Quantcast
Channel: MPEKUZI
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live

Amtaka Mama yake Amtunzie Watoto Baada ya Kumuua Mkewe kwa Kumchinja na Kisha na Yeye Kujinyonga

$
0
0

Watu watatu wamefanya mauaji ya kutisha, wawili wamechinja wake zao, huku mmoja akiacha ujumbe wa kumtaka mama yake mzazi amtunzuie watoto na mwingine amemuua mama yake.

Katika tukio la Dodoma, Samson Joramu(44), mkazi wa Chololo, Kata ya Kikombo, alimchinja mke wake, Rehema Joram (43) kabla ya kujiua kwa kunyonga katika shamba lake.

Watu walioshuhudia walisema, Joramu baada ya kumuua mkewe alijinyonga na aliandika ujumbe uliokutwa mfukoni kwake, ukisomeka: “Mama tunza wanangu, mimi nimekufa.” Kadhalika aliandika orodha ya watu anaowadai.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa akizungumzia tukio hilo alisema kuwa: “Ni kweli taarifa za vifo kutoka Kikombo ninazo, yule mmoja alimuua mama yake kwa kumkatakata sehemu mbalimbali za mwili jana (juzi), na huyu mwingine alimuua mke wake asubuhi ya leo (jana) kisha naye akajinyonga,” alisema.

Katika tukio jingine, Amos Kalenda, mkazi wa Kikombo, Dodoma anadaiwa kumuua mama yake mzazi, Joyce Kalenda kwa kumchinja. Chanzo cha mauaji hayo kinadaiwa ni mama huyo kumnyima chakula.

Mkoani Mara katika Wilaya ya Tarime, Wambura Mariba (50) mkazi wa Matongo, Nyamongo, Tarime, anadaiwa kumuua kwa kumchinja mkewe, Maria Wambura(40) kwa madai anamroga.

Kamanda wa Polisi Tarime/Rorya, Andrew Satta alisema tukio hilo lilitokea Juni 8 saa tisa alasiri.

Satta alisema baada ya mtuhumiwa kutekeleza mauaji hayo, alichoma moto nyumba zao mbili, zilizokuwa zimeezekwa kwa nyasi.

“Baada ya tukio hilo kutokea, wananchi walijichukulia sheria mkononi na kumjeruhi mtuhumiwa kichwani na kitu chenye ncha kali,”alisema Satta.

Wakizungumzia tukio hilo ndugu wa marehemu, Samwel Wambura alisema tukio la mwanamke huyo kuuawa, lilitekelezwa mbele ya watoto wake wakati akiwaandalia chakula.

“Alipomaliza kumuua, alianza kuandaa moto achome nyumba ili mwili wa mkewe uungulie ndani, majirani waliwahi kuuchukua mwili, lakini alianza kuwafukuza huku akiwa ameshika panga,” alisema na kuongeza: “Wananchi baada ya kuona tukio hilo walipiga simu kituo cha polisi ambao walifika na kumkamata mtuhumiwa.”

Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Nyangoto, Kagumiwa Kaijage alisema, alipokea mwili wa marehemu ukiwa umekatwa shingoni na mtuhumiwa amelazwa hospitali hapo akiwa na majeraha sehemu mbalimbali mwilini.

Hawara wa Mfanyakazi wa ndani Atiwa Mbaroni Akihusishwa na Mauaji ya Aneth Msuya ( Dada wa Bilionea Msuya )

$
0
0
Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limewakamata watu wengine wawili, akiwamo mpenzi wa mfanyakazi wa ndani wa Aneth Msuya, aliyeuawa kwa kuchinjwa nyumbani kwake.

Aneth, ambaye ni dada wa Bilionea Erasto Msuya, aliuawa kwa kuchinjwa na watu wasiojulikana Mei 26 nyumbani kwake Kibada, Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Wauaji hao hawakuchukua chochote kwenye nyumba hiyo. Bilionea Msuya aliuawa Agosti mwaka jana kwa kupigwa risasi na tayari watu 12 wamekatwa, wakituhumiwa kuhusika na mauaji hayo.

Kamanda wa Kanda hiyo, Simon Sirro alisema hadi sasa wamekamata watuhumiwa wanne wakihusishwa na mauaji ya dada wa bilionea huyo.

Kati ya watuhumiwa waliokamatwa, yumo mume wa Aneth, msaidizi wa ndani wa Aneth na mtuhumiwa mwingine ambaye Kamanda Sirro hakumtaja jina.

“Mwanzo tulimkamata mume wa marehemu na msaidizi wa ndani wa marehemu, lakini sasa wameongezeka wengine wawili, akiwamo hawara wa msaidizi wa ndani. Tunaendelea kuwahoji na upelelezi ukikamilika tutawafikisha mahakamani,” alisema Sirro.

Kwa mujibu wa mama mdogo wa marehemu, Lilian Benjamin, msaidizi wa ndani wa dada wa bilionea huyo aliondoka saa sita mchana na kuacha funguo nyumba ya jirani.

Lilian alisema msaidizi huyo alimpigia simu ghafla bosi wake mchana na kumwambia anaondoka na hataendelea na kazi.

Mauaji ya Aneth ni mwendelezo wa mauaji yanayoikumba familia hiyo ya Msuya baada ya kaka yake, Erasto ambaye alikuwa ni mfanyabiashara tajiri wa madini, kuuawa Agosti 7, 2013 kwa kupigwa risasi zaidi ya 12 kwa kutumia bunduki ya SMG katika eneo la Mijohoroni wilayani Hai, Mkoa wa Kilimanjaro.

Februari 10, mawakili wanaosimamia kesi ya Erasto, Hudson Ndusyepo, Majura Magafu, Emanuel Safari na John Lundu, waliiambia mahakama kuwa Serikali inakusudia kuita mashahidi 50 kuthibitisha shtaka hilo na kuwasilisha vielelezo 40, ikiwamo bunduki hiyo.

Mawakili hao walidai mipango ya kumuua bilionea Msuya ilianza Julai 26,2013 jijini Arusha, ikiwahusisha washtakiwa na waliotekeleza mauaji hayo wangelipwa Sh5 milioni kila mmoja.

Wakitoa maelezo ya tukio hilo, mawakili hao waliiambia mahakama kuwa washiriki ambao wasingeenda moja kwa moja kwenye mauaji, wao wangelipwa Sh3 milioni kila mmoja.

Mshtakiwa wa kwanza, Shariff Mohamed anadaiwa kuwa ndiye alikuwa mpangaji mkuu na alitoa fedha za maandalizi yote ya mauaji.

Washtakiwa wengine ni Shaibu Jumanne, ambaye anafahamika kwa jina la utani la Mredii, Mussa Mangu, Jalila Zuberi (Said), Karim Kihundwa, Sadick Jabir (Msudani) na Ally Mussa (Mjeshi).

Wabunge wa Kambi ya Upinzani Wajitoa Kamati ya Bunge ya Ukimwi Baada ya IKULU Kuwanyiima Kibali cha Kwenda Marekani

$
0
0

Ofisi ya Rais Ikulu imewanyima vibali vya kusafiri kwenda Marekani wabunge wawili wa Kambi ya Upinzani, bungeni na kumruhusu mbunge wa Geita Mjini (CCM), John Kanyasu. 

Wabunge hao wa kambi ya upinzani waliochaguliwa kwenda Marekani ni Savelina Mwijage (CUF) na  Mwita Mwaikabwe (Chadema)

Wabunge hao watatu ni wajumbe wa Kamati ya Masuala ya Ukimwi, lakini baada ya kunyimwa vibali hivyo wamejitoa kwenye kamati hiyo wakipinga kitendo hicho.

Akizungumza na waandishi wa habari bungeni mjini Dodoma, mbunge wa Ukonga (Chadema), Mwita Mwikwabe alisema walipata barua ya kuteuliwa kushiriki safari hiyo kutoka Ofisi ya Bunge Mei 24.

“Tunapenda kukufahamisha kuwa Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai amekuteua kushiriki mkutano wa ngazi ya juu ya maamuzi kuhusu Ukimwi duniani utakaofanyika 08-10 New York, Marekani,” alinukuu barua hiyo iliyosainiwa na Patson Sobha kwa niaba ya Katibu wa Bunge.

Katika barua hiyo wametajwa wabunge wengine kwenye safari hiyo kuwa ni mbunge wa viti maalum (CUF), Savelina Mwijage.

“Nikiwa Tarime nilipata simu kutoka kwa Patson kwamba, Naibu Spika alipokea simu kutoka Ikulu kuwa imezuia vibali vyetu vya kwenda Marekani na badala yake Kanyasu ameteuliwa,” alisema Mwikabe.

“Tunashangaa, kuteuliwa tuliambiwa kwa barua, lakini kukataliwa tuliambiwa kwa simu,” alisema Mwita.

Alisema kutokana na kutopewa kibali, wajumbe wote wa kambi hiyo wamejitoa kwenye Kamati ya Bunge ya Ukimwi.

“Hayo yote yanafanyika kwa sababu Naibu Spika hatupendi kabisa wabunge wa upinzani ndiyo maana wametufanyia haya,” alisema.

Kwa upande wake, mbunge wa Vunjo (NCCR-Mageuzi), James Mbatia alisema Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliwaambia katika mkutano wa wabunge wote kuwa hawahusiki katika uombaji wa vibali kutoka Ikulu.

“Mimi mwenyewe nimeshawahi kusafiri zaidi ya mara tatu mbona sijawahi kuomba kibali kutoka Ikulu?” alihoji Mbatia.

Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah alihoji kama wabunge hao ndiyo wenye haki ya kusafiri. Pia alihoji haraka waliyonayo wabunge hao wakati walishapeleka malalamiko yao kwa maandishi dhidi ya Naibu Spika, Dk Tulia Ackson.

“Kwani wanaharaka gani wao? Si walishapeleka malalamiko hayo na yapo kwenye kamati. Wasubiri uamuzi ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge),” alisema.

Kijana Awafungia Ndugu zake Ndani na Kisha Kuchoma Moto Nyumba Jijini Mwanza

$
0
0


Nyumba moja iliyopo mtaa wa Kiseke Wilayani Ilemela Mkoani Mwanza imeteketea kwa moto leo asubuhi na kuunguza vitu vingi huku wakazi wa nyumba hiyo wakinusurika. 

Taarifa zinaarifu kuwa,  nyumba hiyo imewaka moto baada ya mmoja wa watoto wa familia hiyo kuamka asubuhi na kumwaga mafuta ya taa katika moja ya chumba cha nyumba hiyo na kisha kuwasha moto 

Imeelezwa kuwa,  kijana huyo ambaye anadaiwa kuwa na matatizo ya akili amekuwa akiwatishia kwa muda mrefu kuwachoma moto lakini wamekuwa wakimpuuza kutokana na matatizo yake ya akili

Baada ya kumwaga mafuta  na kuwasha moto,  kijana huyo alitoweka na kuwafungia ndugu wengine ndani ambapo majirani walifanikiwa kuwahi kuwaokoa

Tamisemi Yakanusha Taarifa Kwenye Mitandao Ya Jamii Juu Ya Kusitisha Ajira Za Walimu Wapya 2015/2016

$
0
0

Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), imekanusha taarifa zilizosambaa katika mitandao ya kijamii kuwa imesitisha ajira za ualimu kwa mwaka wa fedha 2016/17.

Hivi karibuni taarifa hizo zilieleza kuwa  utafiti uliofanywa na Tamisemi umebaini kuwapo kwa ziada ya walimu 7,988 wa masomo ya sanaa na biashara hivyo haitaajiri walimu hao badala wataajiri wa masomo sayansi na hisabati.

Akizungumza na wanahabari  Katibu Mkuu wa Tamisemi, Mhandisi Mussa Iyombe amewataka wananchi kupuuza taarifa hizo kwani hazina ukweli wowote na zinalenga kugombanisha,kujenga chuki kati ya Serikali na walimu wa masomo hayo.

"Siyo kwamba ajira za walimu hakuna, ajira zipo. Ila wakati ukifika tutawangazia tunachosubiri sasa hivi suala la bajeti kuu liishe kwanza,"  amesema Mhandisi Iyombe.

Ajali Mbaya Yaua 6 na Kujeruhi 8, Same kilimanjaro

$
0
0
WATU sita wamefariki dunia na wengine nane wamejeruhiwa vibaya katika ajali iliyohusisha basi dogo la abiria aina ya Hiace lililokuwa likitokea Mjini Same kuelekea Njoro wilayani Same, ambapo liligongana na gari ya mizigo aina ya Fuso muda mfupi baada ya kuondoka katika kituo cha abiria cha Same Mjini.

Daktari aliyezungumza na chanzo cha habari hii katika Hospital ya Wilaya ya Same, Dkt Mlay, amesema wamepokea maiti sita ambazo amebainisha kuwa wanaume ni watano na mwanamke ni mmoja.

Aidha, ameongeza kuwa Majeruhi nane walipatikana kufuatia ajali hiyo, ambapo katika Majeruhi hao nane wanawake ni wawili na wanaume sita na kati yao waliopewa rufaa kuelekea Hospitali ya KCMC -Moshi ni watatu, wanaume wawili na mwanamke mmoja.

Majeruhi Noel Bakari Kanumba, aliyekuwa anatokea Mjini Same kwenda Kavambughu, akizungumza na Mwandishi  katika wodi ya Wanaume katika Hospitali ya Same, amesema alikuwa amekaa kwenye kiti cha mbele na dereva ambapo aligundua kuwa dereva yule alikuwa amelewa akamwonya asikimbize gari lakini hakutaka kumwelewa, ndipo gari lilimshinda na kuhama upande wake na kuelekea upande wa pili na kugonga Fuso upande wa dereva la Fuso hali iliyosababisha ajali ambapo dereva na abiria wake waliokuwa wamekaa kiti cha mbele walifariki dunia papo hapo.

Majeruhi wengine ni Musa Chikira (35), alikuwa anatokea Mjini Same kwenda Njoro na Mariam Omary Mbaga aliyekuwa katika wodi ya wanawake.
Majerhi wa ajali hiyo, Noel Bakari Kanumba (36), alikuwa anatokea Same Mjini akienda Kavambughu.
Majeruhi wa ajali hiyo, Musa Chikira (35), akiwa amelazwa katika wodi ya wanaume, hospital ya Wilaya ya Same.
Majeruhi wa ajali hiyo, Musa Chikira (35), akiwa amelazwa katika wodi ya wanaume, hospital ya Wilaya ya Same.

CHADEMA Waishitaki Serikali Mahakamani

$
0
0
MWENYEKITI wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, jana alifungua kesi ya madai katika Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, kupinga amri ya polisi kuzuia mikutano ya vyama vya siasa nchini.

Kesi hiyo namba 79 ya mwaka 2016, ilifunguliwa jana na kusimamiwa na mawakili watatu Gasper Mwanalyela, John Mallya na Paul Kipeja.
 
Licha ya kuwepo na ulinzi mkali wa jeshi la polisi uliowekwa katika barabara zote za kuelekea Mahakama Kuu, viongozi na wafuasi wa Chedema walifanikiwa kuvuka vizuizi hivyo.
 
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutoka mahakamani jana jioni, Mbowe alisema sababu za kufunguliwa kwa kesi hiyo ni baada ya kuona demokrasia ya vyama vingi "inabakwa nchini."
 
Mbowe alisema watu wanne waliotajwa katika kesi hiyo ya madai ni Kamanda wa Polisi wilayani Geita, Kamanda wa Polisi wilayani Kahama, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa polisi (Makao Makuu) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
 
Alisema wadaiwa hao wamefunguliwa kesi kutokana na kukiuka Sheria ya Vyama vya Siasa nchini, kwa kuchukua maamuzi ambayo hayaendani na demokrasia.
 
“Tunaiomba mahakama itangaze amri ya jeshi la polisi ya kuzuia mikutano ya vyama vya siasa ni batili, utekelezaji unaofanywa ni batili, polisi wapewe tangazo la kutowanyanyasa wapinzani na pia itoe amri ya vyama vya siasa kufanya mikutano yake na polisi wawe walinzi wa mikutano hiyo,” alisema Mbowe.
 
Alisema pamoja na polisi kuwabana hawataondoka jijini Mwanza, na wataongezeka zaidi mpaka kieleweke.
 
Alisema upo mkakati wa makusudi kuhakikisha Chadema inafutika katika mikoa ya Kanda ya Ziwa kutokana na baadhi ya viongozi wake kutekwa na kunyanyaswa na polisi.
 
Mkutano huo na waandishi wa habari ulihudhuriwa pia na Makamu Mwenyekiti Zanzibar, Saidi Issa Mohamed, Dk. Vincent Mashinji (Katibu Mkuu), Salum Mwalimu (Naibu Katibu Zanzibar), Halima Mdee (Mwenyekiti Bawacha) na Pastrobass Katambi (Mwenyekiti Bavicha) na baadhi ya wabunge wa chama hicho.
 
Kesi hiyo ya madai inatarajiwa kupangiwa Jaji Jumatatu ijayo.
 
Polisi ilisambaratisha mkutano wa Chadema uliokuwa ufanyike Kahama katikati ya wiki, ambapo mabomu ya machozi na magari ya 'washawasha' vilitumika kuondoa wafuasi wa chama hicho waliokuwa wasikilize hotuba za viongozi wa kitaifa.
 
Chadema imepanga kufanya mikutano nchi nzima kulaani inachodai uonevu unaofanywa dhidi ya wabunge wake Bungeni.

Majaliwa: Uhaba Wa Sukari Kumalizika Nchini.

$
0
0

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewahakikishia  Watanzania kwamba  Serikali inaendelea na jitihada za kuondoa tatizo la uhaba wa sukari nchini ambapo jumla ya tani 20,000 zilisambazwa jana katika maeneo mbalimbali nchini.
 
Amesema shehena nyingine ya tani 35,000  inatarajiwa kusambazwa hivi karibuni katika kanda zote nchini hivyo amewataka wafanyabiashara watakapoipokea kuiuza kwa wananchi bila ya kuificha na bei isizidi shilingi 2,200.
 
Waziri Mkuu Majaliwa ameyasema hayo jana jioni ( Ijumaa, Juni 10, 2016) wakati akizungumza na Masheikh na Viongozi wa Kamati ya Amani ya mkoa wa Dar es Salaam alipowaalika katika futari aliyoiandaa nyumbani kwake.
 
Amesema tayari viwanda vimeanza kufunguliwa na tani 300 zilizotoka katika kiwanda cha Sukari cha Kagera  zitasambazwa katika wilaya za Kakonko, Kibondo, Kasulu, Uvinza na Kigoma ili kutosheleza maeneo hayo.

Hata hivyo amewataka Maofisa Biashara katika Halmashauri zote nchini kuendelea kufanya ufuatiliaji katika maduka ili kuhakikisha bidhaa hiyo inapatikana na hakuna mfanyabiashara atakayeificha.
 
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu aliwataka wafanyabiashara kote nchini  kutopandisha bei za vyakula katika kipindi cha mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
 
Akizungumza kuhusu tabia za baadhi ya wafanyabiashara wanaopandisha bei za bidhaa hasa vyakula katika kipindi hiki cha mfungo amewataka kumuogopa Mwenyezi Mungu kwa sababu kitendo hicho kinawapa wafungaji wakati mgumu.
 
 “Kufunga Ramadhani si jambo la anasa, si matashi binafsi bali ni jambo  la kiimani hivyo tusipandishe bei ya bidhaa kwa lengo la kuwaadhibu Waislam kwa sababu tu wamefunga.
 
 “Katika Quran surat  Baqarah aya ya 183 inasema kwamba enyi mlioamin imefaradhishwa kwenu kufunga kama walivyoamrishwa kufunga kwa waliopita kabla  yenu ili muwe wachamungu, hivyo hatuna budi kufunga” alisisitiza.
 
Alisema tabia hiyo si nzuri na imekuwa ikijitokeza mara kwa mara unapofika wakati wa mfungo kwa wafanyabiashara kuamua kupandisha bei hivyo aliwataka waiache kwani Serikali haitawavumilia na atakayethubutu hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.

Serikali yatangaza utaratibu mpya maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, Pia yafafanua fedha zilizookolewa kutokana na watumishi hewa.

$
0
0

Na. Aron Msigwa – Dar es salaam.
SERIKALI imetangaza utaratibu mpya utakaofuatwa wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma kuanzia Juni 16 hadi 23, 2016 ambapo imewaagiza Watendaji Wakuu katika Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala na Taasisi za Serikali kutenga siku moja ya kukutana na watumishi katika sehemu zao za kazi kwa lengo la kusikiliza kero mbalimbali zinazowakabili na kuzitafutia ufumbuzi.

Aidha, imewaagiza watendaji hao kutenga siku nyingine moja kwa ajili ya kukutana na wananchi, kusikiliza na kuzitafutia ufumbuzi kero zao zinazohusiana na huduma zinazotolewa na Taasisi zao.

Akitangaza utaratibu huo leo jijini Dar es salaam Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Mhe. Angellah Kairuki amesema kuwa Serikali imeamua kubadili mfumo wa maadhimisho hayo kwa lengo la kuongeza ushiriki wa wananchi na watumishi wa umma katika maadhimisho hayo.

Ameongeza kuwa wakati wa maadhimisho hayo Watendaji hao watatakiwa kukutana wananchi na kusikiliza kero zinazohusiana na huduma zinazotolewa na taasisi zao pia kukutana na watumishi wa umma katika sehemu zao za kazi kusikiliza kwa lengo la kusikiliza kero zinazowakabili zikiwemo za upandishwaji wa vyeo, madai mbalimbali na taratibu mbalimbali kuhusu utumishi wa umma.

Amesema kuwa baada ya maadhimisho hayo kila Wizara, Mamlaka ya Serikali za Mitaa na Taasisi ya Umma itapaswa kuandaa taarifa jinsi ilivyotekeleza maagizo yaliyotolewa kwa kuiwasilisha Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma kabla ya Juni 30, 2016.

Ameeleza kuwa Tanzania inaungana na mataifa mengine ya Bara la Afrika kuadhimisha Wiki ya Utumishi wa Umma Barani Afrika  chini ya Kaulimbiu isemayo Uongozi wa Umma kwa Ukuaji Jumuishi:kuelekea katika Afrika tunayoitaka.

Mhe. Angellah amebainisha kuwa maadhimisho ya mwaka huu yatajikita katika kuangalia mchango wa Utumishi wa Umma katika ukuaji wa uchumi Barani Afrika, mchango wa Utumishi wa Umma katika kuiwezesha Ajenda ya Afrika ya 20163 ambayo inaweka mkazo katika maendeleo ya Afrika na Haki za Wanawake.

Amesisitiza kuwa malengo na mkakati wa Serikali ya awamu ya tano ni kufikia uchumi wa viwanda uliofungamanishwa na maendeleo ya watu, Tanzania ikiwa imejiwekea malengo ya kupiga hatua katika ukuaji wa uchumi kupitia maendeleo ya viwanda.

Amesema ili kufikia azma hiyo Serikali kupitia Utumishi wa Umma ina wajibu wa kuwawezesha wananchi kushiriki katika shughuli za uzalishaji ili kukuza uchumi huku watumishi wa umma wakitakiwa kufanya kazi kwa bidii, maarifa na weledi, kutoa huduma kwa wananchi wote kwa wakati pasipo urasimu wala ukiritimba pia kuepuka vitendo vya rushwa katika utekelezaji wa majukumu yao.

“Katika hili Watumishi wa umma lazima wawe na utendaji unaoweza kupimika, ili kulitekeleza hili kuanzia tarehe 1 Julai tutaanzisha dhana ya mfumo wa utendaji wa taasisi mbalimbali kwa lengo la kupima utendaji wa taasisi kulingana na matokeo tunayoyapata” Amesisitiza.

Ameongeza kuwa watumishi wa umma Serikalini wanatakiwa kuwa na utendaji unaojali matokeo, kuepuka vitendo vya wizi, ufisadi na udanganyifu vinavyosababisha upotevu wa fedha za Serikali.

Akizungumza kuhusu Haki za Wanawake katika utumishi wa umma amesema kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa  kuna uwiano wa jinsia katika nafasi na fursa mbalimbali katika ajira , Uteuzi wa nafasi za uongozi , mafunzo kazini na upandishwaji vyeo.

UFAFANUZI KUHUSU WATUMISHI HEWA.
Kuhusu suala la kuwaondoa Watumishi hewa katika orodha ya malipo ya Serikali  Mhe. Angellah amefafanua kuwa tayari Ofisi yake imekwishatoa maelekezo kwa Makatibu Wakuu, Wakuu wa Taasisi zote za Umma pamoja na Mamlaka za Serikali za Mitaa yanayowataka kuwasilisha taarifa ya mwisho ya watumishi hewa ifikapo Juni 15, 2016.

Amesema taarifa itakayowasilishwa itatakiwa kubainisha majina , namba za utambulisho wa watumishi hewa/ cheki namba, tarehe waliyotakiwa kuondolewa kwenye mfumo wa malipo na kiasi kilichopotea  na kile kilichookolewa ikiwa imesainiwa na Mkuu wa Wizara, Mamlaka ya Serikali za Mitaa na Taasisi husika.

Ameeleza kuwa mara baada ya kuzipokea taarifa hizo Serikali itazifanyia tathmini ili kupata uhakika wa zoezi zima la kuondoa watumishi hao kuanzia  tarehe 15 Machi 2016 siku ambayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli alitoa agizo.

“Kama mmekuwa mkifuatilia taarifa mbalimbali Serikali tumekuwa tukilishughulikia kwa nguvu suala hili la watumishi hewa kuanzia mwezi Machi mwaka huu  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli alipotoa agizo la kuwaondoa watumishi hewa katika orodha ya malipo ya Serikali” Ameeleza.

Amebainisha kuwa kuanzia Machi, 1, 2016 hadi Mei 30, 2016 watumishi 12,246 wameondolewa kwenye mfumo wa malipo ya mishahara kwa sababu mbalimbali zikiwemo za kutimiza umri wa kustaafu kwa lazima au kufukuzwa kazi ,vifo,kuhitimishwa kwa mikataba na ugonjwa.

Jumla ya shilingi 25,091,292,688.82 zingepotea kama watumishi hao wasingeondolewa kwenye mfumo wa malipo ikilinganishwa na watumishi 10,295 walioondolewa kwenye mfumo hadi Aprili 30, 201 huku kiasi kilichookolewa kikifikia shilingi 23,206,547,598.82 likiwa ni ongezeko la watumishi 1,951 na shilingi 1,884,745,090.

Serikali Haitamvumilia Kiongozi Yeyote Atakayedonoa Fedha Za Michango Ya Madawati- Majaliwa.

$
0
0

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itamchukua hatua kiongozi yeyote atakayedonoa fedha za michango ya madawati inayotolewa na wadau mbalimbali wa maendeleo.

Pia amewaagiza watendaji wote wa Serikali, Walimu Wakuu wa Shule za Msingi na Sekondari, Maofisa Elimu, Wakurugenzi wa Halmashauri, Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa, kuhakikisha michango hiyo inayotolewa inawafikia walengwa.

Aidha, amezitaka wilaya zote nchini zianzishe mpango endelevu wa kuhakikisha kwamba upungufu wa madawati unasahaulika kabisa katika maeneo yao na kwamba utendaji wa viongozi wa elimu na Serikali katika ngazi mbalimbali utapimwa kutokana na jinsi ambavyo wametekeleza maagizo hayo.

Waziri Mkuu Majaliwa ameyasema hayo leo (Jumamosi, Juni 11, 2016) wakati wa matembezi ya hisani ya kukusanya fedha za kununulia madawati kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Benki Kuu ya Tanzania (BOT).

Katika maadhimisho hayo yaliyoanzia BOT hadi viwanjja vya Mnazi Mmoja, Gavana wa BOT, Profesa Benno Ndulu alimkabidhi Waziri Mkuu hundi ya shilingi milioni 263 zilizochangwa na benki hiyo pamoja na watumishi wake kama mchango wao kwa ajili ya ununuzi wa madawati.

Waziri Mkuu aliwapongeza watumishi wa BOT kwa kushirikiana na Serikali katika kutatua changamoto hiyo ambapo alitoa wito kwa taasisi zote katika sekta ya umma na binafsi pamoja na watu binafsi kuchangia uboreshaji wa elimu nchini kama sehemu ya “Majukumu ya Taasisi kwa Jamii” (Corporate Social Responsibility).

Amesema kuwa na elimu bora, siyo tu faida kwa Taifa, bali kwa waajiri pia, kwani itahakikisha kwamba taasisi za umma na binafsi zinapata wafanyakazi ambao wameiva na wenye weledi wa kutekeleza majukumu mbalimbali ya uzalishaji katika taasisi hizo.

“Nitoe wito pia kwa wanafunzi wote ambao watafaidika na kuboreshwa kwa mazingira ya kusomea, ikiwemo kupewa madawati na mahitaji mengine, kuhakikisha wanasoma kwa bidii kwa faida yao na Taifa kwa ujumla na kwa kufanya hivyo, wanafunzi watakuwa wanaenzi jitihada za Serikali, taasisi za umma, taasisi binafsi na watu binafsi katika kuboresha elimu nchini,” amesema.

Amesema Serikali ya Awamu ya Tano imeazimia kupambana na changamoto za sekta ya elimu na kwamba tangu Uhuru, Serikali za Awamu zote zimekuwa zikifanya jitihada mbalimbali katika kuboresha elimu kwa wananchi wake.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU.

BoT imetoa Sh. Milioni 273 kuchangia ununuzi wa madawati nchini.

$
0
0
Hussein Makame-MAELEZO
Benki Kuu ya Tanzania (BOT) na wafanyakazi wake wa matawi yote nchini kwa kushirikana na baadhi ya Taasisi za kifedha na kampuni za simu nchini, imetoa Shilingi Milioni 273 kuchangia ununuzi wa madawati ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Miaka 50 ya Benki hiyo.

Fedha hizo zilikabidhiwa leo kupitia hundi ya mfano kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa baada ya matembezi ya hisani yaliyolenga kuchangia madawati, yaliyoanzia Ofisi za BOT hadi kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja  jijini Dar es Salaam.

Akizungumza kabla ya kukabidhi fedha hizo, Gavana wa BOT Prof. Benno Ndulu alisema lengo la mchango huo ni kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano katika kuongeza ubora wa elimu kupitia upatikanaji wa madawati kwa shule za msingi na sekondari nchini.

“Tunatambua kwamba changamoto hiyo (uhaba wa madawati) ni kubwa, lakini tunaamini mchango wetu utasaidia kupunguza makali ya tatizo hilo na kuongeza idadi ya watoto wetu ambao wanasoma wakiwa wamekaa kwenye madawati” alisema Gavana Prof. Ndulu

Akifafanua mchango huo, Gavana Prof. Ndulu alisema kati ya fedha hizo, BOT imetoa Shilingi Milioni 167, Wafanyakazi Milioni 29.8, Taasisi za Kifedha Milioni 22 na kampuni za simu Milioni 54.3 na kwamba madawati hayo yatasambazwa kwenye shule zenye upungufu au ukosefu wa madawati za Dar es Salaam na zilizoko mikoa ambayo Benki hiyo ina matawi yake.

Alitaja mikoa hiyo na fedha zilizochangwa na wafanyakazi wa BOT wa matawi ya mikoa hiyo kuwa ni Makao Makuu Dar es Salaam waliochangia Shilingi Milioni 22, Mwanza (Milioni 1.24), Chuo cha Benki Mwanza (680,000) Arusha (Milioni 1.23) Mbeya (Milioni 1.186), Mtwara (850,000) na Dodoma (Milioni 1.18).

Alisema taasisi zilizochangia fedha hizo ni Benki ya India Shilingi Milioni 5, Benki ya Habib (Milioni 5), Benki ya Exim (Milioni 5), Benki ya UBA (United Bank for Africa, Milioni 2), Tanzania Mortgage Refinance (Milioni 2), China Community Bank (Milioni 2) na NIC Bank aliyotoa Milioni 1.

Kwa upande wa kampuni za simu zilizotoa fedha ni kampuni ya Vodacom iliyotoa Dola za Kimarekani 10,000, kampuni ya Tigo Dola za Kimarekani 10,000 na kampuni ya Selcom iliyotoa Dola za Kimarekani 5,000.

Akizungumza baada ya kupokea hundi ya mfano, Waziri Mkuu Majaliwa alisisitiza fedha hizo zitumike kama zilivyokusudiwa na yeyote atakayetumia fedha hizo kinyume na malengo achukuliwe hatua mara moja.

Katika kuthamini sekta ya elimu nchini, Gavana Prof. Ndulu alisema benki hiyo ilianzisha Mfuko wa Udhamini wa Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere ambapo hadi sasa umetoa ufadhili kwa wanafunzi 22 kusoma shahada za kwanza na za uzamivu katika vyuo vikuu hapa nchini katika masomo ya sayansi, hisabati, uchumi, fedha, uhasibu na TEHAMA.

“Lengo kubwa la mfuko huu ni kuhamasisha wanafunzi wa kike kusoma masomo ya sayansi na hisabati yakiwemo masomo kuhusu gesi na mafuta.Katika idadi hiyo, 16 ni wanafunzi wa kike na waliobaki 8 ni wanaume” alisema Gavana Prof. Ndulu.

Benki Kuu ya Tanzania (BOT) ilianza kutoa huduma kwa wananchi mnamo tarehe 14 Juni mwaka 1966 na Juni 14 mwaka huu inatimiza Miaka 50 na katika kuadhimisha miaka hiyo wafanyakaz wa matawi yote nchini wanafanya matembezi hayo ili kutoa mchango kwa jamii.

Rais Magufuli Amteua Mwigulu Nchemba Kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Jumapili ya June 12

Wabunge Waionya Serikali

$
0
0

WABUNGE wameonesha wasiwasi kuhusu kupunguzwa kwa fungu la fedha katika Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali na kuonya kuwa huenda hatua hiyo ikampunguzia Rais John Magufuli kasi ya utumbuaji majipu, anayoifanya kwa wabadhirifu wa fedha za umma au kuua kabisa utaratibu huo.

Wabunge hao walionesha wasiwasi huo kwa nyakati tofauti bungeni mjini hapa Dodoma, wakati wakichangia hotuba ya Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2O16/17 inayoanza kutekelezwa Julai mosi, mwaka huu.

Miongoni mwa wabunge hao ni wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM), aliyeeleza kuwa, kupunguza fedha katika ofisi hiyo ni kumkwamisha Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya kazi yake kwa ufanisi na tija.

Kwa mujibu wake, kumkwamisha huko pia ni dalili ya kuukumbatia ufisadi kwa sababu ofisi hiyo ya CAG ndio inayofanya kazi ngumu na kubwa ya kuwafichua mafisadi nchini, hivyo inahitaji kujitosheleza kibajeti na kuepuka kuhitaji msaada kutoka kokote kwingine.

“Kitendo cha kuminya fungu la ofisi ya CAG kwa kupunguza kiasi cha fedha inachopewa kutoka shilingi bilioni 74 kwa mwaka wa fedha unaoisha hadi shilingi bilioni 44 kwa mwaka mpya wa fedha unaoanzia Julai Mosi, ni kuifanya ofisi hiyo ishindwe kuyabaini majipu (wabadhirifu, mafisadi),” Lugola alisema.

Wanafunzi 316 Waliofukuzwa Chuo Kikuu cha St. Joseph Wafungua Kesi Mahakamani

$
0
0

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imetoa kibali cha kufungua kesi ya uwakilishi, kwa wanafunzi wanne, waliofukuzwa katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph kwa madai ya kutokuwa na sifa za kudahiliwa kwenye vyuo vikuu.

Jaji Eliezer Feleshi alitoa kibali hicho baada ya wanafunzi hao kuwasilisha maombi ya kibali cha kuwakilisha wenzao mahakamani pamoja na kusitisha masomo wakati kesi ya msingi ikiendelea kusikilizwa.

Wanafunzi hao, walisimamishwa masomo baada ya kutolewa amri ya Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Joyce Ndalichako kwamba kutokana na tatizo la ufundishaji wa Stashahada ya Elimu (Sayansi, Hisabati na Teknolojia) wanafunzi wote wanatakiwa kurejea nyumbani.

Akiwasilisha maombi ya wanafunzi hao, Wakili Emmanuel Muga aliomba wanafunzi 316 waliofukuzwa chuo, wapewe kibali cha kufungua kesi ya uwakilishi pia Mahakama itoe amri ya kusitisha masomo wakati wa usikilizwaji wa kesi.

Akitoa uamuzi, Jaji Feleshi alisema Mahakama imekubali ombi hilo, isipokuwa la kusimamishwa masomo wanafunzi wote na kufafanua kuwa “masomo yataendelea kusimama kwa wanafunzi 316 waliosimamishwa”.

Aidha alisema wanafunzi hao wanatakiwa kuwa na wawakilishi wanne tu, badala ya 316, kwa sababu idadi yao ni kubwa. Baada ya uamuzi huo, Wakili Muga aliwataja wanafunzi wanne watakaowawakilisha wenzao mahakamani hapo kuwa ni Innocent Peter, Ramadhan Kipenya, Oswald Mwinuka na Faith Kyando.

Jaji Feleshi alisema Mahakama imetoa kibali na itapanga tarehe ya kusikilizwa kwa kesi baada ya walalamikaji hao kufungua kesi yao. 

Katika madai yao, wanafunzi hao wanadai fidia ya miaka mitatu waliyokaa chuoni hapo dhidi ya Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) iliyowakilishwa na Wakili Rose Lwita na Judith Misokia na Chuo cha Mtakatifu Joseph, kikiwakilishwa na wakili Jeromah Msemwa.

CHADEMA, CCM Watofautiana Kuhusu Naibu Spika, Dk Tulia Ackson

$
0
0
Wakati Halmashauri Kuu ya CCM mkoani Mbeya ikiutaka uongozi wa Bunge kuwachukulia hatua kali wabunge wa upinzani wanaosusia vikao vya Bunge, Chadema, Kanda ya Magharibi, imemtaka Naibu Spika, Dk Tulia Ackson kujitafakari upya kama anafaa kuendelea na nafasi hiyo.

Kwa nyakati tofauti, viongozi wa CCM na Chadema walitoa kauli hizo ikiwa ni siku ya 12 tangu wabunge wa upinzani kususia vikao vinavyoendesha na Dk Tulia.

CCM walisema kitendo kinachofanywa na Chadema kinachochea siasa za kibaguzi badala ya kufanya kazi ya kutunga sheria ya kusimamia Serikali kwa maslahi ya wananchi.

Katibu wa Siasa Itikadi na uenezi Mkoa wa Mbeya, Bashuru Madodi aliwaambia waandishi wa habari ofisini kwake kuwa kitendo kinachofanywa ni kinyume cha maadili na mwongozo wa nchi na kumpongeza Dk Tulia kwa msimamo wake wa kuliongoza Bunge bila kujali ubabaishaji wa wabunge wa upinzani.

“Kitendo cha wabunge kutoka nje wakati wa vikao na kupiga soga ni utovu wa nidhamu na kutoheshimu kiti cha spika na hivyo wajiulize bungeni walikwenda kwa maslahi ya wananchi au la? ”alihoji.

Madodi alisema pia halmashauri kuu inalaani vikali matamko yanayotolewa ya wabunge wa upinzani ya kuzunguka nchi nzima kufanya siasa za kuwahadaa wananchi kuwa wameonewa bila kutambua kuwa wao ni chanzo cha uvunjifu wa amani kwa kutozingatia na kufuata kanuni na taratibu za Bunge.

Kadhalika alisema ni vyema Bunge kufanya maamuzi ya kutowalipa posho wabunge watakaokuwa wakishindwa kuhudhuria vikao vyake.

“Uongozi wa Bunge usitetereke kwa vitendo vya ubabaishaji wa vyama vya upinzani na uendelee kuchukua hatua stahiki dhidi ya wabunge wanaoendelea na vitendo vya utovu wa nidhamu badala ya kuwasilisha kero za wananchi waliowachagua,” alisema.

Kaimu Katibu CCM Mkoa wa Mbeya, Lobe Zongo alipongeza jitihada zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli ya kurejesha nidhamu ya utendaji wa kazi serikalini hali itakayosaidia uchumi wa nchi kusonga mbele na kurejesha nidhamu.

 “Haya yote ni matunda ya Rais wa awamu ya tano kwa kweli anastahili pongezi kwa uwajibikaji na utendaji wa kazi kwa watendaji ndani ya chama na serikalini,” alisema.

Katibu wa Chadema Kanda ya Magharibi, General Kaduma alimlaumu Tulia akidai hana uchungu na wananchi kwa kuwa hakuchaguliwa kwa kupigiwa kura kama walivyokuwa manaibu waliomtangulia.

 Kaduma alidai Naibu spika huyo amevunja kanuni za Bunge na kuwadhalilisha wabunge wa upinzani kwa kushiriki kuondoa vipengele muhimu katika hotuba ya waziri kivuli wa mambo ya ndani, Godbles Lema.

Katibu huyo ambaye amechukua nafasi ya aliyekuwa Katibu wa Chadema Kanda hiyo, Christopher Nyamwanji, aliitaka Serikali kuingilia kati uamuzi uliotolewa na Kamati ya Maadili ya Bunge akidai hayakuwa sahihi.

“Mchango wa wabunge waliozuiliwa kuingia bungeni ni mkubwa katika Bunge hili la bajeti ila utakosekana kutokana na uamuzi uliochukuliwa na naibu spika ambao kimsingi unaminya demokrasia nchini,” alidai.

Pia, alikemea kitendo cha Jeshi la Polisi kuzuia mikutano na kutumia silaha za moto kutawanya umma akisema kinasababisha uvunjifu wa amani.

Amelitaka jeshi hilo kuacha kufanya kazi kwa maslahi ya CCM na badala yake wawe walinzi wa amani nchini kwa kufanya kazi bila upendeleo.

Mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Tabora, Francis Msuka alisema wajibu wa kufanya mikutano ya siasa nchini ni wa muda wote kabla na baada ya Uchaguzi Mkuu mwaka jana.

Alisema kumekuwa na matukio ya viongozi wa Chadema kunyanyaswa na Jeshi la Polisi huku viongozi wake ngazi ya vijiji wakifanyiwa mizengwe ili wasitimize majukumu yao kikamilifu.

Serikali Yatangaza Vita Dhidi ya Majambazi na Watu Wanaojihusisha na Mauaji

$
0
0
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuf Masauni ametangaza vita dhidi ya majambazi na watu wanaojihusha na mauaji.

Alisema Serikali imelazimika kutangaza vita hivyo baada ya kutokea matukio 41 yaliyohusisha mauaji ya kinyama tangu Januari hadi mwezi uliopita.

“Serikali ipo kazini, sasa inatangaza vita dhidi ya watu wanaojihusisha na ujambazi, watakaobainika hakika wataangamizwa hatuwezi kukubali watu wazidi kupoteza maisha pasipo na sababu za msingi,” alisema Masauni.

Waziri huyo alitembelea Msikiti wa Rahman Mtaa wa Utemini Kata ya Mkolani wilayani Nyamagana, Mwanza na kusema matukio hayo yanapaswa kutokomezwa na kukemewa kwa nguvu zote.

 “Mauaji hayo yalikuwa ya kutisha hivyo ilikuwa ni lazima watuhumiwa wakamatwe, hata hao waliokimbia wanapaswa kutiwa mbaroni,” alisema.

Pia, alionya tabia ya baadhi ya polisi kujihusha na vitendo vya uhalifu na kupoteza imani na uaminifu kwa wananchi.

 Aliwataka polisi wanaofanya vitendo hivyo kuacha na badala yake wapambane na wahalifu.

Masauni alisema nia ya Serikali ni kuhakikisha Watanzania wanaishi kwa utulivu, hivyo haitakubali watu wachache kuvuruga amani iliyopo

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella alisema vyombo vya usalama vipo imara kwani baadhi ya wahalifu wameuawa na wengine kukamatwa na wanaendelea kuhojiwa.

Mjumbe wa baraza la masheikh Wilaya ya Nyamagana, Saidi Darwesh alisema tukio la mauaji ya msikitini limesababisha hofu kwa waumini, hususan kipindi hiki cha mfungo wa Ramadhani kwani wengine hawaendi msikitini kuswali.

 Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Utemini, Jukael Kiula alisema wakazi wa Kata ya Mkolani wamejitolea kujenga kituo cha polisi katika mtaa huo ili kudhibiti uhalifu unaotokea mara kwa mara. 
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (wa pili kushoto) akimuuliza jambo Mkuu wa Jeshi la Polisi mkoani Mwanza, Ahmed Msangi (kushoto) wakati walipokuwa wanawasili msikiti wa Rahmani mkoani humo uliovamiwa na majambazi na kuua waumini watatu ndani ya msikini huo. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (wa pili kulia) akimsikiliza Mkuu wa Jeshi la Polisi mkoani Mwanza, Ahmed Msangi (kulia) wakati walipokuwa wanatoka msikitini mara baada ya kuzungumza na waumini wa msikiti huo wa Rahmani mkoani humo. Msikiti huo ulivamiwa na majambazi hivi karinbuni na watu watatu waliuawa. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Mzee wa Msikiti wa Rahmani uliopo Mkolani, jijini Mwanza, Abeid Gati (kushoto), akimpa fedha mke wa mmoja wa watu waliouawa na majambazi ndani ya msikiti huo. Fedha hizo zilitolewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (aliyevaa Kaunda suti) ikiwa ni rambirambi yake kwa wafiwa wote watatu ambao walipoteza wenza wao katika mauaji hayo.  Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (kushoto) akimpa pole askari Polisi, Mageni Kaseha aliyepigwa risasi ya mguu na majambazi wakati wa mapambano kati ya polisi na majamabazi hao katika mapango ya utemini, jijini Mwanza. Askari huyo amelazwa katika Zahanati ya Jeshi hilo iliyopo katika Kambi ya Mabatini, jijini humo. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Wapinzani Wataka Wabunge wa CCM Wasioongea Bungeni Nao Wanyimwe Posho

$
0
0

KAMBI Rasmi ya Upinzani Bungeni, imelitaka Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuwafutia posho wabunge wa CCM  wanaofika kwenye vikao vya Bunge hilo na kukaa kimya bila kuchangia jambo lolote hata kwa maandishi kwa maelezo kuwa hawafanyi kazi.

Msemaji Mkuu wa Kambi hiyo, ambaye ni Mbunge wa Momba, David Silinde (Chadema), alitoa pendekezo hilo jana bungeni mjini hapa muda mfupi kabla ya kuwasilisha maoni ya Kambi ya Rasmi ya Upinzani Bungeni, kuhusu hotuba ya Mapendekezo ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali katika mwaka wa Fedha 2016/17.

Hotuba hiyo ya Bajeti iliwasilishwa bungeni Juni 8, mwaka huu na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango. Silinde alisema; 

“Kabla ya kutoa maoni ya Kambi ya Upinzani, ninaomba niweke sawa taarifa zinazopotoshwa na kiti cha Naibu Spika kuhusu posho na kueleza kuwa sisi ndio kila wakati tumetaka posho ziondolewe na kupelekwa kwenye shughuli za maendeleo, lakini Serikali imekuwa ikisuasua kutekeleza jambo hilo.”

Kwa mujibu wa Silinde, suala kwao sio posho kwa sababu hata wakati wa Bunge la Katiba kila Mbunge wa upinzani aliacha Sh milioni 30. 

Akizungumzia wabunge wa CCM wakaa kimya, Silinde alisema wapo na wanapokea posho kama kawaida ilhali hakuna kazi yoyote wanayoifanya na kwamba umefika wakati sasa Bunge liongeze umakini zaidi kwa kuwadhibiti wabunge wa aina hiyo kwa kuwakata posho za vikao.

Alipendekeza kuwa Hansard (kitabu cha taarifa rasmi za Bunge) zitumike kuwabaini kwa sababu wapo na wanajulikana. 

Hata hivyo, kabla ya kueleza suala hili, Silinde alivunja utaratibu kwa kumtaja Naibu Spika kwa jina ‘Kiti cha Spika’ badala ya Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lililosababisha alazimishwe kutumia busara kuheshimu kiti hicho na hatimaye kutii.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana,Ajira na Wenye Ulemavu), Jenister Mhagama, ndiye aliyesimama kuomba mtoa hoja (Silinde), aheshimu utaratibu wa Bunge hilo.

Uongozi Mpya Wa Yanga Watangazwa Baada Ya Kura Zote Kuhesabiwa.......Mwenyekiti ni Yusuf Manji, Makamu wake ni Clement Sanga

$
0
0
Yusuf Manji ameshinda nafasi ya uenyekiti wa Yanga kiulaini kutokana na kutokuwa na mpinzani kwenye nafasi hiyo hivyo kupita bila kupingwa kwenye nafasi ambayo alikuwa akiitetea.

Clemen Sanga nae amepenya katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti kwa kumbwaga mpinzani wake Titus Osoro.

Shughuli pevu ilikuwa kwa wagombea nafasi ya ujumbe ambapo jumla ya wagombea 20 walikuwa wakiwania nafasi 8 za ujumbe.

Mwenyekiti
Yusuf Manji ameibuka mshindi wa nafasi ya uenyekiti akipenya bila kupingwa na kupata idadi ya kura 1468 zilizopigwa na wanachama, huku kura 2 pekee zikiwa zimeharibika.

Makamu Mwenyekiti
Clement Sanga amemgaragaza mpinzani wake baada ya kupata kura 1428 wakati mpinzani wake Titus Osoro akiambulia kura 80 pekee.

Wajumbe
Ayoub Nyenzi (889), Salim Mkemi (894), Bakar Malima (577), Godfrey Mheluka (430), David Ruhago (582), Lameck Nyambaya (655), Sylvester Haule (197), Pascal Laizer (178), Samwel Lukumay (818), Hashim Abdallah (727), George Manyama (249), Hussein Nyika (770), Siza Lyimo (1027), Beda Tindwa (452),Tobias Lingalangala (889), Athumani Kihamia (558), Mchafu Chakoma (69), Edgar W  Chibura (72), Ramadhani M. Kampira (182), Omary S. Amei (1069)

Kwa Matokeo hayo, uongozi mpya wa Yanga uliochaguliwa na wanachama unaundwa na Mwenyekiti Yusuf Manji, Makamu Mwenyekiti Clement Sanga huku wajumbe wakiwa ni Omary S. Amei, Siza Lyimo, Salim Mkemi, Tobias Lingalangala, Ayoub Nyenzi, Samwel Lukumay, Hussein Nyika na Hashim Abdallah

Maalim Seif ziarani Marekani......Anatarajiwa Kuieleza Jumuiya ya Kimataifa Kilichojiri Kwenye Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar

$
0
0
Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad amekwenda Marekani na kesho ataiambia jumuiya ya kimataifa, kilichojiri kwenye Uchaguzi Mkuu na kusababisha chama chake kususia uchaguzi wa marudio wa Rais wa Zanzibar ulioipa CCM ushindi. 

Mkutano huo umeandaliwa na Kituo cha Elimu ya Kimkakati na Kimataifa cha Marekani (CSIS) na utafanyika makao makuu ya taasisi hiyo yaliyoko Washington DC kuanzia saa 4:00 asubuhi. 

“Tumewambia Wazanzibari kuwa ni lazima tudai haki yao ya maamuzi ya kidemokrasia waliyoyafanya tarehe 25 Oktoba 2015 kupitia kura zao. 

"Tumewaambia tutadai haki yao ndani ya Zanzibar, ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na katika jumuiya ya kimataifa,” alisema Maalim wakati akiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam. 

Katika barua ya mwaliko iliyoandikwa na mkurugenzi wa CSIS, Jennifer Cooke, Maalim Seif atatoa mada kwenye mjadala uliopewa jina la “The Zanzibar Elections: Democracy Deferred (Chaguzi za Zanzibar: Demokrasia iliyocheleweshwa)”. 

Maalim atakuwa miongoni mwa watoa mada watatu. Wengine ni balozi wa zamani wa Marekani nchini Tanzania,Mark Green na naibu mkurugenzi wa kanda wa Kusini na Mashariki mwa Afrika wa Taasisi ya Taifa ya Kidemokrasia (NDI), Mercedeh Momeni.

“Tafadhali jiunge nasi katika kikao hiki, ambacho Bwana Hamad atachangia mtazamo wake kuhusu uchaguzi wa 2015 na ni jinsi gani Zanzibar na Tanzania zinaweza kutatua migogoro ya kikatiba na kisiasa yanayosababishwa (na mambo hayo),” inasema tovuti ya CSIS ikizungumzia mjadala huo wa kesho.

Maalim Seif alikuwa mgombea urais wa Zanzibar mwenye upinzani mkubwa kwa mgombea wa CCM, Dk Ali Mohamed Shein na ameshagombea urais kwenye chaguzi zote tangu siasa za ushindani zirejeshwe mwaka 1992.

Mara zote amekuwa akilalamikia kuchezewa rafu na mwaka jana mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC), Jecha Salim Jecha alitangaza kufuta matokeo ya urais, wawakilishi na madiwani kwa maelezo kuwa sheria na kanuni za uchaguzi zilikiukwa.

Jecha alifanya uamuzi huo Oktoba 28, siku ambayo alitakiwa atangaza mshindi wa kiti cha urais baada ya matokeo ya majimbo 31 kuwa yameshatangazwa na mengine tisa yaliyosalia kuwa yameshahakikiwa.

Kabla ya kutangaza uamuzi huo, hakuonekana Oktoba 27 na siku iliyofuata alitangaza kufuta matokeo akiwa studio za kituo cha televisheni cha Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC).

Katika uchaguzi wa marudio uliofanyika Machi 20, CUF haikushiriki na imeshatangaza kutoitambua Serikali ya Dk Shein.

Maalim Seif aliondoka juzi jioni akiwa ameambatana na mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa CUF, Ismail Jussa Ladhu, na katibu wake, Issa Kheir Hussein. 

Kadhalika taarifa kutoka CSIS zinasema mkutano huo utashirikisha viongozi mashuhuri duniani, wakiwamo wa viongozi wa Ivory Coast na Sierra Leone.

NDI imeeleza kuwa wamemwalika Rais Alessane Watarra wa Siera Leone ili kutoa ushuhuda wa namna demokrasia ilivyoporwa katika nchi yake kabla vyombo vya kimataifa na umma kutumika na kuwaondoa madarakani viongozi waliokuwa madarakani.

Mkutano huo unafanyika wakati ambao wakuu wa NDI wamemwandikia Rais Barack Obama wa Marekani wakimlaumu kwa kuacha mambo yaendelee kama yalivyo nchini Tanzania.

Barua kwenda kwa Obama inasema Rais huyo wa taifa kubwa duniani ameshindwa kusimamia demokrasia barani Afrika, kutofanya maamuzi ya haraka dhidi ya kile kilichojiri Tanzania katika uchaguzi wa mwaka 2015.

“Tanzania imepoteza sifa yake ya kuwa kipimo cha demokrasia na utawala bora miongoni mwa Nchi za Afrika Mashariki na Kati,” inasema barua hiyo ya NDI iliyoandikwa na Cooke.

“Vipi uhusiano wa Marekani uendelee wakati tunajua Tanzania ilipoteza sifa yake ya kutekeleza demokrasia? Na vipi tuweke mazingira ya kusaidia sehemu ambayo demokrasia imeporwa na maamuzi ya watu wa Zanzibar hayakuheshimiwa?”
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live




Latest Images

<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>
<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596344.js" async> </script>