Quantcast
Channel: MPEKUZI
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live

Wadaiwa Sugu Bodi ya Mikopo Kitanzini......CAG Apewa Jukumu La Kuwasaka Popote Walipo,Kutoajiriwa Sio Kigezo Cha Kukwepa Deni

$
0
0

BODI ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) imetoa onyo kwa wadaiwa sugu ambao hawajajitokeza kuanza kulipa madeni yao, kwamba hatua mbalimbali dhidi yao zinatafuata kokote waliko.

Miongoni mwa hatua hizo, bodi hiyo imetaja kuwa ni kuwatoza wadaiwa hao sugu riba ya asilimia kumi katika deni lao na kutumia taarifa zao kuwazuia kufanya safari za nje ya nchi.

Taarifa ya hivi karibuni ya bodi hiyo , imeeleza kuwa wadaiwa hao wa tangu mwaka wa masomo wa 1994/95, wataanza kusakwa kupitia Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ambaye anawajibika kukagua mali zote za Serikali.

Mbali na CAG, ambaye ana mkono mrefu wa kuwasaka katika ofisi zote za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma, Serikali za Mitaa na katika miradi ambayo Serikali ina ubia na sekta binafsi, pia kampuni binafsi za ukaguzi wa hesabu, zenye mkono mrefu katika sekta binafsi, zitatumika kuwasaka katika kampuni binafsi na asasi za kiraia.

“Jukumu la CAG na kampuni zingine binafsi za ukaguzi wa mahesabu, ni kulazimisha waajiri kuwasilisha taarifa za wafanyakazi wao ambao ni wahitimu wa elimu ya juu na makato ya mkopo waliopewa,” imeeleza taarifa hiyo.

Taarifa hiyo imefanya marejeo ya Sheria ya Bodi namba 9 ya 2004 na marekebisho yake, inayomtaka kila mwajiri kutoa maelezo kwa maandishi kwa bodi, kuhusu mwajiriwa ambaye ni mnufaika wa mkopo huo, ndani ya siku 28 tangu mdaiwa alipoajiriwa.

Hatua
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mdaiwa yeyote wa bodi hiyo atakayeshindwa kulipa deni lake bila sababu za msingi, kwanza atakuwa akikabiliwa na kesi ya madai chini ya kifungu cha 6 C na H cha Sheria ya Bodi ya Mikopo namba 9 ya mwaka 2004.

Mbali na kukabiliwa na kesi hiyo, pia mkopo wake kwa namna unavyochelewa kuanza kulipwa, utakuwa ukijilimbikizia riba ya asilimia 10.

Taarifa hiyo ya bodi imeeleza kuwa mdaiwa huyo taarifa zake zitapelekwa katika taasisi za kumbukumbu ya mikopo zilizo chini ya Benki Kuu (BoT), ambazo zitazuia wadaiwa hao kupata mikopo katika mabenki na asasi zote za fedha.

Mdaiwa huyo pia atazuiwa kupata udhamini wa Serikali katika muendelezo wa masomo yake, lakini pia atazuiwa kujiunga na chuo chochote cha elimu ya juu ndani na nje ya nchi.

Aidha kwa mujibu wa taarifa hiyo, taarifa zao pia zitawasilishwa katika Idara ya Uhamiaji iliyo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na katika ofisi zote za kibalozi, ili wakose kibali cha kusafiri nje ya nchi.

Hasara nyingine watakayokabiliwa nayo wadaiwa hao, ni Tozo ya Kulinda Thamani ya Mkopo (VRF) ya asilimia sita kila mwaka, itakayotozwa kwa kila mkopo, ili wadaiwa watakapoanza kulipa mkopo waliochukua, walipe kwa thamani ya sasa.

Tozo hiyo imelenga kuepuka athari ya mfumuko wa bei tangu mdaiwa aliponufaika, lakini pia kuwezesha urejeshwaji wa deni, uwe na thamani ya kumhudumia mwanafunzi mwingine mwenye mahitaji kwa sasa na baadaye.

Ambao hawajaajiriwa
Taarifa hiyo pia imeonya wadaiwa wanaodhani kuwa kutokuajiriwa ni sababu ya kutolipa mkopo huo, kwamba mkopo huo unatakiwa kulipwa baada ya kumalizika kwa mwaka mmoja tangu mdaiwa alipofanikiwa kuhitimu masomo yake, au mwaka mmoja tangu mhusika alipokatisha masomo yake kwa sababu yoyote.

Aidha, taarifa hiyo imeelekeza watakaojitokeza, kama wameajiriwa, asilimia nane ya mshahara wao wa kila mwezi, itatakiwa kukatwa na kuwasilishwa kwenye Bodi ili kulipa deni husika.

Lakini pia Bodi hiyo imetengeneza utaratibu kwa ambao hawajaajiriwa, kwamba wanaweza kulipa kiasi cha chini cha Sh laki moja kila mwezi katika akaunti za Bodi zilizopo Benki ya Posta yenye namba CCA0240000032; Benki ya NMB namba 2011100205 na Benki ya CRDB namba 01J1028467503.

Deni lenyewe
Kwa mujibu wa Ripoti ya CAG, hadi Juni 2014, bodi hiyo ilikuwa imewakopesha wanafunzi Sh trilioni 1.8 kuanzia mwaka wa masomo 1994/95 na kati ya fedha hizo, Sh bilioni 51 zilitolewa na iliyokuwa Wizara ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia.

Taarifa hiyo ya HESLB imetolewa siku chache kabla ya Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako  kusitisha ajira ya Mkurugenzi Mtendaji wa bodi hiyo, George Nyatega kwa tuhuma za udhaifu katika fedha za mikopo zaidi ya Sh bilioni 3.2.


Wata Watatu Watiwa Mbaroni Kwa Kuvamia Kituo Cha Polisi Na Kuvunja Mlango Ili Kuwatoa Wenzao

$
0
0

Watu watatu wamekamatwa na polisi mkoani Morogoro kwa tuhuma za kuvamia Kituo cha Polisi cha Duthumi na kuvunja mlango kwa lengo la kuwatoa wenzao watatu wanaotuhumiwa kwa wizi wa mifugo.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Graifton Mushi alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea juzi saa 12.40 jioni.

Alisema polisi walilazimika kutumia silaha za moto na mabomu ya machozi kuwatawanya watu hao.

Mushi alitaja silaha hizo kuwa ni mapanga, shoka na marungu. Hata hivyo, alisema wakati watu hao wanavamia kituo hicho watuhumiwa hao walishaondolewa kituoni hapo na kupelekwa katika Kituo Kikuu cha Polisi Kati. Alisema watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani mara baada ya uchunguzi kukamilika.

Katika tukio jingine; watu zaidi ya 20 wa Kitongoji cha Mazizini Kijiji cha Maseye Wilaya ya Morogoro wamevamia eneo la mwekezaji Ayubu Mngimbwa na kuteketeza vibanda vilivyokuwa na vifaa mbalimbali vya uchimbaji wa madini na kumshambulia kwa vipigo.

Kaimu Kamanda huyo alisema thamani ya vibanda na vifaa vilivyoteketezwa bado haijafahamika.

Alisema chanzo cha tukio hilo ni mgogoro kati ya wananchi wa kitongoji hicho na mwekezaji anayedaiwa kutiririsha maji yenye kemikali za sumu.

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Jumapili ya Februari 21

Bandari ya Tanga Yaamriwa Kurejesha Mita za Kupimia Mafuta

$
0
0
Serikali imetoa wiki moja kwa Mamlaka ya Usimamisi wa Bandari(TPA) mkoa wa Tanga kuhakikisha inarejesha tena matumizi ya mita ya kupimia mafuta (Flow Meters), kabla ya shehena ya meli ya mafuta kutia nanga bandarini hapo.

Hatua hiyo ya serikali inafuatia uamuzi wa TPA kuacha ufungaji wa mita hizo uliofanywa zaidi ya miaka mitano iliyopita ambapo kwa kipindi chote hicho serikali ilikuwa ikiingia hasara na kupoteza mapato.

Hayo yalibainishwa jana na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi, Edwin Ngonyani wakati akizungumza katika majumuisho ya ziara yake ya kikazi ya siku moja iliyolenga kuangalia mwenendo wa utendaji wa Bandari ya Tanga.

Katika ziara hiyo, pia Naibu Waziri alifanya ukaguzi wa Flow meters pamoja na matishari matatu ambayo yamedumu kwa zaidi ya miaka minne bila kufanya kazi bandarini hapo.

Mhandisi Ngonyani alisema serikali imesikia kwamba kufungwa kwa mita za kupimia mafuta(Flow Meters)kwenye bandari za hapa nchini kumetokana na ushiriki  wa baadhi ya wafanyakazi wa TPA waliokuwa wamelenga kunufaika kupitia wafanyabiashara wakubwa ambao kimsingi mita hizo zilikuwa zikiwabana katika ulipaji wa kodi.

Pia imeelezwa kuwa baadhi ya wafanyakazi hao wanajihusisha kufanya uchochezi kwa wananchi ambao walitakiwa kupisha maeneo yao kwa ajili ya ujenzi wa bandari ya Mwambani, ambao licha ya kulipwa fidia lakini wameendelea kugoma kuachia ardhi hiyo.

“Uamuzi wa kuondoa Flow meters ulikuwa ni wa kipuuzi kabisa na tumesikia uchochezi huu pia ulihusisha baadhi ya wafanyakazi," alisema Ngonyani. "Inasikitisha sana kwani nia yao ilikuwa ni kuwanufaisha wafanyabiashara."

Alisema iwapo watumishi wa TPA wangekuwa na umoja katika kupigia kelele maamuzi yaliyofanywa kipindi hicho, ni dhahiri kuwa hali ya ukwepaji wa kodi kwenye shehena ya mafuta yanayoingia nchini isingefikia ilivyo sasa.

Alisisitiza kwamba serikali itawachukulia hatua za kisheria waliohusika na manunuzi ya matishari matatu kwenye Bandari ya Tanga ambayo hayakidhi vigezo vya kiutendaji.

Aidha, aliitaka Menejimenti ya mamlaka hiyo kupitia upya mkataba wa mzabuni aliyeagiza vifaa hivyo kuona kama wataweza kunusuru kiasi cha fedha zilizotumika.

“Kuna haja ya kuupitia upya mkataba wa mzabuni tuone kama kuna njia yoyote ya kuokoa zile fedha lakini bado tuendelee pia kuangalia namna ya haya matishari yatakavyotumika kwa njia mbadala.

"Kama alivyosema Waziri Mkuu (juzi) nasisitiza kwamba aliyehusika tutamshughulikia.”

Mhandisi Ngonyani alisisitiza kuwa wananchi wajenge imani na serikali ya awamu ya tano kwamba Bandari mpya ya Mwambani itajengwa na kamwe haitakuwa ndoto; hatua itakayoenda sambamba na ujenzi wa njia ya reli kutoka Tanga mpaka Musoma.

Awali, Kaimu Meneja wa TPA Mkoa wa Tanga, Kapteni Andrew Matillya alisema kwa wastani wa kila mwezi Meli ya moja ya shehena ya mafuta inapukuliwa bandarini hapo na kwamba utaratibu unaotumika kupima mafuta hayo si wa flow meters kwani ziliondolewa tangu mwaka 2011.

“Kila mwezi kuna wastani wa meli moja inapakua mafuta kwenye bandari hii lakini utaratibu unaotumika ni wa bye-pass kwa maana kwamba flow meters hazitumiki kupima kiasi cha mafuta kinachoingia nchini,” alisema.

Naye Mbunge wa Jimbo la Tanga, Mussa Mbaruku (CUF), aliishukuru serikali ya awamu ya tano kwa hatua mbalimbali inazochukua kama kurudisha matumizi ya Flow meters na ahadi ya ujenzi wa bandari ya Mwambani.

Alisema maamuzi hayo yanajenga matumaini mapya kwa wananchi wa Tanga ambao walishakata tamaa.

Hivi karibuni Serikali ilimsimamisha kazi Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo nchini (WMA), Magdalena Chuwa na Meneja Vipimo Kitengo cha Bandari, Bernadina Mwijarubi.
Mwijarubi ndiye anashughulikia kitengo cha mafuta bandarini.

Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Jumatatu Ya Februari 22

CHADEMA Waanza Kutimuana Jijini Mbeya

$
0
0
Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Mbeya Mjini, John Mwambigija pamoja na wajumbe wa kamati ya utendaji ya wilaya hiyo wamevuliwa uongozi kwa kile kilichodaiwa kuwapo kwa msuguano miongoni mwao.
 
Uamuzi huo ulifikiwa usiku wa kuamkia jana kwenye kikao cha mashauriano kilichoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Zanzibar), Issa Said Mohamed.
 
Mohamed alipoulizwa kuhusu uamuzi huo, aligoma kulizungumzia kwa undani akidai hayo mambo ya ndani ya chama.
 
Hata hivyo, alikiri kusimamia kikao hicho ambacho kilianza saa 2.00 usiku na kumalizika saa 11.00 alfajiri.
 
Kikao hicho kilifanyika katika ukumbi wa Kanisa Katoliki uliopo Maghorofani jijini Mbeya.
 
Taarifa za ndani ya chama zilizopatikana jana asubuhi, zilidai kuwa awali, wajumbe walimuomba makamu mwenyekiti huyo kufika jijini hapa na kuitisha kikao hicho kujadili msuguano uliopo.
 
Mmoja wa wajumbe waliokuwapo kwenye kikao hicho ambaye hakutaka kuandikwa  jina , alisema kuliibuka malumbano makali huku wajumbe wakinyoosheana vidole kwa kutuhumiana.
 
Alisema wajumbe ndiyo wanaoharibu chama na kutengeneza makundi yasiyokuwa na tija.
 
“Ile kamati ya utendaji ya Wilaya iligawanyika kitambo sana, tangu wakati ule wa kuwapata wagombea kupitia viti maalumu, sasa baada ya kuona vile na mpasuko ukizidi kuwa mkubwa, ndiyo kundi moja likamuomba makamu mwenyekiti aje aitishe kikao cha mashauriano cha jimbo.
 
“Sasa kwenye kikao cha usiku ilionekana mpasuko ni mkubwa na hakuna anayeweza kuendesha chama,” alisema mjumbe huyo.
 
Alisema kutokana na malumbano yaliyojitokeza kwenye kujenga hoja baina ya makundi hayo mawili, Mohamed akaamuru kumsimamisha kila mjumbe huku akiwauliza kama wana sababu ya kuendelea kuwapo kwenye nyadhifa zao.
 
Alisema mwisho wa kikao wajumbe hao wakakubaliana kukaa pembeni na kutoa nafasi kufanyika kwa uchunguzi wa kina.
 
Baada ya kamati hiyo kuvuliwa nyadhifa zao, makamu mwenyekti huyo aliamuru ofisi ya chama hicho wilaya iongozwe na madiwani kwa muda wakisaidiwa na uongozi wa chama Mkoa wa Mbeya.
 
Akiendelea kuzungumzia uamuzi huo wa chama Mohamed alisema: 
 
“Kilikuwa kikao cha ndani ya chama ambacho ni siri yetu, hivyo siwezi kukwambia kilichojadiliwa wala hatua zilizochukuliwa. 
 
“Uamuzi wote wa ndani unaamriwa na kumalizwa ndani ya vikao vya kamati ya utendaji, kwa hiyo subiri hadi kamati kuu itakapoamua kuzungumza nje.” 
 
Hata hivyo, Mwambigija alikiri kuondolewa kwa kamati nzima huku akisema chanzo ni makundi yaliyojitokeza kwenye harakati za kumpa mgombea umeya wa Mbeya mjini ndani ya chama hicho.
 
“Nilichokiona, ni kwamba eti nilikuwa upande wa meya aliyepita (Mchungaji David Mwashilindi) hivyo kundi lile ambalo lilishindwa ndiyo limetengeneza zengwe,” alisema Mwambigija.

Taarifa ya Msajili Wa Vyama Vya Siasa Kukanusha Habari Iliyoandikwa Na Gazeti La Tanzania Daima Kuhusu Vyama Kutopewa Ruzuku

Paul Makonda Na Meya Wa Kinondoni ( Chadema ) ' Washikana Mashati ' Kuhusu Mipaka Ya Kiutendaji

$
0
0
Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Boniface Jacob na Mkuu wa wilaya hiyo, Paul Makonda wameingia kwenye mvutano kuhusu kuvuka mipaka ya utendaji wa halmashauri hiyo.

Mvutano huo umekuja baada ya Jacob kumtuhumu Makonda kuwa ametoa taarifa za kikao cha kamati za fedha ya halmashauri hiyo kilichofanyika wiki iliyopita kinyume na taratibu.

“…Tena hata kwenye kikao hakuwepo, lakini nashangaa kuona ameenda kutangaza kwenye vyombo vya habari kuwa Wilaya ya Kinondoni inatarajia kupata dola 300 milioni za Marekani sawa na Sh600 bilioni kutoka Benki ya Dunia kwa ajili ya miradi ya maendeleo,” alisema Jacob jana kwenye mkutano na waandishi wa habari.

“Vikao vyote vya halmashauri ni siri… huo ni upotoshaji na Makonda anaingilia mamlaka zisizokuwa za kwake, ” alisema.

Jacob alisema halmashauri hiyo imeshindwa kufumbia macho jambo hilo kwani linaweza kuleta mvutano baadaye.

“Mimi nalalamikiwa na wajumbe wa kamati, wanasema kwa nini taarifa za kikao ambazo ni za siri zinatangazwa wakati bado michakato yake inaendelea?” alihoji Jacob.

Meya huyo alisema Makonda ambaye alipewa taarifa hizo na maofisa tarafa waliohudhuria kikao hicho, alitakiwa kuuliza uongozi wa halmashauri kabla ya kutangaza kwa umma.

“Sasa leo ikitokea wajumbe wamegoma kupitisha maazimio kuhusu mchakato huo hizo hela atatoa wapi?” aliendelea kuhoji.

Alisema endapo Makonda ataendelea na tabia hiyo, maofisa tarafa watazuiliwa kuhudhuria kwenye vikao vya kamati za fedha za halmashauri hiyo.

Hata hivyo, Jacob alisema si mara ya kwanza kwa mkuu huyo wa wilaya kuvuka mipaka na kuingilia shughuli za halmashauri, ambazo kimsingi zinapaswa kufanywa na meya, mkurugenzi au msemaji wa halmashauri.

Meya huyo alisema mara ya kwanza Makonda alisema halmashauri itajenga machinjio ya kisasa, wakati anafahamu hana uwezo wa kupata fedha za kufanikisha mradi huo.

Jacob alisema halmashauri ndiyo yenye dhamana na kuidhinisha fedha kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo.

Pili, aliwahi kuwaita wenyeviti wa Kinondoni Leaders Club kwa ajili ya kuzungumzia mchakato wa kuvunja maeneo ya wazi yaliyojengwa.

Alipotafutwa Makonda kueleza kuhusu madai hayo, alisema Jacob bado ni mwanafunzi hivyo hawezi kuzungumza chochote juu ya madai hayo.

“Amechaguliwa kuwa meya juzi tu bado mwanafunzi, hafahamu mipaka ya mamlaka yangu. Akijifunza na kuelewa hizo kelele hamtazisikia tena,” alisema Makonda

Shirika la Elimu Kibaha Kuchunguzwa

$
0
0
Waziri wa nchi ofisi ya rais TAMISEMI, utumishi na utawala bora, George Simbachawene wa kwanza kushoto akiwaambia jambo mkuu wa mkoa wa Pwani mhandisi Evarist Ndikilo wa katikati na wa kulia mganga mkuu hospital ya Rufaa ya Tumbi dk. Peter Datan wakati alipotembelea shirika la elimu Kibaha juzi. (Picha na Mwamvua Mwinyi)
***
Waziri wa nchi ofisi ya rais TAMISEMI, utumishi na utawala bora, George Simbachawene amesema ataunda tume ya watu wachache kutoka wizara hiyo haraka iwezekanavyo ili kuchunguza idara na vitengo vyote katika shirika la elimu Kibaha (KEC) ndani ya wiki mbili.

Amesema amefikia hatua hiyo baada ya kubaini tatizo kubwa la uongozi hivyo ipo haja ya kuchunguza hali iliyopo kuanzia juu hadi chini.

Aidha Simbachawene alisema tume hiyo itakuwa na kazi ya kupita kila idara na kitengo kuchunguza mambo atakayoyaelekeza kwa siku 14 kisha mwezi march mwaka huu atarejea kufanya ziara na kuzungumza na watumishi.

Alielezea kuwa kuna kila sababu ya kutafakari muundo mzima wa shirika na kuweka mikakati, sheria na mipango ya kisasa na kuondokana na ile iliyopitwa na wakati.

Aliyasema hayo juzi katika ziara yake ya kikazi ya siku moja aliyoifanya shirika la elimu Kibaha ambapo alipata fursa ya kutembelea maeneo ya uwekezaji na shirika kijumla.

Simbachawene alisema katika shirika hilo kuna wachache wanaonufaika na kuneemeka kwa kula hadi wamevimbiwa huku wengine wakiwa wanadidimizwa kimaslahi na kukosa haki zao za msingi.

Alimtaka mwenyekiti wa bodi mpya ya shirika hilo Patrick Makungu na viongozi wengine katika bodi hiyo, kuwa na mawazo mapya ya kuendesha shirika badala ya kufanya kazi kwa mazoea ili kurudisha maendeleo yaliyokuwepo miaka ya nyuma.

Alisema shirika la elimu Kibaha lina miradi mingi, ardhi kubwa na uwekezaji mkubwa hivyo waitumie kujiongezea kipato kwa maslahi ya Taifa na vizazi vijavyo.

Simbachawene alieleza KEC inayumba na kuondoa taswira ya maendeleo na uchumi wake wakati ina vitega uchumi na ardhi kubwa.

“Serikali ya awamu ya tano chini ya rais Magufuli ipo kwa ajili ya kuinua uchumi wa nchi na haitokuwa tayari kuona mashirika ya aina hii yanashushwa hadhi yake na watu wachache na kuwanyima haki watumishi uhuru wa kutembea kiajira na haki zao za msingi “

” Ipo haja ya kuchunguzana na kufanya maamuzi makini kwa kufuata misingi, sheria, kanuni na haki za kiutumishi”alisema Simbachawene.

Hata hivyo alisema uwekezaji wa kampuni ya organia kutoka Egypt iliyowekeza kwenye shirika hilo ni mzuri na wenye tija lakini unaonekana haufuata taratibu na kusababisha maswali kutoka kwa watumishi.

Awali mkurugenzi wa shirika la elimu Kibaha Dk. cyprian Mpemba alisema shirika linakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kupokea wagonjwa wengi 400 hadi 450 kwa siku na madawa.

Dk. Mpemba alitaka serikali kufikisha fedha kwa wakati kwani ni muda mrefu sasa fedha wanazoahidiwa wanatumiwa pungufu tofauti na kiwango wanachoomba hivyo kushindwa kukidhi mahitaji.

Nae mganga mkuu wa hospital ya Rufaa ya Tumbi, dk. Peter Datan alisema kitengo cha maafa hususan ajali (Trauma center) kinakabiliwa na ukosefu wa fedha kwa zaidi ya miaka mitatu sasa.

Katika hatua nyingine waziri huyo alipokea kero mbalimbali kutoka kwa watumishi wa shirika hilo ikiwa ni sanjali na wastaafu shirikani hapo kukosa stahiki zao.

Kero nyingine ni kuondolewa mradi wa kuku ulikuwa ukiingiza bil. 1 na kuingizwa mradi wa mkataba wa Organia ambao hawauelewi maslahi yake, upungufu wa nyuzi, madawa, fedha za allowance na walimu kutopandishwa madaraja kwa miaka sita sasa.

Simbachawene alipokea kero hizo na kuahidi kuzifanyia kazi ambapo kwa upande mwingine aliitaka mganga mkuu dk. Datan kukumbushia fedha walizoahidiwa serikalini ili ombi lao lishughulikiwe haraka.

Uchaguzi wa Marudio Zanzibar: Jecha Adai Maalim Seif Ni Mgombea Halali Na ZEC Haitambui Kujitoa Kwake

$
0
0

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, ameibuka tena na kutangaza kukamilika kwa matayarisho ya uchaguzi wa marejeo Machi 20, mwaka huu huku akikataa kutoa majina ya wagombea.

Jecha ambaye tangu afute uchaguzi alionekana hadharani Januari 12, 2016 wakati wa sherehe za Mapinduzi na baadaye kwenye televisheni akitangaza tarehe ya uchaguzi huo wa marudio, alisema wagombea wote ‘waliojitoa’ watapewa haki zote wanazostahiki kupewa kama wagombea kwa kuwa hawakufuata taratibu za kisheria za tume hiyo akimaanisha kuwa hakuna mgombea aliyejitoa kauli ambayo inapingana na msimamo wa CUF ambayo imetangaza kuwa mgombea wake wa urais Maalim Seif Sharif Hamad hatagombea.

Kama alivyofanya wakati anatangaza tarehe ya uchaguzi wa marudio, jana alizungumza kupitia mwandishi wa Televisheni ya Taifa (TBC), akiwaacha waandishi waliokuwa wameitwa kwa ajili ya mkutano wake nje ya ofisi hiyo.

Jecha ambaye amekuwa haonekani hadharani isipokuwa katika matukio machache, alisema tume yake inawahesabu waliokuwa wagombea katika uchaguzi ulio futwa kuwa ni halali, licha ya kuandika barua za kujitoa katika tume hiyo. 

“Pamoja na kuwa wagombea wengi, hasa wa CUF, kuandika barua za kujitoa katika ofisi za ZEC wilaya na makao makuu, hakuna barua hata moja ambayo imefuata utaratibu wa kisheria na kwa mantiki hiyo, bado tunahesabu wagombea hao ni halali katika uchaguzi mkuu wa marejeo,” alisema Jecha. 

Katika taarifa hiyo, Jecha alisema vyama vinane vimeshathibitisha ushiriki wake katika uchaguzi huo vikiwamo Tadea, ACT, ADC, AFP, SAU, TLP na CCM na utaratibu wa kuwapatia ulinzi wagombea hao umeshaanza. 

Jecha alisema ofisi yake imeshafanya mawasiliano na vyama na wagombea na kuwapa taarifa mbalimbali za matayarisho ya uchaguzi, ili waanze taratibu za kupanga mawakala wao.

Alisema baadhi ya vyama vimetoa taarifa kupitia vyombo vya habari kuwa havitashiriki katika uchaguzi, na kuwataka wagombea wao kuandika barua za kutoshiriki katika upigaji kura huo.

“Swala hili naomba nilitolee ufafanuzi kidogo kwa kuwa kauli za vyama hivyo zimewachanganya baadhi ya wagombea waliodhaminiwa na vyama hivyo, ambao bado wanataka kugombea katika uchaguzi huo,” alisema Jecha.

Alisema kila chama cha siasa kilichosajiliwa kinachokusudia kushiriki uchaguzi wa Rais kitawasilisha jina la mgombea wake wa urais kwa tume, na ili mtu awe ameteuliwa kihalali kuwa mgombea urais ni lazima awe amedhaminiwa kwa maandishi na watu wasiopungua 200 ambao wameandikishwa kuwa wapiga kura kutoka kila mkoa wa Zanzibar.

“Kwa bahati mbaya mpaka tunapowasilisha taarifa hii, hakuna chama hata kimoja kati ya vyama ambavyo vimejinadi kuwa havitashiriki katika uchaguzi kilichoiandikia Tume kuwa kimefuta udhamini wa wagombea wake kushiriki katika uchaguzi,” alisema Jecha katika taarifa yake.

“La pili ni kuwa utaratibu wa kujitoa kwa wagombea katika uchaguzi umefafanuliwa vizuri sana katika kanuni ya uchaguzi ya mwaka 2015,” alisema mwenyekiti huyo akisisitiza kuwa haukufuatwa.

Kwa mujibu wa vifungu hivyo, alisema mgombea wa urais anaweza kujiondoa kwa kutoa taarifa ya maandishi aliyoitia saini mwenyewe atakayoiwasilisha kwa mwenyekiti si zaidi ya saa 10 jioni siku ya uteuzi.

“Mgombea uwakilishi na udiwani anaweza kujiondoa kwa kutoa taarifa ya maandishi aliyoitia saini mwenyewe atakayoiwasilisha kwa msimamizi wa uchaguzi si zaidi ya saa 10 jioni ya siku inayofuatia siku ya uteuzi."

Jecha alifafanua kuwa tarifa ya kujiondoa chini ya kanuni hizo inatakiwa iambatanishwe na tamko la kisheria lililotolewa na kutiwa saini na mgombeya mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu kwa mgombea wa urais na hakimu kwa mgombea wa uwakilishi au udiwani, mambo ambayo hayakufanyika.

Kuhusu daftari la wapigakura, Jecha alisema kazi ya uchapishaji wa madaftari na vituo vya kupigia kura ndani na nje imeshakamilika, na wanatarajia mwisho wa mwezi huu majina hayo kubandikwa.

Alisema ratiba ya mafunzo kwa wasaidizi na wasimamizi wa majimbo imeshakamilika, na mafunzo hayo kwa Unguja na Pemba yataendeshwa Februari 22-28 na wasimamizi wa uchaguzi wa majimbo watapewa mafunzo Machi 2 hadi Machi 5.

Alisema mafunzo mengine yatakayotolewa ni ya wasaidizi wa vituo vya kupigia kuwa ambayo yamepangwa kufanyika Machi 11 -13 na mafunzo ya mawakala wa uchaguzi siku ya Machi 14 na mafunzo ya walinzi wa vituo vya kupigia kura Machi 15, 2016.

Jecha alisema kazi ya upangaji wa vifaa vya kupigia kura kwa ajili ya kusambazwa wilayani tayari imeanza katika ghala za ZEC za Unguja na Pemba na baada ya kukamilika kwa kazi hiyo, utaratibu wa kuvisafirisha katika wilaya husika utaandaliwa.

Kuhusu uchapishaji karatasi za kura, mwenyekiti huyo alisema matayarisho yamekamilika baada ya tume kumpitisha mchapishaji wa karatasi hizo.

Rais Magufuli Kuwatema Wakuu wa Mikoa 20

$
0
0

Wakati  Rais Dk. John Magufuli akitarajia kutangaza safu ya wakuu wa mikoa  na wilaya wapya, imebainika wapo zaidi ya 20 ambao watatemwa kutokana na sababu mbalimbali za utendaji.

Habari za kuaminika zinasema miongoni mwa  wakuu wa mikoa watakaoachwa wamo walioshindwa kutatua kero sugu zikiwamo za mapigano ya wakulima na migogoro ya ardhi ambayo kila kukicha imesababisha watu kadhaa kufariki dunia.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, pia wamo wakuu wa mikoa  ambao wanaweza kuachwa kutokana na kuwa na umri mkubwa na wanaonyesha wazi hawawezi kwendana na kasi ya utendaji kazi wa serikali ya awamu ya tano ambayo inatumia falsafa ya Hapa Kazi Tu.

Habari hizo zinasema wapo wakuu wa mikoa ambao wameshindwa kutatua migogoro ya ardhi katika maeneo yao kwa zaidi ya miaka 10 hadi 15 na kusababisha vurugu kuibuka kila wakati.Miongoni mwa mikoa iliyokithiri kwa migogoro hiyo ni Morogoro, Tanga na Manyara.

“Wapo wakuu wa mikoa  ambao hawatarudi kutokana na rekodi za matukio, wapo ambao kwenye maeneo yao   migogoro imedumu kwa zaidi ya miaka 10 na kuendelea, sasa viongozi wa aina hii unadhani watabaki kweli kwenye Serikali?

“Nakuhakikisha kule ambako kuna migogoro ya ardhi na mapigano ya kila siku wako hatarini kupoteza kibarua… unajua mheshimiwa kila siku anajiuliza hivi inakuwaje mkoa ambao una kamati za ulinzi na usalama za wilaya zinashindwa kuchukua hatua za kumaliza mapigano haya?

“Inawezekana zinafanya kazi kwa kutegeana au wengine wanakula kwa wafugaji na wakulima.

“Mpaka wiki iliyopita tumedokezwa kwamba ma-RC  20 hawatarudi katika nafasi zao kwa sababu wameshindwa kuonyesha kama wanaweza kuwajibika ipasavyo,” kilisema chanzo cha habari hii.

Chanzo  hicho kilisema pia kuwa wengine ambao wako hatarini kutemwa ni wale wenye umri mkubwa ambao kwa namna moja au nyingine wanapaswa kustaafu.

“Sikutajii ni mikoa gani kwa sababu hawa wanajulikana vizuri…pale kanda ya ziwa, nyanda za juu kusini na mikoa ya kaskazini ni maeneo  ambayo yataguswa mno.

“Unajua Dk. Magufuli na timu yake wanaangalia kwa kina mno  hata mikoa ya kanda ya magharibi nao hawako salama kwa sababu wapo wazee wetu ambao inaonekana wazi umefika wakati wa kupisha kizazi kingine ambacho kitasaidia kusukuma mbele gurudumu la maendeleo,”kilisema chanzo chetu.

Kuhusu wakuu wa wilaya, chanzo hicho kilisema hakuna tofauti na wakuu wa mikoa kwa vile kila mmoja atapimwa kutokana na namna alivyoweza kusimamia majukumu ya Serikali tangu alipoteuliwa.

“Jambo moja kubwa ndugu yangu, hapa kila mmoja atapimwa kutokana na uwezo wake… nadhani unakumbua Rais mwenyewe alisema anawachunguza, tutarajie mabadiliko makubwa,” kilisema chanzo chetu.

Hivi karibu Rais Magufuli, alisema wakuu wa mikoa na wilaya wajiandae kuwajibika endapo maeneo wanayoongoza yatakuwa na ukosefu wa chakula na kusababisha wananchi kukumbwa na njaa wakati maeneo mengi ya nchi yamepata mvua ya kutosha.

Mikoa ambayo imekuwa ikikumbwa   na njaa mara kwa mara  ni pamoja na Mara, Iringa, Dodoma,Tanga na Shinyanga.

Mpinzani wa Museveni, Dr. Besigye Akamatwa Tena........Museven Aeleza Sababu za Kumpa Kifungo Cha Nyumbani

$
0
0

Kiongozi wa chama cha upinzani cha Forum for Democratic Change (FDC) nchini Uganda Kizza Besigye amekamatwa tena na maafisa wa polisi. Dr. Besigye amekamatwa alipokuwa akijaribu kuondoka nyumbani kwake.
 
Rais Yoweri Museveni  leo asubuhi  aliongea  na  BBC na kusema kuwa  serikali yake iliamua kumpa kifungo cha nyumbani  ili kuzuia vurugu baada ya zoezi la kupiga kura na kutangaza matokeo.

Museveni alieleza kuwa walichukua uamuzi huo baada ya kubaini kuwa Dk. Besigye alipanga kutangaza matokeo yake mwenyewe ambayo sio ya kweli na kuhamasisha wafuasi wake kufanya fujo, vitendo ambavyo havikubaliki.

“Walikuwa wanataka kufanya fujo. Kwanza walikuwa wanataka kutangaza matokeo yao wenyewe ya uongo. Pili walitaka kufanya fujo za kuharibu mali,” alisema Museveni.

Kadhalika, Museveni alieleza kuwa serikali yake haina mpango wa kuweka ukomo wa Urais nchini humo kwakuwa tayari Bunge liliona ni vyema kuwa na kipindi kisichokuwa na ukomo. Hata hivyo, alisema kuwa hana mpango wa kufanyia marekebisho katiba ya nchi hiyo ili aendelee kubakia madarakani.

“Hakuna mpango wowote. Hatujazungumzia hilo. Lilikuja kwenye baraza la mawaziri tukasema hapana, hakuna haja ya kuongeza,”Museveni anakaririwa.
Katika hatua nyingine, Museveni ambaye anaiongoza Uganda tangu mwaka 1986, amepinga ripoti za waangalizi zilizodai kuwa uchaguzi huo haukuwa huru na haki.

Alisema kuwa wanaotoa madai hayo kwa madai kuwa nguvu ya jeshi ilitumika zaidi hawaijui siasa ya Uganda kwani wanasiasa wengi hawajakomaa kisiasa hivyo wanaweza kuanzisha fujo muda wowote.

Shule ya Sekondari Ilboru sasa Kuchuja Wanafunzi

$
0
0

Kufuatia kutofanya vizuri kitaifa katika mtihani wa kidato cha nne, shule ya sekondari ya watoto wenye vipaji maalumu, IIboru itaanza kuwachuja wanafunzi wasio na uwezo wanaopangiwa kusoma shuleni hapo.
 
Mkuu wa shule hiyo, Julius Shula amesema licha ya Ilboru kuwa ya kwanza kwa shule za Serikali nchini, lakini imebaini upungufu katika upatikanaji wanafunzi.
 
Amesema kuna wanafunzi kutoka shule za binafsi wanaopangiwa IIboru, wamebainika hawana uwezo, hivyo kutilia shaka alama walizopata katika mitihani yao ya kuhitimu darasa la saba.
 
“Tayari tumewapa mitihani waliongia kidato cha kwanza, huwezi amini kuna wanafunzi wanapata alama 0, lakini ukifuatilia matokeo ya kuja hapa wana wastani wa alama zaidi ya 200 sasa hili ni tatizo kubwa,” alisema. 

Majipu Yaendelea Kutumbuliwa......Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma (TPSC) Asimamishwa Kazi

$
0
0

WAZIRI  wa nchi,ofisi ya Rais menejimenti ya utumishi  wa Umma na Utawala bora,Angella Kairuki amemsimisha kazi mkuu wa chuo cha utumishi wa umma nchini Said Nassoro kutoka na uzembe ulioisababishia serikali  hasara  ya  bilioni 1.
 
Vilevile Waziri Kairuki amewasimamisha  kaziMkuu wa chuo hicho tawi la Dar es salaam,Joseph  Mbwilo na Silvanus  Ngata ambaye naye ni Mkuu wa chuo hicho tawi la Tabora.
 
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam,Waziri Kairuki amesema amefikia hatua hiyo ya kuwasimamisha kazi watumishi hao baada ya kubaini utendaji usioridhisha katika vyuo hivyo.
 
Amesema Nassoro amemsimisha kazi baada ya kushindwa kuwasimamia watumishi wa chini yake katika  chuo hicho.
 
“Mwaka  2011 hadi  2013 bwana Silvanus Ngata aliongeza gharama za ujenzi wa jengo la chuo hicho tawi la  Mtwara tofauti nafedha iliyokuwa imepangwa.  

"Chakushangaza,huyu Nassoro ambaye ni mkuu wao,  baada ya kugundua kosa hilo alishindwa kumuwajibisha na badala yake aliamua kumhamishia tawi la chuo cha Tabora. Sasa mimi nawasimamisha kazi wote ."Amesema Kairuki
 
Pia waziri Kairuki amesema amemsimamisha Mbwiro kutokana na matumizi mabaya ya fedha za chuo.
 
“Huyu Mbwiro kwa mwaka 2013 alitumia vibaya fedha za ada za wanafunzi  kiasi cha bilioni 1,lakini licha ya ubadhilifu huo,Nassoro alimteua bwana Mbwiro kuwa Kaimu mkuu wa chuo kwa upande wa fedha." Alisema Waziri Kairuki.
 
Wakati Waziri Kairuki akitumbua majipu hayo,mmoja wa watendaji hao,Said Nassoroalikuwepo kwenye mkutano huo na wanahabari huku akiwa hajui kinatakachotokea

Mahakama yatupilia mbali kesi ya Frederick Mwakalebela Kupinga Ubunge wa Mchungaji Peter Msigwa (Chadema)

$
0
0

Mahakama Kuu Kanda ya Iringa imetupilia mbali kesi ya kupinga matokeo yaliyompa Ubunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema), iliyofunguliwa na aliyekuwa mpinzani wake kwenye Uchaguzi huo, Frederick Mwakalebela (CCM).
 
Mahakama hiyo pia imeamuru Mwakalebela kumlipa Mchungaji Msigwa gharama za kesi hiyo iliyofunguliwa mwaka jana na kupata usajili wa mahakama hiyo Novemba 30.
  
Katika shauri la msingi la kesi hiyo namba 5 ya mwaka 2015 ya kupinga matoke, Mwakalebela aliwatuhumu Mchungaji Peter Msigwa na msimamizi wa uchaguzi wa jimbo la Iringa Mjini, Ahmed Sawa kwa kukiuka sheria na taratibu za uchaguzi hali iliyopelekea yeye kupata matokeo mabaya yasiyo halali.

Kesi ya mwakalebela yatupwa anatakiwa kulipa gharama . Nikiwa na wakili msomi wangu Jane Masey
Posted by Peter Msigwa on Sunday, February 21, 2016

Kesi Ya Kafulila Yahirishwa Mpaka March 9, 2016 Baada Ya Mawakili Wa Serikali Kutofika Mahakamani Leo

$
0
0

KESI No. 2 ya mwaka 2015 ya kupinga matokeo ya uchaguzi jimbo la Kigoma kusini iliyofunguliwa na mlalamikaji  David Kafulila dhidi ya mbunge Hasna Mwilima,Msimamizi wa uchaguzi na Mwanasheria mkuu wa serikali imeahirishwa leo na mahakama kuu kanda ya Tabora mpaka  marchi 9, mwaka huu itakapoanza kusikilizwa tena.

Kesi hiyo ambayo ilikuwa  ianze mapema leo katika mahakama ya hakimu mkazi Kigoma,  Mbele ya Jaji Dr Wambari ambae pia ni Mkuu wa chuo cha sheria lushoto mkoani Tanga, imeahirishwa kwasababu mshatakiwa Hasna pamoja na wakili wake Kennedy Fungamtama pamoja na mawikili wa serikali kushindwa kufika mahakamani hapo, kwa madai ya kuchelewa kupata wito wa mahakama hiyo, huku mlalamikaji David Kafulila akifika na wakili wake Prof Safari.

Katika mazingira hayo Jaji Wambari aliagiza mawasiliano yafanyike kwa pande hizo ili kujua ni lini kwa hakika mawakili hao wataweza kushiriki katika kesi hiyo.

Kutokufika kwa mlalamikiwa  na mawakili wake na wale wa upande wa serikali ilipelekea zoezi la kusikiliza kesi hiyo kusimama kwa saa mbili kutoka saa tano asubuhi  mpaka saa saba mchana na baada ya hapo hakimu mfawidhi wa Mkoa wa Kigoma kwa niaba ya Jaji silivesta Kahinda alisema  kuwa kesi itaendelea march 9 mwaka huu na kwamba kwakuwa tarehe hiyo imependekezwa na mawakili na pande zote mbili.

Akiongea na mtandao huu mlalamikaji wa kesi hiyo David Kafulila alisema kuwa anakubaliana na uamuzi wa mahakama hivyo aliwataka wananchi wawe na subiri hadi hiyi tarehe 9 march mwaka huu.

Bodi ya Wakurugenzi wa Magazeti ya Serikali,(TSN) Yamsimamisha Kazi Mhariri Mtendaji

$
0
0

BODI ya wakurugenzi wa magazeti ya Serikali,(TSN) imemsimashisha kazi Mhariri Mtendaji wa magazeti hayo Bw Gabrieli Nderumaki kupisha uchunguzi kutokana na utendaji usioridhisha ndani ya kampuni hiyo.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa Bodi hiyo Bw Prof Moses Warioba amesema hatua za kumsimamisha kazi Mhariri Mtendaji huyo umetokana na kuwepo kwa malalamiko mengi kutoka kwa wafanyakazi wa kampuni hiyo ambapo nafasi yake itachukuliwa na Naibu Mhariri Bi Tumma Abdalah.

“Kumekuwa na mambo mengi yanayofanyika bila kufuata utaratibu ndani ya kampuni hii ikiwemo wafanyakazi kutoelewana na menejimenti katika kulipwa stahili zao, pamoja na wafanyakazi kupewa majukumu ambayo hawana uwezo wa kuyatekeleza”.Alisema Prof Warioba.

Aidha Prof Warioba ametengua uteuzi wa Bw Felix Mushi aliyekuwa Meneja mauzo na masoko katika kiwanda cha uzalishaji kwa kukosa sifa na utendaji mbovu uliopelekea kampuni kushuka katika uzalishaji.

Hatua hiyo ya kuwawajibisha watendaji hao imetokana na Ziara ya Mhe. Nape Nnauye Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo katika Kampuni hiyo ambapo pia hakuridhiswa na utendaji mbovu uliopelekea wafanyakazi 21 kuacha kazi.

“Nataka Bodi itafakari juu ya malalamiko yaliopo kwa wafanyakazi na wachukue hatua kabla mimi sijakutana na wafanyakazi hao wiki ijayo ili kujua mapungufu yako wapi.”Alisema Mhe Nape.

Hata hivyo Bodi hiyo ya wakurugenzi inaendelea kutafuta namna ya kuboresha utendaji ndani ya kampuni ili iendane na kasi iliyopo katika uzalisahaji wa magazeti kwa kiwango kikubwa.

TCRA Yaifungia Video mpya ya Wimbo ‘Zigo remix’ ya AY Aliyomshirikisha Diamond Platnumz

$
0
0

Ambwene Yessaya ‘AY’ amethibitisha kupokea taarifa ya kufungiwa kwa video ya wimbo ‘ Zigo remix’ aliyomshirikisha Diamond Platnumz.

Akizungumza na 225 katika kipindi cha XXL cha Clouds FM, Jumatatu hii, AY amesema alipokea barua yenye amri hiyo kutoka kwa rafiki yake ambae anafanya kazi katika chombo kimoja cha habari.

“Sijaelewa maadili gani kwa sababu kama maadili niliyokosea mimi ni kushoot kwenye swimming pool, na kama kwenye swimmig pool watu nimevalisha jeans au maturubai hapo nitakuwa nimekosa maadili,” alisema AY.

“Mavazi ya kwenye swimming pool yako kila mahali, hata kwenye taarifa za habari (Michezo) wanaonyesha waogeleaji, kama hiyo pia ni kukiuka maadili ni sawa. Inashangaza mamlaka zetu wanafocus kwenye kufungia nyimbo zetu na kuacha video za nje. Sijawahi sikia muziki wa Kenya, Uganda au Marekani umefungiwa, kama wanaona nyimbo za Nicki Minaj zina maadili halafu Zigo ya AY haina maadili baasi unaacha tu iwe hivyo ,” aliongeza AY.
 
Pia AY alisema barua hiyo ilitoka kwa Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) ikisema kwamba video hiyo inakiuka maadili.
Kwa mujibu wa Meneja Mawasiliano wa TCRA, Innocent Mungi, amethibitisha kuvitumia vituo vya luninga nchini taarifa ya namna ya kupembua kazi za wasanii zisizo na maadili.

Taarifa ya TBS Ya Kupotea Stakabadhi Tatu

Bilioni 4/-Zaokolewa kwa Kuzuia Safari za Ndani

$
0
0

OFISI ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imeokoa Sh bilioni 4.38 ambazo zingetumika na watumishi wa Halmashauri mbalimbali nchini kwa ajili ya safari za ndani.

Waziri wa Tamisemi, George Simbachawene alibainisha hayo katika kipindi maalumu cha Siku 100 za Serikali ya Awamu ya Tano kinachorushwa na kituo cha televisheni cha TBC1 cha Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).

“Katika kipindi cha siku 95, tumeweza kuokoa kiasi kikubwa cha fedha ambazo watumishi wa halmashauri wangezitumia katika safari za ndani zisizo na tija na hazijalenga kumkomboa mwananchi huyu ambaye hana dawa na hana barabara,” alisema Simbachawene.

Akizungumzia uwajibikaji wa watumishi katika halmashauri nchini, Simbachawene alisema ili kuhakikisha halmashauri hizo zinafanya kazi ipasavyo, wameunda kitengo cha ukaguzi ambacho kina kazi ya kudhibiti na kufuatilia utendaji wa kazi za halmashauri.

“Tamisemi tuna deni kubwa, kwani sisi ndio tunaotegemewa na wizara kutafsiri mipango yao ya elimu afya, miundombinu na sekta nyingine. Tamisemi ni wakala wa serikali kwa wananchi,” alisema na kuongeza kuwa watendaji wa halmashauri ambao hawataki kwenda na kasi ya Rais Magufuli, basi wataondolewa katika nafasi zao bila kuonewa haya.

“Tutahakikisha tunawachukulia hatua wezi wote, wabadhirifu na wasio waadilifu, huwezi utupishe. Tutawapima kwa jinsi wanavyoondoa kero kwa wananchi,” alisema na kukiri kuwa katika halmashauri kuna matatizo ya uadilifu jambo linalofanya miradi mingi kushindwa kukamilika na ikikamilika inakuwa chini ya kiwango.

Aidha, amewataka wakurugenzi kuhakikisha wanawafikia wananchi na kumaliza kero za wananchi kinyume chake kazi wataiona chungu.

Kuhusu ukusanyaji wa mapato, Simbachawene alisema asilimia 95 ya halmashauri zote zimeanza kutumia mfumo wa elektroniki katika kukusanya mapato na kuwa zile chache ambazo hazijaanza zimetakiwa kufanya hivyo baada ya kuongezewa muda kidogo.
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live




Latest Images