Katika jitihada za kuhakikisha sekta ya kilimo inakua na wakulima wananufaika, Halmashauri ya Mji wa Kahama mkoani Shinyanga imetoa ruzuku ya pembejeo bure zenye thamani ya shilingi milioni 17.9 kwa wakulima vijana 39 ambao wanalima mazao ya biashara.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji,Anderson Msumba wakati akisoma taarifa ya utekelezaji ya miradi ya mbalimbali ya maendeleo iliyotekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano katika kikao cha Baraza la Mwisho la Madiwani, alisema Ruzuku hiyo inatolewa kwa lengo la kuwapa motisha wakulima vijana ambao wameamua kuwekeza katika sekta hiyo.
Alisema kuwa kila Mwaka Halmashauri hiyo hutenga shilingi milioni 50 kila mwaka wa fedha kama ruzuku ya kilimo kwaajili ya vijana wanaolima zaidi ya hekari tano za mazao ya biashara ili kuwawezesha kukabiliana na changamoto mbalimbali katika msimu wa kilimo.
“Fedha hizi zinatokana na mapato ya ndani ya Halmashauri yetu kwa ajili ya kununua pembejeo za kilimo kama mbolea za kupandia(NPK),Mahindi, mbegu za alizeti na sumu za kuua wadudu wanaoshambulia zao la pamba na kuzigawa kwa wakulima,”alisema Msumba.
Alifafanua kuwa, Mwaka 2018/19 Halmashauri ilitenga kiasi cha shilingi Milioni 54 ambapo jumla ya shilingi Milioni 14.19 pekee ndio zilitumika kutokana na mwitikio wa wakulima vijana kutotojitokeza kwa wingi na kuwataka katika msimu ujao 2020/21 kujitokeza kwa wingi.
Masunga kisena Mkulima na mkazi wa kata ya kilago alisema wamejikita katika kilimo cha kibiashara kwa kulima mazao yanayoendana na masoko yaliyopo ukilinganisha na kipindi cha nyuma,vijana walikuwa wakishinda vijiwezi na kubishana masuala ya kisiasa bila ya kufanyakazi za maendeleo.
Mwaka jana tulipatiwa pembejeo bure zenye dhamani ya shilingi Milioni 17.9 na kila kijana mwenye shamba la hekari tano kutoka kata 20 zilizopo Halmashauri ya Mji kahama alipatiwa mbolea za kupandia(NPK),Mahindi, mbegu za alizeti na sumu ya kuua wadudu wanaoshambulia zao la pamba.
Nae John Mayunga ameiomba Halmashauri hiyo kuwatafutia masoko kwa mazao wanayozalisha kama vile mpunga,pamba na alizeti ambayo mwaka huu wamezalisha kwa wingi sambamba na kupatiwa elimu ya kilimo cha kisasa kutoka ili kuongeza tija katika sekta hiyo.
Jumla ya ekari 195 za mazao mbalimbali ya biashara zimelimwa katika msimu huu wa kilimo 2020/21 katika Halmashauri ya Mji kahama na inakuwa yakwanza nchini kutoa ruzuku ya pembejeo za kilimo bure kwa wakulima wake.
Mwisho.