Serikali wilayani Kahama mkoani Shinyanga imesema itachukua hatua kali za kisheria kwa Wagombea wa nafasi za Udiwani na Ubunge ambao watabainika kuanza kampeni kabla ya muda utakaopangwa na Tume ya taifa ya Uchaguzi ili kudhibiti vitendo vya rushwa.
Kauli hiyo imetolewa June 22, 2020 na Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Anamringi Macha wakati akifungua Jengo la kupumzikia watu wanaokwenda kuwaona wagonjwa katika hospitali ya halmashauri ya Mji wa Kahama lililojengwa na Kampuni ya KOM lililogharimu zaidi ya milioni 11.
Alisema kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha inawadhibiti wagombea wanaopenda kutoa rushwa kwa wananchi pindi uchaguzi mkuu unapokaribia hawapati nafasi na watakaobainika wanajikuta mikononi mwa vyombo vya dola.
“Wapo baadhi ya wagombea kwenye jamii wameanza kutoa zawadi na misaada mbalimbali kwa wananchi yenye viashiria vya kuomba kuchaguliwa kuchaguliwa huu sio wakati wake misaada ya aina hiyo haina nafasi kwa sasa kwani inadalili zote za rushwa na kwanini haikutolewa kipindi cha nyuma,”alisema Macha.
Sambamba Macha aimepongeza Kampuni hiyo kwa kujenga jengo hilo ambalo ni muhimu kutokana na Hospitali hiyo kutokuwa na eneo la kupumzikia wagonjwa kwa muda mrefu hali ambayo ilikuwa ikisababisha baadhi ya ndugu jamaa na marafiki wanaokwenda kusalimia wagonjwa wao kukaa nje ya uzio.
“KOMU ni kampuni ya Wazawa wa kahama ambao ni wazalendo kwani wamekuwa wakitusaidia misaada mbalimbali pindi tunapowaomba,nitoe rai kwa Makampuni mengine kuiga mfano wa KOMU kwa kuchangia shughuli za maendeleo katika jamii inayowazunguka,”alisema Macha.
Kwa upande wake Meneja Uzalishaji wa Kampuni hiyo Brayson Edward alisema kuwa jengo hilo limegharimu shilingi milioni 11 na laki nane hadi kukamilika kwake na kuumba uongozi wa hospitali hiyo kulitunza ili lilete tija kama ilivyokusudiwa.
Aliongeza kuwa KOMU itaendelea kushirikiana na serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk John Pombe Magufuli ili kuhakikisha kero mbalimbali ambazo zinawakabili wananchi zinapatiwa ufumbuzi wa haraka na shughuli za maendeleo zikiendelea kushika kasi.
Asha Said ni mmoja ya wananchi waliohudhuria hafla hiyo alisema kuwa hapo awali walikuwa wanalazimika kukaa nje ya fensi ya Hospitali hiyo juani na nyakati za masika walikuwa wananyeshwa na mvua kutokana na kukosekana kwa eneo maalumu la kupumzikia wagonjwa.
Mwisho.