Wakulima wa zao la kahawa Wilayani Missenyi Mkoani Kagera wametakiwa kuzingatia usafi na ubora wa zao hilo ili kuweza kuteka soko la zao ilo hapa nchini.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa wilaya ya Missenyi Kanali Denis Mwila katika kikao cha bodi ya kahawa kilicho jumuisha wajumbe wa vyama vya msingi kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri iyo mapema hii leo.
Aidha kanali Mwila amesema zao la kahawa linatakiwa kuzingatia usafi pale linapokuwa shambani, uvunaji pamoja na usafirishaji ili kuweza kupata faida kwani ubora wa kahawa unamsaidia mkulima kupata faida zaidi.
Sambamba na hayo Kanali Mwila amesema kuwa ukusanyaji wa kahawa hiyo utahusisha wanunuzi binafsi kwa kupatiwa kibali cha kununua zao hilo ili kumuwezesha mkulima kupata haki yake.
Kwa upande wake mnunuzi wa kahawa kutoka Tugabe Company Limited bwana Abdulazack Kashasha amewaambia wajumbe na viongozi katika kikao hicho kuwa yupo tayari kununua kahawa kwa sh. 1500 kwa kilo moja ambapo sh 150 ni kwa ajili ya vyama vya msingi na sh 1350 ni kwa ajili ya mkulima
Vile vile Kashasha amesema kuwa ataongeza asilimia 3 kwa ajili ya serikali iwapo atapatiwa kibali hicho na ataanza kazi mara moja na baadhi ya wajumbe wa kikao wameelezwa kufurahishwa na bei hiyo kutoka 1200 hadi 1350.
Kwa upande wake Afisa ushirika Wilayani Missenyi bwana Gabinus Mtonga amewataka wajumbe wa vyama vya msingi kuendelea kukusanya kahawa kutoka kwa wakulima ili kuwezesha kuendelea kuunga mkono tamko la serikali.
Afisa Kilimo wa wilaya ya Missenyi bwana Bita Solomon amesema wamejipanga kutoa zaidi ya miche elfu 1500 kwa wakulima ili kuwezesha kupunguza ugonjwa wa kahawa na kuwasaidia wakulima kuvuna kahawa yenye ubora hivyo amewataka kuchimba mashimo na kuweka mbolea huku wakifuata ushauri wa wataalamu.