Quantcast
Channel: MPEKUZI
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live

NSSF Yapigwa Marufuku Ujenzi wa Miradi Mipya

$
0
0

Bunge limesimamisha utekelezaji wa miradi yote mipya ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) mpaka hapo Kamati na Wizara itakapopitia taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG), sambamba na kuitisha taarifa za utekelezaji wa miradi yote iliyofanywa na mifuko ya hifadhi ya jamii nchini.

Aidha, imeagiza ukaguzi wa kina wa ujenzi wa jengo jipya la Ofisi za Makamu wa Rais kwa kuangalia usalama wa jengo, hesabu zilizotumika kama zinaendana na thamani ya jengo na kama washauri walitoa ushauri wao ipasavyo.

Akizungumza katika kuhitimisha ukaguzi wa miradi mbalimbali ya serikali iliyofanywa na Kamati ya Katiba na Sheria, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mohamed Mchengerwa alisema NSSF ilitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi ikiwa haijitoshelezi kwa kutoonesha gharama zilizotumika mpaka sasa, bajeti iliyopangwa kutumiwa na kiasi kilichosalia ili kubaini kama fedha zilizotumika zinalingana na thamani ya ujenzi wenyewe.

Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria kwa takribani siku tano kuanzia Machi 29, mwaka huu, ilitembelea Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu na Mahakama.

Akizungumzia taarifa za utekelezaji wa miradi iliyofanywa na mifuko yote ya hifadhi za jamii, Mchegerwa alisema kamati yake inataka kupitia taarifa zote za utekelezaji wa miradi sambamba na kupitia sera ya uwekezaji ili kuangalia kama yamefuata taratibu na hakuna upotoshaji.

“Kwanza kuna madeni makubwa ambayo mifuko hiyo inadai kwa wapangaji wao. Pia tunaangalia sera ya uwekezaji ili kujiridhisha kama ushauri wa kitaalamu uliotolewa unakidhi matakwa ya ujenzi unaoendelea.

Aliongeza: “Kuna majengo mengi yamejengwa hayana wapangaji lakini sera ya uwekezaji itatusaidia kujua kama inafuatwa. Pia itatusaidia kubaini mapungufu yaliyojiri, maana wajumbe wengi wana wasiwasi kuwa huenda ujenzi wa majengo unalenga kwa wahusika kupata asilimia 10 bila kuangalia mahitaji halisi, kwani majengo mengi yako wazi.”

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla aagiza hekta 5,000 zirejeshwe kwa wananchi

$
0
0

Mkuu  wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla ameamuru hekta 5,000 za ardhi zilizokuwa za Chama cha Ushirika cha Luhanga Amcos zirejeshwe kwa wananchi wa kijiji cha Luhanga wilayani Mbarali kutokana na mchakato wa kutoa ardhi hiyo kuwa batili.

Makala alitoa agizo hilo jana mbele ya wakazi wa kijiji cha Luhanga, katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini hapo, huku akimtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbarali, Jeremiah Mahinya kuwachukulia hatua viongozi wa kijiji waliohusika kutoa ardhi hiyo.

“Ardhi hiyo sasa ni ya wananchi kwa kuwa mchakato uliofanyika ni batili na lazima Mkurugenzi uchukue hatua dhidi ya yeyote aliyehusika kwenye mchakato huu. Iwe alighushi mihtasari au alifanya nini lazima achukuliwe hatua”, alisema.

Alisema wanachama wa Luhanga Amcos walikubaliana na kijiji hicho kupewa ekari 800 za ardhi kwa ajili ya shughuli za kilimo na wao kuahidi kuwa watasaidia kutatua tatizo la maji lililokuwa likiwakabili wakazi wa kijiji hicho ambao ni wakulima na wafugaji.

Hata hivyo, ilielezwa kuwa baadaye nyaraka zilibadilishwa na kubainisha kuwa ardhi waliyopewa wawekezaji hao ni hekta 5,000, hatua iliyoleta mkanganyiko na malumbano baina ya wananchi, uongozi wa kijiji na wawekezaji.

Alisema pamoja na malalamiko ya ongezeko kubwa la ardhi pia wawekezaji hao hawakutimiza ahadi ya kupeleka maji hadi sasa wakati wao wameanza kutumia sehemu ya ardhi waliyopora kwa kijiji hicho.

Makalla alisema, kurejeshwa kwa hekta 5,000 za ardhi kwa wananchi kunazingatia vigezo muhimu kikiwemo cha kijiji kutoruhusiwa kuuza au kutoa ardhi inayozidi ekari 50 kwa mtu yeyote sambamba na kutotimizwa kwa ahadi ya kupelekwa maji kijijini hapo.

Alisema kwa sasa serikali inahimiza kila mtu kujituma katika kazi lakini iwapo hakuna maeneo kwa ajili ya shughuli za kilimo vijana watakuwa wanaonewa pale inaposisitizwa kaulimbiu ya Hapa Kazi Tu.

Aliitaja wilaya ya Mbarali kuwa miongoni mwa maeneo yanayoongoza kwa migogoro mingi ya ardhi aliyosema mingine ni ya kujitakia au ile inayotokana na watendaji kutosikiliza wananchi.

Mzazi amlawiti mtoto wa mwaka mmoja na nusu, serikali yatoa tamko

$
0
0

Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imesikitishwa na kukemea vikali tukio la mzazi kumbaka na kumlawiti mtoto wake wa kufikia mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu, kitendo kilichofanywa na John Donald (35) mkazi wa Kiyangu, Manispaa ya Mikindani mkoani Mtwara. 

Tukio hili la kubaka na kulawitiwa ni ukatili wa hali ya juu dhidi ya mtoto maana husababisha maumivu makali ikiwa ni pamoja na kumdhuru mtoto kimwili, kisaikolojia, kijamii na kihisia. 

Aidha, vitendo hivi, vinaacha kovu la kudumu kimwilini, kiakili, kimaadili, kijamii, ulemavu, maumivu, na wakati mwingine husababisha kifo; jambo ambalo linahitaji ulinzi thabiti katika kuhakikisha watoto wanaishi mazingira salama na rafiki. 

Ukatili aliofanyiwa mtoto eneo la Kinyangu, manispaa ya Mikindani, ni ukiukwaji mkubwa wa haki za mtoto ambao huchangia kurudisha nyuma ustawi na maendeleo ya Mtoto na ni kinyume cha Sheria ya Mtoto Na. 21 ya mwaka 2009.

Wizara inatoa pongezi kwa Jeshi la Polisi mkoani Mtwara kwa kumkamata mtuhumiwa na kumfikisha mahakamani ili hatua za kisheria zichukuliwe. 

Vile vile, Wizara inaipongeza Mahakama ya Wilaya ya Ilala, mkoani Dar es salaam dhidi ya  Omary hamisi (25), mkazi wa Gongo la Mboto, Dar es salaam, ya kutumikia kifungo cha maisha jela, baada ya kupatikana na hatia ya kumlawiti mtoto wa miaka tisa mwenye ulemavu wa kusikia na kuongea. 

Uamuzi huu ni kielelezo kuwa, wananchi wakitoa ushahidi wa matukio ya ukatili dhidi ya watoto, watuhumiwa watachukuliwa hatua kali ili kuwa fundisho kwa wananchi wanaowanyanysa watoto.

Wizara inamwelekeza Afisa Ustawi wa Jamii na Afisa Maendeleo ya Jamii wa Mkoa wa Mtwara kuwasiliana na wadau wengine katika ngazi zote kuhakikisha mama na mtoto wanapata huduma ya afya na  ushauri na kufuatilia mwenendo wa shauri hili. 

Imetolewa na

Erasto Ching’oro
Msemaji wa Wizara
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

Afungwa Kifungo cha Maisha Jela Kwa Kumlawiti Mtoto Mlemavu wa kusikia na kuongea.

$
0
0

Mkazi wa Gongo la Mboto, Omary Hamis (25) amehukumiwa kifungo cha maisha jela baada ya kupatikana na hatia ya kumlawiti mtoto wa miaka tisa ambaye ni mlemavu wa kusikia na kuongea.

Hakimu Mkazi, Flora Haule wa Mahakama ya Wilaya ya Ilala, alisema mahakama imeridhishwa na ushahidi wa mashahidi tisa ukiwamo wa daktari na fomu namba tatu ya polisi (PF3), iliyotolewa mahakamani hapo kama kielelezo dhidi ya mshtakiwa huyo.

“Mahakama imekukuta na hatia hivyo inakuhukumu kifungo cha maisha jela, baada ya kupatikana na kosa la kumlawiti mvulana wa miaka tisa ambaye ni mlemavu wa kusikia na kuzungumza, ili iwe fundisho kwa jamii,” alisema hakimu Haule.

Katika ushahidi uliotolewa mahakamani hapo, ilidaiwa kuwa mtoto huyo siku ya tukio alifika kwenye banda la kuonyeshea video ambalo linamilikiwa na Hamisi saa za jioni, kwa ajili ya kuangalia video, lakini Hamis alimfukuza kutokana na kutokuwa na pesa ya kiingilio.

Baada ya kumfukuza mtoto huyo aliondoka, lakini baadaye alirudi bila ya Hamis kuwa na taarifa akakaa ndani ya banda na kisha kupitiwa na usingizi uliosababisha abaki kwenye banda hilo peke yake hadi usiku.

Hamis alitumia mwanya huo kumlawiti mtoto huyo kwenye jumba bovu lililopo jirani na ofisi yake hiyo.

Mashahidi waliieleza mahakama kuwa walisikia sauti ya mtu ambayo ilikuwa haisikiki vizuri akiomba msaada, ndipo waliposogea na kumkuta Hamis akitekeleza kitendi hicho huku akijua kuwa ni kosa kisheria.

Mashahidi walidai hata walipomkaribia, Hamis aliendelea kutekeleza kitendo hicho hadi walipolazimika kumpiga mateke. Hamis alikiri kuwa siku hiyo watoto walifika kwenye banda lake hilo.

Wakili wa Serikali, Ester Kyara aliiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali kwa mtuhumiwa ili iwe fundisho kwa wote wanaotumia mabanda ya kuonyesha video kufanya ukatili kwa watoto.

Katika utetezi wake, Hamisi alisema ana familia inayomtegemea hivyo apunguziwe adhabu, maombi ambayo yalitupiliwa mbali na mahakama hiyo na kuhukumiwa kifungo cha maisha jela.

Hamisi anadaiwa kutenda kosa hilo Agost 26, 2014 eneo la Gongo la Mboto.

Jeshi la Polisi lapewa siku 7 Liwe Limepeleka Mikataba Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC)

$
0
0

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imelipa siku saba kuanzia jana Jeshi la Polisi nchini kupeleka mkataba walioingia baina yao na Kampuni ya Lugumi, iliyopewa zabuni ya kufunga mashine za kuchukua alama za vidole kwenye vituo vya Polisi vya wilaya nchi nzima.

Hadi sasa kampuni hiyo imeshalipwa asilimia 99 ya fedha, ilihali vituo vilivyofunga mashine hizo ni 14 kati ya 108.

Maagizo ya kamati hiyo yaliyotolewa jana Dar es Salaam na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Aeshi Hilal wakati kamati hiyo ilipokutana na Jeshi hilo kupitia taarifa ya hesabu zao za mwaka 2013/14 zilizokaguliwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Aeshi alisema jeshi hilo mwaka 2011 liliingia mkataba na Kampuni ya Lugumi Enterprises kwa ajili ya kufunga mashine za kuchukua alama za vidole katika vituo vya Polisi vya wilaya nchi nzima ambavyo viko 108.

Alisema mkataba huo ulikuwa wa Sh bilioni 37 pamoja na kodi na kwamba hadi sasa kampuni hiyo imeshapewa asilimia 99 ya fedha zote ili hali vituo vilivyofungwa mashine hizo ni 14 tu, kati ya vituo vyote 108.

“Ukiangalia kazi iliyofanywa tangu mwaka 2011 hadi leo ni kidogo na pesa hawa kampuni wameshachukua asilimia 99, sasa tumewaagiza watuletee huo mkataba ndani ya wiki moja walioingia na kampuni hiyo ili tuupitie,” alisema Aeshi.

Kuhusu mali zinazokamatwa na polisi kwenye matukio mbalimbali nchini yakiwemo ya wizi, Kamati imewaagiza CAG, Polisi na Mhakiki Mali wa Serikali kufanya ukaguzi wa mali zote zinazokamatwa na polisi ili kuzifahamu kuzipa thamani halisi kulingana na idadi yake.

Alisema hivi sasa mali zinazokamatwa na polisi hazifanyiwi uhakiki kujua idadi na thamani yake hivyo nyingi zinapotea bila kujua zilipokwenda na nyingine ambazo kesi zake zimeisha, zinauzwa kwa bei ndogo kuliko thamani halisi.

Kuhusu maduka ya bidhaa ya majeshi nchini, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limeiomba serikali idhini ya ukaguzi na utoaji mizigo ya maduka ya jeshi bandarini ufanywe na jeshi hilo badala ya utaratibu wa sasa ambao mzabuni ndiye anayesimamia jambo hilo.

Akizungumzia hilo, Aeshi alisema maombi hayo ya jeshi yalitolewa wakati kamati hiyo ilipokutana na JWTZ juzi na kuomba ukaguzi wa bidhaa zinazoagizwa kwa ajili ya maduka yao zifanyiwe ukaguzi na wao kwani inawezekana bidhaa zinazoingizwa zikawa nyingi au zikachanganywa na vitu vingine kwa kuwa wao hawana dhamana ya kukagua.

Kwa upande wake, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali Ernest Mangu alisema jeshi hilo linakabiliwa na changamoto mbalimbali kama vile uhaba wa nyumba na kwamba mikakati yao hivi sasa ni kufanya mabadiliko na kulifanya jeshi hilo liwe la kisasa zaidi.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ateketea kwa Moto Akiwa Ndani ya Gari Lake

$
0
0

Mhadhiri  wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Idara ya Sayansi na Uhandisi wa Kompyuta (CoICT), Dk Richard Mgaya amefariki baada ya kuteketea ndani ya gari lake jijini Dar es Salaam juzi.

Gari la Dk Mgaya liliteketea baada ya kugongana na lori katika eneo la Mbezi Africana, Wilaya ya Kinondoni usiku wa kuamkia juzi na kuwaka moto uliosababisha kifo chake.

Juzi picha mbalimbali zilisambaa zikionesha gari aina ya Toyota Prado lililopata ajali eneo hilo la Africana baada ya kugongana na lori, baadaye ilibainika kuwa aliyekuwa katika gari hilo ni Dk Mgaya.

Akizungumza  kwa njia ya simu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Christopher Fuime alisema gari la Dk Mgaya liliteketea na hata kushindwa kujulikana dereva wa gari hilo.

Alisema baadaye ndugu wa marehemu ndio walithibitisha kuwa gari hilo lililoteketea na dereva aliyekuwemo ni Dk Mgaya ambaye hata hivyo naye aliteketea ndani ya gari hilo.

“Lile gari liliungua na hakuna kitu kilichopatikana, hata wakati polisi wanafika eneo la tukio walikuta tayari dereva amekuwa majivu kutokana na kuteketea kwa moto… labda baada ya kupima vinasaba ndio itathibitika kama ilikuwa ni yeye,” alisema Kamanda Fuime.

Alisema hata gari hilo hawakuweza kulitambua mara moja na baada ya kufuatilia Mamlaka ya Mapato (TRA) ilibainika kuwa mmiliki wake ni Dk Mgaya.

Alisema “ndugu wa marehemu ndio wamesema kuwa ni ndugu yao.” 

Dk Mgaya alijiunga na idara hiyo miaka kadhaa iliyopita akitokea masomoni nchini Marekani na alikuwa ni mtaalamu wa artificial intelligence.

Mishahara ya vigogo wa Serikali Waliokuwa Wanalipwa Milioni 36 hadi milioni 40 kwa mwezi yaanza kufyekwa

$
0
0

Siku chache baada ya Rais Dk. John Magufuli kutoa agizo la kupunguza mishahara mikubwa ya watendaji wa mashirika ya umma, hatimaye Serikali kupitia Bodi ya Mishahara imeanza kazi ya kufanya marekebisho hayo.

Hatua hiyo imekuja baada ya Rais Magufuli, kuagiza kushushwa kwa viwango vya mishahara ya viongozi wa mashirika ya umma ambapo wengine hulipwa Sh milioni 36 hadi milioni 40 kwa mwezi.

Jana  Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki, alisema katika kipindi cha miezi 15 kuanzia sasa mishahara ya watumishi hao itapunguzwa na kuwa yenye uwiano.

“Katika kuhakikisha agizo hilo linatekelezwa tunayo Bodi ya Mishahara ambayo ilianzishwa katika Serikali ya awamu ya nne na jukumu lake kubwa ni kufanya mapitio ya mishahara mbalimbali na kuhakikisha mishahara ya watumishi wa umma haipishani sana.

“Hatua ambazo tumeanza kuzitekeleza, tayari mamlaka zetu zimeanza kukutana kupitia Utumishi, Hazina na Msajili wa Hazina ili kuangalia namna ya kulitekeleza agizo hilo,” alisema Waziri Kairuki.

Alisema kutokana na hali hiyo mamlaka hizo hivi sasa zinaangalia mishahara ya taasisi mbalimbali na watumishi ili kuweza kubaini wale wanaolipwa zaidi ya Sh milioni 15 ni wangapi na itakatwa vipi.

Akizungumzia taasisi zinazozalisha kwa kiwango kikubwa na kuwa na uwezo wa kujiendesha, Waziri Kairuki, alisema Bodi ya Mishahara hivi sasa ina jukumu la kuangalia uwiano baina ya mtumishi wa umma na mashirika ya Serikali.

“Unakuta mtumishi wa taasisi X kiwango chake cha elimu, uzoefu, ujuzi, muda wa kuingia kazini pamoja na kazi anayoifanya ni sawa na ya mtumishi wa taasisi Y lakini unakuta mtumishi X analipwa mshahara mkubwa zaidi ya mara tano ya mtumishi Y jambo ambalo si haki katika utumishi,” alisema.

Kauli ya Rais Magufuli
Machi 30, mwaka huu akiwa wilayani Chato, Mkuu huyo wa nchi, alisema kuna watu wanalipwa kiwango kikubwa cha mishahara na wamekuwa wakiishi kuliko hata malaika na sasa ni lazima washushwe ili waishi kama shetani.

Hatua ya Rais Magufuli, kupitisha panga na kuweka uwiano wa mishahara kwa watendaji wa taasisi hizo unaelezwa kuwa utaisaidia uwajibikaji na usawa kwa watendaji.

Katika mkutano huo, Rais Magufuli, alishangazwa na baadhi ya bodi za wakurugenzi kushindwa kufanyakazi zao kwa mujibu wa sheria na badala yake wamekuwa na kazi ya kupandisha mishahara kwa watendaji.

Alisema anashangazwa na bodi hizo, kwani kila kukicha zimekuwa zikifanya kazi ya kupandisha mishahara pamoja na kufanya vikao nje ya nchi.

Alisema hivi sasa ameunda timu ya wataalamu ambayo imeanza kufanya kazi ya upunguzaji mishahara mikubwa kwa watendaji wakuu wa mashirika ya umma.

“Tena hawa wakurugenzi ndio wanaongoza kwa kulipwa fedha nyingi na hata kwenda kufanya vikao ulaya. Ninasema hapa kwamba suala hili litaanza kushughulikiwa katika bajeti hivi karibuni,” alisema Rais Magufuli.

Alisema tayari ameunda timu ya wataalamu ambayo inafanya kazi ya kupunguza mishahara hiyo na kufikia Sh milioni 15 kwa mwezi ili asipatikane Mtanzania anayelipwa zaidi ya kiwango hicho.

“Kuna watu wanaishi kuliko hata malaika lazima tuwashushe waishi kama shetani,” alisema Rais Magufuli.

Dr. Shein: Upinzani haujakidhi vigezo vya kutoa Makamu wa Rais

$
0
0

Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein amesema hakuna chama kilichokidhi matakwa ya kikatiba kutoa makamu wa kwanza wa Rais.

Rais Shein aliyasema hayo jana alipokuwa akizungumza na Baraza la Wawakilishi visiwani Zanzibar kwa mara ya kwanza tangu kuchaguliwa kwake kwa mara ya pili kuongoza Umma wa Wazanzibar.

''Hakuna Chama chama kinachokidhi kutoa makamu wa kwanza wa Rais huo ni uamuzi wa wananchi na ni uamuzi wa kidemokrasia unaostahili kuheshimiwa ''Alisema Rais Shein.

Aidha Rais Shein katika hotuba yake kwa Baraza hipo pamoja na wananchi wa Zanzibar aliahidi kuhakikisha Zanzibar inasonga mbele kimaendeleo kwa kujenga viwanda maeneo mbalimbali na kuboresha huduma za kijamii pamoja na kupandisha mishahara hadi kufikia shilingi laki 3 kwa kima cha chini.

Pia Rais Shein alisema ataongoza Zanzibar kwa haki na watu wote ni lazima wafahamu kwamba yeye ndiye Rais ambaye alichaguliwa kwa asilimia 91.4 hivyo uchaguzi haupo tena hadi mwaka 2020.

Hatimaye Utumishi Wafafanua Kuhusu Mshahara wa Rais Magufuli na Kikwete

$
0
0
Siku chache baada ya Rais Dk. John Magufuli, kutaja mshahara wake kuwa ni Sh. milioni 9.5 kwa mwezi, Wizara ya Ofisi ya Rais, Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, imefafanua mshahara aliokuwa anapokea Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, kuwa unalingana na wa kiongozi huyo.

Katibu Mkuu Utumishi, Dk. Laurean Ndumbaro jana  alisema Kikwete aliondoka madarakani akiwa anapokea Sh. milioni 9.5, ikiwa ni kiwango sawa na cha Rais Magufuli.

“Hadi Kikwete anaondoka madarakani, mshahara wake kwa mwezi ulikuwa Sh. milioni 9.5, siyo kweli kuwa alikuwa akipokea Sh. milioni 34 kama ilivyowahi kuelezwa kwenye baadhi ya vyombo vya habari,” alisema.

Mwishoni mwa wiki akiwa kwenye mapumziko nyumbani kwake Wilaya ya Chato mkoani Geita, Rais Magufuli alitaja mshahara wake, huku akiahidi kuweka hadharani stakabadhi za mshahara (salary slip) atakaporudi Dar es Salaam.

Rais alilazimika kufanya hivyo kufuatia Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), kumpa changamoto ya kutaja mshahara wake, baada ya kueleza nia ya serikali yake kupunguza mishahara ya watumishi wa mashirika na taasisi zake kutoka Sh. milioni 40 hadi milioni 15.

Iwapo Rais mstaafu Kikwete, alikuwa analipwa kiasi hicho, kwa mujibu wa sheria, kwa sasa analipwa asilimia 80 ya mshahara huo ambayo ni Sh. milioni 7.6 ya mshahara wa Rais aliyeko madarakani.

Hivi karibuni, baadhi ya vyombo vya habari vilinukuu taarifa iliyotolewa Julai, mwaka jana na mtandao wa Africa Review ulioandika kuwa Rais Kikwete wakati akiwa madarakani alikuwa akishika nafasi ya tano miongoni mwa marais 38 wa Afrika kwa kulipwa mshahara mnono wa Dola 16,000 za Marekani (sawa na Sh. milioni 34 wakati huo).

Taarifa hizo zilikanushwa vikali na Ikulu, lakini hakukuwa na ufafanuzi wa mshahara halisi anaopokea Rais kwa wakati huo.

Kwa mujibu wa Katiba ibara ya 43 (1), Rais atalipwa mshahara na malipo mengineyo na atakapostaafu, atapokea malipo ya uzeeni, kiinua mgongo, posho, kadiri itakavyoamuliwa na Bunge na mshahara, malipo hayo mengineyo, malipo ya uzeeni na kiinua mgongo hicho, vyote vitatokana na Mfuko Mkuu wa Hazina ya serikali na vitatolewa kwa mujibu wa masharti ya ibara hiyo.

Ibara ndogo ya pili inasema mshahara na malipo mengineyo yote ya Rais havitapunguzwa wakati Rais atakapokuwa bado ameshika madaraka yake kwa mujibu wa masharti ya Katiba.

Rais Magufuli Na Rais Wa Rwanda Paul Kagame Wazindua Rasmi Daraja La Kimataifa La Rusumo Na Kituo Cha Huduma

$
0
0

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amefanya ziara yake ya kwanza nje ya nchi leo tarehe 06 April, 2016 kwa kutembelea nchi jirani ya Rwanda, ambapo yeye na Mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Rwanda Mheshimiwa Paul Kagame wamefungua Kituo cha Pamoja cha Utoaji wa Huduma za Mpakani (One Stop Border Post) na Daraja la Kimataifa la Mto Rusumo katika Mpaka wa Tanzania na Rwanda. 

Rais Magufuli ambaye ameongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli, ameingia nchini Rwanda kwa usafiri wa magari akitokea nyumbani kwake Lubambangwe, katika kijiji cha Mlimani, Wilaya ya Chato Mkoani Geita ambako alikuwa mapumziko tangu tarehe 29 Machi, 2016. 

Katika eneo la Rusumo, Rais Magufuli na Rais Kagame kwanza wamefungua majengo ya Kituo cha Pamoja cha Utoaji wa Huduma za Mpakani kilichopo upande wa Tanzania, kisha wakafungua daraja la mto Rusumo, na baadaye wakafungua Majengo ya Kituo cha Pamoja cha Utoaji wa Huduma za Mpakani kilichopo upande wa Rwanda.

Mradi huu wa ujenzi wa Kituo cha Pamoja cha utoaji wa Huduma za Mpakani cha Rusumo, umehusisha ujenzi wa majengo ya mamlaka ya Mapato katika pande zote mbili na daraja lenye urefu wa mita 80 na upana wa mita 9.5, na umegharimu shilingi Bilioni 61.4 zilizotolewa kwa ufadhili wa serikali ya Japan kupitia shirika lake la JICA. 

Akizungumza katika sherehe ya ufunguzi wa mradi huo Rais Magufuli ameishukuru Japan kwa kutoa fedha za kuwezesha utekelezaji wa mradi huo na ametoa wito kwa wafanyabiashara wa Rwanda kupitisha mizigo yao Tanzania kupitia mpaka huo, pamoja na kuitumia bandari ya Dar es salaam. 

Dkt. Magufuli amewasihi wananchi wa Rwanda na wanajumuiya ya Afrika Mashariki kwa ujumla, kushirikiana kibiashara kwa kutumia fursa zilizopo huku akibainisha kuwa Tanzania imeanza juhudi za kuimarisha miundombinu yake ya barabara na kujenga reli ya kati, ambayo tayari washirika 13 wameonesha nia ya kufanikisha ujenzi huo. 

Aidha, Rais Magufuli amewaonya maafisa forodha na vituo vya ukaguzi kuacha mara moja tabia ya ucheleweshaji wa upitishaji wa mizigo, na amesema serikali imeshaamua kuwa barabara ya Rusumo hadi Dar es salaam itakuwa na vituo vitatu ambavyo ni Rusahunga, Singida na Vigwaza ili magari yatumie muda wa siku 3 badala ya kutumia siku zaidi ya 10, 

Kwa upande wake Rais Paul Kagame wa Rwanda ambaye ameongozana na mkewe Mama Janeth Kagame, pamoja na kuishukuru Japan kwa kufadhili mradi huo amesema Tanzania na Rwanda zina kila sababu ya kushirikiana kiuchumi na ameongeza kuwa ni matumaini yake kujengwa kituo hicho kutaongeza biashara na idadi ya watu wanaovuka daraja kutoka 2,000 wa sasa hadi watu zaidi ya 15,000 kwa siku. 

Akiwa Rwanda Rais, Magufuli amefanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais Paul Kagame na hapo Kesho Rais Magufuli atashiriki maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 22 ya mauaji wa Kimbari yaliyotokea mwaka 1994 ambapo watu takribani milioni 1,000,000 waliuawa.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Kigali
06 April, 2016
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Rais wa Rwanda Mhe. Paul Kagame wakikata utepe kwa pamoja kuashiria uzinduzi rasmi wa daraja la kimataifa la Rusumo na Kituo cha Huduma kwa Pamoja Mpakani (OSBP) cha Rusumo. Tukio hilo limehudhuriwa na viongozi wa ngazi za juu serkalini kutoka Nchi zote mbili, Mabalozi, na Viongozi wa Taasisi mbambali za Kitaifa na Kimataifa.

Ujenzi wa Daraja la Kimataifa la Rusumo na Kituo cha huduma Pamoja Mpakani Rusumo ni moja ya miradi inayotekelezwa kwa msaada kutoka Serikali ya Japan kwa Nchi za Tanzania na Rwanda kupitia shirika lake la maendeleo la JICA. 

Mradi huu kwa upande wa Tanzania umegharimu takribani kiasi cha TShs. 33,206,508,072.07 hadi kukamilika. Miradi mingine inayotekelezwa kwa kushirikiana na Serikali ya Japan kupitia JICA ni pamoja na ujenzi wa Barabara ya Arusha – Namanga, Iringa – Dodoma, Namtumbo – Kilimasera – Matemanga – Tunduru pamoja na barabara ya Masasi - Mangaka. 
 Muonekano wa sehemu ya Daraja hilo la Rusumo
 Jiwe la msingi lililowekwa baada ya uzinduzi wa daraja hilo
  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Rais wa Rwanda Mhe. Paul Kagame wakipita kwenye Daraja hilo la Rusumo mara baada ya uzinduzi
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Rais wa Rwanda Mhe. Paul Kagame wakikata utepe kwa pamoja kuashiria uzinduzi  wa Kituo cha Huduma kwa Pamoja Mpakani (OSBP) cha Rusumo. Tukio hilo limehudhuriwa na viongozi wa ngazi za juu serkalini kutoka Nchi zote mbili, Mabalozi, na Viongozi wa Taasisi mbambali za Kitaifa na Kimataifa.
 Picha ya pamoja mara baada ya uzinduzi wa huo

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Felix Ntibenda Apiga Marufuku kilevi aina ya Kiroba

$
0
0

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Felix Ntibenda amepiga marufuku uuzwaji wa kilevi aina ya kiroba katika mkoa huo.

Alisema uamuzi huo unatokana na vijana ambao ni nguvu kazi ya taifa kushindwa kufanya kazi na kulewa wakati wa kazi.

Aidha mkuu huyo wa mkoa alisema anafanyia kazi sakata la mkazi wa Kata ya Ngarenaro anayedaiwa kujihusisha na uuzaji na uingizaji wa dawa za kulevya ambaye baada ya kukamatwa na polisi aliachiwa katika mazingira ya kutatanisha.

Ntibenda alisema hayo jana Arusha wakati akizungumza na watendaji wa serikali za mitaa 154, maofisa watendaji kata 25 pamoja na wenyeviti wa serikali za mitaa. 

Alisema suala la kilevi aina ya kiroba ni kero kwa vijana kufanya kazi wakiwa wamelewa au kuwa navyo mifukoni hasa madereva wa pikipiki, daladala na wapiga debe.

Alisema kutokana na vijana kunywa kinywaji hicho nyakati za kazi, amepiga marufuku uuzwaji wa kilevi hicho, atakayekiuka agizo hilo hatua za kisheria zitachukuliwa.

“Sitaki kuona viroba vikiuzwa katika Mkoa wa Arusha na atakayekiuka nitamchukulia hatua za kisheria, lakini huyu anayeuza dawa za kulevya halafu polisi wanamwachia na wananchi hawajui kwanini anaachiwa huku akiendelea kuuza dawa, sasa nasema mwisho wake umefika, nitafuatilia kwa makini suala hili.”

Baadhi ya wenyeviti wa serikali za mitaa walihoji sababu za kutokuwa na ofisi za kufanyia kazi badala yake wanalazimika kutumia nyumba zao au kukodisha ofisi ili kufanya kazi za jamii lakini pia hawana posho za vikao.

Wenyeviti hao akiwemo Amani Mwakalinga wa mtaa wa Darajani na Hilary Mkonyi wa mtaa wa Ngarenaro, walisema awali Mkurugenzi wa Jiji, Juma Idd aliahidi kuwajengea ofisi lakini hadi sasa hakuna utekelezaji.

Serikali yadhamiria kurejesha heshima ya wazee nchini

$
0
0

SERIKALI imesema imedhamiria kurejesha heshima ya wazee wote hapa nchini kwa kuisimamia jamii kuwathamini wazee na kuwapa kipaumbele katika huduma zote za jamii.

Tamko hilo limetolewa na Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu mjini Morogoro wakati wa uzinduzi wa kampeni ya Mzee Kwanza inayolenga kuwapa kipaumbele wazee katika huduma zote za kijamii. 

“Nataka heshima ya wazee irudi...wapate huduma kwa kupewa heshima yao, ifike mahali mzee anapofika sehemu yoyote akihitaji huduma apewe kipaumbele, ni lazima tuwape heshima yao kwa sababu wameifanyia nchi mambo makubwa wakati wa ujana wao,” alisema Waziri.

Alisema kuwa wazee katika jamii yoyote wana nafasi kubwa katika ujenzi wa taifa kwa kuwa wao ni hazina ya busara, hekima, amani na utulivu wa jamii yoyote. 

“Familia isiyoheshimu wazee aghalabu itakuwa na vurugu na ugomvi kila kukicha. Lakini jamii au familia inayoenzi wazee na kuwapa nafasi zao katika kushauri, kukosoa na kuelekeza utendaji wa siku hadi siku, jamii au familia hiyo itakuwa na baraka siku zote hivyo nikiwa Waziri mwenye dhamana nitahakikisha hili linawezekana,” alisema Waziri Ummy.

Alisema kuwa Serikali imeona ni vyema kurejea kwenye desturi hii kwa kuanzisha kampeni maalumu ya Mzee Kwanza ambaypo ni wajibu wa kila Mtanzania kuona kuwa anafanya kila awezalo kurejesha hadhi ya wazee na kuwapa umuhimu wa kwanza katika kupata huduma za kijamii.

Waziri Ummy alisema kuwa takwimu za sensa za mwaka 2012 zinaonesha kuna jumla ya wazee 2,507,568 wenye miaka kati ya 60 na kuendelea huku kukiwa na wazee takriban 474,053 wenye miaka 80 na kuendelea.

Alisema kuwa ili kuhakikisha wazee wanakuwa kwenye mazingira mazuri, Serikali kupitia Wizara ya Afya imeandaa Muswaada wa kutungwa kwa Sheria ya Wazee ambayo itapelekwa Bungeni ili ipitishwe kuwa Sheria ambayo itasimamia upatikanaji wa haki na ustawi wa wazee Sheria hii itatoa ahueni kubwa kwa wazee na kuboresha sana maisha yao ya uzeeni.

Aidha alisema kuwa Serikali imeagiza kila halmashauri kubaini wazee walio katika maeneo yao na kuhakikisha wanapata huduma zote za msingi ikiwa ni pamoja na huduma za afya kutoka kwenye mapato yao wenyewe.

Akizungumzia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya aliupongeza kwa mwitikio waliochukua kushirikiana na Wizara katika Uzinduzi wa kampeni ya Mzee Kwanza katika huduma kwa nchi yetu.

“Najua hamasa hii wameipata kutokana na ukweli kwamba Mfuko huu unawahudumia wanachama wastaafu ambao nao wako katika kundi hili la wazee, nawapongeza NHIF kwa hatua mliyochukua ya kufanya mkutano na wanachama wenu wastaafu wiki chache zilizopita,” alisema.

Katibu Mkuu Kiongozi awaasa Wakuu wa Mashirika na Taasisi za Umma kuzingatia Maadili ya Viongozi wa Umma

$
0
0

Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Mhandisi John William Kijazi amewaasa Wakuu wa Mashirika na Taasisi za Umma kuzingatia Maadili ya Viongozi wa Umma katika kutekeleza makujumu yao.

Katibu Mkuu alisema hayo jana jijini Dar es salaam wakati wa akifungua mafunzo ya viongozi hao yalioandaliwa na Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ili kuhakikisha wanaendana Uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Mgufuli.

“Maadili yana umuhimu wake mkubwa katika utawala wa maendeleo ya nchi, kupitia maadili mema wananchi wanajenga imani na viongozi pamoja na Serikali yao kwa ujumla” alisema  Balozi Mhandisi Kijazi.

Ili kuhakikisha mafunzo yanakuwa yenye tija, Balozi Mhandisi Kijazi amewasisitiza viongozi hao kutumia muda vizuri na kujikumbusha na kujifunza maadili hayo kwa manufaa ya mashirika na taasisi zao pamoja na taifa kwa ujumla.

Balozi Mhandisi Kijazi alitaja umuhimu wa maadili katika jamii na kusema kuwa yanasaidia kusimamia rasilimali za umma na kuzitumia kwa maslahi ya wote, kuongeza tija na thamani ya huduma, zinazotolewa na Serikali, kudhibiti mianya ya ukiukwaji wa  maadili na vitendo vya rushwa, kujenga ujasiri wa kusimamia Sheria, Kanuni na Taratibu za utumishi wa umma.

Maadili pia yanasaidia wananchi, viongozi na Watumishi wa Umma kutoa mchango wa haraka katika kutekeleza maendeleo ya nchi, kuepuka utata wa maamuzi ya migongano ya kimaslahi, kuwavutia wawekezaji, kujenga na kudumisha amani na utulivu pamoja na kuondoa na kukomesha ubinafsi kwa viongozi.

Aidha, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi  Kijazi alisema kuwa ukiukwaji wa maadili unaathari hasi kwa taifa ambapo alizitaja baadhi ya athari hizo kuwa ni rasilimali za nchi kunufaisha wachache, wananchi kukosa haki zao za msingi kutokana na rushwa na upendeleo, viongozi wa umma kujilimbikizia mali isivyostahili bila kujali hali za wananchi wanaowaongoza, kupungua kasi ya uwekezaji pamoja na kudhohofika kwa uchumi wa nchi.

Madhara mengine ya kutojali maadili ni wananchi kukosa imani na Serikali yao, kuchochea vurugu pamoja na wananchi kutotii sheria za nchi na hivyo kuhatarisha usalama, amani na utulivu wa nchi.
 
Kwa upande wake Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Jaji Mstaafu Salome Kaganda alipokuwa maelezo mafupi kwa Mgeni Rasmi alisema kuwa misingi ya maadili na maadili yanalenga katika kuzuia mgongano wa maslahi, upendeleo, matumizi mabaya ya rasilimali za umma na taarifa za ofisi na mwenendo usiofaa kwa viongozi wa umma ili kuimarisha na kuendeleza dhana za uadilifu, uwajibikaji na uwazi  ambazo ni sifa muhimu za kiongozi.

Ili kuongeza ufanisi katika utendaji kazi, Jaji Mstaafu Kaganda alisema kuwa ofisi yake inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu wa watumishi ambapo kuna zaidi ya viongozi 15,000 huku Sekretarieti ina wafanyakazi 200 nchi nzima.

 Mafunzo hayo yalihudhuriwa na washiriki 40 ambapo yalifanyika kwa Mawaziri, Manaibu Waziri, Mkatibu Wakuu, Manaibu Katibu Wakuu, Wenza wa Viongozi, Wakuu wa Mikoa.

Mtoto wa Miaka saba Ajinyonga kwa kamba

$
0
0

Mtoto George Elias (7) amekutwa amekufa kwa kujinyonga kwa kamba ya katani katika Kijiji cha Buganzu, Kata ya Uyovu wilayani Bukombe, Mkoa wa Geita, tukio linalodaiwa kusababishwa na michezo ya kitoto.

Baba wa mtoto huyo, Elias Martin alisema mwanawe alikuwa anasoma darasa la awali katika shule ya msingi ya kijiji hicho na siku ya tukio alikwenda kucheza na watoto wenzake.

Martin alisema akiwa nyumbani kwake akipata chakula cha mchana na wageni waliokwenda kumtembelea, walifika watoto watatu wa jirani yake wakidai mtoto wake ananing’inia juu ya mti.

Alisema baada ya kupokea taarifa hiyo aliambatana na wageni wake mpaka eneo la tukio na kumkuta mtoto huyo akining’inia kwenye mti uliopo pembeni ya nyumba yake.

Mzazi huyo alisema chanzo cha tukio hilo ni michezo ya watoto na huenda alidanganywa na wenzake kuweka shingo kwenye kamba walipokuwa wakicheza.

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Matayo Paschal alisema kuwa alipokea taarifa ya kifo hicho na kulijulisha Jeshi la Polisi.

Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Mpojoli Mwabulambo alisema wamefungua jalada la uchunguzi kuhusu tukio hilo, lengo likiwa kujua chanzo cha kifo hicho.

Mbunge wa Zamani na Moshi Vijijini (CCM) Apandishwa Kizimbani

$
0
0

Kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Thomas Ngawaiya amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akikabiliwa na shtaka la kujenga hoteli kwa kutumia makandarasi wasiosajiliwa.

Ngawaiya ambaye aliwahi kuwa Mbunge wa Moshi Vijijini na pia Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Kilimanjaro, alipandishwa kizimbani jana na kusomewa shtaka hilo, siku moja baada ya kutiwa mbaroni na Polisi Kinondoni.

Kabla ya kumsomea shtaka, Mwendesha Mashtaka kutoka Bodi ya Usajili wa Makandarasi (ERB), Saddy Kambona alisema Ngawaiya amefikishwa mahakamani hapo kwa kukaidi amri ya Mahakama.

Pia, Wakili Kambona alimsomea mshtakiwa huyo shtaka linalomkabili, lakini Ngawaiya alikana na kuachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti.

Wakili Kambona alidai kuwa Machi 24, 2015 majira ya mchana, mshtakiwa alitenda kosa la kuagiza ujenzi wa jengo la hoteli, kwa watu ambao hawajasajiliwa na Bodi ya Usajili wa Makandarasi.

Alidai kuwa jengo hilo lipo Kiwanja Namba 32, makutano ya mitaa wa Dosi na Wazani, eneo la Magomeni Mapipa, Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Aliendelea kudai kuwa mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo kinyume cha kifungu namba 22 cha Sheria ya Bodi Usajili wa Makandarasi, Namba 17 ya Mwaka 1997.

Akitoa ufafanuzi nje ya Mahakama, Wakili Kambona alibainisha kuwa sheria hiyo inamtaka kila anayejenga jengo ambalo ni kwa matumizi ya umma lazima atumie makandarasi waliosajiliwa na ERB.

Baada ya kusomewa shtaka hilo, kisha kuulizwa na Hakimu Hellen Liwa iwapo ni kweli au la, Ngawaiya alianza kujitetea.

Hakimu Liwa alimzuia na kumtaka ajibu shtaka kabla ya Wakili wake, Desidery Ndibalema kuingilia kati na kumuelekeza kwa kumnong’oneza cha kufanya, ndipo akakanusha shtaka.

Wakili Kambona baada ya kumsomea mshtakiwa shtaka hilo, alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo unaendelea na kuomba Mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa. Hakimu Liwa aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili, 11.

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Alhamisi ya April 7

Hamad Rashid: Serikali ya Muungano isibabaishwe na wahisani

$
0
0

Mjumbe wa Kuteuliwa wa Baraza la Wawakilishi, Hamad Rashid (ADC) ametaka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutobabaishwa na nchi washirika wa maendeleo kwa kususa misaada yao kwa kile alichosema, nafasi ipo ya kutumia rasilimali ziliopo kikamilifu.

Rashid, ambaye alikuwa mgombea wa nafasi ya urais wa Zanzibar kwa tiketi ya ADC katika uchaguzi wa marudio, alisema hayo wakati akichangia hotuba ya rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein aliyoitoa katika uzinduzi wa baraza la wawakilishi.

Mwakilishi huyo alionya nchi hizo akitaka zisitumie uwezo wao kwa ajili ya kulazimisha matakwa yao na kupinda sheria za nchi zinazotokana na demokrasia iliopo.

Alisema Tanzania bado inao uwezo mkubwa wa kutumia rasilimali zake zinazotokana na utajiri mkubwa kwa ajili ya kujenga nchi na kupambana na umasikini lakini viongozi walikuwa wakibweteka kutokana na kuwepo kwa misaada ya nchi matajiri.

“Tusibabaishwe na wahisani kwa tishio lao la kusitisha misaada ya maendeleo...wakati umefika wa kufanya kazi na kutumia rasilimali zetu kikamilifu ikiwemo kukusanya mapato na kupambana na viongozi wazembe na wabadhirifu."

Rashid mwanasiasa mkongwe ambaye aliwahi kuwa naibu waziri wa fedha na uchumi wa Serikali ya Muungano katika miaka ya 1987, alisema huu ni wakati wa kuiga mfano wa nchi ya Kenya wahisani walizuia misaada kwa asilimia 80 lakini walitumia walichonacho kwa ajili ya matumizi ya ndani.

Mapema Rashid alimpongeza Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohmed Shein kwa kumteua kuwa mwakilishi, hatua ambayo imetimiza ndoto zake za kuunda serikali itakayovishirikisha vyama vya siasa nchini kinyume ma matarajio ya wapinzani.

“Hii siyo serikali ya umoja wa kitaifa lakini ni serikali iliyowajumuisha wananchi na vyama vyote vya siasa na sasa tupo tayari kufanya kazi kwa ajili ya kuleta na kusimamia maendeleo kwa faida ya wananchi wote kwa sababu uchaguzi umekwisha,’’alisema.

Viongozi CUF washutumiwa kwa kukosa uzalendo

$
0
0

Baadhi ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wamekishiutumu Chama cha Wananchi (Cuf) pamoja na viongozi wao kwa kukosa uzalendo kutokana na kauli zao za kuunga mkono wahisani kuisitishia misaada Tanzania.

Hayo yalisemwa na Mwakilishi wa kuteuliwa kutoka katika chama cha Ada-Tadea, Juma Ali Khatib ambaye aligombea urais wa Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu wa marudio, alipokuwa akichangia hotuba ya Rais wa Zanzibar kwenye baraza hilo mjini hapa.

Alisema, viongozi wa Cuf wameonesha udhaifu mkubwa wa kukosa uzalendo kwa kitendo chao cha kuunga mkono nchi washiriki wa maendeleo kususa misaada kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Alisema, Zanzibar ni nchi yenye kufuata katiba yake kwa hiyo ilikuwa na mamlaka kamili kupitia Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), kuitisha uchaguzi wa marudio baada ya kuufuta wa Oktoba 25, mwaka jana.

“Nimesikitishwa na kauli za viongozi wa Cuf kuunga mkono nchi washiriki wa maendeleo kuhusu uamuzi wa kususia misaada kwa Tanzania. Viongozi hao wameonesha udhaifu na kukosa uzalendo,” alisema Khatib.

Alisema chama chake kiliamua kuingia katika uchaguzi wa marudio wa Machi 20 kwa sababu umeitishwa na chombo halali kwa mujibu wa katiba, chenye majukumu ya kusimamia uchaguzi kikiwa hakiingiliwi na mtu yeyote.

Mwakilishi wa Jimbo la Mfenesini , Machano Othman Said, alisema kitendo cha viongozi wa Cuf kuunga mkono nchi washiriki wa maendeleo kususa kutoa misaada kwa Tanzania hakikubaliki hata kidogo kikionesha udhaifu mkubwa wa viongozi hao katika uzalendo wa nchi.

Watu Watano Wafariki Dunia Jijini Dar Kwa Kuangukiwa Na Kifusi.

$
0
0

Watu watano wamefariki dunia na wengine watano kujeruhiwa, baada ya nyumba waliyokuwa wakiishi kuangukiwa na kifusi na mti wakiwa wamelala, ajali hiyo ilisababishwa na kupasuka kwa karo la majitaka la nyumba ya jirani iliyo juu ya mlima.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Christopher Fuime alisema chanzo cha ajali hiyo ni kupasuka kwa karo hilo na kwamba maji yaliyotoka kwa kasi yaling’oa mti, kifusi na kisha kuifunika nyumba ya jirani iliyojengwa bondeni na kusababisha vifo hivyo.

Alisema tukio hilo lilitokea jana alfajiri katika Mtaa wa Ukwamani Kata ya Kawe jijini Dar es Salaam, na waliokufa ni Ephraim Manguli (47), watoto wake Daniel Ephraim (5) na Frederick Ephraim (1). Wengine ni mjukuu wa mwenye nyumba hiyo, Greyson Clarence (3) pamoja na msichana wa kazi za ndani aliyetambulika kwa jina moja la Maria.

“Majeruhi ni pamoja na Emilia Nakiete (19) aliyejeruhiwa mkono wa kulia na kidevu na Fadhili Fariji (8) aliyejeruhiwa mguu wa kulia. Wengine watatu walitibiwa katika Hospitali ya Mwananyamala na kuruhusiwa. Majeruhi wawili bado wamelazwa na miili ya marehemu imehifadhiwa hospitalini hapo,” alisema Kamanda Fuime.

Baada ya kutafutwa, mmiliki wa nyumba hiyo Blandina Clarence Akilizao (49), alisema nyumba yake ilikuwa na wapangaji sita wenye familia, huku familia yake ikiwa na watu saba.

“Ndani ya nyumba nilikuwa na watoto wawili, wadogo zangu wawili na wajukuu wawili, pia kulikuwa na familia tano zilizokuwa na watu 17 jumla,” alisema mama huyo kwa uchungu.

Blandina alisema nyumba hiyo aliachiwa na mumewe aliyefariki dunia mwaka 2000 na kwamba hivi sasa hana msaada wowote, kwani akiba ya fedha aliyokuwa nayo kiasi cha Sh200,000 imefukiwa na kifusi na hajui namna ya kuipata.

Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo ambaye ni mpangaji, Msafiri Nyamolelo alisema ajali hiyo ilitokea ghafla na kabla ya ukuta kuanguka, ulisikika mlipuko na baadaye kelele za maji, kisha kishindo kikubwa juu ya paa.

“Karo lilipasuka na kwa kuwa ardhi hiyo hapo juu kwa muda mrefu ni dampo lenye mifuko mingi, ardhi ilikuwa imeoza, hivyo miti mikubwa ambayo iliota huko iling’oka baada ya karo kupasuka na kutua juu ya paa la nyumba sambamba na udongo kutoka juu nao ukafunika,” alisimulia Nyamolelo.

Akizungumzia tukio hilo, Katibu Mtendaji wa Mtaa wa Ukwamani, Kata ya Kawe Kassim Mbezi alisema chanzo cha ajali ni kupasuka kwa karo la choo na maji yaliyomwagika ambayo yaliuzoa mti huo na kifusi kilisombwa na kuifunika nyumba hiyo.

“Tulipofika eneo la tukio tuliwakimbiza majeruhi wote Mwananyamala, lakini kwa bahati mbaya walifariki baada ya kufika mapokezi wote walitoka wakiwa bado wanahema, lakini ilipofika saa tatu asubuhi tukaambiwa kwamba kulikuwa na ‘house girl’ hivyo baada ya kufukuafukua tukaupata mkono na baadaye kuufikia mwili mzima, huyu tulimtoa akiwa tayari amefariki,” alisema Mbezi.

Mbezi alitoa wito kwa wakazi wa bonde hilo kuhama kwa kuwa gema bado linaonekana na ni hatari na changamoto kubwa ni namna ya kukabiliana na maafa kabla ya kutokea. 

Bajeti ya Serikali 2016/ 2017 ni Trilioni 29.5.....Matumizi ya Kawaida ni Trilioni 17.7, Mikopo ni Trilioni 11.1. Bofya Hapa Kuona Vipaumbele Vilivyotajwa

$
0
0
Bajeti ya kwanza ya Serikali ya Awamu ya Tano itaizidi ya Serikali ya Awamu ya Nne kwa Sh7.1 trilioni baada ya Waziri wa Fedha kutangaza sura ya bajeti ya mwaka 2016/17 inayoonyesha kutakuwa na makusanyo na matumizi ya Sh29.5 trilioni.

Sura hiyo ya bajeti ya mwaka 2016/17 inatofautiana na iliyopita iliyokuwa ya Sh22.45 trilioni katika maeneo mengi, ikiwa ni pamoja na kiwango cha fedha kitakachotengwa kwa ajili ya shughuli za maendeleo, ambacho ni zaidi ya mara mbili ya fedha za eneo hilo katika bajeti iliyopita.

Waziri wa Fedha, Dk Phillip Mpango alisema wakati akiwasilisha mapendekezo ya kiwango cha ukomo wa bajeti jijini Dar es Salaam jana kuwa kati ya fedha hizo, Sh18.46 trilioni, ambazo ni sawa na asilimia 62.5 ya bajeti yote, zitatokana na jumla ya mapato ya ndani yanayohusisha na halmashauri.

Kiwango hicho kimezidi Sh3.64 trilioni ya bajeti iliyopita ambayo ililenga kukusanya Sh14.82 trilioni.

“Kati ya mapato hayo, Serikali inalenga kukusanya mapato ya kodi ya jumla ya Sh15,105 bilioni, sawa na asilimia 82 ya mapato ya ndani,”alisema Dk Mpango.

Alisema makisio ya mapato ya kodi na yasiyo ya kodi yameongezeka kwa kuwa kuna viashiria vingi vinavyoonyesha kwamba Mamlaka ya Mapato (TRA) kwa kushirikiana na wizara na taasisi zinazokusanya maduhuli, zina uwezo wa kukusanya kiasi hicho.

Alisema: “Kipaumbele cha kwanza cha Serikali kitakuwa ni kujizatiti katika ukusanyaji wa mapato kwa kubuni vyanzo vipya na kuendelea kudhibiti mianya mbalimbali ya ukwepaji wa kodi. Suala hili linahitaji ushirikiano wa karibu na wananchi ili tujiletee maendeleo ya haraka kwa kushiriki kulipa kodi na kuwafichua wakwepa kodi kwa kuwaona kama maadui wa maendeleo yetu.”

Kwa mujibu wa Dk Mpango, Sh17.72 trilioni zitakuwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida, wakati Sh11.82 trilioni, sawa na asilimia 40 ya bajeti nzima, zimetengwa kwa ajili ya shughuli za maendeleo.

Katika bajeti iliyopita, matumizi ya kawaida yalitengewa Sh16.7 trilioni, sawa na asilimia 74.3 wakati shughuli za maendeleo zilipangiwa Sh5.76 sawa na asilimia 25.9.

“Asilimia 40 kwenda kwenye mipango ya maendeleo, hili ni jambo jema,” alisema Freeman Mbowe, ambaye ni mwenyekiti wa Chadema na kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni, alipoongea na waandishi.

“Kwamba tumepunguza matumizi ya kawaida ya Serikali na kuelekeza fedha zaidi kwenye mipango ya maendeleo, nasema hili ni jambo jema kama litatekelezeka.” 

Vipaumbele 
Kwa mujibu wa Dk Mpango, shughuli zitakazopewa kipaumbele kwenye mipango hiyo ya maendeleo zimegawanywa katika maeneo manne ambayo ni viwanda vya kukuza uchumi na ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda, kufungamanisha maendeleo ya uchumi na rasilimali watu, mazingira wezeshi kwa uendeshaji biashara na uwekezaji na pia usimamizi wa utekelezaji wa mpango.

Dk Mpango alisema washirika wa maendeleo wanatarajiwa kuchangia Sh3.6 trilioni, ikiwa ni ongezeko la Sh1.7 trilioni kulinganisha na Sh1.88 trilioni zilizokuwa zinategemewa kwenye bajeti iliyopita.

Fedha hizo zitakuwa za misaada na mikopo nafuu kutoka nje ambayo ni pamoja na GBS, Basket Fund na miradi ya maendeleo.

Aidha Serikali inatarajia kukopa Sh5,374.3 bilioni kutoka soko la ndani kwa ajili ya kulipia hati fungani na dhamana za Serikali zinazoiva pamoja, wakati kutoka kwenye soko la nje kwa masharti ya kibiashara inatarajia kukopa Sh2.1 trilioni.

Awali Spika Job Ndugai alisema kwa mujibu wa utaratibu mapendezo hayo yalipaswa kuwasilishwa tangu Machi 11, lakini kutokana na ratiba za wabunge wengi kuwa kwenye majimbo yao, aliamua kuongeza siku.

“ Sasa ninawashauri wabunge wote kwenda kuyasoma mapendekezo hayo vyema ili mpate nafasi ya kuchangia fedha bajeti itakapowasilishwa bungeni. Pia mhudhurie kwenye vikao vya kamati zenu ili kujipanga vyema. Wale watakaokuwa hawaonekani kwenye vikao, tutawasilisha majina yao kwenye vyama vyao ili wachukuliwe hatua zinazostahili.”

Miradi ya maendeleo 
Katika kuongeza wigo wa makusanyo ya kodi, Dk Mpango alisema sera za mapato kwa mwaka 2016/2017 itajielekeza kufanya tathimini ya mkupuo ya majengo ili kuongeza mapato.

Katika mpango wa kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda, Dk Mpango alisema kipaumbele kitakuwa ni mradi wa magadi soda ulioko kwenye Bonde la Engaruka ambako utafiti umebaini kuna magadi ya mita za ujazo bilioni 4.68 ambazo huongezeka kila mwaka kwa mita milioni 1.9 za ujazo.

“Mradi utahusisha kiwanda cha kuzalisha tani milioni moja za magadi kwa mwaka kwa ajili ya matumizi ya viwanda, hususan madawa, vioo na sabuni,”alisema.

Mradi huo utakapokamilika utaliingizia taifa Sh 400 bilioni kwa mwaka.

Eneo jingine ni kufufua kiwanda cha General Tyre cha Arusha, ambacho kimetengewa Sh2 bilioni kwa kazi hiyo. Pia kiwanda cha viuadudu kilichopo Kibaha mkoani Pwani ambacho mradi wake utatekelezwa kwa awamu tatu, mbili za mwisho zikihusisha ujenzi wa kiwanda cha mbolea na cha virutubisho.

Pia mpango huo utahusisha uendelezaji wa viwanda vidogo mkoani Morogoro, Dar es Salaam, Mbeya na Mwanza.

Katika kufunganisha maendeleo ya uchumi na rasilimali watu, Serikali itaweka nguvu kwenye elimu na mafunzo ya ufundi, ikihusisha kuimarisha mifumo, majengo na miundombinu katika shule za awali, msingi na sekondari.

Pia itahusisha ukarabati, upanuzi na ujenzi wa vyuo vikuu, mradi wa upanuzi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu (Mkwawa, Duce, Udom na OUT, Ardhi, Mzumbe, Sokoine, Muhimbili, Ushirika, Chuo Kikuu cha Sayansi cha Mwalimu Nyerere na pia mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu.

Eneo hilo litahusisha uendelezaji ustawi wa jamii kwa kuangalia huduma za afya, maji, kazi na ajira, na uwezeshaji wananchi kwa kutoa Sh50 milioni kwa kila kijiji.

Mazingira wezeshi 
Katika kujenga mazingira wezeshi, Serikali itaongeza uwezo wa uzalishaji umeme, usambazaji umeme mijini na vijijini, ujenzi wa kiwanda cha kupokea, kuchakata na kubadilisha gesi asilia kuwa katika kimiminika kwa ajili ya kusafirisha nje, ujenzi wa miundombinu ya kusafirisha gesi asilia, ujenzi wa miundombinu ya usafiri, teknolojia ya habari na mawasiliano, miradi ya makaa ya mawe na mradi wa chuma wa Liganga.
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live




Latest Images