Quantcast
Channel: MPEKUZI
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live

Msafara wa Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais (Tamisemi), Seleman Jafo Wapotea Dodoma

0
0

Msafara wa Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais (Tamisemi), Seleman Jafo leo asubuhi ulipotea njia kutokana na watumishi wa Manispaa ya Dodoma kutojua eneo ambalo waziri huyo alikuwa analitembelea.
 
Waziri Jafo alikuwa amepanga kufanya ziara kwenye Shule ya Msingi ya Nzuguni B kwa lengo la kuangalia mapungufu, hasa tatizo la uhaba wa madawati, lakini hakufika kama alivyotarajia kutokana na watumishi hao kutojua eneo ambalo shule hiyo iko.
 
Shule hiyo haijawahi kutembelewa na ofisa elimu tangu mwaka 2007 licha ya kuwa kilomita 6 kutoka katikati ya mji.
 
Naibu Waziri alikasirishwa na kitendo hicho akawataka watumishi wa idara ya Elimu wajipime kama wanastahili kuendelea kufanya kazi.
 
“Mstahiki Meya, mimi niliona wazi kuwa watumishi wako wananipoteza," alisema Waziri Jafo.
 
"Nimechukia sana na hawa watu. Tatizo lao ni kwamba hawajawahi kuja katika shule hii tangu mwaka 2007, lakini wamekaa ofisini tu. Ikiwezekana waondolewe na kupelekwa vijijini,” alisema Jafo.

Katibu Mkuu wa Chama cha ACT-WAZALENDO, Samson Mwigamba Atangaza Kujiuzulu Leo

0
0

Katibu Mkuu wa Chama cha ACT - Wazalendo, Samson Mwigamba amejiuzulu nafasi yake ili apate nafasi ya kwenda masomoni Chuo Kikuu cha Kenyatta nchini Kenya.

Kwa mujibu wa ACT-Wazalendo, kamati ya uongozi imekubali maombi ya Mwigamba na kumruhusu kwenda masomoni na kuwa mchakato wa kujaza nafasi hiyo utaanza mara moja.

Naye Mwigamba ameushukuru uongozi wa chama chake kwa ushirikiano waliompatia tangu chama hicho kinaanzishwa. Amesisitiza kwamba bado ni mwanachama na ataendelea kutoa ushirikiano hata akiwa nje ya nchi.

Mwanasiasa huyo anakwenda kusoma shahada ya uzamili katika masuala ya utawala na usimamizi wa biashara (MBA) na baada ya masomo hayo ataendelea na shahada ya uzamivu (PhD).

Watu Wanne Watiwa Mbaroni Sengerema Kwa Kunywa Pombe Mchana

0
0

Wilaya ya Sengerema imeanza kutekeleza kwa vitendo agizo la Rais baada ya kukamata watu wanane waliokutwa wakinywa pombe saa za kazi.

Amri ya kukamatwa na kuwekwa mahabusu kwa watu hao ilitolewa juzi na Mkuu wa Wilaya Zainabu Terack baada ya kukuta baa zimefunguliwa asubuhi zikiwa na wateja waliokuwa wakipata kinywaji kabla ya saa 9:30 alasiri, muda ambao ofisi za Serikali hufungwa.

Rais John Magufuli alitoa agizo hilo la kupiga marufuku unywaji pombe na uchezaji pool nyakati za kazi wakati alipokuwa akiwaapisha wakuu wa mikoa mwezi uliopita. Alitaka vijana ambao watakaidi maelezo ya kuambiwa, nguvu itumike kuwalazimisha kufanya kazi.

Kwa mujibu wa mkuu huyo wa wilaya, aliyeongoza oparesheni ya dakika 45 ya kusaka wanaokunywa pombe na kucheza pool muda wa kazi, watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani kwa makosa ya uzembe na kukiuka amri halali ya serikali.

Wakijitetea baada ya kutiwa mbaroni, baadhi ya waliokamatwa walidai kuwa walienda baa kujiliwaza wakati wa msiba wa ndugu yao waliyemtaja kwa jina la Petro Shoyo, na kumwomba mkuu wa wilaya kuwasamehe kwa sababu ni kosa lao la kwanza.

Lakini mkuu huyo wa wilaya alisisitiza wapelekwe mahakamani.

Humphrey Polepole , Ali Salum Hapi Waapishwa Rasmi Kuwa Wakuu wa Wilaya

0
0

Wakuu wa wilaya za Kinondoni na Musoma wameapishwa leo baada ya kuteuliwa mapema wiki hii na Rais John Magufuli.
 
Jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Mkoa Paul Makonda amemwapisha mkuu mpya wa Wilaya ya Kinondoni, Ali Salum Hapi, aliyeteuliwa Aprili 18.
 
Ali Hapi amechukua nafasi iliyoachwa wazi na Makonda ambaye aliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam mwezi uliopita.
 
RC Makonda amempa DC huyo vipaumbele saba vya wilaya hiyo, ambavyo alisema kuwa ni pamoja na afya, haki ardhi, rushwa, kero na kushughulikia migogoro.
 
"Natuma salamu kwa wala rushwa na mafisadi wote waliopo Wilaya ya Kinondoni, wanaopora haki za wananchi na rasilimali za nchi ili kujinufaisha wao na familia zao. Nitapambana nao usiku na mchana kuhakikisha ninashinda vita hii," alisema Ali Salum Hapi.
 
Naye mkuu wa Mkoa wa Mara, Magesa Mulongo amemwapisha Humphrey Polepole kuwa mkuu wa Wilaya ya Musoma baada ya kuteuliwa Aprili 18 kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Zelothe Stephen aliyeteuliwa kuwa mkuu wa Mkoa wa Rukwa.

UVCCM Wamjibu Zitto Kabwe

0
0
Kaimu Mkuu wa Idara ya Uhamasishaji,Sera,Utafiti na Mawasiliano,Abubakar D. Asenga 
 
Nimeona taarifa ya Kaka Zitto kabwe akielezea hoja zake kwa msingi wa kukana kumhujumu Rais Magufuli na kuwa waliotoa taarifa hizo wanatumiwa na mmoja wa Mawaziri ( ) wa Serikali ya awamu ya tano.

Kaka Zitto ameenda mbali zaidi akiandika,namnukuu

 “maneno hayo yanaenezwa na watu wanaotumwa na Waziri(anamtaja jina) nina ushahidi usio na mashaka wa waziri( ) kupanga vijana wanaojiita wa UVCCM kufanya Mikutano  na waandishi wa habari na anawalipa fedha kufanya hivyo” mwisho wa nukuu.

Mosi, nimpongeze Mh. Zitto Kabwe kukana kwa sauti ya juu kabisa kuwa hampingi Rais Magufuli na anamuunga mkono katika Ujenzi wa Nchi kama alivyofanya kwa Serikali ya awamu ya nne.Kama ni kweli na lipo kwa matendo Ni jambo jema sana kwa maslahi ya nchi yetu ambalo wapinzani wengine wanapaswa kuliiga.

Pili,Nimthibitishie pasi na shaka ndugu Zitto Kabwe kuwa Vijana hao kama alivyosema (wanajiita wa UVCCM) ni wanajiita tu. 

Vijana wa CCM kama Jumuiya imara ya Vijana wa Tanzania haiwezi kutumika na kulipwa pesa na mtu ili kutumika kwa maslahi binafsi. 

Na kwa kuwa ndugu Zitto amelisema jambo hili kwenye umma na kuwa anao ushahidi wa hao wanaojiita wa UVCCM, tupo tayari kushirikiana nae na ikithibitika kuchukua hatua zaidi kwa mujibu wa Kanuni yetu, vinginevyo tunaona jina la Jumuiya yetu linatumika kama Nyanya kwenye mboga za watu,na hatutakubali hilo.

Tatu. UVCCM inaimani kubwa na Rais Magufuli kuwa hawezi kuwa mtetezi wa Majipu ata kama mwenyejipu kwa madai yako ni rafiki yake, na UVCCM ni kisu cha kumsaidia Rais kutumbua majipu hayo. 

Lakini tunajua kuwa Rais Magufuli ni Rais makini katika atua anazochukua pasi na kumuonea mtu, kwa kuwa  kutumbuliwa jipu kunamaumivu makali sana yanayoweza kuvumiliwa tu na mwenye jipu, asiekuwa na jipu hawezi kutumbuliwa.

Hivyo kama kweli tuhuma hizo zinazotolewa kwa Waziri huyo zina ukweli na zinahusu rushwa na ufisadi Rais angeshamtumbua waziri ama atakuja kumtumbua tu ikishathibitika, tusiwe na haraka,"haraka haraka haina baraka"

MWISHO.
Ushauri kwa kaka Zitto Kabwe, kwa kuwa yeye ni Mbunge na Waziri anaemtuhumu anaingia Bungeni basi ni vizuri akatumia jukwaa hilo kuweka ushahidi wa hoja zake ili zipate majibu ya kina na anaetuhumiwa, kwani nae atakuwa na fursa ya kujibu kwa hoja na ushahidi. 

UVCCM tunachotaka ni mazingatio ya maslahi ya watanzania hasa wengi ambao bado ni masikini.

Tumeendelea mara zote kuwaomba kupata habari sahihi za jumuiya na kuepuka uzushi unaofanywa mara kwa mara kuichafua jumuiya yetu,

UVCCM hutoa taarifa zake kwa utaratibu wake wa kanuni chini ya Mwenyekiti SADIFA JUMA HAMIS kama msemaji Mkuu ama Makamo Mwenyekiti wake Bi.MBONI MHITA ama Kaimu Katibu mkuu SHAKA HAMDU SHAKA au Kaimu katibu wa Idara ya Uhamasishaji,Sera,Utafiti na Mawasiliano MR Abubakar Asenga,pia Naibu Katibu Mkuu Bara Ndugu MFAUME KIZIGO

Kaimu Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Ndugu ABDUGHAFAR IDRISSA ama itakavyoelekezwa vinginevyo

kwa lolote wasiliana nasi kwa
email.uvccm1978@gmail.com
simu - 0627 968 722 AU 0222150743.
 
imetolewa na.
Abubakar D. Asenga
Kaimu Mkuu wa Idara ya Uhamasishaji,Sera,Utafiti na Mawasiliano

UVCCM MAKAO MAKUU
S.L.P 19989
DAR ES SALAAM
April 20,2016

Rais Magufuli Akutana Na Wenyeviti Wa CCM Na Makatibu Wa Mkoa na Wilaya za Tanzania

0
0
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwahutubia Wenyeviti, Makatibu wa Chama cha Mapinduzi wa mikoa na Wilaya za Tanzania bara na Visiwani Ikulu jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya Wenyeviti wa CCM wa Mikoa mbalimbali wakipiga makofi kumshangilia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli wakati akitoa hotuba yake Ikulu jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya Wenyeviti wa CCM wa Mikoa mbalimbali wakipiga makofi kumshangilia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli wakati akitoa hotuba yake Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisikiliza kwa makini taarifa zilizokuwa zikitolewa na baadhi ya Wenyeviti na Makatibu wa CCM kutoka mikoa mbalimbali nchini. Kulia kwake ni makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Makamu Mwenyekiti CCM Taifa Philip Mangula na Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mtwara Mohamed Sinani Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza jambo na mwenyekiti wa CCM mkoa wa Lindi Mzee Ally Mtopa Ikulu jijini Dar es Salaam.

Rais Magufuli Atema Cheche Kuhusu Mafisadi Wanaolalamika Kutumbuliwa Hadharani

0
0

Rais Magufuli leo amekutana na Viongozi wa CCM ngazi za Mikoa na Wilaya kwa lengo la kuwashukuru  kwa kazi nzuri walizofanya wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

Katika hafla hiyo, Rais Magufuli ameeleza kusikitishwa kwake na baadhi ya watu wanaowaonea huruma mafisadi ambao wamekuwa wakitumbuliwa hadharani

Amesema fisadi hastahili huruma kwa sababu yeye wakati anawaibia wananchi hakuwa na huruma

"Wapo Wanaodai Tunakiuka haki za Binadamu Kuwatangaza Wanaotumbuliwa.....Wao walikuwa Wanafanya sawa Kuwaibia Hadharani Watanzania? " Amehoji Rais Magufuli

==> Zaidi, msikilize kwenye video hii akiongea

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Ijumaa ya April 22


Jaji Warioba Azungumzia Uchaguzi Mkuu wa 2015

0
0

Waziri Mkuu mstaafu, Joseph Warioba amesema Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana (2015) ulifanyika kwa haki huku akitaka vyama vya siasa kuwa na demokrasia ndani yao, kuhakikisha wanayotaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) iwafanyie, wao pia wayafanye kwenye vyama vyao.

Amesema nchi inatakiwa kuangalia na kujadili uchaguzi usiwe bidhaa inayotafutwa kwa fedha kama ambavyo ilijitokeza katika uchaguzi wa mwaka jana ambao rushwa ilitumika kwa kiwango kikubwa.

Akizungumza katika mdahalo wa kitaifa kuhusu uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka jana, Warioba pia ametoa angalizo kwa asasi za kiraia kuwa makini na wafadhili wao kuepuka kuingiza matakwa yao (wafadhili) kwenye siasa za ndani.

Mdahalo huo uliofanyika jana jijini Dar es Salaam, ulioandaliwa na Mpango wa Elimu ya Demokrasia Tanzania (REDET) na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, (LHRC).

Akiwasilisha mada, Warioba ambaye amepongeza utendaji wa Rais John Magufuli, alisema uchaguzi mkuu ulikuwa na hamasa ambayo haijapata kutokea lakini ulikuwa huru na ulimalizika kwa amani na utulivu .

Alisema akiwa mmoja wa waangalizi aliyewahi kusimamia chaguzi za Zambia, Malawi, Nigeria, Ghana, Ethiopia na Sudan, anafahamu masuala ya uangalizi na kutoa ripoti. Alisema ni kweli uchaguzi ulienda vizuri. Alisema alipoangalia maoni ya waangalizi wa nje alishangaa kwa mara ya kwanza kusifu mchakato mzima wa uchaguzi.

Alisema licha ya kuwapo kwa upungufu mdogo, waangalizi hao walisifu mchakato mzima na zaidi alishangaa kuona waangalizi ambao wagumu kusifia ; mfano Umoja wa Ulaya (EU), waliridhishwa na uchaguzi huo.

Vyama, asasi vyamulikwa
Hata hivyo alisema, katika kukuza demokrasia kwenye vyama, yapo matatizo na ipo kazi ya kufanya kwa kuwa rushwa imekuwa ikitumika kwa kuwepo matumizi mabaya ya madaraka.

Alisema bila kuleta demokrasia ndani ya chama, ni vigumu kufanikiwa katika kukuza demokrasia nchini.

“Ni rahisi kulaumu Tume ya Uchaguzi (NEC) lakini ndani ya vyama hawafuati yale wanayotaka NEC iwafanyie hivyo lazima kuwe na demokrasia ndani ya chama kwani kukiwa na vyama bila demokrasia hatupati nchi yenye demokrasia hivyo wanasiasa tupige kelele ndani ya vyama siyo NEC,”alisisitiza.

Kwa upande wa asasi za kiraia kuwa walifanya kazi ipasavyo lakini alishauri elimu kwa mpigakura iwekwe kwenye mtaala wa shule nchini na isisubiri kutolewa wakati wa uchaguzi.

Asasi na wafadhili
Akizungumzia nafasi ya asasi za kiraia, alisema zipo baadhi katika kutoa elimu, ziligeuka wanaharakati na kufikia kuhamasisha wachague chama au mgombea yupi .

Alisema walifanya hivyo ikidaiwa ni matakwa ya wafadhili jambo alilosema kwamba ni hatari masharti ya wafadhili kuingilia siasa za nchi.

Wanahabari
Jaji Warioba alizungumzia pia ushiriki wa vyombo vya habari katika uchaguzi huo na kusema vyote vilikuwa na upendeleo. Alisema hata magazeti yaliyosifika kwamba hayana upendeleo, yalizidi na mpaka sasa vyombo hivyo vina upande wake.

Alitaja baadhi ya mambo ya kuboresha ni mfumo wa kisheria na kitaasisi kwa kuboresha katiba kukuza demokrasia.

Alisema ushindi wa rais uhojiwe mahakamani na kuwepo kwa kura za uwiano kwa wabunge kuleta usawa wa kijinsia pamoja na vyama vidogo vya siasa kukua.

NEC kulalamikiwa
Alisema lazima kuwa na tume inayoaminika na wote ambayo haitawekwa wanasiasa.

Akizungumzia suala la gharama za uchaguzi,Warioba alisema sheria ipo lakini haitekelezwi kwani vyama vikubwa vinapata faida kuliko vidogo .

Alisema uchaguzi mkuu wa mwaka jana ulikuwa ni wa fedha hivyo kugeuka bidhaa kwa wenye fedha kushinda.

Alisema athari zilizojitokeza katika uchaguzi mkuu ni lugha iliyotumika ya kukebehi ,kukejeli na matusi ikiunganishwa na ushabiki hali iliyoacha makovu na uhasama katika jamii na miongoni mwa viongozi .

Alisema kumekuwa na nyufa katika taifa kwa kuwepo rushwa na ubaguzi kwani rushwa imekuwepo katika ngazi zote za mchakato wa uchaguzi kuanzia uteuzi wa wagombea ndani ya vyama mpaka kutangaza matokeo.

Alisema kumekuwa na ubaguzi wa kila aina ikiwemo ukabila, dini na kikanda ambao nyuma ulijulikana kijiografia lakini sasa zinatumika kisiasa .

Alisema zipo nyufa mpya zinazoanza kujitokeza baina ya wazee na vijana.

Mdahalo huo uliokuwa na kaulimbiu ya ‘Tathmini ya Uchaguzi Mkuu wa Tanzania mwaka 2015: Mchango wa waangalizi wa ndani kuelekea uchaguzi bora, huru na haki’, mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe.

Mwakyembe alisema takwimu za mwaka 2013-2014 zinaonesha kuwa kwa ujumla demokrasia nchini inazidi kuimarika na kushamiri.

Waziri alisema inaonesha kuwa Tanzania ilikuwa nchi ya 83 ikiwa na alama 50.5 kwa kukidhi vigezo vya demokrasia, ikilinganishwa na Kenya iliyochukua nafasi ya 93 ikiwa na alama 48.1. Zambia ilichukua nafasi ya 94 alama 48.1; Nigeria nafasi ya 107, alama 40.6 na Afrika ya Kusini ikichukua nafasi ya 71 alama 54.7.

Majambazi Yaua Wanne na Kupora Supermarket

0
0

Wakazi wanne wa jijini Tanga wamekufa papo hapo na wengine wawili kujeruhiwa kwa risasi na majambazi .

Majambazi hao waliokuwa na bunduki aina ya SMG , walivamia juzi duka kuu (supermarket) la mfanyabiashara Hamoud Ali lililopo Mtaa wa Swahili katika kata ya Central jijini Tanga .

Waliokufa katika tukio hilo ni Ahmed John, Vitus Manfred ambaye ni dereva wa gari la Mahakama ya Hakimu Mkazi Tanga, Athumani Seya pamoja na Ali Mpemba ambaye ni mfanyakazi kwenye duka hilo.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga, Leonard Paul tukio hilo ni la juzi saa 1.30 usiku.

‘’Wakati biashara inaendelea ndani ya hilo duka kuu , ghafla waliingia watu wengine zaidi kama wateja ambao baada ya muda mfupi walibadilika na kutoa silaha za moto”, alisema.

Aliongeza“Kitendo chao hicho kilienda sambamba na amri ya kuwataka watu wote waliokuwa humo dukani kulala chini ambapo inadaiwa walitii na kisha wakaamua kuwapiga risasi maeneo ya kichwani wateja wanne waliokuwemo.”

Kamanda alisema majambazi hao walipora Sh milioni 2.7 na kukimbilia kusikojulikana.

UKAWA Waibuka Kidedea, CCM Wabwagwa Unaibu Meya Jiji la Dar es Salaam

0
0

Diwani  wa Kata ya Kiwalani, Mussa Kafana (Cuf), ameibuka mshindi katika uchaguzi wa Naibu Meya wa Jiji la Dar es Salaam, kwa kumbwaga mpinzani wake kwa kura nne.

Uchaguzi huo ulifanyika jana katika ukumbi wa Karimjee, baada ya madiwani wa jiji hilo, ambao pia ni wajumbe wa Baraza la Halmashauri ya jiji hilo kuapishwa.

Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo, Kaimu Mkurugenzi wa jiji hilo, Sarah Yohana alisema, Kafana ameibuka mshindi kwa kura 10 huku mpinzani wake Mariam Lulida (CCM) akipata kura sita. 

“Kura zilizopigwa ni 16 na hakuna iliyoharibika. Namtangaza Mussa Kafana kuwa Naibu Meya wa Jiji la Dar es Salaam,” alisema Yohana. 

Awali Meya wa jiji hilo, Isaya Mwita alisema, baraza hilo lina jukumu la kuhakikisha linatekeleza majukumu yake ipasavyo na kila mjumbe kupitia chama chake anapaswa kutoa mchango utakaoweza kulibadilisha Jiji la Dar es Salaam.

Akizungumza baada ya kutangazwa kuwa mshindi, Kafana aliwashukuru wajumbe wa baraza hilo huku akiahidi kushirikiana nao bila kubagua itikadi za vyama vyao, kwani wanafanya kazi kwa ajili ya wananchi na si vyama vyao. 

Alisema kwa sasa vyama havina nafasi bali maendeleo ya wananchi wa jiji hilo ndio muhimu.

Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Huduma za Sheria kutoka Ofisi ya Rais, Tamisemi, Eustard Ngate, alisema, Halmashauri ya jiji hilo ilishawahi kuvunjika mara mbili mwaka 1983 na mwaka 1996 kutokana na viongozi wake kushindwa kuwajibika hivyo hawategemei hilo litokee

Mkuu wa Mkoa wa Lindi Amtumbua JIPU Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Lindi

0
0

Serikali ya Mkoa wa Lindi imemsimamisha kazi Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Lindi, Oliver Vavunge na kumwomba Waziri Mkuu amsimamishe kazi Kaimu Mkurugenzi wa Tume ya Kilimo cha Umwagiliaji Maji Taifa kutokana na hasara ya Sh milioni 500 katika mradi wa umwagiliaji maji wa Kiwalala Narunyu, Lindi.

Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi aliyasema hayo jana wakati alipozungumza na wananchi kwenye Uwanja wa shule ya msingi ya Kiwalala wilayani humo juzi.

Zambi alisema kati ya fedha zilizowekwa kwa ajili ya kutekeleza mradi wa umwagiliaji maji ni Sh milioni 700, kati ya hizo Sh milioni 500 zilishatumika na kubakia Sh milioni 200.

Alisema mradi huo ulioanza mwaka 2011 mpaka mwaka huu haujakamilika na fedha zilishachukuliwa, na kufafanua kuwa mkurugenzi anaingia hatiani kutokana kutokuwa makini juu ya mradi huo katika usimamizi.

Alitoa fedha kwa nyakati tofauti kumlipa mkandarasi wa kwanza na kuvunja mkataba naye Sh milioni 121, wa pili alivunja na alitoa Sh milioni 226 na Sh milioni 116, mwaka jana.

Zambi alisema fedha hizo zilikuwa zinachukuliwa baada ya makandarasi wakidai kwa kazi walizokuwa wakizifanya kwa kuweka miundombinu ya shamba hilo.

Alisema Tume ya Umwagiliaji Maji nayo wataalamu wake hawakuwajibika ipasavyo juu ya usimamizi wa mradi huo kwani wao ndiyo waliotia hasara kwa mamlaka kutokana na barua zao walizokuwa wanaziandika juu ya mradi huo.

Barua ya kutoka Ofisi ya Kanda ya Kusini Tume ya Umwagiliaji Maji iliyoandikwa Septemba mwaka jana ilieleza kuwa mradi huo unatekelezeka kwa kiwango hicho cha fedha, na Novemba 27, mwaka jana, Kaimu Mkurugenzi wa Umwagiliaji Maji alifika na kuandika barua kuwa mradi huo hauwezi kutekelezeka, kinachotakiwa ni kufanya tathmini upya.

Alitoa ushauri kujenga banio dogo. Zambi alisema kwa jumla ushauri wao haukuwa mzuri na kusababisha hasara kwa mamlaka husika.

Watumishi 105 Kupelekwa Ofisi za Balozi Nje ya Nchi.....79 Kurejeshwa Nchini

0
0

Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki Kikanda na Kimataifa imejipanga kuwapeleka kwenye Balozi zake nje Watumishi wapatao 105 na kuwarejesha nchini wengine 79 ambao miongoni mwao muda wao wa utumishi balozini (Tour of Duty) umemalizika na wengine kustaafu kwa mujibu wa sheria za Utumishi wa Umma. Kwa kawaida tour of duty kwa Watumishi nje ni ya muda wa miaka minne (4).

Tanzania ina Balozi 35 nje ya nchi ambazo kwa ujumla wake zina Watumishi 234. Miongoni mwa Watumishi watakaorejea nchini wamo Mabalozi, Maafisa, Wahasibu na Makatibu Muhtasi.

Hadi sasa Mabalozi waliorejea nchini ni watatu (3) ambao ni Balozi Peter Kalaghe aliyekuwa Uingereza, Balozi James Msekela aliyekuwa Italia na Balozi Batilda Burian aliyekuwa Japan.

Itakumbukwa kuwa, Januari 25, 2016 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli aliiagiza Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa kuwarejesha nyumbani mara moja Mabalozi hao ambao mikataba yao iliisha na wengine kwa ajili ya kupangiwa majukumu mengine.

Aidha, jumla ya Watumishi tisa  wa kada mbalimbali waliokuwa Balozini wamerejea nchini hadi sasa na wengine wanaendelea kurejea kulingana na upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kufanikisha jukumu hilo.

Utaratibu wa kuwapeleka na kuwarejesha Watumishi Balozini ni wa kawaida na upo duniani kote kwa mujibu wa sheria za kimataifa ukiwemo Mkataba wa Vienna unaotoa mwongozo kwenye masuala ya kidiplomasia.

Wizara itaendelea kupeleka Watumishi wenye sifa na tija kwa taifa ili kuiwakilisha nchi kikamilifu.

WAKATI HUOHUO, Waziri wa Viwanda na Biashara wa Oman Mhe. Dkt. Ali Bin Masoud Al Sunaidy alifanya ziara  ya kikazi nchini Tanzania kuanzia tarehe 12 April hadi 14 April, 2016.

Lengo la ziara hiyo lilikuwa ni  kushiriki Kongamano la Biashara na Uwekezaji baina ya Tanzania na Oman, kongamano hili lilikuwa na kauli mbiu ya ‘’ Oman Tanzania Road show : Exploring Opportunities in Investment and Business between Tanzania and Oman’’.

Ziara na kongamano hili  imelenga zaidi katika sekta za Madini, Kilimo na uboreshaji wa mazao ya Kilimo, Mifugo, Miundombinu na Mawasilisno, Uvuvi, Usafirishaji, Utalii, Petroli na Gesi. Mgeni Rasmi katika kongamano hili alikuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan

Katika ziara hii, Mhe. Waziri Al Sunaidy aliongozana na ujumbe wa watu 108 ambapo 12 walikuwa ni Maafisa kutoka Taasisi mbalimbali za Serikali ya Oman na wengine waliobaki kutoka Sekta Binafsi kutoka nchi hiyo kwa lengo la kukutana na Taasisi kama hizo hapa nchini.

Kwa upande wa Tanzania wafanyabiashara 190 walishiriki na wenzao kutoka Oman katika kongamano na baadae katika mikutano ya ana kwa ana (Business to Business meetings).

MAFANIKIO YA ZIARA

1.Wakati wa ziara hiyo, Tanzania na Oman zilisaini mkataba wa makubaliano ya ushirikiano baina ya Tanzania Chambers of Commerce  na Oman Chambers of Commerce wa kuanzisha Kampuni ya Oman Tanzania Investment Company (OTIC). Kampuni imeanzishwa kwa lengo la kutafuta fursa za uwekezaji Tanzania na Oman na imeazimia kuanza na mtaji wa Dola za Marekani milioni 25 ambazo zitatumika kutoa mikopo kwa wawekezaji ;

2.Serikali ya Oman imeonesha nia ya kuwekeza katika kiwanda cha Sukari cha Kagera (Kagera Sugar) na kukipa uwezo wa kuzalisha tani 400,000 ambazo zitauzwa katika soko la Tanzania. Uzalishaji huu pia utahusisha uzalishaji wa Umeme, spiriti na hamira  itokanayo na mabaki katika kuchakata sukari. Umeme utaingizwa katika gridi ya Taifa wakati spiriti ambayo ni muhimu katika matumizi ya tiba itauzwa katika masoko ya ndani na nje ya Tanzania. Aidha, Oman inahitaji hamira ambayo inahitajika kwa kiasi kikubwa nchini humo na nchi zingine za mashariki ya kati ;

3.Mbali na uzalishaji wa sukari, Serikali ya Oman pia inakusudia kuingia ubia na Kagera Sugar katika kilimo cha umwagiliaji cha uzalishaji wa mazao ya chakula kwa ajili ya matumizi ya Oman na Tanzania. Utekelezaji wa miradi hii utaleta faida kwa Tanzania ikiwa ni kuongeza uzalishaji wa sukari na hivyo kupunguza pengo kati ya uzalishaji na mahitaji halisi ya sukari, lakini pia unategemea kuzalisha nafasi zaidi ya 5,000 za ajira na hivyo kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira ;

4.Serikali ya Oman pia ilionyesha nia yake ya kuangalia uwezekano wa kuwekeza katika mradi wa uboreshaji na upanuzi wa bandari ya Tanga lakini pia kuziwezesha bandari za Tanzania kuwa na ushirikiano na zile za Oman ;

5.Wawekezaji kutoka Oman pia wameonyesha nia ya kuwekeza katika ujenzi wa nyumba za kisasa mkoani Mtwara ili kuondoa tatizo la makazi stahili kwa watendaji wakuu wa makampuni ya mafuta na shughuli zinazoendana na sekta hii ambao hulazimika kila siku kusafiri kwa ndege kutoka Dar Es Salaam kwenda Mtwara na kurudi jambo ambalo lina gharama kubwa pamoja na ombi la ekari 1,000 kwa ajili ya kilimo cha mboga mboga na maua;

6.Wawekezaji kutoka Oman pia wameonyesha nia ya kuwekeza katika maeneo kadhaa ikiwemo uzalishaji wa mitamba na chakula cha mifugo huko Mivumoni, Tanga, ranchi na machinjio ya Ruvu, miundombinu na viwanja vya ndege, ujenzi wa nyumba za kisasa  Kigamboni na Zanzibar pamoja na miradi mingine katika sekta ya utalii  pamoja na kuwekeza katika sekta ya viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo na mifugo ;

7.Wafanyabiashara wa Tanzania wamepata nafasi ya kutambua fursa zilizopo Oman ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa soko kwa bidhaa za chakula kama vile matunda, nyama, unga, sukari, hamira nk; na

8.Tanzania kwa ujumla ilinufaika kwa kutangaza fursa za uwekezaji ambazo zipo katika sekta zinazolengwa na wawekezaji wa Oman lakini pia kubaini fursa zilizopo Oman ambazo wafanya biashara wa Tanzania wanaweza kunufaika nazo pamoja na kuwaunganisha wafanya biashara wa Tanzania na wenzao wa Oman katika kukuza biashara na uwekezaji baina ya nchi zetu.

Hivyo, utekelezaji wa matarajio haya unategemea kuongeza ajira, kuongeza ubora na thamani ya mazao ya kilimo na kutanua wigo wa masoko kwa bidhaa za Tanzania na pia kukuza sekta ya viwanda nchini.

Imetolewa na:
Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki Kikanda na Kimataifa 

Hatima ya Mkataba Tata wa Lugumi Mikononi mwa Spika Job Nduagai

0
0

Hatima ya mkataba tata wa kampuni ya Lugumi Enterprises ipo mikononi mwa Spika wa Bunge, Job Ndugai baada ya jana, Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuwasilisha muhtasari wa ilichokibaini baada ya kupitia maelezo ya utekelezaji wake.

Moja kati ya mambo yaliyomo katika muhtasari huo ni kulitaka Bunge kutoa ruhusa kwa kamati ndogo iliyoundwa na PAC juzi kuchunguza kwa kina mkataba huo wa kufunga mtambo wa utambuzi wa vidole (AFIS), ikiwa ni pamoja na kutembelea vituo vinavyodaiwa kufungwa mashine hizo.

Kamati ya PAC ilinusa ufisadi kwenye mkataba huo wa AFIS ulioitaka Lugumi kufunga mitambo kwenye vituo vya polisi 108 kwa gharama ya Sh37 bilioni lakini ilibainika kwamba kampuni hiyo ililipwa kiasi cha Sh34 bilioni zaidi ya asilimia 90 ya fedha zote ilhali imefunga mashine 14 tu mkoani Dar es Salaam.

Makamu Mwenyekiti wa PAC, Aeshi Hilaly alisema jana muda mfupi baada ya kukutana na Spika kuwa wamepeleka mapendekezo hayo na wanachokisubiri ni kauli ya ofisi yake.

Muhtasari huo umekuja siku moja baada ya PAC kuwaweka kitimoto Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Jenerali Projest Rwegasira na Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi, Abdulrahman Kaniki kuhusu mkataba huo. 

Bunge liliagiza maelezo ya kina kwa maandishi kuhusu utekelezaji wa mradi huo baada ya kubaini kuwa una maswali mengi kuliko majibu na liliwaita viongozi hao ili kupata ufafanuzi wa kina.

Katika maelezo yake jana, Aeshi alisema kesho watakuwa wameshapata majibu kutoka Ofisi ya Spika na wataweka wazi mambo yote waliyokuwa wakiyajadili kuhusu Lugumi.

“Hili ni jambo zito ambalo linahusu usalama kwa hiyo ni lazima twende nalo taratibu ili kujua ukweli na kuja na majibu ya kueleweka... kila kitu tutawaeleza Jumamosi,” alisema.

Daladala kuingia katikati ya Jiji la Dar es Salaam mwisho Mei 2, kupisha Mabasi yaendayo kasi ya Dart

0
0

Daladala zinazofanya safari zake katikati ya jiji la Dar es Salaam  zimetakiwa  kuondoka   ifikapo Mei 2 Mwaka huu ilikupisha mradi wa mabasi yaendayo kasi kuweza kufanya shughuli zake kuanzia hiyo Mei 10.
 
Juzi, Waziri wa Nchi, ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene alisema mradi huo utaanza kutoa huduma kwa wakazi wa jiji hilo Mei 10.

Msemaji wa mradi huo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Mkoa wa Dar es Salaam (Dacoboa), Sabri Mabrouk alisema wamiliki wote wa daladala walilipwa fidia ya kubadili njia.

“Wamiliki wa mabasi walishalipwa fedha zao tangu Desemba mwaka jana, hakuna anayedai na tumewapa siku saba kuondoka barabarani kabla ya Mei 10,’’ alisema.

Mabasi hayo zaidi ya 30 ya Darts yalianza kupita kwenye njia zote za mradi huo. Changamoto kubwa inayolalamikiwa ni muingiliano wa daladala, magari binafsi, pikipiki na raia kupita bila tahadhari kwenye njia za mradi.

Moja ya mabasi hayo jana lilipata ajali baada ya kukwaruzana na pikipiki eneo la Kinondoni.

“Nasikitika pikipiki zinapita wala madereva hawaangalii, wameshakwaruzana na basi la mradi, sijui itakuwaje mradi utakapoanza, elimu inahitaji kwa wananchi bila hivyo tutawapoteza wengi,” alisema Mabrouk 

Alisema wamelazimika kufanya majaribio bila ya kubeba abiria kwa zaidi ya wiki kwa kuwa nauli mwafaka haijajulikana.

Milioni 50 za Rais Magufuli Kila Kijiji Zazuzua Kizaazaa

0
0

WAZIRI wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama alisema serikali imeweka utaratibu mzuri wa fedha za ahadi ya Rais ya milioni 50 kila kijiji, ili Watanzania wote wanufaike bila kujali itikadi zao za kisiasa.

Alisema hayo bungeni mjini Dodoma jana wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Buyungu, Kasuku Bilango(Chadema) aliyetaka kusikia kauli ya serikali juu ya mgawanyo wa fedha hizo akisema ipo mizengwe kwamba fedha hizo zitatolewa kwa wanachama wa CCM .

“Serikali itoe kauli fedha hizo zitatolewa kwa utaratibu gani,” alihoji.

Mhagama alisema fedha hizo ni ahadi ya Rais aliyotoa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu ambao Watanzania walichagua Serikali ya CCM.

Alisema serikali inatumikia Watanzania wote bila kujali itikadi za vyama vyao.

Alisema Baraza la Uwezeshaji Kiuchumi limeanza kutengeneza utaratibu wa namna ambavyo fedha hizo zitanufaisha Watanzania wote.

Alisisitiza kuwa serikali iko imara kuhakikisha fedha hizo zinanufaisha Watanzania wote.

Awali, Mbunge wa Viti Maalumu, Halima Bulembo (CCM), katika swali la msingi, alitaka kufahamu ni lini ahadi hiyo ya kutoa Sh milioni 50 kwa kila kijiji itatekelezwa.

Alitaka kufahamu pia vijana watapata mgao wao kwa asilimia ngapi.

Mbunge huyo pia alitaka kujua mikakati ya serikali katika kuwawezesha vijana wawe wajasiriamali kwa kuwapa mitaji, mikopo na vigezo gani vitakavyosimamia na kuwalinda na kuweka usawa wa upatikanaji wa ushiriki wao katika fursa hizo.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Antony Mavunde alisema ahadi ya Rais ya Sh milioni 50 kwa kila kijiji itaanza kutekelezwa kwa mwaka wa fedha ujao 2016/2017.

Alisema utaratibu wa kugawa fedha hizo unaandaliwa na Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kwa kushirikiana na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.

Mshahara wa Rais Magufuli Watua Bungeni.......Mbunge wa Chadema Ataka Upunguzwe na Akatwe Kodi

0
0

Suala la mshahara wa Rais, limeibuka tena bungeni ambapo Bunge limeelezwa kwamba kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais hawezi kujipunguzia mshahara pindi anapoapishwa kushika wadhifa huo.

Hayo yalisemwa bungeni mjini Dodoma  jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Simbachawene, kupitia taarifa aliyoitoa kwa Bunge baada ya Mbunge wa Viti Maalumu, Upendo Peneza (Chadema) kumuomba Rais John Magufuli kujipunguzia mshahara.

Mbunge huyo aliyasema hayo wakati akijadili Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa 2016/17 hadi 2021, ambapo pamoja na kusifu jitihada za Rais Magufuli kwa kuonesha dhamira ya wazi ya kuwajali wananchi masikini na kudhibiti matumizi ya serikali, alimuomba kupunguza mshahara wake na pia kuruhusu ukatwe kodi.

“Kwa kweli kwa dhati kabisa nampongeza sana Rais Magufuli kwa namna anavyoonesha wazi kwamba ana dhamira ya kuwatumikia Watanzania. Kwa namna anavyokwenda ni wazi kwamba Rais Magufuli anakuwa Rais wa pili kuwa na mapenzi ya dhati kwa Watanzania baada ya Rais Nyerere (Julius- Baba wa Taifa).

“Pamoja na hayo, kama anataka awe kama Mwalimu Nyerere basi ni wakati sasa wa Rais Magufuli kuchukua hatua za kujipunguzia mshahara wake na pia kuruhusu mshahara wake kukatwa kodi, hili litampa heshima kubwa sana Rais wetu,” alisema Peneza.

Akitoa taarifa kwa Bunge, Waziri Simbachawene alisema kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 pamoja na marekebisho yake, Ibara ya 43, Ibara ndogo ya 3, Ukurasa wa 62 inamzuia Rais kupunguza mshahara akiwa madarakani.

Alisema; “Ibara hiyo inasema hivi: ‘Mshahara na malipo ya Rais, havitapunguzwa wakati Rais anapokuwa bado anashika madaraka yake. 

“Rais aliyepo sasa hawezi kujipunguzia mshahara wake yeye mwenyewe isipokuwa anapoondoka anaweza kuweka kiwango cha mshahara cha Rais ajaye.

"Kwa hiyo wakati wabunge mnaendelea kumuomba Rais apunguze mshahara wake ni lazima mjue jambo hilo ni kinyume cha Katiba”. 

Ufafanuzi huo wa Waziri umekuja siku chache wakati Rais Magufuli akiwa tayari amejitangazia mbele ya umma kiwango cha mshahara anacholipwa akisema ni Sh milioni 9.5 kwa mwezi.

Rais aliyasema hayo akiwa nyumbani kwake Chato mkoani Geita wakati alipokwenda kwa mapumziko mafupi hivi karibuni, hatua ambayo ilipokelewa kwa shangwe na wananchi wengi

Asilimia 18 Ya Simu Za Kiganjani Zaonekana Ni Bandia ,huku Asilimia 79 Zikiwa Salama

0
0

MAMLAKA ya mawasiliano Tanzania (TCRA) imesema kuwa asilimia 79 ya simu za kiganjani zilizofanyiwa utafiti kwa kipindi cha desemba hadi February mwaka huu ziko salama na sio za bandia ,huku asilimia 18 zikionekana zikiwa za bandia hivyo kuwataka wananchi kutambua kuwa simu feki zilizoko sokoni ni chache tofauti na kipindi cha nyuma.

Pia imebainika kuwa asilimia kubwa ya nyumba zinazoungua na umeme ni kutokana na simu bandia ambazo betri zake au vifaa vyake hushindwa kuhimili  mionzi pindi zinapokuwa zinachajiwa hivyo kusababisha mlipuko wa moto na hivyo kuleta madhara .

Hayo yalisemwa na meneja uhusiano wa mamlaka ya mawasiliano Tanzania Innocent Mungi alipokuwa akizungumza katika semina ya mfumo wa rajisi ya  namba za utambulisho wa simu za kiganjani iliyowashirikisha wadau na wafanyabiashara wa jijini hapa.

Alisema kuwa kutokana na elimu ambayo wameitoa kwa wafanyabiashara wa simu  hizo ya kuhakiki kwanza kabla ya kuwauzia wananchi imepunguza uingizaji wa simu feki na kwamba wamebaini kuwa asilimia 79 ni salama hazina matatizo ya aina yeyote.

Alidai kuwa kufuatia uzimaji wa simu bandia litakalofanyika juni 16 mamlaka hiyo imeweza kutoa elimu kwa wauzaji,watumiaji ili kuhakikisha kuwa wanabini simu zao kama ni salama ili kuweza kuepuka zoezi la kuzimiwa simu zao bila yawao kujiandaa.

“Wakati tumeanza kubaini zoezi la kutambua simu feki tulibaini kuwa asilimia 30 zilikuwa bandia ila kutokana na elimu iliyotolewa hadi February simu bandia zimepungua hadi kufikia asilimia 18 hii inaonyesha kuwa simu feki zilizoko sokoni ni chache mno “aliongeza .

Aidha Innocent alitaja faida za kuzimiwa simu bandia kuwa ni pamoja na kuongeza usalama mtandaoni kwa watumiaji wa simu ,kupunguza wizi wa simu  na kupunguza matukio ya uhalifu ambayo yamekuwa yakitumika mara nyingi kwanjia ya simu hizo pamoja na kuzuia matumizi ya simu zisizokuwa na viwango.

Awali mkurugenzi mkuu wa mamlaka hiyo Ally Simba aliwataka wananchikufanya zoezi la kuhakiki simu zao kwa kufuata maelekezo sahii ili waweze kubaini simu feki kabla ya kuzimiwa simu hizo juni 16 ,kwani wengi wa watumiaji wa simu hawafuati malekezo ya kutambua simu bandia .

Simba aliseama kuwa ni vema wananchi wakatumia mfumo waliowekewa wa kubaini  simu zao kama ziko salama kwani ifikapo juni simu zote bandia zitazimwa na kuwataka wafanyabiashara nao wawe makini pindi wanaponunua mizigo yao ya bashara ili kuepuka hasara watakazozipata wao na pia hasara watakazopata wanunuzi wa simu hizo .

Rais Magufuli Afanya Mazungumzo Na Mabalozi Watatu Kutoka Nchi Mbalimbali Ikulu Jijini Dar Es Salaam Leo.

0
0
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana Balozi wa Vatican hapa nchini anayemaliza muda wake Francisco Montecillo Ikulu jijini Dar es Salaam. Balozi huyo wa Vatican alifika Ikulu kwa ajili ya kuagana na Rais Dkt. Magufuli mara baada ya kumaliza muda wake ya Ubalozi nchini.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na mgeni wake Balozi wa Vatican hapa nchini anayemaliza muda wake nchini Francisco Montecillo

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiagana na Balozi wa Vatican hapa nchini anayemaliza muda wake Francisco Montecillo  Ikulu jijini Dar es Salaam.

Balozi wa Algeria hapa nchini Belabed Saada akikabidhi ujumbe uliotoka kwa Rais wa Algeria kuja kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Balozi wa Canada hapa nchini Alexandre Leveque Ikulu jijini Dar es Salaam. Balozi huyo wa Canada alifika Ikulu na ujumbe wake  kwa ajili ya kufanya mazungumzo na Rais Dkt. Magufuli

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha na Balozi wa Canada hapa nchini Alexandre Leveque wapili kutoka kulia pamoja na waakilishi wengine wa Serikali pamoja na Ubalozi wa Canada.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli  akiagana na Balozi wa Canada hapa nchini Alexandre Leveque mara baada ya kumaliza mazungumzo yao Ikulu jijini Dar es Salaam. 
 
PICHA NA IKULU

Taarifa ya Ikulu Baada ya Rais Magufuli Kukutana na mabalozi wa Canada na Aljeria

0
0
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameikaribisha nchi ya Canada kushirikiana na serikali yake ya awamu ya tano katika kuleta mageuzi ya kiuchumi, hususani katika uwekezaji kwenye sekta ya Kilimo, Madini, Uvuvi na Huduma za kijamii.

Rais Magufuli ametoa ujumbe huo alipokuwa akizungumza na Balozi wa Canada hapa nchini Mheshimiwa Alexandre Le've'que aliyekutana nae Ikulu Jijini Dar es salaam na kupokea barua yenye ujumbe wa Waziri Mkuu wa Canada Mheshimiwa Justin Trudeau.

Katika mazungumzo hayo, Rais Magufuli amesema serikali yake hairidhishwi na jinsi kilimo cha Tanzania kisivyowanufaisha wakulima ipasavyo, na hivyo ameikaribisha nchi ya Canada hususani sekta binafsi ya nchi hiyo kushirikiana na Tanzania kujenga viwanda vya kusindika mazao ya kilimo na uvuvi ili kuzalisha ajira na kuongeza thamani ya mazao kwa manufaa ya wananchi wa nchi zote mbili.

Dkt. Magufuli pia ametaka Canada yenye uwezo mkubwa kiteknolojia na mtaji ishirikiane na Tanzania katika uwekezaji kwenye sekta ya madini na gesi kwa kujenga viwanda vya kuchakata madini ndani ya nchi ya Tanzania na pia rasilimali ya gesi ambayo mpaka sasa Tanzania imethibitika kuwa na hifadhi ya futi za ujazo zaidi ya Trilioni 57.

"Mheshimiwa Balozi Alexandre Le've'que naomba ukamweleze Waziri Mkuu wa Canada Mheshimiwa Justin Trudeau kuwa Tanzania na Canada sio tu ni nchi marafiki bali pia ni ndugu wenye uhusiano wa kihistoria. Ningependa kuona Canada inashirikiana na serikali yangu, katika juhudi zake za kuachana na usafirishaji wa mchanga wa madini badala ya madini yaliyochakatwa na pia kuachana na usafirishaji wa mazao yakiwa ghafi" Amesema Rais Magufuli.

Kwa upande wake Balozi wa Canada hapa nchini Mheshimiwa Alexandre Le've'que amemhakikishia Rais Magufuli kuwa atafikisha ujumbe huo kwa Waziri Mkuu Canada Mheshimiwa Justin Trudeau, na amebainisha kuwa nchi hiyo ipo tayari kushirikiana na Tanzania katika juhudi zake za kuimarisha uchumi, hasa baada ya kujionea juhudi za Rais Magufuli katika kukabiliana na rushwa, kuongeza ukusanyaji wa mapato na kusimamia nidhamu ya kazi kwa watumishi wa umma.

Wakati huo huo, Rais Magufuli amepokea ujumbe kutoka kwa Rais wa Aljeria Mheshimiwa Abdelaziz Bouteflika ambaye pamoja na kumpongeza kwa hatua anazochukua katika uendeshaji wa serikali, amemhakikishia kuwa Aljeria ipo tayari kuendeleza na kuimarisha ushirikiano uliopo kati yake na Tanzania huku akitaja maeneo ya kipaumbele kuwa ni nishati na kilimo.

Ujumbe wa Rais Bouteflika umewasilishwa kwa Rais Magufuli Ikulu Jijini Dar es salaam na Balozi wa Aljeria hapa nchini Mheshimiwa Belabed Saada.

Rais Magufuli amemhakikishia Rais Bouteflika kuwa Serikali yake itaendeleza na kuimarisha uhusiano na ushirikiano na Aljeria, na kwamba hivi karibuni imepanga kuanzisha ofisi za Ubalozi katika nchi hiyo.

Kuhusu sekta za nishati na kilimo, Rais Magufuli amesema serikali yake inakaribisha uwekezaji kutoka Aljeria hasa wakati huu ambapo Tanzania imethibitika kuwa na kiasi kikubwa cha gesi, na kwa upande wa kilimo ametoa wito kwa Aljeria kushirikiana na Tanzania katika mpango wake wa kujenga viwanda vya kuongeza thamani ya mazao, ikiwemo usindikaji wa zabibu, viwanda vya nguo, viwanda vya ngozi na nyama na viwanda vya kusindika minofu ya samaki.

"Naomba ukamweleze Mheshimiwa Rais Bouteflika kuwa Tanzania itaendeleza na kuimarisha zaidi ushirikiano wake na Aljeria na kwamba imefurahishwa sana kuona Aljeria ipo tayari kusaidia juhudi za kuendeleza sekta ya kilimo nchini Tanzania"  Rais Magufuli amemweleza Balozi Belabed Saada.

Katika hatua nyingine, Rais Dkt. John Pombe Magufuli ameagana na Balozi wa Vatican hapa nchini Mheshimiwa Francisco Montecillo ambaye anamaliza muda wake baada ya kuiwakilisha Vatican kwa muda wa miaka minne na nusu.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
22 Aprili, 2016
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live




Latest Images