Quantcast
Channel: MPEKUZI
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live

Wabunge UKAWA Wamaliza Bunge La Bajeti Kwa Mtindo Mpya.....Wavaa Nguo Nyeusi Na Kutoka Nje Wakiwa Na Mabango

$
0
0
Wabunge wa Kambi Rasmi ya Upinzani leo asubuhi wameingia bungeni wakiwa wote wamevalia nguo nyeusi walipohudhuria kikao cha 54 cha Bunge la Bajeti mjini Dodoma.

Baada ya Naibu Spika Dk Tulia Ackson kuingia bungeni na kuongoza dua ya kuliombea Bunge, walianza kunyanyua mabango mbalimbali na kutoka nje.

Wabunge watatu wa CHADEMA wasimamishwa kuhudhuria vikao vya Bunge

$
0
0
Mbunge wa Mbeya mjini kwa tiketi ya Chama cha Demokrasi na  Maendeleo (CHADEMA), Joseph Mbilinyi amesimamishwa kuhudhuria na vikao 10 vya Bunge kuanzi leo kufuatia kitendo cha kuonyesha kidole cha kati bungeni.

Joseph Mbilinyi alitenda kosa hilo alipokuwa akitoka nje ya ukumbi wa Bunge baada ya kile alichoeleza kuwa kuna mbunge wa CCM aliyemtusi mama yake. Hata hivyo alipohojiwa kama anamfahamu mbunge huyo, Mbilinyi alisema kuwa hamfahamu.

Hukumu hiyo imesomwa leo na Naibu Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Bunge kueleza kuwa kamati hiyo ilijiridhisha kuwa kitendo kilichofanywa na mbunge huyo kuwa ni kosa.

Aidha wabunge wangine waliosimamishwa kuhudhuria vikao vya Bunge ni pamoja na Saed Kubenea, Mbunge wa Ubungo, James Ole Millya  Mbunge wa Simanjiro kwa makosa yanayofanana ya kusema uongo bungeni. Wabunge hawa wamesimamishwa kuhudhuria vikao vitano kuanzi leo.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameahirisha mkutano wa tatu wa Bunge lililokuwa na lengo la kujadili na kupitisha bajeti ya serikali ya mwaka wa fedha 2016 2017. Kufuatia kuahirishwa huko, kuanzia kesho Julai Mosi, serikali itaanza kutekeleza miradi na mpango mingine iliyoanishwa katika bajeti hiyo.

Kesi ya Uchochezi: Tundu Lissu apandishwa kizimbani, apata dhamana....Kesi yaahirishwa hadi Agosti 2

$
0
0

Tundu Lissu (48) amesomewa mashtaka ya kutoa lugha ya uchochezi ikiwemo kudharaulisha watanzania dhidi ya mamlaka halali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Lissu alisomewa mashtaka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam leo Juni 30, 2016.

Upande wa Jamhuri uliongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu Bernad Kongola akisaidiana na Mawakili wa Serikali Waandamizi, Nassoro Katuga na Salum Mohammed.

Kongola alidai kuwa Juni 28,2016 eneo la Mahakama ya Kisutu Ilala Dar es Salaam mshtakiwa alitamka maneno ya dhihaka  kwa nia ya kushawishi na kudharaurisha watanzania dhidi ya mamlaka halali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Alinukuu maneno ya Lissu kwamba"Mamlaka ya Serikali mbovu ya kidikteta uchwara inahitaji kupingwa na kila mtanzania kwa nguvu zote, huyu dikteta uchwara lazima apingwe kila sehemu kama uongozi utafanywa na utawala wa kijinga nchi inaingia  ndani ya giza nene"

Mshtakiwa alikana mashtaka hayo.Upande wa jamhuri ulidai upelelezi umekamilika na uliomba tarehe ya kusikilizwa maelezo ya awali.

Upande wa utetezi ukiongozwa na jopo la mawakili 11 akiwemo Michael Ngalo, Peter Kibatala na wenzao uliomba dhamana kwa mshtakiwa kwa kuwa ni mbunge atakuwa mwaminifu hataacha kufika mahakamani.

Hakimu Yongolo alisema mshtakiwa atakua nje kwa dhamana kwa kuwa na wadhamini wawili watakaosaini hati ya dhamana ya sh milioni 2.

Tundu Lissu alitimiza masharti na kuachiwa kwa dhama, atasomewa maelezo ya awali Agosti 2,2016.

Mkurugenzi Mkuu Wa Shirika La Viwango Tanzania(TBS),joseph Masikitiko Asimamishwa Kazi Kupisha Uchunguzi.

$
0
0
Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania(TBS), Joseph Masikitiko.

Zoezi La Uhakiki Wa Silaha Nchini Lafikia Tamati, Angalizo Latolewa Kwa Wasiohakiki

$
0
0


Leo tarehe 30.6.2016 ndiyo tarehe na siku ya mwisho wa zoezi la kuhakiki silaha. Kwa mujibu wa takwimu za silaha tulizonazo inaonyesha kwamba wapo baadhi ya wamiliki wa silaha ambao hawajatekeleza agizo la kuhakiki silaha wanazozimiliki.

Kufutia hali hiyo, natoa angalizo kwa wale wote ambao hawajahikiki silaha zao kwamba muda wowote kuanzia sasa tutaanza operesheni maalum ya kutafuta silaha ambazo hazijahikikiwa. Ifahamike kwamba yeyote atakaye kutwa na silaha ambayo haijahakikiwa atachuliwa hatua kali za kisheria ikiwemo kupoteza sifa ya kuwa mmiliki halali wa silaha hiyo.

Tunatoa agizo kwa wamiliki binafsi wa maghala ya silaha waziwasilishe silaha hizo pamoja na nyaraka zake katika vituo vya karibu vya Polisi kwa ajili ya uhakiki.

Imetolewa:-
Nsato M. Mssanzya – CP
Kamishina wa Polisi Operesheni na Mafunzo
Makao Makuu ya Polisi

Waziri Mkuu Awataka Wanufaika wa Mikopo ya Elimu Juu Kurejesha mikopo waliyopewa.

$
0
0
Wanufaika wa Mikopo ya Elimu ya Juu ambao tayari wapo katika ajira wametakiwa kurejesha marejesho ya mikopo waliyopewa kutokana na mfuko wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) kutegemea fedha hizo kuendelea kuwakopesha wanafunzi wengine.

Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa ameyasema hayo leo Bungeni, Mjini Dodoma alipokuwa akiwasilisha hotuba ya kuhitimisha mkutano wa tatu wa Bunge la kumi na moja.

“Uwezo wa Bodi ya mikopo ya Elimu ya Juu kuwahudumia walengwa unajengwa na fedha zinazotengwa kila mwaka katika mipango na Bajeti pamoja na marejesho ya mikopo iliyoiva kutoka kwa wanufaika,” alisisitiza Mhe. Majaliwa.

Aliendelea  kusema kuwa Serikali inaendelea kufanya maboresho ya kimfumo na kisheria ili kuimarisha urejeshwaji wa mikopo. 

Aidha amewaagiza waajiri wote Nchini kutekeleza wajibu wao wa kuingiza makato ya marejesho wa mikopo ya wanufaika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa baada ya kuwasiliana na Bodi ya Mikopo.

Vile vile Mhe. Majaliwa amesema kuwa Serikali inaendelea kuimarisha mfumo wa utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu sambamba na kushughulikia changamoto mbalimbali zilizopo katika Bodi ya mikopo ili kuhakikisha utoaji wa mikopo unafanyika kwa ufanisi.

Pia Serikali inategemea kubadilisha utaratibu wa kutoa mikopo ili kuwafikia wanafunzi wote wenye uhitaji zaidi wakiwemo yatima na wenye uwezo mdogo kiuchumi bila kujali aina gani ya program wanazozisomea.

Waziri Mkuu awataka wabunge wa upinzani kurejea Bungeni .

$
0
0

Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa leo, Bungeni Mjini Dodoma amewataka wabunge wa upinzani ambao wamesusia vikao vya Bunge tangu Mei 30 kuingia Bungeni na kuacha kususia vikao vya Bunge kwani hakuna tija kwa Taifa.

Mhe. Majaliwa ameyasema hayo alipokuwa akitoa hutuba ya kuhitimisha mkutano wa tatu wa Bunge la kumi na moja.

“Kitendo cha baadhi ya waheshimiwa wabunge kususia vikao vya Bunge hakitoi picha nzuri kwa wananchi waliotuchagua kuwasilisha matatizo yao katika Bunge hili, hivyo natoa rai kwa waheshimiwa wabunge hao kutafakari upya uamuzi wao na niwasihi kwa busara zao waingie ili kwa pamoja na kwa ushirikiano tuweze kutoa ushauri kwa Serikali,” alisema Mhe. Majaliwa.

Aidha Mhe. Majaliwa alitoa ufafanuzi juu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ambayo imetoa haki na kinga kwa waheshimiwa wabunge ili kujadili na kuhoji utendaji wa Serikali kwa uhuru bila mashaka yoyote ya kuweza kushitakiwa wanapotimiza wajibu wao wakiwa Bungeni.

Aliendelea kwa kusema kuwa kinga ya aina hiyo haijatolewa kwa mwananchi yeyote yule Nchini ila kwa Wabunge, hivyo basi hakuna mbunge aliyefungwa mdomo labda aamue kujifunga mdomo yeye mwenyewe.

Mhe. Majaliwa amesema kuwa Bunge linaongozwa na Katiba, Sheria na Kanuni za Kudumu za Bunge, hivyo ni vyema zikafuatwa kuondoa manung’uniko yasiyo ya lazima na endapo kuna utata katika jambo lolote ndani ya Bunge zipo taratibu zilizowekwa na kanuni za kufuata ili kupata ufumbuzi na si kwa kususa kuingia Bungeni kwani hakuna tija kwa Taifa.

Wabunge wa upinzani wamesusia vikao vya Bunge tangu Mei 30, 2016 mpaka leo Juni 30 ambapo Bunge limehitimishwa.

Aidha wabunge hao wamekuwa wakiingia Bungeni kila asubuhi na jioni kisha kutoka mara tu Naibu Spika Mhe. Dkt. Tulia Ackson anapomaliza kusoma Dua maalum la kuliombea Bunge na Taifa.

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Ijumaa ya July 1


Serikali Yamtaka Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Achukue Hatua Stahiki Dhidi ya Aliyemtukana Rais Magufuli

$
0
0
SERIKALI imemtaka Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuchukua hatua stahiki katika shauri la kesi ya jinai namba 100 ya Jamhuri dhidi ya Isaac Emily aliyeadhibiwa kulipa faini kwa kumtukana Rais John Magufuli mtandaoni.

Hayo yamesemwa jana bungeni na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe wakati akitoa kauli ya serikali baada ya mwongozo ulioombwa na wabunge wa CCM, Juma Nkamia wa Jimbo la Chemba na Livingstone Lusinde wa Mtera, baada ya hukumu hiyo kutolewa hivi karibuni. Hata hivyo, hatua stahiki hizo hazikuelezwa.

Alisema nia ya maagizo hayo kwa DPP ni kulinda dhana na dhamira ya adhabu katika mfumo wa haki jinai ambayo hutaka mhukumiwa kujutia kosa lake na wengine kujifunza kutoka kwake.

Katika maelezo yake, Waziri Mwakyembe alisema kwa hali ilivyo katika shauri hilo, dhana na dhamira ya adhabu haikuweza kufikiwa kwa mwenendo wa kuingiza siasa katika utekelezaji wa hukumu.

Alisema serikali imejiridhisha na kilichotokea katika shauri hilo na kauli za wabunge walioomba mwongozo kwamba masharti ya adhabu yalikuwa mepesi mno usiolingana na shauri lenyewe.

Alisema aliyehukumiwa analifanyia siasa suala hilo na kuigeuza adhabu rafiki aliyopewa kuwa burudani ya kisiasa katika mitandao ya kijamii.

“Mheshimiwa spika, nimejiridhisha na kilichotokea. Madhara ya mwelekeo huu mpya katika haki jinai, ni kuchochea vitendo zaidi vya ukaidi kwa mamlaka za nchi na hivyo kujenga msingi wa vurugu. Hili halikubaliki katika utawala wa sheria. Mdharau mwiba mguu huota tende,” alisema..

Alisema kosa kama hilo lilitokea Kenya mwaka jana ambapo mwanafunzi wa Chuo Kikuu nchini humo, Alan Okengo (25) alihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja na kulipa faini ya dola 2,000 (Sh milioni 3.2) kwa kumtukana rais wa nchi hiyo kwenye mitandao ya kijamii.

Alisema pamoja na umri wake na uwezo wake mdogo wa kulipa faini, adhabu ilibaki palepale ili mkosaji ajutie kosa lake asije akarudia na jamii ijisikie salama.

Alisema pamoja na kutokuingilia mhimili wa mahakama na taratibu zake kitendo cha kuwapo kwa adhabu ambayo haijutiwi inakiuka dhana na dhamira ya adhabu.

Alisema kwa shauri la Emily, pamoja na kutiwa hatiani wakili wake aliomba mtuhumiwa alipe faini kwa kuwa hakusumbua mahakama na pia ni kosa lake la kwanza na ana familia.

Alisema wakati hakimu anamuuliza wakili wa serikali aliiachia mahakama kutoa maamuzi ambayo ilimpatia wakili wa utetezi maombi yake.

Mwakyembe alisema pamoja na maagizo ya serikali kwa DPP amewakumbusha waendesha mashitaka nchini kuwa macho na waweke mbele weledi na maslahi mapana ya taifa na kamwe wasiyumbishwe na mihemko ya kisiasa katika jamii.

Waziri Mkuu: Serikali Itatoa Waraka Juu Ya Ukusanyaji Mapato Kupitia Mawakala

$
0
0
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Halmashauri zitaelekezwa kwa waraka ni vyanzo vipi vitahitaji kutumia wawakala wa ukusanyaji mapato kwani siyo kila chanzo cha mapato ya Halmashauri kitakusanywa kwa ufanisi kwa kutumia au kwa kutotumia mawakala.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jana mchana (Alhamisi, Juni 30, 2016) wakati akitoa hoja ya kuhitimisha mkutano wa tatu wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye ukumbi wa Bunge mjini Dodoma.

Alisema katika ukusanyaji wa mapato, baadhi ya vyanzo vitapaswa kukusanywa na Halmashauri zenyewe kwa kuzingatia miongozo iliyotolewa na Serikali. 

“Moja ya miongozo hiyo ni kwamba kuanzia sasa, iwe kwa kutumia mawakala au Halmashauri zenyewe ni lazima fedha zinazokusanywa ziwekwe kwenye akaunti ya Halmashauri na kutumia mifumo ya kielektroniki ili kupunguza au kumaliza kabisa masuala ya kutumia malipo kwa fedha taslimu (cash transactions),” alisema.

Alisema katika kutekeleza agizo hilo, Halmashauri itabidi zikubaliane na wakala ni kiasi gani cha asilimia ya makusanyo kitalipwa kwa wakala na malipo yafanyike baada ya kukusanya na kuingizwa kwenye akaunti ya Halmashauri.

Alisema Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa Sura ya 290, inazipa uwezo Mamlaka za Serikali za Serikali za Mitaa kutoza na kukusanya kodi, ushuru na ada mbalimbali kama vyanzo vya mapato vya Mamlaka za Serikali za Mitaa.

“Sheria hiyo pia inazipa mamlaka hizo kuteua mawakala wa kukusanya mapato hayo kwa niaba ya Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu. Lakini Serikali imebaini changamoto za kiufundi katika kufanya tathmini ya vyanzo vya mapato; ugumu katika kupata mawakala wenye weledi katika ukusanyaji mapato na kubuni vyanzo vipya vya mapato, na wakati mwingine watumishi wenyewe kujipa uwakala kinyume na taratibu zinazomzuia mtumishi kufanya biashara na taasisi yake,” alisema.

Alisema hatua ya Mamlaka za Serikali za Mitaa kutumia mawakala ni miongoni mwa mikakati ya kuboresha ukusanyaji mapato na pia kutoa muda mwingi zaidi kwa watumishi wa mamlaka hizo kushughulika na majukumu ya msingi ya Halmashauri na hasa utoaji wa huduma kwa wananchi na usimamizi wa miradi ya maendeleo.

“Pamoja na dhamira nzuri ya hatua hizo, tunayo mifano ya baadhi ya Halmashauri kama vile Nzega ambayo baadhi ya wahusika wameshinikiza wakitaka zabuni zote wapewe madiwani. Jambo hili halikubaliki na tena ni kinyume cha maadili ya utumishi,” alisisitiza.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameziagiza Halmashauri zote nchini kwamba kuanzia Julai Mosi, 2016 zihakikishe zinatumia mifumo ya kielektroniki katika kukusanya mapato, katika kulipa, kuweka na kutekeleza kikamilifu mikakati madhubuti ya kuboresha makusanyo iwe yanakusanywa na Halmashauri au na wakala.

Alisema Mamlaka za Serikali za Mitaa zina wajibu wa kutoa taarifa kwa wananchi kuhusu mapato na matumizi ya Serikali pamoja na michango ya wananchi licha ya kuwa uzoefu unaonesha kuwa mamlaka hizo zina tatizo la kukaa na fedha kwa muda mrefu kabla ya kuzielekeza kwenye matumizi yaliyokusudiwa.

“Kuchelewesha kutoa fedha zilizotengwa kwa shughuli zilizopangwa ni kuchelewesha kufikisha huduma muhimu kwa wananchi. Napenda kuhimiza uzingatiaji wa utaratibu wa kutoa taarifa kwa wananchi kuhusu mapato na matumizi ya fedha za Serikali katika ngazi zote ili kuongeza uwazi na uwajibikaji katika sekta ya umma,” aliongeza.

Mkutano huo wa tatu wa Bunge ulioanza Aprili 19, 2016 ulikuwa mahsusi kwa ajili ya kujadili na kupitisha bajeti ya kwanza ya Serikali ya Awamu ya Tano pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2016/2017. Bunge limeahirishwa hadi Septemba 6, mwaka huu litakapokutana tena mjini Dodoma.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S.L. P. 980,
DODOMA.
ALHAMISI, JUNI 30, 2016

Askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Auawa kwa Fimbo

$
0
0
ASKARI wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kikosi cha 212 kilichopo Milambo mkoani Tabora, ameuawa kwa kipigo kutoka kwa wafugaji akiwa eneo lake la ujenzi.

Aliyeuawa katika tukio hilo la juzi katika kijiji cha Usule kata ya Mbugani, Manispaa ya Tabora ni Crius Mkumozi mwenye umri wa miaka 35.

Mtuhumiwa wa mauaji hayo inadaiwa alikuwa akichunga mifugo kwenye eneo la askari huyo.

Akizungumza ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tabora, Hamisi Issa alisema askari huyo alipigwa fimbo kichwani na begani baada ya kujaribu kuondoa ng’ombe waliokuwa kwenye eneo lake.

Kamanda alisema mtuhumiwa ambaye hakutaka kutaja jina lake, anashikiliwa kwa mahojiano zaidi na atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma za mauaji.

Mahakama ya Mafisadi Kuanza Rasmi Leo

$
0
0
MAHAKAMA Maalumu ya kushughulikia Makosa ya Rushwa na Ufisadi, inaanza rasmi leo Julai mosi.

Pamoja na kuanza kwa mahakama hiyo, serikali imeanza mchakato kuifanyia marekebisho Sheria Namba 11 ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini ya Mwaka 2007 ili kuongeza ukubwa wa adhabu zinazotolewa sasa.

Mahakama hiyo iliyoahidiwa na Rais John Magufuli wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 na imo katika Ilani ya Uchaguzi wa Chama Cha Mapinduzi, itaimarisha zaidi taasisi za uwajibikaji zinazohusika na mapambano dhidi ya rushwa.

Ahadi hiyo ambayo inatimizwa ndani ya kipindi cha miezi isiyozidi saba tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani ni sehemu ya mapambano ya kujenga misingi ya uchumi kwa kudhibiti rushwa na mianya yake na kuleta uwajibikaji.

Akiahirisha Bunge jana mjini Dodoma, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema utekelezaji wa ahadi hiyo unakwenda sambamba na kuonesha dhamira ya serikali ya kushughulikia makosa ya rushwa na kuweka misingi imara ya uwajibikaji katika sekta zote.

“Mahakama itawafanya watu waliozoea rushwa na ufisadi kujiuliza mara mbili kabla ya kufanya uhalifu huo yaani kuwa deterrent,” alisema Waziri Mkuu na kuongeza kuwa kuwapo kwake kutahamasisha wafanyabiashara kufanya shughuli zao bila shaka huku umuhimu kwao, ikiwa ni kulipa kodi.

Akielezea umuhimu wa mahakama hiyo, alisema kwamba itasaidia kuendeleza nia ya serikali ya watu kulipa kodi kwa maendeleo ya taifa.

Akielezea umuhimu wa kodi, alisema kuna mahitaji makubwa ya fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo na uendeshaji wa shughuli za serikali na hivyo serikali itaendelea ukusanyaji wa mapato ya ndani na kudhibiti mianya ya ukwepaji kodi.

Aidha, alisema serikali itaanzisha Kikosi Maalumu cha kufuatilia kwa karibu matumizi ya mashine za kielektroniki (EFDs) za kutoa risiti kila mfanyabiashara anapouza bidhaa au huduma na kuhakikisha kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) wanashirikiana na Wakala wa Serikali wa Serikali Mtandao kutekeleza mfumo wa kuwa na dirisha moja na pia kudhibiti kikamilifu mizigo inayoingia na kutoka bandari kavu.

Udhibiti wa matumizi
Akizungumzia matumizi, Waziri Mkuu alisema serikali itaendelea na kudhibiti matumizi yasiyokuwa ya lazima na kufuatilia bajeti na matumizi ya fedha za umma.

Na ili kufanikisha hilo, itafanya mapitio ya majukumu ya wizara na taasisi za umma ili kuwianisha majukumu ya vyombo vya serikali na hivyo kupunguza gharama za uendeshaji.

Aidha, uhakiki wa wafanyakazi utaendelea na watendaji wakitakiwa wanadhibiti matumizi ya fedha za umma kwa kuzingatia ukomo wa bajeti ya fungu husika lililoidhinishwa na Bunge.

Aidha, Waziri Mkuu aliagiza halmashauri zote nchini kuanzia leo kuhakikisha kwamba zinatumia mifumo ya kielektroniki katika kukusanya mapato, kulipa, kuweka na kutekeleza kikamilifu mikakati madhubuti ya kuboresha makusanyo iwe yanafanywa na halmashauri au kupitia wakala wake.

Waziri Mkuu alisema wabunge wamepitisha Bajeti ya Serikali inayotegemea sana ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kupunguza utegemezi kutoka nje na kuhimiza uwajibikaji katika kuongeza juhudi za kukusanya na kupanua wigo wa kutoza kodi ili mapato yaongezeke.

Aidha, alisema ipo haja ya wananchi kudai risiti kwa huduma mbalimbali wanazonunua na kushirikiana na serikali kubaini wakwepa kodi na kuziba mianya ya upotevu wa mapato ya serikali.

Aliwataka watumishi wa umma kuendelea kufanya kazi kwa maadili katika maeneo yao wakijenga utamaduni wa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu katika utumishi wa umma ili kuongeza ufanisi na tija.

Mpango wa Maendeleo
Akizungumzia maeneo manne ya Mpango wa Maendeleo, Waziri Mkuu alisema kwa sasa Serikali ya Awamu ya Tano imeweka msingi kupitia Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Taifa wa kukuza na kujenga uchumi wa viwanda kwa kuweka mazingira yatakayochochea maendeleo ya viwanda.

Aidha, imejiweka katika hali ya kufungamanisha maendeleo ya uchumi na maendeleo ya watu kwa kuhakikisha kwamba elimu inayotolewa ni bora na inayojenga msingi wa rasilimali watu wanaohitajika kuipeleka nchi katika uchumi wa kati.

Alisema ili kufanikisha hayo serikali itaimarisha mifumo ya kisheria kuwa rafiki na kuvutia wawekezaji wa ndani na nje huku ikiimarisha miundombinu ili iweze kutumika kirahisi na kupunguza gharama zake.

Ili kufanikisha ufanisi na tija, Waziri Mkuu alisema serikali itaimarisha usimamizi, ufuatiliaji na tathmini ya mpango wenyewe wa maendeleo mara kwa mara.

Ili kufanikiwa ametaka tabia ya vijana kushinda katika pombe na kucheza pool table kuachwa na kuwataka viongozi waliochaguliwa sasa wilayani na mikoani kuhakikisha kwamba maeneo ya starehe hayafunguliwi wakati wa muda wa kazi ili vijana washiriki katika uzalishaji mali.

Akizungumzia mkakati wa ujenzi wa uchumi wa viwanda, Waziri Mkuu alisema serikali itategemea zaidi sekta binafsi kama injini ya ukuzaji uchumi na maendeleo na kwamba serikali haitajiingiza moja kwa moja katika kujenga viwanda na kufanya biashara.

Miradi ya umeme
Akizungumzia uimarishaji wa uchumi kwa kuwa na uhakika wa nichati hadi vijijini, alisema serikali imetenga fedha kwa ajili ya kuyapatia maeneo yaliyo nje ya gridi ya taifa nishati bora ikiwa ni pamoja na maeneo ya visiwani.

Alisema Serikali ya Uingereza na Sweden zinachangia katika kuhakikisha kwamba mifumo hiyo ya kupeleka umeme maeneo yaliyo nje ya gridi inafanikiwa. Alisema serikali imetenga zaidi ya Sh trilioni moja kutoka ndani na benki ya dunia kwa ajili ya kuendeleza nishati vijijini.

Serikali Yajipanga Kuanza Kutekeleza Miradi ya Maendeleo kwa Fedha za Ndani Baada ya Wafadhili Kupunguza Misaada

$
0
0

SERIKALI imesema muda si mrefu inatarajia kuanza kutekeleza miradi ya maendeleo kwa kutumia fedha za ndani kwa asilimia 100, kutokana na washirika wa maendeleo kuanza kupunguza ufadhili na misaada katika miradi hiyo.

Hayo yameelezwa jana na Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Gerson Lwenge, wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Ludewa, Deo Ngalawa(CCM), aliyetaka kujua ni lini serikali itaacha kutegemea wafadhili katika kutekeleza miradi ya maendeleo.

Ngalawa pia alitaka kujua ni lini serikali itajenga miundombinu ya umwagiliaji nchi nzima ili kuboresha kilimo cha umwagiliaji. Lwenge alisema kwa sasa washirika wa maendeleo wamepunguza kusaidia miradi ya maendeleo, jambo ambalo limeifanya serikali kujipanga kuanza kutekeleza miradi ya maendeleo kwa fedha za ndani kwa asilimia 100.

Akijibu swali la pili la nyongeza la Ngalawa, Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Isack Kamwelwe alisema zipo hekta milioni 29.4 za kutekeleza miradi ya umwagiliaji kwa kuziwekea miundombinu na kwa mwaka huu, hekta milioni 12 zitajengwa miundombinu ya umwagiliaji.

Katika swali la msingi, Ngalawa alitaka kujua mpango wa serikali wa kuliendeleza bonde la Mto Ruhuhu lililopo katika kata ya Ruhuhu wilaya ya Ludewa, ambalo ni eneo muhimu sana na linaweza kuzalisha mazao mengi na kupunguza uhaba wa chakula Tanzania.

Kamwelwe alisema Serikali inatambua umuhimu wa bonde hilo, ambapo katika maandalizi ya uendelezaji wa bonde hilo upembuzi wa awali ulifanyika kati ya mwaka 2013 na 2014.

Alisema walibaini uwezekano wa kujenga bwawa kubwa katika eneo la Kikonge kwa ajili ya matumizi mbalimbali ikiwemo kudhibiti mafuriko katika bonde la mto Ruhuhu, kuendesha kilimo cha umwagiliaji kwa eneo la takribani hekta 4,000 na kufua umeme mkubwa utakaounganishwa kwenye gridi ya Taifa.

Alisema kwa sasa serikali kwa kushirikiana na benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), ipo katika hatua ya kutafuta fedha kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa bwawa na miundombinu ya umwagiliaji.

Hatimaye TAKUKURU na TRA Wamtaja Mtu Aliyekuwa Akiibia Serikali Milioni 7 Kwa Kila Dakika

$
0
0
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) hatimaye wametaja mfanyabiashara ambaye alibainishwa na Rais John Magufuli katika hafla ya kuwaapisha Wakuu wa Mikoa na Wilaya, Ikulu Dar es Salaam juzi.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Valentino Mlowola alimtaja mfanyabiashara huyo kuwa ni Mohammed Mustafa Yusuf Ali anayetuhumiwa kuiibia Serikali matrilioni ya shilingi kwa kutumia mashine za kielektroniki (EFDs) ambazo hazijasajiliwa na TRA na kutoa risiti bandia.

Alisema TRA kwa kushirikiana na TAKUKURU inaendelea na uchunguzi ili kubaini makampuni yote yanayojihusisha na udanganyifu huu, ambapo hadi sasa jumla ya makampuni manne yamebainika kujihusisha na ukwepaji kodi kwa mtindo huu kuanzia mwaka 2010 hadi 2014; na jumla ya Sh 29,216,900,301.7 imebainika kutokulipwa serikalini na makampuni hayo kwa kipindi hicho.

Alisema kwa sasa wanaendelea na mahojiano naye zaidi ili kuwabaini wote wanaohusika na mfumo huo na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

Kwa mujibu wa Kamishna Mkuu wa TRA, Alfayo Kidata aliyeambatana na Mlowola katika mkutano huo wa waandishi wa habari, makampuni hayo yamekuwa yakinunua risiti za manunuzi bandia kutoka kwa watu wanaomiliki mashine za EFDs ambazo hazijasajiliwa.

“Makampuni hayo wakishanunua risiti za manunuzi bandia, hatimaye huzitumia risiti hizo kudai marejesho ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) bila kuwepo na bidhaa au huduma halisi iliyouzwa au kutolewa na mhusika, kitendo ambacho kinainyima serikali mapato stahiki kwa mujibu wa sheria,” alisema.

Aliyataja makampuni hayo kuwa ni pamoja na Skol Building Material Ltd ambayo tangu mwaka 2012 hadi 2013 haikulipa jumla ya VAT ya Sh 5,464,915,963 na Kodi ya Mapato yenye thamani ya Sh 10,960,787,861 ambayo jumla ya kodi inayodaiwa ni Sh 16,425,703,824 kwa kipindi hicho.

Kampuni nyingine ni Farm Plant (T) Limited ambayo tangu mwaka 2010 hadi 2014 haikulipa jumla ya VAT ya Sh 5,930,170,573 na kodi ya mapato yenye thamani ya Sh 4,948,393,516 ambayo jumla ya kodi inayodaiwa ni Sh 10,878,564,089.

Pia imo kampuni ya A.M.Steel & Iron Mills Limited ambayo kuanzia mwaka 2013 hadi 2014 haikulipa jumla ya VAT ya Sh 79,016,112 na kodi ya mapato yenye thamani ya Sh 131,693,518 ambayo jumla ya kodi inayodaiwa ni Sh 210,709,630.

Kampuni nyingine ni A.M Trailer Manufacturers Limited ambayo tangu mwaka 2013 hadi 2014 haikulipa VAT ya Sh 638,221,034.80 na kodi ya mapato yenye thamani ya Sh 1,063,701,724. 00 ambayo jumla ya kodi inayodaiwa ni Sh 1,701,922,758.00.

Alisema baada ya kubaini ukwepaji kodi huo kwa kushirikiana na TAKUKURU inaendelea na uchunguzi wa tuhuma hizo na mara baada ya uchunguzi kukamilika hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watakaobainika kukwepa kodi.

Alitoa mwito kwa wafanyabiashara wote kutojihusisha na kununua risiti za bandia na kudai marejesho ya VAT yasiyostahili kwa kuwa mamlaka imejizatiti kuendelea kuwabaini wafanyabiashara wanaokwepa kodi na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria kwa hatua stahiki.

Aidha alisema uchunguzi wa awali pia umebaini kuwepo makampuni hewa 228 na kusisitiza kwamba wameusimamisha mfumo huo bandia na kutoa siku tatu kwa kampuni zote zinazodaiwa kulipa fedha hizo.

“Hakuna yeyote anayekwepa kodi atasalimika, wote ni lazima walipe na sasa tumedhibiti mfumo huo bandia,” alisema.

Juzi Magufuli akizungumza na Ma RC na Ma DC wapya, aliwataka wakasimamie vyema mapato katika maeneo yao kwani kumekuwepo na baadhi ya watu wajanja wanaotumia vibaya taasisi za Serikali ikiwemo Wakala wa Usajili wa Kampuni (Brela) TRA kujinufaisha wenyewe na kuliingizia taifa hasara.

Alisema: “Tulikuwa tunafuatilia mashine za EFDs zinazokusanya mapato, yupo mtu mmoja alitengeneza kampuni nyingi zilizokuwa zikimlipa asilimia tano ya VAT na yeye anacheza na TRA halipi asilimia 18 ya kodi hiyo. Alikuwa anaingiza kati ya shilingi milioni saba mpaka nane kwa dakika. Serikali ilipoteza matrilioni ya fedha. Huyu mtu yupo kwenye mikono salama kwa sasa”.

Mjadala wa Sakata la Lugumi WAZIKWA Rasmi.......Naibu Spika Aipa Serikali Miezi Mitatu

$
0
0

Kiu ya wabunge kujadili sakata la utekelezwa mbovu wa mkataba baina ya Jeshi la Polisi na kampuni ya Lugumi Enteprises Limited, imezimwa baada Naibu Spika, Dk Tulia Ackson kuiagiza Serikali kukamilisha utekelezaji wa mradi huo ndani ya miezi mitatu ijayo. 

Kwa muda mrefu, wabunge walikuwa wakisubiri ripoti ya uchunguzi kutoka Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (PAC) ili waweze kujadili kwa kina sakata hilo linalohusisha mradi wa Sh37 bilioni wa kufunga vifaa vya kielektroniki vya kuchukua alama za vidole (AFIS). 

Mapema Aprili mwaka huu, wakati PAC ikipitia taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka ulioshia Juni 30, 2014 ilibaini kuwa Lugumi ilikuwa imefunga mashine katika vituo 14 tu kati ya 108 ilivyotakiwa kuvifunga wakati ikiwa imeshapokea asilimia 99 ya malipo yote.

 PAC ilimuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani apeleke taarifa ya utekelezaji wa mradi huo ambayo aliipeleka Aprili 18 na kubaini kuwa vifaa hivyo vilifungwa katika vituo 153 pamoja na makao makuu ya polisi. 

Kutokana na utofauti wa takwimu za CAG na PAC iliunda kamati ndogo kufanya uhakiki wa vifaa vya AFIS na sababu za kuchelewa kutekelezwa kwa mradi, huku wengi wakitarajia ripoti hiyo ingejadiliwa bungeni. 

Katika sakata hilo, wabunge walimtuhumu aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga kuwa na masilahi kwa madai kuwa alikuwa mmoja wa wanahisa wa kampuni ya Infosys iliyoshirikishwa kwenye mradi huo na kushinikiza ajiuzulu kupisha uchunguzi. 

Hata hivyo, Kitwanga alitimuliwa kazi kwa kosa jingine la kuingia bungeni kujibu maswali ya wizara yake akiwa amelewa. 

Jana, Dk Tulia alitumia kanuni 117(17) kukabidhi matokeo ya uhakiki huo kwa Serikali, yakiwemo maoni, ushauri, mapendekezo ya namna ya kutatua changamoto zilizoanishwa na taarifa ya kamati ya PAC na kutoruhusu mjadala kwa wabunge

Dk Tulia alieleza kuwa amefanya uamuzi huo baada ya kupokea taarifa hiyo na kuangalia maudhui yake, kuzingatia matokeo ya uhakiki huo uliofanywa na kamati ndogo na PAC kujiridhisha uwepo wa vifaa hivyo, ukiacha kasoro zilizojitokeza. 

Pia, alisema suala hilo si jipya kwa kuwa linatokana na hoja ya ukaguzi wa miaka ya nyuma na kilichokuwa kimebaki ni vifaa hivyo kufanya kazi.

“Naagiza sasa kwamba Serikali ihakikishe mfumo huu unafanya kazi ndani ya miezi mitatu kuanzia leo (jana) ili kuboresha uwezo wa Jeshi la Polisi kuwa na utambuzi wa haraka wa wahusika wa matukio ya kihalifu katika vituo vyote nchini,” alisema huku akishangiliwa. 

Dk Tulia aliitaka pia Serikali kuyapatia ufumbuzi haraka masuala yote yaliyobainika kuwa na dosari za kiutendaji. 

Alisema ameielekeza kamati ya PAC kuhakiki maagizo aliyoyatoa kwa Serikali na baada ya uhakiki huo itoe taarifa bungeni wakati ikiwasilisha taarifa yake ya mwaka. 

“Natarajia kuwa suala hili sasa litafikia mwisho na CAG atafunga hoja yake baada ya kujiridhisha na utekelezaji wa maagizo niliyoyatoa,” alisema Dk Tulia. 

Mwenyekiti wa PAC, Aeshi Hilaly alisema walishamaliza kazi yao baada kumkabidhi Naibu Spika ripoti hiyo, kama kanuni zinavyotaka na kwamba yeye ndiye mwenye uamuzi wa mwisho. 

Aliyekuwa mwenyekiti wa kamati hiyo ndogo ya kuchunguza suala hilo, Japhet Asunga alisema baada ya uchunguzi, walibaini vituo 15 tu kati ya 153 ndivyo vimeunganishwa na mfumo wa taarifa za polisi. 

Asunga, ambaye ni mbunge wa Vwawa (CCM), alimwambia mwandishi wetu kuwa kamati ilibaini kuwa vifaa vyote vya AFIS vilivyokuwapo katika vituo vimetelekezwa bila kuunganishwa katika mfumo wa mtandao.

Alisema sehemu nyingine walikuta vifaa vimetupwa huku vingine vimeharibika kwa sababu vimekaa muda mrefu kama wino wa printa umeisha muda wake. 

“Tumeagiza Serikali ichukue hatua stahiki kuhakikisha vifaa vinatumika na kuwaadhibu wote waliochelewesha na nani hakufanya kazi ipasavyo.

“Ndiyo maana Naibu Spika baada kupima maagizo yaliyotolewa ameona Serikali ianze kuyafanyia kazi mapungufu badala ya kusubiri kuyawasilisha Septemba. Naona busara imetumika,” alisema Asunga. 

Alisema kamati haina tatizo na maazimio ya miezi mitatu aliyotoa Spika kwa kuwa ndiyo mapendekezo yao na kwamba PAC wao awali walipendekeza miezi sita.

Kodi ya Miamala ya Tigopesa, M-Pesa, Benki na Airtel Money kuanza Kutozwa Rasmi Leo

$
0
0

Leo ndiyo mwanzo wa utekelezaji wa Sheria Fedha (Finance Act, 2016) iliyopitishwa katika Bajeti ya 2016/17 ambapo Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) itatozwa katika huduma za mitandao ya simu, benki na taasisi za fedha.

Akisoma hotuba ya bajeti bungeni hivi karibuni, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango pamoja na mambo mengine, alipendekeza kuongeza kodi hiyo katika huduma za  kibenki zinazotozwa na benki hizo ili kupanua wigo wa kodi isipokuwa riba kwenye mikopo.

Vilevile, Waziri Mpango alieleza azma ya Serikali kutoza ushuru wa bidhaa wa asilimia 10 kwenye ada zinazotozwa na watoa huduma katika kutuma na kupokea fedha badala ya ushuru huo kutozwa tu kwenye kutuma fedha pekee.

Akizungumzia uamuzi huo, mtaalamu wa kodi wa kujitegemea, Deogratias Peter alisema ongezeko hilo litawakatisha tamaa wateja wa benki na watumiaji wa miamala ya simu.

“Kwa zaidi ya miaka 10 sasa, Serikali inafanya jitihada za kuongeza watumiaji wa benki kwani katika nchi za Afrika Mashariki ilikuwa nchi ya nne mbele ya Burundi kwa kuwa na idadi ndogo ya watu wanaotumia benki. Lakini hatua hii inaweza kurudisha nyuma jitihada hizo,” alisema Peter.

Alisema Serikali ilianzisha utaratibu wa Saccos, Vicoba na kulegeza masharti ya kuwa na akaunti ya benki ili kuwawezesha wananchi wa kawaida kumudu kuweka fedha kwenye taasisi za fedha na ilianzisha Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB), Benki ya Wanawake Tanzania (TWB), wakala wa benki na miamala ya simu ili kuongeza watumiaji wa benki.

“Watanzania wengi wasio na utamaduni wa kuweka fedha benki watakubali kukatwa fedha zao kiasi hicho?” alihoji.

Alisema mfumo huo kwa sasa haueleweki hasa kwa watumiaji wa miamala ya simu kwa kuwa mawakala wake hawatoi risiti kama ilivyoagizwa na Serikali.

Aliongeza kuwa hata katika mashine za ATM, hakuna mashine za kukata kodi ya VAT hivyo hakuna maandalizi ya kukokotoa kodi hizo.

Mkurugenzi wa Elimu na Huduma kwa Mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Richard Kayombo alipoulizwa kuhusu makato hayo, asisitiza azma ya Serikali kukusanya mapato kwa njia yoyote ile, bora tu iwe ni ya kisheria.

“Sina tafsiri yoyote ya kodi hiyo. Sisi kazi yetu ni kukusanya tu mapato… Sheria zinaruhusu kuwa na mabadiliko ya kodi kama hayo, kwa hiyo sisi tunatekeleza maagizo tu ya Serikali, haturuhusiwi kutafsiri kwa njia yoyote,” alisema Kayombo.

Jana, benki za CRDB,NMB na Standard Chartered zilitoa maelekezo kwa wateja wake juu ya kuwapo kwa makato hayo zikisema kuwa kutakuwa na ongezeko la asilimia 18 litakalotozwa katika gharama za huduma za benki kunzia leo, zikiungana na NBC ambayo ilitangaza azma hiyo wiki iliyopita.

“Kufuatana na Sheria ya Fedha (Finance Act, 2016) ongezeko la asilimia 18 litatozwa katika gharama za huduma za benki kuanzia Julai 1, 2016. Ongezeko hili (VAT) litakatwa kutoka katika akaunti na kama muamala hautapia kwenye akaunti, mteja atalipa kwa fedha taslimu,” ilisema sehemu ya taarifa ya Benki ya CRDB.

Hata hivyo, kama zilivyo taarifa za benki nyingine, ilisema ongezeko hilo halitahusika katika riba kwenye mikopo. Benki ya NMB, ilisema katika taarifa yake kuwa ongezeko hilo litakuwa katika gharama zote za miamala ya kibenki kuanzia leo.

Hata hivyo, Meneja Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa NMB, Vicent Mnyanyika alipoulizwa kuhusu taarifa hiyo hasa kiasi ambacho wateja watakatwa alijibu kupitia ujumbe mfupi wa simu: “Sipo ofisini ila nahisi tangazo linajitosheleza.”

Rais Wa Rwanda Paul Kagame Awasili Hapa Nchini

$
0
0
Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Rwanda,Paul Kagame amewasili katika uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Nyerere  leo na Kupokelewa na Mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Joseph Pombe Magufuli. Baada ya Hapo ataelekea Ikulu jijini Dar es Salaam kwaajili ya Kufanya Mazungumzo.
 
Baada ya hapo wataelekea katika Viwanja wa Maonesho ya Kimataifa ya Sabasaba jijini Dar es Salaam kwaajili ya Kufungua rasmi maonesho ya 40 ya Kimataifa katika viwanja vya Sabasaba  leo.

Ajali Mbaya Yaua Watu 11 Mkoani Morogoro

$
0
0

Habari iliyoripotiwa hivi punde na kituo cha ITV ni kuhusu ajali ambayo imetokea eneo la Veta Dakawa mkoani Morogoro ikihusisha magari matatu ambayo ni lori la mafuta, kontena lililobeba mchele pamoja na basi.

Taarifa hiyo inasema kuwa watu 11 wamefariki dunia na wengine ambao idadi yao bado haijajulikana wamejeruhiwa.

Tunaendelea kufuatilia taarifa zaidi kuhusu ajali hiyo.

Rais Magufuli Asema Mamlaka ya Bandari Tanzania TPA itafunga ofisi katika nchi ya Rwanda......Pia Kasema Serikali Imetenga Trilioni 1 Kwa Ajili ya Ujenzi wa Reli Kwenda Rwanda

$
0
0
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewahakikishia wafanyabiashara wa Rwanda kuwa bandari ya Dar es salaam ni salama kwa wao kupitisha mizigo na ameahidi kuwa Serikali ya Tanzania inaendelea kuchukua hatua za kuiboresha bandari hiyo na kurahisisha biashara kati ya nchi hizi mbili.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo leo tarehe 01 Julai, 2016 alipokuwa akizungumza na wananchi wa Tanzania na Rwanda kupitia vyombo vya habari wakati wa ziara rasmi ya kiserikali ya Rais wa Jamhuri ya Rwanda Mhe. Paul Kagame inayofanyika kwa siku mbili hapa nchini.

Dkt. Magufuli amesema pamoja na kuchukua hatua kadhaa za kuboresha bandari ya Dar es salaam kwa manufaa ya wafanyabiashara wanaopitisha mizigo, Tanzania imeamua kuipatia Rwanda eneo la kujenga bandari kavu kwa ajili ya mizigo ya wafanyabiashara wake na pia Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) itafungua ofisi Mjini Kigali nchini Rwanda ikiwa ni juhudi za kurahisisha na kuongeza biashara kati ya nchi hizi mbili.

Aidha, Rais Magufuli amesema kwa kutambua umuhimu wa reli ya kati kwa uchumi wa Tanzania na Rwanda, Tanzania imetenga shilingi Trilioni moja katika bajeti mpya ya serikali kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Reli hiyo kwa kiwango cha kisasa yaani “Standard Gauge” na kwamba ni matarajio kuwa wadau wengine wa maendeleo watajitokeza kuunga mkono juhudi za ujenzi wa reli hiyo hapa Tanzania na nchini Rwanda huku akidokeza kuwa China imeonesha nia ya kuunga mkono mradi huo.

Dkt. Magufuli ameongeza kuwa serikali yake pia imechukua hatua madhubuti za kulifufua shirika la ndege la Taifa na kwamba tayari mipango imefanywa kuhakikisha ndege mbili aina Bombadier Q400 zinanunuliwa na zitatua hapa nchini kabla ya mwisho wa mwezi Septemba Mwaka huu 2016.

Kwa upande wake Rais wa Jamhuri ya Rwanda Mhe. Paul Kagame amemshukuru Rais Magufuli kwa kumualika kufanya ziara rasmi ya kiserikali hapa nchini na amemhakikishia kuwa serikali yake itaendeleza na kuimarisha zaidi ushirikiano uliopo kati ya nchi yake na Tanzania kwa manufaa ya wananchi wa nchi zote mbili.

Majira ya jioni Rais Kagame akiwa na mwenyeji wake Rais Magufuli, amefungua rasmi maonesho ya 40 ya kimataifa ya Biashara Dar es salaam yanayofanyika katika viwanja vya Sabasaba vilivyopo Barabara ya Kilwa, Wilaya ya Temeke, Mkoani Dar es salaam.

Akizungumza kabla ya kuzindua rasmi maonesho hayo, Rais Kagame ametoa wito kwa Tanzania na Rwanda pamoja na nchi nyingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki kushirikiana na sekta binafsi katika kutumia fursa nyingi za kibiashara zilizopo baina yake na kuwaletea manufaa wananchi.

Nae Rais Magufuli amezipongeza nchi takribani 30 zilizojitokeza kushiriki katika maadhimisho hayo zikiwemo kampuni zaidi ya 650 na wadau zaidi ya 2,000 na amesisitiza umuhimu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zenye watu takribani milioni 165 na nchi nyingine za Jumuiya ya maendeleo kusini mwa Afrika (SADC) kuongeza biashara baina yake kwa kuwa hivi sasa kiwango cha biashara baina ya nchi hizo ni cha chini mno.

Baada ya kufungua maonesho hayo, Rais Kagame na mwenyeji wake Rais Magufuli wametembelea mabanda mbalimbali ya maonesho ya bidhaa na huduma katika viwanja vya Sabasaba na baadaye Rais Kagame atahudhuria dhifa ya Kitaifa iliyoandaliwa na mwenyekiji wake Rais John Pombe Magufuli Ikulu Jijini Dar es salaam.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
01 Julai, 2016

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Jumamosi ya July 2

Viewing all 45270 articles
Browse latest View live




Latest Images