Quantcast
Channel: MPEKUZI
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live

Kamati ya Bunge ya Bajeti yafanya ziara katika kiwanda cha Transfoma na kupongeza uzalishaji

$
0
0
Na Teresia Mhagama
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati, George Simbachawene wametembelea kiwanda cha kuzalisha transfoma cha TANELEC kilichoko jijini Arusha ili kukagua masuala mbalimbali ikiwemo uwezo wake katika uzalishaji wa transfoma lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa nchi inakuwa na vifaa vya umeme vya kutosha.

Katika ziara hiyo waliambatana na Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani na watendaji mbalimbali kutoka Wizara ya Nishati, Shirika la Umeme Tanzania ( TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Baada ya kukagua shughuli za uzalishaji wa transfoma katika Kiwanda hicho, Wajumbe hao kwa nyakati tofauti waliwapongeza watendaji wa Kiwanda hicho kwa kuzalisha transfoma nyingi ambazo ni 14,000  kwa mwaka huku mahitaji ya transfoma nchini kwa mwaka yakiwa ni 10,000.

Aidha Wajumbe hao walipongeza uamuzi wa Serikali wa mwaka 2017 ambao ulielekeza kuwa miradi yote ya umeme nchini itumie vifaa vya umeme vinavyopatikana nchini hali inayopelekea miradi hiyo kutekelezwa kwa kasi.

Wajumbe hao pia walimtaka Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo kuongeza uzalishaji na kuwa mbunifu kwa kuangalia pia masoko mengine ya transfoma na si kulenga miradi ya umeme ya ndani ya nchi pekee.

Awali, Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani alisema kuwa, Serikali ilichukua uamuzi wa kusitisha kuagiza nje vifaa vya umeme vinavyopatikana nchini ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya umeme.

Alitoa mfano kuwa upatikanaji wa transfoma nje ya nchi unaweza kuchukua hadi miezi 12  hali wakati transfoma zinazozalishwa ndani ya nchi zinachukua muda mfupi kufika katika eneo zinapohitajika.

Aidha Waziri wa Nishati alisema kuwa, uagizaji wa transfoma nje ya nchi ni gharama kubwa kwani transfoma moja kutoka nje ya nchi inauzwa kwa takriban shilingi milioni Tisa wakati zinazozalishwa nchini ni takriban shilingi milioni 6.5.

Akitoa taarifa ya kiwanda hicho, Mkurugenzi Mkuu wa TANELEC, Zahir Saleh alisema kuwa kiwanda hicho kilichoanzishwa mwaka 1981 kwa sasa kinazalisha transfoma kiasi cha 14,000 kwa mwaka.

Alisema kuwa,  kiwanda kinazalisha transfoma za uwezo wa kvA 50 hadi kVA 5000 na kufanya matengenezo ya transfoma kutoka nchi mbalimbali za Afrika kama Rwanda, Burundi na Kenya.

Aliongeza kuwa, uamuzi wa Serikali kuzuia kuagiza vifaa nje ya nchi umekinufaisha kiwanda hicho kwani kabla ya uamuzi walikuwa wakizalisha transfoma 7000 kwa mwaka lakini sasa wanazalisha transfoma 14,000.

Kuhusu ajira alisema kuwa, awali waliajiri wafanyakazi 30 lakini kwa sasa wafanyakazi walioajiriwa ni 70 na kwa mwaka huu wataajiri wafanyakazi wengine 40.

Vilevile alisema kuwa, kutokana na uamuzi huo wa Serikali, Kiwanda kinafanya kazi kwa faida na wameanza kupeleka gawio serikalini la takribani shilingi milioni 500 kwa mwaka 2018 na wanategemea kuongeza kiasi cha gawio hilo kwa miaka inayokuja.

Madaktari wamuondolea Virusi vya Ukimwi muathirika....Huyu Sasa ni Mgonjwa wa Pili Kuondolewa Virusi Hivyo

$
0
0
Jopo la Madaktari jijini London nchini Uingereza limefanikiwa kumuondolea kabisa virusi vya ukimwi muathirika na kumfanya kuwa mtu wa pili duniani kuondolewa virusi hivyo.

Taarifa ya tukio hilo iliyochapishwa kwenye jarida la ‘Nature’ imeeeleza kuwa madaktari hao walifanikiwa kwa kutumia njia ya kupandikiza uboho kutoka kwa mtu ambaye hapokei virusi hivyo (HIV resistant donor).

Kiongozi wa jopo hilo la madaktari, Profesa Ravindra Gupta ambaye ni mtaalamu wa bailojia ya Virusi vya Ukimwi, ameeleza kuwa mgonjwa aliyepewa huduma hiyo ameondolewa virusi vya ukimwi lakini akaonya kuwa ni mapema kusema amepona kabisa.

“Hakuna virusi vya ukimwi ndani yake ambavyo tunaweza kuvipima na kubaini, hatuwezi kubaini chochote… lakini ni mapema kusema kuwa amepona kabisa,” Reuters wanamkariri Profesa Gupta.

Mtu huyo ambaye madaktari wameeleza kuwa ameomba jina lake lisitajwe amekuwa mtu wa pili baada ya Timothy Brown kuondolewa virusi vya ukimwi mwaka 2007, jijini Berlin nchini Ujerumani.

Kama ilivyokuwa kwa Brown aliyebatizwa jina la ‘Berlin Man’ (Mtu wa Berlin), huyu pia amepewa jina la ‘London Man’ (Mtu wa London).

Matibabu pamoja na matokeo ya tiba hiyo yanatarajiwa kuwasilishwa rasmi kwenye mkutano utakaohusu masuala ya tiba, utakaofanyika Jumanne huko Seatle, Washington, Marekani.

Waziri Wa Kilimo Na Naibu Spika Waahidi Kutatua Kero Zinazowakabili Wakulima Wa Viazi Mviringo

$
0
0
Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Mbeya
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga kwa pamoja na Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Tulia Mwansasu wamekubaliana kuvalia njuga kero sugu zinazowakabili wakulima wa viazi mviringo Mkoani Mbeya.

Kero zinazowakabili wakulima hao ni pamoja na faini zisizo rafiki za vifungashio, Ufungaji wa mifuko (zipu) wakati wa kusafirisha usumbufu wa mawakala wa kilimo wakati wa kusafirisha viazi pamoja na sheria ya vipimo kutokuwa rafiki kwani viazi hutofautiana uzito kutokana na msimu.

Kero nyingine ni pamoja na Rushwa kwa baadhi ya watumishi wa viwango hususani katika vituo wakati wa kupima katika vituo vya ukaguzi visivyo rasmi vilivyopo katika eneo la Makambako, Iringa, Morogoro, Mikese na Kibaha.

Katika taarifa iliyosomwa na wakulima hao jana tarehe 5 Machi 2019 mbele ya Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga pamoja na Naibu Spika wa Bunge Dkt Tulia Ackson wakulima hao waliiomba serikali kutatua changamoto hizo ambazo kwa muda mrefu zimekuwa kero bila kupatiwa majibu.

Mhe Hasunga alisema kuwa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe Rais Dkt John Pombe Magufuli imedhamiria kwa dhati kutatua kero zisizo rafiki kwa wakulima na watanzania wote.

“Kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu sasa kwenye zao hili muhimu la viazi mviringo nami niwaahidi kutekeleza kwa haraka kadhia hii inayowasumbua Alikaririwa Mhe Hasunga

Kadhalika, aliwaeleza wakulima hao waliojitokeza katika mkutano huo kuwa Wizara yake imejipanga kuhakikisha kuwa wakulima wote nchini wanasajiliwa ili kubaini kiwango cha mashamba wanayolima na uwezo wa uzalishaji wa mazao.

Vilevile alieleza kuwa serikali imeanza mkakati wa kuwa na Bima ya mazao kwani kufanya hivyo wakulima watakuwa na ahueni pindi yanapotokea majanga katika mazao wanayolima.

Naye Naibu Spika wa Bunge Dkt Tulia Ackson amewapongeza wakulima hao wa viazi mviringo kwa kuwa wavumilivu wakati serikali inatafuta ufumbuzi wa kadhia hizo zinazowakabili.

Alisema kuwa wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara zitakutana kutatua kadhia hizo ili wakulima mkoani Mbeya na mikoa mingine nchini waweze kuzalisha na kusafirisha mazao yao pasina kadhia yoyote.

MWISHO

Clouds Media wapata ajali wakitokea msibani kwa Ruge

$
0
0
Sehemu ya Timu ya Production ya Clouds Media ikiwa na Watu 6 ikitokea katika Msiba wa Ruge Mutahaba  Kagera imepata ajali ya gari Dodoma ambapo limepinduka mara tatu.

Hakuna aliepata madhara makubwa kutokana na ajali hiyo ambapo kwa sasa wanaendelea na matibabu Dodoma.

PICHA:Rais Magufuli Ashiriki Katika Ibada Ya Jumatano Ya Majivu Kanisa Kuu La Mtakatifu Joseph Jijini Dar Es Salaam Leo

$
0
0
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akipakwa majivu na Paroko Msaidizi wa Parokia ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph jijini Dar es salaam Joseph Mosha wakati wa Ibada ya Jumatano ya Majivu kanisani hapo leo Machi 6, 2019
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akipokea Mkate wa Sakramenti Takatifu kutoka kwa Paroko Msaidizi wa Parokia ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph jijini Dar es salaam Joseph Mosha wakati wa Ibada ya Jumatano ya Majivu kanisani hapo leo Machi 6, 2019
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, akiwa ameongozana na mkewe Mama Janeth Magufuli, akila Mkate wa Sakramenti aliopokea toka kwa Paroko Msaidizi wa Parokia ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph jijini Dar es salaam Joseph Mosha wakati wa Ibada ya Jumatano ya Majivu kanisani hapo leo Machi 6, 2019
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, akiwa ameongozana na mkewe Mama Janeth Magufuli, akiaga waumini wenzie katika  Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph jijini Dar es salaam Joseph Mosha baada ya kuhudhuria  Ibada ya Jumatano ya Majivu kanisani hapo leo Machi 6, 2019 

PICHA NA IKULU

Mamia ya abiria wakwama kufuatia mgomo katika uwanja wa Kimataifa wa ndege Kenya....Ndege Zaelekezwa Kutua Tanzania

$
0
0
Ndege za uchukuzi wa abiria na mizigo zilizoratibiwa kutua katika uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta Nairobi Kenya zimeelekezwa kutua uwanja wa Julius Nyerere Dar es Salaam Tanzania kufuatia mgomo wa wafanya kazi wa mamlaka inayosimamia viwanja vya ndege.

Mapema asubuhi leo Wafanyakazi wa uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta wamefanya mgomo uliosababisha abiria kukwama kusafiri mjini Nairobi

Wafanyakazi wa usafiri wa ndege wameanza mgomo kupinga mpango wa kuunganishwa shughuli za usimamizi vya uwanja huo wa ndege kati ya shirika kuu la ndege nchini Kenya Airways na mamlaka ya usimamizi wa viwanja wa ndege KAA.

Muungano wa wafanyakazi hao (KAWU) umeuliza maswali kuhusu mipango hiyo ya kuunganisha shughuli kati ya pande hizo mbili na sasa unaitisha mageuzi katika usimamizi wa Kenya Airways na shirika la usimamizi wa viwanja vya ndege KAA.

Sambamba na hilo wafanyakazi wanatuhumu na kupinga makosa yanayofanyika katika uajiri wa wafanyakazi. 

Credit:BBC

BREAKING: Mgeja Awakimbia CHADEMA......Amfuata Lowassa CCM

$
0
0
Aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja, ambaye aliondoka chama hicho na kuhamia Chadema, leo Machi 06, 2019  naye ametangaza rasmi kurudi CCM

Mgeja amerudi CCM ikiwa ni siku chache  tu kupita baada ya mwanasiasa maarufu nchini na waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuondoka Chadema na kurudi CCM

Mgeja amedai wakati akiwa katika mapumziko ya kisiasa alijitathimini na kuona sababu zilizomfanya ahamie Chadema wakati wa uchaguzi mwaka 2015  sasa hazipo.

"Nimeamua kurudi nyumbani, sijafuata mkumbo wala kushawishiwa na mtu bali utendakazi wa Serikali yangu ya awamu ya tano umenifanya nirudi."

"Leo tarehe sita kwa utashi wangu naamua kurudi CCM na sitawaunga mkono tena Chadema," amesema.

Amesema sababu nyingine inayomfanya atoke Chadema ni kwa sababu chama hicho kimejaa ubinafsi na kisichosikiliza ushauri wa watu wengine.

"Nikiwa Chadema nimewashauri sana waachane na siasa za kiwanaharakati lakini hawakunisikiliza. Sasa ninaomba niwaambie kwa sababu hawakusikiliza ushauri wangu  wanakwenda kuwa na anguko kubwa la kisiasa uchaguzi wa 2020,” amesema.

Mgeja aliondoka CCM na kutimukia Chadema mwaka 2015 baada ya Lowassa kujiunga na chama hicho Julai 28, 2015 na kupewa fursa ya kugombea urais.

BREAKING: Mwalimu Respicius Mutazangira Anayetuhumiwa Kumchapa Mwanafunzi Hadi Kufariki Ahukumiwa Kunyongwa Hadi Kufa

$
0
0
Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba imemhukumu kunyongwa hadi kufa mwalimu Respicius Mutazangira kwa mauaji ya aliekuwa mwanafunzi wa shule ya msingi Kibeta, Sperius Eradius. Mwalimu Heriet Gerald aliekuwa akikabiliwa na mashtaka kama hayo ameachiwa huru. 

Walimu hao walishitakiwa kwa kumuua kwa kukusudia Sperius Eradius aliyekuwa mwanafunzi wa darasa la tano katika shule hiyo mwishoni mwa mwaka 2018.

Upande wa Jamhuri uliwasilisha mashahidi tisa katika kesi hiyo iliyosikilizwa kwa mwezi mmoja na Jaji Lameck Mlacha, ilianza Februari 6, 2019.

Inadaiwa walimu hao walitenda kosa la kumuadhibu kwa kipigo mwanafunzi Sperius Eradius kwa madai kuwa aliiba mkoba wa mwalimu  ukiwa na fedha.
 

DPP Adai Rufani ya Mbowe na Matiko Haina Mashiko......Mawakili Wao Wapangua Hoja, Mahakama Kutoa Uamuzi Kesho

$
0
0
Mawakili wa upande wa  Freeman Mbowe na Ester Matiko, Peter Kibatala na Jeremia Mtobesya wameiomba Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kuwarejeshea washtakiwa hao dhamana yao na kwamba rufani yao ina mashiko ya kisheria.

Mahakama hiyo iliyoketi chini ya Jaji Sam Rumanyika inasikiliza rufani ya walalamikaji Mwenyekiti Taifa wa Chadema,Freedman Mbowe na Mbunge wa Tarime mjini Esther Matiko wakipinga Mahakama ya Kisutu kuwafutia dhamana.

Kibatala amedai Mahakama ya Kisutu ilikosea kufuta dhamana ya walalamikaji na kwamba hakukua na hoja za msingi za kufanya hivyo.

Akijibu hoja hizo, Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) ambaye ni mlalamikiwa katika rufani hiyo ameiomba mahakama Kuu kutupilia mbali rufani hiyo kwa sababu haina mashiko maana walalamikaji walikiuka masharti ya dhamana.

DPP amesema sababu za wadhamini na walalamikiwa kushindwa kueleweka na mahakama ya Kisutu ni  sababu zilizosababisha  kutenguliwa dhamana hiyo, hivyo uamuzi huo ulikuwa  halali kwa kuwa kutokufika kwao mahakamani kumesababisha kesi kushindwa kuendelea kusikilizwa.

Jaji Sam Rumanyika baada ya kusikiliza hoja za rufani kwa pande zote mbili amesema atatoa uamuzi wake kesho saa 7:00 mchana.

Serikali yakasirishwa na tabia ya uongozi wa juu wa mgodi wa Acacia North Mara

$
0
0
Na Issa Mtuwa – Wizara ya Madini Tarime
Waziri wa madini Mhe. Doto Biteko ameonyesha kukerwa na tabia zinazofanywa na uongozi wa juu wa mgodi wa Acacia North Mara kwa serikali  kwa kushindwa kuhudhuria vikao mbalimbali vinavyo andaliwa baina ya pande hizo mbili, licha ya baadhi ya vikao kuongozwa na Waziri wa Madini lakini viongozi wa juu wa mgodi ambao ndio wafanya maamuzi na watekelezaji wa maagizo ya serikali wamekuwa wakishindwa kuhudhuria . 

Biteko amesema hayo wakati akihutubia wananchi kwenye mkutano wa hadhara jana Machi 5, 2019 katika kijiji cha Nyamongo  wilayani Tarime ikiwa  ni muendelezo wa ziara yake ya kikazi kwenye migodi ya North Mara na Buhemba. Biteko amesema anakerwa na tabia za uongozi wa mgodi huo kwa kushindwa kuhudhuria mara kwa mara mikutano mbalimbali ya ndani na ile ya hadhara badala yake wamekuwa wakituma wawakilishi.  

“ Kuanzia leo, haki ya mungu, haki ya mungu, haki ya mungu, mimi Waziri wa Madini leo ni siku ya mwisho kukaa na hawa wawakilishi kwenye vikao, hasa kama hivi vinavyo husu hatima ya maisha ya watu alafu wafanya maamuzi hawahudhurii. Niwambie ukweli nasikitishwa sana na tabia hii. Hawa walipo sio saizi yangu, kama ni hawa hata mimi ningewaleta maafisa wa wizara tena wale wanaolingana na hawa. 

Wanataka wawepo hadi afike Rais…!? nendeni mkawambie kwenye ngazi ya Wizara mimi ndio wamwisho katika kufanya maamuzi, kama mimi nipo kwa nini wao wasiwepoo…!? nyinyi mliokuja hapa nendeni mkawaambie hii ni mara ya mwisho wasifikiri serikali hii wanaweza kuiweka mfukoni, haikubaliki, hii tabia lazima ifike mwisho” alisema Biteko huku akisikitika sana. 

Amesema kwa ujumla hafurahishwi na namna mambo yanavyokwenda mgodini hapo ukilinganisha na migodi mingine. Mgodi wa North Mara umezungukwa na matatizo mengi sana yakiwemo ya malipo yafidiaza wananchi, utiririshaji wa maji yenye sumu kwenda kwenye makazi ya wananchi.

Serikali Yajitosa Kutatua Mgogoro Wa Wawekezaji Wa Kilimo Cha Kahawa Wilayani Hai Mkoani Kilimanjaro

$
0
0
Na Josephine Majura na Peter Haule, WFM, Kilimanjaro
Serikali  imeitaka Kampuni ya Tudeley Estates Limited  kutoka Uingereza  iliyoingia mkataba na vyama vya Ushirika Wilayani Hai Mkoani Kilimanjaro vinavyojishughulisha na uwekezaji wa Kilimo cha Kahawa (Murososangi), kurudi nchini ili kufanikisha utatuzi wa mgogoro uliosababishwa na kuibuka kwa mwekezaji mpya ambae mkataba wake haujulikani.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Isdor Mpango na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anaeshughulikia Uwekezaji Angela Kairuki walipofanya mkutano na Wawekezaji, Vyama vya Ushirika na Wadau wengine kuhusu mgogoro na Mwekezaji huyo Wilayani Hai Mkoani Kilimanjaro.

Dkt. Mpango alisema kuwa, Vyama vya Ushirika vya Murososangi, viliingia mkataba na Kampuni ya Tudeley Estates Limited ya nchini Uingereza ambapo washirika hao wenye mashamba eneo la Kibo na Kikafu  wilayani Hai, yenye ukubwa wa hekari 2054 walimpa Mwekezaji huyo ili kuendeleza zao la kahawa kuanzia mwaka 1998.

Alisema kuwa baada ya mwekezaji  huyo, Bw. Conrad Legg, kuonesha nia ya kutoendelea na uwekezaji huo aliondoka nchini, wakaja wawekezaji wengine kutoka Ujerumani ambao waliingia mkataba na Kampuni ya Tudeley Estates Limited, kwa kununua hisa bila  kuvishirikisha Vyama vya Ushirika vilivyoingia mkataba wa awali jambo lililosababisha sintofahamu kwa wana ushirika hao.

“Aliyeingia mkataba na Murososange, arudi nchini ili kutatua mgogoro huo ili kuona Wananchi wanawezaje kuingia mkataba mwingine na mwekezaji mpya ambao utalinda maslahi ya wananchi wenye mashamba hayo na pia mwekezaji”, alisema Dkt. Mpango.

Alisema Wanaushirika hao wanataka Mwekezaji wa kwanza arudi nchini ili wavunje mkataba wa awali kwa kuwa mkataba huo haujaisha muda wake hivyo hawawezi kuingia mkataba na mwekezaji mpya wakati ule wa awali bado unaendelea.

Aidha, alisema kuwa mwekezaji mpya kutoka Ujerumanim Bw. Marcus Shiber,  alianza kuleta fedha katika eneo la uwekezaji  na kulipa baadhi ya kodi za mtangulizi wake, madeni, mishahara na kuboresha miundombinu ya mashamba hayo bila kupata muafaka na Vyama vya Ushirika jambo ambalo liliendelea kuleta mgogoro.

Dkt. Mpango alisema kuwa, wamepata maelezo kutoka pande zote na baadhi ya maelezo hayo yanahitaji ushauri wa kisheria hivyo tumeiomba Ofisi ya Mwanasheria Mkuu kuyafanyia kazi mambo hayo ili kuweza kumshauri Rais wa Jamhuri ya Muungano wa  Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, namna bora ya kumaliza mgogoro huo bila kuingizia Serikali hasara.

Aliwatahadharisha watendaji wakuu wa serikali kutotumia ubabe na vitisho kwa wawekezaji ili kutoharibu taswira ya taifa katika masuala ya uwekezaji unaopigiwa chapuo hivi sasa na Serikali ya Awamu ya Tano, ili kuvutia mitaji, mapato ya serikali, ajira kwa vijana na kuvutia teknolojia za kisasa kwa maendeleo ya Taifa.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Angela Kairuki, alisema kuwa kutokana na mgogoro huo wa kiuwekezaji akaunti za Mwekezaji mpya kutoka Ujerumani ikiwemo ya Kampuni ya Kuza Afrika inayojishughulisha na kilimo cha parachichi Mkoani Mbeya ilifungwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA, kuhusiana na masualaya kodi, jambo lililosababisha baadhi ya shughuli za Mwekezaji huyo kukwama.

Alisema kuwa kikosi chao kupitia Waziri wa Fedha na Mipango aliyetumwa na Mhe. Rais Dkt. John Magufuli kutatua mgogoro huo, wameangalia iwapo taratibu za kufungwa akaunti hizo zilifuatwa na kutafuta njia bora ya kutatua tatizo hilo na pia kuona ni Mwekezaji yupi anafaa kuingia mkataba na Vyama vya Ushirika vya Murososangi, nia ikiwa ni kuona Vyama hivyo vinanufaika na Uwekezaji unakua nchini.

Kwa Upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Bi. Anna Mgwira, aliishukuru Serikali kwa hatua yake ya kutuma Mawaziri ili kutatua mgogoro huo wa muda mrefu ambao utatuzi wake utasaidia Wananchi kukuza uchumi wao na Taifa kwa ujumla.

Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Uwekezaji nchini-TIC, Bw. Geofrey Mwambe, alisema kuwa katika mkutano kati ya Mawaziri, Wawekezaji na Vyama vya Ushirika wamebaini kuwa utaratibu walioukuta Wawekezaji kutoka Ujerumani haukuwa sawa na ule ambao waliwekeana na Mwekezaji wa kwanza kutoka Uingereza, hivyo kuleta ugumu kiutendaji kwa Mwekezaji wa pili.

Alisema kuwa, Serikali inahitaji uwekezaji katika Sekta ya Kilimo ili  kupata malighafi ya viwanda nchini, kuongeza mnyororo wa thamani na kukuza pato la Taifa, hivyo inafanya jitihadi za kuvutia wawekezaji watakaoleta mitaji na teknolojia ya kisasa ili Taifa liweze kukabiliana na ushindani wa bidhaa katika soko la Kimataifa.

Mwakilishi wa mwekezaji mpya kutoka Ujerumani Bw. Robert Clowes, alimshukuru Mhe. Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa kuwatuma Mawaziri wake kuja kutatatua mgogoro huo, alisema Tanzania kuna fursa nyingi za uwekezaji hivyo yupo tayari kuendelea kuwekeza zaidi nchini kwa lengo la kupata manufaa kwa pande zote ikiwa ni pamoja na Kampuni yake na vyama vya ushirika wa kilimo cha Kahawa Wilayani Hai Mkoani Kilimanjaro.

Mwisho.

Serikali Yatishia Kuufunga mgodi wa North Mara

$
0
0
Na Issa Mtuwa - Tarime
Serikali imesema itaufunga mgodi wa North Mara ifikapo Machi 30, 2019 endapo mgodi huo utashindwa kuyadhibiti maji yenye sumu yanayo tiririka kutoka kwenye mabwawa ya kuhifadhia maji (topesumu) (Tailings Storage Facility -TSF). 
ya mgodi huo kuelekea kwenye makazi ya watu. 

Hayo yamesemwa leo machi 5, 2019 na Waziri wa Madini Mhe. Doto Biteko alipotembelea mgodini hapo kwa ziara ya kikazi ambapo pamoja na mambo mengine alitembelea mabwawa wa topesumu (TSF) na kuzungumza na uongozi wa mgodi na baadae na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Nyamongo wilaya ya Tarime kuzungumzia hatima ya malipo ya fidia za wananchi waliohamishwa kupisha shuguli  za mgodi. 

Biteko amesema serikali hairidhishwi na namna mgodi wa North Mara kwa jinsi wanavyo zingatia swala la utunzaji wa maji yenye sumu kwenye (TSF) zao. Amesema serikali inathamini sana maisha ya watu na mtu mmoja mmoja, na kwamba maisha ya mtu mmoja ni bora kuliko shuguli zote za mgodi. 

“ Naomba niseme ukweli, tena kutoka moyoni, sijaridhishwa na hili jambo la utiririshaji wa maji yenye sumu kuelekea kwenye makazi ya watu. Serikali hii ya awamu ya tano ya Dkt. John Pombe Magufuli inathamini sana maisha ya watu wake kuliko kitu chochote. Thamani yamaisha ya mtanzania mmoja ni bora kuliko kinachochibwa hapa. Nitoe rai kwa mgodi ifikapo Machi 30, mwaka huu, hili jambo liwe limekwisha, kinyume cha hapo, nitafunga mgodi mpaka pale mtakapo tekeleza jambo hili” alisema Biteko. 

Kwa upande wa uongozi wa mgodi umesema, utatekeleza agizo hilo na kwamba juhudi za kudhibiti topesumu kuelekea kwenye makazi ya watu limepewa kipaumbele na kwamba ndani ya muda huo litakuwa limekamilika.  

Katika ziara hiyo, Waziri Biteko aliambatana na baadhi ya Maafisa wa Wizara hiyo akiwemo Kamishna wa Madini Mha. David Mlabwa na Afisa Madini mkoa wa Mara Mha. Nyaisara Mgaya, wengine ni kamati ya ulinzi na usalama mkoa wa mara wakiongwa na mwenyekiti wake ambae pia ni mkuu wa mkoa wa Mara bwana Adam Kigoma Malima. 

Ziara hiyo inafuatia vikao mbalimbali vya awali vilivyofanyika mwaka huu vikilenga masuala mbalimbali yanoyo husu mgodi huo likiwemo swala la udhibiti wa maji yenye sumu (topesumu) yanayo lalamikiwa na wananchi wanaoishi kuzunguka mgodi huo, kikao cha kwanza kilifanyika Januari 19, chini ya makatibu wakuu wa wizara saba ((Madini, Makamu wa Rais Mazingira (NEMC), Ardhi, TAMISEMI, Afya, Fedha na Maji)) ambapo serikali ilitoa miezi nane kutekeleza maagizo yaliyopewa.
 

Waziri Mkuu Atembelea TFDA na TBS....Awataka Mawaziri Watano Wakutane Haraka na Wampe Majibu Ifikapo March 30

$
0
0
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Mawaziri wa Kilimo, Uwekezaji, Viwandana Biashara, Mifugo na Uvuvi na Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wakutane na wafanye mapitio ya taasisi zao na kuangalia maeneo yanayogongana kiutendaji ili kila mmoja abaki na jukumu lake.

Ametoa agizo hilo leo (Jumatano, Machi 6, 2019) alipotembelea Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na kukagua shughuli mbalimbali zinazofanywa na taasisi hizo na amewaagiza mawaziri wakutane na wampelekee taarifa ya mapendekezo yao ifikapo Machi 30, 2019.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya kuwepo kwa malalamiko na manung’uniko kutoka kwa baadhi ya wafanyabiashara ambao wamedai kuwepo kwa muingiliano wa majukumu ya kiutendaji ya taasisi hizo, hivyo kuwasababisha washindwe kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Waziri Mkuu amesema taasisi hizo zinashughuli ambazo zinaingiliana na kusababisha malalamiko kwa wateja wao, ambapo ametolea mfano suala la kudhibiti ubora wa bidhaa ambalo linafanywa na TFDA na TBS kwa mujibu wa sheria. Amewataka wapitie sheria zao na wajue ukomo majukumu yao.

“Kutaneni pitieni maelekezo ya Serikali yanayoelekeza namna ya kuzifanya taasisi hizi na zingine zinazofanya shughuli zinazofanana zilizo katika wizara zenu bila kusanau Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara (blue print). Ifikapo tarehe 30 mwezi huu niwe nimepata mapendekezo yenu,” amesisitiza.

Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka watendaji wa taasisi hizo wabadilike na waache urasimu kwasababu hauna tija katika utekelezaji wa majukumu yao na badala yake unaweza kuwayumbisha kwenye ufanyaji wao wa kazi. “Kila mmoja atekeleze majukumu yake kwa uzingatia maadili ya taaluma yake.”

Pia, Waziri Mkuu amewataka waangalie namna ya kuwahisha majibu ya vipimo vya bidhaa wanazoletewa na wateja, kama watakuwa wamekamilisha kabla ya siku za kisheria wawajulishe wateja wao na kuhusu sampuli ambazo zitakuwa hazijaharibika wakati wa vipimo wawarudishie.

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuzitaka taasisi hizo ziangalie namna ya kusogeza huduma kwa wananchi kwa kuwa na watumishi katika ngazi za wilaya na kwa TFDA ameitaka ianzishe maabara nyingine mbili kwenye kanda ya Nyanda za Juu Kusini na ya Kaskazini ili kusogeza huduma kwa wananchi.

 (mwisho)

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, MACHI 6, 2019.

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Alhamisi ya March 7

BREAKING: Mtangazaji wa Clouds FM Ephraim Samson Kibonde Afariki Dunia

$
0
0
Mtangazaji wa Clouds FM Ephraim Samson Kibonde, amefariki dunia Alfajiri ya leo Machi 7, 2019 akiwa mkoani Mwanza.

Kibonde ambaye alikuwa MC kwenye msiba wa Ruge amekutwa na umauti kwenye hospitali ya Bugando mkoani Mwanza.

Mtangazaji huyo alikuwa miongoni mwa waombolezaji waliomsindikiza Ruge hadi katika maziko yake wilayani Bukoba.

Kwa mujibu wa Sebastian Maganga, taratibu zinafanyika kupanga mipango ya msiba huo.


Rais Mpya DRC Felix Tshisekedi na mtangulizi wake Joseph Kabila waamua kuunda serikali ya muungano

$
0
0
Rais mpya wa  Jamhuri ya Kidmeokrasi ya Congo, Felix Tshisekedi na mtangulizi wake Joseph Kabila wamesema wameamua kuunda serikali ya muungano kufuatia mazungumzo, shirika la habari la AFP linaripoti.

Licha ya ushindi wa rais Tshisekedi -- kiongozi huyo amejikuta akilazimika kugawanya uongozi tangu uchaguzi huo wa urais.

Mpaka sasa hajafanikiwa kumteua waziri mkuu kutokana na kwamba muungano wa Kabila - Common Front for Congo (FCC) una uwingi katika bunge la taifa.

Katika taarifa ya pamoja hapo jana Jumatano, Tshisekedi na Kabila wamesema kwamba licha ya "FCC kuwa na uwingi mkubwa bungeni" katika kuidhinisha matakwa yalioelezewa na wapiga kura, FCC na CACH wanaonesha uwajibikaji "wa malengo yao ya pamoja kuongoza pamoja kama sehemu ya serikali ya muungano" linaripoti AFP.
 
Taarifa hiyo inafuata ziara ya Tshisekedi nchini Namibia wiki iliyopita ambapo alielezea kukasirishwa kwake kwa kutoweza kuwa na uwingi  wa wabunge wa kuunga mkono chaguo lake la wadhifa wa waziri mkuu.

India na Pakistan Zashambuliana Tena

$
0
0
Wanajeshi wa India na Pakistan wameshambulia vituo vya kijeshi na vjiji kwenye mpaka wao wenye shughuli nyingi za kijeshi wa jimbo linalogombaniwa la Kashmir, katika machafuko mapya licha ya nchi hizo mbili kuongeza juhudi za kutuliza mvutano. 

Wanajeshi wa nchi hizo wametuhumiana kwa kuanzisha mashambulizi katika eneo hilo. Hakuna habari zozote zilizotolewa maramoja kuhusu hasara iliyotokea. 

Hofu imekuwa kubwa tangu ndege ya India iliporuka katika anga ya Pakistan wiki iliyopita ikifanya kile ambacho India ilisema ni shambulizi dhidi ya wanamgambo waliohusika na mlipuko wa bomu wa kujitoa mhanga Februari 14 katika eneo la Kashmir linalodhibitiwa na India, ambalo liliwauwa wanajeshi 40 wa India. 

Katika juhudi nyingine za kutuliza mvutano na India, Pakistan jana iliwakamata watu kadhaa akiwemo kaka wa kiongozi wa kundi la wanamgambo lililopigwa marufuku la Jaish e Mohammad, ambalo lilidai kuhusika na shambulizi la bomu la kujitoa muhanga Kashmir. 

-DW

Iran yasema hakuna nafasi ya mazungumzo na Marekani

$
0
0
Rais wa Iran Hassan Rouhani amesema  kuwa hakuna uwezekano wa kufanya mazungumzo wala kufikia makubaliano na Marekani, kwa madai kuwa Marekani inataka kuiangusha serikali ya Jamhuri hiyo ya Kiislamu. 

Katika hotuba kwa njia ya televisheni, Rouhani alisema Marekani inasema Iran inapaswa kubadilika, na kurudi nyuma kama ilivyokuwa kabla ya mapinduzi ya Kiislamu ya 1979, wakati ikitawaliwa na ufalme ulioungwa mkono na Marekani. 

Utawala wa Trump umechukua msimamo mkali dhidi ya Iran lakini inasisitiza kuwa Marekani haijaribu kuiangusha serikali. 

Hata hivyo, mvutano kati ya nchi hizo mbili umeongezeka baada ya Marekani kujiondoa mwaka jana katika mkataba wa nyuklia wa 2015 na kuiwekea Iran vikwazo vipya ambavyo vimeiathiri sana sekta muhimu ya mafuta nchini Iran. 

Rouhani amesema nchi yake iko kwenye vita vya kiuchumi kwa sababu ya vikwazo ilivyowekewa na Marekani na haiwezi kusalimu amri. 
 
-DW

Korea Kaskazini yadaiwa Kuanza kujenga upya vinu vya nyuklia

$
0
0
Picha mpya zilizopigwa kwa kutumia Satellite zimebaini kuwa Korea Kaskazini inajenga tena vinu vya makombora ya nyuklia, siku chache baada ya mkutano kati ya kiongozi wake Kim Jong Un na Rais wa Marekani, Donald Trump kuvunjika.

Kwa mujibu wa taarifa za wachambuzi ambazo zimeripotiwa na shirika la habari la Reuters, vinu hivyo vimeonekana katika eneo la Tongchang-ri ambalo lilikuwa likitumika kuzindua na kufanya majaribio ya makombora ya nyuklia.

Kazi ya kuteketeza vinu hivyo ilianza mwaka jana, lakini ilisitishwa tena baada ya mazungumzo kati ya nchi hizo kuanza kuwa na muenendo usioridhisha.

Hivi karibuni, Marekani imeonya kuwa Korea Kaskazini inaweza kukabiliwa na vikwazo zaidi endapo itajaribu kuendeleza uundwaji wa silaha za kinyuklia.

Uthibitisho wa picha za satellite umewekwa wazi na wataalam wa intelijensia kutoka Korea Kusini ambao wamedai kuwa huenda kuna ukuaji wa haraka wa uzalishaji mpya wa roketi za makombora na mabomu ya nyuklia katika kituo hicho.

Kikao kati ya Trump na Kim Jong Un kilivunjika kwa kile ambacho Rais huyo wa Marekani alidai kuwa walitaka kuondolewa vikwazo vyote kama sharti la kuteketeza vinu vya silaha za nyuklia, lakini Marekani haikuwa tayari.

Lipumba: Lowassa Alikuwa ni Zaidi Ya Mzigo

$
0
0
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amesema kwamba japokuwa upo usemi wa kuwa mzigo mzito anapewa Mnyamwezi aubebe, mzigo wa kumnadi Lowassa ulikuwa mzito sana.
 
Lipumba amesema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari suala la Lowassa kuhamia CCM.

Lipumba alisema kwamba hakukubaliana na uamuzi wa washirika wenzake kumchagua Lowassa kuwa mgombea urais wa Ukawa mwaka 2015 na kwamba baada ya muda mfupi naye alitangaza nia ya kugombea urais, uamuzi ambao uliwaudhi wenzake wa Ukawa.

"Nijikute kweli Lipumba mimi nasimama jukwaani namnadi Lowassa?, Japo wanasema mzigo mzito mpe Mnywamwezi, mzigo ule ulikuwa mzito sana," alisema Profesa Lipumba.

Pamoja na hayo, Mwenyekiti huyo anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa amesema kwamba Katubu Mkuu wa Chama chao Maalim Seif hana tofauti na Lowassa kwa kuwa wote walihamia upinzani kutafuta nafasi ya kugombea urais jambo ambalo kwake amelitafsiri kama ulafi wa madaraka.

Amesema kwamba hata ndani ya CUF, Maalim Seif amekuwa akiutaka urais kwa nguvu na kusahau malengo mengine ya kitaifa ya chama, jambo ambalo amesema lingekiwezesha chama hicho kuunda Serikali ya Zanzibar.
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live




Latest Images