SALVATORY NTANDU
Wananchi zaidi ya 100 waliokumbwa na maafa ya kubomolewa kwa nyumba zao kutokana na mafuriko katika kata Ngaya,Bulige na Kashishi katika Halmashauri ya Msalala Wilayani Kahama mkoani Shinyanga wameomba kupatiwa elimu ya ujenzi wa makazi bora ili kuwawezesha kujenga nyumba za kisasa .
Wananchi zaidi ya 100 waliokumbwa na maafa ya kubomolewa kwa nyumba zao kutokana na mafuriko katika kata Ngaya,Bulige na Kashishi katika Halmashauri ya Msalala Wilayani Kahama mkoani Shinyanga wameomba kupatiwa elimu ya ujenzi wa makazi bora ili kuwawezesha kujenga nyumba za kisasa .
Wakizungumza katika hafla maalumu ya kukabidhiwa misaada ya Magodoro,chandarua,blanketi na ndoo za maji yaliyotolewa na Shirika la Msalaba Mwekundu iliyofanyika June 4 Mwaka huu katika kata za Ngaya na Bulige iliyoongozwa na Mkuu wa wilaya ya Kahama Anamringi Macha.
Merry Shija ni mmoja wa wahanga wa mafuriko hayo alisema kuwa endapo serikali ikiwapatia elimu hiyo itawasaidia wao kujenga nyumba za kisasa ambazo hazitapata athari zitokanazo na mafuriko pindi yanapotokea hususani katika maeneo ya vijijini.
“Mwaka huu sisi tumevuna mazao ya kutosha,tunatarajia kuanza ujenzi wa nyumba zetu zilizobomolewa na mafuriko yaliyosababishwa na mvua za masika ambazo mwaka huu zimenyesha kwa wingi,tutahakikisha tunatenga fedha kwaajili ya ujenzi wa nyumba zetu,”alisema Shija.
Nae Felista Bula alisema kuwa ukosefu wa elimu ya ujenzi hususani vijijni bado ni tatizo kutokana na wengi wao kutokuwa na maarifa ya ujenzi wa nyumba za kisasa hivyo ni budi serikali ikaona umuhimu wa kutoa elimu ya ujenzi kwa wananchi.
Kwa upande wake meneja wa maafa nchini kutoka shirika la msalaba mwekundu Simon Kadogosa alisema kuwa misaada hiyo ni sehemu ya mchango wao kwa jamii ili kuiunga mkono serikali hususani maafa yanapotokea na kuwataka wananchi wa maeneo hayo kuhakikisha wanazingatia maelekezo ya serikali kuhusiana na ujenzi wa makazi bora.
“Misaada hii imegharimu zaidi ya shilingi milioni 40 ambayo ni ndoo za maji,vyandarua,mashuka(Blanket) na Magodoro ambayo yamegawiwa kwa wakazi zaidi ya 100 waliopata maafa hayo,”alisema Kadogosa.
Akitolea ufafanuzi suala hilo Mkuu wa wilaya ya Kahama Anamringi Macha aliwataka wakazi hao kuhama mabondeni pamoja na maeneo yenye mikondo ya Maji ili kuondokana na tatizo hilo ambalo limekuwa likisababisha wanachi kuhangaika hususani kipindi cha Mvua zinapoanza kunyesha.
“Jengeni makazi bora kwa kutumia tofali za kuchoma tumieni pumba za mpunga kuchomea tofali zenu ili muweze kuondokana natatizo hilo ambalo linaweza kuzuilika sambamaba kujenga katika maeneo ambayo ni salama yaliyotengwa kwaajili ya shughuli za Mkazi.
Mwisho.