Quantcast
Channel: MPEKUZI
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live

Picha: Billicanas Ya Mbowe Yabomolewa Rasmi

$
0
0
Shirika  la Nyumba la Taifa (NHC) limeanza kubomoa jengo la iliyokuwa Klabu Bilicanas na ofisi za Free Media inayomiliki gazeti la Tanzania Daima zinazomilikiwa na Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Taifa, Freeman Mbowe, lililopo makutano ya barabara ya Mkwepu na Indira Gandhi lenye kitalu namba 725-726/24 na hati namba C. T No. 186018/15 and C. T No. 186018/10.

Ubomoaji huo ulioanza jana unafanyika wakati Mbowe ameingia katika mgogoro na NHC baada ya kampuni ya udalali ya Poster and General Traders kumtolea vyombo nje mwanzoni mwa Septemba, mwaka jana kwa kudaiwa Sh bilioni 1.2 ambayo ni deni la pango ya miaka 20.

Mwanzoni mwa Septemba, mwaka jana NHC kwa kushirikiana na Kampuni ya Poster and General Traders, ilifika katika jengo hilo kwa maelekezo ya kutoa  thamani mbalimbali zilizokuwa katika ofisi za jengo hilo na kumpa Mbowe siku 14  kulipa deni analodaiwa na kuweza kugomboa mali hizo.

Mpango huo ulisimamiwa na Meneja wa Ukusanyaji Madeni wa NHC, Japhet Mwanasenga na alisema Mbowe alikuwa na muda wa wiki mbili kwa wakati huo kulipa fedha hizo kabla ya vifaa vyake kupigwa mnada.

Mwanasenga alisema taratibu zote zilifuatwa kabla ya kumwondoa mteja huyo ikiwamo notisi na kwamba vifaa hivyo vitashikiliwa kwa muda huo na endapo akishindwa kulipa jengo hilo atapangishwa mtu mwingine.

Alisema shirika hilo linahitaji fedha kwa ajili ya ujenzi na uendelezaji wa majengo yake hivyo mteja anayedaiwa ajiandae kuondolewa wakati wowote huku baadhi ya watu wakilihusisha tukio la Mbowe kuondolewa katika ofisi hizo na masuala ya siasa.

Hata hivyo, Mwanasenga, alisema uamuzi wa kumwondoa katika ofisi hizo hauna uhusiano na masuala ya siasa.

Kutokana na hali hiyo, Mbowe kupitia Mawakili wake, John Malya na Peter Kibatala, walifungua shauri la kupinga kuondolewa katika jengo hilo Mahakama Kuu ya Tanzania na kutaka kurudishwa katika jengo hilo.

Hata hivyo, maombi hayo yalitupiliwa mbali Oktoba 17, mwaka jana na Jaji Sivangilwa Mwangesi na kusema kuwa mahakama hiyo imechukua uamuzi huo baada ya kujiridhisha na hoja kuu tatu kuwa hakuna mkataba wa ubia uliopo baina ya NHC na Mbowe Hotels Limited na kuwa uhusiano pekee uliosalia ni wa mpangaji na mpangishaji.

Pia Jaji Mwangesi alisema mahakama imejiridhisha kuwa NHC imefuata taratibu zote katika kuiondoa Mbowe Hotels Limited kwa kutoa ilani ya siku 30 na baadaye siku 14 kabla ya kumtoa mteja wao huyo.

Kuhusu kusajiliwa au kutosajiliwa kama dalali rasmi wa mahakama wa kuendesha mchakato wa kumhamisha Mbowe katika jengo hilo, alisema hiyo nayo haikuwa hoja yenye mashiko na kwamba waombaji walitakiwa kuwasiliana na Msajili wa Mabaraza ya Ardhi.

Katika shauri hilo, NHC iliongozwa na Wakili Kiongozi, Aloyce Sekule na Ipilinga Panya na mawakili wake wengine waliojikita katika kujibu hoja zilizokuwa zikitolewa na wateja wao.



Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Atembelea Mgodi Wa Makaa Ya Mawe Ya Ngaka.....Anusa Madudu, Aahidi kutuma Gavana, CAG, Msajili wa Hazina kufanya ukaguzi

$
0
0
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa atamtuma mara moja Msajili wa Hazina aende kufanya uchunguzi wa kina na wa kijinai (forensic investigation) ili kijiridhisha kama mapato na matumizi ya kampuni ya TANCOAL ni halali.

Ametoa kauli hiyo jana  mchana (Ijumaa, Januari 6, 2017) mara baada ya kupokea taarifa na kutembelea mgodi huo ili kuona shughuli za uzalishaji zikoje.

Waziri Mkuu amesema atamwagiza pia mdhibiti na mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ili apitie mahesabu ya kampuni tangu mwaka 2011 walipoanza uzalishaji. 

“Mbali na CAG, itabidi Gavana wa Benki Kuu naye aangalie utumaji wa fedha uliokuwa ukifanywa kama ulifanyika kwa halali,” alisema.

Katika maswali aliyoyauliza Waziri Mkuu, alitaka kujua ni kwa nini kampuni hiyo haijalipa gawio kwa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) ambao ni mbia (asilimia 30) na kampuni ya Intra Energy Limited (asilimia 70) licha ya kuwa imekuwa ikifanya uzalishaji wa makaa ya mawe na kuyasafirisha kwenye viwanda hapa nchini na nje ya nchi.
 
“Taarifa zenu zinaonyesha kuwa mmepata kila mwaka lakini rekodi nilizonazo zinanionyesha kuwa mwaka 2013 mlipanga kuzalisha tani 50,000 na mkauza zaidi ya hapo. Mkaguzi wa hesabu anasema kampuni imepata hasara, hii itawezekanaje?” alisema wakati akimhoji Mkurugenzi Mtendaji wa NDC, Bw. Mlingi Mkucha.
 
“Desemba 2013 mliuza tani 39,000 kwa wamiliki wa viwanda vya nguo, pia mliuza tani 2,000 kwa kampuni ya saruji ya Zambia, Novemba 2013 mliingia makubaliano ya kuuza tani 165,000 kwa kampuni ya saruji ya Kitanzania na ziliuzwa. Mbona financial statement zenu zinasema mwaka huo nao mlipata hasara?”
 
“Mnasema gawio (dividend) hutolewa baada ya mtu kutangaza faida. Mbona mlivuka lengo lakini mkatangaza kuwa kampuni imepata hasara katika mwaka huo wa fedha?”
 
Waziri Mkuu alimbana Bw. Mkucha aeleze ni kwa nini akiwa mwanasheria wa NDC aliruhusu kuwepo kwa mkataba unaotoa mwanya kwa kampuni ya TANCOAL kulipia gharama za menejimenti kwa wakurugenzi ambao wako Australia wakati hawahusiki na utendaji wa kila siku wa TANCOAL hapa nchini.
 
Pia alihoji ni kwa nini aliyekuwa Mkurugenzi wa NDC, Bw. Gideon Nassari alikuwa ni mjumbe wa Bodi ya TANCOAL na mjumbe wa Bodi ya Intra Energy Corporation ya Australia huku akiwa ni Mtendaji Mkuu wa NDC. 

“Wewe ulikuwa mwanasheria wa NDC na ulilijua hilo lakini hukuona taabu ya kiutendaji katika hilo? Au ulishindwa kusema kwa sababu alikuwa ni bosi wako?”
 
Waziri Mkuu amemtaka Bw. Mkucha aupeleke mikataba huo kwa Mwanasheri Mkuu wa Serikali ili aupitie upya na hasa kipengele cha kufungua akaunti za NDC kwa kutumia kanuni za Australia na suala la utaratibu wa gawio kwa wanahisa ambapo kifungu kilichopo kinaipa Bodi ya TANCOAL mamlaka ya kuamua kutoa au kutokutoa kwa wanahisa.

“Kipengele kama hiki kwenye mikataba kinazuia ninyi kupata gawio, na ndiyo maana hesabu zao kila mwaka zimekuwa zinasoma hasara na ninyi mnaona sawa tu huku Serikali ikiendelea kukosa mapato yake,” alisema.

Waziri Mkuu ameutaka uongozi wa kampuni ya TANCOAL uongeze uzalishaji ili iweze kukidhi mahitaji ya ndani kwani makampuni mengi yamebaini gharama kubwa iliyopo kwenye matumizi ya mafuta ya dizeli na sasa yanahitaji makaa ya mawe kwa uzalishaji.
 
“Nimetembelea mgodi na kujiridhisha kuwa makaa ya mawe yapo ya kutosha. Uongozi wa kampuni mmesema mashine ziko bandarini Mtwara, lipieni mkamilishe taratibu ili mashine na mitambo yenu vije kusaidia kuongeza uzalishaji,” alisema.
 
“Nirudie wito wa Serikali kuwa hatutaruhusu uagizaji wa makaa ya mawe kutoka nje ya nchi na kwa maana nyingine tumewaongezea wigo wa soko lakini ninyi mnakosa teknolojia ya uchimbaji makaa kwa wingi. Fanyeni haraka kuleta hivyo vifaa vilivyoko bandarini,” alisisitiza.
 
Akiwa kwenye mgodi huo, Waziri Mkuu alielezwa kuwa kampuni hiyo imepanga kuongeza uzalishaji na kufikia tani 60,000 kutoka tani 2,500 za sasa. Hivi sasa, uchimbaji kwenye mgodi wa Ngaka unafanyika kwenye eneo la Mbalawala na Mbuyura ambayo yana mashapo (deposits) ya tani milioni 423.
 
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU


Tanzania Yapata Fursa Kubwa ya Biashara....Yaingizwa Katika Mpango Mkubwa wa Biashara na China

$
0
0
Jitihada za Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan za kuiingiza Tanzania katika mpango mkubwa wa biashara kwenye Bara la Asia, Mashariki ya Kati, Ulaya na Afrika, umefanikiwa.

Ni baada ya Tanzania kuchaguliwa kuwa miongoni mwa nchi saba zilizoingizwa katika mpango, unaojulikana kama ‘China One Belt, One Road Stratergy’. Nchi nyingine ambazo zimechaguliwa na kuingizwa kwenye mpango huo ni Malaysia, Sri Lanka, Nepal, Bangladesh, Pakistan na Thailand.

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais, jana, ilisema baada ya Tanzania kuingizwa rasmi katika mpango huo, Makamu wa Rais, Samia ambaye pia mjumbe katika jopo la Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa la Kumuwezesha Mwanamke Kiuchumi, akiwakilisha nchi za Ukanda wa Kusini na Mashariki mwa Afrika, alikutana na watendaji kutoka Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Chama cha Wafanyabiashara Wenye Viwanda na Biashara (TCCIA) na Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI), kuwaeleza kuhusu muhimu wa Tanzania kuingizwa kwenye mpango huo.

Makamu wa Rais alisema Tanzania imepata uanachama ndani ya mpango huo, baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na mfanyabiashara wa madini na vito kutoka China, Dk Helen Lau kuhusu manufaa ya mpango huo.

Alisema alimuomba mfanyabiashara huyo, kuisaidia Tanzania kuingia kwenye mpango wa China One Belt, One Road Stratergy, jambo ambalo limefanikiwa.

Taarifa hiyo iliendelea kusema kuwa mwezi Septemba mwaka 2016, ulifanyika mkutano Guangdong nchini China kujadili maombi ya kujiunga na mpango huo, ambapo Makamu wa Rais alimuomba Dk Helen, kwa niaba ya Tanzania, awasilishe maombi ya kutaka kujiunga.

Kwa bahati nzuri, ombi la Tanzania lilikubaliwa na kupata uanachama katika mpango huo mkubwa wa China One Belt, One Road Stratergy.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Makamu wa Rais alisema kuwa moja ya fursa zinazotolewa na Serikali ya China katika mpango huo, kila nchi mwanachama hupewa vyumba vya ofisi katika jengo linaloitwa 21st Century Maritime Silk Road Expo bila kulipa kodi ya pango kwa miaka mitatu.

Baadhi ya vyumba vya jengo hilo, vitatumiwa na nchi husika kuonesha na kutangaza bidhaa zao. Kufutia Tanzania kuingizwa kwenye mpango huo, Samia aliwaagiza watendaji wa sekta binafsi aliokutana nao Ikulu jijini Dar es Salaam, wajipange na kuweka mikakati ya namna ya kunufaika na mpango huo haraka iwezekanavyo.

Alibainisha kuwa mpango huo wa China One Belt, One Road Stratergy, ulibuniwa na serikali ya China kwa dhamira ya kuzikutanisha jumuiya za wafanyabiashara za Mashariki mwa Bara Asia, Mashariki ya Kati, Ulaya na Afrika ili wabadilishane mawazo, kuonesha njia na kupeana ushauri wa jinsi ya kukuza biashara kati ya nchi wanachama wa mpango huo ili kuiwezesha sekta ya biashara, kuchangia vyema kwenye uchumi wa mataifa yao.

Makamu wa Rais alisema baada ya Tanzania kuingia kwenye mpango huo, itanufaika na fedha za mfuko kwa ajili ya maendeleo ya miundombinu, ambazo zinatolewa kwa nchi zilizojiunga na mpango huo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TPSF, Godfrey Simbeye na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Wenye Viwanda na Wakulima Zanzibar, Taufik Turki walimuahidi Makamu wa Rais kuwa watatumia fursa hiyo ipasavyo ili kukuza biashara kati ya Tanzania na nchi wanachama wa mpango huo.

Zitto Kabwe Aitaka Serikali Itangaze Balaa la Njaa

$
0
0
Kiongozi wa Chama cha ACT –Wazalendo, Zitto Kabwe ameitaka Serikali kutangaza rasmi baa la njaa kwa mujibu wa sheria kutokana na hali ya chakula kuwa mbaya nchini.

Kauli ya Zitto imetolewa wakati Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisisitiza utunzaji wa chakula baada ya kukagua maghala ya nafaka yanayomilikiwa na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), Kanda ya Songea.

Agizo la Majaliwa pia limetolewa siku mbili baada ya Waziri wa Kilimo, Dk Charles Tizeba kutofautiana na Zitto kuhusu hali ya chakula ambapo Waziri huyo alisema hali ya chakula nchini ni shwari huku Mbunge huyo wa Kigoma Mjini akisema ni mbaya.

Jana, mbunge huyo akihutubia mkutano wa kampeni ya kumnadi mgombea udiwani Kata ya Nkome, Geita aliendelea kupigilia msumari kauli yake akisema, “Hali ya chakula ni mbaya, ni mbaya, ni mbaya.”

Alisema baada ya ziara ya Waziri Mkuu kwenye maghala ya Taifa na kujionea hali ya chakula nchini, ni vyema Serikali ikachukua hatua.

“Ninapendekeza Serikali ichukue hatua muhimu ya kisheria ya kutangaza baa la njaa nchini. Tamko la baa la njaa litaisaidia Serikali kupata bajeti ya dharura ya kununua chakula na kutoa uhuru kwa wakuu wa wilaya kutangaza bila woga kuwa maeneo yao yana njaa,” alisema Zitto huku akimpongeza Majaliwa kwa ziara hiyo.

Lowassa, Maalim Seif Kutikisa Zanzibar Kesho

$
0
0
Wanasiasa wakongwe nchini, Maalim Seif Sharif Hamad aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar na Edward Lowassa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika, kesho wanatarajia kuungana kwa mara ya kwanza jukwaani tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

Vigogo hao wa vyama vya CUF (Maalim Seif) na Chadema (Lowassa) wataunguruma katika viwanja vya Skuli ya Fuoni visiwani Zanzibar kumnadi mgombea ubunge wa jimbo la Dimani kwa tiketi ya CUF, Abdulrazaq Khatib Ramadhani, katika uchaguzi mdogo utakaofanyika Januri 22 kuziba nafasi ya aliyekua mbunge wa jimbo hilo, Hafidh Ally Tahir aliyefariki dunia Novemba 11  mwaka jana.

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Salum Mwalimu  amesema kuwa chama chake kimemua kuungana na CUF katika uchaguzi huo ili kuhakikisha mshirika wake huyo wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) anamshinda mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Aidha, Mwalimu aliongeza kuwa baada ya Lowassa kushiriki uzinduzi wa kampeni hizo kesho, viongozi wengine wa Chadema watafuata kwa kufanya mikutano mbalimbali jimboni humo. Alisema kuwa baada ya Lowassa atafuata Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe pamoja Tundu Lissu kwa nyakati tofauti, kisha wengine wataendelea hadi mwisho wa kampeni hizo.

Akizungumzia uamuzi huo wa Chadema, Mkurugenzi wa Habari,Uenezi na Mawasiliano kwa Umma, Salim Bimani alieleza kufurahishwa na uamuzi huo wa Chadema na kueleza kuwa hatua ya Lowassa kuhudhuria uzinduzi huo itaongeza hamasa kubwa kwa wapenzi wa chama hicho.

“Umenambia hadi Lowassa atakuwepo? Ni furaha iliyoje, Wanzibari wana shauku kumuona. Siku ya kampeni patakuwa hapatoshi Skuli ya Fuoni, hapa Simba (Maalim Seif) kule Lowassa kipenzi kingine cha Wazanzibar,” Bimani anakaririwa na Mwananchi.

Aliongeza kuwa kama Lowassa atahudhuria mkutano huo atakuwa na mambo mawili makubwa ya kufanya, la kwanza likiwa kuwashukuru Wazanzibar kwa kura walizompa katika uchaguzi Mkuu wa mwaka jana. Na la pili litakuwa kumpigia kampeni mgombea wa CUF, Abdulrazaq Khatib Ramadhani.

Lowassa ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema na Maalim Seif ambaye ni Katibu Mkuu wa CUF, wataingia katika jimbo hilo ikiwa ni siku chache baada ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kufanya uzinduzi wa kampeni hizo akiambatana na viongozi wengine wa kitaifa wa chama hicho.

Hivyo, kwa muktadha wa kisiasa, vigogo hao wa Ukawa wana kazi ya kusawazisha matuta yaliyowekwa na timu ya chama tawala iliyoongozwa na Kinana.

Kaimu Kamishna Jenerali Wa Magereza Afanya Mabadiliko Ya Uongozi Kwa Maafisa Waandamizi Wa Magereza

$
0
0
Kaimu Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza nchini, Dkt. Juma Ally Malewa(pichani) amefanya Mabadiliko ya Uongozi kwa baadhi ya Wakuu wa Magereza Mikoa na vituo mbalimbali hapa nchini.

Mabadiliko hayo ni pamoja na aliyekuwa Mkuu wa Magereza Mkoa wa Morogoro Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza SACP Katos Rugainunura amehamishiwa Makao Makuu ya Magereza sehemu ya Utawala na nafasi yake inakaimiwa na Kamishna Msaidizi wa Magereza ACP Mzee Nyamka aliyekuwa Mkuu wa Utawala Magereza Mkoani Morogoro.

Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza SACP Antonino Kilumbi aliyekuwa Mkuu wa Magereza Mkoa wa Dodoma amehamishwa kwenda Makao Makuu ya Magereza kuwa Mkuu wa Kikosi cha Ujenzi na nafasi yake inachukuliwa na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza SACP Julius Sang’udi aliyekuwa Mkuu wa Magereza Mkoa wa Mbeya.

Aliyekuwa Mkuu wa Magereza Mkoa wa Kilimanjaro Kamishna Msaidizi wa Magereza ACP Anderson Kamtiaro anaenda kuwa Afisa Mnadhimu Magereza Mkoani Arusha na nafasi yake inachukuliwa na Kamishna Msaidizi wa Magereza ACP Hassan Mkwiche ambaye alikuwa ni Mkuu wa Gereza Kuu Karanga, Moshi.
Aliyekuwa Mkuu wa Gereza Same Kamishna Msaidizi wa Magereza ACP Evarist Katego anakwenda kuwa Mkuu wa Gereza Kuu Karanga, Moshi. Aliyekuwa Mkuu wa Magereza Mkoa wa Mwanza Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza SACP Uwesu Ngarama amehamishiwa Makao Makuu kuwa Boharia Mkuu wa Jeshi na nafasi yake inachukuliwa na aliyekuwa Afisa Mipango wa Jeshi ACP Athuman Kitiku.

Aidha, aliyekuwa Mkuu wa Magereza Mkoani Mtwara, Kamishna Msaidizi wa Magereza ACP Musa Kaswaka anakwenda Makao Makuu Kitengo cha Ukaguzi na nafasi yake kuchukuliwa na Kamishna Msaidizi wa Magereza ACP Ismail Mlawa aliyekuwa Mkuu wa Kiwanda cha Samani Gereza Kuu Ukonga. Aliyekuwa Afisa Mdhibiti wa Fedha wa Jeshi Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza SACP Gideon Nkana anakwenda kuwa Mkuu wa Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji, Ukonga, Dar es Salaam na nafasi yake kuchukuliwa na Kamishna Msaidizi wa Magereza ACP Chacha Jakson.

Wengine ni pamoja na aliyekuwa Afisa Mnadhimu wa Magereza Mkoa wa Mbeya ACP Kijida Mwakingi anakaimu nafasi ya Mkuu wa Magereza Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi wa Magereza ACP Abdalah Misanga anayetoka Gereza Mgumu kwenda kuwa Mkuu wa Gereza Msalato, Kamishna Msaidizi wa Magereza ACP John Itambu anayetoka Gereza Kilosa kwenda kuwa Mkuu wa Kiwanda cha Samani Gereza Kuu Ukonga.

Kamishna Msaidizi wa Magereza ACP Erasmus Kundy anayetoka Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Ukonga kwenda Makao Makuu Kitengo cha Habari, Kamishna Msaidizi wa Magereza ACP Julius Ntambala aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Ujenzi Makao Makuu anabakia Makao Makuu Kitengo cha ujenzi kuwa Msaidizi wa Mkuu wa Kitengo, Kamishna Msaidizi wa Magereza ACP Sylivester Mrema anayetoka Gereza Idete kwenda Gereza Ubena kuwa Mkuu wa Gereza.
Aliyekuwa Mkuu wa Gereza Ubena Kamishna Msaidizi wa Magereza ACP Shaba Zephania anakwenda Magereza Mkoa wa Pwani kuwa Afisa Mnadhimu, Kamishna Msaidizi wa Magereza ACP Solomon Urio anayetoka Makao Makuu kwenda Magereza Mkoa wa Dar es Salaam kuwa Afisa Mnadhimu pamoja na aliyekuwa Boharia Mkuu wa Jeshi la Magereza Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza SACP George Kiria amehamishiwa Makao Makuu Kitengo cha Uhasibu .

Mabadiliko hayo ni ya kawaida na yanalenga kuboresha utendaji kazi na ufanisi wa Jeshi la Magereza.

Imetolewa na:
Lucas Mboje - ASP
Ofisa Habari wa Jeshi la Magereza
Makao Makuu ya Magereza Tanzania Bara
07 Januari, 2017.

Agizo la Makamu wa Rais kwa Majaji na Mahakimu wanawake katika kukabiliana vitendo vya rushwa,unyanyasaji kijinsia na rushwa ya ngono

$
0
0
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewaagiza majaji na mahakimu wanawake kote nchini kupambana ipasavyo katika kukabiliana vitendo vya rushwa,unyanyasaji kijinsia na rushwa ya ngono ili kusaidia wanawake kupata haki zao za msingi bila kubaguliwa katika jamii.

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa agizo hilo jijini Dar es Salaam wakati anafungua Mkutano Mkuu wa NANE wa Chama cha Majaji na Mahakimu wanawake Tanzania (TAWJA).

Makamu wa Rais pia ameonya kuhusu vitendo vya rushwa ya ngono inayofanywa na baadhi ya watendaji wenye madaraka na kusema tabia hiyo ni mbaya na lazima ikomeshwa mara moja katika jamii.

Amesema kuwa vitendo hivyo vya rushwa ya ngono huzuia na kukwamisha juhudi za wanawake kufikia huduma za kijamii na za kiserikali ipasavyo ikiwemo elimu, ajira na haki kwa ajili ya ustawi wa wanawake.

Aidha Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amekishukuru Chama cha Dunia cha Majaji Wanawake (IAWJ) kwa mchango na msaada wake kwa TAWJA katika programu ya miaka mitatu ya kupambana na matumizi mabaya ya madaraka na rushwa ya ngono.

Makamu wa Rais pia ameipongeza Wizara ya Katiba na Sheria, Shirika la UN Women na wadau wengine wa TAWJA kwa kuunga mkono mapambano ya aina zote za ubaguzi na ukatili dhidi ya wanawake na watoto nchini.

Amesema elimu ya haki za Binadamu iliyotolewa na Chama hicho imeleta badiliko kwa wengi kwa njia ya mafunzo na machapisho na jitihada hivyo lazima ziongezwe ili huduma hiyo iweze kuwafikia wananchi wengi zaidi kote nchini.

Amesisitiza wanachama wa Chama cha TAWJA waendelee kutoa msaada katika kuwasaidia wanawake na watoto ambao wanakandamizwa kwa kunyimwa haki zao katika jamii ili waweze kupata haki zao nchini.

Kwa upande wake, Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mohamed Chande Othman amemhakikishia Makamu wa Rais kuwa mkakati wa uimarishaji wa shughuli za mahakama nchini unaendelea vyema lengo likiwa ni kutenda haki kwa wananchi kote nchini bila ubaguzi.

Kauli mbiu ya Mkutano Mkuu wa NANE wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (TAWJA) “Kuongoza njia kufikia hitajio la upatikanaji wa haki kwa wote na kwa wakati”.

Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
Dar es Salaam
7-Jan-2017.

Alikiba kufungua mwaka na tour za kimataifa, kuanza na Afrika Kusini

$
0
0
Mkali wa wimbo Aje na mshindi wa tuzo ya mwanamuziki bora wa EATV Award 2016, Alikiba amefungua mwaka kwa kutangaza tour yake ya kimataifa.

Muimbaji huyo ambaye mwaka 2016 ulikuwa mzuri kwa upande wake baada ya kuchukua tuzo 13 za kitaifa na kimataifa, tour yake itaanza February nchini Afrika Kusini.

“Happy New Year. It’s time to meet my fans across the world. I start with South Africa in February 2017! . KING KIBA LIVE ON TOUR IN SOUTH AFRICA. Contact Exclusive Agent & PR @matthewmensah for additional bookings & endorsements in SA/Southern Africa. #MTVEMABestAfricanAct#AlikibaSATour2K17#KingKibaWorldTour2K17 #KingKiba,” aliandika Alikiba kupitia facebook yake.

Muimbaji huyo hivi karibuni alifanya show ya funga mwaka nchini Uganda, show ambao ilidaiwa kuweka historia nchini humo kutokana na kuhudhuriwa na watu wengi.

Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Jumapili ya January 8

Waziri Mkuu Ataka TANCOAL Itimize Masharti Ya Mkataba Mgodi Wa Ngaka

$
0
0
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameitaka kampuni ya TANCOAL Energy inayochimba makaa ya mawe kwenye mgodi wa Ngaka itimize masharti ya mkataba iliouingia na Serikali mwaka 2008.

Kampuni ya TANCOAL iliundwa Aprili 3, 2008 na kampuni tanzu ya Atomic Resources Limited ambayo wakati huo ilikuwa ikijulikana kama Pacific Corporation East Africa (PCEA) na kwa sasa inaitwa Intra Energy (T) Limited ambayo hisa zake ni asilimia 70 na Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) lenye asilimia 30 ya hisa.

Ametoa kauli hiyo Ijumaa, Januari 6, 2017 mara baada ya kutembelea mgodi huo na kukagua shughuli za uzalishaji. Mgodi wa Ngaka uko wilaya ya Mbinga, mkoani Ruvuma na unamilikiwa na kampuni ya TANCOAL kwa ubia baina ya Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) na kampuni ya Intra Energy Corporation ya Australia.

Kwa mujibu wa mkataba huo, ilikubaliwa kwamba mbali ya kuzalisha makaa ya mawe, kampuni hiyo ilipaswa kuzalisha umeme wa megawati 400 kutokana na makaa hayo. TANCOAL ina migodi miwili; Mbalawala na Mbuyura ambao umetengwa mahsusi kwa ajili ya kuzalisha umeme.

“Kwenye mkataba tulikubaliana kuwa mtazalisha umeme lakini hadi hadi leo hamjaanza mnadai kuwa TANESCO wanawachelewesha. Nitafuatilia nione kama ni wao au la ili tujue ukweli,” alisema.

Kwa mujibu wa mikataba huo, TANCOAL ilipaswa kugharamia dola za Marekani milioni 14.49 kwa ajili ya ujenzi wa barabara na madaraja ili kuwezesha malori makubwa na madogo yaweze kufika mgodini na kusomba makaa hayo.

“Mlisema mngetengeneza barabara lakini hadi sasa bado hamjafanya hivyo na ndiyo maana malori yanaishia kule. Yangefika hapa moja kwa moja, mngeweza kubaini kwa urahisi mahitaji ya makaa ya mawe ni kiasi gani,” alisema Waziri Mkuu.

Hivi sasa, malori ya kutoka mgodini yanashusha makaa yaliyochimbwa kwenye eneo lililokodishwa na TANCOAL la Amani Makolo ambalo liko umbali wa km.55 kutoka mgodini na malori makubwa yanapakia makaa hayo kutoka kwenye eneo hilo jambo ambalo linazidisha gharama za usafirishaji.

Kwa mujibu wa mkataba huo, TANCOAL ilipaswa kuwekeza mtaji wa Dola za Marekani milioni 82 lakini hadi sasa imewekeza kiasi cha dola milioni 14 ambazo ni sawa na asilimia 12 tu ya ahadi iliyotolewa.

“Makubaliano yalikuwa ninyi mtawekeza Dola za Marekani milioni 81.69 lakini hadi sasa mmetumia dola za Marekani milioni 14, hamjafikia hata nusu,” alisema Waziri Mkuu.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amemtaka Mwenyekiti wa Bodi ya NDC, Dk. Samuel Nyantahe afuatilie kwa makini mambo yanayoendelea ndani ya shirika hilo. “Wewe unaendesha vikao lakini haya ndiyo mambo yanayoendelea kwenye taasisi unayoiongoza,” alisema.

Alimtaka afuatilie pia uwasilishaji wa mkataba huo kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili vipengele vinavyoibana NDC kiuendeshaji na kupata gawio viweze kuangaliwa upya.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amewapongeza viongozi wa kampuni ya TANCOAL kwa kuwashirikisha wajasiriamali wadogo kupata teknolojia ambayo itasaidia kupunguza tatizo la ukataji miti kwa matumizi ya kuni na mkaa.

Alisema mgodi huo umeanza kuwanufaisha wenyeji kwani ameona kazi nzuri inayofanywa na kikundi cha akinamama cha Mbalawala (mbalawala Women Group) ambacho kinatumia vumbi la makaa hayo (ambayo ni mabaki) kutengeneza mkaa wa kupikia majumbani (briquettes).

“Hii teknolojia ikisambazwa kwenye shule, mahospitali na kwenye magereza itasaidia kupunguza matumizi makubwa ya kuni yanayofanywa na taasisi hizi,” alisema.

Meneja wa kikundi hicho, Bibi Leah Kayombo alisema wanatumia chengachenga na vumbi la makaa hayo kwa kuchanganya na kemikali nyingine ili kupunguza joto halisi la makaa hayo, jambo linalowezesha mkaa huo kutumika majumbani bila kuharibu masufuria.

IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU

Lowassa Atema Cheche Arusha Akimnadi Mgombea Udiwani wa CHADEMA

$
0
0
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amesema mabadiliko makubwa ya kisiasa yanayotokea duniani katika kipindi hiki hayawezi kuzuiliwa na mifumo iliyopo.

Akizungumza jana na mamia ya wananchi waliojitokeza kwenye uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani Kata ya Mateves katika Halmashauri ya Arusha Vijijini, Lowassa alisema nguvu kubwa ya mabadiliko inayoonyeshwa na Chadema itawaletea wananchi maendeleo.

Lowassa ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema alisema katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, chama chake kilipata kura nyingi kwenye maeneo mengi licha ya kutokuwa washindi na kwamba wamejipanga katika uchaguzi wowote utakaofanyika kuhakikisha kinashinda kwa kishindo.

“Ninazindua kampeni za uchaguzi huu mdogo nikiwa na imani kubwa kwa Chadema. Nina imani kuwa mgombea wa chama hiki atatekeleza anayoyaahidi na kuondoa kero zenu na ndiyo maana Chadema inaungwa mkono zaidi nchini,” alisema Lowassa.

Alisema katika mpango wa kukiimarisha chama hicho, wajumbe wa Kamati Kuu ya Chadema wanazunguka nchi nzima kuanzia ngazi ya tawi hadi Taifa.

Katika harakati za kuhakikisha kwamba upinzani unaibuka na ushindi katika chaguzi ndogo zote zilizopangwa kufanyika Januari 22, Lowassa alisema leo atakuwa Zanzibar katika uzinduzi wa kampeni za mgombea ubunge wa Dimani kwa tiketi ya CUF, Abdulrazaq Khatib Ramadhan na baada ya hapo ataelekea Bukoba katika kampeni za Ukawa.

Uchaguzi wa Kata ya Mateves unafanyika baada ya Mahakama kuagiza urudiwe kutokana na kasoro zilizojitokeza kwenye uchaguzi ulipita ambao mgombea wa CCM alitangazwa mshindi.

Diamond kufunika ufunguzi wa Kombe la Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2017’

$
0
0
Ule wimbo unaosikika mtaani wa ‘pesa kupotea mifukoni’ haumhusu Bosi wa WCB, Diamond Platinumz anayeendelea kuzihesabu ‘deals’ kubwa zaidi za matukio ambayo dunia nzima inayaangalia kwa macho yote.

Siku chache baada ya kutumbuiza kwa ustadi mkubwa kwenye tuzo za CAF jijini Abuja nchini Nigeria, Diamond amealikwa kutumbuiza kwenye ufunguzi wa Kombe la Mataifa ya Africa 2017 (AFCON 2017), Januari 14 nchini Gabon.

Chibu Dangote amewapa habari hiyo njema mashabiki wake kupitia mitandao ya twitter na Instagram, kwa kupost taarifa ya show yake hiyo iliyowekwa kwenye akaunti maalum ya AFCON 2017.

“GABON!!! You know we gat to make a World History on the 14th January right?? See you this this Coming Weekend then…👈 #WcbWasafi” aliandika.

Ingawa Tanzania haipo miongoni mwa nchi zinazoshiriki kombe hilo kubwa zaidi la soka barani Afrika, mwaka huu bendera itapeperushwa kupitia tasnia ya Muziki na kuiacha alama ya Tanzania kwenye mashindano hayo.

Lowassa atoa neno kwa waliomtabiria kifo

$
0
0
Waziri Mkuu aliyejiuzuru Edward Lowassa, amesema kuwa Serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM), ina watu wenye roho mbaya kwani waliwahi kumuombea kifo,lakini hadi leo anadunda.
 
Lowassa ambaye alikuwa mgombea urais wa Chadema na kuungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi(Ukawa), amesema baadhi ya waliomwombea kifo leo hawapo duniani,kwani mungu ndiye anayepanga maisha ya mwanadamu.
 
“Kule kwa wenzetu kuna watu wenye roho mbaya,kwani hata mimi waliniombea kifo,waliniombea kifo muda mrefu kweli lakini mpaka sasa bado nadunda tu wakati baadhi ya walioniombea hivyo,leo hawapo duniani kwa mapenzi ya mungu”alisema Lowassa.
 
Lowassa aliyasema hayo jana baada ya wananchi waliokuwa kwenye mkutano wa ufunguzi wa uchaguzi mdogo wa udiwani kata ya Matevezi jimbo la Arumeru Magharibi,kupaza sauti wakimuuliza juu ya hatima ya mbunge wao Lema ambaye yupo Gereza la kisongo kwa miezi miwili sasa.
 
Katika hatua nyingine, Lowassa  aliwataka timu ya kampeni na wananchi kuhakikisha kura haziibiwi kwa kile alichoeleza kuwa Chadema ina nguvu.

Wizara 7 Vitani Sakata la Uvuvi Haramu

$
0
0
Kukithiri kwa uvuvi haramu hasa wa kutumia mabomu kumesababisha mawaziri wa wizara saba kukutana ghafla ili kujadiliana namna ya kukabiliana na tatizo hilo. 

 Mawaziri hao ni January Makamba (Muungano na Mazingira ), Dk Charles Tizeba (Kilimo na Mifugo na Uvuvi), Dk Hussein Mwinyi (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa) na Mwigulu Nchemba (Mambo ya Ndani ya Nchi). Wengine ni Profesa Jumanne Maghembe (Maliasili na Utalii) na Seleman Jafo (Naibu Waziri wa Tamisemi) wakati Wizara ya Uchukuzi iliwakilishwa na katibu mkuu, Dk Leonard Chamulilo. 

Akizungumza na wanahabari jana baada ya kikao hicho, Makamba alisema lengo la mkutano huo lilikuwa ni kujadiliana namna ya kuchukua hatua za kukabiliana na uvuvi huo. 

Makamba ambaye alikuwa mwenyekiti wa kikao hicho, alisema Tanzania imebarikiwa kuwa na rasilimali za bahari na samaki, lakini zinaathiriwa na uvuvi haramu. 

“Tumejadiliana kwa kirefu na tumetafakari hatua za kuchukua ili kukomesha tabia hii. Kikao kilikuwa cha kazi, mikakati na mbinu za kukabiliana na watu wanaofanya uvuvi haramu,” alisema Makamba. 

Hata hivyo, hakuwa tayari kuzitaja hatua walizokubaliana na mawaziri wenzake badala yake alisema taarifa kwa kina itatolewa siku zijazo. 

Kwa mujibu wa Makamba, baada ya miezi sita mawaziri hao watakutana na kupeana mrejesho wa kujua hatua walizokubaliana zimefanikiwa kwa kiwango gani. 

“Shughuli hii ni vita, lazima tupambane. Nguvu ya Serikali iliyopo hapa (mawaziri) itawashukia wahusika pasipo kujua,” alisema Makamba. 


Dk Tizeba alisema mazingira ya bahari yanazidi kuharibika na kwamba asilimia 40 ya matumbawe ya samaki yameathiriwa na uvuvi huo. 

“Lazima tuchukue hatua madhubuti kukomesha uvuvi haramu. Tumejipangia hatua za muda mrefu na mfupi katika hili,” alisema. 

Waziri huyo aliongeza kuwa Tanzania ndiyo nchi iliyobaki na aibu ya kuvua samaki kwa kutumia milipuko ya mabomu, jambo linaloiletea sifa mbaya. 

Nchemba alieleza kuwa kila Mtanzania ana wajibu wa kushirikiana na Serikali kukomesha vitendo hivyo kwa kutoa taarifa kwenye vyombo vya dola. 

“Wafichueni wote wanaofanya vitendo hivi na motisha ipo kwa mtoa taarifa,” alisema Nchemba.

Mwanza: RC John Mongella akumbana na vilio vya njaa Sumve

$
0
0
Wakazi zaidi ya 300 wa Kata ya Mwagi wakiongozwa na mbunge wao wa Sumve, Richard Ndassa wamepokea msafara wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella kwa mabua ya mahindi mikononi mwao, kuashiria namna zao hilo lilivyoathiriwa na ukame.

Mongella ambaye alikuwa ameambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya hiyo, wakati wa ziara yake kukagua maendeleo ya kilimo wilayani hapa, alikutana na hali hiyo katika Kijiji cha Mwabilanda wakati akitokea Kijiji cha Manawa kukagua mashamba ya pamba.

Wakazi hao walisema wametekeleza wajibu wao, lakini ukame umevuruga malengo yao huku wakiomba msaada wapelekewe chakula haraka.

Awali, akiwa Kijiji cha Manawa wakazi wake walisimama barabarani kwa lengo la kutaka wapatiwe ufumbuzi wa namna Serikali ilivyojipanga kuwanusuru na njaa iliyosababishwa na ukame.

 “Kwa kweli hali yetu ya chakula hapa kijijini ni mbaya. Mimi na umri wangu sijawahi kushuhudia hali kama hii kwa zaidi ya miaka 40,” alisema mwenyekiti wa Serikali ya kijiji hicho, Joseph Nkonoki.

 Alifafanua kuwa baadhi ya wanaume wameanza kutelekeza familia zao kutokana na kukosa namna ya kupata fedha kwa ajili ya kununua chakula.

Akijibu malalamiko hayo Mongella alisema: “Timu ya mkoa itakutana na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya wiki ijayo ili kuandaa taarifa ambayo baadaye Serikali itaifanyia kazi.Matokeo yake mtayaona muda siyo mrefu.” 

Mongella aliwashauri wakazi hao kulima mazao yanayostahimili ukame katika kipindi hiki ambacho mvua zimekuwa za kusuasua.

Aliwataka kuwa na subira wakati Serikali ikiendelea kujipanga, huku akisema ukame unachangiwa na mabadiliko ya hali ya hewa.

 Pia, Mongella alimuagiza mkuu wa wilaya hiyo, Mtemi Simeon kuwakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria wananchi watakaobainika kukata miti bila kibali chake.

Tarime: Mkurugenzi Awatumbua Watumishi Wawili....Aapa Kumuwajibisha Yeyote Ataripotiwa wa Utovu wa Maadili

$
0
0
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Elias Ntiruhungwa amewasimamisha kazi watumishi wawili wa halmashauri hiyo mbele ya kikao kwa madai ya kushindwa kufuata maadili ya kazi.

Waliosimamisha kazi ni, Jeveryson Kaguna kwa madai ya kushindwa kuandaa taarifa za watumishi kwa wakati zilizokuwa zinahitajika Ofisi ya Rais, zikiwamo za kupandisha madaraja na ongezeko la mishahara.

Mwingine aliyesimamishwa ni muuguzi wa Hospitali ya Wilaya ya Tarime, Kegosa Nega kwa madai ya kuwatukana wagonjwa hospitalini, utoro kazini na ukaidi. 

Mkurugenzi huyo aliwasimamisha kazi katika kikao cha watumishi wa halmashauri alichokiitisha kwa ajili ya kuwakumbusha wajibu wao na kufuata maadili ya kazi.

“Kuanzia sasa ninamsimamisha kazi ofisa utumishi kwa uzembe wa kushindwa kuandaa taarifa iliyokuwa inahitajika Ofisi ya Rais mwezi uliopita. Tuliambiwa tuandae majina ya watumishi wanaotakiwa kupanda madaraja waongezewe mishahara na kueleza mahitaji ya watumishi.

“Lakini hajaandaa na nilikuwa namkazania kila mara sasa sijui kama watu watapandishwa madaraja maana muda umeisha taarifa hazijakwenda,” alisema.

Kuhusu kusimamishwa kazi kwa muuguzi, alisema alikaidi agizo la mkubwa wake wa kazi la kumsaidia mgonjwa aliyekuwa amebebwa kwenye kitanda kumsukuma kumpeleka wodini.

Alisema hospitali ya wilaya imekuwa ikilalamikiwa kuwa baadhi ya watumishi hutoa kauli chafu kwa wagonjwa na kupokea rushwa kutoka kwa wagonjwa. 

Alisema mtumishi yeyote atakayeripotiwa kwa vitendo vya uvunjifu wa maadili atamuwajibisha.

 “Mtu anakwenda kazini kwa muda anaotaka yeye halafu ni wa kwanza kutoka kazini,” alisema Ntiruhungwa. 

Mratibu Elimu Kata ya Nyamisangura, Emanuel Mwihechi alisema suala hilo la watumishi kupandishwa madaraja ni muhimu, lakini kwa halmashauri ya mji limekuwa ni kero kwa watumishi kucheleweshewa madaraja.

Katibu Tawala wa Wilaya ya Tarime, John Marwa aliwataka watumishi wote wa Serikali kutekeleza wajibu wao kwa kuzingatia sheria na taratibu za kazi ili kuepuka matatizo yanayoweza kuzuilika.

Kahama: Mkuu Wa Wilaya Awapiga Marufuku Walimu Kuzuia kuandikisha Wanafunzi Kisa Vyeti vya Kuzaliwa

$
0
0
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Fadhili Nkurlu amewapiga marufuku walimu wakuu wa shule za msingi na sekondari kuzuia kuandikisha wanafunzi wa kidato cha kwanza na darasa la kwanza hadi wawe na vyeti vya kuzaliwa. 

Nkurlu alitoa agizo hilo baada ya baadhi ya wazazi na wanafunzi kufika ofisini kwake kusaka vyeti na wengine kulalamika kitendo cha walimu kuwazuia kuanza kidato cha kwanza.

“Ni marufuku kwa mwalimu yeyote au kiongozi kuzuia wanafunzi kuandikisha kwa madai ya cheti cha kuzaliwa kama wanataka kujiridhisha wapate barua kutoka kwa mwenyekiti wa kitongoji au watendaji wa kijiji na siyo cheti hicho,” alisema Nkurlu.

Mmoja wa maofisa elimu kutoka Halmashauri ya Mji wa Kahama, Aruko Lukolela alisema agizo la mkuu wa wilaya litatekelezwa mara moja. 

Pwani: Bunduki Ya Kivita SMG Iliyokuwa Imeibiwa na Mfanyakazi wa Hifadhi ya Saadani Yakutwa Kichakani

$
0
0
Silaha ya kivita aina ya SMG na risasi 30 mali ya Hifadhi ya Taifa ya Saadani vimekutwa vimefichwa kwenye kichaka jirani na Mto Kitame katika Kata ya Makurunge wilayani Bagamoyo, Mkoa wa Pwani. 

Silaha hiyo inadaiwa iliibiwa kwenye Geti la Gama saa tisa usiku Desemba 24, mwaka jana wakati askari wa hifadhi hiyo, Jackson Shirima (23) akiwa kazini. 

Kamanda wa Polisi mkoani humo, Bonaventura Mushongi alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea muda mfupi baada ya askari huyo kutoka zamu ya lindo la geti hilo na kujipumzisha kwenye moja ya mahema akiwa na silaha hiyo. 

“Huyu askari alikuwa zamu na kama ilivyo ada huwa wanapokezana zamu ya ulinzi hivyo alitoka na silaha yake akaenda kujipumzisha kwenye hema maana hifadhini hutumia mahema na alipitiwa na usingizi na ndipo ilipoibiwa na mtuhumiwa aliyewahi kuwa mtumishi wa hifadhi hiyo,” alisema. 

Mushongi alibainisha kuwa baada ya wizi huo, askari kwa kushirikiana na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa) walianza msako na kupitia taarifa ya msamaria mwema walimkamata mtuhumiwa huyo, mkazi wa Tegeta Kibaoni ambaye alikwenda kuonyesha alipokuwa ameificha kichakani ikiwa na risasi 30. 

Mkuu wa hifadhi hiyo, Dk James Wakibara alisema wameshtushwa na tukio hilo kwani halijawahi kutokea na kwamba, zaidi ni baada ya kukuta mtuhumiwa huyo aliwahi kuwa mtumishi wao na aliacha kazi miezi kadhaa iliyopita yeye mwenyewe. 

Dk Wakibara alilishukuru Jeshi la Polisi kwa ushirikiano lilioutoa toka siku ilipoibiwa silaha hiyo hadi ilipopatikana.

Basi la Mohammed Trans Laua Watatu na Kujeruhi Watano Singida

$
0
0
Matukio ya ajali za barabarani yameendelea kuutikisa Mkoa wa Singida baada ya abiria 10 kupoteza maisha na wengine zaidi ya 30 kujeruhiwa ndani ya siku tisa. 

Desemba 30, mwaka jana katika Kijiji cha Tumuli Wilaya ya Iramba abiria watatu walikufa na wengine 25 kujeruhiwa na ajali nyingine ilitokea Januari Mosi katika Kijiji cha Kintukuntu wilaya humo na kuua abiria mmoja na kujeruhi watatu. 

Ajali nyingine iliyohusisha bajaji ilitokea jana  Januari 7 katika Barabara ya Mwankoko na  kumuua dereva na abiria wawili. 

Siku moja kabla ya tukio hilo, ajali ya basi la Mohammed Trans lililokuwa linatokea Tanga kwenda Shinyanga ilisababisha vifo vya abiria watatu na kujeruhi wengine watano wote wakiwa ni walimu. 

Akitoa taarifa ya ajali ya basi la Mohammed Trans jana, Kaimu Kamanda Polisi mkoani hapa, Mayala Towo alisema ilitokea Januari 6, saa nne usiku katika Kijiji cha Mseko wilayani Iramba. 

Kamanda huyo aliwataja waliofariki dunia kuwa ni Mussa Rajabu (55), Farahan Manyama (34) na John Tungaraza (39) wote wakiwa ni walimu, wakazi wa Geita. 

Pia, alisema majeruhi ambao pia ni walimu wamelazwa katika hospitali ya wilaya hiyo. 

Kamanda huyo aliongeza kuwa walimu hao walikuwa wametokea kwenye Chuo cha Eckenford mkoani Tanga walikokuwa wakichukua mafunzo mbalimbali. Alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa dereva. 

Towo alisema basi hilo lenye namba za usajili T 786 AWJ aina ya Scania lilikuwa linaendeshwa na Jovin Jackson (38), mkazi wa Shinyanga liligonga kwa nyuma lori lenye namba B.6705A lililokuwa likivuta tela B.0568A lililokuwa likienda Burundi. 

Akifafanua, alisema dereva wa basi alitaka kulipitia lori hilo, lakini alipogundua hataweza aliamua kurudi ghafla kushoto na mwendo kasi aliokuwa nao alijikuta analigonga lori hilo kwa nyuma. 

Towo alisema baada ya kusababisha ajali hiyo dereva alitoroka na kukimbilia kusikojulikana. Juhudi zinaendelea kumsaka ili afikishwe mahakamani.

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Jumatatu ya January 9

Viewing all 45270 articles
Browse latest View live




Latest Images