Quantcast
Channel: MPEKUZI
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live

Waziri Mkuu wa India Kutua Nchini Leo

0
0

WAZIRI Mkuu wa India, Narendra Modi anawasili leo nchini kwa ajili ya ziara ya kitaifa ya siku mbili kwa lengo la kudumisha ushirikiano katika sekta mbalimbali kati ya nchi hizo mbili.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Augustine Mahiga alisema Modi atatumia fursa hiyo kukuza uhusiano wa kihistoria baina ya nchi hizi mbili pamoja na kufungua maeneo mapya ya ushirikiano wa kiuchumi.

Alisema Modi atakutana na Rais John Magufuli Ikulu na kufanya naye mazungumzo. Pia kuweka saini kwenye mikataba mbalimbali ya ushirikiano kati ya sekta za viwanda, maji, elimu, sayansi na teknolojia na baadaye kuzungumza na waandishi wa habari.

Dk Mahiga alisema Modi pia atazungumza na jumuiya ya wafanyabiashara wakubwa wa India ambao baadhi yao wameshaonesha nia ya kuwekeza katika sekta ya ujenzi wa viwanda vya kutengeneza chuma, saruji, dawa ya binadamu na maji ya matunda.

“Natoa mwito kwa wafanyabiashara mbalimbali hapa nchini watumie fursa hii kushiriki ili waweze kukutana na wenzao, Kongamano hilo litafanyika kwenye ukumbi wa Benki Kuu (BoT) na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa atakuwa mgeni rasmi,” alisema.

Rais Magufuli Amteua Dkt. Leonard Lutegama Maboko kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS)

0
0

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Dkt. Leonard Lutegama Maboko kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS).

Taarifa ya Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi imeeleza kuwa uteuzi huu umeanza tarehe 07 Julai, 2016.

Kabla ya uteuzi huu Dkt. Leonard Lutegama Maboko alikuwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya binadamu Mbeya (NIMR Mbeya).

Dkt. Leonard Lutegama Maboko anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Dkt. Fatma Mrisho ambaye mkataba wake umemalizika tangu tarehe 30 Juni, 2016.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
08 Julai, 2016

Watoto Wanne wa Familia Moja Wateketea Kwa Moto Wakiwa Usingizini

0
0
HUZUNI imetanda katika wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma, baada ya ajali ya moto wa kibatari kuteketeza watoto wanne wa mama mmoja, waliokuwa wamefungiwa chumbani na dada anayewalea.

Ajali hiyo ilitokea usiku wa kuamkia jana katika mtaa wa Nyerere, mji mdogo wa Kibaigwa wilayani Kongwa, wakati mama wa watoto hao aliposafiri kwenda shambani Kiteto mkoani Manyara, kwa ajili ya kuvuna mazao na kuwaacha watoto wake mikononi mwa dada, aliyekuwa akimsaidia kuwalea.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi mkoani Dodoma, Lazaro Mambosasa alisema chanzo cha ajali hiyo ni mlipuko wa kibatari kilichokuwa ndani ya chumba walicholala watoto hao, ambacho kilichoma godoro na kuteketeza nyumba yote.

Moto huo ulioanzia katika chumba hicho, umeelezwa kuteketeza nyumba yote ya vyumba sita iliyojengwa kwa tofali za udongo mali ya Nelson Mdachi.

Kamanda Mambosasa aliwataja watoto hao kuwa ni Elizabeth Nelson (11) mwanafunzi wa darasa la saba, Samweli Mdachi (7) anayesoma darasa la kwanza na Nase Mgomba (9) anayesoma darasa la pili katika shule ya msingi Miembeni na Peter Lema (9) mwanafunzi darasa la tatu shule ya msingi St Paulo.

Kutokana na ajali hiyo, Kamanda Mambosasa amewakumbusha wazazi wasiache watoto peke yao nyumbani kwa kuwa ni hatari kwani ajali ikitokea ni vigumu kuokolewa.

Taarifa kutoka kwa watu wa karibu na majirani wa familia hiyo, zimedai kuwa mama wa familia hiyo alikwenda shambani kuvuna mazao katika wilaya ya Kiteto, mkoani Manyara na kuwaacha watoto hao chini ya uangalizi wa msichana aliyefahamika kwa jina moja la Ester.

Kwa mujibu wa madai yao, ilipofika usiku Ester anayetajwa kuwa na jukumu la kulea watoto hao, alitoka na kwenda kusikojulikana huku akiwafungia watoto hao kwa nje.

Mkazi wa Kibaigwa, Denis Luhunga, alipozungumza na mwandishi kuhusu ajali hiyo alidai kuwa kibatari kilipolipuka, kilisababisha godoro kushika moto na kuteketea kwa watoto hao. 

“Aliwafungia watoto ndani akaacha kibatari kinawaka, baada ya kulipuka moshi mwingi ulijaa ndani,” alidai Luhunga.

Kuhusu alipo baba wa familia hiyo, mkazi mwingine wa eneo la tukio hilo, Paulo Sauli alisema baba wa watoto hao, aliyemtaja kwa jina la Nelson Mdachi, alishakufa miaka mitatu iliyopita na jukumu la kuwalea aliachiwa mama yao.

Alifafanua kuwa baba huyo ambaye wakati wa uhai wake alifahamika kwa jina maarufu la ‘Moja kwa moja’, alikufa baada ya kuanguka kutoka juu ya mti alipokuwa akirina asali na tangu hapo, jukumu la kulea likabaki kwa mama mzazi wa watoto hao.

“Tukio hilo limetusikitisha sana ni tukio baya maana wameteketea kabisa hajulikani nani ni nani,” alisema Sauli na kuongeza, “Hata Ester hafahamiki alipo, kuna watu wengi lakini tumemuangalia hapa msibani hatumuoni.”

Taarifa nyingine kutoka eneo la tukio, zilidai kuwa Mdachi alizaa na mama huyo watoto wawili na baada ya kufariki, mama huyo alizaa watoto wengine wawili na wanaume wengine.

Taasisi 680 Kufutwa.....Zipo za Kidini na za Kisiasa

0
0
WAKALA wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), inakusudia kuzifutia usajili bodi za udhamini 680 za taasisi mbalimbali; ambazo zimekiuka masharti, ikiwa ni pamoja na kutokuwa hai.

Aidha, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe ameuruhusu wakala huo kuanza kusajili bodi za udhamini; huku akiutaka kuhakikisha bodi zitakazosajiliwa zinaendeshwa kwa mujibu wa sheria na taratibu.

Akizungumza jana Dar es Salaam katika mkutano wa Bodi ya Wadhamini ya Rita, Dk Mwakyembe alisema, wakala huo unatakiwa kuzifuta haraka bodi hizo ili kuwepo na bodi chache ambazo ziko hai.

“Mmefanya kazi nzuri ya kuhakiki baadhi ya hizi bodi, endeleeni kuhakikisha tuna vyombo vichache ambavyo viko hai…kuna bodi kama 500 ambazo haziko hai na mnakusudia kuzifuta, zifuteni haraka,” alisema Dk Mwakyembe.

Alisema serikali imedhamiria kudhibiti mapato na ndio sababu katika mkutano wake na Bodi ya Rita alitoa agizo kwa wakala huo kusitisha usajili mpya wa wadhamini wa asasi, vyama, misikiti, makanisa na taasisi mbalimbali huku akitoa siku 90 wakala huo ukamilishe uhakiki wa bodi hizo.

Alisema baadhi ya vikundi hivyo ambavyo vingine vimekuwa vikiibuka wakati wa kampeni na uchaguzi vimekuwa vikitumika vibaya kupata misamaha ya kodi na vingine kuomba ruzuku.

Dk Mwakyembe alifafanua kuwa katika kikao chake na mamlaka zote zinazohusika na usajili wa vikundi vya kijamii, mashirika, kampuni na asasi mbalimbali ulikuwa na lengo la kuimarisha taratibu za usajili ili kudhibiti utitiri wa vikundi hivyo.

Aidha, alisema mkutano huo pia ulikuwa na lengo la kufanya maboresho kwa mamlaka hizo ili mifumo yao iweze kuwasiliana ili kulinda maslahi mapana ya Taifa. 

Awali Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Rita, Emmy Hudson alisema, tayari tangazo la kusudio la kuzifutia usajili bodi za wadhamini limeshaandaliwa na litatolewa muda wowote kuanzia sasa.

Alisema jumla ya bodi za wadhamini zilizosajiliwa ni 5,262 ambazo kati ya hizo zilizohakikiwa ni 1,544 na kwamba katika uhakiki huo walikumbana na changamoto ya malalamiko kutoka kwa bodi hizo kuwa nyingine ziko mbali.

Hudson alisema kati ya hao 5,262 ambao wako kwenye kanzi data ya wakala huo walichambua na kubaini walioko hai ni 4,287 pekee.

“Bodi za Udhamini 500 zimebainika kuwa haziko hai…zoezi la kuingiza taarifa kwenye databae (kanzidata) linaendelea lakini pia tunaomba tuongezewe muda au ikiwezekana liwe endelevu,” alisema.

Alisema kabla ya kuanza kwa uhakiki wa bodi hizo tayari walikuwa na idadi ya bodi 200 ambazo zilitakia kufutiwa usajili na zilipelekewa notisi za kufutiwa usajili wao ambapo kati ya hizo 20 tu ndizo zilizojibu na kuomba kutofutiwa usajili wao.

Hata hivyo, alisema wakala huo umekuwa ukikabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo za taasisi kumiliki mali bila kuwa na idhini ya bodi ya wadhamini kinyume cha sheria, muda wa kutembelea taasisi hizo kuwa mdogo, baadhi ya taasisi kubadili majina na anuani zao bila kutoa taarifa.

“Lakini pia tumebaini kuwepo kwa baadhi ya bodi ambazo hazitambui wajibu wao na pia mkanganyiko wa tafsiri ya sheria kutoka katika taasisi mbalimbali zinazoshughulika na usajili,” alisema Hudson.

Kazi kubwa zinazofanywa na bodi za udhamini ni kusimamia rasilimali fedha pamoja na uendeshwaji wa kampuni au taasisi husika.

Polisi Watano wauawa katika maandamano ya kupinga mauaji ya Weusi Marekani

0
0
Askari watano wa Jeshi la Polisi jana waliuawa kwa kudunguliwa na mtu asiyejulikana mitaa ya Dallas nchini Marekani, wakati wa maandamano makubwa ya kupinga mauaji ya watu wawili weusi yaliyofanywa na askari wa kizungu wiki hii.

Ripoti ya jeshi la polisi limeeleza kuwa mbali na askari hao waliouawa, askari wengine wanne wa jeshi la polisi na afisa mmoja wa usafiri wa mwendo kasi walijeruhiwa vibaya.

Mkuu wa Jeshi la Polisi wa Dallas, David Brown aliwaambia waandishi wa habari kuwa maafisa wa Polisi walikuwa katika hatua za kumtia nguvuni mtuhumiwa mmoja kutokana na tukio hilo,  na kwamba wakati wanajaribu kuzungumza naye akiwa mbali akiwa ameshikilia bunduki alieleza kuwa alikuwa amekasirishwa na vitendo vya mauaji ya polisi wazungu dhidi ya weusi yaliyofanyika Alhamisi.

“Alisema alitaka kuwaua wazungu,” Brown alieleza.

Baada ya majibizano ya risasi na mtu huyo aliyetajwa kwa jina la Micah Xavier Johnson, polisi walituma robot lenye vilipuzi ambavyo vilimuua.

Kodi ya Utalii Tanzania Yashtua mataifa Ulaya

0
0
Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye shughuli za utalii iliyoanza mwezi huu, imezishtua nchi 30 za Ulaya ambazo zimeiandikia barua Serikali ya Tanzania zikiomba ifikirie upya au isianze kutumika hadi mwaka ujao. 

Kodi hiyo, ambayo ni sehemu ya mkakati wa Serikali kukusanya mapato ili kuondokana na utegemezi, ilitangazwa kwenye Bunge la Bajeti lililopita na tayari Sheria ya Fedha imeshapitishwa kubariki matumizi yake, licha ya wabunge kuipinga kwa maelezo kuwa itazipa nchi washindani mwanya wa kukuza utalii. 

Dk Philip Mpango alisema walipata wazo la kuanzisha kodi hiyo kutoka nchi jirani ya Kenya, lakini wakati akitangaza hayo waziri mwenzake wa nchi hiyo alitangaza kuiondoa baada ya utalii kuathirika kutokana na mashambulizi ya kigaidi.

Wakati sheria hiyo ikianza kutumika nchini, nchi hizo za Ulaya ambazo ni wadau wakuu katika sekta ya utalii zimemwandikia barua hiyo Dk Mpango, naibu wake, Dk Ashatu Kijaji na Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe.

Chama cha Kitaifa wa Mawakala wa Usafiri na Wasimamizi wa Utalii (ECTAA) kutoka nchi 30 za Ulaya ndicho kinachoziwakilisha kampuni zaidi ya 70,000 za utalii barani humo. Nchi hizo ndizo zinazotoa asilimia 50 ya watalii wote duniani.

Katika barua yao iliyoandikwa na Katibu Mkuu wa ECTAA, Michel de Blust, nchi hizo zilieleza wasiwasi wao kutokana na utambulishwaji wa ghafla wa kodi hiyo katika huduma za utalii, zikisema uamuzi huo unaongeza gharama za safari nchini.

“Najua utakubaliana na mimi kuwa kodi ina umuhimu wake na ina madhumuni yake, lakini inaweza kubadili mawazo ya watalii na wakachagua maeneo mengine,” inasema barua ya Blust.

Waziri wa Fedha na Mipango, “Mfano mzuri ni Kenya, utambulishaji wa kodi katika huduma za utalii mwaka jana ulishusha idadi ya watalii kwa asilimia nne na baadaye Kenya waliamua kuachana na kodi hiyo ili kudumisha ushindani wake.”

Barua hiyo inasema kodi hiyo katika huduma za utalii itaathiri waandaaji wa safari za watalii wanaotoa huduma nchini kwa sababu hakukuwa na tangazo la kuwaandaa kabla ya kuanzishwa kwa tozo hiyo.

“Waandaaji wa safari wa Ulaya wanawajibika na sheria inayomlinda mteja, hivyo wanatakiwa wawe wanafahamu bei na kodi mpya kabla. Kwa sasa ni vigumu mno kwa waandaji kubadili bei zao ghafla,” inasema barua hiyo.

Kadhalika, barua hiyo inaeleza kuwa Wakala wa Utalii wa Tanzania uliwasiliana na Wakala wa Ulaya kuhusu kodi hiyo na mawakala wa Ulaya wanatafakari kama wanaweza kuingia gharama hiyo au kujiondoa katika mpango huo.

Kama kodi hii ikiahirishwa, basi waandaaji wa safari za watalii watajipanga kuingia gharama hizi na kubadili mfumo wote wa huduma hizo Ulaya,” inasema barua hiyo.

Hivi karibuni, Waziri Maghembe alinukuliwa kwenye mkutano wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), akisema kuwa Serikali haitabadili msimamo huo.

Alisema Sh7 bilioni wanazotarajia kupata kwa kutoza VAT kwenye huduma za utalii, zitawapa uwezo wa kutangaza utalii nje ya nchi na kuziba pengo la bajeti linalotokana na kushuka kwa utalii wa uwindaji. Alisema VAT itakayokatwa ni asilimia 18 ya kitu kilichonunuliwa na inatozwa wakati wa kununua huduma ya utalii.

Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi alisema hajaiona barua ya ECTAA, lakini akasema watafanya kikao na Chama cha Wafanyabiashara za Utalii Tanzania (Tato) ili kujadili nini kifanyike ili sekta ya utalii isiyumbe.

“Hili ni suala mtambuka na hii VAT ilipitishwa na kikao cha bajeti, wizara kwa sasa haina la kufanya zaidi ya kutafuta njia mbadala ili sekta isiyumbe,” alisema.

Tovuti kwa ajili ya watalii ya Afrika, Safaribookings.com imeeleza kuwa wamekuwa wakipata barua pepe kutoka kwa wateja ambao wamepewa taarifa kutoka kwa wasimamizi wa watalii kulipa fedha za ziada.

Marc Harris, mkurugenzi wa kampuni ya Tanzania Odyssey inayotoa huduma za kitalii na yenye makazi yake nchini, aliliambia gazeti la Daily Telegraph la Uingereza kuwa kodi mpya ni janga kubwa ambalo halikutarajiwa na wengi.

“Watanzania wanaweza kufanya chochote kuhusu kodi, lakini suala la muda ndiyo tatizo. Wametupa taarifa hizi Juni 23, wiki moja tu kabla ya kodi kuanza kutozwa,” alikaririwa na gazeti hilo.

Alisema gharama kubwa itaonekana kwenye malazi ambayo inaonekana kuongezeka kwa asilimia saba.

“Kinachoshangaza ni kuwa Hifadhi za Taifa hazijasajiliwa VAT, lakini inatoza fedha hizo. Sijui watazitumiaje,” alisema Harris.

Mmiliki wa kampuni ya kitalii ya Safaribooking.com, Wouter Vergeer alisema muda mfupi waliopewa umewashtua.

“Maelfu ya wateja wameshtushwa na chaji hizo ambazo hazikutarajiwa. Wengi hawajapata muda wa kujipanga kwa tozo hizo, hata risiti zenyewe za VAT hatuna,”alisema.

Mizengwe Yasukwa Kumng’oa Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Vuai Ali Vuai

0
0
Wakati Mkutano Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) unatarajiwa kujadili ajenda kadhaa ikiwamo ya Rais John Magufuli kukabidhiwa uenyekiti wa chama ngazi ya taifa, baadhi ya wajumbe wameanza kupika zengwe kutaka baadhi ya viongozi wa Zanzibar watimuliwe.

Katika mkutano huo uliopangwa kufanyika Julai 23, Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais mstaafu Jakaya Kikwete anatarajiwa kumkabidhi kijiti hicho Rais Magufuli ikiwa ni sehemu ya utamaduni wa chama hicho viongozi kukabidhiana nafasi hiyo kabla ya kumaliza muda. 

Marais wastaafu wamekuwa na utamaduni wa kumwachia nafasi ya uenyekiti wa chama Rais aliyeko madarakani kabla ya muda wao wa miaka mitanio kumalizika, kama alivyofanya Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa. 

Makabidhiano ya kijiti hicho yatawezekana tu baada ya Rais Magufuli ambaye atakuwa mgombea pekee wa uenyekiti kupigiwa kura nyingi za ndiyo na wajumbe mkutano huo mkuu na hivyo chama kuandika historia nyingine kwa Kikwete kung’atuka katika uongozi wa chama. 

Hata hivyo, habari zilizotufikia  jana zinasema mbali ya ajenda ya kubadilishana kijiti cha uongozi na kupokea taarifa ya hali ya siasa na mabadiliko ya muundo wa chama, mikakati inasukwa ili baadhi ya viongozi wa sekretarieti ya chama kutoka Zanzibar akiwemo Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Vuai Ali Vuai, wang’olewe kwa kukitelekeza chama. 

Habari hizo zinasema Vuai ni miongoni mwa viongozi ambao mwaka 2014 walijikita zaidi katika Bunge Maalum la Katiba (BMK) mjini Dodoma kwa zaidi ya miezi minne (siku 130) na kuacha kufanya shughuli za chama jambo lilosababisha upinzani kutumia nafasi hiyo kujikita zaidi ndani ya visiwa hivyo. 

“Sasa ndani ya chama kuna fukuto, inasemekana kuwa kitendo cha wanachama hao kujikita katika Bunge Maalumu la Katiba lililofanyika mwaka 2014 kilisababisha matokeo mabovu ndani ya chama kwa upande wa CCM Zanzibar hivyo inaonyesha wazi Naibu Katibu Mkuu ameshindwa kutimiza wajibu wake hivyo ni lazima wawajibishwe,” kilisema chanzo cha habari hizo. 

Bunge hilo lililotarajiwa kukamilisha kazi kwa siku 70, lilianza Februari 18 lakini hadi Aprili 25 lilikuwa halijakamilisha na ndipo liliongezewa siku 60 kuanzia Agosti 5 hadi Oktoba 4. Vuai alikuwa miongoni mwa wajumbe 201 nchini ambao hawakuwa wabunge. 

Kiongozi huyo alipoulizwa kama anajua kwamba anashutumiwa na wenzake kwa madai ya kukitelekeza chama hadi kikawa na wakati mgumu wakati wa uchaguzi mkuu, Vuai alisema anajua na kwamba mizengwe hiyo inasukwa na kikundi cha watu wasiozidi 15. 

“Suala la kwenda Bunge Maalumu la Katiba mimi kwangu siyo news (habari). Wanaoeneza taarifa hizi nawajua na hawapendi mimi niwe katika nafasi hii kutokana na maovu yao wanayoyafanya,” alieleza Vuai. 

“Hili suala la mimi kwenda Bunge Maalumu la Katiba linawauma na kuwakereketa rohoni kikundi fulani... Nilishasema huko nyuma mimi sikujipendekeza kwenda katika bunge hilo, bali nilifuata tarataibu zinazotakiwa.” 

Vuai alilisisitiza kuwa yeye kama kiongozi alifanya kazi kwa mujibu wa katiba ya chama na madai ya uchaguzi wa Zanzibar kuwa mgumu alisema suala hilo limeshatolewa ufafanuzi na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha. 

Alisema anachojua CCM wana utaratibu wa kubadilisha viongozi baada ya kipindi fulani, hivyo kama viongozi wake wakuu watamwona anafaa kuendelea nafasi hiyo ataendelea kama kawaida na endapo wataona hafai kuendelea yuko radhi nafasi hiyo ichukuliwe na mwingine.

“Kama nitaendelea Inshallah. Lakini nafasi ya unaibu sikuomba, sitokuja kuiomba na siwezi kuing’ang’ania ila najua kuna kikundi hapa Zanzibar kinanifisidi kwa kujipendekeza kwa viongozi na kuongea uongo juu yangu,” alisema.

 “Nawaambia hivi, mimi sina tabia ya kujipendekeza nafanya kazi kwa uadilifu kwa mujibu wa Katiba ya chama. Hili ndilo linawaumiza na kueneza chuki dhidi yangu lakini hawanitishi kwa hilo kwa sababu CCM Zanzibar si Vuai,” alieleza. 

Vuai alisema kikundi hicho ni cha wanaCCM wa Zanzibar na hakizidi watu 15 na kimekuwa na tabia ya kufanya mambo ya kifisadi kuanzia ndani ya chama hadi kwenye jumuiya za chama na muda ukifika atakitaja hadharani na matendo wanayoyafanya dhidi ya CCM. 

“Narudia tena muda ukifika nitawaumbua hadharani. Najua hawanipendi kwa sababu najua ufisadi wao. Mimi sitorudi nyuma na msimamo wangu wa kufanya kazi kwa uadilifu kwa sababu sikupata nafasi hii kwa ufisadi,” alisisitiza. 

Habari zaidi zinasema kuwa sekretarieti ya chama hicho kwa sasa inatumia muda mrefu kubuni muundo mpya wa kuirejesha CCM kwenye ushindani ili iweze kukabiliana vilivyo na joto la vyama vingine vya upinzani vinavyoelekea kuwa na ushawishi mkubwa hasa kwa vijana. 

Katika muundo huo, viongozi mbalimbali wanatajwa kutolewa katika nyadhifa zao akiwamo Katibu wa Itikadi na Uenezi Nape Nnauye ambaye kwa sasa ameteuliwa kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo. 

Kwenye mabadiliko hayo, Rais Magufuli anatajwa kujielekeza kwanza kwenye Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ambayo kwa mfumo wa chama hicho ndiyo injini ya mwelekeo na mafanikio ya chama kwa jumla.

Video: Kijana apachikwa jina ‘Mkereketwa wa Mwendokasi’ baada ya kumfanyia Rais Magufuli kitendo hiki

0
0
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli hivi karibuni katika ziara zake alikutana na kijana aliyemshangilia kwa nguvu zake zote hali ambayo ilimfanya mkuu huyo wa nchi kumwita na kupiga naye picha.

Kijana huyo ambaye anaitwa Omar Abdalah Ramadhani ‘Mkereketwa wa Mwendokasi’ alisikika akisema “Magufili kule aliko, aminia mzazi, Mungu akupe baraka zote mzazi, na asiyekupenda Mungu atamtokomeza, Watanzania tuko nyuma yako” kauli iliyomfanya Rais Magufuli amwite ili apige naye picha na baadaye kuombewa dua na kijana huyo.
 
Baada ya tukio hilo kufanyika na kurekodiwa, kijana huyo anaendelea kuwa maarufu katika mitandao ya kijamii huku baadhi ya watu wakimpachika  jina la ‘Shabiki wa Mwendokasi’.


Mhasibu Mkuu wa Jeshi la Polisi Asimamishwa Kazi Kwa Kosa la Kulipa Malipo Hewa

0
0

Katibu  Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Meja Jenerali Projest Rwegasira amemsimamisha kazi Mhasibu Mkuu wa Jeshi la Frank Charles Msaki kutokana na makosa ya kufanya malipo hewa yaani kulipa  posho ya chakula kwa watu ambao si askari.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Wizarani hapo ambayo nakala tumeipata, Mhasibu Mkuu huyo Bw. Frank Msaki  anasimamishwa kazi kwa kufanya malipo ya kiasi cha sh. 305,820,000  kama posho ya chakula kwa watu ambao sio askari kwa kipindi cha kuanzia mwaka  wa fedha 2013/2014 hadi 2015/2016.

Meja Jenerali Rwegasira amesema kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu za Kijeshi  anayetakiwa kulipwa posho ya chakula yaani ‘ration allowance’ ni askari peke yake na si mtu mwingine yeyote yule.


Meja Jenerali Rwegasira amesema anamsimisha kazi Mhasibu Mkuu huyo tangu leo tarehe 9 Julai, 2016 ili kupisha uchunguzi ufanyike juu ya tuhuma zinazomkabili.

Katibu Mkuu huyo amesema baada ya jalada la uchunguzi kufunguliwa na Ukaguzi Maalumu kufanywa na Mkaguzi wa Ndani wa Jeshi la Polisi imebainika kuwa mbinu mbalimbali zimetumika ili kufanikisha  malipo hayo hewa.

Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Jumapili ya July 10

Wakurugenzi Wateule Kukaguliwa vyeti vyao....Ikulu Yaagiza Wafike na Nakala Halisi za Vyeti Kabla Ya Kuapa

0
0
WAKURUGENZI wa halmashauri za majiji, manispaa, miji na wilaya walioteuliwa Jumatano ya wiki hii, wametakiwa kuwasilisha nakala halisi za vyeti vyao vya taaluma, kabla ya kuapa.

Wakurugenzi hao wa majiji matano, manispaa 21, miji 22 na wilaya 137 nchi nzima, wanatarajiwa kuapishwa Ikulu Dar es Salaam keshokutwa.

Taarifa ya Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi, iliyotumwa jana kwa vyombo vya habari, imewataka wakurugenzi hao kuwa watakapofika kwa ajili ya kiapo cha uadilifu wa uongozi wa umma, wahakikishe wanafika na nakala zao halisi za vyeti vya kitaaluma kwa ajili ya ukaguzi.

“Ieleweke kuwa uhakiki wa vyeti halisi vya kitaaluma, unafanywa kwa lengo la kujiridhisha baada ya mchakato wa kawaida wa uhakiki kufanywa kwa kutumia vyeti visivyokuwa halisi yaani vivuli,” imeeleza taarifa hiyo iliyotumwa na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa.

Taarifa hiyo imesema kuwa uhakiki huo wa vyeti utaanza saa mbili asubuhi na kuwataka wahusika wote kuingia Ikulu kwa kupitia geti kuu lililopo upande wa Mashariki, linalotazamana na bahari ya Hindi. Hatua hiyo ya Ikulu imekuja wakati taifa likikabiliwa na changamoto ya kukithiri kwa udanganyifu katika vyeti wakati wa kuomba ajira.

Takwimu za mwaka juzi zilionesha kuwa ndani ya mwaka huo, watumishi 1,360 walikutwa na vyeti visivyo halali. 

Uhakiki wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) katika mwaka huo, ulibaini kuwa baadhi ya watumishi wakiwemo wa serikali walikutwa wakitumia vyeti vya kughushi ambavyo vimebadilishwa matokeo, wengine walikutwa na vyeti vya bandia huku wengine wakitumia vyeti vya watu wengine.

Mwaka huo huo, Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, ilitoa taarifa ikieleza kubaini kuwepo kwa udanganyifu wa vyeti 677, kwa watumishi serikalini.

Takwimu zinaonesha kuwa kati ya watu 13,554 walioomba ajira katika miaka mitatu yaani 2010, 2011 na 2012; watu 816 walibainika kudanganya kwa kutumia vyeti vya taasisi mbalimbali za elimu, vyeti vya kuzaliwa na vinginevyo.

Kutokana na hali hiyo, Necta ilitangaza kuanza kujipanga kushirikiana kwa karibu na mamlaka za ajira na udahili, ili kuhakikisha uhakiki wa vyeti vinavyotolewa na baraza hilo, unafanyika kabla ya mtahiniwa kuajiriwa au kudahiliwa.

Jeshi la Polisi Latoa ONYO Kali Kwa Vyama vya Siasa.....Ladai Halihitaji Msaada wa Chama Chochote Katika Shughuli za Kiulinzi

0
0
ONYO limetolewa kwa vyama vya siasa vinavyojaribu kusuguana na Jeshi la Polisi kukumbuka kuwa hilo ni jeshi, ambalo liko tayari kutumia nguvu na rasilimali zote, kuhakikisha raia na mali zao ni salama.

Jeshi hilo pia limesema halihitaji msaada wowote kutoka kwa vyama vya siasa na wakihitaji msaada, wataomba kutoka katika vyombo vingine vya kiusalama.

Kauli hiyo imetolewa jana na Kaimu Kamishna wa Polisi Operesheni na Mafunzo, Nsato Mssanzya, baada ya Baraza la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bavicha), kudai kuandaa vijana kwenda Dodoma kusaidia polisi kuzuia Mkutano Mkuu wa CCM unaotarajiwa kufanyika Julai 23 mwaka huu.

“Nawaasa vijana, watoto msisuguane na jeshi, si busara kusuguana na jeshi, fanyeni mambo ambayo nchi itakuwa salama, polisi itatumia nguvu zote pamoja na rasilimali tulizonazo kuhakikisha raia na mali zao wanabaki salama.

“Hakuna suala la kusaidia Jeshi la Polisi au nini, sisi tunajitosheleza wenyewe, kama tutahitaji msaada wowote katika ulinzi basi msaada huo tutauomba kwa vyombo vingine vya ulinzi, ambavyo vina mafunzo kama sisi na si kwa vyama vya siasa,” alionya.

Alisema anatumia neno ‘ole’ kwa watu watakaojaribu kuvuruga amani kwa madai ya kusaidia kuzuia mkutano, kwamba polisi haitasita kuchukua hatua.

Alifafanua kuwa Jeshi la Polisi halijazuia mikutano yote ya kisiasa na kwamba limelazimika kutoa ufafanuzi, kutokana na kuibuka kwa tafsiri tofauti kutoka kwa vyama vya siasa na makundi ya watu, baada ya polisi kutoa tamko Juni 7 mwaka huu la kupigwa marufuku mikutano ya hadhara.

Mssanzya alisema hakuna sehemu yoyote tamko hilo lilipiga marufuku mikutano ya kiutendaji na kiutawala ya vyama vya siasa iliyofanywa kwa mujibu wa kanuni za vyama husika.

“Ndio maana baada ya tamko lile, baadhi ya vyama vimefanya na kupanga kufanya mikutano ya kiutendaji na kiutawala bila kuingiliwa au kuzuiwa na Jeshi la Polisi,” alisema Mssanzya akitolea mfano mkutano wa Bavicha kuzungumza na vyombo vya habari Julai 3, mwaka huu.

Alisema shughuli ya Jumuiya ya Wanafunzi wa Vyuo Vikuu vya Chadema (Chaso) iliyopanga kufanyika Dodoma na ule wa chama cha ACT Wazalendo, ilizuiliwa kwa sababu ujumbe uliolengwa katika shughuli hizo, ulikuwa wa uchochezi na haikuwa mikutano ya kiutendaji au kiutawala.

Hata hivyo alisema pamoja na vyama vya siasa kuruhusiwa kufanya mikutano hiyo ya ndani, bado jeshi hilo lina mamlaka ya kuzuia pale itakapobainika ina lengo la kuhamasisha uchochezi au kuharibu amani na utulivu.

Alitoa mwito kwa wananchi wote na vyama vya siasa, kuheshimu sheria za nchi na kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo katika kuhakikisha usalama wa raia na mali zake unaendelea kuimarika.

Viongozi Watatu wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) Watiwa mbaroni Mkoani Dodoma

0
0

JESHI la Polisi mkoani Dodoma linawashikilia viongozi watatu wa Baraza la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bavicha) Taifa, kwa uchochezi na kuikashifu serikali.

Pia viongozi hao wanadaiwa kuvaa fulana zenye maandishi demokrasia imenyongwa, huku nyingine zikiandikwa dikteta uchwara.

Wanaoshikiliwa ni pamoja na Mwenyekiti wa Bavicha- Taifa, Patrobas Katambi, Katibu wa Bavicha-Taifa, Julius Mwita na Mwenyekiti wa Bavicha mkoani Mbeya, George Tito.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa alisema watuhumiwa hao watashikiliwa mpaka Jumatatu watakapofikishwa mahakamani.

“Hawatadhaminiwa mpaka Jumatatu, watakapofikishwa mahakamani,” alisema.

Kamanda Mambosasa alisema kitendo cha viongozi hao kuvaa fulana inayosema demokrasia imenyongwa, inamaanisha serikali inanyonga demokrasia, jambo ambalo ni la uchochezi.

Akizungumza na waandishi wa habari kuelezea tukio hilo Mjumbe wa Baraza Kuu la Chadema-Taifa, Joseph Kasambala alidai walikuwa katika ziara katika baadhi ya mikoa, wakianzia mkoani Mara katika Kijiji cha Mwitongo, Mwanza kabla hawajafika Dodoma juzi saa 8:00 mchana.

Alisema jana walikusudia kukutana na vyombo vya habari mjini Dodoma kuelezea hatua iliyofikiwa katika mpango wao wa Bavicha – Taifa kushirikiana na Jeshi la Polisi mkoani Dodoma, kuzuia wanachama wa CCM kufanya Mkutano Mkuu wa Taifa, Julai 23 mwaka huu.

Alidai wakiwa katika baa ya Cape Town, usiku aliwaacha wenzake na kwenda kukutana na jamaa yake mwingine na baadaye alipata taarifa za wenzake kukamatwa na polisi.

Kwa mujibu wa madai ya Kasambala, kilichomsikitisha ni kukataliwa kuonana nao alipofika kwenye kituo kikuu cha polisi jana asubuhi ambapo alitakiwa kwanza akaonane na viongozi wa Polisi wa wilaya na mkoa (OCD, RPC).

Kasambala alidai taarifa alizopatiwa kwenye kituo hicho cha polisi, zilieleza kuwa kosa wanalotuhumiwa kufanya ni kukashifu serikali, kwa kuvaa fulana yenye maandishi ‘Dikteta Uchwara’, tuhuma alizodai kuwa si za kweli.

Alionesha fulana aliyokuwa amevaa, yenye rangi nyeusi na maandiko meupe yanayosema, ‘Mwl. Nyerere: Demokrasia inanyongwa’ upande wa mbele ikiwa na maandishi ‘haki na amani’.

Alidai kuwa ziara yao inajumuisha viongozi sita wa Bavicha, akiwemo yeye, watatu waliokamatwa ambao ni Katibu Mwenezi wa Bavicha – Taifa, Edward Simbeye na Katibu wa Bavichamkoani Temeke, Hilda Newton.

Kasambala alidai kuwa baada ya kikao hicho, wangerejea Dar es Salaam, ili kukamilisha mikakati hiyo akisema ingawa wanafahamu kuwa hawana mamlaka ya kuzuia mkutano huo wa CCM, lakini wanao wajibu wa kushirikiana na polisi kama raia wema, kuhakikisha maagizo ya serikali yanazingatiwa.

Hivi karibuni, viongozi wa BAVICHA wakiwa jijini Dar es Salaam, walitangaza msimamo wao wa kuzuia mkutano huo kwa kutumia wanachama wake wapatao 4,000.

Makamu Mwenyekiti wa Bavicha, Patrick ole Sosopi, alidai kuwa vijana hao watatoka sehemu mbalimbali ili kuzuia mkutano huo wa CCM ili kusaidia Jeshi la Polisi kutekeleza amri yake ya kuzuia mikutano ya kisiasa hadi 2020.

Mtatiro Amtaka Profesa Lipumba Apumzike Uongozi......Asema CUF Inahitaji Mwenyekiti Mwingine , Adai Hana Mpango Wa Kugombea Uenyekiti

0
0
ALIYEKUWA Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara), Julius Mtatiro amesema hana mpango wa kugombea nafasi ya Uenyekiti wa chama hicho, licha ya kuwepo kwa msukumo mkubwa wa kumtaka agombee.

Katika taarifa yake aliyoitoa jana kwa vyombo vya habari, Mtatiro alisema kwa kipindi kirefu amekuwa akipata msukumo kutoka kwa viongozi wa chama hicho ngazi ya wilaya, wabunge, wafuasi na makada wa chama hicho kumtaka ashiriki katika kinyang’anyiro cha kugombea nafasi ya uenyekiti.

“Katika kipindi chote cha misukumo hiyo nimekuwa nikiwajibu wahusika wote kuwa “sina nia ya kuchukua uongozi wa juu wa chama” kwa sababu bado nahitaji muda wa kujiimarisha,” alisema Mtatiro katika taarifa yake.

Alisema hata aliposhauri kuwa Mwenyekiti wa zamani wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba anapaswa kupumzika wapo walioona kuwa anatumia nafasi hiyo kuutaka uenyekiti wa CUF jambo ambalo alisema si kweli.

Aidha, Mtatiro alisisitiza kuwa hajawahi kuwa na nia ya kuutaka uenyekiti wa CUF lakini hadi sasa msimamo wake ni kuwa haungi mkono Profesa Lipumba kurudi katika nafasi yake kwa sababu siasa za sasa zinahitaji viongozi wapya na wanaoweza kutazama mambo kisasa kwa mahitaji ya kizazi kipya.

“... Na kwa sababu Profesa Lipumba anayo heshima kubwa kwa CUF na watanzania, ni muhimu zaidi alinde heshima yake na abaki kuwa mshauri mkuu wa chama. CUF ya sasa inahitaji mwenyekiti imara anayeweza kukisimamia chama na kikajijenga lakini pia mwenye uwezo na ushawishi wa kufanya siasa za ushirikiano na haki,” ilieleza taarifa hiyo.

Hata hivyo, Mtatiro alisema anawatakia kila la heri wanachama wa CUF ili waweze kuchagua mwenyekiti mzuri kwa ajili ya kukiendeleza chama hicho, na kusisitiza kuwa jukumu lake litaendelea kukisaidia chama katika masuala mbalimbali ya kiushauri.

Wanawake walia Magufuli ‘kuwabania’ katika uteuzi

0
0
Mashirika yanayotetea haki za wanawake na usawa wa kijinsi nchini yamesema uteuzi wa nafasi muhimu za uongozi serikalini unaofanywa na Rais John Magufuli, hauzingatii hali halisi ya uwakilishi wa kijinsia. 

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam kwa niaba ya mashirika hayo, Mkurugenzi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Lilian Liundi alisema licha ya kupiga kelele tangu uteuzi wa Baraza la Mawaziri kuwa haukuzingatia usawa huo, bado hali inaonekana kuwa tete kwa upande wa wanawake. 

Alisema katika baraza hilo, kati ya mawaziri 19, wanne pekee ndiyo wanawake sawa na asilimia 21.1 ya mawaziri wote ikilinganishwa na uteuzi wa baraza la Serikali ya Awamu ya Nne ambalo lilikuwa na mawaziri wanawake 10 sawa na asilimia 33.3. 

Alisema manaibu waziri kati ya 16 waliopo, wanawake ni watano sawa na asilimia 31.25. 

“Ukiangalia upande wa makatibu wakuu, walioteuliwa ni 29 kati ya hao, wanaume ni 26 sawa na asilimia 89.7 huku wanawake wakipungua kutoka watano sawa na asilimia 21.7 ya mwaka 2014 hadi kufikia watatu sawa na asilimia 10.3 kwa sasa,” alisema Liundi. 

Alisema uteuzi wa wanawake katika nafasi hizo umepungua kwa asilimia 10. Katika nafasi ya wakuu wa mikoa, Liundi alisema idadi ya wanawake imeshuka zaidi, kati ya wakuu wa mikoa 26 Tanzania Bara, 21 ni wanaume sawa na asilimia 80 na wanawake ni watano sawa na asilimia mbili.

Kadhalika, alisema idadi ya wakuu wa wilaya imezidi kuporomoka ikilinganishwa na ya Februari mwaka jana ambako wanawake walikuwa asilimia 35.07:“Kwa maana nyingine, hapa uteuzi umepungua kwa asilimia saba.” 

Liundi alisema mikoa mitatu ya Simiyu, Songwe na Singida haina wawakilishi wanawake kwa nafasi ya ukuu wa wilaya. 

“Hii iko hata kwenye nafasi za makatibu tawala wa mikoa na wilaya na wakurugenzi wa halmashauri, hatuoni idadi ya wanawake ikiongezeka na badala yake inashuka,” alisema. 

Mwakilishi wa Taasisi ya Women Fund Tanzania (WFT), Dk Dinna Mbaga alisema Tanzania ni kati ya mataifa duniani yaliyoridhia na kusaini mikataba mbalimbali ya kimataifa na kikanda inayoweka misingi ya usawa kwa binadamu ikiwamo ushiriki katika ngazi zote za uamuzi, lakini haitekelezi mikataba hiyo kwa ridhaa mpaka isukumwe na asasi za kiraia jambo linaloleta ukakasi. 

Alisema miongoni mwa mikataba hiyo ni Tamko la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu (UDHR: 1948), Mkataba wa Kimataifa wa Kutokomeza aina zote za Ubaguzi dhidi ya Wanawake (CEDAW: 1979), Mpango kazi wa Beijing (1995), Mkataba wa Ziada wa Maputo na Mkataba wa Nyongeza wa Jinsia na Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC). 

Mwakilishi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), Gladness Munuo alisema Tanzania kupitia Dira ya Maendeleo ya 2025, imetambua kuwa mojawapo ya vichocheo vya ukuaji wa uchumi ni pamoja na kuwa na jamii yenye maono ya kimaendeleo na utamaduni wezeshi kwa wanawake na makundi mengine.

Lowassa afunguka kuhusu hali ya Siasa nchini, awapa Chadema ‘ukweli mchungu’

0
0

Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amewataka viongozi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutokatishwa tamaa na hali ya kisiasa nchini hususan marufuku za mikutano yao ya kisiasa pamoja na misukosuko mingine wanayopitia.

Lowassa ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, ameyasema hayo jana jijini Arusha alipokutana na Mameya na Wenyeviti wa Halmashauri zinazoongozwa na Chama hicho. 

Aliwataka wasiogope bali washikamane zaidi na kutambua ukweli kuwa hakuna Serikali yoyote duniani inayovipenda vyama vya upinzani.

Alisema kuwa Chama hicho kinatakiwa kujikita katika kushikamana na wananchi zaidi kwani uchaguzi wa mwaka jana ulionesha dhahiri kuwa wana imani na vyama vya upinzani na hadi sasa bado wananchi wana imani kubwa nao.

“Kuna uanaharakati na kuna siasa. Chama chetu cha Chadema ni hodari sana, tume-graduate. Tumevuka ngazi ya uanaharakati. Uanaharakati ni mzuri lakini unafika mahali unavuka ngazi katika kitu kingine ambacho ni chama cha siasa,” alisema.

“Chama cha siasa kazi yake ni kukamata dola. Hakuna kitu kingine duniani. Kwahiyo mnapokaa hapa mnajipanga kukamata dola na sio kitu kingine. Maandamano ni process tu, na sisi tumekaa hapa kutafuta namna ya kukamata dola, wanataka hawataki wanajua hilo. 

"Na wenyewe watakazana kuzuia tusikamate dola. Mliona walivyotufanyia kwenye uchaguzi, kwa gharama yoyote. Na sisi kwa gharama yoyote tutataka tuwanyang’anye dola na ndio tunakuwa chama cha siasa,” aliongeza.

Alisema kuwa CCM wanahofu kwakuwa bado wanakumbuka walichokipata wakati wa uchaguzi mkuu uliopita na akawataka Chadema kutofanya kazi kwa mazoea bali kukijenga chama kuanzia ngazi za mashina na matawi.

Katika hatua nyingine, Lowassa aliwataka Chadema pamoja na vyama vingine vya upinzani kulinda Ukawa kwani ndio chanzo kikuu cha mafanikio yao. Alisema wanapotofautiana wakae chini na kutafuta ufumbuzi.

“Ndugu zangu tulinde umoja wetu na tuhakikishe kuwa Ukawa inaendelea kuwapo hasa. Umoja wetu ndio nguzo kubwa na tutumie busara kukosoana. Tunapokosea tuache maneno ya mitaani. Tuwalinde viongozi wetu,” alisema.

Mwanasiasa huyo mkongwe alitoa wito kwa viongozi hao wa halmashauri kuhakikisha wanafanya kazi nzuri na kuwaletea maendeleo wananchi ili wasione ‘bora CCM’. 

Aliwataka kuhakikisha hawaangalii maslahi binafsi bali maslahi ya wananchi na kujieupusha na migogoro na viongozi wa CCM watakaotaka kuwakwamisha katika shughuli zao.

Riwaya: Mwanafunzi Mchawi (A Wizard Student) - Sehemu ya 12

0
0

 Mtunzi: Enea Faidy

....DORICE alimtazama malkia yule kwa woga huku fimbo ile ya dhahabu ikiwa kifuani mwake. Alihisi kifo chake kipo njiani lakini akajipa moyo wa imani kuwa hawezi kufa kwani hakutenda kosa lolote. Malkia Yule alicheka kicheko kikali cha kutisha.

"Dorice wewe ni mchawi sio?" Alisema Malkia yule huku akiwa na sura ya kutisha sana.
"Mimi sio mchawi!" Alijibu Dorice kwa kutetemeka.
"Mbona ulipovamiwa na chatu pale njiani uliongea maneno ya kichawi?"

"Ndio niliyaongea lakini mimi so mchawi, maneno hayo nilifundishwa na babu yangu ambaye ni mganga!" Dorice alishikwa na woga kupita kiasi.
"Hahah Dorice... Kuwa mkweli?"
"Kweli kabisa.. Mimi si mchawi.. Tafadhali naomba mniruhusu niende!" Alisema Dorice huku akilia.
"Unaenda wapi?"
"Naenda Singida kwa babu yangu!"

Aliomba Dorice akiwa amepiga magoti huku akilia kwa hofu.
"Huwezi kwenda Dorice... Sahau kuhusu kuondoka hapa!" Alisema malkia yule kisha akamwamrisha mlinzi wake amwondoe pale Dorice ampeleke sehemu nyingine.
Mlinzi alitii agizo la malkia akamtoa Dorice pale na kumpeleka eneo lingine.

Kilikuwa kama chumba kidogo chenye mwanga hafifu lakini kilikuwa na mapambo mengi sana ya dhahabu. Kilipendeza sana na kilivutia macho kupita kiasi, Dorice alibaki anashangaa.Aliingizwa chumbani mle bila kuambiwa kitu chochote na mlango ukafungwa. Akabaki peke yake.

Hofu ilimzidia sana alitetemeka kama MTU aliyekumbwa na baridi Kali sana, hakupata fursa ya kutazama kitu chochote ndani ya chumba kile akabaki ameinama huku akilia. Alijuta kutoroka shule kwaajili ya Doreen, aliona heri angebaki tu kuliko kuchukuliwa na viumbe wale wa ajabu.

Ghafla akiwa katika dimbwi zito la mawazo alishtuliwa na sauti nzito ya kiume ikimwita jina lake."Dorice" Dorice alishtuka sana kwani alipoingizwa mle hakukuwa na mtu yeyote wala hakusikia mlango ukifunguliwa.Aliinua kichwa na kumtazama aliyemwita.

"Usiogope Dorice.. Naitwa Mansoor, ni mtoto wa Malkia.." Alijitambulisha mwanaume Huyo mwenye sura nzuri ajabu, alinukia marashi mazuri sana yasioisha hamu kuyanusa. Dorice alishangazwa na uzuri wa kiumbe yule mwenye umbo tofauti na viumbe wengine aliowaona kwenye eneo lile. Kwa haraka alimkadiria kuwa na umri wa miaka kama 21 au 22.

"Dorice! Nimeshangazwa sana na uzuri wako uliojaaliwa.. Ama kweli umeumbika! Karibu kwenye himaya yetu!" Alisema kijana yule aliyejitambulisha kwa jina la Mansoor huku akitabasamu na kumpa mkono Dorice. Dorice alibaki ameduwaa kwa mshangao.

Mnyika ajibu kuhusu taarifa za kumkataa Lowassa, Kuhama Chadema

0
0
Baada ya kuenea kwa uvumi kuwa Naibu Katiba Mkuu wa Chadema, John Mnyika anataka kuachana na chama hicho, kiongozi huyo ameibuka na kukanusha akisema: “Hakuna kitu kama hicho na wala sina mpango wa kuhama.” 

Mnyika alisema hayo jana alipopigiwa simu ili azungumzie taarifa hizo. Mbunge huyo wa Kibamba alisisitiza kwamba huo ni uzushi. 

Habari za kujiuzulu kwa Mnyika zilianza kusambaa katika vyombo vya habari kwa mara ya kwanza mwaka 2013 baada ya aliyekuwa naibu katibu mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe kufukuzwa uanachama. 

Wakati huo, uvumi ulienea kwenye mitando kwamba amejivua nyadhifa zake zote na kwamba ameshakabidhi barua yake kwa katibu mkuu wakati huo, Dk Willibrod Slaa. 

Habari hizo zilijirudia mara baada ya Dk Slaa kutangaza kujivua nyadhifa zake zote ndani ya chama hicho huku akipinga hatua yake ya kumtangaza Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuwa mgombea wake wa nafasi ya urais.

Licha ya kushindwa kujitokeza hadharani kukanusha wala kuthibitisha tetesi hizo, Mnyika alionekana kuendelea na shughuli zake za kisiasa kama kawaida.

Uvumi wa tatu uliibuka mwishoni mwa wiki iliyopita safari hii ilidaiwa kueleza msimamo wake kuhusu Lowassa kupitishwa na Chadema na kisha Ukawa kuwania urais ikidaiwa kwamba anataka kiongozi huyo ahojiwe na kuchukuliwa hatua kutokana na ushiriki wake katika kashfa ya Richmond.

Habari hiyo iliyoibua hisia za wengi ilimnukuu Mnyika akisema: “Msimamo wangu haujabadilika kama ambavyo niliwahi kusema nikiwa mkurugenzi wa vijana wa Chadema tarehe 25 Februari 2008 na kipindi chote nikiwa Mbunge wa Ubungo…. Hivyo nategemea kuanzishwa kwa Mahakama ya Mafisadi Lowassa ndiye atakuwa wa kwanza. Siwezi kusaliti msimamo wangu bora nipoteze ubunge wangu.” 

Katika mwendelezo wake, baadaye uvumi mwingine uliibuka kwamba baadhi ya viongozi wa chama hicho walionekana nyumbani kwa Mnyika wakimsihi asichukue uamuzi huo. 

Hata hivyo, hakuna kiongozi yeyote wa Chadema aliyewahi kuzungumzia suala hilo kabla ya hivi karibuni, Ofisa Habari Mwandamizi wa Chadema, Tumaini Makene kutoa taarifa ya kukanusha akisema huo ni mradi wa kutengeneza uongo unaofadhiliwa na watu kwa ajili ya kukisumbua chama na Watanzania akisema wakati habari hizo zinaenezwa, Mnyika alikuwa akifanya shughuli za chama. 

India yaipatia Tanzania dola milioni 500 za Kimarekani kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo

0
0
India imeipatia Tanzania dola za Kimarekani milioni 500 kwa ajili ya miradi ya maendeleo ili kukuza ushirikiano wa kiuchumi baina nchi hizi mbili.

Hayo yamesemwa leo  na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli katika dhifa ya kitaifa aliyomwandalia mgeni wake , Waziri Mkuu wa India, Mheshimiwa Narendra Modi,Ikulu jijini Dar es Salaam.

“Tunaishukuru India ambayo imeonyesha utayari wa kushirikiana nasi kiuchumi katika kilimo, TEHAMA, maji, Elimu, Afya na Ulinzi,” amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli pia amesema ushirikiano wetu na India utatoa fursa kwa Tanzania kutimiza azma yake ya kuwa na uchumi wa viwanda kwani katika ziara hii Waziri Mkuu ameambatana na wafanyabiashara takriban 50 ambao wanaangalia fursa za kibiashara hapa nchini.

“India ni mdau wetu mkubwa wa  kibiashara  na uhusiano huu umekuwa ukikua kwani mauzo ya bidhaa za Tanzania nchini India yameongezaka toka thamani ya  dola za kimarekani milioni 187 mwaka 2005 hadi dola bilioni 1.29 mwaka 2015,”alisema Rais Magufuli.

Aidha, Rais Magufuli amesema kuwa India itatoa fedha kwa nchi ya Tanzania kwa ajili ya kilimo cha Dengu ambayo ni fursa ya ajira kwa watanzania na kuinua kipato cha wananchi.

Rais Magufuli ameeleza kufurahishwa kwake na miradi ya India ikiwemo mradi unaojulikana kama Making India, mradi ambao unatumia malighafi zinazopatikana nchini na kutumia nguvu kazi ya nchini ambao utapunguza tatizo  la ajira katika Taifa la Tanzania.

Amebainisha kuwa India iko tayari kushirikiana na Tanzania kwenye miradi ya gesi ikizingatiwa kuwa aina mbali mbali za gesi zinazidi kugunduliwa hapa nchini. Katika suala la gesi India iko tayari kutoa utaalamu na wataalamu kwa ajili miradi ya gesi.

Kwa upande wake Waziri Mkuu wa India , Mhe. Narendra Modi ameishukuru Tanzania kwa ukarimu alioupata hapa nchini na akaahidi kuendeleza ushirikiano wa kibiashara baina ya nchi hizi mbili.
 
Amesema India italeta watu wake, utaalaamu na teknolojia yake kwa Tanzania, jambo ambalo litaongeza ushirikiano wa kiuchuni kati India na Tanzania.

Waziri Mkuu huyo amemaliza ziara yake ya kiserikali  ya siku mbili nchini na kuondoka kuendelea na ziara katika nchi nyingine za Ukanda wa Afrika Mashariki.

India na Tanzania zasaini mikataba ya miradi ya maendeleo. 

0
0

Serikali ya India na Tanzania zimesaini mikataba ya miradi ya maendeleo katika sekta za maji, kilimo, viwanda, teknolojia ya habari na mawasiliano na afya katika kuimarisha mahusiano ya nchi hizo mbili ili kusaidia wananchi wake.

Mikataba hiyo imesainiwa leo, wakati Waziri Mkuu wa India Mhe. Narendra Modi alipokuakifanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam.

Mikataba wa kwanza uliosainiwa inahusisha mradi wa kusambaza maji katika mikoa ya Pwani na Dar es Salaam.

Aidha, mkataba wa pili unahusisha mradi wa kusambaza maji Zanzibar ambao unatarajiwa kugharimu dola  za kimarekani milioni 92 ambapo mradi huo unatarajiwa kufikia miji 17 nchini na mkataba mwingine utahusisha mafunzo ya ufundi yatakayosaidia kuzalisha wataalamu mbalimbali.

“Lengo letu ni kusaidiana  na kuimarisha mahusianao yetu katika kukuza uchumi na kutengeneza fursa mpya za ajira kwa wananchi wetu” alisema Waziri Modi.

Waziri Modi aliongeza kuwa Serikali ya India itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika masuala mbalimbali ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kuongeza wigo wa biashara na hatimaye kukuza uchumi wa nchi hizo.

Kwa upande wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli alisema Serikali India imekua na ushirikiano mzuri na Tanzania hasa katika masuala ya maendeleo ambapo imeweza kuwekeza nchini kiasi shilingi za Kimarekani dola bilioni 2.4 na kuzalisha  ajira 54,176.

Baadhi ya misaada iliyotolewa na Serikali ya India ni pamoja na  mashine ya vipimo vya ugonjwa wa kansa katika hospitali ya Bugando, itakayosaidia wakazi wa kanda ya ziwa na nchi nzima kwa ujumla pamoja na kuongeza na kuimarisha ushirikiano kati ya Shirika la viwanda vidogo vigodo la India kushirikiana na Tanzania katika kukuza viwanda vidogo na vya kati nchini.

Katika masuala ya teknolojia ya habari na mawasiliano, Serikali hiyo imeahidi kuleta wataalamu wao nchini Tanzania kwa lengo la kutengeneza program mbalimbali ili kuisaidia Tanzania katika masuala ya ulinzi wa mitandao pamoja na kutengeneza namna bora za ukusanyaji wa mapato ya nchi.

Katika masuala ya viwanda, Serikali ya India imeahidi kuanzisha viwanda vya kutengeneza dawa za binadamu  zitakazotibu   magonjwa mbalimbali ikiwemo malaria, figo na kisukari, ikiwa ni pamoja na kutengeneza vifaa tiba vitakavyotumika katika hospitali mbalimbali nchini kwa lengo la kupunguza gharama ya kununua vifaa hivyo nje ya nchi.

Aidha, Rais Magufuli alisema kuwa nchi ya India ina uhitaji mkubwa wa mazao ya kilimo hasa jamii ya kunde hivyo akawataka wakulima kutumia fursa hiyo kuzalisha mazao hayo kwa wingi.

“India inauhitaji wa tani 200 za mazao jamii ya kunde, wakulima mnatakiwa kuzalisha mazao hayo kwa wingi kwa vile tayari kuna soko la uhakika, na tutahakikisha madalali hawatakuwepo ili mkulima asikandamizwe” alisema Rais Magufuli.

Katika sekta ya uwekezaji nchini, India ni nchi ya tatu kwa uwekezaji Tanzania ikifuatiwa na Uingereza pamoja na China.
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live




Latest Images