Quantcast
Channel: MPEKUZI
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live

Mzee wa Upako afunguka kuhusu yeye kunywa pombe.....Atangaza maamuzi mapya kwa waandishi aliowatabiria kifo.

$
0
0
Mchungaji Anthony Lusekelo amefunguka kuhusu tuhuma za yeye kunywa pombe, na kuweka wazi kuwa hanywi pombe bali anakunywa 'wine' isiyo na kilevi, huku akisita kusema endapo unywaji pombe ni dhambi au siyo dhambi.

Amefunguka hilo alipokuwa kwenye kipindi cha KIKAANGONI cha EATV, na kuweka wazi kuwa wanaomtuhumu kuwa yeye anakunywa pombe wanapaswa kutoa ushahidi juu ya tuhuma hizo, na kwamba unywaji pombe unaweza kuwa dhambi ama usiwe dhambi kulingana na imani na dini ya mtu.

"Hao wanaotuhumu kuwa nakunywa pombe, waeleze ni pombe gani nakunywa, nilikuwa nakuywa wapi na aliyeniona ni nani... kuna sehemu nyingine pombe siyo dhambi, dini nyingine mpaka kanisani kuna bar".

Je, kunywa bia kiasi bila kulewa ni dhambi au siyo dhambi?

Hilo ni swali lingine alilokutana nalo kuhusu unywaji Pombe, ambapo katika majibu yake amesema hawezi kusema kama ni dhambi au lah, maana inategemea na imani ya mtu, huku akiongeza kuwa Bibilia haijazuia unywaji pombe

"Inategemea na makanisa, kuna mengine hata kunywa soda ni dhambi. Dhambi ni makubaliano yenu kwenye dini yenu. Bibilia inasema kula kitu chochote hata chakula kama ukila kupitiliza ni dhambi, hata unywaji wa pombe ukinywa ukapitiliza ni dhambi. Biliblia haijaandika moja kwa moja kwamba msinywe pombe, imesema msilewe kwa kuwa ndani ya ulevi kuna ufisadi, cha msingi mbadilishe ulevi wenu uwe ni roho mtakatifu"

Ikumbukwe kuwa sekeseke lililosababisha Mzee wa upako adaiwe kunywa pombe, lilihusisha kurushiana maneno na jirani zake ambapo baada ya hapo vyombo vya habari hasa magazeti yaliripoti tukio hilo kwa namna ambayo Mzee wa Upako hakuipenda, na hata kufikia hatua ya kuwatabiria kifo waandishi walioandika habari hiyo.

Alipoulizwa kuhusiana na ahadi yake hiyo ya kuwatabiria vifo, alisema kuwa tayari amewasamehe ingawa uwezo wa kuwaombea kifo anao.

"Tulisema hatuwezi kutumia nguvu kubwa sana kuwaombea watu kifo, kwa sababu sisi ni wanadamu, na wanadamu tuna mapungufu kwahiyo nikaona ni bora kumuachia Mungu. Uwezo huo wa kuwaombea watu wakafa, mimi ninao, lakini nikaona inasaidia nini mtu kumuombea mabaya, kwahiyo nikaamua kusamehe"

Baadhi ya watu walitaka kujua ni kwanini haendi kuombea wagonjwa hospitalini ili wapone, ambapo alijibu kuwa maombi hufanywa katika mazingira maalum, na kwamba hospitali kila mgonjwa ana imani yake.

"Maombi lazima kuandaa mazingira, na sehemu ambayo Mungu amesema tukutane ni kanisani, ndiyo maana hata wakati wa Yesu wagonjwa ndiyo walimfuata Yesu, siyo Yesu aliwafuata wagonjwa.. Kinachoponya ni imani ya mtu, pale hospitali kila mtu ana imani yake, wakati mwingine hata kumuombea mtu inabidi umuombe kwanza maana wengine hawapendi kuombewa"

Jumuiya ya Kiisilamu yataka MATEJA Wote washtakiwe na Pia Mali za Paul Makonda Zichunguzwe

$
0
0
Jumuiya  na Taasisi za Kiislamu nchini imevitaka vyombo vya kisheria na uchunguzi kuacha kupuuza kauli zilizotolewa na wabunge zilizomtuhumu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kumiliki mali zisizoendana na kipato chake halali.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kaimu Msemaji wa Jumuiya hiyo Sheikh Rajabu Katimba, alisema wakati wa mkutano wa Bunge lililopita baadhi ya wabunge walimtuhumu Makonda hivyo tuhuma hizo zinapaswa kufanyiwa kazi kwa mujibu wa sheria.

Alisema vyombo vyenye mamlaka ya uchunguzi vinapaswa  kufanya uhakiki wa mali za Makonda ili kuondoa shaka katika umiliki wa mali aliyonayo na uhalali wa misaada ya kifedha zinazotolewa kwake na taasisi rafiki.

Sheikh Katimba alisema kifungu cha (11) cha sheria ya maadili ya viongozi wa umma inamtaka kiongozi kutaja hadharani mali zake ikiwemo zawadi anazopewa.

Hivi karibuni, Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini (Chadema) wakati akichangia taarifa za Kamati ya Bunge na Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama alisema Makonda amenunua jengo ‘(Apartment ) lenye thamani ya shilingi mil 600 jijini Dar es  Salaam.

Selesini aliliambia Bunge kuwa Makonda amempa gari mkewe aina ya Mercedez Benzi lenye thamani ya Dola 250,000 za Marekani ambazo ni sawa na Sh milioni 550.

Mbali na Selesini, Mbunge mwingine aliyemtuhumu Makonda kujilimbikizia mali ni Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Msukuma (CCM) ambaye naye wakati akizungumza bungeni alihoji ni wapi  Makonda alipata fedha za kusafiri kwenye ndege  daraja la juu kwenda Marekani.

Wakati huo huo, Sheikh Katimba alisema vita dhidi ya dawa za kulevya inaweza kwenda vibaya iwapo itasimamiwa na wanasiasa.

Alisema ili kuepuka hilo vyombo vya dola vyenye mamlaka ya kisheria vinapaswa kuifanya kazi hiyo kwa weledi mkubwa.

Sheikh Katimba alisema taasisi za kiislamu zinaunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali kupambana na biashara hiyo na kusisitiza kuwa vyombo vyenye mamlaka kuisimamia kwa mujibu wa Sheria ya Kudhibiti na Kupambana Dawa za Kulevya nchini ya mwaka 2014.

‘’Hatuoni ni kwa mantiki ipi watumiaji wengine washitakiwe kwa kutumia dawa na wengine waachiwe huku zitumike na fedha za kuwatibia nje ya nchi.

‘’Wasanii kama Rehema Chalamila, maarufu kwa jina la Ray C’  msanii TID nao pia walipaswa kushitakiwa kama walivyofanywa wengine na vilevile watumiaji walioko mitaani na kwenye vituo vya daladala wote wasombwe wakapimwe na kisha washitakiwe.

“Pamoja na nia ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuongoza na kuendesha vita hiyo lakini vita isimamiwe na vyombo vyenye weledi na si wateule wa kisiasa au wanasiasa,’’ alisema.

Aidha, alizungumza kesi za ugaidi inawakabili baadhi ya viongozi wa dini kwa kueleza kuwa haitakuwa na tija wala heshima iwapo viongozi  hao wataendelea kushikiliwa gerezani.

“Ni kweli serikali inatutaka tuiunge mkono kwenye vita hiyo nasi tuko tayari lakini ni vuziri jitihada hii ikawa kwa watu wote, tunaiona serikali inashindwa kutenda haki kwa viongozi wa dini yetu na ni kesi gani isiyokwisha? inatia aibu masheikh kufungwa bila hatia miaka mitatu ni sawa na kufungwa bila hatia,’’ alisema Sheikh Katimba.

ACT Wazalendo Bado Yalia na Hali ya Chakula Nchini

$
0
0
Chama  cha ACT Wazalendo kimemtaka Rais John Magufuli kutumia mamlaka yake kikatiba kutangaza janga la ukame na hali mbaya ya chakula nchini.

Aidha kimeitaka Serikali kuchukua hatua madhubuti dhidi ya baa la njaa.

Hatua ya chama hicho inafuatia kile ilichoeleza kutoridhishwa na hatua ya Serikali katika kuzuia baa la njaa, huku ikikikusanya takwimu ya bei za vyakula nchini.

Katibu wa Kamati ya Maendeleo ya Jamii wa chama hicho, Janeth Rithe alieleza hayo jana Dar es Salaam.

Alisema hali ya chakula nchini bado haijatengamaa na kwamba ACT hakiridhishwi na hatua ambazo Serikali imechukua katika kuzuia tishio hilo la baa la njaa.

“Tumeshtushwa na taarifa mpya za Serikali juu ya hali ya chakula nchini, hasa juu ya uhaba wa vyakula, tishio la baa la njaa na mfumuko mkubwa wa bei za vyakula, na hali ya ukuaji wa kiuchumi wa wananchi kwa ujumla,”alisema.

Alisema Sekretarieti ya ACT ilikusanya takwimu kwa wiki mbili kuhusu bei ya vyakula mbalimbali nchini na kubaini bei ya unga, maharage na vyakula vingine imepanda kwa takriban Sh1,100 kutoka Sh 900 kwa kilo kwa miezi mitatu iliyopita hadi Sh 2000 mwezi huu.

Rithe alisema uamuzi wa Serikali ya Chama cha Mapinduzi(CCM) kwa kupunguza bajeti ya ruzuku ya mbolea kutoka Sh. bilioni 78 mwaka 2015/16 hadi Sh. bilioni 10 mwaka 2016/17 haukuwa sahihi na kwamba sasa inapaswa kuchochea tija kwenye kilimo.

“Uamuzi huo umechangia kuwapunguzia wananchi uwezo wa kuzalisha.Takwimu zinaonesha kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazotumia mbolea kwa kiwango kidogo zaidi ulimwenguni.

“Ni kwa sababu hii takwimu za Serikali zilizotolewa na Waziri wa Fedha zinaonesha kuwa kwa mwaka 2016 kasi ya ukuaji wa kilimo imeshuka kutoka asilimia 2.5 hadi 0.6,”alisema.

Alisema Serikali inapaswa kutenga fedha kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji ili kupunguza utegemezi wa kilimo cha mvua zisizotabilika.

Kwa mujibu wa ACT, Serikali inatakiwa kujenga maghala ya kutosha pamoja na Bunge kuongeza bajeti ya hifadhi ya Chakula ya Taifa.

Kuhusu Benki Kuu, ACT ilisema taarifa za benki hiyo kuhusu hali ya uchumi wa nchi kwa Desemba 2016 zinaonesha kuna mfumuko mkubwa wa bei za vyakula, hasa chakula kikuu kwa Watanzania.

Alitaja baadhi ya vyakula kama mahindi, ambapo mfumuko wa bei yake umekua kwa zaidi ya asilimia 30 na kusababisha kupanda kwa gharama za maisha za wananchi wote.

Mama Atiwa mbaroni kwa kumpaka mtoto pilipili machoni

$
0
0
Mwanamke mmoja aliyejulikana kwa jina la ‘Mama Saidi’ anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumuwekea pilipili kwenye macho mtoto wake wa kambo anayesoma darasa la sita kwa madai ya kutofua nguo za shule.

Tukio hilo limetokea Mtaa wa Tabata Magharibi na kuripotiwa kwenye ofisi ya Serikali ya Mtaa huo juzi, kabla ya mwanamke huyo kukamatwa na kupelekwa Kituo cha Polisi Tabata ambapo anashikiliwa hadi sasa.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala, Salum Amaduni alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema upelelezi bado unaendelea.

“Mtuhumiwa atafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika, ikiwa ni pamoja na kupokea taarifa ya daktari ambayo itaonyesha ni kwa kiasi gani mtoto huyo ameumia au madhara aliyoyapata kutokana na kitendo kile,” alisema Amaduni na kuongeza:

“Bado tunakusanya ushahidi, ukikamilika tutapeleka jalada kwa mwanasheria wa Serikali kwa hatua za mashtaka.”

Awali majirani walidai imekuwa kawaida kwa mwanamke huyo kumnyanyasa mtoto huyo wa kambo, lakini Kamanda Amaduni alisema tukio hilo ni la kwanza kuripotiwa kutoka kwa mwanamke huyo na si kama wanavyoeleza majirani zake.

Mtendaji wa mtaa huo, Hamza Ramadhani alisema mtoto huyo alipofikishwa ofisini kwake alikuwa haoni kutokana na athari za pilipili, ndipo alipopelekwa Kituo cha Afya Tabata.

“Lakini walipomuangalia waliamua kumpeleka Hospitali ya Amana na taarifa nilizanazo kwa sasa jana(juzi) amesharuhusiwa yupo nyumbani na mwenzake ila mama ndio bado yupo polisi,” alisema.

Jirani wa mtoto huyo, Gowely Anthoy alisema kwa kipindi kirefu kulikuwa na viashiria vya mtoto huyo kunyanyaswa lakini hakuna aliyeweza kuhoji.

“Mtoto mwenyewe amekuwa akisema tangu siku nyingi mama hamhudumii ipasavyo, lakini tulikuwa tukichukulia kama masuala ya kawaida ya watoto, lakini sasa tumejua ni kweli,” alisema.

Wanasheria wa CHADEMA Wamtaka Mbowe Asijisalimishe Polisi

$
0
0
Wanasheria wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wamesema wamemshauri Mwenyekiti wao wa Taifa, Freeman Mbowe, asiende kuripoti polisi leo.

Mwanasheria wa Chadema, John Mallya, amesema Mbowe hatakwenda kuripoti polisi leo kwa sababu amefungua kesi ya kikatiba Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam na inaanza kusikilizwa Februari 21 mwaka huu.

“Mbowe haendi polisi, tumemshauri asiende kwa sababu kesi yake inaanza kusikilizwa Jumanne (kesho).

“Kama wanamhitaji, waje keshokutwa (kesho) Mahakama Kuu, watampata hapo,”alisema Mallya.

Kwa upande wake, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, alisema yuko Mwanza na hajawasiliana na Mbowe.

“Hapa niko Mwanza sijawasiliana na mwenyekiti, lakini kama nikiwasiliana naye, nitamshauri asiende huko polisi.

“Kwa hiyo, naweza kusema kilichofanywa na Kamishna Sirro si wito wa kipolisi bali ni siasa kama ambavyo alifanya Makonda kwa kutangaza majina ya watu hadharani.

“Wito wa polisi huwa ni wa kimaandishi, hawajamwandikia barua, hawajampigia simu.

“Hawa maafande wana namba zetu za simu sisi kama mawakili wa chama, kama wanamhitaji Mbowe kwanini wasitupigie simu mpaka watangaze kwenye vyombo vya habari,”alihoji Lissu.

Alipoulizwa kama Mbowe atakamatwa wakati wowote kuanzia sasa, Lissu alisema watalazimika kulishtaki mahakamani Jeshi la Polisi kwa kitendo hicho.

“Hatuwezi kukubali utaratibu huu, waache kufanya siasa, wakimhitaji mwenyekiti wetu wamwandikie barua,”alisema Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki.

Mwanzoni mwa mwezi huu, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, alitaja majina 65 ya watu wanaodaiwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya akiwamo Mbowe.

Pamoja na kutaja majina hayo, Makonda aliwaagiza watuhumiwa hao kuripoti Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam kwa ajili ya kuhojiwa dhidi ya tuhuma hizo.

Februari 10 mwaka huu, akiwa mjini Dodoma, Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai, alizungumza na waandishi wa habari na kusema hajawahi kujihusisha kwa namna yoyote na biashara ya dawa za kulevya na pia hatakwenda polisi kuhojiwa kama alivyoagizwa na Makonda.

Hata hivyo, alisema atakwenda polisi, kama jeshi hilo litafuata taratibu za kumuita kwa mujibu wa sheria.

“Siwezi kwenda polisi kwa wito wa Makonda kwa sababu hana mamlaka hiyo kisheria. Kama polisi wananihitaji, waniite kwa kufuata utaratibu, nitakwenda kwa sababu mimi siogopi kwenda polisi,”alisema Mbowe.

Wakati Mbowe akisema hayo, juzi Kamanda wa Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro, alisema Jeshi la Polisi linamtafuta Mbowe na kwamba limeshindwa kumpata kwa sababu amezima simu.

Kutokana na hali hiyo, Kamanda Sirro alitoa saa 48 kwa Mbowe kuripoti polisi na endapo hatafanya hivyo atatafutwa kwa namna ambayo jeshi hilo litaona inafaa.

 “Jumatatu (leo) asiporipoti kutakuwa hakuna namna ya kulizuia tena Jeshi la Polisi kutafuta namna ya kumhoji.

 “Mbaya zaidi juzi tumejitahidi kumtafuta hapatikani, tulikwenda nyumbani kwake hakupatikana, tulikwenda mahali anakoishi sasa, pia hakupatikana,”alisema Sirro

NECTA yawataka wananchi kupuuza taarifa ya Gazeti la Nipashe kuhusu mchujo kidato cha kwanza

Jokate akutana na Mastaa Jay Z na Beyonce nchini Marekani

$
0
0
Asubuhi ya leo, mrembo Jokate Mwegelo kutoka nchini Tanzania amepokea pongezi kutoka kwa watu mbalimbali baada ya kuchapisha picha kwenye kurasa zake za Insagram na Twitter akiwa pamoja na wanamuziki maarufu duniani.
Jokate ameweka picha yake aliyopigwa akiwa pamoja na Jay Z na Beyonce pamoja na mtoto wao, Blue Ivy Carter wakati wa mchezo wa mpira wa kikapu nchini Marekani.
 
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Jokate ameandika ujumbe alioambatanisha na picha hiyo akionyesha furaha yake baada ya kukutana na ‘mastaa’ hao wakubwa duniani.
 
“So NBA Africa took me courtside and I haaaaaaad to say hello to the Carters. OMG 😭😭😭😭. @beyonce is super cute and I can’t believe she shook my hand and was like nice to meet you. 😍😍🤗🤗. I was like wait I need a picture, I came all the way from Tanzania for this B 😕. She’s so sweeeeeet and I’m so lucky lmao. Thank you @beylite@balleralert for this pic I couldn’t snap one as I was shocked and still in disbelief. 😳#Beyonce#Beylite#NBAAfricaGame#NBAAllStar#Kidoti🇹🇿🇹🇿🇹🇿🇹🇿” aliandika Jokate.

Muigizaji Shamsa Ford amlilia mumewe aliyekamatwa kwa kesi ya dawa za kulevya

$
0
0
Mwigizaji Shamsa Ford ambaye ni mke wa Mfanyabiashara Chidi Mapenzi aliyeitwa Polisi kwa tuhuma za kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya, ameandika yafuatayo ikiwa ni mara ya kwanza toka aitwe Polisi kuhojiwa.

Shamsa amepost ujumbe huu kupitia Instagram “nilipoolewa nilijua ipo siku nitapitia hivi vitu huzuni,furaha, maudhi, kudharauliwa, kuchekwa na nk.ila pamoja na yote hayo haitabadilisha mapenzi yangu kwa mume wangu kipenzi”

“Nina amini kuwa wewe ni mume aliyenipa Mungu na wala Mungu hakutukutanisha kwa bahati mbaya.Dunia nzima ikuzomee na kuamini kile wanachoamini lakini jua una mke anayekupenda kwa dhati“

“Ninakujua, ninakuamini na kukupenda sana ndomaana niliolewa na wewe kwasababu nilijua utakuwa baba bora kwa mwanangu kama ambavyo ulivyo sasa..Nina amini Mungu anapotaka kukupeleka sehemu anayoitaka yeye lazima akupitishe kwenye mitihani”

“Hii ni mitihani ya Mwenyezi Mungu na nina imani inshaallah yatapita..Nakupenda sana mume Wangu kipenzi Rashidi..“

Serikali yatangaza utaratibu utakaotumika kuzuia pombe za ‘viroba’

$
0
0
Kufuatia kauli ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa aliyotoa tarehe 16/02/2017 huko Mererani, Mkoani  Manyara kuhusu kusitisha utengenezaji, uuzaji na matumizi ya pombe zinazofungashwa kwenye vifungashio vya plastiki kuanzia tarehe 1 Machi 2017; na kufuatia  Tamko la Serikali kuhusu dhamira hiyo lililotolewa Bungeni tarehe 2 Mei, 2016 na kwenye matangazo yaliyotolewa kwenye vyombo vya habari tarehe 01 Desemba, 2016, Ofisi ya Makamu wa Rais  inachukua fursa hii kutangaza utaratibu wa utekelezaji wa maamuzi hayo ya Serikali.
  • Waziri mwenye dhamana ya Mazingira atatunga Kanuni zitakazodhibiti uzalishaji wa vifungashio (viroba) vya pombe kali, kwa mujibu wa Kifungu 230 (2) (F) cha Sheria ya Mazingira ya  Kanuni hizi  zitaweka sharti la kutaka pombe kali inayozalishwa viwandani zifungashwe kwenye chupa zinazoweza kurejelezwa (recycled) na kwa ujazo usiopungua milligram 250.
Pia Kanuni hizo zitapiga marufuku uzalishaji, uuzaji, uingizaji nchini na matumizi  pombe  zilizofungwa kwenye viroba na mitambo ya malighafi ya vifungashio vya plastiki (viroba) vitakavyotumika kufungashia pombe kali.   Atakayebainika kukiuka masharti ya Kanuni hizi atawajibishwa kulipa faini, kufungwa jela au vyote kwa pamoja kama itakavyoainishwa kwenye Kanuni.
  • Dhamira ya Serikali sio kupiga marufuku vinywaji vya pombe kali bali ni kutekeleza Ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977 ambayo inatoa haki ya kuishi katika mazingira yaliyo safi, salama na yenye afya. Haki hiyo pia imetiliwa mkazo katika sheria ya Mazingira ya 2004.  Hivyo, dhamira  ya Serikali ni kudhibiti upatikanaji kwa urahisi wa pombe kali kunakotokana na kufungwa katika plastiki na kwa ujazo mdogo, kunakopelekea kuongezeka kwa matumizi ya pombe kali hadi kwa watoto wadogo; kudhibiti uchafuzi wa mazingira unaotokana na kuzagaa kwa vifungashio hivyo; na kudhibiti ukwepaji mkubwa wa kodi kutokana na urahisi wa teknolojia na gharama za kutengeneza  pombe kali  inayofungashwa kwenye viroba. Inakadiriwa kwamba Serikali inapoteza shilingi bilioni 600 kwa mwaka kutokana na ukwepaji kodi kwenye biashara ya pombe za viroba.
  • Utekelezaji wa maamuzi haya ya Serikali unaanza mara moja. Ingawa haitegemewi, lakini iwapo kuna Wazalishaji watakaohitaji muda wa ziada wa kuhamia kwenye teknolojia ya chupa, wataomba kibali maalum cha muda mfupi ambacho hakitatolewa hadi muombaji awasilishe kabla ya tarehe 28/02/2017:- yafuatayo:-
  1. Ushahidi/Barua kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwamba amelipa kodi katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.
  2. Ushahidi/Barua/Cheti kutoka Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) kwamba mzalishaji amekuwa na  kibali cha usalama wa kinywaji kwa miaka yote ambayo amekuwa anazalisha;
  • Cheti au Barua kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwamba mzalishaji  anauza bidhaa inayokidhi viwango
  1. Cheti cha Tathmini ya Athari kwa Mazingira (EIA) au Ukaguzi wa Mazingira (EA) kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC)/Ofisi ya Makamu wa Rais;
  2. Ushahidi kwamba katika kipindi cha mpito mzalishaji atatumia teknolojia ya kudhibiti utengenezaji wa vifungashio bandia (anti-counterfeit technology);
  3. Uthibitisho kutoka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kuhusu usajili wa kampuni na usajili wa chapa ya kinywaji (brand).
Zipo pombe za viroba zinazoingizwa nchini kutoka nje ya nchi, hasa kwenye Mikoa na Miji ya mipakani.  Wakuu wa Wilaya , kupitia Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya na Kamati za Mazingira, wanaelekezwa kufanya operesheni ya kukamata na kuzuia viroba vinavyoingizwa nchini kinyume cha utaratibu. Operesheni hii pia inahusu udhibiti wa pombe haramu ya gongo.
 
Serikali imeunda Kikosi Kazi cha Kitaifa kwa ajili ya kufanya ukaguzi na ufuatiliaji na hatua hizi.  Kikosi hicho kinajumuisha Ofisi ya Makamu wa Rais, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Wizara ya Fedha na Mipango,  Wizara ya Viwanda Biashara na Uwekezaji, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira, Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Kodi ya Mapato Tanzania (TRA), Idara ya Uhamiaji na Jeshi la Polisi.  Doria za ukaguzi  wa utekelezaji wa hatua hizi zitaanza wakati wowote kuanzia sasa na hatua kali zitachukuliwa kwa watakaokiuka.  Ofisi ya Makamu wa Rais itaratibu Kikosi hiki.
 
Kuhusu mifuko ya plastiki, Kanuni za Udhibiti zinaandaliwa na zuio litatangazwa wakati wowote.  Tunapenda kuwaasa wazalishaji, waagizaji na wauzaji  wa mifuko hiyo nao kujiandaa.
 
Hatua hizi za Serikali sio za ghafla au kushtukiza kwani taarifa ilitolewa Bungeni takribani mwaka mmoja sasa. Aidha Serikali ilitoa taarifa rasmi mwezi Agosti 2016 na Desemba 2016 kuhusu dhamira ya kuchukua hatua hizi.  Serikali ilitarajia kwamba wazalishaji wa pombe za viroba na mifuko ya plastiki watakuwa wamejiandaa kubadilisha teknolojia.
Ofisi ya Makamu wa Rais
20/02/2017

Sakata la Dawa za Kulevya: Freeman Mbowe akamatwa na Jeshi la Polisi

$
0
0
Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe  amekamatwa  na Jeshi la Polisi ili kuhojiwa kuhusiana na tuhuma za madawa ya kulevya.

Taarifa za kukamatwa kwa Mbowe zimethibitishwa na Kamishna wa kanda maalumu Dar es salaam Simon Sirro
 

Msemaji wa CHADEMA Boniface Makene,amesema Mbowe amekamatwa wakati akiwa njiani kuelekea kituo cha polisi kwa mahojiano.

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Jumanne ya February 21

Mbowe Apekuliwa Usiku......Arudishwa Polisi

$
0
0
Jana  mchana Mwenyekiti wa chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Freeman Mbowe alihojiwa na Polisi kuhusu sakata la dawa za kulevya baada ya jina lake kutajwa kwenye orodha ya Makonda  February 8.

Baada ya kukaa kituoni hapo kwa zaidi ya masaa mawili Waandishi wa habari waliokua nje ya eneo hilo walishuhudia Mwenyekiti huyo akichukuliwa na Gari aina ya Land Cruiser iliyofatwa na magari mengine nyuma yake na kuelekea ambako Waandishi hawakufahamu mara moja.

Baadaye msemaji  wa CHADEMA Tumaini Makene alisema  Polisi walienda na Mbowe kupekua nyumba zake na kuandikisha maelezo ya majirani ambapo alisema kwenye mida ya saa sita usiku wa kuamkia leo Polisi walimrudisha Mbowe kwenye kituo cha Polisi kati na wakamfungulia jalada la Uchunguzi….

Mbowe Kaachiwa Huru baada ya Kuhojiwa na Kupekuliwa Usiku

$
0
0
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe ameachiwa saa saba na robo usiku wa kuamkia leo baada ya kuhojiwa na kupekuliwa na Jeshi la Polisi.
 
Mbowe alikamatwa jana Jumatatu jioni wakati akienda kujisalimisha polisi na kupekuliwa nyumbani kwake kabla ya kuhojiwa hadi alipoachiwa usiku wa manane.
 
Ofisa habari wa chama hicho, Tumaini Makene amethibitisha  taarifa za kuachiwa mwanasiasa huyo kuwa ni za kweli.
 
Hata hivyo, taarifa iliyosambazwa na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Salum Mwalimu kupitia mitandao ya kijamii imesema kuwa chama hicho kitatoa taarifa zaidi juu ya tukio hilo leo.
 
“Tunawashukuru wote kwa sala, maombi na subira na hivyo kuhitimisha salama saa kumi za mwenyekiti wetu kuwa chini ya Jeshi la Polisi katika Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam,” Mwalimu amesema.

Makonda, Kamanda Sirro Waitwa Mahakamani Leo Kutokana na Kesi Aliyifungua Mbowe

$
0
0
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam (RC), Paul Makonda, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam (ZPC), Kamishna Simon Sirro na Mkuu wa Upelelezi wa kanda hiyo (ZCO), Camilius Wambura, wamepelekewa barua za mwito za kuwataka wafike Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam leo.

Viongozi hao wamepelekewa mwito huo kutokana na kesi ya Kikatiba iliyofunguliwa na Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe dhidi yao.

Mbowe amefungua kesi hiyo kupinga Makonda kumtaja katika orodha yake ya watuhumiwa 65 wanaojihusisha na dawa za kulevya katika awamu ya pili na kumtaka afike katika Kituo Kikuu cha Polisi, Februari 10 mwaka huu, kwa ajili ya mahojiano.

Katika kesi hiyo Namba Moja ya Mwaka 2017, Mbowe pamoja na mambo mengine, anapinga mamlaka ya RC kumkamata kwa kile anachokiita kudhalilisha watu.

Kesi hiyo imepangwa kutajwa leo na itasikilizwa na jopo la majaji watatu, Sekieti Kihiyo ambaye ni kiongozi wa jopo hilo, akisaidiana na Jaji Lugano Mwandambo na Jaji Pellagia Kaday.

Mbowe anaiomba mahakama hiyo itamke kuwa vifungu vya Sheria ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa vinavyowapa mamlaka wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya kuwakamata watu na kuwatia mbaroni viko kinyume cha Katiba.

Aidha, Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai mkoani Kilimanjaro na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, jana alifungua maombi mahakamani hapo akipinga kusudio la Kamanda Sirro la kumkamata kama hatajisalimisha katika kituo cha polisi kwa mahojiano.

Mahakama hiyo imetoa hati za mwito wa kufika mahakamani hapo kwa wadaiwa hao ambao ni Makonda, Sirro na Wambura. Hata hivyo, inadaiwa Kamanda Sirro alikataa kupokea mwito huo akielekeza kuwa hati hiyo ya mwito ipelekwe kwa Wambura.

Wadaiwa kukataa kusaini 
Kwa mujibu wa Ofisa wa mahakama, Yusuph Juma ambaye alipeleka mwito huo, alidai kuwa baada ya kuelekezwa na Kamanda Sirro kuwa ampelekee mwito huo Wambura, alipokwenda kwa Wambura, hakumkuta.

Juma alidai hati ya mwito wa mkuu wa mkoa alipoupeleka hakumkuta na kwamba wasaidizi wake nao walikataa kuusaini mwito huo.

Mwishoni mwa wiki, Kamanda Sirro akizungumza na waandishi wa habari alimtaka Mbowe ajisalimishe mwenyewe kituo cha Polisi na kwamba kama hatafanya hivyo basi watamsaka popote alipo na kumtia mbaroni.

Katika maombi hayo, Mbowe anaiomba mahakama iwazuie wadaiwa kutekeleza azma yake ya kumtia mbaroni pamoja na mambo mengine akidai kuwa kuna kesi ya kikatiba ambayo tayari ameifungua mahakamani hapo.

Katika maombi hayo, Mbowe anaiomba mahakama hiyo pia itoe amri ya kuwazuia kumkamata hadi hapo kesi hiyo ya kikatiba itakapomalizika na kwamba Mahakama Kuu imwachie na polisi wasiendelee na mchakato wowote dhidi yake hadi hapo kesi hiyo itakapomalizika.

Katika kesi ya Msingi ya Kikatiba, Mbowe anapinga kitendo cha Polisi kumtaka afike kituoni kwa madai kuwa ni utekelezaji wa amri ya Mkuu wa Mkoa.

Anadai kuwa sheria inayompa Mkuu wa Mkoa mamlaka ya kutoa amri ya kumkamata na kumweka ndani mtu iko kinyume cha Katiba kwa madai kuwa ilitungwa katika mazingira ambayo hapakuwa na vituo vya polisi vya kutosha.

Anadai kuwa kwa mazingira ya sasa sheria hiyo imeshapitwa na wakati na anaiomba mahakama itamke kuwa ni kinyume cha Katiba.

Mbowe pia anadai kuwa hata kama Mkuu wa Mkoa alikuwa anatekeleza mamlaka yake kwa mujibu wa sheria hiyo, basi hakutimiza matakwa ya kisheria, ambayo ni pamoja na kutoa taarifa kwa Hakimu wa Mahakama ya Wilaya au ya Hakimu Mkazi.

Vile vile, anaiomba mahakama kama itaona kuwa Mkuu wa Mkoa alikuwa sawa kutoa amri hiyo basi imwamuru afuate matakwa ya kisheria, ikiwa ni pamoja na kulinda haki za binadamu katika kutekeleza madaraka yake hayo.

CCM Yamweka Kiporo Yusuf Manji

$
0
0
Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Temeke, kimesema hakitamjadili Diwani wa Kata ya Mbagala Kuu, Yusuph Manji, hadi kesi yake kuhusu madai ya kutumia dawa za kulevya itakapomalizika mahakamani.

Msimamo huo umetolewa baada ya kuwapo  taarifa kwamba chama hicho kimepanga kumjadili Manji kuhusiana na tuhuma zinazomkabili.

Taarifa hizo zilieleza kuwa diwani huyo atajadiliwa vikaoni ili afukuzwe uanachama kwa kuwa chama hicho hakitaki wanachama wenye tuhuma na wanaovunja amri za nchi.

“Kikao cha kamati ya utendaji ya chama kitaitishwa mapema mwezi huu kutekeleza maazimio ya vikao vilivyokwisha kufanyika kuanzia tawi hadi kata ambavyo vilikuwa na agenda ya kumjadili Manji kuhusu tuhuma zake,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Jana, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Temeke, Yahaya Sikunjema, alisema hawawezi kuingilia suala ambalo bado liko kwenye vyombo vya sheria.

“Wakati utakapofika na ikaonekana ipo sababu baada ya vyombo husika vya sheria kama mahakama kumtia hatiani.

“Kama chama tutakaa tuangalie katiba yetu inatuelekeza vipi na hapo ndipo tutachukua hatua,” alisema Sikunjema.

Wiki iliyopita Manji ambaye pia ni Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga, alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akidaiwa kutumia dawa za kulevya.

Manji alikana shtaka hilo na kuachiwa kwa dhamana.

Tundu Lissu: Serikali Ina Hofu Na Mimi TLS

$
0
0
Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA), Tundu Lissu, amesema ameanza kuogopwa na viongozi wa serikali  baada ya jina lake kuwa miongoni mwa majina matano bora ya wagombea wa nafasi ya urais katika Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kutokana na misimamo yake ya kuitetea Katiba ya Tanzania.

Akizumgumza na waandishi wa habari  Mwanza jana, Lissu alisema  tangu atangaze nia yake ya kugombea urais wa TLS ameanza kuogopwa  kutokana  na kujulikana kwa   misimamo yake kuhusu  masuala ya   sheria,  siasa na  katiba ya nchi hii.

Alisema TLS ina majukumu makubwa katika nchi ya kulinda utawala wa sheria na wanasheria ndiyo wanaojua kuliko mtu yeyote  zinapotungwa sheria mbovu na zile za kikandamizaji, pia wao ndiyo wanapaswa kuwa wa kwanza kuanza kuzipigia kelele sheria hizo.

“Kwa miaka mingi  TLS imeongozwa  na watu ambao hawafikiri kwamba wajibu wao wa kwanza kulinda utawala wa sheria,  wao wanafikiri wajibu wao wa kwanza ni kuwapendeza  wanasiasa na matokeo yake TLS imepotea, wanachoogopa  ni kwamba hii raha ambayo wameipata miaka yote hii wakati  wanasheria wa  TLS wakiwa  usingizini akija huyu Lissu itaisha,” alisema Lissu.

Alisema aligombea nafasi hiyo  baada ya kumsikia Rais Dk. John Magufuli akizungumza mbele  ya watanzania kwamba wakili  yeyote  atakayewatetea  watuhumiwa wanaokutwa na  dawa ya kulevya au nyara za serikali wakamatwe na kuwekwa ndani.

Alisema aliposikia kauli hiyo alicheka na kusema sasa ni wakati wa yeye kuwa rais wa TLS ili kauli za aina hiyo zikome na siku mbili kabla ya Rais Dk. John Magufuli kutoa kauli hiyo,  Bunge lilipitisha sheria ya msaada wa sheria.

“Sheria hiyo inasema mtu yeyote anayefunguliwa kesi ya jinai, au madai kama ni maskini hana uwezo wa kumlipa wakili atapatiwa huduma hiyo na wakili atalipwa  na  mtendaji mkuu wa mahakama.

“Sheria hiyo inampatia haki  mwananchi yeyote atakayekuwa  na kesi ya mauaji, pembe za ndovu au dawa za kulevya  kupata wakili atakayelipwa na serikali.

“Siku mbili baadaye Rais anakinzana na sheria hiyo nilishangaa kweli.  Tayari sheria hiyo imetungwa  ni jambo muhimu kweli kwa sababu katika  nchi hii watu wanasingiziwa sana, kwenye maegereza nyingi   nchini wamejazana wananchi ambao hawana hatia na wapo huko kwa sababu hawakuwa na mawakili wa kuwatetea,” alisema Lissu.

Lissu alisema  endapo atachaguliwa kuwa rais wa TLS atahakikisha sheria ya msaada wa  sheria  inatekelezwa.

Kuhusu hoja ya  Waziri wa katiba na  Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe ya kutishia kukifuta chama hicho hicho kwa kuwa kimeanza kujiingiza katika masuala ya siasa, Lissu alisema wanaoleta hoja za kutaka kukifuta chama hicho kama ni wanasheria ujuzi wao wa sheria ni wa shaka lakini kama ni wasiojua sheria wanasamehewa.

Alisema  sheria ya iliyoanzisha TLS inasema mwanachama yeyote aliyekidhi vigezo  vya chama hicho ana haki ya kuwa mgombea wa nafasi yoyote ya uongozi na haijasema  ukiwa mwanachama wa chama chochote cha siasa unapungukiwa sifa  ya kugombea.

“Watu wanazungumza   kana kwamba ni makosa mwanasheria kuwa mwanasiasa, katika nchi hii katiba imeruhusu  siasa za vyama vingi, kuwa wanachamaau  kiongozi wa chama.

“Kuwa tu mwanachama una kuwa na fursa ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi serikalini lakini sasa watu wanataka kuaminishwa kuwa ukiwa mwanasiasa huna haki,” alisema

Nay wa Mitego adai Atangaza kuanzisha kanisa lake

$
0
0
Nay wa Mitego anasema anafungua kanisa lake la kumuabudu Mungu. 
 
Amedai kuwa kanisa lake litakuwa si la biashara, bali la kumuadu mwenyezi Mungu aliye hai.
 
“Acha kanisa likamilike, mwenye Mungu asimamie tutajua nini kinaenda kutokea lakini sio kanisa kwaajili ya kupiga hela,” Nay aliiambia E-News.
 
Nay amedai kuwa mchungaji wa kanisa lake atakuwa tofauti na hatotegemea sadaka za waumini ili kuendesha maisha yake, bali kazi yake nyingine itakayoweza kumuingizia kipato.
Rapper huyo amejinadi kuwa anatarajia kupata waumini wengi kupitia kanisa lake na kwamba litakuwa chanzo cha mafanikio katika mambo yao.
 
Nay amedai kuwa kanisa lake litajengwa Mbezi ya Kimara jijini Dar es Salaam.

SORRY MADAM -Sehemu ya 33 & 34 (Destination of my enemies)

$
0
0
MWANDISHI: EDDAZARIA G.MSULWAILIPOISHIA

ILIPOISHIA
Kitendo hicho kikiwa kinaendelea Shamsa aliweza kushuhudia damu ikimtoka mtu ambaye anaamini amekuja kuwasaidia na kuwaokoa.Bila ya uwoga na wala pasipo kuhofia maisha yake, Shamsa akasimama wima na kuanza kupiga hatua za kwenda walipo simama watu hao walio muweka kati mtu aliye valia mavazi meusi tupu.

Eddy akabaki akiwa katika mshangao mkubwa, baada ya kumuona Shamsa akikaribia katika eneo hilo ambalo ni hatari kwa maisha yake. Eddy akajaribu kutingisha kichwa chake kumzuia Shamsa asiweze kusogelea eneo hilo, ila ndio kwanza Shamsa akaongeza mwendo wa kuwasogelea akiwa amejiandaa tayari kwa kupigania watu wote waliomo ndani ya jengo hilo.

ENDELEA
“Am sorry dady”(Samahani baba)
Shamsa alizungumza huku akiruka hewani na kushusha teke zito kwa Lukuman akitambua kwamba ni baba yake. Eddy akataka kuzungumza kitu ila akastukia akipigwa mtama na Briton, ulio mpeleka chini, hakutaka kupoteza hata sekunde moja kwa kofia lake kuweza kuanguka alicho kifanya ni kuliweka sawa na kunyanyuka huku akichechemea.
“Baba kwa nini umeamua kufanya hivi?”

Shamsa alizungumza huku machozi yakimwagika usoni, Lukuman akabaki akiwa ameshangaa kwa kuitwa baba, ili kupotezea akarusha ngumi nzito kifuani mwa Shamsa, na kumfanya binti huyo kuto ukelele wa maumivu huku akianguka chini na kujikunja. Briton na Eddy wakajikuta wote wakimtazama Shamsa anaye garagara chini kwa maumivu makali. Kumbukumbu na sura ya Shamsa vikaanza kumjia Briton, akaanza kufikiria ni wapi alipo isikia sauti hiyo ya maumivu ya msichana huyo mwenye asili ya kiasia.

Kumbukumbu zake zikatua kipindi ambacho, walikuwa ni miongoni mwa mateka walio weza kuingizwa katika kambi ya kundi la Al-Shababu, akiwa ni kijana mdogo mwenye umri wa miaka kumi na tano. Miongoni mwa mateka ambao waliokuwa kipindi hicho, Shamsa ni mmoja wapo kipindi hicho Shamsa alikuwa bado binti mdogo.

Anakumbuka siku moja wakiwa katika mazoezi ya lazima, Shamsa alipewa kijana mwengine ambaye walimkuta ndani ya kambi hiyo, apambane naye, kutokana Shamsa hakuwa mzoefu na alikuwa ni binti mdogo na mpole sana, kijana huyo pasipo huruma aliweza kumbutua vya kutosha Shamsa, na kitu ambacho anakikumbuka zaidi, ni pale kijana huyo alipo mpiga Shamsa ngumi ya kifuani na binti huyo akaanguka hivyo hivyo kama alivyo anguka sasa hivi.

Britona akakumbuka alipo jitoa katikati ya vijana wezake walio zunguka duara hilo wakiwatazama Shamsa na kijana mwengine jinsi walivyo kuwa wakipigna. Akamvaa kijana huyo na kumshindilia ngumi za hasira hadi kijana huyo akapoteza maisha yake.

‘Naitwa Shamsa’
Sauti hiyo ilipita masikioni mwa Briton na kukumbuka siku alipo muuliza jina bintyi huyo na kutokea kumpenda, kupita maelezo. Briton akastushwa na buti zito la Lukuman lililo tua tumboni mwa Shamsa, dadi akanyanyuka kidogo juu na kutua chini puu.

“Ahagraaaaaaaaaa”
Briton akamuacha Eddy na kwenda kumvaa Lukuman, na kumuangusha chini kama mzoga, hadi Eddy akabaki akishangaa. Briton akaanza kumshindilia mangumi ya uso Lukuman, kila alivyo zidi kumshindilia mangumi mazito hayo ndivyo alivyo kuwa akikumbuka tukio la Lukuman kumpiga msichana ambaye alizama ndani ya moyo wake na kuahidi atamtunza ndani ya moyo wake hadi siku ambayo atakuja kumuona. Eddy kwa haraka akapiga goti moja chini na kumnyanyua Shamsa aliye poteza fahamu.

“WOTE TOKENI NJEEEEEE”
Ikawa kama fungulia mbwa, kila mmoja aliye jiweza alijitahdi kutoka nje akikimbia, hapakuwa na mtu aliye hitaji kujihusisha na ugovi wa watekaji hao wawili, kila mtu alijitahidi kuizingatia roho yake kwanza mambo mengine yatafwata baadaye. Eddy akamuweka Shamsa kwenye moja ya meza, baada ya kugundua yupo hai, kisha yeye akandoka akihofia askari walio anza kuingia ndani ya jengo hilo kuweza kumkuta na kumtambua.

Ndani ya dakika moja Brina na watui wake wote wawili, walijikuta wakiwa wamelala chini, kila mmoja akishika eneo la mwili wake lililo tole pande la nyama, kwa kucha kali ambazo Samson alizitumia katika kuwadhuru waasi hao.

 Mmoja wao koromeo lake liliweza kutolewa nje, na yupo katika hatua za mwisho mwisho za kuiaga dunia huku mikono yake miwili ikiwa imeshika sehemu koromeo lake lilipo chomolewa, ili damu isitoke.

Mwengine alitobolewa tumboni na utombo wake wote ukavutwa nje pasipo huruma. Brian miguu yake yote miwili, ilivunjwa vunjwa vipingili pingili zaidi ya kumi kwa kila mguu, na kuacha akiendelea kulia kwa maumivu makali.

Samson alipo hakikisha kazi yake imekamilika akatoka ndani ya chumba hicho na kuwaachia woga mwingi mafundi mitambo, kila mmoja akiwa haamini kama amepota, na hapakuwa na aliye weza kutoka katika sehemu aliyo jificha hadi walipo sikia sauti za polisi,walio jitambulisha mara baada ya kuingia ndani ya chumba hicho.

“Upo salama?”
Samson alimuuliza Eddy mara baada ya kumkuta akiwa amesimama juu ya paa akiwatazama jinsi wananchi wanavyo pokelewa na ndugu zao walio weka kambi katika eneo hilo kuhakikisha kwamba wanawaona ndugu zao.

Japo si desturi ya watu wengi kukumbatiana ila kila aliye muona ndugu yake alijikuta akimkumbatia kwa furaha, wengine wakiendelea kuita majina ya ndugu zao wakizidi kuwatafuta katikati ya mamia ya watu walio weza kutoka ndani ya jengo hilo. Wachache kati ya waliopo nje ya jengo, walijikuta wakiingiwa na wasiwasi mwingi na wengine wakiangua vilio baada ya kupata taarifa au kuona miili ya ndugu zao walio fariki.

“Ndio japo si sana”
Eddy alizungumza kwa ufupi huku akiendelea kutazama huku na huku, akabahatika kuweza kumuona Shamsa akiwa amebebwa kwenye machela na kuingizwa ndani ya gari ya wagonjwa, hapo roho yake ikaweza kutulia
“Tuondoke zetu muheshimiwa”
“Usiniite muheshiwa niite……..”
“BLACK SHADOW”

 ***
“I.T.V:WANANCHI WALIO TEKWA WAMEACHIWA USIKU HUU”
“T.B,C:MAMIA YA WANANCHI WALIO TEKWA NDANI YA JENGO LA BIASHARA MLIMANI CITY WAACHIWA HURU”
“Star Tv:GAIDI MMOJA AKAMATWA, NA ALIYE KUWA WAZIRI WA ULINZINA NDIO MTEKAJI MKUU AMEKUTWA AMEKUFA”

Kila muandishi wa kitua cha habari aliye kuwepo katika eneo la tukio la Mlimani City aliweza kuzungumza taarifa hiyo kwa jinsi ya habari aliyo weza kuipata kwa wakati huyo. Watu wote walio kuwemo ndani ya ofisi ya maalumu ya matukio ya raisi Praygod Makuya wakajikuta wakipiga makofi wakifurahia tukio hilo, kila mmoja alikumkumbatia raisi kwa furaha, wakimpongeza kwa kazi nzuri, Rahab naye wakampongeza kwa kuwa pamoja nao katika kazi nzito ya kushinda kwenye mativ makubwa yaliyomo ndani ya ofisi hiyo wakilifwatilia tukio zima.

“Ila hili ni fundisho inaonyesha ni jinsi gani serikali yetu haijajipanga katika kuimarisha ulinzi. Hivyo basi kuanzia leo maeneo yote ya mipaka nitahakikisha ninaongeza vikosi vya ulinzi na usalama, ili kuhakikisha hawa maharamia hawawezi kuingia tena ndani ya nchi yetu”
Raisi Praygod alizungumza kwa sauti ya juu, watu wote wakampiga makofi kwa wazo hilo alilo weza kulitoa.

‘KUSEMA KWELI MIMI NIMSHUKURU YULE MTU ALIYE VALIA NGUO NYEUSI, KWELI ALIAMUA KUJITOA YAANI HUWEZI AMINI MWANANGU ALIMUONA AKI…………”
Dada huyo anaye hojiwa na mundishi alijikuta akimwaga machozi huku akiwa ameshikilia mkono mwanye wa kike, akajipungusa machozi kidogo kisha akendelea kuzungumza,
‘YAANI KUSEMA KWELI YULE KAKA NI JASIRI SANA, NITAMSHUKURU TENA SANA’
Muandishi wa habari akamuhoji mtu mwengine aliye vua shati lake na kulishika mkononi, akionekana kuwa katika hali ya furaha.

‘AISEE  CHALAA WANGU MIMI HUKU DAR SIRUDI TENE, YAANI NIMEKUJA FANYA SHOPING HATA UKINIULIZA SASA HVI SIKUMBUKI NI KIPI KILICHO NILETA HAPA, TENA YULE MAN WANGU ALIYEKUWA ANARUSHA RUSHA MATEKE YANII YULE MAN NIME MMAINDI KICHIZI, YAANI CHALAA ANARUSHA VISU HUYO, JAPO NILIKUWA NIMELALA CHINI, ILA NIKAWA NACHABO MARA KWA MARA KUONA JINSI JAMAA ANAVYO WAANGUSHA WALE NGEDERE YANII CHALAA WANGU NAKUKUBALI SANA’
Kijana huyo mwenye lafudhi ya kichaga alizungumza bila hata ya kupumzika kwa furaha aliyo kuwa nayo hadi ikamlazimu muandishi wa habari kumkatisha na kumuhoji mtu mwengine.

    ***
Eddy na Samson wakafika nyumbani, moja kwa moja wakelekea kwenye chumba cha siri cha Eddy, ikawa ni kazi ya Samson kuhamisha vitu baadhi vilivyomo ndani ya chumba hicho na kuviingiza ndani ya gari. Mamumivu makali yakazidi kuutesa mguu wa Eddy, jasho jingi likanza kumwagika mwilini mwake, kwani hakuweza kumumbia Samson kama ana jeraha kwenye mguu wake, kwa kiasi cha damu kilicho weza kumtoka akajikuta akilegea na kupoteza fahamu.

“Eddy Eddy”
Samson aliita huku akimtingisha Eddy aliye jilaza kwenye kochi mara baada ya kuingia ndani ya chumba hicho, akitoka kupoleka baadhi ya vitu. Katika kumtazama vizuri suruali yeka mguu mmoja umelowana na damu nyingi, katika kumkagua kagua akakuta shimo lililo ingia risasi.

“Shitttttt”
Samson akanyanyuka kwa haraka na kukimbilia kwenye kabati lenye sawa pamoja na vifaha vya kutibia majeraha kwa haraka akaanza kumuhudumia kujaribu kuitoa risasi iliyomo ndani ya paja kabla hata sumu yake kusambaa kila eneo la mwili. Ndani ya muda mchache akafanikiwa kuitoa risasi hivyo na kulifunga jeraha hilo.

“Damu”
Samson akataka kutoa damu yake ili amuongezee Eddy, ila akasita akachukua simu yake na kumpigia Rahab ila simu yake haikuwa hewani, ikabidi atume ujumbe wa maandishi mafupi(massage).

Akataka kumbeba Eddy na kumpeleka ndani ya gari, ila akasikia vishindi vya kama watu wakikimbia nje ya nyumba, kwa haraka akaufunga mlango, akachukua moja ya kiti cha chuma kilichopo ndani ya chumba hicho, akakisogeza karibu na ukutani kisha akapanda juu yake kuchungulia kwenye kijidirisha kidogo kilichopo upande wa juu kabisa wa dirisha hilo. Kundi kubwa la wanajeshi wenye silaha wapo nje ya nyumba ya Eddy wakijiandaa kuvamia ndani ya nyumba hiyo.

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Jumatano ya February 22

Mahakama Yamkingia Kifua Mboe.....Yaamuru Asikamatwe

$
0
0
Mahakama  Kuu Kanda ya Dar es Salaam imetoa zuio la muda kuzuia Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe asikamatwe na Polisi hadi maombi yake, aliyoyaomba ya kutaka asikamatwe, yatakaposikilizwa kesho.

Katika kesi hiyo ya kikatiba namba 1 ya mwaka 2017, Mbowe anapinga mamlaka ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum, Simon Sirro na Mkuu wa Upelelezi wa kanda hiyo (ZCO), Camilius Wambura, ya kutaka kumkamata hadi maombi hayo yatakaposikilizwa.

Maombi ya kesi hiyo yataanza kusikilizwa Februari 23, mwaka huu saa 7:30 mchana katika chumba cha wazi cha mahakama ili kuruhusu watu mbalimbali kusikiliza kesi hiyo.

Jopo la majaji watatu likiongozwa na Sekieti Kihiyo akisaidiana na Jaji Lugano Mwandambo na Jaji Pellagia Kaday lilitoa zuio hilo, hata hivyo walisema Polisi wanaweza kumuita Mbowe kwa mahojiano pindi watakapomhitaji.

Kesi hiyo ambayo ilisikilizwa kwa vipindi vitatu kuanzia saa 4 asubuhi hadi saa 7 mchana, mahakama iliamuru upande wa wadai ambao uliongozwa na Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, kurekebisha maombi yao kwa kuwa hawakumuingiza Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) licha ya kuishitaki serikali.

Hali hiyo ilitokana na mawakili wa upande wa wadai, Lissu ambaye alipinga kitendo cha Mwanasheria wa Serikali, Gabriel Malata kuwatetea wadaiwa hao ambao ni RC, RPC na ZCO katika kesi hiyo kwa kuwa hawajaitaja serikali.

Akijibu hoja hiyo, Malata alidai kuwa waliofunguliwa madai hayo sio Makonda, Sirro wala Wambura, bali ni serikali hivyo ana mamlaka yote ya kuwawakilisha.

Baada ya pande zote kuwasilisha hoja zake, mahakama ilimruhusu Malata kuendelea kusikiliza kesi hiyo ambapo pia iliagiza upande wa wadai kufanya marekebisho ya maombi hayo na kumuongeza AG kama mdaiwa.

Hata hivyo, Lissu aliomba waruhusiwe kufanya marekebisho hayo kwa kumuongeza AG, ombi ambalo halikuwa na pingamizi.

‘’Tutafanya marekebisho ya maombi yetu na marekebisho mengine madogo madogo kwa namna tutakavyoona inafaa siku ya Jumatatu na tutawapa wajibu maombi Machi 6 mwaka huu na Machi 8 mwaka huu itatajwa kwa ajili ya kusikiliza maombi hayo,’’ alidai Lissu.

Mbowe aliwasili mahakamani hapo akiwa na gari lenye usajili namba T 830 aina ya Land Cruiser, saa chache kabla ya kesi yake kuitwa katika chumba namba 64 kwa ajili ya kusikilizwa.

Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai mkoani Kilimanjaro, alifika mahakamani hapo baada ya kutoka Kituo Kikuu cha Polisi saa 7 usiku, alikokuwa anahojiwa na kupekuliwa kuhusu sakata la dawa za kulevya.

Aidha, viongozi mbalimbali wa chama hicho wakiwemo Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, madiwani na wafuasi wao walijitokeza kwa wingi, kusikiliza kesi hiyo huku wakifurahia amri ya mahakama ya kuzuia kutokamatwa kwa mwenyekiti huyo.

Katika kesi ya msingi, Mbowe anaomba mahakama iwazuie wadaiwa kutekeleza azma yake ya kumtia mbaroni, pia itoe amri ya kuwazuia kumkamata hadi hapo kesi hiyo ya kikatiba, itakapomalizika na kwamba polisi wasiendelee na mchakato wowote dhidi yake hadi hapo kesi hiyo itakapomalizika.

Anadai kuwa sheria inayompa Mkuu wa Mkoa mamlaka ya kutoa amri ya kumkamata na kumweka ndani mtu, iko kinyume cha katiba, kwa madai kuwa ilitungwa katika mazingira ambayo hapakuwa na vituo vya polisi vya kutosha.

Pia anadai kuwa kwa mazingira ya sasa, sheria hiyo imeshapitwa na wakati na anaiomba mahakama itamke kuwa ni kinyume cha katiba.

Mbowe pia anadai kuwa hata kama Mkuu wa Mkoa alikuwa anatekeleza mamlaka yake kwa mujibu wa sheria hiyo, basi hakutimiza matakwa ya kisheria, ambayo ni pamoja na kutoa taarifa kwa Hakimu wa Mahakama ya Wilaya au ya Hakimu Mkazi.

Vile vile, anaiomba mahakama kama itaona kuwa Mkuu wa Mkoa alikuwa sawa kutoa amri hiyo, basi imwamuru afuate matakwa ya kisheria, ikiwa ni pamoja na kulinda haki za binadamu katika kutekeleza madaraka yake hayo.
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live




Latest Images