Quantcast
Channel: MPEKUZI
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live

Bwawa Nyumba ya Mungu Lafungwa kwa Miezi 12

0
0
SERIKALI za mikoa ya Kilimanjaro na Manyara zimelifunga Bwawa la Nyumba ya Mungu kwa kipindi cha mwaka mmoja ili kuepusha kutoweka kwa viumbe hai wakiwamo samaki kutokana na kushamiri kwa uvuvi haramu.

Aidha, wakuu wa wilaya za Moshi, Mwanga na Simanjiro wametakiwa kusimamia maamuzi hayo na kuchukua hatua kali za kisheria kwa watakaokaidi agizo hilo.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Said Mecky Sadiki alisema hayo wakati wa hafla maalumu ya kuwaapisha wakuu wapya wa wilaya mkoani Kilimanjaro iliyofanyika mjini Moshi, juzi.

Alisema uamuzi huo ulifikiwa katika kikao cha ujirani mwema baina ya mikoa hiyo kupitia wilaya tatu zinazolizunguka bwawa hilo na kwamba utekelezaji wa agizo hilo umeanza rasmi Julai Mosi mwaka huu.

“Hali ya uvuvi haramu katika Bwawa la Nyumba ya Mungu ni mbaya sana, mazingira yameharibiwa, kuna athari nyingi zinajitokeza ikiwamo ya kupungua kwa maji katika bwawa hilo na hii huenda ikaathiri uzalishaji umeme na kutoweka kwa viumbe hai....kama serikali hatuwezi kuvumilia tena,” alisema Sadiki.

Pamoja na bwawa hilo, Sadiki alitaka wakuu wa wilaya kusimamia agizo la Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC), kupiga marufuku misumeno ya mnyororo, kwani imebaini ni adui mkubwa wa misitu.

Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa aliwakabidhi wakuu hao wa wilaya migogoro mikubwa mitano iliyopo katika hatua mbalimbali za utatuzi wake kupitia viongozi waliowatangulia na kutaka kufuata sheria katika kuishughulikia.

Miongoni mwa migogoro aliyoitaja ni unaohusisha jamii ya wafugaji wanaozunguka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) na kampuni inayohudumia uwanja huo ya KADCO kuhusu umiliki wa eneo la ardhi.

Mgogoro mwingine ni wananchi wa wilaya ya Longido mkoani Arusha na mwekezaji wa eneo la utalii la Ndarakwai uliowahi kusababisha kuchomwa moto kwa eneo hilo.

Maghembe: Tanzania Haitegemei Kenya Kupanga Kodi Zake

0
0
Wakati Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe amesema Tanzania haitegemei Kenya kupanga kodi kwa maendeleo ya wananchi, amebainisha kuwa Serikali inafuatilia taarifa kuwa baadhi ya mawakala wa utalii nchini, wanafungua akaunti nchini humo kukwepa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT). 

Profesa Maghembe alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki kufuatia malalamiko ya mawakala wa Utalii wanaodai hatua ya Serikali kutoza VAT kwenye utalii kutaathiri sekta hiyo.

Mawakala hao wamekaririwa na vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi, wakidai watalii wengi wamesitisha safari zao na wengi wameamua kwenda Kenya kwa vile nchi hiyo imeondoa VAT.

Taarifa hizo zilidai hatua hiyo ya Serikali imesababisha watalii 8,000 kusitisha safari zao na kufanya Tanzania kupoteza mapato ya Sh13 bilioni. 

Mtendaji Mkuu wa chama cha mawakala wa Utalii Tanzania (Tato), Cyril Arko alisema wanachama wao walishapokea maombi ya safari (bookings) mwaka mzima nyuma na wengine kulipwa kabisa, hivyo ni vigumu kurudi kumwambia mteja kuwa kuna mabadiliko, ndio sababu wakaenda Kenya. 

Arko alisema watalii wameamua kwenda Kenya kwa sababu nyumbu ni wale wale wanaotoka Serengeti na kuingia Masai Mara, Kenya, lakini faida ya Kenya ni kwamba hakuna kodi ya VAT. 

Kauli ya Profesa Maghembe
Akijibu malalamiko hayo, Waziri Maghembe alisema Tanzania si koloni la Kenya, kwamba kila mipango yake ya maendeleo itegemee taifa hilo. 

“Kenya siyo sehemu ya Tanzania na sisi (Tanzania) si koloni la Kenya. Kenya ni nchi tofauti, Uganda ni nchi tofauti, Uingereza  ni nchi tofauti,” alisema Profesa Maghembe na kuongeza;“Hizi ni kodi ndani ya Tanzania. Kenya ina mazingira tofauti kabisa na Tanzania. Hatuwezi kupanga kodi kwa maendeleo ya nchi yetu tukiwatazama wao,” alisema. 

Kwa mujibu wa Profesa Maghembe, katika kipindi cha miaka minne mfululizo, idadi ya watalii wanaotembelea Kenya imeendelea kupungua kutoka milioni mbili hadi milioni 1.3 mwaka jana.

“Na katika kipindi hicho huku kwetu wamekuwa wakiongezeka kutoka 800,000 hadi 1.2 milioni,” alisema. 

“Kule (Kenya) wana sababu  ya kuondoa VAT ili waone kama watavutia watalii wasiendelee kupungua. Hapa tulikuwa hatuna kodi hata siku moja. Hili jambo linapotoshwa sana,” alisisitiza. 

Profesa Maghembe alisema kinachoonekana ni kama kuna propaganda na mgomo baridi kutoka kwa baadhi ya mawakala wanaotaka kuihadaa dunia ili ione Tanzania kutoza VAT ni tatizo. 

Hata hivyo alisema Serikali inafuatilia kuangalia mwenendo kwa mwezi mmoja, miezi miwili ili kuona hali inakwendaje na baada ya kufanya tathmini ya kina, Serikali itatoa taarifa kwa umma. 

Alitolea mfano kuwa kuingia hifadhi ya Arusha ni Dola 45 za Marekani na Serikali ikitoza asilimia 18 ya VAT, ada ya kuingia katika hifadhi hiyo kwa siku inakuwa Dola 53.10, ambayo bado ni ndogo. 

“Sasa kusema kati ya Dola 45 na Dola 53 basi itafanya mtalii kutoka Marekani asije Tanzania hii ni dhana ngumu kuelewa. Serikali itafuatilia jambo hilo kwa kina,” alisema Waziri.

Mjamzito ajifungulia kwenye korido Baada ya Wauguzi Kugoma Kumsaidia

0
0
Mjamzito mmoja, Magreth Charles (22), mkazi wa Kata ya Lyabukande Wilaya ya Shinyanga amejifungulia kwenye korido la Kituo cha Afya cha Lyabukande baada ya kukosa huduma kutoka kwa wauguzi.

Mjamzito huyo alilazimika kujifungulia kwenye korido kutokana na wauguzi katika kituo hicho kugoma kutoa msaada wakidai wako kwenye mapumziko na kumtaka aende sehemu nyingine.

Mama mkwe wa mjamzito huyo, Rachel Mpanda alisema walifika kituoni hapo wakitokea kijiji cha Kizungu jirani na kituo hicho na walielezwa na mtu waliyemkuta kuwa wauguzi wako mapumzikoni, hivyo hakutakuwa na huduma yeyote.

“Baada ya muda kidogo tukiwa tunatafuta namna ya kwenda kituo kingine, mwari wangu alianza kusukuma mtoto, hivyo nikaamua kuomba msaada kwa wapitanjia ili wamsaidie ajifungue, alifanikiwa kujifungua mtoto wa kiume,” alisema Mpanda.

Diwani wa kata hiyo, Joseph Misiri alisema tukio la mwanamke huyo kujifungua kwenye korido si la kwanza na kwamba kuna mwanamke mwingine alikosa huduma hiyo na kusababisha mtoto kufariki dunia.

“Serikali haina budi kuwachukulia hatua wauguzi katika kituo hiki kwani wanasababisha kupoteza maisha ya watoto wachanga, mwishowe watasababisha kupoteza maisha kwa wajawazito kwa kukosa huduma ya matibabu,” alisema Misiri.

Mmoja wa wauguzi katika kituo hicho, Zulfa Mussa alisema kituo hicho kina watumishi watatu; muuguzi mmoja alikuwa amempeleka mgonjwa hospitali ya rufaa, daktari mfawidhi wa kituo, Kadela Mashaka alikuwa semina na yeye alikuwa zamu usiku, hivyo alitakiwa kupumika mchana huo.

“Kwa kawaida aliyekuwa zamu ya usiku anatakiwa kwenda kupumzika kujiandaa na zamu yake nyingine, hivyo niliondoka kituoni na kumwacha mtaalamu wa maabara,” alisema Zulfa.

Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Kiomoni Kibamba alipohojiwa alisema hana taarifa na kuahidi kufuatilia.

Waumini wa Kanisa la Ufufuo na Uzima Wahoji Kuhusu Afya ya Askofu Gwajima

0
0
Waumini wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, wamesali Jumapili ya tatu bila kuwapo kwa Askofu wao, Josephat Gwajima,lakini wameshtushwa na taarifa kuwa kiongozi huyo wa kiroho ni mgonjwa na anapata matibabu nje ya nchi. 

Waumini hao walisema wamekuwa wakisikia kuwa askofu wao anatafutwa na Jeshi la Polisi na juzi wamesikia kuwa anapata matibabu nje ya nchi wakati wao hawajatangaziwa rasmi kuhusu taarifa hizo. 

Juzi, Wakili wa Askofu Gwajima, Peter Kibatala aliileza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa mteja wake hakufika mahakamani kwa kuwa yuko nje ya nchi kwa ajili ya matibabu. 

Askofu Gwajima alitakiwa kufika mahakamani hapo anakokabiliwa na kesi ya kumtolea lugha chafu Askofu Mkuu Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo inayosikilizwa na Hakimu Mkazi, Cyprian Mkeha. 

Mbali na taarifa za kuumwa, pia Gwajima anatafutwa na Polisi baada ya kusambaa kwa sauti inayosikika kama yake ikitaka Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete afikishwe mahakamani kwa yote yaliyofanyika katika utawala wake. 

Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro alisema jana kuwa atalizungumzia suala hilo leo Jumatatu. 

Katika ibada ya jana, kama kawaida, Mchungaji Adriano Edward hakuwaeleza chochote waumini wa kanisa hilo kuhusu alipo Askofu Gwajima wala hali ya afya yake. 

Mchungaji Adriano alipotakiwa kuzungumzia suala la afya ya Gwajima, alisema kupitia msaidizi wake kuwa hawezi kuzungumza chochote na vyombo vya habari. 

Majambazi Yatikisa Moshi....Yaua Walinzi Wawili na Kupora Milioni 65

0
0
Wakati jeshi la polisi likisema linajiimarisha, vitendo vya ujambazi vinazidi kuitikisa nchi baada ya kundi la watu wasiojulikana kuvamia ofisi za Kampuni ya Ahsante Tours ya mjini Moshi, kuua walinzi wawili na kuiba Sh 65.5milioni. 

Tukio hilo limekuja siku chache baada ya watu wasiojulikana kuvunja duka la kubadilisha fedha la Chase Forex Bureau De Change la mjini Moshi na kuiba zaidi ya Sh120 milioni. 

Mbali na tukio hilo, Juni 12 mwaka huu, watu watano wakiwa na bunduki aina ya SMG, walivamia mji wa Magugu wilayani Babati mkoani Manyara na kupora Sh2.5 milioni. 

Tofauti na tukio hilo la Magugu, hivi karibuni Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam waliwaua watu watatu eneo la Masaki katika majibizano ya risasi na Polisi. 

Ukiachilia matukio hayo, taarifa kutoka mikoa mbalimbali nchini zinaonyesha uporaji wa fedha na mali kwa kutumia pikipiki maarufu kama bodaboda, unazidi kushika kasi maeneo mbalimbali. 

Wengi wa wanaolengwa na wahalifu hao ni wateja wanaotoka kuchukua pesa benki au wanaokwenda kuchukua fedha jambo ambalo limezua hofu kuwa huenda baadhi ya wafanyakazi wa benki wanashirikiana na wahalifu. 

Lakini, tishio kubwa zaidi la uhalifu linatokana na kuibuka kwa makundi ya kihalifu yanayokuwa yamejihami kwa silaha za kivita, yakiwamo mabomu ya kurushwa kwa mkono, yakichinja raia na kupora. 

Hivi karibuni, Polisi Jijini Dar es Salaam waliwaua watuhumiwa hatari wawili waliokuwa wamejihami kwa bunduki na mabomu, wanaotuhumiwa kuchinja watu nane Jijini Tanga na watatu Jijini Mwanza 

Hali hii ndio imemsukuma Rais John Pombe Magufuli, kuwaagiza polisi kuhakikisha ‘wanawanyang’anya’ majambazi silaha haraka kabla ya kuwadhuru polisi ama raia wasio na hatia. 

Uporaji Ahsante Tours
Tukio la mauaji ya walinzi wawili ofisi za Ahsante Tours, lilitokea usiku wa kuamkia jana, baada ya watu hao kuwazidi nguvu walinzi na kuwafunga kamba kisha kuwapiga kwa kitu butu kichwani. 

Kampuni hiyo inamilikiwa na mfanyabiashara Cathbert Swai na mkewe Stella Shangali, ambao pia wanamiliki hoteli ya kitalii ya Weruweru River Lodge iliyopo Mailisita, nje kidogo ya mji wa Moshi. 

Taarifa kutoka kwa baadhi ya wafanyakazi wa kampuni hiyo ambayo ni moja kati ya kampuni zinazoongoza kwa kupokea watalii wengi, zinadai huenda tukio hilo ni mpango wa ndani. 

 “Kuna maswali mengi tunajiuliza. Walijuaje kuna kiasi hicho kikubwa cha fedha kama taarifa hazikutoka miongoni mwetu?” alihoji mmoja wa wafanyakazi aliyeomba jina lake lisitajwe. 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Wilbroad Mutafungwa, alisema kati ya fedha zilizoibwa, kulikuwa na Dola  za Marekani (Sh50 milioni) na Sh15 milioni za Tanzania.

 Walinzi waliouawa wametajwa kuwa ni Omar Mohamed (48), mkazi wa Matindigani Pasua na Dominick Cheddy (41), mkazi wa Mailisita na wote ni wenyeji wa mkoa wa Tanga. 

Kamanda Mutafungwa alisema tukio hilo liligunduliwa saa 1.00 asubuhi na wasamaria wema waliotoa taarifa polisi, na uchunguzi wa awali umebaini watu hao walikata uzio wa ofisi hizo. 

“Baada ya kuingia ndani ya jengo hilo la ofisi walivunja ofisi ya meneja mkuu na baadaye ofisi ya mhasibu ndio wakaiba Dola 23,300 na pesa za Tanzania Sh15 milioni,”alisema Kamanda Mutafungwa. 

“Tunashuku kuwa huenda hao majambazi waliamua kuwaua hao walinzi baada ya hao walinzi kuwatambua. Bahati mbaya hawakuwa na silaha yoyote hata panga hawakuwa nalo,”alisisitiza. 

Kamanda Mutafungwa alisema Polisi inamshikilia mtu mmoja ambaye inaonekana alikuwepo wakati mauaji na uporaji huo ukifanyika lakini, majambazi hao hawakumdhuru sehemu yoyote. 

Hata hivyo, Kamanda Mutafungwa, aliwataka wafanyabiashara kupeleka pesa benki badala ya kuzihifadhi ndani au ofisini na kuwataka pia kuimarisha ulinzi ikiwamo kuweka CCCTV Camera. 

Alitoa wito kwa wananchi wenye taarifa za waliohusika na tukio hilo, kulisaidia Jeshi la Polisi kama ilivyotokea wiki moja iliyopita ambapo taarifa zao zilisaidia kuwatia mbaroni wahalifu mbalimbali 30.

UVCCM Yawapa Onyo Kali Vijana wa CHADEMA Walioandaliwa Kuvuruga Mkutano wa CCM Dodoma

0
0
Umoja wa Vijana CCM (UVCCM) umeingia katika mvutano mkubwa na Baraza la Vijana wa Chadema (BAVICHA) kuhusu Mkutano Mkuu Maalum wa chama hicho tawala uliopangwa kufanyika Julai 23 mwaka huu mjini Dodoma.

UVCCM wameionya BAVICHA kuhusu mpango wao wa kutaka kukusanyika mjini Dodoma siku hiyo kwa lengo la kuzuia mkutano huo kwa madai kuwa unakiuka amri halali ya polisi ya kupiga marufuku kufanyika kwa mikutano yote ya kisiasa nchini.

Onyo hiyo limetolewa na  Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamda Shaka ambaye aliwaambia waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuwa watawakabili kwa nguvu zote BAVICHA endapo wataamua kuendesha siasa zinazolenga kuvuruga amani na kuleta hofu katika jamii na kutishia maisha.

Alisema umoja huo hautaona shaka kutumia mbinu zilizotumiwa na wapiganaji wa Maumau miongo kadhaa iliyopita nchini Kenya.

“Hatutaona muhali kupita njia zilizotumiwa na wapiganaji wa Maumau wa Kenya ili kukihami chama, kulinda viongozi wake na kupigania hadhi na heshima yetu,” alisema Kaimu Katibu Mkuu huyo wa UVCCM.

CCM inatarajia kufanya mkutano mkuu maalum Julai 23 mwaka huu ambapo Rais John Magufuli atakabidhiwa rasmi uenyekiti wa chama hicho kutoka kwa mtangulizi wake, Dk. Jakaya Kikwete.

Shelukindo Kuzikwa Alhamis Jijini Arusha

0
0

MWILI wa Mbunge wa zamani wa Kilindi, Beatrice Shelukindo (CCM), unatarajiwa kuzikwa Alhamis wiki hii.

Taarifa iliyotolewa jana na kaka wa marehemu, Enock Madimilo, ilisema taratibu za mazishi zinaendelea kufanywa nyumbani kwa marehemu Dar as Salaam na Arusha.

“Tunaendelea na mipango ya mazishi hapa Arusha na nyumbani kwa marehemu, Ada Estate jijini Dar es Salaam.

“Mazishi yatafanyika hapa Arusha Alhamisi wii hii. Kwa hiyo, tunawaomba ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu, waje kumuaga mpendwa na kiongozi wao,” alisema Madimilo.

Shelukindo alifariki juzi usiku saa 2:30 akiwa nyumbani kwa mama yake mzazi, katika eneo la Olorien, jijini Arusha baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Mwili wa marehemu Beatrice uliondolewa nyumbani kwa mama yake huyo alipokuwa akiuguzwa usiku huo huo na kupelekwa Hospitali ya Mount Meru.

Kutokana na msiba huo, tayari waombolezaji mbalimbali wameendelea kufika nyumbani kwa mama wa marehemu kwa ajili ya kutoa pole.

Abiria 10 Wahofiwa kufa maji, 20 Wanusurika

0
0
ABIRIA 10 kati ya abiria 30 waliokuwa wakisafiri kwenye boti wakitokea Mitomoni, wilaya ya Songea Vijinini, mkoani Ruvuma kwenda mnadani katika wilaya hiyo wanahofiwa kufa maji baada ya boti hiyo kuzama kwenye Mto Ruvuma.

Habari zilizopatikana jana mjini hapa zilieza kuwa, boti hiyo ilikuwa imejaza abiria pamoja na mizigo iliyokuwa ikipekwa kwenye mnada wa hadhara ambao upo jirani na kijiji cha Mitomoni mpakani mwa Tanzania na Msumbiji.
 
Jitihada za  kumtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Zuberi Mwombeji, hazikufanikiwa baada ya kuelezwa kuwa alikuwa ameungana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Ruvuma kwenda kwenye eneo la tukio hilo.
 
Ofisa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Ruvuma, Hamis Kutiku, alisema Kamanda Mwombeji amekwenda kwenye eneo la tukio ili kujiridhisha ukweli wa tukio hilo.
 
Alisema taarifa kamili juu ya tukio hilo zitatolewa baada ya Kamati ya Ulinzi na Usalama kufika eneo la tukio na kurudi mjini  kwa ajili ya hatua zaidi kuchukuliwa.

RIWAYA: Mwanafunzi Mchawi ( A Wizard Student ) - Sehemu ya Tisa

0
0
Mtunzi: Enea Faidy


..Mwalimu John alipelekwa makuburini kwaajili ya mazishi ingawa yeye alijiona yuko hai. Dorice alikuwa njiani baada ya kutoroka shulen, na alipofika kwenye kijito kidogo alishtushwa na kishindo kikali.
 
Eddy alifikia hatua ya Mwisho kutaka kufanya mapenzi na Doreen lakini kabla ya kufanya hivyo aliachia yowe Kali.

SONGA NAYO UJUE KILICHOJIRI....
....VIJANA wanne wenye nguvu walinyanyua jeneza alililokuwamo Mwalimu John kisha taratibu walipiga hatua kuelekea kwenye nyumba yenye pembe NNE na kina kirefu kiasi aliyotengenezewa mwalimu John.

Sauti za vilio zilizidi kutia simanzi katika eneo lile LA makaburini. Nyimbo za huzuni zilitawala eneo hili huku kila mmoja akisikitika moyoni mwake.

Ndani ya jeneza hilo mwalimu John alikuwa akihangaika sana kuwaita vijana wale ili wasimzike lakini katu hakusikika. 

Alizidi kupiga kelele za kuomba msaada lakini ikabaki kuwa kazi bure. Sauti iliyojaa huzuni kuu ya mkewe Monalisa ilizidi kupenya vyema masikioni mwake, hali hii ilizidi kumtia simanzi mwalimu huyo ambaye sasa alikuwa amekata tamaa ya kuishi tena.

"Daah Doreen hafai" alijisemea mwalimu John huku machozi yakimtiririka kwa kasi kwani bado alikuwa haamini kama kweli anazikwa akiwa mzima.Vijana wale walilishusha jeneza lile lenye mapambo ya kupendeza ndani ya kaburi kisha wakatulia kidogo ili mchungaji atupie neno La mwisho.

Mchungaji alichukua udongo kidogo na kusogelea vyema kwenye shimo alilowekwa mwalimu John."Uliumbwa kwa mavumbi hakika utarudi mavumbini, Bwana alitoa Bwana ametwaa jina La Bwana lihimidiwe... " Mchungaji aliyasema maneno hayo kwa huzuni kisha akaumwaga kaburini udongo ule aliokuwa ameushika mkononi.

Mwalimu John aliyasikia vyema maneno hayo yaliyouchoma moyo wake kama mkuki wenye sumu. Hakika mwalimu John alikiri kuwa kweli duniani kuna watu na viatu, Doreen alikuwa kiatu chakavu kisichofaa kuvaliwa hata na kichaa.

Vijana walishika vyema sepetu zao ili waanze kutupa udongo kaburini na kumzika mwalimu John lakini kabla hawajaanza kutupa udongo, kilizuka kimbunga kikali cha ghafla kilichofanya watu wapoteane. Jeneza likafunuka ghafla mwalimu John akainuka kutoka kwenye jeneza.

Agizo La Kuzuia Uvutaji Wa Sigara Na Matumizi Ya Bidhaa Za Tumbaku Katika Maeneo Ya Umma.

0
0
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inampongeza Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kwa kupiga marufuku matumizi ya Shisha na uvutaji wa Sigara hadharani kama afua ya kupunguza madhara ya tumbaku na madawa ya kulevya katika jamii.

Uchunguzi wa kitalaam uliofanyika umebaini kuwa Shisha ina madhara kwa afya ya watumiaji hasa vijana na watoto. Watumiaji wa Shisha wanatumia kiwango kikubwa cha tumbaku kwa muda mfupi, hali inayoongeza madhara yatokanayo na tumbaku kama vile: – Saratani, Magonjwa ya Mapafu, Kibofu cha mkojo, Tezi dume, Koo, Mdomo na Kiywa, Ngozi, Ini, Ubongo.

Pia imebainika kwamba matumizi ya Shisha huambatana na kuongezewa dawa nyingine za kulevya na hivyo hufanya watumiaji wa Shisha kupata uraibu wa dawa za kulevya. Matumizi ya dawa hizo za kulevya ni kosa la jinai.

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inapenda kurejea na kusisitiza agizo lake la tarehe 12 Machi 2015 la kuzuia matumizi ya sigara na matumizi ya bidhaa za tumbaku katika maeneo ya umma

Inakumbushwa kwamba agizo hili limezingatia utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Bidhaa za Tumbaku, Sura ya 121 T.L 2002, ya Sheria za Tanzania kipengele cha 12 (1) ambacho kinakataza matumizi ya Tumbaku katika Maeneo ya Umma.

Madhumu ya Agizo hili ni kuilinda Jamii kwa ujumla kutokana na madhara yatokanayo na moshi wa sigara. Wizara inawakumbusha wananchi wanaotumia bidhaa za tumbaku kupunguza au kuacha kabisa matumizi ya tumbaku. Aidha, agizo hili linaijumuisha jamii yote katika kubaini madhara ya tumbaku na umuhimu wa kuzuia matumizi ya tumbaku katika maeneo ya kazi na maeneo yote ya umma.

Agizo hili linawahusu wananchi wote nchini wanaopata huduma katika maeneo ya umma kama ilivyotafsiriwa na sheria husika.

Matumizi ya tumbaku hayaruhusiwi katika maeneo yote ya umma. Maeneo haya yanajumuisha ofisi zote za Serikali na tasisi zake zote, watu binafsi, vyuo, vituo vya huduma za Afya zikiwemo Hospitali, vituo vya Afya na zahanati, vituo vya usafiri wa Anga, Mabasi, bandari na treni, sehemu za mikutano, mapumziko, bustani na fuko za maji,sherehe,michezo,masoko,maduka makubwa pamoja na sehemu za kuabudu.Na kwa mtu yeyote anayeendesha shughuli katika maeneo ya umma analazimika kutenga eneo maalum kwa ajili ya wavuta sigara.

Kwa kuwa Mhe. Waziri mwenye dhamana na masuala ya Afya nchini ameona hatari hii ya Uvutaji wa sigara na utumiaji wa bidhaa za tumbaku kwa afya ya Wananchi, kuanzia leo tarehe 4/7/2016 matumizi ya Shisha nchini yamepigwa marufuku kwa wote wanaojihusisha na matumizi hayo, na kwa wafanyabiashara wote wanaojihusisha na upatikanaji wa Shisha nchini

Hivyo basi, kwa agizo hili katika maeneo yote nchini ambako matumizi ya Shisha hufanyika ni marufuku matumizi hayo kuendelea kutumika.

Aidha vyombo vya Dola na mamlaka husika vinahimizwa kusimamia kwa ukamilifu katazo hili.

Dk. Kigwangalla ametoa taarifa hii kuhusu wanaosapoti mapenzi ya jinsia moja

0
0
]Ishu ya watu ambao wanashiriki mapenzi ya jinsia moja imekuwa kubwa kiasi kwamba viongozi mbalimbali wamekuwa wakizungumza katika maeneo mbalimbali ambayo wanapata nafasi ya kuzungumza na kukemea vitendo hivyo.

Naibu Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hamisi Kigwangalla ameendelea kusisitiza kuhusu vitendo hivyo na kueleza kuwa serikali haipo tayari kuona vitendo hivyo vinafanyika kwa wananchi wake lakini pia kuzitangazia mwisho wake taasisi ambazo zinafanya jitihada kutetea watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja.

Dk. Kigwangalla ametoa taarifa hiyo kupitia ukurasa wake wa Twitter ambapo aliposti video ambayo ikimwonyesha akikemea vitendo hivyo na kusema kuwa serikali itazifutia usajili mara moja taasisi zote ambazo zitabainika kupokea pesa kutoka mataifa ya nje ili kutetea mashoga.

Mahakama Yawataka Wabunge Halima Mdee na Mwita Waitara kuheshimu taratibu za kisheria

0
0
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, imetoa onyo kwa  Wabunge Halima Mdee (Kawe)  na Mwita Waitara (Ukonga) kwa kushindwa kufika mahakamani kusikiliza kesi inayowakabili dhidi ya  kumjeruhi Katibu Tawala wa jiji, Theresia Mbando.

Kesi hiyo imepangwa kusikilizwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shahidi na leo kesi hiyo ilipangwa kusikilizwa maelezo ya awali dhidi ya washtakiwa.

Upande wa Jamhuri ukiongozwa na Esterlia Wilson alidai kuwa kesi hiyo ilipangwa kusikilizwa maelezo ya awali lakini washtakiwa Mdee na Waitara hawapo mahakamani.

Utetezi ulidai kuwa Mdee ameshindwa kufika mahakamani kwa kuwa amesafiri kwenda nchini Canada na Waitara ni mgonjwa.

Hakimu alisema sababu zilizotolewa na upande wa utetezi hazina mashiko kisheria kwa kuwa wameshindwa kuwasilisha vielelezo vya kuithibitishia mahakama kwanini washtakiwa wameshindwa kufika kusikiliza kesi yao.

“Kama kweli mshtakiwa Waitara ni mgonjwa upande wa utetezi mlipaswa kuwasikilisha vyeti mahakamani na kuhusu mshtakiwa Mdee aliyesafiri kwa safari zake binafsi kwenda Canada, siyo sahihi tunapaswa tuheshimu hizi taratibu ili kila kitu kifanyike kwa haki ya pande zote” alisema Hakimu Shahidi.

Mbali na Mdee na Waitara, wengine ni, Mbunge wa Jimbo la Ubungo, Saed Kubenea , Diwani wa Kata ya Tabata Kimanga, Manase Njema , Diwani wa Kata ya Kimara, Ephrein Kinyafu na mfanyabiashara Rafii Juma.

Wengine waliounganishwa katika kesi hiyo ni, Diwani wa Kata ya Segerea Edwin Mwakatobe (31) na Mkazi wa Tabata Edwin Mwaipaja (40).

Katika kesi ya msingi, ilidaiwa kuwa  Februari 27, mwaka huu katika Ukumbi wa Karimjee, Wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam walimjeruhi Theresa Mbando  na kumsababishia maumivu mwilini mwake.

Washtakiwa hao walikana mashtaka hayo kwa nyakati tofauti na  upande wa Jamhuri  ulidai upelelezi wa kesi hiyo umekamilika, uliomba tarehe nyingine ya kuwasomea washtakiwa maelezo ya awali.

Hakimu alisema kesi hiyo itasikilizwa maelezo ya awali  Julai 27, mwaka huu, dhamana ya washtakiwa inaendelea.

Watu Wenye Ulemavu wa ngozi kuwafukuzisha Kazi Wakuu wa Wilaya , Mwanza

0
0
Mkuu wa mkoa wa Mwanza John Mongella, amewaapisha wakuu wapya wa Wilaya za Mkoa wa Mwanza na kuwapa vitendea kazi ikiwapo katiba ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania na Ilani ya Chama Tawala Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Mwaka 2015- 2020, kwaajili ya kwenda kutimiza wajibu wao wa kikatiba kwenye wilaya walizo pangiwa.

Akizungumza baada yakuwaapisha, Mhe. Mongella, amewataka waende wakasimamie shughuli za kuhimiza maendeleo, suala la ulinzi na usalama kwenye wilaya zao, huku akitilia mkazo ukomeshwaji wa mauwaji ya watu wenye ulemavu wa Ngozi albino pamoja na Vikongwe. Amesema, ikiwa jamii ya watu hao itapata madhara basi ni dhahiri Mkuu huyo wa Wilaya atakuwa ameshindwa kusimamia majukumu yake.

Mkuu huyo wa mkoa pia, amerudia kauli yake nakuwataka viongozi hao wapya watambue wanajukumu zito lililoko mbele yao, ikiwa ni pamoja na kukomesha Utumiaji wa dawa zakulevya.

Aidha ameonya uchezaji wa Pool na unywaji wa Pombe wakati wa saa kazi, huku akimsisitiza mkuu wa Wilaya ya Nyamagana kuhakikisha ifikapo Agosti mosi, suala la wafanyabiashara wanaofanya biashara kwenye maeneo ambayo hayaruhusiwi liwe limepatiwa ufumbuzi.

Mongella amesema, katika mkoa wa Mwanza, Hotel na Clabu, yeyote ile, iwe ya kawaida au ya Kitalii, ikibainika inafanya biashara ya Shisha, hawataivumilia na badala yake wataifutia Leseni ya biashara.

Walio apa mbele ya Mkuu wa Mkoa, ambao waliteuliwa na Mhe. Rais Tarehe 26, Juni, 2016 ni Emmanuel Enock Kipole, Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Estomin Francis Chang’a Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Hadija Rashid Nyembo Mkuu wa Wilaya ya Magu, wengine ni Juma Samwel Sweda Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Dkt. Leonard Moses Masale Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Mary Onesmo Tesha Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana na Mhandisi Mtemi Msafiri Simioni Mkuu wa Wilaya ya Kwimba.

Imetolewa na
Atley J. Kuni
Afisa habari na Mahusiano
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
MWANZA.
04, Julai, 2016.

Shahidi akwamisha Kesi ya IPTL dhidi ya Zitto Kabwe

0
0
Kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) ilifungua kesi ya madai ya fidia ya Sh. bilioni 500  Mahakama kuu, kanda ya Dar es Salaam dhidi ya Zitto Kabwe. 

IPTL pamoja na wadai wenzake waliiomba mahakama imwamuru Zitto kulipa fidia hiyo kwa madai ya kutoa kashfa dhidi yao kimaandishi

Kesi hiyo dhidi ya Zitto Kabwe na gazeti la Raia Mwema leo imeahirishwa na Mahakama Kuu ya Tanzania mpaka August 24 2016 baada ya mawakili wa IPTL kusema shahidi wao muhimu ameumwa ghafla hivyo hataweza kutoa ushahidi.

Katika kesi hiyo IPTL na mmiliki wake wanadai walipwe Tshs Bilioni mia tano kwa madai kwamba gazeti la Raia Mwema liliandika uongo dhidi ya IPTL kuhusu hela zilizoibiwa kwenye Escrow Akaunti.

PICHA: Watu 29 wapoteza maisha katika ajali ya mabasi ya City Boy, Rais Magufuli atuma salamu za rambirambi

0
0
Ajali mbaya imeyohusisha mabasi mawili ya kampuni ya City Boy imetokea katika kijiji cha Maweni wilaya ya Manyoni, Singida na kusababisha watu 29 kupoteza maisha papo hapo huku chanzo cha ajali kikitajwa kuwa ni mwendo kasi.

Mabasi hayo yenye namba za usajili T531 DCE na T247 DCD, moja lilikuwa likitokea Dar es Salaam kuelekea Kahama na lingine likitokea Kahama kuelekea Dar es Salaam.

Moja ya mashuhuda wa ajali hiyo amesema kuwa madereva wa mabasi yote walikuwa katika mwendo kasi na wakati ajali inatokea walikuwa wakisalimiana kwa kunyosheana mikono kisha basi moja kupoteza mwelekeo na kuingia upande wa basi lingine na ndipo yakakutana uso kwa uso na kusababisha ajali hiyo.

Kamanda wa Polisi Singida, Thobias Sedoyeka tayari amethibittisha kutokea ajali hiyo na uchunguzi zaidi unaendelea kufanyika.

Katika hatua nyingine Rais Magufuli ametuma salamu za rambirambi na kueleza kuwa amepokea taarifa hiyo kwa mshtuko na amesikitishwa na ajali hiyo ambayo imechukua maisha ya watanzania.

Maiti Yazuiliwa hospitali ya Muhimbili ikidaiwa fedha.

0
0

Hospitali ya Taifa Muhimbili imegoma kuruhusu mwili wa marehemu Bi Hilda Lukas miaka 30 aliyefariki dunia June 26 katika hospitali hiyo, akisumbuliwa na ugonjwa wa utumbo kutoboka huku ikidai lazima fedha yote wanayomdai marehemu ilipwe ambayo ni sawa na shilingi milioni moja na laki moja na nusu kwa mujibu wa ndugu wa familia kama gharama za kumuhudumia mgonjwa huyo.
 
Mama wa marehemu Bi Anna Zuaro na Bibi wa marehemu wameiomba serikali na wadau mbalimbali kuona namna wanavyoweza kuwasaidia kwani wao mpaka sasa hawana fedha za kuuondoa mwili wa mpendwa wao, huku gharama za kuuhifadhi mwili huo katika chumba cha kuhifadhi maiti zikizidi kuongezeka.
Maafisaa wa Muhimbili wanakiri marehemu Hilda Lukas alikuwa amelazwa katika wodi ya kibasira chumba namba 9 ingawa haikuwa rahisi kuzungumza na maafisa hao.
Uongozi wa mtaa wa Chang’ombe umesema umefanya juhudi nyingi tu zikiwemo za kuchangisha wananchi na wadau mablimbali lakini mpaka sasa bado hawajaweza kukamilisha kiasi hicho cha fedha kinachohitajika Muhimbili ambapo gharama za mochwari pekee mpka sasa ni shilingi 210,000.

Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Jumanne ya July 5

Mbunge wa Mwibara Kangi Lugola Aionya Jamhuri Kumsotesha Mahakamani

0
0
KANGI Lugala, Mbunge wa Mwibara ameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kutoa onyo kwa Jamhuri kwa kukwamisha kuwasomea maelezo ya awali katika kesi inayowakabili.

Lugola, Victor Mwambalaswa, Mbunge wa Lupa na Murad Sadiq, Mbunge wa Mvomero wanatuhumiwa kuomba rushwa ya Sh. 30 mil kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Gairo tarehe 15 Machi mwaka huu.

Lugola alitoa madai hayo jana mbele ya Thomas Simba, Hakimu Mkazi katika mahakama hiyo baada ya wakili wa serikali Denis Lekayo kueleza kuwa, waendesha mashtaka wa kesi hiyo hawapo.

Wakili Lekayo alidai kuwa, shauri hilo liliitishwa kwa ajili maelezo ya awali lakini waendesha mashtaka hawakupo.

Kutokana na maelezo hayo Lugola aliiomba mahakama ikemee tabia hiyo ya kuahirishwa kesi mara kwa mara.

Lugola alisema kitendo hicho kinawanyima haki yao ya msingi ya kufanya shughuli zao za Bunge.

Baada ya Lugola kueleza hayo, wakili wa Serikali, Denis Lekayo aliiomba mahakama radhi na kusema ‘tutafanya haraka kesi iendelee.’

Hakimu Simba alisema, kauli iliyotolea na mshitakiwa ni ya msingi. Baada ya kueleza hayo aliahirisha kesi hiyo hadi tarehe 12 Julai mwaka huu kwa ajili ya kuwasomea maelezo ya awali.

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Yaanza Maandalizi ya Uchaguzi Mkuu 2020

0
0
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) inaendelea na maandalizi ya uchaguzi ujao wa mwaka 2020 kwa kuboresha daftari la wapiga kura ili kuweka taarifa za walengwa wakiwemo watakaopiga kura baada ya kufikisha umri wa kupiga kura.

Aidha, itawahusu walioshindwa kupiga kura katika chaguzi zilizopita kutokana na sababu mbalimbali. Hayo yalisemwa jana mjini Kibaha na Ofisa Uchaguzi wa Tume hiyo, Adam Nyando wakati akikabidhi taarifa za Uchaguzi Mkuu wa 2015 kwa mkoa wa Pwani.

Alisema, baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa mwaka 2015, wameanza maandalizi ya uchaguzi mkuu ujao na si kwamba kwa sasa Tume imelala.

“Watu wanafikiri uchaguzi ukishaisha ndio kazi imekwisha kumalizika kwa uchaguzi mmoja ni maandalizi ya uchaguzi ujao kwani kwa sasa tunaendelea na uboreshaji wa daftari la wapigakura pamoja na kura za maoni,” alisema Nyando.

Alisema uchaguzi uliopita ulikwenda vizuri na hakukuwa na matatizo makubwa licha ya matumizi ya mfumo mpya wa BVR, lakini matokeo yake umekuwa mfumo mzuri na umepata mafanikio makubwa.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo, akizungumza alitumia fursa hiyo kuwapongeza Watanzania kwa kufanya uchaguzi mzuri usiokuwa na vurugu wala uvunjifu wa amani.

Ndikilo alisema nchi nyingine kipindi cha uchaguzi ni kipindi kibaya cha uvunjifu wa amani, ikiwa ni pamoja na umwagikaji mkubwa wa damu, hasa kwa pande zisizokubaliana matokeo.

“Uchaguzi ulienda vizuri licha ya changamoto zilizojitokeza za hapa na pale lakini watu walivumiliana na kukubaliana na matokeo kilichobaki sasa ni kufanya kazi ili kuwaletea maendeleo wananchi, kikubwa ni tume kufanyia kazi changamoto zilizojitokeza ikiwa ni pamoja na usafiri na ucheleweshwaji wa matokeo kwa baadhi ya sehemu,” alisema Ndikilo.

Akikabidhi taarifa hizo kwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Ofisa Uchaguzi wa mkoa, Shangwe Twamala alisema mkoa huo umepata nakala 47 ambazo zitasambazwa kwa wadau mbalimbali wa uchaguzi. 

Alisema taarifa hizo zitasambazwa kwenye ofisi za mkuu wa mkoa, wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri za miji na wilaya na taasisi za elimu ya juu.

RAHCO Yaanza kuweka alama za X na kutoa notisi kwa wananchi wote waliovamia hifadhi ya reli

0
0

Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (RAHCO) ilianzishwa mwaka 2007 kupitia sheria ya Reli namba 4 ya mwaka 2002. 

Lengo kubwa la kuanzishwa kwake ni kusimamia na kuendeleza miundombinu ya rasilimali za reli nchini. Kifungu cha 57(2) cha sheria ya reli kinabainisha wazi kuwa mtu yeyote haruhusiwi kufanya ujenzi wowote katika hifadhi ya njia za reli pasipo kibali kutoka RAHCO. 

Vile vile kifungu cha 4 cha sheria hiyo kinaelekeza kuwa hifadhi ya reli ni mita 15 kutoka katikati ya njia ya reli kwa pande zote kwa maeneo ya mjini na mita 30 kwa pande zote kwa maeneo ya vijijini. 

Kufuatia ukaguzi wa miundombinu na rasilimali za reli, RAHCO imebaini kuwa baadhi ya hifadhi ya reli pamoja na maeneo mengine inayoyasimamia yamevamiwa na wananchi. Kitendo cha kuvamia maeneo hayo ni ukiukaji wa sheria. 

Kwa hiyo, uongozi wa RAHCO unatoa taarifa ya kuwataka wale wote waliovamia na kujenga ndani ya hifadhi za reli na maeneo mengine inayoyasimamia kubomoa majengo yao ndani ya siku 30 baada ya kutolewa kwa tangazo hili. 

Kwa wale watakaokaidi agizo hili, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao ikiwa ni pamoja na RAHCO kuyabomoa majengo kwa gharama za wahusika waliokiuka sheria.

Imetolewa tarehe 25-04-2016 na:
MKURUGENZI MTENDAJI
Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (
RAHCO)
Simu: +255 (0)22 2127403 Barua pepe: md@rahco.go.tz
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live




Latest Images