Quantcast
Channel: MPEKUZI
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live

Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Jumatano ya May 4


Mawaziri Waja juu Jeshi kuhusishwa na Siasa

$
0
0

MAWAZIRI wa Serikali ya Awamu ya Tano wamewajia juu wabunge wa upinzani na wananchi wanaovishutumu kila mara vyombo vya ulinzi nchini na kuwataka kuacha kuvihusisha vyombo hivyo na masuala ya kisiasa.

Mawaziri hao ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yussuf Masauni na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba.

Wamewataka wananchi na hususani wabunge wa vyama vya upinzani, kutambua kuwa vyombo hivyo vya ulinzi ambavyo ni pamoja na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Polisi wajibu wake mkubwa ni kulinda mipaka ya nchi na usalama wa raia na mali zao.

Akizungumza wakati wa mjadala wa kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara inayoshughulikia Muungano na Mazingira, Dk Mwinyi alisema haijawahi kutokea na wala haitotokea jeshi kutumika kisiasa.

Alisema Jeshi la Tanzania limekuwa likitekeleza majukumu yake kwa kufuata sheria iliyojiwekea pamoja na za kimataifa na wala hata siku moja haliwezi kutumika kwa ajili ya kutumiza malengo ya kundi fulani.

“Jeshi letu lina sifa ya kimataifa ya ulinzi wa amani, dunia kote tunasifika kwa weledi, kulinda amani na mipaka yetu. Haijawahi kutokea wala haitotokea jeshi kujiingiza kwenye shughuli za kisiasa,” alisisitiza Dk Mwinyi.

Alisema tangu mjadala wa makadirio ya bajeti hiyo uanze, baadhi ya wabunge hususani wabunge wa upinzani wamekuwa wakilitupia shutuma nzito jeshi na vyombo vya dola kwa ujumla kuwa limetumika vibaya kwenye uchaguzi wa Zanzibar na chaguzi nyingine.

Aliwataka wabunge hao pamoja na wananchi wanaovilaumu mara kwa mara vyombo hivyo vya dola kumuogopa Mungu kwa kutoa madai ya uongo dhidi ya vyombo vyao vya ulinzi na usalama.

Alisema madai kuwa jeshi hilo limetumika na kuandikisha wananchi kwenye kambi zao za jeshi visiwani Zanzibar si ya kweli na kama kuna mwenye ushahidi auwasilishe ili ukweli ujulikane.

Dk Mwinyi alisema amesikitishwa na madai ya Msemaji wa Kambi ya Upinzani kuhusu masuala ya Muungano, Ally Abdallah Saleh kwamba Zanzibar imetekwa na jeshi la Tanganyika kana kwamba nchi iko katika vita.

“Naomba nikujibu kwanza ili ufahamu kuwa hakuna jeshi la Tanganyika, jeshi ni moja na ni la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania. Naomba nimuelimishe kazi kubwa za jeshi ni ulinzi wa mipaka, ulinzi wa amani na kutoa msaada kwa mamlaka za kiraia au vyombo vingine vya ulinzi na usalama inapohitajika kufanya hivyo,” alisema.

Alisema inapotokea matukio makubwa kama shughuli ya uchaguzi, duniani kote si Tanzania pekee, majeshi yote yanakuwa tayari kukabiliana na hali yoyote na ndio maana askari wake wanakuwa kwenye sare za kombati.

Kuhusu madai ya kambi hiyo ya upinzani kuwa Jeshi limekuwa likitumika kulazimisha Muungano, Dk Mwinyi alisema JWTZ ni kielelezo cha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Alisema tangu Tanganyika na Zanzibar ziungane mwaka 1964, jeshi ni moja na kamwe halijawahi kulazimisha utawala, ila lipo hadi Zanzibar kwa sababu ya kulinda mipaka ya Tanzania, na Zanzibar ni sehemu ya Tanzania.

“Tangu mwaka 1964 jeshi lina vikosi vyake Zanzibar na siku zote vikosi hivi huwa na silaha, sasa tuna haja gani ya kupeleka wanajeshi na silaha wakati miaka yote vyote viko huko? "Alihoji Dk Mwinyi. 

Naye Naibu Waziri Masauni alisema hoja kwamba jeshi lilitumia mabavu Zanzibar na askari walikuwa ni wengi si ya kweli.

Alisema kwa mujibu wa taratibu za uchaguzi, kila kituo cha uchaguzi kinahitajika angalau askari wawili wakati Zanzibar kulikuwa na vituo vya uchaguzi zaidi ya 3,000 na askari waliopo visiwani humo ni 5,000.

Alisema kwa hali ilivyokuwa askari wa Zanzibar walikuwa hawatoshi kwani wangesambazwa wote wasingetosha kuweka ulinzi na kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa utulivu na usalama.

Kuhusu madai kwamba Katiba imekiukwa, aliutaka upande wa upinzani kujiuliza kati ya madai yao ya kumtaka Rais John Magufuli aingilie mamlaka ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) au Polisi kulinda raia na mali zao, kipi ni uvunjifu wa Katiba.

Alifafanua kuwa majukumu ya Jeshi la Polisi na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ni kulinda usalama wa raia na mali zao hivyo bila kujali cheo au utajiri wa mtu yeyote endapo atavunja sheria atachukuliwa hatua za kisheria.

Naye Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju alisema uchaguzi wa Zanzibar ulikamilika kwa usalama na kwamba pamoja na malalamiko ya vichochoroni kuhusu uchaguzi huo, hakuna hata mmoja aliyefungua kesi kupinga matokeo mahakamani.

Alisema kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi ni ruhusa mtu asiporidhika na matokeo ya uchaguzi, kufungua kesi ya kuyapinga, lakini tangu uchaguzi huo umalizike hakuna mtu kutoka jimbo lolote visiwani humo aliyefungua kesi.

Naye January alisema kuhusu uchaguzi wa Zanzibar, Mahakama Kuu ya Zanzibar ndio pekee yenye uwezo wa kusikiliza na kuamua masuala yote yanayohusu uchaguzi wa Zanzibar.

Uchumi wa Tanzania Waongoza Afrika Mashariki Ukifuatiwa na Kenya

$
0
0

Tanzania inatarajiwa kusajili kiwango cha juu zaidi cha ukuaji wa uchumi wake mwaka huu katika kanda ya Afrika Mashariki na kati. Hii ni kwa mujibu wa ripoti ya shirika la fedha la kimataifa - IMF.

Katika ripoti yake iliyotolewa jana Tanzania inatarajiwa kusajili kiwango cha juu cha ukuaji wa uchumi wake wa asilimia 6.9% mwaka  2016.

Kasi hiyo ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania ni ya pili tu nyuma ya Ivory Coast baina ya mataifa ya Kusini mwa jangwa la Sahara .Ivory Coast inatarajiwa kukuwa kwa kasi ya asilimia 8.5%.
 
Katika kanda ya Afrika Mashariki ,uchumi wa Kenya ndio wa pili kwa kasi ya ukuaji kwa asilimia 6%.

IMF hata hivyo inasema kuwa kasi ya ukuaji wa uchumi kusini mwa jangwa la Sahara unatarajiwa kupungua kwa mwaka wa pili mfululizo kutokana na kudorora kwa viwango vya uzalishaji na hivyo uwekezaji.

Kwa mujibu wa shirika la fedha la kimataifa - IMF, eneo hilo linakadiria kushuka kwa ukuwaji wa uchumi kwa asilimia 3 mwaka huu.Kiwango hicho ni cha chini kabisa kuwahi kushuhudiwa katika miaka 15.
 
Mataifa yanayotegemea mapato yanayotokana na mafuta ndiyo yalioathirika zaidi kama vile Nigeria na Angola. Aidha Zambia pia imeathirika vibaya kutokana na ukosefu wa soko la kimataifa la shaba yake.

Ripoti hiyo inaitaja Afrika Kusini kama moja ya mataifa ambayo kiwango chake cha ukuaji kimedorora kwa kiasi kikubwa mno.

Katika orodha ya mataifa yanayotarajiwa kuwa na kiwango cha juu cha ukuaji Kusini mwa jangwa la sahara Ivory Coast ndio inayoongoza.
 
Orodha ya mataifa ya kanda ya Kusini mwa Jangwa la Sahara na viwango vya kasi ya ukuaji wa uchumi 2016.
  1.     Ivory Coast 8.5%
  2.     Tanzania 6.9%
  3.     Senegal 6.6%
  4.     Kenya 6%
  5.     Zambia 3.4%
  6.     Nigeria 2.3%
  7.     Afrika Kusini 0.6%

Credit: BBC

CCM Kimeeleweka.......Rais Magufuli Akubali Kupokea Kijiti cha JK Kabla ya 2017, Wabunge 21 Wapitishwa Kuwania Nafasi 10 za NEC

$
0
0
KAMATI Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imepitisha majina ya wabunge 21 walioomba nafasi ya ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho.

Msemaji Mkuu wa CCM, Christopher Ole Sendeka alisema Kamati Kuu ilifanya maamuzi hayo kupitia kikao chake kilichofanyika jana, Ikulu ya Chamwino Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma chini ya Mwenyekiti wake, Jakaya Kikwete na kuhudhuriwa pia na Rais John Magufuli.

Pamoja na kupitishwa kwa majina hayo, Kamati Kuu imewataka wagombea wote kufuata sheria na taratibu za chama na kwamba atakayekiuka, atachukuliwa hatua za kinidhamu, ikiwa ni pamoja na kuenguliwa kwa jina lake katika nafasi za wagombea.

Waliopitishwa kuwania nafasi 10 za NEC kutoka Bunge la Tanzania kwa CCM ni 
  1. Munde Tambwe, 
  2. Jamal Kassim Ali, 
  3. Faida Mohamed Bakari, 
  4. Mbaraka Dau, Alex Gashaza,
  5. Hawa Ghasia, 
  6. Ibrahim Hassanali Raza, 
  7. Angela Kairuki, 
  8. Dk Hamis Kingwangalla, 
  9. Profesa Norman King, 
  10. Livingstone Lusinde na 
  11. Angelina Mabula.
Wengine ni Almasi Maige, Angelina Malembeka, Agness Marwa, Yahaya Massare, Steven Ngonyani ‘Maji Marefu,’ Stanslaus Nyongo, Mattar Ali Salum, Peter Serukamba na Hafidh Ali Tahir. 

Pia Kamati Kuu imepitisha majina 19 ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, walioomba kugombea nafasi ya ujumbe wa NEC kupitia Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Waliopitishwa ni Nassoro Salim Ally, Ally Hamisi Bakari, Salma Mussa Bilal, Mgeni Hassan Juma, Riziki Pemba Juma, Yussuph Hassan Idd, Khadija Omary Kibano, Shamata Shaame Khamisi, Mmanga Mjawiri na Dk Khalid Salum Mohamed.

 Pia wamo Aska Abdallah Mussa, Mihayo Juma N’hunga, Zulfa Mmaka Omar, Hamad Abdallah Rashid, Mohamed Ahmada Salum, Harusi Saidi Suleiman, Haroun Ali Suleiman, Issa Haji Ussi na Bahati Khamisi Kombo.

Aidha, Sendeka alisema kuwa Kamati Kuu pia imepitisha majina ya wabunge wa CCM wanne, walioomba nafasi ya Katibu wa Kamati ya Wabunge wote wa CCM. 

Waliopitishwa ni Mbunge wa Bukoba Vijijini, Jasson Rweikiza, Mbunge wa Korogwe Mjini, Mary Chatanda, Mbunge wa Viti Maalumu, Mariam Kisangi na Mbunge wa Mkuranga, Abdallah Ulega.

Nafasi hiyo ilikuwa inashikiliwa na Mbunge wa Peramiho na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama.Katibu wa wabunge huingia moja kwa moja katika Kamati Kuu. 

Pia imepitisha majina matatu ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi walioomba nafasi ya Katibu wa Kamati ya Wajumbe wa Baraza hilo kupitia CCM.Hao ni Ali Suleiman Ali (Shihata), Ali Salum Haji na Abdallah Ali Kombo. 

Msemaji huyo wa CCM alieleza kuwa Kamati Kuu pia imepitisha majina ya wana CCM walioomba nafasi wazi mbalimbali za uongozi, ikiwamo ya Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma ambayo wamepitishwa Josephat Ntambindi, Gilbert Kagoma na Malck Rudugu. 

Kwa nafasi ya Mjumbe wa NEC Wilaya ya Handeni mkoani Tanga, waliopitishwa ni Omar Kigoda, Maajabu Hamis, Mussa Kidato, Hamisi Mnondwa na Athuman Lukoya.

Aidha, nafasi ya Katibu wa Uchumi na Fedha, Mkoa wa Mbeya, Sendeka aliwataja waliopitishwa kugombea ni Charles Mwakipesile, James Mwasunga na Stephen Mwakajumulo. 

Kwa nafasi ya Katibu wa Uchumi na Fedha, Mkoa wa Njombe waliopitishwa ni Creiton Lulambo, Salu Sanga na Erick Nyagawa. 

Katika hatua nyingine, Kamati Kuu imempongeza Dk Ali Mohamed Shein kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar kwa kura nyingi katika uchaguzi wa marudio uliofanyika Machi 20, mwaka huu.

Aidha, Kamati Kuu imewapongeza wananchi wa Zanzibar kwa kuendelea kukiamini Chama Cha Mapinduzi kwa kukipa ushindi wa kishindo katika nafasi ya Rais, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani.

Wakati huo huo, Msemaji wa CCM, Christopher Ole Sendeka amesema chama hicho kiko katika hatua za mwisho za makabidhiano ya nafasi ya Uenyekiti wa Taifa kati ya Mwenyekiti wa sasa, Jakaya Kikwete na Rais John Magufuli.

Akizungumza jana wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari, Sendeka alisema suala la kukabidhiana mikoba kati ya Kikwete na Rais Magufuli kwa mujibu wa uzoefu wa CCM anayechaguliwa kuwa Rais kwa tiketi ya chama hicho ndiye anayepokea nafasi ya uenyekiti wa CCM.

“Bahati nzuri hawa wakubwa walikuwa wameshauriana kwamba Uenyekiti ni miaka mitano, Dk Kikwete angeweza kuendelea kuwa mwenyekiti, lakini uzoefu wa kupokezana vijiti na uongozi tangu wakati wa Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na sasa ni Kikwete unaonesha kwamba umekuwa ukifanyika mwaka unaofuata baada ya uchaguzi kwenye mwezi Juni,” alieleza Sendeka.

“Mwaka huu wakubwa hawa walishashauriana,Kikwete alishatangaza wazi kwamba anakusudia kumkabidhi nafasi ya uenyekiti Rais wa sasa, Dk Magufuli wakati wowote mwaka huu na kinachofanyika sasa ni maandalizi .

"Tarehe na mwezi ambao Mkutano Mkuu utafanyika tutawaarifu lakini tumekubaliana tupo kwenye mchakato wa Mkutano Mkuu Maalumu ili Kikwete aweze kukabidhi uenyekiti kwa Magufuli.”

Alisema nafasi ya Mwenyekiti wa chama kikubwa kama CCM inapotokea mamlaka ya Rais ipo kwa mtu mwingine inaweza kuleta mkanganyiko wa kudhoofisha lengo la mtu aliyekabidhiwa nchi ya kuyafanya. 

“Ni mazoea na utamaduni wetu wa CCM kwamba  Mwana CCM mwingine ataweza kujitokeza kugombea hazuiwi Katiba ipo kanuni zipo ataelekezwa,” alisema Sendeka.

Kangi Lugola Afurahia Sefue Kutumbuliwa.....Ataka Majipu Sugu Wizara ya Kilimo Yaliyoota Sehemu Nyeti Yatumbuliwe

$
0
0
Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola jana alichangia Bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa hisia kali huku akimpongeza Rais John Magufuli kwa kumtumbua Katibu Mkuu Kiongozi.

Ingawa hakumtaja kwa jina, Balozi Ombeni Sefue ndiye Katibu Mkuu Kiongozi aliyeondolewa na Rais Magufuli Machi mwaka huu bila kubainisha sababu ikielezwa kwamba angepangiwa kazi nyingine.

Lugola alisema Rais Magufuli ameonyesha kwa vitendo kuwa anamuenzi Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kwa kauli yake kuwa Ikulu ni mahali patakatifu.

Mbunge huyo alitoa kauli hiyo Bungeni mjini Dodoma wakati akichangia hotuba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba.

Lugola alisema kwa kuwa alikuwa akichangia kwa mara ya kwanza bajeti ya Serikali ya Awamu ya Tano, ni vyema akampongeza Rais kwa namna anavyotumbua majipu kwa ujasiri na bila kupepesa macho.

Lugola akirejea kauli inayosema “kama unataka mali utaipata shambani”, alimtaka Waziri Nchemba kutumbua majipu katika wizara yake. 

“Hatuwezi kupata mali shambani kama hutatumbua majipu kwenye wizara yako ambayo yameota sehemu nyeti .. Rais ametumbua jipu la watumishi hewa. Wizara ya Kilimo ina wakulima hewa na ni jipu ambalo unatakiwa ulitumbue nchi nzima.”

Huku akiungwa mkono na baadhi ya wabunge alisema vocha za pembejeo kwa wakulima ni jipu akisema baadhi ya watumishi wanasajili wakulima hewa na wengine wakiwa ni marehemu na Serikali inaendelea kuwalipa.

Huku akiwataja baadhi yao kwa majina, Lugola alitoa mfano wa kata moja jimboni kwake ambako wakulima hewa wamelipwa vocha zenye thamani ya Sh46.3.

Alisema jipu jingine ni mbegu za pamba aina ya Quton ambazo hazioti akisema zimelalamikiwa na wabunge lakini mwekezaji anakumbatiwa. “Hili ni jipu ikiwezekana ukitoka hapa ukatumbue jipu hili."

Mbunge ahoji kilimo cha mirungi
Mbunge wa Same Mashariki (Chadema), Naghenjwa Kaboyoka aliitaka Serikali kuzungumza na Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, ili kujua ni kwa nini wamehalalisha kilimo cha mirungi.

Alisema Rais huyo ametoa Dola za Marekani milioni mbili, sawa na Sh4 bilioni za Tanzania ili kusaidia ustawi wa kilimo hicho, ambacho kwa Tanzania ni kosa la jinai kulima na kusafirisha.

“Rais Kenyatta ameruhusu kilimo hiki tukizingatia kwamba tuko Jumuiya ya Afrika Mashariki. Tutahakikishaje kwamba hii mirungi haitaingia kwetu?” alihoji.

Alimtaka Waziri wa Kilimo awasiliane na Kenya ili kujua sababu za kuruhusu kilimo hicho na namna ambavyo wataweza kudhibiti kisilete madhara Tanzania.

Ataka marufuku ya nyavu
Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CCM), Peter Serukamba aliitaka Serikali kupiga marufuku uzalishaji wa nyavu za kuvulia samaki  ambazo haziruhusiwi badala ya kuwakamata wavuvi. “Kwa nini nguvu kubwa isielekezwe katika kudhibiti uzalishaji wa hizi nyavu. Mpige marufuku uzalishaji wake badala ya kwenda kuzikamata kwa wakulima na kuzichoma,” alisema Serukamba.

Wizara ihame Dar
Mbunge wa Nchemba (CCM), Juma Nkamia alitaka makao makuu ya Wizara ya Kilimo yahame kutoka jijini Dar es Salaam na kwenda katika mikoa yenye mifugo mingi.

Pia aliishauri Serikali kujenga mazingira yatakayovutia kujengwa kwa viwanda vya nyama kwenye mikoa yenye mifugo mingi badala ya kusafirisha mifugo hai umbali mrefu.

Msimamo wa kambi ya upinzani
Akiwasilisha hotuba ya msemaji mkuu wa kambi rasmi ya upinzani Bungeni, waziri kivuli wa wizara hiyo, Magdalena Sakaya (CUF), alisema itaendelea kulaani ubakaji wa demokrasia Zanzibar.

“Tutaendelea kulaani kubakwa kwa demokrasia kulikotokea huko Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba mwaka jana,” alisema.

Akizungumzia wizara hiyo, Sakaya alisema taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) inaonyesha asilimia 75 ya machinjio nchini hayana huduma na vifaa vinavyozingatia usafi na ubora wa nyama.

 “Hali hii si nzuri hata kidogo kwa kuwa   magonjwa ya kuambukiza nchini hayataisha kutokana na uchafu uliopo katika machinjio ambayo yanalisha maelfu ya walaji wa nyama,” alisema.

Pia kambi hiyo imeitaka Serikali kupitia upya mikataba yote iliyoingiwa na wawekezaji katika mashamba makubwa kuona kama ina masilahi kwa nchi.

Kambi hiyo ilisema kati ya Sh60.3 bilioni ambazo ziliidhinishwa na Bunge katika mwaka fedha 2015/2016, Sh19.3 zilizotengwa kwa ajili ya maendeleo hazikupokewa.

Alisema taarifa ya wizara inaonyesha kuwa hadi Machi 31,2016, wizara hiyo ilikuwa haijapokea hata shilingi moja, hivyo akasema hata mipango inayotaka kutekelezwa sasa itakuwa ni ngonjera.

 “Hii mipango ambayo ipo kwenye taarifa ya wizara na ile iliyotolewa katika hotuba ya Waziri Mkuu ni ngonjera tu za kuwafariji wadau lakini ukweli sekta ya mifugo na uvuvi iko mahututi.

"Kambi rasmi ya upinzani inaona kwamba kukua kwa sekta hizi itakuwa ni ndoto kwani hali halisi ni kwamba hakuna fedha za kuendeleza malengo yaliyowekwa katika awamu ya kwanza,” alisema.

Aliikumbusha Serikali kuwa inatakiwa kulipa Sh2 bilioni zilizotokana na amri ya Mahakama kutokana na kesi ya kukamatwa kwa meli ya uvuvi maarufu “samaki wa Magufuli.”

Alisema Serikali inawajibika kulipa fedha hizo kutokana na kufanyika kwa uamuzi ambao haukuzingatia sheria.

Polisi Yaua Majambazi Wanne Katika Mapango ya Amboni Tanga

$
0
0
Watu wanne wameuawa katika mapambano na polisi yaliyotokea kwenye mapango ya Amboni mjini Tamga, eneo ambalo polisi mmoja aliuawa Februari mwaka jana katika tukio lililohusishwa na ugaidi.

Katika tukio hilo la Februari mwaka jana, polisi walilazimika kuomba msaada wa askari wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) kukabiliana na watu waliokuwa wamejificha kwenye mapango hayo na kupiga kambi hapo hadi walipokisambaratisha kikundi hicho kilichoelezwa kuwa na sura ya ugaidi.

Mapambano ya jana yametokea kwenye eneo hilo la kihistoria wakati polisi wakiendesha operesheni ya kusaka majambazi waliofanya mauaji katika duka la Central Bakery.

Majambazi hao walivamia duka maarufu la Central Bakery mwezi uliopita na kuwaua watu wanne, kujeruhi wawili na kupora Sh2.7 milioni baada ya kufanikiwa kuvunja kasiki.

Jana ilikuwa siku ya tatu tangu milio ya risasi ianze kusikika katika mapango ya Amboni na baadaye taarifa kuenea jijini Tanga kuwa kulikuwa na majibizano ya risasi.

Kamanda wa polisi wa mkoa, Leonard Paulo aliwataja waliouawa katika mashambulizi ya risasi yaliyotokea katika mapango ya Amboni kuwa ni Nasibu Bakari, Abuu Katada, Abuu Mussa na raia wa kigeni aliyetambulika kwa jina la Idrisa Berato.

Kamanda Leonard alisema mbali na kuwathibiti majambazi hao, pia jeshi hilo limefanikiwa kukamata vifaa mbalimbali vinavyosadikika kuwa vilikuwa vinatumika katika matukio ya ujambazi.

Alivitaja vifaa vilivyokamatwa kuwa ni vocha mbalimbali za simu 195, majambia saba, mapanga manne, msumeno mmoja, risasi 17 za shortgun, sare za mgambo, kofia inayofanana na ya sare za JWTZ na pikipiki mbili.

Alisema wakati wakiendelea na uchunguzi, watu wanne walikamatwa na waliwataja wenzao ambao walijificha kwenye mapango hayo na ndipo jeshi likavamia eneo hilo na kufanikiwa  kuua watu wanne na kujeruhi mmoja.

Alisema Katika majibizano ya risasi, askari wawili walijeruhiwa, akiwataja kuwa ni Gwantwa Mwakisole, mkaguzi msaidizi wa polisi mkoani Tanga na PC Charles.

Habari zinaarifu  kuwa viongozi waandamizi wa Jeshi la Polisi kutoka makao makuu wako jijini Tanga tangu kutokea kwa mauaji hayo.

Taasisi ya Misaada ya Kijamii ya Naibu Waziri wa Afya Dr. Hamisi Kigwangalla Yajitolea Kumsomesha Getrude Clement

$
0
0

Kwa kutambua umuhimu wa elimu kwa kizazi cha miaka ijayo, Taasisi ya Misaada ya Kijamii ya Hamisi Kigwangalla iliyoanzishwa na Naibu Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Hamisi Kigwangalla imejitolea kumlipia ada Getrude Clement kwa masomo yake ya kidato cha tano na sita.

Uamuzi huo wa kumsomesha Getrude umekuja baada ya jana kukaribishwa kuongea kwenye kikao cha wabunge watetezi wa haki za watoto ambapo Getrude alipata nafasi ya kutoa historia yake ambayo iliwatoa baadhi ya wabunge machozi.

Getrude aliwaeleza wabunge historia yake na hali yake ya kimaisha na kusema kuwa baba yake ni kinyozi na mama yake anafanya biashara ndogo ndogo za nyanya na vitunguu lakini bado amekuwa akijtuma katika masomo yake ambapo kwa sasa yupo kidato cha tatu katika shule ya Sekondari Mnarani, Mwanza.

Baada ya kusema hivyo, ndipo Dkt. Kigwangalla aliamua kujitolea kumsaidia mtoto huyo ili aweze kujiendeleza zaidi kielimu na kufikia malengo yake na zaidi akiahidi kumsomesha katika shule za kisasa ili apate elimu bora zaidi.

“Kwa kuthamini kipaji chake na mchango wake na kutambua nafasi yangu kama Naibu Waziri kwenye Wizara inayosimamia mambo ya Watoto na kama mbunge na mzazi wa mabinti, lakini zaidi kama mtu kutoka kwenye background ya maisha ya chini na ninayethamini mchango wa elimu kwenye maisha yangu, nimeamua kujitolea kumsomesha kidato cha tano na cha sita kwenye shule za kisasa,

“Taasisi yangu ya misaada ya kijamii ya Hamisi Kigwangalla Development Foundation itamlipia ada za masomo yake ya high school,” alisema Dkt. Kigwangalla.

Getrude Clement ambaye ana miaka 16 amepata nafasi hiyo ya kipekee baada ya kupata nafasi ya kutoa hotuba kwa niaba ya watoto na vijana wengine duniani katika mkutano wa Umoja wa Mataifa ambapo alikaribishwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon na kusifiwa na watu mbalimbali duniani kutokana na hotuba yake nzuri.

Rais Mstaafu Jakaya Kikwete Alitabiri Rais Ajaye ( Magufuli ) Atapata Sifa ya Punguzo la Kodi ( PAYE )

$
0
0
Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete alimtabiria Rais John Magufuli kuwa atapunguza kiwango cha Kodi ya Mshahara (PAYE) kutoka tarakimu mbili hadi kufikia moja.

Jumapili akiwa kwenye maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani, yaliyofanyika kitaifa mkoani Dodoma, Rais Magufuli alitangaza kupunguza kodi ya mshahara kutoka asilimia 11 hadi 9.

Punguzo hilo la PAYE ambalo litaanza kutumika katika mwaka huu wa fedha unaonza Julai mosi, lilitabiriwa na Kikwete, mwaka jana katika maadhimisho ya siku kama hiyo.

Katika hotuba yake, Kikwete alisema kodi ya mshahara imekuwa ikipunguzwa mwaka hadi mwaka katika kipindi cha uongozi wake.

“Tumeendelea kupunguza kiwango cha kodi ya mapato kwa wafanyakazi mwaka hadi mwaka.

“Tulikuta kodi ikiwa asilimia 18.5. Sasa imefikia asilimia 12 na mwaka huu tutaendelea kupunguza kodi ya mapato kwa wafanyakazi,” alisema Rais Kikwete.

Ukiwa mwaka wake wa mwisho madarakani, hakuwa na uhakika wa kufikia kiwango hicho kutoka kodi ya mshahara kuwa tarakimu mbili hadi moja.

“Ndiyo tuko kwenye mchakato wa bajeti sijui kama kweli tutafikia kwenye asilimia tisa ninayosema lakini naamini hatutakuwa mbali sana kama hatutafikia,”alisema na kuongeza:

“Kama tutabakisha patakuwa ni padogo kiasi ambacho naamini kwamba huyo Rais anayefutia atamalizia halafu sifa atapata yeye… kwamba yule mzee tulipiga risala hasikii. Amejitahidi kupunguza, lakini hakufikia pale, wewe umefika asilimia tisa mwaka huo huo.”

Pia Rais huyo mstaafu aligusia suala la kima cha chini cha mshahara kwa wafanyakazi wa sekta binafsi na kusema kuwa hupangwa na bodi za mishahara ya sekta hizo, ambazo zinaundwa na waziri wa kazi.

“Hadi kufikia mwaka 2011, tulikuwa na bodi za mishahara za kisekta 12, ambazo zimeweza kufanya majadiliano na waajiri na waajiriwa katika sekta binafsi,” alisema Kikwete.

Chama cha ACT-Wazalendo chawasilisha mahesabu kwa CAG

$
0
0
CHAMA Cha ACT-Wazalendo, jana kiliwasilisha rasmi hesabu zake katika Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Hatua hiyo inatokana na agizo lililotolewa na Msajili wa Vyama vya Siasa, la kuvitaka vyama ambavyo havijawasilisha hesabu kwa CAG, kutekeleza jambo hilo ndani miezi mitatu, kuanzia Aprili 27, mwaka huu.
 
Akizumgumza jana jijini Dar es Salaam, baada ya kuwasilisha hesabu hizo, Ofisa Habari wa ACT-Wazalendo, Abdallah Khamis, alisema mfumo wa chama hicho ni wa uwazi hali inayowafanya watekeleze na kuweka hadharani kila baada ya miezi mitatu.
 
“Baada ya kuwasilisha hesabu zetu katika ofisi ya msajili, tulipata barua iliyotuelekeza tupeleke hesabu zetu kwa CAG na wakati huo tulikuwa kwenye mchakato wa uchaguzi wa marudio katika baadhi ya majimbo, hali iliyotufanya tushindwe kutekeleza agizo hilo,” alisema Khamis.
 
Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mitungi, katika barua yake ya Aprili 27, mwaka huu, kwenda ACT-Wazalendo, aliwaeleza kuwa baada ya miezi mitatu kupita bila chama hicho kuwasilisha hesabu zake kwa CAG, watatakiwa kujieleza kwa nini wasichukuliwe hatua za kisheria.
 
Katika taarifa ya CAG iliyosomwa bungeni hivi karibuni ni chama kimoja pekee kilichotajwa kupeleka hesabu zake katika ofisi ya CAG.
 
Katika hatua nyingine, chama hicho kesho kinatarajia kuadhimisha miaka miwili, tangu kipate usajili wa kudumu, Mkuranga mkoani Pwani.

Serikali Kuajiri Watumishi 71, 496 Kuanzia Julai Mwaka Huu

$
0
0
SERIKALI itaajiri watumishi wa kada mbalimbali 71,496 mwaka wa fedha 2016/17.Hayo yalisemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Angela Kairuki, wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Mbulu Mjini (CCM), Zacharia Issaay.

Mbunge huyo alihoji kuwa nafasi za watendaji wa vijiji na kata zimekuwa wazi ni kwanini serikali isione umuhimu wa kutoa nafasi kwa vijana waliomaliza vyuo kuanza kujitolea katika kipindi cha mpito ili baadae waingie kwenye mfumo wa ajira.
 
Kairuki alisema pamoja na ufinyu wa bajeti, serikali katika mwaka ujao wa fedha unaoanza Julai, mwaka huu, itaajiri watumishi wa kada mbalimbali, wakiwamo watendaji wa vijiji na kata ambapo ajira zao zitaanza kutolewa mwezi huu. 
 
“Serikali imekuwa ikipandisha kima cha chini cha mshahara kulingana na uwezo wa bajeti (mapato ya ndani) na kwa kuzingatia gharama za maisha,” alisema.
 
Kairuki alisema maombi ya nafasi za ajira serikalini hufanyika kwa uwazi kupitia bajeti ya serikali ambayo huidhinishwa na Bunge.
 
Alisema nafasi hizo za ajira hutolewa baada ya waajiri kuwasilisha maombi yao serikalini na kuidhinishwa kwa kuzingatia ukomo wa bajeti ya mishahara serikalini.
 
Aidha, Kairuki alisema Tanzania ni moja ya nchi za Afrika ambazo hulipa kima cha chini cha mshahara sawa na asilimia 80 ya kiwango cha gharama za maisha.

Snura afungiwa kujihusisha na sanaa, TCRA waagizwa kuifuta video ya Chura mtandaoni

$
0
0

Wizara ya Habari,Utamaduni, Sanaa na Michezo leo imetangaza kumfungia Snura kujihusisha na masuala ya sanaa.

Pia imeufungia wimbo wake Chura pamoja na video yake kutochezwa kwenye redio na TV nchini. Taarifa hiyo imetolewa na wizara hiyo kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika kwenye ukumbi wake wa mikutano wizarani hapo jijini Dar.

Uamuzi wa kumfungia umekuja kutokana msanii huyo kutojisajili kwenye Baraza la Sanaa la Taifa, BASATA.

Akiongea na waandishi wa habari, Mkuu wa Kitengo cha mawasiliano wa wizara hiyo, Zawadi Msalla, amewaonya watu kutousambaza wimbo huo kwenye mitandao ya kijamii ikiwemo WhatsApp.

Amedai kuwa wale watakaokiuka agizo hilo watashtakiwa kwa kutumia sheria ya makosa ya mtandao.

Bodi ya Filamu yasitisha usambazaji wa Filamu ya “Imebuma”

$
0
0
Bodi ya Filamu Tanzania imesitisha usambazaji wa filamu ya “Imebuma” mpaka pale maudhui yake yatakapofanyiwa marekebisho.

Akisitisha usambazaji wa filamu hiyo, Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania Bi Joyce Fisso amesema mtengenezaji wa filamu hiyo hana kibali cha kutengenza filamu kutoka Bodi ya Filamu na hajazingatia Sheria na kanuni za utengenezaji wa filamu.

Bi Joyce Fisso amesema filamu hiyo imesitishwa kwenda sokoni kutokana na kukiuka vifungu vya kanuni za sheria ya Filamu na Michezo ya Kuigiza ya mwaka 2011 ambayo inakataza kuonesha namna yoyote ya udhalilishaji wa kibinadamu katika filamu na maigizo.

“Baada ya kuangalia kwa makini filamu hii na kuona mapungufu ambayo yanakinzana na Kanuni za Sheria ya filamu na Michezo ya kuigiza  nimeamua kuisitisha usambazaji wake mpaka pale wahusika watakaporekebisha maudhi yake” Alisema Bi Joyce.

Bi Joyce amefafanua kuwa filamu hiyo imeonesha baadhi ya matukio ya udhalilishaji wa kibinadamu, ushawishi wa matendo ya ngono na ushoga ambayo ni kinyume na madili ya mtanzania.

Aidha kwa upande wake Afisa Utamaduni kutoka Bodi ya Filamu Tanzania Bw. Julius Tairo amewataka waandaaji na waigizaji wa filamu nchini kufanya utafiti wa kutosha kuhusu maudhui ya filamu kabla ya kutengeneza ili kuondokana na  utengenezaji wa filamu zisizofata Sheria na kanuni za utengenezaji wa filamu Tanzania.
Muhusika Mkuu katika filamu ya “Imebuma” Bw. Eliasa Mkaly (Rashidi kisoda) akimbembeleza muigizaji na mtayarishaji wa filamu hiyo  Bi Sarah  Nyika (Asha Mauno) mara baada ya Bodi ya Filamu Tanzania kusitizasha  usambazaji wa filamu hiyo leo. Picha na Raymond Mushumbusi MAELEZO

Kesi ya Gwajima: Wakili wa serikali Agoma kupeleka mashahidi

$
0
0

Upande wa Mashitaka katika kesi ya Josephat Gwajima, Askafu wa Mkuu wa Kanisa la Ufufuo umekataa kuendelea kupeleka mashahidi wake katika Mahahaka ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa madai ya kutaka kesi isimamishwe ili isikilizwe rufaa yao.

Upande wa mashitaka ulipeleka mahakamani hapo notisi ya rufani tarehe 25 Aprili mwaka huu, kupinga kutopokelewa kwa ushahidi wao wa CD na picha zilizopelekwa mahakamani hapo.

Shadrack Kimaro, Mwanasheria Mwandamizi wa Serikali aliiomba mahakama kuwa, kesi hiyo isimamishwe mpaka utakapotolewa uamuzi wa rufaa ya kupinga kukataliwa kwa ushahdi wa CD na picha zilizofikishwa mahakamani hapo kama kielelezo cha kesi hiyo.
 
Shadrack amesema kuwa, ushahidi huo ulioambatana na ripoti ya mtaalamu wa picha na barua ya ZCO iliyokwenda kwa mtaalamu wa picha, vyote vilikataliwa mahakamani hapo.
 
Hata hivyo, upande wa mshtakiwa uliomba mahakama kufuta kesi hiyo kutokana na upande wa mashitaka kukosa ushahidi na kwamba kesi haiwezi kusimamishwa kutokana na kungojaa rufaa iliyokuwa bado haijafunguliwa.
 
Cyprian Mkeha, Hakimu Mfawidhi baada ya kusikiliza pande zote mbili amesema kuwa, kesi hiyo itatajwa tena tarehe 2 Juni mwaka huu.

Rais Magufuli Amteua Dk Asha-Rose Migiro Kuwa Balozi wa Tanzania nchini Uingereza

$
0
0

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Dkt. Asha-Rose Migiro kuwa Balozi wa Tanzania nchini Uingereza.

Dkt. Asha-Rose Migiro anakwenda kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Balozi Peter Kalaghe ambaye amerudishwa nyumbani.

Dkt. Asha-Rose Migiro ataapishwa kesho Alhamisi tarehe 05 Mei, 2016 katika Ikulu ndogo ya Chamwino Mkoani Dodoma.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dodoma
04 Mei, 2016
-------------------------------

Mapito ya Dk. Migiro
Dk. Migiro alizaliwa tarehe 9 Julai  1956 katika Wilaya ya Songea, Ruvuma. Alisoma Shule ya Msingi Mnazi Mmoja, Dar es Salaam mwaka 1963 hadi mwaka 1966.

Dk. Migiro alihamia Shule ya Msingi Korogwe, Tanga ambapo aliendela na elimu ya msingi mwaka 1967–1969.

Baadaye akajiunga kidato cha kwanza mpaka cha nne katika Shule ya Sekondari Weruweru, Kilimanjaro mwaka 1970 hadi 1973 na Kidato cha Tano na Sita katika Shule ya Sekondari Korogwe mwaka 1974 -1975.

Dk. Migiro alikuwa mmoja wa wasichana waliofaulu vizuri Korogwe Sekondari na alipojiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) mwaka 1977, alichukua masomo ya sheria na kuhitimu Shahada yake (LLB) mwaka 1980.

Baadaye aliajiriwa UDSM kufundisha masomo ya sheria kama Mhadhiri Msaidizi. Alifanya kazi hiyo kwa miaka miwili kabla ya kuendelea tena na masomo ya juu ya sheria mwaka 1982–1984 hapohapo UDSM na kutunukiwa shahada ya uzamili (LLM).

Kati ya mwaka 1985–1988, alifundisha UDSM. Mwaka 1988 alikwenda Chuo Kikuu cha Konstanz, Ujerumani ambako alisoma na kutunukiwa Shahada ya Uzamivu (PhD) katika masuala ya Sheria mwaka 1992.

Dk. Migiro alirejea Tanzania akiwa Mhadhiri Mwandamizi na aliendelea kufundisha katika Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam hadi mwaka 2000 alipoingia kwenye siasa.

Akiwa UDSM kati ya mwaka 1992 – 1994 Dk. Migiro alikuwa Mkuu wa Idara ya Sheria za Katiba na Utawala.

Kati ya mwaka 1994 – 1997 aliongoza Idara ya Sheria za Makosa ya Jinai (Idara zote zipo katika Kitivo cha Sheria UDSM).

Dk Migiro ni mzungumzaji mzuri katika lugha ya Kiingereza, Kifaransa na Kijerumani. Ni mke wa Profesa Cleophas Migiro na wana watoto wawili wa kike.

Dk Migiro alianza na siasa za kujijenga akitokea katika taaluma. Mwaka 2000, Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa alimteua kuwa waziri kwenye Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Wanawake na Watoto.

Alitumikia wadhifa huo hadi mwaka 2005 bila kubadilishwa akisimamia mambo mengi ya kisera na kimiundombinu, bila kusahau utekelezaji na upiganiaji wa haki za wanawake na watoto.

Rais Jakaya Kikwete alipoingia madarakani mwaka 2005, alimteua kuwa Mbunge na Waziri wa Mambo ya Nje, Januari 2006 na kuwa mwanamke wa kwanza kuwahi kushikilia wadhifa huo. Katika kipindi cha mwaka mmoja tu, alifanya kazi nyingi za kimataifa zilizomweka katika anga nyingine kisiasa.

Januari 5, 2007, aliteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu (UN) mpaka 2012 alipomaliza muda wake. Januari mwaka 2013, Dk Migiro aliteuliwa kuwa Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) na Desemba 2013 aliteuliwa kuwa mbunge katika Bunge la Tanzania.

Januari 2014 aliteuliwa kuwa Waziri wa Sheria na Katiba, nafasi ambayo alidumu nayo mpaka Rais Kikwete alipomaliza muda wake mwaka jana.

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Alhamisi ya May 5


Rais Magufuli Aokoa Asilimia 4 ya Bajeti

$
0
0

Ndani ya miezi sita tangu aingie madarakani, Rais John Magufuli amefanikiwa kuokoa asilimia nne ya bajeti yake ya kwanza katika hatua alizochukua katika kubana matumizi na kudhibiti ufisadi.

Rais Magufuli aliyeapishwa Novemba  5, mwaka jana alianza kwa kusisitiza kubana matumizi ya Serikali na kuongeza ukusanyaji wa mapato kutoka vyanzo mbalimbali, jambo alilolifanikisha kulingana na ripoti za kila mwezi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

TRA ilitangaza kukusanya Sh1.4 trilioni Desemba mwaka jana, Januari ikakusanya Sh1.08 trilioni na Sh1.04 trilioni Februari kabla haijakusanya Sh1.316 triioni mwezi Machi.

Makusanyo hayo yote yalikuwa ni zaidi ya matarajio. Licha ya mapato hayo yaliyokusanywa kwa taratibu za mamlaka hiyo, Rais Magufuli amefanikiwa kuokoa zaidi ya Sh1.02 trilioni ndani ya muda aliokaa madarakani.

Serikali imependekeza bajeti ya Sh29.5 trilioni kwa mwaka ujao wa fedha. Akisoma makadirio ya mapato na matumizi hayo kwenye kamati za Bunge, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema Sh17.7 trilioni zitakuwa ni za matumizi ya kawaida na Sh11.8 trilioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo. 

Kiasi kilichookolewa na Rais Magufuli  ni takribani nusu ya mapato yatakayotokana na vyanzo visivyo vya kodi na pia zaidi ya mara mbili ya mapato yatakayokusanywa na halmashauri zote nchini kwa kipindi hicho.

Ni fedha nyingi zikilinganishwa na zile zilotolewa na Shirika la Msaada la Marekani (MCC) awamu ya kwanza kutekeleza usambazaji wa umeme vijijini. Ndani ya siku 30 za kwanza; baada ya kufanya safari ya kushtukiza hazina na kutembelea bandarini mara kadhaa aliokoa takribani Sh1 trilioni.

Makontena zaidi ya 2,500 yaliyobainika kuondoshwa bila kulipiwa ushuru na tozo nyinginezo yaliipa Serikali Sh637.2 bilioni. Fedha hizo zilitokana na malipo ya lazima pamoja na faini kwa wakwepaji.

Bado Novemba mwaka jana wakati anazindua Bunge, Rais alikataa kufanya sherehe zilizoandaliwa na wabunge na akaagiza Sh225 milioni zielekezwe kwenye maeneo yenye uhitaji. Maamuzi hayo yalizipeleka fedha hizo kununua vitanda 300, magodoro 300, mablanketi 1,675 na viti vya magurudumu 30 ambavyo vilikabidhiwa kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Kwenye mkutano huo, Rais aliliambia Bunge kuwa hatua yake ya kuzuia safari za nje kwa watumishi wa umma imeokoa Sh356.3 bilioni ambazo zinaweza kujenga kilometa 400 za barabara ya lami.

Desemba 9, mwaka jana, Dk Magufuli aliahirisha sherehe za uhuru na akaagiza Sh4 bilioni zilizotengwa zitumike kupanua barabara kutoka Morocco mpaka Mwenge, jijini hapa. Utekelezaji wa agizo hilo unaendelea.

Muda mfupi baada ya kuteua mawaziri na manaibu wao, alifuta semina elekezi kwa viongozi hao. Hapa aliokoa Sh2 bilioni ambazo zilipangiwa matumizi mengine.

Mapema Aprili alifuta sherehe za Maadhimisho ya Muungano na kuelekeza Sh2 bilioni zilizotengwa kwa ajili hiyo zitumike kupanua barabara ya Uwanja wa Ndege-Mwanza.

Katika kile kilichoonekana kuwa ni kuunga mkono juhudi za kubana matumizi, Bunge liliokoa Sh6 bilioni ambazo ilizikabidhi kwa Rais ili zinunue madawati kwa shule zenye upungufu nchini.

Madaktari Wawili na Muuguzi Wasimamishwa Kazi Kwa Kumtolea Lugha Chafu Mjamzito Aliyejifungulia Chooni

$
0
0

Hospitali ya Rufaa ya Amana, Ilala imewasimamisha kazi madaktari wawili na muuguzi mmoja, kwa madai ya kumtolea lugha isiyostahili mjamzito Asha Said (17), aliyejifungulia chooni.

Tukio hilo lilitokea mwezi uliopita katika hospitali hiyo, baada ya Asha kujifungulia chooni na madaktari na wauguzi hao kumtolea lugha chafu, bila kuelezwa sababu za kufanya hivyo.

Mganga Mkuu wa Amana, Dk Meshack Shimwela alisema jana kwamba watumishi hao ambao hakuwataja wamepelekwa katika Baraza la Watumishi na Madaktari la hospitali hiyo kwa uchunguzi zaidi.

“Kilichotokea siku ile ni kauli zilizotoka kwa watumishi hao kwenda kwa mama aliyejifungua, ambaye pia alikuwa mdogo kiumri.

“Sisi madaktari na waaguzi tuna taratibu za kinidhamu, huwa tunazifuata baada ya watumishi kubainika kufanya makosa, hatua ya kwanza ndiyo hiyo tusubiri nyingine wakati uchunguzi ukiendelea dhidi yao,” alisema Dk Shimwela.

Dk Shimwela ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), alisema kilichohitajika ni lugha nzuri kwa sababu kisheria ni lazima kwa mgonjwa yeyote kuoga akifika hospitali, ili kumkinga na maradhi mbalimbali.

Wakati hayo yakitokea Amana, Chama cha Wakunga Tanzania (TAMA) kimeitaka jamii kuendelea kuibua matukio ya unyanyasaji na huduma mbaya wanazofanyiwa na wakunga wakati wa kujifungua, ili vyombo vinavyohusika viweze kuliona tatizo kwa ukubwa wake na kulifanyia kazi.

Akizungumza katika kongamano la siku mbili la kujadili maendeleo ya wakunga nchini, rais wa chama hicho, Feddy Mwanga alisema kila wanaposikia malalamiko kuhusiana na unyanyasaji na huduma mbaya kwa wajawazito, chama hicho hufanya utafiti na kuchukua hatua stahiki kwa wahusika.

Mitandao yaharibu soko la magazeti, takwimu zaonyesha magazeti yanapitwa na wasomaji wa mitandao

$
0
0

Vyombo vya habari vya asilia hususani magazeti vinakufa. Hivi sasa vvyombo hivyo vinajikongoja kutokana na mauzo hafifu  na mdororo wa mapato kutoka matangazo na kupunguza wafanyakazi.

Ila wakati idadi ya wasomaji wa habari mtandaoni ikizidi kukua, wanaoperuzi mtandaoni  humo hawatumii muda mwingi kwenye magazeti tando, utafiti wa Pew Research Centre unaeleza. 

Katika utafiti wake wa hali ya vyombo vya habari 2015 (“State of the News Media 2015,”) imeonesha kwamba katika vyombo vya habari vya karatasi (print media), Digitali na TV, imeonesha Dhahiri kwamba magazeti yanaelekea kuzimu.

Utafiti huo umetolea mfano magazeti makubwa ambapo wasomaji wake wa mtandaoni wamewashinda kwa mbali kwa idadi ya wasomaji wa makaratasini, ambapo gazeti kubwa sana la New York Times la Marekani limetangaza kuwa nakala zake zipatazo 650,000 kwa wiki zimepitwa kwa mbali sana na wa mitandaoni
Hivi sasa kuna mjadala mitandaoni endapo kama Tanzania iko ama itafika huko. Mabishano ni makali ambapo wa makaratasini wanashikilia msimamo wao kuwa nchini hapa tasni ya habari mtandaoni bado ni change sana kuweza kutishia amani ya magazeti.

Upande wa digitali unajibu kwamba endapo kama kuna wahariri viburi wanaobeza kasi ya mitandao, basi wakae mkao wa kulala njaa muda si mrefu ujao, maana ni wachache wanaoendelea kupata habari kwa njia asili ya magazeti.

Upande wa digitali umeyasifia magazeti ya Global Publishers na la Mwananchi  anbayo ni dhahiri yana wahariri wanaokwenda na wakati na wanaojua nini wanachokifanya kwa kuanza na mapema kuogelea bahari ya maendeleo ya tasnia kwa vitendo kwa kuwa na vitengo vya mtandao vinavyopelekesha mbio magazeti yanayobeza technolojia hio kwa kubuni.

“Ni kweli kwamba Tanzania  bado sana kiteknolojia na miundombini kiasi cha habari za mtandaoni zikatishia uhai wa habari za makaratasini, lakini si uongo kwamba ukizingatia uharaka na gharama pamoja na kwenda na wakati muda si mrefu print media itakwenda na maji”, amesema blogger mmoja ambaye pia ni mwanahabari kwenye moja ya magazeti makubwa nchini.
 

Wanaodai bunge kuonyeshwa live watakiwa kuomba kwa utulivu

$
0
0
Katibu Mkuu wa National Reconstruction Alliance (NRA), Hassan Kisabya Almas amewataka  Watanzania wanaoomba Bunge  la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuonyeshwa  kupitia matangazo ya moja kwa moja (Live) kuomba  kwa utaratibu bila kuharibu amani ya Tanzania.

Aidha Katibu Mkuu wa Chama hicho, amesema  kwamba   amani iliyoko ni hazina kubwa ambayo nchi nyingine inatamani kuwa nayo.

Almas aliyasema hayo jana alipokuwa akiongea na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa Idara ya Habari(MAELEZO).

“Leo hii tupo tunaopigania kutaka kuona Bunge Live, lakini yote haya ni kwa kuwa Tanzania amani tunayo, sidhani kama nchi kama Afghastan siku watakayoamua kuonyesha Bunge Live kwa mwaka mzima, kwa saa 24 kama wataweza kukaa kuangalia Bunge hilo, hivyo basi wale wanaotaka hayo, kwanza tudumishe amani  yetu,” alisema Almas.

Almas alieleza kuwa, amani ya Tanzania ni zaidi ya dhahabu ambayo Tanzania inajivunia hivyo ni lazima Watanzania kuitunza na kuithamini amani ambayo ipo kwa sasa na kuacha kuchochea mambo ambayo yanaweza kuleta machafuko katika nchi na amani ambayo leo haithaminiwi ikaja kukumbukwa siku moja.

Pia, alisema yeye ni mmojawapo wa watu wanaopenda kuona Bunge Live lakini jambo hilo halishadadii kama inavyofanywa na watu wengine kwani anajua kwa kufanya hivyo anaweza kuhatarisha Amani ya Tanzania na hata hilo Bunge halitaweza kuliona tena kutokana na kutokuwa na Amani ndani ya nchi.

Vilevile, amewataka waandishi wa habari kuandika yale yaliyo mazuri ya nchi kuliko mabaya machache ili kuzidi kuitangaza Tanzania vyema kimataifa, kwani sio uzalendo kuona mambo yote mabaya yanakuwa ukurasa wa kwanza, bali kwanza yarekebishwe kwakuwa ni makosa yanayoweza kurekebishwa. Kalamu za waandishi wa habari ni chachu ya amani na maendeleo ya Taifa la Tanzania.

Shirika la Hifadhi la Taifa (TANAPA) Sasa Kuendeshwa Kijeshi

$
0
0

WIZARA ya Maliasili na Utalii imeridhia maombi ya Shirika la Hifadhi la Taifa (TANAPA) kubadili mfumo wa utendaji kazi kutoka ule wa kiraia na kuwa jeshi usu (Paramilitary) ili kukabiliana na tatizo sugu la ujangili wa wanyamapori, misitu, na rasilimali nyingine za nchi.

Akizungumza wakati akifunga mafunzo ya askari na wahifadhi wa shirika hilo, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Jenerali Gaudence Milanzi alisema maombi ya shirika hilo kutaka kubadilishwa na kuendeshwa kwa sheria za kijeshi ni ya msingi katika kipindi hiki ambacho Tanzania inakabiliwa na tatizo sugu la ujangili wa wanyamapori.

Ufungaji wa mafunzo hayo ulifanyika juzi katika kambi ya Mlele ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Katavi mkoani Katavi ambako askari 101 na wahifadhi 26 walihitimu mafunzo ya kijeshi ya miezi mitatu hadi sita 

“Kwa sasa uhifadhi unakabiliwa na changamoto kubwa ya ujangili,hususan tembo na faru kuporomoka kwa maadili ya askari na uingizaji wa mifugo hifadhini,” alisema Meja Jenerali Milanzi.

Aliongeza: “Maombi yenu yamekuja kwa wakati muafaka hivyo tutawasilisha katika mamlaka nyingine za juu za kiserikali, ili yatungiwe sheria na hatimaye kuwasilishwa bungeni ili yajadiliwe na kupitishwa kuwa sheria.”

Hata hivyo, aliwataka askari hao pamoja na Menejimenti ya Tanapa kufanya maandalizi ya kutosha kwa msingi kuwa sheria itakapopitishwa baadhi ya mambo yatabadilika na kuendeshwa kwa mujibu wa taratibu za kijeshi kama ilivyo kwa majeshi mengine nchini.

Awali akiwasilisha maombi hayo, Mkurugenzi Mkuu wa Tanapa, Allan Kijazi alisema shirika hilo baada ya kutafakari kwa kina wakitumia wataalamu wa ndani ya shirika walibaini umuhimu wa askari wao kutumia sheria za kijeshi kutokana na changamoto ya sasa ya katika masuala ya uhifadhi.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Meja Jenerali Mstaafu Raphael Muhuga alielezea umuhimu wa kutunza maeneo yaliyohifadhiwa huku akionya kuwa makundi ya wafugaji yanayovamia maeneo hayo lazima yaondolewe haraka.
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live




Latest Images