Quantcast
Channel: MPEKUZI
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live

Chenge Akaidi Agizo la Jeshi la Polisi

0
0

Agizo la Jeshi la Polisi nchini la kusitisha kufanyika kwa mikutano ya hadhara ya kisiasa imeonekana kutoathiri ratiba za Mbunge wa Bariadi, John Chenge ambaye ameendelea na mikutano ya hadhara jimboni kwake.

Taarifa kutoka jimboni humo zimeeleza kuwa Chenge amekuwa akifanya mikutano ya hadhara katika vijiji mbalimbali na Alhamisi iliyopita alianza na eneo la Buchani, mkutano uliomalizika salama bila kuwepo kizuizi chochote.

Katika mikutano hiyo, Mtemi Chenge ameendelea kuwasisitiza wananchi wake kupuuza kauli za kisiasa zinazotolewa na wapinzani wake bali waangalie namna anavyotekeleza ahadi alizozitoa kwenye kampeni za uchaguzi mkuu.

Mikutano hiyo ya Chenge hutanguliwa na matangazo yanayofanywa kwa kutumia magari yenye vipaza sauti katika eneo husika.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Onesmo Lyanga alipotafutwa kwa njia ya simu alisema kuwa yeye hahusiki kutoa vibali vya mikutano na kwamba mhusika ni Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD). Hata hivyo, OCD hakupatikana kwa wakati.

Hali hiyo imedaiwa kuzua manung’uniko kwa vyama vya upinzani mkoani humo ambavyo vimeshindwa kufanya mikutano ya hadhara kutokana na kuwepo kwa zuio la Mikutano hiyo nchi nzima.

Mwezi uliopita, Kamishna wa Jeshi la Polisi, Operesheni ya Mafunzo, Nsato Msanzya alitangaza kupiga marufuku kufanyika kwa mikutano ya kisiasa kwa sababu za kiusalama.

“Polisi kupitia vyanzo vyake mbalimbali, imebaini kuwea mikutano hiyo ina lengo la kuwahamasisha wananchi kutotii sheria za nchi,” alisema Kamishna Nsato.

Kufuatia agizo hilo, Jeshi la Polisi lilizuia kufanyika kwa mikutano iliyokuwa imepangwa na Chadema na ACT-Wazalendo kwa nyakati tofauti.

Umoja wa Vijana wa Chama cha Wananchi (JUVICUF) Wataka Halmashauri Zinazoongozwa na CUF Zikatae Kutekeleza Maagizo ya Serikali

0
0
UMOJA wa Vijana wa Chama cha Wananchi  (JUVICUF), umeapa kutotoa ushirikiano wa kikazi kwa viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) walioteuliwa na Rais John Magufuli ambao wanatoa matamko yasiyo na tija kwa wananchi.

Mkuu wa Idara ya Habari na Uenezi wa JUVICUF, Dahlia Majid alisema katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuwa uteuzi wa makada wa CCM katika nafasi za wakuu wa wilaya pamoja na wakurugenzi utavuruga nchi hususani katika kipindi cha uchaguzi.

Akisoma tamko hilo kwa niaba ya Mwenyekiti wa JUVICUF Taifa, Hamidu Bobali, Dahlia alisema viongozi wa awamu ya tano wanakurupuka na kutoa matamko yasiyo na tija yanayobaka mamlaka ya Jeshi la Polisi.

“Haiwezekani viongozi wa awamu ya tano wanakurupuka tu wanatoa matamko yasiyo na tija kila siku tena mengine yanabaka mamlaka hata ya mahakama na wanajifanya wao ndio polisi, wao ndio mahakama na wao ndio magereza, tutawaagiza viongozi wetu katika halmashauri zinazoongozwa na CUF kukataa kauli na matamko ya namna hiyo.

“JUVICUF tunakitaka Chama cha CUF kuwaagiza viongozi wake katika halmashauri tunazoziongoza kwamba waache mara moja kutekeleza maagizo yasiyo na tija kutoka kwa viongozi waliolewa madaraka.

“Tunawasihi vijana waendelee na shughuli zao za kujiletea maendeleo bila kujali matamko yanayotolewa na viongozi waliolewa madaraka na kujifanya miungu watu,” alisema.

Dahlia alitolea mfano wa agizo lililotolewa hivi karibuni na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda la kuwakamata wananchi wasiokuwa na kazi maalumu ambapo alisema hayo ni miongoni mwa maagizo ya ovyo na hayapaswi kutekelezwa.

Kiongozi huyo wa vijana alisema agizo hilo ni kinyume cha sheria huku akitahadharisha kuwa utekelezaji wake utahusisha askari kupiga watu, visa na vijana kubambikiwa kesi zisizokuwa na sababu.

“Ni ajabu sana na hii haipo kote duniani kibali cha kuwakaguwa wananchi majumbani kutolewa na viongozi wa kisiasa, mahakama zina kazi gani? serikali imefanya maisha kuwa magumu na ajira kuwa ngumu kupatikana halafu wao wanaibuka na sera ya kukamata watu wasio na ajira,” alisema Dahlia.

RIWAYA: Mwanafunzi Mchawi (A Wizard Student) - Sehemu ya 16

0
0
Mtunzi: Enea Faidy

....DOREEN alikuwa bado hana hali nzuri kiafya, mwili wake ulikuwa hauna nguvu kabisa kwani ile adhabu aliyoipata usiku ilimwadhibu haswa. Alijikuta anamwogopa Nadia kupita kiasi, moyoni mwake alikiri kuwa kweli Nadia Joseph alikuwa Mchamungu kweli.

Wakati huo akiwa bado yupo kitandani akiugulia maumivu, Doreen alifikiria jinsi ya kuweza kupata titi la msichana mrembo ili akamilishe kazi yake aliyotumwa kuifanya. Siku zilikuwa zimeisha sana lakini alijipa moyo kuwa ameshamaliza kazi kwani kupata titi aliona kama kazi rahisi tu ingawa ilishaanza kupata vikwazo.

Doreen alishuka kitandani kwake. Akavua nguo zote kisha akasogelea begi lake na kuchukua shanga nyeusi akaivaa shingoni mwake.
 
Na kwakuwa alikuwa peke take chumbani mle Doreen alifanya mambo yake bila woga. Akachukua kichupa kimoja kidogo kwenye begi lake halafu akamimina kidogo unga unga uliokuwamo mle na kujipaka usoni kisha akapiga magoti chini na kuinamisha kichwa chake huku akitamka maneno Fulani.
 
Ghafla karatasi ambayo ilifanya mauaji ya walimu ofisini ikamjia mkononi make.
 
Ikumbukwe kuwa karatasi ile ilichukuliwa na mwalimu Jason ambapo kulikuwa na maandishi yaliyomuonya kuwa asimpe mtu mwingine, hivyo Mwalimu Jason aliamua kukimbia nayo na alikuwa akikaa Nayo kwa siku zote zile.
 
Doreen alitabasamu baada ya kuitazama karatasi ile, akaishika vizuri kwa mikono miwili kisha akasema "NENDA KWA MWALIMU JASON! MWAMBIE ANILETEE TITI LA MSICHANA MREMBO! NAKUAMINI!" alisema Doreen kisha akaiachia karatasi ile, ikapaa hewani na ikapotea.
 
Doreen alifurahi sana akajua tayari amekwisha maliza kazi yake. Akiwa bado ameketi pale chini akiendelea na mambo yake mengine ghafla mlango wa bweni lake ukagongwa halafu akakumbuka kuwa hakuubana mlango ule vizuri kwa komeo Doreen alishtuka sana kwani alikuwa mtupu na alikuwa na maunga unga usoni. Akahisi fumanizi la uchawi tayari limemfikia.

Naibu Makamishna wa Polisi (DCP) na Makamishna Wasaidizi Waandamizi wa Polisi (SACP) waapa Kiapo cha Uaminifu kwa Viongozi wa Umma Ikulu jijini Dar es salaam leo

0
0
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Naibu Makamishna wa Polisi (DCP) na  Makamishna Wasaidizi Waandamizi wa Polisi (SACP) na Viongozi mbalimbali wa Serikali mara baada ya Makamishna hao kula Kiapo cha Uaminifu kwa Viongozi wa Umma Ikulu jijini Dar es salaam leo.Mhe. Rais, Dkt. John Pombe Magufuli amewataka wasimamie utekelezaji wa Sheria bila woga na kuahidi kuboresha maslahi ya Jeshi la Polisi nchini.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Naibu Makamishna wa Polisi (DCP) na  Makamishna Wasaidizi Waandamizi wa Polisi (SACP)  mara baada ya kula Kiapo cha Uaminifu kwa Viongozi wa Umma Ikulu jijini Dar es salaam leo.
Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Jaji Mstaafu Salome Kaganda akiwaongoza Naibu Makamishna wa Polisi (DCP) 35 na  Makamishna Wasaidizi Waandamizi wa Polisi (SACP) 23 kula Kiapo cha Uaminifu kwa Viongozi wa Umma mara baada yakupandishwa vyeo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, leo Ikulu jijini Dar es salaam.
 Naibu Makamishna wa Polisi (DCP) na  Makamishna Wasaidizi Waandamizi wa Polisi (SACP) wakila Kiapo cha Uaminifu kwa Viongozi wa Umma mara baada yakupandishwa vyeo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, leo Ikulu jijini Dar es salaam.
 Naibu Makamishna wa Polisi (DCP) na  Makamishna Wasaidizi Waandamizi wa Polisi (SACP) wakifuatilia kwa Makini hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli mara baada ya kula Kiapo cha Uaminifu kwa Viongozi wa Umma leo Ikulu jijini Dar es salaam.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Utumishi na Utawala Bora Mhe. Angellah Kairuki(kushoto) akizungumza jambo na Katibu Mkuu Kiongozi BaloziEng. John William Herbert Kijazi (wa pili kutoka kushoto) Ikulu jijini Dar es salaam mara baada ya Naibu Makamishna wa Polisi (DCP) na  Makamishna Wasaidizi Waandamizi wa Polisi (SACP) kula kiapo cha Uaminifu kwa Viongozi wa Umma.Wengine ni Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Jaji Mstaafu Salome Kaganda na Inspekta Jenerali wa Polisi Ernest Mangu.
Katibu MkuuwaWizara ya Mambo ya Ndaniya Nchi, Meja Jenerali ProjestRwegasira(wa pili kutoka kushoto)akizungumza jambo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) George Masaju (kushoto) leo Ikulu jijini Dar es salaam mara baada ya Naibu Makamishna wa Polisi (DCP) na  Makamishna Wasaidizi Waandamizi wa Polisi (SACP) kula kiapo cha Uaminifu kwa Viongozi wa Umma.Wengine kulia ni Waziri na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba (Kulia) na Mhe. Hamad Masauni.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa Serikali mara baada ya Naibu Makamishna wa Polisi (DCP) na  Makamishna Wasaidizi Waandamizi wa Polisi (SACP) kula Kiapocha Uaminifu kwa Viongozi wa Umma Ikulu jijini Dar es salaam leo.Kutoka kushoto ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) George Masaju,Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Ndani ya NchiMeja Jenerali ProjestRwegasira(wa pili kutoka kushoto), Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Mhe. Hamad Masauni, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba, Wengine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Utumishi na Utawala Bora Mhe. Angellah Kairuki(kushoto), Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Jaji Mstaafu Salome Kaganda na Inspekta Jenerali wa Polisi Ernest Mangu.  
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa Serikali mara baada ya Naibu Makamishna wa Polisi (DCP) na  Makamishna Wasaidizi Waandamizi wa Polisi (SACP, Ikulu jijini Dar es salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa Serikali na Viongozi wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama leo Ikulu jijini Dar es salaam mara baada ya Naibu Makamishna wa Polisi (DCP) na  Makamishna Wasaidizi Waandamizi wa Polisi (SACP).Picha/A.Msigwa.

Rais Magufuli atema cheche Wakati akiwaapisha makamishna wa polisi waliopanda vyeo

0
0
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amewataka Makamishna Wasaidizi Waandimizi na Mananibu Kamishna wa Jeshi la Polisi kufanya kazi kwa bidii zote bila ya kumuogopa mtu yeyote katika kuhakikisha maslahi ya nchi yanawekwa mbele.

Rais Magufuli ameyasema hayo leo Ikulu, Jijini Dar es Salaam alipokuwa akiwaapisha wa umma waliopandishwa vyeo hivi karibuni na Rais mwenyewe kutoka  Makamishna Wasaidizi kuwa Makamisha Wasaidizi Waandamizi na waliokuwa Makamishna Wasaidizi Waandimizi kuwa Manaibu Kamishna Wasaidizi.

Amewataka watumishi hao wa umma kufanya kazi kwa moyo mmoja na kutenda haki kwa watu bila kujali cheo wala umaarufu wa watu.

Akitolea mfano wa Askari wa Usalama barabarani Rais Magufuli amesema wamekuwa wakishindwa kukamata baadhi ya magari  yanayomilikiwa na baadhi ya polisi kama Happy Nation na Buffalo pale yanapofanya makosa na pindi wanapochukua hatua dhidi ya magari ya aina hiyo basi wanatishiwa kushushwa cheo au kuhamishwa kutoka pale walipo.

"Nataka mkafanye kazi kwa haki bila kuogopa mtu hata kama ni gari la IGP, Waziri au hata Rais sheria lazima ichukue mkondo wake na mhusika wa gari hilo atakwenda kujieleza polisi mwenyewe." amesema Rais Magufuli

Rais Magufuli amewataka makamishna hao waliopandishwa vyeo kuhakikisha sekta zote zinazotakiwa kulipa kodi kama bandari na utalii zinafanya hivyo kama sheria inavyosema huku akiwashangaa wale wanaosema kuwa meli zimepungua bandarini na watalii kupungua nchini.

“Meli zilizopungua bandarini ni zile ambazo zimekuwa hazilipi kodi kwakuwa sasa mianya yote ya kukwepa kodi imezibwa. Ni afadhali zile meli chache zitakazolipa kodi kuliko nyingi ambazo hazilipi kodi na vivyo hivyo katika sekta ya utalii ni bora watalii wasije kama hawataki kulipa VAT iliyotengwa na Serikali,” amesema Rais Magufuli.

Aidha, amewataka makamishna hao kwenda kupambana na Tatizo la watumishi hewa katika maeneo yao ya kazi ili kuhakikisha tatizo hilo ambalo limeigharimu serikali mabilioni ya pesa halijirudii tena na kama bado lipo linatokomezwa kabisa.

Akiongelea suala la Polisi Jamii, Rais Magufuli amewataka makamishna hao kufanya kazi bila kujali utaratibu huo wa polisi jamii na kuongeza kuwa amekuwa akiupinga utaratibu huo tangu akiwa Waziri wa Uvuvi na kusisitiza kuwa dunia ya sasa ni tofauti na ile tuliyoizoea.

“Ilikuwa unaweza kumkuta mvuvi katikati ya ziwa akiwa anafanya vitu kinyume na sheria alafu unataka kuleta mambo ya polisi jamii kwa kuanzisha majadiliano na mhalifu, hili halikubaliki na nililipinga kwani ni lazima ifike mahali polisi aheshimiwe na tofauti iwepo kati ya polisi na raia wa kawaida,” amesisitiza Rais Magufuli.

Jumla ya Makamishna Wasaidizi Waandimizi na Mananibu Kamishna 60 wa Jeshi la Polisi wamepandishwa cheo na Rais Magufuli hivi karibuni na leo wamekula kiapo cha uadilifu isipokuwa Manaibu Makamishna wawili ambao wapo nje ya nchi kwa mafunzo maalum.

Rais Magufuli aibua ufisadi mwingine wa mabilioni ya shilingi ndani ya Jeshi la Polisi

0
0
Rais Magufuli amelitaka Jeshi la Polisi kujiepusha na vitendo vya rushwa ambavyo vilinafanya jeshi hilo kukosa heshima katika jamii huku akisema kuwa ana taarifa za jeshi hilo kuingia katika makubaliano ya kifisadi ya mabilioni ya shilingi kwa ajili ya kununua sare za jeshi hilo.

Rais Magufuli ameyasema hayo leo alipokuwa akiwaapisha makamishna wa Jeshi la Polisi waliopandishwa vyeo na kuongeza kuwa ni jambo la kusikitisha kwamba mabilioni hayo yalitolewa kwa siku moja lakini hadi leo hakuna hata sare moja ya iliyonuuliwa.

Ameshangazwa na jeshi hilo kutoa kiasi cha fedha kinachokadiriwa kuwa kati ya shilingi bilioni 40 hadi 60 kwa ajili ya sare za polisi ambazo hadi leo hakuna hata moja iliyonunuliwa na wakati huohuo jeshi hilo likikosa shilingi bilioni 4 tu za kukomboa magari yao zaidi ya 70 yanayoshikiliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) huko bandarini.

Aidha, Rais Magufuli ameagiza uchunguzi ufanyike na wahusika wafikishwe mbele ya haki ila angalau hata nusu ya fedha hizo ziweze kurudishwa zikalipie magari ya polisi yaweze kutoka bandarini maramoja.

Amelitaka pia Jeshi la Polisi kuachana na utaratibu wa kuwa na watumishi ambao ni raia wa kawaida na badala yake polisi wenyewe ndio washike nafasi hizo kulingana na taaluma husika na kushangazwa na taarifa kuwa  Mhasibu Mkuu wa Polisi aliyetumbuliwa hivi karibuni kwa tuhuma za ubadhirifu alikuwa raia wa kawaida na sio polisi.

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo July 19

Rais Magufuli amteua Mkurugenzi Mkuu wa SIDO, na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa Dodoma

0
0
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Prof. Sylvester Michael Mpanduji kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO).
 
Taarifa iliyotolewa jana Ikulu Jijini Dar es salaam na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi imeeleza kuwa uteuzi wa Prof. Sylvester Michael Mpanduji umeanzia jana tarehe 18 Julai, 2016.
 
Kabla ya uteuzi huu Prof. Sylvester Michael Mpanduji alikuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA).
 
Prof. Sylvester Michael Mpanduji anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Mhandisi Omary Jumanne Bakari ambaye uteuzi wake umetenguliwa.
 
Wakati huo huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Dkt.Winnie Mpanju-Shumbusho kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamini Mkapa - Dodoma.
 
Kabla ya Uteuzi huo, Dkt. Winnie Mpanju-Shumbusho alikuwa Mkurugenzi Mkuu Msaidizi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) lenye makao yake makuu Mjini Geneva nchini Uswisi na alimaliza mkataba wake tangu Mwezi Desemba 2015.
 
Uteuzi wa Dkt. Winnie Mpanju-Shumbusho umeanza jana tarehe 18 Julai, 2016.
 
Dkt. Winnie Mpanju-Shumbusho anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Dkt. Donan William Mmbando ambaye ameomba kupumzika kutokana na sababu binafsi.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
18 Julai, 2016

Wakurugenzi 6 wa NSSF Wasimamishwa Kazi Kupisha Uchunguzi

0
0
BODI ya Wadhamini ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) imeagiza kusimamishwa kwa wakurugenzi sita, mameneja watano na mhandisi mmoja wa shirika hilo kupisha uchunguzi, kubaini wahusika katika tuhuma za ubadhirifu, matumizi mabaya ya ofisi na kutofuata kanuni, sheria na taratibu katika uwekezaji, usimamizi wa miradi, manunuzi ya ardhi na ajira.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya NSSF, Profesa Samwel Wangwe, alikiri  jana usiku kusimamishwa kwa vigogo hao 11, kupisha uchunguzi wa tuhuma zilizoelekezwa kwao.

“Ni taarifa sahihi hizo. Kulikuwa na tuhuma katika ripoti ya ukaguzi, kwa hiyo tumeamua wakae pembeni ili kupisha uchunguzi, hawajafukuzwa kazi. Taarifa hiyo ya kusimamishwa ni sawa sawa,” alisema Profesa Wangwe jana usiku.

Kwa mujibu wa taarifa kwa wafanyakazi, iliyotolewa na Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, iliwataja wakurugenzi sita waliosimamishwa kuwa ni Yacob Kidula (Mkurugenzi wa Mipango, Uwekezaji na Miradi), Ludovick Mrosso (Mkurugenzi wa Fedha) na Chiku Matessa (Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala).

Wengine ni Sadi Shemilwa (Mkurugenzi wa Udhibiti Hadhara na Majanga), Pauline Mtunda (Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Mahesabu ya Ndani) na Crescentius Magori (Mkurugenzi wa Uendeshaji).

Aidha, taarifa hiyo iliwataja mameneja waliosimamishwa kuwa ni Amina Abdallah (Meneja Utawala), Abdallah Mseli (Meneja wa Uwekezaji), Mhandisi John Msemo (Meneja wa Miradi), Davis Kalanje (Mhasibu Mkuu), Wakili Chedrik Komba (Meneja Kiongozi – Mkoa wa Temeke) na Mhandisi John Ndazi (Meneja Mradi).

Taarifa hiyo kutoka Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, ilisema kwamba uamuzi huo umefanywa na Bodi chini ya Profesa Wangwe iliyokutana Julai 15, mwaka huu kutokana na taarifa mbalimbali za wakaguzi wa hesabu na shughuli za uendeshaji wa shirika hilo la umma.

“Bodi ya Wadhamini ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii chini ya Uenyekiti wa Profesa Samwel Wangwe katika kikao chake cha 106 kilichofanyika tarehe 15 Julai, 2016 kimeagiza kusimamishwa kazi kwa wakurugenzi sita (6), mameneja watano (5) na mhandisi mmoja ili kupisha uchunguzi kubaini wahusika katika tuhuma za ubadhirifu, matumizi mabaya ya ofisi na kutofuata kanuni, sheria na taratibu katika uwekezaji, usimamizi wa miradi na manunuzi ya umma na ajira,” ilieleza taarifa hiyo.

Hivi karibuni, NSSF ilitajwa katika vyombo vya habari kuhusu tuhuma zikiwamo za ununuzi wa ardhi usiofuata taratibu za manunuzi ya umma, kuwapo kwa ubadhirifu na ajira za upendeleo katika shirika hilo, ukiwataja wahusika kuwa ni baadhi ya wakurugenzi wa shirika hilo.

Sendeka: Mkutano Mkuu wa CCM siyo wa kupokezana vijiti Bali ni wa Kuchagua Mwenyekiti wa Chama ambaye Lazima Apate Kura za Ndiyo Zaidi ya Nusu

0
0
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kwamba Mkutano Mkuu Maalumu wa chama hicho, utakaofanyika mwishoni mwa wiki hii si wa kupokezana vijiti, kwa sababu nafasi za Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti unapofika wakati wa uchaguzi haziombwi, bali yanapendekezwa majina ya watu wanaofaa kushika nyadhifa huo.

Aidha, kimesema maandalizi ya mkutano huo utakaofanyika Jumamosi wiki hii, yamekamilika na unatarajiwa kushirikisha wajumbe 2,456 na mpaka sasa wamekodi hoteli 306 ambazo zitawalaza zaidi ya watu 3,331 mjini Dodoma.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari jana, Msemaji wa CCM, Christopher ole Sendeka alisema Mkutano Mkuu Maalumu wa Taifa utamchagua Mwenyekiti wa CCM Taifa baada ya Mwenyekiti wa sasa, Jakaya Kikwete kung’atuka na kutoa nafasi hiyo kwa Rais John Magufuli kugombea.

Alisema Rais Magufuli atakuwa Mwenyekiti wa CCM wa tano baada ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Kikwete.

“Kwa mujibu wa Katiba ya CCM, nafasi ya Mwenyekiti wa CCM na Makamu Mwenyekiti wawili unapofikia wakati wa uchaguzi nafasi hizi haziombwi isipokuwa Kamati Kuu inafikiria na kupendekeza majina na kuyawasilisha kwa Halmashauri Kuu ya Taifa ambayo humteua,” alisema Sendeka.

Alisema kisha Mkutano Mkuu wa Taifa unamchagua kwa kumpigia kura. Alisema wanaopendekezwa hawajazi fomu za kugombea nafasi hizo na katika mchakato huo kinachofanyika si kupokezana kijiti, kama wengi wanavyopenda kuita, bali ni uchaguzi wa kumpata mwenyekiti wa CCM.

Alisema katika uchaguzi huo itapigwa kura ya ‘ndio’ au ‘hapana’ ili kupata mwenyekiti na lazima apate nusu ya kura na akipata chini ya nusu mapendekezo yataanza upya.

“Tuna imani wajumbe wote watampa mwenyekiti mpya kura zote za ‘ndio’ ili achukue nafasi ya kuongoza kitaifa,” alisema na kuongeza kuwa akipatikana mwenyekiti ataunda ‘jeshi’ lake, kwani hiyo ni desturi ya chama na walio katika Sektetarieti, watapisha ili mwenyekiti mpya aunde jeshi lake.

Rais Magufuli anatarajiwa kufanya mabadiliko makubwa ya uongozi ndani ya CCM baada ya kukabidhiwa uenyekiti wa Taifa, kwa kupanga upya safu yake ya viongozi, ambao anaamini anaweza kufanya kazi nao kwa ajili ya kuleta mabadiliko ndani ya Chama.

Viongozi watakaojiuzulu ili kupisha Dk Magufuli kupanga safu hiyo ni Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, manaibu katibu mkuu wawili na watendaji wengine.

Wajumbe wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa ni pamoja na Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu Bara, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Katibu wa Oganaizesheni, Katibu wa Siasa na Uhusiano ya Kimataifa, Katibu wa Uchumi na Fedha na wa Itikadi na Uenezi.

“Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana atakabidhi barua yake kwa mwenyekiti wa chama kupisha Rais Magufuli aweze kuunda safu yake ya watu atakaofanya nao kazi,” alieleza Sendeka na kuongeza kuwa anaamini Magufuli ataunda safu nzuri itakayoleta mabadiliko.

“Chama madhubuti huzaa serikali madhubuti na chama legelege huzaa serikali legelege,” aliongeza na kubainisha kuwa maandalizi kwa ajili ya mkutano huo, yamekamilika na tayari fedha zimetumwa mikoani ili kuwezesha wajumbe wote kufika; na magari yatakodishwa kuwaleta mjini hapa.

Alisema jumla ya wajumbe 2,456 watahudhuria mkutano huo, lakini pia wanajitahidi kuweka hesabu vizuri kwa kuondoa wajumbe wenye kofia mbili. Alisema wamekodi hoteli 306. Akizungumzia hali ya usalama alisema wamejipanga kuhakikisha mkutano huo unafanyika kwa amani.

“Dodoma ni shwari na salama watu wasiwe na hofu na tuna imani mkutano utamalizika vizuri,” alifafanua na kuongeza kuwa wajumbe wa NEC watawasili Alhamisi tayari kwa kikao cha Ijumaa na wajumbe wengine watawasili Ijumaa.

Makamu wa Rais: Tutaendelea kufanya kazi kwa karibu na nchi za AU

0
0
TANZANIA imeuhakikishia Umoja wa Afrika (AU) kwamba itaendelea kufanya kazi kwa karibu na nchi wanachama wa umoja huo, kujadili changamoto za kiusalama zinazolikabili bara la Afrika, kwa njia ya mazungumzo na upatanishi, kama inavyoelekeza Katiba ya AU.

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, alitoa kauli hiyo wakati akichangia mada kuhusu hali ya amani na usalama katika bara la Afrika, kwenye Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU), uliofanyika mjini Kigali, Rwanda.

Samia alisema Tanzania inasikitishwa na inalaani matukio ya uvunjifu wa amani yanayoendelea kujitokeza katika baadhi ya nchi za Afrika kiasi cha kutishia usalama wa raia.

Alielezea mauaji ya Hafsa Mossi aliyekuwa Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) na Waziri wa zamani wa Burundi na mapigano ya hivi karibuni Sudan Kusini ambako mamia ya raia wasiokuwa na hatia waliuawa na wengine maelfu wameachwa bila makazi, kwamba ni mwendelezo wa uvunjifu wa amani katika nchi hizo.

Aliwataka wadau husika katika nchi za Burundi na Sudan Kusini kushiriki kikamilifu katika mazungumzo yanayoendelea kwa kuwa hiyo ndiyo njia muafaka ya kuleta amani, usalama na utulivu wa kudumu katika nchi zao.

Aidha, aliiomba Jumuiya ya Kimataifa kuendelea kuisaidia Sudan Kusini kutafuta ufumbuzi wa kudumu katika mgogoro ulioikumba nchi hiyo.

Akichangia kuhusu mageuzi ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Makamu wa Rais alisema Tanzania kwa ujumla inaunga mkono msimamo wa Afrika wa kuwa na viti viwili katika baraza hilo na kura ya turufu bila ya masharti yoyote.

Jaji Mkuu Afafanua Sababu za Kutangaza Nafasi za Majaji

0
0
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman amesema Tume ya Utumishi wa Mahakama imeamua kutangaza nafasi na ajira za majaji ili kuongeza uwazi katika ajira zao. 

Utaratibu huu mpya na wa kwanza kutumiwa na tume hiyo, nchini ulianza kutekelezwa jana baada ya gazeti la serikali la Habari Leo kuchapisha tangazo hilo, likianisha sifa za kitaaluma na uzoefu zinazohitajika na uzoefu wa waombaji na viambatanisho vya uthibitisho wa sifa hizo na uzoefu wa kitaaluma vinavyohitaji.

Akizungumza  kuhusu utaratibu huo, Jaji Chande ambaye ndiye mwenyekiti wa tume hiyo alisema wameamua kutumia utaratibu huo kuongeza uwazi, kupanua wigo na kuongeza ushindani ili kuwapata majaji wenye sifa.

Hata hivyo, Jaji Chande alisema utaratibu huo si kwamba ni mpya bali upo, kwa kuwa ni miongoni mwa taratibu za tume hiyo katika hatua ya kwanza ya upatikanaji wa majaji, yaani ya kupata orodha ya majina ya watu wenye sifa za kuteuliwa kuwa majaji.

“Huu ni utaratibu wa tume, upo kwenye tume na tumekuwa tukiuongea mara kwa mara kwenye tume, lakini tulikuwa hatujautekeleza tu.

"Sasa safari hii tumeona ngoja tujaribu kupanua wigo kwa kutangaza,” alisema Jaji Chande.

Alifafanua kwamba katika taratibu za tume hiyo kupata majina ya kuingia kwenye mchakato wa kuteuliwa kuwa majaji kuna njia tatu ikiwamo ya tume yenyewe kuwasaka.

Njia nyingine ni kuziandikia taasisi za kisheria kama vile Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Wakuu wa vitivo vya sheria wa katika vyuo vikuu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ili kutoa mapendekezo ya majina ya watu wenye sifa hizo.

Pia, alisema njia nyingine ni utaratibu wa kuwapandisha watumishi wa ndani ya mahakama, kama vile mahakimu wakazi na wasajili.

“Lakini pia, hili la kutangaza ni utaratibu wa nchi za Jumuiya ya Madola. Kuna kanuni kwamba uteuzi wa majaji uwe wa wazi ili kuongeza ushindani na ulenge uzoefu, umakini na ujuzi na uzingatie jinsia bila ubaguzi,” alisisitiza Jaji Chande.

Akizungumzia uzoefu wa nchi nyingine katika utaratibu huu wa kutangaza nafasi hizo, Jaji Chande alisema kuwa kuna nchi ambazo zimefanikiwa kuwapata majaji wenye sifa, lakini pia kuna nyingine hazikufanikiwa.

Alitoa mfano wa Kenya ambayo ilianza utaratibu huo kulingana na Katiba Mpya pamoja na Uingereza, lakini akasema Botswana licha ya kutumia utaratibu huo haikufanikiwa kuwapata watu wenye sifa kama ilivyokuwa ikitarajia.

Akizungumzia uteuzi wa majaji, Jaji Chande alisema kuwa hupitia katika hatua tano kabla ya hatua ya uteuzi wa mwisho ambao hufanywa na Rais.

Alizitaja hatua hizo kuwa ni kwanza hatua ya kupendekeza majina, ambayo hufanywa ama kwa watu kuomba au kupendekezwa na taasisi na mamlaka husika; hatua ya uchambuzi wa sifa na mafanikio yao na hatua ya usaili. 

Hatua ya nne, Jaji Chande alisema ni kupendekeza au kuandaa orodha ndogo na ya tano ni hatua ya uchunguzi ambayo hufanywa na vyombo mbalimbali vya dola, kama vile Usalama wa Taifa na vinginevyo.

“Baada ya hatua hizo, ndipo Rais hupelekewa orodha ya majina ya watu wenye sifa na kufanya uteuzi kutoka miongoni mwa majina hayo kulingana na idadi ya nafasi zilizopo. Kwa kila nafasi moja, yanatakiwa majina angalau matatu kwa nafasi moja,” alifafanua.

Kutokana na mchakato huo wa upatikanaji wa majaji, Jaji Chande alikanusha madai ambayo yamekuwa yakitolewa na baadhi ya wanasiasa kuwa wakati mwingine Rais huteua majaji wasio na sifa au ambao hawakupendekezwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama.

“Hakuna jaji aliyewahi kuteuliwa bila kupendekezwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama, hiyo haijawahi kutokea. Majina yote yanapendekezwa na Tume na hakuna jina linaloteuliwa nje ya mapendekezo ya Tume kwani huo si utaratibu wa kikatiba,” alisema Jaji Chande.

Rais Magufuli Akataa Kuwapandisha vyeo Maofisa 17 wa Polisi

0
0
Rais John Magufuli, amekataa kuwapandisha vyeo maofisa 17 wa polisi waolipendekezwa na amewapa nafasi ya kujipanga zaidi. 

Rais Magufuli aliwapandisha vyeo maofisa 60 kuanzia Jumamosi iliyopita, kati yao 25 kutoka cheo cha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) kuwa Naibu Kamishna wa Polisi (DCP). 

Wengine 35 aliwapandisha kutoa cheo cha Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) kuwa Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi. 

Akizungumza jana muda mfupi baada ya maofisa hao kuapa kiapo cha maadili ya umma, Rais Magufuli alisema waliokuwa makamishna wasaidizi waandamizi waliopelekwa kwake katika mapendekezo walikuwa 31, lakini wamerudi 25. 

Pia, alisema waliokuwa makamishna wasaidizi wa polisi waliopendekezwa kuwa makamishna wasaidizi waandamizi wa polisi walikuwa 46, “ wamerudi 35.” 

“Wale ambao hawakurudi tuwape nafasi ya kujipanga tena zaidi. Nataka niwaeleze ukweli kwa sababu inawezekana wako wengine walisikia kwamba majina yao yalipelekwa…Sasa mkawaambie hayakurudi kwa sababu yangu. Wala wasihangaike kutafuta mchawi,” alisema Rais Magufuli. 

Alisema baada ya kupata taarifa na data zote walizonazo, “Nikaona tuwape muda wa kujirekebisha. Kwa hiyo nyinyi mliofanikiwa mpaka mmefikia hapa nawapongeza sana. “Mchakato ulikuwa mrefu na mzito,” alisema Rais Magufuli. 

Aliongeza, “Nyinyi sasa ni makamanda tunaowategemea katika nchi hii. Mmechaguliwa siyo kwa makosa. Mnastahili. Katekelezeni wajibu wenu bila woga kwa kuzingatia sheria.” 

Kuhusu mchakato huo, Rais Magufuli alisema alimwagiza, IGP Ernest Mangu karibu miezi mitano iliyopita kuanza mchakato huo.

Alisema mchakato ulianzia na ukapita kwa wakuu wao (wa polisi) kwa kuangalia historia za wale ambayo majina yao yalikuwa pamoja na kazi zao. 

“Wakapita (majina ya wapendekezwa) mahali pengine mpaka yamefikia kwangu…Ninajua hamtaki kusema lakini mimi nimeumbwa kusema ukweli.” 

Watumishi ‘raia’ kuondolewa 
Katika hotuba yake ya takriban dakika 30 aliyotoa bila kusoma popote, Rais Magufuli alisema inawezekana wapo watendaji wachache ndani ya Jeshi la Polisi ambao aidha kwa makusudi au kwa nia yao mbaya wanalichafua jeshi hilo. 

“Ninawaomba mkawashauri na kuwaelekeza, ikishindikana mkawaondoe katika Jeshi la Polisi. Mfano mzuri ni mhasibu ambaye aliorodhesha watumishi ambao si maaskari kulipwa pensheni wanayolipwa maaskari. 

“Mtu mwenyewe siyo askari, la kujiuliza nyinyi lakini mmeshindwa kumshika,” alihoji. 

Mhasibu huyo, Frank Msaki (ambaye si polisi) alisimamishwa kazi na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira, kwa makosa ya kufanya malipo hewa ya posho ya chakula kwa watu wasio askari. 

Kutokana na hilo, Rais Magufuli alisema kama wanafikiri kuwa na raia kwenye Jeshi la Polisi wanaliharibia jeshi, wahamishwe na wapelekwe utumishi. 

“IGP kaorodheshe raia wote wanaofanya katika Jeshi la Polisi watoke. Tuwapangie kazi nyingine kazi za kiraia. Ili kusudi hawa raia wanaokaa kwenye nafasi za jeshi waondoke. Bila kufanya hivyo inawezekana wataendelea kuwachafulia. Naomba hilo lishughulikiwe,” alisema. 

Mbali na agizo hilo, alimtaka IGP kufuatilia mtu aliyelipwa kati ya Sh20 bilioni hadi Sh60 bilioni kwa ajili ya kutengeneza sare za polisi tangu mwaka jana, lakini hadi sasa bado hajakabidhi sare hizo. 

“Tupate hizo fedha zetu ili mkakomboe magari yenu. Ninategemea siku moja waliohusika na hilo watapelekwa mbele ya haki,” alisema. 

Mwigulu Nchemba
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba aliwataka walioapishwa kufanya kazi kwa bidii na uadilifu. “…Sheria isipofuata mkondo wake wananchi wanachukua sheria mkononi. Tuzuie hilo na kuhakikisha sheria zinafuatwa,” alisema. 

Kamishna wa maadili, Jaji mstaafu Salome Kaganda aliwashauri maofisa hao wa Jeshi la Polisi kuunda kamati za maadili kwa ajili ya kusikiliza manung’uniko yao. 

IGP, Mangu alimshukuru Rais kwa kupokea mapendekezo yao na kuahidi kuwa atahakikisha maofisa hao wanatekeleza kiapo walichokula.

Makonda: Mashoga wanataka kuniangamiza

0
0
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amesema tangu alipotangaza kuanza kukamatwa kwa mashoga, amebaini kuna mkakati unawaohusisha watu hao zaidi ya 150 kutaka kumwangamiza.

Kauli hiyo aliitoa jana Dar es Salaam baada ya kumaliza mahojiano katika kituo cha redio Clouds FM, ambako alikuwa akifafanua hoja na changamoto mbalimbali za mkoa wake.

Alisema kuwa baada ya kubainika kwa mipango hiyo, mashoga wanane wamekamatwa na Jeshi la Polisi kwa hatua zaidi.

“Lazima watu wajue jitihada na harakati za kusimamia katiba na usawa hapa nchini. Hakuna anayezipenda, vita inakuwa kubwa… Nimebaini kuwa mashoga zaidi ya 150 waliketi katika baa moja Kinondoni wakipanga njama za kunimaliza kwa namna moja ama nyingine, lakini kutokana  na taarifa za kiintelijensia, watu kadhaa, wengi wao wakiwa ni mashoga wameshakamatwa,” alisema Makonda.

Katika hatua nyingine, Makonda aliwatolea uvivu watu wanaosambaza ujumbe wa tofauti juu ya maagizo yake katika mitandao ya kijamii, ikiwamo kutengeneza akaunti feki.

“Kwanza wanapaswa kujua kuwa sina akaunti ambayo inaanza na cheo changu, hivyo akaunti zote zangu zimeandikwa kwa jina langu Paul Makonda si vinginevyo, hivyo kila mtu anapaswa kuwa makini na hilo,” alisema Makonda.

Aliweka wazi kuwa kuna agizo batili lililowekwa katika mitandao ya kijamii, akidaiwa kusema kuwa watu wasiokuwa na kazi watakwenda jela, lakini ukweli ni kwamba ameagiza wenyeviti wa Serikali za mtaa kuhakikisha kuwa wanafanya uhakiki wa wakazi wao nyumba kwa nyumba kwa ajili ya usalama wa maeneo wanayoishi.

Aidha Makonda alisisitiza kuwa kutokana na matatizo yaliyopo, kamwe Hatoacha kupambana na mafisadi katika halmashauri zote tatu za mkoa wake, pamoja na wauza unga, wafanyabiashara wa shisha na mashoga.

Polisi Warudisha Vifaa vya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Vilivyokuwa Vinashikiliwa Tangu Mwaka Jana Baada ya Uchaguzi

0
0
Baada ya vifaa vyao vya ofisi zikiwamo kompyuta 25 kushikiliwa na polisi kwa miezi 10, hatimaye jana Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) wamerejeshewa.

Oktoba mwaka jana, polisi walikwenda katika tawi la ofisi ya LHRC Kawe, kisha kuchukua kompyuta za mezani 24 na mpakato tatu huku wakiwashikilia waangalizi 25 wa uchaguzi, kwa kile ilichodai kituo hicho kilikuwa kinakusanya na kusambaza taarifa za matokeo ya urais yasiyo rasmi.

Mkurugenzi wa kituo hicho, Dk Hellen Kijo-Bisimba alithibitishia  kupata vifaa hivyo vilivyokuwa vikishikiliwa na Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.

Dk Bisimba alisema wiki iliyopita waliwapigia simu polisi kuwaomba kurejeshewa vifaa hivyo, zikiwamo simu 25.

“Jana (juzi) polisi walitupigia simu.Leo (jana) tumekwenda kuchukua mali zetu na zote zipo kamili isipokuwa kuna kompyuta moja haifanyika kazi,” alisema.

Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo, Simon Sirro alipopigiwa simu yake ilipokewa na msaidizi wake na kudai yupo mkutanoni. 

Mrema Ataka Watanzania Waupime Utendaji Kazi wake Baada ya Siku 100

0
0
Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Msamaha kwa Wafungwa (Parole), Augustine Mrema amemmwagia sifa Rais John Magufuli huku akiwataka Watanzania kumpa siku 100 aonyeshe mabadiliko katika magereza nchini. 

Mrema aliyasema hayo jana alipohojiwa katika kipindi cha Amka Tuongee kinachorushwa na Kituo cha Televisheni cha Star tv.

“Ni Rais mzuri tuliyempata, ni mchapa kazi, tumpe muda kwa sababu ndiyo kwanza ana miezi minane, lakini ni mchapa kazi kiasi kwamba marais wenzake wanatembea yeye anakimbia,” alisema. 

Julai 16, Rais Magufuli alimteua Mrema ambaye ni Mwenyekiti TLP baada ya kumkumbusha ahadi aliyompa wakati wa kampeni eneo la Himo Kilimanjaro kuwa wasipomchagua kuwa Mbunge wa Vunjo atampatia kazi. 

“Nina uhakika nitafanikiwa kwa sababu nilipokuwa Waziri wa Mambo ya Ndani nilifanya mambo makubwa hadi nikapewa cheo cha Naibu Waziri Mkuu,” alisema.

Bavicha: Msimamo Wetu ni Ule Ule, Lazima Nasisi Tufanye Kikao Chetu Dodoma

0
0

Ikiwa zimebaki siku tatu kabla ya Mkutano Mkuu wa CCM kufanyika, Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) limesema azma yao ya kufanya kikao chao cha kamati ya utendaji mjini Dodoma ipo palepale. 

Julai 16, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa alisema kikao cha Bavicha hakitofanyika kwa sababu itakuwa ni mwendelezo wa vurugu zao. 

Mkutano Mkuu wa CCM, utakuwa na ajenda mbalimbali ikiwamo ya Mwenyekiti wa chama hicho, Jakaya Kikwete kumkabidhi kijiti cha uongozi Rais John Magufuli. 

Katibu Mkuu wa Bavicha, Julius Mwita jana alisema  baraza hilo lipo kwenye hatua ya mwisho ya maandalizi ya kikao hicho kitakachohudhuriwa na zaidi ya wajumbe 50 kutoka mikoa yote. 

“Wajumbe wataanza kuwasili kesho (leo) mjini Dodoma. Hatuna wasiwasi na kikao hiki kwa sababu ni cha ndani siyo mkutano wa hadhara, ambao umepigwa marufuku na polisi,” alisema Mwita. 

Mwita alisema kikao hicho kitakuwa cha siku mbili kuanzia Julai 20 hadi 21 na kwamba, kitahudhuriwa na mameya na wenyeviti vijana wa halmshauri zinazoongozwa na Chadema. 

Alipotafutwa Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Boniface Jacob ambaye ni mwanachama wa Bavicha kujua kama atahudhuria kikao hicho alijibu: “Nitakwenda kwa sababu mimi ni kijana, sina sababu ya kukataa wito wa viongozi wangu wa juu wa Bavicha taifa.” 

Kuhusu kauli ya Kamanda Mambosasa, Mwita alisema polisi ilishatoa maelekezo ya kuruhusu vikao vya ndani. 

“Taarifa ya Mambosasa hatujaishangaa kwa sababu ni desturi yake kujichanganya, leo anasema hivi kesho vile. Tunamtaka atulie asubiri tumpe taarifa ni wapi kikao chetu kitanyika kwa njia ya amani,” alisema Mwita

TCU kuanza kudahili wanafunzi wa kujiunga vyuo vikuu kesho

0
0

Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), itaanza kudahili wanafunzi waliomaliza kidato cha sita wanaoomba kujiunga na vyuo vikuu kuanzia kesho. 

Akizungumza jana, Kaimu Mkurugenzi wa Udahili na Nyaraka wa TCU, Dk Kokubelwa Mollel alisema udahili kwa wenye diploma utaanza Julai 31. 

Dk Mollel alisema kazi hiyo itaendelea kwa mwezi mzima ili kuruhusu wananchi wengi zaidi kupata fursa ya kuomba kudahiliwa na udahili huo utafanyika kwa njia ya mtandao.

Alisema ili wanafunzi waweze kuelewa programu zinazotolewa na vyuo vikuu, tume hiyo imeandaa maonyesho ya 11 yatakayofanyika kuanzia Julai 20 hadi 22, mwaka huu. 

Alisema maonyesho hayo yatafanyika katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam na kufunguliwa na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako.

Waziri Mkuu Majaliwa: Maliasili Na Utalii Jipangeni Vizuri

0
0

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kujipanga vizuri na kufanya mapitio ya idara zake hususan ya misitu baada ya kubainika kuwepo kwa matatizo makubwa.

“Eneo la misitu limekuwa na matatizo makubwa, watendaji wengi si waaminifu na sura ya wizara si nzuri miti mingi inakatwa na fedha haiingii Serikalini. Huu ni mgogoro mpya,” alisema.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jana alipokutana na watumishi wa wizara hiyo jana (Jumatatu, Julai 18, 2018) jijini Dar es Salaam, na kusisitiza kwamba hakuna sababu ya Serikali kuendelea kuwa na watumishi wasiokuwa na uaminifu, uadilifu na uwajibikaji.

Alisema lengo la mkutano huo ni kukutana na watumishi kusikiliza changamoto zao, kukumbushana wajibu, pamoja na kutoa maagizo ili  yatekelezwe kwa utaratibu unaokubalika kisheria.

Alisema mtumishi ambaye atabainika kuwa haitendei haki nafasi yake kwa kutokutimiza majukumu ipasavyo hana sababu ya kuwepo kwa sababu serikali inapoteza fedha nyingi kuwalipa watu wasio na tija. 

Waziri Mkuu alisema sababu inayoikosesha Serikali mapato ni uwepo wa watumishi wasio waadilifu kwenye ofisi za Serikali ikiwemo Wizara ya Maliasili na Utalii hivyo kuna umuhimu wa kuzisafisha.

Alisema kuna uvunaji mkubwa wa misitu kuliko upandaji huku asilimia 50 ya mapato yatokanayo na uvunaji huo yanapotea na kuisababishia Serikali hasara ambapo alihoji sababu ya wizara kushindwa kusimamia jambo hilo. 

Katika hatua nyingine; Waziri Mkuu aliitaka wizara hiyo kupunguza idadi ya vizuizi vya ukaguzi wa mazao ya misitu kwenye barababara mbalimbali baada ya kukosa tija kutokana na upotevu wa misitu unaotokea kila siku.

Alitoa mfano wa barabara ya kwenda mikoa ya kusini  kuanzia Dar es Salaam ambapo alisema ina vizuizi visivyopungua sita na kila kizuizi kinatumika kwa ajili ya kukagua mazao ya misitu na maliasili inayotoka kuvunwa. 

“Vizuizi vya katikati ya safari havina umuhimu na badala yake kuwe na vizuizi mwanzo na mwisho ili rasilimali zingine zitumike kuongeza nguvu na umakini wa ukaguzi kwenye vituo vichache vitakavyosalia,”.

“Kwa mfano ukitokea Ikwiriri kuja Dar, kuna vituo vya ukaguzi wa maliasili visivyopungua sita, kuna Ikwiriri, Kibiti,  Jaribu Mpakani,Mkuranga, Vikindu  kote huku wanakagua lakini linapofika kituo cha mwisho cha Mbagala linakutwa na makosa kwenye mzigo kwanini’?

“Yule mkaguzi wa kwanza alifanya kazi gani? Kuna tatizo la uadilifu na ninyi ni mashahidi, sasa naagiza ongezeni nguvu kwenye vituo vikuu vya ukaguzi yaani mwanzo na mwisho,” alisema. 

Aidha alisema ni muhimu kukawa na mabadiliko kwenye mfumo wa mauzo ya misitu kutoka wa sasa (kuuza kwa eneo) na kuhamia kwenye mfumo wa mnada ambao utaongeza mapato ya Taifa na utaweka uwazi.

Pia aliwataka watumie mashine za malipo za kielektroniki (EFD),wanapofanya mauzo ya mazao ya misitu ili kuepusha matumizi ya daftari na risiti bandia ambazo hazitambuliwi na
wizara.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S.  L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM.

JUMANNE, JULAI 19, 2016

Kiwanda Cha Nguo Cha 21st Century Chateketea Kwa Moto

0
0
BAADHI ya mitambo, nguo na malighafi katika Kiwanda cha Nguo cha 21st Century kilichopo Kihonda, Morogoro vimeteketea kwa moto na kusababisha hasara.

Akizungumzia moto huo Clement Munisi, meneja uzalishaji wa kiwanda hicho amesema kuwa, moto huo ulianza saa 12:00 asubuhi leo katika  mashine moja ya kuzalishia  nguo kwa ulianza kwa kutoa cheche.

Amesema, wafanyakazi walijaribu kuuzima kwa kutumia kifaa maalumu cha kuzima moto (Fire extinguisher ) bila mafanikio yoyote.

Munisi amesema kuwa, moto huo uliunguza baadhi ya mitambo na malighafi zilizokuwa katika chumba kimoja ndani ya kiwanda hicho na kusababisha hasara kubwa.

Amesema kuwa, moto huo uliendelea kuenea katika vyumba vingine ndani ya kiwanda hicho jambo ambalo lililosababisha baadhi ya nguo zilizokuwa zikiendelea kutengenezwa kuungua. Hata hivyo, hajaeleza dhamani halisi ya vitu vilivyoteketea kwa moto.

Ramadhani  Pilipili, Kamanda wa Kikosi cha Zimamoto  Mkoa wa Morogoro amesema kuwa, licha ya kuwahi kufika mapema katika eneo la tukio na juhudi za kuuzima moto, bado miundombinu ya kiwanda hicho imekuwa  kikwazo.

“Miundombinu ya kiwanda ni tatizo kutokana na kukosekana eneo sahihi la kupitishi mipira ya maji na hivyo kulazimika kutumia muda mwingi kwa kuvunja ukuta ili kufanikisha zoezi la uzimaji,” amesema.

Viewing all 45270 articles
Browse latest View live




Latest Images