Quantcast
Channel: MPEKUZI
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live

Mahakama Yamwachia Huru Kijana Aliyeiba Debe Moja la Mahindi Kisha Likanasa Kichwani

$
0
0
Mahakama ya Mwanzo Mlandizi mkoani Pwani imemuachia huru, kijana Frank Joseph (23) aliyeiba kiroba cha Mahindi debe 1 na kumnasia kichwani baada ya mlalamikaji kutofika mahakamani hapo mara 3 mfululizo.

Frank ambaye ni mkazi wa Mbezi DSM, ameachiwa huru na Hakimu Mfawidhi, Nabwike Mbaba wakati shauri hilo lilipoitishwa kwa ajili mlalamikaji (mtendewa) kutoa maelezo ya jinsi alivyoibiwa.

Hakimu Mbaba amesema kuwa kutokana na mlalamikaji (mtendewa) kushindwa kufika mahakamani hapo mara 3 mfululizo kutoa maelezo ya kuibiwa kwake anaifuta kesi huyo.

“Mtendewa ameshindwa kufika mahakamani licha ya kupewa wito mara 3 mfululizo, hivyo naifutilia mbali kesi hii na mshtakiwa kuanzia sasa upo huru,” amesema Hakimu Mbaba.

Awali mshtakiwa alishindwa kufikishwa mahakamani mara 2 mfululizo kutokana na gari la Magereza kuharibika.

Katika kesi hiyo namba 124/2018 Frank anadaiwa kutenda kosa la wizi May 3, 2018 saa 7 usiku maeneo ya Mlandizi ambapo aliiba Mahindi debe 1 likiwa na thamani ya Sh.20, 000 ikiwa mali ya Seve Seleman.

Kenyatta Atia saini sheria ya makosa ya mtandaoni Ambapo Faini yake ni Milioni 100 Ukikutwa na Hatia

$
0
0
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ametia saini mswada wa Sheria ya Uhalifu wa Kompyuta na Mtandaoni ya mwaka 2018 kuwa Sheria, hatua hii itatoa adhabu kali kwa watakaopatikana na makossa ya mtandaoni.

Sheria hiyo inatoa adhabu ya faini ya Milioni 100 (dola 50,000 za Marekani) au kifungo cha miaka miwili jela, au adhabu zote mbili, kwa atakayepatikana na kosa la uenezaji wa habari za uzushi.

Mtu atakayepatikana na kosa la kueneza taarifa ambazo zinaweza kuzua taharuki au kuzua vurugu atafungwa jela zaidi ya miaka kumi.

Hatua hiyo imepokelewa kwa hisia na maoni tofauti kwa watu mbalimbali ambapo kiongozi wa zamani wa chama cha wanasheria Kenya Apollo Mboya amenukuliwa na vyombo vya habari akisema kifungu hicho kinaweza kuwapa watawala ‘uhuru’ wa kukandamiza vyombo vya habari.

Kwa upande mwingine shirika la kimataifa la kutetea uhuru wa wanahabari Committee to Protect Journalists (CPJ) nalo limekuwa likipinga uidhinishaji wa mswada huo.

BOT Yaziunganisha benki ya Twiga na Benki ya TPB

$
0
0
Benki kuu ya Tanzania imepitisha ombi la kuunganishwa kwa benki za Twiga Bancorp (Twiga Bancorp Limited) na benki ya TPB (TPB Bank Plc) na kuwa benki moja kuanzia tarehe 17 Mei 2018 itakayoendelea kuitwa benki ya TPB (TPB Bank Plc).

Kufuatia hatua hiyo Wateja, wafanyakazi, mali na madeni yote ya benki ya Twiga yatahamishiwa kwenda benki ya TPB.

Taarifa hiyo imetolewa leo Mei 16, 2018 na Benki Kuu ya Tanzania chini ya Mamlaka iliyopewa ya kifungu cha 30(1)(a) cha Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006.

Ikumbukwe kuwa benki ya Twiga iliwekwa chini ya usimamizi wa Benki Kuu kuanzia tarehe 28 Oktoba 2016 kutokana na kuwa na upungufu mkubwa wa mtaji.

Hivyo, muungano huu utaifanya Benki Kuu kusitisha usimamizi wa benki ya Twiga na mambo yote kuhusiana na benki hiyo yatafanywa na benki ya TPB kuanzia tarehe 17 Mei 2018.

Benki mpya ya TPB itakuwa ina mtaji wa kutosha kama inavyotakiwa chini ya kifungu cha 17 cha Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006.

Uamuzi huu umechukuliwa ili kuboresha uangalizi na utendaji wa benki zinazomilikiwa na Serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania.

Benki Kuu ya Tanzania inapenda kuuhakikishia umma kuwa itaendelea kulinda maslahi ya wenye amana katika mabenki kwa lengo la kuleta ustahimilivu katika sekta ya fedha.

Bashe awataka wabunge kutopitisha bajeti ya Wizara ya Kilimo

$
0
0
Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe amewataka wabunge wenzake kuungana na kuikataa bajeti ya Wizara ya Kilimo ya mwaka 2018/19 ili kuipa nafasi Serikali kuwasilisha bungeni bajeti itakayogusa maisha ya Watanzania.

Bashe ametoa kauli hiyo leo Mei 16, 2018 bungeni mjini Dodoma katika mjadala wa bajeti ya wizara hiyo.

“Nataka niwaombe wabunge bajeti hii tutumie kanuni ya 69 ya Bunge tuirudishe Wizara ya Kilimo na Wizara ya Fedha zikaketi ili kuja na bajeti inayogusa maisha ya watu,” amesema Bashe.

Amesema haiwezekani sekta inayogusa asilimia 70 ya Watanzania na kuchangia asilimia 30 katika pato la Taifa ikatengewa asilimia 0.8 ya fedha za maendeleo katika bajeti kuu ya Serikali.

“Sekta hii imeendelea kuonewa kwa muda mrefu na siyo sahihi, hasa  wabunge wa CCM tuna wajibu wa kumlinda mkulima,” amesema Bashe.

Bunge labadili ratiba kuwapa fursa wabunge mfungo wa Ramadhan

$
0
0
Bunge limebadilisha ratiba ili kuruhusu waumini wa dini ya Kiislamu kushiriki kikamilifu mfungo mtukufu wa Ramadhan bila kuathiri shughuli za chombo hicho cha Dola.

Utenguaji wa kanuni hizo umefanywa bungeni leo Jumatano Mei 16, 2018 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama na kuungwa mkono na wabunge.

Kwa mujibu wa Mhagama, ratiba iliyobadilika ni ya kipindi cha mchana ambapo sasa Bunge litaanza saa 10:00 jioni badala ya saa 11.00 jioni na kumalizika saa 12.00 jioni badala ya saa 1.45 usiku.

Amesema mara baada ya kumalizika kwa mfungo huo, ratiba itarudi kama kawaida.

Mahakama Yaibana Serikali kesi ya mhasibu Takukuru

$
0
0
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imetoa siku 14 kwa upande wa mashtaka kuhakikisha wanakamilisha kuchapa maelezo ya washtakiwa wa kesi ya kumiliki mali zisizoendana na kipato, inayomkabili mhasibu mkuu wa Taasisi na Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Godfrey Gugai na wenzake watatu.

Mbali na Gugai, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni George Makaranga, Leonard Aloys na Yasini Katera na wote wanakabiliwa na mashitaka 43 yakiwemo 20 ya utakatishaji wa fedha haramu, kumiliki mali zisizoendana na kipato na kughushi mikataba ya mauziano ya viwanja katika maeneo mbalimbali.

Uamuzi huo umetolewa leo Mei 16, 2018 na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba baada ya kesi hiyo kuahirishwa kwa zaidi ya mara saba,ikiwa katika hatua ya kuwasomea hoja za awali (PH), washtakiwa hao.

Hatua hiyo, inatokana na upande wa mashtaka kuieleza Mahakama hiyo kuwa wapo katika hatua za mwisho za kuchapa maelezo ya washtakiwa.

Awali, wakili wa Serikali Mkuu, Vitalis Peter amedai mahakamani hapo kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo ya awali, lakini walikuwa hawajakamilisha uchapaji wa maelezo ya washtakiwa hao.

“Kesi imekuja kwa ajili ya upande wa Jamhuri kuwasomea maelezo ya awali washtakiwa wote , lakini tunaiomba Mahakama itupe ahirisho la mwisho ili tuweze kukamilisha uchapaji wa maelezo ya washtakiwa,” amedai wakili Peter.
 
“Tayari maelezo ya washtakiwa tumeshaanda na kilichobaki ni kuchapwa tu, hivyo tunaiomba Mahakama yako itupe ahirisho la mwisho.”

Baada ya maelezo hayo, wakili wa utetezi, Semi Malimi na Alex Mgongolwa wamedai kuwa maelezo ya awali yameahirishwa kusomwa kwa zaidi ya mara saba kuanzia April 4, 2018.

Baada ya kupitia maelezo ya pande zote, hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi Mei 30, 2018 na kuutaka upande wa mashtaka kuhakikisha wanakamilisha kuchapa maelezo hayo ili washtakiwa hao waweze kusomewa maelezo ya awali.

Rais Magufuli Akubali Kuikabidhi Kombe Simba SC

$
0
0
Shirikisho la soka nchini TFF leo Mei 16, limethibitisha kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amekubali ombi la kuwa mgeni rasmi na kukabidhi vikombe vya ubingwa wa Serengeti Boys na Simba.

Mtendaji mkuu wa TFF Wilfred Kidao amesema wamethibitishiwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe kuwa Rais Magufuli amekubali kuwa mgeni rasmi kwenye mchezo wa Simba SC dhidi ya Kagera Sugar jumamosi hii.

''Rais Magufuli amekubali ombi la TFF kuwakabidhi vijana wa Serengeti Boys Kombe la CECAFA waliloshinda hivi karibuni nchini Burundi, tukio ambalo litaambatana pia na kuikabidhi Simba SC kombe la ubingwa wa VPL msimu huu'',  amesema.

Serengeti Boys wameibuka mabingwa wa soka katika ukanda wa Africa Mashariki na Kati baada ya kutwaa ubingwa huo kwa kuwafunga vijana wa Somalia kwa mabao 2-0 kwenye mchezo wa fainali.

Simba imetwaa ubingwa wa Ligi kuu soka Tanzania Bara msimu wa 2017/18 baada ya kufikisha alama 68 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote kati ya 16 za ligi kuu msimu huu.

Kampuni ya Tanzanite One yakubali kuilipa Serikali fidia

$
0
0
Kampuni ya uchimbaji madini ya Tanzanite One imekubali kuilipa Serikali fidia pamoja na kodi watakayokubaliana kutokana na dosari zilizokuwepo hapo awali.

Makubaliano hayo yametiwa saini Jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Kamati iliyoundwa na Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli Profesa Palamagamba Kabuni na  Mkurugenzi wa Tanzanite One Bw.Faisal Juma.

Akizungumza mara baada ya kutia saini makubaliano hayo, Mwenyekiti wa  kamati ya majadiliano kwa upande wa Serikali, Prof. Palamagamba Kabudi amesema Tanzanite One imekubali kulipa fidia Serikali kutokana na mambo iliyofanya ambayo yalikuwa kinyume na utaratibu ulioleta hasara kwa Serikali.

Amesema fidia hiyo inatakiwa kulipwa kwa awamu ambapo awamu ya kwanza italipwa ndani ya wiki mbili kuanzia leo  na haitahusisha Kodi. Pia Kampuni hiyo Tanzanite One italazimika kulipa kodi kama kawaida inazodaiwa na Serikali na tozo nyingine zote zinazodaiwa na Serikali.

Pia  Serikali  imekubaliana na Kampuni ya Tanzanite One kuwa itafuata masharti yote ya sheria ya madini ya mwaka 2010 ambayo inaeleza kuwa ni Watanzania tu ndio wanaoruhusiwa kuchimba madini ya Vito na pale ambapo watanzania hawana uwezo huo ndipo wanapoweza kuingia ubia na wageni.

Aidha Prof. Kabudi amesema kuhusu wachimbaji wadogo wadogo wa Tanzanite katika eneo la Mirerani  utaratibu mpya unawekwa lengo kubwa ikiwa ni kutekeleza sheria ya madini ya mwaka 2010 ambayo inalenga madini ya vito kuwa mikononi mwa Watanzania.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya Tanzanite One Faisal Juma amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuunda kamati hiyo ya kizalendo katika kufuatilia rasilimali za madini nchini ambapo wameweza kujadiliana na kufikia muafaka wa kulipa fidia ikiwa ni mbali na malipo yote yaliyotakiwa kulipwa serikali ikiwemo kodi.

Amesema Tanzanite One itahakikisha inafuata taratibu zote za Sheria ya Madini ya mwaka 2010 kwa lengo la kuhakikisha rasilimali ya madini inawanufaisha Watanzania na kwamba uvunjifu wa sheria uliofanywa na kampuni hiyo hautajirudia tena.

“Sisi kama Tanzanite One tunaihakikishia Serikali kuwa uaminifu uliotuonyesha na sisi pia kama Kampuni tutahakikisha tunakuwa waaminifu na kuwa zao hili linanufaisha taifa kutokana na imani aliyotuonyesha Mhe. Rais kama wananchi wake kutupa nafasi na fursa ya kusikilizwa ili kurekebisha makosa tuliyoyatenda” amesema   Faisal.

Faisal amesema Tanzanite One itahakikisha haitafanya makosa iliyofanya mara ya kwanza na hivyo kuwa mfano wa kampuni nyingine za madini kuhakikisha rasilimali za madini zinawanufaisha Watanzania.

Jaffar Haniu
Naibu Mkurugenzi Mawasiliano ya Rais, IKULU.
Dar es Salaam
16 Mei, 2018

Kondakta Atiwa mbaroni kwa kukutwa na vipodozi vilivyopigwa marufuku

$
0
0
Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro linamshikilia  kondakta wa kampuni  moja ya mabasi yanayofanya safari kati ya Dar es Salaam na Mbeya,baada ya kumkuta na vipodozi vilivyopigwa marufuku.

Mtuhumiwa huyo mkazi wa Kitunda jijini Dar es Salaam alikutwa akiwa amehifadhi vipodozi hivyo katika mifuko miwili ya plasitiki na kwenye boksi.

Akizungumza leo Jumatano Mei 16, 2018 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei amesema mtuhumiwa huyo amekamatwa baada ya polisi kusimamisha basi na kulifanyia upekuzi.

Amesema tukio hilo limetokea Mei 15, 2018  saa mbili usiku huko maeneo ya Melela Barabara Kuu ya Iringa-Morogoro.

Matei amesema mtuhumiwa alikutwa na vipodozi katoni 56 vya aina tofauti na kwamba vipodozi hivyo vimepigwa marufuku kuingizwa nchini.

Alivitaja vipondozi hiyo kuwa ni Extra Claire tube katoni 23,Lemon Vert Cream katoni 12, perfect white cream  6, betason 4, carolite 3, beiaton 2, extra cream1, sivop cream 1, dyna Claire 1, lemonvet cream 1, princes tube cream 1, epiderm cream 1, exoplus boksi 1, actilua lotion dazen 11, demon Claire pakti 3, oranvet jelly pakti 3 na Claire for men 11

Katika tukio lingine kamanda Matei amesema polisi wanamshikilia  mkazi wa Kikwalaza tarafa ya Mikumi wilayani Kilosa kwa tuhuma za kukutwa na meno ya tembo yenye uzito wa kilogramu 10 zenye thamani ya Sh34 milioni , akiwa amezipakia kwenye baiskeli.

Kamanda Matei amesema mtuhumiwa huyo alikamatwa Mei 15, 2018 na polisi wakishilikiana na maofisa wanyamapori.

Amesema alikutwa akiwa amepakia meno hayo katika baiskeli.

Makamu Wa Rais Apokea Vifaa Vya Upasuaji Kutoka Ubalozi Wa Kuwait

$
0
0
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema uboreshaji wa huduma katika hospitali zetu za kibingwa kama MOI, zitaipunguzia Serikali mzigo wa kupeleka wagonjwa nje ya nchi na hivyo kutekeleza azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuboresha huduma za afya kwa wananchi.

Makamu wa Rais ameyasema hayo wakati wa kupokea vifaa vya Chumba Cha Upasuaji wa Watoto vilivyotolewa na Ubalozi wa Kuwait kwa Taasisi ya Mifupa (MOI) jana tarehe 15 Mei, 2018.

“ Aidha kwa namna ya kipekee nakushukuru Mheshimiwa Balozi wewe binafsi na Serikali ya Kuwait kwa ushirikiano ambao mnaendelea kuipatia Serikali yetu ya awamu ya Tano katika Sekta mbalimbali za maendeleo lakini hasa hasa katika sekta ya afya” alishukuru Makamu wa Rais.

Makamu wa Rais alisema kuwa Balozi wa Kuwait Mhe. Jasem Al Najem amekuwa mstari wa mbele katika kuendeleza sekta ya Afya hapa nchini ambapo leo wamesaidia vifaa vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 258 ambavyo vitaiwezesha Taasisi kuimarisha utoaji wa huduma ya upasuaji hasa kwa watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi.

Makamu wa Rais amlisema msaada huo utaiwezesha Taasisi kuwa na chumba cha upasuaji ambacho kitakuwa maalum kwa watoto tu, hivyo idadi ya wagonjwa watakaopata huduma ya upasuaji itaongezeka kutoka 500-700 kwa mwezi, kufikia zaidi ya wagonjwa 1000 kwa mwezi na watahudumiwa kwa haraka zaidi.

Wakati huo huo Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Faustine Ndugulile  amesema Tanzania iatendelea kuimarisha uhusiano na nchi ya Kuwait kwani wamekuwa mstari wa mbele katika kutoa msaada haswa msaada inayohusu sekta ya afya.

Balozi wa Kuwait hapa nchini Mhe. Jasem Al Najem alisema kuwa Wananchi wa Kuwait wana mapenzi makubwa na Watanzania na kuahidi wataendelea kutoa msaada.

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Alhamisi ya May 17

Wageni Wanaoingia Nchini Waanza Kupimwa Ebola

$
0
0
Serikali Kagera imeanza kuwapima watu wanaoingia kutoka nchi jirani kupitia mkoa huu, ili kubaini kama wana maambukizi ya ugonjwa wa ebola.

Hatua hiyo inafuatia kutangzwa kwa mlipuko wa ugonjwa huo kaskazini magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Manispaa ya Bukoba jana, Kaimu Ofisa Afya Mkoa wa Kagera, Geraz Ishengoma alisema kuwa kila mgeni anayeingia nchini anapimwa na anayeonekana ana dalili zinazofanana na ugonjwa huo, hupelekwa kupimwa zaidi.

Ni mara ya pili katika mwaka mmoja kwa serikali kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya ebola. Mei 29, mwaka jana Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsi, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alisema wageni kutoka nchi hiyo wangesajiliwa na kufuatiliwa hadi wanakoishi ili kujiridhisha kama hawana virusi vya ebola.

Kaimu Ofisa Afya Mkoa wa Kagera, Ishengoma alisema jana: “Tumeweka kambi katika maeneo ya mpakani hasa Mutukula, Murongo, Kabanga na Rusumo, (na) kila mtu anayeingia anapimwa ikiwamo joto la mwili.

"Tunayekuwa na shaka naye, tunamtenga na kumchunguza zaidi.”

Alisema kuwa kambi hizo za mpakani ziliwekwa baada ya serikali kutangaza kuwapo kwa ugonjwa huo DRC Mei 8, mwaka huu, na kuwa hadi sasa hakuna mtu yeyote aliyebainika kuwa na maambukizi ya virusi vya ugonjwa huo.

Alisema virusi vya ugonjwa huo vinaambukizwa kwa kugusa damu au majimaji, kugusa maiti ya mtu aliyekufa kwa ugonjwa huo na kugusa wanyama wenye maambukizi, na kuwa dalili zake huanza kuonekana kuanzia siku mbili hadi 21 tangu mtu anapoambukizwa.

Ishengoma alitaja dalili za ugonjwa huo kuwa ni homa kali, kulegea mwili, kichwa kuuma kunakoambatana na kutapika na kutokwa na damu sehemu tofauti za mwili, ikiwamo puani.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali mstaafu Salum Kijuu, alisema serikali imechukua kila tahadhari ili kuhakikisha ugonjwa huo hauingii nchini kupitia mkoa wa Kagera.

“Kumbukeni Kagera ni mkoa ambao unapakana na nchi nyingi, zikiwamo za Rwanda, Burundi na Uganda, lakini pia unapakana na mkoa wa Kigoma ambao watu kutoka Congo hupitia katika mkoa huo na kuingia Kagera hasa kupitia eneo la Murusagamba,” alisema.

Kijuu aliwataka wananchi kutoa taarifa haraka endapo watabaini kuwapo kwa mtu mwenye dalili kama za ebola katika maeneo yao, ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa.

“Lakini pia wananchi hawapaswi kugusana na mgonjwa mfano kugusa mate, majimaji na damu, kuepuka kugusa maiti, kutochelewa kupata huduma na kuzingatia usafi wa mwili,” alisema.

Alisema kuwa serikali inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali, ili kuhakikisha ugonjwa huo hauingii nchini.

TRA Yatishia Kuuza Makontena 20 ya Paul Makonda

$
0
0
Mamlaka ya Mapato (TRA), imetangaza kusudio la kupiga mnada kontena 20 za Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, ikiwa atashindwa kuzilipia ushuru na kuzichukua ndani ya siku 30 kuanzia Jumatatu.

Kontena hizo za Makonda ambazo zimesubiri utaratibu wa kuzitoa TRA kwa zaidi ya siku 90 zinazokubalika kwa mujibu wa sheria za kodi, zimesheheni samani za ndani na ofisini.

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo, jana alisema kuwa kwa kawaida bidhaa zote zinapoagizwa na kufika bandarini zinatakiwa kuondolewa ndani ya siku 90.

Kayombo alisema inapotokea muda huo ukapita bila wahusika kuondoa mizigo yao, hujulishwa na mamlaka hiyo kwa kupewa notisi ya siku 30 ili waondoe.

Kwa mujibu wa tangazo la TRA lililotoka kwenye vyombo vya habari Jumatatu, Mamlaka hiyo imetoa notisi ya siku 30 kwa wateja nane akiwamo "Paul Makonda" ambao mizigo yao imekaa bandarini zaidi ya muda unaotakiwa.

Katika tangazo hilo, Kamishna wa Idara ya Kodi ya Ushuru wa Forodha na Bidhaa, ametoa siku 30 kwa wamiliki wa mali mbalimbali zilizopo katika ghala la TRA kwenda kuzichukua la sivyo baada ya muda huo zitapigwa mnada kwa mujibu wa sheria na utaratibu wa ushuru wa forodha.

Kayombo alisema kuwa, mzigo unapopitiliza muda wa kukaa bandarini, TRA huwakumbusha wahusika kwa kuwapa notisi kama ya siku hiyo.

"Tumetoa tangazo hili ili kontena ambazo ziko bandarini ambazo zimepitiliza siku 90 wahusika waende kuziondoa; wasipotekeleza ndani ya muda tuliowapa tutazipiga mnada kwa mujibu wa sheria," alisema.

Kayombo alisema nyaraka za bidhaa hizo ziko sawa tatizo ni muda wa kuziondoa bandarini hapo ndiyo haujafuatwa.

"Siwezi kusema kama wameshindwa kulipa kodi au la lakini hata ikitokea bidhaa ambazo zina msamaha wa kodi zimekaa zaidi ya siku zilizowekwa na wamiliki wakapewa notisi bila kutekeleza, muda wa notisi ukiisha bidhaa husika hupigwa mnada na kwenye hili hatuangalii bidhaa zimetoka wapi, ni msaada au sio msaada," alisema Kayombo.

"Bidhaa ikipitiliza siku za kukaa bandarini kwa mujibu wa taratibu, tunatangaza bila kuangalia zimeagizwa na nani, kuna nini ndani yake, zimelipiwa ama hazijalipiwa kama hazijaondolewa bandarini, tunatangaza, ndivyo tulivyofanya."

Kibatala Aiomba Mahakama Ifute Mashtaka Kesi ya Mbowe na Wenzake

$
0
0
Upande wa utetezi katika kesi ya uchochezi inayowakabili viongozi tisa wa Chadema akiwemo Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe, umeomba Mahakama ya hakimu Mkazi Kisutu kutupilia mbali mashtaka dhidi ya washtakiwa kwa kuwa yanamapungufu, kisheria.

Maombi hayo yamewasilishwa jana Mei 16, 2018 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilabard Mashauri na Wakili Peter Kibatala, ambaye aliwasilisha mapingamizi nane ya kisheria ‘yanayoshambulia’ uhalali wa hati ya mashtaka na mashtaka dhidi ya washtakiwa.

Katika Mapingamizi hayo, Kibatala alidai, kibali cha DPP kina mapungufu ya kisheria kwa sababu haioneshi imetolewa kwa mashtaka yapi na pia hati ya mashtaka imewataja majina washtakiwa wote bila ya kufafanua na pia imetaja tu kifungu cha sheria ambacho washtakiwa wameshtakiwa nacho huku akidai pia kwamba, hakuna kibali kilichowasilishwa mahakamani hapo kwa maana hiyo mashtaka dhidi ya washtakiwa yamepelekwa mahakamani hapo bila ridhaa ya DPP.

Aidha, Kibatala alitoa ombi mbadala na kuomba, iwapo mahakama itashindwa kuifuta hati nzima ya mashtaka yanayowakabili washtakiwa hao basi iyafutilie mbali mashtaka ambayo yanamapungufu kisheria, likiwamo shtaka la nne, latano, la sita na la saba.

Alidai, maelezo ya mashtaka hayo yanawachanganya washtakiwa na hawawezi kujitetea ipasavyo, pia mashtaka hayo kufunguliwa kwake kunahitaji ridhaa ya (DPP) ambayo haipo kutokana na mapungufu hayo, inaonesha hakuna ridhaa yake.

“Kwa kuwa mashtaka hayo tajwa kufunguliwa kwake kunahitaji ridhaa ya DPP, lakini kuwa haipo tunaomba yafutiliwe mbali. Hati ya mashtaka inamapungufu kwa sababu shtaka la pili na la tatu hayana maelezo ya kutosheleza ya kuwapa washtakiwa msingi na uwezo wa kuweza kujitetea kikamilifu katika kesi hiyo ya jinai.

“Katika shtaka la kufanya mkusanyiko bila kibali hati haijataja watu waliotishiwa na kwamba wametajwa kwa wingi hivyo haijulikani ni washtakiwa ama ni watu wengine. Mashtaka yanayowakabili washtakiwa yamejichanganya na hayaonyeshi walipelekeaje kifo cha Akwilina na hao majeruhi walijeruhiwa na nani na kwa kutumia nini,” alisema Kibatala.

Amedai maelezo katika hati ya mashtaka yamerundikana kiasi kwamba ni vigumu mtu kujitetea na kwamba unapomshtaki mtu kwa kisababisha kifo ni lazima utoe Maelezo ya kutosha kuonesha unamaanisha kitu Fulani ili mtu aweze kujitetea.

Alidai mapungufu mengine yaliyomo kwenye hati hiyo ni kuwa hayaoneshi dhumuni la pamoja ambalo washtakiwa walikutana kulitenda hivyo linawanyang’anya washtakiwa haki ya kujitetea. Kibatala alidai kuwa hati ya mashtaka inamapungufu kwa sababu vifungu vilivyotajwa katika shtaka la Tatu, tano na saba siyo sahihi.

Alidai kuwa katika shtaka la kumi, kumi na moja na kumi na mbili yanamapungufu kisheria kwa sababu hayaonyeshi watu waliochochewa kufanya makosa ni wakina nani waliohudhuria mkutano, wakazi wa Kinondoni ama wapiga kura bila kujali itikadi zao.

Akijibu mapingamizi hayo, Wakili wa serikali Mkuu, Paul Kadushi aliiomba mahakama kuyatupilia mbali mapingamizi yote hayo ya upande kwa kuwa hayana mashiko kisheria.

Kuhusu kibali cha DPP kinachoipa mahakama ridhaa ya kusikiliza kesi, Kadushi alidai kuwa hakuna uamuzi wowote ulioweka msingi kwamba ni lazima kiwepo na nini ama hakipaswi kuwepo.
 
Akiahirisha kesi hiyo, hakimu Mashauri alisema atatoa uamuzi kuhusu pingamizi hizo Juni 11, mwaka huu.

Mbali na Mbowe ambaye ni mwenyekiti wa Chadema, washtakiwa wengine ni mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa; naibu katibu mkuu wa chama hicho Zanzibar, Salum Mwalimu; na wa Bara ambaye pia ni mbunge wa Kibamba, John Mnyika.

Wengine ni mbunge wa Tarime Mjini Esther Matiko; katibu mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji; mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche; mbunge wa Kawe, Halima Mdee na wa Bunda, Ester Bulaya.

TRA Yakamata Malori Yenye Bidhaa za Magendo

$
0
0
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imekamata malori mawili yenye bidhaa mbalimbali eneo la Loliondo Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha kupitia njia ya magendo yakitokea nchini Kenya zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 20.

Akizungumza jana jijini Arusha, Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Charles Kichere alisema kuwa, malori hayo yenye namba T 985 AJP na T 840 ABF yalikamatwa usiku wa tarehe 10 Mei, 2018 na kusisitiza kuwa wafanyabiashara wenye bidhaa hizo wamevunja sheria kwa kuwa hawakulipa kodi stahiki kama inavyotakiwa.

Kichere alifafanua kuwa, wafanyabiashara wenye bidhaa hizi zilizokamatwa, wamevunja kifungu cha sheria namba 82 na 200 cha Sheria ya Usimamizi wa Kodi ya Mwaka 2015 na Sheria ya Forodha ya Afrika Mashariki ya Mwaka 2004.

"Kwa ujumla bidhaa hizi zote zina thamani ya shilingi 20,037,330.15 ambayo kodi ya bidhaa hizi ni shillingi 28,524,758.11 na adhabu au faini ya bidhaa hizi ni shilingi 10,768,665.08. Hivyo jumla ya mapato
yanayotakiwa kulipwa Serikalini ni shilingi 39,293,423.19," Kichere.

Ameongeza kuwa "Hivyo kwa Sheria hizo, wafanyabiashara hawa wanatakiwa kulipa kodi pamoja na faini ya shilingi milioni 39 na magari yao kutaifishwa".

Amezitaja bidhaa zilizokamatwa kuwa ni pamoja na mifuko 362 ya sukari yenye uzito wa kilo 50 kila mmoja, maboksi 40 ya mafuta ya kula yanayoitwa Karibu, maboksi matatu ya mafuta ya kula yanayoitwa Daria, magaloni 100 ya mafuta ya kula yanayoitwa Nyata na maboksi matatu ya viungo vya mboga

Kufuatia tukio hilo, Kamishna Mkuu Kichere amewakumbusha wafanyabiashara wote kuzingatia taratibu za uingizaji bidhaa nchini ili kuepuka hasara kwenye biashara zao na kuongeza kuwa, TRA haitavumilia ukiukwaji wowote utakaofanywa na wafanyabiashara kwa kutozingatia sheria na taratibu hizo.

Serikali: Malipo ya mawakala ni baada ya uhakiki

$
0
0
Serikali imesema itawalipa mawakala wote wa pembejeo za kilimo baada ya vyombo vya uchunguzi kukamilisha uchunguzi wa watumishi waliodanyanga kuhusu malipo na uhakiki wa madeni unaendelea.

Akijibu baadhi ya hoja za wabunge waliozitoa wakati wakijadili bajeti ya wizara ya kilimo ya mwaka 2018/19, jana jioni Mei 16, 2018, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji alisema malipo ni mara baada ya uchunguzi kukamika.

“Nani kaiibia Serikali, katika maombi haya vyombo vya uchunguzi vipo kazini, sisi kama wabunge wasimamizi wa rasilimali, vyombo vya uchunguzi ni muhimu na kama ni mtumishi nani aliongeza sifuri katika milioni 20 ikawa bilioni, fedha si tatizo na tutawalipa wote wanaoidai Serikali,” alisema Dk Kijaji

Kuhusu kutengwa kwa bajeti kidogo, Dk Kijaji alisema Serikali inatambua umuhimu wa sekta ya kilimo lakini utengaji wa bajeti unategemea rasilimali zilizopo.

“Rasilimali ziko chache kuliko mahitaji, sote tupo hapa, mlisema bajeti ya afya iongezwe, maji iongezwe na ifahamike Serikali inatoa kipaumbele kwa kilimo na sisi tunatambua kuwekeza katika kilimo,” alisema Dk Kijaji

Alisema miongoni mwa jitihada hizo ni kuiwezesha Benki ya Kilimo: “Tumewekeza Sh60 bilioni na mpaka sasa wana Sh66 bilioni, wameweza kuongeza kiwango hiki katika utendaji wetu na tumechukua mkopo zaidi ya Sh250 bilioni na kuipa benki hii.”

Akigusia benki hiyo kuwa jijini Dar es Salaam, alisema mwezi huu itafungua tawi jijini Dodoma, Juni jijini Mbeya na Julai jijini Mwanza na dhamira yetu ni kuwafikia wananchi kule waliko.

Kwa upande wake, Naibu waziri wa Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Joseph Kakunda alitoa maagizo kwa maofisa kilimo kutoka ofisini na kwenda kuelimisha wakulima na wale watakaoshindwa watachukuliwa hatua.

“Lazima wakulima wapate haki yao ya elimu kuhusu kilimo na utaratibu wa kusubiri posho ili aende kufanya kazi yake tumeshapiga marufuku,” alisema Kakunda.

Kakunda alisema, “maofisa ushirika lazima wahakikishe wanafanya mapitio ya vyama vya ushirika ili kujua kama utendaji ni mzuri na kama ni mbovu wavifute na kuvisajili upya.”

“Maofisa ugani wafanye kazi ya kuwatambua wakulima wote ili Serikali ifanye maandalizi ya haraka ya kuandaa pembejeo, walio chini ya Tamisemi wapate huko hizi taarifa na uzembe hautavumiliwa,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso alisema Serikali imetenga zaidi ya Sh29 bilioni kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji na, “sisi kama wizara tutalisimamia hili na tunaahidi kushirikiana vizuri na wadau wa wizara ya kilimo.”

Wabunge wataka vyama vya ushirika viondolewe, mahindi kuuzwa nje ya nchi

$
0
0
Wabunge wameitaka Serikali kuviondoa vyama vya ushirika na kuruhusu uuzwaji wa mahindi nje ya nchi.

Hayo wameyasema jana  jioni Mei 16, 2018 wakati wakichangia bajeti ya wizara ya kilimo ya mwaka 2018/19 bungeni jijini Dodoma.

Mbunge wa Magu (CCM), Kiswaga Destery alisema, “kuna tatizo, wananchi wanalalamika, wabunge wanalalamika, wananchi wamebaini wanaowapeleka katika ushirika ni sisi wabunge na viongozi.”

“Suala la ushirika wabunge wamelalamika wasikilizeni. Viongozi wa ushirika na wahasibu wametumia rushwa kupita, wanakwenda kuwaibia wakulima na wanunuzi wa pamba, mikataba tuliyonayo ni ya kukopa,” aliongeza.

Alisema, “viongozi wamechaguliwa na watu saba au kumi, bora wangechaguliwa na wananchi, mtawapa shida ma DC (wakuu wa wilaya), wakuu wa mikoa, hakuna kazi watakayokuwa wanaifanya zaidi ya kulinda wezi.”

Kuhusu zuio la mahindi, Destery alisema, “wabunge wanalalamika mahindi hapa, bila kuweka utaratibu yataoza, ni vizuri serikali ikafungua na mahindi haya yakiuzwa ndio mchango wenyewe na ndio maendeleo.”

Mbunge wa Mlimba (Chadema), Susan Kiwanga alisema, “inasikitisha sana kuona kilimo kinaachwa kiholela holela, unaanzaje kumzuia mtu asiuze nje, ninyi vipi mlitugea ninyi mtaji.”

Alisema wanapolima na kupata fedha “ndipo tunakwenda kuchangia huduma za jamii, sasa tunawezaje kujenga kama hatuna fedha.”

Kiwanga alisema, “huu ushirika ni kama janga la taifa, Serikali imechukua hatua gani kwa wale viongozi walioharibu ushirika, kama hamjachukua hatua mtawafunga wengi na mtagombana na wengi sana.”

Alisema bajeti ya kilimo iongezeke, masoko yawe wazi, mkulima aweze kuuza kokote na kama mnataka kudhibiti wekeni mazao yenu lakini si kwa fedha zake.

Mbunge wa Urambo (CCM), Margaret  Sitta alihoji kama wizara ya kilimo ina kalenda ya misimu ya kilimo kwa kila mkoa kwani imezoeleka mbolea kuwafikia wakulima kipindi cha kupalilia.

“Katika mazao yenye matatizo ni tumbaku, tumbaku inaiingizia nchi hii zaidi ya asilimia 40 ya fedha za kigeni. Hii changamoto tumekuwa tunazungumza kila tunapopata nafasi, tatizo ni nini,” alihoji Sitta

Mwenyekiti BAVICHA: Tundu Lisu Ni Hazina ya Tanzania, Tunataka Akirudi Asiwe Mtu wa Clinic Tena

$
0
0
Mwenyekiti wa Baraza la Vijana CHADEMA, Patrick Ole Sosopi amesema kwamba hawataki Mwanasheria wa chama chao, Tundu Lissu  akirudi Tanzania  awe mtu wa kuhudhuria kliniki kwa ajili ya matibabu bali wanatarajia aingie kwenye 'struggle' moja kwa moja.

Ole Sosopi ameyasema hayo jana  wakati akijibu swali kwenye Kipindi cha Kikaangoni kinachorushwa na EATV,  na kuongeza kwamba wanatarajia kiongozi wao atarudi nchini mara tu atakapomaliza matibabu yake anayoendelea nayo huko nchini Ubelgiji.

"Tundu Lissu tunataka akirudi asirudi ku-atend clinic, aje aingie kwenye mapambano moja kwa moja. Lissu ni kama kaka kwangu, alipopigwa risasi nilifadhaika sana, mpaka kesho nawaza hawa watu walikuwa na dhamira gani" Ole Sosopi.

Aidha Mwenyekiti huyo ameongeza kuwa "Lissu ni 'asset' kwa Tanzania na Mungu amemponya kutuonyesha, na ndio maana yupo mpaka leo". 

Lissu ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki na Mwanasheria wa Chadema alipigwa risasi na watu wasiojulikana Septemba 7, 2017 alipokuwa kwenye maeneo ya nyumbani kwake Area D Jijini Dodoma wakati alipokuwa akirejea kutoka katika majukumu yake.

Watanzania Watakiwa Kutumia Takwimu Zinazotokana na Sensa Mbalimbali Kujiletea Maendeleo

$
0
0
Na: Lilian Lundo – MAELEZO, Dodoma.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.  Luhaga Mpina amewataka Watanzania  kutumia takwimu za sensa mbalimbali  zinazotolewa na ofisi ya Taifa ya Takwimu ili kuongeza tija na hatimaye kupunguza umasikini nchini.

Mhe. Mpina ametoa wito huo jana Jijini Dodoma, alipokuwa akizindua matokeo ya utafiti wa Kilimo wa mwaka 2016/2017 ukiwa ni utafiti wa pili kufanyika nchini ambapo wa kwanza ulifanyika mwaka 2014/2015.

“Tunapenda kufanya sensa lakini mwisho wa siku hakuna anayetumia sensa hiyo. Huwezi kufanya mapinduzi ya kiuchumi bila ya kutumia matokeo mbalimbali ya tafiti,” alisema Mhe. Mpina.

Aliendelea kusema, matokeo ya tafiti hizo yametumika katika kupima mchango wa shughuli za kilimo katika Pato la Taifa, ambapo takwimu zinaonesha kuwa mwaka 2014 uchumi ulikuwa kwa asilimia 7.10 wakati mwaka 2017 uchumi ulikuwa kwa asilimia 7.1. Aidha mchango wa shughuli za kilimo kwa mwaka 2014 ulikuwa asilimia 28.8 wakati mwaka 2017 ulikuwa asilimia 30.1.

Vile vile amesema, matokeo ya utafiti yanaonesha kuwa zao la mahindi mwaka 2016/2017 uzalishaji wake ulikuwa tani 5,766,984 na kwa takwimu za utawala za mwaka 2017/2018uzalishaji ni tani 6,681,000. Katika mwaka 2017 ongezeko la thamani ya shughuli za kilimo cha mazao iliongezeka na kufikia shilingi trilioni 5.3 kutoka shilingi trilioni 5.1 mwaka 2016.

Mhe. Mpina amesema, kwa upande wa Tanzania Baramkoa wa Mbeya umeendelea kuongoza katika uzalishaji wa zao la mahindi kwa tani 578,280 (10%) wakati Mkoa wa Morogoro umeongoza.

Aidha kwa upande wa mifugo, Tanzania Bara inaidadi ya ng’ombe 30,496,687, mbuzi 18,947,657, kondoo 5,565,468 na kuku wa asili 38,595,106 ambapo mikoa inayoongoza kwa asilimia kubwa ya ng’ombe ni pamoja na Tabora (8.7%), Mwanza (7.9%) na Manyara (7.2%). 

Tanzania Zanzibar ina idadi ya ng’ombe wapatao 175,314, mbuzi 107,993, kondoo 517 na kuku wa asili 1,754,786 na mikoa inayoongoza kwa asilimia kubwa ya ng’ombe kwa Tanzania Zanzibar ni Kaskazini Pemba (30.3%) ikifuatiwa na Kusini Pemba (19.9%).

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Dkt. Albina Chuwa amewaomba watumiaji wa takwimu hizo kuzitumia kwa manufaa ya kufuatilia na kutathimini mipango ya maendeleo ya sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi na si vinginevyo.

Hata hivyo amesema, Tanzania bado ni nchi ya pili katika Bara la Afrika kwa kuwa na mifugo mingi hivyo ni dhahiri kuwa uwezo wa viwanda vya nyama hapa nchini  na kuuza nyama na bidhaa zake zinazozalishwa kwa lengo la kujipatia fedha za kigeni.

Halmashauri Zatakiwa Kutumia Fedha za Mgawo wa Ada ya Wanyamapori Kutoa Ulinzi kwa Wananchi

$
0
0
Na: Lilian Lundo – MAELEZO, Dodoma.
Serikali  imezitaka Halmashauri za Wilaya Nchini zinazopata mgawo wa mapato yatokanayo na ada ya wanyamapori wanaowindwa kwenye vitalu kutumia asilimia 40 ya fedha hizo kwa ajili ya uhifadhi ikiwa ni pamoja na ulinzi wa maisha ya wananchi na mali zao dhidi ya wanyamapori wakali kama ilivyokubalika.

Hayo yameelezwa jana Bungeni, Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Japhet Hasunga alipokuwa akijibu swali la mbunge wa Viti Maalum Mhe. Leah Jeremiah Komanya juu ya lini Serikali itaanza kupeleka takwimu ya mapato yanayopatikana ili Halmashauri ziweze kujua stahiki zake.

“Takwimu za mapato yanayotokana na wanyamapori waliowindwa na upigaji picha katika vitalu  vya uwindaji na utalii wa picha nchini huandaliwa na kutolewa taarifa mbalimbali,” alisema Mhe. Hasunga.

Aidha amesema, Wizara imekuwa ikitoa mgawo wa asilimia 25 ya mapato yatokanayo na ada ya wanyamapori wanaowindwa kwenye vitalu vilivyopo kwenye maeneo ya wilaya husika.

Hata hivyo amesema, Wizara ipo katika hatua za mwisho za kukalisha mfumo wa kielektroniki  ujulikanao kama “MNRT Portal” ambapo taarifa zinazohusu Wizara ikiwa ni pamoja na mapato ya uwindaji wa kitalii zitapatikana humo .

Mfumo huo unatarajiwa kuzinduliwa rasmi tarehe 01 Julai, 2018 ambapo nakala ngumu za taarifa zitakuwa zikitumwa kwenda wilaya husika.

Wakati huo huo Mhe. Hasunga alipokuwa akijibu swali la mbunge wa Viti Maalum Mhe. Maryam Salum Msabaha juu ya mkakati wa Serikali katika kuboresha vivutio vya utalii nchini ikiwemo Bagamoyo ili kupata wageni wengi zaidi na kukuza pato la Taifa, amesema Wizara imeandaa mkakati wa kuvitambua na kuvitangaza vivutio vyote nchini ukiwemo mji wa Bagamoyo.

Amesema mpango unalenga kushirikisha mashirika yaliyo chini ya Wizara yaani Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAMWA) na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).

Ameendelea kusema,  vituo vya malikale vilivyopo Bagamoyo ni miongoni mwa maeneo yatakayoendelezwa kwa ushirikiano wa Mashirika hayo. Aidha, vivutio vyote vya utalii nchini vitaendelea kutangazwa kupitia Taasisi zinazohusika ikiwemo Bodi ya utalii Tanzania (TTB).

Ametaja kazi zitakazotekelezwa na mashirika hayo kuwa ni kuweka huduma muhimu kwa watalii, kuboresha miundombinu ya vituo hususani majengo na barabara ili kuwezesha kufikika kwa urahisi na kuwa na muonekano unaovutia , kujenga vituo vya kumbukumbu na taarifa pale ambapo vinahitajika, kuboresha vioneshwa na kuvitangaza , kuhamasisha wawekezaji wa hoteli, michezo na vivutio vingine vya watalii.

Hata hivyo, Wizara ya MaliAsili na Utalii itaendelea kusimamia majukumu yote ya uhifadhi, utafiti na kuandaa taarifazitakazosaidia kuboresha na kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini, kwa kutoa elimu kwa Umma juu ya uhifadhi na matumizi endelevu ya malikale na maliasili za nchi yetu.
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live


Latest Images