Quantcast
Channel: MPEKUZI
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live

Arusha: Askofu Mkuu Jimbo Katoliki Aachia Ngazi

$
0
0
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Arusha, Joseph Lebulu ameng’atuka katika nafasi yake hiyo leo baada ya Baba Mtakatifu Francis kukubali ombi lililowasilishwa kwake.

Katibu mkuu wa TEC, Raymond Saba amethibitisha na kusema kuwa Papa Francis amemteua Askofu Isaac Massawe wa Jimbo Katoliki Moshi, kuwa Askofu Mkuu mpya wa Jimbo Kuu la Arusha.

Kwa mujibu wa redio Vatican, Askofu Mkuu mteule Massawe alizaliwa Juni 10, 1951 huko Mango, Jimbo Katoliki la Moshi.

Alipata upadri Juni 29,1975 na Novemba 21, 2007 aliteuliwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedict XVI kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Moshi na aliwekwa wakfu Februari 22,2008 na Kardinali Polycarp Pengo, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam akisaidiana na Askofu Mkuu Lebulu na Askofu Amedeus Msarikie (sasa marehemu) wa Jimbo Katoliki la Moshi. Hivi karibuni, aliteuliwa kuwa msimamizi wa kitume Jimbo Katoliki la Mbulu.

BASATA yaikana kamati ya Miss Tanzania

$
0
0
Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) limekanusha taarifa iliyotolewa na waandaaji wa shindano la Miss Tanzania ya LINO Agency, kwamba Baraza hilo ni moja ya chanzo cha kukwamisha shindano hilo kufanyika.

Kweye taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari, BASATA imesema ilitoa kibali cha muda kwa kampuni hiyo kuweza kushughulikia matatizo yake, pamoja na kuratibu safari ya Miss Tanzania 2017 aliyeshiriki mashindano ya Miss World mwaka huu.

Taarifa hiyo imeendelea kwa kutoa wito kwa makampuni yanayoandaa mashindano ya sanaa kuongeza weledi, na kuzingatia sheria, ili kuepuka matatizo kama hayo.

Isome hapo chini

Naibu Spika Aumwagia Sifa Wimbo wa Kivuruge wa Nandy

$
0
0
Naibu Spika, Dk Tulia Ackson ameusifia wimbo wa Kivuruge ulioimbwa na msanii wa muziki wa kizazi kipya, Nandy akieleza kuwa umebeba ujumbe mzuri wa masuala yanayotokea kweli katika jamii.

Wimbo huo unamuelezea mwanamke  anayelalamikia kusumbuliwa katika mapenzi  licha ya kuwa anafanya kila awezalo kumridhisha mpenzi wake.

Kwenye mtandao wa Youtube video ya wimbo huo imetazamwa na watu zaidi ya 600,000, ikiwa ni siku ya nane tangu ilipowekwa kwenye mtandao huo.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram Dk Tulia ameandika “Kwa jitihada hizi natumaini utafika mbali zaidi, uvumilivu na nidhamu ni vya kuzingatia kwenda kwenye mafanikio. Wimbo wako Kivuruge tumeupokea kwa mikono miwili,”

Mbali na kufuatiliwa zaidi katika mtandao wa youtube, Kivuruge pia imekuwa ikifanya vyema katika vituo mbalimbali vya redio na televisheni kutokana na kuchezwa mara kwa mara.

Nandy ameingia kwenye orodha ya wasanii wa kike waliofanya kazi kubwa kwenye muziki mwaka 2017 kupitia kazi zake mbalimbali na nyingine alizoshirikishwa.

Lukuvi atoa onyo kwa vishoka wa Ardhi

$
0
0
Serikali imekemea baadhi ya wawekezaji wanaotumia vibaya jina la Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kuwatoa wananchi katika maeneo yao kwa kisingizio cha kupewa kibali na wizara hiyo wakati sio kweli.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri mwenye dhamana ya Wizara ya Ardhi William Lukuvi ambapo amewaonya baadhi ya wawekezaji ambao wameonekana kushirikiana na baadhi ya watumishi wa serikali katika kunyang'anya haki za wananchi kitendo ambacho amesema kwa utawala wa serikali hii ya awamu ya tano hakina nafasi.

Ameongeza kwamba, kwa sasa serikali inaendelea na zoezi la kurudisha ardhi ya wananchi mikononi mwao bila ya gharama yeyote na kwa yale maeneo ambayo yatabainika kuwa na ukiukwaji wa umiliki watayarudisha kwa wenyewe ili kuendelezwa.

Mh. Lukuvi amesema zoezi la utambuzi wa umiliki wa maeneo na urasimishaji ni endelevu kwa mikoa yote nchini lengo ni kujua maeneo yanayomilikiwa kihalali na kumaliza migogoro ya ardhi ambayo imeonekana bado ni changamoto kwa maeneo mengi mijini na vijijini.

Meya wa CHADEMA akanusha Tuhuma kuhamia CCM

$
0
0
Meya wa Manispaa ya Moshi Mkoani Kilimanjaro, Raymond Mboya amekanusha tetesi za kujivua wadhifa wake huo na kuhama chake cha Chadema na kuhamia CCM.

Mboya ambaye ni diwani wa Kata ya Longuo ametajwa kwamba ana lengo la  kukihama chama hicho, lakini amekanusha na kusema kuhama chama na kuacha kazi sio kuunga mkono Serikali  bali ni kuchezea rasilimali za nchi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Desemba 27  ofisini kwake alisema, taarifa zinazosambaa katika mitandao ya kijamii kuhusu kutaka kuhama chama sio za kweli na wananchi wapuuze.

“Kila mmoja anaunga mkono Serikali  lakini sio kwa kuacha kazi na kumuunga mkono mtu anayefanya kazi” amesema  Mboya.

Alisema wanaofanya hivyo hawazitendei haki kazi ambazo wamepewa na wananchi hivyo wanatakiwa kuunga mkono kazi za Serikali kwa kufanya kazi ili kuleta maendeleo kwa wananchi na taifa kwa ujumla.

Alisema “ tumechaguliwa na wananchi ili tuwatumikie na sio wametuchagua ili tuharibu rasilimali”

Hata hivyo alisema katika kuunga mkono sera ya viwanda, manispaa hiyo inatarajia kuanzisha kiwanda kidogo cha mbolea inayotokana na takataka zinazolalishwa na wakazi wake.

Alisema  kiwanda hicho ambacho kitaanzishwa kwa kushirikiana na serikali ya Ujerumani kitajengwa katika eneo la dampo kuu la takataka ambalo liko Kaloleni.

“Tunamuunga mkono Rais (Magufuli) katika suala la ujenzi wa viwanda na kweli juhudi zake zimetupendeza na tumeamua tutamuunga mkono mwezi Februari mwaka 2018, kwa kujenga kiwanda kipya cha kutengeneza mbolea eneo la Kaloleni…Tunasubiri barua rasmi ya uwekezaji wa mradi huo kutoka kwa wenzetu ambao ni mji dada wa Tübingen,” alisema.

Katika taarifa yake, Meya huyo alisema mwezi Januari, mwakani, Tubingen na Manispaa ya Moshi, watasaini makubaliano ya ujenzi wa kiwanda hicho kinachotarajiwa kutumia malighafi ambayo ni takataka zinazokusanywa katika Manispaa ya Moshi.

Alisema kwa sasa wanajiandaa kwenda kutoa taarifa na kutambulisha mradi huo kwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage.

Kwa mujibu wa Raymond, kila siku mji wa Moshi unazalisha taka, kati ya tani 180 hadi 200 na kwamba timu ya wataalamu wa ujenzi wa kiwanda hicho kutoka nchini Ujerumani, wameshakuja na kufanya tathmini na kujiridhisha malighafi hiyo inaweza kuendesha uzalishaji wa mbolea.

Ujenzi wa kiwanda hicho, unatokana na kukosekana kwa teknolojia ya kubadili taka ngumu zinazozalishwa na wakazi wa Manispaa ya Moshi ili zitumike kama nishati.

Nandy Amshukuru Naibu Spika kwa Kuusifia Wimbo wake wa Kivuruge

$
0
0
Msanii wa muziki wa bongo fleva Nandy, amesema anamshukuru Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa pongezi alizompa, kwani ni kitu ambacho hakikutarajia.

Nandy amesema kuwa ni kitu cha faraja kuona anapongezwa na kiongozi mkubwa serikalini, hivyo kimempa faraja.

“Nimefurahi kwa sababu ni mtu ambaye ananisapoti sana, na imenipa faraja sana kwani sikutarajia, kwa sababu mi nilitumiwa kwenye group nikaiona, basi nikampigia simu nikaongea naye nikamshukuru”, amesema Nandy.

Jana  Naibu Spika Tulia Ackson alipost kwenye instagram yake akimpongeza Nandy kwa jitihada zake anazozifanya kwenye kazi yake ya sana ya muziki.

Jeshi la Polisi Lasema Litamkamata na Kumhoji Askofu Zakaria Kakobe kwa Uchochezi

$
0
0
Licha  ya kutokiri moja kwa moja juu ya taarifa zinazosambaa mitandaoni kuhusu kumkamata Askofu Zakaria Kakobe wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGFC) lililoko Mwenge jijini Dar es Salaam, Jeshi la Polisi limesema ni lazima litamhoji kiongozi huyo wa kiroho.

Kuhojiwa huko kumetokana na kauli yake dhidi ya serikali aliyoitoa wakati wa ibada ya Krismasi.

Jana, kulienea taarifa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii kueleza kwamba askofu huyo alitiwa mbaroni jana asubuhi na askari wa Jeshi la Polisi huku sababu za kukamatwa zikielezwa kuwa ni ujumbe alioutoa wakati wa mahubiri yake ya ibada ya Krismasi.

Akizungumza na Nipashe jana kuhusiana na ukweli wa taarifa za kutiwa mbaroni kwa Askofu Kakobe, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alisema kuwa ni kweli walishakuwa katika harakati za kumkamata.

"Ametoa maneno ya kashfa katika mahubiri yake, lakini sina taarifa kama amekamatwa," Kamanda Mambosasa alisema na kuongeza:

"Taarifa za kumkamata zipo, lazima tumkamate. Tutamhoji…tutamhoji alikuwa na maana gani.

“Mtu akitenda kosa la jinai ni lazima akamatwe…kwa sasa niko msibani, sijapokea taarifa kama amekamatwa au kuhojiwa. Nitawaarifu kama kutakuwa na taarifa zaidi.”

Askofu Kakobe (62), anadaiwa kuyatumia mahubiri yake siku hiyo kuzungumzia mwenendo wa serikali na masuala mbalimbali ya kisiasa nchini.

Mojawapo ya sauti inayodaiwa kuwa ya Askofu Kakobe na kusambaa kwenye mitandao ya kijamii ilidai kwamba hivi sasa Tanzania si nchi ya chama kimoja kama viongozi wanavyotaka.

Chanzo: Nipashe

Polisi adaiwa kumuua kwa risasi mchumba wake JWTZ

$
0
0
Askari  wa kike wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Kikosi cha 514 KJ Makambako mkoani Njombe, ameuawa kwa kupigwa risasi na mchumba wake ambaye ni askari wa Jeshi la Polisi, Inadaiwa kuwa tukio hilo, lilitokana na kuibuka ugomvi kati yao.

Inadaiwa askari huyo namba H 2299 Zakaria Dotto, alimpiga risasi mbili mchumba wake, Neema Masanja (25) mkazi wa Mtaa wa Jeshini Kata ya Maguvani Halmashauri ya Mji wa Makambako mkoani Njombe, baada ya kuibuka ugomvi kati yao saa 12 jana alfajiri.

Wakizungumza katika eneo la tukio, majirani wa marehemu walisema majira ya alfajiri walisikia risasi zikirindima katika chumba cha marehemu na walipoangalia nje ya nyumba hiyo walimuona mdogo wake akimkimbiza mtu ambaye hawakumuona sura.

Mmiliki wa nyumba hiyo ambayo marehemu alikuwa amepanga, Asty Lusambo, alisema alisikia kishindo cha risasi na alipofungua dirisha akiwa na mkewe, walimuona mdogo wa marehemu akimkimbiza mtu.

Mke wa Lusambo, Sophia Manyika, alisema alimfuata mdogo wa marehemu na baadaye alimkuta katika msitu wa Jeshi akiwa amechoka na chini yake kukiwa na bunduki aina ya SMG ambayo ilitupwa na mtuhumiwa wa mauaji hayo na kupotelea msituni.

Ofisa Mtendaji wa Mtaa wa Jeshini, Afrah Mbunju, alisema tukio hilo lilitokea mtaani kwake na alipofika eneo la tukio alisimuliwa na mashuhuda kuhusiana na kilichotokea.

Mtendaji huyo alieleza kuwa wawili hao walikuwa wachumba ambao ni wakazi wa mtaa wake.

“Mwanaume ambaye ni askari wa Jeshi la Polisi alikuwa anatakiwa kwenda lindo latika moja ya taasisi za kifedha ambapo alimkuta huyo binti nyumbani kwake akijiandaa kwenda kazini, ndipo ukaibuka ugomvi na marehemu amekutwa akiwa na mikwaruzo shingoni akiwa ameuawa,” alisema Mbunju.

Alisema askari hao ni wakazi wa kijiji kimoja mkoani Mwanza na walikuwa wanatarajia kuoana kwa kuwa mwanaume alikuwa ameshapeleka mahari.

Aliongeza: “Walikuwa ni wachumba tayari miezi michache iliyopita wametoleana mahari na walikuwa wanatarajia kuoana Februari mwakani.”

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Makambako, Dk. Kesha Mgunda, alithibitisha kuupokea mwili wa marehemu kwa ajili ya uchunguzi na baada ya uchunguzi waliukabidhi kwa ndugu wa marehemu ambao wameuhifadhi katika hospitali ya Ilembula kwa ajili ya taratibu za maziko.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Njombe, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Pudensiana Protas, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwa mtuhumiwa alikuwa kazini, lakini alitoroka lindo kabla ya tukio hilo.

Alisema Jeshi hilo linaendelea na msako wa askari huyo na kuwataka wananchi kutoa taarifa popote watakapomuona.


Taifa Stars yalamba udhamini mnono wa Jezi

$
0
0
Shirikisho  la Soka nchini (TFF), limeingia mkataba mnono na Kampuni ya Macron ambayo kuanzia sasa ndiyo mdhamini mkuu wa jezi za timu zote za Taifa; Taifa Stars, Twiga Stars na Serengeti Boys.

Aidha, udhamini huo wa miaka miwili wenye thamani ya Euro 700,000 zaidi ya Sh. bilioni 1.8 za Tanzania umegawanyika katika sehemu kuu mbili ambazo ni jezi na vifaa vingine vya michezo, pamoja na fedha taslimu.

Akizungumza wakati wa utiaji rasmi saini ya makubaliano hayo wakati wa mkutano wa TFF na Wahariri wa Vyombo vya Habari nchini, Kaimu Katibu Mkuu wa shirikisho hilo, Wilfred Kidau, alisema hiii ni mara ya kwanza kwa timu za Taifa kupata mkataba mnono kama huo.

"Kwa mwaka tutakuwa tukipata euro 150,000 ambapo kwa miaka miwili ni euro 300,000 (takriban Sh. milioni 800) hizo zikiwa ni mbali ya kupewa jezi na vifaa vingine, hii ni mara ya kwanza kwa timu zetu za taifa kupata udhamini wa jezi mkubwa kama huu," alisema Kidau.

Kwa upande wa Rais wa TFF, alisema bado wanaendelea kutafuta wadhamini kwa timu hiyo na ile ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars ambayo haihusiki katika udhamini huo wa Macron.

"Mchakato huu umechukua muda mrefu na walikuwapo washindani wengi, lakini Kampuni ya Macron ndiyo imeshinda, na hatuishii hapo tu bado tunahitaji wadhamini wengine watakaoidhamini pia Kilimanjaro Stars.

"Kuna mengi tutakayofaidika katika mkataba huu, kwani pia tutakuwa tukipata sehemu ya mauzo ya jezi za timu ya Taifa na pia sasa itakuwa ni vigumu kutengenezwa na kuuzwa kiholela," alisema Karia.

Aliongeza kwa kufafanua kuwa awali ilikuwa vigumu kudhibiti watengenezaji na wauzaji holela kwa kuwa hata nembo ya TFF ilikuwa haijasajiliwa jambo ambalo kwa sasa limefanyika kabla ya kukamilisha mchakato huo wa udhamini.

Karia alisema faida ya uuzwaji wa jezi hiyo itaonekana kwa sasa kwa kuwa anaamini kutokana na Rais John Magufuli, kudhibiti uingizwaji uholela wa bidhaa nchini kwa kuimarisha ulinzi mipakani na bandarini, itakuwa ni vigumu kwa wale waliokuwa wakitumia ujanja huo kujinufaisha.

Mke wa Bilionea Msuya sasa kula Mwaka Mpya mahabusu

$
0
0
Mke wa marehemu Bilionea Erasto Msuya, Miriam Mrita na mwenzake, wanaokabiliwa na kesi ya mauaji ya dada wa bilionea huyo, Aneth Msuya, bado wanaendelea kukaa mahabusu baada ya upande wa Jamhuri kudai upelelezi haujakamilika.

Kesi hiyo ilitajwa jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Patrick Mwita, alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuomba mahakama kupanga tarehe nyingine ya kutajwa.

Hakimu alisema kesi hiyo itatajwa Januari 8, 2018 na washtakiwa wataendelea kukaa mahabusu.Mbali ya Miriam, mshtakiwa mwingine ni mfanyabiashara Revocatus Muyela.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa wanadaiwa kuwa Mei 25, 2016 walimuua kwa makusudi dada wa marehemu bilionea Erasto Msuya, Aneth Msuya.

Mkurugenzi Mtendaji CRDB Atangaza Kung'atuka

$
0
0
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dk Charles Kimei amesema hatoongeza muda wa kuiongoza taasisi hiyo baada ya mkataba wake kukamilika Mei, 2019.

Mkurugenzi huyo atakayekuwa ameiongoza CRDB kwa miaka 21 atakapostaafu, amesema uamuzi huo anaufanya kupisha damu mpya kuendeleza mafanikio ya benki hiyo kubwa nchini.

“Si vizuri kung’ang’ania madaraka. Tunao wakurugenzi tuliowaandaa kwa muda mrefu ambao wanaweza kuendeleza nitakapoishia. Ninapisha damu changa nami nitaendelea kuwa mwanahisa wa kawaida,” amesema Dk Kimei leo Alhamisi Desemba 28,2017.

Kwa utaratibu wa benki hiyo, mchakato wa kumpata mkurugenzi mtendaji huchukua miezi 18 lakini Dk Kimei ameongeza mwezi mmoja na kuifanya 19 ili kuipa bodi ya wakurugenzi nafasi zaidi ya kukamilisha hatua hizo.

Amesema ingawa upo mfumo mzuri wa kurithishana madaraka ndani ya benki hiyo, lakini mwenyekiti na bodi wana uhuru wa kumchagua mtu mwenye sifa za ziada kutoka nje na kushirikiana na familia ya benki kuendeleza mafanikio.

“Katiba yetu inataka Mtanzania ndiye aiongoze CRDB. Ninaiamini timu niliyoshirikiana nayo tangu niingie hapa. Hata benki nyingine zinazotafuta wakurugenzi watendaji, ningezishauri zije CRDB,” amesema.

Ndani ya muda uliobaki kabla mkurugenzi mpya hajakaribishwa, Dk Kimei amesema angependa kuona inapata faida kama ya mwaka 2015 ilipotengeneza Sh187 bilioni ikiongezeka kutoka Sh148 mwaka 2014.

Mtumishi wa PPF Atiwa mbaroni kwa tuhuma za kusafirisha mirungi

$
0
0
Polisi mkoani Kilimanjaro inamshikilia mfanyakazi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (PPF) kwa tuhuma za kusafirisha dawa za kulevya.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamis Issah alimtaja mtuhumiwa huyo kuwa ni Anitha Oswald (32).

“Askari wakiwa doria walimkamata Anitha Oswald, ambaye ni mkazi wa Karanga, Manispaa ya Moshi, akiwa anasafirisha dawa za kulevya aina ya mirungi kilo 216 na gramu 370 kwa kutumia gari lake analomiliki aina ya Toyota Sienta rangi ya silva,” alisema kamanda Issah.

Kamanda Issah alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa eneo la Majengo kwa Mtei Desemba 19 akitokea Njia Panda ya Himo kuchukua mzigo huo.

“Jeshi la polisi mkoani hapa liko makini, operesheni inaendelea na hatutamvumilia mtu yeyote ambaye atabainika kujihusisha na biashara hii”, alisema.

Kamanda huyo alisema polisi wanaendelea kumtafuta dereva wa gari hilo ambaye alikimbia baada ya kulitelekeza lilipogonga mti wakati akiwakimbia askari.

Waziri Ndalichako amkatalia mbunge kusajili shule

$
0
0
Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako amekataa kutoa usajili kwa Shule ya Msingi Njalu iliyopo wilayani Itilima, Mkoa wa Simiyu kutokana na kutokidhi vigezo.

Shule hiyo imejengwa na wananchi kwa kushirikiana na mbunge wa Itilima (CCM), Njalu Silanga.

Akizungumza katika mkutano uliofanyika jana katika shule hiyo iliyopewa jina la Njalu kutokana na mchango wa mbunge huyo katika ujenzi, Profesa Ndalichako alisema shule hiyo haijakidhi vigezo vya usajili.

Mbele ya wakazi wa Kijiji cha Habiya ilipo shule hiyo, waziri Ndalichako alikataa ombi la mbunge huyo kuisajili na kuagiza upungufu uliopo urekebishwe kwanza kabla ya wizara kuisajili shule hiyo ya umma.

Miongoni mwa upungufu huo ni kuwa na vyumba vitano pekee vya madarasa badala ya vinane vinavyohitajika.

Mengine ni matundu ya vyoo, ambayo kati ya 10 yanayohitajika, yapo matano pekee, huku ikiwa na chumba kimoja cha ofisi ya walimu.

Profesa Ndalichako alisema wizara itatoa mifuko 100 ya saruji kusaidia kuondoa upungufu uliopo.

“Tumeona kuna upungufu hatutaweza kutoa kibali cha kuisajili, badala yake mkamilishe yanayohitajika kwa utaratibu wa kisheria wa kufungua shule. Niwahakikishie kuwa, Wizara ya Elimu hatuna urasimu ni lazima tuwe makini kwa kusimamia vigezo hivyo,” alisema Profesa Ndalichako.

Alisema licha ya kuwapo kwa mahitaji ya shule katika eneo hilo ambalo lina wanafunzi wapatao 633, ni lazima kuzingatia vigezo ambavyo vitakaguliwa na wataalamu kutoka idara ya udhibiti ubora wa elimu na ofisi ya ofisa elimu wilaya.

Awali, Silanga alielekeza lawama kwa watumishi wa Serikali na hasa wa idara ya elimu mkoani Simiyu kwa kushindwa kutumia utaalamu wao kuwaelimisha wananchi kuhusu vigezo vinavyotakiwa kabla ya shule kusajiliwa.

“Timu ya wataalamu ishuke itoe maelekezo. Majengo mengi yanavunjwa, wasimamizi tunao lakini hawatekelezi majukumu yao hivyo watimize wajibu wao kuliko kuwakatisha tamaa wananchi katika kuchangia shughuli za maendeleo,” alisema.

Silanga alimwomba Waziri Ndalichako kuwapatia usajili wakati wakiendelea kushughulikia upungufu uliojitokeza kwa kipindi cha muda mfupi kabla ya shule kufunguliwa Januari 8 mwakani ombi ambalo hata hivyo, lilikataliwa.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka alisema hawawezi kuwaadhibu wananchi na mbunge, hivyo ni lazima wahakikishe upungufu uliopo unaondolewa kabla ya Januari 15 mwakani.

Katika kuunga mkono jitihada hizo, Mtaka alitoa mifuko 50 ya saruji; huku mkuu wa Wilaya ya Itilima, Benson Chilangi pia akitoa mifuko 50.

Halmashauri ya Wilaya ya Itilima imeahidi kutoa mabati na mbao zitakazohitajika katika ujenzi.

Wafanyakazi TTCL wajitosa sakata la Airtel

$
0
0
Chama cha Wafanyakazi wa Sekta ya Huduma za Mtandao wa Mawasiliano Tanzania (Tewuta) kimepongeza hatua ya Rais John Magufuli kumtaka Waziri wa Fedha kuanza uchunguzi kubaini ukweli kuhusu ubinafsishwaji wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL).

Katibu Mkuu wa Tewuta, Junus Ndaro amesema chama hicho kinatambua fika kuwepo mchezo mchafu uliosababishwa na Watanzania wachache wenye uchu wa fedha wakisaidiana na wawekezaji kupora rasilimali hiyo ya Taifa.

Ndaro amesema leo Alhamisi Desemba 28,2017 kuwa, kwa muda mrefu chama hicho kimekuwa kikitoa malalamiko kuhusu ufisadi huo serikalini lakini hakikusikilizwa.

“Tunampongeza Rais Magufuli kwa kuthubutu kutamka pasipo shaka kuwa taarifa alizonazo zinaonyesha kampuni ya Airtel ni mali ya TTCL, jambo hili tulilipigia kelele kwa muda mrefu,” amesema.

Ndaro amesema mara zote hawakusita kutamka kuwa Celtel ambayo sasa ni Airtel ni mali ya TTCL iliyoporwa pasipo kulipwa chochote.

“Wafanyakazi tunatambua kuwa TTCL haikuporwa Celtel pekee bali ilinyang’anywa pia Chuo cha Posta na Simu hali iliyosababisha tukose mahali pa kupata mafunzo,” amesema Ndaro.

Kutokana na kuanza uchunguzi wa sakata hilo, Ndaro amesema viongozi wa Tewuta wako tayari kutoa kila aina ya ushirikiano kuhakikisha Serikali inashinda na kuirudisha Airtel mikononi mwa TTCL.

“Tuna ushahidi wa kutosha na tuko tayari kutoa ushirikiano kwa Serikali katika hatua zote kuleta haki iliyopotea ya Kampuni ya Simu Tanzania,” amesema.

Breaking News: Rais Magufuli awasilisha fomu inayotaja mali na madeni yake

$
0
0
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 28 Desemba, 2017 amewasilisha fomu yake ya tamko kuhusu rasilimali na madeni katika ofisi ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma iliyopo Mtaa wa Ohio, Wilaya ya Ilala Jijini Dar es Salaam.

Baada ya kuwasilisha fomu hiyo Mhe. Rais Magufuli ameipongeza Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa kazi inazofanya na amemtaka Kamishna wa Maadili Jaji Mstaafu Harold Nsekela kutopokea fomu ya kiongozi yeyote ambaye atakuwa hajawasilisha tamko lake ifikapo tarehe 31 Desemba, 2017.

“Mhe. Jaji Nsekela ikifika tarehe 31 Desemba, ambayo ni siku ya mwisho kwa Mujibu wa Sheria, weka mstari na usipokee fomu zingine, halafu tuone sheria itafanyaje, nakutakia kazi njema” amesisistiza Mhe. Rais Magufuli.

Kwa upande wake Mhe. Jaji Mstaafu Harold Nsekela amemshukuru na kumpongeza Mhe. Rais Magufuli kwa kutekeleza matakwa ya kisheria yanayomlazimu kujaza fomu hizo na amesisitiza kuwa ujazaji wa fomu hizo kwa viongozi wa umma sio ombi.

“Viongozi hawaombwi kujaza fomu hizi, kuna baadhi wanadhani labda kutuletea hilo tamko ni fadhila, hapana, sheria ya nchi inahitaji hivyo na kuna sababu zake za msingi” amesema Mhe. Jaji Mstaafu Nsekela.

Aidha, Mhe. Jaji Mstaafu Nsekela amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa kuwasilisha taarifa ya akaunti yake ya benki sambamba na tamko hilo, na amekiri kuwa ameonesha mfano wa kuigwa na viongozi wengine.

Tamko la viongozi wa umma kuhusu rasilimali na madeni linatolewa kwa mujibu wa kifungu cha 9 na cha 11 cha sheria ya maadili ya viongozi wa umma namba 13 ya mwaka 1995.
Rais Wa Jamhuri Ya Muungano Wa Tanzania Mhe.Dkt.John Pombe Magufuli akiwasili Katika Ofisi Za Sekretarieti Ya Maadili Ya Viongozi Wa Umma Jijini Dar Es Salaam kuwasilisha fomu zake za tamko la Rasilimali na madeni kwa Viongozi wa Umma Disemba 28,2017.
Rais Wa Jamhuri Ya Muungano Wa Tanzania Mhe.Dkt.John Pombe Magufuli akisalimiana na Kamishina wa Maadili Jaji Mstaafu Haroild Nsekela alipowasili Katika Ofisi Za Sekretarieti Ya Maadili Ya Viongozi Wa Umma Jijini Dar Es Salaam kuwasilisha fomu zake za tamko la Rasilimali na madeni kwa Viongozi wa Umma Disemba 28,2017.
Rais Wa Jamhuri Ya Muungano Wa Tanzania Mhe.Dkt.John Pombe Magufuli akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili Katika Ofisi Za Sekretarieti Ya Maadili Ya Viongozi Wa Umma Jijini Dar Es Salaam kuwasilisha fomu zake za tamko la Rasilimali na madeni kwa Viongozi wa Umma Disemba 28,2017.
Rais Wa Jamhuri Ya Muungano Wa Tanzania Mhe.Dkt.John Pombe Magufuli akihakiki fomu zake kabla ya kuziwasilisha kwa Kamishina wa Maadili Jaji Mstaafu Haroild Nsekela Katika Ofisi Za Sekretarieti Ya Maadili Ya Viongozi Wa Umma Jijini Dar Es Salaam Disemba 28,2017.
Rais Wa Jamhuri Ya Muungano Wa Tanzania Mhe.Dkt.John Pombe Magufuli  akimsikiliza Kamishina wa Maadili Jaji Mstaafu Haroild Nsekela mara baada ya kuwasilisha fomu zake za tamko la Rasilimali na madeni kwa Viongozi wa Umma Katika Ofisi Za Sekretarieti Ya Maadili Ya Viongozi Wa Umma Jijini Dar Es Salaam Disemba 28,2017.
Rais Wa Jamhuri Ya Muungano Wa Tanzania Mhe.Dkt.John Pombe Magufuli akimshukuru Kamishina wa Maadili Jaji Mstaafu Haroild Nsekela mara baada ya kuwasilisha fomu zake za tamko la Rasilimali na madeni kwa Viongozi wa Umma katika Ofisi Za Sekretarieti Ya Maadili Ya Viongozi Wa Umma Jijini Dar Es Salaam Disemba 28,2017.
Rais Wa Jamhuri Ya Muungano Wa Tanzania Mhe.Dkt.John Pombe Magufuli akiwa pamoja na Kamishina wa Maadili Jaji Mstaafu Haroild Nsekela wakiangalia moja ya ofisi  za Serikali zilizopo katika jengo la Sukari House mara baada ya kuwasilisha fomu zake za tamko la Rasilimali na madeni kwa Viongozi wa Umma katika Ofisi Za Sekretarieti Ya Maadili Ya Viongozi Wa Umma Jijini Dar Es Salaam Disemba 28,2017.
Rais Wa Jamhuri Ya Muungano Wa Tanzania Mhe.Dkt.John Pombe Magufuli akisindikizwa na Kamishina wa Maadili Jaji Mstaafu Haroild Nsekela wakiangalia moja ya ofisi  za Serikali zilizopo katika jengo la Sukari House mara baada ya kuwasilisha fomu zake za tamko la Rasilimali na madeni kwa Viongozi wa Umma katika Ofisi Za Sekretarieti Ya Maadili Ya Viongozi Wa Umma Jijini Dar Es Salaam Disemba 28,2017.
Rais Wa Jamhuri Ya Muungano Wa Tanzania Mhe.Dkt.John Pombe Magufuli akiwapungia mkono Wananchi waliokuwepo nje ya jengo la Sukari House mara baada ya kuwasilisha fomu zake za tamko la Rasilimali na madeni kwa Viongozi wa Umma katika Ofisi Za Sekretarieti Ya Maadili Ya Viongozi Wa Umma Jijini Dar Es Salaam Disemba 28,2017.Disemba 28,2017.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
28 Desemba, 2017

Rais Magufuli aipa meno kamati ya kuhakiki mali za CCM

$
0
0
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 28 Desemba, 2017 amekutana kwa mara ya kwanza na kamati maalum aliyoiunda kwa lengo la kuhakiki mali za chama hicho, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Kamati hiyo aliitangazwa tarehe 20 Desemba, 2017 Mkoani Dodoma na inaongozwa na Dkt. Bashir Ally.

Katika Mazungumzo hayo Mhe. Rais Magufuli amewataka wajumbe wa kamati hiyo kufuatilia na kuhakiki mali zote za chama, kumhoji mtu yeyote ambaye atahitajika kutoa taarifa juu mali za chama na kubaini thamani ya mali, mahali zilipo, makusanyo ya mapato na wanaozishikilia ama kutumia mali hizo.

Mhe. Rais Magufuli pia ametoa wito kwa wanachama wa CCM na wananchi wengine kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa zote zinazohusu mali za chama kwa kamati hiyo, na watakaoitwa kuhojiwa waitikie wito huo.

“Nataka mali za chama zikinufaishe chama, nataka mkamhoji mtu yeyote, awe kiongozi, awe mwanachama, awe mfanyabiashara, mtu yeyote. Mkazihakiki mali zote ili chama kipate haki yake” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Akizungumza kwa niaba ya kamati hiyo, Dkt. Bashiru Ally amesema kamati imeanza kazi rasmi na ametoa wito kwa wanachama, wananchi na wote wanaozitumia mali za chama kutoa ushirikiano watakapoitwa kuhojiwa.

“Tumezungumza na Mwenyekiti kwa karibu saa mbili, katueleza matarajio yake, sababu za kuunda tume hii, kazi zake na faida zake kwa chama na kwa nchi, kwa hiyo ametukabidhi vitendea kazi na taarifa mbalimbali na ametueleza kazi yetu ni kuhakiki mali zote za chama kwa kushirikiana na wanachama na wale wanaoshirikiana na chama kuzitumia hizo mali kama vile wapangaji, wasimamizi, nakadhalika” amesema Dkt. Bashiru Ally.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
28 Desemba, 2017

Benki Kuu ya Tanzania (BOT ) yatoa gawio la Tsh. 300 bilioni kwa Serikali

Taarifa ya Serikali kuhusu viongozi wanaotumia mahubiri yao kuchambua masuala ya kisiasa.

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Ijumaa ya Disemba 29

Waziri Mkuu akagua miradi ya jimboni mwake

$
0
0
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameanza ziara fupi ya siku tatu, kukagua miradi ya maendeleo jimboni kwake katika wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi.

Waziri Mkuu ambaye yuko kwenye mapumziko ya mwisho wa mwaka, amekagua miradi ya maji, ujenzi wa zahanati na kuzungumza na wananchi kaika vijiji vya Mibure, Namakuku, Chienjere, Namahema A na Namahema B.

Akizungumza na wakazi wa kijiji cha Mibure jana mchana (Alhamisi, Desemba 28, 2017) mara baada ya kukagua zahanati ya kijiji hicho, Waziri Mkuu alisema ameridhishwa na ujenzi unavyoendelea na akamwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ruangwa ahakikishe zahanati hiyo ikikamilika inapata kifaa cha kuwatunzia watoto njiti kwa sababu kijiji hicho kiko mbali na Hospitali ya Wilaya ya Ruangwa.

“Nilileta makontena yenye vifaa vya hospitali, na humo ndani mlikuwa na vifaa vya kuwatunza watoto njiti (watoto wanaozaliwa kabla ya muda kutimia). Hakikisha hawa wanapata kifaa hicho kwa sababu hawana gari la kubeba wagonjwa, na pia wako mbali na hospitali ya wilaya na pia kituo cha afya cha jirani kiko mbali pia,” alisisitiza.

Akizingumzia kuhusu upatikanaji wa umeme kijiji hapo, Waziri Mkuu alisema: “Mibure ipo kwenye mipango ya kupata umeme ambao unatoka Nagurukuru, -Nghimbwa-Chienjere-Namakuku-Mibure.”

Aliwataka vijana wa kata hiyo, wachangamkie fursa kwa muanda mitaji ya kuwa na gereji za kuchomelea vyuma, saluni na viwanda vidogo vya usindikaji.

Mapema, akisoma taarifa ya ujenzi wa zahanati ya Mibure mbele ya Waziri Mkuu, Mwenyeiti wa kijiji hicho, Bw. Samwel Chilemba alisema mradi huo umekwishagharimu sh. milioni 52, ambapo kazi zilizokamiliak ni jengo la zahanati, kichomea taka na choo chenye matundu matatu.

Alisema wanakabiliwa na changamoto ya kupanda holela kwa gharama za vifaa vya ujenzi, kupokea michango kidogo kutoka kwa wananchi, ukosefu wa nyumba ya mganga na wauguzi na kiasi cha fedha cha sh. milioni 8.26 za kununulia samani.

Bw. Chilemba alisema kukamilika kwa ujenzi wa zahanati hiyo kutasaidia wakazi wa vijiji jirani vya Njawale, Namakuku, na vijiji jirani vya wilaya ya Nachingwea ambavyo vinapakana na wilaya ya Ruangwa.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,

Viewing all 45270 articles
Browse latest View live




Latest Images