Quantcast
Channel: MPEKUZI
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo JAlhamisi ya Disemba 7


Watuhumiwa watatu wauawa kwa risasi na Polisi

$
0
0
Watu watatu wanaodaiwa kuwa majambazi wameuawa kwa kupigwa risasi na polisi mkoani Kilimanjaro.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamis Issah amesema watu hao waliuawa Jumanne Desemba 5,2017 jioni katika msitu wa Njoro wakati wa majibizano ya risasi na polisi.

Amesema watuhumiwa hao wa ujambazi walikuwa wakiishi chumba kimoja eneo la Njoro ambako polisi walipofika hawakuwakuta na walipata taarifa kuwa wamejificha msituni.

Kamanda Issah amesema kwa kushirikiana na wananchi walikwenda ndani ya msitu huo ambako walisikia milio ya risasi ndipo askari walipofyatua risasi na kusababisha vifo vyao.

Amewataja waliouawa kuwa ni Yusufu Juma Mdoe aliyekuwa akikabiliwa na kesi ya mauaji mwaka 2015; Francis Hamis Kinyaia ‘Wakudata’ ambaye amesema alikuwa akikabiliwa na kesi ya mauaji mwaka 2013.

Kamanda Issah amemtaja mwingine kuwa ni Valerian Joackim ‘Mdoe’ aliyekuwa na kesi ya mauaji ya mwaka 2013.

Amesema uchunguzi wa polisi umebaini watuhumiwa hao walihusika katika tukio la kufungwa miguu, mikono na kuzibwa mdomo mlinzi lililotokea Novemba 24,2017 eneo la Uru Shimbwe. Katika tukio hilo, bunduki mbili aina ya shotgun ziliporwa.

Kamanda Issah amesema katika msitu wa Njoro walikuta bunduki moja aina ya shotgun iliyokatwa mtutu na kitako, huku namba zikiwa zimefutwa, risasi tatu, maganda matatu ya risasi, mapanga mawili, mkasi unaotumika kukata makufuli, kirungu cha polisi, tindo na misokoto miwili ya bangi.

Ameema miili ya watuhumiwa  imehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Kilimanjaro ya Mawenzi.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM sasa Ashitakiwa kwa Uhujumu Uchumi

$
0
0
Aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhani Madabida na wenzake watano jana Jumatano walipanda kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka sita ya uhujumu uchumi ikiwamo kusambaza dawa bandia za kufubaza virusi vya Ukimwi ' ARV’s ' na kusababisha hasara ya Sh 148 milioni.

Kabla ya kusomewa mashtaka ya kesi hiyo mpya ya uhujumu uchumi namba 80 ya 2017, mahakama ilimfutia kesi iliyokuwa na mashtaka matano yanayofanana na hiyo iliyofunguliwa mwaka 2014.

Kesi hiyo ilifutwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Victoria Nongwa baada ya Wakili wa Serikali, Shedrack Kimaro kuomba iondolewe kwa kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) hana nia ya kuendeleza mashtaka dhidi yao.

Kesi hiyo ilikuwa katika hatua ya usikilizwaji wa ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka na mashadi tisa walikuwa wamekwishatoa ushahidi wao na washtakiwa walikuwa nje kwa dhamana.

Baada ya kesi hiyo kufutwa, Madabida ambaye ni ofisa mtendaji mkuu wa kiwanda hicho na wenzake walikamatwa tena na kufunguliwa kesi hiyo mpya ya uhujumu uchumi.

Mbali na Madabida wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Seif Shamte ambaye ni mkurugenzi wa uendeshaji,  Simon Msoffe (meneja masoko) na  Fatma Shango (mhasibu msaidizi) wa Tanzania Pharmaceutical Industries Ltd. Pamoja na Sadick Materu na Evans Mwemezi ambao ni maofisa wa Bohari Kuu ya Dawa. 

Baada ya kusomewa mashtaka washtakiwa hao hawakurusiwa kuongea chochote kwa sababu mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo hadi Mahakama Kuu.

Wakili wa Serikali, Pius Hilla alisema upelelezi wa kesi hiyo umekamilika lakini DPP bado hajafanya maamuzi kama isikilizwe Kisutu ama Mahakama Kuu.

Washtakiwa hao wanatetewa na Mawakili Denis Msafiri, Makaki Masatu na Nehemiah Nkoko.

Wakili Msafiri alisema Mahakama ya Kisutu inayo mamlaka ya kuisikiliza hiyo kwa sababu kiwango chake cha fedha kipo chini ya Sh 1 bilioni  ambayo ndiyo inapaswa kusikilizwa Mahakama Kuu.

Kutokana na hoja hiyo Wakili Hilla aliomba wapewe muda hadi leo  Alhamisi ndiyo wajibu hoja ya upande wa utetezi.

Hakimu Nongwa aliiahirisha kesi hiyo hadi leo  Alhamisi kutokana na ombi hilo na kuamuru washtakiwa wapelekwe polisi hadi leo  Alhamisi itakaposikilizwa hoja kama mahakama hiyo ina mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo ama la.

Mbunge wa Mtwara Mjini (CUF), Maftaha Nachuma Akanusha Kuhamia CCM

$
0
0

Mbunge wa Mtwara Mjini (CUF), Maftaha Nachuma amewataka wananchi wa jimbo hilo kupuuza taarifa zinazosambaa kwamba ana mpango wa kujiondoa katika chama hicho.

Amesema anaendelea kuwatetea wakazi hao ili wapate maendeleo.

“CUF hawana historia ya kuhamahama vyama, hata huyo aliyeondoka ameondoka kwa masilahi binafsi. Mimi Maftaha Nachuma nitakuwa wa mwisho kuondoka CUF,” alisema jana Jumatano Desemba 6,2017.

Alisema suala la wabunge kujitoa katika nafasi zao linasababishwa na njaa kutokana na kuangalia masilahi binafsi bila kutetea wananchi.

Nachuma alisema wabunge wengi walidhani wakipata nyadhifa hizo watakuwa wananufaika kwa kupata fedha lakini sasa hilo halipo kwa kuwa ubunge siyo dili bali ni kwa ajili ya kuwatumia wananchi.

Kupitia mitandao ya kijamii imeelezwa kwamba mbunge huyo ana mpango wa kujiondoa CUF na kujiunga na CCM.

Nachuma alisema wanaosambaza taarifa hizo wana nia mbaya ya kumchafua kwa masilahi binafsi.

Mtatiro : “Sina Mpango wa Kuhamia CCM na Wala Sina mpango wa kugombea Kinondoni.

$
0
0
Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro amekanusha uvumi unaonea kwenye mitandao ya kijamii kwamba ana mpango wa kukihama chama hicho na kuhamia Chama tawala cha CCM.

Kupitia taarifa yake kwa umma aliyoitoa jana  Disemba 6,2017, Mtatiro pia hana mpango wa kugombea jimbo la Kinondoni lililo achwa wazi kufuatia aliyekuwa Mbunge wake kupitia CUF, Maulid Mtulia kujiuzulu na kujiunga na CCM.

“Ndugu zangu, nimeona propaganda nyingi kwenye mitandao juu ya mimi kuhamia CCM au kuwa na mipango ya kuhamia CCM. 

"Nataka niwahakikishie watanzania kuwa SIJAPANGA mipango hiyo na sina nia hiyo. Na naomba niwajulishe kuwa mtu akiwa anahamia CCM, hamuwezi kuwa na tetesi, na mimi sina kawaida ya kufanya maamuzi ghafla na kwa kujificha. 

"Ningelikuwa na nia ya kuhamia CCM ningewataarifu hapa hadharani, miezi kadhaa kabla ya kufanya hivyo, walau jambo moja ambalo Mungu alinijalia ni kutokuwa mwoga na mnafiki na alinipa uwezo mkubwa wa kufanya jambo naloliamini,” alisema na kuongeza.

“Pili, nimepokea meseji nyingi sana zikiniomba nigombee ubunge jimbo la Kinondoni baada ya Mbunge wa (CUF – Lipumba), Ndugu yetu Maulid Mtulia kuhamia CCM. Nataka niweke msimamo wangu mapema, kwamba sina na sikuwahi kuwa na ndoto za kugombea ubunge wa jimbo la Kinondoni,

Masuala ya kugombea ubunge kwenye majimbo ni masuala mapana, yanahitaji maandalizi, ukaribu wako na wapiga kura na historia yako na jimbo hilo. Kwa kiasi kikubwa hakuna kigezo hata kimoja kati ya hivyo ambacho nimekikaribia, kwa hiyo sitoweza kugombea kama nilivyoona baadhi ya fikra za watu mitandaoni.”

Mtatiro amewahakikisha wanachama wa CUF kwamba anaendelea na majukumu yake ya Kamati ya Uongozi CUF, pamoja na kushirikiana na kila mtanzania kwa njia mbalimbali katika kuijenga nchi.

“Na kupitia michango yangu hiyo naendelea kuijenga Tanzania na hata kuunga mkono juhudi chanya za Rais wetu kuijenga Tanzania huku zile juhudi hasi za Rais huyo huyo hasa kwenye eneo la Demokrasia, Utawala Bora na Uchumi, nikizikemea kila siku.

"Mwisho, wapo wendawazimu wanachekelea, wanafurahia na ama kutamani vyama vya upinzani vife. Ukiona elimu ni ghali, hebu jaribu ujinga,” amesema.

Hata hivyo, Mtatiro amesema anaendelea kuwaheshimu wanaohamia CCM, kwa uhuru, utashi na mapenzi yao au kwa kununuliwa, kutokana kwamba sio wa kwanza wala hawatakuwa wa mwisho kufanya hivyo.

Polepole Awapiga Dongo CHADEMA.......Kadai Wamefulia, Wanajiandaa Kususia Uchaguzi

$
0
0
Katibu wa itikadi na Uenezi wa CCM Humphrey Polepole amesema  CHADEMA wamefanya kikao cha dharura  kususia uchaguzi wa marudio wa majimbo na kata unaotarajiwa kufanyika January 13 mwakani.

Polepole amewatuhumu  CHADEMA  kuwa wanatumia mgongo wa kuminywa kwa Demokrasia nchini kususia uchaguzi huo wakati ukweli ni kwamba wamefulia baada ya kutumia vibaya hela ya mfuko wa chama chao. 

"Watani wanakutana leo, agenda ni kutoshiriki uchaguzi unaokuja wa marudio kwa kisingizio cha demokrasia lakini ukweli ni matumizi mabaya ya fedha yamefuja mfuko wa chama. Tafuteni visingizio vingine lakini sio demokrasia. Watu wamechoka siasa za matukio. Kikao chema!" Ameandika polepole katika ukurasa wake wa Twitter.

==>Angalia hapo chini alichoandika

Taarifa kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuhusu Mfumo wa kuagiza na kusafirisha mizigo nje ya nchi.

Ratiba ya Rais Magufuli Baada ya Kuwasili Dodoma Leo

$
0
0
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 07 Desemba, 2017 amewasili Mkoani Dodoma ambako pamoja na mambo mengine atakuwa mgeni rasmi katika sherehe za maadhimisho ya miaka 56 ya Uhuru zitakazofanyika katika uwanja wa Jamhuri Mjini Dodoma Jumamosi tarehe 09 Desemba, 2017.

Katika Ikulu ya Chamwino, Mhe. Rais Magufuli amepokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Satano Mahenge.

Akiwa Mkoani Dodoma Mhe. Rais Magufuli ambaye ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) atafungua vikao vya Jumuiya za CCM na pia atakuwa mgeni rasmi katika shughuli mbalimbali za kiserikali.

Mhe. Rais Magufuli ameongozana na Mkewe Mhe. Mama Janeth Magufuli.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
07 Desemba, 2017

Wanafunzi 650,862 wachaguliwa kidato cha kwanza

$
0
0
Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Tamisemi, Selemani Jafo, amesema jumla ya wanafunzi 650,862 ambao sawa na asilimia 98.31, wamefanikiwa kuchaguliwa kujiunga na masomo ya kidato cha kwanza katika awamu ya kwanza mwaka 2018.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma, Waziri Jafo amesema wanafunzi wengine 11,173 ambao ni sawa na asilimia 1.69 ya waliofaulu hawakuweza kupata nafasi ya kuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika awamu hiyo kutokana na uhaba wa miundombinu.

Amesema idadi ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu imeongezeka kwa 124,209 likiwa ongezeko la asilimia 23.58 ikilinganishwa na wanafunzi 526,653 waliochaguliwa awamu ya kwanza mwaka huu.

Aidha, amesema baadhi ya wanafunzi wa mikoa ya Lindi, Mbeya, Rukwa, Manyara, Katavi na Simiyu, wamekosa nafasi kutokana na uhaba wa miundombinu ya elimu katika mikoa yao vikiwemo vyumba vya madarasa.

Taarifa ya Vikao vya Kitaifa vya Chama Cha Mapinduzi (CCM)

Majaliwa aizungumzia Dar es salaam itakavyobaki Baada ya Serikali Kuhamia Dodoma

$
0
0
Serikali imesema kwamba kuhamia Dodoma haiondoi hadhi ya Jiji la Dar es Salaam, na kwamba mji huo utabaki kuwa sehemu ya biashara.

Hayo yamesemwa leo na Waziri  Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa wakati akifungua  ofisi  ya Shirika la maendeleo ya Umoja wa Mataifa na kuongeza kuwa kuwepo kwa ofisi ya Umoja wa Mataifa mkoani Dodoma ni ishara ya kukamilika kwa serikali kuhamia rasmi mkoani humo.

"Leo nafungua ofisi ya Shirika la Umoja wa Mataifa hapa Dodoma, zaidi ya watumishi 2376 wameshahamia Dodoma, mimi tayari nimehamia mapema, Makamu wa Rais Samia Suluhu ataungana nasi mwishoni mwa mwezi huu , mwakani tunategemea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli atahamia huku", amesema Majaliwa.

Pia ameongeza kwa kusema, "Umoja wa Mataifa una mchango mkubwa sana katika Taifa letu, imechangia mipango mingi ya maendeleo , mpango wa kwanza ulianza mwaka 2011, wakati huu wa pili umeanza 2016 na utaishia 2021".

Aidha Majaliwa amesema hadhi ya mkoa wa Dar es salaam haitopungua ila itakuwa sehemu rasmi ya biashara.

"Viongozi kuhamia Dodoma hakuharibu hadhi ya mkoa huo, utabakia kuwa ni sehemu sahihi ya biashara, tunatengeneza njia sita ambazo zitatoka Ubungo hadi  Chalinze, tunaimarisha mwendokasi ufike maeneo mengi pamoja na njia za reli iendayo haraka" , ameongeza Majaliwa.

Mpango wa kuhamia Dodoma ulianzishwa na aliyekuwa Baba wa Taifa  Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mwaka 1973, utekelezaji umeanza kufanyika mwaka 2017 ndani ya uongozi wa Rais John Pombe Magufuli.

CHADEMA chawataka wabunge wake kujiondoa michuano ya mabunge EAC

$
0
0
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeazimia kuwa wabunge wake wote wanaoshiriki Michezo ya Mabunge ya Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wanatakiwa kuondoka mara moja kwenye kambi ya timu ya Tanzania.

CHADEMA kimefikia uamuzi huo katika kikao chake cha dharura kinachoendelea ambacho kiliitishwa kwa lengo la kutafakari kwa kina maendeleo ya hali ya siasa nchini.

Chama hicho kimesema kuwa maagizo hayo yameanza kutekelezwa usiku wa Jumatano, Disemba 6 mwaka huu baada ya kupitishwa kwa azimio hilo ambapo Kamati Kuu ilimuagiza Katibu wa Bunge kuwafikishia wabunge wahusika mara moja

Baada ya kupokea tathmini ya kina ya Uchaguzi wa marudio katika Kata 43 uliofanyika hivi karibuni CHADEMA kimebaini kuwa ulitawaliwa na uvunjifu Mkubwa wa Haki za binadamu.

Aidha CHADEMA kimesema kuwa maazimio mengine ya kikao cha Kamati Kuu ambacho kinaendelea jijini Dar yatatolewa katika hatua ya baadae ambapo umma utaarifiwa rasmi.

Baada ya Shilole kufunga ndoa Nuh Mziwanda atupa kijembe

$
0
0
Msanii Zuwena Mohamed ‘Shilole’ (katikati) akiwa na mpenzi wake waliyefunga naye ndoa, Ashraf Uchebe (kushoto) katika picha ya pamoja baada ya ndoa hiyo jijini Dar es Salaam usiku wa kuamkia leo.

==>Hatimaye msanii wa Bongo Fleva, Shilole amefungua ndoa na mpenzi wake Ashraf Uchebe huko Masaki usiku wa kuamkia leo jijini Dar es Salaam.

Staa huyo alikuwa akisisitiza kufunga ndoa mwaka huu lakini watu walikuwa wakichukulia poa kwa sababu si mara ya kwanza kutoa kauli kama hiyo lakini jana Desemba 6 akafanya kweli.

Baada ya picha kusambaa mtandaoni aliyekuwa mpenzi wa Shilole, Nuh Mziwanda ameandika ujumbe katika ukurasa wa Instagram ambao unaweza kutafsiriwa kama ametupa kijembe kwenye ndoa hiyo.  Nuh ameandika;

Alie LaLa na BiBi harusi’wiki Moja KabLa ya harusi’Na wala sio Bwana Harusi’Bado mnanishauri harusi 😏 (all girls are pretenders )

Alichokiandika Nuh Mziwanda ni mistari kutoka kwenye wimbo wa Mwana FA ‘Bado Nipo Nipo’ ambao ulitoka takribani miaka 10 iliyopita.

Rais Magufuli akutana na Jaji Mkuu wa Tanzania Dodoma

$
0
0
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 07 Desemba, 2017 amekutana na kufanya mazungumzo na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma katika Ikulu ya Chamwino Mkoani Dodoma.

Baada ya mazungumzo hayo Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amesema Mhe. Rais Magufuli amemuahidi kuwa Serikali itatoa eneo kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama Kuu Mkoani Dodoma na kwamba ujenzi wa majengo utaanza mwezi ujao.

Ameongeza kuwa ujenzi huo utakuwa ni wa Makao Makuu ya Mahakama na Mahakama ya Rufani, na pia utaambatana na ujenzi wa makazi ya Majaji.

Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ameongeza kuwa pamoja na kuanza kwa ujenzi huo Mkoani Dodoma Mahakama inaendelea na ujenzi wa majengo ya Mahakama Kuu katika Mikoa ya Mara, Kigoma, Morogoro na Singida.

Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa ushirikiano wake kwa Mahakama na ameahidi kuwa Mahakama itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa weledi na ufanisi zaidi ikiwemo kupunguza msongamano wa mashauri mahakamani.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chamwino, Dodoma
07 Desemba, 2017

Waziri Mkuu Amaliza Mgogoro Wa Loliondo

$
0
0
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemaliza mgogoro wa matumizi ya pori tengefu la Loliondo ambao umedumu kwa takriban miaka 26.

Hatma hiyo imefikiwa jana (Jumatano, Desemba 6, 2017) kwenye kikao kilichoitishwa na Waziri Mkuu ofisini kwake Mlimwa, Manispaa ya Dodoma ili kutoa mrejesho uliofikiwa na Serikali kuhusu utatuzi wa mgogoro huo baada ya kupokea taarifa ya Kamati ya Uchunguzi.

Waziri Mkuu alisema Serikali imekubali mapendekezo ya kuunda chombo maalum kitakachosimamia eneo la Loliondo ili kunusuru ikolojia ya Hifadhi ya Serengeti na kulinda mazingira na eneo mahsusi la mazalia ya wanyamapori, mapito na vyanzo vya maji.

“Baada ya kupitia mifumo mbalimbali, timu ya wataalam ilipendekeza kuwa utumike mfumo maalum utakaounda chombo maalum, kwa kuwa una maslahi mapana kwa pande zote husika na unalenga kuleta amani na kufikia lengo la kuwa na uhifadhi endelevu katika eneo la Loliondo,” alisema.

Waziri Mkuu aliiagiza Wizara ya Maliasili iandae muswada wa kutunga sheria mahsusi ya kuwa na chombo maalum au mamlaka ya kusimamia eneo la Loliondo ili kunusuru ikolojia ya Hifadhi ya Serengeti pamoja na kulinda mazingira na eneo mahsusi la mazalia ya wanyamapori, mapito na vyanzo vya maji kwa ajili ya ustawi wa hifadhi muhimu zenye maliasili na rasilimali za Taifa kwa manufaa ya wananchi wenyewe na Taifa kwa ujumla.

“Sheria itakayotungwa ihakikishe inawekewa masharti yanayozingatia maslahi ya jamii iliyopo katika eneo la Loliondo, mila zao na desturi zao pamoja na mahusiano yao na matumizi ya ardhi,” alisisitiza Waziri Mkuu na kushangiliwa na wajumbe zaidi ya 60 waliohudhuria kikao hicho.

Vilevile, Waziri Mkuu aliiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii iandae waraka maalum utakaowasilishwa Serikalini kupitia Baraza la Mawaziri kuhusu umuhimu wa kutunga sheria mahsusi ya eneo la Loliondo.

Alisema kuna ulazima wa kushirikisha wadau wote mara baada ya rasimu ya kwanza kukamilika ili wadau waipitie kwanza. Alisisitiza rasimu ya pili iwe imefanyiwa mapitio na kukamilika ifikapo Februari au Machi, 2018 ili mahitaji ya fedha yaingizwe kwenye mchakato wa Bajeti ya Serikali ya Mwaka 2018/2019.

Aliwataka Waheshimiwa Mawaziri na Makatibu Wakuu wa Wizara za Kisekta zinazohusika na mgogoro wa matumizi ya ardhi ya Pori Tengefu la Loliondo wafanye ziara ya kutembelea eneo hilo ili wawe na uelewa mpana kuhusu changamoto za kisekta zilizopo katika eneo husika.

Kikao hicho kilihudhuriwa na Mawaziri wa Maliasili na Utalii; TAMISEMI; Ardhi na Maendeleo na Makazi; Naibu Mawaziri wa Kilimo; Maji; Mifugo na Uvuvi na Elimu na Mafuzo. Pia kilihudhuriwa na wakuu wa taasisi za Serikali, wawekezaji walioko Loliondo, uongozi wa mkoa wa Arusha, madiwani na wananchi kutoka Loliondo.

Desemba 2016, Waziri Mkuu alifanya ziara ya kikazi wilayani Ngorongoro ambako alipokea taarifa ya kuwepo mgogoro wa matumizi ya ardhi katika Pori Tengefu la Loliondo. Januari 2017, aliunda Kamati ya Uchunguzi iliyokuwa na wajumbe 27 ambayo iliongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Bw. Mrisho Gambo.

Washiriki wa kikao hicho waliopata fursa ya kutoa maoni, walipongeza uamuzi wa Serikali ya awamu ya tano wa kuwashirikisha wananchi hadi ngazi ya chini katika kutafuta suluhu la mgogoro huo.

Akichangia kwa niaba ya NGOs, Mkurugenzi wa taasisi isiyo ya Kiserikali ya Pastoralist Women Council, Bi. Manda Neritiko aliishukuru Serikali kwa kuwashirikisha wananchi kutafuta suluhu ya mgogoro huo, hatua ambayo alisema haijawahi kufanyika miaka yote ya nyuma.

“Huko nyuma tulikuwa tukipewa maagizo tu, Serikali imeamua hivi, Serikai imesema vile, lakini kwa awamu hii, tumeweza kuitwa kwenye vikao mbalimbali na kutoa maoni yetu na hata kupewa mrejesho,” alisema.

Aliomba hata katika chombo kipya kitakachoundwa, kuwe na uwakilishi wa wananchi kutoka ngazi ya chini ili waweze kushiriki kikamilifu katika kupanga namna bora ya kuendeleza eneo hilo.

Kwa upande wa wawekezaji, Bw. Scott Tineja Mollel kutoka kampuni ya AndBeyond Tanzania, alisema wao kama wawekezaji wanataka kuhakikishiwa kuwepo kwa utalii wa kesho. “Hatuwezi kuwa na utalii wa kesho kama hatutunzi mazingira ya sasa,” alisema.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,

Wapalestina wazima taa za Krismasi mjini Bethlehem kupinga tangazo la Trump

$
0
0
Wapalestina wamezima taa za krismasi kwenye mji mtakatifu wa Bethlehem alikozaliwa Bwana Yesu, kupinga hatua ya Rais wa Marekani Donald Trump ya kuutambua mji wa Yerusalem kama mji mkuu wa Israel.

Afisa Habari wa Manispaa ya Bethelehem, Fady Ghattas amesema Mti wa Krismasi ulioko kwenye kanisa la Bethlehem ambako wakristo huamini Bwana Yesu alizaliwa, ulizimwa taa zake kwa amri ya Meya wa Manispaa hiyo.

Miji mingine iliyozimwa taa ni Ramallah ulio karibu na mahali alipozikwa kiongozi wa zamani wa Palestina Yasser Arafat.

Waarabu na waislamu katika nchi za Mashariki ya kati wamepinga hatua ya Trump ya kutangaza kutambua Yerusalem kuwa mji mkuu wa Israel.

Marekani yamtaka Odinga kusitisha mpango wa kuapishwa kuwa Rais

$
0
0
Nchi ya Marekani imemtaka Kiongozi Mkuu wa Upinzani nchini Kenya Raila Odinga kuacha mpango wake wa kuapishwa kama rais wa nchi hiyo wiki ijayo Desemba 12, 2017.

Msaidizi wa Katibu wa Masuala ya Afrika Marekani, Donald Yamamoto alipotembelea Kenya,  ametaka kuwepo majadiliano ya pande zote mbili baina ya upinzani na serikali iliyoko madarakani.

Licha ya wito huo, baadhi ya viongozi wa serikali wameonya kwamba tukio hilo la kuapishwa Odinga, linaweza kuhusishwa na kosa la uhaini.

Odinga baada ya uchaguzi Mkuu wa Kenya kufanyika alitoa malalamiko kuhusu mapungufu yaliyojitokeza kwenye uchaguzi huo na kupelekea uchaguzi kurudiwa ambapo Uhuru Kenyata alishinda kwa kishindo.

Chanzo: BBC

Makamu wa Rais azindua rasmi kampeni ya Kitaifa ya usafi awamu ya pili,Dodoma

$
0
0
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameagiza utekelezaji wa Kampeni ya Taifa ya Usafi wa Mazingira uwe ni ajenda ya kudumu ya kila ngazi ya Uongozi.

Makamu wa Rais ameyasema hayol eo wakati wa Uzinduzi wa Kamapeni ya Taifa ya Usafi wa Mazingira awamu ya Pili ukiofanyika katika Viwanja vya Shule ya Msingi Chang’ombe,mkoani Dodoma.

Makamu wa Rais alisema Serikali imejiwekea mikakati mbali mbali ya kupambana na maradhi ya kuambukiza ambapo usafi wa mazingira ni njia mojawapo ambapo katika awamu ya kwanza ya kampeni ya Taifa ya Usafi wa Mazingira ambapo jumla ya kaya 1,662,550 zilijengwa vyoo na shule 2,133 vilijengwa vyoo bora.

Katika awamu ya Pili iliyozinduliwa leo kaya 5,600,000 zinatarajiwa  kuongeza idadi ya vyoo bora na shule za msingi 3,500 na sekondari 700 zitapata huduma ya vyoo bora na sehemu maalum ya kunawa mikono baada ya kutoka chooni.

 “Wahenga walisema Samaki mkunje angali mbichi, methali hii inatukumbusha jukumu la kuwafundisha watoto wetu umuhimu wa usafi wa mazingira tangia wadogo wakiwa mashuleni”alisisitiza   Makamu wa Rais.

Makamu wa Rais alitoa Wito kwa Wanawake wote nchini kujifunga Kibwebwe na kujenga vyoo, alisema Wanawake wamekuwa na vikundi mbali mbali vya kusaidiana na kuwezeshana hivyo kwa kupitia vikundi hivyo wanaweza kufanikisha ujenzi wa vyoo bora majumbani.

Makamu wa Rais aliwapongeza Washindi wote wa Afya na Usafi wa Mazingira kwa mwaka 2016/17. Pia aliwashukuru wadau mbali mbali ambao wamechangia kwa namna moja au nyingine  kufanikisha uzinduzi wa awamu ya pili ya kampeni ya Taifa ya Usafi wa Mazingira.

Mvutano waibuka kesi ya Madabida na wenzake....Mahakama kutoa uamuzi Kesho

$
0
0
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kesho Ijumaa inatarajiwa kutoka uamuzi katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhani Madabida na wenzake watano  kama ina mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo ama la.

Uamuzi huo unatarajiwa kutolewa na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Victoria Nongwa.

Utatolewa baada ya kusikilizwa hoja zilizowasilishwa na upande wa mawakili wa Serikali, Pius Hilla na Shedrack Kimaro na mawakili wa utetezi, Denis Msafiri, Makaki Masatu na Nehemia Nkoko.

Wakili wa Serikali, Kimaro akiwasilisha hoja zao leo Alhamisi alidai kuwa hoja ya mawakili wa utetezi kuwa Mahakama ya Kisutu ina mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo kwa sababu ipo chini ya Sh 1 bilioni siyo sahihi.

Amedai kuwa ni dhahiri kuwa makosa hayo ni ya uhujumu uchumi na mamlaka yenye mamlaka ya kuisikiliza ni Mahakama Kuu Kitengo cha Rushwa na Uhujumu Uchumi maarufu Mahakama ya Mafisadi.

“Hivyo mahakama za chini kama Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo labda kuwepo na kibali cha kulipa mamlaka ya kuisikiliza kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).”

Kutokana na hilo aliiomba Mahakama kutupilia mbali hoja za upande wa utetezi.

Wakili wa utetezi, Msafiri alidai kuwa ameusikia upande wa mashtaka, ila ni rai yao kuwa marekebisho ya sheria ya uhujumu uchumi ya 2016 yanaipa moja kwa moja Mahakama ya Kisutu kuisikiliza kesi hiyo.

Alidai kuwa kosa lolote lililopo chini ya Sh 1 bilioni haliwezi kusikilizwa na Mahakama Kuu Kitengo cha Rushwa na Uhujumu Uchumi ni Mahakama za chini ikiwamo Mahakama ya Kisutu.

Alisisitiza kuwa Mahakama ya Kisutu ina mamlaka kamili ya kuisikiliza kesi hiyo kwa vile shtaka halizidi Sh 1 bilioni na kwamba mahakama hiyo ndiyo yenye mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo na siyo Mahakama Kuu.

Pia alidai kuwa kibali cha DPP cha kuipa mamlaka mahakama kusikiliza kesi kinapaswa kipelekwe mahakamani pamoja na hati ya mashtaka.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi kesho Ijumaa ambapo mahakama itatoa uamuzi na washtakiwa waliamuliwa wapelekwe polisi.

Hata hivyo, Wakili wa Serikali, Pius Hilla aliomba wapelekwe magereza kwa sababu washtakiwa hao kuendelea kuwa mikononi mwa polisi kuna suala la gharama na polisi hawana fungu.

Baada ya kutolewa kwa ombi hilo, Wakili Nkoko aliomba Mahakama kusimamia amri yake kama ilivyoitoa.

Wakili Masatu naye aliiomba mahakama iendelee na oda yake ilivyoitoa jana Jumatano.

Hakimu Nongwa amesema suala la gharama hawawezi kulikwepa pale haki inapotafutwa na kuamuru washtakiwa wapelekwe polisi hadi kesho Ijumaa atakapotoa uamuzi kama mahakama hiyo ina mamlaka ama la.

Madabida na wenzake wanakabiliwa na mashtaka sita ya uhujumu uchumi ikiwamo kusambaza dawa bandia za kufubaza virusi vya Ukimwi ' ARV’s ' na kusababisha hasara ya Sh 148 milioni.

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Ijumaa ya Disemba 8

Viewing all 45270 articles
Browse latest View live




Latest Images