Quantcast
Channel: MPEKUZI
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live

IPTL yageuziwa kibao Sakata la Escrow.......Yatakiwa Kuirejeshea Tanesco Bilioni 216

0
0
Kampuni  ya Kufua Umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) imegeuziwa kibao katika suala la Escrow, imefahamika.


Kampuni hiyo imetakiwa kurejesha zaidi ya Dola za Marekani milioni 100   (Sh bilioni 216.2 ) kwa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco)  zikiwa fedha za  ziada ambazo  ililipwa kabla ya hesabu kufanywa upya.

Hatua hiyo inatokana na uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Biashara uliotolewa Septemba 12 mwaka huu unaoitaka Tanesco kuilipa Chartered ya Hong Kong (SCB-HK) Dola za Marekani milioni 148.

Mahakama hiyo ilitoa uamuzi huo kutokana na kesi iliyofunguliwa na Benki ya Standard Chartered ya Hong Kong (SCB-HK) dhidi ya Tanesco ikidai kulipwa Dola za Marekani milioni 369.

Kwa mujibu wa Wakili wa Tanesco, Richard Rweyongeza, amesema walichokuwa wanabishania mahakamani si Tanesco kulipa bali walikuwa wanabishania shirika hilo litalipa kiasi gani na linamlipa nani.

“Kabla hatujaingia katika kutetea kesi hiyo, mwaka 2014 mahakama hiyo ilisema inayo madaraka na ikaamuru Tanesco kuilipa  SCB-HK.

“Sisi tuliingia kutetea baada ya uamuzi huo,  Mei, 2014 tukaomba hesabu zifanyike upya kwa malekezo yaliyotolewa na mahakama hiyo  kujua deni halisi.

“Hesabu zilipofanyika kwa mtaji wa mwekezaji, walichukua mkopo wakahesabu kuwa ni mtaji, hatua hiyo ilikataliwa na mahakama.

“Kabla ya hesabu kufanyika ndipo likaingia suala la akaunti ya Tegeta Escrow. Fedha zilipochukuliwa katika akaunti hiyo, SCB-HK wakabadilika wakasema hakuna haja ya kufanya hesabu upya kwa sababu Tanesco wamekubali viwango hivyo ndiyo sababu waliwalipa IPTL.

“Tulibishania hoja hiyo ya kulipa kwa viwango vya zamani ikaamuriwa hesabu zifanyike upya, mahakama ilikubali hesabu ifanyike kwa kutumia mkopo wa wana hisa.

“Baada ya kuamuru hivyo, deni likashuka kutoka walichokuwa wakidai Dola za Marekani milioni 369 hadi kuamuriwa kulipa Dola za Marekani milioni 148,”anasema Wakili Rweyongeza.

Alisema IPTL walilipwa Dola za Marekani milioni 246 kwa kutumia viwango vya zamani na kwamba uamuzi uliotolewa unaanza kutumika katika kipindi chote ambacho Tanesco ilikuwa inadaiwa mpaka mwaka 2015.

“Kutokana na hesabu hizo gharama ilikuwa chini, IPTL ililipwa zaidi hivyo inatakiwa kurejesha Dola za Marekani zaidi ya milioni 100 kwa Tanesco,”alisema.

Rweyongeza alisema walipendekeza SCB-HK wadai fedha zao kwa IPTL lakini mahakama hiyo ilikataa na kuamuru Tanesco ndiyo walipe hivyo kwa mtazamo wa kawaida IPTL inatakiwa kurejesha fedha kwa shirika hilo.

Katika kuhitimisha, mahakama hiyo ilisema pande zote mbili zinazopingana zilishinda katika maeneo muhimu waliyokuwa wakibishania lakini zilipoteza katika hoja nyingine.

Baada ya kumaliza kusikiliza kesi hiyo mahakama iliamuru pande hizo mbili kulipa gharama za usuluhishi na nyingine kwa viwango sawa.

Malipo hayo na anayelipwa katika mabano ni Dola za Marekani 254,775.02 (Profesa MC Rae), Dola 171,278.36 (Profesa Douglas) na Dola 370,126.76 kwa ajili ya Profesa Stem.

Gharama nyingine zilizokadiriwa moja kwa moja ni Dola za Marekani 157,336.26 na gharama za utawala kwa mahakama hiyo Dola za Marekani 180,000 ambako jumla ya gharama zote wanazotakiwa kulipa Tanesco na SCB-HK ni Dola za Marekani 1,133,516.42.

Hata hivyo Rweyongeza alisema pamoja na ushindi huo hawakuridhishwa na uamuzi huo kwa sababu katika uamuzi wa kwanza, mahakama hiyo ilikataa hesabu kupigwa kwa kutumia kiwango cha 22.31 lakini bado katika uamuzi huu walitumia kiwango hicho kufanya hesabu hivyo walikosea kufanya hivyo.

Hoja ya pili, alisema SCB-HK si mwekezaji hivyo hakustahili kupeleka kesi hiyo mahakamani na kwamba hapakuwa na hoja.

“Sababu nyingine ya kutoridhishwa na uamuzi huo ni kwamba hatukupewa nafasi ya kujibu hoja mpya zilizowasilishwa kuhusu Tanesco kwamba ilidanganya, tulipaswa kujibu kwa maelezo ya mashahidi si mawakili.

“Tuliwasilisha hoja kwa maandishi, zilipotokea hoja mpya tulitakiwa kuzijibu kwa kuleta mashahidi, tunapinga pia uamuzi ulioitambua SCB-HK kuwa ilistahili kisheria,”alisena Rweyongeza.

Suala hilo limeibuka ikiwa imepita miaka mitatu tangu Serikali kupitia Mwanasheria Mkuu wa Serikali na viongozi wa Wizara ya Nishati na Madini kuruhusu kufanyika kwa malipo ya Dola za Marekani milioni 200 (zaidi ya Sh bilioni 300) kutoka katika Akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa imefunguliwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Fedha hizo zilitolewa na kwenda kwa mmiliki wa Kampuni ya Pan Africa Power Solutions Tanzania Limited (PAP), Harbindar Singh Sethi mwenye makazi yake nchini na Afrika Kusini.

Katika kesi hiyo Tanesco ilikuwa inawakilishwa na mawakili wa kampuni za R.K Rweyongeza & Advocates na Crax Law Partners.

Chanzo cha Escrow
Mwanzoni mwa miaka ya 1990  nchi ilikuwa na upungufu wa umeme kutokana na upungufu wa maji kwenye mabwawa, ambapo 1994 serikali ilitoa kazi ya uwekezaji kwa IPTL ilikuwa iliyokuwa ikimilikiwa na VIP ya Tanzania iliyokuwa na asilimia 30 na Mechmar ya Malaysia yenye asilimia 70.

Tanesco na IPTL walisainiana mkataba wa miaka 20, hata hivyo uzalishaji haukuanza mara moja kutokana na mgogoro ulioibuka baina yao (Tanesco na IPTL) .

Mwaka 2002  IPTL ilianza kuzalisha umeme na mkataba ukaanza kuhesabiwa hapo, lakini kutokana na mgogoro ikafunguliwa akaunti ya Escrow na mwaka 2004 Tanesco ilifungua shauri kupinga tozo la Capacity Charge

Uwiano wa mtaji ni 70 kwa 30 na uamuzi haujabadilishwa na mahakama yoyote. Mwaka 2004 Kampuni ya Mkono &  CO advocates iliishauri Tanesco iendelee kupinga Capacity Charge London.

Inaelezwa kuwa Agosti 2005, benki ya SCB-HK ilinunua kwa bei ya punguzo ya dola za Marekani 76.1 kutoka Benki ya Malaysia ya Danaharta baada ya kushindwa kurejesha deni la muda mrefu kutoka IPTL.

Bei halisi ya deni hilo ilikuwa ni dola milioni 101.7 kwa mujibu wa ushahidi uliopo ambako IPTL ilikopa dola milioni 100 mwaka 1998 kutoka kwa mbia wa benki ya Malaysia ili kujenga mtambo wa kufua umeme wa megawati 100 wa Tegeta.

Kwa mujibu wa  makubaliano hayo, SCB-HK ilipewa kandarasi kadhaa ikiwamo haki ya kulipwa deni la 1997, ambako mkataba wa utekelezaji na hatia ya makubaliano ya dhamana iliyosainiwa  kati ya IPTL na Serikali.

Fedha zilivyotolewa
Akaunti ya Tegeta Escrow ilifunguliwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kuhifadhi fedha za malipo ya tozo ya ufuaji umeme baada ya Tanesco kuingia kwenye mgogoro na Kampuni ya IPTL  na  suala hilo lilipelekwa mahakamani.

Kwa mujibu wa masharti ya uendeshaji wa akaunti ya Escrow, fedha zilitakiwa zitolewe baada ya Mahakama kutoa uamuzi wa mgogoro huo, lakini wakati ilitaka pande hizo mbili zikutane na kukokotoa viwango vya tozo, fedha hizo zilitolewa na kulipwa mmiliki wa Kampuni ya Pan Africa Power Solution (PAP) jambo lililosababisha kuibuka  kashfa hiyo.

Ilivyotua bungeni
Aliyekuwa wa kwanza kulifikisha bungeni suala hilo ni aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, ambaye aliwalipua baadhi ya mawaziri wa Serikali ya awamu ya nne kuhusika na mpango huo.

Hatua hiyo ilisababisha Spika wa Bunge la 10 kuagiza uchunguzi wa vyombo vya dola  kuweza kuchimbua kwa undani wizi huo.

Baada ya kukamilika ilikabidhiwa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAP) chini ya aliyekuwa Mwenyekiti wake Zitto Kabwe na Makamu wake, marehemu Deo Filikunjombe.

Novemba 28 mwaka  2014, Bunge la 10 lilitoa maazimio manane kuhusu suala  hilo huku Harbinder Singh Sethi, James Rugemalira  wa (VIP), aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Umeme wa Umeme Tanzania (TANESCO) walionekana kuhusika kwa namna moja au nyingine katika kufanikisha kufanyika miamala haramu ya fedha za Akaunti ya Escrow ya Tegeta kwenda Pan African Power Solutions Ltd (PAP) na VIP.

Bunge pia liliazimia mawaziri wa wakati huo wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo,  Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Fredrick Werema, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini wa kati huo, Eliachim Maswi na wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa TANESCO wawajibishwe kwa kuishauri mamlaka yao ya uteuzi kutengua uteuzi wao.

Mawaziri hao walipoteza nyadhifa zao huku Profesa Muhongo akijiuzulu na Tibaijuka uteuzi wake ukifutwa na Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete.

Credit: Mtanzania

Mwalimu Ahukumiwa Miaka Mitatu Jela Kwa Kuomba Rushwa ya Sh. 130,000

0
0

Mahakama  ya Hakimu Mkazi ya Bukombe mkoani Geita imemhukumu Mwalimu wa Shule ya Msingi Umoja, Daniel Nyingati kwenda jela miaka mitatu au kulipa faini ya Sh milioni 1.6 baada ya kupatikana na makosa ya  kuomba na kupokea rushwa.

Hukumu hiyo ilitolewa juzi na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Bukombe, Gabriel Kurwijila.

Alisema  mshitakiwa Nyingati amekutwa  na hatia ya kuomba  rushwa ya  Sh 130,000 kutoka kwa Marco Elias  aweze kumdahili mtoto wake aliyekuwa amehitimu  masomo ya shule ya msingi kinyume na sheria.

Hakimu Kurwijila alisema   ushahidi ulitolewa mahakamani pande zote mbele ya  waendesha mashitaka kutoka  Taasisi ya Kuzuia na Kudhibiti Rushwa Tanzania (Takukuru), Kelvin Murusuri na  Husna Kiboko umejitosheleza na kumtia hatiani mwalimu Nyingati.

Alisema mahakama inamhukumu mwalimu Nyingati kwenda jela miaka mitatu au kulipa faini ya Sh milioni 1.6 kwa kuwa alitenda kosa la kuomba na kupokea rushwa.

Serikali yaonya dhidi ya kampuni za ajira Zinazotapeli Watu

0
0

WIZARA ya Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu imetaka wananchi kuepuka kampuni za uwakala wa ajira nchini ambazo hutangaza nafasi za ajira huku zikiwataka waombaji kulipia ili kusailiwa.

Msemaji wa Wizara hiyo, Ridhiwan Wema jana  alisema kampuni za namna hiyo hawazitambui na hivyo hazina usajili wa kufanya shughuli hiyo nchini.

“Hizi kampuni sisi hatuzitambui, mtafuta kazi hatakiwi kutozwa fedha isipokuwa kampuni inaingia makubaliano na mwajiri ambaye amempa kazi ya kumtafutia wafanyakazi,” alisema Wema.

Alitaka wananchi wawe makini na wasikurupuke kutuma maombi kabla ya kujiridhisha kama kampuni zimesajiliwa na ili kupata taarifa sahihi, mwombaji anaweza kufika Wizara ya Kazi na kuuliza, kwa kuwa wao ndio wasajili pia wakibaini uwepo wa kampuni hizo watoe taarifa wizarani na Polisi ili hatua za kisheria zichukuliwe.

Aidha, aliwasihi wananchi hususan vijana, wasiwe wepesi kulipia gharama, kwa sababu huduma ya ajira haipaswi kutozwa fedha kwa kuwa si haki kutoa kazi kwa masharti ya kulipwa, hali ambayo inaashiria vitendo vya rushwa.

Wema alibainisha kuwa kampuni zinazofanya shughuli za uwakala wa ajira nchini zimesajiliwa na Wizara ambapo moja ya masharti yanayotakiwa kuzingatiwa ni pamoja na kutowatoza waombaji wa nafasi za ajira zinazotangazwa.

Alisema kuna vigezo vingine pia vinavyozingatiwa, ili kukidhi usajili ambapo huainishwa kwa majina na taarifa za mahali pa kudumu zilipo ofisi za kampuni na kufahamu kama zimesajiliwa kwenye mamlaka husika, mfano Brela, hayo yote ni kwa ajili ya kufanya urahisi wa kizifuatilia pindi kunapozuka utata.

Aliongeza kwamba vigezo vingine ni kujiridhisha kama ina wataalamu wa kutosha kwenye masuala ya ajira, ambapo baada ya kujiridhisha husajiliwa na kuzitangaza kwenye vyombo vya habari.

Wema alitaka wananchi watambue kuwa kampuni zinazotangaza nafasi za ajira huku zikitaka waombaji walipie fedha kwa ajili ya usaili si salama kwao, hivyo wanatakiwa kuepukana nazo na kutoa taarifa.

Nuh Yusuf ambaye ni Ofisa wa kampuni ya Zoom ambayo ni wakala wa ajira nchini, alisema sababu kubwa ya kuendelea kwa utapeli wa mtandao ni kukosekana kwa ushikiano wa karibu na vyombo vya sheria hususan Jeshi la Polisi katika kudhibiti suala hilo.

“Tumejaribu kufuatilia suala hilo TCRA kitengo cha TZ-CERT, tukashauriwa twende Polisi na mmoja ambaye alipatwa na hilo tatizo, tulipofika kituo cha Polisi cha Oysterbay hawakuonesha ushirikiano wowote,” alisema Yusuf.

Bodi kutotoa mikopo kwa wadahili wapya baada ya TCU kushusha viwango

0
0

BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), imesema haiwezi kutoa mikopo kwa waombaji wapya walioomba baada ya Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) kushusha viwango vya udahili.

Wiki iliyopita, TCU ilitangaza kushusha viwango vya udahili bila kueleza sababu za kufanya hivyo.

Mkurugenzi Msaidizi wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa HESLB, Cosmas Mwaisobwa, amesema tume  hiyo haiwezi kuongeza muda kwa wanafunzi wapya kwa ajili ya kuomba mkopo kutokana na mchakato huo kufungwa.

Amesema tofauti na tume ya vyuo vikuu ambayo inaweza kufungua udahili na kutoa majina ya wale waliopata nafasi ndani ya siku tatu, HESLB huhitaji muda mrefu kupitia taarifa za waombaji hadi kutoa matokeo.

Kuhusu marejesho ya mikopo kwa wahitimu wa elimu ya juu waliokopeshwa na bodi hiyo, Mwaisobwa amesema idadi kubwa ya wadaiwa na waajiri wamejitokeza kulipa madeni yao na kuhakiki taarifa za madeni yao.

“Idadi kubwa ya wadaiwa wamejitokeza kulipa na kuhakiki taarifa zao, pia hata waajiri wengi wamejitokeza na kuthibitisha hili ni kwamba mapato tuliyokusanya yameongezeka kwa kiasi kikubwa” amesema Mwaisobwa.

Amesema wanaokaidi kulipa, watambue kuna sheria zitakazowabana, ikiwa ni pamoja na vifungo na penati, lakini hilo halitangulizwi bali mpaka mkopaji aonekane kukaidi.

Kikwete Atunukiwa Tuzo Ya Uongozi Wa Kisiasa Na Utetezi

0
0

 Na  Mwandishi Maalum, New York

Shirika lisilo la  Kiserikali    la Speak  Up for Afrika    limemtunukia tuzo, Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete kutokana na uongozi wake wa kisiasa na utetezi wake  kwa  makundi ya jamii yaliyo katika mazingira magumu hususani wanawake na watoto.
 
Utoaji wa  Tuzo hiyo  ya  uongozi wa kisiasa na utetezi , umekwenda sambamba na   hafla ya  miaka mitano ya kuanzishwa kwa  Taasisi ya Speak up  Afrika. Hafla  hiyo iliyofanyika jana Alhamisi Jijini New York   ilikuwa  pia  ni sehemu ya kuhamasisha uchangiaji   wa shughuli za  Taasisi hiyo.
 
Mchango ambao umetambuliwa na  Speak Up  Afrika,   taasisi ambayo imekuwa ikifanya kazi  kwa Karibu na Rais Mstaafu Kikwete, ni  katika maeneo ya  upelekaji na usambazaji wa huduma za msingi za afya hususani afya ya mama na mtoto,  udhibiti wa  ugonjwa  wa malaria kupitia kampeni  ya malaria haikubaliki ,usambazaji wa vyandarua  vyenye viatilifu, kampeni ya  lishe bora, na  kampeni ya   chanjo kwa watoto.
 
Pamoja  na  kutambua  juhudi za   Rais Mstaafu  Kikwete katika  kuyasemea maeneo hayo,  Taasisi hiyo kupitia  Mkurugenzi wake  Mtendaji Bi. Kate Campana pia imemtambua  kama kiongozi ambaye    amekuwa mstari wa mbele  wa kulisema Bara la Afrika kila  mara alipopata  fursa  ya  kufanya hivyo wakati akiwa madarakani na hata baada ya kustaafu.
 
Rais kikwete ameelezwa katika hafla hiyo iliyowashirikisha  wadau wa kada mbalimbali, kama kiongozi wa kisiasa ambaye amezigusa nyoyo za watu wengi kujitolea kwaajili ya watu wenye mahitajio ya kupata huduma za msingi za kijamii ambazo  au wameshindwa kuzipata kutokana na kipato kidogo au haziwafikii kabisa.
 
Akipokea  Tuzo hiyo, Rais  Mstaafu Kikwete , amesema Tuzo hiyo ni ya watoto wote  waafrika ambao ndio  waliomfanya asimame   mbele ya wageni waalikwa.
 
“ Ni kwa sababu yenu ndio sababu nimetenga muda wangu  baada ya kustaafu kusukuma mbele agenda ya  kuboresha maisha yanu. Ninafanya hivyo kwasababu makuzi yangu yalikuwa kama  ya mtoto yeyote yule wa  kiafrika, nimeyaishi maisha  wanayo ishi. Na kwa hiyo ninaelewa fika  hamu na kiu yao ya kuwa  na maisha bora na afya njema”. Akasema Kikwete na kushangiliwa na wageni waalikwa.
 
Akaongeza kuwa  ,  mafaniko ambayo ameyapata katika  juhudi hizo  za kufikisha huduma za msingi  za kijamii kwa makundi  yenye mahitaji  yametokana na mambo mawili makubwa moja ni   aina ya uongozi  alioutumia kusukuma harakati hizo. Na pili  uhamasishaji uliofanyika katika  kupiga vita malaria kupitia Speak Up Afrika na    kampeni yao ya  malaria haikubaliki.
 
“ Nisingeweza kuyafanya niliyoyafanya   bila uungugwaji mkono na  ushirikiano  wa karibu nilioupata  na ninaoupata kutoka taasisi za kimataifa  ikiwamo hii ya  Speak Up  Afrika. Ndio maana  kwa mfano,  tumeweza kupunguza visa vya malaria kwa   theluthi mbilli,  tumefanikisha  upatikanaji wa chanjo kwa asilimia 96 kwa watoto wote na kupunguza vifo vitokanavyo na  malaria kwa   nusu.” Akaeleza Kikwete na kushangiliwa  tena.
 
Akasema, anamini katika ushirikiano na wadau mbalimbali  kama akina Ray Chambers kupitia kampeni ya  hakuna tena malaria, Taasisi ya  Bili na Melinda Gates na Gavi Vaccination   Alliance ambayo anashirikiano  nayo kwa karibu katika  kampeni ya chanjo kwa wote.
 
Rais  Mstaafu amewahakikishia   watendaji wa Speak  Up Afrika kwamba  ataendelea kufanya kazi nao kwa karibu  kutokana  kile alichosema amejionea mwenye kazi nzuri wanayoifana.
 
 Akawasihi  wadau mbalimbali  kuichangia taasisi hiyo  kwa kile alichosema, inafanya kazi kubwa  ya siyo tu kufikisha huduma za kijamii pale zinapotakiwa lakini  pia imekuwa ni kipaza sauti cha Afrika.
 
Wengine waliopewa Tuzo kwa kutambua michango yao kwa jamii ni  pamoja na   Professa Awa Marie Coll- Seck, Waziri wa Afya  wa Senegal, Bibi Toyin  Saraki,  mwanzilishi wa Taasisi ya  Wellbeing  Afrika ambayo  pia imekuwa ikitoa  elimu na misaada kwa wanawake na watoto pamoja na elimu  kwa wakunga na kutambua kazi nzuri, kubwa na ngumu  ya kuwahudumia wanawake wenzao wanapojifungua.  Na  Bwana Kabirou Mbodje ambaye ni Mkurugenzi mtendaji wa  Taasisi ya  Wari.
 
Taasisi ya  Speak  Up  Afrika  imeanzishwa  na wanawake na inaongozwa na wanawake. Ni taasisi ambayo imejijengea uweo na sifa kubwa ndani  ya kipindi cha miaka mitano tangu  kuanzishwa kwake.  

Rais Magufuli atengua uteuzi wa Mtendaji Mkuu wa TTCL.......Amteua Bw. Waziri Waziri Kindamba Kuchukua Nafasi Hiyo

0
0

Kufuatia hatua ya Serikali kununua hisa zote za Bharti Airtel ambaye alikuwa mbia mwenza wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) na hivyo Serikali kumiliki hisa za Kampuni hiyo kwa asilimia 100, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, amemteua Bw. Waziri Waziri Kindamba kuwa Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL.

Bw. Waziri Waziri Kindamba ameteuliwa kushika nafasi hiyo kuanzia leo tarehe 23 Septemba, 2016.

Kufuatia uteuzi huo, aliyekuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL Dkt. Kamugisha Kazaura atapangiwa kazi nyingine.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam

23 Septemba, 2016

Mhadhiri chuo kikuu mbaroni kwa kumkashfu Rais Magufuli

0
0

Idadi ya watu wanaokamatwa kwa tuhuma za kumkashfu Rais John Magufuli kupitia mitandao ya kijamii imezidi kuongezeka baada ya polisi kumkamata Mhadhiri wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu cha Mkwawa (Muce), Dk Oscar Magava (48).

Dk Magava amekuwa mtu wa kumi kukamatwa na polisi katika kampeni za jeshi hilo kudhibiti uhalifu chini ya sheria ya uhalifu wa mtandaoni.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Julius Mjengi alisema Dk Magava alikamatwa akiwa Sumbawanga na alirudishwa mkoani Iringa.

Mjengi alisema Septemba 15, mwaka huu walipata taarifa kuwa mhadhiri huyo anatumia mitandao ya kijamii kumkashfu Rais. Alisema waliamua kumsaka na walipopata taarifa kuwa Dk Magava amekwenda Sumbawanga waliwasiliana na polisi wa huko wakamkamata na kumrudisha Iringa.

Hata hivyo, Kamanda Mjengi hakuyataja maneno aliyotumia Dk Magava kumkashfu Rais kwa madai kuwa bado wanaendelea na uchunguzi na kwamba ukikamilika atafikishwa mahakamani.

Kamanda Mjengi aliwatahadharisha wananchi kuwa makini na matumizi ya mitandao ya kijamii kwa kuitumia kwa ajili ya maendeleo na si kutukana wala kukashfu viongozi au watu wengine.

Watu mbalimbali wamekuwa wakikamatwa na kufikishwa mahakamani kwa kosa la kumkashifu Rais au jeshi la polisi.

Picha : Lowassa alipotembelea waathirika wa tetemeko la ardhi Bukoba

0
0
Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, Edward Lowassa, leo amewasili Bukoba mkoani Kagera kuwatembelea na kuwajulia hali waathirika wa tetemeko la ardhi.

Tetemeko la ardhi lililotokea Bukoba mkoani Kagera Septemba 10 lilisababisha vifo vya watu 19 huku wengine zaidi ya 250 wakiachwa na maejeraha mbalimbali.

Alipofikika katika uwanja wa ndege wa Bukoba, Edward Lowassa aliyeambatana na  Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema , Sheikh Katimba, Khamis Mgeja na Mbunge wa Bukoba Mjini, Wilfred Lwakatare waliongozana hadi eneo la Hamugembe na Kashai kujionea madhara ya tetemeko la ardhi.

Akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa maeneo hayo, Lowassa aliwapa pole sana kwa yote yaliowafika na kusisitiza kwamba anaamini serikali itachukua jukumu la kuwasaidia.

Aidha, amesema kuwa msaada wake yeye atampatia Mkuu wa Mkoa, Meja Jenerali Mstaafu, Salum Kijuu ili uweze kuwasaidia wananchi wa Kagera.

Shirika La Ndege La Tanzania (Atcl) Lapewa Miezi 3 Kufumua Uongozi Uliopo.

0
0

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ametoa miezi mitatu kwa Bodi mpya ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kusuka upya uongozi uliopo ili kuweza kuleta ufanisi wa utendaji kazi wa Shirika hilo.

Akizungumza jijini Dar es salaam mara baada ya kuitambulisha Bodi hiyo, Waziri Mbarawa amesema kuwa Uteuzi wa Bodi hiyo utasimamia kuleta tija na ufanisi wa shirika hilo ambalo kwa kipindi kirefu lilikuwa na changamoto nyingi.

“Nataka kuona mabadiliko makubwa kuanzia kwenye Menejimenti hadi uongozi wa chini, hakikisheni mnaweka uongozi amabao utafuata maadili, utakuwa na ufanisi, ubunifu na kasi katika utendaji kazi” amesema Profesa Mbarawa.

Aidha, ameitaka Bodi hiyo kusimamia na kuboresha mpango wa kibiashara wa usafirishaji (Business Plan) katika Shirika hilo ili kuweza kumudu soko la ushindani na kuweza kuongeza mapato ya Shirika hilo.

“Kama mnavyojua usafiri wa anga una ushindani mkubwa, hivyo ili Serikali iweze kupata faida katika biashara hii ni lazima tuboreshe mpango wa kibiashara unaoendana na wakati”, amesisistiza Waziri Mbarawa.

Profesa Mbarawa ameitaka Bodi hiyo kuipa ATCL mifumo imara, makini na mahiri ili kuweza kutatua changamoto zinazoikabili Shirika hilo ikwemo wizi wa mafuta ya ndege na upotevu wa mapato.

Ili kupima ufanisi wa utendaji wa Shirika hilo Profesa Mbarawa ameitaka Bodi hiyo kuandaa mkataba kwa kila mfanyakazi kuanzia ngazi ya juu hadi chini.

Katika hatua nyingine Waziri Mbarawa amesema kuwa Serikali ina mpango wa kununua ndege mbili mpya aina ya Jet ifikapo mwaka 2017 kwa lengo la kuboresha sekta ya usafirishaji wa anga nchini.

Kwa Upande wake, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani, ameitaka Bodi hiyo kutumia fursa walioipata katika kufanya kazi vizuri ili kufufua shirika hilo na kuwapatia watanzania huduma sahihi na bora za usafirishaji.

Naye, Mwenyekiti wa Bodi hiyo Mhandisi Emmanuel Korosso, ameahidi kushirikiana na wajumbe wa bodi yake katika kutekeleza maelekezo ya Waziri haraka iwezekanavyo ikiwemo kubadilisha menejimenti ya shirika hilo.

Imetolewa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Rais Magufuli Hajakataa Kuonana Na Viongozi Wa Dini:sheikh Alhad.

0
0

 Na.Sheila Samba & Abushehe Nondo,Maelezo
Viongozi wa Dini nchini, wamesema Rais JOHN MAGUFULI Hajakataa kuzungumza wala kuwapuuza viongozi hao ambao wamemuomba kukutana naye, kama inavyoenezwa na baadhi ya vyombo vya habari.

Akizungumza leo jijini, Dar es Salaam na waandishi wa habari Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam Alhad Mussa Salum, amesema taarifa zilizochapishwa na gazeti la Tanzania Daima la Septemba 21 ISSN 0856 9762 toleo na.4310 sio za kweli.

“Taarifa hizo sio za kweli, taarifa hizo zimelenga kumgombanisha Rais na Viongozi wa Dini na watanzania kwa ujumla na hilo halitafanikiwa,” alisema Sheikh Alhad

Aidha Viongozi hao wamesema uamuzi wao wa kumuomba Rais kuonana naye, haujatokana na kuagizwa na UKAWA, bali umetokana na maono waliyopewa na Mwenyezi Mungu.

Amefafanua kuwa Rais MAGUFULI anawaheshimu Viongozi wa dini na mara zote amekua akiwaomba wamuombee na kusema leo ni siku ya tano tangu wamuandikie barua ya kumuomba kukutana naye na wanaimani Rais atakutana na Viongozi hao.

Ameeleza kuwa Barua hiyo imeandikwa Septemba 19 na kupelekwa siku hiyo hiyo Ikulu, ikiwa imesainiwa na Katibu Mkuu wa Bakwata, Katibu Mkuu wa CCT na Katibu Mkuu wa TEC.

“Naomba watanzania wasisikilize maneno hayo kwasababu hayana nia njema kwa Taifa letu, naamini Mh Rais tutaonana nae na tutaongelea mustakbali wa nchi katika mambo mbalimbali,” alisistisa Sheikh Alhad

 Akizungumzia utendaji wa Serikali ya Rais MAGUFULI, Sheikh ALHAD amesema Rais amerejesha nidhamu Serikalini, ukusanyaji mapato umeimarika na pia pengo kati ya wasionacho na walionacho linaanza kupungua.

Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Jumamosi ya Septemba 24

Majaliwa Aipa Siku 10 Taasisi Ya Hifadhi Ya Bahari Kulipa Deni La Sh. Milioni 100

0
0
WAZIRI MKUU  Mhe. Kassim Majaliwa ametoa muda wa siku 10 kwa Taasisi ya Hifadhi ya Bahari na Maeneo Tengefu kulipa deni la sh. milioni 100 inayodaiwa na Halmashauri ya wilaya ya Mafia.
 
Deni hilo linatokana na malimbikizo ya miaka mitatu ya maduhuri yatokanayo na makusanyo yanayofanywa na taasisi hiyo katika maeneo ya hifadhi ya bahari wilayani humo.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo Ijumaa, Septemba 23, 2016wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya wilaya hiyo katika ukumbi Caltas akiwa katika siku ya kwanza ya ziara yake ya kikazi siku mbili.
 
“Waandikieni barua na muitume leo hii kwa njia ya mtandao (email) kuwajulisha kuwa wanatakiwa kulipa deni hilo ndani ya siku 10. Hakikisheni wanalipa deni hili ili Halmashauri iweze kufanya kazi zake vizuri,” amesema.
 
Waziri Mkuu amesema Serikali inataka kuona Halmashauri hiyo ikinufaika kutokana na vyanzo vyake vya mapato, hivyo haitakuwa tayari kuona ikihangaika.
 
Mbali na agizo hilo, Waziri Mkuun amesema atafuatilia kuona wajibu wa taasisi hiyo na mipaka yao ikiwa ni pamoja na kujua mapato yatokanayo na shughuli hizo katika maeneo ya hifadhi.
 
Awali mkuu wa wilaya ya Mafia Shaib Nnunduma alisema kuwa miongoni mwa changamoto zinazoikabili wilaya hiyo ni kutolipwa kwa wakati fedha za maduhuri yatokanayo na makusanyo yanayofanywa na Taasisi ya Hifadhi ya Bahari.
 
Mkuu huyo wa wilaya ameiomba Serikali kuangalia upya majukumu ya taasisi hiyo na nafasi ya halmashauri katika kuendesha shughuli za uwekezaji pamoja na kupata mapato yatokanayo na shughuli hizo katika maeneo ya hifadhi.

Jipatie Vitabu vya Haditi za Kusisimua Toka kwa Mtunzi Aliyebobea Eddazaria g.Msulwa

Wafuasi wa Lipumba wakusanyika Buguruni kumwingiza ofisini

0
0
Vikundi vya wafuasi wa Profesa Ibrahim Lipumba wamekusanyika katika Ofisi za CUF Buguruni wakisubiri kumpokea mwenyekiti huyo wa zamani na kumwingiza ofisini.

Wanachama hao wanadai wana barua ya Msajili wa vyama vya siasa inayomtambua Profesa Lipumba kama mwenyekiti halali wa CUF.

Geti la ofisi za CUF limefungwa na ndani hakuna kiongozi yeyote wa chama.

Mashabiki hao wa Lipumba wanaoimba na kucheza, wanasema msafara wa Profesa uko njiani kuelekea kwenye ofisi hizo za makao makuu ya chama hicho.

Alipoulizwa kuhusu hali hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF, Julius Mtatiro amesema ndio wamepokea barua ya msajili na bado wanaisoma ili kuona imeelekeza kitu gani.

Hata hivyo, Mtatiro amesema kwa vyovyote vile msajili wa vyama vya siasa hana mamlaka ya kuingilia maamuzi ya vikao vya chama chochote cha siasa.

Wizara ya Nishati na Madini Yakanusha Profesa Muhongo Kuchangisha Shilingi 40,000 Kwa Ajili Ya Tetemeko Kagera

0
0
Gazeti la Mwananchi la tarehe 23 Septemba, 2016 katika ukurasa wake wa Tano imeandikwa habari yenye kichwa cha habari “Harambee ya Profesa Muhongo yakusanya Sh 40,000 Bukoba”.
 
Mwandishi wa Habari hiyo ameandika kuwa ziara aliyoifanya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo katika Kata ya Hamugembe, Bukoba wakati akikagua miundombinu ya umeme, iligeuka kuwa harambee baada ya waathirika wa tetemeko la ardhi kudai msaada wa chakula na mahema.

Tunapenda kuuarifu Umma wa Watanzania kuwa, siyo kweli kwamba Profesa Muhongo aliitisha harambee ya kuchangia maafa hayo kama ilivyoandikwa na Mwandishi ambaye kwa sababu zake binafsi aliamua kupindisha ukweli na kueleza kuwa, “ilimlazimu Profesa Muhongo kuitisha mchango wa fedha kutoka kwa maofisa aliokuwa ameambatana nao na kufanikiwa kupata shilingi 40,000 na kuwakabidhi wakazi hao”.
 
Ikumbukwe kuwa Waziri wa Nishati na Madini alikuwa mkoani Kagera kukagua shughuli za kiutafiti zinazofanywa na Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) baada ya kutokea kwa tetemeko la ardhi tarehe 10 Septemba, 2016 na kusababisha athari mbalimbali ikiwemo kwa miundombinu ya umeme.
 
Hivyo, taarifa kuwa Profesa Muhongo aliitisha harambee ya kuchangisha fedha za kusaidia waathirika wa maafa siyo sahihi kwani Profesa Muhongo hakuomba wala kuagiza Maofisa alioambatana nao kuchangia fedha kama ambavyo mwandishi anataka kuwaaminisha wananchi.
 
Akiwa katika kata ya Hamugembe mkoani humo ambapo alikwenda kukagua nyumba ambazo zimekatiwa huduma ya umeme kwa sababu ya kuathiriwa na tetemeko hilo, baadhi ya wananchi walidai kuwa shida yao ni chakula na malazi, na mmoja wa wananchi alisema kuwa Meneja wa TANESCO Mkoa wa Kagera aliyeambatana na Profesa Muhongo, alishafika kata hiyo na kuwasaidia kiasi cha fedha.
 
Hata hivyo, Profesa Muhongo aliwaeleza wananchi hao kuwa, yeye alikwenda hapo kwa ajili ya kushughulikia masuala ya kitaalam anayoyasimamia na kwamba kilio chao kuhusu kucheleweshewa huduma atakifikisha kwenye Kamati inayoshughulikia Maafa aliyokutana nayo tarehe 22 Septemba, 2016.
 
Baada ya wananchi kumtaja Meneja wa TANESCO wa Mkoa Kagera aliyewahi kuwasaidia wananchi hao fedha kutokana na tetemeko hilo, Meneja huyo aliamua kuongeza kiasi cha Fedha na kumpa mmoja wa wananchi hao, tofauti na ilivyoandikwa kwenye gazeti kuwa Waziri wa Nishati na Madini ndiye aliyekabidhi pesa kwa wananchi.
 
Tunawaasa waandishi wa habari kuzingatia ukweli na usahihi katika uandishi wa habari ili kupeleka habari sahihi kwa wananchi.
 
Imetolewa na;
WIZARA YA NISHATI NA MADINI

Msajili wa vyama vya siasa nchini, Jaji Francis Mutungi kasema Prof Ibrahim Haruna Lipumba,bado ni mwenyekiti halali wa CUF.

0
0
Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi amesema kuwa Prof. Ibrahim Lipumba bado ni mwenyekiti halali wa Chama cha Wananchi (CUF).

Jaji Mutungi ameyasema hayo leo baada ya shauri hilo kufikishwa mezani kwake siku kadhaa zilizopita kuhusu nafasi ya uenyekiti ndani ya CUF.

Awali Prof. Lipumba ndiye alikuwa mwenyekiti, lakini alijiuzulu Agosti 2015, mwezi Agosti 2016 chama hicho kikamteua Julius Mtatiro kuwa mwenyekiti wa muda hadi hapo uchaguzi wa kumtafuta mwenyekiti mwingine utakapofanyika.

Lakini Prof Lipumba alirudi na kusema yeye ndiye mwenyekiti halali wa CUF kwa sababu barua yake ya kujiuzulu haikuwa imekubaliwa na Mkutano Mkuu wa CUF. 

Baada ya mvutano wa muda mrefu ndani ya chama hicho, shauri hilo lilifikishwa katika ofisi ya msajili wa vyama vya siasa ambapo ametangaza rasmi kuwa Prof. Lipumba bado ni mwenyekiti.

Hapa chini ni maamuzi ya Msajili wa Vyama vya Siasa. 

Msimamo wa CUF kuhusu uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Mutungi kuamua kuwa Prof. Lipumba bado ni Mwenyekiti.

0
0

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

The Civic United Front (CUF – Chama Cha Wananchi) kimepokea kutoka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kile kinachoitwa “Msimamo na Ushauri wa Vyama vya Siasa kuhusu Mgogoro wa Uongozi wa Kitaifa wa Chama cha Civic United Front (CUF)” ambao uliwasilishwa Ofisi Kuu ya Chama, Buguruni, jana usiku.

Baada ya kupokea Ushauri huo, The Civic United Front (CUF – Chama Cha Wananchi) kinapenda kueleza yafuatayo:

1. Sheria ya Vyama vya Siasa (Political Parties Act, No. 5 of 1992) haimpi mamlaka wala uwezo wowote Msajili wa Vyama vya Siasa kutoa ushauri, msimamo au mwongozo kwa vyama vya siasa kuhusiana na maamuzi ya vikao vya Chama.

2. Msimamo huo wa kisheria wa nchi hii umetiliwa nguvu na kuthibitishwa na Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia UAMUZI wa tarehe 9/5/2005 wa Jaji T.B. Mihayo katika kesi ya Emmanuel Nyenyemela na Magnus Msambila v/s Registrar of Political Parties & Others (Civil Case No. 6 of 2003) ambapo Jaji Mihayo aliamua kwamba:

“… I do not see anywhere in the Political Parties Act where the Registrar has power to bless or condemn meetings of political parties or decisions that they make.”

Tafsiri ya uamuzi huo ni kwamba, “… Sioni popote katika Sheria ya Vyama vya Siasa ambapo Msajili ana madaraka ya kubariki au kupinga vikao vya vyama vya siasa au maamuzi ambayo vikao hivyo vinafanya.”

3. Kwa msingi huo, CUF hatukuomba ushauri kwa Msajili na hivyo tunamwambia ushauri wake abaki nao mwenyewe.

4. Kwa msingi huo huo, tunawataka wanachama wa CUF na wananchi wote kutambua kwamba Msajili hana uwezo kisheria wa kusikiliza mashauri yanayohusiana na malalamiko dhidi ya maamuzi ya vikao vya vyama vya siasa na na kuyatolea uamuzi. Uwezo huo ni wa Mahakama. Hivyo tunawataka wanachama wa CUF na wananchi wote kupuuza ushauri huo wa Msajili na wamwachie mwenyewe ndoto zake na propaganda za kitoto.

5. Ni fedheha na aibu kwa Msajili wa Vyama vya Siasa mwenye hadhi ya Ujaji kukubali kutumiwa kiasi hicho na kushindwa hata kufanya rejea kuhusu uamuzi wa Mahakama Kuu tulioutaja hapo juu ambao umeweka bayana kwamba hana madaraka na uwezo aliojifanya anao. 

Itakumbukwa kwamba Wabunge wa CUF walifanya mkutano na waandishi wa habari mjini Dodoma tarehe 15 Septemba, 2016 na kumtahadharisha Msajili asikubali kutumiwa kufanya alichokuwa anatakiwa kukifanya. Ni bahati mbaya sana kwamba amefanya kile kile ambacho Wabunge wa CUF walieleza kwamba walikuwa na taarifa kuwa ameagizwa kukifanya.

6. Tunajua kwamba baada ya hatua hiyo ya Msajili kufanya kazi asiyo na uwezo wala mamalaka nayo na katika kutimiza malengo ya wanaomtuma, mchana wa leo Prof. Ibrahim Lipumba na kikundi chake cha wahuni kimevamia Ofisi Kuu ya CUF, Buguruni, Dar es Salaam na kupiga watu na kufanya uharibifu wa mali. Tunamwambia Msajili wa Vyama vya Siasa atabeba dhamana kwa yote yaliyofanywa na yatakayofanywa na kikundi hicho ikiwemo watu watakaoumizwa na uharibifu wa mali utakaofanywa kutokana na tamko lake hilo ambalo halina msingi wa kisheria.

7. Tunatambua yote haya yanafanywa kwa sababu watawala wameingiwa kiwewe kutokana na hatua kubwa ambazo zimefikiwa na CUF katika kupigania haki yake ya ushindi ulioporwa katika uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa tarehe 25 Oktoba, 2015.

 CCM haijakaa sawa tokea iliposhindwa vibaya na CUF katika uchaguzi wa Rais, Wawakilishi na Madiwani mwaka 2015 na sasa imepata mfadhaiko kutokana na jinsi jumuiya ya kimataifa ilivyosimama kidete kutetea maamuzi hayo ya
kidemokrasia na haki za binadamu za Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla.

 Ni vyema watawala na kibaraka wao Prof. Ibrahim Lipumba na kikundi chake pamoja Msajili anayewatumikia wakatambua kwamba CUF haiyumbishwi na michezo yao ya kitoto na itaendelea kusimamia malengo yake ya kupigania haki za kidemokrasia za wananchi wa Zanzibar na Tanzania kikamilifu.

8. Chama kinasisitiza tena kwamba maamuzi ya Mkutano Mkuu Maalum wa Taifa wa tarehe 21 Agosti, 2016 na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la tarehe 28 Agosti, 2016 ni halali na yako pale pale na kwamba Prof. Ibrahim Lipumba si Mwenyekiti wa CUF na wanachama waliosimamishwa au kufukuzwa wataendelea kubakia wamesimamishwa au kufukuzwa isipokuwa tu iwapo vikao vya Chama vitakapofanya maamuzi mengine.

9. Chama kinawataka viongozi wake wote na wanachama wake katika ngazi zote kuanzia Taifa hadi Tawi kuendelea na kazi zao za ujenzi wa Chama kama kawaida na kuendelea kufuatilia harakati za Chama chao kupigania ushindi wetu wa tarehe 25 Oktoba, 2015.

HAKI SAWA KWA WOTE

NASSOR AHMED MAZRUI
NAIBU KATIBU MKUU - CUF

RIWAYA: She is My Wife- Sehemu ya 13 & 14

0
0
MWANDISHI : EDDAZARIA G.MSULWA

ILIPOISHIA....
“Meneja hizo pesa nitoe za benki au zako binafsi?”
“Toa za benki mtu akikuuliza, muambia aje kwangu”
Bwana Turma akiwa anasubiria zoezi la kufungiliwa akauti, gafla milio mingi ya risasi ikaanza kusikika ikitokea nje na kuanza kuwachanganya bwana Turma na muhasibu wake


ENDELEA......
Kitendo cha wasichana, makatili kuiingilia bank ya CNB, na kuwazalilisha wananchi walio kuwemo ndani ya benki kwa kuwatoa nje uchi kinazidi kuiumiza serrikali.Isitoshe inamuwia ugumu Bwana Turma, na akashikiliwa na jeshi la polisi kwa ajili ya kufanyiwa mahojiano maalumu kwani gari lake la thamani, limehusika katika matumizi ya uvamizi wa Benki.
                                                                                            
Dickson anatoa nje ya kibanda chake, huku akiwa na wasiwasi mwingi akiwatazama askari wawili wanaokuja kwenye kibanda chake
“Habari yako kaka?”
Askari mmoja alimsalimia Dickson
“Salama tuu mambo vipi?”

Dickson alizungumza kwa kujikaza tuu, kuuficha wasiwasi wake kwa maana msichana ambaye ni Rahab aliye muacha ndani anaonekana hana masihara kabisa katika matumizi ya silaha

“Hukuona, msichana aliye vaa akipita katika maeneo haya?”
“Ahaaa kusema kweli, sijamuona kwa maana hizi bunduki kwa jinsi zilivyokuwa zikinguruma huko nje sikudhubutu hata kuitoa miguu yangu”

Askari wakamtzama kwa umakini Dickson, ambaye anazungumza kwa kubabaika
“ Basi tunakuomba ufunge duka lako”
“Sawa”
Askari wakaanza kuondoka na kurudi katika eneo walipo wazao, Dickson akarudi ndani huku jasho jingi lkimwagika mithili ya maji.
“Waameniambia nifunge”

Dickson alimsemesha Rahab ambaye kichwa chake amekiinamisha kwenye ukuta huku sura yake ikitazama juu.
“Dada, dada.Wamesema nifunge duka langu”
Rahab hakujibu kitu chochote zaidi ya kukaa kimya, huku akimtazama Dickson jinsi sura yake inavyo mwaga jasho jingi
“Powa”
Rahab alijibu kwa kifupi, na kuzidi kumchanganya Dickson
“U...takaa humu ndani?”
“Ndio wewe funga”
“Mmmm”

Dickson akabaki akiwa anashangaa  shangaa, Rahab akainyanyua bastola yake na kumuwekea Dickson ya kichwa, mwili mzima wa Dickson ukawa kama umepigwa na shoti ya umeme, taratibu suruali yake ikaanza kutengeneza mchoro sehemua ya zipu, kwani woga umemfanya hadi ameshindwa kuzuia haja ndogo
“Huwa sipendi, nizungumze mara mbili mbili.Potea”

Rahab alizungumza huku sura yake akiwa ameikunja, na anaonekana kuwa na hasira kali.Kwa hahara Dickson akatoka nje ya kibanda chake, na kuaanza kufunga geti la kaduka kake hata baiskeli anazo zitengeneza hakukumbuka kuziingiza ndani.Kwa kuchanganyikiwa akajikuta akitembea asijue ni wapi anaelekea
                                                                                                            
Wote wanne wakiwa na bunduki zao mikononi, wakawa wanaitazama njia ambayo ni yakuingilia kwenye eneo lao la handaki.
“Tutawanyike wawili wawili”

Fetty alizungumza huku akiikoki bunduki yake, Anna akamfwata Fetty huku Halima na Agnes wakiwa wamesimama sehemu moja.Wakatazamana kwa muda pasipo mtu yoyote kuzungumza neno , kisha wakaanza kukimbia mtuni, wakiwa wameganawana kila watu wawili sehemu yao.Fetty na Anna walielekea magharibi mwa msitu wao, huku Agnes na Halima wakielekea Mashariki mwa msitu wao.

Askari wakiongozwa na mbwa wao, walio fundishwa mafunzo maalumu ya kunusa kila sehemu ambayo amepita mtu ambaye askari wanamuhitaji, ndivyo walizidi kuendelea kuingia msituni wakiwa na bunduki zao.Huku kila mmoja akiwa na hasira kali juu, ya maauaji yaliyo tokea siku chache zilizo pita juu ya wezao walio uwawa kwenye kituo cha gesi kwa mlipuko mkali.Amri mmoja iliyo tolewa na mkuu wa jeshi la polisi Bwana Gudluck Nyangoi ni kwamba wahakikishe wanawatia nguvuni ili wahukumiwe kifungo kikali kitakacho ishangaza dunia

Askari wakiongozwa na Kamishina Msaidizi wa Polisi(ACP) Ngurumo, wanaendelea kuuzingira msitu huku wakiwa na imani ya kufanikiwa na abushi yao wanayo kwenda kuifanya kwenye msitu unao sadikika ndipo walipo ingia majambazi kipindi wakitokea kufanya tukioa benki, na maelezo haya yalitolewa na msamaria mwema ambaye, gari lao lilisimamisha kipindi askari wa usalama barabarani walipokuwa wakifanya uchunguzi kwa kila gari ambalo lilikuwa likikatiza katika barabara kuu ya kuelekea mikoa ya Tanga na Arusha

Waziri Mkuu Majaliwa Atembelea Kiwanda Cha Samaki, Mafia, Ataka Doria Kuzuia Uvuvi Haramu Ziimarishwe

0
0

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaagiza mkuu wa wilaya ya Mafia mkoani Pwani, Bw. Shaib Nnunduma pamoja na mkurugenzi wa halmashauri hiyo Bw. Eric Mapunda kuimarisha doria kwenye eneo la bahari ili kuzuia uvuvi haramu.

Amesema vitendo vya uvuvi haramu vinavyoendelea katika wilaya hiyo vinapaswa kudhibitiwa haraka kwa sababu vinasababisha halmashauri hiyo kukosa mapato na kushindwa kuboresha maendeleo ya wananchi.
Waziri mkuu ametoa agizo hilo kwa nyakati tofauti  (Jumamosi, Septemba 24, 2016) wakati alipotembelea kiwanda cha samaki cha Tanpesca na alipowahutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kijiji cha Kirongwe wilaya ya Mafia.

Amesema uvuvi ndiyo shughuli kuu ya uchumi na chanzo muhimu cha mapato kwa wilaya ya Mafia na suala la uvuvi haramu linaathiri sana mapato ya halmashauri hivyo ni vema wakaimarisha doria ili kukomesha vitendo hivyo.

“Lazima jambo hili lidhibitiwe. Uvuvi wa kutumia mabomu unaharibu mazingira ya chini ya bahari hivyo samaki wanashindwa kuzaliana kwa wingi. Hakikisheni watu hao wanakamatwa na kuchukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kuteketeza zana wanazotumia,” amesema.

Naye Mkurugenzi wa kampuni ya Alphakrust inayomiliki kiwanda cha Tanpesca, Ganeshen Vedagiri amesema kampuni hiyo imeajiri watumishi 855 kati yake 445 ni wakazi wa wilaya ya Mafia huku wanawake wakiwa 250.

Amesema wanajumla ya mabwawa 76 ya kufugia samaki aina ya kamba na kwa sasa yanayotumika ni 30 na kila moja lina uwezo wa kuzalisha kilo 5,000 katika siku siku 150 na kufanikiwa kuvuna tani 300 kwa mwaka.

Mkurugenzi huyo amesema katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2016.2017 wanatarajia kupata wastani wa sh. bilioni 120 katika mauzo ya nje na sh. bilioni 62 kutoka katika mauzo ya ndani. Wanaltarajia kulipa kodi ya zaidi ya bilioni 15 kwa mwaka huu.

Kwa upande wake Mohamed Gomvu ambaye ni Diwani wa kata ya Kirongwe na Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Mafia alisema maeneo yaliyoathirika zaidi na uvuvi haramu ni vijiji vya Ndagoni (Kiega), Kifinge, Chunguruma (Tumbuju) na kisiwa cha Nyororo.

Amesema jambo linalokwamisha ukamatwaji wa uvuvi haramu ni kutokana na watumishi kukosa uamini na kuvujisha siri kwa wavuvi hao hivyo wanashindwa kuwanasa kwenye mitego yao.

Serikali Kufanya Zoezi La Utambuzi Na Usajili Kwa Watumishi Wake Kuanzia Oktoba 3

0
0


Na Frank Shija, MAELEZO
SERIKALI inatarajia kufanya zoezi la utambuzi na usajili wa taarifa za watumishi wa umma kuanzia tarehe 3 Oktoba ili kutoa vitambulisho vya Taifa vilivyo na taarifa zote muhimu za mtumishi husika.
 
Hayo yamebainisha na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Angellah Kairuki alipokutana na waandishi wa habari ofisini kwake jana Jijini Dar es Salaam.
 
Kairuki alisema kuwa zoezi hilo la utambuzi na usajili wa wananchi ambalo linaanza na watumishi wa umma ni muhimu na litasaidia kupunguza gharama kwa Serikali na kuondoa usumbufu kwa wananchi kwani taarifa zao zote muhimu zitakuwa sehemu moja hivyo kupunguza kero ya kuulizwa taarifa kila uendapo.
 
Waziri Kairuki alisema kuwa zoezi hilo litashirikisha Wizara yake pamoja na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia  Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), ambapo taarifa zitakazotumika ni zilizilizopo katika vitambulisho vya mpiga kura.
 
“Kama mnavyofahamu kuwa Serikali ipo katika maboresho makubwa ya utendaji wake, hivyo ili kuendana na hali hiyo tutaanza zoezi la utambuzi na usajili wa watumishi wa umma kuanzia tarehe 3 Oktoba, zoezi litakalochukua takribani wiki mbili, zoezi hili ni muendelezo wa Serikali kukabiliana na matatizo ya kutokuwa na taarifa sahihi.” Alisema Kairuki.
 
Aidha Kairuki aliwata watumishi wote wa umma kushiriki zaoezi hilo wakiwa na taarifa zote muhimu zinazowatambulisha ambazo ni pamoja na Cheti cha kuzaliwa, vyeti vya elimu, kitambulisho cha kazi, Kitambulisho cha Mzanzibar Mkazi, hati ya malipo ya Mshahara, hati ya kusafiria na kadi ya mpiga kura.
 
Waziri huyo ametoa wito kwa waajiri kuweka mazingira wezesha ili kufanikisha zoezi hilo ikiwemo kutenga ofisi itakayotumiwa na kwa kazi hiyo pamoja na kusisitiza waajiri wahakikishe watumishi wao wanasajiliwa bila kukusa na taarifa ya zoezi hilo iwasilishe Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawabora ndani ya siku 14 tangu zoezi hilo kukamilika kwake.
 
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Dkt. Laurian Ndumbaro aliwataka watumishi wote wa umma kulipa umuhimu mkubwa zaozi hilo na kusisitiza kuwa Serikali haita sita kucghukua hatuia za kinidhamu kwa mujibu wa kanuni za utumishi wa umma kwa mtumishi yeyote atakaye kaidi zoezi hilo.
 
Awali akijibu swali la mwandishi wa habari kuhusu namna zoezi hilo litakavyotekelezwa nchi nzima kwa muda wa wiki mbili tu, Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) Mohammed Khamis Abdallah alisema kuwa zoezi hilo litafanikiwa kwani wanao wafanyakazi zaidi ya 460 nchini nzima ambao wapo katika Ofisi za Halmashauri.
 
Pia aligusia suala la vifaa na kusema kuwa tayari wamewasiliana na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ambayo imewapa mashine za BVR kwa ajili ya kuzitumia katika zoezi hilo la utambuzi na usajili.

Zoezi la utambuzi na usajili wa wananchi hasa watumishi wa uuma kukabiliana na vyanzo vya watumishi hewa kwa kuunganisha mifumo ya utambuzi wa watu na mifumo mingine ikiwemo usimamizi wa rasilimali watu na mishahara katika utumishi wa umma ambapo kuunganishwa kwa mifumo hiyo kutawezesha mifumo hiyo kuwasiliana na kutumia taarifa zilizo kwenye kanzi data ya NIDA suala litakalokuwa limerahisisha upatikanaji wa taarifa.
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live




Latest Images