” alisema.
 
Mbali na nafasi kadhaa za Wakuu wa Wilaya ambako habari za uhakika zinasema wengi watabadilishwa, Rais Magufuli pia ana nafasi ya uteuzi ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi, baada ya kuteungua uteuzi wa Charles Kitwanga kwa sababu ya ulevi, Ijumaa iliyopita.
 
Aidha, Rais Magufuli hajateua Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga tangu atengue uteuzi wa Anne Kilango Malecela kwa kutoa taarifa ya uongo kuwa mkoa wake haukuwa na watumishi hewa Aprili, mwaka huu.
 
Rais Magufuli pia hajafikisha jumla ya Wabunge 10 anaoruhusiwa kuwateua kwa mujibu wa katiba, hivyo kuweka uwezekano wa kuwapo kwa vijana wengi zaidi serikalini kwa mara ya kwanza katika miaka 55 ya Uhuru.

Rais Dkt Magufuli Akutana Na Kufanya Mazungumzo Na Rais Mstaafu Wa Awamu Ya Nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete

$
0
0
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa pamoja na  Rais Mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Kikwete wakifurahia jambo mara baada ya kumaliza mazungumzo yao Ikulu jijini Dar es Salaam
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Rais Mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Kikwete Ikulu jijini Dar es Salaam
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Rais Mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Kikwete Ikulu jijini Dar es Salaam

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Akagua Mradi Wa Mabasi Ya Mwendokasi (DART) Jijini Dar Leo

$
0
0
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekagua utendaji kazi kwenye mabasi ya mwendokasi yanayotoa huduma katika Jiji la Dar es Salaam na kubaini changamoto kadhaa ambazo amesema zitarekebishwa kadri mradi unavyoendelea.

Waziri Mkuu ambaye alilipa nauli na kupanda basi namba 23 lenye usajili namba T125 DGW kuanzia kituo cha Ferry, Kivukoni, ametumia muda wa dakika 50 kufika Kimara mwisho kwa kutumia usafiri huo.

Waziri Mkuu alipanda basi hilo saa 3:30 asubuhi na lilianza safari saa 3:33 baada ya kusubiri wengine wapande. Kwa wastani ililtumia kati ya dakika mbili hadi tatu kutoka kituo kimoja hadi kingine. Basi hilo liliwasili Kimara Mwisho saa 4:23 asubuhi.

Akizungumza na waandishi wa habari akiwa Kimara mwisho mara baada ya kumaliza ziara hiyo fupi ya ukaguzi leo (Ijumaa, Mei 27, 2016), Waziri Mkuu alisema aliamua kufanya ziara hiyo ya ghafla ili kuangalia matumizi ya njia za mabasi yakoje na pia kuona abiria wanaelewa vizuri namna ya kuitumia huduma hiyo.

Amesema ameridhishwa na mradi unavyofanya kazi ila ameelezwa kuna usumbufu kwenye mageti wakati abiria wanapotaka kuthibitisha tiketi zao hasa wakati wa asubuhi kunapokuwa na msongamano wa abiria. Pia alielezwa kwamba kuna baadhi ya abiria wanakuja na tiketi za jana yake jambo ambalo linaleta usumbufu kwa sababu hazitambuliki kwenye mfumo wao.

“Nimeridhishwa na uharaka wa njia kwa sababu na mimi mwenyewe nimetumia dakika 50 kufika hapa ingawa kuna maeneo nimeona kuna haja ya kuwa na taa maalum za kuzuia magari (special sensors) wakati mabasi yakipita ili kuepusha ajali,” alisema.

Aliyataja maeneo hayo kuwa ni kwenye makutano ya barabara ya Morogoro na mtaa wa Samora, Morogoro na Jamhuri na makutano ya Morogoro na Kisutu.

Waziri Mkuu aliwataka Watanzania waende na tiketi rasmi badala ya kutumia tiketi za jana kwa sababu kufanya hivyo ni makosa na  mtu anakuwa amedhamiria. 


“Hawa watachukuliwa hatua za kinidhamu. Mtu akija na tiketi ya jana akamatwe na kupelekwa polisi, huyu atakuwa amedhamiria,” alisema Waziri Mkuu wakati akiongea na mhudumu mmoja katika kituo cha Kimara Mwisho.

“Ninawasihi wananchi wanaotumia usafiri huu wajifunze kufuata utaratibu na kuwasisitizia kuwa kila abiria aje na tiketi ambayo ni rasmi,” alisema na kuongeza: “Haya mabasi nimebaini yako vizuri. Ninatoa msukumo kwa watumishi wa umma wapande mabasi haya ili kupunguza msongamnao wa magari barabarani.”

Katika kupiunguza baadhi ya changamoto, Waziri Mkuu alisema Serikali itasimamia uboreshaji wa ukataji tiketi ili kuondoa usumbufu kwa abiria. Pia alivionya vyombo vya moto viache kutumia njia maalum ya mabasi hayo.

Pia aliwataka polisi wanaofanya doria za usiku kupita kwenye fly-overs na kuwaondoa watu wanaolala kwenye maeneo kwani wanahatarisha usalama wa watu wanaotumia njia hizo. “Zile siyo sehemu za kulala, wanaofanya hivyo wanahatarisha usalama wa watumiaji wa njia hizo, kwa hiyo polisi wakiwakuta watu wa aina hiyo wawakamate mara moja,” alisema.

Kwa upande wake, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Mohammed Mpinga ambaye alifuatana na Waziri Mkuu kaktika ziara hiyo, alisema amepiga marufuku magari na pikipiki kutumia njia hiyo hata kama ni magari ya Serikali.

“Tulishapiga marufuku magari na pikipiki kutumia njia hiyo hata kama ni magari ya Serikali, ninawasihi madereva watambue hili na watii,” alisema.

Machi 22, mwaka huu Waziri Mkuu alitembelea soko la Feri kwa lengo la kuangalia mfumo wa majiko ya gesi sokoni hapo (kuzuia moshi) na kukagua ujenzi wa ukuta unaotenganisha soko hilo na mabasi yaendayo kasi.

Aprili 15, mwaka huu, Waziri Mkuu alifanya kikao na kuwaagiza wakuu wa taasisi zinazohusika na utekelezaji wa mradi huo kuhakikisha wanatoa elimu kwa umma ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza pindi majaribio yakianza.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Kassim Majaliwa akizungumza na mwanafunzi Amina Abdallah wa darasa la sita katika shule ya msingi ya Ukombozi jijini Dar es salaam ambaye amepanda basi la Mwendo Kasi Ajentina na kushuka Manzese, Katikati ni Bw. David Mwaibula aliyekuwa Mwenyekiti Mamlaka ya Usafiri wa Daladala Dar es salaam (DRTLA) zamani 
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Kassim Majaliwa akifurahia jambo wakati Mkurugenzi wa DART Bw. David Mgwasa akisamimiana na Bw. David Mwaibula aliyekuwa Mwenyekiti Mamlaka ya Usafiri wa Daladala Dar es salaam (DRTLA) zamani 

Juma Nkamia Adai Wapinzani Wanasura Mbaya Kiasi Kwamba Wanataka Kutapika na Wengine Meno Yao Yameoza!

$
0
0

Kanuni inayozuia lugha ya kuudhi bungeni ni kiinimacho kwani mbunge wa upinzani akitoa lugha inayokera, mbunge wa CCM ataomba mwongozo kwa Spika na mara akijibiwa atasimama mbunge wa CCM na kutumia lugha hiyo hiyo iliyoombewa mwongozo.

Jana Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia (CCM) aliporomosha lugha za kuudhi baada ya kuwaambia wabunge wa upinzani waliokuwa wakishangilia kuwa wanasura mbaya hadi wanatamani kutapika.

Akichangia hotuba ya makadirio na matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa mwaka 2016/17, Nkamia alionyesha kukerwa na hotuba ya upinzani kuhusu wizara hiyo kwenye sehemu iliyozungumzia uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka jana.

Nkamia alisema uchaguzi umepita na mshindi alipatikana ambaye ni CCM na aliufananisha uchaguzi na mpira kwamba unapoisha uwanjani mtu hawezi kulalamika nje.

“Uchaguzi umeisha, leo mtu anasimama hapa anasema ‘ooh tuliibiwa kura’ mlikuwa wapi wakati mnaibiwa kura?”alihoji na kuwataka wapinzani watafute sababu kwa nini walishindwa na si vinginevyo.

"Wanajua mchezaji mmoja akiumia katika timu unachukua mwingine kwenye timu ile ile lakini inakuwaje unachukua mchezaji kutoka upinzani? Kwa hiyo niwaombe tu muwe mnatafakari kwanza,” alisema.

Hali hiyo iliibua kelele na minong’ono kutoka kwa wapinzani, jambo ambalo lilimlazimu Naibu Spika, Dk Tulia Ackson kuwataka wabunge huku akiwataja majina watulie ili mbunge huyo amalizie mchango wake.

Nkamia aliendelea, “We nyosha midomo, fanya nini lakini that is the truth (huo ndiyo ukweli). Utaongea sana na utapiga kelele sana lakini ukweli ndio huo na umekuingia vizuri. 

"Mimi kelele wala hazinisumbui. Mimi nataka niwashauri kama wakati ujao mnataka kuwa chama kizuri anzeni kutafuta wachezaji wenu,” alisema.

“Nyie pigeni kelele lakini ukweli ndio huo, wenye akili wanajua na wapiga kelele wanajua na najua limewaingia vizuri sana.”

Kijembe hiki kiliwalenga Ukawa ambao katika uchaguzi mkuu uliopita walimteua aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowasa. Ukawa walimteua Lowasa baada ya kuitema na kuihama CCM ambapo alipambana na John Magufuli (CCM) aliyeshinda.

Nkamia akionekana kumlenga mbunge fulani ambaye hakumtaja jina alisema, “We piga kelele, kwanza meno yako yameoza.”

Kwa kuzingatia kanuni, lugha hiyo ni ya kuudhi lakini Dk Tulia asisitiza Nkamia amalizie kuchangia ambapo alitoa mfano wa mwandishi wa vitabu Bernard Taper aliyewahi kusema kwamba kuna watu wakiamka asubuhi wakijiangalia kwenye kioo wanatamani kutapika.

“Sasa nyie mnaoshangilia humu mna sura mbaya na mnatamani kutapika,” alisema Nkamia

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan Anaondoka Nchini Leo Kumwakilisha Rais Magufuli Mkutanoni Papua New Guinea

$
0
0
Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan anaondoka nchini leo kwenda Papua New Guinea ambako atamwakilisha Rais John Magufuli katika mkutano wa Wakuu wa nchi za Afrika,Caribbean na Pacific (ACP) ambao utafanyika kuanzia Mei 30 hadi Juni 01, mwaka huu.

Chumba Cha Dereva Tax Chazua Kizaa Zaa Mtaa Wa Mbezi Mtoni Gold Star, Jijini Dar Baada ya Kukutwa Kimejaa Makopo ya MIKOJO na KINYESI

$
0
0
Na Ripota wa Sufianimafoto ,Dar
UKIHADITHIWA na kuonyeshwa chumba cha Dereva Tax anayeonekana kitaani na katika kazi zake akiwa amepiga pamba wala hutaamini masikio yako wala macho yako pindi utakapopata bahati ya kufika na kushuhudia chumba hicho kilichopo maeneo ya Gold Star Mtaa wa Mbezi Mtoni Bondeni jijini Dar es Salaam.

Mwandishi wa habari hiialipata fursa ya kufika na kushuhudia yale yaliyokuwa yakisemwa na baadhi ya wakazi wa mtaa huo jana majira ya saa tano usiku baada ya kutokea mtafaruku na sintofahamu katika nyumba hiyo ya Mama Mwakajinga, anayoishi Dereva huyo aliyejulikana kwa jina la Steven al-maarufu kama ‘NYATI’.

Akizungumza na mwandishi kuhusu tukio hilo, Mama mwenye nyumba, alisema kuwa siku ya Mei 23, akiwa ameketi uwaji karibu kabisa na Chumba cha Jamaa huyo huku akichambua mboga, alihisi harufu kali na mbaya iliyokuwa ikivuma kutoka chumbani kwa Dereva huyo aliyepanga katika nyumba yake tangu mwaka 2008 na kuona wadudu aina ya funza wakitoka chumba hicho kupitia chini ya mlango.

Kesho yake Mei 24 baada ya kuona wadudu hao huku harufu ikizidi kuwa kali, alimuita jirani yake na kumshirikisha jambo hilo huku wote wakishikwa na butwaa na kuwa na mashaka na chumba hicho.

Mei 25 Mama mwenye nyumba aliamua kwenda kwa Mjumbe wa eneo hilo Badili Makoye, kutoa taarifa juu ya wasiwasi uliotanda katika nyumba hiyo na kuongozana na Viongozi wengine, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa huo, Frank Kyaruzi, Wajumbe wengine  Abdalla Mlaliya na Matrida Paston, waliofika na kujionea hali halisi ya chumba hicho.

Baada ya viongozi hao kufika eneo la tukio walimuamuru Mama mwenye nyumba kwenda kutoa taarifa kituo cha Polisi.  Mama huyo alitekeleza agizo na kwenda kuripoti Kituo cha Mbezi Garden na kuongozana na Mkuu wa Kituo hicho na baadhi ya askari hadi nyumbani na kukuta hali hiyo ya sintofahamu.

Walipofika eneo la tukio na kushuhudia hali hiyo, Mkuu wa Kituo aliamuru mlango huo uvunjwe huku wananchi na Viongozi wa Mtaa huo wakishuhudia na kuingia ndani ambako walikuta Chumba kizima kikiwa kimejaa Chupa za Plastiki zilizojaa mikojo, Mifuko ya Rambo ikiwa na Vinyesi, Feni moja iliyochomekwa kwenye Soketi ya Umeme ukutani, Pakiti nyingi tupu za Sigara aina ya Embassy na Kondomu zilizotumika na zisizotumika.

Baada ya zoezi hilo, Mwenyenyumba alimpigia simu mpangaji wake na kumtaka kurejea nyumbani, lakini Dereva huyo alijibu kuwa kwa muda huo alikuwa mbali maeneo ya Kunduchi na kuahidi kuwagongea usiku pindi atakaporejea.

Hadi Mwandishi anaondoka eneo la tukio majira ya saa tano usiku bado wakazi wa maeneo hayo walikuwa wamejazana nje ya Chumba hicho wakiendelea kumsubiri arudi ili kupata ukweli kuhusu mambo waliyoyaona katika chumba chake.

Aidha Mama mwenye nyumba alisema kuwa mpangaji wake huyo, tangu alipohamia katika nyumba hiyo mwaka 2008, hakuwahi kumuona akiingia na mwanamke katika chumba hicho, wala kumuona mgeni wa aina yeyote kwa Dereva huyo,jambo lililomshangaza kukuta Kondom zilizotumika katika chumba hicho. Ama kweli ukistaajabu ya Mussa utayaona ya Filaun.

Leo hii Mei 27, Mama mwenye nyumba ameripoti kuwa mpangaji wake huyo,hajatokea nyumbani hapo tangu kutokea kwa tukio hilo ambapo leo, amechukua uamuzi wakuwalipa vijana wa mtaa huo ili wasafishe chumba hicho.

"Tayari tumewalipa pesa vijana kiasi cha sh.200,000/= ili wafanya usafi na wameshamaliza na kwenda kufukia bonde la mto Mbezi." Amesema mama huyo
Wananchi na mwenye nyumba wakifungua mlango
Chupa zinazodaiwa kuwa na mikojo zikiwa zimetapakaa ndani ya chumba hicho.
Huyu Ndiye Dereva wa Tax Nyati anayedaiwa kumiliki chumba hicho.

Lowassa Akutana na Kufanya Mazungumzo na Balozi wa Japani Hapa Nchini

$
0
0
May 27 2016, aliyekuwa mgombea Urais mwaka jana kwa tiketi ya Chadema na Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Japan hapa nchini, Masahau Yoshida.

Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Lowassa ameandika; "Nimekutana na rafiki yetu Balozi wa Japan hapa nchini Masaharu Yoshida, nikiwa pamoja na viongozi wote wa wilaya yetu ya Monduli.

"Mbali ya kumshukuru Balozi Yoshida kwa misaada mbalimbali wanayoitoa ila zaidi tulijadiliana jinsi gani ya kufanya muendelezo na mikakati ya kuchukulia misaada hii kama nyezo za kufikia malengo ya maendeleo na sio njia ya utegemezi kiuchumi"-Lowassa

Kijana Anusurika Kifo Baada Ya Kupanda na Kujirusha Kutoka Kwenye Mnara Wa Simu Jijini Mwanza

$
0
0
Kijana Mmoja (pichani aliyeshikiliwa ) ambaye jina lake halikupatikana kwa haraka, mkazi wa Jijini Mwanza amenusurika kifo baada ya kujirusha kutoka katikati moja ya minara wa simu iliopo jijini humo, mchana wa leo.

Tukio hilo limetokea hii leo na kuvuta watu wengi waliofika kumshuhudia kijana huo ambae amepanda katika mnara huo tangu majira ya asubuhi na kukatalia mnarani hadi majira ya saa sita mchana.

Mashuhuda wa tukio hilo ambao pia ni marafiki wa karibu na kijana huyo, wamesema huenda kijana huyo amefikia maamuzi hayo kutokana na ugumu wa maisha ambao amekuwa akiulalamikia huku wengine wakisema ni kutokana na kuathiriwa na matumizi ya dawa za kulevya ikiwemo gundi ambayo amekuwa akiyatumia.

Akizungumza kwa niaba ya Kamanda wa Jeshi la Uokoaji na Zima Moto mkoani Mwanza, mmoja wa maafisa wa uokoaji Mussa Kaboni, ametoa rai kwa makampuni yenye minara ya simu kuimarisha ulinzi katika minara hiyo ili kuondoa hatari inayoweza kujitokeza kutoka kwa raia wasio wema.

Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo walionekana kuchukizwa na kitendo cha kijana huyo na kusikika wakifoka kwa hasira na makelele ya hali ya juu "rukaa, ruka sasa, jirushe kama wewe ni mwanaume" hali ambayo ilikuwa ikimuongezea morari kijana huyo na hivyo kujirusha kweli kutoka katikati ya mnara huo.

Baada ya kijana huyo kujirusha kutoka katikati ya mnara hadi chini, alipoteza fahamu na kukimbizwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Mwanza, Sekour Toure kwa ajili ya huduma ya kwanza. 

Fly Over 7 Kujengwa Jijini Dar es Salaam - Prof. Mbarawa

$
0
0
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano imeanza mazungumzo na Kampuni ya MABE BRIDGE ya Uingereza kwa ajili ya kujenga barabara za juu (fly over) saba katikati ya jiji la Dar es Salaam ili kupunguza msongamano wa magari.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, amesema mazungumzo kuhusu ujenzi huo yako katika hatua nzuri na kwa kuanzia zitajengwa fly over nne za watembea kwa miguu na tatu za magari.

Amesema Fly over hizo zitazojengwa zitatumia miezi mitatu hadi sita kukamilika kwakwe na zitagharamiwa na fedha za ndani za Serikali ambapo ujenzi wake unatarajiwa kuanza Desemba mwaka huu.

“Wataalamu wanaendelea kubaini maeneo yatakayojengwa fly over hizo ikiwemo eneo la Mwenge ambalo tayari wataalamu wamekubali kujenga fly over moja ya magari”, amesema Prof. Mbarawa.

Hatua hiyo ni mkakati wa Serikali kupunguza msongamano wa magari jijini Dar es Salaam unaogharimu fedha nyingi kutokana na watu kupoteza muda mwingi barabarani.

Katika hatua nyingine Waziri Prof. Mbarawa amekagua maendeleo ya utoaji huduma katika Daraja la Nyerere na kuagiza vitengenezwe vitambulisho vya msimu vitakavyowawezesha watumiaji wa daraja kulipa tozo kwa miezi sita au mwaka ili kupunguza msongamano wa kulipa kila siku.

“Hakikisheni mnatengeneza na kuuza kadi za kuvukia katika daraja sehemu mbalimbali ili kuwawezesha watumiaji kupata huduma hiyo kabla ya kufika darajani”, amesema Prof. Mbarawa.

Aidha amemtaka Mtendaji Mkuu wa Daraja la Nyerere Bw. Gerald Sondo kuhakikisha tozo zinakusanywa inavyostahili na kupanga njia maalumu za kupita magari makubwa na madogo ili kuwezesha huduma ya kupita darajani iwe ya haraka.

“Magari yote yanayopita katika daraja hili yakiwemo ya Serikali ni lazima yalipe tozo inayostahili isipokuwa yale yenye vibali maalumu yakiwemo ya Jeshi la Wananchi, Zimamoto, Polisi, na yanayobeba wagonjwa (Ambulance)”, amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.

Waziri Mbarawa amesisitiza umuhimu wa wananchi kutunza na kulilinda Daraja hilo ili lidumu kwa muda mrefu na kusisitiza adhabu kali kwa wataohujumu miundombinu yake.

Naye Mtendaji Mkuu wa Daraja la Nyerere Bw. Gerald Sondo amemueleza Waziri Mbarawa kuwa chanagamoto zinazowakabili kwa sasa ni kubaini magari yenye vibali maalumu, malalamiko ya magari ya abiria (daladala), uelewa mdogo wa matumizi ya daraja na mazoea ya kupita bila ya kulipa tozo.

Zaidi ya magari elfu nane hadi elfu kumi na tatu hupita katika daraja hilo kwa siku huku watembea kwa miguu, baiskeli wakipita bila kulipa tozo.
Meneja Mradi wa Daraja la Nyerere kutoka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Eng. Karim Mattaka, akitoa maelezo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa (kushoto), wakati alipotembelea daraja hilo leo jijini Dar es salaam.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa (kulia), akitoka kukagua moja ya Ofisi zilizopo katika daraja la Nyerere. Kushoto ni Msimamizi wa daraja hilo kutoka NSSF Gerald Sondo.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa (kulia), akipata maelezo ya ujenzi wa bomba la kupima mafuta (flow meter) kutoka kwa Fundi mitambo wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Simon Dottto (kushoto).

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Jumamosi ya May 28

Serikali YASITISHA Mchakato wa Ada Elekezi Kwa Shule Binafsi

$
0
0
SERIKALI imefuta mchakato wa kutangaza ada elekezi tangu katikati ya Mei mwaka huu, ambapo udhibiti wa ada hizo sasa utafanywa na Kamishna wa Elimu na Idara ya Ukaguzi.

Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako alisema hayo jana jioni alipokuwa akihitimisha mjadala wa bajeti ya wizara hiyo na kuongeza kuwa mchakato huo umefungwa baada ya kujadiliana na wamiliki na Kamati ya Bunge.

Kwa mujibu wa Profesa Ndalichako, usimamizi wa utoaji wa michango na ada holela katika shule hizo utashughulikiwa kwa mujibu wa sera, ambapo kutatakiwa kuwepo kwa kibali kwanza.

Alisema kutokana na hatua hiyo ya Serikali, ambayo inalenga kupata muda wa kutafakari suala hilo na kutafuta namna bora ya udhibiti, sasa hakutakuwa na ada elekezi ila michango itadhibitiwa.

Awali katika mjadala, baadhi ya wabunge walipinga mchakato huo na kutaka Serikali kujikita katika kuboresha shule zake na kuachana na utoaji wa ada elekezi. 

Akizungumza katika mjadala huo, Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM) alisema hakuna sababu ya kuwa na ada elekezi kwa shule binafsi.

Lugola alisema kama Serikali ikitaka shule binafsi zife, ni kuwalipa vizuri walimu wake, kuwajengea nyumba zao, kuwa na madarasa na kuweka chakula na hayo yakikamilika, hakuna mtu binafsi atakayepandisha ada. 

Kwa mujibu wa Lugola, kama hayo hayatafanyika, kila mtu ana uamuzi wa kumpeleka mtoto katika shule anayotaka hata Ulaya.

“Kuna tatizo gani na hizi shule za binafsi? Kwanza wamerundikiwa kodi nyingi mara kupaka rangi magari na mengineyo, sasa watarudishaje hizo fedha? Ndiyo maana wanatoza ada kubwa,” alitetea.

Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Zubeda Hassan (Chadema), alielezea kushangaa ni kwa jinsi gani ada elekezi itawekwa, wakati hakuna viwango vya utoaji elimu kwa watoto. 

Mbunge wa Maswa, Mashimba Ndaki (CCM), alisema suala hilo la ada elekezi watakaonufaika ni watu wenye fedha kwani ndiyo wanaowapeleka watoto katika shule binafsi na kusahau kuboresha shule za Serikali ambazo ni kwa watu wenye vipato vya kawaida.

Ndaki alisema iwapo shule za Serikali zingekuwa bora, zingechukua wanafunzi wote na zile za binafsi zingekosa wateja kwa gharama zao hizo kubwa, hivyo hakuna sababu ya kuwawekea ada elekezi.

“Shule binafsi wanapata wateja kutokana na miundombinu mibovu, matatizo ya walimu yanayotokana na kutotendewa haki katika shule za Serikali tofauti na shule binafsi ambazo wanawathamini walimu na kufanya watoe elimu bora,” alisisitiza.

Alitaka waziri, badala ya ada elekezi angekuja na mkakati madhubuti wa kuboresha shule za Serikali kwa kuwapa mahitaji yao walimu, kununua vitabu mashuleni na kuboresha miundombinu na shule hizo na hilo lingesababisha wapunguze wenyewe ada zao.

Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Mahawe (CCM) alisema Sheria ya Elimu ya 1978, inasema elimu siyo biashara bali huduma, lakini sasa wanaotoa elimu hiyo binafsi wanaonekana kama wao ni maadui.

Alisema shule binafsi, zinasaidia kusomesha Watanzania lakini bila kuthaminiwa wakati nchi nyingine watu binafsi wanasaidiwa kuwalipa mishahara, hapa nchini wanawapiga chini licha ya kuwa wanasaidia kusomesha hata watoto yatima, ili kuondoa watoto wa mitaani huku akieleza yeye katika shule yake anasomesha watoto 67.

Mahawe alisema shule binafsi wanalipa kodi zaidi ya 10, licha ya kuwa wameokoa kupeleka watoto kusomeshwa katika nchi za Kenya na Uganda huku akiomba wizara kuwapatia dawati wizarani ili wawape ushauri hususan katika mitaala.

Mbunge huyo alilalamikia shule binafsi kutengwa na wizara kwani hivi karibuni walitoa mafunzo kwa walimu wa watoto wa darasa la kwanza mkoani Dodoma bila kuwashirikisha.

Mbaroni Kwa Kukutwa Wakitoa Mamilioni Kwa ATM Za Watu 19

$
0
0
Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za kukamatwa wakiwa wanatoa fedha benki ya NMB tawi la Mpanda kiasi cha shilingi 3,680,000 wakiwa na kadi za ATM 19 mali za watu tofauti pamoja na namba za siri za kadi hizo. .

Kaimu Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Katavi Damasi Nyanda amesema watuhumiwa hao watatu walikamatwa jana majira ya saa tatu usiku katika Tawi la NMB Mpanda .

Watuhumiwa hao ambao majina yao yamehifadhiwa kwa kuwa upelelezi bado unaendelea, wamekamatwa na askari wa jeshi la polisi waliokuwa wakilinda Benki hiyo.

Nyanda ameeleza kuwa watumiwa walikamatwa baada ya askari polisi kuwatilia mashaka kutokana na kuwaona wakiwa wamekaa muda mrefu kwenye chumba cha mashine ya kutolea fedha .

Amesema baada ya kuwatilia mashaka polisi waliingia ndani ya chumba hicho na kuwakuta watuhumiwa hao wakiwa wanaendelea kutoa fedha katika mashine tatu zilizomo kwenye mashine za kutolea fedha.

Kaimu Kamanda alieleza ndipo askari polisi walipoamua kuwapekua watuhumiwa na waliwakuta wakiwa na kadi za ATM 19 mali za watu tofauti pamoja na namba za siri za kadi h izo na walikuwa tayari wameishatoa kiasi cha fedha taslimu shilingi 3,680,000.

Amezitaja Namba za Kadi za ATM walizokamatwa nazo watuhumiwa kuwa ni AC 61908000058,AC 61902403196,AC61902400417,AC61908000427,AC 61902240100,AC 61908000237, AC 61902400518 AC 61910000645, AC 61910004240,AC 61908000609 AC 61902403168.

Kaimu kamanda Nyanda amezitaja kadi za ATM zingine zilizokamatwa kuwa ni zenye namba AC 61910000537,AC 61902402653, AC 61910000250, Ac 61902400818, AC 61908000449,AC1902403219 AC 61910002329 na AC 70408100131.

Amesema watuhumiwa wanatarajia kufikishwa mahakamani baada ya uchunguzi wa tukio hilo kukamilika na bado watuhumiwa wote watatu wanaendelea kushikiliwa na jeshi la polisi kwa mahojiano zaidi .

Kaimu kamanda ametoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kutoa siri kwa watu za namba zao za siri za kadi wanazozitumia kwenye  ATM za  benki .
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live




Latest Images

<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>
<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596344.js" async> </script>