Quantcast
Channel: MPEKUZI
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live

Benard Membe Akaribishwa CHADEMA

$
0
0

Waziri wa zamani wa Mamboya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe amekaribishwa kujiunga na Chama Cga Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ikiwa ni siku chache tangu atoe maoni yake akiikosoa serikali ya Rais John Magufuli.

Mwanasiasa huyo mkongwe amekaribishwa na Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Boniface Jacob ambaye alimshawishi kwa kutumia mifano ya wanasiasa wakongwe waliokuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), waliohamia Chadema na Ukawa kwa ujumla akiwemo Edward Lowassa, Frederick Sumaye na Kingunge Ngombale Mwiru.

Wiki iliyopita Membe alinukuliwa akimkosoa Dk Magufuli katika maeneo kadhaa, likiwamo la kubana matumizi, kudhibiti safari za nje na uteuzi wa Baraza la Mawaziri.

Jana, meya huyo kutoka Chadema alisema watu wanamshangaa Membe na kumshambulia siyo kwa sababu amesema mambo ya ajabu, ila yeye si mtu sahihi wa kutoa kauli hiyo.

“Watu hawashangai alichosema (Membe) kwa sababu siyo hoja ngeni, zimesemwa sana na wapinzani. Wanachoshangaa ni yeye (Membe) kusema hayo. Hafanani na hoja anazoziongea,” alisema.

Jacob ambaye alikuwa diwani katika manispaa hiyo katika Serikali ya Awamu ya Nne alisema, hoja zilizotolewa na Membe ni nzuri na kama zingetolewa na mpinzani zingeonekana zina mashiko zaidi.

"Asiwe vuguvugu, hicho ndicho kinachompa shida. Kama anataka kuja huku asiwe na wasiwasi chama changu kitampokea na hata hayo anayoyaongea yatakuwa na mantiki na watu watamsikiliza kwa sababu ni upinzani,” alisema na kuongeza;

“Avuke moja kwa moja kama walivyofanya akina Kingunge (Ngombale Mwiru), (Edward) Lowassa, na (Frederick) Sumaye kuhamia upinzani.”

Jacob alisema Sumaye na Lowassa ambao waliwahi kuwa mawaziri wakuu na Kingunge aliyekuwa kada mkongwe wa CCM, walikuwa viongozi wa ngazi za juu, lakini walihamia upande wa pili (upinzani) na sasa wanaisimamia na kuikosa Serikali kwa uhuru.

“Asiwe mwoga kwamba ataishi maisha gani, Sumaye na Lowassa wamekuwa mawaziri wakuu wakaondoka na maisha yanaendelea.”

Hata hivyo, Jacob alisema Membe hakupaswa kukosoa sera ya Rais Magufuli ya matumizi na Rais kudhibiti safari za nje, kwa sababu yeye amenufaika nayo.

“Nadhani hakuwa mtu sahihi kusema hayo, alipaswa kwanza kumtafuta mtu mwingine aseme halafu yeye afuate baadaye, lakini kuanza kusema yeye moja kwa moja wakati alikuwa ananufaika na anachopinga Rais, anaonekana anamwonea wivu na mgongano wa masilahi.

“Sasa anapoanza yeye kujibu inashangaza. Kwa sababu yeye alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje, iliyokuwa inafanya matumizi makubwa halafu unakosoa unaonekana kabisa unaonyesha kuna mgongano wa masilahi,” alisema na kuongeza:

Jacob alisema kwa mpinzani kusema hivyo angeonekana anataka kumuwajibisha Rais ili hayo mambo yaangaliwe kwa kina zaidi.

Alitoa mfano wa waziri wa zamani, Dk Makongoro Mahanga na kusema alipoikosa Serikali hakushambuliwa kwa sababu alishahama kutoka CCM na sasa yupo upinzani.

“Alipozungumzia suala la matumizi ya ardhi, Serikali haikujibu ilikaa kimya kwa sababu aliyeongea ni mtu sahihi,” alisema na kuongeza.

" Kwanza alikuwa kwenye Baraza la Mawaziri na pili hivi sasa yupo kwenye upande wa kuishambulia na kuikosoa Serikali na kuiwajibisha.”

Membe Azungumzia Mpango wa Kustaafu Siasa..... Aanza Kuandika Vitabu Kama Samwel Sitta

$
0
0

Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe amesema hana mpango wa kustaafu siasa kwa sababu haina mwisho.

Pia, amesema kwa sasa anafanya kazi ya uandishi wa vitabu kwa lengo la kuwashirikisha na kuwarithisha Watanzania mazuri aliyonayo baada ya utumishi wake wa kisiasa wa miaka 35.

Amesema anaandaa vitabu vinne vyenye maudhui tofauti. “Hilo la kuandika vitabu nimeshalianza, nina vitabu zaidi ya 265 nimehifadhi na kuvisoma katika maktaba yangu kuhusu mambo mbalimbali ya dunia, nami ninatengeneza vinne, muda ukifika nitatoa taarifa,” alisema Membe.

Waziri huyo aliyehudumu katika Serikali ya Awamu ya Nne katika wizara hiyo kwa miaka tisa, alisema kati ya vitabu anavyoandika viwili vitatoka mwaka huu.

“Kimoja cha maisha yangu, ni vitabu vizuri sana, nimekuwa mwanasiasa kwa miaka 35, nimejihusisha zaidi na masuala ya utatuzi wa migogoro barani Afrika... kitabu kingine kitahusu migogoro na Serikali za Afrika,” alisema.

Alitaja vingine kuwa ni kuhusu uongozi na cha mwisho kitahusu siasa za Tanzania kinachowalenga zaidi vijana kikieleza namna nchi inavyoweza kulinda heshima yake duniani.

“Nchi hii tumeirithi kutoka kwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere. Yeye alikuwa mwana ukombozi halisi. Mwaka 1963 alianzisha harakati za ukombozi, Tanzania ikawa makao makuu ya nchi zote zinazopigania uhuru. Vyama vya ukombozi vikaweka makao makuu yake hapa, vingine vikaanzia harakati zake hapa,” alisema Membe.

Alisema sifa ya kwanza ya Tanzania duniani ni ukombozi na ilikuwa mwenyekiti wa nchi tano zilizokuwa mstari wa mbele katika ukombozi Kusini mwa Afrika.

Akizungumzia kuhusu hatima yake kisiasa, Membe aliyewania kuteuliwa kugombea urais kwa tiketi ya CCM kabla jina la Dk John Magufuli ambaye sasa ndiye rais kuteuliwa, alisisitiza kuwa siasa haina mwisho.

“Tafsiri ya siasa ni mchakato wa namna ya kuyashughulikia matatizo ya watu, usipoyashughulikia vizuri, utaibadilisha siasa kutoka kwenye amani kwenda kwenye mtafaruku,” alisema.

Akimnukuu aliyekuwa Rais wa Marekani, Bill Clinton, Membe alisema mwanasiasa mzuri duniani ni yule aliyeondoka kwa heshima na anayeheshimu familia yake.

Membe aliwataka wanasiasa walioshindwa katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 kuacha kujipenyeza na kuendeleza ubabe wa kisiasa, akisema kufanya hivyo ni sawa na upuuzi, badala yake wasubiri muda wao watakapochaguliwa.    

Vyama Vya Siasa Vyaaswa Kushiriki Uchaguzi Wa Zanzibar

$
0
0
Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Mhe.Jaji Francis Mutungi ameviasa Vyama vya Siasa kushiriki chaguzi zinazotangazwa na tume za uchaguzi nchini ikiwemo uchaguzi wa Machi 20, mwaka 2016 uliotangzwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).

Kwa mujibu wa barua iliyotolewa  kwa vyama hivyo leo na kusainiwa na  Jaji Mutungi  ilieleza kwamba,  kimsingi Sheria ya Vyama Vya Siasa Sura ya 258 inasisitiza vyama vya siasa  kushiriki katika chaguzi zote zinazotangazwa na tume za uchaguzi ili kufikia malengo yake ya kushika dola.

“Katika nchi kidemokrasia na kwa chama cha siasa kinachoamini misingi ya kidemorasia ya vyama vingi vya siasa, hakuna njia mbadala kwa chama cha siasa kufikia malengo yake zaidi ya kushiriki uchaguzi.

“Ni wajibu wa kila chama cha siasa nchini  kama wakala wa kukuza demokrasia, utawala wa sheria na amani ya nchi, kuwa wa kwanza kutii matamko ya kisheria yanayotolewa na mamlaka  husika .

" Kama kuna chama cha siasa hakiridhiki au kimekwazwa kwa njia moja au nyingine na suala lolote kuhusu masuala ya uchaguzi, njia stahiki na inayonyesha ukomavu wa kisiasa si kuhamasisha kugomea uchaguzi, bali ni vema kikafuata utaratibu uliowekwa katika sheria za uchaguzi,” alisema Jaji Mutungi.

Aidha Msajili huyo amesema kwa mujibu wa Sheria za Nchi bado ni suala la hiari kwa chama kushiriki uchaguzi lakini utashi huo wa hiari unaenda sanjari na umuhimu wa kila chama kushiriki kila uchaguzi unaotangazwa na tume ya uchaguzi.

“Hivyo ni muhimu basi kila chama cha siasa kuelewa kuwa,uchaguzi ni kipimo cha uhai wa chama cha siasa. Chama cha siasa kisiposhiriki uchaguzi kinaua uhai wake katika mtazamo wa harakati za kisiasa,” alisisitiza.

Aliongeza kwamba hivi sasa, mfumo wa demokrasia ya vyama vingi na vyama vya siasa vimeimarika, hivyo sio vyema kwa chama cha siasa kujirudisha nyuma au kujiua kisiasa kwa kutoshiriki uchaguzi wakati kina uwezo wa kufanya hivyo.

Taarifa Ya Ufafanuzi Kuhusu Malipo Ya Umeme Kwa Askari Polisi

$
0
0

Katika gazeti la Tanzania Daima ukurasa wa 5, toleo namba 4070 la tarehe 25 Januari, 2016, lilichapisha habari yenye kichwa cha habari Polisi “waisoma” namba. Sehemu ya taarifa hiyo inaeleza kuwa askari Polisi hivi sasa wanatakiwa kujilipia gharama za umeme.

Jeshi la Polisi nchini, linakanusha vikali taarifa hiyo kwamba siyo sahihi. Ukweli ni kwamba askari polisi wote makambini wanalipiwa umeme na serikali, ikiwemo wale ambao nyumba zao zimefungiwa luku kama njia ya kuboresha huduma na matumizi sahihi ya umeme. 

Baada ya askari kununua umeme hutakiwa kuwasilisha stakabadhi ya malipo ya umeme kwa ajili ya kurudishiwa kiasi cha fedha walichonunulia umeme kila mwisho wa mwezi.

Aidha, habari iliyochapishwa na Tanzania Daima ililenga kupotosha umma na mwandishi wa habari hiyo hakutafuta ufafanuzi kutoka kwenye mamlaka husika.

Kufuatia hali hiyo, Jeshi la Polisi nchini, linamtaka mhariri wa gazeti la Tanzania Daima na waandishi wake wa habari kuwa makini na habari wanazoziandika hasusani taarifa zinazohusu vyombo vya ulinzi na usalama ili kuepuka madhara ya kiusalama yanayoweza kutokea kutokana na habari wanazozitoa zisizo na usahihi.

Imetolewa na:-
Advera Bulimba -SSP
Msemaji wa Jeshi la Polisi,
Makao Makuu.

TRA Yawaomba Wananchi Kutoa Ushirikiano

$
0
0

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yawaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa za Maafisa wanaofanya kazi kinyume na maadili.

Akiongea na mwandishi wa habari hii leo Jijini Dar es salaam Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi Richard Kayombo amesema kuwa TRA ina Idara Maalumu ijulikanayo kama Idara ya Mambo ya Ndani ya TRA ambayo inashughulika na kufuatilia maadili ya watumishi wa sekta hiyo nchi nzima.

“Tunawaomba wananchi kushirikiana na Idara ya Mambo ya Ndani ya TRA kwa kuwapa taarifa juu ya maafisa wa TRA wanaokwenda kinyume na Maadili ya Utumishi wa Umma,”alisema Kayombo.

Mkurugenzi Kayombo ameongeza kuwa wananchi wanaweza kutoa taarifa kwa kupiga simu kwa namba 0689122515 au kwa kutuma ujumbe mfupi kwa simu namba 0689122516  na kuwahakikishia kuwa taarifa zao zitakua zimefika sehemu husika na zitafanyiwa kazi.

Aidha Kayombo amependa kuwatoa wasiwasi wananchi kuwa namba hizo ni za siri na hakuna mwananchi atakayepata tatizo lolote kwa kutoa taarifa za maafisa wasio na maadili.

TRA kupitia Idara yake ya Mambo ya Ndani imepokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi juu ya watumishi wa TRA wanaoenda kinyume na maadili, wameyafanyia uchunguzi na baadhi ya watumishi wamefukuzwa na wengine kupewa adhabu kali.

Chadema Yaishushia Tuhuma CCM Kwa Udhalilishaji

$
0
0

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimelaani vitendo vya vurugu vinavyochochewa na viongozi wa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Kauli hiyo imetokana na kitendo kilichotokea jana katika Halmashauri ya Kilombero kwenye uchaguzi wa mwenyekiti wa halmashauri hiyo.

Mbunge wa Kilombero, Peter Lijualikali aliondolewa kwenye ukumbu wa mkutano kwa kukokotwa na polisi baada ya aliyekuwa mwenyekiti wa kikao hicho, Azimina Mbilinyi kutoa amri atolewe nje.

Sababu za kutolewa mbunge huyo zilielezwa kuwa hakupaswa kuwepo na kushiriki upigaji kura ambapo mwenyekiti huyo alidai amepokea maelekezo hayo kutoka kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene.

Akizungumza na waandishi wa habari leo kwenye Makao Makuu ya Chadema jijini Dar es Salaam, Kaimu Katibu Mkuu chama hicho, Salim Mwalimu amesema, kitendo alichofanyiwa Lijualikalini ni cha uzalilishaji.

“Naamini kwamba matukio yanayofanywa katika halmashauri ambazo Ukawa tumeshinda yanapangwa na CCM kwa kushirikiana na serikali yake.

“Kwanini matukio ya uzalilishaji yafanyike kwenye maeneo ambayo sisi tumeshinda na si maeneo ambayo wao wameshinda?” amehoji Mwalim.

Mwalim amesema, Halmashauri ya Kilombero inaongozwa na Ukawa kutoka na kuwa na madiwani na wabunge wengi kuliko CCM na kwamba uchaguzi huo umeghairishwa kwa mara ya tatu. CCM wana madiwani pamoja na wabunge viti maalumu 18 huku Ukawa wakiwa na 20.

“Pamoja na ushindi wa Ukawa kuonekana waziwazi lakini bado CCM wanaleta filigisufiligisu ya kuleta hata wabunge wa nje ilimradi tu washinde.

“Hawataweza kutushinda hata kwanini maana hata sisi tukipeleka wabunge toka nje bado tutawapita. Na hiyo ni ishara ya kutuogopa,” amesema Mwalimu.

Hata hivyo, Mwalim amesema kutokana na kitendo alichofanyiwa mbunge huyo jana wanaitaka serikali kulichukulia uzito suala hilo na kuhakikisha mkurugenzi huyo aliyetoa amri kwa polisi kutumia mabavu kumtoa nje mbunge huyo achukuliwe hatua za kinidhamu.

Pia, wamemtaka mkurugenzi huyo ambaye alikuwa mwenyekiti wa kikao hicho kuonesha barua aliyotumiwa na Simbachawene ya kutoa amri ya kumtoa nje mbunge huyo.

Mbali na hilo, pia ametoa rai kwa serikali kufuata misingi bora ya uongozi haswa katika kusimamia masuala ya nayowahusu wananchi hususani suala la Meya wa Jiji ambalo bado halijafanyika.

Idara Ya Uhamiaji Yaja Na Hati Mbili Za Muda Mfupi Kwa Wageni.

$
0
0

Idara ya Uhamiaji imeanzisha hati mbili ambazo zitatumika kwa wageni wanaoingia na wanaotoka nje na kuondokana na hati ya awali ya muda mfupi (CTA).

Akizungumza leo na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Msemaji Mkuu Idara ya Uhamiaji, Naibu Kamishina Abbas Irovya amesema kuwa hati ya kwanza ni ile ya muda atayeingia nchini kwa muda usiozidi siku 90 na baada hapo anatakiwa kurudi alikotoka.

Naibu Kamishina, Irovya amesema kuwa wanaoingia kwa ajili ya kutoa utalaam wafanye hivyo kwa kuwa na hati hiyo na sio kuwa na ajira katika sehemu hizo.

Amesema hati ya pili ni ile ile katika nchi zilizoingia makubaliano ya kutumia viza, watatumia ya muda mfupi kwa kukaa kwa muda huo.

Aidha amesema wananchi watambue kuwepo kwa huduma hiyo ikiwa na kutoa ushirikiano pale wanapowaona watu ambao wanatumia hati ya muda lakini wanaendelea.

Irovya amesema hati hizo mbili hazihusiani kwa wale wanaoingia nchini kwa kutafuta ajira na wakitaka kufanya hivyo wanatakiwa kuomba kibali cha kazi kutoka idara ya kazi.

CUF Kuandamana Kesho

$
0
0

VIJANA wa Chama cha Wananchi kupitia jumuiya yao (JUVI-CUF) wameweka msimamo kuwa ‘iwe iwavyo’ watafanya maandamano kesho visiwani humo kwa kuwa ni haki yao kufanya hivyo licha ya Jeshi la Polisi kupinga.

Maandamano hayo yameelezwa kuwa ni sehemu kumbukumbu ya Wazanzibari waliouawa mwaka 2000 kutokana na vurugu za kisiasa zilizotokea chini ya Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Maandamano hayo yametangazwa ikiwa ni siku chache baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha kutangaza tarehe 20 Machi mwaka huu kuwa siku ya kurudia uchaguzi visiwani humo.

Jecha alifuta matokeo ya uchaguzi mkuu visiwani humo uliofanyika tarehe 25 Oktoba mwaka jana kwa madai ya kuwepo kwa kasoro mbalimbali jambo ambalo lilipingwa na CUF, taasisi za kiraia na baadhi ya makada wa CCM.

JUVI-CUF wamepanga kufanya maandamano makubwa visiwani humo kwa lengo la kupinga dhuluma hiyo licha ya Jeshi la Polisi kuyagomea.

Wameeleza kuwa maandamano hayo watayafanya ili kuieleza dunia kwamba, Zanzibar haki inaminywa na kwamba, maandamano hayo yatakakuwa ujumbe mahsusi kwa wapenda demokrasia duniani.

Vijana hao wamesema kuwa, hawawezi kuona haki yao inapokwa na serikali kwa maslahi ya CCM na kwamba, maandamano hayo yatafanyika visiwani humo kama ilivyopangwa.

Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa JUVI-CUF, Abeid Ali amesema kuwa, wananchi wa visiwa hivyo hawatokoma kudai haki yao mpaka pale itakaposimama.

Mkurugenzi huyo ameeleza kwamba, wana imani kuwa si risasi wala mizinga ambayo inaweza kusimamisha haki visiwani humo na kwamba, watapigania haki hata kama wengine watauawa.

Kiongozi huyo amekumbushia mauaji yaliyofanywa na Serikali ya Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa baada ya Uchaguzi Mkuu 2000 na kwamba, wananchi hawajaingia woga wala kurudi nyuma kudai haki yao.

“Sisi ni raia wakizanzibari, tuna uhuru wa kuandamana kwani CCM waliachiwa kuandamana na ulinzi wakapewa, na sisi tuna haki ya kufanya maandamano,” amesema Ali.

Amesema kuwa, maandamano hayo yatafanyika kuanzia Mtendeni kwenda Mnazimmoja na kumalizikia kwenye viwanja vya Maisara.

Mbowe ahoji askari wa Bara kupiga kura Z'bar.

$
0
0

MBUNGE wa Hai na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema ), Freeman Mbowe ameibana serikali leo na kutaka ieleze ni kwanini askari wa jeshi kutoka bara wanapelekwa Zanzibar kwa ajili ya kupiga kura wakati wa kipindi cha uchaguzi jambo ambalo linaweza kuzua vurugu.

Mbowe alitoa kauli hiyo bungeni alipokuwa akiuliza swali la nyongeza kwa kutaka kujua ni lini serikali itaacha kufanya mchezo huo ambao unaweza kusababisha vurugu.

Pia Mbowe alitaka kujua kama serikali inatambua kuwepo kwa vitendo hivyo vya askari kutumika kutoka Bara na kama inajua jambo hilo na ni hatua gani zinafanyika ili kukomesha vitendo hivyo ambavyo vinavyoweza kusababisha kuwepo kwa vurugu za kisiasa.

Awali katika swali la msingi la mbunge wa Shaurimoyo Mattar Ali Salum (CCM) alitaka kujua serikali ina mapango gani madhubuti wa utoaji ajira kwa upande wa Tanzania Zanzibar.

Katika swali hilo la msingi pia Salum, alitaka kujua ni asilimia ngapi ya vijana wanaoajiriwa kutoka upande wa Zanzibar na ni kwanini utoaji wa ajira katika Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa upande wa Zanzibar usijielekeze kwenye kikosi cha Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) tu.

Akijibu maswali hayo Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi akianza na swali la nyongeza la Mbowe amesema, majeshi yote ni vyombo vya Muungano .

Akizungumzia kupiga kura amesema utaratibu wa kupiga kura unafahamika na hivyo siyo rahisi askari wanaokwenda Zanzibar wanaweza kupiga kura bila kufuata utaratibu wa eneo husika.

Akijibu swali la msingi Dk. Mwinyi amesema jeshi la wananchi wa Tanzania lina utaratibu wa kuandikisha askari wake wapya kupitia makambi ya Jeshi la Kujenga Taifa.

Amesema Jeshi la Ulinzi la Wananchi halina wa Tanzania halina utaratibu wa kuandikisha vijana kwa kufuata asilimia bali ni vijana wanaokuwa na sifa zinazohitajika bila kujali anatoka pande gani ya Muungano.

Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Jumatano Ya Januari 27

Kampuni ya Lake Oil Yakamuliwa Bilioni 8.5 Kwa Kuingiza Mafuta Na Kukwepa Kodi.........Vigogo TRL,NIDA, Mikononi Mwa TAKUKURU

$
0
0

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (Takukuru), imetoa onyo kwa taasisi nyeti nne hapa nchini ikiwemo wanaohusika na matumizi ya fedha za Umma kufuata sheria, taratibu na kanuni.
 
Pia,Takukuru inashughulikia kukamilisha kesi kubwa 36, zinazowahusu watumishi wenye ushawishi na hadhi kubwa hapa nchini ambapo kati ya hizo zipo zilizokamilika na kupelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka.
 
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana , Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo, Valentino Mlowola alisema kumekuwepo na malalamiko mengi kwa wananchi kuwajulisha matendo ya rushwa na ufisadi yanayoendelea hapa nchini.
 
Alisema kutokana na hali ya wananchi kuona nia ya serikali ya awamu ya tano katika kushughulikia matatizo ya rushwa na ufisadi hapa nchini ametoa onyo kwa maofisa wa umma wanaofanya rushwa na ufisadi kuwa sehemu yao ya kazi na miradi ya kuwaingizia kipato.
 
“Natoa onyo kwa maofisa wa umma ambao wamefanya rushwa na ufisadi kuwa ni sehemu ya kazi zao na miradi ya kuwaingizia kipato, wajitafakari kabla hawajaamua kujihusisha na vitendo vya rushwa,”alisema.
 
Alisema  hawatasita kuchukua hatua kali za kisheria kwa watumishi watakaojiingiza katika kulihujumu taifa na wananchi kwani wananchi wanakiu ya kupata maendeleo na maisha bora na kuwataka watambue wananchi wa jana si wa leo kwani wamedhamiria kuunga mkono juhudi za serikali yao.
 
Mlowola alitoa onyo kwa maofisa maduhuli na watekelezaji wa jukumu la kukusanya kodi za wananchi kwa kutomuonea mtu haya kwa atakayejihusisha na ubadhirifu wa fedha na mali ya umma.
 
“Wakusanye kodi halali ya serikali kwa kufuata sheria, taratibu na Kanuni zinazowaongoza kukusanya kodi, tutachukua hatua stahiki pale kutakapokuwa na ukiukwaji wa sheria, taratibu na kanuni zilizopo,”alisema.
 
Pia, Mlowola alitoa onyo kwa watakaohusika kwenye matumizi ya fedha za umma kwamba wafuate sheria, taratibu na kanuni  zinazowaongoza kwani taasisi hiyo haitawavumilia watakaokiuka fedha za serikali isiyo halali.
 
Mbali na hilo, pia Kaimu huo alitoa onyo kwa watumishi wa umma wenye jukumu la kuhudumia mahitaji ya umma kwa kutojihusisha na rushwa kwa kutekeleza majukumu yao katika muda uliotakiwa, weledi na uaminifu.
 
Alisema taasisi hiyo haipo kwa lengo la maslahi ya watu wabadhilifu wa mali ya umma kwani uchunguzi wa kesi ya kuisababishia hasara serikali shilingi bilioni 8.5 kutokana na ukwepaji wa kodi wa kampuni ya Mafuta ya Lake Oil kwa kufanya udanganyifu wa kuuza mafuta ndani ya nchi Petrol lita 17,461,111.58 kwa kudanganya zilisafirishwa umefikia hatua nzuri.
 
“Takukuru imekamilisha shauri  hili na mtuhumiwa wamepewa miezi miwili kurejesha mikononi fedha zote .Tutawarudisha mahakamani endapo watashindwa kurejesha kiasi hicho,”alisema.
 
Alisema mbali na shauri hilo, wapo kwenye hatua nzuri ya kukamilisha ya uchunguzi wa kesi ya hati fungani ya malipo yaliyolipwa na kampuni ya Enterprise Growth Markert Advisor(EGMA), kiasi cha dola 6,000,000 kwa lengo la kuisaidai Tanzania kupata mkopo wa dola 600,000,000.
 
“Takukuru imebaini fedha hizo dola 6,000,000 zilitakatishwa na watumishi wa umma wasio waaminifu wakishirikiana na baadhi kutoka sekta binafsi huku wakijua fedha hizo wamezipata kwa njia haramu,”alisema.
 
Akizungumzia hatua aliyochukua rais, Dk. John Magufuli kwa kutengua uteuzi wa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa RAHCO, Mhandisi Benhadard Tito kwa tuhuma zinazomkabili tayari wanachunguza shirika hilo la reli.
 
Alisema kulikuwepo na ukiukwaji wa kuwapata wazabuni kwenye ujenzi wa reli ya kisasa ya kimataifa(Standard Gauge) unaosimamiwa na Shirika la Hodhi la Reli Nchini(RAHCO), watuhumiwa wamekamatwa akiwemo raia wa Kenya aliyekuwa kwenye mchakato huo, Kanji Muhando.
 
Kaimu huyo alisema shauri la kesi ya mabehewa ya kokoto 25 ya shirika la reili nchini (TRL), ya kukiuka sheria ya manunuzi ya umma Na.21/2004 pamoja na kanuni zake kutoka kampuni ya Hindustha Engineering and Industries Limited limekamilika.
 
“Uchunguzi umekamilika na tumeshapeleka kwa mkurugenzi wa Mashtaka kuomba kibali cha kuwafikisha watuhumiwa waliobainika kujihusisha na matendo ya rushwa na ukiukwaji wa sheria, taratibu na kanuni za ununuzi wa umma mahakamani,”alisema.
 
Alisema rais alijipa kazi ya kutumbua majipu hivyo aliwasihi watumishi wa taasisi hiyo kutumikia wananchi kwa weledi huku akibainisha tayari wanatekeleza azma na dhamira ya rais ya kupambana na rushwa.
 
Akitolea ufafanuzi swala la kumsubiri rais kutumbua majipu ndio taasisi hiyo ifanye ufafanuzi, Mlowola alisema taasisi hiyo imejipanga vilivyo tangu Novemba 20 mwaka jana wakati rais alipohutubia bungeni alipoonesha dhamira  na nia ya dhati ya kupambana na rushwa na ufisadi bila kumuonea mtu haya.
 
“Nitoe rai kwa wananchi kutoa taarifa ili tuweze kujua kabla hatujapigwa, tukiweza kuisaidia serikali kuokoa fedha kabla hatujapigwa zitasaidia wananchi  kutoa elimu bure, upatikanaji wa dawa na mishahara mizuri,”alisema.
 
Alisema tayari wameshaanza kuchunguza madai ya aliyekuwa mkurugenzi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), kwani tayari wapo hata viongozi wakubwa.
 
Akizungumzia maofisa takukuru waliofukuzwa kazi a rais baada ya kukiuka maagizo ya rais ya kupata kibali cha kusafiri nje, alisema maofisa hao walikwenda kwenye mkutano wa taasisi za kupambana na rushwa uliofanyika Congo-Kinshasa.

Hakimu Agoma Kujitoa Kesi ya Kulawiti

$
0
0

Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Said Mkasiwa amekataa kujitoa katika kesi ya kulawiti na kutuma picha kwenye mitandao ya kijamii inayowakabili washitakiwa Erick Kassira (39) na Juma Richard (31).

Mkasiwa alisema sababu zilizotolewa na washitakiwa hao kwamba wanatishwa na kulazimishwa kesi isikilizwe wakiwa wanaumwa, si za kisheria ambazo zitamfanya asiendelee kusikiliza shauri hilo.

Wakitoa pingamizi jana, washitakiwa hao walidai kuwa hakimu huyo anawalazimisha kusikiliza kesi wakiwa wanaumwa na kwamba anawakataa wadhamini ambao washitakiwa hao waliwapeleka mahakamani hapo.

Mshitakiwa Kassira alidai kuwa Januari 4, mwaka huu alimuandikia barua Hakimu huyo kumuomba asiendelee kusikiliza kesi hiyo, badala yake achague mwingine atakayeweza kusikiliza. 

Alidai kuwa hawana imani na hakimu huyo kwa kuwa anawapendelea zaidi upande wa mashitaka na kushindwa kuwasikiliza.

Hata hivyo, Hakimu huyo aliwaeleza washitakiwa hao kuwa sababu walizozitoa sio za kisheria na kwamba ataendelea kusikiliza shauri hilo. 

Wakati huo huo, shahidi wa tano katika kesi hiyo, Tegemea Chaula (52), mkazi wa Kiwalani na mhudumu wa nyumba ya kulala wageni ya Maembe iliyopo Yombo Kiwalani, alidai kuwa mlalamikaji alifika katika nyumba hiyo na kuulizia kama vyumba vipo.

Chaula alidai kuwa, Agosti 23, mwaka 2014 mlalamikaji aliingia saa 7:00 mchana ambapo alipatiwa chumba namba sita pamoja na funguo. 

Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Sylvia Mitanto, shahidi huyo alieleza kuwa anamfahamu mlalamikaji kwa muda mrefu kama mshauri wa masuala ya Ukimwi na kwamba alikuwa anapeleka wateja katika nyumba hiyo ya kulala wageni.

Alidai saa 12:00 jioni alimuona mlalamikaji akiwa katika mlango wa kutokea akiwa amevaa shati na taulo huku akiwa hajavaa viatu. 

“Aliniita na kuniulizia Meneja wa gesti hii, Mohamed Hamza, nilimuita na kuongozana kwa pamoja kwenda chumbani kwa mlalamikaji ambapo alikuwa anaonekana hana furaha,’’ alidai Chaula.

Viongozi wa UKAWA Kutoa Msimamo Wao Juu ya Suala la Zanzibar

$
0
0

UMOJA wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) umesema utatoa msimamo juu ya hali ya siasa ya Zanzibar baada ya kikao cha kamati tendaji kuketi na kutoa msimamo. Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe alisema hayo jana katika mkutano wake na waandishi wa habari mjini Dodoma.

Alisema walifanya mazungumzo ya mashauriano ya hali ya siasa ya Zanzibar, yaliyohudhuriwa na viongozi wa ngazi za juu wa nyama vya upinzani, wakiongozwa na aliyekuwa mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF, Maalim Seif Shariff Hamad na mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowasa.

“Januari 28 keshokutwa kutakuwa na kamati ya utendaji na kikao hicho, kitatoa msimamo wa kitu gani kifanyike kuhusiana na siasa za Zanzibar,” alisema. Pia, alisema Baraza Kuu la Chama cha Wananchi (CUF), litatoa msimamo wake kuhusu suala la Zanzibar.

Mbunge wa Malindi kwa tiketi ya CUF, Ally Salehe alisema wanaamini Rais John Magufuli, anaweza kuingilia mgogoro wa Zanzibar na kuupatia ufumbuzi.

Andrew Chenge Achaguliwa Kuwa Mwenyekiti wa Bunge.....Asema Suala La Escrow Likirudi Bungeni Atakaa Pembeni

$
0
0

MBUNGE wa Bariadi, Andrew Chenge na wabunge wawili wa Viti Maalumu, Dk Mary Mwanjelwa na Najma Giga, wamechaguliwa kuwa Wenyeviti wa Bunge kwa kipindi cha miaka miwili na nusu.

Uchaguzi huo ulifanyika jana baada ya majina yao kupendekezwa na Kamati ya Uongozi na kuyawasilisha bungeni kwa ajili ya uchaguzi.

 Katika uchaguzi huo, uliotanguliwa na wabunge hao kujieleza mbele ya wenzao na kuulizwa maswali, sakata la Tegeta Escrow liliibuka baada ya Chenge kujieleza.

“Katika Bunge lililopita, chama chako na wabunge walikuwajibisha kwa kashfa ya Escrow, je, siku ukiliongoza Bunge na hoja ikarudi ndani uko tayari kuisimamia,” Mbunge wa Ndanda, Cecil Mwambe (Chadema) alimuuliza Chenge.

Akijibu swali hilo, Chenge alisema Bunge linaongozwa na Kanuni na itakapokuja mbele ya Bunge au kwenye Kamati, ikaonekana kuna maslahi ama inamhusu mbunge, ni busara kuzingatia kanuni nafasi hiyo ikaachwa mwingine aifanye shughuli za Bunge zisiwe na makandokando ya aina yoyote.

“Naona niishie hapo, ningeweza kusema zaidi ya hapo,” alisema Chenge ambaye alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa zaidi ya miaka 10 na pia Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti ya Bunge la 10 kabla ya kujiuzulu kutokana na sakata la Tegeta Escrow.

Awali akijieleza Chenge ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo, alisema “napenda niliahidi Bunge na Watanzania kwa ujumla, kwamba hii ni dhamana nzito ya kumsaidia Spika na Naibu.

“Lakini niwahakikishie nitatekeleza jukumu hilo kwa uadilifu, na kwa uaminifu ili nitende haki inayoonekana na bila chuki, wala upendeleo wowote kwa faida ya kujenga misingi bora ya Bunge hili lakini pia kwa kuwatumikia Watanzania wote,” alisema.

Kuhusu swali la Mbunge wa Nsimbo, Richard Mbogo (CCM) aliyetaka kufahamu ni namna gani Chenge atadhibiti matumizi ya lugha ya kuudhi au kudhalilisha wengine, Chenge alisema Kanuni za Bunge kama zilivyo sheria za nchi, zinakata pande zote kama ilivyo msumeno.

Alisema ikithibitika kwamba mbunge amekiuka kanuni, kiti kitazingatia baada ya kupima kauli na maelezo aliyotoa bungeni.

“Baada ya kupima, tuhakikishe kwamba tunayosema humu bungeni yawe ya kweli, kweli tupu yasiwe ya uongo,” alisisitiza.

Mwanjelwa ambaye ni Mbunge wa Viti Maalumu mkoani Mbeya, katika kujieleza mbele ya wabunge, aliomba wamwamini na kuahidi kuwatumikia bila kujali itikadi kwa faida ya wananchi wote.

Mwanjelwa alikiri kwamba Bunge hili lina changamoto nyingi, lakini atakachozingatia ni utaifa kwanza. 

Najma, ambaye kitaaluma ni Mwanasheria, aliahidi kuwa msaada mkubwa kwa Spika. Aliahidi kuwa atahakikisha anaweka maslahi ya taifa mbele kwa kutoa haki sawa kwa wabunge wote bila kujali vyama vyao.

Spika wa Bunge, Job Ndugai alihoji kwa pamoja wanaoafiki mapendekezo ya Kamati ya Uongozi, ndipo wabunge walio wengi wakaridhia Chenge, Mwanjelwa na Najma wawe wenyeviti. Wenyeviti wa Bunge hufanya kazi wakati ambao Spika au Naibu Spika wakiwa hawapo bungeni.

Katika Bunge la 10, wenyeviti walikuwa Mussa Azzan Zungu, Kidawa Himid Saleh, Lediana Mng’ong’o, Muhammed Seif Khatib, Sylvester Masele na Jenista Mhagama.

Kwa mujibu wa Ndugai, Kamati yau Uongozi imejiwekea utaratibu wa kupendekeza majina na ilipokutana chini ya uenyekiti wa spika, iliamua kuwapendekeza wabunge hao watatu ambao wote ni kutoka CCM.

Amuua Mwenzake Kwa Kipigo Baada Ya Kumkuta Akimtongoza Dada Yake

$
0
0

Mkazi wa kijiji cha Kalovya – Inyonga wilayani Mlele, Ramadhani Ally (20) amefariki dunia akipatiwa matibabu hospitalini baada kupigwa  na  kijana  mwenzake.

Akizungumzia  tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Dhahri Kidavashari amesema  kuwa Ramadhani alifikwa na umauti baada ya kujeruhiwa na kijana mwenzake Ntema Kabembenya( 26), mkazi wa kijiji cha Ipwaga. 

Kidavashari amesema tukio hilo  lilitokea Januari 22, mwaka huu saa 12:55 jioni ambapo Ntema alimkuta Ramadhani (marehemu) akimtongoza dada yake (Ntemwa) mwenye umri wa miaka 12 (jina limehifadhiwa).

“Ntemwa alikasirishwa na kitendo cha Ramadhani kumtongoza dada yake mwenye umri wa miaka 12, alimshambulia Ramadhani kwa kumpiga na fimbo na kumjeruhi vibaya,” alieleza Kamanda Kidavashari.

Inadaiwa Ramadhani alikimbizwa katika Hospitali ya wilaya ya Mlele kwa matibabu lakini alifariki dunia siku iliyofuata akiwa anatibiwa. 

Kwa mujibu wa Kidavashari, mtuhumiwa anashikiliwa na Jeshi la Polisi ambapo anatarajiwa kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma inayomkabili.

Hotel ya Mtoto wa Amani Karume yateketea kwa moto, Vijana wawili wahusishwa

$
0
0

Moto mkubwa umeteketeza hoteli ya kitalii ya Konokono Beach Resort iliyoko Michamvi mkoa wa kusini Unguja, inayomilikiwa na mtoto wa rais wa zamani wa Zanzibar, Amina Karume pamoja na wawekezaji wawili kutoka nje ya nchi.

Kamanda wa polisi mkoa wa Kusini Unguja, Juma Saadi amesema kuwa moto huo uliteketeza nyumba tatu na mgahawa mmoja katika hoteli hiyo, ni watu wawili waliokuwa wakichoma nyasi karibu na hotel hiyo. Aliwataja vijana hao kuwa ni Meshak Amos Elisha na Mohamed Abdallah Hassan.

Kamanda Saadi aliwataka wananchi kupuuza habari zilizoenea zinazohusisha tukio hilo na mambo ya kisiasa, husasan vyombo vya habari vya kimataifa vilivyoripoti habari hiyo.

“Wakati wa kuchoma moto ndani ya uzio huo, ulizuka upepo mkali majira ya saa tano na nusu na kusababisha nyumba moja ya makuti katika hoteli ile kushika moto na kusababisha hasara hiyo,” kamanda Saadi alifafanua.

Kikosi cha zima moto na uokoaji kilifika katika eneo hilo na kufanya kazi za kuzima moto huo.

Waziri Kitwanga Aanika Siri Ya Kutumbuliwa Kwa Vigogo wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida)

$
0
0

Baadhi ya wafanyakazi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) waliokumbwa na ‘operesheni tumbua majipu’, walikutwa na mali nyingi “kupita maelezo”, kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga.

Operesheni hiyo, ambayo inatekelezwa tangu kuingia madarakani kwa Serikali ya Awamu ya Tano, juzi ilimkumba Dickson Maimu, ambaye alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Nida, Joseph Makani (Mkurugenzi wa Tehama), Rahel Mapande (Ofisa Ugavi Mkuu), Sabrina Nyoni (Mkurugenzi wa Sheria) na George Ntalima ambaye ni Ofisa Usafirishaji.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga alisema hatua ya kutengua na kusimamisha watumishi hao imechukuliwa baada ya uchunguzi wa hali ya juu kwenye mamlaka hiyo.

Ingawa hakutana kuingia kwa undani akihofia kuingilia uchunguzi, Kitwanga alisema katika uchunguzi wao, moja ya hatua ilikuwa ni kukamata mali za wafanyakazi hao wa  Nida.

“Walipoulizwa, walisema wamepata mali hizo kutokana na mikopo, hivyo uchunguzi utajielekeza katika kulinganisha kiwango cha mikopo na mali walizonazo,” alisema.

Waziri huyo alisema uchunguzi zaidi unajielekeza katika ni jinsi gani Sh180 bilioni zilitumika kusajili watu milioni sita tu na kati yao kuwapata vitambulisho watu milioni 2.5 tu.

“Ninayo taarifa niliyopewa na Nida ikionyesha kwamba imepanga ofisi nyingi Dar es Salaam zisizo na matumizi na wakati fulani walinunua ‘seva’ 100 zisizo na matumizi,” alisema.

“Haielezeki, NEC ilitumia kiasi kama hicho kuandikisha watu milioni 20 katika miezi isiyozidi mitano, lakini Nida wametumia Sh180 bilioni kuandikisha watu milioni 2.5 kwa miaka mitatu.”

Mbali na kuwaweka kando watendaji hao, Rais aliagiza vyombo mbalimbali kufanya uchunguzi wa matumizi ya fedha katika mamlaka hiyo.

Vyombo vilivyoagizwa ni pamoja na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Mamlaka ya Udhibiti ya Ununuzi ya Umma (PPRA).

Wapambe Wa Wassira Kukata Rufaa Kupinga Hukumu Ya Mahakama Kuu Iliyohalalisha Ushindi Wa Esther Bulaya

$
0
0

Baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mwanza, kuipiga chini kesi iliyokuwa ikimkabili mbunge wa Bunda Mjini (Chadema), Esther Bulaya, wadai katika kesi hiyo wanatarajiwa kupinga uamuzi huo  Mahakama ya Rufani.

Mwanasheria wa wadai hao, Constantine Mutalemwa, jana alisema wateja wake hawajaridhika na hukumu hiyo iliyotolewa na Jaji Gwae.

Juzi katika mahakama hiyo, Bulaya aliwashinda wakazi wanne wa jimbo hilo waliofungua kesi ya kumpinga baada ya ushindi alioupata kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana. Katika uchaguzi huo, Bulaya olimshinda mpinzani wake, Stephen Wasira wa CCM.

Bulaya, katika kesi hiyo, alikuwa akitetewa na mwanasheria maarufu, Tundu Lissu.

Waliofungua kesi hiyo ni Magambo Masato, Matwiga Matwiga, Janes Ezekiel na Ascetic Malagira, ambao walikuwa na mawakili wawili ambao ni Mutalemwa na Denis Kahangwa.

Mutalemwa alisema baada ya kutoridhika na uamuzi huo, wateja wake wamekusudia kufungua kesi Mahakama ya Rufani ili kupata ufafanuzi wa Jaji juu ya uhalali wao wa kutokuwa na mamlaka kisheria ya kufungua kesi kama hiyo.

Katika hatua nyingine, kesi ya madai iliyofunguliwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza na mbunge wa zamani wa Nyamagana (Chadema), Hezekiah Wenje, jana iliahirishwa hadi Februari 2, mwaka huu.

Uamuzi wa kuahirisha kesi hiyo, ulitolewa na Jaji Joaquine De Mello wa mahakama hiyo, aliposikiliza kwa muda kabla ya kupangiwa jaji wa kuisikiliza kesi hiyo ya kupinga ushindi wa Stanslaus Mabula (CCM).

Hausigeli Afariki Kwa Kulawitiwa Na Bosi Wake

$
0
0

Mtumishi  wa nyumbani mwenye umri wa miaka 23, aliyekuwa akifanyakazi katika nyumba iliyo eneo la Mwika-Mrimbo, Moshi Vijijini, mkoani Kilimanjaro, amekufa kwa madai ya kulawitiwa na bosi wake, Zablon Shaaban (32).

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, William Nyello jana alithibitisha akisema tukio hilo ni la Januari 25, mwaka huu saa 3 usiku katika kata hiyo. 

Alisema mtumishi huyo wa nyumbani alifanyiwa kitendo hicho na bosi wake aliyekuwa akiishi naye baada ya kurejea nyumbani wakitokea matembezini jioni.

“Mtuhumiwa alikuwa akiishi na marehemu nyumba moja, waliporejea katika matembezi ya jioni na wakati wa kulala, mtuhumiwa alimfuata marehemu chumbani kwake na kumkaba koo na kumlawiti,” alisema Nyello.

Kaimu Kamanda alisema kutokana na kitendo hicho, kilichothibitishwa pia kwa uchunguzi wa daktari, polisi inamshikilia mtuhumiwa huyo na atafikishwa mahakamani.

Matukio Mbalimbali Ya Bunge Leo Mjini Dodoma

$
0
0
Waziri Mkuu, Kassim Majalliwa akiteta na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama Buneni mjini Dodoma Januari 27, 2016.
Spika wa Bunge, Job Ndugai (kulia)  akimwapisha Waziri wa Elimu , Sayansi, Tekinolojia na Mafunzo ya Ufundi Joyce  Ndarichako, bungeni mjini Dodoma Januari 27, 2016.
Waziri wa Habari,Utamaduni, Wasanii,na Michezo  Nape Nnauye akitoa  kauli Bungeni mjini Dodoma Januari 27, 2016.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiteta na Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, Bungeni mjini Dodoma January 27, 2016.
Mwenyekiti wa Bunge, Mtemi Andrew Chenge  akiongoza kikao cha Bunge mjini Dodoma Januari 27, 2016.
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live


Latest Images