Quantcast
Channel: MPEKUZI
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live

Taarifa Kwa Umma Kutoka Jeshi La Polisi Makao Makuu.

$
0
0

Jeshi la Polisi nchini, katika kuhakikisha usalama wa raia na mali zao unaimarika, limeendelea na operesheni za kukamata wahalifu wa makosa mbalimbali yakiwemo makosa ya usalama barabarani katika mikoa yote ili kudhibiti vitendo vya uhalifu na wahalifu. 

Katika operesheni hizo, Jeshi la Polisi limefanikiwa kukamata silaha na katika baadhi ya mikoa, wananchi wameweza kusalimisha silaha kwa hiari katika vituo vya Polisi.

Operesheni hizi ni endelevu, na ili tuweze kufanikiwa zaidi katika kudhibiti uhalifu na wahalifu hususani katika kipindi hiki tunapoelekea mwisho wa mwaka, wananchi wanatakiwa kuwa makini na kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu haraka kwa kutumia namba za bure 111 na 112 pindi wanapowatilia shaka watu wasiowajua katika maeneo yao ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa.

Kwa wamiliki wa maduka makubwa, hoteli na maduka ya kufanyia miamala ya fedha kwa njia ya simu waangalie namna ya kuweka vifaa maalumu vyenye uwezo wa kurekodi mienendo ya watu wanaoingia na kutoka ama kufuata huduma katika maeneo yao ya biashara.

Pia, wananchi katika makazi yao waimarishe ulinzi kwa kutumia mpango wa ulinzi jirani kwa kuhakikisha wanakuwa na utaratibu wa kubadilishana taarifa za hali ya usalama ili kuhakikisha mitaa yao inakuwa salama wakati wote.

Aidha, Jeshi la Polisi nchini linawataka madereva wa vyombo vya moto kuheshimu na kutii sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali na kuokoa maisha ya abiria na watumiaji wengine wa barabara. 

Jeshi la polisi nchini, litaendelea kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria, bila woga ama upendeleo katika kuhakikisha usalama wa raia na mali zao unaimarika.

Imetolewa na:
Advera John Bulimba - Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP)
Msemaji wa Jeshi la Polisi,
Makao Makuu ya Polisi.

VIDEO: Mabishano ya Mbowe na Naibu Spika Kuhusu Tuhuma za Wabunge wa CCM Kuhongwa Milioni 10 Kila Mmoja ili Wapitishe Muswada wa Habari

$
0
0
Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni Freeman Mbowe katika kipindi cha Maswali kwa Waziri Mkuu leo asubuhi  alidai kuwa, mnamo siku ya Jumanne tarehe 25/10/2016 saa mbili usiku kiliitishwa kikao cha wabunge wa CCM ambacho Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alikuwa Mwenyekiti, na kilihudhuriwa na Katibu MKuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, kwa ajili ya kujadili Muswada wa Habari.

Mbowe alisema kuwa Wabunge wakiwemo Mawaziri walihongwa shilingi milioni 10 kila mmoja ili waweze kusaidia kupitisha Muswada wa Habari unaotarajiwa kuwasilishwa Bungeni kesho.

Lakini Naibu spika alikataa  Waziri mkuu kujibu swali la Mbowe kwa  madai kuwa swali hilo halihusu sera, huku Mbowe akidai linahusu sera kwa kuwa ni rushwa kwa wabunge 

==> Wasikilize Hapo chini

Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema aswekwa mahabusu kwa mahojiano zaidi.

$
0
0

Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema, amesafirishwa kutoka Mkoani Dodoma usiku wa kumkia jana na kuswekwa kwa mara nyingine tena Mahabusu Mkoani Arusha kwa mahojiano ya kutoa lugha za uchochezi.

Akizungumza leo na waandishi wa habari ofisini kwake , Kamanda wa Polisi Mkoani Arusha, Charles Mkumbo, amesema Lema wamemweka mahabusu mpaka watakapomaliza mahojiano.

Amesema kuwa endapo watamaliza mahojiano atafikishwa mahakamani wakati wowote, ili kujibu makosa anayokabiliwa nayo.

Mkumbo amesema Lema amekuwa akitoa maneno na lugha za uchochezi na kuzirudia kila mara, hivyo wameona vema wamweke ndani.

Amesema juzi walimkamata na kumuhoji, kisha kumwachia kwa dhamana, lakini kuna baadhi ya makosa hakuhojiwa, na ndiyo wanamuhoji.

Aidha licha ya kumkamata Lema na kuendelea kumuhoji, lakini hakutaja maneno yapi na lugha za uchochezi alizotoa Mbunge huyo.

Novemba Mosi mwaka huu, Kamanda Mkumbo akiwa anazungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, alitaja maneno ya uchochezi anayodaiwa Lema kutaja kuwa ni: “Mheshimiwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania akiendelea kukandamiza demokrasia,siasa za ukandamizaji taifa litaingia katika umwagaji wa damu,nchi hii inaandaliwa kwenda katika utawala wa kidikteta,”

Rais Magufuli Aishauri Benki ya Dunia kutoa Mikopo kwa wakati unaofaa ili utekelezaji wa miradi ufanyike kwa haraka.

$
0
0
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 03 Novemba, 2016 amekutana na Mwakilishi wa Benki ya Dunia katika nchi za Tanzania, Burundi, Malawi na Somalia Bi. Bella Bird na kuzungumzia utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini Tanzania yenye thamani ya jumla ya Dola za Marekani Bilioni 1.6 zikiwa ni mkopo kutoka benki hiyo.

Akizungumza baada ya kumaliza mazungumzo yake na Rais Magufuli, Bi. Bella Bird amesema mikopo hiyo inalenga kusaidia juhudi za maendeleo nchini Tanzania na itatolewa katika sekta mbalimbali zikiwemo nishati, usafirishaji, elimu na maji.

"Miradi hii yote imelenga zaidi kuharakisha maendeleo na kuleta matokeo katika maisha ya Watanzania, ni miradi ambayo inahitaji uongozi na msukumo mzuri kutoka Serikalini na tunafurahi kwamba Rais Magufuli ni kiongozi ambaye ana dhamira ya dhati ya kusimamia maendeleo" amesema Bi. Bella Bird.

Kwa upande wake Rais Magufuli ameishukuru Benki ya Dunia kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania katika maendeleo na ametoa wito kwa Benki hiyo kuharakisha utoaji wa mikopo kwa ajili ya kutekeleza miradi.

"Tunataka kuona mambo yanatokea badala ya kutumia muda mwingi kuzungumza, miradi hii ina manufaa makubwa kwa watanzania na tungependa utekelezaji wake ufanyike haraka, na ili ufanyike haraka Benki ya Dunia inapaswa kutupatia mikopo kwa wakati unaofaa" amesisitiza Rais Magufuli.

Aidha, Rais Magufuli amemhakikishia Bi. Bella Bird kuwa Serikali yake ya Awamu ya Tano imejipanga kusimamia utekelezaji wa miradi yote inayotekelezwa sasa na itakayoanza kutekelezwa katika siku zijazo kwa mkopo kutoka Benki ya Dunia.

Kwa hivi sasa miradi 26 yenye thamani ya Jumla ya Dola za Marekani Bilioni 4.5 inatekelezwa hapa nchini kwa mkopo kutoka Benki ya Dunia.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam

03 Novemba, 2016

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Ijumaa ya Novemba 4

Waziri Mkuu: Serikali Haijafilisika

$
0
0

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema hadi kufikia Oktoba mwaka huu, Serikali imekwishapeleka zaidi ya sh. bilioni 177 kwenye halmashauri mbalimbali nchini ili kutekeleza miradi ya maendeleo.

Ametoa kauli hiyo jana (Alhamisi, Novemba 3, 2016) Bungeni mjini Dodoma wakati akijibu swali lililoulizwa na Mbunge wa Viti Maalumu, Bibi Munde Tambwe aliyetaka kupata kauli ya Serikali kuhusu ucheleweshwaji wa fedha za bajeti ya maendeleo katika halmashauri mbalimbali nchini.

“Kwa kuwa Serikali ina mifumo, miongozo, sheria na taratibu za kupeleka fedha kwenye halmashauri mara baada ya kikao cha bajeti. Mheshimiwa Waziri Mkuu unatoa kauli gani kuhusu ucheleweshwaji wa fedha hizo katika halmashauri nchini zikiwemo za mkoa wa Tabora? Alihoji Mheshimiwa Munde.

Akijibu swali hilo, Waziri Mkuu alisema:“Baada ya Bunge kuridhia na kutoa mamlaka ya matumizi ya fedha, Serikali ilianza kujiridhisha uwepo wa mfumo sahihi ya makusanyo na mapato na matumizi yake. Ni kweli kwamba Serikali yetu baada ya kikao cha bajeti inawajibika kutekeleza maamuzi ya Bunge kwa kupeleka fedha zilizopangwa.”

Waziri Mkuu alisema Serikali ilianza kupeleka watumishi watakaosimamia ukusanyaji mapato katika halmashauri zote nchini. Kutathmini miradi yote iliyoanza ambayo haijaendelezwa pamoja na mipya ili kutambua thamani na kisha kupeleka fedha.

Alisema Serikali itaendelea na upelekaji wa fedha kwenye halmashauri kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo. Alizisisitiza halmashauri hizo kuendelea kukusanya mapato ndani ili kuongezea bajeti kwa fedha wanazopelekewa na watumie mfumo wa kielektroniki ili kudhibiti mapato hayo.

Aidha, Waziri Mkuu alizitaka halmashauri zote nchini zihakikishe fedha zinazopelekwa katika maeneo yao zinatumika kama ilivyokusudiwa kwa miradi husuka. Aliwasihi Wabunge wafuatilie na wasimamie matumizi ya fedha hizo ili miradi iliyopangwa iweze kukamilika.

Wakati huo huo; Waziri Mkuu alisema Serikali haijafilisika na kuhusu suala la mfuko wa jimbo bado unatambulika na fedha zitapelekwa kwenye majimbo na wabunge watajulishwa kiasi kilichopelekwa ili waweze kuratibu miradi yao ya maendeleo.

Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo wakati akijibu swali la mbunge wa jimbo la Ukonga Mheshimiwa Mwita Waitara aliyetaka kupatiwa kauli ya Serikali kuhusu kutopelekwa kwa fedha za mfuko wa jimbo.

Pia Mheshimiwa Waitara alilalamikia kitendo cha jimbo lake kutengewa fedha kidogo katika mgawo wa mfuko wa jimbo ambazo ni sh. milioni 16 licha ya kuwa na wananchi wengi huku jimbo la Segerea alilosemma lina watu wachache likitengewa sh. milioni 33. Aliiomba Serikali ingalie upya ugawaji huo kulingana na mazingira ya jimbo husika.

Waziri Mkuu alisema kumejitokeza matatizo kwenye halmashauri zenye majimbo zaidi ya moja na Serikali inaendelea kufanya sensa kutambua idadi ya wananchi kwenye majimbo hayo ili itakapopeleka fedha iweze kuzingatia idadi hiyo na kuwawezesha wabunge kupanga miradi ya maendeleo.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,

TMA yatahadharisha nchi kukumbwa na ukame

$
0
0

Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini (TMA) - imeendelea kuwataka Wakulima kufuatilia kwa ukaribu Taarifa za hali ya hewa pamoja na kuzingatia maelekezo ya wataalamu wa kilimo.

Hatua hiyo inatokana na uwepo wa dalili za upungufu wa mvua katika mwezi Novemba kwenye maeneo mengi nchini jambo ambalo linaweza kuathiri uzalishaji katika kilimo.

Hayo yamebainishwa jana Jijini Dar es salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini Dkt. Agnes Kijazi alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari ambapo alisema hadi sasa bado kuna viashiria vingi vya upungufu wa mvua ikiwa ni pamoja na kupungua kwa Joto katika eneo la kati la Bahari ya Pasifiki kitendo ambacho kinafahamika kama LANINA.

Alibainisha kuwa hali hiyo inapojitokeza husababisha ukame hivyo kwa wakulima kuzingatia maelekezo ya wataalam wa kilimo kwa kulima mazao ya muda mfupi na yanayostahamili ukame.

Dkt. Kijazi aliongeza kuwa Mamlaka hiyo imekuwa ikifuatilia kwa ukaribu mienendo ya ya unyevunyevu katika maeneo mbalimbali nchini pamoja na Joto katika Bahari ya Hindi ambapo imebainika kuwa hali ya unyevunyevu inaendelea kupungua katika maeneo mbalimbali nchini huku Joto katika Bahari ya Hindi ikionekana kuendelea kupungua mambo ambayo ni dalili za upungufu wa mvua na ukame.

Aidha Dkt. Kijazi alizungumzia tatizo la kutokea kwa mvua za mawe katika baadhi ya maeneo nchini ambapo alibainisha kuwa tatizo hilo linasababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa ambayo hupelekea kutokea kwa aina ya mawingu inayofahamika kama mawingu ng’amba hivyo suala hilo halina sababu za kuhusianishwa na Imani za kishirikina kama ambavyo baadhi ya watu wamekua wakidhania.

Lugora: Mawaziri acheni kumpotosha Rais

$
0
0

MBUNGE wa Mwibara, Kangi Lugora (CCM) amewaonya baadhi ya mawaziri kutompotosha Rais John Magufuli kuwa fedha zimepotea, kutokana na baadhi ya watu kuficha majumbani kwenye magodoro wakati hiyo si sababu.

Sambamba na hilo, amewaonya wabunge wa upinzani, kuacha kuwatumia vibaya wananchi na kuwachonganisha na Rais wao, baada ya kuona wamebanwa kulipa kodi.

Mbunge huyo alitoa onyo hilo jana wakati akichangia Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2017/2018 na Mwongozo wa kuandaa mpango wa bajeti ya serikali kwa mwaka 2017/2018 uliowasilishwa juzi na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango.

“Nyinyi mawaziri ni abiria na mmekaa siti za mbele kwenye gari analoendesha Rais Magufuli msimkimbize, baadhi yenu msimpotoshe rais yeye si mchumi mtamletea matatizo mbeleni, pesa zimepotea si kwa sababu zimefichwa kwenye magodoro ila zimepotea kwa sababu pesa zote zimewekwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), zitoeni pesa hizo ziende kwenye mabenki,” alisema.

Alisema Bunge limepoteza mwelekeo, limekuwa la kulialia na kumlaumu Rais Magufuli kwa sababu amebana wakwepa kodi na kufafanua “Rais aliliomba Bunge hili limsaidie kutumbua majibu, tumsaidie mipango ya serikali iweze kutekelezeka ili kujenga nchi yetu, najua Rais ana nia njema na nchi, Hapa Kazi Tu inawafanya wafanyabiashara waliozoea kukwepa kodi wamebanwa sasa wanalia biashara imekufa, watumishi waliozoea posho za hapa na pale, kusafiri wamebanwa, wabunge tuliozoea kula andazi la inchi 18 sasa tunakula la sentimita mbili, kwenye kamati tumebanwa posho, tunalialia kisa tumeshikwa pabaya na kuwaingiza wananchi wanyonge eti hawana pesa.

"Kiongozi wa Upinzani, Freeman Mbowe umepewa gari na serikali na mafuta unawekewa, yamejaa kwenye gari, kiyoyozi kipo saa 24 unasema serikali imefilisika huku unawachonganisha wananchi na Rais wao, unawatumia vibaya wananchi, Msigwa kama Mchungaji (Peter, Mbunge wa Iringa Mjini) tumia taaluma yako kuwashauri wenzako wawe kwenye safari hii... Rais Magufuli anatupeleka Kaanani kuishi maisha mazuri, ametupandisha basi kutupeleka nchi ya ahadi.

"Nashauri anapoendesha gari ajue kuna matuta, akiendesha vibaya Watanzania atatuangusha, kuna zebra na wanafunzi wanavuka, akiona spidi iko 50 apunguze mwendo... na nyinyi mawaziri mmekaa siti za mbele za gari la Rais, msimpotoshe”, alifafanua.

Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde(CCM) alisema ni lazima uchumi unapokua, uoneshe kwenye maisha ya wananchi wa vijijini ; na si kuonesha ujuaji wa pointi kwenye makaratasi.

Alisema “Upinzani msizunguke kusema serikali imefilisika, semeni ukweli, Mbowe umefilisika, umeshindwa kulipa madeni, serikali haijafilisika, inalipa mishahara, inalipa madeni yake”.

Naye Mbunge wa Bunda Mjini, Esther Bulaya (Chadema) alisema kila sehemu kuna njaa, mtaani wananchi wanalia hakuna pesa na hata wabunge wamepauka kwa kukosa fedha.

Walimu Watatu Watiwa Mbaroni Kwa Kuwazuia Wanafunzi Kufanya Mtihani wa Kidato cha Nne

$
0
0

POLISI mkoani Dodoma inawashikilia walimu watatu wa shule za sekondari kwa tuhuma ya kuwazuia wanafunzi wa kidato cha nne, kufanya Mtihani wa Taifa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa alisema kwamba walimu hao wa shule za sekondari za Zoissa na Mnyakongo wilayani Kongwa, walikamatwa Novemba Mosi mwaka huu.

Kamanda Mambosasa alisema kwamba, wakati wa mtihani wa somo la Kiingereza, walimu hao walimzuia mwanafunzi Amina Said wa shule ya sekondari Zoissa kwa madai ya kuwa ni mjamzito na kumpeleka kituo cha afya, kupimwa muda wa mtihani, lakini majibu yalionesha hakuwa na ujauzito.

Aidha, mwanafunzi Bahati Ntigonza wa shule ya sekondari Mnyakongo, alizuiliwa kuingia katika chumba cha mtihani kwa kuwa hakuvaa sare ya viatu, hivyo alirudishwa nyumbani kuvaa viatu huku wenzake wakiendelea na mtihani.

Kamanda Mambosasa aliwataja watuhumiwa waliokamatwa kuwa ni Lukonge Mwezo ambaye ni Mkuu wa Shule ya Sekondari Mnyakongo, Omari Athumani Mkuu wa Shule ya Sekondari Zoissa na Daud Suleimani John aliyekuwa mwalimu wa zamu katika shule ya sekondari Mnyakongo.

Kesi ya kwanza yaanza Kusikilizwa Mahakama ya Mafisadi Dar

$
0
0

Hatimaye Mahakama Kuu Kitengo cha Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi maarufu kama Mahakama ya Ufisadi imeanza rasmi usikilizaji wa kesi jana.

Kesi ya kwanza kutua na kusikilizwa na Mahakama hiyo ambayo inatokana na ahadi za Rais John Magufuli aliyoitoa wakati wa kampeni zake ni ya uhujumu uchumi inayowakabili Mtanzania mmoja na raia wa China na mwingine wa India. 

Kwa pamoja washtakiwa hao wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi wakidaiwa kukutwa na nyavu haramu za kuvulia samaki zilizopigwa marufuku zenye thamani ya zaidi ya Sh7.4 bilioni.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na kesi ya msingi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, lakini wamefungua maombi ya dhamana katika Mahakama hiyo na hivyo kuweka rekodi ya kuwa kesi ya kwanza kusikilizwa.

Hata hivyo, maombi hayo yamewekewa pingamizi na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), akipinga washtakiwa hao kupewa dhamana akidai yamefunguliwa kwenye Mahakama isiyo sahihi.

Pingamizi hilo lilisikilizwa jana na Jaji Rehema Mkuye na baada ya hoja za pande zote alipanga kutoa uamuzi Novemba 14.

Wakati wa usikilizwaji wa pingamizi hilo mvutano mkali wa kisheria uliibuka baina ya upande wa mashtaka na utetezi kuhusu tafsiri ya Mahakama Kuu.

Wakili wa Serikali Mkuu (PSA), Timon Vitalis alidai kuwa sheria inatamka kuwa Mahakama Kuu na siyo Mahakama ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.

Wakili huyo alidai Mahakama hiyo (ya ufisadi) inakuwa na uwezo wa kutoa dhamana pale kesi ya msingi inakuwa tayari imeshafunguliwa mahakamani hapo.

Hata hivyo, wakili wa washtakiwa hao, Roman Lamwai alipinga hoja hizo akidai Mahakama hiyo ni mahali sahihi kwa mujibu wa tafsiri ya Sheria ya Uhujumu Uchumi kama ilivyofanyiwa marekebisho.

Alisisitiza kuwa hata ukubwa wa gharama zinazohusika katika kesi ni lazima maombi hayo yafunguliwe kwenye Mahakama hiyo yenye jukumu la kusikiliza na kuamua kesi za rushwa na uhujumu uchumi.

Moja ya vigezo vya kesi zinazofunguliwa katika Mahakama hiyo ni kiwango cha fedha za rushwa au uhujumu uchumi kinachohusika ambacho ni kuanzia Sh1 bilioni.

Hata hivyo, DPP anaweza kufungua kesi mahakamani hapo chini ya kiwango hicho kulingana na mazingira maalumu kadri atakavyoona kuwa inafaa.

Katika kesi ya msingi inayosikilizwa na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, Godfrey Mwambapa kwenye shitaka la kwanza washtakiwa Feng na Kerenge wanadaiwa kutenda kosa la uhujumu uchumi kwa kuagiza nyavu haramu nje ya nchi.

Rais Magufuli kufanya mahojiano na waandishi wa habari LEO

$
0
0

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 04 Novemba, 2016 atafanya mahojiano ya kwanza na waandishi wa habari tangu aingie madarakani mwaka mmoja uliopita.
 
Mahojiano haya yatarushwa moja kwa moja na vituo vya habari vya redio na televisheni kutoka ukumbi wa Ikulu Jijini Dar es Salaam na yataanza saa 4:00 asubuhi.
 
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais inapenda kuwaalika wananchi wote kusikiliza na kutazama mahojiano hayo ili mpate fursa ya kujua mambo mbalimbali ambayo Mheshimiwa Rais atayatolea majibu. 
 
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam

LIVE KUTOKA IKULU: Matangazo ya Moja Kwa Moja ya Rais Magufuli Akilihutubia Taifa Muda Huu

Ufafanuzi wa tuhuma za Freeman Mbowe Kwa wabunge wa CCM kupewa rushwa ya mil 10

$
0
0
Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe jana alisababisha taharuki katika kikao cha Bunge baada ya kuzusha tuhuma za rushwa kwa wabunge wa CCM katika kipindi cha maswali na majibu na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Ingawa swali lake hilo lenye tuhuma lilizuiwa kujibiwa na Naibu Spika, Dk Tulia Akson kwa kuwa halikuwa swali la kisera, hoja iliibuliwa tena na wabunge wengine wakati wa kuingia kipindi cha majadiliano, kama miongozo.

Mbowe katika swali lake kwa Waziri Mkuu alituhumu wabunge wa CCM, kupewa rushwa ya Sh milioni 10 kila mmoja na serikali ya chama hicho ili kuupitisha Muswada wa Huduma za Habari unaowasilishwa bungeni leo.

Aidha alidai rushwa hiyo, pia imetolewa kupitisha Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2017/18. Pamoja na tuhuma hizo kutojibiwa na Waziri Mkuu kutokana na muundo wa maswali ya papo kwa hapo kugusa sera, Mbunge wa Momba, David Silinde (Chadema) aliomba mwongozo wa Spika huku akitaka kuundwe Tume Huru ya Kimahakama ya Bunge, kuchunguza tuhuma hizo.

Naye Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia (CCM) alisimama na kuomba mwongozo, na kumtaka Mbowe athibitishe tuhuma hizo au achukuliwe hatua.

Nkamia alisema yeye akiwa Mbunge wa CCM, hajapata rushwa hiyo wala hakuiona na kuhoji kwa nini Mbowe ahoji wakati yeye si Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), hivyo akitaka Mbowe athibitishe tuhuma hizo na akishindwa, alitaka mwongozo ni hatua gani Bunge itamchukulia.

Akijibu hoja zote hizo za wabunge, Naibu Spika alimtaka Mbowe kupeleka tuhuma zake kwa vyombo husika ili vichukuliwe hatua stahiki.

Akifafanua zaidi, Naibu Spika katika majibu yake ya miongozo hiyo alisema :“Wabunge tuwe makini, ukisema kuna rushwa ujue kuna vyombo vyake maalumu vya kushughulikia hilo, Bunge haliwezi kusikiliza kesi hizo, Bunge na Waziri Mkuu hawana mamlaka kwa mambo yasiyohusiana nayo, nashauri suala hilo lipelekwe kwenye vyombo husika.”

Kuhusu mwongozo wa Nkamia, alisema kwamba hatomtaka Mbowe athibitishe kwani alimzuia kuliongelea, lakini mwenye uthibitisho apeleke kwenye chombo kinachohusika na rushwa ili kifanye kazi yake.

Mbowe aitisha mkutano
Baada ya tafrani hiyo kuzuka bungeni na kumalizwa na Naibu Spika kwa kutoruhusu mjadala wake, Mbowe aliitisha mkutano na waandishi wa habari katika ukumbi wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Bunge mjini hapa, akiwa na Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu na viongozi wengine wa Chama cha Wananchi (CUF).

Katika mkutano huo, Mbowe alimtaka Rais Magufuli kumtumbua Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa kile alichoeleza kuwa yeye (Majaliwa) pamoja na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana walihusika kutoa kwa wabunge hao wa CCM 272 fedha hizo.

Alisema pia kuwa, wanamuandikia barua Rais kutaka aunde Tume ya Kimahakama ya Uchunguzi, kuchunguza suala hilo kwa kuwa linawahusu wabunge, na Bunge haliwezi kujichunguza lenyewe.

Akifafanua kuhusu fedha hizo, Mbowe alisema taarifa walizonazo, zinathibitisha kuwa katika kikao cha wabunge wa CCM cha Oktoba 25, mwaka huu, Majaliwa na Kinana waligawa fedha Sh milioni 10 kwa kila mbunge wa CCM ili kuwapooza kuhusu hali ya mdororo wa uchumi.

Alisema pia kuwa fedha hizo, zilizoanza kutolewa Oktoba 26, zililenga pia kuwashawishi wabunge hao wa CCM, kupitisha Muswada wa Huduma za Habari wa mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2017/18, ambao mapendekezo yake yamewasilishwa bungeni.

Mbowe alisema tuhuma hizo ni nzito na Bunge haliwezi kujichunguza lenyewe, hivyo ni lazima iundwe tume huru ya kimahakama kuchunguza jambo hilo. Mbowe alisema ushahidi wa kutosha wanao na watautoa mbele ya tume hiyo.

Mbowe alisema walimshangaa Naibu Spika, Dk Akson kwa kuwazuia kutoa ushahidi ndani ya Bunge, kama walivyoombewa mwongozo na Nkamia. Alieleza kuwa hiyo ni mara ya kwanza kwa upinzani, kuzuiwa kutoa ushahidi kwa jambo, ambapo linaonekana kama ni uongo.

Lisu naye azungumza
Kwa upande wake, Lissu alisema watamuandikia Rais Magufuli barua rasmi kueleza kilichofanywa na viongozi wake, na kumtaka achukue hatua kuhusu suala hilo.

“Magufuli amejinadi yeye anapambana na ufisadi, mtihani wa pili aufanye na aufaulu ni huu. Magufuli amtumbue Kassim Majaliwa kutoka kwenye nafasi hiyo ya uwaziri mkuu,” alisema Lissu.

Lissu alisema Sheria ya Tume za Uchunguzi, inampa Rais mamlaka ya kuunda tume ya uchunguzi kwenye jambo kubwa na muhimu, linalohusu mambo ya umma.

“Katika barua hiyo tunamgusia Tulia Ackson. Kwa maoni yangu kisheria, kiongozi wa kuteuliwa anaondolewa na mamlaka ya uteuzi, Rais amuondoe huyu mama bungeni, hafai,” alisema Lissu.

Viongozi wa CUF waliokuwa katika mkutano huo ni pamoja na Mbunge wa Viti Maalum, Riziki Mngwali.

Awali, ndani ya Bunge baada ya Naibu Spika kuzuia swali hilo kwa kuwa si la kisera, Mbowe akinukuu Sheria ya Maadili ya Utumishi wa Umma ya mwaka 1995 na Sheria ya Rushwa ya mwaka 2007, alisema masuala ya rushwa ni ya kisera.

Hata hivyo, Dk Akson alimtaka Mbowe kuheshimu kiti na kanuni, na kusisitiza kuwa, yeye (Naibu Spika) anaongozwa kwa kanuni na kanuni zinaeleza kuwa swali hilo si la kisera.

Taarifa ya hatua iliyofikiwa katika mchakato wa ujenzi wa reli ya standard gauge

$
0
0
Serikali ya Awamu ya Tano ndani ya mwaka mmoja imeanza mipango ya kuboresha usafiri wa reli ya Kati kwa kuijenga kwa kiwango cha kimataifa yaani Standard Gauge. Usafiri huu utaongeza fursa za kiuchumi kwani mazao ya chakula na biashara toka mikoa ya Kigoma, Kagera, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Tabora na Singida kuelekea Dar es Salaam yatasafirishwa kwa haraka.

Reli hii itarahisisha pia usafiri wa abiria wa mikoa ya Kanda ya Ziwa, Kati na Magharibi. Usafiri wa treni kwa kiwango kikubwa huwa ni wa uhakika na wa gharama nafuu. Hivyo ujenzi wa reli kwa Standard Gauge uteleta ukombozi mkubwa wa kiuchumi kwa watu wa maeneo hayo na Taifa kwa ujumla.

Kwa kipindi kirefu huduma ya usafiri wa treni kupitia Reli ya Kati (Central Line Railway) imekuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa mkoa wa Kigoma na maeneo ya Kanda ya ziwa na nchi za jirani zikiwemo Burundi, Rwanda, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Historia inaonesha kuwa Reli ya Kati kama inavyojulikana sasa ilijengwa kati ya mwaka 1905 hadi 1914 wakati huo ikiitwa Reli ya Tanganyika kwa kuwa ilikuwa ikielekea Mkoani Kigoma ambako Ziwa Tanganyika linapatikana.

Kutokana na umuhimu wake katika kukuza uchumi kupitia usafirishaji bidhaa na huduma mbalimbali ndani na nje ya Tanzania, Katika mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali imeamua kuja na mpango kabambe wa kuifanyia maboresho miundombinu ya reli hiyo ili iweze kwenda na wakati na kasi ya ukuaji wa uchumi.

Mpango huo unahusisha ujenzi wa mtandao wa Reli mpya ya Kati katika Viwango vya Kimataifa (Standard Gauge 80’) ili kuendana na kasi ya ongezeko la mizigo.

Msemaji wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Bw. William Budoya anaeleza kuwa gharama iliyokaidiriwa kutumika kukamilisha mradi huo ni Dola za Kimarekani Bilioni 7.6 ambazo ni sawa na shilingi za Kitanzania Trilioni 16.

Fedha hizo zitatumika kugharamia ujenzi wa Kilomita 2,561 za reli kwa kiwango cha Kimataifa . Ili kufanikisha mradi huo Serikali imepata ufadhili kutoka Benki ya Exim ya China ambayo imekubali kutoa mkopo wenye masharti nafuu.

Aidha, katika kuhakikisha kuwa ujenzi huo unafanikiwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli anakutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Benki ya Exim ya China Bw. Liu Liang Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Katika mazungumzo yao Rais wa benki hiyo anamuhakikishia Rais Dkt. John Magufuli kuwa Benki hiyo iko tayari kutoa kiasi hicho cha fedha ili kufanikisha ujenzi wa kilometa 2,190 za reli. Pia anamuhakikishia Rais kuwa Benki hiyo itashirikiana na Tanzania katika kubadilishana uzoefu na utaalamu katika ujenzi na uendeshaji wa reli hiyo.
 
Akiuzungumzia ujenzi wa Reli hiyo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli anabainisha kuwa kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kuinua uchumi wa Tanzania na nchi jirani zisizopakana na bahari zikiwemo Uganda, Rwanda, Burundi, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Anasema reli hiyo mpya itakua tofauti na inayotumika sasa kutokana na uwezo wake wa kuhimili usafirishaji wa mizigo mingi kwa kuwa inajengwa kwa kiwango cha Kimataifa “Standard Gauge railway ” na itaanzia Dar es Salaam Mpaka Kigoma, kupitia Tabora, Mwanza,Isaka hadi Rusumo; Kaliua -Mpanda -Karema na Uvinza -Musongati nchini Burundi.

Katika ufafanuzi alioutoa hivi karibuni kuhusu ujenzi wa reli hiyo wakati wa Mkutano Mkuu Maalum wa Chama cha Mapinduzi mjini Dodoma hivi karibuni, Rais John Pombe Magufuli alisema tayari mchakato wa ujenzi wa reli hiyo umeanza kwa kutangaza zabuni ili kumpata mkandarasi atakaye jenga Reli hiyo.

Anasema sambamba na kazi hiyo Serikali itakarabati matawi ya reli ya kati sehemu ya Kaliua-Mpanda ili kuboresha ufanisi wake, kwa kutenga Sh. bilioni 5.5 za ajili ya usanifu.

Aidha, Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano uliowasilishwa bungeni Dodoma na Waziri wa Fedha na Mipango ,Dk. Philip Mpango unaeleza kuwa Serikali imejipanga kufanya usanifu na ujenzi wa madaraja 16 kati ya 28 yaliyochakaa kati ya Dar es Salaam na Tabora.

Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Servaciaus Likwelile akizungumza mara baada ya utiaji saini wa makubaliano wa ujenzi wa reli hiyo kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Naibu Meneja Mikopo Nafuu wa Benki ya Exim ya China Bw. Zhu Ying anasema kuwa Dola za Kimarekani bilioni 7.6 ambazo ni sawa na Shilingi Trilioni 16 zitatumika kutekeleza mradi huo.

Dkt. Likwelile anasema hatua hiyo inawezesha kuanza kwa kazi ya upembuzi yakinifu, usanifu na uundwaji wa timu za pamoja kuanza kuainisha mahitaji halisi ya ujenzi wa mradi huo.

Anasema mradi huu umekuja wakati muafaka kutokana na kwamba reli iliyopo sasa ambayo ni ya Kiwango cha “meter gauge” haina uwezo mkubwa katika ubebaji wake wa mizigo, hata baada ya kufanyiwa ukarabati.

Kwa mwaka ni tani Milioni 5 za mizigo ndizo zinaweza kupitishwa na reli ya sasa, ambazo haziwezi kukabili mahitaji ya mizigo ya Kanda hii ambayo itafikia tani Milioni 30 ifikapo mwaka 2025.

Kutokana na uhitaji huo wa kukabiliana na uongezaji wa mizigo kwa kujenga uwezo wa kuihudumia kwa kuwa na reli ambayo pamoja na kuwa na uwezo wa kubeba mizigo hiyo itakuwa na uwezo wa kubeba abiria wengi zaidi na kwa starehe lakini pia kwa kasi ya spidi ya wastani wa kilometa 100 kwa saa hivyo kuwezesha abiria kufika haraka zaidi sehemu wanazokwenda.

Pia wakati wa ujenzi wa reli hiyo watanzania takribani 300,000 watapata ajira kutokana na kushiriki katika ujenzi wa reli hiyo.

Na Frank Shija, MAELEZO

Yaliyojiri Kutoka Ikulu: Mahojiano ya Rais John Magufuli na Wahariri wa Vyombo vya Habari

$
0
0
Rais Magufuli: Niwashukuru sana kwa michango yenu mikubwa katika maeneo yenu ya kazi.

Swali(Tido Mhando): Ulichukua muda kuunda baraza la mawaziri, Je Katika tathmini hiyo wanafanya kazi kulingana na ulichotegemea wakifanye

Jibu(Magufuli): Serikali niliyounda imenisaidia sana na wanafanya kazi zao vizuri, niliona niwe na baraza la watu wachache katika kuwatumikia wananchi, changamoto zipo lakini nina imani kubwa.

Swali(Lulu Sanga TV 1): Kuna changamoto kubwa sana ya dawa, watoto wengi wanakufa kutokana na kukosa dawa, unaoneje ukibana matumizi kupata dawa ukazigawa hospitali kubwa au kampeni kama ile ya madawati.

Jibu(Rais Magufuli): Katika bajeti yetu tumetenga bilioni 1.99 na tumeongeza bajeti ya kununulia madawa karibu mara kumi. Tumebadilisha utaratibu badala ya kununua kutoka kwa suppliers sasa tunanunua moja kwa moja kutoka viwandani pia kuna nchi zinataka kuwekeza kujenga viwanda vya kutengeneza madawa hapahapa.

Swali kuhusu kukandamiza demokrasia:

Jibu: Katika kazi yoyote Sijakandamiza demokrasia ndio maana unaona bunge linaendelea na chaguzi zinaendelea hata hapa wamechagua UKAWA, demokrasia ina mipaka yake, baada ya uchaguzi lazima watu waendelee na production

Swali(Tido)-Nyongeza: Kuna watu wanasema unataka kuelekea kwenye udikteta

JIBU: Tafsiri kila mmoja ana yake na kila mmoja ana uhuru wa kufukiria anavyofikiria hata wewe Tido ulihama BBC, TBC na sasa uko Azam, mwingine anaweza kufikiri uko ulikokuwa kulikuwa na udikteta wa aina fulani.

Swali(Rioba): Unasisitiza uchumi wa viwanda, Tanzania imeshawahi kuwa na viwanda vikafa, kuna watu wanaona hili swala waachiwe watu binafsi, wewe unaoneje?

Jibu: Ilani inasema tunataka kujenga nchi ya viwanda, huwezi kutegemea serikali katika kujenga viwanda ndio maana nikasema kuna makampuni kutoka Kenya na sio makampuni ya watu binafsi.

Swali(Mtanzania): Serikali imeweka mkazo kwenye kupambana na majangili lakini tishio ni kubwa,

Jibu(Rais Magufuli): Umezungumza ukweli na ni changamoto ila pia ina historia yake, sheria ya mifugo ya mwaka 59 ila tumejipanga kuhakikisha haya masuala yasije yakawa parmanent na tumeibadilisha wizara ya maliasili na nimeteua majenerali kuongoza wizara nadhani umeshajua tunataka kufanya nini. Hatuna viwanda vya nyama nchi hii ndio maana mifugo haina pakwenda.

Swali(Magazeti ya serikali): Ni nini mkakati wa kuwafanya watanzania kuona fursa katika sekta nyingine

Jibu(Rais Magufuli): Sisi kama serikali ni kuwaelimisha waweze kutumia fursa zilizopo katika nchi nyingine, mfano sisi tunasifika kwenye Kiswahili, kila mmoja ajipange badala ya kusubiri serikali. Fursa zipo ikiwemo EAC na SADC ambako Tanzania ni mwanachama. Ni wajibu sisi wa watanzania kuchangamkia fursa.

Swali(Tido Mhando): Ulitilia mkazo Rushwa na ufisadi, mwaka mmoja sasa unasemaje?

Jibu(Rais Magufuli): Matunda yameanza kuonekana, nidhamu kazini imeanza kuonekana, tumepitisha sheria ya mafisadi na kesi ya kwanza imeanza kusikilizwa jana. Rushwa na swala mtambuka na haliwezi kushughulikiwa na Rais peke yake. Nitoe wito kwa watanzania wote tukatae Rushwa, ni kansa ya maendeleo.

Swali(Rioba): Kuna maswala umeyasimamia kwa ujasiri ikiwemo ujangili na dawa za kulevya, nini kinakuumiza kichwa

Jibu(Rais Magufuli): Yanayoniumizwa kichwa ni mengi pamoja na swali lako, yale niyoahidi katika miaka mitano bado sijayamaliza na hayawezi kumalizika ndani ya mwaka mmoja. Kwenda mbele unahitaji support ya watu wengi. Mwenyezi Mungu pamoja na support ya watanzania.

Swali(Tuma-Radio Tumaini): Hongera sana, Kura yangu ilifanya kazi, Walemavu wa chini hali bado ni mbaya, tunazo sheria nyingi tunaishukuru serikali. Mazingira yetu(walemavu) bado ni magumu, tunaomba watu wa chini watu iwaangalie.

Jibu(Rais Magufuli): Nimelipokea ombi lako na tutaendelea kulishughulikia na serikali inajali sana walemavu kwani hata sisi ni walemavu wa kesho, nimeunda wizara maalum ya walemuavu, nimewateua walemavu katika baraza langu ikiwemo Dr Possy, Amon Mpanju.

Swali(Bakari Machumu Mwananchi): Viwanda na utajiri wa madini, umeelezea umuhimu wa PPP, kuna wafanyabiashara wanahisi wanatengwa, upande wa madini, tunaunganisha vipi

Jibu(Rais Magufuli): Wafanyabiashara hawajatengwa na tunawahitaji sana, na mimi nawapenda kweli wafanyabiashara lakini nataka wanaolipa kodi. Mfanyabiashara ambae hajalipa kodi anawaumiza ambao wamelipa kodi, ukishakua na wafabiashara wa aina mbili unawaumiza wanaolipa. Palikuwa na mamabo ya hovyo, sitaki kwenda kwenye detail sana maana mambo mengine yapo mahakamani, wafabiashara matapeli siwapendi.

Jibu(Rais Magufuli): Kuhusu madini, ni kweli nchi hii ina madini mengi sana, madini yanatakiwa kunufaisha nchi hii, siku moja yatakwisha, nina uhakika sasa mambo yataanza kwenda vizuri baada ya kusaini regulations. Sisi tuna mafuta pia, tutaunganisha bomba la hoima kwenda Tanga, Tanzanite inapatikana Tanzania tu lakini nchi iliyoongoza kuuza ni India ikifuatiwa na Kenya. 


Sasa hivi umeanzishwa mnada hapa. Watu wanasafirisha makontena kwenda nje kusafishwa na sisi wenyewe tunayasindikiza. Kwa nini tusitengeneze hapa, haya ndio ndio najaribu kuyazungumza ili nchi yetu isiendelee kuibiwa, kwenini kila sehemu kwenye madini kuna kiwanja cha ndege, hili sio suala la Rais pekee ili pesa zinazopatikana ziwanufaishe watanzania wote. Unachosema ni sawa na kinachotakiwa sasa kusonga mbele.

Swali(Joseph Kulambwa): Tanzania ya viwanda, serikali imejipangaje kutrain mafundi mchundo kuliko wasimamizi wa viawanda

Jibu(Rais Magufuli): Vyuo vya kati tulivibadilisha kuwa vyuo vikuu, ilikua bad direction ndio maana sasa tunajenga vyuo vya VETA ikiwezekata kila mkoa. Hata chuo cha usafirishaji kimekua chuo kikuu na inawezakana kwa sababu kulikua na mikopo ambayo hairudishwi ndio maana sasa kuna deni la trilioni 3.5.

Swali: Wafanyakazi hewa wameondolewa lakini bado mishahara inayolipwa ni mikubwa?

Jibu(Rais Magufuli): Siku za nyuma kuna madai mengi ambayo yamepelekea serikali kulipa kiasi cha bilion 22.6 na bado kuna madai 39,000 yenye thamani ya sh bilioni 23
Suala la OC bado halitakuwepo kwani mambo yanaenda vizuri.
Aidha serikali itaendele kulipa madeni ya walimu na wakandarasi wanaodai.

Swali(Angalieni Mpendu): Suala la utamaduni na maadili, umeliwekaji katika utawala wako?

Jibu(Rais Magufuli): Jukumu la ku-maintain utamaduni wetu ni la kila mtanzania, kuna wizara inayoshughulika suala hili. Kila mtanzania ana wajibu wa kutunza utamaduni wetu.
Vyombo vya habari vitoe ushrikiano kwa kuhakikisha utamaduni wetu unakuwa mzuri.

Swali(Bukuku): Serikali ya china na Tanzania ni Marafiki, Unaonaje kama ungefanya mazungumzo ma Wachina kukawa na ushirikiano katika mafunzo na mashine ndogondogo?

Jibu(Rais Magufuli): Nimeshazungumza nao, wachina wamekubali na wanataka kuchukua eneo la Bagamoyo wajenge viwanda 1000. Pia tumezungumza na serikali ya India katika suala kama hilo hilo. Tumezungumza na serikali ya Morocco na kutakuwa na ndege ya moja kwa moja kutoka Kasablanca hadi JNIA.

Tumeweka fedha katika benki ya TIB kwa ajili ya kukopesha wajasiriamali. Tatizo ni kwamba watu wanakopa lakini hawarudishi ikiwemo wanasiasa. Tatizo la waandishi wa habari hawaaniki watu hawa.

Swali(Tido Muhando): Mchakato wa katiba Mpya umefikia wapi?

Jibu(Rais Magufuli): Katika kampeni yangu hakuna sehemu ambayo nimezungumzia suala la Katiba Mpya, hata hivyo suala la katiba mpya limefika mahali pazuri lakini niacheni kwanza ninyooshe nchi.

Swali(Edoni Mwanika): Kwa nini miswada ya habari inakuwa haipewi muda wa kutosha kujadiliwa na huletwa kidharura tu?

Jibu(Rais Magufuli): Sheria yeyote ina misingi yake, mchakato wa sheria hizi umeanza toka mwaka 2010 hadi mwaka huu, hakuna muda sahihi ungetosha kujiandaa.

Hata hivyo hili ni suala ambalo lipo ndani ya maamuzi ya bunge hivyo siwezi kuingilia,
Punde musuada huu utakaponifikia nitaisaini na kama ni marekebisho yatafuata.

Swali(Frank): Umeokoa kiasi gani kwa kutosafiri nje? umechukua hatua gani kuhakikisha ukanda wa Afrika mashariki unakuwa salama? Suala la diaspora kutoweza kuwa tena raia wa Tanzania unalizungumziaje?

Jibu(Rais Magufuli): Fedha tulizookoa ni mabilioni, hata hivyo siyo kwamba hatusafiri kabisa ila tunahakikisha kunakuwa na uwakilishi ambao unapunguza gharama.

Tumekuwa tunashughulikia migogoro inayoendelea, DRC nimemtuma mwenyekiti wa mawaziri kwenda ili kutafuta suluhu. Suala la migogoro linadiliwa mezani, Burundi tumemteua Mh Mkapa na anasuluhisha na mambo yanaenda vizuri.

Kuhusu diaspora lipo kisheria zaidi.

Swali(Sanga): Una maoni gani katika ishu ya Zanzibar na Utawala bora?

Jibu(Rais Magufuli): Hali ya Zanzibar ni nzuri, wamefanya uchaguzi wao vizuri na Dr Shein anafanya vizuri na mambo yanaenda vizuri

Swali(Manyere): Upi ni msimamo wetu kuhusu Morocco; Je Ikulu haiwezi kuandaa tuzo kwa waandishi wanaondika mambo mazuri kuhusu nchi?

Jibu(Rais Magufuli): Tanzania ni nchi isiyofungamana na upande wowote na hivyo tuna uhuru wa kushirikiana na nchi yeyote.
Hata hivyo Moroco tunashirikiana nao katika kukuza biashara

Vyombo vya habari vinafanya kazi nzuri kwelikweli,
Nashirikiana na kila mtu hata Masoud anavyonichora kichwa kimevimba hapa, nashirikiana naye.

Swali(Pasco Mayala): Ulitumia mamlaka gani kuamuru bunge na mahakama kufanya unayoyataka? ulitumia mamlaka gani kuzuia mikuatana ya kisiasa?

Jibu(Rais Magufuli): Serikali ndiyo inahusika na kugawa fedha zote kupitia bajeti, fedha zikitumika vibaya anayehusika ni serikali.

Swali: Unalizungumziaje suala la ajira? Umekuta mambo yapoje ikulu? Na ulikuwa unatazamia nini

Jibu(Rais Magufuli): Ajira zilikuwa hazijazuiliwa, serikali imetoa ajira za madaktari na manesi wa hospitali ya Rweganzira.
Zuio la ajira lilikuwa la muda tuu. Mpaka sasa kuna benki iliyorudisha fedha za wafanyakazi hewa kiasi cha shilingi bilioni 6.7.

Serikali inaajiri kwa uangalifu mkubwa ili kuhakikisha suala la wafanyakazi hewa
Serikali imeajiri zaidi za watumishi 5000 kwenye vyombo mbalimbali.

Serikali inaendelea kuboresha maslahi ya wakulima kwa mfano wa korosho; Kilo ya korosho imeongezeka bei kutoka shilingi 600 hadi sh 4000.


Credit: JF

Rais Magufuli ajibu madai ya kukandamiza demokrasia na Udikteta

$
0
0

Rais John Magufuli ameyatolea majibu malalamiko yaliyokuwa yakitolewa na baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani nchini kuwa amekuwa akikandamiza demokrasia tangu alipoingia madarakani.

Akijibu swali lililoulizwa na mmoja kati ya wahariri wa vyombo vya habari leo Ikulu jijini Dar es Salaam, aliyetaka ufafanuzi kuhusu malalamiko hayo, Rais Magufuli alisema kuwa hajawahi kukandamiza demokrasia nchini na kwamba anachofanya ni kuihuisha.

“Katika kazi yoyote, critic ni kitu cha kawaida na pongezi ni kitu cha kawaida. Lakini ukweli ni kwamba katika muda wote ambao nimechaguliwa kuwa Rais sija-suppress democracy (sijakandamiza demokrasia) na bahati nzuri ninapromote demokrasia,” alisema Rais Magufuli.

“Na ndio maana unaona Bunge linaendelea vizuri. Na ndio maana unaona uchaguzi unafanyika hata hapa Dar es Salaam kuna maeneo wamechagua Ukawa na kuna maeneo wamechagua CCM. Hiyo ni demokrasia. Mikutano yao ya ndani ya vyama mmekuwa mkishuhudia, na hivi juzijuzi kumekuwa na mkutano wa chama fulani, wakagombana wenyewe na wakafukuzana wenyewe,” aliongeza.

Aidha, akijibu swali la nyongeza lililoulizwa na mwanahabari mkongwe, Tido Mhando (Azam TV) kuhusu mtazamo wa baadhi ya watu kuwa huenda anaendesha mambo kidikteta bila kufuata taratibu zilizowekwa, Rais Magufuli alisema hiyo ni tafsiri ya mtu ambayo inatokana na uhuru wa kufikiria.

“Kila mmoja anaweza akatafsiri vyovyote… wewe(Tido) ulipokuwa BBC ukahama ukaenda TBC, ukahama leo uko Azam, mtu mwingine anaweza akatafsiri kuwa huenda huo ni udikteta wa namna fulani wa kuhamishwahamishwa. Kwa hiyo kila mmoja ana uhuru wa kufikiria anavyofikiria,” alisema.

Rais Magufuli leo amefanya mkutano na Wahariri wa vyombo vya habari kwa lengo la kujibu maswali yao

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Jumamosi ya Novemba 5

Rais Magufuli Awataka Watanzania Kutumia Fursa Zilizopo

$
0
0
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli amewataka watanzania kutumia fursa zilizopo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) kwa ajili ya kuliletea maendeleo ya taifa.

Aliyasema hayo jana Jijini Dar es Saalam wakati wa mkutano wake na Wahariri wa vyombo vya habari nchini katika kuadhimisha mwaka mmoja wa Utawala wake, ambapo alisema kuwa ipo haja ya kuzungumza na kuelimisha watanzania juu ya fursa zilizopo katika taasisi hizo.

“Katika Jumuiya hizo zipo fursa nyingi kwa ajili ya maendeleo ingawa inahitajika elimu ya kutosha kwa watanzania kuona fursa zilizopo ikiwemo ufundishaji wa lugha ya Kiswahili nchi za nje” alisema Rais Magufuli.

Mbali na hayo, akizungumza kuhusu suala la kupambana na Rushwa nchini Rais Magufuli alitoa wito kwa vyombo vinavyohusika na kupambana na rushwa kufichua watu wote wanaojihusisha na vitendo hivyo.

Rais Magufuli alisema kuwa vita ya Rushwa ni ya kila mwananchi, ambapo alitoa wito kwa watanzania wote kwa ujumla kujiepisha na masuala ya rushwa kwani rushwa ni kansa ya maendeleo nchini.

“Taifa litakwama tukiacha suala la rushwa liendelee, tumeumia kweli kweli katika hili hivyo nitoe wito kwa watanzania wote kwa ujumla kujiepusha na masuala haya kwa ajili ya maendeleo ya nchi kwani kesi ya rushwa ni yetu sote” alifafanua Rais Magufuli.

Magufuli: Vyombo Vya Habari Simamieni Kujenga Maadili Na Utamaduni Wa Mtanzania

$
0
0
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.John Pombe Magufuli ametoa wito kwa vyombo vya Habari nchini kuwa mbele katika kusimamia Maadili na kuutangaza Utamaduni wa Mtanzania.

Rais Magufuli aliyasema hayo jana Ikulu Jijini Dar es Salaam wakati wa Mahojiano ya mwaka na waandishi wa habari kwa mara ya kwanza tangu aingie madaraka.

“Jukumu la kulinda Utamaduni na Maadili ya mtanzania ni la kila mzalendo, mtanzania, mzazi na Wizara husika ipo kwa ajili ya kusimamia jambo hili na vyombo vya habari mnatakiwa kuwa mstari wa mbele kulisimamia kwa kuanzia katika vyombo vyenu vya Habari kutokana na kile mnachoonyesha”Alisema Rais Magufuli.

Aidha Rais Magufuli alivitaka vyombo vya Habari kuwa wazalendo katika kutengeneza vipindi vyenye mahadhi ya kitanzania ili kuisaidia jamii kukua katika utamaduni wetu na kusaidia kujenga maadili yaliyo bora.

Mbali na hayo Rais Magufuli alizungumzia mafanikio mbalimbali yaliyopatikana katika kipindi chake cha mwaka mmoja toka aingie madarakani ikiwemo kuongezeka kwa mapato kutoka bilioni 800 mpaka makusanyo ya shilingi trilioni 1.5 kwa mwezi.

Pia alisema kuwa Bajeti ya mwaka 2016 ya trilioni 29.5 iliyotenga asilimia 40 kwenye miradi ya maendeleo imekuwa yenye mageuzi makubwa ukilinganisha na bajeti ya miradi hapo nyuma mabayo ilikuwa asilimia 26 tu.

Pamoja na hayo Rais magufuli alisema kuwa Serikali imeagiza ndege nyingine mbili zambazo inategemewa kufika nchini mwanzoni mwa mwaka 2018 ili kuboresha sekta ya utalii nchini.

Akizungumzia uundwaji wa serikali alisema mategemeo yake katika serikali aliyoiunda imefanikiwa kwa kuwa Baraza aliloliunda la watu wachache limekuwa la mafanikio makubwa na hili limetokana na ushirikiano mkubwa wa mawaziri wake.

Rais Magufuli alivitaka vyombo vya habari nchini kubadili mtazamo wao katika uandishi wao wa habari na kuandika habari ambazo zina maslahi kwa Taifa na kuwahakikishia waandishi wa habari kushirikiana nao kwa kuwa anatambua kazi nzuri wanayoifanya.

Majibu ya JPM kwa wanahabari kuhusu muswada wa Sheria ya Huduma za Habari 2016

$
0
0

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Magufuli amesema kuwa huu ni wakati mwafaka kwa muswada wa sheria ya huduma za vyombo vya habari kukubaliwa na kuwa sheria kwa vile tasnia ya habari inakumbwa na changamoto nyingi zitakazotatuliwa na sheria hiyo.

Akizungumza na wahariri pamoja na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari jana, Ikulu jijini Dar es Salaam Rais Magufuli alisema kuwa muswada huo ni wa muda mrefu na sasa ni wakati mwafaka kwa vile tansia ya habari inakumbwa na changamoto nyingi zinazoweza kutatuliwa na muswada huo.

“Hii sheria ya huduma za vyombo vya habari imechelewa kwa vile mchakato wake ulianza tangu mwaka 2011 hadi sasa mwaka 2016 wadau walikuwa na muda wa kutosha wa kujiandaa na kutoa maoni yao ambayo yangeweza kuboresha muswada huo” alisema Rais Magufuli

Ameongeza kuwa, Sheria hii italeta mabadiliko katika tasnia ya habari kwa vile kutakuwepo na Bodi ambayo itashughulikia masuala ya taaluma ya habari, pamoja na mambo mengine yaliyoanishwa katika muswada huo ambayo ni maslahi ya waandishi wa habari nchini.

Muswada huu unatazamiwa kuwajengea uwezo waandishi wa habari ili waweze kufanyakazi kitaalamu kwa kuandika na kutangaza habari zenye ukweli zitakazochangia katika harakati za kuleta maendeleo kwa nia ya kuwasaidia watanzania na serikali kwa ujumla katika kufikia malengo yake.

Muswada wa Sheria ya huduma za habari umesomwa jana Novemba 4, 2016 katika kikao cha tano cha Bunge na mkutano wa 11, ambapo utajadiliwa na kufuata taratibu zingine kabla ya kuwa sheria. 

==>Msikilize hapo chini akiongea
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live




Latest Images