Quantcast
Channel: MPEKUZI
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live

Diamond ajibu tuhuma za Wimbo wa ‘Salome’ kujaa Matusi

$
0
0
Maoni ya baadhi ya wadau wa muziki kuwa kila wanapousikiliza ‘Salome’ wa Diamond na RayVanny wanapata picha ya matusi, yamekutana na majibu ya Boss huyo wa WCB.

Akifunguka jana kwenye kipindi cha Ngazi Kwa Ngazi kinachorushwa na EATV, Diamond alisema kuwa ‘Salome’ haina matusi bali imebeba lugha ya mahaba mazito.

“Ukiangalia wimbo wa Salome, hauna matusi, ila una maneno ya kimahaba,” alisema Mond.

“Unapozungumzia wimbo wa kimahaba, matusi yanatokea pale. Matusi yapo kwenye mahaba. Unapokuwa unaelezea masuala ya kimahaba utaonekana kama unatukana. Lakini sisi tumejitahidi kadri ya uwezo wetu mahaba yale kuyazungumza katika lugha ambayo ni ngumu sana mtu kuielewa,” alifafanua.

Kwa upande wake Ray Van, alisema kuwa pamoja na yote yanayosikika kwenye wimbo ule, wamejitahidi kutumia tafsida kuyaficha na ndio sababu wimbo ule unapendwa na watu wa rika zote na unaweza kusikilizwa hata katika jumuiya ya watu wanaoheshimiana.

Salome ni wimbo uliochukua mahadhi ya wimbo wa zamani wa Saida Kalori ‘Chambua Kama Karanga’ na umepata nafasi na mafanikio makubwa katika vituo vya runinga vya kimataifa na kuweka rekodi ya aina yake kwenye mtando wa YouTube.

Video ya Salome imeangaliwa zaidi ya mara milioni 13 na laki 7 kwenye YouTube.

CCM Kufanya Mkutano Mkuu Machi 12

$
0
0
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinatarajia kufanya mkutano mkuu maalumu Machi 12, mwaka huu mkoani Dodoma.

Mkutano huo unakuwa wa kwanza kwa Mwenyekiti mpya wa CCM, Rais Dk. John Magufuli baada ya kupokea kijiti kutoka kwa mtangulizi wake Jakaya Kikwete.

Desemba  mwaka jana, Halmashauri Kuu ya CCM Taifa chini ya mwenyekiti wake Rais Magufuli iliridhia mabadiliko makubwa ikiwemo kupunguza idadi ya vikao na wajumbe. 

Desemba 12 mwaka jana aliyekuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye alisema baadhi ya mabadiliko hayo yanaanza mara moja na mengine yatasubiri mabadiliko ya katiba ya chama hicho.

Mbali na mabadiliko hayo, mkutano huo uliofanyika mwishoni mwaka jana ulimpitisha Rodrick Mpogolo kuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho (bara) akichukua nafasi ya Rajab Luhwavi ambaye aliteuliwa kuwa balozi huku Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana akiendelea na wadhifa huo kama ilivyo kwa wajumbe wengine watatu wa Sekretarieti.

Mkutano huo pia ulimpitisha aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Humphrey Polepole kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi huku Kanali Ngemela Lubinga akiteuliwa kuwa Katibu wa Halmashauri Kuu (Siasa na Uhusiano wa Kimataifa), akijaza nafasi iliyoachwa wazi na Dk. Asha Rose Migiro.

Akizungumza jana na waandishi wa habari mjini Dodoma, Mpogolo alisema pamoja na mambo mengine mkutano huo utafanyika kutokana na mageuzi makubwa yanayofanyika ndani ya chama hicho.

Naibu Katibu Mkuu huyo alisema mageuzi hayo ni pamoja na kufanya marekebisho ya kanuni na katiba ya CCM.

 “Mkutano huu pamoja na mambo mengine utafanya kazi yakujadili na kupitisha marekebisho ya katiba ya CCM ya mwaka 1977 toleo la 2012, pamoja na kanuni za chama cha mapinduzi na jumuiya zake,”alisema Mpogolo.

Alisema kuwa kazi nyingine ya mkutano huo ni kupokea taarifa ya ratiba ya uchaguzi mkuu wa chama hicho na jumuiya zake utakaofanyika nchini kote mwaka huu.

“Marekebisho haya ya katiba na kanuni za CCM na jumuiya zake yanafanyika kufuatia maamuzi ya Halmashauri Kuu ya CCM iliyofanyika Desemba mwaka jana mjini Dar es Salaam,’’alisema Mpogolo.

Akizungumzia idadi ya wajumbe watakaoshiriki mkutano huo, Mpogolo alisema kuwa mpaka sasa bado hawana idadi kamili kutokana na uhakiki unaoendelea wa wajumbe hao.

“Bado uhakiki wa wajumbe unaendelea ukishakamilika tutatoa idadi kamili kwani kuna ambao wameshatangulia mbele ya haki na wengine wamehama chama,”alisema Mpogolo.

Aidha Mpogolo alisema mkutano huo utatanguliwa na mkutano wa Kamati Kuu (CC) Machi 10, 2017 na Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Machi 11 mwaka huu.

Mgombea Ubunge CHADEMA auawa kikatili

$
0
0
Kada wa Chadema katika Jimbo la Hai mkoani Kilimanjaro, Anitha Swai ameuawa katika tukio lililogubikwa na wingu zito.

Taarifa za awali zilizopatikana usiku wa kuamkia  leo zimedai kuwa Anitha ambaye aligombea ubunge wa viti maalum mwaka 2015, alitekwa nyara wilayani Rombo na kuuawa maeneo ya TPC nje kidogo ya mji wa Moshi.

Vyanzo mbalimbali vya habari vimedokeza kuwa mara ya mwisho mwanasiasa huyo alionekana akiwa na watu wawili wilayani Rombo siku ya Jumatatu, Februari 27 na kuaga wanaelekea Arusha.

Hata hivyo, tangu siku hiyo Anitha hakuonekana hadi maiti yake ilipogunduliwa jana (Alhamisi) jioni maeneo ya TPC huku gari lake likiwa limetelekezwa maeneo ya Bomambuzi mjini Moshi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Wilbroad Mutafungwa amethibitisha kuokotwa kwa mwili huo, lakini amekataa kuthibitisha kama ni wa kada huyo wa Chadema.

"Ni kweli kuna tukio hilo, lakini ninachoweza kusema bado hajatambuliwa na mwili wake umepelekwa KCMC ili ndugu waweze kuutambua," amesema.

Hata hivyo, Diwani wa Viti Maalumu wa Kata ya Mawenzi mjini Moshi, Hawa Mushi amethibitisha kuwa aliyeuawa ni kada wa chama chao, lakini chanzo na nani waliohusika hakijajulikana.

Hawa amesema taarifa zilizothibitishwa ni kuwa mwili wake ulipatikana maeneo ya TPC huku simu iliyopatikana katika gari yake ndiyo iliyosaidia kumtambua.

Kigogo ALAT atumbuliwa kwa ubadhirifu wa milioni 90

$
0
0
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa nchini ALAT Bwana Gulam Mukadam.
 *****
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa nchini ALAT Bwana Gulam Mukadam amemsimamisha kazi Katibu Mtendaji wa Jumuiya hiyo Bw Abraham Shemoboyo kupisha uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu wa shilingi milioni 150 za ufadhili wa jumuiya hiyo mwaka 2015.

Akiongea katika ofisi za jumuiya hiyo Jijini Dar es salaam, Gulam ambaye pia ni Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga amesema, benki ya NMB ilitoa kiasi hicho cha pesa kwa jumuiya hiyo kwaajili ya ufadhili wa Tuzo ya Meya (Mayor Awards) na kwamba Katibu huyo  hakuwasilisha kiasi chote na badala yake aliwasilisha shilingi milioni 60 huku kiasi cha shilingi milioni 90 kikiwa hakijulikani kilipo.

Mukadam amesema, uamuzi wa kumsimamisha uliamuliwa na kamati tendaji ya ALAT Taifa na mkutano mkuu wa ALAT taifa, ambapo iliundwa tume ndogo kuchunguza upotevu wa kiasi hicho cha pesa na kuamuliwa kuwa apishe uchunguzi dhidi yake kwa upotevu wa pesa hizo.

Aidha Mstahiki Mukadam amesema, uchunguzi dhidi yake utafanywa na CAG na kwamba pesa hizo hazikuwekwa kwenye akaunt ya ALAT na badala yake zilihifadhiwa kwenye akaunti binafsi ijulikanayo kama 'Vision Investment'.

Hatima ya dhamana ya Godbless Lema Kujulikana Leo

$
0
0
Mahakama Kuu Kanda ya Arusha leo inatarajiwa kusikiliza maombi ya dhamana ya Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema ambaye amekuwa akiisaka kwa miezi minne sasa.

Mbunge huyo ambaye amekamatwa tangu Novemba 2 mwaka jana akiwa bungeni Dodoma, amewekwa mahabusu katika Gereza la Kisongo, Arusha.

Jaji Salma Magimbi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha ndiye atakayesikiliza rufaa hiyo namba 126 ya mwaka jana ambayo iliwasilishwa na mawakili wanaomtetea, Kibatala, John Mallya na Sheck Mfinanga.

Maombi hayo yanatokana na mapingamizi ya kisheria yaliyowekwa na Serikali mara baada ya uamuzi uliotolewa Novemba 11 mwaka jana na Hakimu Mkazi Arusha, Desderi Kamugisha kumpa dhamana katika kesi inayomkabili ya kutoa kauli za uchochezi dhidi ya Rais John Magufuli.

Hata hivyo, Lema alikwama baada ya mawakili wa Serikali kuwasilisha kusudio la kukata rufaa. Mawakili wa Lema waliwasilisha Mahakama Kuu, maombi ya kutaka mapitio ya kesi hiyo, lakini yalitupwa na Kaimu Jaji Mfawidhi, Sekela Moshi kutokana na upungufu na kutakiwa kukata rufaa.

Walifanya hivyo Desemba 2 mwaka jana lakini maombi yao yalitupwa kutokana na mapingamizi ya mawakili wa Serikali.

Waliomba kuongezewa muda wa kukata rufaa na Desemba 20 mwaka jana na Jaji Modesta Opiyo alikubali maombi hayo na kutupa mapingamizi ya Serikali.

Hata hivyo, siku ambayo ilipangwa Jaji Maghimbi kutoa uamuzi juu ya rufaa hiyo Jamhuri iliwasilisha notisi ya kupinga kusikilizwa.

Jaji Magimbi alisema kutokana na hilo, rufaa nyingine zitasubiri uamuzi wa Mahakama ya Rufaa.

Februari 27, mapingamizi yote ya Jamhuri yalitupwa na Mahakama ya Rufaa, baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuondoa mapingamizi hayo.

Majaji waliotupa mapingamizi hayo ni Bernard Luanda, Kipenka Mussa na Stela Mugasha ambao walieleza kusikitishwa na mwenendo wa kesi hiyo.

Katika kesi ya msingi, Lema anatuhumiwa kuwa kati ya Oktoba 23 hadi 26 mwaka jana alitoa kauli za uchochezi dhidi ya Rais Magufuli katika maeneo tofauti katika mikutano yake ya hadhara.

Lowassa, Sumaye Wawasili Mahakamani Kusikiliza kesi ya Lema

$
0
0
Viongozi mbalimbali wa Chadema wakiongozwa Katibu Mkuu wa Chadema Dr Vicent Mashinji, Waziri Mkuu Mstaafu na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema Edward Lowasa, Waziri Mkuu Msaatafu Sumaye na Meya wa Jiji la Arusha Mjini Kalisti Lazaro wakiwa mahakamani  kusikiliza uamuzi wa Mahakama kuhusu dhamana ya Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema unaotolewa leo
Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini Godbless  Lema akishuka kwenye gari kuingia mahakamani.

Breaking: Mahakama yamuachia Mbunge Godbless Lema kwa dhamana

$
0
0
Mahakama Kuu Kanda ya Arusha leo imemuachia kwa dhamana Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema baada ya kukaa mahabusu kwa muda wa miezi mine.

Lema aliyekamatwa mapema mwezi Novemba mwaka jana amekuwa akikwama mara kwa mara kupatiwa dhamana katika kesi inayomkabili ya uchochezi dhidi ya Rais Dkt John Pombe Magufuli.

Mahakama imemuachi baada ya kutimiza masharti ya dhamana yaliyokuwa yakimtaka kuwa na wadhamini wawili na TZS milioni 1.

Waziri wa Elimu ataka wanafunzi wapimwe dawa za kulevya

$
0
0
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amewaagiza wakuu wote wa vyuo nchini kuwatambua wanafunzi wao wanaojihusisha na matumizi ya dawa za kulevya na kupeleka taarifa kwake.

Profesa Joyce Ndalichako ambaye ni mjumbe wa Tume ya Kudhibiti Dawa ya kulevya kutokana na wadhifa wake ametoa kauli hiyo leo wakati akifungua kikao cha kazi cha wakuu wa vyuo vya maendeleo ya wananchi (FDCs) kilichofanyika katika ukumbi wa Veta mjini hapa.

Amesema agizo hilo amelitoa kwa wakuu wa vyuo vyote nchini kuona kuwa wanakuwa makini kuhakikisha kuwa kwanza vyuo vyao havigeuzwi kuwa vijiwe vya watu wanaotumia madawa ya kulevya lakini pili kuwatambua vijana wote wanaosoma katika vyuo vyao kama wanatumia madawa ya kulevya.

“Kama serikali tumejiwekea malengo ya kuwa na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 kwa kujenga viwanda na rasilimali kubwa tunayoitegemea ni vijana wetu walioko mashuleni, hivyo kama juhudi za makusudi hazitafanyika katika kupambana na madawa ya kulevya malengo yetu hayatafikiwa kwa kuwa madawa ya kulevya yanaharibu vijana wetu,” alisema Profesa Ndalichako.

Amesema vijana wengi walioko vyuo vikuu wameharibikiwa kutokana na madawa ya kulevya hivyo nguvu kubwa inahitajika katika mapambano hayo ili kulinusuru taifa kwa kuwa wizara hiyo ndiyo yenye dhamana kubwa ya kuhakikisha kuwa Tanzania ya viwanda inafikiwa.

“Hii vita ya madawa ya kulevya siyo ya lelemama inatakiwa ujitoe mhanga kwa kuwa tunapambana na watu wenye nguvu,” alisema Profesa Ndalichako.

Mbali na hilo ameviagiza vyuo vya maendeleo ya Wananchi kuhakikisha kuwa vinajitangaza kwa jamii ili vionekane kuwa vipo kwa kuwa vyuo vingi havina wanafunzi wa kutosha huku ikibainika kuwa chuo kimojawapo (hakukitaja jina) kina mwanafunzi mmoja tu.

AUDIO: Kauli ya Mama Salma Kikwete Baada ya Kuteuliwa Kuwa Mbunge

$
0
0
Tarehe 1 Mwezi wa 3,  2017 Rais Dk. John Magufuli alimteua mke wa Rais mstaafu wa awamu ya Nne mama Salma Kikwete kuwa mbunge wa bunge la Jamuhuri ya muungano wa Tanzania. 

Leo March 3 2017 akiwa mkoani Lindi amezungumza kuhusu kuteuliwa kwake na kumshukuru Rais Magufuli. 

==>Msikilize hapo chini akiongea

Magufuli amtia kitanzini mkandarasi wa maji......Aagiza Kushikiliwa Kwa Hati Zake za Kusafiria

$
0
0
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, ameagiza kushikiliwa kwa hati za kusafiria za mwakilishi wa kampuni ya ukandarasi ya Overseas Infranstructure Alliance Private Limited ya India Bw. Rajendra Kumar pamoja na wasaidizi wake mpaka hapo kampuni hiyo itakapokamilisha ujenzi wa mradi wa maji wa Ng'apa Mjini Lindi ambao ulipaswa kuwa umekamilika tangu tarehe 17 Machi, 2015.

Mhe. Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo tarehe 03 Machi, 2017 alipotembelea mradi huo ambao unatarajiwa kuzalisha zaidi ya lita za ujazo milioni 5 za maji kwa siku kwa ajili ya wakazi wa Mji wa Lindi ambao wanakabiliwa na tatizo kubwa la maji.

Mhe. Dkt. Magufuli ameelezea kusikitishwa na usimamizi mbaya wa mradi huo ambao tayari kiasi cha Shilingi Bilioni 21.8 zimetolewa kati ya Shilingi Bilioni 29 zilizopangwa kutumika hadi kukamilika kwake, na ameonya kuwa endapo mradi huo hautakamilika katika kipindi cha miezi 4 kuanzia sasa atachukua hatua dhidi ya wanaopaswa kuusimamia.

"Ikipita miezi minne nisilaumiwe, hatuwezi kukubali wananchi wa Lindi wanashida ya maji, fedha zimetolewa, mkandarasi anaamua kupeleka fedha India, mradi umecheleweshwa kwa miaka miwili na mkandarasi hayupo kwenye eneo la ujenzi halafu mnaopaswa kumsimamia mnamuangalia tu wakati sheria zipo, kwa nini hamkumfukuza muda wote huu?" amehoji Mhe. Rais Magufuli.

Mapema akitoa maelezo kuhusu mradi huo Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Gerson Lwenge amesema mradi huo unatekelezwa kwa mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KFW) na Jumuiya ya Ulaya (EU) ambapo hadi sasa umefikia asilimia 85 na kwamba mkandarasi amesimamisha kazi kutokana na kuishiwa fedha.

Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na ameiomba bodi hiyo ishirikiane na Tanzania kutekeleza miradi mikubwa ya uzalishaji wa umeme na ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa "Standard Gauge".

Pamoja na kutoa ombi hilo Mhe. Dkt. Magufuli ameipongeza benki hiyo kwa kutoa mikopo nafuu iliyowezesha kutekelezwa kwa miradi mingi ya maendeleo hapa nchini hususani ujenzi wa barabara lakini ameomba mchakato wa upatikanaji wa mikopo hiyo urahisishwe na kuharakishwa ili miradi mingi zaidi itekelezwe kwa wakati.

"Hapa Tanzania AfDB imefanya mambo makubwa sana, tunaipenda sana benki hii kwa sababu imetuwezesha kujenga barabara nyingi zikiwemo ya Iringa - Dodoma inayounganisha Cape Town Afrika Kusini hadi Misri, barabara ya Namtumbo - Tunduru - Masasi na nyingine nyingi, kwa kweli hawa ni wadau muhimu wa maendeleo" amesema Mhe. Rais Magufuli.

Akizungumza baada ya kikao hicho kiongozi wa Bodi ya Wakurugenzi waliokutana na Mhe. Rais Magufuli katika Ikulu ndogo ya Lindi Bi. Lekhethe Mmakgoshi amempongeza Mhe. Dkt. Magufuli kwa juhudi zake za kuleta mageuzi ya kiuchumi nchini Tanzania na ameahidi kuwaAfDB itaendelea kuwa mshirika muhimu wa maendeleo ya Tanzania ikiwemo kufanyia kazi  maombi aliyoyatoa kwa Bodi hiyo.

Nae Dkt. Namajeje Weggoro ambaye ni mmoja wa wakurugenzi hao anayewakilisha nchi saba za Afrika ikiwemo Tanzania amesema Tanzania ni nchi inayoongoza kwa kupata mikopo mingi kutoka AfDB na ameongeza kuwa maombi yaliyotolewa na Mhe. Rais Magufuli yatapewa kipaumbele.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Lindi
03 Machi, 2017

Zuio La Usafirishaji Wa Makinikia (Concentrates) Na Mawe Yenye Madini (Ore) Kwenda Nje Ya Nchi

AUDIO: Watuhumiwa 11,503 wa dawa za kulevya watiwa mbaroni

$
0
0
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema jumla ya watuhumiwa  11,503 wa uzalishaji, usambazaji, uuzaji na utumiaji wa dawa za kulevya wamekamatwa kwa kipindi cha Julai mwaka jana hadi Januari mwaka huu nchini.

Akizungumza leo katika kikao cha Baraza la Mawaziri cha kwanza tangu Serikali kuhamia mjini Dodoma, Majaliwa amesema katika kipindi hicho kesi za kujibu zilikuwa ni 9,811 ambapo watuhumiwa 941 walikutwa na kesi za kujibu huku 238 wakiachiwa huru na kesi 478 bado zinaendelea mahakamani.

Kuhusu pombe za viroba, Majaliwa  amesema oparesheni inaendelea katika mikoa mbalimbali baada ya kupigwa marufuku March Mosi mwaka huu na kwamba kupitia oparesheni hiyo wamegundua mambo mengine ikiwemo uwepo wa makampuni yaliyokuwa hayalipi kodi.

Kwa upande wa ajenda za kikao hicho cha mawaziri, Majaliwa amesema wizara zitatoa takwimu za watumishi wangapi waliohamia, idadi ya watumishi wote,  wamepanga awamu ngapi za kuhamia Dodoma .

==>Msikilize hapo chiniakiongea

VIDEO: Kauli ya Godbless Lema baada ya kuachiwa Huru kwa dhamana

$
0
0
Hatimaye Mahakama Kuu Kanda ya Arusha imemuachia kwa dhamana Mbunge wa Arusha Mjini kupitia CHADEMA, Godbless Lema baada ya kusota gerezani kwa zaidi ya miezi minne.

Mahakama hiyo imefikia uamuzi huo baada ya kupitia hoja za pande zote mbili zilizowasilishwa mahakamani hapo leo na kuamua kuzitupitilia mbali hoja za upande wa serikali za kumnyima Lema dhamana.

Hatua hiyo imekuja ikiwa ni siku chache kupita tangu mahakama rufaa kutupilia mbali rufaa ya jamhuri, huku ikishangazwa na hatua ya Lema kukosa dhama hadi wakati huo.

Mbunge huyo ameachiwa kwa dhamana yenye masharti ya wadhamini wawili wanaoaminika pamoja na kusaini bondi ya shilingi milioni 1 ambapo nje ya mahakama Lema ametoa shukrani zake kwa wote waliohusika na kubainisha kuwa serikali haikuwa na nia njema na yeye, lakini yeye amesimama na Mungu.

"Ninamshukuru sana mwenyezi Mungu, mke wangu, familia yangu, mawakili, viongozi wa chama na wananchi wote waliokuwa na mimi. Na kwa namna ya pekee mke wangu, kama ningepata nafasi ya kuoa tena, ningemuoa yeye. Pia mtoto wangu alifikia hatua akasema anatamani kufanya kosa ili aje alale na mimi gerezani, na akauliza ni kosa gani afanye ili aletwe gerezani" Amesema Lema

Kwa upande wa wakili wake Peter Kibatala amesema hatimaye kazi ya kwanza ya kuhakikisha Lema anapata dhamana imekamilika na kwamba sasa wanajipanga kwa ajili ya kushughulika na kesi ya msingi.

Kwa niaba ya CHADEMA, Mwenyekiti wake Freeman Mbowe, amelaani nguvu iliyotumiwa na jeshi la polisi siku ya leo ya kuwapiga, kuwakamata na kuwatawanya wafuasi wa chama hicho waliofika mahakamani hapo kufuatilia kesi ya mbunge wao, huku akitangaza kuwa kwa leo hakutakuwa na tukio lolote la kisiasa mpaka watakapotangaziwa tena.

==> Tazama Tukio zima hapo chini

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Jumamosi ya March 4

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Jumapili ya March 5


Rais Magufuli Akataa Mwekezaji Badarini.......Atoa maagizo kwa Waziri wa Fedha kuhusu Benki ya NMB

$
0
0
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, ameitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kuachana na utaratibu wa kutoa zabuni za uendeshaji wa bandari kwa kampuni binafsi ambazo huingia mikataba isiyo na manufaa kwa nchi na kusababisha uwepo mianya ya upotevu wa fedha za umma.

Mhe. Rais Magufuli ametoa agizo hilo jana  tarehe 04 Machi, 2017 muda mfupi kabla ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa gati namba 2 ya bandari ya Mtwara ambayo ujenzi wake unatarajiwa kuchukua muda wa miezi 21 kuanzia sasa.

“Kwa sababu mmeamua kuichimba hii bandari ili kuongeza kina mpaka mita 15 kwa kutumia fedha zetu, sitegemei TPA na Wizara kuingia tena mkataba na wawekezaji wengine, kwa sababu imekuwa ni kawaida hapa Tanzania, tunatumia fedha zetu halafu wanakuja watu wengine kufanya biashara na fedha zetu kana kwamba nchi hii haina wasomi, na wanaokuja kuendesha kweli wanaiba” alisema Mhe. Rais Magufuli.

Mapema Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa alisema gati namba 2 itakayojengwa katika bandari ya Mtwara itakuwa na urefu wa mita 350 na ujenzi wake utagharimu Shilingi Bilioni 137.5 zote zikiwa zimetolewa na Serikali ya Tanzania.

Nae Mkurugenzi Mkuu wa TPA Mhandisi Deusdedit Kakoko alisema imelazimu kuongeza gati katika bandari ya Mtwara baada ya kuwepo ongezeko la mizigo inayosafirishwa kupitia bandari hiyo ambapo kiwango cha mizigo inayohudumiwa kinatarajiwa kuongezeka kutoka tani 273,886 mwaka 2015/2016 hadi kufikia tani 388,000 mwaka 2016/2017 kiwango ambacho kinakaribia ukomo wa uwezo wa bandari hiyo yenye uwezo wa kuhudumia tani 400,000 kwa mwaka.

Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amefungua Kituo cha Biashara cha Benki ya NMB Mjini Mtwara na kutoa maagizo kwa Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango kutoa maelekezo ili fedha zote za Serikali zipitie Benki ya NMB ambayo licha ya hisa zake kumilikiwa na Serikali kwa asilimia 32 imekuwa ikitoa gawio kwa Serikali kila mwaka ambapo mwaka 2016 ilitoa Shilingi Bilioni 16.5 na mwaka huu inatarajia kutoa zaidi ya kiwango hicho cha gawio.

“Na nikuombe Waziri, kwa sababu wewe ndio unayesimamia fedha za Serikali, toa maelekezo ili fedha zote zipitie benki ya NMB, labda kama kutakuwa na umuhimu sana wa kupitia benki nyingine” alisema Mhe. Rais Magufuli.

Mhe. Rais Magufuli ambaye ameipongeza benki ya NMB kwa kujikita kutoa huduma za kibenki kwa wananchi wa kawaida na wafanyakazi nchi nzima ametoa wito kwa benki zote nchi kupunguza viwango vya riba ili Watanzania wengi waweze kukopa na kufanya shughuli za uzalishaji mali.

Katika hatua nyingine, Mhe. Rais Magufuli amefungua jengo la Benki Kuu ya Tanzania (BOT) Mjini Mtwara ambalo limejengwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 31 na linatoa huduma za Benki Kuu katika kanda ya kusini inayojumuisha Mikoa ya Mtwara, Lindi na sehemu za Mikoa ya Pwani na Ruvuma.

Pamoja na kumpongeza Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuridhia ujenzi wa jengo hilo na kuipongeza BOT kwa kufanikisha ujenzi huo na kusimamia vizuri uchumi wa nchi, Mhe. Rais Magufuli ameitaka benki hiyo kuu kuchukua hatua kali dhidi ya benki ambazo zimekuwa zikikiuka maadili na taratibu za kibenki ikiwemo kushiriki njama za kuiba fedha za Serikali kupitia mikopo na utakatishaji wa fedha.

Aidha, amemtaka Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Prof. Benno Ndulu aandae utaratibu utakaozibana benki zinazofanya biashara hapa nchini ili zilazimike kuwakopesha wananchi, kupunguza viwango vya riba na kuendeleza shughuli za uzalishaji mali.

Mhe. Rais Magufuli pia amefungua nyumba 40 za makazi za Rahaleo zilizojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Mjini Mtwara kwa gharama ya Shilingi Bilioni 10.5 na ameipongeza NHC kwa kazi nzuri ya ujenzi wa nyumba za makazi ya wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.

Akiwa katika mradi huu Mhe. Dkt. Magufuli ameagiza kuanzia sasa Mkoa, Wilaya ama Kiongozi yeyote atakayeomba kujengewa makazi na NHC ahakikishe eneo lililoandaliwa kwa ajili ya kujengwa makazi hayo linafikishiwa barabara, umeme na maji na ameitaka NHC kuacha kutumia wakandarasi katika ujenzi wa majengo yake na badala yake waunde vikosi kazi vya ujenzi kwa kutumia wataalamu waliopo ndani ya nchi ili kuzalisha ajira zaidi na kupunguza gharama za ujenzi wa majengo.

Mhe. Dkt. Magufuli ambaye jana ameingia Mkoani Mtwara akitokea Mkoani Lindi alisimamishwa na wananchi wa Kijiji cha Mnolela Kilichopo Lindi Vijijini ambapo baada ya kupokea kero ya Kijiji hicho kushindwa kumalizia jengo la zahanati aliamua kulikagua na kisha akatoa mchango wa Shilingi Milioni 15, zitakazojumlishwa na Shilingi Milioni 10 zitakazotolewa na Mbunge wa Jimbo la Mtama Mhe. Nape Nnauye na Shilingi Milioni 30 zitakazotolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Lindi Vijijini, na ameagiza ujenzi huo ukamilike ndani ya miezi 3 kuanzia sasa.

Halikadhalika, Mhe. Rais Magufuli alisimamishwa na kuzungumza na wananchi wa Kijiji cha Madangwa kilichopo Lindi Vijijini ambapo baada ya kupokea kero ya ubadhirifu wa fedha za wakulima wa Korosho ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Lindi kuwasaka viongozi wote wa vyama vya ushirika wanaotuhumiwa kula fedha za wakulima na kuwachukulia hatua za kisheria.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Mtwara

04 Machi, 2017

Rais Magufuli Ashangaa Mkandarasi MVIVU Kupewa Zabuni Mtwara

$
0
0
Rais John Magufuli ameigiza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kumsimamia kwa karibu mkandarasi aliyeshinda zabuni ya ujenzi wa barabara ya Mtwara, Tandahimba, Newala hadi Masasi kwa kuwa ana historia ya kutofanya vizuri.

Kampuni iliyoshinda zabuni ya ujenzi wa kilometa 50 kati ya 210 za barabara hiyo ni DOTT Services LTD kutoka nchini Uganda inayodaiwa kuwa ilichelewesha kazi ilipokuwa inajenga barabara ya Same hadi Mkambala wakati huo Magufuli akiwa Waziri mwenye dhamana ya ujenzi.

"Nina mashaka sana na huyu mkandarasi mliyempa kazi ya ujenzi wa hii barabara...namjua huyu alitusumbua, alijenga barabara ya Same hadi Mkambala alicheleweshakazi," amesema Rais Magufuli.

Alisema kushinda zabuni kwa kuweka kiasi kidogo kuliko wote si sababu pekee ya kuifanya kampuni kupata kazi kwani anaweza kutaja kiasi kidogo lakini akachelewesha kazi na hivyo kuongeza gharama maradufu.

"Ninaposema haya najua mnanielewa...kama ningekuwa ni mimi nisingempa kazi huyu maana namjua, nimeshangaa kumkuta huku tena...sasa hiyo kazi isimamiwe kwa karibu kuhakikisha hatusumbui," amesema Rais Magufuli.

Amesema kuwa kwa kuwa wameshampa kazi ni wajibu kwa wizara na vitengo vyake vyote akiwemo Wakala wa Taifa wa Barabara (Tanroads) Mkoa wa Mtwara kuhakikisha wanamsimamia kwa karibu ili kazi hiyo ikamilike kwa wakati na kwa ubora unaokubalika.

"Hakikisheni kazi hii inafanyika vizuri, ikitokea yale ya kule mimi nitajua nini cha kufanya na ninyi maana mnanijua...kwa kuwa nitakuja kuweka jiwe la msingi basi mwambieni hizi ni salamu zake kutoka kwangu," amesema Rais Magufuli.

Kampuni hiyo tayari imeshasaini Mkataba wa ujenzi wa barabara hiyo kutoka mjini Mtwara hadi Mnivata umbali wa kilometa 50 kwa thamani ya Sh bilioni 89.6 ambapo Mkataba huo ulisainiwa Januari 19, mwaka huu, huku kazi ya ujenzi ikitarajiwa kuchukua miezi 21 pamoja na muda wa maandalizi.

Aidha Kampuni ya Kyong Dong Engineering Co LTD kutoka Korea ikishirikiana na Core Consulting PLC kutoka Ethiopia na kampuni ya Mhandisi Consultancy LTD ya Tanzania ndio zilizoshinda zabuni ya ushauri wakati wa ujenzi huo kwa gharama ya Sh bilioni 2.9 na tayari Mkataba umeshasainiwa.

Raisi Magufuli yupo mkoani Mtwara kwa ziara ya kikazi ya siku mbili ambapo pamoja na uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa gati, pia alifungua jengo la Benki Kuu (BoT0), Kanda ya Kusini, Kituo cha Biashara cha Benki ya NMB na kufungua nyumba za makazi za Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).

Leo Rais atatembelea Kiwanda cha Saruji cha Dangote na baadaye kuhutubia mkutano wa hadhara utakaofanyika katika Uwanja wa Mashujaa mjini Mtwara.

Taarifa Kutoka Ofisi Ya Mkuu Wa Mkoa Dodoma

Askofu Gwajima afanyiwa upekuzi nyumbani kwake

$
0
0
Wakili  wa Mchungaji wa Kanisa la Ufufuo na uzima, Askofu Josephati Gwajima,  Peter Kibatala amesema kuwa polisi wamefanya upekuzi kwa mara nyingine nyumbani kwa Askofu huyo.
 
Kibatala ambaye ni wakili wa Askofu Gwajima amesema kuwa mbali na kupekuwa nakupiga picha kila kona ya nyumba pia walikwenda katika kanisa lake lililopo Ubungo kwa ajili ya upekuzi.
 
“Waache wafanye yao na sisi tutafanya yetu kisheria, Kwani hatuwezi kuwazuia Polisi kufanya shughuli yao na baada ya kumaliza na sisi tutajua nini cha kufanya,” amesema Kibatala.
 
Msemaji wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, David Mngongolwa amesema Gwajima alikwenda polisi kuripoti kama alivyoamriwa kufanya hivyo.
 
Aidha, Mngongolwa ameongeza kuwa baada ya kuripoti askari walimchukua na kwenda naye nyumbani kwake kwa ajili ya upekuzi na baada ya hapo waliondoka naye.
 
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Suzan Kaganda amesema hana taarifa za kukamatwa kwa Gwajima kwa maelezo kuwa alikuwa katika kikao.

Rais Trump Amtuhumu Obama Kwa Kudukua Simu Yake

$
0
0
Rais wa Marekani, Donald Trump amesema kuwa amegundua Rais mstaafu wa nchi hiyo ambaye ni mtangulizi wake, Barack Obama alikuwa akidukua simu yake mwezi mmoja kabla ya kuchaguliwa kuliongoza taifa hilo.

Rais Trump ametoa shutuma hizo kupitia ujumbe wake wa Twitter Jumamosi ambapo ameandika kuwa: ‘Makosa sana! Nimegundua kwamba rais Obama alikuwa akidukua simu yangu katika ofisi yangu iliyopo Trump Tower kabla ya mimi kupata ushindi.’

Pamoja na shutuma hizo, Rais Trump hajatoa ushahidi wowote ili kuthibitisha madai hayo ama hata kusema ni agizo gani la mahakama alilonukuu.

Aidha, vyombo vya habari Marekani vimetoa ripoti zinazoeleza kuwa shirika la kijasusi la FBI liliomba agizo la kuwachunguza maafisa wa karibu wa Rais Trump kutoka kwa shirika la kigeni la kijasusi Fisa kubaini iwapo wamekuwa wakiwasiliana na maafisa wa Urusi.

Pamoja na kwamba agizo hilo lilikataliwa lakini baadaye likakubaliwa mwezi Oktoba kulingana na ripoti hizo za vyombo vya habari.

Viewing all 45270 articles
Browse latest View live




Latest Images