Quantcast
Channel: MPEKUZI
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live

Wakunga Wazembe Kufutiwa Leseni

$
0
0
Wakunga wanaokiuka maadili ya kazi ikiwemo kuwatolea wajawazito maneno ya kashfa na kejeli, wametangaziwa ‘kiama’ baada ya serikali kuagiza Baraza la Wakunga kuhakikisha wanaobainika, wanafutiwa leseni.

Aidha, serikali imeamua kuanzia mwaka ujao wa fedha, halmashauri zote zitapaswa kuorodhesha idadi ya watakaopoteza maisha wakati wa kujifungua sanjari na sababu za vifo na kama upo uzembe, ifahamike mtu wa kumwajibisha.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema hayo jana kwenye maadhimisho ya Siku ya Wakunga Duniani yaliyofanyika jijini Dar es Salaam. 

Alisema ingawa wapo wakunga wengi wazuri na waadilifu, wapo wachache wasio waadilifu ambao amesisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli haitawavumilia.

“Ukweli ni kuwa wakunga wengi ni wazuri na waadilifu, kwani wanafanya kazi katika mazingira yenye changamoto nyingi. Lakini wapo wachache ambao siyo waadilifu, … wakumbusheni wanachama wenu maadili ya kazi zao mara kwa mara, ” alisisitizia Baraza la Wakunga.

Katika maadhimisho hayo yenye kaulimbiu ya ‘Wanawake na watoto mhimili wa wakunga’, Waziri alisema ili kuwawajibisha wakunga wenye tabia hizo, ni vyema wananchi wanaofanyiwa ukatili kuwataja wahusika moja kwa moja badala ya kuunganisha wakunga wote kwenye kituo husika.

Alisema katika masomo ya ukunga, wanataaluma hao wanafundishwa jinsi ya kuhudumia mjamzito. “Anayeona hawezi kazi hiyo ni vyema kuacha na kutafuta kazi nyingine,” alisema.

Alisema serikali haitamwonea huruma yeyote atakayesababisha vifo kwa wajawazito. Alisema watapitia halmashauri zote kuangalia zilivyotenga bajeti kwa ajili ya kukabili vifo hivyo.

Alifafanua kuwa pamoja na wakunga kukabiliwa na mzigo mzito wa kufanya kazi katika mazingira magumu ya ukosefu wa vitendea kazi, kuhudumia wajawazito wengi kuliko viwango vinavyotakiwa, hiyo si sababu ya kufanya vitendo hivyo vya ukatili kwa wajawazito.

Waziri alikiri wanataaluma hao kukabiliwa na changamoto kwa kusema, kwa sasa mkunga mmoja anahudumia wajawazito kati ya 10 na 80 wakati viwango vya kawaida inapaswa mkunga mmoja kuhudumia mjamzito mmoja hadi sita.

Hata hivyo alisema, kuanzia mwaka ujao wa fedha, serikali itaongeza idadi ya wanafunzi wanaojiunga kusomea masuala ya ukunga ikiwa ni pamoja na kuongeza ajira kwa wakunga serikalini.

Marekebisho elimu ya ukunga
Akizungumzia ubora wa elimu kwa wakunga, alisema wameanza kufanyia marekebisho kwani baadhi ya mambo yanatokea kutokana na kutoa elimu kwa muda mfupi wa miaka miwili tofauti na ilivyokuwa awali miaka minne.

“Hivyo tumeanza kuboresha utoaji wa elimu kwa kushirikiana na Baraza la Wakunga na tayari imefika Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) ambapo majadiliano yanaendelea na watakapokamilisha, suala la mishahara nalo litaangaliwa kwa watakaosoma miaka mingi tofauti na sasa,” alisema.

Awali Mkurugenzi wa Chama cha Wakunga Tanzania (Tama), Feddy Mwanga alisema kwa sasa wana matawi 23 na wanachama 4,000 . 

Alisema serikali itakapowekeza kwa wakunga kwa kuwapa utaalamu wa stadi zote zinazotakiwa watapunguza vifo vya wanaojifungua kwa asilimia 70.

Alisema mkunga akipata utaalamu huo ana uwezo wa kumhudumia mjamzito kwa asilimia 87 na zinazobaki ni kwa wachache wanaotakiwa kufanyiwa upasuaji.

“Hivyo tunaona ni vyema kuangalia upya elimu ya uuguzi na ukunga iliyopunguzwa kutoka miaka minne hadi miwili kwani muda hautoshi kumtengeneza mkunga ipasavyo,”alisisitiza.

Alisema Tama inasikitishwa na tabia ya wakunga wachache wanaokiuka maadili kwa kutoa huduma isiyostahili. Alisema wataendelea kuwachukulia hatua watakaobainika.

Hata hivyo, akizungumzia changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwemo lawama na tuhuma kwa wakunga, alisema wakati mwingine hutokana na uelewa mdogo wa huduma za afya ya uzazi.

Alitoa mfano wa tukio la hivi karibuni lililoripotiwa kwenye baadhi ya vyombo vya habari; ambalo mjamzito alilalamika kutupiwa mtoto kifuani baada ya kujifungua, alisema haikuwa unyanyasaji bali ni suala la kitaalamu.

“Tunaomba wananchi watutie moyo kwa kazi nzito tunayofanya na wasitupige pale kunapotokea tatizo kwani wakati mwingine ni kutokana na uelewa wa kazi yetu kama ilivyokuwa kwa mama aliyewekwa mtoto kifuani,” alisema.

Alikiri kwamba bado hawajaelimisha kuhusu suala hilo la kuweka kifuani mtoto anayezaliwa kwa ajili ya kumpatia joto jambo ambalo lilitafsiriwa na mama huyo kuwa ni unyanyasaji

Barabara za mchepuko Dodoma zitajengwa miaka 100 ijayo

$
0
0

WIZARA ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano imesema ina mpango kabambe wa kujenga barabara za mchepuko katika Manispaa ya Dodoma na nje ya hapo katika kipindi cha miaka 100 ijayo.

Akizungumza bungeni Dodoma jana, Naibu Waziri, Edwin Ngonyani alisema utekelezaji wa ujenzi wa barabara hizo utaanza rasmi pindi fedha zitakapopatikana.

Ngonyani alikuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Felister Bura (CCM) aliyetaka kujua hatua zilizoanza kuchukuliwa hadi sasa na Serikali kutokana na ahadi aliyoitoa Rais John Magufuli wakati alipokuwa Waziri wa Ujenzi ya kujenga barabara za mchepuko katika manispaa hiyo.

Aidha, Bura alitaka kufahamu ni lini ujenzi wa barabara maarufu ya Great North ambayo hadi sasa ni sehemu ya Tanzania pekee ndio haijakamilika, itakamilika lini.

Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri huyo alimtaka mbunge huyo asiwe na wasiwasi kwa kuwa aliyetoa ahadi ya ujenzi wa barabara hizo za mchepuko wakati akiwa Waziri wa Ujenzi ndiye Rais wa Tanzania.

“Labda nikujulishe tu hapa nina ramani, tayari kuna mpango kabambe wa kujenga barabara za mchepuko ndani na nje ya manispaa ya Dodoma katika kipindi cha miaka 100 ijayo,” alisisitiza.

Alisema katika mpango huo kwa mji wa Dodoma kutakuwa na barabara nane za mchepuko zenye urefu wa kilometa 147.

Akijibu swali la Barabara ya Great North, Waziri huyo alisema kipande cha barabara yenye urefu wa kilometa 8.65 eneo la Msalato ni sehemu ya barabara ya Dodoma-Kondoa-Babati yenye urefu wa kilometa 251. Alisema barabara hiyo inaendelea kujengwa kwa kiwango cha lami na imegawanyika katika sehemu tatu.

Waziri Mkuu Asema Ahadi zote Zilizotolewa Wakati wa Kampeni Zitatekelezwa

$
0
0
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesisitiza kuwa ahadi zote zilizotolewa kipindi cha kampeni mwaka jana pamoja na zilizoko kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), zitatekelezwa kama zilivyoahidiwa.

Pia amesisitiza kuwa kupitia ahadi hizo, wamedhamiria kutekeleza kwa vitendo ujenzi wa barabara zote kwa kiwango cha lami na kwa sasa wanatarajia kuanza na barabara zinazounganisha mikoa.

Kauli hiyo ilitolewa na kiongozi huyo bungeni Dodoma jana wakati akijibu swali la Mbunge wa Nachingwea, Hassan Masala (CCM) aliyebainisha kuwa katika moja ya ahadi zilizopo kwenye ilani ya CCM ni pamoja na ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami.

Mbunge huyo alihoji, je Serikali ya Awamu ya Tano imejipangaje katika kutekeleza ahadi hiyo? Akijibu swali hilo, Majaliwa alisema CCM kupitia ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2015, imebainisha ahadi mbalimbali ambazo chama hicho kimeamua zitekelezwe katika kipindi cha miaka mitano.

Alisema pamoja na ahadi ya ujenzi wa barabara katika kiwango cha lami, ahadi zote zilizomo kwenye ilani hiyo zitatekelezwa kama zilivyoahidiwa. 

“Ni kweli kwamba tumedhamiria kujenga barabara zetu kwa kiwango cha lami. Na tumeanza na mkakati wa kuunganisha barabara kwa ngazi ya mikoa, tukishakamilisha tunaingia kwenye barabara zinazounganisha wilaya,” alisema. 

Alisema pia barabara zote zilizoainishwa katika ilani hiyo ya CCM katika awamu hiyo ya tano, zitakamilishwa kupitia bajeti itakayopitishwa na Bunge hilo ya mwaka 2016/17.

“Naomba niwashawishi waheshimiwa wabunge muipitishe bajeti hii ili tuweze kukamilisha barabara ambazo mmezitaja sana humu ndani. Pale ambapo barabara za mikoa hazijakamilika tunataka tuzikamilishe,”alisema.

Wabunge wa UKAWA Wamzomea Profesa Tibaijuka huku Wakimwita Mwizi.......Ni Baada Ya Kupingana na Hoja za Tundu Lissu Aliyedai Zanzibar Ni Koloni La Tanganyika

$
0
0
Mbunge wa Muleba Kusini (CCM), Profesa Anna Tibaijuka jana alikuwa mkali bungeni akisema yeye si mwizi na kuwabeza wanaomuita hivyo kuwa wataisoma namba.

Profesa Tibaijuka alifikia hatua hiyo baada ya kuhamaki kutokana na baadhi ya wabunge wa upinzani kupaza sauti na kumuita mwizi wakati akichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria.

Profesa Tibaijuka alianza kwa kuwataka wabunge wamuunge mkono Rais John Magufuli kwa kuwa amechaguliwa na wananchi.

“Wenzetu ambao kazi yao ni kuja kutusimamia sisi (upinzani) wana haki ya kusema wanayoyasema, lakini hata sisi tuna haki ya kuyaweka vizuri ili yaeleweke kwa wananchi,” alisema.

Profesa Tibaijuka alisema upinzani ukifilisika utabaki kukemea kwa sababu ni lazima tu useme kitu, Bunge linageuka kijiwe na bungeni si mahali pa kupeleka hoja za vijiweni.

Kauli hiyo iliwakera wabunge wa upinzani ambao walianza kupaza sauti zao dhidi yake, hali iliyoonekana kumchanganya.

Akirejea hotuba ya msemaji wa kambi ya upinzani bungeni, Tundu Lissu kuwa Tanganyika inainyonya Zanzibar na kuifanya koloni lake, Profesa Tibaijuka alihoji: “Tanganyika inainyonya Zanzibar katika lipi? Hili ni jambo la kujiuliza. Nimejiuliza mimi kama mchumi. Kazi yangu ya kwanza nyinyi mnanijua nilikuwa kwenye shirika la makazi duniani, hamjui kwamba nilikuwa kwenye Shirika la Biashara la Dunia?” alihoji.

Kutokana na zomeazomea kuendelea, Spika wa Bunge, Job Ndugai aliingilia kati: “Waheshimiwa wabunge namlinda mzungumzaji, naomba muwe wavumilivu. Mheshimiwa Profesa endelea."

“Kwa wale wanaosema nimeiba mtaisoma namba, mimi si mtu wa kutishwa na vitu vya ovyoovyo.

"Mimi sitishwi na hoja za ovyoovyo, huyo (mtu) akaisome namba. Nasimama hapa kwa sababu nataka nitetee vitu. Mtu anapopotosha anaweza kuleta hatari. Tanganyika kwa mtizamo wa kiuchumi haiwezi kuinyonya Zanzibar.

“Katika Dunia ya ustaarabu unasikia hoja. Lissu hapa angeweza kuzomewa, lakini wastaarabu wakamsikiliza wamekomaa kisiasa,” alisema huku baadhi ya wabunge wakiendelea kumzomea.

Tibaijuka aliwahi kuwa waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi wakati wa utawala wa Rais Jakaya Kikwete na aliondolewa baada ya kutuhumiwa kupata mgawo wa fedha za Tegeta Escrow.

Waziri Mkuu: Mamlaka ( halmashauri ) kusimamia uwekezaji wake Ili Zinufaike na Uwekezaji Huo

$
0
0

SERIKALI inaandaa utaratibu utakaowezesha mamlaka husika zikiwemo halmashauri kusimamia zenyewe uwekezaji wake katika maeneo yao ili zinufaike na uwekezaji huo. 

Imesema imeamua kuchukua hatua hiyo mara baada ya kubaini kupitia mapitio katika eneo la uwekezaji na kubaini mapungufu yaliyopo katika eneo zima la uwekezaji.

Akijibu swali la Mbunge wa Temeke, Abdallah Mtulia (CUF) bungeni jana, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema utaratibu huo utatoa fursa kwa mamlaka zenyewe kusimamia uwekezaji katika maeneo yake na kunufaika zaidi kuliko sasa.

Katika swali la Mtulia, alitaka kufahamu kwa nini Serikali isiipatie Halmashauri ya Temeke hisa ya angalau asilimia 10 kutokana na uwekezaji wa Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji (EPZA) kutokana na halmashauri hiyo kutoa ardhi yake yenye thamani ya Sh bilioni 100.

“Mheshimiwa Waziri Mkuu kitendo cha halmashauri kutegemea tu tozo ya mali na huduma kupitia mradi huu ni uonevu kwani, ardhi ile uliopo mradi wa EPZA ina thamani ya Sh bilioni 100,” alisema.

Akijibu swali hilo, Majaliwa alikiri kuwa kwa sasa Serikali imefungua wigo mkubwa wa uwekezaji ambao unatumia njia mbili kupitia Kituo cha Uwekezaji (TIC) na halmashauri.

 Alisema uwekezaji kupitia TIC ambayo inayo benki yake ya ardhi ambayo pia hutolewa na halmashauri husika ambayo yenyewe hunufaika kwa tozo pekee.

Alisema uwekezaji mwingine ni kupitia halmashauri yenyewe kuwa na benki yake ya ardhi na hivyo kuamua kutafuta mwekezaji. Hunufaika kwa kupata tozo na kuwa mwanahisa kupitia mradi husika.

TCRA : Watumiaji Simu FEKI wazidi Kupungua Kutoka asilimia 30 hadi 13

$
0
0

Kadri siku ya kuzima simu feki kote nchini inavyokaribia imebainika kuwa wanaozitumia wanazidi kupungua nchini.

Meneja Mawasiliano wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Mawasiliano Tanzania (TCRA), Innocent Mungy amesema tangu ilipotangaza mwaka jana kuwa itazima simu feki ifikapo mwishoni mwa Juni, idadi ya watumiaji imepungua kutoka asilimia 30 hadi 13.

Alisema wakati wa uhakiki wa matumizi ya simu feki Desemba mwaka jana, mamlaka hiyo ilibaini kuwapo asilimia 30 ya simu bandia zinatotumika nchini.

TCRA ilifanya uhakiki mwingine Februari ambao ulibaini matumizi ya simu feki kupungua hadi asilimia 18.

“Uhakiki wa Machi ulibaini matumizi yameshuka zaidi hadi kufikia asilimia 13,” alisema Mungy na kubainisha kuwa TCRA itafanya tathmini nyingine kabla ya muda kumalizika.

“Tunatumaini matumizi ya simu feki yataendelea kupungua. Hadi kufikia Juni mwishoni kusiwe na mtu anayetumia simu feki,” alisema Mungy. 

Meneja huyo alisema matokeo ya tathmini hizo ni kinyume na matarajio yao.

“Watu wameonyesha mwitikio mzuri. Wengi wameacha kuzitumia kabla hatujazizima,” alisema. 

Alisema wananchi wamekuwa na mwitikio huo kwa sababu mamlaka hiyo imekuwa ikitoa elimu kote nchini juu ya matumizi ya simu hizo.

Hadi sasa, TCRA imeshatoa elimu kuhusu wananchi kuacha kutumia simu feki, katika Kanda ya Kaskazini, Nyanda za Juu Kusini na Kanda ya Kati na wiki ijayo mamlaka hiyo itakuwa Kanda ya Ziwa.

Alisema elimu hiyo pia itatolewa kwa wananchi wa mikoa ya Pwani, Morogoro, Lindi na Mtwara.

Alisema Mkoa wa Dar es Salaam ambao una watumiaji wengi wa simu feki utakuwa wa mwisho kupatiwa elimu hiyo, Juni kabla ya kuzima simu hizo.

Kuhusu watu wanaoweka namba feki za utambulisho (IMEI) kwenye vifaa vya elektroniki, alisema wanafanya kazi bure kwa sababu hata hizo zitazimwa siku ikifika.

“Mitambo yetu ina uwezo wa kugundua namba za IMEI halisi na feki,” alisema Mungy.

Alisema hata mtu akibadilisha namba ya IMEI halisi kwenye siku feki, siku ya kuzima simu feki itazima tu.

Pia, alisema ni vigumu kuwagundua watu wanaofanya ujanja huo kwa sababu wanapokuwa wanazibadilisha simu inakuwa imezimwa.

Walimu Wagoma, kisa mwenzao kuzabwa kofi darasani na Ofisa Elimu

$
0
0
WALIMU wa shule ya msingi Kianda wameanza mgomo wa siku mbili wa kutofundisha shuleni hapo huku wakilaani kitendo cha Ofisa Elimu (Shule za Msingi) wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa, Peter Fusi kumshambulia na kumpiga makofi mwalimu mwenzao akiwa darasani mbele ya wanafunzi wake.

Makamu Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Flora Kipesha alisema wameitisha mgomo huo wa siku mbili kupinga kitendo cha Fusi kumshambulia na kumpiga makofi mwalimu mwenzao Jacob Msengezi (25) ambaye anafundisha somo la Hisabati Darasa la Saba shuleni hapo.

“Licha ya kulaani vikali kitendo hiki cha udhalilishaji alichofanyiwa mwalimu mwenzetu na Ofisa Elimu (DEO) wetu (Peter Fusi) kumcharaza makofi mbele ya wanafunzi wake akiwa darasani ….Ametudhalilisha sote yaani hata hamasa ya kufundisha imetoweka ….. 

“Sasa hatutaingia darasani kufundisha kwa siku mbili tukimshinikiza Mkurugenzi wa Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga (Adam Missana) achukue hatua dhidi ya ofisa huyo wa elimu ……yaani tunadhalilishwa hivi mbele ya wanafunzi wetu wenyewe wakati kazi hii tumeisomea na tuna vyeti halali ….Tukiwa na sifa stahiki za taaluma ya ualimu,” alieleza Kipesha. 

Akifafanua, alisema walimu hawataingia kufundisha kwa siku hizo mbili na watakuwa ofisini wakiandaa mitihani huku wanafunzi wakiendelea kuhudhuria shuleni hapo kama kawaida.

Mwalimu Msengezi alisema tukio hilo lilitokea Jumatano saa tatu asubuhi shuleni hapo baada ya ofisa elimu huyo kufanya ziara ya kikazi.

“Nilikuwa na kipindi cha somo la hesabu kuanzia saa mbili hadi saa 2.40 asubuhi kwa kuwa mwalimu wa somo la Kiingereza alikuwa ‘busy’ niliamua kubakia darasani humo nikisahihisha madaftari ya wanafunzi wangu, ndipo nikamwona akiwa eneo la shule, hivyo nikaamua kwenda ofisini kujiandaa na ukaguzi,” alisema.

Aliongeza kuwa,“Wakati nikiwa ofisini aliingia chumba cha darasa la saba na kukuta wanafunzi wakiwa pekee yao, ndipo alipoamuru aitwe mwalimu aliyekuwa akifundisha darasa hilo.

“Nilikwenda darasani na kukutana naye, nilimweleza ilivyokuwa, basi akaniuliza kwani sasa ni saa ngapi?

"Nilipomjibu kuwa ni saa tatu asubuhi alighadhabika na kunipiga makofi. Nilipohisi anajiandaa kuniadhibu zaidi nilitimua mbio na kutoka darasani,”
alisema mwalimu huyo.

Aliongeza kuwa tayari ameshafikisha malalamiko yake kwa Katibu wa Chama cha Walimu nchini (CWT)Wilaya ya Sumbawanga Vijijini, Vicent Ndewele kwa hatua zaidi.

Ndewele amekiri kutokea kwa tukio hilo huku akiahidi kuwa chama hicho kitatoa msimamo wake kwa vyombo vya habari.

Mwita Waitara Azusha Tafrani Bungeni.......Ni Baada ya Kutaka Kumchapa Ngumi Mbunge wa Kasulu Aliyedai Tundu Lissu na Mnyika Ni Vichaa

$
0
0
Mbunge  wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema) ametolewa nje ya Bunge baada ya kutaka kumkwida Mbunge wa Kasulu Vijijini, Agustine Holle (CCM) aliyedai kuwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na Mbunge wa Kibamba, John Mnyika wote wa Chadema kuwa wanaugua kichaa.

Waitara alionesha kukerwa na kauli hiyo hasa pale Holle alipokataa kufuta kauli yake, licha ya kutakiwa kufanya hivyo na Naibu Spika, Dk Tulia Akson.

Wakati Holle akichangia, Waitara alinyanyuka kwenye kiti chake na alipofika alipo mbunge huyo alimzungumzisha maneno ambayo hayakusikika na kuonesha kama kutaka kumpiga kabla ya kukaa kwenye kiti kilicho mbele yake ndipo, Holle alisikika akisema “wewe unataka nini” ndipo Naibu Spika alipogundua kuwa Waitara anataka kumpiga Holle na kumuamuru atoke nje lakini hakutii amri hiyo.

Kutokana na kutotii, Naibu Spika aliamuru askari wamtoe ndipo walipoingia zaidi ya askari watano na kutoka naye hadi nje ya geti kubwa la kuingilia bungeni.

Holle wakati anachangia bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka wa fedha 2016/2017, alimtaja Lissu ambaye ni Waziri Kivuli wa Wizara hiyo kuwa ana taarifa kuwa Lissu amewahi kuugua ugonjwa wa kichaa na hadi sasa ana faili kwenye Hospitali ya Vichaa ya Mirembe iliyopo mkoani Dodoma.

Hata hivyo, alipopewa nafasi na Naibu Spika kufuta kauli yake akasema “nafuta kauli yangu lakini kwa taarifa zilizozagaa nimeamini ni kweli na mbona kwao(Chadema) wapo wengi hata Mnyika sasa hivi yupo Muhimbili anatibiwa kichaa”.

Kutokana na kauli hiyo, Lissu alisema licha ya kuifahamu Hospitali ya Mirembe, hajawahi hata kuingia kwenye geti la hospitali hiyo wala kuugua ugonjwa huo na kutaka kiti cha Naibu Spika kimtake Holle athibitishe ; na akishindwa kanuni zielekeze hatua za kuchukua kama zilivyowekwa.

Rais Magufuli Aongea na Wananchi wa Singida akiwa njiani kuelekea jijini Arusha kwa barabara

$
0
0

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli akiongea na wananchi  wa Mji wa Singida, wakati aliposimama kwa muda akiwa njiani kuelekea Jijini Arusha kwa njia ya barabara akitokea Mkoani Dodoma, leo Mei 6, 2016.

Rais Magufuli Awaonya Walioficha Sukari......Atishia Kuichukua Sukari Hiyo na Kuigawa Bure Kwa Wananchi

$
0
0

Rais Magufuli ametoa onyo kali kwa wafanyabiashara walioficha sukari ili baadae waiuze kwa bei kubwa.

Amesema wafanyabiashara hao wenye tamaa ya pesa walikuwa wakifuata sukari iliyo Expire huko Brazili   na kuileta nchini ili watengeneze faida na ndo maana serikali iliwapiga marufuku kuagiza

Rais Magufuli ameyasema hayo leo wakati akiwasalimia wananchi wa Katesh, Mkoani Manyara. Rais ametoka Mkoani Dodoma leo, anaelekea Mkoani Arusha kwa usafiri wa gari.

Akiongea na mamia ya wananchi hao waliojitokeza kumlaki njiani, Rais Magufuli amewatoa hofu wananchi kuhusu uhaba wa sukari kwa kuwa tayari wako  katika mchakato wa kuagiza makontena ya sukari nje ya nchi ili kuwakabili wafanyabiashara walioficha bidhaa hiyo.

Amesema kwa taarifa alizonazo kuna mfanyabiashara alienda akanunua sukari pale Kilombero zaid ya tani 3000 na hataki kuzichukua hadi leo

Pia amesema kuna mwingine ana godauni huko Mbagala yenye tani 4000  ambazo hataki kuzitoa ili wananchi wakose sukari

Rais Magufuli amesema ameviagiza vyombo vya dola viwafuatilie ili ikithibitika sukari waliificha basi ichukuliwe na kugawiwa bure kwa wananchi na pia watapigwa marufuku kufanya biashara yoyote hapa nchini

==> Zaidi, Msikilize hapo chini akiongea

Wabunge Wanawake wa UKAWA watoka nje ya Bunge baada ya Mbunge wa CCM Kuwatuhumu Kwamba Wamepata Ubunge Kwa Kufanya Mapenzi na Viongozi Wao

$
0
0
Wabunge wanawake wa Upinzani wametoka wote nje ya Bunge kwa madai ya kudhalilishwa bungeni na Mbunge wa jimbo la Ulanga Goodluck Mlinga (CCM ) aliyedai jana kuwa viti maalum Ukawa hutolewa kwa rushwa ya ngono.

Mlinga alitoa kauli hiyo jana wakati akichangia hotuba Wizara ya Katiba na Sheria  ambapo alisema ili uweze kuwa mbunge wa viti maalum chadema, lazima ufanye mapenzi na kiongozi wako wa chama.
 
Wabunge hao leo asubuhi  waliomba mwongozo kwa Naibu Spika 
kupitia kwa Mbunge Sophia Mwakagenda wa viti maalumu (Chadema) kumtaka mbunge huyo athibtishe kauli yake  lakini hawakusikilizwa na badala yake Naibu spika aliwataka wakae chini.

Baada yamabishano ya dakika kadhaa pasi kusikilizwa, wabunge hao  walisimama wote na kuamua kutoka nje  ya ukumbi wa bunge huku wakiahidi kuja na tamko kali kuhusu udhalilishaji waliofanyiwa.
 
==>Msikilize hapa Mbunge wa Kawe na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake CHADEMA, Halima Mdee akizungumza na waandishi wa habari nje ya ukumbi wa Bunge mjini Dodoma, baada ya wabunge hao kutoka nje

Wafanyabiashara zaidi ya 300 wakamatwa kwa kutotoa Risiti za EFD’S

$
0
0

Na Raymond Mushumbusi -MAELEZO
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imewakamata zaidi wafanyabiashara 300 kwa kosa la kutotumia mashine za (Electronic Fiscal Devices) EFD’S katika biashara zao.

Akizungumzia na waandishi wa habari  Jijini Dare s Salaam, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA) Alphayo Kidata amesema mamlaka yake imefanya uchunguzi wa kina na kuwabaini wafanyabiashara hao katika maeneo mbalimbali nchini wakikiuka agizo la kuwa na mashine hizo.

“Tumeshaanza kuwapeleka mahakamani wafanyabiashara ambao wanakwepa kulipa kodi kwa kuuza bidhaa bila risiti na pia tumetaifisha bidhaa mbalimbali zilizoingizwa nchini kwa njia ya magendo na kukwepa kodi “ Alisema Kidata.

Kamishna Kidata amefafanua kuwa mamlaka haitowavumilia wafanyabiashara wanaoikosesha mapato Serikali kwa kuuza na kutoa huduma bila risiti za EFD’s kwa makusudi na hasa wale wafanyabiashara wanaouza kazi za wasanii bila stempu za kodi pamoja na wafanyabiashara wanaojihusisha na magendo.

Vilevile amefafanua kuwa, kwa wafanyabiashara waliopelekwa mahakamani mara baada ya kumalizika kwa kesi zao na kupewa adhabu ya kulipa faini, wakibainika tena kurudia makosa hayo adhabu kali zaidi zitachukuliwa dhidi yao ikiwemo kifungo cha miaka mitatu jela kwa kukaidi agizo la Serikali.

Aidha, Mamlaka imetoza faini ya Shillingi Mil 746 kwa wafanyabiashara waliokutwa na makosa mbalimbali yakiwemo kutotumia mashine za kielotroniki za EFD’s , kuingiza bidhaa kimagendo na kuuza kazi za wasanii bila ya stempu ya kodi.

Mamlaka inatoa wito kwa wananchi wote  kuwa mabalozi wa kodi na kichocheo cha ukusanyaji wa mapato kwakutimiza wajibu wao wa kudai risiti  wanaponunua bidhaa au kupatiwa  huduma mbalimbali.

Mahakama Kuu Yaitupilia Mbali Rufaa iliyoletwa na Mwendesha Mashtaka wa Serikali(DPP) dhidi ya Kesi ya aliyekuwa Kamishna Mkuu wa TRA na Wenzake

$
0
0

Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imetupilia mbali rufaa iliyokatwa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) iliyokuwa ikipinga kuondolewa kwa shitaka la 8 la utakatishaji fedha linalomkabili aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Harry Kitilya na wenzake wawili.

Uamuzi huo umetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Mheshimiwa Moses Mzuna alipokuwa akitoa majibu ya rufaa iliyokuwa imekatwa na DPP.

“Ninafahamu kila kesi inaamuliwa kutokana na mazingira yake lakini nimefuta rufaa hii kwa kuwa hoja zilizotolewa hazina nguvu kisheria” alisema Jaji Mzuna.

Aidha Jaji Mzuna amefafanua kuwa hata kama amefuta rufaa hiyo lakini upande wa Jamuhuri bado una nafasi ya kubadilisha shitaka au hati nzima ya mashtaka inayowakabili washtakiwa hao.

Kwa upande wake Wakili Mkuu wa Serikali Timony Vitalis amekubaliana na uamuzi uliotolewa na Mahakama hiyo juu ya pingamizi lake ingawa bado anasimamia watuhumiwa kutofutiwa shitaka la utakatishaji wa fedha.

Naye Wakili wa Utetezi Majula Magafu amesema kuwa wao wanasubiri maamuzi yatakayotolewa na Wakili wa Serikali ili wajue namna ya kuikabili kesi hiyo.

TRA Yazidi Kuvuka Malengo Ya Ukusanyaji Mapato ....Yakusanya Trioni 1.035 Mwezi Uliopita Sawa na Asilimia 99.5

$
0
0

MAMLAKA ya Mapato Nchini  (TRA)  kwa mwezi uliopita imekusanya Sh.Trioni 1.035   ambayo ni sawa na asilimia 99.5  ya lengo  kukusanya sh.trioni 1.040 .

Akizungumza  leo na  waandishi wa habari  jijini Dar es Salaam, Kamishina Mkuu wa TRA, Alphayo Kidata amesema kuwa katika makusanyo ya miezi  10  wameweza kukusanya sh. Trioni 10.92  ambayo sawa na asilimia 99 ya lengo ya sh.trioni 11.02  katika lengo la kipindi hicho.

Amesema kuwa  TRA imedhamiria  kukusanya zaidi ya sh. Trioni 1.4 na kuvuka lengo la mwaka wa fedha wa 2015/2016 katika  miezi miwili ya kumaliza mwaka wa fedha  ambalo ni sh. Trioni 12.3.

Kidata amesema kuwa TRA itaendelea na jitihada mbalimbali kuhakikisha  inafikia lengo la makusanyo kwa mwaka wa fedha 2015 / 2016 licha kuwepo kwa changamoto ambazo wamekuwa wakikabiliana nazo.

Amesema kuwa wananchi wamejua umuhimu wa kodi na kuanza kutoa ushirikiano katika kudhibiti mianya ya magaendo, pamoja na kuziba mianya ya upotevu wa mapato ikiwa katika usimamizi wa mifumo ya mlipa kodi kulipa kodi anayostahili bila usumbufu wowote.

Tamko la wizara ya Afya Kulaani Mauaji ya Mama na Mtoto Huko Bagamoyo

$
0
0
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto inasikitishwa na inalaani vikali tukio la kuuawa kwa kuchinjwa, mwanamke Oliver Erasto (23) na mtoto wake Emmanuel (3), wakazi wa eneo la Zinga, kata ya Dunda, wilayani Bagamoyo, kutokana na wivu wa kimapenzi.

Wizara inakemea maauji hayo, yanayodaiwa kutekelezwa na Frowin Mbwale  mkazi wa Kawe, Dar es salaam, ambaye ni mme wa marehemu, kwani yamesababisha kukatisha maisha ya mama na mtoto, katika kipindi ambacho Taifa linahimiza uzingatiaji wa mchango na haki za wanawake katika maendeleo ya taifa, na mwitikio wa haki ya kuishi ya Mtoto katika mipango na programu za maendeleo endelevu.

Wizara inasisitiza kutambua kuwa jukumu la ulinzi na usalama wa wanafamilia liko mikononi mwa kila mwananchi, hivyo jamii inawajibu wa kusaidia udhibiti wa ukatili na mauaji katika familia na jamii zetu.

Jamii ikiwa na uelewa wa pamoja katika haki za wanawake na watoto katika jamii, itawezesha kuwekeza katika haki ya kuishi ya Mtoto, na  kuendelea kuwaamini wanawake kwamba wanaweza kutoa mchango mkubwa wa kuendeleza familia zao, na taifa likaweza kupiga hatua kufikia maendeleo endelevu. 

Wizara inapenda kupongeza Polisi mkoa wa Pwani na wananchi walitoa taarifa za kuwakamata watuhumiwa wa mauaji haya, na tunaamini kuwa watakapofikishwa mbele ya vyombo vya sheria haki itaweza kutendeka.

Wizara inapenda kutoa pole kwa familia za marehemu hao waliopoteza maisha kwa kuchinjwa na kuawa, na kuwaombea kuwa na moyo wa subira katika kipindi hiki cha majonzi makubwa. Wizara inaitaka jamii itambue kuwa hakuna mwenye haki ya kukatisha uhai wa mtu mwingine, na mwanamke na mtoto anahaki ya kuthaminiwa utu wake, bila ubaguzi wowote ambao unaweza kukatisha maisha yao.

      Erasto T. Ching’oro (Msemaji)
     Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee

Chuo Cha Usimamizi Wa Fedha ( IFM ) Chatoa Ufafanuzi Kuhusu Tuhuma za Ufisadi wa Mamilioni Ya Fedha

$
0
0

Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) kimesikitishwa na habari zilizochapishwa na gazeti la RAI Toleo la 1249 la tarehe 5 – 11 Mei 2016 ambazo ni za upotoshaji.

Tunapenda kufafanua kuwa taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zinaeleza kuwa, Chuo cha Usimamizi wa Fedha kilipokea fedha za ziada kutoka Wizara ya Fedha kwa ajili ya mishahara na fedha hizo zilishapangwa kurudishwa ndani ya mwaka wa fedha 2015/2016 kama ripoti ya Mkaguzi ilivyoagiza katika mwaka wa fedha wa 2014/2015.  Kwa hiyo fedha hizo hazijatafunwa wala kupotea.

Kuhusu ukusanyaji wa madeni yaliyoripotiwa, nusu ya deni ni karo ya wanafunzi wanaolipiwa na Bodi ya Mikopo na fedha hiyo ililipwa Chuoni ndani ya mwaka wa fedha 2014/2015.  

Madeni mengine ni ya wanafunzi walioshindwa kuendelea na masomo kwa sababu mbalimbali na madeni hayo yanafutwa kwa kufuata taratibu za kifedha (Financial Regulation) kama Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali alivyoelekeza.

Ufanunuzi huu ulitolewa kwa mwandishi wa gazeti hili (Bwana Gabriel Mushi) mnamo tarehe 04-05-2016 alipoongea na Naibu Mkuu wa Chuo Mipango, Fedha na Utawala.

Kwa kumalizia Chuo cha Usimamizi wa Fedha kinafanya kazi zake kwa kufuata taratibu zilizowekwa na kwa zaidi ya miaka 30 mfululizo Chuo kimepata hati safi za mahesabu (Clean Audit Report) kwa mujibu wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali (CAG).

Jengo La NSSF La Eneo La Akiba Lawaka Moto

$
0
0
Jengo lililoko eneo la akiba posta jijini Dar es salaam limeripotiwa kuwaka moto kuanzia majira ya jioni na chanzo cha moto huo kinasemekana ni mtungi wa gesi kulipuka na kusababisha moto.

Inasemekana hakuna madhara makubwa kutokana na zimamoto kufika kwa wakati katika eneo la tukio.  

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Jumamosi ya Mei 7

Jason Rweikiza Achaguliwa Kuwa Katibu wa Wabunge wa CCM

$
0
0

WABUNGE wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamemchagua Mbunge wa Bukoba Vijijini, Jason Rweikiza kuwa Katibu wao.

Rweikiza anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Mbunge wa Peramiho, Jenista Mhagama, ambaye safari hii hakuwania nafasi hiyo.

Katika uchaguzi huo uliofanyika juzi usiku katika ukumbi wa Msekwa uliopo ndani ya viwanja vya Bunge, Katibu huyo mpya wa Wabunge wa CCM alikuwa akipambana na Mary Chatanda, Mariam Kisangi na Abdalah Ulega.

Wabunge wote wa CCM pia walipiga kura kuwachagua wabunge 10 kati ya 21 walioomba ujumbe wa NEC.

Waliochaguliwa ni Livingstone Lusinde, Dk Hamis Kigwangalla, Stanslaus Nyongo, Steven Ngonyani, Peter Serukamba, Faida Bakari, Agness Marwa, Munde Tambwe, Angella Kairuki na Jamal Kassim Ali.

Wabunge ambao kura hazikutosha ni Mbaraka Dau, Alex Gashaza, Hawa Ghasia, Ibrahim Raza, Profesa Norman Sigalla ‘King’, Almas Maige, Angelina Malembeka, Yahya Massare, Mattar Ali Salum na Hafidh Ali Tahir.

Mbunge Ataka Walawiti na Wabakaji Wahasiwe

$
0
0
MBUNGE wa Viti Maalumu, Angelina Malembeka (CCM) ametaka watu wanaohukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kosa la ubakaji na ulawiti, wahasiwe ili wawapo gerezani wasiendeleze tabia hizo.

“Tumeshaona wanaohukumiwa kifungo cha maisha, wakiwa huko gerezani wanaendeleza vitendo vya kulawitiana, kwa nini sasa wasihasiwe?” Alihoji. 

Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe, wakati akimjibu jana alisema, “siwezi kuwa na jibu kwa sababu Bunge ndilo linalotunga sheria, mbunge aje na wazo lake hapa bungeni lipitishwe kama sheria sisi Serikali hatuwezi.”

Akitoa ufafanuzi zaidi juu ya hali ya ubakaji na ulawiti, Dk Mwakyembe alisema kila siku nchini kunaripotiwa matukio 19 ya kubakwa na kulawitiwa.

Alisema hali ni mbaya sana na sasa kuna mashauri 2,031 yaliyoripotiwa mahakamani katika kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu. 

Kati yake mashauri hayo, 111 yameshakamilishwa kwa kuhukumiwa ambapo watu 99 wamefungwa, watuhumiwa 18 wameachiwa huru kwa kukosa ushahidi na kesi 1,920 hazijakamilika.

Akijibu swali la msingi la mbunge huyo aliyehoji mpango wa Serikali kuhakikisha kesi za kubakwa na kulawitiwa hazimalizwi kifamilia, Dk Mwakyembe alisema kumalizwa kwa kesi kifamilia kunachochea vitendo hivyo kuendelea katika jamii.

“Tatizo la kuficha ushahidi na kumaliza kesi hizo kifamilia, haliwezi kumalizwa na vyombo vya dola peke yake bila ushirikiano na wananchi wanaoishi na watuhumiwa. Hivyo Serikali imekuwa ikitoa elimu kwa umma kuwa kuficha ushahidi na kuyamaliza matukio hayo ya jinai kifamilia si kosa peke yake, bali vilevile utaratibu huo unachochea vitendo hivyo kuendelea katika jamii,” alifafanua.

Ili kuweka mazingira rafiki kwa waathirika na wananchi wenye taarifa au ushahidi wa aina hiyo, alisema Serikali imeanzisha madawati ya jinsia katika vituo mbalimbali vya Polisi yanayopokea taarifa mbalimbali kutoka kwa wananchi na kuliwezesha Jeshi la Polisi kuendesha upelelezi kwa ufanisi.

“Pindi tukio la kubaka au kulawiti litakaporipotiwa, upelelezi hufanyika na mtuhumiwa kufunguliwa mashitaka mara moja, kwa utaratibu huu Serikali inahakikisha kuwa matukio haya hayamalizwi nje ya utaratibu wa haki jinai,” alisema.

Sheria ya Kanuni ya Adhabu sura ya 16 imeweka adhabu ya kifungo cha maisha kwa mtu yeyote anayekutwa na hatia ya kumbaka msichana. Pia sheria imeweka adhabu ya kifungo cha miaka 14 kwa kosa la kulawiti.
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live




Latest Images