Quantcast
Channel: MPEKUZI
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live

Mfumuko wa bei waongezeka hadi asilimia 3.1

$
0
0
Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwaka ulioishia Machi 2019 umeongezeka hadi asilimia 3.1 kutoka 3.0 kwa mwaka ulioishia Februari 2019.

Hali hiyo, imechangiwa na bidhaa zisizo za vyakula kama vile mavazi na viatu, kodi ya pango, mafuta ya taa, mkaa, kuni, huduma za afya, dizeli, chakula na vinywaji.

Hayo yamesemwa jana  jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Sensa ya Takwimu za Kijamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Ephraim Kwesigabo, wakati akitoa taarifa ya hali ya mfumuko wa bei wa kipindi hicho. 

Kwisegabo alitaja baadhi ya bidhaa hizo kuwa ni pamoja na mavazi na viatu(4.4%),  kodi ya pango(4.7%), mafuta ya taa(1.8%), dizeli(8.3%), chakula na vinywaji kwenye migahawa(4.6%) na malazi kwenye mahoteli(5.7).

Hata hivyo alifafanua  kuwa mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa machi mwaka huu umepungua hadi asilimia 0.1 kutoka asilimia 0.5 kwa mwaka ulioishia Februari mwaka huu.

Rais Magufuli Atengua Uteuzi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa

$
0
0

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ametengua uteuzi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa Mkoani Ruvuma Dkt. Oscar Albano Mbyuzi.

Kufuatia uamuzi huo, Rais Magufuli amemteua Jimson Peter Mhagama kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa ni kuwa uteuzi wa Mhagama unaanza leo tarehe 09 Aprili, 2019.


Msajili Vyama vya Siasa Aanza Kuichambua Barua ya ACT- Wazalendo

$
0
0
Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza, amesema wanaifanyia kazi barua ya Chama cha ACT-Wazalendo baada ya kutakiwa kujieleza kwanini kisifutwe kutokana na kukiuka taratibu na sheria na ya vyama vya siasa nchini.

Akizungumza Jijini Dar es salaam, Msajili Msaidizi Sisty Nyahoza amesema, “Tumepokea barua ya ACT ya kujibu tuliyowaandikia kwenye Machi 25, ya kuwataka kujibu hoja, ikiwamo ya kutowasilisha hesabu za ukaguzi za 2013/14, hivyo kutokidhi matakwa ya barua ya Msajili wa Vyama vya Siasa, hatua inayokiuka sheria ya vyama vya siasa sura ya 258,”.

Aliongeza kuwa kutokana na hali hiyo, barua hiyo itafanyiwa kazi kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa ili waweze kutoa haki kulingana na matakwa ya kisheria.

Machi 25, 2019 Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, alitishia kukifutia usajili Chama cha ACT-Wazalendo, kutokana na kukiuka Sheria ya Vyama vya Siasa ikiwamo kuchoma moto bendera ya Chama cha Wananchi (CUF).

Mtungi kupitia barua yake kwa ACT Wazalendo, alitoa siku 14 kwa chama hicho kuwasilisha maelezo ya maandishi kuwa ni kwanini usajili wake wa kudumu usifutwe kutokana na kukosa sifa kukiuka Sheria za Vyama vya Siasa na kutowasilisha ripoti ya ukaguzi kuanzia mwaka 2013 hadi 2017.

Taarifa iliyotolewa na Msajili wa Vyama vya Siasa Machi 25, imesema kutowasilisha ripoti ya ukaguzi ya mwaka wa fedha 2013/14, chama hicho kinakuwa bado hakijakidhi matakwa ya Msajili wa Vyama vya Siasa na hivyo chama hicho pia kinakuwa kimekiuka Sheria ya Vyama vya Siasa Sura ya 258.

LIVE: Rais Magufuli akizindua Kituo cha Afya cha Madaba

$
0
0
LIVE: Rais Magufuli akizindua Kituo cha Afya cha Madaba

Mbunge CHADEMA Awalalamikia MA RC na Wakuu wa Wilaya Wanaowakamata Wananchi na Kuwaweka Ndani

$
0
0
Mbunge wa Rombo (CHADEMA)  Joseph Selesini   amewalalamikia baadhi ya viongozi wa Serikali wakiwamo wakuu wa mikoa na wilaya kufanya vitendo aalivyoviita vya ovyo kwa wananchi.

Akiuliza swali bungeni leo, Selasini amesema anatambua juhudi mbalimbali ambazo zimekuwa zikifanywa na Serikali katika kutatua tatizo hilo.

Hata hivyo, amesema mkuu wa wilaya ya Hai amekuwa akiendelea na vitendo alivyoviita vya ovyo vya kuwakamata wawekezaji na wananchi pamoja na kushinikiza baadhi ya wanasiasa kwa kutumia askari wahame kwenye vyama vyao.

Hivyo, akahoji ni hatua gani zinachukuliwa na  Serikali kukomesha jambo hilo.

Akijibu swali hilo , Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Suleiman Jafo amesema ni kweli awali hali ilikuwa ni  mbaya kwa sababu idadi ya waliokuwa wanafanya vitendo hivyo ilikuwa ni kubwa.

“Wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi hasa wakuu wa wilaya walikuwa wakifanya mambo yasivyo lakini tunajua sisi ndani tumefanya tathimini hali imebadilika sana,” amesema.

Jafo amesema bado kuna baadhi ya kesi wanaendelea kushughulikia na hata mambo wanayozungumza (wabunge) mengine yapo katika utaratibu wa kuyashughulikia.

“Tuvute subira si kila kitu kukitangaze public  lengo letu ni utii wa sheria bila shurti kwa wananchi wote lakini kanuni na sheria kwa viongozi wote lazima zifuatwe,” amesema.

Wizara Ya Afya Kupeleka Mapendekezo Ya Mswada Wa Sheria Bungeni Wa Kila Mtanzania Kuwa Na Bima Ya Afya

$
0
0
Na Amiri kilagalila-Njombe
Wizara ya afya maendeleo ya jamii jinsia wazee na watoto,inatarajia kufikisha bungeni mapendekezo ya muswada wa sheria  ya bima ya afya kuwa ni lazima kwa kila Mtanzania.

Hayo yamebainishwa na waziri wa afya maendeleo ya jamii jinsia wazee na watoto Ummy mwalimu,wakati akikagua huduma ya afya inayotolewa katika hospital ya mkoa wa Njombe Kibena.

“Ndani ya mwezi huu nadhani nitapeleka mapendekezo ya muswada wa sheria bungeni ambapo bima ya afya itakuwa ni lazima kwa kila mtanzania mwenye uwezo,nitoe wito kwa wananchi wa Njombe na Tanzania kwa ujumla wajiandae kwa kuwa ili tuweze kupata huduma bora za afya bila kikwazo cha fedha suruhisho ni kuwa na bima ya afya”alisema Ummy mwalimu

Aidha amewataka watoa huduma za afya za serikali kujipanga kuboresha mazingira ya huduma zao ili wateja waweze kuvutiwa na huduma za serikali kama ilivyo katika hospital za binafsi.

Hata hivyo waziri Ummy amesema ameridhishwa na hali ya utoaji huduma za afya katika hospital hiyo huku akikiri  uwepo wa upatikanaji wa dawa muhimu katika hospital zote nchini kwa zaidi ya asilimia 90%.

“Kwa kiasi kikubwa hali ya utoaji huduma inaridhisha lakini pia kwa upande wa upatikanaji  wa dawa nchini ,tunaposema dawa zinapatikana kwa asilimia 90% sio maneno ya kwenye makaratasi  au majukwaani,ninyi wenyewe ni mashahidi na mmeona dawa muhimu zote zinapatikana katika hospital hii na tumehoji wagonjwa dawa mmepata wamesema wanapata vizuri.

"Changamoto kubwa hapa nimebaini kule wodi ya wazazi kuna msongamano mkubwa wa akina mama wajawazito tunaamini hospital mpya ya rufaa ya mkoa wa Njombe itakayowekwa jiwe la msingi na Rais ikikamilika basi changamoto hii itapungua kwa kiasi kikubwa” aliongeza Ummy

Naye katibu mkuu wa wizara ya afya Dkt.Zainab Chaula ameridhishwa na utendaji kazi wa hospital ya mkoa wa Njombe Kibena huku akiwataka watendaji kuwahamasisha wagonjwa wote kuwa na bima ya afya.

“Niombe tuwahamasishe wagonjwa wetu wote wawe na bima ya afya kwa kuwa ukiangalia watumishi wa serikali wote tuna bima na sio kwamba tuna pesa hapana ila ni utaratibu tu uliowekwa na ukiaangalia watumishi ni asilimia 7 tu asilimia 93% ipo nje ya mfumo, hii itatuondolea mgogoro kwasababu wale wenye bima wote wanaenda hospital binafsi wale ambao tunasema hawana uwezo ndio wanakuja huku kwa hiyo tunataka kufanya mabadiliko kila mwenye bima aje hapa mtu awe na uhuru wa kuchagua lakini sio tu kuwa na huduma mbovu”alisema Dkt.Zainab

Winfrid Kiambile ni mganga mfawidhi wa hospital ya rufaa ya mkoa wa Njombe amesema hali ya watumia bima katika hospital hiyo ni nzuri kwa kuwa awali walikuwa wagonjwa 600 kwa mwezi lakini kwa sasa wamefikia 1200 mpaka 1300.

“Kwanza hali ya watoto kufariki kwa sasa imepungua sana ukilinganisha na awali kutokana na maboresho ya mazingira yetu mfano kwa kukarabati jengo la x-ray na kuleta mashine ya kisasa na mambo mengine mengi, lakini pia maambukizi yalisababisha watoto wengi kufariki kwa kweli kwa sasa kwa wiki watoto waliokuwa wakifariki walikuwa ni 12 mpaka 15 tofauti na sasa watoto 3 mpaka 5,kwa upande wa watumiaji bima wameongezeka sana kwa kuwa mwanzo tulianza na 600 na sasa hivi wamefika 1200 mpaka 1300 kwa mwezi”alisema Dkt.kiambile

Baadhi ya wagonjwa waliozungumza na mtandao huu hospitalini hapo wakiwemo akina mama wajawazito wanakiri kuridhishwa na huduma inayotolewa katika hospital ya kibena ikiwemo upatikanaji wa dawa huku wakiomba kuboreshewa upatikanaji wa maji kwani yamekuwa yakikatika mara kwa mara.

NEC Yatangaza Uchaguzi Mdogo Wa Udiwani Katika Kata 6

$
0
0
Na. Idara ya Habari-NEC
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza uchaguzi mdogo wa madiwani kwenye kata sita (6) zilizopo kwenye halmashauri sita (6) katika mikoa sita (6) ya Tanzania Bara.

Mwenyekiti wa Tume Jaji (Rufaa) Semistocles Kaijage amesema Jijini Dar es Salaam leo (Jumanne 09.04.2019) kwamba uchaguzi huo utafanyika tarehe 19 Mei mwaka huu.

Akisoma taarifa kwa umma iliyotolewa na Tume, Jaji Kaijage amesema kwamba fomu za uteuzi wa wagombea zitatolewa kati ya  tarehe  15  hadi tarehe 19, Aprili mwaka huu.

Aidha Mwenyekiti  huyo wa Tume amesema kwamba uteuzi wa wagombea pia utafanyika tarehe  19, Aprili mwaka huu na kampeni za uchaguzi zitafanyika kuanzia tarehe 20, Aprili hadi tarehe 18 Mei mwaka huu.

Alifafanua kwamba uchaguzi katika kata hizo, utafanyika sambamba  na Uchaguzi Mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Arumeru Mashariki.

“Tume inapenda kuvikumbusha Vyama vya Siasa na wadau wote wa Uchaguzi kuzingatia Sheria, Kanuni, Maadili ya Uchaguzi, Taratibu, Miongozo na Maelekezo yanayotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi wakati wa kipindi chote cha Uchaguzi huu mdogo,” alisema Jaji Kaijage.

Awali Jaji Kaijage alisema kwamba maamuzi ya kutangaza uchaguzi kwenye kata hizo yamefanyika baada ya Tume kupokea taarifa kutoka kwa Waziri mwenye  dhamana na Serikali za Mitaa ambaye kwa kutumia mamlaka aliyopewa chini ya Kifungu cha 13(1) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292 aliitaarifu Tume juu ya uwepo wazi wa nafasi hizo.

Alisema kwamba nafasi hizo wazi zimetokana na vifo vya Madiwani watano (5) na mmoja (1) kujiuzulu.

Kata hizo ni pamoja na Uwanja wa Ndege iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda Mkoani Katavi, Kitobo iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi Mkoani Kagera, Kyela iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Kyela Mkoani Mbeya, Mikocheni iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni Mkoani Dar es Salaam, Mvuleni iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Lindi Mkoani Lindi na Manda iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma.

Mwisho

Mbunge Mlinga ataka RC Makonda, Hapi, Mnyeti Gambo, wapewe Tuzo Kwa Utendaji Mzuri.....Waziri Jafo Amjibu

$
0
0
Mbunge wa Ulanga(CCM), Goodluck Mlinga ametaka wakuu wa mikoa na wilaya waliofanya vizuri katika utendaji wao kupewa tuzo za utendaji bora.

Mlinga amewataja baadhi ya wakuu mikoa kuwa ni Ally Hapi (Iringa), Mrisho Gambo (Arusha), Paul Makonda (Dar es Salaam) na Alexender Mnyeti (Manyara).

Hivyo, akahoji Wizara  ina mpango gani wa kuwaandalia motisha au Tuzo Wakuu hao wa Mikoa  na Wakuu wa Wilaya ambao wanafanya kazi vizuri.

 Swali hilo limejibiwa na Waziri wa Tamisemi, Selemani Jafo  ambapo amesema kuwa tayari suala hilo lipo katika ajenda za vikao vinavyoendelea kwani ni kweli anatambua juhudi zinazofanywa na baadhi ya wakuu wa mikoa na wakuu wilaya kwani kwa kiasi kikubwa matatizo mengi ya wananchi yamepungua. 


”Nikiri wazi kweli kuna wakuu wa mikoa hivi sasa wanaofanya kazi vizuri sana, ajenda ya kuwapa motisha kwa baadhi ya wakuu wa mikoa tumeshaanza kuifanya katika vikao vyetu, na juzi baadhi ya Wakuu wa Mikoa tumewapa vyeti kwa jinsi gani wanasimamia mambo ya serikali vizuri” amesema Jafo

Wimbo Mpya: Amini Ft. Linah - Nimenasa

$
0
0
Wimbo Mpya: Amini Ft. Linah - Nimenasa

Wimbo Mpya: Man Fongo - Longa

VIDEO: Harmonize Ft Yemi Alade - Show Me What You Got

$
0
0
VIDEO: Harmonize Ft Yemi Alade - Show Me What You Got

Serikali Kuanzisha Makumbusho Ya Wanamichezo

$
0
0
Na Shamim Nyaki – WHUSM,Dodoma.
Serikali imejipanga kuanzisha Makumbusho Maalum katika Uwanja wa Taifa ya kuhifadhi taarifa na picha za wanamichezo walioliletea Taifa heshima katika mashindano mbalimbali ya Kimataifa.

Hayo yamesemwa leo Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe.Juliana Shonza alipokuwa akijibu swali la msingi la Mhe.Ester Mahawe (Viti Maalum) kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM) aliyeuliza ni lini serikali itaandaa utaratibu wa kuwaenzi wanariadha nchini.

Mhe.Shonza alieleza kuwa Serikali inawatambua na kuwaenzi wanamichezo wote ambao wameletea nchi sifa kubwa wakiwemo Mwanariadha Filbert Bayi aliyevunja rekodi ya dunia ya mbio za mita 1500 mwaka 1974 ambaye ni Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania, Jumaa Ikanga mshindi wa Medali ya Shaba Mashindano ya All- Africa Games mwaka 1978 na Medali ya Fedha Michezo ya Olimpiki 1980 kwa mbio za mita 5000 hivi sasa ni Kocha wa Riadha wa Taifa Brunei.

“Kanuni ya mafanikio katika michezo popote duniani yanatokana na mwanamichezo mwenyewe kuonyesha juhudi binafsi za kujituma na kujipambanua kuwa bora miongoni mwa wanamichezo wengine,hivyo wanamichezo lazima waendelee na jitihada za kujituma.”alisema Mhe.Shonza.

Aidha, Mhe.Shonza alipojibu swali la nyongeza la Mhe.Anna Gidarya Mbunge Viti Maalum (CHADEMA) Mkoa wa Manyara aliyeuliza ni lini Serikali itaboresha miundombinu ya viwanja katika vyuo vya elimu ya juu, ameeleza kuwa suala la kuboresha miundombinu linahitaji ushirikiano kati ya Serikali na wadau hivyo amewataka waheshimiwa wabunge kuona changamoto hiyo na kuifanyia kazi.

Kesi ya Zitto Kabwe Yakwama Tena

$
0
0
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imepanga kusikiliza kwa siku mbili mfululizo kesi ya Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Zuberi Kabwe.

Kesi hiyo ya 'uchochezi' ya Jinai Na. 327 ya Mwaka 2018, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu aleo iliitwa kwa ajili ya kusikiliza ushahidi wa upande wa mashtaka, ambapo imeahirishwa hadi tarehe 24 na 25 Aprili 2019.

Uamuzi huo umetolewa na Hakimu Huruma Shaidi kutokana na upande wa mashtaka kwa mara nyingine kushindwa kumleta mahakamani shahidi wao kwa madai kwamba shahidi huyo yupo kwenye operesheni maalum ya Jeshi la Polisi.

Mawakili wa utetezi Wakili Peter Kibatala na Wakili Stephen Mwakibolwa hawakuwa na pingamizi kwa maombi ya shauri hilo kupangiwa tarehe nyingine.

Hakimu Huruma Shaidi amesema kwamba amepanga kusikiliza ushahidi wa kesi hiyo kwa siku mbili mfululizo ili imalizike kwa muda uliopangwa hivyo upande wa mashtaka uhakikishe unaleta mashahidi wake wake kwenye muda uliopangwa.

Inadaiwa kuwa Oktoba 28,2018 katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi za makao makuu ya Chama cha ACT Wazalendo, kiongozi huyo alitumia maneno yenye kuleta kuleta chuki miongoni mwa wananchi wa Tanzania dhidi ya Jeshi la Polisi.

Mbunge huyo alifikishwa Mahakama ya Kisutu kwa mara ya  kwanza, Novemba 2, 2018, kwa sasa bado Zitto anaendelea na dhamana.

Serikali Yanunua Mtambo Mkubwa wa Madini

$
0
0
Na Immaculate Makilika- MAELEZO
Serikali imenunua mtambo mkubwa wa madini ambao utasaidia kufanya utafiti wa madini, sambamba na kuwasaidia wachimbaji wadogo katika shughuli za madini nchini

Akizungumza  Bungeni leo jijini Dodoma, Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo alisema kuwa Serikali imefikia uamuzi huo kwa lengo kuunga mkono wachimbaji wadogo nchini kote wakiwemo wachimbaji wa kijiji cha Busiri wilaya ya Biharamulo.

Naibu Waziri Nyongo alisema kuwa ili  kuwasaidia wachimbaji wadogo nchini, Serikali  kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO)  imenunua mtambo mkubwa wa kumsaidia kufanya utafiti wa kina kwa kuchoronga miamba kwa bei nafuu ili kubaini mashapo zaidi na kuongeza uzalishaji.

Naibu Waziri, Nyongo aliongeza kuwa Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya biashara kwa wachimbaji wadogo ili wanufaike zaidi na kazi ya uchimbaji.

Wizara kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini inakamilisha uandaaji wa kitabu cha madini yapatikanayo Tanzania toleo la nne ambacho kitaonesha uwepo wa madini katika mikoa, wilaya  na vijiji, ambapo kitasaidia wachimbaji wadogo kutambua madini yaliyopo katika maeneo mbalimbali nchini pamoja na matumizi ya madini hayo.

Aidha, Wizara kupitia Mradi wa Usimamizi endelevu wa Raslimali Madini (SMMRP), inakamilisha kujenga vituo vya  umahiri katika wilaya ya Bukoba, Bariadi, Songea, Handeni, Musoma, Mpanda na Chunya ili kuwezesha wachimbaji wadogo kujifunza  kwa vitendo.

Waziri Mkuu: Mifuko Ya Plastiki Mwisho Juni Mosi

$
0
0
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema kuanzia Juni mosi mwaka huu, itakuwa ni marufuku kutengeneza, kuingiza, kuuza na kutumia mifuko ya plastiki kwa ajili ya kubebea bidhaa za aina yoyote na matumizi yake yatakoma ifikapo Mei 31, 2019.

“Hivi karibuni nimemwagiza Waziri anayesimamia masuala ya mazingira ikiwemo kuzungumza na wadau mbalimbali, ikiwemo wenye viwanda vya kutengeneza mifuko ya plastiki kwa ajili ya kuhakikisha jambo hili linatekelezwa kwa haraka.”

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumanne, Aprili 9, 2019) Bungeni jijini Dodoma, kwenye mkutano wa 15 wakati akihitimisha hoja ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2019/2020.

“Kuanzia sasa tunatoa fursa ya viwanda kubadilisha teknolojia, wauzaji kuondoa mzigo uliopo, Ofisi ya Waziri wa Nchi, Makamu wa Rais itajiandaa kutumia kanuni chini ya Sheria ya Mazingira ili kulifanya katazo hili kuwa na nguvu ya kisheria. Tunachukua hatua hii ili kulinda afya ya jamii, wanyama, mazingira na miundombinu dhidi ya athari kubwa zinazotokana na taka za plastiki,” amesema.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema Serikali inatambua kwamba kuna baadhi ya bidhaa lazima zifungwe kwenye vifungashio vya plastiki na kwamba vifungashio kwa bidhaa hizo havitapigwa marufuku.

“Kwa msingi huo, katika hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais, yatatolewa maelezo ya kina kuhusu katazo la vifungashio vya aina hii, hasa katika maeneo ya uzalishaji viwanda, sekta ya afya, na kilimo,” amesema.

Amesema ana imani kuwa utaratibu huo pamoja na kutunza mazingira, utatoa fursa ya kutengeneza ajira nyingi husasan za watu wa chini kupitia utengenezaji wa mifuko mbadala ya plastiki pamoja na kutumia kikamilifu fursa ya viwanda vya karatasi vilivyopo nchini ikiwemo cha Mgololo.

Amesema matumizi ya plastiki nchini yameendelea kuleta madhara makubwa ikiwemo vifo vya mifugo kwa kula plastiki, kuziba kwa mifereji, uchafuzi wa mazingira na kushindikana kwa kuozesha taka kwenye vituo vya kukusanya taka.

Bunge lilikubali kupitisha sh. 148,886,523,581/- kwa ajili ya Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake kwa mwaka 2019/2020. Kati ya hizo, sh. 86,290,355,000/- ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh. 62,596,168,581/- ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.

Vilevile, Bunge liliidhinisha sh. 124,182,537,600 kwa ajili ya Mfuko wa Bunge ambapo kati ya hizo 116,573,026,000/- ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh. 7,609,511,600/- ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.

(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,

Tume Ya Uchaguzi Haiwezi Kusimamaia Uchaguzi Wa Serikali Za Mitaa - Majaliwa ..... Asema Si Jukumu Lake Kwa Mujibu Wa Katiba Ya Tanzania

$
0
0
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Tume ya Taifa ya Uchaguzi haiwezi kusimamia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kama ambavyo imependekezwa na baadhi ya Wabunge.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumanne, Aprili 9, 2019) Bungeni jijini Dodoma, kwenye mkutano wa 15 wakati akihitimisha hoja ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2019/2020.

Alikuwa akijibu hoja iliyotolewa kwamba Uchaguzi wa Serikali za Mitaa usisimamiwe na Ofisi ya Rais- TAMISEMI na badala yake usimamiwe na Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Pia waliitaka Serikali ishughulikie jambo hilo mapema ili kuepuka usumbufu unaoweza kutokea.

Akitoa ufafanuzi wa hoja hiyo, Waziri Mkuu alisema Serikali inawashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa imani kubwa walioionesha kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ambayo ni huru, juu ya utekelezaji wa majukumu yake, na kuona umuhimu wa kuiongezea jukumu la kusimamia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Hata hivyo, Waziri Waziri Mkuu alisema, majukumu ya Tume hiyo, yameainishwa katika Ibara ya 74(6) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwa ni pamoja na kusimamia Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Hivyo, jukumu la kusimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa si miongoni mwa majukumu ya Tume kwa mujibu wa Katiba,” alisema.

Katika hatua nyingine, akizungumzia kuhusu uwekezaji kwenye zao la pamba, Waziri Mkuu alisema sekta ya pamba na mnyororo wake wote wa thamani ni sekta ya kipaumbele ambayo mbali na kuwahakikishia soko wakulima na kuongeza kipato chao, uwekezaji katika viwanda vya nguo unatengeneza ajira nyingi kwa vijana hivyo kuinua kipato chao na kuboresha maisha ya watu wengi.

“Kwa kutumia mkakati wa kuzalisha nguo na mavazi mbalimbali (Cotton to Clothing - C2C), Serikali itaendelea kuhamasisha uwekezaji wa viwanda kwa kutumia teknolojia za kisasa za kutengeneza nguo kuanzia kuchakata pamba hadi nguo kwa kuhakikisha kuwa taratibu zote zinafanyika nchini na msisitizo uwe kwenye utengenezaji wa nyuzi,” alisema.

Alikuwa akijibu hoja iliyotolewa kwamba bado zao la pamba halijatumiwa vizuri katika kuongeza pato la Taifa na kuinua maisha ya Watanzania.  Pia Wabunge walitaka Serikali ijizatiti kusimamia uwekezaji kwenye kilimo cha zao la pamba ili kufanikisha utekelezaji wa mkakati wa viwanda vya nguo nchini wa kufikia malengo ya kuwa Taifa lenye uchumi wa kati. 

Wakati huohuo, Waziri Mkuu alisema Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi mwaka 2017, ilifanya tathmini ya kina na kuandaa Blueprint ambayo imebainisha masuala yote muhimu yanayokwamisha uwekezaji na kuainisha maeneo yote muhimu yayohitaji kurekebishwa ikiwemo sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia uwekezaji nchini kwa kila taasisi.

Alikuwa akijibu hoja kuhusu umuhimu wa Serikali kufanya tathmini na kuangalia vikwazo vinavyokwamisha harakati za uwekezaji nchini, kutunga sheria mpya, kurekebisha baadhi ya sheria ili kuendana na mahitaji ya Blueprint.

Alisema sambamba na hatua hiyo, huduma zimeimarishwa kwa kuanzisha mifumo ya kielektroniki ambapo wawekezaji wataweza kufanya maombi ya vibali mbalimbali wakiwa popote bila kulazimika kufika kituoni.

“Mifumo hii itaondoa urasimu na kuharakisha utoaji wa vyeti vya uwekezaji, leseni na vibali mbalimbali. Hatua hizi zitapunguza gharama na muda wa mwekezaji kufuatilia vibali na leseni kwa kila taasisi,” alisema.

Alisema, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) hivi sasa kina ofisi saba za kanda ambazo ni Mwanza, Dodoma, Moshi, Kigoma, Mtwara, Mbeya na Dar es Salaam ambazo zimeanzishwa kwa lengo la kusogeza huduma karibu na wawekezaji.

Bunge lilikubali kupitisha sh. 148,886,523,581/- kwa ajili ya Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake kwa mwaka 2019/2020. Kati ya hizo, sh. 86,290,355,000/- ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh. 62,596,168,581/- ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.

Vilevile, Bunge liliidhinisha sh. 124,182,537,600 kwa ajili ya Mfuko wa Bunge ambapo kati ya hizo sh. 116,573,026,000/- ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh. 7,609,511,600/- ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.

(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Jumatano ya April 10

Tasnia Ya Ngozi Yawekewa Mikakati Ya Kuongezewa Thamani

$
0
0
Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imesema imeweka mipango maalum ya kuboresha tasnia ya ngozi hapa nchini ili kuiongezea thamani kwa kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa zinazotokana na ngozi kupitia viwanda villivyopo hapa nchini.

Akizungumza na wadau wa sekta ya ngozi jijini Dar es Salaam (09.04.2019) katika ofisi ndogo za Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel, amesema wizara imekuwa ikihakikisha inasikiliza na kuelewa changamoto, ushauri na fursa wanazokutana nazo wadau wa sekta mbalimbali ili wizara iweze kutekeleza kwa kasi yale yenye tija kwa ukuaji wa uchumi wa nchi.

“Ni lazima tuhakikishe tunaongeza thamani katika bidhaa zetu za ngozi, hili ni jambo kubwa ambalo tutakuwa tumeunga mkono azma ya serikali ya awamu ya tano ya uchumi unaoendana na kukua kwa viwanda ili tasnia ya ngozi ipate viwanda vingi, ni vyema tuongeze thamani badala ya kuuza ngozi tuuze bidhaa zitokanazo na ngozi.” Amesema Prof. Gabriel

Prof. Gabriel amewataka pia watanzania kubadili fikra kwa kutumia bidhaa za ngozi zinazotengenezwa hapa nchini kwa kuwa zina bei nafuu na zinadumu kwa muda mrefu ili wazalishe wawe na soko kubwa la ndani kabla ya kuuza  nje ya nchi huku akiwataka pia watengenezaji wa bidhaa hizo kutengeneza zenye ubora zaidi ili ziweze kupata masoko ya uhakika.

Aidha katibu mkuu huyo amesema ni vyema yawepo maboresho ya mitaala ili kupata wataalam wa ngozi ambao watawasaidia wadau na wananchi katika nyanja mbalimbali zihusuzo tasnia ya ngozi yakiwemo masoko.

Ili tasnia ya ngozi izidi kukuza uchumi wa taifa Prof. Gabriel amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekuwa ikihakikisha inasimamia ubora wa ngozi ya ng’ombe kuanzia kwenye mbegu bora ya ng’ombe inayoweza kuzalisha ngozi bora.

“Katika wizara yetu hatushughuliki tu na mnyama ambaye tayari amezaliwa anakaribia kuchinjwa sisi tunaanza na mbegu yenyewe kwanza ili kuhakikisha mnyama anayezaliwa anakuwa na ngozi bora na kuhakikisha anatunzwa au kutayarishwa ili atoe ngozi bora.”

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Chama cha Wadau wa ngozi nchini Bw. Joram Wakari amesema tasnia ya ngozi imekuwa na changamoto kadhaa ambazo tayari Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekuwa ikizitatua hivyo kuiomba wizara kuzidi kusimamia tasnia ya ngozi ili iweze kuchangia kwa kiasi kikubwa uchumi wa taifa.

Baadhi ya wadau walioshiriki katika mkutano huo wameishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa jitihada ambazo viongozi wake wamekuwa wakifanya kwa kukutana na wadau wa sekta mbalimbali kwa lengo la kuhakikisha wanapata maoni na ushauri wa namna ya kuendeleza sekta hizo kwa kushirikiana na wananchi.

Mwisho.

Waziri Mpango: Tanzania Kutetea Maslahi Yake Katika Mikutano Ya Benki Ya Dunia Na IMF- Washington DC

$
0
0
Na Benny Mwaipaja, Washington DC
WAZIRI wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango, ameongoza ujumbe wa Tanzania kwenye mikutano ya kipupwe(Spring Meetings)  ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) inayofanyika mjini Washington DC, Marekani.

Akizungumza kwenye Ofisi za Ubalozi wa Tanzania Mjini Washigton DC, Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, amesema kuwa ujumbe wa Tanzania unaojumuisha pia wajumbe kutoka Serikali ya Mapinduzi-Zanzibar, utasimamia maslahi ya pande zote mbili za Muungano.

Mikutano hiyo inatoa fursa kwa Mawaziri wa Fedha na Magavana wa Benki Kuu kutoka katika nchi wanachama ambao pia mi Magavana wa Benki ya Dunia na IMF, kujadili maendeleo na changamoto mbalimbali zilizojitokeza katika utekelezaji wa masuala mbalimbali ya maendeleo na ushirikiano.

Aidha Mikutano hiyo hutoa fursa kwa nchi kushiriki kama mwanahisa kwenye mikutano ya kiutawala (Board of Governors) ya Taasisi hizo mbili ambapo maamuzi ya kiuendeshaji na kisera hufanyika

Tanzania itapata fursa ya kushiriki kwenye Kamati Maalum za Benki ya Dunia na IMF na baadhi ya mikutano hiyo ni Mkutano wa Mawaziri wa Fedha inayoshughulikia sera na utulivu wa Sekta ya fedha (International Monetary Committee and Finance Committee-IMFC

Dkt. Mpango atashiriki katika majadiliano na viongozi wa juu wa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF wanaoshughulikia masuala ya Afrika kuhusu utekelezaji wa program za sera za kiuchumi, mikopo nafuu na misaada ya kitaalam kwa Tanzania.

Mazungumzo hayo yatajikita kwenye maeneo ya mwenendo wa uchumi wa dunia; miradi ya maendeleo iliyopendekezwa na Benki ya Dunia kwa mwaka 2019/20, kujenga uwezo wa rasilimali watu, mahitaji ya kujenga uchumi wa kidijitali na maeneo mengine ambayo Benki ya Dunia inaweza kusaidia kupatikana mikopo nafuu  ya kugharamia miradi ya kipaumbele hasa reli na umeme.

Waziri wa Fedha pia anatarajia kupata fursa ya kukutana na Taasisi na mashirika mbalimbali ya kimataifa, washirika wa maendeleo na wawekezaji wenye nia ya kuwekeza katika sekta mbalimbali nchini.

Dkt. Mpango pia ameihakikishia Jumuiya ya Kimataifa na watanzania kwa ujumla kwamba Tanzania inafanya vizuri kiuchumi na kijamii na kumpongeza Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Wilson Masilingi, kwa jitihada kubwa anazozifanya kuitangaza nchi na kusukuma mbele agenda za nchi

Kwa Upande wake, Balozi Wilson Masilingi, akiukaribisha ujumbe wa Tanzania nchini Marekani, amebainisha kuwa yeye na timu yake wamejipanga kuhakikisha ushiriki wa nchi katika mikutano hiyo unakuwa mzuri na wenye manufaa na mafanikio kwa Taifa.

Mwisho

Waziri Mkuu: Wakandarasi Wa Maji Wamelipwa 138bn....Asema Sh. Bilioni 44 Zinaandaliwa Kuwalipa Wengine

$
0
0
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema hadi sasa, Serikali imeshahakiki madai ya wakandarasi waliotekeleza miradi ya maji nchini na imewalipa shilingi bilioni 138.

“Hivi karibuni tutalipa fedha nyingine kiasi cha shilingi bilioni 44. Ninaielekeza Wizara husika ihakikishe kuwa watendaji wa Serikali wanafuatilia ufanisi wa wakandarasi na wajiridhishe kuwa wakati wote unakuwa wa kiwango cha kuridhisha,” amesema.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo jana (Jumanne, Aprili 9, 2019) Bungeni jijini Dodoma, kwenye mkutano wa 15 wakati akihitimisha hoja ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2019/2020.

Alisema wakati wa michango yao, Waheshimiwa Wabunge walizungumzia upatikanaji wa maji katika maeneo mbalimbali nchini sambamba na baadhi yao walikosoa utekelezaji na ubora duni wa baadhi ya miradi ya maji. Alisema wengine walionesha kutoridhishwa na utekelezaji huo kwani baadhi ya maeneo hayajafikiwa na miradi hiyo.

Waziri Mkuu alisema licha ya changamoto hizo, Serikali inaendelea na usambazaji wa maji, na itachukua hatua stahiki kuhakikisha kuwa miradi yote ya maji inayotekelezwa, inatoa matokeo yaliyokusudiwa.

“Kwa kuanzia, Mheshimiwa Rais aliunda tume maalum ili kupitia, kufanya tathmini na kutoa mapendekezo juu ya hatua za haraka zinazostahili kuchukuliwa, kwa lengo la kuhakikisha thamani ya fedha kwa miradi hiyo inapatikana na kuleta tija,” alisema.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alisema changamoto nyingine katika eneo la maji ni uharibifu wa mazingira ambao umeshika kasi kubwa na kwamba hatua za haraka hazina budi kuchukuliwa ili kuiepusha nchi na janga la ukame.

“Katika kuhakikisha kuwa tunaondokana na janga hili, Bunge lilipitisha Sheria ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira ya Mwaka 2019 yenye lengo la kuimarisha mfumo wa utoaji huduma za maji na usafi wa mazingira nchini.”

Alisema sheria hiyo pia itaongeza uwajibikaji katika utoaji wa huduma ya maji; kuleta uendelevu kwa miradi ya maji vijijini; kuimarisha ujenzi, usimamizi na uendeshaji wa miradi ya maji baada ya kuundwa kwa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA).

“Nawaagiza viongozi wote kuanzia ngazi ya vijiji, wachukue hatua za makusudi katika kusimamia utunzaji wa vyanzo vya maji na kudhibiti vitendo vya uharibifu wa mazingira. Viongozi na watendaji watakaobainika kutosimamia ipasavyo sheria husika, hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi yao. Nawaomba Waheshimiwa Wabunge muunge mkono jitihada hizi za Serikali,” alisisitiza.

Bunge lilikubali kupitisha sh. 148,886,523,581/- kwa ajili ya Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake kwa mwaka 2019/2020. Kati ya hizo, sh. 86,290,355,000/- ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh. 62,596,168,581/- ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.

Vilevile, Bunge liliidhinisha sh. 124,182,537,600 kwa ajili ya Mfuko wa Bunge ambapo kati ya hizo sh. 116,573,026,000/- ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh. 7,609,511,600/- ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.

(mwisho)

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live




Latest Images