Quantcast
Channel: MPEKUZI
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live

Wabunge wa CCM Wapinga Shinikizo la Wapinzani Kutaka Kumng'oa Naibu Spika, Dk.Tulia Ackson

$
0
0

WABUNGE watatu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wakiongozwa na Dk Abdallah Possi ambaye ni Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge,Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu), wameutaka umma uelewe kuwa shinikizo la wapinzani bungeni kuhusu utendaji wa Naibu Spika, Dk Tulia Ackson lina uonevu wa kijinsia.

Katika mkutano huo na wanahabari uliofanyika ofisi za Waandishi wa Habari, bungeni mjini Dodoma  jana, Dk Possi aliongozana na Mbunge wa Muleba Kusini, Profesa Anna Tibaijuka na Mbunge wa Sikonge, Joseph Kakunda.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, walisema hawakubaliani na mkakati wa kambi ya upinzani kutaka kumng’oa Naibu Spika, Dk Tulia Ackson, kwa sababu ni mkakati wenye shinikizo la kisiasa na ubaguzi dhidi ya wanawake.

Dk Possi alisema wabunge wa kambi ya upinzani hawana hoja za msingi kutaka kutekeleza mkakati wao huo kwa sababu si mara ya kwanza kwa wanaokiuka kanuni na taratibu za Bunge kutolewa au kusimamishwa.

“Tunaamini kinachotokea sasa ni msukumo wa kisiasa kwa kuwa wabunge wana njia ya kufanya kuwasilisha malalamiko yao, ikiwa wanaona wameonewa na si kupanga mkakati wa kumtoa madarakani wanayeamini anawakosea. Wana nafasi ya kukata rufaa,” alisema Dk Possi.

Profesa Tibaijuka alisema wakati Samwel Sitta akiwa Spika aliwatoa wabunge wasiofuata kanuni na hakukuwa na yanayotokea sasa, jambo linaloonesha kuwa wanamlenga Dk Tulia kwa sababu ni mwanamke.

Kakunda alisema anaamini pia kuwa maamuzi hayo ya kambi ya upinzani yana msukumo wa kisiasa kwa sababu hoja zao hazina msingi.

Kauli za Rais Magufuli Zawa Gumzo Nchini

$
0
0

Kauli mbalimbali zinazoendelea kutolewa na Rais John Magufuli, zimezua mjadala miongoni mwa wasomi nchini.

Kwa mfano, wanasema kauli ya kukosoa udahili wa wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) na ile ya kuelekeza hatua za kuchukua dhidi ya watu wanaotumia kimakosa barabara za Mabasi Yaendayo Haraka (Udart), inaashiria kuna tatizo kubwa la utendaji serikalini.

Walisema ni jambo lisiloingia akilini, wanafunzi wadahiliwe na kuanza masomo kisha baadaye wafukuzwe kwa maelezo kuwa Serikali haiwezi kulipia ada wanafunzi ‘vilaza’.

Akizungumzia kauli hizo jana, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Dk James Jesse alisema hakuna sheria za usalama barabarani zinazotamka mtu akifanya kosa gari lake litolewe magurudumu.

Juzi wakati akiweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa maktaba ya kisasa ya UDSM, Rais Magufuli alisema mpango maalumu uliopitishwa na Serikali ya Awamu ya Nne wa wanafunzi kusoma diploma ya ualimu Udom, unajumuisha waliofeli.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria (OUT), Hamad Salim alihoji: “Rais amesema wanafunzi waliopo Udom ni vilaza ila waziri wa elimu (Profesa Joyce Ndalichako) alisema wanafunzi wanaosoma mafunzo hayo hakuna aliyepata daraja la nne. Sasa hapo nani mkweli.”

“Kupishana huku kwa kauli kunatupa mashaka na utendaji kazi wa baadhi ya viongozi serikalini."

Hamad alisema suala kama hilo lilipaswa kutolewa ufafanuzi na waziri husika na si Rais.

Alisema umefikia wakati wa kiongozi huyo mkuu wa nchi kubaini changamoto na kutoa maelekezo na si kuzungumzia kila kitu.

Waziri Mpango Aomba Apewe Majina ya MAJIPU BoT

$
0
0

WAZIRI wa Fedha, Dk Phillip Mpango, amemtaka Mbunge wa Tabora Kaskazini, Almas Maige (CCM) kumpa ushahidi ikiwemo majina ya wafanyakazi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), aliowatuhumu kufanya biashara na mwajiri wao.

Dk Mpango alisema hayo Jumatano usiku alipokuwa akijibu hoja za wabunge kuhusu Bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango na kuongeza kuwa akipewa ushahidi huo, ataufanyia kazi.

Awali katika mchango wake, Maige alisema anao ushahidi wa maandishi (huku akiwa ameushika), unaoonesha kuwa kati ya mashirika ya umma yanayovunja Sheria ya Manunuzi, BoT ipo.

Alidai kuwa Sheria ya Manunuzi imetoa fursa ya kuanzishwa kwa vitengo na idara za manunuzi (PMU), lakini fursa hiyo imekuwa ikitumiwa vibaya na vijana wa vitengo, hivyo kuiibia Serikali.

Kwa mujibu wa madai ya Maige, katika benki hiyo kuna vijana wamefungua makampuni ambao wamekuwa wakiyatumia kuomba zabuni za benki hiyo na kuyalipa.

Mbali na tuhuma hiyo, Maige ambaye alitangaza maslahi kuwa yeye ni mkandarasi wa daraja la kwanza, alidai pia kuna vijana wengine wamekuwa wakitoa zabuni kwa kampuni za nje ya nchi, ili watumie zabuni hiyo kupata safari za nje.

Alidai kuwa vijana hao baada ya kutoa zabuni kwa kampuni za nje, hutengeneza safari za kwenda kufanya uhakiki (due diligence) katika nchi zinakotoka kampuni hizo, ambako huko hupokea rushwa.

Katika kuthibitisha hilo, Maige alidai kuwa vijana hao wamediriki kutoa zabuni kwa kampuni iliyofungiwa na Mamlaka ya Manunuzi ya Umma Tanzania (PPRA).

Akijibu hoja hiyo, Dk Mpango alisema tuhuma hizo ndio kazisikia bungeni, hivyo hana uhakika ila akipewa ushahidi ataufanyia kazi kwa kuwa, utumbuaji majipu umesaidia kuongeza mapato na kutoka mfano wa makusanyo ya Sh trilioni moja kila mwezi.

Hivi karibuni, Serikali ilisitisha utoaji wa Sh bilioni 925 zilizokuwa zimeidhishwa na BoT kwa ajili ya kulipa malimbikizo ya madeni ya Serikali.

Mbali na hilo, Serikali iliagiza Kitengo cha Madeni ya Nje ambacho awali kilikuwa chini ya BoT na baadaye kupelekwa wizarani, kirejeshwe mara moja ili kuimarisha udhibiti wa ukopaji na ulipaji wa madeni.

Kabla ya agizo hilo, ilielezwa kuwa malipo hayo yalikuwa yameidhinishwa na BoT kwa ajili ya kulipa malimbikizo ya madeni mbalimbali lakini Serikali ikaagiza fedha hizo zirejeshwe Wizara ya Fedha na Mipango kwa ajili ya kufanyiwa uhakiki upya.

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Jumamosi ya Juni 4

Vitisho Kwa Njia ya Simu Vyamfikisha Mahakamani.

$
0
0
Mkazi wa Kijiji cha Misasi Mariamu Nestory (20) amefikishwa Mahakama ya Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza kujibu shtaka la kutoa lugha ya vitisho kwa njia ya simu.

Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Doroth Mgenyi alidai kuwa Mei 2  saa 8:15 mchana,  mshtakiwa  huyo kwa kutumia simu  aliandika ujumbe wa vitisho kwa Diana Kabula kinyume cha sheria ya makosa ya mtandao kifungu 18 (1) ya mwaka 2015.

Alinukuu ujumbe huyo akidai:  “Ujiandae siku utakayoingia anga zangu, sali sala ya mwisho, ulisikia kisa cha Sengerema ndivyo nitakavyokufanya... ikishindikana kukuua kwa mikono yangu nitakuroga uwe kichaa.” 

Hata hivyo, mshtakiwa huyo alikana shtaka.

Mambo Mawili Yanayoibana Serikali Katika Mgogoro wa Wanafunzi 7000 Waliotimuliwa UDOM

$
0
0
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Kitilla Mkumbo amesema kuna mambo mawili yanayoibana Serikali katika mgogoro wa wanafunzi waliotimuliwa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom).

Akizungumza jana kwenye kipindi cha ‘Kipima Joto’ kinachorushwa na kituo cha luninga cha ITV, Profesa Mkumbo alisema Serikali haiwezi kukwepa lawama, kwa sababu ndiyo iliyoanzisha utaratibu wa kudahili wanafunzi wa kidato cha nne kupitia mfumo maalumu kabla ya kuanza kusoma shahada ya chuo kikuu.

Pia, alisema Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), haiwezi kuhusika moja kwa moja kwenye udhaifu uliojitokeza katika udahili wa wanafunzi hao, bali Seneti ya Udom inapaswa kuwajibika katika hilo.

Alisema kuna udhaifu wa kiutendaji kwa seneti hiyo yenye mamlaka ya kudahili wanafunzi wenye sifa ambayo iliiacha kazi hiyo  mikononi mwa TCU.

Mkumbo alisema kazi ya TCU ni kuidhinisha majina ya wanafunzi waliokwisha dahiliwa na chuo husika na si kuchagua.

“Chuo chochote ndicho kinachagua wanafunzi wenye sifa wanazozihitaji, inashangaza kuona Udom imefanyiwa kazi hiyo, baraza na seneti wanapaswa  kuwajibika kwanza, TCU haiwezi kukichagulia chuo wanafunzi,” alisema Profesa Mkumbo.

Hata hivyo, alitoa angalizo kwa Serikali kutodharau mfumo huo wa udahili kwa wanafunzi ambao hawakuhitimu Kidato cha Sita kama ilivyoamriwa na Serikali ya Awamu ya Nne, kuwa upo na unatumika duniani kote.

“Ila kama Rais (John) Magufuli hautaki na ameona turudi kwenye mfumo wa zamani ambao mwanafunzi anapaswa kufaulu  kidato cha sita ndiyo ajiunge na chuo kikuu sawa,  lakini atambue kuwa kuna hasara na faida zake, vyuo vingi vinaweza kufungwa,” alisema Mkumbo

Mbali ya mfumo huo, profesa huyo alisema upo mfumo mwingine wa udahili kwa mtu yeyote mwenye umahili katika taaluma yake kusoma shahada kwa kuzingatia vigezo maalumu vilivyowekwa.

“Ila hakuna jinsi, nadhani  TCU wamemsikia Rais kuwa hataki njia za mkato tena.”

Mei 29, Udom iliwasimamisha masomo zaidi ya wanafunzi 7,000 wa kozi maalumu ya ualimu wa sayansi kwa ngazi ya stashahada na kuwataka waondoke chuoni mara moja.

Amri hiyo iliyotolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, ilisema Serikali imeamua warejee kwao na wataelezwa mustakabali wao mapema iwezekanavyo.

Hata hivyo, Rais John Magufuli juzi alisema baadhi yao walikuwa vilaza, hivyo wajitafutie mahali pa kwenda huku wenye ufaulu wa daraja la kwanza na pili aliahaidi kuwa wataandaliwa utaratibu.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Ya Nchi , Hamad Yussuf Masauni Alalamikiwa na Wabunge Kwa Kutoa Majibu ya Dharau na Kiburi Kwa Wabunge

$
0
0
SIKU chache baada ya Rais John Magufuli kutengua uteuzi wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga kutokana na ulevi, Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Hamad Yussuf Masauni, ameshtakiwa kwa uongozi wa Bunge akidaiwa kutoa majibu ya dharau bungeni.

Wakati wizara hiyo bado haijapata Waziri tangu 'kutumbuliwa' kwa Kitwanga Mei 20, mwaka huu, katika Kikao cha 36 cha Mkutano wa Tatu wa Bunge la 11 mjini hapa, jana Mbunge wa Nkasi (CCM), Ally Keissy alisimama na kuomba mwongozo wa Spika akidai Mhandisi Masauni amekuwa akitoa majibu ya dharau kwa wabunge.
 
Keissy alidai Naibu Waziri huyo amekuwa akitoa majibu ya kejeli na kiburi na kwamba wabunge wengi hawaridhishwi na majibu yake.
 
"Nasimama kwa Kanuni ya 68(7), naomba mwongozo wako kuhusu majibu ya nyongeza aliyojibu Naibu Waziri, na tangu jana (juzi), amezoea kujibu kwamba wabunge watumie fedha za mfuko wa Jimbo kukarabati majengo ya polisi," Keissy alisema.
 
"Ndugu Mheshimiwa Naibu Spika, majengo ya Karando na Kabwe (jimbo la Nkasi) yamechakaa hata mfuko wa jimbo... nadhani Mheshimiwa Waziri hajui tunapata shilingi ngapi za mfuko wa jimbo kutosha kukarabati hayo majengo.
 
"Hayo majibu yanaridhisha? Anajibu kwa jeuri na kiburi. Kusema kweli wabunge haturidhishwi na majibu ya Naibu Waziri. Sikubalini na majibu ya aina hii. 
 
"Katika majibu ya msingi ya swali langu, wamesema serikali itakarabati majengo ya Kabwe, lakini anasema baadaye (kwenye swali la nyongeza) Mbunge akarabati majengo ya Kabwe, si dharau hii? Anataka kunichionganisha mimi na wananchi. Hili jibu sijaridhika nalo. Mnanijibu nikakarabati mimi. Sina uwezo."
 
Baada ya maelezo hayo ya Keissy, Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson aliyekuwa anaongoza kikao hicho, alisema atatoa mwongozo wake baada ya kupitia taarifa za Bunge (Hansard) kuhusu suala hilo.
 
"Waheshimiwa wabunge, ili nijue swali liliulizwa kwa namna gani na Mheshimiwa Naibu Waziri amelijibu kwa namna gani, mpaka nipitie taarifa za Bunge, yaani Hansard," alisema Naibu Spika. 
 
"Kwa hiyo, mwongozo huo nitautoa baada ya kupitia taarifa rasmi za Bunge kwamba swali liliulizwa vipi na majibu yametoka namna gani."
 
Ikiwa Kiti cha Spika kitabaini majibu ya Naibu Waziri hayakusadifu swali la Keissy, kitaagiza swali hilo lirudiwe kujibiwa kwenye kipindi cha maswali na majibu bungeni.
 
Uteuzi wa Kitwanga ulitenguliwa na Rais Magufuli ikiwa ni muda mfupi baada ya Mbunge huyo wa Misungwi (CCM) kuingia bungeni akiwa amelewa na kijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Devotha Minja lililoelekezwa kwenye Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
 
Kiti cha Spika kiliagiza swali hilo lirudiwe kujibiwa katika kipindi cha maswali na majibu bungeni Mei 23, baada ya Kitwanga kutoa majibu ambayo hayakuridhisha.

Hatimaye Rais Shein Amjibu Maalim Seif.......Asema Hamuogopi Kwa Sababu Hana Vifaru Wala Roketi za Kivita

$
0
0

MAKAMU Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amesema hakuna kiongozi yeyote wa kisissa nchini anayemuogopa.

Aidha, Dk. Shein ambaye pia ni Rais wa Zanzibar ameahidi kumchukulia hatua yeyote atakayevunja sheria za nchi.
 
Amesema kuna baadhi ya wananchi, hasa Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharrif Hamad, ambaye amekuwa akivunja sheria za nchi kwa makusudi huku akijisifu na kuona kama serikali inamuogopa jambo ambalo sio sahihi.
 
Makamu Mwenyekiti huyo alitoa msimamo huo wakati akizungumza na mamia ya viongozi wa CCM, wakiwemo Mabalozi, Wenyeviti na Makatibu wa Matawi na Maskani za Wilaya ya Mfenesini Kichama.
 
Mkutano huo ulifanyika katika Chuo cha Kumbukumbu cha Mwalimu Nyerere, Bububu nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
 
Dk. Shein alisema Zanzibar ina Rais mmoja ambaye ni yeye na kama kuna watu wanatamani nafasi hiyo ni lazima wachaguliwe kihalali.
 
Alikemea tabia za Maalim Seif ya kujaribu kila mara kuingiza nchi katika machafuko na aliahidi kuwa vyombo vya dola havitavumilia.
 
Alisema tayari dola inaendelea na taratibu za kisheria na endapo akitiwa hatiani atahukumiwa kisheria.
 
Maalim Seif alihojiwa na Polisi kwa saa tatu katikati ya wiki kabla ya kuachiwa kwa dhamana ya wadhamini wawili.
 
“Mimi simuogopi Maalim Seif kwani ni kiongozi wa kisiasa kama mimi, ila tofauti yetu ni kwamba mimi ni Rais wa Zanzibar na yeye ni kiongozi wa chama," alisema na kueleza "hivyo haniwezi kwa lolote."
 
"Kwa mambo anayofanya, endapo akishitakiwa na kutiwa hatiani ajue kwamba kisheria kosa lolote la jinai halifi na wakati wowote anaweza kukamatwa na kushitakiwa endapo mahakama ikiona kuna haja ya kufanya hivyo."

Dk. Shein alisema Maalim Seif hawezi kuogopwa kwani hana vifaru, roketi renja za kivita vya kuwatisha watu wamuogope.
 
Alisema sheria ndio kinga dhidi ya migogoro ya Zanzibar na kiongozi yeyote atakayejifanya mbabe, hata akiwa rais wa nchi, sheria zitamshughulikia.
 
Aliwaambia wananchi wa Zanzibar wanaoona Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 inavunjwa ama inataka kuvunjwa, wana haki ya kufungua mashtaka Mahakamani kwa mujibu wa kifungu cha 25 1(a).
 
Aidha aliahidi kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020 hadi ifikie asilimia 90 ili wananchi waendelee kupata maendeleo kwa wakati.
 
Dk. Shein alisema ahadi hiyo itatekelezwa kwa wakati endapo wananchi wataendelea kushirikiana vizuri na serikali katika shughuli na harakati mbali mbali za maendeleo ya nchi.
 
Rais shein alifafanua kwamba katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, CCM Zanzibar imetekeleza Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2010/2015 kwa asilimia 80.
 
Alisema kwamba mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mzuri baina ya wananchi na viongozi mbali mbali wa Chama na serikali kwenye kuharakisha maendeleo ya nchi.
 
Aidha aliwapongeza wafuasi wa CCM katika Wilaya hiyo kwa kuichagua kwa kura nyingi CCM, katika Uchaguzi wa Marudio wa Machi 20 na kupata ushindi wa zaidi ya asilimia 90.
 
Alisema kwamba ushindi huo ni taswira ya mafanikio ya Chama na serikali katika kuwatumikia wananchi kwa uadilifu mkubwa huku ikijipanga kuimarisha uchumi wa nchi kufikia uchumi wa kati.
 
“Uchaguzi Mkuu umekwisha hivyo kwa sasa tufanye kazi kwa pamoja kuendeleza maendeleo ya Zanzibar kwani kila jambo lenye tija na manufaa linahitaji umoja na ushirikiano kutoka kwa wananchi,” alisema Dk. Shein na kuongeza:
 
“Pia nakuombeni wafuasi wa CCM muendelee kuwa wavumilivu licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali za kisiasa kutoka kwa wapinzani.
 
"Jambo  hilo linatafutiwa ufumbuzi na vyombo vya kisheria." 

Dk. Shein alisema ataendelea kusimamia Sheria na Katiba ya Zanzibar kwa misingi ya uadilifu, lakini hatawavumilia watu wanaovunja sheria kwa makusudi.

Rais Magufuli Amuapisha Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

$
0
0
 TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 04 Juni, 2016 amemuapisha Mhe. Gerson John Mdemu kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Kabla ya kuteuliwa kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Gerson John Mdemu alikuwa Karani wa Baraza la Mawaziri (Cabinet Clerk)
 
Mhe. Gerson John Mdemu amechukua nafasi iliyoachwa wazi na Mhe. Dkt. Tulia Ackson ambaye ni Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
04 Juni, 2016

Rais Magufuli Akutana Na Kufanya Mazungumzo Na Kiongozi Wa Chama Cha Kikomunisti Cha China Luo Zhijun Ikulu Jijini Dar Es Salaam

$
0
0
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewaalika wawekezaji kutoka Jimbo la Jiangsu la nchini China kuungana na Tanzania katika utekezaji wa mpango wa ujenzi wa viwanda na ujenzi wa miundombinu hususani reli, na amewahakikishia kuwa serikali yake ya awamu ya tano itatoa ushirikiano wa karibu kufanikisha uwekezaji huo.

Rais Magufuli ametoa mwaliko huo leo tarehe 04 Juni, 2016 Ikulu Jijini Dar es salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na Kiongozi wa Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) wa Jimbo la Jiangsu Mheshimiwa Luo Zhijun ambaye yupo hapa nchini akiwa na viongozi wengine wa serikali wa jimbo hilo kwa ziara ya kikazi.

Dkt. John Pombe Magufuli amemueleza Mheshimiwa Luo Zhijun kuwa serikali yake ya awamu ya tano imedhamiria kuhakikisha asilimia 40 ya watanzania wanapata ajira kupitia viwanda ifikapo mwaka 2020, hivyo ili jitihada hizo zifanikiwe inawakaribisha wafanyabiashara wa Jiangsu kuanzisha viwanda vitakavyosindika na kuzalisha bidhaa za mazao ya kilimo na ufugaji yakiwemo pamba, kahawa, korosho, samaki na nyama kwa kuwa malighafi zipo na pia fursa za kupanua uzalishaji wa malighafi hizo zipo.

Amemhakikishia Kiongozi huyo wa Jimbo la Jiangsu ambalo lina viwanda vingi nchini China kuwa licha ya uwekezaji wa viwanda kuinufaisha Tanzania kwa wananchi wake kupata ajira na serikali kukusanya mapato, wawekezaji wa China watanufaika na fursa ya soko kubwa la ndani ya Tanzania na nchi saba zinazoizunguka Tanzania, Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) zenye watu zaidi ya milioni 650.

"Mheshimiwa Luo Zhijun naomba uwaeleze wafanyabiashara wa Jimbo lako la Jiangsu kwamba ninawakaribisha kwa mikono miwili, waje hata kesho waseme wanataka kuanzisha kiwanda gani na sisi tutawapa ushirikiano.

"Tunayo maeneo ya kutosha ya kuanzisha viwanda, kwa Pwani na Dar es salaam tuna eneo la Bagamoyo tunaloweza kuweka viwanda zaidi ya 1,000 halikadharika Kigamboni na maeneo mengine mengi katika mikoa mbalimbali nchini nzima" Amesema Rais Magufuli.

Rais Dkt. John Pombe Magufuli pia amemueleza Mheshimiwa Luo Zhijun kuwa serikali yake inayakaribisha makampuni ya Jiangsu kuungana na Tanzania katika ujenzi wa miundombinu ikiwemo ujenzi wa reli ya kati ambao tayari Tanzania imetenga shilingi Trilioni 1 kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) katika bajeti ijayo, ujenzi wa kilometa 1,200 za barabara ya njia sita kutoka Dar es salaam hadi Chalinze na miradi mingine.

Kwa upande wake Mheshimiwa Luo Zhijun amemshukuru Rais Magufuli kwa utayari wake wa kuwapokea wawekezaji kutoka Jimbo la Jiangsu na amemuahidi kuwa pamoja na kwamba Jimbo hilo tayari limewekeza hapa nchini kiasi cha dola za Marekani Bilioni 1 (Sawa na Shilingi Trilion 2.2) atahakikisha anawashawishi wawekezaji wengi zaidi wa viwanda katika jimbo lake,  kuja Tanzania haraka iwezekanavyo ili kufanikisha mpango wa kujenga viwanda na kuzalisha ajira.

Balozi wa China hapa nchini Dkt. Lu Youqing aliyeambatana na Mheshimiwa Luo Zhijun amemueleza Rais Magufuli kuwa pamoja na kuwekeza Dola Bilioni 1 kati ya Dola Bilioni 6.62 zilizowekezwa na China hapa nchini kwa mwaka 2014/2015 wawekezaji wa jimbo la Jiangsu wanakusudia kuwekeza Dola za Marekani Bilioni 5 (Sawa na Shilingi Trilion 11) nchini Tanzania katika miaka mitano ijayo.

Mazungumzo hayo yamehudhuriwa pia na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Bw. Paul Makonda ambaye jana tarehe 03 Juni, 2016 ametiliana saini makubaliano ya ushirikiano wa kimaendeleo kati ya Mkoa wa Dar es salaam na Jimbo la Jiangsu ambapo jimbo hilo limeahidi kuwekeza katika miradi mbalimbali ya viwanda vya mazao ya kilimo, ujenzi na huduma za kijamii.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
04 Juni, 2016

DC Kinondoni Awashukia Wahujumu Wa Miundombinu Ya Mwendokasi......49 Watiwa Mbaroni

$
0
0

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mh. Ally Hapi leo amekutana na kuzungumza na waandishi wa habari kuhusiana na tatizo la uhujumu wa miundombinu ya Mwendokasi.
 
Katika taarifa yake Mh. Hapi ameeleza kuwa katika kipindi cha siku mbili watu 49 wamekamatwa na polisi wilayani Kinondoni wakiwemo wamiliki wa magari, bajaji na bodaboda kwa makosa ya kuingilia miundombinu ya Mwendokasi kinyume cha sheria.

Kati yao watuhumiwa 43 watapelekwa mahakamani siku ya jumatatu ijayo hali inaowafanya kuyatumia mapumziko ya Juma wakiwa mahabusu.

Mh. Hapi amewataka wananchi wa Kinondoni na hasa madereva kufuata sheria, vinginevyo watakabiliana na rungu la dola.

Aidha, Mh. Mkuu wa Wilaya ameagiza Polisi wilayani Kinondoni kuendelea na zoezi la kuwakamata wale wote wanaogeuza vivuko vya barabara za DART kuwa sehemu za kulala na kujisaidia.

"Tumewaagiza Polisi kuwakamata wote wanaolala na kujisaidia kwenye vivuko vya barabara. Hata wale ambao wamesimama kule juu saa za usiku bila kazi yoyote wakamatwe na washitakiwe kwa sheria za uzembe na uzururaji. Wengine hawa ni vibaka na wengine ndio wanaolala na kujisaidia huko usiku." Alisema Hapi.

Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Magufuli akizungumza na wasomi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam alizungumzia juu ya uhujumu wa miundombinu ya mwendokasi na kuagiza watu hao kushughulikiwa ipasavyo.

Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa wilaya aliutaka uongozi wa DART kuchukua tahadhari za kiusalama katika vituo vya mabasi ili kuzuia uwezekano wa kutokea tishio la usalama.

Hapi aliwataka DART kuweka utaratibu wa kuwakagua abiria kwa mashine za mikono za ukaguzi ili kuhakikisha usalama wa wananchi wanaopanda mabasi hayo.

Kinondoni Yawafukuza Kazi Maofisa Watendaji 6 Kwa Tuhuma za Ubadhirifu wa Zaidi ya Sh. Milioni 400

$
0
0

Manispaa ya Kinondoni, imewasimamisha kazi maofisa watendaji sita, wakiwamo wanne wa kata na wawili wa mitaa kwa tuhuma za ubadhirifu wa zaidi ya Sh400 milioni.

Kati yao, watendaji wawili wa kata na mmoja wa mtaa wameshafukuzwa kazi, huku manispaa ikiendelea na uchunguzi.

Uamuzi huo ulitangazwa jana na Meya wa Manispaa hiyo, Boniface Jacob wakati akizungumza na maofisa watendaji wa kata 34 za manispaa yao. 

Jacob aliyeambatana na Mkuu wa Wilaya hiyo, Ally Hapi aliwataja waliofukuzwa kazi kuwa ni Ernest Missa, Ally Bwamkuu na Aneth Lema. 

Waliosimamishwa kazi ni Shaaban Kambi, Dustan Kikweshi na Richard Supu ambaye alikuwa anakaimu nafasi ya ofisa mtendaji wa kata.

“Hii ni aibu, Sh38 milioni hazionekani halafu meya yupo, kwa hali hii tutaoneana huruma kweli, sasa hivi hakuna kuchezeana ni muda wa kufanya kazi.

“Najua mtandao huu upo hadi makao makuu ya wilaya, ila niwaambie sasa hivi ukisimamishwa utahojiwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama itakayowashirikisha Takukuru na ukibainika unapelekwa mahakamani na Baraza la Madiwani linakufukuza kazi,” alisema Jacob.

Alifafanua kwamba kati ya fedha hizo Sh400 milioni kila mtendaji anadaiwa kutumia kiwango tofauti kwa nyakati tofauti, jambo ambalo linasababisha mgawanyo wa fedha kutofika ngazi ya chini kwa ajili ya shughuli za maendeleo.

“Ndiyo maana kila siku migogoro kati ya wenyeviti wa mitaa na maofisa watendaji haiishi, tatizo mojawapo ni hili. Tutaikomesha,” alisema Jacob.

Jacob alitumia nafasi hiyo kuwaagiza watendaji kukusanya kodi kwa ufanisi ili manispaa hiyo ifikie lengo la kukusanya Sh47 bilioni, kati ya Januari hadi Juni kutoka Sh39 bilioni ambazo zimekusanywa hadi sasa.

Alizitaja baadhi ya kata zilizoko nyuma katika ukusanyaji wa mapato kuwa ni Mburahati, Kibamba, Kimara, Mabibo na Mabwepande huku na kata za Msasani na Sinza zikiongoza katika ukusanyaji.

Mwenyekiti wa maofisa watendaji kata, John Njunde alisema maagizo yote watayafanyia kazi.

Mwenyekiti wa watendaji wa Mitaa, Suleiman Sangongh’o alisema mkutano huo unaowashirikisha viongozi wakuu wa manispaa unasaidia kuleta maendeleo ya halmashauri hiyo.

Tanzania Yatolewa na Misri Michuano ya AFCON 2017 Kwa Kipigo cha Mabao 2-0

$
0
0

Tanzania itaendelea kusubiri hadi mwaka 2019 kucheza fainali za mataifa ya Afrika (Afcon) baada ya hesabu zake za kuishinda Misri kwa mabao mengi kugoma na kuyeyuka kabisa kwa kipigo cha mabao 2-0 nyumbani.

Huku mashabiki wachache wa Misri waliojitokeza Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakibeba bango lenye kaulimbiu hiyo maarufu ya Rais John Magufuli ‘Hapa Kazi Tu’, waliitumia kuishangilia timu yao kila ilipoandika bao kupitia kwa mshambuliaji wao hatari aliyewahi kuichezea Chelsea ya England, Mohamed Salah, moja kila kipindi.

Ushindi huo umeirejesha kwenye ramani ya soka nchi ya Misri ambayo leo itafikisha miaka 41 kamili tangu icheze kwa mara ya kwanza dhidi ya Tanzania na kuambulia sare ya bao 1-1.

Timu hiyo, maarufu Mafarao imekuwa ya kwanza barani Afrika kufuzu kwa fainali zijazo zitakazofanyika Gabon mwakani, ikiwa na pointi 10 na kuziacha Tanzania na Nigeria zikisubiri Septemba 3 ili kucheza kwa kutimiza wajibu.

Misri, imecheza mechi 11 dhidi ya Tanzania ikiwamo mechi ya jana, imeshinda mara kumi na kupachika mabao 40, dhidi ya kumi ya Tanzania.

Hata hivyo, kama wasemavyo waswahili, sikio la kufa halisikii dawa baada ya nahodha Mbwana Samatta kupoteza nafasi adhimu kuandika bao kwa mkwaju wa penalti uliopaa, dakika ya 53 ya mchezo huo. 

Penalti hiyo ilitokana na Amri Warda aliyeingia kipindi cha pili kumuangusha kiungo Himid Mao katika eneo la hatari.

Salah anayeichezea klabu ya AS Roma ya Italia alifunga bao la kwanza, dakika ya 43 kwa mpira wa adhabu ndogo iliyokwenda moja kwa moja wavuni baada ya beki Haji Mwinyi kumfanyia madhambi Mohamed Elneny, kiungo wa Arsenal ya England, nje kidogo ya 18.

Kuingia kwa bao hilo kulisababisha mashabiki wachache wa Misri kushangilia kwa nguvu huku wakitumia bango hilo la ‘Hapa Kazi Tu’.

Salah aliyekuwa mwiba mkali kwa mabeki wa Taifa Stars ambayo sasa watasubiri kwa miaka 38 kucheza Afcon, aliipatia timu yake bao la pili kwa shuti kali baada ya kuwatoka mabeki wa Tanzania waliozubaa kuokoa mpira.

Misri iliyohitaji sare ya aina yoyote katika mchezo huo wa jana ilipata ushindi huo ambao ni faraja kubwa kwao baada ya kukosa fainali hizo kubwa Afrika tangu mwaka 2010. Mafarao hao wamefuzu moja kwa moja wakiwa na pointi 10 kutoka kundi G.

Katika mchezo huo wa jana,Taifa Stars ilionekana kukamatwa zaidi katika eneo la kiungo kutokana na Misri ikiongozwa na kiungo wa Arsenal Mohamed Elneny kutawala kwa muda mrefu wa mchezo, Kocha Charles Mkwasa alishindwa kusoma vyema wapinzani wake. 

Kocha huyo alifanya mabadiliko kwa kuwatoa Elius Maguli, Haji Mwinyi na Thomas Ulimwengu na nafasi zao kuchukuliwa nao, John Bocco,Mohamed Hussein na Deus Kaseke, mabailiko ambayo hayakuisaidia chochote timu hiyo.

Awali, Stars ilianza mchezo kwa kasi na matumaini makubwa na katika dakika ya 19, Samatta alikosa bao baada ya beki wa Misri Ahmed Hegazy kuokoa mpira huo.

Dakika ya 28, Krosi ya Himid Mao ilitua kichwani mwa Thomas Ulimwengu ambaye hata hivyo alipiga kichwa kilichookolewa kistadi na kipa wa Misri, Essam El-Hadary. Nusura Samatta awainue vitini Watanzania dakika ya 30 baada ya kuachia shuti kali, lakini beki wa Misri aliokoa na kuwa kona tasa.

Walimu 5 Waishi Darasani Kwa Miaka Mitatu

$
0
0

FAMILIA tano za walimu wa shule ya sekondari Shishani Kata ya Migato Halmashauri ya Itilima Mkoani Simiyu, zinaishi jengo la utawala tangu mwaka 2013.

Hali hiyo inatokana na ukosefu wa nyumba za walimu ambapo sasa shughuli za utawala shuleni hapo zinafanyika chini ya mti.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Tito Kwilasa alisema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari, waliofika shuleni hapo kwa ajili ya kikao cha maendeleo ya kata kilichojadili changamoto mbalimbali zilizopo.

Kwilasa alibainisha kuwa shule hiyo yenye wanafunzi 160, iliyoanzishwa mwaka 2007 ina uhaba mkubwa wa nyumba za walimu.

Nyumba za walimu zilizopo shuleni hapo ni mbili wakati kuna walimu 15 walioajiriwa, ambapo wanawake ni watatu na wanaume 12. Kwa sasa walimu hao wanaishi jengo la utawala, ambapo shule ina madarasa manne na maabara iliyofikia usawa wa madirisha.

‘’Kipindi cha mvua za masika inabidi kutoa darasa moja likachanganywe na lingine ili walimu tukakae darasani na kufanya shughuli za utawala huku wanafunzi hao wakikosa masomo,” alisema.

Alisema kuwa kipindi cha nyuma walimu walikuwa wachache, hivyo walibanana katika nyumba hizo mbili. Mwaka 2013 walimu waliongezeka, hivyo waligeuza jengo la utawala kuwa nyumba ya kuishi. Mwalimu mmoja alisema ni kero kubwa kwa familia hizo kuishi jengo la utawala ambalo pia halina vyoo.

Diwani wa Kata hiyo, Mbuga Ntobi alieleza kuwa watahakikisha walimu wanajengewa nyumba ili waishi katika mazingira ya ufundishaji.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Itilima, Kelisa Wambura alithibitisha kuwepo kwa hali hiyo. Alisema halmashauri imepanga kwenye bajeti ya 2016/17 kupunguza uhaba wa nyumba za walimu, hasa shule ya sekondari Shishani.

Auawa kwa Kuchomwa Moto Jijini Mwanza Baada ya Kupora Simu Aina ya Tecno

$
0
0

Watu watatu wamefariki dunia katika matukio tofauti, akiwamo aliyeuawa kwa kipigo na kuchomwa moto kwa tuhuma ya kupora simu ya mkononi aina ya Tecno.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alisema Juni 2, mtu huyo ambaye jina lake halikupatika anayekadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 25 hadi 30, aliuawa baada ya kumpora simu mpitanjia eneo la Ngaza, Kata ya Nyegezi jijini Mwanza.

“Kabla ya kupora simu mtu aliyejulikana kwa jina la Aanicia Rwezaura alitishwa na yule aliyeuawa kwa panga, lakini wananchi wenye hasira kali walimwandama, kumpiga na hatimaye kumchoma moto hadi kufa,” alisema Kamanda Msangi 

Katika tukio jingine, kamanda huyo amesema watu wawili wamefariki dunia na wengine wanne kujeruhiwa katika ajali ya gari iliyotokea Kijiji cha Isunganh’olo wilayani Sengerema.

Aliwataja waliofariki kuwa ni dereva wa gari aina ya Toyota Prado, Samson Kasala na mwendesha baiskeli, John Manyilizu aliyekuwa akipita pembezoni mwa barabara.

“Gari hilo lililokuwa kwenye mwendo kasi lilipasuka gurudumu na kuacha njia kabla ya kupinduka na kusababisha vifo na majeruhi,” alisema Msangi 

Waliojeruhiwa katika ajali hiyo ni Mandago Misana, Thobias Kitenge, Jesca Andrew na Mehob Peter ambao wamelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Sengerema kwa matibabu.

Kamanda Msangi aliwataka madereva kuwa watulivu barabarani na kuzingatia sheria za usalama barabarani na kuwaonya wale wasiozizingatia kwamba watabanwa kisheria.

Alisema mwendokasi umekuwa chanzo cha ajali nyingi za barabarani ambazo iwapo wahusika wangekuwa makini zingeweza kuepukika.

9 Waachiwa Huru Mauaji Ya Watu Watatu Msikitini Jijini Mwanza

$
0
0
Watu kati ya 14 waliokuwa wameshikiliwa na polisi kwa tuhuma za mauaji yaliyotokea katika msikiti wa Rahman, Mkolani jijini Mwanza wameachiwa huru baada ya kuonekana hawana hatia.

Akizungumza na nyumbani kwao mtaa wa Nyanghingi jana, mmoja wa watu hao, Hamidu Said (31) alisema akiwa na wenzake tisa, waliachiwa Mei 30 baada ya kuonekana hawahusiki katika tukio hilo.

Said alikamatwa Mei 18, muda mfupi baada ya kufika eneo la tukio kushuhudia mauaji hayo.

“Kati ya watu tisa tulioachiwa, wanaume tulikuwa watano, wanawake wawili na watoto wawili mmoja akiwa na miaka 13, mwingine 16,” alisema Said.

“Sikuamini kama natoka rumande, ila namshukuru Mungu kwa jinsi alivyonitetea hadi kuona sina hatia,” alisema.

Akizungumzia tukio la mtoto wake kukamatwa, baba wa Hamidu, Said Bahebe, alisema ni vigumu kuelezea mshtuko na machungu waliyoyapata baada ya kijana wao kukamatwa na polisi, hivyo alilazimika kumuombea dua kwa kuachiwa baada ya kukutwa hana hatia.

Alisema kama ambavyo hawakuamini siku waliposikia kijana wao amekamatwa wakati ameenda kushuhudia tukio, kadhalika hawakuamini kuona anaruhusiwa kurudi nyumbani.

“Hatukutegemea kama angetoka ndani mapema,” alisema.

Bahebe alisema kwa siku 13 alizokaa rumande kijana wake, familia haikuwa na amani na ilikosa raha wakidhani ataishia jela.
 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahamed Msangi alisema wamewaachia watu hao ambao walionekana hawana hatia, lakini bado wanafuatilia wengine ambao wanaonekana kuhusika na tukio hilo bila ya kutaja idadi ya watu waliochiwa.

“Wapo baadhi walioachiwa, wengine watafikishwa mahakamani wakati wowote baada ya kuona ushahidi una kila aina ya dalili za kuhusika na tukio hilo,”alisema Msangi.

Katika mauaji hayo, watu watatu waliuawa kwa kukatwa mapanga wakiswali msikitini akiwamo Imamu wa Msikiti wa Rahman, Feruz Ismail (27), Mbwana Rajab (40) na Khamisi Mponda (28).

Ilielezwa kuwa kabla ya kuanza kuwashambulia waumini kwa mapanga, wavamizi hao waliamuru watoto waliokuwamo msikitini humo kutoka nje kupitia mlango wa nyuma unaotumiwa na wanawake.

Katika tukio hilo, mtoto Ismail Abeid (13) alinusurika baada ya kupita kwenye mlango mwingine, tofauti na ule ambao wavamizi walielekeza utumike ambako walijeruhiwa kwa kukatwa na mapanga vichwani walipopita.

Familia za Watu 8 Waliouawa Kwa Kuchinjwa Tanga Kujengewa Nyumba

$
0
0

Wabunge wa majimbo ya Mkoa wa Tanga wameahidi kujenga nyumba nne kwa ajili ya makazi ya kaya ambazo ndugu zao waliuawa kwa kuchinjwa na watu wasiojulikana katika kitongoji cha Kibatini, Jumanne ya wiki iliyopita.

Wakazi hao walihamia katika eneo la Kona Z baada ya ndugu zao wanane kuchinjwa na watu hao katika tukio linaloonekana kama kulipiza kisasi baada ya wakazi hao kuwaripoti polisi watoto wanane walioonekana kwenye kitongoji chao na kutiliwa shaka.

Wabunge waliahidi kujenga nyumba hizo baada ya kukuta familia hizo zikiishi katika mazingira magumu kwenye makazi yao mapya huku vyombo vyao vikihifadhiwa uwanjani.

Walitoa ahadi hiyo jana walipokwenda kutoa rambirambi kwa familia hizo.

Wabunge hao wote wakiwa wa CCM ni Adadi Rajabu wa Muheza, Jumaa Awesso na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.

“Hii haiwezekani, binadamu hawezi kuishi katika mazingira kama haya, hawa wananchi wapo katika machungu ya kufiwa, inatia simanzi kuona wamehamia huku, lakini hawana pa kuishi,” alisema Ummy ambaye pia ni mbunge wa viti maalumu.

Alisema wabunge wa mkoa wa Tanga kupitia CCM watajenga nyumba nne Kona Z kwa ajili ya familia hizo, wakiwamo ndugu watatu wa familia moja ya marehemu Issa Hussein aliyekuwa mwenyekiti wa kitongoji.

“Tumekubaliana kwamba ujenzi huu utaanza mara moja wiki ijayo na tunataka nyumba zikamilike haraka ili wafiwa hawa waondokane na adha ya kukosa makazi,” alisema Awesso ambaye ni Mbunge wa Pangani.

Awesso aliitaka Serikali kuhakikisha inalinda maisha ya wakazi wa maeneo hayo pamoja na kufanya uchunguzi utakaowezesha kuwanasa walioshiriki mauaji hayo.

Wafiwa hao waliwaomba wabunge kuvishinikiza vyombo vya ulinzi na usalama kuweka ulinzi katika eneo hilo ili wasichinjwe watu wengine kwa kuwa bado wana hofu kwamba wanaweza kufuatwa.

“Kama mnavyoona tumekuja huku sisi kama tulivyo, tumeacha kila kitu Kibatini, mazao mashambani na mifugo tumeamua kukimbia ili kuokoa maisha yetu kwa hivyo tunakabiliwa na ukosefu wa chakula,” alisema Mwanaisha Hassan.

Polisi Jijini Mwanza Waua Jambazi Mmoja Usiku Huu.......Jambazi Mwingine Akimbia, Polisi Mmoja Ajeruhiwa

$
0
0

Polisi mkoani Mwanza wamemuua jambazi mmoja baada ya kujibizana kwa risasi mida  ya  saa 7 ( saba ) usiku 

Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Ahmed Msangi ambaye alikuwa  kwenye eneo la tukio, amesema katika tukio hilo, askari mmoja amejeruhiwa kwa kupigwa risasi mguuni na jambazi huyo aliyeuawa ambaye alikuwa na mwenzake anayedaiwa kukimbilia kwenye majabali ya mawe.

Amesema majibizano hayo yalianza saa 6.20 katika Mtaa wa Utemini, baada ya polisi waliokuwa doria kufuatilia nyendo za watu hao.

“Tulipokea taarifa kutoka kwa raia  wema kuwa katika eneo hilo kuna watu wanaowatilia shaka, ndipo askari wakaamua kuwafuatilia. "

Hata hivyo, amesema wamefanikiwa kukamata bastola moja iliyokuwa ikitumiwa na jambazi huyo.

“Unasikia milio hiyo ya risasi, askari wanaendelea kumsaka huyo mmoja aliyejificha kwenye mawe, naimani tutampata tu na hatuondoki hapa mpaka tumtie mikononi,” alisema Msangi na kuongeza:

“Hawa ni majambazi sugu ambao walikuwa wakituhumiwa kufanya matukio ya uporaji na mauaji jijini hapa, tulikuwa tukiwasaka kwa muda mrefu.”

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Jumapili ya June 5

CHADEMA Kuishitaki Serikali Kwa Wananchi

$
0
0

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimetangaza kuanza ziara ya kuishtaki Serikali kwa wananchi kuhusiana na utumbuaji majipu usiofuata maadili ya kazi na kutoonyeshwa kwa matangazo ya moja kwa moja ya televisheni ya vikao vya Bunge.

Mratibu wa ziara hiyo, Singo Benson alisema ziara itaanza Juni 7 katika Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga na kuendelea mikoa mingine, lengo ni kuelimisha wananchi juu ya ubakwaji wa demokrasia.

“Wananchi wananyimwa haki ya msingi ya kutoona matangazo ya Bunge moja kwa moja na hakuna sababu ya msingi iliyotolewa, hivyo lazima tuwaelimishe na tuwatetee wananchi haki zao,” alisema Benson.

Aliongeza kuwa katika utumbuaji majipu unaofanyika, umekuwa kwa asilimia kubwa ukilenga majipu madogo (viongozi wa chini) na kuacha viongozi wakubwa mafisadi bila kuchukuliwa hatua yoyote.

Benson alitoa mfano wa ubakwaji wa demokrasia akisema ni kitendo cha Serikali kuingilia mihimili mingine, Bunge na Mahakama, ambapo kwa Bunge Serikali ina daiwa kuingilia uchaguzi wa mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali(PAC) ambaye anatakiwa kutoka kambi ya upinzani.

Alisema ziara hiyo itakayojumuisha Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji itakuwa na awamu nne nchi nzima huku wabunge wote na wajumbe wakuu wa chama watashiriki, akiwamo aliyekuwa mgombea urais 2015, Edward Lowassa.

Awamu ya kwanza itakayochukua siku 14 itaendelea kwa kugawana maeneo na kundi moja la viongozi wa Chadema litaenda maeneo ya Chato, Katoro, Busanda, Biharamulo, Muleba, Bukoba Mjini, Karagwe, Ngara na Geita; Kundi la pili Shinyanga mjini, Meatu, Maswa, Bariadi, Lamadi, Musoma Mjini, Bunda, Tarime na kuhitimisha Mwanza Mjini.

Benson ambaye pia ni Mkurugenzi wa Uratibu na Mafunzo wa Chadema, alieleza kuwa awamu ya pili itahusisha nyanda za juu kusini na kati, awamu ya tatu itakuwa mikoa ya kaskazini na kusini na kuhitimisha jijini Dar es Salaam.

“Ziara hizi zinawakaribishwa wabunge na wanasiasa wa vyama vyote wenye lengo la kutetea haki za wananchi kwa viongozi waliowachagua,” alieleza Benson.
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live




Latest Images