Quantcast
Channel: MPEKUZI
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live

Taswira Mbalimbali Za Rais Magufuli Na Rais Kagame Wakiwa Nchini Rwanda


Taarifa Za Uzushi Kuhusu Walimu Kushonewa Sare Inayosambazwa Katika Mitandao Ya Kijamii

$
0
0

WIZARA YA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI
TAARIFA KWA UMMA

YAH: TAARIFA ZA UZUSHI KUHUSU WALIMU KUSHONEWA SARE INAYOSAMBAZWA KATIKA MITANDAO YA KIJAMII

Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi inakanusha taarifa inayosambazwa katika mitandao ya kijamii yenye kichwa cha habari “NDALICHAKO NA WALIMU TZ”.

Taarifa hiyo inadai kuwa Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi Prof. Joyce Ndalichako amesema kuwa walimu wanaandaliwa sare watakazo vaa wakati wa kazi.

Tunapenda kuufahamisha umma kuwa Taarifa hizi si za kweli. Aidha, Wizara inawataka watu wanaoeneza taarifa za kizushi za aina hii waache kufanya hivyo ili kuepusha usumbufu unaojitokeza.

Hatua za kisheria zitachukuliwa kwa watakaobainika kuanzisha na kueneza uzushi huu.

IMETOLEWA NA

KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI
07/04/2016

Rais Magufuli ashiriki katika maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 22 ya mauaji wa Kimbari nchini Rwanda

$
0
0
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli na mkewe Mama Janeth Magufuli wakishuhudia  wenyeji wao Rais Paul Kagame na Mama Janeth Kagame pamoja na binti yao wakiweka shada la maua katika viwanja vya Kumbukumbu ya Mauaji ya Kimbali mjijini Kigali, Rwanda, leo

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli na mkewe Mama Janeth Magufuli wakiwa na wenyeji wao Rais Paul Kagame na Mama Janeth Kagame wakiwasili katika viwanja vya Kumbukumbu ya Mauaji ya Kimbali mjini Kigali, Rwanda, leo katika maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 22 ya mauaji hayo yaliyotokea mwaka 1994 ambapo watu takribani milioni 1,000,000 waliuawa.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli na mkewe Mama Janeth Magufuli wakiweka shada la maua wakishuhudiwa na  wenyeji wao Rais Paul Kagame na Mama Janeth Kagame wakiweka shada la maua katika viwanja vya Kumbukumbu ya Mauaji ya Kimbali mjijini Kigali, Rwanda, leo
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli na Rais Paul Kagame kwa pamoja wakiwasha "Urumuri Rutazima"  (Mwenge/mwali wa Matumaini)  katika maadhimisho Kumbukumbu ya miaka  22 ya Mauaji ya Kimbali mjijini Kigali, Rwanda, leo

Rais Magufuli Arejea Nyumbani Kutoka Rwanda Katika Safari Yake Ya Kwanza Nje Ya Nchi

$
0
0
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli akilakiwa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam akitokea nchini Rwanda alikokuwa katika ziara ya kikazi ya siku mbili leo Alhamisi April 7, 2016.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli akilakiwa na Mkuu wa Majeshi Jenerali Davis Mwamunyange huku Inspekta jenerali wa Polisi IGP Ernest Mangu akisubiri zamu yake  mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam akitokea nchini Rwanda alikokuwa katika ziara ya kikazi ya siku mbili leo Alhamisi April 7, 2016.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli akilakiwa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es salaam Kamishna Simon Sirro mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam akitokea nchini Rwanda alikokuwa katika ziara ya kikazi ya siku mbili leo Alhamisi April 7, 2016.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli akilakiwa na Msajili wa vyama vya Siasa Mhe Jaji Francis Mutungi mara baada ya kutua  katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam akitokea nchini Rwanda alikokuwa katika ziara ya kikazi ya siku mbili leo Alhamisi April 7, 2016.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli na mkewe Mama Janeth Magufuli wakiongozana na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe Paul Makonda mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam akitokea nchini Rwanda alikokuwa katika ziara ya kikazi ya siku mbili leo Alhamisi April 7, 2016.

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Ijumaa ya April 8

Rais Magufuli Mgeni Rasmi Maadhimisho ya Mei Mosi

$
0
0

RAIS John Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya sherehe ya Siku ya Wafanyakazi Duniani maarufu Mei Mosi ambayo kitaifa yatafanyika mkoani Dodoma.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Nicholas Mgaya alisema Tucta waliwasilisha maombi rasmi ya kumuomba Rais Magufuli kuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo na tayari wamepata taarifa rasmi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu kuwa Rais amekubali kuwa mgeni rasmi.

Mgaya alisema hayo jana mjini Dodoma wakati wa mkutano baina ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana na timu ya maandalizi ya sherehe za Mei Mosi Kitaifa, ambao mkutano huo ulikuwa na lengo la kujadili na kuendelea kuweka mipango na maandalizi ya kufanikisha sherehe za mwaka huu kwa mafanikio makubwa.

Alisema ili kufanikisha sherehe za Mei Mosi, Tucta Makao makuu watachangia nusu ya gharama zote za sherehe nzima na nusu inayobaki itachangiwa na wadau mbalimbali wakiwemo waajiri ambapo kwa mujibu wa Kamati ya Maandalizi Bajeti nzima ya sherehe ya mwaka huu ni Sh milioni 29.6.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa Rugimbana aliishukuru Tucta na Serikali kwa ujumla kwa kuupa Mkoa wa Dodoma ambao ni Makao Makuu ya Nchi heshima ya kipekee ya kuwa mwenyeji wa maadhimisho ya sherehe ya Sikukuu ya Mei Mosi Kitaifa mwaka huu.

Naye Katibu wa Tucta Mkoa wa Dodoma, Ramadhani Mwendwa alisema tayari wameunda kamati ya maandalizi ya sherehe na jukumu kubwa lililoko mbele ni kutafuta fedha na michango kutoka kwa wadau, wengi wao wakiwa ni waajiri serikalini.

Bajeti 2016/2017 kuanza kuchambuliwa leo

$
0
0

Kama za Kudumu za Kisekta leo zinatarajia kuanza kuchambua taarifa za utekelezaji wa Bajeti za Wizara zinazosimamiwa na kamati hizo.

Hatua hiyo inafanywa kwa mujibu wa Kanuni ya 98 (2) ya Kanuni za Kudumu za Bunge.

Akizungumza jana Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano cha Bunge, Owen Mwandumbya alisema kwa takribani siku tisa Kamati za Kisekta zitakuwa na kazi ya kuchambua na kuangalia kama vipaumbele vimezingatiwa katika bajeti ya wizara husika.

Mwandumbya alisema katika kipindi hicho, Kamati ya Bajeti itafanya uchambuzi wa Mapendekezo ya Mpango na kiwango cha ukomo wa Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

“Kamati zina mamlaka ya kuhamisha kasma moja kwenda nyingine, na kama inaona kuna haja ya kupunguza au kuongeza bajeti ya wizara husika basi mapendekezo hayo yanapelekwa kwenye Kamati ya Bajeti ambayo itashauriana na Serikali,” alisema.

Mwandumbya alisema kwa mujibu wa Kanuni ya 98(3) ya Kanuni za Bunge, Aprili 15, mwaka huu kutakuwa na kikao cha pamoja kati ya Kamati ya Uongozi na Kamati ya Bajeti ili kujadili mambo muhimu yaliyojitokeza kwenye Kamati za Kisekta wakati wa kujadili utekelezaji wa Bajeti za Wizara mbalimbali.

Juzi Serikali iliwasilisha mbele ya wabunge wote Mapendekezo ya Kiwango na Ukomo wa Bajeti kwa mwaka 2016/2017 inayotarajiwa kuwa ya Sh trilioni 29.539.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Zelothe Steven Awaagiza Polisi Kuwakamata Watumishi HEWA

$
0
0
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Zelothe Steven
 
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Zelothe Steven amemwagiza Kamanda wa Polisi mkoa huo, Jacob Mwaruanda kuwasaka na kuwakamata watumishi hewa 18 waliobainika katika uhakiki uliofanyika katika halmashauri zote mkoani humo hivi karibuni.

Pia ameagiza fedha hizo zilizolipwa kwa watumishi hao hewa na kuiingizia hasara kubwa Serikali zirudishwe mara moja.

Akifafanua alisema katika uhakiki huo, watumishi hewa tisa walibainika katika wilaya ya Nkasi, wanane katika Manispaa ya Sumbawanga na mmoja wilaya ya Sumbawanga wakati Kalambo ikiwa haina mtumishi hewa.

Uhakiki huo unatokana na maagizo aliyotoa Rais John Magufuli baada ya kuwaapisha wakuu wa mikoa aliowateua, aliwaambia wakafanye kazi ya kutatua kero za wananchi na sio kwenda kufanya siasa.

Pia Rais Magufuli aliwapa wakurugenzi wa halmashauri siku 15 wawatoe katika orodha ya malipo ya mshahara wafanyakazi hewa wote katika halmashauri zote nchini.

Zelothe alitoa agizo hilo jana katika kikao maalumu cha kufahamiana kilichojumuisha wazee , viongozi wa dini , watendaji wa umma na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa huo kilichofanyika mjini hapa.

Alisisitiza kuwa hajaridhishwa na uhakiki huo, hivyo akaagiza halmashuri zote kurudia upya uhakiki wa watumishi.

“Siku ile ile nilipoapishwa kabla sijavuka geti kutoka nje ya Ikulu nilipiga simu na kuagiza halmashauri zote (Manispaa, Nkasi, Kalambo na Sumbawanga) kuanza uhakiki mara moja wasinisubiri hadi niripoti mkoani hapa,” alieleza.

Aliongeza kuwa aliporudi mkoani humo na kuripoti kazini katika siku yake ya kwanza ofisini alikabidhiwa kitabu chenye orodha ya watumishi wa umma wa halmashauri zote akielezwa kuwa hakuna mtumishi hewa katika mkoa wa Rukwa.

“Sikukubaliana nao nilikataa, nikaagiza ufanyike uhakiki mara moja ndipo wamepatikana watumishi hewa 18 na watumishi wengine 137 wapowapo tu wakiwa na taarifa zinazotia mashaka. Wote wamebainika kwenye hicho kitabu nilichokabidhiwa kikionesha hakuna mtumishi hewa,” alisisitiza.

UKAWA Wasusia Uchaguzi wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa nchini (ALATt)

$
0
0

Wajumbe wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa nchini (Alat), wanaotokana na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wamesusia uchaguzi kwa madai ya kuminywa kwa demokrasia.

Mkutano huo uliofanyika jana katika ukumbi mpya wa CCM mjini Dodoma, wajumbe wake ni wakurugenzi na wenyeviti wa halmashauri zote, mameya wa miji na majiji na mbunge mmoja kutoka kila mkoa wa Tanzania Bara.

Nafasi zilizokuwa zikigombewa ni mwenyekiti, makamu wake na wajumbe 16 wa kamati ya utendaji.

Awali, Mwanasheria wa Alat, Cleofas Manyangu aliwataja waliochukua na kurejesha fomu za kugombea uenyekiti ni Gulam Mukadam (Meya wa Shinyanga), Murshid Ngeze (Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bukoba Vijijini), Chief Kalumuna (Meya wa Bukoba Mjini) na Isaya Charles (Meya wa Jiji la Dar es Salaam).

Hata hivyo, alisema waliokidhi vigezo kwa mujibu wa Katiba ya Alat, kanuni za kudumu na mwongozo ni Mukadam na Ngeze wote kutoka CCM na waliosalia wa Ukawa hawakukidhi.

Alisema Charles na Kalumuna walishindwa kurejesha fomu katika muda uliowekwa wa saa 6.00 mchana siku moja kabla ya uchaguzi na pia hawakupata wadhamini 10 kutoka kanda tano za Alat Taifa.

Kutokana na kauli ya mwanasheria huyo, mwenyekiti wa muda wa mkutano huo ambaye pia ni Meya wa Manispaa ya Dodoma, Jaffar Mwanyemba alitangaza kuwa wagombea katika uchaguzi huo ni wawili.

Kauli hiyo ilibadilisha hali katika ukumbi, huku wajumbe wa Ukawa wakitaka wagombea wote waruhusiwe kuingia katika kinyang’anyiro hicho.

Meya wa Jiji la Arusha, Kalist Lazaro aliomba wagombea hao waruhusiwe kwa kuwa maandalizi ya uchaguzi yalikiuka mwongozo, hali ambayo ilifanya baadhi yao kutokidhi vigezo.

Alisema taarifa ya mkutano huo ilitakiwa kuwafikia siku zisizopungua 28 kabla ya uchaguzi, lakini wengi wao walipata barua hizo chini ya muda huo.

Akijibu hoja hizo, Manyangu alisema taarifa za mkutano huo kwa mara ya kwanza zilipelekwa kwenye halmashauri Novemba 2, mwaka jana.

“Tatizo lililotokea ni baadhi ya halmashauri kuchelewa kukamilisha uchaguzi, hali iliyosababisha mkutano kuahirishwa mara mbili,” alisema.

Baada ya hoja hizo, wajumbe wote wanaotokana na Ukawa walitoka nje ya ukumbi, huku wakiahidi kufanya kazi na Serikali Kuu pekee.

Akizungumza nje ya ukumbi, Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Charles alisema kutokana na kuchelewa kwa uchaguzi jijini humo hakupata taarifa mapema kuhusu mkutano na uchaguzi huo.

Hata hivyo, Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe na meya wa Manispaa ya Kigoma walishiriki uchaguzi kama kawaida.

“Mimi sijui chochote. Sijui wametoka kwa sababu gani maana nimefika hapa nikiwa nimechelewa,” alisema Zitto.

Katika uchaguzi huo, Mukadam alichaguliwa kuwa mwenyekiti kwa kura 179 kati ya 276 na makamu wake ni Stephen Muhapa aliyepata kura 152 kati ya 272.

Serikali Yasema Itawafukuza Kazi Maofisa wa Serikali Wanaowawekea Vikwazo Waandishi wa Habari

$
0
0

Serikali  imesema itawafukuza kazi maofisa wa Serikali ambao wanaweka vikwazo na kuwakwamisha waandishi wa habari kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa kupata habari na taarifa mbalimbali kutoka serikalini.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye aliyasema hayo jijini Mwanza wakati alipozungumza na wadau wa utamaduni, habari na michezo kutoka wilaya zote za mkoa wa Mwanza.

Alisema hayo wakati akitoa ufafanuzi wa swali lililoulizwa na Mwandishi wa Habari wa ITV/ Radio One anayefanyia kazi zake mikoa ya Kanda ya Ziwa, Cosmas Makongo ambaye alitaka apate msimamo wa Serikali juu ya hatua zitakazochukuliwa na serikali kutokana na wimbi la unyanyasaji wa kijinsia unaofanywa na baadhi ya watendaji wa Serikali kwa waandishi wa habari nchini.

Makongo alisema akiwa wilayani Chato mkoani Geita hivi karibuni alizuiliwa kuandika habari na ofisa mmoja wa Serikali hadi pale atakapopata kibali kutoka kwa Mkuu wa Wilaya.

“Kumeibuka wimbi la unyanyasaji wa kijinsia kwa waandishi wa habari, ukifika Chato huandiki habari mpaka upate kibali kutoka kwa Mkuu wa Wilaya, nilizuiliwa kuandika habari hivi karibuni wakati nafanya habari ya uchunguzi wa mabilioni ya fedha wilayani humo,” alisema Makongo na kuhoji,

 “Mheshimiwa Waziri tukiendelea kusubiri vibali kutoka kwa watawala je, tutafichua maovu?” 

Nape alisema kuwa msimamo wa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli ni kuvitumia vyombo vya habari katika kufichua maovu yanayofanywa na baadhi ya watu katika jamii. 

“Kama kuna Ofisa wa Serikali anaweka kizuizi kwa mwandishi wa habari ili asipate habari na kushindwa kutimiza wajibu wake tutamfukuza kazi,” alisema Nape.

Aliwataka maofisa wa habari kote nchini wawe tayari kutoa taarifa mbalimbali za maendeleo zilizopo kwenye maeneo yao kwa wakati ili waandishi wauhabarishe umma.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella Atoa Masaa 48 Kwa Watumishi Kuhamia Maeneo yao Ya Kazi

$
0
0

Mkuu  wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela ametoa saa 48 kuanzia leo kwa Wakuu wa Idara wa Halmashauri ya Misungwi ambao wana makazi yao Mwanza mjini kuhamia mara moja kwenye maeneo ya kazi.

Mongela alitoa agizo hilo jana wilayani Misungwi alipozungumza na watendaji wa kata na vijiji, madiwani na wakuu wa Idara wa halmashauri kwenye ziara yake ya kwanza ya kikazi tangu ateuliwe kuwa Mkuu mpya wa Mkoa wa Mwanza, na kubaini baadhi ya wakuu wa Idara wanaishi jijini Mwanza.

Alimuagiza Ofisa Usalama wa Taifa wa Wilaya(DSO) ya Misungwi, Stanslaus Mbile awafanyie uhakiki wa kina wakuu hao wa Idara kuhamishia makazi yao Misungwi ili wawahudumie wananchi kwa wakati.

“DSO nenda nyumba hadi nyumba za wakuu hawa wa Idara na uhakikishe kila mtu kwa kuwahesabu akiwa na familia yake wamehamia kwenye nyumba zao, nimekuagiza wewe kwa sababu unajua utaratibu wa vikao vyetu, ukishindwa kulisimamia hilo kikamilifu nitajua pa kukupeleka,” alisema Mongella.

Alisema haiingii akilini kwa mtumishi wa umma aliyeajiriwa na kuishi kwa mshahara unaotokana na kodi za wananchi akiishi nje ya eneo la kazi, jambo ambalo alisema litaleta shaka katika kuwahudumia wananchi.

“Siwezi mimi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, halafu naishi Shinyanga, huwezi kuwa DC wa Misungwi halafu unaishi Sengerema na kwa mtindo huu huwezi kuwahudumia wananchi,” alisema Mongella na kuongeza:

 “Kuanzia leo (jana) na Wakuu wa Idara wanaokaa nje ya Misungwi watumie siku ya Karume (jana) kuhamia Misungwi na niwaambie kuwa utaratibu wa Serikali ya Awamu ya Tano kila mtu awajibike kwenye kipande chake.”

Alisema hakuhamishiwa mkoani Mwanza kwa lengo la kuhubiri kifo au siku ya kustaafu kwa watumishi wa umma bali ameteuliwa na Rais John Magufuli kwenda mkoani Mwanza kufanya kazi za maendeleo ya wananchi na kushughulika na matatizo ya wananchi na kuyatafutia majawabu.

Aidha, alimuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Misungwi, Nathaniel Mshana kuhakikisha watendaji wa kata na vijiji wanaishi kwenye maeneo yao ya kazi ili iwe rahisi kwa wao kuwahudumia wananchi.

Serikali yaandaa mpango wa ajira kwa vijana nchini

$
0
0

Serikali imeanzisha mpango maalumu wa mafunzo kwa wahitimu kutambua ujuzi katika sekta zisizo rasmi, ili kuwajengea vijana wigo mpana wa ajira kwa fani walizosomea.

Mpango huo unalenga kutoa mafunzo ya ufundi katika fani mbalimbali kwa vijana walioishia darasa la saba, kidato cha nne au sita na wanaohitimu vyuo mbalimbali.

Lengo ni kuwawezesha vijana kupata ajira na waajiri nao kupata watu wenye ujuzi wa kutosha.

Akizungumzia mpango huo juzi, Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Ajira Ofisi ya Waziri Mkuu, Robert Masingiri alisema changamoto kubwa kwa vijana ni ukosefu wa ajira hasa wanaomaliza shule bila kuwa na fani yoyote.

Masingiri alisema baada ya Serikali kuona upungufu huo, imeandaa mpango maalumu unaofadhiliwa na Shirika la Kazi Duniani (ILO) ili kutoa mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi na wahitimu wa vyuo mbalimbali.

“Licha ya kutoa mafunzo hayo, tutatambua ujuzi uliopatikana kwa mfumo usio rasmi. Tutawapa wataalamu hao baada ya kukaa nao na kuona uwezo wao, hiyo itawasaidia kupata ajira hasa zinapokuja kampuni za uwekezaji au viwanda,” alisema.

Masingiri aliongeza kuwa nia ya Serikali ni kuongeza ujuzi kwa wafanyakazi ambao wako kazini, mpango huo utaanza na vijana 5,000.

Mkurugenzi wa ILO nchini, Mary Kawar alisema Tanzania imefanikiwa kuandaa mpango utakaosaidia vijana wengi kupata ajira 

“Kwa muda mrefu kumekuwa na pengo kati ya elimu ya darasani na utendaji. Naamini mafunzo haya yatatoa fursa ya pekee kuziba pengo hilo na kuongeza sifa za kuajiriwa,” alisema Kawar.

Mkurugenzi wa Taarifa za Soko la Ajira Ofisi ya Waziri Mkuu, Ahmed Makbel alisema mpango huo utakuwa na manufaa kwa waajiri na waajiriwa, kwa sababu wote watapata wanachohitaji.

Lowassa Auponda Uongozi wa Rais Magufuli.......Asema Uongozi wake ni wa Hamasa na Umaarufu wa Muda Mfupi

$
0
0

Siku 155 baada ya Dk John Magufuli kuapishwa kuwa Rais, aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema katika uchaguzi huo, Edward Lowassa ametaja mambo matano yanayomfanya autilie shaka mustakabali wa Taifa chini ya uongozi wa Rais huyo wa Awamu ya Tano.

Akizungumza na wanazuoni wa ndani na nje ya nchi wakiongozwa na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Profesa Rwekaza Mukandala nyumbani kwake Masaki Dar es Salaam, Lowassa alisema: “Hali ya siasa nchini ni ya hamasa lakini isiyo na msingi endelevu.

Lowassa, ambaye alishika nafasi ya pili katika uchaguzi huo baada ya kupata kura milioni 6.07 sawa na asilimia 39.97 aliyataja mambo hayo kuwa ni Rais kugawa fedha wakati chombo cha kufanya hivyo kipo, watumishi kuachishwa kazi, upitishaji mizigo Bandari ya Dar es Salaam kushuka, nchi kunyimwa misaada na ugumu wa maisha unaowakabili wananchi hivi sasa.

Katika uchaguzi huo, Rais Magufuli alipata kura milioni 8.8 sawa na asilimia 58.47 na kumshinda Lowassa ambaye alikuwa amejiunga Chadema Julai mwaka jana akitokea CCM ambako jina lake lilikatwa katika mchakato wa chama hicho kupata mgombea urais.

Tangu aingie Ikulu, Rais Magufuli amekuwa akichukua hatua mbalimbali za kutengua uteuzi au kuwasimamisha kazi watendaji mbalimbali wa Serikali, kufuta maadhimisho ya sherehe mbalimbali na kuagiza fedha zitumike kutekeleza miradi mingine huku akiwabana wafanyabiashara kulipa kodi.

Uamuzi wake huo unaofanywa pia na mawaziri wake umekuwa ukipongezwa na kukosolewa na watu wa kada mbalimbali na jana Lowassa alikuwa miongoni mwa wakosoaji hao ikiwa ni mara yake ya pili tangu Dk Magufuli aingie madarakani.

Mara ya kwanza, Lowassa alikosoa sera ya elimu bure, alipoitofautisha na ile aliyokuwa ameahidi ya kuanzia awali hadi chuo kikuu na kuhoji iwapo Rais Magufuli mbali na ada angefuta pia michango mingine, jambo ambalo lilifanyiwa kazi.

Alipoulizwa kuhusu mazungumzo hayo, Profesa Mukandala alisema: “Tunafanya utafiti kuhusu masuala mbalimbali ya kisiasa, uchumi, utawala bora na ushindani wa siasa na tunazungumza na watu kutoka vyama mbalimbali na viongozi wa Serikali.”

Waziri wa Habari, Nape Nnauye alipoulizwa kuhusu kauli hiyo ya Lowassa alisema waziri mkuu huyo wa zamani anapingana na viongozi wa Chadema wanaokiri wazi kuwa Rais Magufuli anatekeleza sera na mikakati ya upinzani. 

Taarifa iliyotolewa jana na ofisi ya Lowassa ilisema mwanasiasa huyo aliwaeleza wanazuoni hao kuwa; “hali ya siasa hivi sasa ni ya hamasa kutokana na Serikali mpya na ‘style’ mpya. Kwa kipindi kifupi atakuwa lakini hakuna mafanikio ya kiuchumi mbele ya safari.”

Alisema Rais amekuwa akigawa fedha wakati chombo cha kufanya hivyo kipo ambacho ni Bunge.

Rais Magufuli amekuwa na utaratibu kuidhinisha fedha zilizotengwa kwa ajili ya sherehe mbalimbali kutumika katika shu ghuli nyingine. Juzi, aliagiza Sh2 bilioni zilizokuwa zitumike katika Siku ya Muungano zitumike kupanua barabara inayokwenda Uwanja wa Ndege wa Mwanza.

Pia, amewahi kuamuru Sh4 bilioni za Siku ya Uhuru kupanua Barabara ya Morocco – Mwenge, Dar es Salaam. 

Aliagiza pia fedha za maadhimisho ya siku ya Ukimwi kutumika kununua vifaatiba na Sh225 milioni zilizotengwa kwa ajili ya hafla ya uzinduzi wa Bunge zilinunulia vitanda Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Lowassa pia alieleza kusononeshwa na hali ngumu ya maisha na idadi kubwa ya watu kuachishwa kazi.

“Nasononeshwa ninapoona watu wanaachishwa kazi na mashirika mbalimbali kwa sababu ya hali ngumu ya uendeshaji wa mashirika hayo.

“Bandarini sasa hivi nasikia uingizaji mizigo umeshuka kwa asilimia 50, kampuni nyingi za mizigo zimefunga shughuli zake na pale kulikuwa na vijana wetu wengi wana ajira, sasa hivi wako mitaani, hali inatisha maisha ya mwananchi yanazidi kuwa magumu,” alisema.

Lowassa aligusia uamuzi wa Marekani kupitia bodi yake ya Changamoto za Milenia (MCC) kusitisha msaada wa zaidi ya Sh1 trilioni.

“Ni pigo kwa mustakabali wa uchumi. Halafu tunasema tunataka nchi ya viwanda, hela tutatoa wapi kama si hawa wafadhili wa ndani na nje kusaidia katika hilo?” alihoji.

Lowassa ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema alisema: “Hawa wafadhili siyo watu wa kuwabeza wataturudisha nyuma. Jakaya (Kikwete- Rais mstaafu wa Awamu ya Nne) kwa kiasi kidogo alijitahidi kuvutia wawekezaji, japo kulikuwa na uzembe na ufisadi katika kuwasimamia.

“Hapa kinachotakiwa ni kufanya mabadiliko katika mfumo na kuufanya kuwa endelevu,” alisema.

Alisema si kweli kuwa kila mtu katika Serikali ya Awamu ya Nne alikuwa mla rushwa huku akikiri kuwa mfumo wa Serikali hiyo ulikuwa mbovu na wa kifisadi.

Aliwaeleza wanazuoni hao kuwa: “Uchaguzi ule tulishinda (upinzani) na kila mtu anajua hivyo. Hata Magufuli anajua hilo...,” alisema.

Akizungumzia mikakati ya upinzani, Lowassa alisema wamejipanga kuhakikisha hawaporwi tena ushindi na kusisitiza kuwa joto la kutaka mabadiliko bado ni kubwa na Watanzania wameichoka CCM.

Akijibu hoja zilizotolewa na Lowassa, Nape alisema, “Anajichanganya tu, maana Mbowe (Freeman – Mwenyekiti wa Chadema) amenukuliwa akisema Rais Magufuli anaiga kila kitu cha Chadema, sasa yeye (Lowassa) anaposema hayo maana yake haelewani na Mbowe.”

Alisema litakuwa jambo la ajabu kama Lowassa atakubali kila jambo linalofanywa na Serikali iliyopo madarakani kwa kuwa ndivyo alivyo.

“Katika Uchaguzi Mkuu Lowassa hakuchaguliwa na wananchi ila Magufuli alichaguliwa kwa sababu wananchi walifurahishwa na sera zake, hivyo amuache mwenzake atekeleze ahadi zake kwa wananchi,” alisema Nape.

“Kwanza Lowassa amekuwa mtetezi wa wezi, mafisadi na wala rushwa. Unawateteaje watu wa aina hii wanapofukuzwa kazi. Amebanwa tu na kwake kazi inayofanywa na Magufuli inampa maumivu.”

Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema) Ambaye Pia ni Dada yake Tundu Lissu Afariki Dunia

$
0
0

Aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Christina Mughwai Lissu amefariki dunia kwa ugonjwa wa saratani jana.

Kaka wa marehemu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu alituma taarifa kwenye mitandao ya jamii akisema amepata taarifa za msiba huo akiwa mkoani Kigoma.

Alisema Christina alikuwa amelazwa katika Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam na alianza kuugua tangu mwaka jana.

“Nawasalimu kutoka Kibondo. Nina habari zisizokuwa njema. Dada yangu aliyekuwa mbunge wetu wa viti maalumu, Christina amefariki dunia muda mfupi uliopita katika hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam.

“Marehemu alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa ‘cancer’ tangu mwaka jana. Kwa sasa niko nje ya Dar es Salaam na ndiyo kwanza taarifa hizi zimenifikia…” ilisema taarifa ya Lissu aliyoituma mitandaoni.

Christina alikuwa Mbunge wa Viti Maalumu wa Mkoa wa Singida tangu mwaka 2010 hadi 2015 na alikuwa Naibu Waziri Kivuli wa Wizara ya Fedha. Hakurudi bungeni katika uchaguzi wa 2015.

Polisi Anayemiliki nyumba 40 Ang’olewa....Suzan Kaganda arithi mikoba yake

$
0
0
 Mkuu  wa Jeshi la Polisi, IGP Ernest Mangu
 
Mkuu  wa Jeshi la Polisi, IGP Ernest Mangu, amemwondoa kwenye nafasi yake, Mnunuzi wa Vifaa na Boharia Mkuu wa jeshi hilo, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), Adriano Magayane ili kupisha uchunguzi wa tuhuma dhidi yake.

Kuondolewa kwa DCP Magayane katika nafasi hiyo kunatokana na taarifa zilizochapishwa na vyombo vya habari hivi karibuni, kuwa anamiliki nyumba zaidi ya 40 na kumbi kadhaa za starehe ndani na nje ya Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Gazeti la Mtanzania,  IGP Mangu amefikia uamuzi huo kwa kile kinachodaiwa kuwa tuhuma hizo ni nzito na zinalenga si kumfedhehesha yeye kama ofisa mkuu wa Jeshi la Polisi, lakini kwa jeshi zima.

“IGP Mangu amemwondoa mara moja DCP Magayane kutokana na tuhuma zinazomkabili, kwa kweli ni nzito, nadhani hatua zilizochukuliwa ni sahihi… unajua sisi askari tuna miiko ya utendaji kazi, sasa inapotokea tuhuma kama hizi kwa ofisa kama huyu, lazima uchunguzi wa kina ufanyike,” kilisema chanzo .

Kilisema kuwa uchunguzi dhidi ya ofisa huyo unafanywa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna Diwani Athumani.

Katika mabadiliko hayo, habari za ndani zinasema kuwa DCP Magayane amehamishiwa Makao Makuu ya Polisi, Kitengo cha Uzuiaji wa Makosa.

Alipoulizwa ana, IGP Mangu alikiri kumwondoa ofisa huyo, lakini hakueleza amepangwa kitengo gani.

“Ni kweli nimemwondoa kwenye nafasi yake jana (juzi) ili kupisha uchunguzi wa suala hili kwani ni zito, lazima tujiridhishe kabla ya kuchukua hatua zaidi,” alisema.

Alipoulizwa ni nafasi gani ambayo atapewa DCP Magayane baada ya kuhamishiwa Makao Makuu ya Polisi, IGP Mangu alisema jeshi hilo lina kazi nyingi hivyo atapangiwa majukumu mengine bila kuingia kwa undani.

Aidha, IGP Mangu alisema ameagiza uchunguzi wa tuhuma hizo zilizotolewa kwenye vyombo vya habari, uanze mara moja ili wajiridhishe kabla kuchukua hatua zaidi.

Pamoja na uamuzi huo wa IGP Mangu, tayari vyombo vya dola vimeanza kumuhoji DCP Magayane, ikiwamo kumtaka awasilishe nyaraka zinazohusu umiliki wa mali zake zote.

Kutokana na hali hiyo, IGP Mangu amelazimika kufanya mabadiliko madogo ndani ya jeshi na kumteua Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Suzan Kaganda kushika nafasi ya DCP Magayane.

ACP Kaganda amewahi pia kuwa msaidizi wa Boharia Mkuu miaka kadhaa iliyopita kabla ya kuwa msemaji wa Jeshi la Polisi mwaka 2007 hadi 2008, baada ya kustaafu kwa aliyekuwa msemaji, ACP Abdallah Msika.

Mbali na kushika wadhifa huo, ACP Kaganda aliwahi pia kuwa Ofisa Mnadhimu wa Polisi Mkoa wa Dodoma na baadae kuteuliwa kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma ambako alihudumu kwa miaka miwili kabla ya kuhamishiwa Mkoa wa Tabora.

Ofisi ya Wakili wa Kujietegemea Zanzibar yalipuliwa kwa bomu

$
0
0

Watu wasiofahamika wamelipua kwa kitu kinachohisiwa kuwa ni bomu Ofisi ya Wakili wa Kujitegemea, Omar Said Shabani, iliyopo Kiembe Samaki Zanzibar.

Tukio hilo lilitokea saa 7:00 usiku wa kuamkia jana. Hata hivyo, hakuna mtu aliyejeruhiwa kutokana na mlipuko huo isipokuwa jengo la ofisi hiyo limeharibika katika baadhi ya maeneo ikiwamo kuvunjika kwa vioo vya madirisha.

“Majira ya saa saba usiku, nilipata taarifa kuwa mlipuko umetokea katika ofisi yangu na nilipofika nilikuta mipasuko kidogo ya vioo vya nyumba yangu," alisema Wakili Omar.

Omar, ambae pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria Zanzibar, alisema gharama za uharibifu wa mali hiyo bado hajazijua.

Aidha, alisema analiachia Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Mkadam Khamis Mkadam, alithibitisha kutokea kwa mlipuko huo na kusema kuwa Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi ili kubaini aina ya bomu lililotumika.

Alisema taarifa kamili kuhusu mlipuko huo, atautoa baadaye kwa vile polisi wanaedelea na uchunguzi.

Aidha, Kamanda Mkadam aliwataka wananchi kuendelea kulinda amani na utulivu na kutoa taarifa ya vitendo vyote vinavyoashiria uhalifu.

CUF Wamuomba Rais Magufuli na Waziri Mkuu Majaliwa Waingilie kati mgogoro wa Umeya Tanga

$
0
0
Chama  cha Wananchi (CUF) kimemuomba, Rais John Magufuli na Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa, kutumia busara kumaliza mgogo wa umeya katika jiji la Tanga kama ilikuwa kwenye mgogoro wa umeya jiji la Dar es Salaam na kuagiza uchaguzi huo urudiwe.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Naibu Katibu Mkuu wa CUF Tanzania Bara, Magdalena Sakaya, alisema chama hicho hakimtambui meya aliyeko hivi sasa kwa madi kuwa si mshindi halali katika uchaguzi uliofanyika Desemba 19, mwaka jana.

Alidai katika uchaguzi huo, mgombea wa CUF, Rashid Jumbe, ndiye aliyeshinda dhidi ya mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Seleman Mustafa, lakini ushindi wake uliporwa na msimamizi wa uchaguzi huo kwa kutangaza matokeo tofauti.

Sakaya alisema kilichotokea katika uchaguzi huo ni uporaji wa matokeo, jambo ambalo limesababisha meya huyo kutokubalika.

“Kutokana na mvurugano uliopo katika suala hilo, shughuli za maendeleo katika jijini la Tanga zimesimama na tangu kufanyika kwa uchaguzi huo hakuna kikao hata kimoja cha baraza la madiwani kilichofanyika kwa sababu madiwani wa CUF wamegoma kushiriki,” alisema.

“CUF inamuomba Rais Magufuli ama Waziri Mkuu kutumia busara kama zile zilizotumika kumaliza mgogoro wa umeya Dar es Salaam ili vikao vya baraza la madiwani viweze kuanza na kuharakisha shughuli za maendeleo ya jiji,” alisema Sakaya.

Kwa upande wake, Mbunge wa Tanga Mjini (CUF), Mussa Mbarowe, alisema ana amini Rais atatumia busara kumaliza mgogoro huo ili kuwanusuru wananchi wa jiji hilo.

Mabula Ambwaga Ezekiel Wenje Kesi Ya Ubunge Jijini Mwaza Leo

$
0
0

Mbunge wa jimbo la Nyamagama,jijini Mwanza pichani akifurahia mara baada ya kutangazwa mshindi wa jimbo hilo na Mahakama kuu ya jijini Mwanza dhidi ya aliyekuwa Mgombea Ubunge wa jimbo hilo kupitia chama cha CHADEMA,Mh.Ezekiel Wenje.
****
Kesi ya kupinga matokeo ya Ubunge wa Jimbo la Nyamagana iliyofunguliwa na aliyekuwa mbunge wa Nyamagana Ezekiel Wenje (CHADEMA) dhidi ya Mbunge wa sasa wa Nyamagana Stanslaus Mabula (CCM) ilikuwa ikiendelea katika mahakama Kuu Mwanza ambapo Ezekiel Wenje alifungua kesi hiyo akipinga matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) yakimpa ushindi Mbunge wa sasa, Stanslaus Mabula.

Leo April 8 2016, maamuzi ya kesi hiyo yametangazwa rasmi ambapo Mbunge Stanslaus Mabula ameshinda kesi hiyo, baada ya kubainika upande wa madai hauna ushahidi unaokidhi kuithibitishia mahakama.

Rais Magufuli Amteua Bwana G. Byakanwa Kuwa Mkuu Wa Wilaya Ya Hai .

$
0
0

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Bw. Gelasius Gaspar Byakanwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Mkoani Kilimanjaro.

Taarifa iliyotolewa leo Ikulu Jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi, imeeleza kuwa uteuzi huo umeanzia tarehe 08 April, 2016. Bw. Byakanwa anajaza nafasi iliyoachwa wazi na Bw. Antony Mtaka aliyeteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu.

Kabla ya Uteuzi huo, Bw. Byakanwa alikuwa Katibu wa Rais Msaidizi Mwandamizi.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es Salaam
08 Aprili, 2016

Taarifa Kutoka JWTZ Kuhusu Wanajensi wa Tanzania Kutuhumiwa Kuhusika na Unyanyasi wa Kingono Congo

$
0
0

Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania limeshitushwa na kusikitishwa kwa taarifa zinazo lituhumu JWTZ kuhusu unyanyasaji wa kijinsia unaodaiwa kufanywa na Wanajeshi wetu kwa Wananchi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

JWTZ chini ya Umoja wa Mataifa (MUNUSCO) limekuwa likitekeleza majukumu ya Ulinzi wa amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo takribani miaka mitatu sasa.Katika muda ambao JWTZ limekuwa nchini Congo hapakuwepo na tuhuma kama hizo.

Aidha, JWTZ limetekeleza na limeendelea kutekeleza majukumu kama hayo katika nchi mbalimbali duniani kama vile Msumbiji, Liberia, Visiwa vya Comoro (Anjouan), Lebanon, Sudan katika jimbo la Darfur na sehemu nyingi kama hizo.

Katika kutekeleza majukumu hayo JWTZ limeyatekeleza kwa nidhamu na weledi wa hali ya juu.JWTZ limekuwa moja ya majeshi mengi yanayofanya vizuri na kutoa mchango mkubwa katika Ulinzi wa amani katika nchi ambazo limetekeleza majukumu hayo.

Hivi karibuni kumezuka tuhuma nchini Congo kuhusu Wanajeshi wa JWTZ kuwanyayasa kijinsia wananchi wa Congo. 

Kimsingi JWTZ haliwezi kupuuzia taarifa hizo, hivyo limeanza kuchukuwa hatua za kiuchunguzi ili kubaini ukweli wa tuhuma hizo ingawa rekodi za majukumu ya ulinzi wa amani zilizokwisha fanywa na JWTZ sehemu mbalimbali zinaonesha kuwa hakukuwa na tuhuma kama hizo.

Kufuatia tuhuma hizo, JWTZ kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa unafanya uchunguzi wa kina ili kujiridhisha na ukweli wake. JWTZ halitasita kuchukua hatua kali kwa watakaobainika katika tuhuma hizo.

JWTZ bado lipo imara na linaendelea kutekeleza majukumu yake nchini Congo kwa kufuata sheria na taratibu za Umoja wa Mataifa.

Imetolewa na Kurugenzi ya Habari na Uhusiano
Makao Makuu ya Jeshi, Upanga
S.L.P 9203, Simu: 0784-477638/0756-716085
Email:ulinzimagazine@yahoo.co.uk
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live




Latest Images