Quantcast
Channel: MPEKUZI
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live

Rais Magufuli Kuanza Ziara Ya Kikazi Mkoani Mtwara.

$
0
0
Na Bakari Chijumba, Mtwara.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mh.Dkt.John Pombe Magufuli, anatarajia kufanya ziara ya kikazi mkoani Mtwara kuanzia 02 April hadi April 04, Mwaka huu wa 2019 .

Akizungumza na wanahabari leo Jumamosi 30 Machi 2019, mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa amesema katika ziara hiyo Rais Magufuli atazindua na kuweka mawe ya msingi katika miradi mbalimbali ya maendeleo.

Amesema ataweka jiwe la msingi la upanuzi wa uwanja wa ndege wa Mtwara na lingine la ujenzi wa barabara ya Mtwara-Mnivata (Km 50),pia ataweka jiwe la msingi kwenye kiwanda cha kubangua korosho cha Yalin kilichopo Msijute na ataweka pia jiwe la msingi katika chuo cha ualimu cha Kitangali.

Mh.Byakanwa amesema licha ya kuweka mawe ya msingi katika miradi mbalimbali, Rais Magufuli atazindua kituo cha afya cha Mbonde wilayani Masasi na barabara ya Mangaka-Mtambaswala na pia Mangaka -Nakapanya iliyojengwa kwa kiwango cha lami.

"Miradi inayozinduliwa ni mikubwa ambayo itasaidia kuchochea kukua kwa uchumi wa Mtwara na kwa uchumi wa Mtwara na nchi kwa ujumla na pia ni miradi ambayo kwa Mtwara ina tija kubwa sana, hivyo amewaomba wananchi wajitokeze kwa wingi katika maeneo yote yenye miradi ya maendeleo itakayozinduliwa ili kumsikiliza Mh.Rais" amesema   Mkuu wa mkoa huyo wa Mtwara.

Hii ni ziara ya pili kwa Rais Magufuli kutembelea Mkoa wa Mtwara tangu alipoapishwa kuwa Rais mwaka 2015, ambapo safari hii anatarajia kuzunguka katika wilaya zote za Mkoa huu.

Lugola Atangaza Vita Dhidi Ya Matrafiki Wala Rushwa Akifungua Kongamano La Taifa La Usalama Barabarani

$
0
0
Na Felix Mwagara, MOHA.
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amewataka Askari Polisi Kikosi cha Usalama barabarani nchini, kusimamia sheria kikamilifu na kujiepusha na vitendo vya rushwa ili kuokoa maisha ya watu wasio na hatia ambao hufariki, kupata ulemavu wa kudumu kutokana na ajali.

Akizungumza kabla ya kulizindua kongamano la kitaifa la wadau wa usalama barabarani nchini, Lugola ambaye pia alikuwa mgeni rasmi katika kongamano hilo, alisema wasimamizi wa Sheria wakisimamia sheria kikamilifu na elimu ikaendelea kutolewa kwa watumiaji wengine wa barabarani na wakabadili tabia zao, uwezekano wa kupunguza ajali zaidi ni mkubwa.

“Usalama Barabarani unaanza na kila mmoja wetu, nawaomba sana tutumie fursa hii kikamilifu kwa kutoa mawazo na maoni yetu katika kongamano hili kwa manufaa na mustakabali wa Usalama wetu hivi sasa na vizazi vijavyo,” alisema Lugola.

Pia aliwataka wadau hao, watumie fursa ya kongamano hilo kuzungumza kwa uwazi, kutoa mawazo yao ambayo yanalenga kuboresha utendaji wa Baraza Usalama Barabarani na vyombo vingine ambavyo vinasimamia Sheria ya Usalama Barabarani.

Lugola alisema Lengo la Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ni kutokomeza ajali za barabarani nchini, hivyo aliwataka wadau wa usalama barabarani wajipange kikamilifu kwa kiuweka mikakati thabiti kwa lengo la kutokomeza ajalin nchini.

“Ni wazi kwamba wasimamizi wa Sheria wakisimamia sheria kikamilifu na elimu ikaendelea kutolewa kwa watumiaji wengine wa barabarani na wakabadili tabia zao, uwezekano wa kupunguza ajali zaidi ni mkubwa,” alisema Lugola.

Pia Waziri Lugola alilitaka Baraza la Usalama barabarani kusimamia utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Baraza Awamu ya Nne, ambao umezinduliwa Waziri huyo ameuzindua na Muongozo wa Utendaji na Utekelezaji wa majukumu ya Kamati za Usalama Barabarani za Mikoa na Wilaya ili kudhibiti ajali za Barabarani na Kuimarisha Utendaji wa Kamati.

Lugola pia aliwataka kusimamia ukaguzi wa magari ili Kuhakikisha Magari mabovu yanaondoka barabarani, na Baraza likamilishe Uundwaji wa Kamati za Usalama Barabarani za Mikoa na Wilaya haraka ili Kamati hizo zianze kazi ili kwenda na Mabadiliko yanayofanyika ndani ya Baraza.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza Taifa la Usalama Barabarani, Mhandisi Hamad Masuani alisema takwimu za usalama barabarani zimepungua nchini kutokana na Baraza lake kuweka mikakati za kupambana na ajali nchini.

Kongamano hilo ni mbadala wa Wiki ya Nenda kwa usalama barabarani ambayo kila mwaka ufanyika katika mkoa ambao uchaguliwa na wajumbe wa Baraza hilo.

Uteuzi Mpya Uliofanywa na Rais Magufuli Lro Jumapili March 31

$
0
0
Rais wa Tanzania, John Magufuli amemteua Adolf Ndunguru kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango anayeshughulikia sera.

Taarifa  iliyotolewa leo Jumapili Machi 31, 2019 na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu imesema Ndunguru ameteuliwa kushika nafasi hiyo kujaza nafasi iliyokuwa wazi.

Imesema kabla ya uteuzi huo, Ndunguru alikuwa Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Kufuatia Uteuzi huo, Rais Magufuli amemteua Msafiri Lameck Mbibo kuwa Naibu Kamishna Mkuu wa TRA.

Kabla ya uteuzi huo, Mbibo alikuwa Meneja wa TRA Mkoa wa Kilimanjaro.

Uteuzi wa viongozi hao umeanza leo Jumapili Machi 31, 2019.

NEC Yatangaza Tarehe Ya Uchaguzi Jimbo la Joshua Nassari

$
0
0
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema uchaguzi mdogo katika jimbo la Arumeru Mashariki ni Mei 19, 2019.

Mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage akizungumza na waandishi wa habari leo Jumapili Machi 31, 2919 mkoani Morogoro amesema tume ilipokea barua kutoka kwa Spika wa Bunge la Tanzania ambaye kwa kuzingatia kifungu cha 37(3) cha sheria ya taifa ya uchaguzi aliitaarifu Tume kuwepo kwa nafasi wazi ya ubunge katika jimbo hilo.

“Nafasi ya jimbo la Arumeru ipo wazi na imetokana na aliyekuwa mbunge Joshua Samwel Nassari kupoteza sifa ya kuwa mbunge kutokana na kutohudhuria mikutano mitatu ya Bunge mfululizo bila ruhusa ya Spika,” amesema Jaji Kaijage

Amesema amevitaka vyama vya siasa na wadau wote wa uchaguzi kuzingatia sheria, kanuni, maadili ya uchaguzi, taratibu, miongozo na maelekezo ya uchaguzi wakati wa kipindi cha uchaguzi mdogo.

Machi 14, 2019 Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai alimuandikia barua Mwenyekiti wa NEC, Jaji Kaijage kumtaarifu jimbo la Arumeru Mashariki lipo wazi kutokana na kutohudhuria vikao vya mikutano mitatu mfululizo.

CAG akabidhi ripoti 17 za ukaguzi kwa Rais Magufuli

$
0
0
Ripoti 17 za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad, kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 30, 2018 zimekabidhiwa rasmi kwa Rais Dk. John Magufuli.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Dar es Salaam na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT), ripoti hiyo imewasilishwa na CAG katika hafla fupi iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam juzi na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka ofisi hiyo.

CAG alimkabidhi Magufuli ripoti ya Ukaguzi wa Serikali Kuu, Ripoti ya Ukaguzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, Ripoti ya Ukaguzi wa Mashirika ya Umma na Ripoti ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo.

Pia alikabidhi Ripoti ya Ukaguzi wa Mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Ripoti ya Ukaguzi wa Ufanisi na ripoti 11 za ukaguzi wa ufanisi katika sekta mbalimbali.

Sekta hizo ni pamoja na usimamizi wa shughuli za ujenzi wa miradi ya umwagiliaji, usimamizi wa miradi ya maji vijijini, usimamizi wa miradi ya maji itokanayo na visima virefu.

Nyingine ni matengenezo ya mitambo ya kuzalisha umeme, usimamizi wa elimu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu, usimamizi wa mfumo wa ununuzi wa magari ya Serikali kwa pamoja pia sekta ya ufuatiliaji wa shughuli za ujenzi na majengo ya mijini, usimamizi wa utoaji wa huduma za afya za rufaa na dharura kwa hospitali za rufaa ngazi ya juu, upatikanaji na usambazaji wa pembejeo za kilimo, usimamizi wa utoaji wa huduma ya bima ya afya na ufuatiliaji wa mapendekezo ya ukaguzi wa ufanisi.

Akizungumza baada ya kupokea ripoti hiyo, Magufuli aliipongeza ofisi ya CAG kwa kazi nzuri inayofanya na pia kuahidi kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nao kwa karibu na katika kukabiliana na kudhibiti matumizi mabaya na upotevu wa fedha za umma.

Kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania Ibara ya 143 kifungu kidogo 2 na 4, kinamtaka CAG kukabidhi ripoti hizo kwa Rais kabla ya Machi 31, kila mwaka na baada ya hapo zinawasilishwa bungeni siku saba za mwanzo za kikao cha Bunge kinachofuata.

DC Jokate Mwegelo Amuomba Radhi Pierre Liquid

$
0
0
Baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda kumkosoa Mchekeshaji aliyejizolea umaarufu kwenye vyombo vya habari pamoja na mitandao, Pierre Maarufu kama Mzee wa Liquid ,Mkuu wa wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo amemuomba Radhi kwa tukio hilo.

 
Katika hafla iliyoandaliwa na Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo yenye malengo ya kutokomeza Zero katika wilayani humo, Makonda alisema kwamba watu wa 'hovyo' kama Pierre hawapaswi kupewa nafasi kwenye vyombo vya habari.

"Wakina mama kama hawa wanaojituma na kuhangaika kwa ajili ya watoto, wao ndio tuwape kipaumbele, sio hawa walevi walevi kama akina Pierre. Yaani unakuwa na taifa ambalo watu wa hovyo ndio wanakuwa maarufu”, Alisema Paul Makonda.


Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya Jokate kupitia ukurasa wake Instagram amemuomba Radhi Pierre na kumkaribisha Kisarawe ikiwa ni pamoja na kumpatia fursa ya kutengeneza samani za shule mpya inayotegemewa kujengwa katika Wilaya hiyo. 

==Haya ni Maneno ya Jokate

"Hakuna maneno Muhimu na Machache katika ustawi wa maisha ya Binadamu kama Tafadhali, Asante na Samahani.

Katika Dhifa niliyoiandaa jana, nilialika watu wengi, Wanasiasa, Taasisi za Kiserikali, Mabalozi, Wafanyabiashara, Wajasiriamali, Wasanii, Wadau wa Burudani N.k.

Na Makusudio ya yote hayo wote tunayajua, ni kutafuta MOTISHA juu ya ELIMU ya Mtoto wa kike, Kisarawe na kote nchini.
Na kwangu mimi na Wilaya nzima ya Kisarawe wote waliofika jana ni muhimu sana sana kwangu na kwetu.

Kipekee kabisa nimshukuru @officialpiere_liquid wako watu maarufu wengi mno tuliowaalika lakini hawakufika. Ila wewe ulichukua muda wako kuhamamisha na kufika na zaidi ya hapo ukatoa mchango wa TSH LAKI MOJA!!! Hukuja kuuza sura tu!! Nasema ASANTE SANA.

Wana Kisarawe tunakupenda na tunakukaribisha kuwekeza Kisarawe uanzishe hata mgahawa tutakusaidia kupata eneo. Lakini pia nimesikia ni mtengeneza mzuri sana wa furniture. Hii Shule tunayoenda kujenga inahitaji madawati Naomba tufanye kazi nawewe katika hii fursa. Tuangalie namna japo kidogo tukuwezeshe.

Tunasema Karibu Kisarawe Ukae. Kisarawe Kunogile. Tunasema Samahani kwa kukwazika lakini zaidi Asante Sana kwa kushiriki kwenye #TokomezaZeroKisarawe
#ElimuItabakiKuwaJuuKileleni
 #KisaraweMpya

Ubarikiwe!!!" - DC Jokate Mwegelo

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Keo Jumatatu ya April 1

Dudu Baya aiomba radhi familia ya Ruge Mutahaba

$
0
0
Msanii wa Bongo Fleva, Dudu Baya ameipigia magoti familia ya aliyekuwa Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji, Ruge Mutahaba akiomba radhi kwa maneno ya kashfa aliyoyatoa dhidi ya nguli huyo katika tasnia ya habari wakati wa msiba.

Dudu Baya ametumia mtandao wa Instagram kuomba familia ya marehemu,  Serikali pamoja na Watanzania kwa ujumla kwa alichokifanya wakati wa msiba huo.

“Nachukua fursa hii kuomba radhi ikiwa ni mwezi wa Kwaresma, mwezi wa kuomba msamaha na mwezi wa kusamehe, naomba msamaha kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Baraza la Sanaa la Taifa na jamii nzima ya Watanzania, na Familia [ya Marehemu Ruge] na watu wote walioguswa kwa maneno ya dhihaka niliyoyatoa wakati msiba ulipotokea,” amesema Dudu Baya.

“Naomba msamaha kwa moyo wa unyenyekevu nikiamini Mwenyezi Mungu amenisamehe, na watu wote niliowakosea naomba mnisamhe,” ameongeza.

Dudu Baya alitoa maneno ya kashfa dhidi ya Marehemu Ruge, hali iliyosababisha Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe kuliagiza jeshi la polisi pamoja na Basata kumchukulia hatua.

Msanii huyo alijisalimisha katika kituo cha polisi cha Oysterbay jijini Dar es Salaam ambapo aliachiwa kwa dhamana baada ya siku kadhaa na amekuwa akiendelea kuripoti katika kituo hicho.

Basata walichukua hatua ya kusimamisha leseni yake ya sanaa, hali inayomfanya kutofanya kazi yoyote ya muziki.

Spika Ndugai: Hatukunufaika na madini, haikuwa ajenda ya Kitaifa

$
0
0
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugani, amesema awali, Taifa halikunufaika na rasilimali madini kwa kuwa sekta hiyo haikuwa ajenda ya Kitaifa.
 
“Madini yaliachwa kwa wabunge ambao rasilimali hiyo inapatikana kwenye maeneo yao, haikuwa ajenda ya taifa, wengine walizungumzia zaidi masuala yanayowagusa kama korosho, pamba na mambo mengine, nashukuru tumefanya mabadiliko na sasa matokeo yameanza kuonekana,” amesema Spika Ndugai.
 
Amesema  kwa mwelekeo wa sasa, serikali imefika mahali ambapo manufaa ya rasilimali hiyo yameanza kuonekana kutokana na  mageuzi makubwa yaliyofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli na kumpongeza kutokana na namna anavyohakikisha rasilimali madini inalinufaisha taifa, na kuongeza, “kilio cha watanzania cha kutokunufaika na madini kimepata mwenyewe, Rais Magufuli amefanya uthubutu”.
 
Spika Ndugai ameyasema hayo Machi 30, 2019, wakati akifungua Semina kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini na baadhi ya Wenyeviti wa Kamati nyingine za bunge wanaohudhuria semina ya siku mbili jijini Dodoma, iliyoandaliwa na Wizara ya Madini kwa lengo la kutoa elimu ili kupata uelewa wa sekta ya madini.
 
Amesema, awali, ikijulikana kama Wizara ya Nishati na Madini ilikuwa ni kazi hata kwa bunge hilo kupitisha Bajeti ya wizara hiyo kutokana na kwamba, sekta zote mbili nishati na madini   hazikuwa zikilinufaisha taifa na kusema, “ kulikuwa na kutokuridhika na sekta zote na hususan madini, kama taifa tulikuwa hatupati haki yetu tuliyoistahili”.
 
Kufuatia hali hiyo, Spika Ndugai amewataka Wabunge  na wananchi kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Rais Magufuli  kwa kuwa  mchango wa sekta ya madini katika uchumi wa taifa utasaidia kusogeza mbele maendeleo ya taifa na watu wake.
 
Aidha, amewaasa viongozi wote waliobeba dhamana ya kusimamia sekta husika kuhakikisha wanaichukulia dhamana waliyopewa kwa uzito wa kipekee  ili kuliwezesha taifa kufanana na nchi nyingine ambazo zimeendelea kutokana na rasilimali madini.
 
Pia, amepongeza mabadiliko yanayofanywa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na kueleza kwamba anafurahi kusikia STAMICO mpya tofauti na ilivyokuwa awali.
 
Akizungumzia Kamati mbili zilizoundwa na bunge kuchunguza biashara ya madini ya Tanzanite na Almasi, amesema kuwa, kamati hizo zilifanya kazi nzuri na kwamba  bunge litaendelea kuishauri serikali  ili kuhakikisha sekta  ya madini inazidi kuchangia zaidi katika uchumi wa taifa.
 
Ameongeza kuwa, ripoti hizo zilipokelewa vizuri na serikali na kwamba juhudi zilizochukuliwa zimewezesha uanzishwaji wa masoko ya madini huku STAMICO ikifanya mabadiliko makubwa.
 
Kwa upande wake, Waziri wa Madini Doto Biteko akizungumza katika semina hiyo, amesema  sekta ya madini ni muhimu kwa uchumi wa taifa la Tanzania na kueleza kuwa, mchango wa taifa umeendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka na kueleza kuwa, mwaka 2017, sekta hiyo ilichangia asilimia 4.8 kwenye pato la taifa ikilinganishwa na asilimia 4.0 mwaka 2015.
 
Akizungumzia ukuaji wa sekta hiyo amesema umeongeza kwa kasi kutoka asilimia 9.0 mwaka 2015 kufikia 17.5 mwaka 2017, na kusema mafanikio hayo yametokana na juhudi za serikali kuhakikisha sekta hiyo inachangia zaidi  ili kufikia lengo la asilimia 10 ya mchango wake ifikapo mwaka 2025.
 
Akizungumzia marekebisho ya Sheria ya Madini yaliyofanywa mwaka 2017,  na usimamizi wa Rasilimali Madini, amesema umewezesha ongezeko la makusanyo ya maduhuli yatokanayo na shughuli za madini kutoka Shilingi bilioni 194 iliyotarajiwa kukusanywa mwaka 2017/18 hadi shilingi bilioni 301.29 sawa na asilimia 154.999 ya lengo la makusanyo kwa mwaka huo.
 
“Mhe. Spika, mwenendo wa ukusanyaji maduhuli kwenye sekta hii kwa mwaka 2018/19 ni wa kuridhisha ambapo hadi Februari kiasi cha shilingi 218,650,392 kimekusanywa hii ikiwa ni sawa na asilimia 105.6,” amesema Waziri Biteko.
 
Ameeleza kuwa, miongoni mwa sababu zilizopelekea mafanikio hayo ni pamoja na kuongezeka kwa mrabaha  kwa baadhi ya madini, kuanzisha kodi  mpya  ya ukaguzi ya asilimia 1; kuimarisha udhibiti wa utoroshaji wa madini; na kwa kushirikiana na wananchi  na vyombo vya ulinzi na usalama na kuzuia usafirishaji wa madini ghafi ya nje ya nchi ili  viwanda vya kusafishia na kuongeza ubora wa madini vijengwe  nchini.
 
Akizungumzia usimamizi wa shughuli za madini ya Tanzanite baada ya kukamilika kwa ukuta unaozunguka machimbo ya tanzanite Mirerani amesema udhibiti wa madini hayo umeimarika  na kusababisha kuongezeka kwa ukusanyaji wa maduhuli yatokanayo na madini hayo
 
Ameongeza kuwa, kufuatia juhudi hizo, ukusanyaji wa maduhuli kutokana na uzalishaji wa tanzanite kwa wachimbaji wa Wadogo na Kati uliongezeka hadi kufikia shilingi 1,436, 427, 228.99 kwa mwaka  2018, ikilinganishwa na  shilingi 71,861,970 kwa mwaka 2016.
 
“Uzalishaji umeongezeka kutoka migodi midogo na ya kati hadi kufikia kilo 781.204 kwa mwaka 2018 ikilinganishwa na kilo 147.7  zilizoripotiwa  kwa mwaka 2017 na kilo 164.6 za mwaka 2016,” amesema Waziri Biteko.
 
Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Dustan Kitandula, ameishukuru Wizara kwa kuandaa semina hiyo kwa wabunge na kueleza kuwa, kamati hiyo itaendelea kupata uelewa kuhusu sekta ya madini.
 
Mbali na wabunge, wengine wanaoshiriki semina hiyo ni Wenyeviti wa Bodi za taasisi za zilizo chini ya wizara, Wataalam kutoka wizarani na taasisi zake.

Serikali Kujenga Mradi Mkubwa Wa Maji Utakaogharimu Usd Milioni 13.5 Mjini Njombe Kupunguza Changamoto Ya Maji Miaka 20 Ijayo

$
0
0
Na Amiri kilagalila
Mamlaka ya Maji Njombe Mjini NJUWASA imesema  kufuatia kuwepo kwa Changamoto ya Maji ndani ya Mji wa Njombe Serikali inamkakati wa Kujenga Mradi Mkubwa wa Maji kwa Ufadhili wa Serikali ya India ili kuhakikisha kuwa Wananchi wanapata Huduma ya uhakika na ya kudumu.

Akiwa katika ziara ya kutembelea Vyanzo mbalimbali vya Maji vinavyohudumia mji Wa Njombe kikiwemo chanzo kipya cha Mto Hagafiro kinachotarajiwa kujengwa,Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya maji Njombe Mjini Mhandisi John Mtyauli amesema kuwa kuanzishwa kwa chanzo hicho kipya kutasaidia kupunguza changamoto ya upatikanaji wa Maji ndani ya mji huo ambao kwa sasa Asilimia kubwa huduma hiyo imekuwa ikitolewa kwa mgao.

"Hiki ni chanzo cha mto hagafiro wenye dhamira,chanzo hiki kipo umbali kama wa km 8 kutoka Njombe mjini kwa hiyo hiki ni chanzo kinachotegemewa kwa maana ya kujenga mradi mkubwa wenye dhamira ya kukidhi mahitaji ya maji kwa wakzi wa mji wa Njombe kwa sasa na baada ya miaka 20 ijayo

"Chanzo hiki kilianza kufanyiwa kazi tangu mwaka 2010 na serikali ilianza kuhangaika kutafuta fedha kupitia wadau na kwa sasa katika bajeti ya mwaka 2018-2019 Njombe ni moja miji iliyoweza kupata fedha na wizara imetafuta ni mkopo kutoka serikali ya India na tumetengewa US DOLA milioni 13.5 ambazo zitaelekezwa kujengwa kwa mradi huu na matarajio kwa mujibu wa serikali mradi utaanza mwezi wa tisa"alisema mhandisi Mtyauli         

Itika Frank Mboka ni Maneja Biashara Mamlaka ya Maji Njombe mjini Ambaye anasema kuwa Mamlaka hiyo bado inaendelea kuhudumia wananchi licha ya Changamoto ya uchache huku akiwaomba wananchi kuendelea kuomba kuunganishwa na huduma hiyo.

"Tunaendelea kutoa huduma ya maji na tunashukuru wateja wetu wanafanya vizuri na maji yanapatikana hata kama ni ya mgao na ukija kwenye uuzaji kwa maana ya mapato ya maji kwa kweli huwa hayatoshi,lakini bado tunaendelea kuwaomba wananchi wateja wetu waendelee kuwa na ushirikiano na mamlaka licha ya kuwa kwa kweli Njombe wananchi wanajitoa sana katika kuhitaji maji huku wengine wakiwa na visima"alisema Itika Mbona

Biteko: Wizara itaendelea kuanzisha masoko ya madini

$
0
0
Imeelezwa kuwa, Wizara ya Madini itaendelea kusimamia Uanzishwaji wa Masoko ya Madini katika maeneo mbalimbali nchini huku ikiendelea kufanya marekebisho ya Kanuni za Uanzishwaji wa masoko hayo.
 
Waziri wa Madini Doto Biteko ameysema hayo Machi 31, 2019 wakati akifunga Semina ya siku mbili iliyoandaliwa na wizara kwa Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini pamoja na baadhi ya Wenyeviti wa Kamati zenye uhusiano na Sekta ya Madini.
 
Semina hiyo ililenga kutoa elimu na kujenga uelewa wa pamoja kwa wabunge hao kuhusu sekta ya madini ambapo mada mbalimbali ziliwasilishwa. 
 
Mada zilizowasilishwa ni pamoja na uanzishwaji wa masoko ya madini, mafanikio na changamoto ya Shirika la Madini la Taifa STAMICO), elimu kuhusu majanga ya asili (hasa matetemeko ya ardhi), ukaguzi migodini, biashara ya madini na shughuli zinazofanywa na Taasisi ya Uwazi na uwajibikaji katika Rasiimali za Madini, Mafuta na Gesi Asilia.
 
Waziri Biteko aliongeza kuwa, Wizara itaendelea kuwaelea wadau wa madini huku akiwataka kubadilika na kutenda matendo yenye manufaa kwa pande mbili na kuwaomba wabunge hao kushirikiana na serikali katika kutoa elimu kwa wadau wa madini ili waweze kuzingatia na kufuata taratibu zilizowekwa. 
 
Pia, alisema serikali itaendelea kufanya kaguzi migodini kwa lengo la kuhakikisha wachimbaji wanachimba kwa usalama na kueleza kuwa, wizara imeomba kibali cha kuongeza maeneo mengine ya ukaguzi wa madini na kusema,“ tumepanga kuongeza vituo vingine 85”. 
 
Aidha, alizungumzia maeneo yenye wizi wa dhahabu katika maeneo ya kuchanjua madini hayo na kuyataja kuwa ni Kahama na Chunya na kuwataka wahusika kuzingatia sheria .
 
Akizungumzia suala la kupunguza zaidi kodi kwa uchimbaji mdogo wa madini, alisema serikali haitapunguza tena kodi hizo kwa sasa mpaka hapo itakapoona manufaa yake.
 
Ikumbukwe kuwa, baada ya mkutano wa Kisekta uliofanyika Januari 22 mwaka huu chini ya Uenyekiti wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli na kuwashirikisha wadau mbalimbali wa madini baada ya wadau hao kuwasilisha kero zao kubwa ikiwa kodi, serikali ilifanya mabadiliko na kuondoa kodi kwenye uchimbaji mdogo wa madini kwa kuwafutia kodi ya ongezeko la thamani yaani VAT  (18%) na  kodi ya zuio( withholding tax).
 
Mbali na wajumbe wa kamati, wengine walioshiriki semina hiyo ni Wenyeviti wa Bodi za Taasisi zilizo chini ya Wizara pamoja na Watendaji na Wataalam kutoka wizara na taasisi zake.

Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani aipa REA siku 28 kuwasha umeme Kyela

$
0
0
Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani ametoa siku 28 kwa Wakala wa Usambazaji Umeme Vijijini (REA) kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania  (Tanesco) kukamilisha ujenzi wa njia ya umeme yenye urefu wa zaidi ya kilometa 20  na kuwashwa kwenye makazi ya wananchi katika kata mbili wilayani Kyela.

 Waziri Kalemani, alitoa agizo hilo jana wakati akizungumza na wananchi kataka Kata ya Ipande ambako alistushwa baada ya kuelezwa na wananchi kuwa kata za Nkokwa na Ipande hazijawahi kufikiwa na umeme hata kwenye kijiji kimoja tangu Serikali ilipoanza mpango wa kusambaza umeme vijijini.

 Alisema haiwezekani kata nzima za Ipande na Nkokwa ziwe hazijafikiriwa na umeme kwa kipindi chote tangu Serikali ilipoanza kupeleka umeme katika vijiji vyote na kitendo hicho kinaonyesha kuna mahali uzembe unafanyika miongoni mwa watekelezaji wa mpango huo.

Aliiagiza  wakala huo kwa kushirikiana na Tanesco kuanza mara moja kazi ya kuchimbia nguzo kuelekea kwenye kata hiyo na kutoa mwezi mmoja kazi hiyo ikamilike na umeme uwashwe kwenye makazi ya wananchi.

“Naagiza kazi ianze  kufikia 28, Aprili, mwaka huu umeme uwashwe kwenye kata hizi za Nkokwa na Ipande, ikiwa agizo hili halitatekelezwa nawambieni watendaji wangu wa Rea na Tanesco mtapungua au kumalizika kabisa kwenye nafasi zenu,” alisema Dk. Kalemani.

 Alisema suala la usambazaji wa umeme vijijini sio la hiyari bali ni la lazima kutokana na Serikali kuazimia vijiji vyote nchini vifikiwe na umeme na kila mwananchi apewe fursa ya kuingiza umeme kwenye nyumba yake.

 Hata hivyo Wakati Dk. Kalemani akitoa agizo hilo, Mbunge wa Kyela ambaye pia ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Hurrison Mwakyembe akainuka na kumweleza kuwa siku hiyo ya April 28, mwaka huu kutakuwa na tukio kubwa la kitaifa hivyo akamuomba awaongeze watendaji wake japo siku tatu mbele.

 “Mheshimiwa Waziri, 28 Aprili timu yetu ya Vijana wenye Umri wa Chini ya Miaka 17, Serengeti Boys watakuwa uwanjani wakiwania taji la Afrika, hivyo naamini watanzania wote watakuwa wakifuatilia mchezo huo, nakuomba usogeze mbele japo kwa siku tatu ili na hawa watendaji nao wapate fursa ya kuiangalia timu yetu ikiwa uwanjani,” alisema Dk. Mwakyembe.

 Baada ya ombi hilo, Dk. Kalemani ambaye alikubali kusogeza Mbele hadi 2 Mai, Mwaka huu aliahidi kurejea tena wilayani Kyela kwenda kukagua utekelezaji wa mradi huo.

Maduka 82 Dar Yakutwa Na Viashiria Vya Utakatishaji

$
0
0
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Profesa Florens Luoga amesema kuwa maduka 82 Dar es Salaam yaliyofanyiwa ukaguzi yamekutwa na viashiria vya utakatishaji fedha.

Prof. Luoga amesema kuwa ukaguzi huo ulifanyika katika jumla ya maduka 87 na uchunguzi zaidi unaendelea dhidi ya maduka yote nchini ili kutoa taarifa kamili.

Gavana huyo amesema hayo jijini Dodoma wakati waziri wa fedha na mipango Dk. Philip Mpango alipokuwa akitoa taarifa juu ya zoezi la ukaguzi wa maduka ya kubadilishia fedha za kigeni nchini lililoanza November mwaka jana.

Maalim Seif Afunguka Kuhusu Kurudisha Kadi Yake ya CUF, Umaarufdu Wake na Mambo Mengine. Tazama Hapa

$
0
0
Makamu wa kwanza wa Rais (Mstaafu) wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amesema hawajarudisha kadi ya chama chake cha zamani cha CUF, lakini wameweka utaratibu maalumu wa kuirudisha yeye na wenzake.


Maalim Seif ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Aprili mosi, 2019 wakati wa mahojiano katika kipindi cha 360 kinachorushwa na Clouds TV.

“Tumeshadhamiria wote  kila aliyekuwa mwanachama wa CUF bendera zote, Katiba, sare  na kadi tunazikusanya na kumkabidhi kiongozi wa chama (Zitto Kabwe) azikabidhi kwa Msajili wa Vyama vya Siasa ambaye atajua cha kufanya,” amesema Maalim Seif.

Mbali na hilo, Maalim Seif amesema uamuzi wake wa kujiunga ACT- Wazalendo haujamshusha umaarufu wake bali upo palepale.

==>.Hapo chini Kuna Nukuu ya Kauli zote Alizoziongea Leo 

1.Nakumbuka wakati tunatia saini muafaka wa Zanzibar Rais  mstaafu wa awamu ya tatu Mhe Benjamini Mkapa alisema hakuna mwenye hatimiliki ya Tanzania kwahiyo sote tuna haki sawa juu nchi hii.


2.Rai yangu kwa Watanzania nawaomba tuungane kwa pamoja kwa ajili ya nchi yetu. Hakuna mwenye hatimiliki ya nchi hii ni mali ya wananchi wote kwahiyo wananchi wasiogope pale tunapoipinga CCM tuna mawazo mbadala juu ya nchi hii.

3.Watawala waliona kuninyang’anya CUF watanimaliza na mimi ntajiunga Chadema bahati mbaya hesabu zao zilikuwa wrong nikajiunga na ACT Wazalendo.

4.Mara ya mwisho kuzungumza na Rais Shein ilikuwa Machi 2016 mpaka sasa huwa tunakutana kwenye shughuli na wala hatuzungumzi hata kidogo. Na walinzi wake wakijua naenda mahali hupigiana simu na kuwaambia wanieke mbali naye.


5.Majengo yaliyokuwa mali ya CUF ni Mtendeni na Kilimahewa majengo yaliyobakia yalikuwa majengo ya wanachama Sasa kama wameamua kuondoka na kujiunga na ACT hawawezi kuyaacha CUF kwa mapenzi yao wameyarudisha ACT Wazalendo.

6.Wale waliochoma Bendera walikuwa tu na hasira na wala sikuunga mkono jambo lile, Jukumu letu na Mhe. zitto Kabwe ni kuwasihi vijana kuwa watulivu .

7.Mimi sina chuki na mtu, nikikutana na msajili nitamsalimu vizuri tu na nitamwambia ajitathmini kama je anatenda haki?

8.Mimi nilikuwa accounting officer wa Chama msajili alipoanza kutoa Fedha za ruzuku kwa Upande wa Lipumba nikamuandikia barua msajili kuhusu uamuzi wa kutoa pesa kwa Lipumba na mimi sijui si sawa basi mimi nikajivua nafasi hiyo.

9.Kwa ninavyomjua msajili wa vyama vya siasa, kama ningesema naanzisha chama changu asingenipa usajili. Msajili huyu kamrejesha Lipumba, amekata ruzuku akisema eti tuna mgogoro lakini kumbe alikuwa anampa Lipumba ruzuku hiyo tena kwa akaunti isiyo ya taifa


10.Hata kama ningeanzisha Chama changu msajili asingenipa usajili, Sikuona sababu ya kuanza upya kama kuna Alternative ya kuendeleza harakati. Maana wakati wa mgogoro wetu na Lipumba alikuwa anampatia pesa za ruzuku Lipumba .

11.Mimi umaarufu ninao tangu nipo CCM. Mimi sikutoka CCM nilifukuzwa, tena nilifukuzwa wakati mbaya sana sababu hapakuwa na chama kingine. Kuna watu wanasema wanafuatwa na  CCM na pesa lakini mimi na umri wangu huu tangu nimetoka sijawahi kufuatwa na eti nirudi CCM.


12.Wakati nikiwa CUF nimetengeneza kina Maalim Seif wengi sana na ndio maana nilikuwa naweza kuondoka nchini kwa hata miezi 6 na mambo yanakwenda, washauri wangu walikuwa wanakuja kwangu kwa ushauri tu”

13.Mimi binafsi nilisema nahama CUF nakwenda ACT Wazalendo nawaomba wanachama na wao waniunge mkono, sikuwaambia kuwa tunahama sote, wanachama kwenda ACT ni hiari yao, lakini wanachama wa CUF hasa wa visiwani walikuwa wamechoshwa na mgogoro
 

14.Tumekwenda ACT-Wazalendo  sio kutafuta vyeo, bali kuongeza nguvu lakini ikitokea wametutunuku vyeo basi tutavipokea. ACT wana utamaduni wao ni kazi kwetu kujibadilisha ili kuendana nao

15.ACT wazalendo ina viongozi vijana wenye nguvu, uongozi wenye malengo ambao wakishaamua jambo wanafanya na kubwa zaidi dhamira yao kwa nchi yetu ni nzuri

Polisi Kigoma Yaua Majambazi Watatu

$
0
0
Watu watatu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi wameuawa huku askari polisi mmoja  akijeruhiwa baada ya kutokea kwa majibizano ya risasi katika tukio la ujambazi wilayani Kibondo mkoani Kigoma..

Inaelezwa majambazi hao  walikuwa wamejipanga kufanya uporaji katika baadhi ya nyumba za wananchi wilayani Kibondo.

Mkuu wa Wilaya ya Kibondo, Louis Bura, alisema juzi usiku   polisi walipokea taarifa kutoka kwa wananchi  kuwa kuna majambazi walikuwa wanataka kuvamia baadhi ya nyumba.

Alisema   walifika eneo la tukio na   kurushiana risasi ambako askari mmoja,     James Mwita (37) na mama mmoja, Sophia Dicksoni (60) walijeruhiwa na   wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Kibondo.

Alisema askari huyo alipatiwa matibabu ya awali na sasa   amepatiwa rufaa   kwenda  kwenye matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kutokana na majeraha ya mguuni.

DC aliwapongeza wananchi kwa kuendelea kuonyesha ushirikiano  kwa vyombo vya ulinzi na usalama kwa kazi kubwa wanayo ifanya kwa kuwa ni kazi ngumu.
 
Amewataka wananchi kuacha kuwaingilia katika utendaji kazi wao kwa kuwa wapo baadhi wanawakamata wakiwatuhumu kwa ujambazi lakini ndugu zao wanawatetea na kudai siyo majambanzi.

Pia aliwataka wananchi kuacha kutoka nje   wanaposikia milio ya risasi kwa ajili ya usalama wao kwa kuwa ni hatari   kufuata milio hiyo inaweza sababisha madhara makubwa.

Serikali Kuandaa kanuni mpya kwa ajili ya biashara ya maduka ya kubadilisha fedha za kigeni

$
0
0
Waziri wa Fedha na Mipango Dk.Philip Mpango amesema serikali inaandaa kanuni mpya kwa ajili ya biashara ya maduka ya kubadilisha fedha za kigeni ambazo zitaelekeza jinsi ya kuomba leseni za uendeshaji wa maduka hayo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu April 1, 2019 jijini Dodoma, Dk.Mpango amesema kanuni hizo zitaelekeza kwa waombaji wa leseni kwa watu binafsi au taasisi yeyote na masharti ya kuzingatiwa wakati wa shughuli hiyo.

Amesema hatua hiyo ya serikali  imetokana na maduka mengi nchini ya kubadilishia fedha za kigeni yamekuwa yakitumika katika utakatishaji wa fedha haramu pamoja na ukwepaji wa mapato ya serikali.

“Hivi karibuni serikali kupitia Benki kuu (BOT) imeendesha zoezi la ukaguzi wa maduka yanayotoa huduma ya ubadilishaji wa fedha za kigeni lakini kumekuwa na tuhuma mbalimbali zilizotolewa za kudai uwepo wa ukiukwaji wa sheria na haki kwa wamiliki hao jambo la kushangaza hakuna mmiliki yeyote wa duka aliyewasilisha malalamiko,”amesema.

Ameeleza kuwa kuandaliwa kwa kanuni hizo kunalenga kuweka mazingira mazuri ya biashara ambayo hayatatoa athari kwa sekta ya fedha na uchumi kwa ujumla.

Aidha amesema kuwa Benki kuu imechukua tahadhari ya kuhakikisha huduma ya ubadilishaji fedha inaendelea nchini kwa kutolewa na benki zote pamoja na Shirika la Posta.

Kuhusu ukaguzi, Dk.Mpango amesema kazi hiyo ilifanywa mikoa ya Arusha na Dar es salaam ambapo imebaini pia upokeaji wa amana kutoka kwa wafanyabishara kinyume cha matakwa ya leseni za biashara husika.

Asasi 65 za Kiraia Zamtaka Msajili wa vyama vya Siasa Aache kuingilia migogoro ya ndani ya vyama vya siasa.

$
0
0
Asasi 65 za Kiraia zimemtaka Msajili wa vyama vya Siasa Nchini aache kuvitisha na kuingilia migogoro ya ndani ya vyama vya siasa.

Aidha, badala yake wamemtaka aongozwe zaidi na hekima katika kusimamia misingi ya demokrasia na haki za wananchi kujiunga na vyama wanavyovitaka bila kuwekewa vikwazo visivyotambulika na sheria za nchi.

Wito huo umetolewa leo na Jukwaa la Wakurugenzi wa AZAKI katika ofisi ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, (LHRC), ambapo pia zimewataka viongozi waheshimu sheria za nchi na katiba kwa kuacha kuzuia mikutano ya siasa ya ndani na nje.

Akitoa tamko kwa niaba ya Azaki hizo, kuhusu hali ya demokrasia, haki ya kujumuika na kujiunga na vyama vya siasa, Onesmo Olengurumwa kutoka THRDC, amesema kumekuwa na matukio yanayoashiria ukiukwaji wa haki za kidemokrasia haki ya uhuru wa kukifanyika na kujiunga na vyama vya siasa.

“Kama Watanzania wenye jukumu kikatiba kulinda mshikamano, umoja,haki na amani ya nchi tumeona ni vyema kuzungumza na kuwashauri viongozi wetu wa kiasiasa kufuata sheria za nchi.

“Tumeshuhudia ukiukwaji wa haki hizo za kisheria na Katiba ya nchi ya mwaka 1977 na kwa kuwa asasi tumekuwa washauri na wakosoaji na wasaidizi wakubwa wa mambo mengi yakitaifa ni busara zaidi kulisemea hili ili kuhakikidha ukiukwaji wa haki hizi tajwa haziwezi kuwa sababu ya kupelekea kupoteza amani na umoja wa kitaifa,” amesema Olengurumwa.

Amesema mwenendo wa muda mrefu wa Msajili wa vyama vya Siasa kuonekana kuchukua upande katika mgogoro wa ndani wa Chama cha Wananchi (CUF) na kusahau yeye ni mlezi wa vyama alipaswa kutokuwa sehemu ya mgogori ndani ya vyama.

Naye mwakilishi kutoka LHRC, Felister Mauya, amesema serikali inatakiwa kuhakikisha uhuru wa kujumuika ikiwa ni pamoja na uhuru wa kufanya maandamanao ya amani unaheshimiwa na kulindwa na vyombo vya usalama kama sheria zinavyoelekeza.
M

Serikali Yakabidhi Ndege Yake Ya Fokker 50 Kwa ATCL

$
0
0
Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi akipeana mikono na
Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Dkt. Leonard Chamriho baada ya kumkabidhi ndege serikali aina ya Fokker 50 ili aikabidhi kwa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kwa ajili ya kubeba abiria wa kawaida  kama ilivyoagizwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwenye hafla fupi iliyofanyika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere leo Aprili 1, 2019. Kulia ni Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Ikulu, Dkt. Moses Kusiluka na kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Ndege la Air Tanzania (ATCL) Injinia Emmanuel Korosso.

Ndege aina ya Fokker 50 iliyokabidhiwa na serikali  kwa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kwa ajili ya kubeba abiria wa kawaida kama ilivyoagizwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli   katika  Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere leo Aprili 1, 2019

Taarifa Kwa Umma Kuhusu Ukaguzi Wa Maduka Ya Kubadilisha Fedha Za Kigeni

$
0
0
Dodoma, 1 Aprili, 2019: Katika kutekeleza majukumu yake ya kuhakikisha kuwa Sekta ya Fedha inachangia ipasavyo utulivu na ukuaji wa uchumi nchini, Benki Kuu ya Tanzania ilibaini uwepo wa maduka ya kubadilisha fedha za kigeni ambayo yalikuwa yakiendeshwa pasipo kuzingatia Sheria ya Foreign Exchange Act 1992, Kanuni za The Foreign Exchange (Bureau de Change) Regulations 2015 na marekebisho ya mwaka 2017 na Taratibu za utoaji wa huduma za ubadilishaji wa fedha za kigeni. Kufuatia hali hiyo, zoezi maalum la ukaguzi wa kina kwa maduka hayo lilifanyika Arusha Novemba 2018 na kwa Dar es Salaam siku ya tarehe 27 Februari 2019, 1 na 8 Machi 2019 kwa kuhusisha vyombo vya Dola na kubaini ukwepaji mkubwa wa kodi na uvunjaji wa Sheria.

Zoezi hili limebaini pia uondoshwaji wa fedha katika mfumo rasmi wa fedha na kuelekezwa kwenye mifumo ya utakasishaji wa fedha haramu, kupokea Amana kutoka kwa wafanyabiashara kinyume cha matakwa ya leseni za biashara husika, kudhoofisha thamani ya shilingi, pamoja na mambo mengine ambayo yalianza kuathiri usalama wa nchi kwa ujumla. Kwa mfano, baadhi ya maduka yaligundulika kutumia fedha nyingi za Tanzania kununua fedha za kigeni lakini fedha kidogo za kigeni ziliuzwa na hakuna taarifa ya matumizi ya fedha za kigeni zilizobaki.

Ni vizuri ieleweke kuwa,  zoezi la ukaguzi wa maduka ya kubadilisha fedha za kigeni lilitekelezwa kwa kuzingatia Sheria za nchi tofauti na malalamiko na tuhuma mbalimbali zilizotolewa za kudai uwepo wa ukiukwaji wa Sheria na haki kwa wamiliki wa maduka hayo. Jambo la kushangaza ni kwamba hakuna mmiliki yeyote wa duka aliyewasilisha malalamiko kuhusiana na zoezi hili kwenye mamlaka husika. Hata hivyo, Benki Kuu ya Tanzania na Mamlaka nyingine za Serikali zinafuatilia kwa umakini ili kubaini ukweli wa tuhuma hizo zinazotolewa.

Serikali ya Awamu ya Tano inatekeleza majukumu yake kwa umakini. Hivyo, Serikali inauthibitishia umma wa Watanzania kuwa katika zoezi la ukaguzi wa Maduka ya Kubadilisha Fedha za Kigeni hakuna fedha au mali yeyote iliyotaifishwa. Taratibu za kisheria zilifuatwa wakati wa kuchukua vielelezo mbalimbali zikiwemo fedha, kompyuta, simu za viganjani, mashine maalum za kuhifadhi taarifa na taarifa mbalimbali ili kusaidia uchunguzi. 

Aidha, lengo la zoezi hili sio kufuta biashara ya maduka ya kubadilishia fedha za kigeni kwa watu binafsi, bali ni kudhibiti ukiukwaji wa sheria uliokithiri, ukwepaji wa kodi na utakatishaji wa fedha haramu. Maduka machache ya kubadilisha fedha za kigeni ambayo yalizingatia Sheria na Kanuni za Foreign Exchange na masharti ya biashara hiyo yaliachwa kuendelea na utoaji wa huduma hiyo.

Hivi sasa Serikali imeandaa Kanuni mpya kwa ajili ya biashara ya maduka ya kubadilisha fedha za kigeni ambazo zitaelekeza jinsi ya kuomba leseni za uendeshaji wa maduka hayo kwa mtu binafsi au taasisi yeyote na masharti ya kuzingatiwa wakati wa shughuli hizo.

Kanuni hizo zinalenga kuweka mazingira mazuri ya biashara ambayo hayatatoa athari kwa sekta ya fedha na uchumi jumla, na inakuwa yenye manufaa kwa nchi. 

Kwa kuzingatia maduka mengi yaliyokaguliwa yamefungwa, Benki Kuu ya Tanzania imechukua tahadhari ya kuhakikisha huduma ya ubadilishaji fedha za kigeni inaendelea nchini kwa kutolewa na benki zote pamoja na Shirika la Posta. 

Benki Kuu ya Tanzania itakuwa inatoa taarifa kuhusu upatikanaji wa huduma hiyo na kuzihimiza benki za biashara na Shirika la Posta kutoa taarifa kwa umma kuhusiana na huduma katika maduka yaliyofunguliwa na benki hizo na Ofisi ya Posta.

Kwa kipindi kifupi cha utekelezaji wa zoezi la udhibiti wa biashara ya kubadilisha fedha za kigeni, thamani ya shilingi imeimarika na upatikanaji wa fedha za kigeni katika benki za biashara umekuwa mzuri. 

Kabla ya zoezi la udhibiti wa biashara ya kubadilisha fedha ya kigeni dola ya Marekani ilikuwa inauzwa kwa wastani wa shilingi 2,450 na baada ya utekelezaji wa zoezi hivi sasa dola ya Marekani inauzwa kwa wastani wa shilingi 2,300. 

Aidha, Benki za biashara kwa wastani hivi sasa zinakusanya jumla ya dola za Marekani milioni 15 kwa siku. Ni matarajio ya Serikali kuwa udhibiti huu utaziwezesha Benki za biashara na taasisi nyingine kuuza fedha za kigeni kwa wingi kwenye soko la fedha za kigeni na hatimaye kuongeza akiba ya fedha za kigeni.

Serikali inatoa tahadhari kwa wananchi kutoshiriki kwenye biashara ya kubadilisha fedha za kigeni kwa njia zisizo halali. Hivi sasa kuna taarifa kwa baadhi ya maeneo ya mipakani na majiji ya Dar es Salaam na Arusha wamejitokeza watu wanaofanya biashara haramu ya kubadilisha fedha za kigeni ambao wamewaathiri baadhi ya wananchi kwa wizi. 

Vyombo vya usalama ikiwemo jeshi la polisi vimeongeza nguvu katika kuhakikisha biashara hii haramu (Black Market) inatokomezwa na hivi sasa wahalifu saba wamekamatwa na kufikishwa mahakamani.

Serikali inapenda kuwahakikishia Watanzania wote kuwa inayo akiba ya fedha za kigeni ya kutosha zipatazo dola za Marekani bilioni 4.67 hadi tarehe 30 Machi 2019 zenye uwezo wa kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa kipindi kisicho pungua miezi 4.8. 

Hivyo, wasiwasi kuwa Serikali imechukua hatua ya kufunga baadhi ya maduka ya kubadilisha fedha za kigeni kwa sababu haina akiba ya fedha za kigeni si ya kweli hata kidogo. 

Aidha, hofu kwamba nchi inarejea katika kipindi cha nyuma ambapo fedha za kigeni zilikuwa zinatolewa kwa vibali (rationing) ili kukidhi mahitaji ya fedha hizo kwenye utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo, nazo hazina msingi.

Mapato ya Nchi yanayotokana na vyanzo vya fedha za kigeni kwa kuuza bidhaa na huduma nje ya nchi yalikuwa na thamani ya dola za Marekani milioni 8,554.5 kwa mwaka unaishia Februari 2019 ikiwa ni ongezeko la asilimia 1.4 ikilinganishwa na fedha za kigeni zilizopatika mwaka unaishia Februari 2018. 

Ongezeko hilo la mapato ya fedha za kigeni kwa Nchi yamechangiwa zaidi na uuzaji wa bidhaa zisizo asilia nje ya nchi zikiwa na thamani ya dola za Marekani milioni 3,878.5 sawa na asilimia 10.3 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia. 

Vile vile, huduma zilizotolewa nje ya nchi kama vile usafiri na usafirishaji na utalii ziliingiza jumla ya dola za Marekani milioni 4,074.1 sawa na ongezeko la asilimia 6.1 ikilinganishwa kiasi kilichopatikana mwaka ulitangulia.

 Aidha, Serikali inachukua fursa hii kuwaeleza wananchi kuwa nchi yetu ina akiba ya chakula cha kutosha ambacho kina utoshelevu wa asilimia 124 kwa mwaka huu wa fedha 2018/19.  Hivyo, Serikali haitarajii kutumia  fedha za kigeni kuagiza chakula kutoka nje ya nchi isipokuwa tu kama ikitokea hali ya ukame ikawa mbaya katika siku zijazo.

Serikali, kupitia Benki Kuu ya Tanzania, inawataka wafanyabiashara ya huduma ya kubadilisha fedha za kigeni kuzingatia na kutii Sheria ya Foreign Exchange 1992, Kanuni ya Foreign Exchange (Bureau de Change) Regulations 2015 na marekebisho ya mwaka 2017, Masharti ya biashara ya huduma ya kubadilisha fedha za kigeni na Maelekezo ya Msimamizi (BOT) wa Sekta ya Fedha Nchi. Mwisho Serikali inawapongeza wananchi wa Tanzania kwa kuwa waelewa na watulivu wakati wote zoezi la ukaguzi likiendelea, licha ya kujitokeza kwa taarifa za upotoshwaji wa zoezi hili.

IMETOLEWA NA:
DKT. PHILIP ISDOR MPANGO
WAZIRI YA FEDHA NA MIPANGO

Rais Magufuli ataka TRA iache kuwa kamua walipa kodi wachache

$
0
0
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amemuapisha Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango atakayeshughulikia sera Adolf Hyasinth Ndunguru na Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Hafla ya kuapishwa kwa viongozi hao imehudhuriwa na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji, Makatibu Wakuu, Viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama na wafanyakazi wa Wizara ya Fedha na Mipango.

Akizungumza baada ya kuwaapisha, Rais Magufuli ameitaka TRA na Wizara ya Fedha na Mipango kupanua uwigo wa kodi kwa kuongeza idadi ya walipa kodi na kuibua vyanzo vipya vya mapato, pamoja na kujenga mazingira rafiki kwa watu wengi zaidi kulipa kodi ili kuongeza makusanyo ya kodi.

Rais Magufuli ameelezea kutoridhishwa kwake na utendaji wa TRA ambayo mpaka sasa inakusanyaji kodi kwa walipa kodi Milioni 2 na Laki 7 tu kati ya Watanzania wote zaidi ya Milioni 55, na amesema kwa mtindo huo TRA itakuwa inazidi kuwakamua walipa kodi wachache wakati ingeweza kupanua uwigo wa kodi na kuweka viwango vya kodi vinavyolipika na vitakavyowavutia watu wengi zaidi kulipa kodi.

“Ukienda mipakani wafanyabiashara wanafungua maduka upande nchi za wenzetu na sio upande wa Tanzania, na sababu ni kwamba wakifungua upande wa Tanzania wanasumbuliwa na TRA, wekeni viwango vya kodi vinavyolipika ili watu wengi waweze kulipa kodi badala ya kukwepa” Rais Magufuli.

Rais Magufuli ameelezea kutofurahishwa na mrundikano wa kesi za kodi mahakamani na ametaka tatizo hilo lifanyiwe kazi kwa kuwa linasababisha kodi nyingi kutolipwa kwa kusubiri mivutano ya kesi.

Amempongeza Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji kwa ufuatiliaji mzuri wa fedha za bajeti zinazoelekezwa katika miradi mbalimbali na kuchukua hatua zinazostahili ikiwemo kuzirejesha hazina na kuzielekeza mahali pengine zinapohitajika.

Aidha, Rais Magufuli amemtaka Naibu Katibu wa Fedha na Mipango Mkuu Ndunguru na Naibu Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Mbibo kwenda kurekebisha dosari zote zilizopo katika ofisi zao ikiwa ni pamoja na kuwaondoa watumishi wanaoonekana kuwa kikwazo cha kutekeleza mipango ya Serikali.

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amesema viongozi hao wanatarajiwa kufanya vizuri zaidi katika nafasi walizopewa hivi sasa hasa ikizingatiwa kuwa wanakwenda kufanya kazi katika ofisi zenye mchango mkubwa katika uchumi wa nchi.

Nae Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji na Kamishna Mkuu wa TRA Charles Kichere wamemshukuru Rais Magufuli kwa uteuzi wa viongozi hao na wameahidi kwenda kusimamia kwa ukaribu zaidi utekelezaji wa fedha za bajeti na kufanyia kazi changamoto ya kupanua uwigo wa kodi na kuongeza idadi ya walipa kodi.

Viewing all 45270 articles
Browse latest View live




Latest Images