Quantcast
Channel: MPEKUZI
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live

Mkulima achomwa mkuki mdomoni, watokea shingoni

$
0
0
MKULIMA na mkazi wa kijiji cha Dodoma Isanga kata ya Masanze wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro, Augustino Mtitu,amechomwa mkuki mdomoni na kutokea shingoni.

Umemjeruhi hivyo kulazimika kukimbizwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, kufanyiwa upasuaji kuondoa mkuki huo na kuokoa maisha yake.

Mtitu na wengine wanane walijeruhiwa katika vurugu zilizohusisha jamii ya wafugaji wa Kimasai na wakulima wa kijiji hicho kilichopo wilayani Kilosa.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei alithibitisha kutokea kwa tukio hilo. Alisema mpaka jana watu watatu walikuwa wanashikiliwa na Polisi, na msako unaendelea kuwasaka wale wote waliohusika katika kufanya vurugu hizo.

Tukio hilo ni la Desemba 25, mwaka huu, baada ya mtu huyo kujaribu kuzuia vurugu hizo, zilizokuwa zimetokea baada ya wafugaji hao kulisha mifugo yao katika shamba la maharage na mahindi katika kijiji hicho.

Mtitu akijaribu kuzuia vurugu hizo, aliishia kuchomwa mkuki na mmoja wa wafugaji wa jamii hiyo, ambao baada ya tukio hilo walikimbia kutoka eneo hilo.

Kutokana na tukio hilo, wananchi wenzake waliamua kumkimbiza katika Hospitali ya Wilaya ya Kilosa kwa ajili ya matibabu.

Lakini, alihamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji na matibabu zaidi ya kuokoa maisha yake.

Baada ya kutokea kwa tukio hilo, muda mfupi baadaye wafugaji hao walirudi tena kijijini hapo, kwa lengo la kuokoa mifugo yao iliyokuwa imekamatwa, na ndipo walipoanzisha tena vurugu kwa kuwashambulia watu wengi wanane akiwemo Mwenyekiti wa Kijiji pamoja na wa Kitongoji.

Watu watano, kati ya waliojeruhiwa, walikimbizwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kilosa kupatiwa matibabu. Diwani wa Kata ya Masanze, Bakari Pilo, akizungumza kwa njia ya simu, alisema hilo ni tukio la tatu kutokea kwenye kata yake katika kipindi kifupi.

Alisema vitendo hivyo vinaendelea kuhatarisha usalama wa wananchi, hasa wakulima, kufuatia mamlaka zinazohusika kushindwa kuwahamishia wafugaji katika eneo walilokuwa wametengewa, licha ya suala hilo kupitishwa kwenye vikao vya Baraza la Madiwani.

Stanley Andrea, ambaye ni ndugu wa Mtitu, yupo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro akimuunguza nduguye, alisema kuwa tukio hilo ni la Desemba 25, mwaka huu majira ya saa 5 asubuhi kwenye mashamba ya wakulima baada ya wafugaji kuingiza mifugo kwenye mashamba ya mahindi na maharage ili kulisha mifugo.

Alisema, wakulima wenye mashamba hayo,waliamua kuifukuza mifugo hiyo, lakini wafugaji wa jamii ya Kimasai, waliingilia kati na kuanza kuwapiga kwa fimbo wakulima na kusababisha kutokea kwa vurugu baina ya pande mbili hizo.

Alisema, mfugaji mmoja wa Kimasai alichukua mkuki na kumchoma Mtitu sehemu ya mdomoni na kutokezea shingoni na kuwajeruhi wengine wanane, akiwemo Mwenyekiti wa Kijiji na wa Kitongoji, ambao baadhi wamelazwa Hospitali ya Wilaya ya Kilosa.

Alisema kuwa vurugu ziliongezeka, pale wafugaji hao waliporudi kijijini hapo kwa ajili ya kuikomboa mifugo yao iliyokuwa inashikiliwa, kabla ya kufika kwa askari polisi kutoka mjini Kilosa.

Muuguzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, Sanifa Mdee, alisema walimpokea mgonjwa huyo akiwa na mkuki mdomoni, ulitokea upande wa shingoni na kuanza kumpatia matibabu na kumtoa mkuki huo, ambapo amelazwa wodi namba moja hospitalini hapo.

Hata hivyo, alisema kutokana na mkuki huo kuchomwa kwa nguvu, ulijeruhi baadhi ya meno yake na kuharibu fizi, hali iliyosababisha jana madaktari kumfanyia upasuaji wa kurekebisha fizi zake, ambapo baada ya kutolewa mkuki huo, hali yake ilikuwa inaendelea vizuri.


Benki Kuu (BoT) yatolea ufafanuzi taarifa za kutotumika tena noti ya shilingi 500

$
0
0
Benki Kuu ya Tanzania inapenda kuwafahamisha wananchi wote kuwa habari inayoenea katika mitandao mbalimbali ya kijamii kwamba noti ya shilingi mia tano haitatumika tena baada ya Disemba 31, 2016 sio taarifa ya kweli na ni uvumi unaopaswa kupuuzwa.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Huduma za kibenki BoT, Marcian Kobello ambapo alifafanua kuwa noti ya shilingi 500 itaendelea kuwepo katika mzunguko sambamba na ile sarafu ya shilingi 500 hadi pale noti hiyo itakapotoweka mikononi mwa wananchi.

Aidha, Kobello amewataka wananchi kupuuza taarifa zinazoeleza vinginevyo kwani si za kweli.

Serikali iliamua kuleta sarafu ya TZS 500 baada ya kuwepo malalamiko kuwa noti ya TZS 500 ambayo ndiyo inazunguka zaidi inachakaa mapema sana.

Polisi Wapigwa Marufuku Kuvisha Mabango Madereva Walevi

$
0
0
Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga amesema wamesitisha kuwatangaza watuhumiwa katika mitandao ya kijamii  baada ya kupata malalamiko ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.

Hata hivyo, amesema hadi wanasitisha walikuwa wamewakamata  madereva 20 wa Dar es Salaam, lengo likiwa ni kuonyesha jamii ili wengine wenye tabia hiyo wajifunze kupitia kwa wenzao na kuacha kuendesha wakiwa wamelewa.

“Kwa sababu watu wengi wapo mtandaoni ilikuwa rahisi ujumbe kuwafikia kwa wakati mmoja. Tulipata malalamiko ya haki za binadamu kuwa kufanya hivyo kunawasababishia kudhalilika katika familia zao, tukaona tusitishe,” amesema Mpinga.

Hata hivyo, amesema pamoja na kusitisha utaratibu huo, madereva wasijisahau kwa sababu vijana wapo kazini na wanaendelea kuwakamata wale wote watakaokiuka sheria za barabarani, ikiwamo hiyo ya kuendesha wakiwa wamelewa.

Awali, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imelitaka Jeshi la Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani, kuacha kuziweka hadharani picha za madereva wanaotuhumiwa kukiuka sheria, badala yake liwafikishe mahakamani kwanza.

Kauli ya Tume hiyo imetokana na utaratibu ulioanzishwa na trafiki wa kuwavisha mabango madereva wanaotuhumiwa kukiuka sheria ambayo yameandikwa makosa yao na kurushwa kwenye mitandao ya kijamii kabla hawajafikishwa mahakamani.

Mwenyekiti wa Tume hiyo, Bahame Nyanduga amesema hayo wakati akifafanua kuhusu kusitisha kuwaanika katika mitandao ya kijamii madereva wanaokamatwa na trafiki kwa makosa ya usalama barabarani ikiwamo ulevi

Moto wateketeza nyumba 50 wamiliki wake wakila Krismasi

$
0
0
MOTO mkubwa umezuka na kuteketeza nyumba zaidi ya 50 katika kisiwa cha Kasalazi kilichopo kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Buchosa mkoani Mwanza.

Tukio hilo lilitokea juzi saa 3:00 usiku, linadaiwa kuwa ni la nne kutokea kisiwani humo katika miaka ya karibuni.

Imeelezwa kuwa moto huo ulizuka na kuteketeza nyumba hizo huku wamiliki wake wakiwa kwenye shamra shamra za Krismasi.

Nyumba zilizoteketea kwa moto ni zile zilizojengwa kwa kutumia mabanzi ya miti, mbao na kuezekwa kwa maturubai, nyasi na baadhi kwa bati.Chanzo cha moto huo bado hakijafahamika.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kasalazi, Andrew Mkama, amesema  kuwa wakati tukio hilo linatokea, wakazi wengi wa kisiwa hicho walikuwa kwenye kumbi mbalimbali za starehe kusherehekea kuzaliwa kwa Yesu Kristo zaidi ya miaka 2,000 iliyopita.

Mkama alisema alilazimika kupuliza filimbi kuashiria hatari na wananchi walijitokeza na kuanza jitihada za kuuzima moto huo licha ya kwamba tayari ulikuwa umeshasababisha madhara makubwa kwa kuunguza mali zote zilizokuwa ndani yake.
 
Hata hivyo alisema hakuna mtu aliyekufa wala kujeruhiwa kutokana na janga hilo.

Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo, walisema moto huo umesababisha hasara kubwa kwao.

Mmoja wa mashuhuda hao, Raphael Bituro, anayemiliki duka la vinywaji, alisema baada ya kupulizwa filimbi kuashiria hali ya hatari, baadhi ya wateja wake walikurupuka bila kulipia vinywaji vyao na hivyo kusababisha apate hasara.

Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Emmanuel Kipole, alithibitisha kisiwa hicho kuungua kwa moto.

Kipole alisema ameagiza kufanyika kwa uchunguzi ili kubaini ukubwa wa madhara hayo na kuahidi kutoa taarifa zaidi atakapopewa ripoti hiyo.

Kisiwa hicho kinakadiriwa kuwa na wakazi zaidi ya 2,400 ambao hujihusisha na shughuli za uvuvi na ni miongoni mwa visiwa vinane vilivyopo kwenye Kata ya Bulyaheke wilayani Sengerema.

Hili ni ombi la Rais Magufuli kwa Watanzania mwaka 2017

$
0
0
Rais wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli amewaomba Watanzania wote kuutunza na kuudumisha umoja katika mwaka 2017 huku akiwataka kufanya kazi kwa bidii.

Rais Magufuli amendika maombi hayo kupitia ukurasa wake wa Twitter ambapo pamoja na kuwaomba Watanzania kutekeleza mambo hayo amewatakiwa Watanzania heri ya mwaka mpya.

“Ombi langu kwa Watanzania wote tuulinde,tuutunze na kuudumisha umoja wetu ktk mwaka 2017 kwa kufanya kazi kwa bidii. MUNGU IBARIKI TANZANIA,” ameandika Rais Magufuli.

Aunty Ezekiel : Siwezi tena 'ku-kiss' Kwenye Movie

$
0
0
Star wa Bongo Movie nchini mwanadada Aunty Ezekiel, amerudi upya kwenye tasnia hiyo huku akiweka wazi baadhi ya mabadiliko aliyoyafanya katika maisha yake kuwa ni pamoja na kutoweza tena 'ku-kiss' kwenye movie atakazocheza.

Aunty ambaye kwa sasa amerejea na movie mpya inayokwenda kwa jina la Chritmass Eve, amesema kilichomfanya afikie maamuzi hayo ni majukumu aliyonayo kwa sasa ya kifamilia ikiwa ni pamoja na malezi ya mtoto.

Akiwa kwenye kipindi cha FNL cha EATV Aunty amesema kuanzia sasa akiwa kwenye movie, kabla hajakubali ku-kiss na mtu kwanza anamkumbuka mtoto wake huku akitaja mabadiliko mengine kuwa ni kuweza kuigiza kama 'house girl' uhusika ambao awali aliwahi kusema hawezi kuuigiza.

"Nimechenji baada ya kuzaa, nimekuwa na mawazo tofauti, nimerudi nyuma mara mbili hata ikitokea kwenye movie natakiwa ku-kiss, najifikiria sana hivi mwanangu akiona atafikiria nini" Alisema

Amesema hivi sasa amebadilika kwa kuwa amekuwa mtu mzima na kusisitiza kuwa kwa sasa ameacha mabo yote ya kitoto aliyokuwa akiyafanya ikiwemo kuishi kwa skendo maana ameona hayana faida.

Katika hatua nyingine Aunt alisema anatarajia kupata mtoto wa pili ambaye angependa awe wa kike

Majina ya waliokuwa wamefaulu katika usaili wa ajira serikalini, kufutwa.

$
0
0
Watu wote waliokuwa wamefanya usaili kwa ajili ya ajira serikalini kupitia Sekretarieti ya Ajira ya Utumishi wa Umma kabla ya ajira kusimamishwa, watafutwa ndani ya miezi 6 na kulazimika kuomba upya kipindi ajira hizo zitakapotangazwa tena.

Hilo limebainishwa na sekretarieti hiyo kupitia majibu kwa wadau mbalimbali kwa mwezi Desemba ambao wamekuwa wakiuliza maswali na kujibiwa kila mwezi kupitia tovuti yake, na kubainisha kuwa suala hilo litawahusu wale ambao walifaulu usaili lakini kabla hawajapangiwa vituo vya kazi au kupewa barua na waajiri wao, ajira zikasimamishwa ili kupisha uhakiki wa watumishi hewa.

Taarifa hiyo imesema kuwa huo ni utaratibu wa kawaida wa sekretarieti hiyo, kwamba majina ya waliofaulu huhifadhiwa kwenye kanzi data (Database) kwa muda usiozidi miezi sita, na baada ya hapo majina hayo hufutwa.

"Kwa mujibu wa Taratibu zetu za uendeshaji wa mchakato wa ajira majina ya waombaji kazi waliofaulu lakini hawakupangiwa vituo vya kazi kwa sasa huhifadhiwa kwenye kanzi data kwa muda usiozidi miezi sita" Imesema taarifa hiyo

Swali lingine kutoka kwa mdau na jibu lake liko kama ifuatavyo:-
Kwa kuwa ajira zilisitishwa mwezi Juni, na sasa ni mwezi Desemba, utaratibu huo unamaanisha kuwa wasailiwa wote waliofaulu lakini hawakupangiwa kazi, watalazimika kusubiri upya matangazo ili waombe upya na kufanya usaili upya.

Aidha Sekretariet hiyo imebainisha kuwa zoezi ya uhakiki wa watumishi hewa bado linaendelea, na kwamba wakipewa ruhusa ya kutangaza ajira wakati wowote watatangaza.

Mbunge Wa Kigoma Mjini Zitto Kabwe Na Mkewe Wapata Mtoto Wa Kike.

$
0
0
July 14, 2016 Mbunge wa Kigoma mjini, Zitto Kabwe aliuacha  rasmi ukapera baada ya kufunga ndoa na mpenzi wake. Leo December 27 2016 Zitto Kabwe na mkewe wamepata mtoto wa kike ambaye wamempa jina la Josina – Umm Kulthum.

Zitto Kabwe amezitoa taarifa hizo kwenye mitandao ya kijamii.
 
Ameandika:''Mimi na Mke wangu mpendwa tumebarikiwa na Allah kupata mtoto wa kike. Mtoto na mama yake wana afya njema kabisa, Mashaallah. Mtoto amezaliwa saa moja na dakika 45 asubuhi leo Disemba 27, 2016''''.
 
''Binti yetu ataitwa Josina - Umm Kulthum. Josina kwa heshima ya mwanamama mpigania Uhuru wa Kusini mwa Afrika, Josina Muthembi Machel wa FRELIMO. Umm Kulthum kwa heshima ya mama yangu mdogo na pia jina la binti wa Mtume Muhammad (SAW)''
 
''Tunamshukuru mungu kwa Baraka hizi za mtoto Josina - Umm Kulthum Zitto''


Huddah Monroe aeleza sababu ya kuitosa Wasafi Beach Party ya Diamond

$
0
0
Wasafi Beach Party iliyofanyika Disemba 24, Jangwani Sea Breezy jijini Dar es Salaam, ilikuwa iwakutanishe mahasimu warembo Huddah Monroe na Vera Sidika jukwaani kama mahost.

Wengi tulikuwa tukisubiri kushuhudia drama ya kufungia mwaka kutoka kwa warembo hao wa Kenya, lakini bahati mbaya fahari mmoja hakutokea. 

Huddah Monroe ametumia Snapchat kuelezea sababu iliyomfanya ashindwe kuja kwenye party hiyo kuwa ni kushindwa kufikia makubaliano waliyokuwa wamejipangia na Diamond na hivyo ikamlazimu kukatisha kuja katika dakika za mwisho.
Hata hivyo Vera na mrembo mwingine wa Uganda, Anita Fabiola walikuwepo na kila kitu kilienda freshhh…

Picha za Ray C akiwa ndani ya muonekano mpya wa kihindi

$
0
0
Huenda huu ukawa ndio ujio mpya wa msanii mkongwe wa muziki wa bongofleva Rehema Chalamika aka Ray C baada ya misukosuko ya hapa na pale katika maisha yake ya muziki.

Muimbaji huyo ambaye amedaiwa kuweza kuachana na matumizi ya Madawa ya kulevya baada ya kushindwa kwa muda mrefu,wiki chache zilizopita aliweka kambi ndani ya studio ya Wanene kwa ajili ya maandalizi ya ujio wake mpya.

Wiki hii amepiga picha zake mpya zinazomuonyesha akiwa na muonekano wa kihindi. Angalia picha.

Mwanafunzi Ajeruhiwa Na Risasi Kichwani Na Walinzi Wa Kampuni Ya Kifaru Jijini Arusha

$
0
0
Mwanafunzi wa kidato cha pili wa shule ya sekondari Mringa, Vanessa Josephat [16] mkazi wa Sakina jijini hapa amejeruhiwa vibaya kwa kupigwa risasi kichwani na walinzi wa kampuni ya ulinzi ya kifaru waliokuwa wakiwatoa kwa nguvu kwenye nyumba yao yenye mgogoro .

Tukio hilo limethibitishwa na kamanda wa jeshi la polisi mkoani Arusha Charles Mkumbo ambaye alisema kuwa polisi inamshikilia Fabian Charles mlinzi wa kampuni ya kifaru pamoja na silaha aina ya shoot gun iliyo tumika katika tukio hilo huku majeruhi amelazwa katika hospitali ya KCMC kutokana na hali yake kuwa mbaya .

Kamanda mkumbo alisema kuwa tukio hilo limetokea jana majira ya saa tatu asubuhi katika eneo la sakina jijini hapa, ambapo alisema walinzi watatu wa kampuni hiyo waliokuwa wakilinda nyumba hiyo inayomilikiwa na Josephat Nehemia walitumia silaha hiyo kuwafyatulia familia inayoishi hapo ili waondoke na ndipo silaha hiyo ilipomjeruhi mwanafunzi huyo .

Taarifa zinaeleza kuwa December 21 mwaka huu kampuni ya udalali ya Marc Recorders Limited wakiwa na mabaunsa na watu wengine walivamia nyumba hiyo na kuwatoa nje wamiliki wa nyumba hiyo na kuondoka na vyombo vyao vya ndani wakidai nyumba hiyo imeshauzwa kwa , Thobias Ludovick Senya baada ya mmiliki kushindwa kulipa deni la shilingi million 3.7 alilokuwa akidaiwa na taasiai ya fedha Heritage.

Baada ya tukio hilo familia hiyo yenye watu wapatao kumi wakiwemo watoto na kichanga walianza kulala nje kando ya geti la nyumba hiyo wakipigwa na baridi kali pasipo kuwa na msaada wowote

Mmiliki wa nyumba hiyo Josephat Nehemia Ogaga alisema baada ya familia yake kutolewa nje wakati yeye akiwa safarini walikuja walinzi hao wa kampuni ya kifaru na kuanza kulinda na baada ya yeye kurejea alifanikiwa kuwaondoa walinzi hao na kuirejesha ndani familia yake akidai taratibu za kuuza nyumba yake hazikufuatwa ila kilichofanyika ni uhuni .

“Nikweli nilikuwa nadaiwa na Heritage financial shilingi milioni 3 .7 na nililipa deni na kubaki shilingi million 1.8 hivyo hatua ya kuja kuuza nyumba yangu yenye thamani shilingi million 200 kwa deni hilo ni uhuni mtupu umefanyika” alisema Nehemia

Hata hivyo siku moja baadae walinzi hao walirejea tena wakiwa na silaha za moto na kuanza kufyatua risasi ovyo ndani ya nyumba hiyo kwa lengo la kuwatisha familia hiyo ili waondoke ndani ya nyumba hiyo ambapo moja ya risasi ilimjeruhi mwanafunzi huyo kichwani ambaye amelazwa katika hospitali ya rufaa ya KCMC Mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya matibabu

Kamanda Mkumbo amezitaka kampuni za ulinzi kutoingilia migogoro bila kufuata utaratibu kwani vyombo vyenye mamlaka ya kushughulikia migogoro kama hiyo vipo na hivyo amezitaka kampuni za ulinzi kufuata taratibu zao za utendaji wa kazi na kuacha kukimbilia maslahi yao ya kupata fedha haraka,

Mkumbo alisema mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kujibu shitaka linalomkabili.

Waziri Mahiga apokea Dola elf 50,000 kwa ajili ya Waathirika wa Kagera

$
0
0
Serikali ya Jamhuri ya Korea imetoa msaada wa Dola za Marekani elf 50,000 takribani milioni 108 kwa fedha za Tanzania kwa ajili ya waathirika wa tetemeko la ardhi lilitokea mkoani Kagera mwezi Septemba 2016.

Msaada huo ulikabidhiwa leo jijini Dar es Salaam na Balozi wa Korea nchini Tanzania, Mhe. Song Geum Young na kupokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga (Mb) kwa niaba ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa (Mb).

Baada ya kupokea msaada huo, Dkt. Mahiga aliishukuru Serikali ya Korea na kuahidi kuwa msaada huo ataukabidhi kwa Mhe. Waziri Mkuu ili uweze kutumika kama ulivyokusudiwa.

Mhe. Mahiga alisema kuwa Korea imekuwa mbia mkubwa wa Tanzania tokea nchi hiyo ilipoanzisha mahusiano ya kidiplomasia na Tanznaia miaka 25 iliyopita. Alieleza kuwa katika kipindi hicho Tanzania imekuwa ikipokea misaada mbalimbali ya kiuchumi, kijamii na ya kibinadamu ukiwemo huu wa leo ulioelekezwa kwa waathirika wa tetemeko la ardhi la mkoani Kagera.

Mhe. Waziri alitaja misaada ambayo Korea imeipatia Tanzania ni pamoja na ujenzi wa daraja la Malagarasi mkoani Kigoma, ujenzi wa hospitali ya kisasa ya Mloganzila na ujenzi wa hospitali ya uchunguzi wa afya ya Mama iliyopo Chanika. Aidha, Korea hivi karibuni itaanza ujenzi wa daraja la Selander ambalo linatarajiwa kuanzia ufukwe wa Coco, Oysterbay hadi maeneo ya hospitali ya Aga Khan, Upanga jijini Dar es Salaam.

Waziri Mahiga alibainisha pia kuwa Jamhuri ya Korea itatoa msaada mkubwa zaidi wa maendeleo kwa Tanzania kuliko nchi yeyote ya Afrika. Taarifa hiyo ilitolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea, Mhe. Yun Byung-se alipofanya naye mazungumzo kando ya Mkutano wa nchi za Afrika na Korea uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia tarehe 06 na 07 Desemba 2016.

Kwa upande wake, Balozi wa Korea nchini aliahidi kuwa nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania hususan kutoa atia misaada ya maendeleo ili iweze kutimiza azima ya Serikali ya awamu ya tano ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda.

Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 27 Desemba 2016.

Waziri Mkuu: Waliofaulu Ni Lazima Waende Sekondari

$
0
0
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali haitavumilia kuona mamia ya vijana waliofaulu mitihani ya darasa la saba na kuchaguliwa kuingia kidato cha kwanza wanabaki nyumbani eti kwa kuwa hakuna madarasa ya kutosha.

“Serikali haitaridhika kuona vijana waliofaulu vizuri wanashindwa kwenda kidato cha kwanza. Halmashauri zilijua tangu mapema ni wanafunzi wanaenda shule za msingi kwa hiyo inataka kuona wote waliofaulu wanakwenda sekondari kwa asilimia 100,” amesema.

Ametoa kauli hiyo jana  mchana wakati akizungumza na viongozi na watendaji wa mkoa wa Lndi mara baada ya kupokea taarifa ya mkoa huo kwenye Ikulu ndogo wilayani Nachingwea. Waziri Mkuu amewasili wilayani Nachingwea akiwa njiani kuelekea Ruangwa kwa mapunziko ya mwisho wa mwaka.

Alisema Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kutoa elimu ya bure kwa kila mtoto sasa iweje watoto wengine wanafaulu na wanashindwa kujiunga na elimu ya sekondari. 

“Tumesema elimu ni bure hakuna sababu ya kufanya wengine wasiende shule wakati azma ya Serikali ni kutoa elimu ya bure. Hakikisheni wote wanaingia katika chaguo la kwanza,” alisema.

Aliwataka Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri ambazo zimefaulisha wanafunzi lakini hazina madarasa na madawati ya kutosha warudi mezani na kujipanga upya ili kuhakikisha wanafunzi wote waliofaulu wanapangwa na kuanza na wenzao katika chaguo la kwanza kwani wakisubiri chaguo la pili wanakuwa wamechelewa.

“Kama tumepokea vijana wengi kwenye udahili wa kidato cha kwanza, ni dhahiri kuwa ,tutapata Vijana wengi watakaomaliza kidato cha nne. Sote tunajua kuna agizo la kila tarafa kuwa na sekondari moja ya kidato cha tano na sita, nataka utekelezaji wa agizo hili usimamiwe kuanzia sasa.”

“Tafuteni moja kati ya shule kwenye tarafa zenu na ipandishwe hadhi kwa kuwekewa miundombinu inayotakiwa ya bwalo, jiko, mabweni, mifumo ya maji, madarasa na vyoo vya kutosha,” alisema.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alisema atafuatilia ili abaini ni kwa nini taasisi ya maghala ya Serikali inadai tozo kwa wakulima wanaohifadhi mazao kwenye maghala hayo.

Waziri Mkuu alisema atapitia sheria ya kuanzishwa kwa taasisi hiyo ili kuona kama inaruhusu tozo hizo na kuangalia sheria gani inawaruhusu kutoza kodi. Alihoji inakuwaje taasisi ya Serikali inatoza tozo kwenye maghala ambayo yamejengwa na wananchi.

Akitoa mfano kuhusu ghala la Liwale, Waziri Mkuu alisema: “Kuna viagency vimeanzishwa kazi yao ni kutoza mapato tu. Inakuwaje kunakuwa na taasisi imekaa tu na kuanza kutoza tozo kwa wananchi wanaotumia facility za Serikali. Sheria ya kutoza tozo imetokana na nini na hizo zinakwenda kwa nani, je srikali imeanza kufanya biashara?,” alihoji.

“Nimepata taarifa kuwa walikuja kuzuia mazao yasitoke hadi wao walipwe, hapana huu siyo utaratibu. Ni kwa nini tuwanyang’anye fedha wale waliojenga ghala? Wao walijenga ghala kutokana na ubunifu halafu unasema unawapa sh. 7/- kwa kilo wakati wewe umetoza sh.25/- kwa kilo moja. Hapana hilo halikubaliki,” alisisitiza.

Waziri Mkuu alisema kama Serikali inaruhusu kuwepo kwa tozo hizo kwa jambo ambalo wananchi wamelibuni wenyewe, basi ilipaswa kudai kodi na hiyo kodi ilitakiwa kukusanywa na Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) na siyo vinginevyo.

Waziri Mkuu alisema atafuatilia wakala mbalimbali walioanzishwa kwenye wizara kwani kuna nyingine zinafanya kazi ambazo zilistathili kufanywa na idara kwenye wizara mama.
    
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU

Malipo ya Korosho: Waziri Mkuu Awasha Moto.....Ataka Majibu Kucheleweshwa kwa Malipo ya Wakulima

$
0
0
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema atamuita Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho, Bw. Hassan Jarufo ili aje amueleze ni kwa nini wakulima wa zao hilo wanacheleweshewa malipo yao kinyume na maagizo ya Serikali.

Ametoa kauli hiyo jana mchana wakati akizungumza na viongozi na watendaji wa mkoa wa Lndi mara baada ya kupokea taarifa ya mkoa huo kwenye Ikulu ndogo wilayani Nachingwea. Waziri Mkuu amewasili wilayani Nachingwea akiwa njiani kuelekea Ruangwa kwa mapumziko ya mwisho wa mwaka.

“Niliagiza wanunuzi waje na bond (dhamana ya mauzo), waziweke benki ndipo waingizwe kwenye mnada. Kwa maana hiyo mnada ukimalizika, benki inakata fedha husika na kuingiza kwenye chama cha wakulima.”

“Hapa tatizo ni kwamba hatukusimamia vizuri zuala hili. Tulipaswa tujiridhishishe kwanza kama mnunuzi amelipa fedha benki. Tatizo la biashara hii watu wengi ni madalali, wanaangalia hali ikoje na wakibaini kuna cha juu, ndiyo anaagiza na kuamua kuja kulipa. Kama angekuwa amelipa benki, ile hela ya awali ingekatwa katika fedha ya dhamana aliyokwishaitoa,” alisisitiza.

Oktoba 16, 2016 wakati akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja cha Sokoine wilayani Nachingwea, mkoani Lindi, Waziri Mkuu alisema alishatoa maelekezo tangu Aprili, mwaka huu kwamba wanunuzi wa korosho ni lazima watoe asilimia 25 ya malipo wanayotaka ili kuepuka tatizo la madalali kuingilia kati biashara hiyo.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Bw. Godfrey Zambi na Wakuu wote wa wilaya za mkoa huo wawahimize wakulima wapande miche mipya ya korosho kwa sababu mikorosho iliyopo imezeeka na haitoi mazao ya kutosha.

“Mnatakiwa muwahimize wananchi wapande miche mipya mara tu mvua zitakapoanza ili ianze kukua wakati wakusubiria kung’oa ile ya zamani. Nimeambiwa korosho bora hazipaswi kuzidi punje 190 ili zijae kwenye kilo  moja. Ubora wa miti ya korosho ukishuka na idadi ya punje pia inapungua,” alisema.

Alisema kigezo kikuu cha ununuzi wa korosho hivi sasa ni idadi ya punje na kwa Ruangwa na Nachingwea, idadi inakuwa kubwa kwa sababu punje zake ni ndogo. “Wenzetu wa Tandahimba walipanda miche mipya tangu miaka minne iliyopita kwa hiyo sasa hivi wanavuna korosho zenye ubora,” ameongeza.

Alimpongeza Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. Charles Tizeba kwa uamuzi wake wa kuvunja mfuko wa wakfu wa korosho (CIDTF) na akamtaka afute mifuko kama hiyo kwenye mazao mengine kama katani, chai na kahawa kwani inafanya kazi ambazo zinaweza kufanywa na bodi za mazao hayo.

“Waziri Tizeba alishaanza na zao la pamba, sasa aende kwenye mazao mengine ili fedha ambazo watu wa mfuko huu walikuwa wakizitumia kulipana posho tu, sasa ziende kwenye bodi kuhamasisha wakulima walime zaidi na ikibidi wapewe hata mashine za kupulizia dawa,” aliongeza.

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Jumatano ya Disemba 28


Auawa Kwa Kuchomwa Kisu Wakati Wakigombea Soda

$
0
0
JESHI la Polisi Mkoa wa Arusha linamshikilia mkazi wa Olasiti, jijini Arusha, Hamisi Amani (17), kwa tuhuma za kumuua mwenzake wakati wakigombea soda.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, tukio hilo lilitokea Desemba 25, mwaka huu, saa mbili usiku katika eneo la Kwa Morombo.

Kamanda Mkumbo alimtaja marehemu kuwa ni Novatus Tadei (26), mkazi wa Kwa Morombo na kwamba aliuawa kwa kuchomwa kisu kifuani upande wa kushoto.

“Marehemu na mtuhumiwa walikuwa wapishi kwenye kampuni inayojulikana kwa jina la ZZ Catering inayomilikiwa na Bashiri Ally.

“Siku ya tukio, marehemu pamoja na wafanyakazi wengine, akiwamo mtuhumiwa, baada ya kumaliza kazi waliyokuwa wanafanya, walipanda gari lenye namba za usajili T 375 CHH, aina ya Toyota Hiace wakirejea nyumbani.

“Wakiwa ndani ya gari hilo, mtuhumiwa Hamis aligundua kuwa soda aliyokuwa ameiweka ndani ya begi lake, haipo na kuanza kuhisi marehemu ndiye aliyeichukua.

“Kwa hiyo, ulizuka ugomvi baina yao na kuanza kutukanana matusi. Wakati ugomvi huo ukiendelea, mtuhumiwa alimkaba marehemu na kuchukua kisu wanachotumia kwenye shughuli zao za mapishi kilichokuwa ndani ya vyombo na kumchoma kifuani.

“Baada ya kuchomwa kisu, Tadei alianguka chini na jitihada za wafanyakazi wenzake waliokuwamo ndani ya gari hilo kuokoa maisha yake zilishindikana, kwani alifariki wakati anapelekwa hospitali kwa ajili ya matibabu,” alisema Kamanda Mkumbo.

Alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru na mtuhumiwa atafikishwa mahakamani wakati wowote baada ya uchunguzi kukamilika.

Agizo la Rais Magufuli kwa Serikali ya mkoa wa Singida laanza kufanyiwa kazi

$
0
0
Na Nathaniel Limu, Singida.
Serikali mkoani Singida, inatarajia kujenga kiwanja kikubwa cha ndege kitakachowezesha ndege kubwa za abiria na mizigo kutua, ikiwa ni maandalizi ya kunufaika na fursa lukuki za kiuchumi na kijamii zitakazopatikana,baada ya makao makuu ya nchi kuhamia jirani Dodoma.

Hayo yamesemwa na mkuu wa mkoa wa Singida, Dk.Rehema Nchimbi wakati akizungumza kwa mara ya kwanza na waandishi wa habari ofisini kwake.

Alisema wakati wo wote kuanzia sasa kazi ya kutafuta eneo la kujenga kiwanja hicho na taratibu zingine muhimu, zitaanza,na amewataka wananchi wawe tayari kutoa ushirikiano.

“Msukumo wa ujenzi wa kiwanja kikubwa cha ndege,umekuja baada ya rais Dk.Magufuli kuutaka uongozi wa mkoa kuangalia uwezekano wa kujenga kiwanja hicho. Ushauri au mapendekezo yanayotolewa na mkuu wananchi, hayo ni maagizo rasmi, kwa hiyo sisi tulio chini yake, tutajitahidi uwanja huo unajengwa haraka,” alisema na kuongeza.

“Maadamu Rais ameona umuhimu wa uwanja huo na yeye katika serikali yake,anao uwezo mzuri wa fedha,sisi wakazi wa mkoa wa Singida tunachopaswa kufanya,ni kuchangamkia haraka uwanja unapatikana na ujenzi unaanza.”

Akifafanua, alisema serikali ya awamu ya tano imelenga nchi kuwa kwenye uchumi wa kati, hivyo kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi inayochochea ukuaji wa uchumi, huwa haina kigugumizi katika kutoa fedha.

Akiijengea nguvu hoja yake hiyo, mkuu huyo wa mkoa, alisema hatapenda kuona aina yo yote ya urasimu wa kuchelewesha ujenzi wa uwanja mkubwa wa ndege.

Kwa upande wa wananchi, amewataka watoe ushirikiano wa hali ya juu katika upatikanaji wa uwanja na ushirikiano huo usiishie hapo, uendelee hadi hapo kiwanja kitakapomalizika kujengwa.

“Mimi nitumie fursa hii kuwasihi wananchi katika hili la ujenzi wa uwanja wa ndege mkubwa, walipe kipaumbele cha kwanza na fidia wawe na subira. Waamini tu kwamba ni lazima watafidiwa. Nina uhakika kiwanja kitakapoanza kufanya kazi, wananchi watanufaika kiuchumi kwa kiwango kikubwa, na pengine watatanza kusema kiwanja hicho kimechelewa kujengwa,” alisema Dk. Nchimbi.

Katika hatua nyingi, alisema Serikali yake itafanya juhudi za kuhakikisha mkoa wa Singida, una kuwa wa viwanda vikubwa, ili kutoa nafasi makao makuu ya nchi Dodoma, kupumua na kujikita zaidi kwenye shughuli ya kuiongoza nchi.

“Pia nitahakikisha mkoa wangu unakuwa na uwezo wa kujilisha na kulisha makao makuu ya nchi. Tuna kila sababu ya kulifikia lengo hilo. Tutahimiza kilimo cha umwagiliaji na kuchimba mabwawa makubwa kwa ajili ya kilimo cha malisho ya mifugo,” alisema.

Ridhiwani Kikwete, Joseph Haule Walaani Kitendo cha Mkulima Kuchomwa Mkuki Mdomoni na Wafugaji

$
0
0
Wabunge  wa Mikumi, Joseph Haule na Chalinze, Ridhiwan Kikwete wamelaani kitendo kilichofanywa na jamii ya wafugaji kwa kujichukulia sheria mkononi na kumjeruhi kwa mkuki mkulima Augustine Mtitu.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, kuhusu tukio hilo lilitokea katika kijiji cha Upangwani, Masanze, Mikumi, wabunge hao waliezea kusikitishwa kwao na kutaka hatua zichukuliwe.

“Ni kitendo cha kusikitisha sana kwa hawa ndugu zetu wafugaji walijiamulia kufanya kitendo cha kinyama kama hiki, huu si ubinadamu kabisa,” alisema Haule.

Alisema mkulima huyo alichomwa mkuki na wafugaji wa Kimasai alipokuwa akimsaidia jirani yake kufukuza ng’ombe wasiharibu mazao shambani mwake.

Alisema Mwenyekiti wa Kijiji na Mwenyekiti wa Kitongoji nao walijeruhiwa na wafugaji hao. “Sisi Ofisi ya Mbunge wa Mikumi tunatoa mwito kwa Serikali kubaini waliofanya vitendo hivyo na kuwakamata ili kuvikomesha,” alisema Haule.

Alisema atashirikiana na Serikali kukomesha migogoro isiyokwisha kati ya wakulima na wafugaji Kilosa.

Ridhiwan naye alilaani vitendo hivyo na kuishauri Serikali kutafuta suluhu ya kudumu ya tatizo hilo.

“Ni lazima Serikali ije na majibu sahihi, ili kunusuru vita vya wenyewe kwa wenyewe visitokee kati ya jamii hizo. Si ajabu kusikia mtu kavunjwa mgongo, mwingine mlemavu, leo kapigwa mkuki wa midomo ukatokea shingoni, kilio hiki kipo katika masikio ya watu wengi kuhusu mapigano ya wakulima na wafugaji,” alisema.

Aliongeza:“Serikali isikie hili na kuchukua hatua stahiki ya kudhibiti kabla damu ya Watanzania wanyonge wanaotegemea kilimo kama kiinua mgongo chao hawajapotea. Kuna sheria na mipango ya matumizi bora ya ardhi, zitumike.”

Ridhiwan alisema jambo la msingi ambalo Serikali inatakiwa kujua ni kwamba hali ilivyo sasa, si ya kufanyia mzaha na waziri husika ayafanyie kazi.

Alisema binafsi analaani vitendo hivyo na kuiasa Serikali kujipanga vizuri kabla mambo hayajaharibika.“Yalianza Kilosa, Mvomero, Chalinze, Handeni, Kiteto na sasa Mikumi. Serikali jipangeni, kabla hapajachafuka,” alihadharisha.

Ushauri wa Zitto Kabwe Kwa Serikali Baada ya Kisa Hiki Alichokutana Nacho Hospitali Wakati Mkewe Akijufungua

$
0
0
Jana December 27 2016 mbunge wa kigoma mjini na kiongozi mkuu wa chama cha ACT Wazalendo Zitto Kabwe na mke wake wamepata mtoto wa kike ambaye wamempa jina la Josina – Umm Kulthum.

Zitto Kabwe kupitia ukurasa wake wa facebook amesimulia alichokutana nacho hospitalini saa chache kabla ya mke wake kujifungua, haya ni maneno yake….

"Usiku wa kuamkia tarehe 26 Desemba 2016 mke wangu alipata uchungu wa uzazi. Nikampeleka hospitali moja hapa Masaki. Hakuweza kujifungua siku hiyo bali tulikaa hospitali mpaka tarehe 27 Desemba, saa moja dk 45 asubuhi alipojifungua mtoto wetu wa kike Josina- Umm Kulthum.

"Masaa ya jioni tarehe 26/12/2016 nikiwa napiga soga na Naibu Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo Msafiri Mtemelwa na shemeji yangu mmoja mbele ya hospitali, wakaja watu 3. Watu hao mmoja mwanaume na wengine wanawake walikuwa na mtoto mdogo.

"Mwanaume huyu alikuwa amembeba mtoto akiwa na taharuki kubwa na mama mmoja mtu mzima na mwingine wa umri wa miaka 30 hivi walikuwa wakilia. Wakaingia hospitalini kwa kasi. Tukaambiana pale kuwa huyu binti atakuwa mahututi. Tukaendelea na soga.

"Mara kina mama wale wakatoka, wanapiga mayowe “mtoto hana damu” na ilitakiwa damu ya haraka Group A+. Wenzangu hawakuwa group hilo au group linaloweza kupeana damu. Mimi sikuwa najua/kukumbuka Group langu.

"Nikawaambia kina mama wale kuwa ngoja nijaribu kupima group langu na pia kuona kama damu yangu inaweza kuokoa maisha ya mtoto yule malaika za mungu. Nikaingia maabara nikapima. Baada ya dakika 10 Hivi nikaitwa kuambiwa damu yangu ni group sawa na mtoto yule na kwamba ni safi inafaa wanitoe muda ule ule ili kumuwahi mtoto. Nikatoa nusu lita muda ule ule.

"Baadaye nikaenda kumjulia Hali mtoto yule, nikaambiwa anaitwa Rahma. Ana umri wa miaka 2 na miezi 3. Nikawatakia kheri wazazi wake ( kumbe yule mwanaume ndie baba wa mtoto na msichana mama yake. Yule bi mkubwa nadhani ni bibi ya Rahma, sina hakika).

"Leo (Jana) asubuhi baada ya mke wangu kujifungua, nikaenda kumwona Rahma wodini. Nimemkuta anaendelea vizuri, anakula na kuongea. Mola ampe umri mrefu zaidi yeye na wazazi wake. Amwondolee maradhi na akue katika maadili mema ya dini. 

"Namshukuru mola kuniweka mahala sahihi na wakati sahihi hivyo kuweza kufanya ibada hii ya kumsaidia binti Rahma. Lau kama sikuwa nimechagua jina la binti yangu mapema, ningemwita Rahma. Hata hivyo inshallah Rahma atakuwa dada yake Umm Kulthum-Josina.

"Naishauri Serikali itengeneze kanuni za kuhakikisha kila hospitali inakuwa na akiba ya damu ya kutosha na mgonjwa mwenye kuhitaji apewe kwanza damu kabla ya kutafuta watu wa kuchangia kiwango husika.

"Juhudi za kuchangia damu kwa hiari ziongezeke kama tufanyavyo wanachama wa ACT Wazalendo ambao kila mwaka Wiki ya kwanza ya Mwezi Mei hujitolea damu kwa hiari kwenye hospitali za umma nchini kote.

"Aidha nimepata somo kubwa kwamba ni muhimu Sana kujua Group lako la damu na kuwa na kumbukumbu nalo kwani inaokoa muda pindi damu ikitakiwa kwa haraka. Sasa najua Group langu, ilikuwa ni makosa makubwa na uzembe wa hali ya juu kwangu kutojua ‘ blood group ‘ yangu. Nawasihi Watanzania wenzangu na mie msiojua blood group, mjue sasa kwani hatujui Siku wala Saa."

Tanzania yachunguza madai ya Malawi kuwakamata wapelelezi wake

$
0
0
Serikali inafanya uchunguzi kuhusu tuhuma zilizoripotiwa na vyombo vya habari vya Malawi kuwa vimewakamata ‘mashushu’ nane wa Tanzania wakijaribu kuingia kinyamela kwenye mgodi wa ‘uranium’.

Taarifa zilizoripotiwa na vyombo vya habari nchini humo juzi zimedai kuwa watu hao nane walikuwa wapelelezi na kwamba walitaka kuingia kwenye mgodi huo kujaribu kuchunguza kama nchi hiyo inatengeneza ‘nyuklia’ katika eneo la Kayerekera. Ripoti iliyowekwa kwenye mitandao mbalimbali ya Malawi pia imedai kuwa watu hao waliingia nchini humo bila kuwa na nyaraka za kusafiria.

Akizungumzia madai hayo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Augustine Mahiga jana alifanya mahojiano na The Citizen na kueleza kuwa hakuwa na taarifa hizo lakini atazifuatilia kwa kina na kufanya uchunguzi kwani ni tuhuma kubwa na nyeti.

“Ndio ninasikia hilo kwa mara ya kwanza kutoka kwako. Hizi ni tuhuma kubwa, nitafuatilia kwa kina leo (jana) jioni kwa kuwasiliana na ubalozi wetu wa Malawi kufahamu kama wanafahamu lolote kuhusu hili,” Dk. Mahiga anakaririwa.

Hata hivyo, tofauti na ripoti zilizotolewa kwenye vyombo vya habari vya Malawi, Msemaji Msaidizi wa Polisi wa eneo la Karonga, George Mlewa alikana ripoti hizo akidai kuwa watu hao nane waliokamatwa wanachukuliwa kama wahamiaji haramu tu.

“Wakati tunaendelea na uchunguzi wetu kuhusu suala hili, naweza kusema kuwa ripoti hizo ni uvumi tu,” alisema Mlewa.

Chanzo: The Citizen
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live




Latest Images