Quantcast
Channel: MPEKUZI
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live

Ndesamburo Amuibua Dr Slaa

$
0
0
Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Wilbroad Slaa amesema kuwa amesikitishwa sana na kifo cha Mzee Philemon Ndesamburo na kueleza jinsi walivyokijenga chama pamoja.

Dk. Slaa amesema kuwa licha ya Ndesamburo kuwa na utajiri mkubwa, lakini hakuuona kuwa ni kitu bali ni nyenzo ya kuwakomboa wananchi katika sekta mbalimbali.

Dk. Slaa ameitoa kauli hiyo ikiwa ni siku moja tangu aliyekuwa Mbunge wa Moshi Mjini kwa miaka 15, Mzee Philemon Ndesamburo alipozikwa nyumbani kwake KDC Moshi baada ya kufariki wiki iliyopita alivyopata matatizo ghafla akiwa ofisini kwake.

Dk. Slaa ambaye sasa anaishi Toroto nchini Canada baada ya kujiuzulu  wadhifa wake na kuachana na siasa tangu mwaka juzi, alisema kuwa ameshtushwa sana na kifo cha ghafla cha kiongozi huyo tegemeo. Alieleza kuwa licha ya wao kubaki na majonzi, lakini anaamini kazi ya Mungu haina makosa wala haihojiwa.

"Ni kweli nimefanya kazi na Ndesamburo, tumejenga CHADEMA kwa pamoja hasa kipindi cha mwaka 2003 hadi 2005 ambapo tulizunguka nchi nzima," alisema Dk. Slaa na kuongeza kuwa licha ya mazingira magumu waliyokutana naye kwenye harakati za kukitangaza chama hicho, Mzee Ndesamburo hakulalamika alipotakiwa kulala chini, lakini aliona hizo ni changamoto za kutafuta ukombozi.

Aidha, Dk. Slaa alisema kuwa Mzee Ndesamburo alikuwa msikivu na mwenye kuelewa na kuwa tayari kuwasaidia wengi kwa hali na mali kwani mara kadhaa alitoa mali zake kuwasaidia wagombea wa CHADEMA na hata yeye mwenyewe kwenda kuwapigia kampeni bila kujali umbali aliotakiwa kwenda.

Akizungumzia kifo chake, Dk. Slaa alisema kuwa kifo hicho ni cha kusikitisha kwa sababu alifariki ghafla, hakupata nafasi ya kuagana na ndugu jamaa na marafiki. 

"Wakati mwingine afadhai mtu akiugua mnajiandaa kisaikolojia, ila akifariki ghafla tu, huwa ni kazi ngumu kuipokea ile hali.Kazi kubwa iliyobaki kwa watanzania sasa ni kutekeleza yale yote ambayo Mzee Ndesamburo amewaachia huku tukimuombea Mungu ailaze roho yake mahala pema peponi."

Dk. Slaa aliondoka nchini mwaka 2015 baada ya kujiuzulu wadhifa wake kufuatia chama chake kumpokea na kumpa nafasi ya kugombea urais, aliyekuwa kada nguli wa CCM, Edward Lowassa.


Bajeti Kuu ya Serikali Kusomwa Leo

$
0
0
Nchi  za Afrika Mashariki ikiwamo Tanzania zinawasilisha bajeti zao kwa mwaka wa fedha 2017/2018. Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango anatarajiwa kuwasilisha bajeti hiyo bungeni leo mjini Dodoma  kuanzia saa 10 kamili jioni.

Kabla ya kufanya hivyo, asubuhi Dk Mpango atawasilisha Taarifa ya Hali ya Uchumi ya nchi, ambayo itajikita katika kueleza mipango ya maendeleo kwa mwaka ujao. 

Kwa mujibu wa ratiba ya Bunge la Tanzania katika Mkutano wake wa Saba wa Bunge la Bajeti, wabunge watatumia kesho kusoma na kutafakari hotuba hiyo.

Kuanzia Jumatatu ijayo Juni 12 hadi Juni 20, mwaka huu, wabunge watajadili Taarifa ya Hali ya Uchumi na Bajeti ya Serikali kwa siku saba kabla ya jioni ya Juni 20, mjadala kuhitimishwa kwa upigaji kura ya wazi.

Live: Yanayojiri Bungeni Dodoma Leo Juni 8, 2017

$
0
0
Fuatilia hapa matangazo ya moja kwa moja kutoka Bungeni Dodoma, katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, leo Juni 8, 2017..

==>Asuhi hii, Waziri wa Fedha   Dk Mpango atawasilisha Taarifa ya Hali ya Uchumi ya nchi, ambayo itajikita katika kueleza mipango ya maendeleo kwa mwaka ujao. 

Makamu wa Rais: Serikali haitagawa chakula cha msaada kwa wananchi wavivu

$
0
0
Makamu wa Rais wa Jmahuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan amesema kamwe Serikali haitagawa chakula kwa wananchi wavivu ambao hawataki kufanya kazi na kusubiri chakula kutoka Serikalini.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassana ametoa kauli hiyo wakati akihutubia mamia ya wananchi wa Manispaa ya Musoma katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Mukendo mjini Musoma.

Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan amesisitiza kuwa Serikali itapeleka chakula kwa wananchi ambao mazao yao yaliharibiwa kwa mvua au yalikauka kwa ukame au kwa  maafa mengine na sio kwa wananchi wanaokaa vijiweni mchana kutwa bila kufanya kazi wakisubiri neema ya chakula kutoka kwa Serikali.

Amewahimiza wananchi kote nchini kuendelea kufanya kwa bidii ikiwemo shughuli za kilimo na pindi wanapovuka wajiwekee akiba na waache tabia ya kuuza mazao yote wanayovuka ili kukabiliana na tatizo la uhaba wa chakula kwenye familia zao.

Makamu wa Rais pia amewataka viongozi wa mkoa wa Mara washirikiane na wananchi katika kuwaelemisha mbinu bora za kilimo ili waweze kupata mazao mengi ikilinganishwa na hali ilivyo kwa sasa.

Kuhusu tatizo la uvuvi haramu, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan ameziagiza Kamati za Ulinzi na Usalama kufanya misako ya hali na mali katika kupambana na tatizo hilo ambalo limechangia kupunguza samaki katika maeneo mbalimbali nchini.

Ametoa mfano kwa mkoa wa Mara kuwa ulikuwa na viwanda Vinne vya kuchakata samaki lakini kutokana na shughuli za uvuvi haramu na wa kutumia sumu umepelekea viwanda Vitatu kukosa malighafi hiyo na kusitisha uzalishaji.

Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan amesema jambo hilo ni baya kwa sababu limeikosesha Serikali mapato na kusababisha wananchi wakose ajira kutoka kwenye viwanda hivyo jitihada za makusudi lazima zifanyike katika kukomesha uvuvi haramu katika maeneo mbalimbali nchini hasa katika Ziwa Victoria.

Aidha, Makamu wa Rais ameeleza kufurahishwa na kukamilika kwa mradi mkubwa wa maji wa Musoma ambao umetekelezwa na Serikali ya Tanzania na Serikali ya Ufaransa  na kusema kuwa mradi huo utaondoa tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi wa wilaya ya Musoma.

Amewataka wananchi wa Manispaa ya Musoma kuulinda na kuutunza mradi huo ili uweze kudumu kwa miaka mingi kwa ajili ya kuhudumia wananchi wa Manispaa hiyo.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Mara Dakta Charles Mlingwa amewahimiza wananchi wa mkoa wa Mara kuweka itikadi zao kando na washirikiane katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani humo.

Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Musoma – Mara
7-June-2017 .

Tundu Lissu: ACT- Wazalendo Sio Wapinzani, Bali Walianzishwa Kwa Kazi Maalumu ya Kuua Upinzani

$
0
0
Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Tundu Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki amefunguka kwa kusema chama ACT-Wazalendo kinatumiwa katika kuvunja upinzani uliopo nchini na serikali ya CCM.

Lissu amebainisha madai hayo baada ya Rais Magufuli kumteua aliyekuwa Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Anna Mghwira kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro aliyeapishwa jana katika viunga vya Ikulu Jijini Dar es Salaam.

"Hao siyo wapinzani hawajawahi kuwa wapinzani, walianzishwa kwa kazi maalumu ya kuua upinzani imeshindikana sasa wanapewa zawadi. ACT na Anna Mghwira walikuwa wakabariane na Lowassa nasiyo CCM walipata kura chache hata laki moja hazikufika. Huu ukuu wa Mkoa ni zawadi tu, Ukatibu Mkuu wa Kitila Mkumbo ni zawadi tu wanawazawadia watu wao hawa siyo wapinzani" alisema Lissu.

Aidha, Lissu amesema Serikali ya Chama cha Mapinduzi haijawahi kuwa na shida ya aina yeyote na viongozi wa ACT bali shida yao kubwa ni CHADEMA na CUF.

"Serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM), haijawahi kuwa na shida na ACT wala Kitila Mkumbo, haijawahi kuwa na shida na Anna Mghwira na hao wanaojiita wapinzani wote, shida yao kubwa ni CHADEMA na CUF ndiyo wapinzani wengine wote hawa ni wana CCM" alisisitiza Lissu.

Pamoja na hayo, Lissu amesema haitoweza kuja kutokea kwa Rais Magufuli kuja kumteua yeye kwa nafasi yeyote na endapo itatokea hivyo basi atamtaka kwanza abadilishe katiba mpya ili waweze kutengeza nchi mpya.

Waziri wa Fedha Dk Philip Mpango aeleza hali ya ukuaji uchumi wa Nchi

$
0
0
Serikali imetoa takwimu ikielezea hali ya ukuaji uchumi katika kipindi cha mwaka 2016 na kueleza kuwa kiwango hicho kimeendelea kukua kwa wastani wa asilimia saba ikiwa ni pungufu kidogo ya kile kilichotarajiwa awali.

Akisoma hotuba ya mwelekeo wa hali ya uchumi wa Taifa bungeni leo Alhamisi,  Waziri wa Fedha na Mpango , Dk Philip Mpango amesema makadirio ya awali yalionyesha kuwa uchumi huo ungekua kwa wastani wa asilimia 7.2.

“ Hali ya ukuaji uchumi imeendelea kushuhudiwa katika kiwango  kilekile cha awali cha asilimia saba na hii imechangiwa na mambo mengi ikiwamo  baadhi ya sekta kutofanya vizuri,” amesema.

Ametaja baadhi ya sababu hizo kuwa ni pamoja na kushuka wa sekta ya kilimo iliyotarajiwa kukua kwa asilimia 2.9, lakini malengo hayo hayakufikiwa na badala yake yalikuwa kwa asilimia 2.1.

Pia, amegusia sekta ya biashara aliyosema ilikuwa kwa asilimia 6.7 hali ambayo ni tofauti na makadirio yaliyowekwa awali yaliyokuwa asilimia 7.8.

Eneo la chakula nalo limetajwa kuchangia kushindwa kufikia kwa malengo ya ukuaji wa uchumi.

“Makadirio yetu yalikuwa kwamba sekta ya chakula ingekua kwa asilimia nane, lakini bahati mbaya ilishuka na kuwa asilimia 3.7,”amesema.

Hata hivyo, alikumbusha namna sekta nyingine zilivyoweza kufanya vizuri na kusaidia uchumi wa Taifa kuendelea kuhifadhi kiwango chake. Baadhi ya sekta hizo ni pamoja na habari na mawasiliano, madini na kiashirio cha kuendelea kukua kwa sekta ya viwanda.

Serikali kuendelea kudhibiti matumizi ya fedha za umma yasiyo ya lazima

$
0
0
Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma
Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina imeahidi kuendelea kusimamia na kufuatilia sheria na miongozo yote iliyotolewa ili kuhakikisha lengo la kudhibiti matumizi yasiyo ya lazima kwenye Mashirika na Taasisi za Umma ikiwemo safari za nje na posho za wajumbe wa Bodi za mashirika na Taasisi zote za Umma linafanikiwa.

Hayo yameelezwa Bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Vwawa (CCM), Mhe. Japhet Hasunga ambaye alitaka kujua hatua ambazo Serikali inatarajia kuchukua kudhibiti matumizi ya fedha za Umma katika Taasisi zake.

Dkt. Kijaji alisema kuwa Serikali imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa matumizi ya fedha za Umma yasiyo ya lazima yanadhibitiwa kikamilifu kupitia Sheria mbalimbali zilizotungwa na Bunge ikiwemo Sheria ya Bajeti Na. 11 ya mwaka 2015 ambayo imebainishwa hatua mbalimbali za kibajeti zenye lengo la kuongeza usimamizi na udhibiti wa matumizi ya fedha za Umma katika Mashirika na Taasisi za Umma.

“Sheria hiyo imebainisha utolewaji wa Mwongozo wa Mipango na Bajeti wa Serikali unaojumuisha Mashirika na Taasisi zote za Serikali ambao unatoa miongozo mbalimbali ya kuzingatiwa katika matumizi ya Umma kwa mwaka husika,” alifafanua Dkt. Kijaji

Alisema kuwa kupitia Sheria hiyo, Ofisi ya Msajili wa Hazina imepewa mamlaka ya kupitia bajeti za Mashirika na Taasisi zilizo chini yake kwa kuzingatia miongozo na mipango ya Serikali inayotarajiwa kutekelezwa.

Mhe. Kijaji alibainisha kuwa katika Sheria hiyo Ofisi ya Msajili wa Hazina imepewa jukumu la kupitia na kuridhia kanuni za fedha za Mashirika na Taasisi zote za Umma ili kuimarisha usimamizi na udhibiti wa matumizi ya fedha za Umma.

“Sheria nyingine iliyopitishwa na Bunge ni marekebisho ya Sheria ya Fedha ya Mwaka 2015 ambayo iliweka ukomo kwa Taasisi na Mashirika ya Umma kutumia asilimia 60 tu ya mapato yake kwa matumizi ya kawaida yasiyojumuisha mishahara,” aliongeza Dkt. Kijaji.

Aidha, Dkt. Kijaji alisema kuwa katika kuhakikisha Ofisi ya Msajili wa Hazina inatekeleza majukumu yake kisheria, imetoa miongozo mbalimbali yenye lengo la kudhibiti matumizi ya Mashirika na Taasisi za Umma ili kupunguza matumizi ya Serikali yasiyo ya lazima.

“Miongoni mwa miongozo hiyo ni barua iliyotolewa na Msajili wa Hazina tarehe 10 Novemba, 2015 ya kudhibiti safari za nje ya nchi zisizo za lazima kwa watumishi wa Mashirika na Taasisi za Umma ambazo awali zilionekana kutumia sehemu kubwa ya fedha za Umma,” alisema Dkt. Kijaji.

Aliongeza kuwa waraka wa Msajili wa Hazina Na. 12 wa mwaka 2015 kuhusu Posho za Vikao vya Bodi ya Wakurugenzi wa Mashirika na Taasisi za Umma pia ni miongoni mwa miongozo ya kuzuia matumizi yasiyo ya lazima kwani waraka huo umefuta posho za vikao vya Bodi na kuondoa utaratibu wa Bodi kuwa na vikao zaidi ya vinne kwa mwaka.

Dkt. Kijaji alisema kuwa Waraka wa Msajili wa Hazina Na. 1 wa mwaka 2016 kuhusu posho za kujikimu kwa Wajumbe wa Bodi za Wakurugenzi wa Mashirika na Taasisi za Umma ulikuwa na lengo la kuendeleza jitihada za Serikali kupunguza matumizi yasiyo ya lazima ya fedha za Umma.

Alisema kuwa Waraka huo uliweka ukomo wa posho hizo kwa Wajumbe wa Bodi kwa safari za ndani na nje ya nchi, huku akisisitiza kuwa bado Serikali itaendelea kuhakikisha matumizi ya fedha za Umma yasiyo ya lazima yanadhibitiwa kikamilifu.


RC Ana Mghwira atembelea familia ya Ndesamburo na kutoa Pole.

$
0
0
Baada ya kutia saini kitabu cha wageni katika ofisi yake mpya leo Alhamisi, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mgwhira, ameenda kuhani msiba wa aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema, mkoa huo, marehemu Philemon Ndesamburo.

Mghwira ametoa rambirambi kwa familia ya Ndesamburo, aliyewahi kuwa mbunge wa Moshi Mjini kwa awamu tatu mfululizo.

Mghwira aliyeteuliwa hivi karibuni na Rais John Magufuli amewasili katika eneo lake jipya la kazi ikiwa ni siku mbili tu baada ya kuapishwa na Rais,  Ikulu jijini Dar es Salaam.

Mghwira anaanza kazi wakati Chama cha ACT-Wazalendo kikimuondoa katika nafasi yake ya Mwenyekiti wa chama hicho kutokana na matakwa ya katiba ya chama hicho.

Hata hivyo, Mgwhira ataendelea kuwa mwanachama wa ACT-Wazalendo.


Anna Mghwira Azungumzia Sakata la Kuvuliwa Uenyekiti wa ACT-Wazalendo

$
0
0
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira amesema kuwa uamuzi wa kumvua uenyekiti uliochukuliwa na chama chake cha ACT-Wazalendo, umefanyika mapema.

Mghwira ameyasema hayo leo Alhamisi katika Ofisi ya Mkoa wa Kilimanjaro mjini hapa, mara baada ya kutia saini kitabu cha wageni.

Hata hivyo, RC huyo mpya amesema hatua hiyo  itampunguzia mzigo na kumrahisishia kazi tofauti na angeendelea kutumikia uenyeketi wa chama huku akiwa mkuu wa mkoa kwa wakati mmoja.

Mghwira ambaye alikuwa Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo na mgombea wa urais kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kupitia chama hicho, aliteuliwa hivi karibuni  na Rais John Magufuli kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro.

"Mimi siyo mpinzani wa maendeleo nimepewa jukumu la kutekeleza maendeleo ya nchi," amesema Mghawira.

Mghwira ameongeza kuwa kwa nafasi aliyopewa atafanya kazi kwa kufuata Ilani ya CCM aliyopewa na Rais John Magufuli.

Waziri Mpango: Tanzania inaagiza bidhaa nje ya nchi kwa asilimia 60

$
0
0
Tanzania inaagiza asilimia 60.6 ya bidhaa kutoka nje ikiwa ni kiwango kikubwa kuliko kile kinachouzwa nje ya nchi kwa mwaka.

Bidhaa nyingi zinazoagizwa kutoka nje zinatoka katika nchi za China, India, Japan, Kenya na Afrika Kusini. Bidhaa hizo ni pamoja na magari, vipuri, chuma na vyombo mbalimbali vya kielekroniki.

Hata hivyo, Tanzania inauza zaidi chai, mahindi, mbogamboga, dhahabu na shaba katika nchi za Kenya na Afrika Kusini.

Akiwasilisha hotuba ya hali ya uchumi bungeni mjini Dodoma leo, Alhamisi, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amesema katika kipindi cha Januari mpaka Machi mwaka huu, mauzo ya bidhaa nje ya nchi yamefikia Dola za Marekani 2.2 bilioni.

Dk Mpango amesema uagizaji wa bidhaa nje ya nchi ulikuwa na thamani ya Dola za Marekani 2 bilioni huku akiba ya fedha za kigeni ikiwa ni Dola za Marekani 4 bilioni na thamani ya dola moja kwa shilingi ilikuwa ni Sh2,229 kufikia Machi mwaka huu.

“Akiba ya fedha za kigeni imesaidia utengamavu wa thamani ya shilingi. Mpaka kufikia Machi mwaka huu, dola moja ilikuwa na thamani ya Sh2,229,” amesema Dk Mpango.

Tanzania ni ya 5 Kwa Idadi Kubwa ya Watu Afrika

$
0
0
Imeelezwa kuwa Tanzania ina wastani wa ongezeko la idadi ya watu la asilimia 4.7 kwa mwaka na kwamba hadi kufikia Machi mwaka huu ilikuwa na jumla ya watu 48.6milioni huku asilimia 30 ya watu hao wakiishi mijini.

Akiwasilisha hali ya uchumi bungeni Dodoma leo Alhamisi, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amesema idadi hiyo ya watu inaifanya Tanzania kuwa nchi ya tano Afrika kwa kuwa na idadi kubwa ya watu baada ya Nigeria, Ethiopia, Misri na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Dk Mpango amesema Tanzania ina wastani wa ustawi wa watu wa asilimia 0.521 na kuwa nchi ya pili kwa ustawi mzuri Afrika Mashariki baada ya nchi ya Kenya ambayo ina wastani wa ustawi wa asilimia 0.555.

“Serikali inajitahidi kuboresha huduma za jamii ili watu wasikimbilie mijini, kwa mfano huduma za ufundi stadi zimezidi kuimarika na kuwawezesha wananchi kujitegemea wenyewe katika maeneo yao,” amesema Dk Mpango.

Mpango amesema kufikia Machi mwaka huu, watu milioni 22.9 walikuwa wanapata maji safi ikilinganishwa na watu milioni 21 waliokuwa wakipata huduma hiyo hadi Juni 2016, ikiwa ni ongezeko la watu zaidi ya milioni moja.

Waziri wa Fedha: Tutasimamia na Kuhakikisha bajeti ya maendeleo inatolewe kwa wakati

$
0
0
Serikali imesema itahakikisha inachukua hatua zote ili kuhakikisha kiwango cha bajeti ya maendeleo kilichotengwa kinatolewa kwa wakati na kinatekelezeka.

Katika mwaka wa fedha 2017-18 Serikali imetenga bajeti ya Sh32 trilioni na kati ya hizo Sh11.9 kitakwenda katika sekta ya maendeleo.

Akisoma mwelekeo wa hali ya uchumi wa taifa bungeni, leo Alhamisi, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amesema kwa vile Serikali ya Awamu ya Tano imejikita katika kukuza sekta ya viwanda, itasimamia jambo hilo litekelezwe kwa kuhakikisha kiwango cha fedha kwa ajili ya maendeleo kinatolewa kwa wakati.

Kwa miaka kadhaa kumekuwa na malalamiko juu ya kutotolewa kwa kiwango chote cha bajeti ya maendeleo licha ya mpango huo kupitishwa na Bunge.

Lakini Waziri Mpango ameahidi kutolewa kwa fedha hizo kwa wakati na kudai kuwa katika kutekeleza hilo Serikali inakusudia kuanzisha vyanzo vipya vya mapato.

Pamoja na kuanzisha vyanzo vipya ya ukusanyaji mapato, Serikali inakusudia kufanyia mabadiliko mfumo mzima wa ukusanyaji kodi ambao utahakikisha mapato hayo yanakusanywa kwa ufanisi kwa wigo mpana.

“Pia tumeona jinsi mashirika ya umma yalivyokuwa na mchango mkubwa katika uchangiaji wa pato la taifa na kwa maana hiyo tutayaagiza mashirika hayo kukupa kupitia dhamana ya mali walizonazo ili waweze kuchangia kwenye shughuli za kukuza pato la taifa,” amesema.

Pato la Mtanzania laongezeka kwa asilimia 11

$
0
0
Na Raymond Mushumbusi MAELEZO DODOMA
Pato la kila mtanzania kwa mwaka 2016 limeongezeka kwa asilimia 11 kutoka shillingi 1,918,897 kwa mwaka 2015 mpaka kufikia shilling 2,131,299 kwa mwaka 2016.

Takwimu hizi zimebainishwa na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt Philip Mpango wakati akiwasilisha Bungeni Mjini Dodoma Taarifa ya Hali ya Uchumi ya mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa mwaka 2017/2018.

Akifafanua kuhusu ongezeko hilo Mhe. Dkt Philip Mpango amesema kuwa Pato la Taifa kwa mwaka 2016 lilifikia Shillingi million 103,744,606 kwa bei za mwaka husika na kiasi hiki kiligawanywa kwa idadi ya watu 48,676,698 walipo Tanzania Bara na kufanya wastani wa Pato la kila mtanzania kufikia kiasi cha Shillingi 2,131,299.

Ameeleza kuwa kwa thamani ya Dola za Marekani, wastani wa pato la Kila mtu liliongezeka kutoka Dola 967.5 mwaka 2015 hadi Dola 979.1 kwa mwaka 2016 ikionesha kuwa Tanzania inaelekea kwenye kundi la Uchumi wa kati.

“Serikali inaendelea kutatua changamoto mbalimbali ili tuweze kufikia Uchumi wa Kati kwa kuongeza fursa mbalimbali za uzalishaji nchini,” alisistiza Mhe. Dkt Mpango.

Mhe. Dkt. Phili Mpango ameongeza kuwa Serikali imejipanga kuboresha shughuli za uzalishaji wa tija katika Sekta zinazoajiri hususan katika Sekta ya Kilimo cha mazao,Ufugaji na Uvuvi.


Mwenyekiti wa kijiji atekwa Ikwiriri, mwingine aokotwa mtoni

$
0
0
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kati, Ikwiriri, Athuman Mtoteka anadaiwa kutekwa na watu wasiojulikana akiwa  nyumbani kwake.

Mwenyekiti huyo ambaye anawakilisha chama cha Wananchi CUF, anadaiwa kutekwa jana kati ya saa moja na mbili usiku.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Onesmo Lyanga amesema  watu wasiojulikana walifika nyumbani kwake kwa miguu kisha kumchukua na  kwenda naye kusikojulikana.

Amesema taarifa za tukio hilo zilitolewa katika kituo cha Polisi Ikwiriri leo Alhamisi asubuhi na mkewe.

Lyanga ameeleza kuwa baada ya kutolewa kwa taarifa hizo kituoni hapo, Polisi tayari wamefungua jalada la uchunguzi dhidi ya tukio hilo.

"Tumepokea taarifa hizo toka kwa mkewe akielezea mumewe kuchukuliwa na watu wasiojulikana na kuondokanae kusikojulikana" amesema Lyanga.

Kadhalika taarifa toka kwa majirani wa mwenyekiti huyo zinaeleza kuwa waliwaona  watu watano waliofika nyumbani hapo wakitembea kwa miguu kisha kumkamata na kuondoka naye.

Katika tukio jingine, maiti ya mtu mmoja ambaye hajatambulika jina lake imekutwa ikielea ndani ya Mto Rufiji,  Kitongoji cha Ngwalo kilichopo katika Kijiji cha Mtunda A, wilayani Kibiti.

Kamanda Lyanga amesema uchunguzi wa daktari juu ya maiti hiyo ulionyesha marehemu alikuwa na jeraha moja kichwani lililotokana na kupigwa risasi.

Lyanga amesema marehemu alikuwa amefungwa kamba katika mikono yake yote na maiti hiyo  ilikuwa imeanza kuharibika  kutokana na kukaa majini kwa muda mrefu.

Amesema kutokana na maiti hiyo kuanza kuharibika waliuruhusu uongozi wa kijiji hicho kuizika jana Jumatano.

Amesema baadhi ya wananchi wa kijiji hicho waliiona maiti hiyo ikielea majini kwenye mikondo ya maji ya Mto Rufiji kisha kutoa taarifa kwa uongozi wa kijiji hicho nao waliotoa taarifa Polisi.

Kutokana na matukio hayo, Jeshi la Polisi mkoani Pwani kupitia kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Onesmo Lyanga  limetoa wito kwa wananchi waishio katika wilaya za Kibiti na Rufiji kuchukua tahadhari dhidi ya vitendo vya mauaji yanayozidi kutokea katika wilaya hizi mara kwa mara.

Hotuba ya Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip I. Mpango (Mb), ya hali ya uchumi 2016 na mpango wa maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2017/18.

$
0
0
Hotuba ya Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip I. Mpango (Mb), ya hali ya uchumi 2016 na mpango wa maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2017/18.

Live: Msikilize Hapa Waziri wa Fedha Akisoma Bajeti Kuu ya Serikali 2017/ 2018

$
0
0
Msikilize Hapa Waziri wa Fedha Akisoma Bajeti Kuu ya Serikali

Bajeti: Road License yafutwa, sasa kulipwa mara moja

$
0
0
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango ametangaza kufutwa rasmi kwa ada ya mwaka ya leseni ya magari.

Amesema uamuzi umechukuliwa ili ada hii ilipwe mara moja pale gari linaposajiliwa na baada ya hapo iendelee kulipwa katika ushuru wa bidhaa katika mafuta ya petroli na dizeli.

Hayo yameelezwa leo Alhamisi bungeni na Waziri Mpango wakati akiwasilisha bajeti ya mwaka 2017/18.

Pamoja na hayo, Waziri Mpango ameshuha ushuru kwa mvinyo unaotengenezwa kwa zabibu zinazozalishwa ndani kutoka Sh202 kwa lita hadi Sh200 kwa lita.

Kadhalika ushuru wa bia zinazotengenezwa kwa nafaka za ndani umepanda kutoka Sh429 hadi 450 kwa lita.

Wakati huo, ushuru wa bia zisizo na kilevi na vinywaji vya kuongeza nguvu kutoka Sh534 hadi Sh564 kwa lita.

Bajeti: Serikali yazuia usafirishaji madini wa moja kwa moja kutoka mgodini

$
0
0
Serikali imesema haitaruhusu usafirishaji wa madini moja kwa moja kutoka mgodini na kupelekwa nje ya nchi.

Hayo yameelezwa leo Alhamisi na Waziri wa Fedha na Mipango, Phillip Mpango wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti kwa mwaka 2017/18.

Badala yake kutakuwa na viwanja maalumu vya kimataifa katika bandari, migodini na madini hayo yatathibitishwa na kupewa kibali kabla ya kusafirishwa nje.

“Kibali hicho kitatozwa ada ya asilimia moja ya thamani ya madini hayo,” amesema.

Amesema Serikali itatangaza rasmi tarehe rasmi ya kuanza kwa ada hiyo.

Bajeti: Serikali yafuta ushuru wa gesti .....Yatangaza Neema Kwa Wafanyabiashara

$
0
0
Serikali imetangaza kufuta ushuru wa huduma kwenye nyumba za kulala wageni.

Hayo yameelezwa leo (Alhamisi) bungeni na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Phillip Mpango wakati akiwasilisha bajeti kuu ya mwaka 2017/18.

Pamoja na ushuru huo, pia Serikali imefuta ushuru wa mabango yanayoelekeza mahali zinapopatikana huduma za kijamii kama vile shule na hospitali.

Katika hatua nyingine, Serikali imetangaza neema kwa wafanyabiashara wadogo wadogo wasio rasmi wakiwamo mama lishe na baba lishe, ikiahidi kuwapa vitambulisho maalumu vitavyosaidia kuwatambua rasmi.

Amesema vitambulisho hivyo vitawasaidia kutengewa maeneo maalumu ya kufanyia biashara.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amesema hatua hiyo inalenga kuwasaidia wafanyabiashara hao ili kukuza mitaji yao.

Hotuba Ya Waziri Wa Fedha Na Mipango, Mheshimiwa Dkt. Philip I. Mpango (Mb), Akiwasilisha Bungeni Mapendekezo Ya Serikali Kuhusu Makadirio Ya Mapato Na Matumizi Kwa Mwaka 2017/18

$
0
0
 I.     UTANGULIZI
1.          Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako tukufu lipokee, lijadili na kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka 2017/18. Bajeti hii inawasilishwa kwa kuzingatia matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Ibara ya 137 ikisomwa pamoja na Sheria ya Bajeti namba 11 ya mwaka 2015 kifungu cha 26.
2.          Mheshimiwa Spika, pamoja na hotuba hii, ninawasilisha vitabu vinne vinavyoelezea kwa kina makadirio ya Bajeti kwa Mafungu. Kitabu cha Kwanza ni Makadirio ya Mapato; Kitabu cha Pili ni Makadirio ya Matumizi ya Kawaida kwa Wizara, Idara zinazojitegemea, Taasisi na Wakala za Serikali; Kitabu cha Tatu ni Makadirio ya Matumizi ya Kawaida kwa Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa; na Kitabu cha Nne ni Makadirio ya Matumizi ya Maendeleo kwa Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Aidha, upo Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2017 pamoja na Muswada wa Sheria ya Matumizi ya Serikali wa mwaka 2017 ambayo ni sehemu ya Bajeti hii.
3.          Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa baraka na amani anayoendelea kuijalia nchi yetu na pia kwa kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kuwasilisha Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2017/18.
4.          Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee napenda nichukue fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuniamini katika dhamana hii kubwa ya kuongoza wizara nyeti ya Fedha na Mipango. Aidha, ninamshukuru sana kwa kuniongoza na kunitia moyo pale mawimbi yalipozidi kuwa makubwa. Maneno yake mazito kwamba aliniteua ili nipigwe mawe badala yake na badala ya Watanzania maskini na kuwa nimtegemee Mungu daima, yamekuwa ndiyo nguvu yangu katika kazi. Vile vile, nampongeza Mheshimiwa Rais pamoja na wasaidizi wake wakuu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa jimbo la Ruangwa kwa kazi kubwa wanayoendelea kuifanya ya kutuletea maendeleo Watanzania wote.
5.          Mheshimiwa Spika,naomba pia kuwapongeza viongozi wakuu wa mihimili ya dola, nikianza na wewe mwenyewe Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa jimbo la Kongwa, na Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson (Mbunge) Naibu Spika. Ninawapongeza kwa umahiri na busara zenu katika kuongoza Bunge hili. Vile vile, ninawapongeza kwa dhati Mheshimiwa Profesa Ibrahim Juma, Kaimu Jaji Mkuu, kwa kuongoza vyema mhimili wa mahakama katika kutoa haki. 

==>Endelea Nayo <<kwa Kubofya Hapa>>
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live




Latest Images