Serikali imeamua kuifumua Sheria ya Uvuvi Namba 22 ya mwaka 2003 na kanuni zake za mwaka 2009 ili kuondoa vikwazo vya kibiashara na uwekezaji katika sekta ya uvuvi.
Pia kwenda na kasi ya mabadiliko ya Serikali ya awamu ya tano inayolenga kujenga Tanzania ya viwanda, kuwatetea na kuwalinda wanyonge.
Akizungumza katika uzinduzi wa ukusanyaji maoni ya wadau kuhusu rasimu ya Sheria ya Uvuvi na Sheria ya Ukuzaji viumbe kwenye maji jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, alitaja sababu nyingine zilizosababisha kuwapo mabadiliko hayo.
Sababu ya kwanza pamoja na kutoa ulinzi madhubuti wa rasilimali za uvuvi, kuongeza uzalishaji na kuwa na masoko ya uhakika sambamba na kudhibiti utoroshwaji na uingizaji holela wa mazao ya uvuvi nchini.
Aidha, Mpina alisema sheria hiyo mpya inatakiwa iendane pia na mabadiliko na matumizi ya sayansi na teknolojia katika uvuvi na ukuzaji viumbe kwenye maji ili kwenda sambamba na mahitaji pamoja na kuwapo mwamko mkubwa wa ufugaji wa samaki kwenye maji uliojitokeza miongoni mwa wananchi.
Alisema pamoja na rasimu ya sheria hizo mbili pia Serikali iko kwenye hatua za mwisho za kuzifanyia marekebisho Sheria ya Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu Namba 29 ya mwaka 1994 na Kanuni zake za mwaka 2009 na Sheria ya Bahari Kuu Cap 388 na Kanuni zake za mwaka 2007 na 2016.
Hivyo Waziri Mpina aliwasihi wananchi kutoa maoni yasiyofungamana na upande wowote na kuacha tabia ya kila mmoja kuvutia upande wake ili kuwezesha kutunga sheria madhubuti.
Aidha Waziri Mpina alieleza utajiri wa kipekee wa rasilimali za uvuvi nchini ikiwamo kuwa na eneo kubwa la maji lenye kilomita za mraba 346,337 sawa na asilimia 36.7 ya eneo lote la nchi, fukwe ndefu na za kuvutia, kuwapo kwa samaki na viumbe vingine ambavyo vimetoweka na vingine vikiwa kwenye tishio la kutoweka duniani.
Pia kuwapo kwa mito, mabwawa na maziwa yenye sifa za kipekee ikiwemo Ziwa Victoria ambalo ni la pili kwa ukubwa duniani na Ziwa Tanganyika ambalo ni la pili kwa kina duniani na la kwanza kwa ujazo wa maji duniani.
Alisisitiza kuwa wakati nchi inakwenda kutunga sheria hiyo mpya ya uvuvi, ni muhimu kama Taifa kujiuliza maswali kadhaa ikiwamo matumizi sahihi ya rasilimali hizo.
"Lazima tujiulize tunapata wapi uhalali wa kuagiza samaki kutoka nje ya nchi?, tujiulize kwa nini tumeshindwa kulihudumia soko la ndani na la nchi jirani, Afrika na dunia?, kwa nini tuzidiwe uzalishaji na mauzo na nchi ambazo tunazizidi kwa mbali kwa rasilimali?,.
"Vilevile Kwanini tuwe na wavuvi masikini tena ambao hawana zana bora za uvuvi, kwanini biashara, uwekezaji na ujenzi wa viwanda ni wa kusuasua ? haya ndio maswali tunayopaswa kujiuliza kama Taifa," alihoji Mpina.
Hivyo Waziri Mpina alisema kutokana na ugumu wa maswali
hayo ndio maana wizara yake ikaamua ni bora kuifumua Sheria ya Uvuvi Namba 22 ya mwaka 2003 na Kanuni zake za mwaka 2009 ili kusaidia kupata majawabu ya namna gani kama taifa litatoka kwenye mkwamo huo.