Quantcast
Channel: MPEKUZI
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live

Kamati ya Bunge yashindwa kujadili Deni la taifa

$
0
0

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imeshindwa kujadili Deni la Taifa na kuagiza kukutana na idara na taasisi sita, zinazohusika na deni hilo.

Uamuzi huo wa kamati ulifikiwa jana jijini Dar es Salaam wakati Kamati hiyo ilipokutana na Wizara ya Fedha na Mipango, kujadili taarifa yao ya fedha kwa mafungu tofauti.

Idara na taasisi hizo ni Idara ya fedha za Nje, Idara ya Sera na Uchambuzi, Ofisi ya Mhasibu Mkuu wa Serikali, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Tume ya Mipango na Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Akitoa uamuzi huo, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Aeshi Hillary, alisema kamati hiyo haiwezi kujadili na Wizara ya Fedha, Deni la Taifa kama ambavyo linaonesha katika kifungu kinachotakiwa kujadiliwa, kwa sababu, wizara hiyo inaelekezwa kulipa tu.

“Tumeshindwa kujadili Deni la Taifa na Wizara ya Fedha leo (jana), hawa wanapokea maelezo ya kulipa tu, hawajui vyanzo vya madeni vimetokea wapi, sasa tumeona tukutane kwanza na hizo idara na taasisi husika watuambie chanzo na deni likoje,” alisema Hillary.

Alisema idara hizo na taasisi zitaandikiwa barua ili wanapokutana na kamati waje na maelezo yanayojitosheleza kuhusu deni hilo la taifa ili baada ya kamati kuhoji na kuelewa, ndipo wakutane na wizara kuendelea na mjadala.

Awali wakati kamati hiyo ikijadili na wizara hiyo kuhusu ripoti yake ya hesabu, wajumbe wa kamati hiyo walihoji kero ya wastaafu ya kucheleweshewa malipo yao ya pensheni na mirathi.

Akichangia mjadala huo, Mjumbe wa kamati hiyo, Mbunge wa Viti Maalumu, Munde Abdallah alihoji ucheleweshaji wa malipo kwa wastaafu kutoka Hazina na kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii.

Alisema wastaafu wengi wakiwemo walimu wamekuwa wakisumbuliwa kupeleka barua za ajira na hati za malipo ya mshahara kwa mwezi, jambo ambalo ni kero na wakati mwingine wastaafu hao huwa wamepoteza kumbukumbu hizo kwa kuwa ni za muda mrefu, jambo ambalo linawafanya wacheleweshewe stahiki zao.

Akijibu hoja hizo na nyingine, Mhasibu Mkuu wa Serikali, Francis Mwakapalila aliomba radhi kwa wastaafu wote ambao wamekuwa wakisumbuliwa kupeleka vielelezo hivyo na kusisitiza kwamba ni wajibu wa mwajiri kuwa na vielelezo vya watumishi wake.

Mwakapalila alisema hivi sasa utaratibu unaotumika kwa wastaafu wanaolipwa na Hazina hauna usumbufu na kwamba mirathi na pensheni zinazolipwa na Hazina huenda moja kwa moja kwenye akaunti za wahusika na hazipitii tena Hazina Ndogo.

Zitto Kabwe Ahojiwa TAKUKURU

$
0
0

Siku tatu baada ya kuibuka kwa kashfa ya rushwa miongoni mwa wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imemuita Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe kumhoji.

Muda mfupi baada ya taarifa za kashfa hiyo kuwa wazi, Zitto na mwenzake wa Nzega Mjini, Hussein Bashe ambao ni wajumbe wa Kamati ya Huduma za Jamii, walimuandikia barua Spika wa Bunge, Job Ndugai kujiondoa kwenye nafasi zao ili kupisha uchunguzi dhidi ya tuhuma hizo.

Zitto alithibitisha kupata wito kutoka makao makuu ya Takukuru ili kuhojiwa juu ya sakata hilo na akapongeza kuwa endapo vyombo vya Serikali vitakuwa makini kushughulikia tuhuma zote zinazoelekezwa kwa wanasiasa na watumishi wengine wa umma, itasaidia kuongeza uwajibikaji na kupunguza uzushi kwa wananchi.

“Nimepata wito huo kupitia Ofisi ya Bunge. Nasikia Bashe ameitwa pia. Nafurahi wito wetu wa uchunguzi umechukuliwa kwa uzito unaostahili na tutatoa ushirikiano wote kwa vyombo vya uchunguzi ili kumaliza zoezi hili kwa haraka na kwa ufanisi,” alisema Zitto.

Alipotafutwa Bashe ili kupata ukweli wa kuitwa kwake, ingawa hakutimiza ahadi yake, alisema:“Sipo kwenye nafasi nzuri ya kuzungumza hivi sasa.”

Mpaka jana, wakati Takukuru ikiendelea kuwahoji wanasiasa na watendaji wa mashirika yaliyotajwa kuhusika kutoa rushwa ili kubadili maoni ya wajumbe juu ya utendaji wao, wabunge wawili walithibitika kuitwa na Takukuru.

Tuhuma hizo zimekwenda sambamba na Ndugai kuwaondoa wenyeviti wa kamati za Ardhi, Maliasili na Utalii; Nishati Madini; Uwekezaji na Mitaji ya Umma huku ile ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na Huduma na Maendeleo ya Jamii lakini akisema ni uhamisho wa kawaida

 Mkurugenzi Mkuu wa Taakukuru, Valentino Mlowola, bila  kuingilia uchunguzi unaoendelea alithibitisha kuwaita wabunge hao na watendaji wa mashirika  waliohojiwa.

“Hili ni suala la uchunguzi Bado linaendelea hivyo si wakati muafaka kutaja watu waliohojiwa mpaka sasa ingawa mahojiano yanaendelea. Kazi ikikamilika utapata taarifa kamili,” alissema Mlowola.

Nimepata wito kwenda makao makuu ya TAKUKURU kupitia Ofisi ya Bunge. Nasikia na ndg. Bashe, mbunge wa Nzega Mjini...
Posted by Zitto Kabwe on Thursday, March 24, 2016

Polisi Arusha Yamnusuru Na Kipigo Meneja Wa Kiwanda Cha Best Pack .

$
0
0

Jeshi la polisi mkoani Arusha jana lilifanikiwa kumnusuru meneja wa kiwanda cha kutengeneza bidha za plastiki  cha Best Pack kilichopo jijini Arusha,Vijay Kumar raia wa India baada ya kunusurika kupigwa na baadhi ya wafanyakazi wa kiwanda hicho.

Katika tukio hilo meneja huyo alifanikiwa kujifungia katika mojawapo ya ofisi kabla ya kuokolewa na polisi ambao walimfikisha katika kituo kikuu cha polisi cha kati na kumhifadhi kabla ya kumwachia kwa sababu za kiusalama

Tukio hilo lilitokea jana katika ofisi za kiwanda hicho zilizopo eneo la Kwa Idd nje kidogo ya jiji la Arusha ambapo wafanyakazi wa kiwanda hicho waligoma kufanya kazi wakipinga kitendo cha kampuni hiyo kutoa tangazo la kusitisha mikataba yao ya ajira kinyume na sheria.

Mbali na madai hayo baadhi ya wafanyakazi wa kiwanda hicho walilalamikia hatua ya kutoplipwa  mishahara yao ya mwezi Machi pamoja na mafao mbalimbali  kama malipo ya muda wa saa za ziada pamoja na kiiunua mgongo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wafanyakazi wa kiwanda hicho walidai kwamba uongozi wa kiwanda hicho juzi ulibandika tangazo la kusitisha mikataba yao ya ajira katika lango kuu la kuingia kiwandani hapo kinyume na sheria jambo lililowastua.

Catherine Samwel na Babaa Kibori ambao ni watumishi wa kiwanda hicho walisema kwa nyakati tofauti kwamba mnamo machi 17 mwaka huu walifanya kikao na uongozi kujadili malipo yao mbalimbali baada ya uongozi wa kiwanda hicho kutaka kukifunga lakini kikao hicho hakikumaliza kwa suluhu.

Walisema kwamba juzi majira ya asubuhi wakati wanaingia kazini walikuta tangazo likiwataarifu kwamba mikataba yao ya ajira imesitishwa bila taratibu na kanuni jambo lililowapelekea kuvamia ofisi ya meneja huyo wakitaka majibu ya uhakika.

Hatahivyo,wakati wakivamia ofisi ya meneja huyo alijitahidi kukwepa na kisha kujifungia katika mojawapo ya ofisi kiwandani hapo ambapo baada ya muda polisi walifika na kumchomoa kabla ya kumfikisha mbele ya mikono ya jeshi hilo kwa sababu za kiusalama.

Akihojiwa na mtanda huu meneja huyo alisema kwamba uongozi wa kiwanda chao tayari umeshaandaa taratibu za malipo ya mishahara na mafao mbalimbali kwa watumisho hao na watakwenda kuwalipa watumishi hao wiki hii.

Meneja huyo alifafanua kwamba wameamua kusitisha  mikataba ya ajira kwa watumishi hao kutokana na kampuni hiyo kutozalisha kwa faida lakini watazingatia taratibu zote za kusitisha mikataba hiyo.

Watumishi hewa 169 wagundulika Kigoma.....Mkuu wa Mkoa awataka wakurugenzi kubainisha kiasi walicholipwa mwaka mzima.

$
0
0

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Brigedia Jenerali Emanuel Maganga amewataka wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wote waliopo katika halmashauri zote kutaja kiasi cha fedha kilichotumika kuwalipa mishahara watumishi hewa 169 kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Akiongea na waandishi wa habari, Brigedia Jenerali Emanuel Maganga alisema kuwa agizo hilo ni kufuatia agizo la Mheshimwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli la kufanya uhakiki wa watumishi katika halmashauri zote ili kuwabaini watumishi hewa wanaolipwa mishahara kinyume na utaratibu za utumishi.

Alisema katika hao watumishi hewa 169 waliowabainika wapo ambao walishafukuzwa kazi, wapo ambao wameshafariki na wengine hawana sifa za kuwa watumishi wa umma.

Mhe. Maganga alisema kuwa suala la kuwa na wafanyakazi hewa ni wizi ambao hauwezi kuvumilika na wizi wa kuibia wanyonge hauwezi kuvumilika.

"Hakuna anayeweza kuvumilia wizi wa waziwazi kiasi hiki unaofanywa na baadhi ya watumishi wasiowaaminifu, wale wote watakaobainika wajiandae kwani hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao"Alisema Maganga.

Alisema kuwa fedha walizokuwa wakilipwa watumishi hao hewa kwaajili ya mishahara zinatakiwa kurudi zote, pia wakurugenzi wawafute watumishi hao hewa kwenye orodha ya malipo.

Mkuu huyo wa Mkoa alisema kuwa sasa hivi katika serekali hii ya awamu ya tano hakuna kufanya kazi kwa mazoea.

Alizitaja halmashauri zenye watumishi hewa kuwa ni halmashauri ya kasulu watumishi 78,halmashauri ya Kigoma 23,Manispaa ya Kigoma Ujiji 29,halmashauri ya Buhigwe 11,Uvinza 19,kibondo 5,ofisi ya Mkuu wa Mkoa 4 na halmashauri ya Kakonko hakuna mtumishi hewa.

Tanzania Yatoa Ufafanuzi Kuhusu Waziri wa Nishati Wa Kenya Kuzuiwa Kuingia Bandari ya Tanga

$
0
0

Waziri wa Nishati wa Kenya, Cherles Keter, na ujumbe wake amezuiwa kuingia katika bandari ya Tanga.

Kutokana na hatua hiyo, serikali mkoani Tanga imetoa ufafanuzi kuhusu kuzuiwa kwa waziri huyo na ujumbe wake wa watu 13 kuwa kulitokana na kutokuwa na taarifa za ujio wao.

Keter na maofisa wake wandamizi wakiwamo makatibu wakuu, walijipenyeza wakati wa ziara ya Waziri wa Nishati na Madini wa Uganda, Irene Muloni.

Ujumbe wa waziri huyo aliyeongozana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati ya nchi hiyo, Joseph Njoroge na mwenzake wa masuiala ya petroli, Andrew Kamau.

Vigogo hao, waliokuwa wameongozana na maofisa mbalimbali akiwamo Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mradi wa Usafirishaji wa Mafuta kutoka Lamu- Sudan Kusini- Ethiopia (Lappset), Sylvester Kasuku, walizuiwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Tanga, baada ya kuwasili.

Muloni na ujumbe wake, alitokea Kenya baada ya kukagua Bandari za Lamu na Mombasa na aliingia nchini kukagua Bandari ya Tanga, ikiwa hatua ya mchakato wa ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta kutoka Ziwa Albert, Uganda hadi Bahari ya Hindi.

Akizungumza hatua hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Tanga, ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa, Martin Shigella, alisema ujumbe wa Keter ulizuiwa kutokana na kutokuwa na taarifa nao na kwamba walikuwa katika viwanja vya ndege kwa ajili ya kungoja ugeni wa Waziri Muloni tu.

Shigella alisema kuwa walishangazwa kuona ujumbe huo wa Kenya umekuja kufuatana na waziri huyo bila kuwapo kwa taarifa yeyote ya awali ya ujio wao.

Keter na maofisa wake waliwasili katika uwanja wa ndege wa Tanga sambamba na ujumbe wa Waziri wa Uganda, ambao wote kwa pamoja waliwasili kwa helikopta nne, zilizotua kwa pamoja uwanjani hapo.

Baada ya kuhojiwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na baada ya Waziri Muloni kumaliza ukaguzi wa Bandari ya Tanga na maeneo ambayo yametengwa kwa ajili ya ujenzi wa bomba la mafuta, iwapo mradi huo utaridhiwa kutekelezwa na serikali ya Uganda, ujumbe huo uliruhusiwa kuondoka.

Hata hivyo, serikali ya Uganda ilieleza kuridhika kwake baada ya kuona hali halisi ya mazingira ya Bandari ya Tanga ikiwa hatua mojawapo ya mchakato wa awali wa ukaguzi kabla ya kupitishwa makubaliano ya ujenzi wa mradi huo.

Kutokana na hatua hiyo, serikali hiyo inatarajia kutuma timu ya watalaamu kutoka Uganda ili kufanya ukaguzi wa kina kwenye Bandari ya Tanga, kubaini uwapo wa vigezo vinavyotakiwa katika utekelezaji wa mradi.

Mabadiliko Ya Ratiba Shughuli Za Kamati Za Bunge

$
0
0
TAARIFA KWA UMMA
Kufuatia mabadiliko ya tarehe ya kupokea Mapendekezo ya Mpango na kiwango cha Ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017, Ofisi ya Bunge imefanya mabadiliko ya tarehe za shughuli za Kamati za Bunge kuelekea Mkutano wa tatu wa Bunge (Mkutano wa Bajeti) ili kuendana na masharti ya Kanuni za Bunge kuhusu shughuli hizo. 

Kwa mabadiliko hayo , ratiba ya shughuli za Kamati itakuwa kama ifuatavyo:-
  1. Tarehe 29/3/2016 hadi tarehe 4/4/2016 Kamati za Kudumu za Kisekta zitatembelea na kukagua utekelezaji wa miradi iliyotengewa Fedha kwa Mwaka wa Fedha 2015/2016 kwa mujibu wa Kanuni ya 98(1) ya Kanuni za Bunge. Hapo awali kazi hii ilipangwa kufanyika tarehe 31/3/2016 hadi 6/4/2016.
  2. Tarehe 5/4/2016 – Kwa mujibu wa Kanuni ya 96 ya Kanuni za Bunge, Serikali itawasilisha Dondoo na Randama za Vitabu vya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017. Awali kazi hii ilipangwa kufanyika tarehe 29/3/2016;
  3. Tarehe 6/4/2016 – Kwa mujibu wa Kanuni ya 97(1)-(2) ya Kanuni za Bunge kutakuwa na Mkutano wa Wabunge wote ambapo Serikali itawasilisha Mapendekezo ya Mpango na kiwango cha ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017. Awali kazi hii ilipangwa kufanyika tarehe 30/3/2016;
  4. Tarehe 7/4/2016 hadi 15/4/2016 – Kwa mujibu wa Kanuni ya 98 (2) ya Kanuni za Bunge, kwa kipindi cha siku tisa (9) Kamati za Kudumu za Kisekta zitachambua taarifa za utekelezaji wa Bajeti za Wizara zinazosimamiwa na Kamati hizo. Katika kipindi hicho, Kamati ya Bajeti itafanya uchambuzi wa Mapendekezo ya Mpango na kiwango cha ukomo wa Bajeti kwa Mwaka wa fedha 2016/2017. Awali Kamati ya Bajeti ingefanya kazi hii kuanzia tarehe 31/3/2016 hadi 6/4/2016;
  5. Tarehe 15/4/2016 – Kwa mujibu wa Kanuni ya 98(3) ya Kanuni za Bunge kutakuwa na Kikao cha pamoja kati ya Kamati ya Uongozi na Kamati ya Bajeti ili kujadili mambo muhimu yaliyojitokeza kwenye Kamati za Kisekta wakati wa kujadili utekelezaji wa Bajeti za Wizara mbalimbali;
  6. Tarehe 16 na 17 Aprili, 2016 kama ilivyokuwa imepangwa awali Wabunge wataelekea Dodoma tayari kwa Shughuli za Mkutano wa Tatu wa Bunge ambao utaanza tarehe 19 Aprili, 2016.

Imetolewa na:
Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano Ofisi ya Bunge
DAR ES SALAAM
25 Machi, 2016.

Zaidi wa Watu 150 Watii Agizo La Mkuu wa Mkoa Wa Dar la Kuhakiki Upya Silaha Zao

$
0
0

Mkurugenzi  wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Kamishna wa Polisi Diwani Athumani amesema hadi kufikia sasa zaidi ya watu 150  wamejitokeza  kuhakiki wa  silaha zao, katika hatua ya  kutii agizo la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul  Makonda.
 
“Baada ya Mheshimiwa Rais John Pombe  Magufuli  kufanya uhakiki wa silaha zake  hivi karibuni, watu zaidi ya 150 wakiwemo viongozi mbalimbali waliopo Serikalini, Viongozi wastaafu, Mabalozi wa nchi mbalimbali, wafanyabiashara na  wabunge wamejitokeza  kuhakiki  silaha zao, na wengine wameonesha nia ya kufanya hivyo,  hata hivyo tusingependa kutaja majina yao kwa sababu za kiusalama” amesema Kamishna wa Polisi Athumani
 
Athumani amesema kuwa, lengo la kufanya uhakiki wa silaha ni pamoja na kuboresha hali ya usalama na kuwajua watumiaji, kuwatambua tena wamiliki wa silaha pamoja na kuwa wanawatambua isipokuwa  zinaweza kutokea sababu mbalimbali zitakazofanya wasiendelee kumiliki silaha hizo ikiwemo vifo na ulemavu na  kusema kuwa  wangependa kufahamu taarifa za namna hiyo, ameongeza kuwa  zoezi hili sasa ni la nchi nzima si kwa Mkoa wa Dar es Salaam pekee kama ilivyokuwa hapo awali.
 
Aidha, wakazi wa  mkoa wa Dar es Salaam wanaweza  kuhakiki silaha zao katika vituo vya  Osterbay Polisi, Temeke Chang’ombe Polisi na Ilala central Polisi, ambapo wanatakiwa kwenda na  kitabu(firearm  licence book), picha ndogo nne za mhusika,  pamoja na  anwani sahihi ya mahali anapoishi mhusika.
 
Vilevile, amewataka viongozi mbalimbali na wananchi wanaomiliki silaha kujitokeza kwa ajili ya kufanya uhakiki wa silaha zao huku akisisitiza kwa wakazi wa Mkoa wa Dar es salaam, wanaweza kuonana na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es salaam, Simon Sirro na kwa wakazi wa Mikoani waonanae na makamanda wa polisi wa Mikoa yao kwa ajili ya kupewa msaada na maelekezo zaidi ya taratibu  za kufuata ili waweze kufanya uhakiki wa  silaha zao.

Zubeir Ali Maulid Achaguliwa Na CCM Kugombea nafasi ya Spika wa Baraza la Wawakilishi

$
0
0

WAJUMBE wa Baraza la Wawakilishi watokanao na Chama Cha Mapinduzi Zanzibar leo wamefanya Uchaguzi wa kumpata mjumbe atakaye peperusha bendera ya CCM katika kinyang’anyiro cha nafasi ya Spika wa Baraza hilo, kwa kipindi cha mwaka 2015 - 2020.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC wa Idara ya Itikadi na Uenezi Mhe. Waride Bakari Jabu, amesema uchaguzi huo ulioendeshwa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Mhe. Balozi Seif Ali Iddi, ulifanyika Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui, Mjini Unguja.

Mwenyekiti wa Uchaguzi huo, uliojumuisha wajumbe 72, alimtangaza Zubeir Ali Maulid kuwa mshindi baada ya kupata kura 55 na kuwashinda wapinzani wake wawili aliyemaliza muda wake Pandu Ameir Kificho aliyepata kura 11 na Jaji Janeth Nora Sekihola aliyepata 4, na kura mbili (2) ziliharibika.

Jumla ya wanachama tisa (9) walijitokeza kuomba ridhaa ya CCM ili wagombee nafasi hiyo ya Spika .

Katika kikao cha Kamati Maalum kilichofanyika Machi 24, mwaka huu, Ofisi Kuu ya CCM Zanzibar, ilipitisha majina matatu ikiwa ni pamoja na Pandu Ameir, Zubeir Ali Maulid na Janeth Nora Sekihola, ambapo uchaguzi wake umefanyika leo.

Akitoa neno la shukrani, Zubeir Ali Maulid, aliwashukuru wajumbe hao kwa imani yao kwake na kuwataka wampe kila aina ya mashirikiano ili aweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

Naye aliyekuwa Spika wa Baraza hilo Pandu Ameir Kificho, amekubali kushindwa na kumuahidi kumpa msaada wowote atakaohitaji, iwapo atatakiwa kufanya hivyo.

Uchaguzi huo wa Spika unatarajiwa kufanyika mara tu baada ya kuitishwa kwa Baraza jipya la Wawakilishi.

KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI.

Sgd
…………….
(Waride B. Jabu),
Mkuu wa Idara ya Itikadi na Uenezi - CCM,
ZANZIBAR.
25/03/2016.

Rais Magufuli Ahudhuria Ibada Ya Ijumaa Kuu Leo Jijini Dar Es Salaam

$
0
0
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akijiandaa kuubusu Msalaba wakati wa Ibada ya Ijumaa kuu katika Kanisa la Mtakatifu Petro Oysterbay jijini Dar es salaam leo Ijumaa April 25, 2016

Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli akibusu Msalaba wakati wa Ibada ya Ijumaa kuu katika Kanisa la Mtakatifu Petro Oysterbay jijini Dar es salaam leo Ijumaa April 25, 2016
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akisalimiana na watu wenye ulemavu baada ya  Ibada ya Ijumaa kuu katika Kanisa la Mtakatifu Petro Oysterbay jijini Dar es salaam leo Ijumaa April 25, 2016. Picha na IKULU
Mke wa Waziri Mkuu Mama Mary Majaliwa akibusu Msalaba wakati wa Ibada ya Ijumaa kuu katika Kanisa la Mtakatifu Petro Oysterbay jijini Dar es salaam leo Ijumaa April 25, 2016

Mutfi Wa Tanzania Amuombea Dua Mkuu Wa Mkoa Wa Dar Es Salaam, Paul Makonda

$
0
0
MUFTI wa Tanzania Sheikh Abubakary Zubery amemuombea dua, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na Rais Dk. John Magufuli ili waweze kulitumikia vema taifa na kuliletea maendeleo.

Zubery alimfanyia dua hiyo Makonda Dar es Salaam leo asubuhi alipofika nyumbani kwake kujitambulisha na kumjulia hali pamoja na kumueleza mambo kadhaa ya maendeleo yaliyofanyika.

"Tunakuomba mola wetu kuwapa moyo wa imani na uzalendo na kuwaepusha na mabaya yote  Mkuu wetu wa Mkoa Paul Makonda, Rais wetu Magufuli pamoja na viongozi wote ili waliongoze taifa letu kwa amani" alisema Mufti Zubery"  wakati akiomba dua hiyo.

Makonda akizungumza na Mufti Zubery nyumbani kwake Mikocheni alimwambia kuwa kuna mambo kadhaa ameyafanya kwa kushirikiana na watendaji wenzake kwa kukutana na waendesha boda boda ili kuwawezesha kupata mkopo utakaowasaidia kupata vitendelea kazi zao kama kupata kofia ngumu mbili za kuvaa dereva na abiria wake ili kuwasaidia katika shughuli zao za kusafirisha abiria.
 
Makonda alitaja mambo mengine kuwa ni suala zima la kupambana na uhalifu ambao bado unaonesha kupamba moto hasa ujambazi wa kutumia silaha za moto.
 
Alitaja mambo mengine kuwa ni mkutano alioufanya hivi karibuni wa kukutana na wenyeviti wa mitaa na maofisa watendaji ili kuzungumzia suala la utunzaji wa mazingira na mambo mengine ambapo alisema ameandaa mpango wa kumzawadia mwenyekiti atakayefanya vizuri kwenye mtaa wake.
 
Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi Musa Salum alisema jambo alilofanya Makonda la kumtembea Mufti ni jambo zuri na kuwa kumuona mufti ni sawa kama amewaona waislam wote nchini.
 
Alisema wanamuombea Makonda mungu amzidishie wepesi katika kazi zake kwani ni viongozi wachache wanaopata madaraka ambao uwakumbuka viongozi wa dini kama alivyofanya Makonda.
 
Katika hatua nyingine Makonda alifanya ukaguzi wa barabara kadhaa za Manispaa ya Kinondoni ambazo hivi karibuni aliagiza zifanyiwe marekebisho ikiwa ni pamoja na kuchimba mifereji baada ya kuharibika kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.
 Mufti Zubery, akifanya mazungumzo na Makonda.
Dua ikiendelea nyumbani kwa mufti Mikocheni. Wapiga picha kutoka vyombo vya habari mbalimbali wakichukua taarifa hiyo.
Makonda akiagana na Sheikh Abubakar Khalid na Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum.

Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Jumamosi ya March 26

Anne Kilango Malecela Akomaa na Watumishi Hewa

$
0
0

MKUU wa Mkoa wa Shinyanga, Anne Kilango Malecela ametoa siku sita kwa Wakurugenzi wa Halmashauri tatu za Ushetu, Msalala na Kahama zilizopo wilayani Kahama kuhakikisha wanawakilisha kwake majina ya watumishi hewa ifikapo Jumatano ijayo.

Mkuu huyo wa Mkoa aliyasema hayo wakati akizungumza na watumishi wa halmashuri zote tatu za Wilaya ya Kahama muda mfupi baada ya kumaliza ziara yake ya siku moja ya kukagua shughuli za maendeleo wilayani Kahama, ikiwa ni sambamba na kuwapa pole waathirika wa mvua kubwa ya mawe katika kijiji na Kata ya Mwakata.

Mvua hiyo ya mwanzoni mwa Machi mwaka jana ilisababisha maafa makubwa, ikiwa ni pamoja na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 38 na kujeruhi wengine zaidi ya 80.

Kilango alisema lundo la watumishi hewa katika halmashauri hizo halikubaliki, hivyo ni wajibu wa wakurugenzi kuhakikisha kuwa majina yao yanawakilishwa ofisi ya mkuu wa mkoa sambamba na maelezo ya kumbukumbu zao za ajira, wanavyolipwa na kiasi wanacholipwa.

“Hata wakurugenzi wakiwaficha, tayari orodha yao ninayo mezani…naomba mniletee majina,” alisema mkuu huyo wa mkoa aliyeanza kazi hivi karibuni baada ya kuteuliwa na Rais John Magufuli.

Katika Awamu iliyopita ya utawala wa Rais Jakaya Kikwete, Anne Kilango alikuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi. 

Pia aliwataka viongozi wa halmashauri hizo kuhakikisha wanaongeza kasi ya kukusanya mapato, ikiwa ni sambamba na kuongeza weledi ili mapato hayo yasipotee.

“Maendeleo ya Kahama yanatuhusu wote. Sipendi kumsimamisha mtu kazi kwa tuhuma za ubadhirifu, lakini ikibidi kufanya hivyo nitafanya kulingana na kasi ya uongozi wa Serikali ya Awamu Tano chini ya uongozi wa Rais John Magufuli,” alisema.

Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Wilaya ya Maswa (MAUWASA) Mbaroni Kwa Ufisadi ya Milioni 108

$
0
0

MKURUGENZI Mtendaji wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Wilaya ya Maswa (MAUWASA) mkoa wa Simiyu, Lema Jeremiah (50) amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Maswa akikabiliwa na makosa ya wizi wa Sh milioni 108 mali ya serikali.

Mwendesha Mashitaka wa Polisi, Nassib Swedy alidai mbele ya Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Tumaini Marwa kuwa mshitakiwa anatuhumiwa kufanya wizi wa fedha akiwa mtumishi wa Umma.

Swedy alidai Machi 7 mwaka 2014 saa 3:00 asubuhi, Jeremiah akiwa katika Ofisi za Mamlaka hiyo zilizoko katika kijiji cha Sola wilayani humo aliiba Sh milioni 108 zikiwa ni mali ya Serikali zilizotolewa na Mwajiri wake ambaye ni Wizara ya Maji na Umwagiliaji.

Alisema kosa hilo ni kinyume na Kifungu cha 270 cha kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2002.

Hata hivyo, mara baada ya kusomewa shitaka hilo mshitakiwa huyo alipoulizwa na hakimu Marwa kuhusika nalo, alikana kosa hilo na mwendesha mashitaka kudai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ili waendelee na upelelezi na kesi hiyo itatajwa tena Aprili 11 mwaka huu.

Hakimu Marwa alisema masharti ya dhamana kwa mshitakiwa anatakiwa awe na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya Sh milioni 50 au hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh milioni 50 na hati hiyo itatakiwa ikaguliwe kama kweli inafikia kiasi hicho.

Mshitakiwa amekidhi vigezo hivyo na kuachiwa kwa dhamana, lakini alipotoka mahakamani akashikiliwa na Maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa madai kuwa anahitajika  kwa mahojiano zaidi kutokana na tuhuma nyingine zinazomkabili.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Adai Yeye Ndo Mwanzilishi wa Wazo la Kuhakiki Silaha Kabla ya Paul Makonda wa Dar

$
0
0

MKUU wa Mkoa wa Arusha, Felix Ntibenda amesema kazi ya kuhakiki silaha iliyoanza kwa wakazi wa Dar es Salaam, ilishaanza mkoani mwake takribani miezi miwili iliyopita na kwamba ndiyo maana matukio ya kihalifu kwa Arusha yamepungua.

Ntibenda alisema hayo jana katika kikao cha Baraza la Ushauri la Mkoa wa Arusha na kusema yeye ndiye mwanzilishi wa wazo la kilichoazishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda hivi karibuni.

Alisema wakati wakisubiri kuapishwa katika viwanja vya Ikulu, Dar es Salaam aliwaeleza wakuu wa mikoa jinsi alivyofanikiwa kudhibiti uhalifu kwa kuwataka wakazi wa Jiji na mkoa wa Arusha kuhakiki silaha zao.

‘’Kazi inayofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ni wazo langu kwani sisi Arusha si mnaona uhalifu umepungua kwa asilimia kubwa sana? Hiyo ni kwa sababu wengi wana silaha, lakini si mali zao,’’ alisema.

Akizungumzia ulinzi, Ntibenda alisema hiyo inatokana na jitihada za kamati ya ulinzi na usalama kuthibiti kwa kiasi kikubwa uhalifu na matukio yasiyokuwa na amani na sasa Jiji la Arusha liko katika hali ya utulivu wa hali ya juu.
Alisema katika kipindi cha Januari mwaka jana hadi Desemba mwaka jana, jumla ya magunia 270 ya bangi yenye uzito wa kilo 2,500 na ekari 25 za mashamba ya bangi yaliteketezwa kwa kuchomwa moto.

Mkuu huyo alisema operesheni hiyo ilifanyika katika vijiji vya Imbibya, Ngarelaoni, Kisimiri Juu na Oldonyosambu na watuhumiwa 180 walikamatwa na kesi 160 zilifikishwa mahakamani.

Akizungumzia zuio la kutocheza `Pool’ saa za kazi, Ntibenda alisema wakuu wa wilaya na wakurugenzi ni lazima washiriki kikamilifu kupiga vita mchezo huo kuchezwa wakati wa kazi kwani ni jukumu la kila mmoja hapa na sio la mtu mmoja mmoja.

Polisi Amtandika Risasi Dereva wa Daladala Baada ya Kupishana Kauli

$
0
0

Polisi mmoja anadaiwa kumpiga risasi dereva daladala, Pistus Ngowi baada ya kutofautiana kauli.

Tukio hilo lililotokea juzi saa tatu usiku, Kariakoo jijini Dar es Sallam  lilisababisha madereva wenzake wanaofanya wote safari za Tandika pamoja na wa Temeke kugoma kwa zaidi ya saa tano wakidai kwamba licha ya kushambuliwa, amebambikiwa kesi katika Kituo cha Polisi cha Msimbazi.

Ilidaiwa kuwa wakiwa katika Mtaa wa Lindi kilipo kituo cha daladala hizo, polisi huyo aliyetajwa kwa jina moja la Dotto akiwa kwenye doria, walitofautiana na dereva huyo kisha kumtolea bastola na kumpiga nayo mkononi.

Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu Dar es Salaam, Simon Sirro alisema jana kuwa awali, alipewa taarifa za askari wake kushambuliwa akiwa doria na alimpiga risasi dereva huyo kujitetea.

“Huyu askari yupo mahabusu anahojiwa na polisi ili kubaini chanzo cha tukio hili,”alisema Kamanda Sirro.

Dereva wa daladala aliyeshuhudia tukio hilo, Mateso Elias alidai kuwa walikuwa madereva 15, waliokuwa wakisubiri abiria ghafla walisikia kelele za Dotto akimfokea dereva huyo akidai kuwa alitaka kumgonga alipokuwa akiwasili kituoni hapo.

Alisema ili kuepusha shari, Ngowi alishuka kwenye basi na kumuomba msamaha akiwa amepiga magoti lakini polisi huyo alikataa kumsamehe.

Alisema kitendo hicho kiliwavuta madereva waliokuwapo hapo ambao walisogea eneo hilo kujua kilichokuwa kinaendelea: “Ghafla alitoa bastola na kutuamuru wote tuondoke. Tulipopiga hatua kama hatua tano, alifyatua risasi na kumpiga Ngowi mkononi na nyingine alipiga hewani.”

Alisema baada ya tukio hilo aliwapigia simu askari wenzake ambao walifika na kumpeleka katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Askari Aporwa Bunduki Aina ya SMG na Majambazi

$
0
0

Watu saba wanaosadikiwa kuwa majambazi wakiwa na silaha mbalimbali za jadi, wamempora bunduki aina ya SMG askari polisi PC Shadrack.

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Dodoma, David Mnyambuga alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 2.36 usiku katika ofisi za Kampuni ya Simu za Mkononi ya Halotel, eneo la Medeli.

“Majambazi wapatao saba wakiwa na mapanga na nondo walifika katika ofisi hizo baada ya kutoboa ukuta na kumjeruhi askari kwa mapanga na nondo na kupora silaha aina ya SMG,” alisema.

Kamanda huyo alisema polisi walifanya msako mkali usiku huo na kufanikiwa kuipata silaha hiyo eneo la Mbuyuni.

“Mtu mmoja amekamatwa kuhusiana na tukio hilo na anaendelea kuhojiwa,” alisema.

Waliokula mishahara HEWA Singida kusherehekea siku ya Wajinga Rumande

$
0
0

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mathew Mtigumwe ameagiza mamlaka zinazohusika kuwakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria watu watakaobainika kutafuna fedha za mishahara hewa kabla ya mwezi huu kumalizika.

Mkuu huyo wa mkoa alitoa agizo hilo juzi kwenye kikao cha kufahamiana kilichohudhuriwa na wakuu wa wilaya, wakuu wa idara ya sekretarieti ya mkoa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa ofisini kwake.

Katika hotuba yake fupi na ambayo haikuwa na mbwembwe za kisiasa, alisema uhakiki uliofanyika hivi karibuni mkoani humo ulibainika kuwa na wafanyakazi hewa wengi, jambo linaloonyesha kuwapo kwa ubadhirifu wa kiwango cha juu cha fedha za umma.

“Naagiza kila mmoja wenu akaangalie kwenye taasisi yake iwapo wafanyakazi wanaolipwa mishahara ndiyo hao waliopo kazini au la. Kuna madai wastaafu, waliohama na hata watumishi waliokufa mishahara yao bado inalipwa hadi hivi leo,”alisema.

“Iwapo itagundulika kuwa kuna watu walioshiriki katika ulaji huo wa fedha za umma, wakamatwe mara moja ifikapo Aprili Mosi, mwaka huu na kufikishwa kunakohusika haraka iwezekanavyo ili sheria ichukue mkondo wake.”

Mtigumwe aliwakumbusha viongozi hao umuhimu wa watumishi walio chini yao kufanya kazi kwa uadilifu na kujiepusha na vitendo vya rushwa.

“Haiwezekani mtu atoke kijijini kisha arudi bila kuhudumiwa, lazima kuwahi kazini na kukaa hadi mwisho wa saa za kazi,” alisema.

Pia, alisisitiza umuhimu wa kila taasisi ya Serikali mkoani humo kufungua kitabu cha kero za wananchi na kuhakikisha zinaorodheshwa na kuonyesha hatua halisi iliyofikiwa katika kuzishughulikia.

Maalim Seif Sharif Hamadi Arejea Zanzibar Baada ya Kukaa Mapumzikoni Serena Hoteli Kwa Siku 17

$
0
0

Siku chache baada ya Rais wa Zanzibar Dr Ali Mohamed Shein kuapishwa baada ya kushinda uchaguzi wa marudio uliosusiwa na baadhi ya vyama vya upinzani, Katibu mkuu wa chama cha wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, amerejea Zanzibar.

Maalim Seif ambaye alikuwa mapumzikoni katika hoteli ya Serena iliyopo jijini Dar es Salaam kwa takribani siku 17, jana alirejea Zanzibar kuendelea na mapumziko yake.

Maalim Seif alilazwa katika Hospitali ya Hindu Mandal ya jijini Dar es Salaam,mara baada ya kuruhusiwa March 8 mwaka huu alishauriwa na Daktari wake kupata mapumziko ya muda mrefu.

Kurejea kwa Maalim Seif visiwani humo kunazidisha shauku na kiu ya baadhi ya Wazanzibar kutaka kusikia atakachokisema kiongozi huyo wa upinzani mwenye ushawishi mkubwa kwenye jamii.

Maalim Seif aliugua wakati Wazanzibar wakiwa katika maandalizi ya kurudia uchaguzi mkuu uliofanyika March 20, mwaka huu baada ya kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi uliofanyika Oktoba 25  mwaka  jana na mwenyekiti wa tume ya uchaguzi ya Zanzibar( ZEC), Jecha Salim Jecha kwa madai kuwa uligubikwa na dosari nyingi.

Gharama za Hotelini
Taarifa zilizoripotiwa kwenye vyombo vya habari siku chache zilizopita zilidai kuwa kila siku aliyokaa kwenye hoteli hiyo, Maalim Seif alikuwa akitumia wastani wa Sh. 6,162,500.

Kutokana  na  takwimu hizo, hadi kufikia jana, Maalim Seif atakuwa ametumia kiasi kisichopungua sh. Milioni 92.4

Chumba alichokuwa akilala Maalim Seif katika Hoteli hiyo yenye hadhi ya nyota tano kinalipiwa dola za Marekani 2,500 kwa usiku mmoja.

Maalim Seif alikuwa akiishi hotelini hapo na wasaidizi wake watano, ambao wote gharama zao zinalipwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ)

Sakata la Tumbili 61 Waliokamatwa Uwanja wa Ndege Lachukua sura Mpya

$
0
0

Serikali imeunda kikosi kazi kinachohusisha taasisi nyeti nchini kuchunguza sakata la kukamatwa kwa raia wawili wa Uholanzi wakiwa katika harakati za kusafirisha tumbili 61 kwenda nchini Albania.

Kikosi hicho kinaundwa na maofisa kutoka ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Usalama wa Taifa, Jeshi la Polisi, Uhamiaji na Kikosi cha Kupambana na Ujangili.

Kamanda wa Polisi Mkoa Kilimanjaro, Wilbroad Mutafungwa aliwathibitishia wanahabari jana kuundwa kwa kikosi kazi hicho na kwamba, upelelezi wa sakata hilo umepamba moto.

“Upelelezi ndiyo kwanza bado mbichi, kwa hiyo siwezi kusema lolote kama lini watuhumiwa watafikishwa mahakamani kwa sababu upelelezi uko chini ya kikosi kazi hicho,” alisema Mutafungwa.

Juzi saa tano asubuhi, Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, alitembelea Kituo cha Polisi cha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia) kushuhudia wanyama hao.

Profesa Maghembe alisema kama kila kitu kitakwenda vizuri katika upelelezi, watuhumiwa wa kosa hilo watafikishwa mahakamani siku ya Jumanne.

Wanyama hao walikamatwa usiku wa kuamkia juzi katika uwanja huo wakati raia hao, Artem Alik Vardanyian (52) na Eduard Alik Vardanyian (44) wakiwa katika harakati za kuwasafirisha kwa kutumia ndege kubwa ya mizigo.

Hata hivyo, raia hao wa Uholanzi walikuwa na vibali vilivyotolewa na Mkurugenzi wa Matumizi Endelevu ya Wanyamapori, Charles Mulokozi ambaye tayari amesimamishwa kazi kwa kashfa hiyo.

Wanajeshi 8 wa JWTZ Watiwa Mbaroni Wakituhumiwa Kumuua Raia Waliyedai Kawaibia Simu Yao

$
0
0

Askari nane wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), wanashikiliwa na Polisi Mkoa wa Kigona wakituhumiwa kwa mauaji ya Erick Nilamewa (16) waliyemtuhumu kuwaibia simu moja aina ya Techno na Sh. 6,000.

Tukio hilo lilitokea juzi jioni Mtaa wa Mabatini Mwanga Manispaa ya Kigoma/Ujiji.

Wanajeshi hao wakiwa nane, walionekana wakimpiga Nilamewa kwa mateke, fimbo na kumchoma na pasi tumboni, kifuani na mgongoni, baada ya kumkamata wakimtuhumu kwa wizi huo.

Mwili wa kijana huyo umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya Mkoa Maweni.

Aidha, Ahamad Mussa, mkazi wa Mabatini eneo la Mwanga Manispaa ya Kigoma/Ujiji, amelazwa wodi namba 7 katika hospitali ya Mkoa Maweni kwa matibabu, kutokana na purukushani hiyo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma Ferdinard Mtui, alithibitisha kukamatwa kwa askari hao nane wa JWTZ  kwa tuhuma za mauaji ya  kijana huyo na kumjeruhi Mussa (16).

Mtui alisema “Ni kweli tunawashikilia wanajeshi nane na tunaendelea na upelelezi, na baada ya uchunguzi tutawapeleka mahakamani ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.”

Akizungumza  kutoka kitandani alikolazwa, Mussa ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Kitwe, alitumiwa ujumbe wa simu na wanajeshi hao akiwa shuleni ambao walisema kwamba wanamhitaji.

“Baada ya kutumiwa ujumbe huo mimi nilimbipu, akanipigia na kujitambulisha kuwa yeye ni afande Aberi, akasema njoo mara moja nakuhitaji," alisema Mussa.

"Kwa sababu tunakaa mtaa mmoja, pia huwa naingiaga kwenye makazi yao wanaponituma vitu mbalimbali kama sigara, sikuwa na wasiwasi wowote kuhusu wito huo.”

Alisema alipofika alibisha hodi na walimwitikia na kumwambia akae uani ndipo baada ya muda alitoka Aberi akiwa amevaa kaptura ambaye alianza kuita wenzake ambao walianza kumsulubu.

“Nilimsikia akiwaita wenzake wakina afande Mayowa, Ally na wengine nimesahau majina yao lakini jumla walikuwa wanajeshi nane ambao walikuwa wakinipiga.

"Waliniambia ninyooshe miguu yangu juu ya ukuta na niliponyoosha walinipiga na ubao na fimbo ya mianzi kichwani… damu zilianza kutoka.

"Wakachukua maji wakasafisha, wakapiga tena kichwa nikaanguka chini kisha wakanipiga mateke na kunichapa na nyaya za umeme huku wakiuliza ilipo simu na Sh 6,000 nilizoiba,” alisema Mussa.

Alisema wakati hali ikizidi kuwa mbaya, "walichukua chupa ya pombe na kunimiminia" kabla ya kujitokeza mwanamke mmoja wa nyumba ya jirani anayefahamika kwa jina la mama Hoza ambaye aliwaambia wamwache "mtoto wa watu maana watamuua bure.
 
“Mimi sijaiba simu wala siku ya leo (jana) sijafika kambini hapo.

"Sijaiba wao wakaendelea kunipiga na kunimwagia maji na kunigalagaza kwenye mchanga wakati huo damu zinaendelea kuvuja kichwani, ndipo mimi nikawambia naomba niende nyumbani nikamwambie mama yangu na tulienda na mwanajeshi mmoja na tulipofika nyumbani tulimkuta mama yangu.

"Mwanajeshi huyo akasimama nje mimi nikaingia ndani nikapita uani na kukimbia na ndiyo ikawa pona yangu la sivyo na mimi ningefariki dunia.”

Alisema baada ya yeye kukimbilia ndipo walipomkamata Erick mtaani na kumpeleka kwenye makazi yao ambako walimpiga na kumtesa hadi walipoona hali yake kuwa mbaya, walikwenda polisi kuchukua fomu namba 3 (PF3)kwa ajili ya kumpeleka hospitali ya Maweni kwa matibabu, lakini alifariki dunia.

Mama mzazi wa majeruhi huyo, Mwaisala Ahamad (36) alisema wanajeshi walimuagiza mtoto mmoja kwenda nyumbani kwake kwamba wanamuitaji mtoto wake na aliwaambia kuwa ameende shuleni.

“Waliniomba namba ya simu ya mtoto wangu nikawapatia kwasabababu wanajeshi hawa walikuwa na mazoea na mwanangu," alisema Mwaisala.

"Nilipowapa nilienda kwenye shughuli zangu kama kawaida sikuwa na wasiwasi wowote, hawa tunawajua.

"Wengine wana nyota moja (luteni nusu) na wengine mbili (luteni) na wengine tatu (kepteni) na kutokana na vyeo walivyokuwa navyo sikutarajia mtoto wangu yamkute yaliyomkuta.”

Aliongeza kuwa kama askari hao walihisi kuwa mtoto wake ndiye aliyeiba simu yao walipaswa kumkamata na kumpeleka kituo cha polisi.

Kwa upande wake, Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mshumbusi Edmond alithibitisha kumpokea marehemu Nilamewa akiwa na majerahe kifuani, tumboni na mgongo lakini akafariki muda mfupi baada ya kufikishwa hospitalini hapo.

Mwili wake uko chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya Mkoa Maweni, alisema.

Viewing all 45270 articles
Browse latest View live




Latest Images