Quantcast
Channel: MPEKUZI
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live

Maalim Seif Aitaka Serikali Isamehe Baadhi ya Kodi Katika Kipindi Hiki cha Ramadhani

$
0
0
Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF, Maalim Seif Sharif Hamad ameitaka serikali iliyopo madarakani visiwani Zanzibar inayoongozwa na Dkt. Ali Mohamed Shein iwahurumie wananchi hasa katika kipindi cha mfungo wa mwezi wa Ramadhani.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi za CUF Vuga mjini Zanzibar, amesema kuwa waliopo madarakani wasiwe hodari kuwataka wafanyabiashara wasipandishe bei za bidhaa wanazouza lakini na wao kodi ambazo hazina tija, zinawakamuwa wananchi waweze kuzipunguza.

"Ni vyema kujifunza kwa serikali ya Kenya ambayo imeweza kuondoa kodi kwa wafanyabiashara wale wote ambao watafanya biashara ya tende katika Mwezi wa Ramadhani", amesema Maalim Seif.

Aidha, Maalim Seif amewataka wananchi kufanya mambo ya kheri katika mwezi huo na kuacha kulumbana, kutoleana maneno yasiyofaa kwani mwezi huo ni mwezi wa rehema hivyo ni vyema kufanya mambo ya kheri yanayompendeza Mungu.

"Ni vyema kupendana,kusaidiana, kuhurumiana,kuacha kugombana na kutohasimiana ili kupata fadhila za Mwezi Mungu", amesisitiza Maalim Seif.

Kwa upande mwingine, Maalim Seif amewataka wafanyabiashara wasiuchukulie kwamba mwezi wa Ramadhani kama ni msimu wa kupata faida ya kupindukia na badala yake wauchukulie ni mwezi wa kuchuma thawabu kwa lengo la kuwasaidia wananchi hasa masikini.

Switzerland Yaahidi Kuimarisha Uhusiano Wa Kimaendeleo Na Tanzania

$
0
0
Switzeland imeahidi kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kusaidia Sekta mbalimbali za Maendeleo hasa katika suala la Afya, kuongeza ajira na kukuza ujuzi .

Hayo yamebainishwa wakati wa Mkutano Jijini Dodoma kati ya Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Philip Isdor Mpango na Balozi wa Switzerland hapa nchini Bi. Florence Tinguely Mattli, ulioangazia uhusiano kati ya nchi hizo mbili na namna ya kuboresha ushirikiano.

Katika Mkutano huo Waziri Mpango amemuomba Balozi huyo kuangalia uwezekano wa kuwapa mafunzo madaktari Bingwa nchini ili kukidhi uhitaji uliopo hasa katika Jiji la Dodoma ambalo ndio makao Makuu ya Nchi na  idadi ya wakazi wake inaongezeka, na pia kufadhili mafunzo kwa Watumishi wa umma ili kuwajengea uwezo katika kada mbalimbali lengo likiwa ni  kuongeza ufanisi wa kazi.

Aidha waziri Mpango aliongeza kuwa miundombinu ya Jiji la Dodoma inahitaji kuboreshwa hivyo Switzerland iangalie uwezekano wa kufadhili miradi ya maendeleo katika Sekta ya Maji na mazingira.

 “Tanzania ni nchi ya tatu kwa kuwa na mifugo mingi Barani Afrika lakini ufugaji wa mifugo hiyo hauna ubora, kwa kuwa Switzerland imeendelea katika Sekta ya Mifugo fursa ipo ya uwekezaji katika eneo hilo hapa nchini” alieleza Dkt. Mpango.

Amesema kuwa Serikali ya Tanzania inafanya jitihada mbalimbalimbali kukabiliana na umasikini hivyo ni vema Washirika wa Maendeleo wakatambua kuwa hatua mbalimbali ambazo Serikali inazichukua kama kupambana na wakwepa kodi na kuboresha mikataba zina lengo la kuboresha maisha ya watanzania  kwa kuhakikisha wananufaika na rasilimali nyingi zilizopo nchini na wawekezaji waweze kunufaika pia.

Waziri Mpango amesema kuwa Switzerland inashiriki kikamilifu katika  miradi ya Matumizi bora ya misitu hususani Mkoani Morogoro, kuboresha ujuzi na kukuza ajira kwa Watanzania.

Kwa upande wake Balozi wa Switzerland nchini Bi. Florence Tinguely Mattli, amesema kuwa Uhusiano kati ya Nchi yake na Tanzania umezidi kuimarika na kuahidi kuendelea kuisaidia Tanzania  katika sekta mbalimbali za maendeleo huku akisisitiza suala la kuzingatia  uwazi na mazingira bora ya uwekezaji  kwa kuwa ni chachu kubwa ya kuvutia uwekezaji wenye tija kwa pande zote mbili.

Dkt. Mpango amemhakikishia Balozi huyo kuwa Serikali inatoa na itaendelea kutoa ushirikiano unaohitajika katika suala la uwekezaji kwa kuwa Tanzania inaongozwa  kwa utawala wa sheria unaozingatia haki.

Imetolewa  na ;
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Fedha na Mipango

Biblia na Qur'an Tukufu kutozwa kodi

$
0
0
Serikali ya Uganda imeagiza kuanzia sasa vitabu vitakatifu vya Biblia na Quran vinavyoingizwa nchini humo vilipiwe kodi.

Viongozi wa Kidini kutoka madhehebu hayo mawili makubwa nchini humo wamepokea uamuzi huo kwa tahadhari kubwa na mshangao huku wakisisitiza kwamba, vitabu hivyo vya kidini havipaswi kutozwa kodi kwani vinatumika kujenga na kuimarisha imani za kiroho za wananchi wa Uganda.

Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislaam Nchini Uganda, Ramadhan Mugalu, ameikosoa serikali kwa kusema kuwa, hatua hiyo imevuka mipaka, na kuhoji inawezaje kutoza kodi neno la Mungu?

Kwa upande wake Kamishna wa Makanisa nchini humo, Mchungaji Joram Kahenano, amesema Kanisa lake litalazimika kuongeza bei ya Biblia moja kutoka shilingi za Uganda elfu tatu hadi elfu 18 ili kufidia gharama za kodi.

Kwa mujibu wa gazeti la Daily Monitor, uamuzi huo umetolewa baada ya miezi kadhaa ya majadiliano kati ya Mamlaka ya Kodi na Taasisi za Kidini.

Mizengo Pinda Atoa Ushauri Kuhusu Tanzania ya Viwanda

$
0
0
Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda amezitaka taasisi za elimu na mafunzo kuhakikisha mageuzi ya kiuchumi yanafanyika nchini kwa kutoa elimu.

Mhe. Pinda ametoa ushauri huo jijini Dar es Salaam leo wakati wa uzinduzi wa Kituo cha Taaluma kuhusu nchi ya China kijulikanacho kama Centre for Chinese Studies yaani CCS, kituo ambacho ni sehemu ya taasisi za Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Mh. Pinda amesema mageuzi ya kiuchumi hususani kupitia ukuaji wa sekta ya viwanda, yanahitaji kuwa na jamii inayopenda kufanya kazi kwa bidii na iliyo tayari kubadilika kifikra.

Uzinduzi wa kituo hicho umefanywa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt Augustine Mahiga, ambaye amesema Tanzania ina uhusiano mzuri na nchi ya China lakini inasikitisha kuona kwamba bado kama nchi haijatumia ipasavyo fursa ambazo taifa la China imezitoa kwa Tanzania.

Aidha kituo hicho kilichozinduliwa kimeelezewa kuwa  jukumu lake ni kukuza uhusiano kati ya China na Tanzania pamoja na kutumia mafanikio iliyoyapata nchi ya China kwa ajili ya kuharakisha mageuzi ya kiuchumi.

Rais Magufuli kuwakabidhi Simba kombe la VPL

$
0
0
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, huenda akawa mgeni rasmi katika mchezo Simba SC dhidi ya Kagera Sugar FC utakaopigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Mei 19 2018.

Kwa mujibu wa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), Wallace Karia, wamemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.Dkt.John Magufuli akabidhi Kombe la Ubingwa wa Cecafa kwa Vijana Mei 19 Uwanja wa Taifa,Maombi ambayo yamepitishiwa kwa Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mh.Dkt.Harrison Mwakyembe.

Karia ameeleza kuwa Rais Magufuli atapata wasaa wa kukabidhi kombe la 19 mabingwa wapya wa Ligi Kuu msimu huu wa 2017/18 ambalo wamelipata wakiwa hawajapoteza mchezo wowote msimu huu.

Sherehe za ubingwa wa Simba na Serengeti Boys zinatarajiwa kuanza majira ya saa 8 mchana huku viiingilio vya mchezo huo (Simba SC vs Kagera Sugar) vikiwa ni 15,000 kwa VIP A, 7000 kwa VIP B na C pia 3000 kwa sehemu ya mzunguko.

Ukiuza sukari zaidi ya 2600 Arusha Jiandae Kulala Selo

$
0
0
Msako wa kamati ya ulinzi na usalama katika maghala ya wafanyabiashara wakubwa umebaini kuwa jijini Arusha kuna mafuta na sukari ya kutosha hivyo ni marufuku kupandisha bei.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 15, 2018 baada ya msako huo jana, Mkuu wa wilaya ya Arusha, Gabriel Daqarro amesema maghala yote ambayo wametembelea licha ya kuwapo uzalishaji mdogo wamebaini bado kuna mafuta na sukari.

"Kamati ya ulinzi na usalama wilaya imetembelea maghala na kuona bado kuna bidhaa na kwa sukari bado bei ya jumla mfuko wa kilo 50 ni kati ya Sh102,000 na Sh110,000,” amesema.

Amesema kutokana  na bei hizo bei ya kilo moja haipaswi kuuzwa zaidi ya Sh2,600 hivyo ambao watauza zaidi watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Daqarro amesema kuhusiana na sukari iliyofungwa bei pia haipaswi kuzidi Sh2,800 na taratibu zinafanywa kuhakikisha bei haiongezeki.

Kuhusiana na mafuta pia amesema yapo ya kutosha ikiwapo ya alizeti licha ya uzalishaji kupungua.

Baadhi ya wakazi  wa Arusha waliomba Serikali kuendelea kudhibiti kupanda bei ya mafuta na sukari hasa kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Jasmin Ally mkazi wa makao mapya amesema katika maduka mengi kati kati ya jiji sukari inauzwa kilo kati ya Sh2,700 na Sh2,800.

Hillal Kusena amesema bei ya mafuta na sukari inaendelea kupanda licha ya matamko ya Serikali.

"Serikali ingefatilia kujua tatizo ni nini kama ni kodi kubwa basi wapunguze lakini kutoa matamko tu hakutoshi," amesema Kusena.

Amesema bei ya mafuta ya kupikia bei ya jumla imepanda kutoka Sh 61,000 hadi Sh 70,000 kwa lita 20 huku lita 10 imepanda kutoka Sh 30,000 hadi Sh35,000.

Mbunge CHADEMA Aishambulia CCM Bungeni

$
0
0
Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Cecilia Paresso amesema wakulima wanatakiwa kutambua kuwa adui yao namba moja ni chama tawala, CCM akisema haiwezekani asilimia 75 ya Watanzania wanaotegemea kilimo, lakini imeshindwa kuwasaidia.

Amesema  Serikali imeshindwa kuwekeza fedha za kutosha katika kilimo huku kwa upande wa asilimia tano ya Watanzania wanaotumia usafiri wa anga ndege zimenunuliwa.

Paresso ametoa kauli hiyo leo Mei 15, 2018 katika mjadala wa bajeti ya Wizara ya Kilimo mwaka 2018/19 ambapo wizara hiyo imeomba kuidhinishiwa Sh170.2bilioni.

Amesema  kwa mujibu wa taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), zinaonyesha ukuaji wa sekta ya kilimo mwaka 2011 ilikuwa asilimia 1.9, mwaka 2012 (3.2), mwaka 2013 (4), mwaka 2014 (3.4), mwaka 2015 (3.2), mwaka 2016 (1.9) na mwaka 2017 kwa asilimia 1.3.

“Sekta hii kama itawekeza vizuri itatoa ajira, kuondoa umasikini na tutafikia hicho mnachosema uchumi wa viwanda, lakini sekta hii imekuwa haipewi fedha kama inavyotakiwa na fedha tunazozitenga hazifiki,” amesema Paresso.

“Serikali ya Awamu ya Nne inaondoka madarakani iliacha kilimo kinakua kwa asilimia 3.2, ila hii Serikali ya Awamu ya Tano inayojiita uchumi wa viwanda, kimeendelea kushuka na kufikia asilimia1.9.”

Amesisitiza, “wakulima wa nchi hii wanapaswa kujua adui yao ni Serikali, asilimia 75 wanategema kilimo lakini asilimia tano ya Watanzania wanaotegemea usafiri wa anga wanawepa ndege. Huku ni kuwahadaa wakulima ambao wanapaswa kujua Serikali ya CCM ndio adui yao.”

Mbunge "Ampa Makavu" Waziri wa Kilimo Bungeni

$
0
0
Mbunge wa Viti MaalumuCCM), Mariamu Ditopile amesemaa Waziri wa Kilimo,  Dk Charles Tizeba amemdanganya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuhusu ununuzi wa tumbaku.

Akichangia bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka wa fedha 2018/19 bungeni leo Mei 15, 2018, amesema Dk Tizeba amemdanganya Majaliwa kwamba wanunuzi wa zao hilo walitaka kununua chini ya dola za kimarekani  0.8.

“Haujatusisimua (kwa bajeti yake) nothing (hakuna kitu),  utashi wako upelekee kukua kwa uchumi wa viwanda lakini  wewe ndiyo unavuruga.

Wanunuzi wanataka kununua Tumbaku kwa dola 1.3 (za kimarekani) lakini wewe unakataa, ukamlisha tango pori waziri mkuu,”amesema.

Amesema ukweli ni kwamba wanunuzi hao walitaka kununua  tumbaku kwa Dola 1.3 ya Marekani lakini waziri wa kilimo alikataa bei hiyo na matokeo yake akasababisha hasara kwa wakulima.

“Wale wakulima hawana vihenge, mvua iliponyesha tumbaku yao ilinyeshewa na mvua matokeo yake wamekuja kuuza chini ya dola 0.8 ya Marekani walichokipata walitumia kulipa madeni,”amesema.

Akizungumzia zuio la kuuza mahindi nje ya nchi, Mariamu amesema: “Mheshimiwa waziri wewe ni swahiba wangu lakini uswahiba wangu hauuzidi wa wakulima. Najua wakulima wanavyotoa jasho na machungu wanayoyapata. Mahindi tunalima kwa ajili ya chakula na biashara. Tumezalisha kwa zaidi ya asilimia 120.”

Hata hivyo, amesema wakulima hao wamekosa soko la mahindi baada ya Serikali kuzuia uuzaji wa mahindi nje ya nchi na kwamba yeye ni mmoja wa waadhirika ambaye amelazimika kuyatupa mahindi baada ya kukosa soko.

Mariamu amesema kuwa wizara hiyo imeleta miche ya mikorosho mkoani Dodoma lakini hakuna mafunzo yaliyotolewa kwa maofisa ugani wala wakulima na kushauri ni vyema Serikali ikawa na mpango wa mazao wa kikanda.

Amesema pia, waziri huyo amekuwa akiwachanganga wakulima kwa kusema kuwa dawa ya kuulia wadudu ya sulpher itatolewa bure kwa wakulima wa korosho lakini baadaye anawataka kulipia.

“Mliombwa mtoe bure? Waliwaambia shida yao ni sulpher? Ghana wameweka mpango baada ya miaka 10 watakuwa wakizalisha korosho ya kutosha. Sisi tunampango wa kulifanya zao hili kuwa endelevu?”amehoji.

Amesema iwapo zao hilo la korosho mkoani Dodoma litastawi kwa asilimia 10 atajiuzulu ubunge.

Mbunge CCM amwaga Machozi bungeni

$
0
0
Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Jacqueline Ngonyani  ‘Msongozi’ ametoa chozi bungeni akiitaka Serikali kuwalipa mawakala wa pembejeo na kuacha kutumia kivuli cha uhakiki wa madeni hayo kutoyalipa.

Akichangia bajeti ya kilimo, leo Mei 15, 2018 bungeni, Msongozi amesema madai hayo yamedumu kwa zaidi ya miaka minne huku baadhi wakifariki kabla hawajalipwa.

“Nashangaa sana mawakala wa pembejeo wanadai miaka minne, walihudumia wakulima wetu na walikwenda kukopa fedha katika taasisi, ambazo sasa zinawadai,” amesema Msongozi.

Huku akishangiliwa na wabunge, Msongozi amesema, “Serikali imekuwa inajificha katika kichaka cha uhakiki, kwa nini hawawalipi? Serikali imekwenda kujificha katika uhakiki, ni uhakiki wa aina gani? Kuna watu wanakufa bila kupewa fedha zao.”

Msongozi akizungumza kwa sauti yenye kuashiria kulia huku mkono wake akiupeleka kufuta uso wake, amesema, “katika nchi hii watu wanatafuta haki zao, kama wameiba kwa nini wasipelekwe mahakamani, kwa nini hawapewi fedha zao, uhakiki gani, mbona watumishi siku mbili walihakikiwa? Kwa nini huku katika mawakala hawalipwi fedha zao.”

Amesema kuna kijana alitaka kujinyonga kwa kudaiwa na taasisi jambo ambalo amesema Serikali ichukue hatua ya kulipa madai kwani wako mawakala saba wamepoteza maisha.”

Msongozi amekuwa mbunge wa tatu kutoka CCM kutokuunga mkono bajeti hiyo akitanguliwa na Richard Ndassa (Sumve) na Mashimba Ndaki (Maswa Magharibi).

Serikali Yaunda Baraza kuchunguza askari wa Tanzania aliyepotea Congo

$
0
0
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi ameziagiza familia za askari waliouawa wakilinda amani Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kumaliza haraka taratibu za mirathi.

Pia, amesema Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Venance Mabeyo amekwisha kuunda Baraza la Uchunguzi, kuchunguza kupotea kwa askari mmoja aliyekuwa akilinda amani DRC.

Waziri Mwinyi ameyasema hayo jana Mei 14 wakati akihitimisha hotuba ya bajeti ya wizara yake ya mwaka 2018/19 ya Sh1.9 trilioni.

Waziri Mwinyi alisema tayari baadhi ya familia za askari hao zimeshakamilisha taratibu za mirathi.

Alisema fedha za mirathi zimetolewa kwa baadhi ya familia lakini zipo baadhi hazijakamilisha taratibu.

 “Familia ambazo hazijakamilisha taratibu za mirathi zikamilishe haraka,” alisema.

Kuhusu askari mmoja aliyepotea siku hiyo ya mapigano Waziri Mwinyi alisema: “Umoja wa Mataifa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, wanaendelea kumtafuta na ikitimia miezi sita kwa Serikali ya Tanzania tutaitisha uchunguzi na Mkuu wa Majeshi ameitisha baraza la uchungizi,” alisema.

Alisema baada ya hapo Mkuu wa Majeshi atatoa taarifa ya kifo. “Lakini huyu kijana amepotea na mpaka sasa anatafutwa, hatuwezi kusema amepotea au yuko hai.” Alisema

Marekani yafungua rasmi ubalozi wake Jerusalem

$
0
0
Marekani imeufungua rasmi ubalozi wake Jerusalem huku Wapalestina zaidi ya 40 wakiuawa na wengine wakijeruhiwa kwenye mapambano na askari wa Israel katika harakati za kuipinga hatua hiyo.

Hatua ya Marekani ya kuuhamishia rasmi ubalozi wake kwenye mji  wa Jerusalem kutoka Tel Aviv imetekelezwa baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump kuitambua Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel.

Aidha, balozi wa Marekani nchini Israel, David Friedman amesema kuwa baada ya miaka 70 ya kuanzishwa kwa taifa la Israel wakati muhimu kama huu ni wa kihistoria kwa sababu ya ujasiri wa mtu mmoja tu ambaye ni rais wa Marekani Donald Trump ameweza kuitambua Jerusalem.

Hata hivyo, Trump amesema kuwa Marekani itaendelea kujitolea kikamilifu katika kuuwezesha mpango wa amani wa Mashariki ya Kati.

Kiongozi wa Kundi la Kigaidi la ADF Uganga Aliyekamatwa Tanzania Afikishwa Mahakamani

$
0
0
Kiongozi wa kundi la waasi la Allied democratic forces Jamil Mukulu, amefikishwa Mahakamani Kuu inayohusika na uhalifu wa kimataifa mjini Kampala, Uganda, Jumatatu miaka 3 baada ya kukamatwa nchini Tanzania.

Kikao cha mahakama cha jana Jumatatu  kilikuwa cha kushauriana jinsi kesi dhidi ya Mukulu na wenzake 38 itaendeshwa.

Akiwa amefungwa pingu mikononi na minyororo miguuni, Jamil Mukulu na wenzake 38 walifikishwa mahakamani chini ya ulinzi mkali wa kikosi cha polisi cha kupambana na ugaidi.

Washukiwa hao waliendelea kufungwa pingu na minyororo hata baada ya kuwa tayari wako ndani ya mahakama hiyo.

Kwa mwongozo wa Jaji Eva Luswata, kikao cha jana  Jumatatu kilikuwa cha kutoa fursa kwa wasimamizi wa mashtaka kuishawishi mahakama kwamba Jamil Mukulu na wenzake, wana kesi ya kujibu kuhusiana na ugaidi ndani ya Uganda.

Upande wa mashtaka umeieleza mahakama kwamba kwa mda mrefu, tangu mwaka 1986, Mukulu, akiwa kiongozi wa kundi la allied democratic forces – ADF, alikuwa akisajili wapiganaji, kutekeleza mauaji, wizi wa kimabavu, kutoa mafunzo ya ugaidi na kutekeleza ugaidi, kujaribu kuua, kuteka nyara na kushirikiana na makundi mengine ya kigaidi kutekeleza mauaji katika nchi za Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Washukiwa wamefuatilia kikao cha mahakama kwa msaada wa wakalimani katika lugha ya Kiswahili na lugha zingine asili kama lusoga, lugisu na Luganda.

Jamil Mukulu, anaripotiwa kupokea mafunzo ya moja kwa moja na aliyekuwa kiongozi wa kundi la kigaidi la Al-Qaeda Osama Bin Laden, upande wa mashtaka umeeleza.

Pia wamesema kuwa , mshukiwa huyu aliwahi kushiriki katika vita nchini Afghanistan. Video iliyotolewa na jeshi la Uganda UPDF inaonyesha kundi la ADF likiwa linafanya mazoezi katika misitu ya DRC kwa kutumia silaha nzito.

Mukulu alikamatwa mnamo mwaka 2015 akiwa nchini Tanzania kabla ya kurejeshwa nchini Uganda, ambako alikuwa akitafutwa kwa mda mrefu na kukwepa mitego ya maafisa wa usalama. Alifanikiwa kuhepa mitego ya maafisa wa usalama kwa kutumia majina bandia Zaidi ya 11 kwenye stakabadhi zake.

Alipokamatwa alipatikana na zaidi ya pasi za kusafiria 10 za nchi tofauti ikiwemo Uganda, Tanzania, Kenya na Uingereza.

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Jumatano ya May 16

Israel, Palestina washambuliana kwenye Mkutano wa Umoja wa Mataifa

$
0
0
Wajumbe wa Israel na wale wa Palestina wameshambuliana kwa maneno makali katika mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ulioanyika jana kwa lengo la kuzungumzia utatuzi wa vurugu na mauaji katika ukanda wa Gaza, zinazotokana na uamuzi wa Marekani kuhalalisha Jerusalem kuwa makao makuu ya Israel.

Zaidi ya watu 58 wameripotiwa kufa kwa kufyatuliwa risasi na askari wa jeshi la Israel ambao wamepambana na waandamanaji wanaopinga uamuzi huo wa Israel na mshirika wake mkuu, Marekani.

Katika mkutano huo wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, wajumbe kutoka Palestina walitumia maneno makali kueleza kuwa kinachofanywa na Israel dhidi ya Wapalestina ni uhalifu dhidi ya binadamu.

Pia, walilaani vikali kitendo cha Israel inayodhibiti Jerusalem kwa kutozingatia maamuzi ya Umoja wa Mataifa pamoja na kutozingatia makubaliano na sheria za kimataifa.

Hata hivyo, wajumbe wa Israel walirusha lawama zote kwa kundi la Hamas ambalo pia linadhibiti sehemu ya eneo la Gaza kwa kuwachukua mateka Waisrael na kwamba wamekuwa wakihamasisha vurugu zilizopelekea vifo hivyo.

Hii ni wiki ya sita ya maandamano makubwa yaliyozua ghasia, wapalestina wakipinga uamuzi wa Israel. Watu 58 walioripotiwa kupoteza maisha walizikwa kwa pamoja jana.

Korea Kaskazini Yaishtukia Marekani Kwa Madai ya Kuifanya Kama Libya.....Yatishia Kufuta Mkutano wake na Trump

$
0
0
Korea Kaskazini imesema kuwa inaweza kuahirisha mpango wa kiongozi wake, Kim Jong-un kukutana na Rais wa Marekani, Donald Trump kutokana na matamko pamoja na mazoezi ya kijeshi ya pamoja yanayofanywa kati ya Marekani na Korea Kusini.

Kupitia tamko lililotolewa na Makamu Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea Kaskazini, nchi hiyo imelaani kauli zilizotolea na Mshauri wa Mambo ya Ulinzi wa Marekani, John Bolton dhidi yake.

Aliielezea kauli ya Bolton aliposikika akidai kuwa Korea Kaskazini inaweza kufuata nyayo za Libya katika kuachana na mpango wa silaha zake kuwa ni kutaka kufananisha hatma ya taifa hilo na ile ya Libya iliyokuwa ikiongozwa na Muammar Gaddafi au Iraq ya Saddam Hussein.

“Ni jambo lisilokubalika na hatua mbaya kutaka kuingiza hisia za hatma ya Libya au Iraq, mataifa ambayo yalianguka kutokana na jitihada za kutaka kuharibu nguvu za nchi hizo,” imeeleza taarifa hiyo.

Aidha, Korea Kaskazini pia imesema kuwa inashangazwa na kauli za Marekani kuitaka isalimishe silaha zake zote za nyuklia bila masharti yoyote kabla ya kufanyika kwa mkutano huo unaosubiriwa kwa hamu kuweka historia.

Imesema kuwa kwa kauli hizo, Marekani imekuwa inafanya uchokozi hata kabla ya mkutano na kutoa taarifa na matamko ambayo yako kinyume na mpango wanaoendelea nao.

Imefafanua kuwa haitaacha kuweka wazi hisia zake dhidi ya hatua yoyote inayochukuliwa na Marekani wakati ambapo viongozi wa mataifa hayo wanajipanga kukutana nchini Singapore kwa lengo la kurejesha hali ya amani na maelewano katika eneo la Rasi ya Korea.

Katika hatua nyingine, Korea Kaskazini imelaani hatua za majeshi ya Marekani na yale ya Korea Kusini kuendelea kufanya mazoezi ya pamoja, ikidai kuwa mazoezi hayo yanaonesha uchokozi wa mpango wa kutaka kufanya uvamizi.

Hata hivyo, Marekani imeeleza kuwa haitaacha kuendelea kufanya maandalizi ya mkutano kati ya Trump na Kim Jong-un, kwani tuhuma zilizotolewa na taifa hilo bado hazijawasilishwa rasmi kwao. 

Pia, taarifa ya Ikulu ya Marekani imeeleza kuwa Kim Jong-un alibariki mazoezi ya kijeshi ya pamoja ya mataifa hayo kwani ni ya kawaida.

Sintofahamu kati ya mataifa hayo yameibuka wakati ambapo Korea Kaskazini imetangaza mpango wake wa kuteketeza maeneo ya majaribio ya silaha za kinyuklia, May 23 hadi 25 mwaka huu, wiki chache kabla ya mkutano wa viongozi wa nchi hizo.

Gigy Money Naye apata dili la ubalozi wa kondomu

$
0
0
Mwanamuziki wa Bongo fleva na video vixen maarufu Gifty Stanford maarufu kama Gigy Money amebahatika kupata dili nono la kuwa balozi wa Kondomu.

Baada ya Amber Lulu kutangaza wiki iliyopita kuwa amekuwa balozi rasmi wa Kondomu hatimaye na Gigy Mahoney amekuwa msanii wa pili kupata dili hilo.

Gigy Money alitangaza habari njema hiyo Kupitia ukurasa wake wa Instagram ambapo aliandika:

"BALOZI WA BULL CONDOM (Jamani sahivi kwichi kwichi zangu zote natumia Kondomu mpaka Myrah akue)”.

Kwa upande wa gigy Money Dili hili limekuja katika wakati muafaka kabisa kwa sababu ndio kwanza amaetoka kujifungua hivyo ni wakati wake wa kusaka pesa.

Ali Kiba Awatupia Dongo Wasanii Wanaonunua ‘Views’ Youtube

$
0
0
Msanii wa BongoFleva mwenye 'hit song' ya 'Mvumo wa Radi' Alikiba maarufu kama King Kiba amefunguka na kudai yeye sio miongoni mwa wasanii wanaotegemea kupata pesa kutoka katika 'views' za Youtube kama baadhi yao wanavyofikilia vichwani mwao.

King Kiba ametoa kauli hiyo ikiwa zimepita siku kadhaa tokea video yake mpya ya 'Mvumo wa Radi' kushindwa kuendelea kuhesabu idadi ya watu walioitazama jambo ambalo wengi wao walidai kuna  mchezo anafanyiwa msanii huyo ili asiweze kufikisha 'views' wengi kama ilivyokuwa kawaida yake kila atowapo video.

"Hii ndio mara ya kwanza kunitokea tatizo hilo ila halijaweza kuniathiri kwa namna yeyote ile. 

"Ila nashukuru watu wamepata walichokuwa wanastahili nasio kwamba mimi nategemea pesa kutoka 'Youtube views', mimi nafanya muziki najua wapi napata pesa katika muziki wangu. 

"Nilichokuwa nahitaji kiukweli ni mashabiki zangu waridhike na waelewe mimi ni msanii wa aina gani", amesema Alikiba.

Pamoja na hayo, Alikiba ameendelea kwa kusema "tunajua kwamba kuna hizi biashara za kuweka ma-robot katika 'Youtube' ili ionekane watu wana 'view' kwa wingi ila mimi binafsi ninaona ni utoto tu. Haitokuja kutokea hata siku moja kwamba Alikiba ameweka 'robot' ili apate 'views' nyingi, mimi nafanya muziki wangu kwa ajili ya watu na kwanini sasa nidanganye watu".

Wimbo wa Alikiba kwa sasa umetazamwa jumla ya watu milioni 1.2 na kushikilia nafasi ya kwanza katika ya video zilizotazamwa kwa kiasi kikubwa kutoka Youtube

Wachungaji Wanusurika Kupigwa na Wananchi Baada ya Kushindwa Kumfufua Marehemu

$
0
0
Wachungaji watatu wamenusurika kipigo kutoka kwa wananchi, baada ya kushindwa kumfufua marehemu katika Kijiji cha Sitalike Tarafa ya Nsimbo Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi.
 
Wachungaji hao walifika kijijini hapo wakidai kuwa wanao uwezo wa kumfufua marehemu mwanakijiji mwenzao aliyefariki dunia hivi karibuni na kuzikwa kwenye makaburi ya Kijiji hicho.

Akisimulia tukio hilo, mwenyekiti wa kijiji hicho, Christopher Angelo, alisema kuwa tukio hilo lililovuta hisia za watu wengi lilitokea Mei 7, majira ya saa 4 za asubuhi kijijini hapo.

Alisema kuwa wachungaji hao ambao walikuwa watatu walifika kwenye ofisi ya Kijiji na kujitambulisha kuwa wao ni wachungaji wanatoka katika Kijiji cha Nsimbo na watakuwapo kijijini hapo wakiwa wameitwa na ndugu wa marehemu, Raymond Mirambo aliyefariki dunia siku moja na kuzikwa kijijini hapo.

Alisema wachungaji hao walifika kijijini hapo wakidai kuwa wanataka kufanya maajabu ambayo ni ya kihistoria nchini ya kufanya maombi mfululizo na kumfufua marehemu Raymond.

Mwenyekiti huyo alisema kutokana na kujitambulisha kwa wachungaji hao kwenye ofisi ya kijiji, uongozi wa kijiji uliwaruhusu wachungaji hao kufanya maombi hayo ya kumfufua marehemu huyo.

Alisema baada ya kuruhusiwa na uongozi wa kijiji walielekea nyumbani kwa marehemu na kuwakuta ndugu wakiwa wanawasubiri kwa ajili ya maombi hayo ya kumfufua ndugu yao.

Alisema maombi hayo yaliendelea kwa muda wa siku saba usiku na mchana pasipo kuwa na mafanikio yoyote, hali ambayo iliwafanya ndugu wa marehemu washikwe na hasira.

“Wananchi, ndugu na jamaa walikasirika kutokana na kuona kuwa wachungaji hao wanawatapeli na kwa sababu waliwasababishia kuingia gharama kubwa ya kulisha watu waliokuwa wakishiriki maombi hayo,” alisema.

Kwa mujibu wa Angelo, baada ya kuona hafufuki, ndugu wakiongozwa na mama mzazi wa marehemu waliamua kwenda kutoa taarifa ofisi ya kijiji, ili kuepusha vurugu ambazo zilitaka kutokea.

Alisema watu walioonekana kuwa na hasira kwa kutoona muujiza wa kumfufuka marehemu walitaka kuwapiga wachungaji hao kwa kuwapotezea muda na kuwatapeli.

Mwenyekiti huyo alisema viongozi wa Kijiji baada ya kufika kwenye eneo hilo walikuta ndugu wa marehemu wakiwa wanafoka kwa hasira huku wakiwa wanawatuhumu wachungaji hao kuwa ni matapeli.

“Sisi uongozi wa Kijiji tulikuta vurugu na wananchi walikuwa wanataka kuwapiga wachungaji hao, tulichofanya kuepusha shari ni kuwaondoa wachungaji hao eneo hilo na kwa kweli walitii agizo hilo na kuondoka zao,” alisema Angelo.

Elimu ya Mlipa Kodi Kutolewa Mashuleni

$
0
0
Na: Lilian Lundo – MAELEZO, Dodoma.
Serikali imeona umuhimu wa kuingiza elimu ya mlipa kodi  kwenye mitaala ya elimu nchini ili kwajengea Watanzania  tabia, mwenendo na mazoea ya  kulipa kodi kwa maendeleo ya Taifa.

Kauli hiyo imetolewa jana, Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Mhe. William Ole Nasha alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Lupembe Mhe. Joram Ismael Hongoli juu ya kwa nini Serikali isiingize kwenye mitaala ya elimu somo la umuhimu wa kulipa kodi ili lifundishwe kuanzia shule ya msingi ili wananchi wapate uelewa wa kodi na waweze  kulipa kodi kama ilivyo kwa nchi zilizoendelea.

 “Serikali inatambua umuhimu wa elimu ya mlipa kodi katika kumjengea mwananchi tabia ya kulipa kodi. Katika somo la Uraia na Maadili kuanzia darasa la III na kuendelea, mtaala umelenga kumjengea na kumuandaa mwanafunzi kuwa mwajibikaji katika kutekeleza majukumu ya kila siku,” alisema Mhe. Ole Nasha.

Vile vile mtaala umelenga kumjengea mwanafunzi kuiheshimu na kuithamini jamii yake kwa kuwa mwadilifu na mzalendo ikiwa ni pamoja na kutekeleza majukumu ya kitaifa ikiwemo kulipa kodi.

Aidha amesema, kutokana na umuhimu wa kuwajengea vijana utamaduni wa kulipa kodi, elimu ya mlipa kodi ni jambo muhimu, Serikali kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kwa kushirikisha Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) itaendelea kuboresha elimu hiyo ili isisitizwe na kuwekewa mkazo katika mitaala ya elimu kuanzia elimu ya Msingi.

Wakati huo huo, Mhe. Ole Nasha amesema Serikali ilifuta ada na michango ya lazima katika shule za umma ngazi ya elimu ya msingi (elimu ya awali hadi kidato cha Nne) na mpango huo hakuhusisha kidato cha tano na sita pamoja na shule binafsi.

Ameyasema hayo alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Seter Alexander Mahawe juu ya lini, Serikali itafuta ada kwa wanafunzi wanaosoma katika shule binafsi.

“Ada na michango iliyokuwa inalipwa na wazazi/walezi kwa sasa hugharamiwa na Serikali. Mpango huu haukuzihusu shule binafsi pamoja na shule za Umma ngazi ya kidato cha Tano na Sita. Hivyo shule hizo zitaendelea na utaratibu wa wazazi/walezi kuchangia gharama za uendeshaji wa elimu ikiwemo kulipa ada za mitihani.

Hata hivyo amesema, Ili kuhakikisha mazingira rafiki katika utoaji wa elimu, Serikali imekuwa ikifanya majadiliano na sekta binafsi kwa lengo la kuondoa changamoto zinazowakabili ambapo hadi sasa Serikali imeweza kuondoa baadhi ya kodi na tozo mbalimbali ambazo awali walikuwa wakitozwa wamiliki wa shule binafsi.

Ametoa mfano wa kodi hizo kuwa ni kodi za mabango, kodi ya kuendeleza ufundi standi stadi (Skills Developmentt Levy), tozo ya Afya na Usalama mahala pa kazi (Occupational Safety and Health Administration – OSHA) na tozo ya zimamoto.

Makamu Wa Rais Apokea Vifaa Vya Upasuaji Kutoka Ubalozi Wa Kuwait

$
0
0
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema uboreshaji wa huduma katika hospitali zetu za kibingwa kama MOI, zitaipunguzia Serikali mzigo wa kupeleka wagonjwa nje ya nchi na hivyo kutekeleza azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuboresha huduma za afya kwa wananchi.

Makamu wa Rais ameyasema hayo wakati wa kupokea vifaa vya Chumba Cha Upasuaji wa Watoto vilivyotolewa na Ubalozi wa Kuwait kwa Taasisi ya Mifupa (MOI) jana tarehe 15 Mei, 2018.

“ Aidha kwa namna ya kipekee nakushukuru Mheshimiwa Balozi wewe binafsi na Serikali ya Kuwait kwa ushirikiano ambao mnaendelea kuipatia Serikali yetu ya awamu ya Tano katika Sekta mbalimbali za maendeleo lakini hasa hasa katika sekta ya afya” alishukuru Makamu wa Rais.

Makamu wa Rais alisema kuwa Balozi wa Kuwait Mhe. Jasem Al Najem amekuwa mstari wa mbele katika kuendeleza sekta ya Afya hapa nchini ambapo leo wamesaidia vifaa vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 258 ambavyo vitaiwezesha Taasisi kuimarisha utoaji wa huduma ya upasuaji hasa kwa watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi.

Makamu wa Rais amlisema msaada huo utaiwezesha Taasisi kuwa na chumba cha upasuaji ambacho kitakuwa maalum kwa watoto tu, hivyo idadi ya wagonjwa watakaopata huduma ya upasuaji itaongezeka kutoka 500-700 kwa mwezi, kufikia zaidi ya wagonjwa 1000 kwa mwezi na watahudumiwa kwa haraka zaidi.

Wakati huo huo Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Faustine Ndugulile  amesema Tanzania iatendelea kuimarisha uhusiano na nchi ya Kuwait kwani wamekuwa mstari wa mbele katika kutoa msaada haswa msaada inayohusu sekta ya afya.

Balozi wa Kuwait hapa nchini Mhe. Jasem Al Najem alisema kuwa Wananchi wa Kuwait wana mapenzi makubwa na Watanzania na kuahidi wataendelea kutoa msaada.
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live




Latest Images