Quantcast
Channel: MPEKUZI
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live

Rais wa Rwanda Paul Kagame Kuwasili nchini Leo kwa ziara ya kikazi ya siku mbili

$
0
0
Mhe. Paul Kagame, Rais wa Jamhuri ya Rwanda na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, atawasili nchini tarehe 7 Machi 2019 kwa ziara ya kikazi ya siku mbili. Ziara hiyo inafanyika kufuatia mwaliko wa Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ziara hii itatoa fursa kwa viongozi hao wawili kujadiliana masuala mbalimbali kuhusu uhusiano na ushirikiano baina ya nchi hizi mbili. Aidha, Viongozi hao wanatarajia kuzungumzia masuala mbalimbali ya mtangamano katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mhe. Kagame, Rais wa Jamhuri ya Rwanda, atawasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere saa Tisa Alasiri tarehe 7 Machi 2019 na kupokelewa na mwenyeji wake, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mhe. Rais Kagame anatarajia kuondoka nchini tarehe 8 Machi, 2019.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dodoma.


Serikali Yaagiza Kuhamishwa Kwa Dampo La Kihesa Kilolo

$
0
0
Na Lulu Mussa-Iringa
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Mussa Sima ameagiza kuhamishwa kwa dampo la Kihesa Kilolo lililopo katika Kata ya Kihesa Manispaa ya Iringa kutokana na kuwepo katika mazingira yasiyo rasmi.

Agizo hilo limetolewa hii jana Mkoani Iringa mara baada ya kufanya ziara ya kikazi ya kukagua namna bora ya kuteketeza taka bila kuathiri mazingira  na kumuagiza Mkuu wa Wilaya ya Iringa Bw. Richard Kasesela kusimamia maelekezo hayo mapema iwezekanavyo ikiwa ni pamoja na kuteketeza taka zilizozagaa katika eneo hilo na kuweka katazo la watu kuingia katika dampo kwa lengo la kuokota chupa za plastiki kwa ajili ya kuziuza.

Akiwa katika eneo hilo la dampo la Kihesa Kilolo Naibu Waziri Sima ameshuhudia maji machafu yakitiririka kutoka katika dampo hilo na kwenda kwenye makazi ya watu jambo ambalo linahatarisha afya za wakazi wa maeneo ya jirani pamoja na tishio la mlipuko wa magonjwa.

Akitoa msimamo wa Serikali Naibu Waziri Mussa Sima ameagiza kwa hatua za haraka kuwekwa utaratibu wa  kudhibiti maji yanayotiririka kutoka katika dampo kwa kujenga mifereji ili kunusuru ikolojia ya vyanzo vya maji katika maeneo hayo.

“Ndugu zangu hali ni mbaya sana katika dampo hili, simamieni uteketezaji wa taka mapema iwezekanavyo, Serikali haiwezi kuvumilia vitendo vya namna hii, wananchi wanalipia gharama za ubebaji wa taka, zinaletwa dampo kisha mnaruhusu tena wananchi kuingia dampo, kwa maana nyingine tunakusanya taka katika mitaa na kuzirudisha tena katika mitaa, hii haikubakiki ” Sima alisisitiza.

Naibu Waziri Sima pia ameagiza eneo lililotengwa na Manispaa kwa matumizi ya dampo lililopo katika Kijiji cha Mkoga, Kata ya Isakalilo lenye ukubwa wa ekari Ishirini na tano kufanyiwa Tathmini ya Athari kwa mazingira kabla ya kuanza kutumiwa, sambamba na kulipa fidia wakazi wa maeneo hayo

Wakati huo huo, Naibu Waziri Sima pia amemuagiza Mratibu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kanda za Nyanda za juu kusini Bw. Godlove Mwamsojo kuhakikisha anafuatilia utekelezaji wa agizo hilo na endapo Halmashauri haitatekeleza kwa kipindi walichokubaliana hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi yao .

Nae Mkuu wa Idara ya Udhibiti wa Mazingira ya Uteketezaji wa taka gumu Bw. Christian Ndenga amekiri kuwa kwa takribani mwezi mmoja taka katika dampo hilo hazijateketezwa kutokana na sababu za kuharibika kwa ‘kijiko – Wheel loader’.

Mkuu wa Wilaya ya Iringa Bw. Richard Kasesela amesema kuwa takriban tani 108 huzalishwa kwa siku katika Manispaa ya Iringa, na kuahidi kusimamia zoezi la kuteketeza taka zilizopo na kuhamisha dampo ndani ya wiki mbili ikiwa ni utekelezaji wa maagizo.

Naibu Waziri Mussa Sima yuko katika ziara ya kikazi ya kukagua maeneo yenye changamoto za kimazingira hususan katika sekta ya afya na udhibiti wa taka ngumu pamoja ikolojia ya vyanzo vya maji vinavyo changia maji katika bonde la Rufiji.

Taarifa ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Kuhusu Kifo cha Mtangazaji wa Clouds, Ephraim Kibonde

$
0
0
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dr. Thomas Rutachunzibwa katika taarifa yake, amesema Mtangazaji wa Clouds Ephraim Kibonde alifariki akiwa njiani kuhamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando Mwanza akitokea Hospitali ya Uhuru.

Waziri Mpina Aongoza Nchi Wanachama Wa Jumuiya Ya Afrika Mashariki Utiaji Saini Udhibiti Uvuvi Haramu

$
0
0
 Na John Mapepele- Arusha
Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zimetiliana saini makubaliano ya kuendesha Operesheni ya pamoja ya kudhibiti uvuvi haramu katika ziwa Victoria.

Makubaliano hayo ni mkakati wa nchi hizo za Kenya, Uganda na Tanzania, kulinda rasilimali hizo ziwe endelevu na zitumike kukuza uchumi wa wananchi wa mataifa hayo. Makubaliano hayo yamefikiwa katika Mkutano wa Mawaziri wa Sekta za uvuvi zinazozungukwa na Ziwa Victoria, uliofanyika Makao makuu ya Jumuiya ya Afrika mashariki Jijini Arusha, Tanzania.

Makamu Mwenyekiti wa Mawaziri wa Sekta za uvuvi wa Jumuiya hiyo, Mhehimiwa Luhaga Mpina, alisema uamuzi huo utawezesha kuongezeka kwa samaki na mazao yake katika Ziwa Victoria.

Alisema hatua itachochea kasi ya ukuaji wa uchumi wa wananchi wanaozunguka ziwa hilo ikiwa ni pamoja na kuongeza kipato chao.

Alisema wananchi wa Afrika mashariki wanaozungukwa na ziwa Victoria walikuwa wanalazimika kuagiza samaki kutoka nchi ambazo hazina hata maziwa,licha ya ziwa hilo kuwa na uwezo wa kulisha bara la Afrika kama litatunzwa vizuri.

Alisema samaki wachanga waliokuwa ziwani chini ya sentimita 50 walikuwa asilimia 96.3lakini kutokana na jitihada zilizofanywa za kudhibiti uvuvi haramu vifaranga vimepungua hadi kufikia asilimia 62.8 kiwango ambacho kinakubalika kwa vifaranga kuwepo majini.

Pia alisema samaki wanaoruhusiwa kati ya sentimita 50 hadi 80 waliokuwa wamebaki majini walikuwa asilimia 3.3 lakini baada ya kazi ya mwaka mmoja wameongezeka hadi kufikia asilimia 32 huku wale wenye urefu wa kati ya sentimita 80 hadi 85 ambao ni samaki wazazi walifikia asilimia 0.4 lakini kwa sasa wameongezeka na kufikia asilimia 5.2 kiwango ambacho kunakubalika.

Alizipongeza Taasisi za utafiti za Kenya, Uganda na Tanzania kwa umakini na umahiri wa kukusanya taarifa za kitafiti ili kuzisaidia nchi wanachama kupanga yale ya usimamizi wa rasilimali za uvuvi.

“Tumefanya maamuzi makubwa ya kupanga mipango ya kufanya opersheni ya pamoja ili kuwa na uwelewa wa mpango ya pamoja ya namna ya kulitunza ziwa letu na kupambana na uvuvi haramu ya mazao ya uvuvi” alisema.

Nchi hizo zimekubaliana ziwe zimelipa madeni yote kkufikia juni, mwaka huu ilil kuwezesha Taasisi ya Uvuvi ziwa victoria (LVFO) kutekeleza mipango yake kwa wakati.

Akizungumza katika mkutano huo Katibu Mtendaji wa Oganaizesheni ya Uvuvi wa Ziwa Victoria (LVFO) Dkt. Shigalla Mahongo alisisitiza kuwa na umoja katika kuhifadhi raslimali za uvuvi katika ziwa hilo kwa kuwa idadi ya watu katika nchi wanachama wa jumuiya ya Afika Mashariki ikekuwa ikikuwa kwa kasi na kuendelea kutegemea samaki wa ziwa hilo kwa kiasi kukubwa.

“Idadi ya watu ilikuwa milioni 23.5 mwaka 1954 wakati Sangara walipowekwa katika ziwa Victoria lakini mwaka 2018 inakadiriwa kuwa idadi ya watu iliongezeka kwa takribani mara 7 na kufikia jumla ya watu wapatao milioni 165.5 ambapo sasa inakadiriwa kufikia mwaka 2050 kuwa na zaidi ya watu milioni 323.1 hiyo ina maana kuwa itakuwa ni mara 14 ya idadi ya watu waliokuwa mwaka 1954 wakati ziwa likiwa bado ni lilelile” alionya Dkt. Mahongo.

Ujumbe wa Nandy Kuhusu Ruge Wazua Gumzo Mtandaoni

$
0
0
Msanii Nandy  amevunja ukimya na kumzunguzia Ruge Mutahaba kwa kuandika ujumbe katika ukurasa wake wa Instagram huku akiambatanisha na video ambayo imezua gumzo mtandaoni.

Msanii huyo  kipindi chote cha msiba aligusa hisia za wengi kutokana na namna alivyoonekana  wakati wote akiwa sehemu ya familia ya Ruge jambo lililoibua maswali kuhusu uhusiano wake na marehemu.

Katika ujumbe wake Nandy amemuelezea Ruge kama rafiki yake wa karibu aliyeelewa ndoto zake na kumpa moyo wa kupambana.

Ujumbe huo uliokwenda sambamba na video inayomuonyesha Ruge akicheza na mbwa unasomeka: “ Kila mtu ana mtu ambaye ameumbwa na Mungu kwa ajili yake, jinsi ya kukutana na huyo mtu inaweza ikawa safari ni ndefu, ikawa na matuta na mara nyingine inaweza ikachosha lakini mwisho wa siku kila kitu kinakuja kuwa sawa.

“Wanaweza kutokea wachache ambao watakuelewa na pia kuelewa ndoto zako hata kama unazifanya mwenyewe. Watanzania wanakupenda umegusa maisha yao kwa namna tofauti ulizaliwa kuwa kiongozi, ulikuwa na moyo wa kutoa.”

Ameendelea kumuelezea Ruge akisema: Ulikuwa rafiki yangu wa karibu sana, ulikuwa kila kitu kwangu. Ruge ulielewa ndoto yangu na ulinipa moyo wa kupambana hata kama nilikuwa nataka kukata tamaa.”

“Nakuhakikishia nitakufanya ujivunie, nitaendelea kuzienzi na kuziishi hekima zako na nitafanya juhudi kufikia malengo tuliyopanga pamoja. Nakupenda sana na nitaendelea kukupenda hata kama haupo nasi




Kila mtu ana mtu ambaye ameumbwa na MUNGU kwa ajili yake. Na jinsi yakukutana na uyo mtu inaweza ikawa ni ndefu ikawa na matuta mara nyingine inaweza ikakuchosha lakini mwisho wa siku kila kitu kinakuja kuwa sawa.. Wanaweza kutokea watu wachache ambao watakuelewa na pia kuelewa ndoto zako hata kama unazifanya mwenyewe.. watakuwa hapo kukupa mrejesho chanya na watakubeba kwenye safari yako kwa moyo wote... Watanzania wanakupenda Umegusa maisha ya watu kwa namna tofauti tofauti Ulizaliwa kuwa kiongozi Ulikuwa na moyo wakutoa.. Ruge ulikuwa rafiki yangu wa karibu sana, ulikuwa kila kitu kwangu Ruge ulielewa ndoto yangu Ruge ulinipa moyo wa kupambana hata kama nilikua nataka ku give up Ruge uliona ndoto yangu na hukuwa na wasiwasi nayo.... Ulivo pumzika naweza kukuhakikishia... Nitakufanya ujivunie... Nitaendelea kuzi enzi na kuziishi hekima zako Na nitafanya juhudi kufikia malengo tuliyo panga pamoja.. Nakupenda sana na nitaendelea kukupenda hata kama haupo nasi YOUR THE BEST THING THAT EVER HAPPEN TO ME ROHO YANGU.. R.I.P
A post shared by Nandy (@officialnandy) on

Wabunge Peter Lijualikali Na Susan Kiwanga Waachiwa Kwa Dhamana

$
0
0
Wabunge wawili wa Chadema Susan Kiwanga, Peter Lijualikali na wenzao 7 wameachiwa kwa dhamana leo baada ya mahakama kutupilia mbali maombi ya Jamhuri ya kupinga dhamana ya washtakiwa hao. 

Mahakama imefikia uamuzi huo Mkoani Morogoro katika kesi ya msingi inayowakabili wabunge hao ambao wanatajwa kutenda kosa la jinai la kuanzisha vurugu na kuchoma mali za umma katika Kata ya Sofi wilayani Malinyi wakati wa uchaguzi mdogo wa madiwani Novemba 26, 2017

Akitoa uamuzi huo Hakimu Elizabert Nyembele amesema madai ya upande wa Jamhuri hayakuwa na msingi hivyo mahakama imeamua kuwapa dhamana washtakiwa.

Breaking News: Freeman Mbowe na Ester Matiko Waachiwa Kwa Dhamana

$
0
0
Mahakama Kuu imetengua uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wa kuwafutia dhamana Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Ester Matiko, ambapo wameruhusiwa kuwa nje kwa dhamana na kuripoti mahakamani mara moja kwa mwezi badala ya polisi kila wiki

Hukumu hiyo imetolewa leo March 7, 2019 na  Jaji Sam Rumanyika.

Wakati Jaji Rumanyika akisoma hukumu hiyo ulinzi mahakamani hapo ulikuwa umeimarishwa kwa askari wengi waliotanda sehemu mbalimbali za Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

"Hii ni rufaa mojawapo sijawahi kuiona Katika kazi yangu ya Ujaji. Maofisa wa mahakama kama mahakimu wanapaswa kutumia utashi wao kuamua haki za watu kwa kuzingatia Haki maana ni hatari sana kumnyima dhamana mtu bila sababu za Msingi

“Hakuna mahala popote warufani wamezuiwa kusafiri Lakini Wakati huo huo wanatakiwa kuripoti Polisi kila Juma. Hii maana yake wamenyimwa Uhuru wa kusafiri na haki ya kufanya kazi .
 

"Kuanzia sasa, naagiza Mbowe na Matiko waachiwe huru mara moja  na  watatakiwa kuripoti mahakamani mara moja kwa mwezi badala ya polisi kila wiki " Amesema  Jaji Rumanyika  wakati akisoma hukumu hiyo.

Novemba 23, 2018 Jaji Wilbard Mashauri akiwa Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, alifuta dhamana ya Mbowe na Matiko kutokana na kukiuka masharti ya dhamana.

Wawili hao walikata rufaa katika Mahakama Kuu ya Tanzania kupinga uamuzi wa Kisutu kufuta dhamana yao ambapo rufani yao ilipangwa kwa Jaji Sam Rumanyika.

Hata hivyo, baada ya Mahakama Kuu chini ya Jaji Sam Rumanyika kusikiliza mapingamizi ya pande zote iliamua kuanza usikilizaji wa rufaa hiyo.

Upande wa serikali ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Paul Kadushi ulidai kuwa wamekata rufaa katika Mahakama ya Rufani kupinga maamuzi yaliyotolewa na Mahakama Kuu.  


Hata hivyo,March 1 mwaka huu, Mahakama ya Rufaa chini ya jopo la majaji watatu Stella Mugasha, Dk Gerald Ndika na Mwanaisha Kwariko ilitupilia mbali pingamizi hilo la Serikali  na kuamuru kesi hiyo irudishwe Mahakama Kuu kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa.

Mwili wa Ephraim Kibonde kuwasili leo Dar Es Salaam.....Mazishi ni Jumamosi

$
0
0
Mwili wa aliyekuwa mtangazaji wa Clouds Media, Ephraim Kibonde, unatarajiwa kuwasili jijini Dar es Salaam leo Alhamisi Machi 7, saa nne usiku katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na kuzikwa Jumamosi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Clouds Media Group, Joseph Kusaga, amesema hayo leo wakati akitoa taarifa za msiba huo ambapo amesema mara baada ya mwili huo kuwasili, utahifadhiwa katika Hospitali ya Jeshi Lugalo jijini Dar es Salaam.

“Jana usiku niliongea na daktari Derrick aliyekuwa anamtibu Ephraim Kibonde akanihakikishia kuwa anaendelea vizuri lakini bahati mbaya wakati wanaajiandaa kurudi Dar es Salaam hali ikabadilika na kusababisha kifo chake.

“Taratibu za mazishi na maombolezo, zitafanyika kesho nyumbani kwake Mbezi na tunatarajia kuaga na kumpumzisha siku ya Jumamosi,” amesema Kusaga.

PICHA: Rais Kagame Wa Rwanda Awasili Nchini Na Kufanya Mazungumzo Na Rais Magufuli Ikulu Jijini Dar Es Salaam

$
0
0
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akimkaribisha Rais wa Rwanda Mheshimiwa Paul Kagame mara baada ya kuwasili Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Rwanda Mheshimiwa Paul Kagame akifurahia zawadi ya Kinyago aliyopewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli mara baada ya kuwasili Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na mgeni wake Rais wa Rwanda Mheshimiwa Paul Kagame mara baada ya kuwasili Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Rwanda Mheshimiwa Paul Kagame akifurahia zawadi ya picha ya Mlima Kilimanjaro mara baada ya kupewa na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akipokea zawadi ya picha kutoka kwa  Rais wa Rwanda Mheshimiwa Paul Kagame mara baada ya kuwasili Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Rais wa Rwanda Mheshimiwa Paul Kagame kabla ya kuanza mazungumzo yao Ikulu jijini Dar es Salaam. PICHA NA IKULU

Kauli ya Zitto Kabwe Baada Ya Freeman Mbowe na Ester Matiko Kuachiwa Huru Kwa Dhamana Leo

$
0
0
Kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amepongeza uamuzi wa Jaji Sam Rumanyika wa Mahakama Kuu baada ya kufuta uamuzi wa kuwafutia dhamana, viongozi wawili wa Chadema, Freeman Mbowe na Esther Matiko.


==>>Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Zitto Kabwe ameandika Yafuatayo; 
Jaji Sam Rumanyika Katika kufuta uamuzi wa mahakama ya Kisutu kuwafutia dhamana Freeman Mbowe na Esther Matiko ametaja misingi 9 ya Mahakimu kuzingatia Katika Maombi ya dhamana.

1. Kesi inadhaminika
2. Kutoa dhamana ni tafsiri dhahiri ya mahakama ya dhana ya katiba ya kuwa mtu hana hatia mpaka mahakama itakapomhukumu vinginevyo.
3. Kufuta dhamana kunahitaji sababu kubwa kuliko sababu za kumpa mtu dhamana
4. Mahakama izingatie Ukubwa wa kosa Kutoa masharti ya dhamana
5. Masharti ya dhamana yawekwe bila kuleta hisia kuwa mpango ni kunyima mtu dhamana.
6. Mahakama izingatie adhabu kwa makosa yaliyopo mbele yake ili Pale ambapo mshatikiwa akitiwa hatiani asiwe amedhibiwa mara 2.
7. Sababu ziwe zinakubalika mahakama yeyote duniani
8. Mahakama izingatie Msongamano uliopo gerezani na je kutoa dhamana au kufuta dhamana kunachangia au kupunguza msongamano gerezani
9. Mahakama izingatie kuwa Uhuru ya mshatakiwa hauna mbadala.

Jaji Rumanyika sio tu amewaachia huru Mbowe na Matiko bali pia amefuta masharti ya dhamana ya kuripoti Polisi kila wiki.

Zitto Kabwe
7/3/2019

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Ijumaa Ya March 8

Walichokiongea Rais Magufuli na Kagame Baada ya Kukutana IKULU

Askari JWTZ Mbaroni Kwa Ujambazi....Wenzake Watatu Wauawa

$
0
0
Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, linamshikilia askari wa Jeshi la Wananchi (JWTZ), Friday Kumingi (29), kwa kushirikiana na majambazi kufanya matukio ya uhalifu.
 
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alisema askari huyo alikamatwa kwenye msako uliofanywa na jeshi hilo Machi 3, mwaka huu.

Alisema askari huyo wa JWTZ Kikosi cha 36KJ Kibaha Msangani, alipohojiwa na polisi baada ya kukamatwa alikiri kumiliki silaha mbili kinyume cha sheria.

Mambosasa alisema mtuhumiwa huyo aliwajulisha askari hao kuwa huwa anazihifadhi silaha hizo nyumbani kwa mke wake mdogo mtaa wa Muheza Kibaha, Pwani na huzitumia kufanyia matukio ya uhalifu katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam na Pwani.

Alisema baada ya mahojiano, askari hao na mtuhumiwa walifika kwenye nyumba hiyo na kufanikiwa kukamata silaha aina ya AK 47 yenye namba NM174844 ikiwa na risasi 20.

Mambosasa alisema askari walikuta boksi moja likiwa na risasi 27, bastola moja yenye namba 3249 ikiwa na risasi saba ndani ya magazine na risasi tatu za silaha aina ya G3.

Aidha, Mambosasa alisema mtuhumiwa huyo alikubali kuwaonyesha wenzake watatu anaoshirikiana nao katika matukio hayo na askari walipofika kwenye nyumba wanayoishi watuhumiwa walianza kukimbia.

Aidha, Mambosasa alisema baada ya watuhumiwa hao kuanza kukimbia kupitia mlango wa nyuma, askari walianza kurusha risasi hewani kuwaamuru wasimame, lakini walikaidi.

"Walikaidi na ndipo askari walipowafyatulia risasi za miguu ambazo ziliwajeruhi na kufariki dunia wakiwa njiani kupelekwa hospitali," alisema Mambosasa bila kutaja majina ya watu hao.

Waziri Kigwangala Atoa Msimamo Vita Dhidi Ya Ujangili

$
0
0
Waziri wa Maliasili na Utalii,  Dkt. Hamisi Kigwangala amewataka Watanzania kuondokana na dhana iliyojengeka miongoni mwao kuwa watumishi wa Wizara hiyo hususan  wahifadhi wa  wanyamapori na Misitu  ni watu katili  wanaowatesa Wananchi.

Kauli hiyo ameitoa jana wakati akifungua mkutano wa 26 wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo uliofanyika katika Chuo cha Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi jijini Mwanza.

Amesema watumishi hao ni watu wenye utu na weledi wa hali ya juu na wanaozingatia  sheria katika kutimiza majukumu yao na hulazimika kutumia nguvu wakati wakipambana na majangili wanaokutwa katika maeneo ya hifadhi wakifanya vitendo vya ujangili.

‘’ Ulinzi wa Rasilimali za nchi ni jukumu letu sote, wizara imepewa dhamana ya kusimamia na kuongoza kwa niaba ya watanzania, kama kuna watumishi wa Wizara hii wanaowanyanyasa wananchi naomba walete ushahidi kwetu ili tuwachukulie hatua’’ amesema Dkt. Kigwangala.

Waziri Kigwangala amesikitishwa na idadi ya watumishi walipoteza maisha kwa ajali na wengine kuuwawa na majangili wakati wakipambana nao katika maeneo yote ya hifadhi  nchini na kutoa wito kwa wananchi wote wenye taarifa au ushahidi juu ya vitendo vyovyote vya kihalifu kuziwasilisha katika mamlaka zinazohusika.

Amesema kuwa Serikali haitasita kuwachukulia hatua wale wote wanaojihusisha na vitendo vya ujangili na uhalifu katika maeneo ya hifadhi na wale wote wanaoshirikiana na makundi ya watu wenye nia ovu ya kukwamisha juhudi za uhifadhi wa rasilimali za Taifa.

Ametoa wito kwa wananchi kuheshimu sheria za uhifadhi na kuepuka kuvamia maeneo ya hifadhi kwa shughuli za kijamii na ufugaji akitoa wito kwa viongozi mbalimbali wa Siasa kuunga mkono juhudi za wizara za ulinzi wa maeneo ya hifadhi kwa kuwaelimisha wananchi wanaowaongoza kujiepusha na vitendo vya uvamizi wa maeneo ya hifadhi badala ya kuwatetea.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Prof.Adolf Mkenda akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho amesema kuwa jumla ya watumishi 23 walifariki dunia  wakati wakitekeleza majukumu ya uhifadhi   na   5 walijeruhiwa na majangili wakiwa kazini.

Prof. Mkenda amesema kuwa waliofanya vitendo hivyo  hawaitakii mema Tanzania na ni maadui wa shughuli za uhifadhi nchini akiongeza kuwa Serikali itaendelea kusimama na kuwatetea watumishi na askari wa wanyamapori wanaotimiza majukumu yao kwa kuzingatia sheria.

Waziri Ndalichako ahimiza ubunifu kuelekea Tanzania ya Viwanda

$
0
0
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Joyce Ndalichako amewaagiza wanafunzi wanaosoma masomo ya Sayansi na wabunifu nchini kubuni vitu ambavyo vitasaidia kurahisisha shughuli mbalimbali.

Amesema hayo jana Alhamisi Machi 7, katika kilele cha Mashindano ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu  (MAKISATU) jijini Dodoma ambayo kauli mbiu yake ni ‘kukuza ujuzi na ubunifu kwa uchumi wa viwanda’ ambapo amesisitiza wananchi kujitokeza kwa wingi kuonyesha ubunifu wao ili kukuza uchumi wa nchi.

“Changamoto tuliyonayo kwa sasa ni muamko kwa wananchi haujafikia katika kiwango ambacho serikali ingependa kukiona, ni wazi kabisa tunapaswa kuwa na ubunifu na kutumia sayansi na teknolojia kuhakikisha tunarahisisha maisha ya wananchi wanaoishi vijijini.

“Ninatoa wito kwa wabunifu wote nchini kuhakikisha wanajikita kuangalia ni kwa namna gani wanarahisisha shughuli zinazofanyika katika mazingira yao na ikumbukwe ubunifu hauna umri na hauchagui kwasababu mwisho wa siku mkono unaenda kinywani,” alisema.

Aidha Ndalichako alisema washindi waliopatikana katika mashindano hayo wataendelezwa ili waweze kukuza tafiti zao kwa lengo la kukuza uchumi.

Kwa upande wake Kaimu Katibu Mkuu Profesa James Mdoe alisema  lengo la Mashindano hayo yaliyohusisha wabunifu kutoka ngazi mbali za Elimu ni kuibua ubunifu, umahiri, kuchochea ugunduzi kwa lengo la kukuza matumizi ya Sayansi na Teknolojia katika maendeleo.

Mashindano hayo  yalifunguliwa rasmi na Naibu Waziri Mhe. William Ole Nasha Machi 5, 2019 na jana yamefikia kilele ambapo washindi mbalimbali walipata zawadi za fedha na kutunukiwa vyeti.

Apandishwa Kizimbani Kwa Kumchana Mtu Kwa Wembe

$
0
0
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni, Dar es Salaam imempandisha kizimbani Asia Mohamed (26), mkazi wa Magomeni Mapipa kwa shtaka la kujeruhi.

Akisomewa shtaka hilo mbele ya Hakimu Hanifa Mwingira, Mwendesha Mashtaka wa Jamhuri, Matarasa Hamisi, alidai kuwa Januari 5, mwaka huu eneo la Magomeni, Wilaya ya Kinondoni, mtuhumiwa alimkata kwa wembe sehemu za kidevu Idd Nasri, akimtuhumu kumchonganisha na mzazi mwenzake kitendo kilichosababisha kukosa matumizi ya mwanaye.

Mshtakiwa alikana kutenda kosa hilo huku upande wa mashtaka ukisema upelelezi bado haujakamilika na kuomba tarehe ya kutajwa tena.

Hata hivyo, Hakimu Mwingira alisema dhamana iko wazi kwa mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili wanaotambulika kisheria watakaotoa bondi ya shilingi laki tano kwa kila mdhamini.

Mshtakiwa alikidhi vigezo vya dhamana na kuachiwa hadi kesi yake itakaposomwa tena Aprili, mwaka huu.

Boomplay Inasheherekea Wanamuziki Wa Kike Katika Siku Ya Wanawake Duniani

$
0
0
Boomplay ni app nambari moja kwa huduma ya kusikiliza na kupakua muziki barani Afrika, inasherehekea Siku Ya Wanawake Duniani 2019 ikiwa na kampeni mpya ya “Boom Queens”.
 
Vanessa Mdee, Rihanna, Tiwa Savage, Fena Gitu na wengine wengi, ni miongoni mwa  wanawake wenye vipaji ambao wameendelea kubadilisha tasnia ya muziki duniani. 

App ya Boomplay itakuwa na muonekano wa tofauti hasa katika Siku Ya Wanawake duniani tarehe 8 Machi, lengo likiwa ni kuonesha na kukuza kazi za wanawake katika muziki. App itapambwa na nyimbo, albamu pamoja na playlist za wanawake katika vipengele vyote kwenye ukurasa wa kwanza.
 
Boomplay pia itakuwa na kampeni kabambe ambayo itatoa fursa ya kukuza mauzo ya kazi za wanawake ambao nyimbo zao zitakuwepo kwenye playlist ya BOOM QUEENS. Playlist hiyo itakuwa na nyimbo za wasanii bora wa kike tu.
 
Katika kampeni hii, Meneja Mahusiano wa kampuni ya Boomplay, Bi Tosin Sorinola amesema, “majadiliano juu ya usawa wa kijinsia ni moja ya mambo ambayo ni muhimu kwetu kama jukwaa lenye nia kubwa ya kukuza wanawake katika muziki, katika njia njema kadri iwezekanavyo. Kampeni hii sio kwa mara moja tu, ni endelevu, na hili litadhihirishwa katika shughuli zetu za kila siku”.
 
Katika mwezi huu wa kuadhimisha Siku Ya Wanawake Duniani, watumiaji wa Boomplay kupitia simu zao za Android na iOS watapata fursa ya kujishindia simu mpya ya iPhone XS na zawadi nyingine kem kem nchini Tanzania, Kenya, Nigeria na Ghana. Ili kuonesha upendo kwa wasanii wa kike katika tasnia ya muziki, basi jishindie zawadi hizi kwa ku-subscribe kwenye app ya Boomplay kwenye vifurushi vinavyopatikana (vya siku, wiki na mwezi) na pia sikiliza playlist ya Boom Queens.
 
App ya Boomplay ambayo ina watumiaji zaidi ya milioni 42 dunia kote, hivi karibuni ilizindua app hiyo kwenye jukwaa la iOS. Hakika Boomplay inajivunia kuwa na nyimbo na video zaidi ya milioni 5 kutoka kwa wasanii wa Tanzania na wakimataifa.

Rais Wa Rwanda Paul Kagame Amaliza Ziara Yake Ya Siku Mbili Nchini Na Kurejea Nchini Rwanda

$
0
0
Rais wa Rwanda, Paul Kagame ameondoka Tanzania baada ya kumaliza ziara ya siku mbili iliyolenga kukutana na kufanya mazungumzo ya faragha na mwenyeji wake Rais John Magufuli.

Kagame aliwasili jana Alhamisi ikiwa ni ziara ya tatu Tanzania  tangu Rais Magufuli aingie madarakani Novemba 5, 2015 na alipokelewa na  Waziri wa Mambo ya Nje na  Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi.

Rais huyo wa Rwanda ambaye ni mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ukanda ambao hivi sasa unakabiliwa na migogoro katika baadhi ya nchi wanachama ikiwamo Rwanda na Uganda.

Kabla ya Kagame kuondoka nchini leo, wakiwa katika uwanja wa ndege wa zamani wa Julius Nyerere Rais huyow Rwanda na Rais Magufuli waliwasalimia baadhi ya wananchi na viongozi wa Serikali wa nchi hizo mbili waliokuwapo uwanjani hapo pamoja na wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama wa Tanzania.

Pia viongozi hao walipata fursa ya kukagua gwaride maalumu lililoandaliwa kwa ajili yao kisha Kagame akaingia katika ndege yake saa 4:11 asubuhi  na ilipotimu saa 4:23 ndege hiyo iliruka hewani kuelekea Rwanda.

Mkuu wa Mkoa Awaagiza Polisi Kumsaka Mganga Aliyawataja Wachawi

$
0
0
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ameliagiza jeshi la polisi Mkoani Humo kuhakikisha wanamsaka na kumkamata mganga wa jadi anayesadikiwa kuwaibua na kuwaadhiri wachawi katika bonde la ziwa Rukwa Wilayani Sumbawanga.

Agizo hilo limekuja baada ya kufanya ziara yake ya kukagua miradi mbalimbali katika bonde hilo pamoja na kujionea maendeleo na changamoto za shule ya sekondari Kipeta iliyoezuliwa paa pamoja na shule ya msingi Msia iliyobomoka madarasa manne kutokana na mvua iliyoambatana na upepo mkali iliyosababisha madhara hayo mwezi Disemba mwaka 2018.

Ameonya kuwa hataki yaliyotokea mkoa wa Njombe yajirejee katika Mkoa wa Rukwa ikiwa bado watu hawajasahau machungu waliyoyapata kutokana na matukio hayo, na kuongeza kuwa mganga huyo wa kienyeji analindwa na kiongozi wa chama cha kisiasa na hivyo kumtaka mkuu wa kituo cha Kijiji cha Kilyamatundu kuhakikisha anamkamta kiongozi huyo hata kama ni wa Chama cha Mapinduzi.

“OCS na vyombo vyako vile fanya upepelezi wa kina na ukamate yeyote yule ambae ametoka nje ya mkoa huu, nje ya Kilyamatundu anayefanya shughuli hizi, kamata weka ndani fanya mahojiano ya kina, na wengine nimeambiwa hap ani viongozi wa vyama vya kisiasa, usijali huyu ni chama tawala, huyu ni nani, kama ukijua kwa uhakika kamata mhoji mpaka kieleweke, sisi hatutaki kuletewa Lambalamba hapa,” Alisisitiza.

Katika hatua nyingine, Mh. Wangabo aliwapongeza waalimu, Uongozi wa vijiji husika pamoja na wananchi kwa ushirikiano waliouonyesha katika kuhakikisha majengo yaliyobomoka na kuezuliwa katika shule hizo yanarudi katika hali yake ya kawaida na hatimae wanafunzi kuendela na masomo.

Pamoja na michango ya wadau mbalimbali iliyohamasishwa na Mh. Wangabo ambayo imesaidia kurudishisa mapaa ya majengo ya utawala, mabweni mawili, nyumba sita za waalimu na vyoo vya wasichana na wavulana kwa shule ya sekondari Kipeta na kujenga madarasa manane kwa shule shule ya Msingi Msia, Wizara ya Elimu pamoja kwa ushirikiano na Wizara ya TAMISEMI imetoa shilingi Milinoni 75.2 kwaajili ya kuongezea ujenzi wa madarasa na vyoo kwa shule hizo.

Naye Diwani wa kata ya Milepa Mh. Apolinari Macheta alipongeza juhudi za Mkuu wa Mkoa kwa kuhakikisha shule hizo zinakuwa bora zaidi ya zilivyokuwa na kumuahidi kuwa Shilingi Milioni 48.6 walizopatiwa kwaajili ya ujenzi wa madarasa mawili na vyoo matundu sita kwa shule ya msingi Msia atahakikisha kwa ushirikiano wa wananchi watapata darasa jingine kwa fedha hizo.

Waziri Lugola Apiga Marufuku Polisi Jamii Kukamata Bodaboda na Askari Polisi Kukamata Vyombo Vya Moto Bila Kuvaa Sare Za Jeshi

$
0
0
Na Felix Mwagara, MOHA-Morogoro.
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amepiga marufuku Polisi jamii kukamata bodaboda zinazofanya makosa ya usalama barabarani nchini.

Pia Waziri huyo amepiga marufuku polisi wa usalama barabarani kukamata vyombo vya moto wakiwa hawajavaa sare za Jeshi.

Akizungumza na mamia ya wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Shule ya Msingi Mafisa, Kata ya Mwembesongo, mjini Morgoro, jana, Lugola alisema Polisi Jamii hawana ujuzi wa kijeshi wa ukamataji wa bodaboda hivyo kuendelea kuifanya kazi hiyo ni kuwanyanyasa wananchi.

“Nimepata malalamiko mengi ninapofanya ziara zangu hapa nchini, wengi wanawalalamikia Polisi Jamii kuwaonea, kuwaomba rushwa na kuwakamata pasipofuata utaratibu unaotakiwa kijeshi, hapa Morogoro pia, katika mkutano huu wa hadhara mnayasema yale yale, sasa natangaza kuanzia leo, marufuku Polisi Jamii kukamata bodaboda,” alisema Lugola.

Waziri Lugola pia alipiga marufuku baadhi ya Polisi wa Usalama barabarani ambao wenye tabia ya kutovaa sare za Jeshi na kuingia barabarani au mitaani na kuyakamata magari na bodaboda.

Lugola alisema lazima polisi wafate sheria za usalama barabarani hasa wanapokamata magari yanayofanya makosa, uvaaji wa sare za Jeshi ni muhimu na unapaswa kufutwa.

Waziri Lugola aliongeza kuwa, bodaboda au vyombo vingine vya moto, zinazovunja sheria za usalama barabarani zinapaswa kukamatwa bila kuwaonea huruma, ila ni kosa Polisi kuwanyanyasa vijana hao ambao wanapata ridhiki kupitia biashara hiyo.

“Mnapaswa kukamata hizi bodaboda zinapofanya makosa, tabia ya kukurupuka huku mkitafuta fedha zisizo halali, huko ni kuwaonea waendesha bodaboda,” alisema Lugola.

Lugola alifafanua kuwa, bodaboda zinazotakiwa kuwepo kituo cha polisi ni zile zilizopo katika makundi matatu ambayo ni Bodaboda zilizohusika kwenye uhalifu, zilizotelekezwa au zilizookotwa na zilizohusika katika ajali.

“Bodaboida hizo ndizo zinapaswa kuwepo vituoni, lakini kuziweka bodaboda ambazo hazipo katika makundi hayo, napiga marufuku na hii nataka Polisi nchi nzima munielewe,” alisema Lugola.

Pia Lugola aliwataka waendesha bodaboda mjini Morogoro na Tanzania kwa ujumla wafate sheria za usalama barabarani zikiwemo kuvaa kofia ngumu, kutokubeba abiria zaidi ya mmoja na pia wakiendesha wanapaswa kuwasha taa.

Lugola ameanza ziara yake ya siku tatu mkoani humo akitembelea Wilaya za Morogoro, Mvomero, Kilosa na Gairo akisikiliza kero za wananchi pamoja na kufuatilia maagizo yake aliyoyatoa kwa vyombo vya ulinzi na usalama vilivyopo ndani ya Wizara yake.

Lugola mwaka jana alitoa maagizo kwa makamanda wa mikoa nchini ambayo ni dhamana zitolewe saa 24 katika vituo vyote vya polisi nchini, na pia kupiga marufuku tabia ya baadhi ya Polisi kubambikizia kesi wananchi, na pamoja na agizo la pikipiki zote zilizopo vituoni ziondolewe.

Waziri Lugola amemaliza ziara Wilaya ya Morogoro na leo ataanza ziara yake katika Wilaya ya Movemero, na Machi 10, 2019 atamalizia Wilaya ya Gairo ambapo katika Wilaya hizo pia atazungumza na wananchi pamoja na watumishi waliopo ndani ya Wizara yake ambao ni Jeshi la Polisi, Idara ya Uhamiaji, Jeshi la Magereza, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, pamoja na Idara ya Probesheni.
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live




Latest Images