Quantcast
Channel: MPEKUZI
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live

Godbless Lema Akwama Tena Mahakamani Baada Ya Mawakili wa Serikali Kuweka Pingamizi .........Amerudishwa Rumande Hadi Disemba 2

$
0
0
Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema leo amefikishwa tena Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kwa ajili ya kusikiliza rufaa yake ya maombi ya dhamana.

Ulinzi ulikuwa umeimarishwa mahakamani hapo huku wafuasi wa Lema wakiwa  wamevaa fulana nyeupe zilizoandikwa Jutice 4 Lema mbele zikiwa na picha yake.

Mbele ya Jaji Fatma Masengi aliyekuwa  amepangwa kusikiliza Rufaa hiyo, Upande wa Jamhuri ambao ulikuwa ukiwakilishwa na mwanasheria Matenus J Marandu umeweka pingamizi kwamba mawakili wa Lema walipaswa kupeleka notisi ya rufaa kwanza na siyo kukata rufaa

Wakili wa Chadema Peter Kibatala amesema wao wameshakamilisha taratibu zote za kisheria, hivyo wanasubiri uamuzi wa pingamizi hilo lililowekwa na upande wa serikali.

Jaji Fatma Masengi ameutaka  upande wa serikali uwasilishe hoja za pingamizi lao  kwa njia ya maandishi kabla ya November 30 ili aweze kutolea uamuzi December 2 mwaka huu.
Ulinzi ukiwa umeimarishwa

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Jumanne ya Novemba 29

Wizara ya Elimu yakanusha taarifa ya wanafunzi wa Diploma kuzuiwa kujiunga vyuo vikuu

$
0
0
WIZARA ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi imetoa ufafanuzi kwamba haijapiga marufuku watu wenye Stashahada wenye sifa kujiunga na vyuo vikuu badala yake walichokataza ni wanafunzi waliofeli kidato cha nne na cha sita kujiunga na vyuo vikuu bila kuwa na vyeti vyenye sifa.

Aidha, imesema kwa waliomaliza kupitia mfumo huo na wapo kazini ni wajibu wa waajiri wao kuhakikisha wana sifa za kazi wanazofanya na kutumia fursa hiyo kufanya mitihani ili kuwa na sifa zinazohitajika.

Naibu Waziri wa wizara hiyo, Stella Manyanya alitoa ufafanuzi huo jana Dar es Salaam kutokana na taarifa za upotoshaji zilizoenea mitandaoni kwamba serikali imepiga marufuku watu wenye Stashahada kujiunga na vyuo vikuu badala yake watakaoingia ni wenye sifa za kidato cha sita.

Manyanya alisema kwa waliopo vyuoni kwa sasa wanatakiwa kuhakikisha wanakuwa na sifa za shahada kwa kusafisha vyeti vyao na wapewe fursa ya kufanya mitihani hiyo waliyofeli na kama wamefaulu kozi hiyo, pia wataweza kufaulu mitihani hiyo itakayowapa sifa ya kusoma vyuo vikuu.

“Ni vitu tunavyovifanya wenyewe ila vina madhara makubwa, unakuta mtu anakaa nafasi kwa sababu ana vyeti, lakini uwezo hana… uhakiki utafanyika kwa vyeti na wanaofanya hivyo ni Utumishi,” alisema Naibu Waziri.

Alisema kwa watakaobainika pia kuingia vyuoni kwa sifa ambazo zilikuwa hazitakiwi kwa wakati huo ni batili zitafutwa na kwa watakaoingia kwa sasa vyuoni kwa kutumia njia zisizo rasmi na kubainika hata ikifika mwaka 2020 watafutwa kwa kuwa taarifa tayari wanayo.

“Kilichoongelewa siku ile ni kuruhusu kidato cha nne na kidato cha sita waliofeli kuingia kwenye ‘foundation course’ na diploma haikutajwa pale kwa kuwa haikuulizwa na hakuna kauli iliyotajwa pale kukataza watu wa diploma kwenda chuo kikuu,” alieleza Manyanya akirejea kauli ya Waziri wake, Profesa Joyce Ndalichako hivi karibuni katika mahafali ya Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT) yaliyofanyika mkoani Pwani.

Profesa Ndalichako alikaririwa akisema vigezo vya udahili vinatakiwa kuzingatiwa.

“Nami ningependa nizungumzie kwamba foundation course hazimuongezei mtu sifa. Kama sifa ya kujiunga na chuo kikuu ni kufaulu kidato cha sita, kama amefeli Baraza la Mitihani linaruhusu kurudia mtihani, kwa nini anakwepa kule? Kwa nini? Kwa nini tunataka tuendeleze uchochoro,” alieleza Waziri Ndalichako.

Naibu Waziri alisema kuna njia mbili za kwenda chuo kikuu ikiwemo njia ya moja kwa moja na njia ya mbadala ya kuwa na vyeti vinavyotambulika na kinasimamiwa na mamlaka husika ambayo ni Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) na wawe na ufaulu mzuri.

“Tanzania imejiwekea mifumo yake ya elimu ambayo inaendana na ngazi za kimataifa katika utoaji wa elimu na hapo awali tulikusudia kuhakikisha elimu inatolewa kwa watu wengi zaidi na hizo fursa zinawafikia wadau wote katika ngazi mbalimbali kwa kupanua elimu ya msingi hadi vyuo vikuu,” alieleza Naibu Waziri.

Alisema walitambua kuna wadau mbalimbali walitamani kusoma vyuo vikuu, lakini hawapati hiyo fursa na ndiyo wakaanzisha mfumo huo wa Chuo Kikuu Huria na mtu anaweza kusoma alipo na mfumo umekuwa ukiboreshwa siku hadi siku.

Alisema iliwekwa mifumo ya vyeti na ngazi zake kulingana na vigezo na hivyo siyo kila cheti kinachotolewa kinaruhusu mtu kwenda ngazi nyingine na kila mamlaka imepewa jukumu ili kulinda ubora wa elimu unaotolewa nchini.

Naibu Waziri alisema kutokana na uanzishwaji wa vyuo mbalimbali kumejitokeza changamoto na watu kutoka katika mfumo rasmi uliopangwa na kujiwekea mifumo binafsi ambayo imeingiza hata wanafunzi wa kidato cha nne ambao hawana sifa kuingia vyuo vikuu.

“Jambo hilo limesababisha kuwepo kwa msuguano, haiwezekani mtu afeli kidato cha nne bila kuwa na cheti kingine chochote anaingizwa katika kozi hiyo halafu anaingizwa chuo kikuu, sisi hatujarasimisha mfumo huo wa ‘foundation course’ na hatuna vipimo vyake,” alieleza.

Alisema kwa kawaida mwanafunzi mwenye diploma inayotambulika wamewekewa usawa wa alama fulani na kidato cha sita hivyo wanakuwa na sifa ya kuingia vyuo, lakini siyo waliofeli hivyo wanatakiwa kufanya utafiti zaidi katika kozi hiyo.

“Haiwezekani kila mtu akajianzishia mfumo wake tu, tulifikia eneo ambalo si zuri kama nchi na sasa tutaimarisha ubora…ukifeli kidato cha nne unatakiwa kwenda kusoma na kupata cheti kwenye mtaala unaotambulika na ukaenda diploma na unapofaulu unaweza kwenda chuo kikuu,” aliongeza.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Simon Msanjila alisema suala la ‘Foundation course’ limelenga kumuandaa mtu mwenye sifa ambaye amekuwa nje ya mfumo kwa muda mrefu ili kuingia chuo kikuu, lakini walichokuwa wakikifanya wengi ni kuwachukua waliofeli kidato cha nne na sita na kuwaingiza katika kozi hiyo na hatimaye kuwaingiza chuo kikuu.

Taarifa kutoka Ikulu: Rais Magufuli na Rais Lungu wakubaliana kufufua miradi ya TAZARA na TAZAMA

$
0
0
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Zambia Mhe. Edgar Chagwa Lungu  tarehe 28 Novemba, 2016 wamekubaliana kuchukua hatua za haraka na madhubuti kuboresha utendaji kazi wa reli ya TAZARA na bomba la mafuta la TAZAMA ili miradi hiyo miwili ilete manufaa yaliyokusudiwa kwa wananchi Tanzania na Zambia.

Marais hao wametangaza kuchukua hatua hizo Ikulu Jijini Dar es Salaam katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika muda mfupi baada viongozi hao kufanya mazungumzo rasmi ikiwa ni sehemu ya ziara ya siku 3 ya Rais Lungu iliyoanza jana hapa nchini kwa mwaliko wa Rais Magufuli.

Katika mkutano huo uliorushwa moja kwa moja na vyombo vya habari vya redio, tevisheni na mitandao ya kijamii Rais Magufuli ameelezea kusikitishwa kwake na kuzorota kwa utendaji kazi wa reli ya TAZARA ambao umeshuka kutoka usafirishaji wa tani 5,000,000 za mizigo mwaka 1976 hadi kufikia usafirishaji wa tani 128,000 kwa mwaka hivi sasa, huku utendaji kazi wa bomba la mafuta la TAZAMA nao ukiporomoka kutoka uwezo wake wa kusafirisha tani 1,100,000 za mafuta hadi kufikia tani 600,000 kwa mwaka hivi sasa.

Marais hao wamekubaliana kuwakutanisha wanasheria wakuu wa Serikali za nchi zote mbili haraka iwezekanavyo kwa lengo la kufanya marekebisho ya kisheria kwa maeneo yote yaliyoonesha kuwa kikwazo na pia kupanga upya menejimenti za TAZARA na TAZAMA ili ziweze kuendesha vyombo hivyo kibiashara na kwa manufaa yaliyokusudiwa wakati vilipoanzishwa na Waasisi wa mataifa haya mawili yaani Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wa Tanzania na Mhe. Dkt. Kenneth Kaunda wa Zambia.

“Tumekubaliana ni lazima tubadilike na tubadilike kwa haraka, vikwazo vinavyotokana na sheria viondolewe na manejimenti ya TAZARA ipangwe upya, na mimi nataka kusema kwa uwazi, ukiwauliza TAZARA watakwambia tatizo ni mtaji lakini ukweli ni kwamba tatizo ni menejimenti, ingekuwa tatizo ni mtaji, ule uliokuwepo mwaka 1976 umekwenda wapi? maana sasa hivi TAZARA ina vichwa 14 tu vya kuendeshea treni na ina upungufu mkubwa wa mabehewa” amesema Rais Magufuli.

Kwa upande wake Rais Lungu amesisitiza kuwa katika kuimarisha TAZARA wamekubaliana kuweka pembeni siasa na kuirejesha TAZARA katika hali yake ya kibiashara kwa kuhakikisha inafanya kazi ya kupunguza gharama za usafirishaji wa mizigo iendayo kusini mwa Tanzania na nchini Zambia.

Mhe. Lungu ameongeza kuwa pamoja na kuimarisha bomba la mafuta la TAZAMA, Zambia inatarajia kunufaika na gesi iliyogunduliwa kwa kiasi kikubwa nchini Tanzania na pia inajipanga kutumia vizuri fursa ya kufunguka kwa ukanda wa maendeleo wa Mtwara (Mtwara Corridor) na mpango wa ujenzi wa reli ya kati ambapo ukanda wa Kaskazini mwa Zambia una mawasiliano ya karibu na bonde la ziwa Tanganyika.

“Mhe. Rais Magufuli una muda wa kutosha katika uongozi wako na mimi nina muda wa kutosha pia, kwa hiyo kwa pamoja tunaweza kuimarisha maeneo yote ya kuinua biashara na uwekezaji kati ya nchi zetu mbili ikiwemo kuimarisha TAZARA na TAZAMA kwa manufaa ya wananchi wetu” amesisitiza Rais Lungu.

Kuhusu hali ya biashara kati ya Tanzania na Zambia, Rais Magufuli amesema Zambia ni nchi inayoongoza kwa kupitisha mizigo mingi katika bandari ya Dar es Salaam ambapo katika mwaka 2015 mizigo yenye uzito wa tani Milioni 1.9 ilipitishwa na kwamba kumekuwa na ongezeko la biashara kati ya Zambia na Tanzania kutoka Shilingi Bilioni 89.2 mwaka 2010 hadi kufikia Shilingi Bilioni 152.2 mwaka 2015.

Dkt. Magufuli amemhakikishia Rais Lungu kuwa Tanzania inaendelea kuboresha mazingira ya kufanyia biashara ikiwa ni pamoja na kuboresha zaidi bandari ya Dar es Salaam, kupunguza vizuizi vya barabarani kutoka 8 hadi 4, kushughulikia tatizo la vizuizi vya polisi na kujenga Kituo cha Pamoja cha Utoaji wa Huduma za Mpakani (One Stop Border Post)

“Tunataka mambo haya yote yaende haraka, wataalamu wetu ni lazima waharakishe kurekebisha vikwazo vyote vilivyokuwa vinatuchelewa, tufanye kazi pamoja kwa manufaa ya wananchi” amesisitiza Rais Magufuli.

Jioni ya leo Rais Edgar Chagwa Lungu anatarajiwa kuhudhuria dhifa ya kitaifa aliyoandaliwa na Mwenyeji wake Rais John Pombe Magufuli Ikulu Jijini Dar es Salaam na kesho Rais Lungu anatarajiwa kumaliza ziara yake ya siku 3 hapa nchini.

Chadema waja na oparesheni Mpya Iitwayo ‘Kata Funua’

$
0
0
Baada ya kuanzisha na hatimaye kukwama kuitekeleza operesheni ya Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta), Chadema imekuja na nyingine itakayokwenda kwa jina la ‘Kata Funua’.

Operesheni hiyo mpya imetangazwa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ikilenga kukipa chama hicho mafanikio katika uchaguzi wa Serikali za mitaa na ule mkuu ujao.

Mbowe amesema hayo katika kikao cha uchaguzi wa mwenyekiti wa kanda wilayani Masasi mkoani Mtwara.

“Kiongozi yeyote atakayeonyesha nia ya kutukwamisha hatutamvumilia, tutamuondoa ili tuweze kuendelea na safari yetu na kumaliza kutembelea kanda zote,” amesema.

Amesema ziara hizo ndizo zitakazoipa nafasi chama hicho kuchukua maeneo mengi zaidi hasa katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2019.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa amesema umoja na mshikamano ndiyo msingi imara utakaowasaidia kuweza kufikia malengo.

“Ili kufanikiwa lazima kuwe na umoja imara baina ya viongozi wa chama. Mtu yeyote atakayekuwa na nia mbaya na umoja huu achukuliwe hatua mara moja ili kuepuka kutokea kwa migogoro,” amesema.

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema – Zanzibar, Salum Mwalimu amemshukuru Rais John Magufuli kwa kukipa fursa adhimu chama hicho kutokana na kuzuia mikutano ya kisiasa majukwaani jambo ambalo limewasaidia kujipanga vizuri katika uchaguzi ujao.

“Safari hii ni fursa kwetu, tumejipanga kiuhakika na si kwa kubahatisha tunapoelekea katika uchaguzi wa serikali za vijiji, vitongoji, mitaa mwaka 2019 na baadaye uchaguzi wa wabunge na Rais ifikapo 2020,” amesema.

Trump atishia kurudisha nia ya kumshtaki Hillary Clinton Baada ya Timu yake Kusema Itashiriki Kuhesabu Kura Upya

$
0
0
RAIS mteule Donald Trump wa Marekani, ametishia kufikiria upya ahadi aliyoitoa ya kutomfungulia mashtaka aliyekuwa mpinzani wake katika kinyang’anyiro cha urais, Hillary Clinton.

Trump ametoa tishio hilo kufuatia taarifa kuwa timu ya kampeni ya Hillary itashiriki kuhesabu kura upya katika Jimbo la Wisconsin, ambalo bilionea huyo alishinda.

Uamuzi wa timu hiyo unatokana na aliyekuwa mgombea urais kupitia Chama cha Kijani, Dk. Jill Stein, kuwasilisha hati ya kuhesabiwa upya kura katika jimbo hilo.

Hili ni pamoja na kuwa tangu mwanzo timu ya Hillary ilishasema haioni ishara zozote za kukiukwa sheria katika kinyang’anyiro hicho cha kuingia White House.

Msaidizi wa Trump, Kellyanne Conway, alisema iwapo timu ya Hillary itaendelea kushinikiza azma ya kutaka kushiriki kuhesabu kura upya, Trump hatasita kufikiria upya ahadi aliyoitoa ya kutomchukulia hatua kutokana na kutumia barua pepe binafsi wakati alipokuwa waziri wa mambo ya nje.

Aidha Trump alimkumbusha Hillary kuwa alishakubali matokeo na kabla ya uchaguzi pia aliahidi atakubali kushindwa.

Lakini wakili wa masuala ya uchaguzi wa Chama cha Democratic, Marc Erik, alisema harakati zao kuwezesha kuhesabu upya kura zitaendelea kufanyika hata katika majimbo mengine mawili ya Michigan na Pennsylvania.

Hata hivyo, wataalamu wa masuala ya uchaguzi walisema kutokana na matokeo ya jumla kuonyesha Hillary alikuwa nyuma ya Trump kwenye majimbo mengi, itakuwa ngumu kubatilisha ushindi.

Tisho la kambi ya Trump limeenda sambamba na bilionea huyo kudai kwamba watu milioni mbili walipiga kura kinyume cha sheria.

Alitoa kauli hiyo kufuatia Hillary kuongoza kwa pengo la kura za wananchi milioni 2, lakini ni Trump ameibuka mshindi kwa kupata kura nyingi za wajumbe kuliko mpinzani wake.

Trump pia alidai kulitokea ulaghai mwingi katika upigaji kura majimbo ya Virginia, New Hampshire na California ambako Hillary alishinda.

Na aliwashutumu wanahabari wa Marekani akisema wamekataa kuangazia suala hilo.

Ndege iliyokuwa imebeba wachezaji wa klabu ya soka ya Brazil imeanguka

$
0
0
Ndege iliyobeba watu 81 wakiwemo wachezaji wa klabu ya soka ya Chapecoense kutoka Brazil imeanguka wakati ikikaribia kutua katika mji wa Medellin nchini Colombia, mamlaka zathibitisha.

Taarifa kutoka eneo la tukio zinaarifu kuwa watu 76 wamefariki dunia huku watano wakipona.

Maofisa wa uwanja wa ndege wa Medellin wamesema wachezaji wa Chapecoense waliokuwa kwenye ndege hiyo walikuwa safarini kwenda kucheza fainali ya Copa Sudemericana dhidi ya Atletico Nacional ya Medellin, Colombia.

Kutokana na ajali hiyo, mechi baina ya timu hizo iliyokuwa ichezwe kesho imeahirishwa hadi itakapotangazwa tena.

Watumishi wa TAKUKURU Waliotumbuliwa tangu Mwaka jana Kwa Kukiuka Agizo la Rais Warejeshwa Kazini

$
0
0

Watumishi waandamizi wanne wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) waliosimamishwa kazi baada ya kusafiri nje ya nchi kinyume na agizo la Rais John Magufuli, wamerejeshwa kazini baada ya takriban mwaka mmoja kupita.

Msemaji wa Takukuru, Mussa Misalaba aliwataja watumishi hao kuwa ni Mkurugenzi wa Elimu kwa Umma, Mary Mosha na Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, Ekwabi Mujungu ambao wamerejeshwa baada ya shauri lao kusikilizwa na ofisi husika.

“Shauri lao lilishughulikiwa na Ofisi ya Rais kutokana na vyeo vyao, wamerejeshwa ofisini na kuanza kazi Novemba 14,” alisema.

Misalaba alisema watumishi wengine waliorejeshwa kazini ni aliyekuwa Msemaji wa Takukuru, Doreen Kapwani na Katibu Muhtasi wa mkurugenzi mkuu, Rukia Nikitas shauri lao lilisikilizwa na mamlaka ya taasisi hiyo na hatua za kinidhamu zilichukuliwa ikiwamo kuhamishwa vitengo.

Watumishi hao walidaiwa kuondoka nchini Novemba 23 mwaka jana, kabla ya kupewa majibu ya vibali walivyoomba baada ya kuandika barua Ikulu kuhusu safari hiyo.

Rais Magufuli alitangaza kufuta safari za nje ya nchi kwa maofisa wa Serikali Novemba 7, 2015 na kutoa mwongozo kwamba safari zitakazoruhusiwa ni zile zenye ruhusa ya Ikulu.

Kusimamishwa kwao kazi kulitangazwa na aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alipozungumza na waandishi wa habari Desemba 16 mwaka jana.

Takukuru iliiandikia Ikulu barua ya kuomba kibali kwa ajili ya safari hiyo, lakini kabla ya kujibiwa, wafanyakazi hao waliamua kusafiri.

Lipumba Amtaka Maalim Seif Aache Kudanganywa na Waganga wa Kienyeji

$
0
0
Mgogoro wa uongozi ndani ya Chama cha Wanachi (CUF) unaendelea kuzua mapya ambapo jana, Mwenyekiti wa chama hicho anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba alimvaa tena Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Makao Makuu ya chama hicho zilizoko Buguruni jijini Dar es Salaam, Profesa Lipumba alimtahadharisha Maalim Seif akimtaka aachane na ‘waganga’ kwani watamdanganya.

Ingawa hakueleza ni waganga wa aina gani, Profesa Lipumba alimtaka Maalim Seif kukubali kuzungumza naye ili wamalize matatizo yao.

“Haiwezi kubadilika kwamba Mwenyekiti wa chama hiki nikiwa hai hadi mwaka 2019… Maalim waganga watakudanganya sana, watakudanganya sana,” alisema Profesa Lipumba.

“Katika hili lilitakiwa lisifike hapa, huna sababu, njoo tuzungumze, pokea simu yangu unajua namba yangu tuzungumze tuyamalize uje nikupangie kazi,” aliongeza.

Mchumi huyo alisisitiza kuwa hatakubali chama hicho kiuzwe kwa bei nafuu kwa vyama vingine vya kisiasa au kwa aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema akiungwa mkono na vyama vya upinzani vinavyounda Ukawa, Edward Lowassa.

Kwa upande wake Maalim Seif ameendelea kushikilia msimamo wake akieleza kuwa Profesa Lipumba ni msaliti wa chama hicho na ana lengo la kukivuruga.

Alisema kuwa yeye yuko tayari kukaa naye meza moja kwa lengo la kueleza hadharani kile alichokiita uongo wake na sababu halisi iliyomfanya ajiuzulu nafasi ya Uenyekiti siku chache kabla ya kuanza kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

Je unahitaji simu kali ya bei nafuu? Wagiftishe uwapendao Tecno Y3+Music kwa Tsh 99,999/= tu!

$
0
0
Je unahitaji simu kali ya bei nafuu? Wagiftishe uwapendao Tecno Y3+Music kwa Tsh 99,999/= tu!

Profesa Muhongo, Waziri Wa Nishati Zambia Wakutana Kuzungumzia Bomba La Tazama

$
0
0
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Waziri wa Nishati wa Zambia, David Mabumba, wamekutana na kufanya mazungumzo kuhusu kuboresha Bomba la Mafuta la TAZAMA ili liweze kuwanufaisha wananchi wa Tanzania na Zambia kama ilivyokusudiwa.

Mazungumzo yao yaliyofanyika mapema leo, ofisini kwa Waziri Muhongo jijini Dar es Salaam, ni kufuatia makubaliano ya marais wa nchi husika, Dk John Magufuli na Edgar Lungu; kuhusu kuboresha zaidi Bomba la TAZAMA na Reli ya TAZARA.

Marais Magufuli na Lungu, walifikia makubaliano hayo jana katika mazungumzo rasmi yaliyofanyika Ikulu ya Dar es Salaam ambayo ni mojawapo ya shughuli mbalimbali zilizopangwa katika ratiba ya ziara ya siku Tatu (3) ya Rais Lungu iliyoanza nchini Jumapili, Novemba 21 mwaka huu.

Waziri Mabumba ambaye alifuatana na Ujumbe wa Viongozi na Maafisa waandamizi kutoka TAZAMA na wizarani kwake; aliafiki mapendekezo yaliyotolewa na Waziri Muhongo kuhusu namna pande hizo mbili zitakavyoshirikiana katika utekelezaji wa agizo la Marais wao ambayo ni pamoja na wataalam wa pande zote kukutana na kufanya majadiliano pamoja na kufanya ziara kukagua utendaji kazi wa Bomba hilo.

Aidha, Mawaziri hao walijadiliana kuhusu namna ambavyo Zambia itanufaika na gesi asilia iliyogunduliwa Kusini mwa Tanzania.

Kikao hicho pia, kilihudhuriwa na viongozi waandamizi wa Wizara ya Nishati na Madini – Tanzania, akiwamo Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara, Profesa James Mdoe.

Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Jumatano ya Novemba 30

Maagizo Aliyoyatoa Rais Magufuli Baada ya Kufanya Ziara ya Kushtukiza Katika Gereza la Ukonga

$
0
0
Amiri Jeshi Mkuu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, Jumanne  tarehe 29 Novemba , 2016  amefanya ziara ya kushtukiza katika Gereza la Ukonga jijini Dar Es Salaam  na kupiga marufuku uuzwaji wa sare za majeshi nchini na watu binafsi na kutaka wale wote wanaouza sare hizo wazikabidhi kwa majeshi husika mara moja.

Rais Magufuli amepiga marufuku hiyo kufuatia maelezo kutoka kwa baadhi ya askari wa Jeshi la Magereza kuwa wamekuwa wakinunua sare za jeshi hilo kutoka kwa watu binafsi kinyume na taratibu za majeshi nchini na kuvitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuwachukulia hatua mara moja wale wote watakaobainika kuuza sare za majeshi ya hapa nchini
 
Hali kadhalika Rais magufuli amepiga marufuku kwa majeshi yote nchini kuingia ubia na watu binafsi kupangisha ama kuuza maeneo yao kwa ajili ya kufanya biashara na kutaka maeneo yote ya majeshi yabaki katika jeshi husika. 
 
''Haiwezekani sare za majeshi yetu hapa nchini kuuzwa na watu binafsi hilo haliwezekani kamwe labda baada ya kumaliza muda wangu , amesema Rais magufuli'' 
 
Aidha Rais Magufuli ametoa shilingi Bilioni Kumi kwa Jeshi la Magereza kwa ajili ya kujenga nyumba mpya zitakazotumika kwa ajili ya makazi ya askari wa Jeshi la Magereza katika Gereza la Ukonga jijini Dar es salaam. 
 
Hatua hiyo inafuatia kilio cha askari Magereza kuwa wengi wao wamekuwa wakiishi uaraiani kitu ambacho ni tofauti na taratibu za majeshi nchini na hata kuzorotesha utendaji kazi wa askari wa Jeshi hilo. 
 
Amiri Jeshi Mkuu na Rais Dkt. John Pombe Magufuli pia ameagiza Jeshi la Magereza kuhakikisha wafungwa wanatumika katika uzalishaji mali badala ya mfumo wa sasa ambapo baadhi ya wafungwa wamekuwa  wakitutumia rasilimali za serikali bila kuzifanyia kazi.
 
 Rais Magufuli amewahakikishia Maafisa na Askari wa Jeshi la Magereza kuwa serikali itaendelea kuboresha maslahi yao na vitendea kazi kama inavyofanya kwa majeshi mengine nchini. 
  Amiri Jeshi Mkuu Rais Dkt John Pombe Joseph Magufuli akiweka saini kitabu cha wageni akiwa na  Kamishna Mkuu wa Magereza John Casmir Minja kabla ya kuongea na maafisa na askari wa Jeshi la Magereza alipofanya ziara ya kushtukiza katika Gereza la Ukonga jijini Dar es salaam  Novemba 29, 2016
 Amiri Jeshi Mkuu Rais Dkt John Pombe Joseph Magufuli akipewa muhtasarai wa kazi  na Kamishna Jenerali wa Magereza John Casmir Minja kabla ya kuongea na maafisa na askari wa Jeshi la Magereza alipofanya ziara ya kustukiza katika Gereza la Ukonga jijini Dar es salaam Novemba 29, 2016
 Amiri Jeshi Mkuu Rais Dkt John Pombe Joseph Magufuli akikaribishwa na Kamishna Jenerali wa Magereza John Casmir Minja ili aongee  na maafisa na askari wa Jeshi la Magereza alipofanya ziara ya kustukiza katika Gereza la Ukonga jijini Dar es salaam Novemba 29, 2016
 Mmoja wa askari wa Kikosi Maalumu cha Magereza akitoa kero zao mbele ya Amiri Jeshi Mkuu Rais Dkt John Pombe Joseph Magufuli  alipofanya ziara ya kushtukiza katika Gereza la Ukonga jijini Dar es salaam leo Novemba 29, 2016
 Amiri Jeshi Mkuu Rais Dkt John Pombe Joseph Magufuli akichukua maelezo kutoka kwa  maafisa na askari wa Jeshi la Magereza alipofanya ziara ya kustukiza katika Gereza la Ukonga jijini Dar es salaam leo Novemba 29, 2016.

Mbunge Mwingine wa CHADEMA Atiwa Mbaroni

$
0
0

Mbunge wa Ukonga kwa tiketi ya Chama cha Demokrsia na Maendeleo (CHADEMA), Mwita Waitara anashikiliwa na Polisi katika kituo cha Polisi Chang’ombe, Temeke, Dar es Salaam.

Mbunge Waitara amekamatwa jana alipokuwa katika eneo la Uvikiuta alikokwenda kufuatilia mgogoro wa ardhi wa muda mrefu kati ya wananchi wa eneo hilo na anayedaiwa kuwa kigogo wa serikali anayetuhumiwa kuwa anataka kupora ardhi hiyo na kuwahamisha wananchi kwa nguvu.

Mbunge huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa serikali ya Mtaa wa Kivule alifika katika eneo hilo lenye mgogoro ambapo shughuli ya kubomoa nyumba 500 za wananchi wa eneo hilo ilikuwa ikiendelea.

Eneo lenye mgogoro lipo mpakani mwa wilaya za Ilala na Temeke (Kivule-Ilala na Mbande-Temeke).

Uongozi wa Kiwanda cha Saruji cha Dangote waeleza sababu ya kusitisha uzalishaji

$
0
0
UZALISHAJI katika kiwanda cha saruji cha Dangote kilichopo Mtwara umesimama kwa muda kutokana na hitilafu za kiufundi zilizojitokeza katika mitambo.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dangote Tanzania, Harpreet Duggal alisema jana kwamba mafundi wa Dangote wapo kazini na shughuli za uzalishaji zitarejea katika siku chache zijazo.

Alisema kiwanda kinachomilikiwa na bilionea namba moja Afrika, Alhaji Aliko Dangote wa Nigeria kilianza uzalishaji wa kibiashara mwaka huu na kama ilivyo kwa kiwanda kingine kama hicho, jambo lolote linaweza kutarajiwa hasa katika miezi ya mwanzo.

Alisisitiza, “hitilafu hizi ni za kawaida na uzalishaji utarejea katika kipindi kifupi kijacho.”

Akizungumzia gharama za uzalishaji, Duggal alisema uendeshaji nchini uko juu huku miongoni mwa sababu ikiwa ni matumizi ya jenereta za dizeli katika kuendesha kiwanda.

Hata hivyo, alisema serikali inaangalia suala hili la gharama na jinsi ya kutafuta njia ya kuwapunguzia mzigo.



Ajali ya Gari Yaua Watu 6

$
0
0
Watu  sita wakiwamo mfungwa na wanafunzi wamekufa huku wengine wanane wakijeruhiwa, baadhi yao vibaya baada ya gari dogo walilokuwa wakisafiria kuacha njia na kupinduka mara nne katika Kijiji cha Kipande wilayani Nkasi katika Mkoa wa Rukwa katika barabara kuu ya Mpanda – Sumbawanga.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa, George Kyando alisema ajali hiyo ilitokea saa 8.10 jana mchana katika Kijiji cha Kipande.

Aliwataja waliokufa kuwa ni mfungwa wa Gereza la Kitete lililopo Nkasi, Gaudensi Nyambo (27), Gasper Malimi (18) na Kenzi Mwambige (18) wote wakiwa wanafunzi wa Kidato cha Nne katika Shule ya Sekondari ya Nkasi na Ofisa Mipango wa Wilaya ya Nkasi, Godfrey Mwanansao.

Alisema marehemu wawili hawajatambuliwa huku miili yote ikiwa imehifadhiwa katika chumba cha maiti katika Hospitali ya Rukwa ya Mkoa wa Rukwa mjini Sumbawanga .

“Mfungwa Nyambo alikuwa akitumikia kifungo katika Gereza la Kitete wilayani Nkasi ambako alikuwa na kesi nyingine mahakamani alikufa wakati akitibiwa hospitalini hapa,” alieleza Kamanda Kyando.

Alisema ajali hiyo ilihusisha gari aina ya Hiace Nissan Vannette lenye namba za usajili T 966 DHP lililokuwa likiendeshwa na Lusanjo Mwaipopo aliyekimbia baada ya ajali hiyo.

Alisema gari hilo lilikuwa likitokea wilayani Nkasi kwenda mjini Sumbawanga ambapo liliacha njia na kupinduka mara nne kabla halijaanguka ndani ya gema.

Alisema chanzo cha ajali hiyo hakijafahamika huku uchunguzi wa kipolisi ukiendelea. Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa, Dk John Lawi alisema majeruhi tisa wamepokewa hospitalini hapo ambao mmoja ambaye ni mfungwa alikufa OPD.

Aliwataja majeruhi kuwa ni pamoja na askari Magereza wa Gereza la Kitete, Fortunatus Saanane (44) aliyelazwa chumba cha uangalizi maalumu (ICU) huku hali yake ikiwa tete. Wengine ni askari Magereza, Francis Elay (30) ambaye alitibiwa na kuruhusiwa.

Kwa mujibu wa Dk Lawi, majeruhi wengine ni Mbagala Hale, Mamadelwa Kafadhila, Mathias Mwandaliwa (28) na wengine ambao majina yao hayakuweza kupatikana mara moja. Alisema hali za majeruhi hao ni mbaya.

Rais Lungu Akataa Biashara ya Uswahiba.....Ataka Ufanisi Zaidi Bandari ya Dar es Salaam

$
0
0
Rais wa Zambia, Edgar Lungu amewataka watendaji wa nchi yake na Tanzania, kuweka siasa pembeni na kujikita kwenye biashara zitakazoinua uchumi wa nchi hizo mbili.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam wakati wa kuhitimisha ziara yake ya siku tatu, Rais Lungu aliyetembelea Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na Shirika la Kusafirisha na Kupokea Mizigo la Zambia (Zamcargo), alisema licha ya kuenzi mchango wa waasisi wa mataifa hayo, Mwalimu Julius Nyerere na Kenneth Kaunda, watajikita zaidi kwenye biashara.

 “Changamoto mliyonayo ni kwenu uongozi na Bodi ya TPA kwa watu wa Kusini au Mashariki au hata nje ya Afrika. Watu wa Zambia wanasema muda wa siasa umekwisha, sasa ni muda wa maendeleo. Hatutawaunga mkono kwa sababu niko karibu sana na Rais (John) Magufuli. Ni kweli niko karibu na Rais Magufuli kama mlikuwa hamjui, lakini hatuwaungi mkono kwa sababu hiyo, bali kwa ufanisi wenu,” alisema Rais Lungu.

Akizungumzia miradi ya reli ya Tazara na bomba la mafuta la Tazama, Rais Lungu alisema nayo inapaswa kufanya kazi kwa ufanisi.

 “Ni kweli sisi ni ndugu lakini hatuangalii hilo. Wazambia wanataka mbolea ifike haraka, shaba isafirishwe haraka kwenda sokoni,” alisema.

Akiwa katika ofisi za Zamcargo, Rais Lungu alirudia wito wake wa ufanisi wa biashara akisema hatasita kuwawajibisha watendaji wa taasisi hiyo.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Deusdedit Kakoko alisema Zambia  imekuwa mteja namba moja katika usafirishaji wa mizigo kupitia Bandari ya Dar es Salaam.

Kakoko alisema mwaka 2014, Zambia ilichangia asilimia 36 ya mizigo ambayo ni sawa na tani milioni 5.2 ikiwa ni mbali ya nchi nane zinazotumia bandari hiyo.

“Takwimu za TPA zinaonyesha kuwa mizigo ya Zambia inayopitia hapa imekuwa ikiendelea kila mwaka. Mwaka 2011, bandari ilipokea tani milioni 1.6 za mizigo inayotoka na kuingia. Lakini mwaka 2014 Zambia ilipokea tani milioni 1.9 za mizigo ya Zambia,” alisema Kakoko.

Alisema kutokana na umuhimu huo, uongozi wa TPA umekuwa ukiboresha huduma ili kufanya kazi kwa ufanisi.

“Kwa mfano, muda wa kutoa mizigo bandarini umepunguzwa hadi siku kumi na moja mwisho wa Oktoba kulinganisha na siku 32 zilizokuwa mwaka 2008. Bandari pia imeboresha mfumo wa malipo ya mizigo kwa wateja wake kwa kutumia mfumo wa kielektroniki,” alisema Kakoko.

Katika ziara hiyo ya bandarini, Lungu aliambatana na Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Kimataifa na Kikanda, Balozi, Augustine Mahiga, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Edwin Ngonyani na katibu mkuu wa wizara hiyo, Dk Leonard Chamuriho.

Mara baada ya ziara hiyo Rais Magufuli aliwaongoza viongozi wengine wa Serikali kumsindikiza mgeni wake huyo uwanja wa ndege na kurejea Zambia.

Viongozi wengine waliofika uwanjani hapo ni Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na viongozi wengine. Rais Lungu aliondoka uwanjani hapo saa 7: 40 mchana.

Pedeshee Ndama mtoto wa Ng’ombe Kortini kwa Kutakatisha Hela

$
0
0
Tuhuma za kughushi, kutakatisha fedha na kujipatia dola za Marekani 540,390 kwa njia ya udanganyifu zimemfanya mfanyabiashara maarufu jijini Dar es Salaam, Ndama Shabani Hussein, maarufu kama Pedeshee Ndama mtoto wa Ng’ombe (44) kupandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Mashtaka hayo yanaangukia katika Sheria ya uhujumu uchumi.

Akisoma hati ya mashtaka jana Wakili wa Serikali, Christopher Msigwa amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Victoria Nongwa kuwa mshtakiwa huyo alifanya hivyo na kujipatia dola za Marekani 540,390 kwa njia ya udanganyifu kati ya Februari 26 na Machi 3,2014.

Msigwa amedai kuwa Februari 20,2014 jijini Dar es Salaam, Ndama alighushi nyaraka ya kibali cha kusafirisha madini na sampuli za madini kwa kusudi la kuonesha kuwa kampuni ya Muru Platnum Tanzania Investment Company Limited iliruhusiwa kusafirisha maboksi manne ya dhahabu yenye kilogramu 207 yakiwa na thamani ya Dola za Marekani 8,280,000.00 kwenda Australia kwa kampuni ya Trade TJL DTYL Limited wakati akijua si kweli.

Mshtakiwa huyo anadaiwa kuwa Machi 6,2014 katika jiji la Dar es Salaam, alighushi kwa kutengeneza hati ya kibali (Certificate of Clearance) ya Umoja wa Mataifa ofisi ya Dar es Salaam, akijaribu kuonesha kilogramu 207 za dhahabu toka nchini Congo zinatarajiwa kusafirishwa na kampuni ya Muru Platnum Tanzania Investment Company Limited kwenda Australia kwa kampuni ya Trade TJL DTYL Limited, zimesafirishwa bila jinai yoyote wakati akijua si kweli.

Wakili huyo wa Serikali ameendelea kudai kuwa Februari 20,2014 mshtakiwa huyo alighushi fomu ya forodha yenye namba za usajili R.28092 akionesha kampuni ya Muru Platnum Tanzania Investment Company Limited imelipa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) dola za Marekani 331,200 kama kodi ya uingizaji wa bidhaa ambazo zina uzito wa kilogramu 207 za dhahabu zenye thamani ya Dola za Marekani 8,280,000 kutoka Congo kitu ambacho si kweli.

Pia, mshtakiwa huyo anadaiwa kuwa kati ya Februari 26 na Machi 2014 katika jiji la Dar es Salaam alijihusisha moja kwa moja na utakatishaji fedha kwa kufanya miammala ya dola za Marekani 540,390 kwa kuelekeza ziwekwe katika akaunti namba 9120000085152 iliyopo katika benki ya Stanbic yenye jina la Muru Platnum Tanzania Investment Company Limited na kuzitoa taslimu wakati akijua fedha hizo zinatokana na zao la uhalifu.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, mshtakiwa hakuruhusiwa kuongea chochote kwa sababu Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo hadi Mahakama Kuu.

Upande wa mashtaka umedai upelelezi bado haujakamilika na mshtakiwa alipelekwa rumande kwa sababu shtaka la kutakatisha fedha linalomkabili ni miongoni mwa mashtaka yasiyo na dhamana.

Kesi imeahirishwa hadi Desemba 13,2016 kwa ajili ya kutajwa

UKIMWI sasa kudhibitiwa kwa njia ya simu

$
0
0

Tanzania imeingia rasmi kwenye mfumo maalum wa kimataifa wa kupata huduma za afya ya UKIMWI kwa njia ya simu bila malipo mfumo ambao umefadhiliwa na nchi ya Marekani.

Akizindua mfumo huo Kaimu Balozi wa Marekani nchini Bi. Virginia Blaser amesema mfumo huo utawafikia zaidi ya watu laki nane huku lengo kuu la mfumo huo likiwa ni kupunguza maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) na Ukimwi kutoka asilimia 7.5 mpaka asilimia 5 hadi kufikia asilimia 0.0.

Amesema watu wote ambao wanadhaniwa kuwa na maambukizi ya virusi vya Ukimwi hadi kufikia mwaka 2020 wawe tayari wamepimwa kwa asilimia 90, asilimia 90 waanze kutumia dawa, na asilimia 90 kiwango chao cha maambukizi kiwe kimepungua.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya TAYOA nchini Bw . Peter Masika amesema katika ufadhili wa mfumo huo wao wakiwa ni wasimamizi wa mfumo watahakikisha unawafikia watanzania wote hasa wale wasiofikiwa na huduma muhimu za kiafya na kuwataka watanzania kujitokeza kwa wingi kutumia mfumo huo ili kutokomeza ugonjwa wa Ukimwi.

Kauli ya Jeshi la Polisi Kuhusu Askari wake Aliyefariki Dunia Kwa Kujipiga Risasi

$
0
0
Jeshi la Polisi mkoani Pwani limezungumzia kifo cha askari wake PC Armand Furaha (33) aliyejipiga risasi kifuani bila kukusudia na kufariki dunia.

Askari huyo alijipiga risasi hiyo usiku akiwa anaelekea kwenye lindo nyumbani kwa Mkuu wa Wilaya ya Kibaha.

Tulio hilo lilitokea saa moja usiku eneo la Mailimoja sokoni usiku wa kuamkia jana, wakati askari huyo akiwa njiani kuelekea kwenye kituo cha lindo alichopangiwa.

Kaimu Kamanda wa Polisi Pwani, Blasius Chatanda amesema askari huyo alijipiga risasi bahati mbaya kwa bunduki aina ya SMG akiwa amekaa kwenye kiti cha mbele katika gari alilokuwa anasafiria kwenda lindoni.

Amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa askari huyo alikuwa tayari ameweka risasi chemba kwenye bunduki hiyo aliyokuwa nayo na kwa bahati mbaya akiwa anashuka kwenye hilo gari ndipo risasi hiyo ikafyatuka na kumpiga kifuani eneo la kushoto na kufa wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Tumbi.

“Kabla ya tukio hilo, askari huyu aliwasili kazini jioni na kukuta amepangiwa kituo cha ulinzi kwa mkuu wa wilaya hivyo kama ilivyo ada alichukua zana za kazi ikiwemo bunduki hiyo na kuanza safari ya kuelekea lindoni kwake huko kwa DC, lakini bahati mbaya hakufika alifariki kwa kujipiga risasi bahati mbaya,” amesema Chatanda.

Akizungumzia suala la askari kujipiga risasi Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Bulimba amesema kila tukio hutokana na mazingira tofauti.
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live




Latest Images