Quantcast
Channel: MPEKUZI
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live

Kamanda Mambosasa aeleza jambazi komando kutoka Burundi wa wenzie 2 walivyouawa na polisi

0
0
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limesema limewauwa majambazi watatu akiwemo raia wa Burundi ambao walikuwa wakifanya uhalifu katika maeneo mbalimbali  ya jiji hilo na nchini kwa ujumla.

Hayo yameelezwa leo na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam ambapo amesema kuwa katika majambazi hao watatu waliouwawa kwenye oparesheni maalum ya jeshi hilo, iliyofanyika kuanzia Novemba 11 hadi 30, 2017 alikuwepo raia mmoja wa Burundi aliyejulikana kwa jina la Fanueli Luchunda Kamana ambaye ana mafunzo ya kijeshi na kufikia ngazi ya Komando.

“Baada ya kuwakamata na kuwafanyia mahojiano walikubali kuonyesha silaha moja aina ya AK 47 pamoja na Magazine mbili zenye jumla ya risasi 57 ambazo zote walikuwa wameficha kwenye vichaka maeneo ya Ubungo Mawasiliano” amesema Kamanda Mambosasa.

Aidha Mambosasa ameeleza kuwa raia huyo wa Burundi ndio alikuwa kiongozi wa kundi hilo ambapo alikuwa anakwenda Burundi kila baada ya kufanya tukio. Ameongeza kuwa baada ya kwenda kuonesha silaha walizokuwa wameficha katika eneo jingine, Mburundi huyo alimvamia askari kwa lengo la kumshambulia ili wajinasue.

“Baada ya kumvamia askari wetu majambazi wale wawili walianza kukimbia lakini askari wetu walifanikiwa kuwadhibiti kwa kuwafyatulia risasi na baadae kuwafikisha katika hospitali ya Mwananyamala ambapo walibainika kuwa wamefariki”, amesema Mambosasa.

Rais Magufuli aitaka kampuni ya Total kuharakisha ujenzi wa bomba la mafuta

0
0
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amekutana na viongozi wa kampuni ya Total ambayo ni mwekezaji mkubwa wa mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi la kutoka Hoima nchini Uganda hadi bandari ya Tanga nchini Tanzania na kuwahakikishia kuwa Tanzania itatoa ushirikiano wa kutosha kwa kampuni hiyo na washirika wengine katika ujenzi wa mradi huo.

Viongozi wa Total waliokutana na Mhe. Rais Magufuli  jana  tarehe 05 Desemba, 2017 Ikulu Jijini Dar es Salaam ni Rais wa masoko na huduma Bw. Momar Nguer, Rais wa Total Afrika Bw. Stanislas Mittelman, Makamu wa Rais wa Total wa Afrika ya Kati na Afrika Mashariki Bw. Jean Christian Bergeron na Mkurugenzi Mtendaji Total Tanzania Bw. Tarik Moufaddal.

Mhe. Rais Magufuli ameitaka Total kuharakisha ujenzi wa bomba hilo uliopangwa kuanza mwezi ujao na kukamilisha mapema hata kabla ya mwaka 2020 uliopangwa ili wananchi wa Tanzania na Uganda waanze kunufaika na mafuta hayo.

“Tuna matumaini makubwa na Total kuwa kazi hii mtaifanya haraka, na naomba niwahakikishie kuwa pamoja na soko la nje, kuna soko kubwa Afrika Mashariki yenye watu Milioni 165, na Serikali ya Tanzania itawapa ushirikiano wa kutosha wakati wote wa ujenzi na uendeshaji wa mradi ili mradi mnalipa kodi vizuri na mnazingatia sheria zetu” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameitaka kampuni hiyo kuzingatia kutoa ajira kwa Watanzania katika wilaya 24 ambazo bomba litapita huku akiwahakikishia kuwa Tanzania inao wakandarasi na wahandisi wa kutosha na wenye uwezo wa kushirikiana nao katika ujenzi wa bomba hilo.

Baada ya mazungumzo hayo Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Bw. Charles Mwijage wamesema pamoja na kuja nchini kuangalia maandalizi ya ujenzi wa bomba, viongozi wa Total wameamua kuimarisha soko la mafuta Tanzania na pia kushirikiana na Serikali katika utafiti wa mafuta katika maeneo ya Ziwa Tanganyika, Eyasi Wembere na Ziwa Rukwa.

Kwa upande wake Bw. Momar Nguer amemshukuru Mhe. Rais Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni kwa msukumo mkubwa walioutoa katika kufanikisha mradi huu na ameahidi kuwa Total itahakikisha inakamilisha haraka mambo machache yaliyobaki ili kuanza ujenzi bila kuchelewa.

Bw. Momar Nguer amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa juhudi zake za kupambana na rushwa jambo lililosaidia kuimarisha mazingira ya uwekezaji na amemuhakikishia kuwa Total ipo tayari kufanya kazi bega kwa bega na Tanzania katika jukumu la utafiti wa mafuta katika maeneo yote yaliyotajwa.

Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli ameagana na Balozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) aliyemaliza muda wake Mhe. Abdulla Ibrahim Alsiwaidi, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mhe. Abdulla Ibrahim Alsiwaidi kwa utumishi wake wa miaka 5 na amemuomba amfikishie salamu za shukrani kwa Rais wa UAE Mtukufu Sheikh Khalifa bin Zayed Al Nahyan kwa ushirikiano ambao Tanzania inaupata katika Nyanja mbalimbali za maendeleo na ustawi wa jamii.

Mnyika aikana barua ya kujiuzulu CHADEMA

0
0
Mbunge wa Kibamba, John Mnyika (CHADEMA) amekanusha vikali taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuwa amejiuzulu nafasi ya Naibu Katibu Mkuu Bara ndani ya chama hicho.

Kupitia mitandao ya kijamii imesambazwa barua inayodaiwa ni ya Mnyika ambayo imedai kuwa amejiuzulu nafasi hiyo ili aweze kupata muda wa kutosha kuwatumikia wapiga kura wake.

Mnyika masema kuwa barua hiyo ni batili na kuwataka wanachama wa CHADEMA na wananchi kwa ujumla kuipuuza kwani ina lengo la kupotosha umma.

Bodi ya Mikopo yatangaza wanafunzi waliopata mikopo baada ya kukata rufaa

0
0
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), imetangaza jumla ya wanafunzi 2679 waliofanikiwa kupata mkopo katika maombi yao ya rufaa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo, Abdul-RAzaq Badru, ameeleza kuwa kati ya wanafuzi 4200 waliokata rufaa, wanafunzi 2679 wamefanikiwa kupata mikopo yao katika mwaka wa masomo 2017/18.

Mkurugenzi Badru ameeleza kuwa kati ya wanafunzi hao 2769 waliopata mikopo, wanafunzi 1847 ni wa mwaka wa kwanza ambao mkopo wao umegharimu kiasi cha shilingi 6.84 bilioni na wanafunzi 832 waliobakia ni wa naoendelea (mwaka wa 2,3 na 4) ambao mkopo wao umegharimu shilingi 2.75 bilioni.

Hatua hii ya kuwapangia wanafunzi wapya mikopo inafanya idadi ya wanafunzi wote wa mwaka wa kwanza walionufaika na mkopo kwa mwaka huu kufikia 33200 ambao mikopo yao ina thamani ya shilingi 108 bilioni.

Aidha Mkurugenzi Badru ameeleza kuwa tayari Bodi ya Mikopo imeanza kuhamisha mikopo ya wanafunzi ambao wamebadilisha vyuo na kuwataka wale ambao bado hawajapata mikopo yao wawe wavumilivu mpaka zoezi la uhamishaji litakapokamilika.

“Mikopo ya wanafunzi 590, hii ni mikopo mbayo ilikuwa imeenda vyuo tofauti, tayari imekwisha kuhamishwa na mikopo hii ina thamani ya shilingi 1.78 bilioni. 

"Sasa hii ndiyo mikopo iliyokuwa imeenda katika vyuo tofauti na tumeanza kuihamisha kutoka vyuo vile ambavyo wanafunzi hawakwenda ili iwafate wanafunzi katika vyuo walivyokuwepo na tutaendelea na utaratibu wa kuhamisha…,” alisema Mkurugenzi Badru.

Taarifa kuhusu uteuzi wa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. William-Andey Lazaro Anangisye.

0
0
Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemteua Prof. William-Andey Lazaro Anangisye kuwa Makamu Mkuu wa chuo hicho kuanzia  Disemba 5, 2017.

Katika taarifa iliyotolewa na chuo hicho imeeleza kuwa, Mkuu wa Chuo, Dkt. Kikwete baada ya kushauriwa na baraza la chuo lakini pia kushauriana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Magufuli amemteua Prof. Anangisye kushika nafasi hiyo ambayo ataitumikia kwa kipindi cha miaka mitano.

Prof. William Andey Anangisye alizaliwa Disemba 26, 1962 Rungwe mkoani Mbeya. Alipata elimu yake ya sekondari Sangu na Musoma kabla ya kujiunga na Chuo cha Mafunzo ya Ualimu Dar es Salaam mwaka 1986 kwa masomo ya Diploma. Amefundisha katika shule za sekondari Lyunga, Mkwawa na Tambaza kwa miaka 11 kuanzia mwaka 1988 hadi 1999.

Alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kama Mkufunzi Msaidizi mwaka 2000. Alipata Shahada ya Sanaa na Elimu mwaka 1992 na Shahada ya Umahiri katika Elimu 1997 kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Aidha, alipata Shahda ya Uzamivu (PhD) kutoka Chuo Kikuu cha Edinburgh.

Baada ya kuhitimu PhD mwaka 2006, Prof. William Andey Anangisye alirejea Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuwa Mkufunzi na kupanda hadi kuwa Mkufunzi Mwandamizi mwaka 2009 na kuwa Profesa Mshiriki (Associate Professor) mwaka 2012.

Hadi wakati wa uteuzi wake, Prof. William Andey Anangisye alikuwa Mkuu wa Shule ya Elimu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (DUCE) nafasi alioishika tangu Machi 2015.

Kabla ya hapo amewahi kutumikia nafasi za Makamu Mkuu (Elimu) wa Kitivo cha Elimu Mkwawa (MUCE) kati ya Mei 2012 hadi Machi 2015, Associate Dean (Elimu) Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Shule ya Elimu 2009-2012 na pia Kaimu Mkuu Idara ya Elimu Msingi (Educational Foundation) tangu 2007-2009.

Agosti 17 mwaka huu aliteuliwa na Rais Dkt Magufuli kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB).

Kwa miaka kadhaa ameshika nafasi mbalimbali kwenye taasisi nyingine kama vile Mjumbe wa Baraza na Mjumbe wa Bodi ya Chuo Kikuu cha Katoliki Ruaha, Chuo Kikuu cha Aga Khan, Mjumbe wa Seneti ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Chuo Kikuu cha Katoliki Ruaha.

Prof. William Andey Anangisye ameshinda tuzo mbalimbali ikiwemo ya Mfanyakazi Bora wa Mwaka 2011 Shule ya Elimu na pia amepata udhamini  na kushirikiana na vyuo mbalimbali katika masuala ya elimu duniani.

Prof. William Andey Anangisye amefanya tafiti na kuchapisha machapisho mengi katika masuala ya elimu. Amechapisha zaidi ya makala 30 ambazo zimechapishwa katika majarida ya kimataifa na kitaifa. Chapisho lake la karibuni ni kitabu cha Fifty Years of Education in Tanzania, 1961-2011: A Historical Account and Review kilichochapishwa mwaka 2014 na Dar es Salaam University Press.

Hafla ya kumuaga Makamu Mkuu anayeondoka Prof. Mukandala na kumkaribisha Makamu Mkuu wa Chuo anayekuja itafanyika Disemba 7 katika Ukumbi wa Nkrumah kuazia saa 7 mchana.

Mwanafunzi Atiwa Mbaroni Baada ya Kukutwa na Sare za JWTZ

0
0
Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam inamshikilia mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Fahari iliyopo Goba kwa kosa la kukutwa na sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Kamanda wa kanda hiyo, Lazaro Mambosasa amesema jana Jumanne Desemba 5,2017 kuwa mwanafunzi huyo mwenye miaka 17 (jina linahifadhiwa) anayesoma kidato cha tatu alikamatwa jirani na Benki ya CRDB maeneo ya Mbezi jijini Dar es Salaam akiwa amevaa sare za JWTZ.

Amesema mwanafunzi huyo akiwa amevaa sare alikuwa akivuta sigara hadharani na kufanya vitendo visivyoendana na maadili ya askari.

Kamanda Mambosasa amesema katika mahojiano ya awali, kijana huyo alijitambulisha kuwa ni askari kutoka  501KJ Lugalo jijini Dar es Salaam.

Amesema baada ya kubanwa alikiri kupata sare hizo kwa rafiki zake na upekuzi ulipofanywa ndani ya begi alilokuwa nalo alikutwa na kofia nyingine moja ya jeshi hilo.

Pia, alikutwa na kitambulisho cha mtoto wa askari wa JWTZ Private Gabriel Kiwila wa 501 KJ.

Kamanda Mambosasa amesema kitambulisho hicho kilikuwa na picha ya mtoto wa askari huyo, Elia Gabriel.

"Mwanafunzi huyo alikuwa akilazimisha kupewa huduma bure, ikiwemo kupanda gari bila kulipa nauli akidai yeye ndiye  askari," amesema Mambosasa.

Amesema uchunguzi unaendelea ili kuwapata rafiki zake ambao inasadikiwa huwa wanashirikiana kufanya uhalifu.

Waziri Lukuvi Awaonya Wamiliki wa Nyumba Wanaowatoza Wapangaji Kodi ya Mwaka Mzima

0
0
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amewaonya wamiliki wa nyumba wanaopangisha na kudai kodi ya mwaka mzima.

Akizungumza jana Jumanne Desemba 5,2017 akifungua jengo la makao makuu ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) jijini Dar es Salaam na sanamu ya Mwalimu Julius Nyerere, alisema kodi ya nyumba inatakiwa kutozwa kila mwezi.

"Mpangaji anatakiwa kulipa kodi kila mwezi labda atake mwenyewe kulipa kwa miezi zaidi ya mmoja," alisema.

Lukuvi alisema hata NHC inatoza kodi kwa wateja wake kwa mwezi. "Acheni tamaa wenye nyumba chukueni kodi kila mwezi," alisema.

Alisema kuna vijana wanaoajiriwa wanashindwa kukaa jirani na mjini kutokana na kutozwa kodi ya nyumba kwa mwaka.

Mbali ya kauli hiyo, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula Novemba 17,2017 akijibu swali la nyongeza la mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Halima Bulembo bungeni alisema Serikali iko katika mchakato wa maandalizi ya muswada wa sheria ambayo itasimamia sekta ya nyumba, hivyo kuondoa changamoto ya wamiliki kudai kodi ya pango ya zaidi ya mwezi mmoja.

Halima katika swali lake alisema vijana ambao ni kati ya asilimia 56 na 60 nchini, wanashindwa kutimiza ndoto zao kutokana na gharama kubwa ya kodi ambayo hutakiwa kulipa kwa kipindi cha mwaka mmoja au miezi sita.

Akijibu swali hilo, Mabula alisema Serikali imeliona tatizo hilo na ipo katika mchakato wa kuandaa muswada wa sheria utakaosimamia sekta hiyo.

Mabula alisema baada ya kukamilika kwa sheria ambayo itaunda chombo cha kusimamia sekta hiyo, wapangaji hawatalipa kodi ya mwaka wala miezi sita tena bali watalipa kwa mwezi na kuweka amana ya miezi mitatu.

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Jumatano ya Disemba 6


JWTZ yaandaa mazoezi ya kijeshi ya pamoja kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

0
0
Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limeandaa mazoezi ya pamoja ya kijeshi kwa maofisa kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Mazoezi hayo yaliyopewa jina ‘Ushirikiano imara’ yanawashirikisha wanajeshi na maofisa wa Serikali kutoka Tanzania, Uganda, Burundi, Kenya na Rwanda.

Mkuu wa Operesheni na Mafunzo ya Jeshi, Brigedia Jenerali Alfred Kapinga alisema jana Jumanne Desemba 5,2017 kuwa watu 300 wanashiriki wakiwamo makamanda wa jeshi na maofisa wa juu kutoka wizara zaidi ya tatu ikiwamo ya Katiba na Sheria.

Alisema kwa Tanzania wanaoshiriki ni makamanda na maofisa watendaji wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Brigedia Jenerali Kapinga alisema kwa upande wa Tanzania washiriki ni 107 na kwamba, mazoezi yameanza  Desemba 4,2017 na yatazinduliwa Desemba  7,2017 na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi.

“Mazoezi yanafanyika katika Kituo cha Mafunzo ya Ulinzi wa Amani cha Kunduchi, Dar es Salaam na yamejikita katika mambo makuu manne,” alisema.

Aliyataja mambo hayo kuwa ni operesheni katika ulinzi wa amani; kupamba na ugaidi; kupambana na uharamia wa aina yoyote ndani ya Bahari ya Hindi; na majanga na maafa.

Alisema lengo la mazoezi hayo ni kuwaandaa na kuwapa uwezo washiriki katika kupanga na kutekeleza majukumu ya operesheni za ulinzi wa amani katika kupambana na ugaidi, uharamia na kukabiliana na maafa.

Brigedia Jenerali Kapinga alisema mazoezi  hayo ni ya siku 17.

Hatima ya Dhamana ya Wabunge Wawili wa CHADEMA Kujulikana Leo.....Ni Baada ya Jana Kurudishwa Rumande

0
0
Wabunge Susan Kiwanga na Peter Lijualikali waliofikishwa jana  katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro pamoja na washtakiwa wengine 36 walirejeshwa rumande.

Mahakama iliyokuwa itoe uamuzi wa dhamana jana  Jumanne Desemba 5,2017 ilikwama kufanya hivyo kutokana na kuibuka hoja za kisheria.

Upande wa mashtaka na ule wa utetezi unavutana kuhusu hati ya kiapo ya kupinga dhamana iliyowasilishwa mahakamani hapo.

Kutokana na mvutano wa kisheria, hakimu Ivan Msack aliahirisha kesi hiyo hadi leo Jumatano Desemba 6,2017 ili kutoa fursa kwa pande zote mbili kujibu hoja kuhusu hati hiyo.
 
Washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka nane likiwamo la kuchoma moto ofisi ya Kata ya Sofi iliyopo wilayani Malinyi.

Washtakiwa wanatetewa na mawakili Peter Kibatala, Ignas Punge, Fredrick Kiwelo na Bartholomew Tarimo.
 
Upande wa mashtaka unawakilishwa na mawakili wa Serikali, Edga Bantulaki na Sunday Hyera.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na mjumbe wa kamati kuu ya chama hicho, Frederick Sumaye walihudhuria mahakamani.

Wengine waliofika mahakamani ni mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche na wa Viti Maalumu, Devota Minja.

Mwanafunzi Aliyesambaza Picha za Nyufa Hostel za UDSM Aachiwa.......Jeshi la Polisi Limetaja Sababu za Kumkamata

0
0
Mbunge wa serikali ya wanafunzi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Daruso), Kumbusho Dawson ameachiwa baada ya kuhojiwa na polisi wa kitengo cha makosa ya mtandao.

Kumbusho alipelekwa Kituo Kikuu cha Polisi jana Jumanne Desemba 5,2017 akitokea Oysterbay alikokwenda kuripoti asubuhi baada ya kuachiwa kwa dhamana juzi usiku.

Wakili Alex Masaba anayewakilisha Kumbusho amesema polisi wamemuachia baada ya mahojiano na wanaendelea na upelelezi hivyo wakimuhitaji watamwita.

Masaba amesema mteja wake alikamatwa kwa kosa la kusambaza picha zinazoonyesha nyufa kwenye jengo la mabweni ya chuo hicho. Hata hivyo, amesema anaamini kilichofanyika si jinai.

"Kosa la kusambaza picha zilizopigwa si jinai hata polisi nimewaeleza kwa kitendo kilichofanyika inabidi apongezwe," amesema Masaba.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alieleza kuwa polisi ilimkamata na kufanya mahojiano na mwanafunzi huyo ili kujua lengo hasa la yeye kusambaza picha hizo pasipo kutoa taarifa kwa wamiliki wa majengo pamoja na wakala wa majengo husika.

“Huyo mwanafunzi alikamatwa na kufikishwa katika kituo cha polisi lakini alihojiwa na kuachiliwa kwa dhamana. 

"Kilichopelekea akamatwe ni ule uzushi awa kuzunguka kwenye kwenye mitando. 

"Sisi tulikuwa tunakitegemea kama angekuwa na taarifa yoyote, wamiliki wa majengo wapo, mkandarasi aliyefanya kazi ile yupo, kwa hiyo mtu ambaye angepaswa kuwa wa kwanza kulalamika angekuwa ni mmiliki wa majengo na sio yeye. 

"Sasa yeye amefikia mahali akarusha, sijui alikuwa na maana gani, hatujaielewa vizuri..,” alisema Kamanda Mambosasa. 

==>Msikilize hapo chini

Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi amtembelea Tundu Lissu hospitalini

0
0
Rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi amemtembelea mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu aliyelazwa Hospitali ya Nairobi nchini Kenya.

Rais Mwinyi akiambatana na mke wake na maofisa wa ubalozi wa Tanzania nchini Kenya, wamemtembelea Lissu hospitalini hapo alipolazwa tangu Septemba 7  anakotibiwa baada ya kuuguza majeraha ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 akiwa nyumbani kwake mjini Dodoma.

Rais Mwinyi anakuwa miongoni mwa viongozi wa juu wa Serikali waliomtembelea Lissu ambaye ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) ambaye hivi karibuni Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan naye alifika hospitalini hapo kumjulia hali.

Maandalizi sherehe ya miaka 56 ya Uhuru Yakamilika

0
0
 Maandalizi ya maadhimisho ya miaka 56 ya Uhuru yamefikia hatua za mwisho huku Serikali ikieleza kuwa sherehe hiyo itapambwa na gwaride la mkoloni litakalofanywa na Jeshi la Polisi.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge alisema itakuwa ni mara ya kwanza kwa gwaride hilo la mkoloni kufanyika katika sherehe hiyo ambayo mgeni rasmi atakuwa Rais John Magufuli.

“Maandalizi muhimu ikiwa ni pamoja na marekebisho ya uwanja na mahitaji mengine muhimu yapo katika hatua za mwisho,” alisema DK Mahenge.

Alifafanua kuwa maonyesho hayo yatakayofanyika Desemba 9 yatajumuisha gwaride maalumu la heshima lililoandaliwa na vikosi vya ulinzi na usalama nchini na onyesho la makomandoo.

Nyinginie ni kwata ya kimya kimya iliyoandaliwa na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Onyesho la Jeshi la mkoloni kutoka Jeshi la Polisi.

“Watoto 225 kutoka shule za sekondari watashiriki katika gwaride hilo,” alisema.

Alisema lengo la Serikali kuwashirikisha ni kuwafundisha na kuwaridhisha tunu ya uhuru, uzalendo, umoja, mshikamano na utaifa.

Pia, kutakuwa na vikundi vya ngoma za asili kutoka Ruvuma, Kigoma, Zanzibar pamoja na kwaya kutoka Chunya mkoani Mbeya.

DK Mahenge aliwasihi Watanzania kumuunga mkono Rais Magufuli kupiga vita rushwa na kufanya kazi kwa bidiii kwa ajili ya kujiletea maendeleo.

Pia, aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika maadhimisho hayo na kutoogopa mizinga itakayopigwa katika sherehe hizo kwasababu haina madhara.
Gwaride la Mkoloni kutoka Jeshi la Polisi likionesha umahiri wake ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Maadhimisho ya sherehe za miaka 56 ya Uhuru wa Tanzania Bara katika Uwanja wa Jamhuri leo Mjini Dodoma.

Kubenea; Sina mpango wa kuhamia CCM

0
0
Mbunge wa Jimbo la Ubungo kwa tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo, Said Kubenea amewataka wananchi wa jimbo lake na nchi nzima kwa ujumla kupuuzia taarifa zinazosambazwa dhidi yake kuhusu yeye kutaka kukihama chama chake.

Kebenea amesema kuwa ataendelea kuwa Mbunge wa jimbo la Ubungo na hana mpango wowote wa kuondoka CHADEMA kuhamia CCM.

“Wananchi wapuuze taarifa zozote zinazonihusisha mimi na kuondoka Chadema na kujiunga na CCM hizo ni za Uzushi mimi bado ni mwananchama wa Chadema na bado ni Mbunge wa Ubungo na sina mpango huo na sijawahi kuzungumza na mtu yoyote.” amesema Kubenea.

Kubenea ameyasema hayo baada ya kuibuka uvumi uliosambazwa katika mitandao mbalimbali ya kijamii zikidai kuwa mbunge huyo anataka kuhamia CCM.

Hivi karibuni kumekuwa na vuguvugu kubwa la kisiasa ambapo wabunge pamoja na wanachama wa vyama mbalimbali wenye nyadhifa tofauti tofauti wakitangaza kujivua uanacham na kujiunga na chama kingine huku Chama Cha Mapinduzi CCM kikishuhudiwa kupata wafuasi wengi wanaokihamia.

Baada ya kurudi CCM, Wema Sepetu Adai Kukatishwa Tamaa

0
0
Baada ya msanii wa filamu, Bongo Wema Sepetu kurudi CCM kutokea Chadema, hatimaye  amevunja ukimya na kufunguka ya moyoni.

Wema amesema hawezi sana kulizungumzia hilo kwa sababu maamuzi yalishafikiwa lakini anajihisi kukatishwa tamaa.

“Yaani it so complicated najikuta sipo kwenye position ya kuielezea in simple English or Swahili, siwezi lakini tubaki tu tunaomba Mwenyenzi Mungu kwamba everything it will be ok one day inshallah” Wema ameiambia K Fm, Rwanda.

“I am strong, nisingekuwa strong nisingekuwa hapa sasa hivi najaribu kusali kwa hii hali, muda mwingine kama bidamu inakuwa inanivunja moyo najihisi nimekatishwa tamaa, yaani ok!  acha nimuachie Mungu” ameongeza.

February 24 mwaka huu Wema alijiunga na Chadema akitokea CCM na December Mosi alitangaza kurudi CCM.

Wabunge wa CHADEMA warudishwa Tena rumande, hakimu anaumwa

0
0
Maombi ya dhamana ya wabunge wawili wa Chadema na washtakiwa wengine 37 yamekwama kusikilizwa ikielezwa hakimu anaumwa.

Katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro, imeelezwa hakimu Ivan Msack anayesikiliza kesi hiyo ni mgonjwa hivyo imeahirishwa na washtakiwa wamepelekwa rumande hadi Desemba 8,2017.

Akiahirisha kesi hiyo leo Jumatano Desemba 6,2017, hakimu Erick Rwehumbiza amesema Msack amepata maradhi ghafla na yuko hospitalini kwa matibabu.

Baada ya kuelezwa mahakamani kuwa hakimu ni mgonjwa, upande wa utetezi ulimuomba Rwehumbiza kesi hiyo ihamishiwe kwa hakimu mwingine.

Wakili wa utetezi, Peter Kibatala amesema kuahirishwa kesi hiyo na kutotolewa dhamana kwa washtakiwa kunalenga kuchelewesha upatikanaji wa haki.

Kibatala pia ameiomba Mahakama iruhusu wananchi kuingia ndani ya ukumbi kufuatilia uendeshaji wa kesi hiyo.

Wakili wa Serikali, Sunday Hyera akizungumzia hoja ya wananchi kuruhusiwa kuingia ndani ya ukumbi wa Mahakama amesema haina msingi katika kesi hiyo na hakuna uwezekano wa kuiwasilisha mahakamani.

Hakimu Rwehumbiza akijibu hoja hizo, amesema alipewa jalada la kesi kwa ajili ya kuiahirisha.

Kuhusu dhamana amesema ombi hilo litashughulikiwa na hakimu anayehusika na iwapo hatakuwepo Desemba 8,2017 wataangalia namna ya kuihamishia kwa hakimu mwingine.

Hakimu Rwehumbiza amesema suala la wananchi kuingia mahakamani haliathiri uendeshaji wa kesi kwa kuwa wanaweza kuwepo wawakilishi wao.

Wabunge Susan Kiwanga wa Mlimba na Peter Lijualikali wa Kilombero na washtakiwa wengine walifikishwa mahakamani Novemba 30,2017 wakidaiwa Novemba 26,2017 katika Kata ya Sofi wilayani Malinyi walifanya uharibifu wa mali.

Wanadaiwa bila uhalali, huku wakijua wanatenda kosa walikula njama na kuchoma moto ofisi ya kata na kufanya uharibifu wa mali.

Hakimu alisema angetoa uamuzi wa dhamana jana Desemba 5,2017 lakini hilo halikufanyika kutokana na kuibuka hoja za kisheria kuhusu hati ya kiapo ya kupinga dhamana iliyowasilishwa mahakamani hapo.

Kutokana na mvutano wa kisheria, hakimu Msack aliahirisha kesi hiyo hadi leo Jumatano Desemba 6,2017 ili kutoa fursa kwa pande zote mbili kujibu hoja kuhusu hati hiyo.

Polisi waachana na Dk Shika....Wasema Kesi Yake Haina Mashiko

0
0
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu yaDar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema kesi ya Dk Louis Shika hawataendelea nayo kwa kuwa nyumba tatu za mfanyabiashara maarufu Said Lugumi alizoahidi kuzinunua zote zipo.

Novemba 9, 2017 kampuni ya udalali ya Yono kwa niaba ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) iliendesha mnada wa nyumba mbili za Lugumi zilizoko Mbweni JKT na moja Upanga jijini Dar es Salaam ambazo zote Dk Shika alifikia bei ya kuzinunua kwa Sh3.2 bilioni.

Mambosasa akizungumza leo Jumatano, amesema kesi yake haina mashiko hivyo hawataendelea nayo kwa kuwa nyumba hizo zipo na hajatia hasara .

Amesema Dk Shika alikuwa akitamba kuwa ana fedha kumbe uwezo wake ni mdogo na kusababisha  kushindwa kulipa asilimia 25 kwa kila nyumba hizo.

‘‘Dk Shika ni wa kumuonea huruma hana kitu tulisema tunamchunguza na tutampeleka mahakamani lakini tumeona kesi yake haina mashiko ndiyo maana hatuendelei nayo,” amesema Mambosasa.

Jeshi la polisi kanda hiyo lilimshikilia na kumwachia kwa dhamana Dk Shika ambaye alikuwa akituhumiwa kwa kuharibu mnada baada ya kushindwa kulipa asilimia 25 ya fedha hizo ambapo nyumba za Mbweni JKT alifika bei kwa Sh900 milioni na nyingine Sh1.1 bilioni, huku ya Upanga alifika bei ya Sh1.2 bilioni

Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara afariki dunia

0
0
Mkuu wa Mkoa wa Manyara mstaafu, Joel Bendera amefariki dunia katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Msemaji wa MNH, Aminiel Aligaesha amesema, “Ni kweli Joel Bendera amefariki. Aliletwa leo na gari la wagonjwa saa 6:30 mchana na ilipofika saa 10:24 jioni alifariki.”

Aligaesha amesema Bendera alipokewa hospitalini hapo akitokea Bagamoyo mkoani Pwani.

Kuhusu chanzo cha kifo chake Aligaesha amesema, ‘’Hilo sasa ni suala la familia lakini kwa wakati huu itoshe kusema amefariki.”

Bendera pia amewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.

Mbali ya ukuu wa mkoa, amewahi kuwa mbunge wa Korogwe Mjini na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo katika utawala uliopita wa Rais mstaafu, Jakaya Kikwete.

Katika mabadiliko ya wakuu wa mikoa yaliyofanywa na Rais John Magufuli Oktoba 26,2017, Bendera alikuwa miongoni mwa waliostaafu.

Nafasi yake imechukuliwa na Alexander Mnyeti aliyepandishwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara akitokea kuwa Mkuu wa Wilaya ya Arumeru.

Rais Magufuli aomboleza kifo cha aliyekuwa RC Manyara

0
0
“Jioni hii nimepokea kwa mshtuko na huzuni kubwa taarifa za kifo cha Mkuu wa Mkoa Mstaafu Dkt. Joel Nkaya Bendera, natoa pole kwa familia yake na wote walioguswa na msiba huu na pia naungana nao katika kipindi hiki cha majonzi”

Hii ni sehemu ya salamu za rambirambi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli alizozitoa kufuatia kifo cha aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara Dkt. Joel Nkaya Bendera kilichotokea jioni ya leo tarehe 06 Desemba, 2017 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Jijini Dar es Salaam alikofikishwa kwa ajili ya kupata matibabu.

Mhe. Rais Magufuli amesema Dkt. Joel Bendera atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa alioutoa kwa Taifa akiwa kiongozi katika nyadhifa mbalimbali zikiwemo Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Naibu Waziri na Mbunge na pia kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya michezo.

“Dkt. Joel Nkaya Bendera alikuwa kiongozi shupavu, mahiri na mchapakazi, alipenda kufanya kazi kwa ushirikiano na daima alitamani kupata mafanikio makubwa katika majukumu aliyokuwa nayo, hakika tutamkumbuka” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.

Pamoja na kutoa pole kwa familia ya marehemu, Mhe. Rais Magufuli amewapa pole wananchi wa Mkoa wa Manyara ambako alikuwa Mkuu wa Mkoa hadi tarehe 26 Oktoba, 2017, wananchi wa Mkoa wa Tanga ambako alikuwa Mbunge, wanachama wote wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wanamichezo wote na wote walioguswa na msiba huu na amemuombea kwa Mwenyezi Mungu aipumzishe roho yake mahali pema peponi, Amina.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
06 Desemba, 2017

Rais Magufuli afanya mabadiliko ya wenyeviti wa taasisi 6 za serikali

0
0
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amefanya uteuzi wa wenyeviti wa bodi 6 za taasisi za Serikali baada ya wenyeviti waliokuwepo kumaliza muda wao.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo tarehe 06 Desemba, 2017 na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi, Kwanza Mhe. Rais Magufuli amemteua Bi. Monica Ngenzi Mbega kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mazao Mchanganyiko kuanzia tarehe 30 Novemba, 2017.

Pili, Mhe. Rais Magufuli amemteua Prof. Egid Beatus Mubofu kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) kuanzia tarehe 01 Desemba, 2017.

Tatu, Mhe. Rais Magufuli amemteua Prof. Abiud Kaswamila kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro kuanzia tarehe 01 Desemba, 2017.

Nne, Mhe. Rais Magufuli amemteua Prof. Esther Hellen Jason kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kuanzia tarehe 01 Desemba, 2017.

Tano, Mhe. Rais Magufuli amemteua Dkt. Kenneth Mdadila kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya taasisi ya kifedha ya Self Microfinance Fund Limited kuanzia tarehe 01 Desemba, 2017.

Sita, Mhe. Rais Magufuli amemteua Dkt. Titus Mlengeya Dismas Kamani kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania kuanzia tarehe 06 Desemba, 2017.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
06 Desemba, 2017
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live




Latest Images