Quantcast
Channel: MPEKUZI
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live

Mhandisi George Sambali Ateuliwa Kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu Wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA)

$
0
0
WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mh. Profesa Makame Mbarawa amemteua aliyekuwa Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Mhandisi George Sambali kukaimu nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), kufuatia kifo cha aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Mhandisi Suleiman S. Suleiman.

Mhandisi Suleiman alifariki dunia tarehe 18 Januari, 2016 wakati akipelekwa katika hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam baada ya kuishiwa nguvu ghafla akiwa katika mazoezi ya kuogelea katika eneo la Feri, jijini Dar es Salaam.

Akitangaza uteuzi huo kwa niaba ya Waziri Mbarawa mbele ya Menejimenti ya TAA Jumatano tarehe 20 Januari, 2016 katika Ofisi za Makao Makuu ya Mamlaka hiyo kwa niaba ya Mh. Waziri, Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Sekta ya Uchukuzi, Dkt. Leonard Chamuliho, alisema uteuzi wa Mhandisi Sambali umeanza rasmi tarehe 20 Januari, 2016.

Mhandisi George Sambali alizaliwa mwaka 1965, mkoani Tabora na ana shahada ya Uzamili ya Sayansi Uhandisi Uchukuzi na Barabara (MSc. Transportation (Transport & Road) Engineering, aliyoipata mwaka 1999- 2001 nchini Uholanzi.

Mhandisi Sambali alihitimu shahada ya Kwanza ya Sayansi ya Uhandisi Ujenzi (BSc.Civil Engineering) katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) mwaka 1995 .

Mhandisi Sambali pia amepata mafunzo na kozi mbalimbali za masuala ya anga kutoka katika vyuo vya hapa nchini na nje ya nchi, ikiwemo Stashahada ya Uongozi wa Viwanja vya Ndege (Certificate in Airport Executive Leadership) mwaka 2014 huko Montreal, Canada.

Pia mwaka 2015 alitunukiwa Stashahada ya Wataalamu wa Kimataifa wa Viwanja vya ndege (Post-Graduate Diploma in International Airports Professionals (AIP) chini ya AMPAP nchini Canada.

Mhandisi Sambali aliajiriwa na TAA mwaka 2001 kama Meneja Mipango, Usanifu na Uthamini (Manager Design, Planning and Evaluation) na mwaka 2012 aliteuliwa kuwa Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Uhandisi na Ufundi.

Mwaka 2013, Mhandisi Sambali aliteuliwa kuwa Mshauri Maalum wa Mkurugenzi Mkuu kabla ya mwishoni mwa mwaka jana kuteuliwa tena kuwa Kaimu Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA).

Mhandisi Sambali ni mwanachama kwenye vyama mbalimbali vya kitaaluma kikiwemo cha Wataalamu wa Kimataifa wa Viwanja vya Ndege chini ya Baraza la Viwanja vya Ndege Duniani (ACI) na Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO).

Pia Mhandisi Sambali ni Mjumbe wa Taasisi ya Wahandisi Tanzania (IET); Mjumbe katika Jukwaa la Kimataifa la Uendeshaji wa Uchukuzi Vijijini (IFRTD); na Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB).

IMETOLEWA NA;
 KITENGO CHA SHERIA NA UHUSIANO –TAA 
Januari 25, 2016

Andrew Chenge Ateuliwa Kuwania Uenyekiti wa Bunge

$
0
0

Kamati ya Uongozi ya Bunge  imepitisha majina matatu ya wabunge watakaowania nafasi ya uenyekiti wa Bunge.

Majina hayo yamepitishwa na kamati hiyo iliyoketi jana  kuanzia saa 3.00 asubuhi hadi saa 7.00 mchana ikiongozwa na  Spika wa Bunge, Job Ndugai.

Taarifa za ndani kutoka katika kikao hicho, zilisema  kikao kilikuwa na ajenda mbili  ambazo ni uteuzi wa majina ya wenyeviti wa Bunge  na kujadili ratiba ya Bunge.

Chanzo hicho cha kuaminika kimesema kuwa waliopitishwa ni Mbunge wa Bariadi, Andrew Chenge, Mbunge wa Viti Maalumu, Dk. Mary Mwanjelwa na Mbunge mwingine wa Viti Maalumu, Najima Murtaza Giga wote kutoka CCM.

Chanzo hicho kilisema   wabunge hao wanakidhi matakwa ya kanuni inayoelekeza kuwa mwenyekiti wa Bunge ni lazima awe aidha mwenyekiti wa kamati au makamu mwenyekiti.

Katika uteuzi wa kamati uliofanyika mwishoni mwa wiki, Chenge ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Sheria Ndogo, wakati Mwanjelwa ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii na Najima ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba na Sheria.

Kwa mujibu chanzo hicho, majina hayo ambayo ni kati ya majina sita yanayotakiwa katika kanuni, yatawasilishwa katika kikao cha kwanza cha mkutano wa pili wa Bunge utakaoanza kesho.

“Kanuni zinasema Spika atawasilisha bungeni majina sita  yapigiwe kura na baadaye yapatikane matatu, hawa ndiyo walioomba wamesimama wamejieleza na kamati imewapitisha.

“Hadi tunafanya uamuzi huu Ukawa walikuwa hawajaleta majina, sisi hatujui kama wataleta au hawaleti, lakini majina yaliyopitishwa leo (jana) ndiyo hayo,” kilisema chanzo hicho.

Bunge lililopita wenyeviti wa Bunge walikuwa ni Mbunge wa Ilala, Mussa Azan Zungu, aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu, Lediyana Mng’ong’o na aliyekuwa Mbunge wa Uzini, Muhammed Seif Khatib.

Zungu amekosa fursa ya kutetea nafasi yake  kutokana na kukosa sifa na  hivi sasa yeye ni mjumbe wa kawaida wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii inayoongozwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Peter Serukamba. Khatib na Mng’ong’o hawakufanikiwa kurejea bungeni.

Kamati ya Uongozi inaundwa na wenyeviti wote wa Kamati za Kudumu za Bunge, akiwamo Spika wa Bunge, Job Ndugai, Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Wengine ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, Freeman Mbowe  ambaye pia ni Mbunge wa Hai (Chadema).

Majina hayo yameteuliwa huku kukiwa na sintofahamu katika kambi ya upinzani bungeni kuhusu uteuzi na mpangilio wa wajumbe katika kamati mbalimbali za Bunge.

Vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), havijaridhidhwa na uteuzi wa kamati hizo, hasa katika Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) na ile ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) zinazopaswa kuongozwa na wapinzani.

Kutoridhishwa huko kumewafanya wabunge wa kambi hiyo kususa shughuli za kamati ikiwa ni pamoja na kutoshiriki uchaguzi wa wenyeviti wa kamati, jambo linaloleta taswira isiyoeleweka.

Sakata la ESCROW: Magufuli mkamate Seth wa IPTL

$
0
0
JUMUIA ya Wanazuoni Watetezi wa Rasilimali nchini (JUWARA), imewataka wabunge wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania linalotarajia kuanza rasmi vikao vyake vya kujadili hotuba ya Rais aliyoitoa wakati wa kulizindua bunge hilo hapo kesho,
kumuomba na kumkumbusha Rais DK. John Pombe Magufuli kutoa agizo la kukamatwa mara moja kwa mfanyabiashara Harbinder Sing Sethi ambaye ni mmiliki wa kampuni ya IPTL/PAP inayoendesha mtambo wa kufua umeme wa dharura uliopo tegeta Salasala kama sehemu ya utekelezaji wa maazimio ya Bunge lililopita .

Wanazuoni hao wamesema kuna kila sababu ya wabunge wa bunge hili la 11 kusimama imara ili kutetea rasilimali za taifa letu zinazoonekana kutafunwa na wajanja wachache wanaotumia visingizio dhaifu vya sheria na uwekezaji kwa kumtaka Rais John Magufuli aharakishe utekelezwaji wa maazimio hayo ya Bunge hasa azimio namba moja lililoitaka serikali kumchukulia hatua kali na kumkamata mmiliki wa Kampuni ya IPTL, Herbinder Sing Seth kwa makosa ya kulisababishia taifa hasara ya zaidi ya bilioni 320 kutokana na wizi uliofanyika katika akaunti ya TEGETA ESCROW.

Pia, jumuia hiyo imesema ina imani kubwa na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo huku ikimtaka awe mwangalifu na asiwe mtetezi wa IPTL safari hii kwa kuwa maamuzi ya bunge yalikuwa sahihi dhidi ya kampuni hiyo, ambayo imeisababishia hasara kubwa serikali kutokana na vitendo vyake vilivyofanya.

Wakizungumza na JAMVI LA HABARI, Mwenyekiti na Katibu wa Jumuia hiyo, Omary Kisambu na Mahmud Salibaba kila mmoja,wameonyesha kusikitishwa na kitendo cha serikali kumkumbatia mfanyabiashara huyo, anayelalamikiwa na watanzania wengi kwa kulitia hasara taifa kutokana na vitendo vyake alivyovifanya kwenye sakata nzima la akaunti ya Tegeta Escrow.

"Tunashangaa mpaka sasa mapendekezo na maazimio muhimu ya Bunge kuhusu TEGETA ESCROW hayajatekelezwa na badala yake wameishia kuwatoa kafala kina William Ngeleja na Anna Tibaijuka, hii haitakiwi kuachwa ipite hivi hivi, lazima kama vijana wasomi tusimame kidete kupigania taifa letu na rasilimali zake" alisema Mwenyekiti huyo.

Naye, Katibu wa Elimu na Mawasiliano wa Jumuia hiyo, Mahmud Salibaba amelinukuu azimio namba moja na kushangaa kuona serikali imekubali kutekeleza azimio namba nane wakaliacha azimio namba moja ambalo linahitaji utekelezaji tu.

Mahmud aliongeza kuwa azimio namba moja linasema
"Bwana Harbinder Singh Seth na wengine,Bunge linaazimia kwamba, TAKUKURU, Jeshi la Polisi na Vyombo vingine husika vya Ulinzi na Usalama, vichukue hatua stahiki kwa mujibu wa sheria za nchi yetu, dhidi ya watu wote waliotajwa na Taarifa Maalumu ya Kamati, kuhusika na vitendo vyote vya kijinai kuhusiana na Miamala ya Akaunti ya Escrow, na watu wengine watakaogundulika kufuatia uchunguzi mbalimbali unaoendelea kuhusika katika vitendo vya jinai". Aliinukuu.

Katibu huyo, alisema "Hatuna wasiwasi na Prof. muhongo, Tunaamini ana mapenzi mema na utayari wa kulitumikia taifa katika sekta hii, lakini kwenye hili tunamtaka aweke mbele maslahi ya Taifa na kamwe asigeuke kuwa mtetezi wa IPTL wala Sethi".

Wanazuoni hao wameendelea kuonyesha matumaini yao kwa Bunge hili huku wakiamini kwamba kama ilivyo kawaida ya mabunge yaliyotangulia, panapotokea masuala ya kitaifa yenye maslahi mapana kwa nchi basi wabunge wav yama vyote huungana na kuweka tofauti zao pembeni na kulisimamia taifa liokoe rasilimali zake.

IPTL/PAP YAMZUIA ZITTO KABWE KUZUNGUMZIA.
Wakati hayo yakiendelea, kampuni hiyo inayolalamikiwa kuingizia hasara ya mabilioni serikali na kupelekea kuwajibishwa kwa watumishi kadhaa wa umma, imejitokeza na kuwataka wabunge waache kulizungumzia suala hilo kwa kuwa bado lipo mahakamani.

Katika taarifa iliyosambazwa kama tangazo iliyosainiwa na Katibu na Mshauri mkuu wa sheria wa Kampuni hiyo, Joseph Makandege, imemtaka Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto kutokuendelea kulizungumzia suala hilo na kwamba aache mpango wake wa kutaka kulifufua upya suala hilo hasa bungeni kwa kuwa tayari kampuni hiyo imeshamshitaki katika kesi ya madai iliyopo mahakama kuu na kwamba haitakuwa busara kwa mbunge huyo kulizungumzia suala hilo ambalo yeye binafsi ana maslahi nalo.

Kadhalika taarifa hiyo inasema kwamba tayari serikali imejibu kupitia hotuba ya Rais mstaafu Jakaya kikwete pindi alipokuwa madarakani kuwa haipo tayari kumkamata Sethi wala kutaifisha mitambo hiyo kwa kuwa itasababisha kuanzishwa kwa mahusiano mabovu na wawekezaji, hivyo Makandege amesisitiza kwamba ni vema mbunge huyo na mbunge mwingine yoyote aachane na mpango wa kuliibua suala hilo bungeni. 

‘’kwa uelewa wetu mdogo kuhusu maswala haya, kauli ya Rais huwa ndio kauli ya mwisho na ni sawa na hukumu, na tayari Rais (Rais Mstaafu Kikwete) alishasema kuwa suala hilo haliwezekani ‘’. Ilisisitiza taarifa hiyo ya Makandege.

‘’katika hali ya kiubinaadamu, si vema kwenda bungeni kushusha lawana na tuhuma kuwatuhumu watu na ama kampuni ambazo zenyewe haziwezi kuingia bungeni kujitetea’’. Ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

‘’Hata mheshimiwa Zitto alifanya makosa kujihusisha na suala la IPTL/PAP wakati akijua kuwa ameshtakiwa mahakamani na kwamba moja kwa moja anakuwa na mgogoro wa kimaslahi, japo hajatamka mahala popote kuwa ana mgogoro wa kimaslahi na sakata husika’’. Iliongeza sehemu ya taarifa hiyo

ZITTO KABWE AWAJIBU .
Naye mbunge wa Kigoma mjini ACT – WAZALENDO ambaye wakati wa mjadala wa sakata hilo la ESCROW alikuwa mwenyekiti wa kamati ya Bunge inayosimamia hesabu za serikali, amejibu taarifa hiyo kwa kusema ni ya uongo inayoambatana na uoga wa kuwajibishwa na bunge baada ya kugundua maovu yao na kwamba IPTL /PAP hawana mamlaka ya kisheria kumzuia mbunge kujadili swala lolote ndani ya bunge akiwa anatimiza wajibu wake wa kikatiba.

‘’Sikuwa na soma ripoti yangu wala kuwasilisha maoni yangu, nilikuwa nawasilisha ripoti ya kamati ya kudumu ya bunge kwa hiyo si sahihi kulihusisha swala lile na mambo binafsi’’inasema taarifa ya Zitto Kabwe

‘’Mpaka wakati nawasilisha taarifa ya kamati bungeni, sikuwa nimewahi kupokea hicho wanachosema ni shitaka lao kwangu, kwa kuwa tumesoma ripoti mwezi November mwaka 2014 na nimeletewa shitaka lao mwezi mei mwaka 2015, kwa hiyo sikuwa na mgogoro wowote wa kimaslahi kama wanavyotaka kuuaminisha umma’’. Iliongeza taarifa ya mbunge huyo.

Zitto aliongeza zaidi kwa kusema kwamba mpaka sasa hajapokea taarifa ya kimahakama ikimzuia kutokujadili hoja inayohusiana na yeye kujadili jambo linahusiana na IPTL/PAP na badala yake amepokea taarifa ya kesi ya madai ya fedha na hivyo haki zake za kutumia katiba kujadili maswala ya kitaifa ndani ya bunge zipo pale pale na kwamba ataendelea kuwawakilisha watanzania kwa kusimamia rasilimali za taifa.

Sakata la IPTL na akaunti ya ESCROW lilibua hisia mbali mbali wakati wa mjadala wake uliodumu kwa zaidi ya miezi saba mwaka juzi na kuhitimishwa mapema January mwaka jana baada ya Waziri Muhongo kujiuzulu

Credit: Jamvi La Habari

Esther Bulaya Ashinda Kesi Ya Kupinga Ushindi Wake Iliyofunguliwa na Stephen Wassira

$
0
0

Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza imetupilia mbali kesi ya uchaguzi iliyofunguliwa na wapambe  wa  aliyekuwa mgombea ubunge wa jimbo la Bunda Mjini kwa tiketi ya CCM, Stephen Wassira kwa madai kuwa waleta maombi hawakuwa na haki kisheria ya kufungua kesi hiyo

Wapambe  wa  Wassira walifungua kesi Mahakama kuu  kupinga matokeo ya uchaguzi huo wakidai kuwa uligubikwa na udanganyifu na hujuma dhidi ya mgombea wao ( Stephen Wassira ) ikiwa ni pamoja na kutofautiana kwa idadi ya wapiga kura kwenye kituo na jumla ya kura zilizoonekana kwenye fomu za matokeo. Wapambe hao waliiomba mahakama kubatilisha ushindi wa Bulaya.

Bulaya alihamia Chadema akitokea CCM na kupewa nafasi ya kugombea ubunge katika uchaguzi mkuu uliopita na hatimaye kumshinda Stephen  Wassira aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo kwa miaka mingi na waziri wa serikali ya awamu ya nne.

==>Kupitia Facebook, Esther Bulaya ameandika kuhusu hukumu ya kesi hiyo:

"Nilimshinda Wasira kwa wananchi, na leo nimemshinda kisheria, Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza imetupilia mbali kesi ya Uchaguzi dhidi yangu, iliyofunguliwa na wapambe wa wasira. 
 
"Mungu husimama na watu waliowema. Nakutumaini mungu wangu na wewe ndiye mlinzi wangu.Asante sana Wananchi wangu wa Bunda Mjini mliokwenda Mwanza kusikiliza Hukumu. 
 
"Mbunge wenu nipo dodoma tayari kwa kuanza vikao vya Bunge Kesho."

Nilimshinda Wasira kwa wananchi, na leo nimemshinda kisheria, Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza imetupilia mbali kesi ya...
Posted by Ester Bulaya on Monday, January 25, 2016

Rais Magufuli Amsimamisha Kazi Mkurugenzi Mkuu wa NIDA......Awarudisha Nyumba Mabalozi 6 na Kumfukuza kazi Katibu Tawala Mkoa wa Katavi, Ndg. Madeni Kipande

$
0
0
1.0           Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA)

1.1 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, ametengua uteuzi wa Bwana Dickson E. MAIMU, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa kuanzia leo, tarehe 25 Januari, 2016.

1.2 Aidha, baada ya utenguzi huo, Bwana Dickson E. MAIMU amesimamishwa kazi kupisha uchunguzi, pamoja na wafuatao:

1.2.1    Bwana Joseph MAKANI, Mkurugenzi wa TEHAMA
1.2.2.   Bi Rahel MAPANDE, Afisa Ugavi Mkuu
1.2.3    Bi Sabrina NYONI, Mkurugenzi wa Sheria
1.2.4    Bwana George NTALIMA, Afisa usafirishaji

1.3  Taarifa zilizomfikia Rais zinaonesha kuwa NIDA hadi sasa imetumia Sh.179.6 bilioni. Kiasi hiki ni kikubwa na Rais angependa ufanyike uchunguzi na ukaguzi jinsi fedha hizi zilivyotumika, maana Rais amekuwa akipokea malalamiko ya wananchi kuhusiana na kasi ndogo ya utoaji wa Vitambulisho vya Taifa.

1.4 Hivyo, Rais ameelekeza Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) wafanye ukaguzi maalum wa manunuzi yote yaliyofanywa na NIDA.

1.5 Rais pia ameelekeza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali afanye ukaguzi maalum wa hesabu za NIDA, ikiwemo ukaguzi wa “value for money” baada ya kuthibitisha idadi halisi ya vitambulisho vilivyotolewa hadi sasa.

1.6 Rais vile vile ameelekeza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ifanye uchunguzi kujiridhisha kama kulikuwa na vitendo vya rushwa au la.

2.0  Wizara ya Mambo ya Nje, Afrika Mashariki na Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa

2.1 Aliyekuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwenye Serikali ya Awamu ya Nne, Mhe. Mahadhi Juma MAALIM ameteuliwa kuwa Balozi wa kwanza wa Tanzania nchini Kuwait, kufuatia uamuzi wa Serikali kufungua Ofisi ya Ubalozi katika nchi hiyo rafiki.

2.2  Rais ameagiza Wizara ya Mambo ya Nje, Afrika Mashariki na Ushirikiano wa Kianda na Kimataifa kuwarejesha nyumbani mara moja Mabalozi wawili ambao mikataba yao imeisha. Leo hii Mabalozi hao wanatakiwa kukabidhi kazi kwa Afisa Mkuu au Mwandamizi aliye chini yao. Mabalozi hao ni:

2.2.1    Bi Batilda Salha BURIANI, aliyeko Tokyo, Japan
2. 2.2   Dkt. James Alex MSEKELA, aliyeko Rome, Italia.

2.3 Rais amemrejesha nyumbani Balozi wa Tanzania aliyeko London, Uingereza, Bwana Peter Allan KALLAGHE. Anarejea Wizara ya Mambo ya Nje, Afrika Mashariki na Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa atakapopangiwa kazi nyingine.

2.4  Kwa maana hiyo, vituo vya Ubalozi vifuatavyo viko wazi:

2.4.1  London, kufuatia kurejea nchini kwa Balozi Peter A. KALLAGHE

2.4.2    Brussels, kufuatia aliyekuwa Balozi, Dkt. Deodorous KAMALA kuchaguliwa kuwa Mbunge.

2.4.3    Rome, Italia, kufuatia kuisha kwa mkataba wa Dkt. James Alex MSEKELA.

2.4.4    Tokyo, Japan, kufuatia kuisha kwa mkataba wa Bibi Batilda BURIANI

2.4.5    Kuala Lumpar, Malaysia, kufuatia aliyekuwa Balozi, Dkt. Aziz Ponray MLIMA, kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje, Afrika Mashariki na Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa.

2.4.6    Brasilia, Brazil, kufuatia kustaafu kwa aliyekuwa Balozi, Bwana Francis MALAMBUGI.

3.0   Tawala za Mikoa

3.1 Rais ametengua uteuzi wa Eng. Madeni Juma KIPANDE kabla hajathibitishwa kwenye cheo cha Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi kutokana na utendaji kazi usioridhisha.

4.0       Utumishi wa Umma

3.2  Nachukua nafasi hii kuwahimiza viongozi wote katika Utumishi wa Umma, na watumishi wote wa umma, kubadilika kwa dhati kwenye utendaji wao na uadilifu wao.

3.3 Napenda kusisitiza kuwa Rais na sisi tunaomsaidia hatuoni raha kuchukua hatua dhidi ya viongozi na watumishi wengine. Tungependa kila mtu mwenyewe ajirekebishe na kutomfikisha Rais mahali ambapo inabidi amchukulie hatua. 

Mambo yafuatayo ni muhimu:

4.2.1 Kila kiongozi na kila mamlaka ya nidhamu isipate kigugumizi kusimamia utendaji na maadili ya kazi.

4.2.2 Kila kiongozi na kila mamlaka ya nidhamu asipate kigugumizi kuchukua hatua za nidhamu, lakini afanye hivyo kwa kuzingatia kwa ukamilifu sheria, kanuni na taratibu katika Utumishi wa Umma.

4.2.3   Lazima uongozi na watumishi wa umma wawahudumie wananchi kwa haki, weledi, uadilifu na heshima. Kwa sababu hiyo:

a)  Kila ofisi ya Serikali iwe na dawati la kusikiliza shida za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi.

b) Kwenye kila Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya wajenge uwezo wa kushughulikia shida za wananchi kwa ukamilifu na kwa wakati. Kwa muundo wa Serikali yetu hakuna sababu kwa mwananchi kufunga safari mpaka Ikulu Dar es Salaam kwa kuamini kuwa ni Rais tu anayeweza kumaliza matatizo yake, maana wawakilishi wa Rais wako kila pembe ya nchi yetu. Ikibidi wananchi wafike Ikulu ina maana hao wawakilishi wa Rais hawakutimiza wajibu wao.

c)  Kuanzia sasa watumishi wote wa umma wavae majina yao ili iwe rahisi kwa mwananchi kumtambua anayemhudumia na hivyo kumsifu mtumishi wa umma anayewahudumia kwa weledi, uaminifu na kwa wakati, na kumtolea taarifa yule anayefanya mambo ya hovyo.

d) Kila ofisi ya Serikali iwe na utaratibu wa kupokea maoni ya wananchi kuhusu huduma inayotolewa kwenye ofisi hizo, na kushughulikia haraka maeneo yote ambayo wananchi wataonesha kutoridhika na huduma.

                                                           
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Arusha
25 Januari, 2016

Diamond Platnumz: Baada Ya Nape Nnauye Mimi Ndo Waziri wa Habari Na Michezo Mtarajiwa

$
0
0
Diamond Platnumz amesema akiachana na muziki anataka kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ili kuweka vitu sawa na kutoa fursa zaidi kwa vijana.

Akizungumza katika kipindi cha Papaso cha TBC FM, Diamond alisema kama akiingia kwenye siasa basi nia yake ni kuwa Waziri wa Michezo.

“Kwa sasa hivi siasa bado ila nikiingia kwenye siasa baadaye akimaliza mheshimiwa Nape nachukua mimi kile cheo cha Waziri wa Michezo,” alisema na kuongeza;

“Kile nakiweza kabisa kwa sababu mimi ukinimbia sijui kuhusu mpira, movie mimi naweza kabisa nikiwa Waziri, nikavifanya na vikawa na maendeleo. 

"Ni kitu ambacho naweza siyo nasema nataka kuwa mbunge ila mimi nataka ile siku nimeacha kufanya muziki naingia kwenye siasa basi nakuwa Waziri  wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na kuboresha vitu”

Diamond ambaye hakuweka wazi kwamba ataingia kwenye siasa kupitia chama gani, mwaka jana katika kampeni za uchaguzi mkuu uliomuingiza rais Magufuli madarakani, alishiriki kikamilifu kwenye kampeni za CCM na kutengeneza wimbo pamoja na video.

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Jumanne ya Januari 26

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Meja Jenerali Rwegasira Ataka Polisi wenye Tabia ya Kuwabambikizia kesi Wananchi Wachukulie Hatua Kali

$
0
0

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira amewataka viongozi wakuu wa Jeshi la Polisi nchini kuhakikisha wanawachukulia hatua kali askari polisi wenye tabia ya kuwabambikizia kesi wananchi.

Meja Jenerali Rwegasira alisema Jeshi hilo lina sifa nzuri nje ya nchi pamoja na hapa nchini lakini kuna baadhi ya askari wasiowaadilifu wanawaonea wananchi mitaani wasiokuwa na hatia kwa kuwabambikizia kesi ambapo wanalitia doa jeshi hilo.

“Jeshi letu lina sifa nzuri, niliwahi kwenda nchini Kenya nikaambiwa Jeshi la Polisi Tanzania lina maadili kwani hata likimkamata mhalifu linafuata sheria na utaratibu na sio kutumia nguvu kubwa kama yalivyo majeshi mengine,” alisema Rwegazira.

Rwegasira aliongeza kuwa, amefurahishwa sana na utendaji kazi wa jeshi hilo na kutaka kuongeza umakini zaidi ili kuliletea sifa zaidi jeshi hilo na yeye yupo karibu nao katika kuliendeleza jeshi hilo ili liweze kufanya kazi kwa weledi.

Alisema kuwa ni askari wachache mno wenye tabia hiyo ya kuwabambikizia kesi wananchi na kutofuata sheria za jeshi, hivyo kazi ya kupambana na askari hao inawezekana endapo viongozi wa jeshi wakiamua kulifanyia kazi.

“Utendaji kazi wenu ni mzuri, nawapongeza sana hasa mlivyosimamia uchaguzi mkuu vizuri kwani wananchi wengi walikuwa na wasiwasi kuhusu usalama wao katika kipindi cha uchaguzi, lakini mlisimama imara kuhakikisha uchaguzi unamalizika salama,” alisema Rwegasira.

Hata hivyo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Balozi Simba Yahya naye alitoa pongezi kwa jeshi hilo na kuwataka kuyapeleka mahitaji yao katika ofisi ya Katibu Mkuu pamoja na yeye ili waweze kuyafanyia kazi na hatimaye kuliboresha jeshi hilo.

Kwa upande wake Mkuu wa Jeshi hilo nchini, IGP Ernest Mangu aliwapongeza Viongozi hao wa Wizara kwa kuwatembelea katika ofisi za Makao Makuu ya Jeshi kwani wamefarijila na kuwahakikishia viongozi hao kuwa wamejipanga vizuri katika kulinda usalama wa raia na mali zao na watayafanyia kazi maagizo waliyopewa.

Katibu Mkuu pamoja na Naibu wake wanamekamilisha ziara yao ya kuzitembelea Idara za Wizara hiyo ambazo ni Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza, Idara ya Uhamiaji, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), ambapo lengo la ziara hizo ni kujitambulisha kwa viongozi hao pamoja na kujifunza kazi mbalimbali zinazofanywa na idara hizo.

Tamko La Serikali Kuhusu Mwenendo Wa Ugonjwa Wa Kipindupindu Nchini

$
0
0
Tamko  La  Serikali   Kuhusu Mwenendo Wa Ugonjwa Wa Kipindupindu Nchini Lililotolewa Na Mhe. Ummy Mwalimu (mb); Waziri Wa Afya, Maendeleo Ya Jamii, Jinsia, Wazee Na Watoto
______________________

Wizara yangu inaendelea kutoa taarifa ya wiki kwa umma kuhusu mwenendo wa ugonjwa wa kipindupindu hapa nchini. 

Hadi kufikia tarehe 24 Januari 2016, jumla ya watu 14,608 wameugua ugonjwa huo, na kati yao watu 228 wamepoteza maisha kwa ugonjwa huu. 

Njombe, Ruvuma na Mtwara ndiyo Mikoa pekee ambayo haijawahi kuripoti mgonjwa yoyote wa kipindupindu, tangu mlipuko huu uanze mnamo mwezi Agosti mwaka huu.

Kwa mujibu wa Takwimu za kuanzia tarehe 18 hadi 24 Januari 2016, ni kuwa jumla ya Mikoa ambayo imeripoti kuwa na wagonjwa ni 15 ambapo idadi ya wagonjwa 524 na vifo 10 vimeripotiwa. 

Idadi ya wagonjwa walioripotiwa wiki hii imepungua ukiliinganisha na idadi ya wiki iliyoishia tarehe 17 ambapo kulikuwa na wagonjwa 621 na vifo 14 ambalo ni punguzo la asilimia (16%). 

Mkoa wa Morogoro bado umeendelea kuripoti idadi kubwa zaidi ya wagonjwa ukilinganishwa na Mikoa mingine, (Manispaa ya Morogoro 89, Halmashauri ya Morogoro 36, Mvomero 17), ukifuatiwa na mikoa ya Mwanza (Ukerewe 36, Nyamagana 19 na Ilemela 13), Simiyu (Bariadi DC 29 na Bariadi municipal 23), Manyara (Simanjiro 48), Mara (Musoma Manispaa 11, Musoma DC 8, Rorya 8 na Butiama 8), Geita (Geita DC 21 na Geita TC 6) na Mbeya (Kyela 26).
 
Mikoa mingine ambayo bado pia imeendelea kuripoti wagonjwa ni pamoja na Dodoma (Wagonjwa 22), Arusha (21), Tabora (18), Singida (18), Lindi (12), Rukwa (7), Kilimanjaro (6) na Kagera (2).
 
Mwanzoni mwa mwezi Januari mwaka huu, Wizara yangu kwa kushirikiana na wadau ilituma timu ya jopo la wataalam kutoka ngazi ya Taifa kwenda kusaidiana na wataalam waliopo katika ngazi ya mkoa na halmashauri katika mikoa 7 iliyokuwa inatoa taarifa ya kuwa na wagonjwa wengi zaidi. Mikoa hiyo ni Arusha, Manyara, Mwanza, Simiyu, Singida, Mara na Morogoro. 

Mafanikio ya kazi iliyofanywa na Jopo hilo yameanza kuonekana kwani katika Mikoa hiyo saba idadi ya wagonjwa wa kipindupindu imeanza kupungua.

 Pamoja na mafanikio hayo zipo changamoto ambazo timu hizo ilizibaini kuwepo ambazo zinachangia kulegalega kwa juhudi za kupambana na Kipindupindu nazo ni;
 
i. Kuwepo na idadi ndogo ya kaya ambazo zinamiliki na kutumia vyoo bora hususani katika maeneo ambayo yameathirika zaidi na ugonjwa huu.
ii. Kutokuwepo kwa miundombinu stahiki ikiwemo vyoo na maji katika Maeneo ya mikusanyiko kama masoko na minada kutokuwa na
iii. Wananchi kutokutii sheria zilizopo kwa kuendelea kuuza chakula bila kuzingatia kanuni za afya na kuuza matunda yaliyokwisha katwakatwa maeneo yasiyo salama.
iv. Utiririshaji wa maji taka kwenye vyanzo vya maji, pamoja na kujisaidia maeneo ya wazi na pembezoni karibu na vyanzo vya maji.
v. Kuwepo kwa idadi ndogo ya watu wanaopata maji safi na salama ya kunywa. Aidha utakasaji wa maji katika ngazi ya kaya kwa kuyachemsha au kwa kutumia vidonge vya kutakasia bado ni changamoto kubwa.
vi. Wagonjwa wa Kipindupindu kuchelewa kufika Kambi za Matibabu.
 
Kutokana na changamoto hizo, napenda kuikumbusha jamii kuwa kipindupindu ni ugonjwa unaochochewa na mazingira machafu ikiwemo ukosekanaji wa vyoo na hivyo kuletea vinyesi vyenye vimelea kuwa chanzo kikuu cha maambukizi, utiririshaji wa maji taka na vinyesi ambao unaweza kupelekea kuchafuka kwa vyanzo vya maji, kutokuzingatia kanuni za afya wakati wa utayarishaji wa vyakula na matunda, Kula vyakula au vinywaji au pombe za kienyeji zisizoandaliwa kwa kufuata kanuni za afya na kugusa matapishi ya mgonjwa wa kipindupindu au kwenye kitu chochote kilichochafuliwa na kinyesi au matapishi ya mgonjwa.
 
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, inaendelea kusisitiza kwa jamii kuzingatia yafuatayo:
– Kunywa maji yaliyo safi na salama.
– Kuepuka kula chakula kilichoandaliwa katika mazingira yasiyo safi na salama.
– Kunawa mikono kwa sabuni na maji safi yanayotiririka hasa kabla ya kula na baada ya kutoka chooni.
– Kutumia vyoo wakati wote na kutokujisaidia ovyo katika vyanzo vya maji vya mito, maziwa na mabwawa.
– Kutokutiririsha maji taka na vinyesi ili kuepuka uchafuzi wa vyanzo vya maji.

Wananchi wanaombwa kuwahi mapema katika vituo vya kutolea huduma za afya mara waonapo dalili kuu za ugonjwa wa kipindupindu kwani Mgonjwa anaweza kupoteza maisha endapo hatapata huduma yoyote ya tiba katika muda mfupi na hasa kutokana na kuishiwa maji. 

Dalili hizo ni pamoja na kuanza ghafla kuharisha mfululizo kinyesi cha majimaji meupe kama maji yaliyooshea mchele na kinaweza kuambatana na kutapika, kulegea, kusikia kiu, midomo kukauka, na kuishiwa nguvu.
 
Napenda kurudia tena kutoa agizo kwa Mamlaka za Mikoa na Halmashauri pamoja na watendaji wake kote nchini kuendeleza juhudi za kuzuia kusambaa kwa mlipuko ambazo ni pamoja na:
 
• Uundaji wa Timu za Mikoa na Wilaya ambazo zitashirikisha kila sekta na wadau mbalimbali katika hatua mbalimbali za kuratibu mikakati ya udhibiti wa ugonjwa wa Kipindupindu.
 
• Ushirikishwaji wa viongozi ngazi mbali mbali, hasa ngazi za Halmashauri kushirikisha madiwani na viongozi wa kata, vijiji, na mitaa hasa katika Kusimamia utekelezwaji wa Sheria ya Afya ya Mazingira na Sheria ndogo ndogo (By-Laws). Matumizi ya Sheria hizi pia yazingatie Haki za Binadamu hususan katika uamuzi wa kutumia nguvu ambayo inaweza kuleta madhara kwa mtu.
 
• Ushirikishwaji wa wadau mbali mbali huko Mikoani, Wilayani na kwenye Halmashauri, ikiwemo Sekta Binafsi na Viongozi wa dini, katika jitihada za kupambana na Kipindupindu.
 
• Mamlaka husika kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama ikiwa ni pamoja na uwekaji wa dawa ya klorini kwenye maji na kupima usalama wa maji mara kwa mara.
 
• Watumishi wa Afya kuhakikisha wanafuatilia kwa karibu maeneo yote walikotoka wagonjwa ili kubaini chanzo na kuchukua hatua haraka.
 
• Upatikanaji wa dawa za kutibu maji (Water Guard, Aqua Tabs) katika maeneo ya mlipuko.
 
• Juhudi kubwa ziongezwe kuhakikisha upatikanaji na matumizi ya vyoo bora kwa kila kaya.
 
• Uelimishwaji wa Baba na Mama Lishe, na wauzaji wengine wa vyakula kuhusu kanuni za afya.
 
• Uhamasishaji wa Wananchi wanaopata ugonjwa huu kutumia maji ya chumvi chumvi (ORS) na kuripoti mapema katika vituo vya huduma.
 
• Kila Halmashauri inapaswa kutoa taarifa mapema na kwa wakati bila kuficha pindi wanapopata wagonjwa wapya na jamii isiwekewe vikwazo vya faini au kunyanyapaliwa wapatapo ugonjwa huu kwani inaweza kusababisha wananchi kuogopa kwenda katika vituo vya afya.
 
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, inatoa rai kwa jamii, wataalamu na viongozi katika ngazi zote kila mmoja kutimiza wajibu wake katika harakati za kuudhibiti ugonjwa huu.

 Aidha, Mikoa yote nchini ni lazima ichukue hatua stahiki ikiwemo Mikoa ambayo haijapata mgonjwa na ile ambayo imepata ugonjwa na umedhibitiwa.

Tunawashukuru wadau wote wanaoshirikiana na Serikali, yakiwemo Mashirika ya Kimataifa kwa mchango wao mkubwa katika jitihada zetu za kupambana na Kipindupindu. Pamoja tukishirikiana tutaweza kuutokomeza ugonjwa huu.

Daraja La Kigamboni Kuanza Kutumika Machi Mosi

$
0
0

Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano sehemu ya Ujenzi Eng. Joseph Nyamhanga amesema daraja la Kigamboni litaanza kutumika kuanzia Machi mwaka huu.

Akizungumza mara baada ya kukagua hatua za ujenzi wa daraja hilo Eng. Nyamhanga amemtaka msimamizi wa ujenzi huo kuhakikisha hatua ya ujenzi iliyobaki inakamilika katikati ya mwezi februari na kuanza kazi mwanzoni mwa mwezi Machi.

“Hakikisheni Machi mosi magari yaanze kupita rasmi kwenye daraja hili na hivyo kufungua ukurasa mpya kwa wakazi wa Kigamboni ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakikabiliwa na msongamano katika eneo la Magogoni”, amesema Eng. Nyamhanga.

Eng. Nyamhanga amesisitiza kuwa Serikali inaangalia uwezekano wa kuunganisha daraja la Kigamboni na barabara ya Charambe,Mlandizi hadi Chalinze ili kupunguza msongamano wa magari katikati ya Jiji.

Amemtaka meneja wa mradi wa ujenzi wa daraja hilo toka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Eng. John Msemo kuhakikisha anatafuta Wakala makini atakayesimamia na kuendesha mradi huo.

Daraja la Kigamboni lenye urefu wa mita 680, unasimamiwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano linatarajiwa kuishi zaidi ya miaka 100 na kuwa na uwezo wa kupitisha mizigo ya tani 56 zinazokubalika katika nchi za jumuiya ya madola.

IMETOLEWA NA ;
KITENGO CHA HABARI NA MAWASILIANO
WIZARA YA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO.

Mbunge wa CHADEMA Atimuliwa Kwenye kikao na Polisi

$
0
0

Mbunge wa Kilombero, Peter Elijualikali jana alijikuta akitolewa nje ya kikao cha Halmashauri ya Kilombero na jeshi la polisi kwa amri ya Mwenyekiti wa kikao hicho kwa madai kuwa sio mjumbe halali wa kikao hicho, hivyo haruhusiwi kupiga kura kumchagua Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo.

Sintofahamu hiyo iliibuka wakati Halmashauri hiyo ikijipanga kufanya uchaguzi wa Mwenyekiti wake, ambapo Mwenyekiti wa kikao alimtaka mbunge huyo kutoka nje kwa madai kuwa sio mjumbe halali na alipogomea agizo la mwenyekiti, aliondolewa nje kwa nguvu na polisi.

Mwenyekiti wa kikao hicho alieleza kuwa wamepokea ufafanuzi kutoka TAMISEMI kuwa mbunge huyo wa Kilombero anapaswa kuwa mjumbe wa vikao vya Halmashauri mpya ya Ifakara na sio halmashauri ya Kilombero.

Hata hivyo, maelekezo hayo yalipingwa vikali na madiwani wa vyama vya upinzani vinavyounda Ukawa pamoja na mbunge huyo ambaye alieleza kuwa amepanga kwenda mahakamani kudai haki yake.

“Waziri wa TAMISEMI kama hataki kuchafuka na Katibu Mkuu wake, naomba wafanye kila wanaloliweza nirudi kwenye Halmashauri yangu. Na wasipofanya hivyo, nakwenda Mahakamani,” alisema Elijualikali.

Hatua hiyo ya kumtoa mbunge huyo na kumuelekeza kuhudhuria vikao vya halmashauri ya mji wa Ifakara ilitafsiriwa na madiwani wa Ukawa kuwa ni mbinu ya kutaka kupunguza idadi ya wajumbe wa vyama hivyo ili kuwezesha CCM kushinda nafasi ya Umeya wa Halmashauri hiyo.

Idadi ya wajumbe halali wa Ukawa ni 19 huku wa CCM wakiwa 18. Hata hivyo, Halmashauri ya Ifakala haina Mbunge kwakuwa sio jimbo. Hivyo, hiyo ni sababu ya kumuelekeza Mbunge huyo kuwa sehemu ya Halmashauri hiyo.

Waziri Lukuvi Awapa Manispaa Siku 30 kubomoa Ghorofa Hili Lililojengwa Chini Ya Kiwango

$
0
0
Jengo refu lilojengwa chini ya kiwango lililopo katika mtaa wa Indiraghandi jijini Dar,kama lionekanavyo pichani.

WAZIRI wa Nyumba, Ardhi na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amewaagiza watendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala na Shirika la Nyumba la Taifa kubomoa jengo refu lilojengwa chini ya kiwango lililopo katika mtaa wa Indira Ghandhi ndani ya mwezi mmoja kuanzia sasa.

Lukuvi ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam kabla ya kuelekea kwenye ziara fupi katika Wilaya ya Bagamoyo Mkoani Pwani ambapo nako pia amebaini matatizo mbalimbali katika sekta ya Ardhi.

“Miezi sita iliyopita Rais Mstaafu alikuja hapa akaagiza jengo hili libomolewe na nyie mkajiridhisha kweli lafaa kubomolewa sasa inakuwaje mpaka leo linaendelea kuwepo? Naagiza mfanye haraka jengo hili ndani ya mwezi mmoja taratibu za ubomoaji ziwe zimeanza ili kulinusuru taifa kuingia katika janga jingine.”alisema Waziri Lukuvi.

Akiwa bagamoyo waziri Lukuvi alibaini katika Wilaya ya Bagamoyo upotevu wa viwanja vya wanachi ambavyo walitakiwa kupewa katika eneo la ukuni ambapo vimetoweka

Mara baada ya kupata taaarifa hiyo mmoja wa wakaazi wa bagamoyo ambaye alitoa malalamiko juu ya viwanja hivyo mbele ya mkutano wa hadhara na kutaja kuwa Halmashauri ilichukua kiasi cha pesa kuanzia laki sita kwa kila mtu mwaka 2005 na kuahaidi kuwapatia viwanja lakini mpaka leo hawajapewa.

Mara baada ya kupata taarifa hiyo waziri Lukuvi aliwagiza watendaji wa wilaya hiyo ndani ya miezi sita wawe wamewapatia wakazi hao viwanja hivyo.
Sehemu ya jengo ambayo inaonekana imepasuka.Picha na Emmanue Massaka

Rais Magufuli Ampongeza Rais Mstaafu Jakaya Kikwete

$
0
0

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amempongeza Rais Mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuteuliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Mheshimiwa Ban Ki-moon kuunda jopo la watu mashuhuri watakaomshauri juu ya namna bora ya kuendeleza na kutekeleza malengo ya maendeleo endelevu hususani katika afya ya uzazi ya Mama na mtoto.

Jopo hilo la watu mashuhuri linaongozwa na wenyeviti wenza ambao ni Rais wa Chile Mheshimiwa Michelle Bachelet na Waziri Mkuu wa Ethiopia Mheshimiwa Hailemariam Desalegn, huku Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete na Rais Mstaafu wa Finland Mheshimiwa Tarja Halonen wakiteuliwa kuwa wenyeviti mbadala.

Katika Pongezi hizo Rais Magufuli amesema kuteuliwa kwa Rais Kikwete kuwa miongoni mwa jopo la kumshauri Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kumeijengea heshima Tanzania na kumechochea matumaini ya mafanikio ya kukabiliana na changamoto za afya ya mama na mtoto hususani kwa nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania.

Rais Magufuli ameahidi kuwa serikali yake ya awamu ya tano itatoa ushirikiano katika kutimiza malengo ya maendeleo endelevu ambayo jopo hilo litamshauri Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ikiwemo katika kuimarisha afya ya uzazi wa mama na mtoto.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
25 Januari, 2016

Watumishi wa Umma Wahimizwa Kuvaa Beji Zianazoonesha Majina Yao.

$
0
0

Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue ameagiza na kusisitiza ofisi zote Umma kusimamia na kuhakikisha kuwa hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu kila watumishi awe na kitambulisho (beji) kinachoonesha jina lake.

Akiongea na waandishi wa habari jijini Dar es salaam Balozi Sefue alisema hatua hiyo ya watumishi wa umma kuvaa beji zenye majina kila wakati wanapotekeleza majukumu yao itasaidia wananchi kuwatambua kwa majina watumishi wanaowahudumia na kuwasaidia kulingana na mahitaji yao kwenye ofisi hizo.

Ili kutekeleza azma ya kuwahudumia wananchi, Balozi Sefue alisema kuwa kuanzia sasa watumishi wote wa umma wavae beji zenye majina yao iwe rahisi kwa mwananchi kumtambua anayemhudumia na hivyo kumsifu mtumishi wa umma anayewahudumia kwa weledi, uaminifu na kwa wakati na kumtolea taarifa yule anayefanya mambo ya hovyo.

Zaidi ya hayo, Balozi Sefue amewahimiza viongozi na watumishi wote katika Utumishi wa Umma kubadilika kwa dhati kwenye utendaji na uadilifu wao na kuwahudumia wananchi kwa haki, weledi, uadilifu na heshima.

“Rais na sisi wote tunaomsaidia hatuoni raha kuchukua hatua dhidi ya viongozi na watumishi wengine, tungependa kila mtu mwenyewe ajirekebishe na kutomfikisha Rais mahali ambapo inabidi amchukulie hatua” alisema Sefue.

Mambo muhimu yanayopaswa kuzingatiwa ni pamoja na kila kiongozi na mamlaka ya nidhamu isipate kigugumizi kusimamia utendaji na maadili ya kazi ili kuchukua hatua za nidhamu, lakini afanye hivyo kwa kuzingatia kwa ukamilifu sheria, kanuni na taratibu katika Utumishi wa Umma.

Balozi Sefue amewahimza viongozi na watumishi wa umma kuwahudumia wananchi kwa haki, weledi, uadilifu na heshima ambapo kila ofisi ya Serikali inapaswa kuwa na dawati la kusikiliza shida za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi.

Kwa upande wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya wote nchini wametakiwa kujenga uwezo wa kushughulikia shida za wananchi kwa ukamilifu na kwa wakati.

“Kwa muundo wa Serikali yetu hakuna sababu kwa mwananchi kufunga safari mpaka Ikulu Dar es Salaam kwa kuamini kuwa ni Rais tu ndiye anayeweza kumaliza matatizo yake, maana wawakilishi wa Rais wako kila pembe ya nchi yetu, ikibidi wananchi wafike Ikulu inamaana hao wawakilishi wa Rais hawakutimiza wajibu wao” aliongeza Balozi Sefue.

Aidha, Balozi Sefue alisema kuwa ofisi zote za Serikali zinatakiwa kuwa na dawati la kupokea maoni ya wananchi kuhusu huduma inayotolewa kwenye ofisi hizo na kushughulikia haraka maeneo yote ambayo wananchi wataonesha kutoridhika na huduma inayotolewa.

Sakata la Vigogo Watatu NEMC Waliosimamishwa na Mh. January Makamba Kazi Lachukua Sura Mpya

$
0
0

Sakata  la maofisa watatu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), waliosimamishwa kazi kwa tuhuma ya kukiuka miiko yao ya kazi, limechukua sura mpya, baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba, kuagiza wafikishwe mbele ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Pamoja na hayo, Waziri huyo amemsimamisha kazi aliyekuwa mwanasheria wa baraza hilo, John Mnyele kwa matumizi mabaya ya ofisi.

Mh. Makamba jana alisema tayari amemwagiza Katibu Mkuu wa wizara hiyo, kuwasilisha mashtaka yanayowakabili maofisa hao watatu Takukuru kwa ajili ya uchunguzi na hatua zaidi, ikiwemo kufikishwa mahakamani.

Maofisa waliosimamishwa kazi kutokana na udhaifu huo ni pamoja na Ofisa Mazingira Mwandamizi Dk Eladius Makene, Mwanasheria Daraja la II Wakili Heche Suguta Manchare ; na Ofisa Mazingira Boniface Benedict Kyaruzi. Wanatuhumiwa kukiuka miiko ya kazi yao katika kusimamia kiwanda cha kusindika minofu ya punda kilichopo mkoani Dodoma.

Pamoja na maofisa hao, pia Mwanasheria Mnyele, anayetuhumiwa kuingia mkataba na Mchungaji Getrude Rwakatare wa kuondoa kesi mahakamani kwa niaba ya NEMC bila kuijulisha ofisi, naye anachunguzwa na taasisi hiyo ya rushwa.

Mama Rwakatare kwa sasa ana kesi mahakamani dhidi ya baraza hilo ya kupinga kubomolewa kwa nyumba yake, inayodaiwa kujengwa mahali pasiporuhusiwa.

Kiwanda hicho cha minofu ya Punda cha China, kilianza kazi hiyo rasmi mwaka 2012 huko Dodoma ambapo pamoja na kuchinja, pia huuza nyama hiyo nje ya nchi, hususan China.

Kiwanda hicho kilipatiwa vibali vyote, ikiwemo cha Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji nchini (EPZA) na cha Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi cha kuchinjia.

Pia, kilikuwa na vibali vingine vya Manispaa. Hata hivyo, hakikuwa na kibali cha masuala ya mazingira kutoka NEMC.

Katika ukaguzi uliofanywa siku za nyuma na Baraza hilo, ilibainika kuwa kiwanda hicho hakina kibali hicho cha mazingira, lakini pia kilikuwa kikilalamikiwa na wananchi wanaokizunguka kutokana na kutofuata taratibu za utunzaji wa mazingira.

NEMC ilibaini kuwa kiwanda hicho, hakikuwa na mfumo wa majitaka, lakini pia kilikuwa kikichoma mabaki yanayotumika kuchinjia ndani ya kiwanda hicho na moshi wake kusambaa maeneo yanayokizunguka.

Kutokana na makosa hayo, baraza hilo lilikifungia kiwanda hicho kama adhabu na kukilipisha faini ya Sh milioni 240.

Bunge la 11 Linaanza Leo.....Haya ni Mambo 8 Yatakayowasha Moto Bungeni

$
0
0

Kikao cha pili cha Bunge la kumi na moja linalotarajiwa kuwa na ushindani mkali wa hoja kati ya wabunge wa vya upinzani vinavyounda Ukawa na wabunge wa CCM kimeanza leo mjini Dodoma huku mambo 8 muhimu yakitarajiwa kuibua mjadala mkubwa.

Jambo la kwanza ni kujadili hotuba ya Rais John Magufuli aliyoitoa bungeni hapo mwaka jana katika kikao cha kwanza cha bunge hilo. Hapo suala la kupambana na ufisadi linatarajia kuleta hoja nzito zaidi kutoka kila upande. Hotuba ya Rais ilisifiwa na takribani kila mwananchi pamoja na wanasiasa mbalimbali.

Pili, Kurudiwa kwa uchaguzi Mkuu wa Zanzibar. Hili ni suala nyeti na linalopaswa kubebwa kwa uangalifu mkubwa. 

Wabunge wa Ukawa na CCM wanatarajiwa kurusha makombora yao ya hoja na maoni katika kusaidia namna ya kupata muafaka. Bila shaka hapo mengi yataibuka na huenda kukawa na mgongano mkubwa wa hoja na mawazo.

Tatu, Zoezi la Bomoabomoa pia linaweza kupewa nafasi yake katika Bunge hilo hususan katika utekelezaji wake na mapungufu yaliyojitokeza.

Nne,Maazimio ya Bunge juu ya sakata la ESCROW linaweza kuwa mada moto zaidi katika bunge hilo kwani tayari kumekuwa na vutankuvute kabla ya Bunge. 

Mbunge wa jimbo la Ubungo Saed Kubenea na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe ambao ni mahasimu wa kisiasa wameonekana kuwa na nia moja katika kulirudisha bungeni sakata la ESCROW. Mmiliki wa Kampuni ya IPTL/PAP, Harbinder Singh Sethi amepinga mahakamani kurudishwa bungeni kwa sakata hilo lakini Zitto amesisitiza kuwa mtu binafsi hawezi kulizuia Bunge kutekeleza majukumu yake.

Tano,Utekelezaji wa sera ya elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha nne pia ni suala ambalo litaleta mjadala katika Bunge hilo, kwa kuzingatia changamoto zilizoanza kuripotiwa.

Sita,Uteuzi wa wajumbe wa kamati za Bunge ambao vyama vya upinzani vinavyounda Ukawa vimeulalamikia na hata kutishia kuususia unatarajiwa kuwa sehemu ya hoja zitakazoleta mjadala mkubwa katika Bunge hilo.

Saba,Ni migogoro iliyoibuka katika chaguzi za Mameya wa majini na Manispaa pamoja na wenyeviti wa Halmashauri. Waziri wa TAMISEMI atakuwa na kazi ya kujibu hoja na maswali yatakayokuwa yanaelekezwa kwake kuhusu zoezi hilo.

Nane, Hoja binafsi za wabunge zinatarajiwa kuibuliwa na kuleta mjadala mzito kwani tayari baadhi ya wabunge wamekwisha eleza nia yao ya kupeleka bungeni hoja binafsi kuhusu masuala mbalimbali.

Bunge hili linatarajiwa kuwa la kipekee  na lenye changamoto kubwa kwa kuwa na idadi kubwa ya vijana na idadi kubwa ya wabunge wa upinzani ambao wameunda umoja wao.

Mama Amuua Mwanae Kwa Kichapo Na Kisha Kuitundika Maiti Yake Mtini

$
0
0

Mtoto wa miaka 11, Nchambi Tungu, ameuawa kikatili na mama yake mzazi kwa kuchapwa fimbo kisha kumfunga kamba shingoni na kumning’iniza kwenye tawi la mwembe ili ionekane kuwa amejinyonga mwenyewe.

Inaelezwa kuwa mama wa mtoto huyo, Sado Roketi (26) mkazi wa kitongoji cha Mnyakasi, kijijini Ikuba, wilayani Mlele, mkoa wa Katavi alimuua mwanawe huyo baada ya kukataa kumfulia nguo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari, jana alithibitisha kutokea kwa kifo hicho.

Alisema tukio hilo ni la Januari 23, mwaka huu saa moja jioni katika Kitongoji cha Mnyakasi. Alisema siku ya tukio mtuhumiwa alimpatia mwanawe huyo nguo amfulie lakini mtoto huyo alikataa kuzifua akaendelea kucheza na wenzake.

“Ndipo mama huyo kwa hasira alipoamua kuchukua fimbo na kuanza kumpiga sehemu mbalimbali za mwili wake na kumsababishia kifo, aliubeba mwili na kuutundika kwenye matawi ya mti wa mwembe baada ya kumfunga kamba shingoni na kumwacha akining`inia ili ionekane alijinyonga mwenyewe,” alieleza Kidavashari .

Alisema mtuhumiwa anashikiliwa na Polisi na atafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.

Waziri Simbachawene Amsimamisha Kazi Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Dodoma

$
0
0

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mh. George Simbachawene amemvua madaraka Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Dodoma, Bw. Augustino Kalinga kufuatia kuruhusu ofisi yake kuwachangisha wazazi michango ambayo serikali imezuia katika kutoa elimu ya msingi bila malipo.

Mh. Simbachawene alifikia uamuzi huo jana mjini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hatua zilizochukuliwa na serikali baada ya kugundua kuwa manispaa ya Dodoma imesambaza barua kwa walimu wakuu wa shule za msingi ambazo zimeagiza kuwatoza wazazi michango ya maji, umeme na mlinzi ambayo imekatazwa na serikali.

Alisema kuwa Bw. Kalinga amevuliwa madaraka yake baada ya kubainika kuwa ameshindwa kuwasimamia watumishi walio chini yake hadi kusababisha kuandika barua na kusambaza kwa walimu wakuu wa shule za msingi katika manispaa ya Dodoma ambayo inatofautiana na maelezo ya serikali yaliyopo kwenye mwongozo.

Mbali na Kapinga, Waziri Simbachawene pia alimsimamisha Ofisa elimu vifaa na takwimu-wa msingi katika Manispaa hiyo, Josephine Akimu kwa kudharau maelekezo ya kiongozi wake na kusaini barua kwa niaba ya mkurugenzi huku akitumia jina la Ofisa Elimu, Scola Kapinga ambaye pia amepewa onyo kali.

Sababu za kuwavua madaraka watumishi hao ni kutokana na kuandika barua yenye kumbukumbu HMD/ED/50/2/VOL 11/61 ya Januari 17, mwaka huu iliyosambazwa kwa walimu wakuu wote wakitakiwa kuchangisha michango katika shule za msingi wakati Serikali ilishazuia.

Barua hiyo ilikuwa na maelekezo ya kuwataka walimu wakuu kuchangisha michango ya maji, mlinzi na umeme, jambo ambalo lilimfanya waziri kufanya safari ya kushtukiza Shule ya Msingi Dodoma Makulu, na kujionea michango hiyo lakini akabaini kulikuwa na barua za maelekezo kutoka ofisi ya mkurugenzi.

“Ieleweke kuwa uchangiaji ulioelekezwa katika barua ya mkurugenzi ni kinyume na maelekezo ya Rais John Magufuli, sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014 ibara ya 3.1.5 na ilani ya Uchaguzi ya CCM ibara ya 52 (a) ya mwaka 2015 ya kutoa elimu bure bila ya malipo,” alisema Simbachawene.

Alisema maelekezo ya maofisa hao ni kinyume na mwongozo namba DB.297/507/01/39 wa Desemba 28, 2015 uliotolewa na ofisi ya Tamisemi kwa makatibu Tawala wa mikoa, wakurugenzi wa majiji, manispaa na halmashauri zote kuhusu matumizi ya fedha za ruzuku ya uendeshaji wa shule za msingi za Serikali katika kutekeleza kaulimbiu ya elimu bure.

Kampuni Ya UDA Yakanusha Kufilisika

$
0
0

Kumekuwepo na taarifa za uwongo kwenye vyombo vya habari, hasa kijarida cha Dira ya Mtanzania, na mitandao ya kijamii kuhusu uongo kuwa kufilisika kwa Shirika la Usafiri Dar Es Salaam (UDA) Limited.

Menejimenti ya Shirika la Usafiri Dar Es Salaam inakanusha uwongo huo kuwa UDA haijafilisika na haina dalili zozote za kufilisika isipokuwa ni Shirika  namba moja nchini na Afrika Mashariki na Kati linalokua kwa kasi ya ajabu kimaendeleo na kibiashara.

Zifuatazo ni takwimu zinazodhihirisha ukweli huu:
  1. UDA imeongeza idadi ya mabasi kutoka mabasi 7 makukuu na mabovu Mwaka 2012 na kufikia takribani mabasi 400 mwaka 2015 yakiwemo mabasi 255 ya kawaida na mabasi makubwa - Hercalus, mapya na ya kisasa kabisa duniani (ya BRT) 140.
  2. Ndani ya miaka 3, kampuni ya UDA imekuwa kwa zaidi ya asilimia 5,000
  3. Kampuni hii imeweza kufanya maandalizi yote ya kuwezesha kuendesha mradi wa mabasi yaendayo haraka (DART Project) kwa ufanisi mkubwa. Mbali na kununua mabasi, kampuni imeweze kununua mtambo bora na wa kisasa kabisa duniani wa kukusanya nauli na kuongezea mabasi (Intelligent Transportation System – ITS) wenye thamani kubwa kutoka Ubelgiji na Ujerumani. Vile vile kampuni imeweza kusaili na kufundisha madereva wa Kitanzania zaidi ya 300 na kuwaajiri kwa ajiri ya kuendesha mradi wa mabasi yaendayo haraka (DART Project)
  4. Kampuni imejenga karakana bora na imara na kununua vitendea kazi vya kisasa kwa ajiri ya mabasi yake ya kawaida na mwendo haraka.
  5. Kampuni imepeleka watendaji wake kwenye miradi mbalimbali ya BRT duniani ili kupata uzoefu wa kuwawezesha kuendesha mradi wa mabasi yaendayo haraka (DART Project) kwa ufanisi. Vile vile Kampuni imeweza kuajiri wataalam kutoka nje (expatriates) kwa ajiri kuongezea nguvu wataalam wake wa ndani.
Kwa takwimu chache hizo hapo juu, Kampuni ya UDA ni namba moja Afrika kwenye sekta ya usafirishaji wa abiria barabarani kwa idadi ya watu inaosafirisha, idadi ya mabasi na ubora wa menejimenti.

Mafanikio haya ya Kampuni ya UDA yanatokana na umahiri wa uendeshaji kutoka Simon Group chini Uongozi thabiti wa Mwenyekiti wake Ndugu Robert Simon Kisena na si vinginevyo, kama washindani wetu wavyojaribu kutuchafua kwamba kuna wanasiasa nyuma yake.

Tunawataka washindani wetu waache tabia ya fisi ya kumfuata mtu anayetembea kwa haraka wakidhani atandondosha mkono wapate kitoweo vinginevyo watakufa njaa.

Imetolewa na Uongozi wa SHIRIKA LA USAFIRI DAR ES SALAAM (UDA) LIMITED

Mwanafunzi Wa Chuo Cha IFM Afikishwa Mahakamani Kwa Kumwingiza Mtoto Vidole Sehemu Za Siri

$
0
0

Mwanafunzi  wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Mussa Msafiri (23), alipandishwa kizimbani   katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni jana akituhumiwa kumwingizia vidole sehemu za siri mtoto  mwenye umri wa miaka minne.

Mbele ya Hakimu Issa Kasailo, Wakili wa Serikali, Matarasa Maharagande, alidai  mtuhumiwa alitenda kosa hilo   Januari 7 mwaka huu maeneo ya Sinza alikokuwa anaishi mwanafunzi huyo.

“Mtuhumiwa ulitenda kosa hilo wakati ukitambua kwamba ni kinyume cha sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alidai wakili.
 
Baada ya maelezo hayo mtuhumiwa alikana kutenda kosa hilo na upelelezi  unaendelea.

Hakimu Kasailo alisema   shitaka hilo linadhaminika hivyo alimtaka mtuhumiwa kuwa na wadhamini wawili waaminifu watakaoweka saini ya maandishi ya Sh milioni tano kwa kila mmoja.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Febuari 27 mwaka huu na mtuhumiwa aliachiwa huru baada ya kutimiza masharti ya dhamana.

Viewing all 45270 articles
Browse latest View live




Latest Images