Quantcast
Channel: MPEKUZI
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Jumamosi Ya April 16


Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) yakana ulinzi wa makapuni binafsi kwenye sehemu nyeti

0
0

Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) imesema kuwa makampuni binafsi ya ulinzi yanayofanya kazi bandarini hayahusiki na ulinzi wa sehemu nyeti za za Mamlaka hiyo.

Akitoa ufafanuzi huo jana jijini Dar es salaam, Meneja Mawasiliano wa Mamlaka hiyo Bi. Janeth Ruzangi alikiri kuwepo kwa makampuni yanayofanya kazi ya ulinzi bandarini na akafafanua kuwa hayahusiki kwa namna yoyote ile kulinda sehemu za ndani za ofisi zilizoko bandarini.

“Ninapenda kuwafahamisha wananchi kuwa Bandari inalindwa na walinzi wa aina tatu ; Jeshi la polisi, Polisi wasaidizi walioajiriwa na Mamlaka ya Bandari Tanzania (Auxilliary Police) pamoja na walinzi wa Makampuni binafsi”

Aliongeza kuwa makampuni hayo yanalinda maeneo ya nje ya bandari yakiwemo maegesho ya magari ya watumishi wa mamlaka kama ilivyo kwenye ofisi nyingine.

Aidha,alifafanua kuwa Polisi wa bandari walioajiriwa na Mamlaka ya Bandari Tanzania wako kwa mujibu wa sheria zilizotungwa na Bunge na wamepata baadhi ya mafunzo ya kipolisi.

Ikumbukwe kuwa agizo la kuwandoa walinzi wa makampuni binafsi kwenye maeneo nyeti ya bandari lilitolewa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa mwezi Februari mwaka huu alipofanya ziara ya kushtukiza bandarini hapo.

Kigwangalla Avifungia Vituo vya Tiba Asili zitolewazo na Kiliniki za Kikorea

0
0

SERIKALI imesitisha huduma za tiba asili zitolewazo na Kiliniki za Kikorea, Maibong Sukidar Medical na Korea Medical Clinic zilizopo Jijini Dar es Salaam kwa kosa la kutokuwa na kibali kwa zaidi ya miaka nane pia kuchanganya tiba asili na za kisasa na mbadala bila ya idhini kutoka baraza la usajili la tiba asili nchini

Hatua ya kufungwa kwa kliniki hizo imechukuliwa jana baada ya Hamisi Kigwangalla, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto kufanya ziara ya kushtukiza kukagua  vibali na huduma zitolewazo katika kiliniki hizo.

Kigwangalla alizitaja sababu zilizopelekea kufungwa kwa Kiliniki ya Korea Medical kuwa ni pamoja na  Kutibu magonjwa ambayo haikupewa kibali kutoka serikalini na kuhifadhi dawa ambazo hazihusiani na magonjwa inayotibu

“Kliniki hii ninaamuru ifungwe kwa makosa matano ikiwemo kosa la kuchanganya tiba asili na kisasa, kutokuwa na kibali, usajili halali, matabibu wake hawajui lugha ya Kiswahili na au kiingereza, usajili ulimtaka kuajiri tabibu wa kitanzania ambaye hapa hayupo,” alisema Kigwangalla.

Alisema kliniki hiyo inatumia dawa kali za maumivu, usingizi, uzazi wa mpango, sindano na dripu.

Kigwangala alimwamuru msajili wa hospitali binafsi kufanya uchunguzi ili kubaini hizo dawa zilikuwa zinafanya kazi gani.

Aidha, Kigwangalla alieleza sababu ya kufungwa Kliniki ya Maibong ni pamoja na kutokuwa na kibali kwa zaidi ya miaka minane, kuchanganya tiba asili na kisasa na kutoplekea vyeti vya matabibu wake kama serikali ilivyomtaka kuvipeleka toka mwaka 2008.

“Kiliniki hii haina kibali walichonionesha ni barua walizoandika za kuomba kibali kutoka serikalini na kwamba serikali iliwaambia kupeleka vyeti vya matabibu wake jambo ambalo hawajalifanya hadi sasa,” alisema.

“Baraza la usajili tiba asili lifungie kliniki hadi itakaporekebisha nyaraka zake pamoja na kufanyiwa uchunguzi kama inakidhi vigezo vya kutoa huduma ya tiba asili na mbadala,” amesema.

Kigwangalla alitoa agizo kwa baraza la usajiri la tiba asili nchini kuzifungia kliniki hizo hadi zitakapofuata utaratibu, pia aliitaka idara ya uhamiaji kuchunguza vibali vya makazi na ufanyaji kazi nchini.

Bunge kuanza kutumia mfumo mpya wa kurusha matangazo kwa njia ya Satellite

0
0

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limefanya mabadiliko ya kurusha matangazo yake ambayo yanaviwezesha vyombo vya habari (redio na tv) kupata matangazo hayo moja kwa moja bila kufunga mitambo yao katika eneo la bunge.

Katika taarifa ambayo imetolewa na kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano cha bungeni imeeleza kuwa mfumo huo utakuwa ukirusha mtangazo kupitia satellite ambapo vituo vya redio na runinga vitakuwa vikitumia satellite kupokea matangazo hayo na kuyarusha katika vituo vyao.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa redio na vituo vya runinga vitakuwa vikiyapata matangazo kupitia satellite Intelsat 17, nyuzi 66 upande wa Mashariki.

SATELLITE: Intelsat 17 @ 66 East

FREQUENCY: 11024.2500MHZ

SYMBOLRATE: 3071.8 Mbps

POLARIZATION: Horizontal

FEC: 1/2

MODULATION: 4PHASE-QPSK

AUDIO: CH. 1…noneI, CH.2…none, CH.3…TV Audio na CH. 4…Radio

Aidha taarifa hiyo imeeleza kuwa mfumo huo ndiyo unaotumika na mabunge mengi duniani na kutumika kwa mfumo huo hakuwazuii waandishi wa habari kwenda bungeni kuchukua habari.

Takukuru kukata rufaa hukumu ya Mhando wa Tanesco

0
0

Siku moja baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kumwachia huru aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, William Mhando, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), inaandaa utaratibu wa kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo. 

Aprili 14, mwaka huu Mahakama hiyo ilimwachia huru Mhando na wenzake wanne akiwamo mkewe, Eva na maofisa watatu wa Tanesco; Francis Mchalange, Sophia Misida na Naftali Kisinga waliokuwa wakikabiliwa na mashtaka ya matumizi mabaya ya fedha. 

Mashtaka mengine yaliyokuwa yakiwakabili ni kughushi  na kuwasilisha nyaraka za uongo kwa mamlaka za Serikali. 

Hata hivyo, washtakiwa hao waliibwaga Takukuru baada ya mahakama kuona kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha tuhuma hizo.

 Akisoma hukumu hiyo kwa niaba ya Hakimu Mkazi Mkuu, Kwey Rusema, Hakimu Hellen Riwa alisema kwa mujibu wa ushahidi, suala la msingi lilikuwa ni mkataba kati ya kampuni ya Santa Clara Supply Limited na Tanesco. 

Alisema katika mkataba, Mhando alikuwa mshtakiwa wa kwanza, akituhumiwa kutumia madaraka yake vibaya kwa kushindwa kutangaza masilahi yake kwa kampuni ya Santa Clara inayomilikiwa na Eva ambaye ni mkewe.

 “Suala la msingi ni kujiuliza ni vipi mshtakiwa huyo alihusika katika utoaji wa zabuni na nani aliyekuwa na uamuzi wa mwisho,” alisema. 

 Taarifa iliyotolewa jana na Ofisa Uhusiano wa Takukuru, Tunu Mley ilisema imefikia uamuzi huo baada ya wadau wengi kuhitaji kujua hatua zitakazochukuliwa na chombo hicho baada ya hukumu hiyo. 

“Takukuru inawataka wadau na wananchi kwa ujumla kutambua kwamba ni utaratibu wa kisheria kwamba upande mmoja usioridhika na hukumu iliyotolewa kukata rufaa katika mahakama ya juu,” ilieleza taarifa hiyo.

Baada ya hukumu hiyo juzi, Wakili wa Takukuru, Leonard Swai aliomba Mahakama kuingilia kati.

Bibi Kizee Abakwa Mkoani Singida

0
0

Pichani ni Bibi kizee mwenye umri wa miaka 84 na mkazi wa Kijiji cha Chungu, tarafa ya Ihanja, wilaya ya Ikungi, Mkoani Singida akiwa amebebwa na mmoja wa ndugu zake wakati akitoka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya mjini Singida kutoa ushahidi katika kesi inayomkabili kijana mmoja mwenye umri wa miaka 32 (jina lake halikupatikana) anayetuhumiwa kumbaka bibi kizee huyo kwa mara ya tatu sasa ndipo walipofanikiwa kumkamata. (Picha Na Jumbe Ismailly)

Waziri wa Ardhi,Nyumba na Makazi William Lukuvi Aziponda Nyumba Zinazojengwa na NHC,PPF

0
0

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, amesema hakuna taasisi ya Serikali wala binafsi nchini iliyojenga nyumba za bei nafuu.

Kutokana na hali hiyo, amesema Serikali imekusudia kuanzisha Sheria ya Mamlaka ya Kuratibu Shughuli za Ujenzi, itakayodhibiti bei za nyumba nchini.

Akizungumza jana katika mkutano na wajenzi kuhusu kusudio hilo la Serikali kuanzisha sheria na mamlaka hiyo, Lukuvi alisema taasisi zote zinazotumia wimbo wa nyumba za bei nafuu, hazisemi ukweli.

Alitoa mfano wa nyumba zilizojenga na Mifuko ya hifadhi za jamii na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) pamoja na mashirika mengine binafsi na kudai ni za gharama nafuu kwamba zinauzwa bei inayoanzisha Sh milioni 50 na kuendelea. Alisema bei hiyo si nafuu hata kidogo kwa Watanzania walio wengi.

Kutokana na changamoto hiyo, Lukuvi alisema Serikali imetafuta wabunifu wa kujenga nyumba ya bei nafuu na kupata Kituo cha Social Business, kilichopo Babati mkoani Manyara wanaojenga nyumba ya vyumba viwili vya kulala kwa Sh milioni 15.

“Hebu fikiria kwa nyumba ya vyumba viwili huko Babati wanajenga kwa gharama hiyo wakati Dar es Salaam vifaa vyote vinapopatikana wanajenga kwa Sh milioni 50 na hapo Mtanzania wa kawaida atalipa kwa miaka 30 ya uhai wake wote,” alisema.

Kuhusu Sheria na Mamlaka ya Kudhibiti Ujenzi, Lukuvi alisema itakamilika mwaka huu kwa ajili ya kulinda wamiliki, wapangaji na Serikali kukusanya mapato yake.

 Alisema ni lazima kuwe na mfumo na sheria wa kusimamia wajenzi kwani wanasababisha kwa kiwango kikubwa miji kutopangika huku serikali za mitaa zikishindwa kukusanya mapato yake.

Lukuvi alisema ni lazima eneo hilo la ujenzi lisimamiwe kwani duniani kote ndiyo linalotumika kutakatisha fedha chafu.

Kuhusu watakaoshindwa kujenga nyumba za gharama nafuu, Lukuvi alisema pia wataweka haki za wapangaji hasa mijini kwani wanaandaa sera ya makazi na nyumba ili mpangaji awe na sheria inayomlinda.

Alisema kwa sasa mjenzi anapangisha nyumba kwa gharama kubwa hata kama haina baadhi ya vitu, hivyo lazima alipe gharama kulingana na ubora wa nyumba inayofanana na thamani ya fedha kwani wapangaji wengi wanalipa kulingana na anachotaka mlipaji.

Alipoulizwa kuhusu kodi kubwa kuchangia gharama za nyumba kuongezeka, Lukuvi alisema taasisi nyingi bado hazijajishughulisha na kutafuta teknolojia za ujenzi wa nyumba za gharama nafuu, badala yake zimekuwa zikilalamika kodi za Ongezeko la Thamani (VAT) pamoja na kodi nyingine.

Alisema kama taasisi hizo zitafuata teknolojia katika nchi zilizoendelea, zitajenga nyumba za gharama nafuu ambazo kila Mtanzania anaweza kumudu. 

“Bado nawapa changamoto, wasilete visingizio vya kodi, watafute teknolojia zilizopo huko duniani. Bado hakuna taasisi inayoniridhisha,” alisema.

Jiji la Dar es Salaam Kufumuliwa na Kupangwa Upya

0
0

Waziri wa Nyumba, Ardhi na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amesema Jiji la Dar es Salaam litafumuliwa na kupangwa upya baada ya Ramani ya Mipango Miji (Master Plan) mpya kukamilika.

Pia, amesema Serikali ipo kwenye mkakati wa kuhakikisha ndani ya miaka 10 ijayo, ardhi yote nchini itakuwa imekamilika kupimwa na kupangwa kwa matumizi mbalimbali. 

Akizungumza na wadau wa Sekta ya Uendelezaji Ujenzi Dar es Salaam jana, Waziri Lukuvi alisema Jiji la Dar es Salaam linaongoza kwa ubovu wa upangaji miji. 

Alisema kwa sababu hiyo, ameagiza kuandaliwa kwa Mpango Mji Mpya ambao utakamilika Julai, baada ya ule wa awali kuoneakana mbovu. 

“Mwanzo hatukufanya vizuri. Tuliajiri Consultant (mshauri) wa Master Plan (Mipango Miji) kutoka Italia sitaki kumtaja na yule Mswahili na wengine walioshirikiana nao, lakini kwa ufupi walifanya vibaya. Fedha imekwisha lakini kazi siyo nzuri,” alisema. 

Mabasi Yaendayo kasi Kuanza Mei 10

0
0

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais anayeshughulikia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Simbachawene amesema mradi wa Mabasi Yaendayo Kasi (Dart), unatarajia kuanza rasmi Mei 10, mwaka huu. 

Akizungumza kwenye majumuisho ya ziara ya Kamati ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Simbachawene alisema baada ya kukutana na wadau wa mradi huo, wamewahakikishia kuwa utaanza rasmi mwezi ujao bila kukosa. 

“Tumeambiwa mradi huu una mikataba mingi na kuwa bado kuna mjadala mkubwa wa mikataba. Hatuwezi kulazimisha maana unaweza kujikuta ukitengeneza mikataba mibaya, hivyo tunaendelea na mijadala ya mikataba,” alisema. 

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Jasson Rweikiza alisema wameutembelea mradi huo zaidi ya mara nne na kugundua tatizo linaloukwamisha kuwa ni fedha na kuitaka Serikali kutoa fedha ili uanze. 

Aliesema lengo la kuanzishwa kwa mradi huo ni kupunguza kero ya usafiri kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wanaokabiliwa na tatizo la usafiri na foleni za barabarani, hivyo kutumia muda mrefu barabarani. 

Rweikiza alisema kukamilika kwa mradi huo na kuanza kufanya kazi kutapunguza kero na kuokoa muda mwingi uliokuwa ukitumia bila uzalishaji.

Washtakiwa wa Tumbili 61 Wanyimwa Dhamana

0
0

Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Moshi imetupilia mbali maombi ya dhamana ya washtakiwa saba wa kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Wanyamapori Matumizi Endelevu, Dk Charles Mulokozi na wenzake sita, wakiwamo raia wawili wa Uholanzi.

Dk Mulokozi na wenzake walikamatwa Machi 23, mwaka huu wakitaka kusafirisha tumbili wekundu 61 kwenda nchini Armenia. Wanyama hao walikamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA). 

Akitoa uamuzi huo juzi, Jaji Mfawidhi wa mahakama hiyo, Aishiel Sumari ambaye anasikiliza shauri hilo namba 1/2016, alisema mahakama hiyo imepima kwa umakini maombi ya dhamana dhidi ya washtakiwa hao na imeona hayana msingi, kwa kuwa suala lililopo mahakamani linagusa masilahi mapana ya Taifa. 

Jaji Sumari alifikia uamuzi huo baada ya kusikiliza maombi ya dhamana yaliyofunguliwa na mawakili wa utetezi, Majura Magafu, John Masangwa, Robert Rogath, Elibariki Maeda na Edward Silvester wakati Jamhuri ilikuwa ikiwakilishwa na mawakili, Wankyo Simon na Salim Msemo. 

Wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Ofisa Mfawidhi wa Matumizi Endelevu ya Wanyamapori, Kanda ya Kaskazini (Cites), Nyangabo Musika, Martina Nyakangara, VeryGerald Anthony (wote wakiwa ni maofisa wa Wizara ya Maliasili na Utalii), Iddy Misanya anayedaiwa kukamata tumbili hao na Artem Verdanian na Eduard Verdanian ambao ni raia wa Uholanzi. 

Kutupiliwa mbali kwa maombi hayo ya dhamana kunafuatia uamuzi wa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kupinga dhamana ya washtakiwa hao baada ya kuwasilisha mahakamani hati ya mwaka huu baada ya upelelezi kutokamilika, huku mahakama ikitoa kibali kwa mshtakiwa namba 6 kupelekwa Hospitali ya Rufaa ya KCMC kwa ajili ya uchunguzi kutokana na kusumbuliwa na mgongo. 

Kunyimwa dhamana kwa watuhumiwa hao kumekuja wakati kukiwa na sintofahamu ya mtuhumiwa wa kesi ya utoroshaji nje ya nchi wanyamapori hai 136 wa aina 14 tofauti, wakiwamo twiga, Kamran Ahmed (29) aliyekuwa nje kwa dhamana, kutoweka nchini mwaka 2011. 

Mtuhumiwa huyo alitoweka siku chache baada ya Mahakama Kuu, Kanda ya Moshi kumpa dhamana na kumtaka kusalimisha hati ya kusafiria. 

Awali, kabla ya kutoweka Ahmed alipewa dhamana yenye masharti ya kutosafiri nje ya Mkoa ya Kilimanjaro. 

Mtuhumiwa huyo alifikishwa mahakamani mara ya kwanza katika Makahama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Kilimanjaro, Juni 11, mwaka huo kwa tuhuma za kusafirisha na kutorosha nje ya nchi wanyamapori hao waliokuwa na thamani ya Sh170,572,000. 

Ahmed na wenzake walisomewa mashtaka sita tofauti, ikiwamo uhujumu uchumi.

Manispaa ya Kinondoni Inayoongozwa na UKAWA Yasema Itawalipia Wananchi wake Wote Bima za Afya

0
0

Manispaa  ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, inayoongozwa na Chama cha Demkrasia na Maendeleo (Chadema), chini ya Ukawa imeanza kazi kwa staili ya aina yake baada ya kutangaza neema ya bima ya afya kwa wananchi wa Manispaa hiyo.

Imeahidi kuanzisha mpango maalum ambao kila mwananchi wa Manispaa hiyo atachangia Sh. 40,000 kwa mwaka ili aunganishwe na mpango wa matibabu wa bima ya afya ambao utawawezesha kupata matibabu ya bure katika hospitali mbalimbali.

Mpango huo utaanza kutekelezwa mwezi Juni mwaka huu, huku bajeti ya Manispaa hiyo ikiongezeka kwa asilimia 59 kutokana na kukua kwa mapato ya ndani.

Wazee wa Manispaa hiyo nao wametangaziwa neema ya matibabu bure kwani watapewa kadi maalum zitakazowawezesha kutibiwa hospitali za umma.

Mapato hayo yametokana na ukusanyaji madhubuti katika kodi za majengo, mabango, leseni za biashara, huduma za kuegesha magari, hoteli na ruzuku ya serikali kuu.

Bajeti ya mwaka 2016/2017 katika Manispaa hiyo inafikia Sh. Bilioni 248.47 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka jana ambayo ilikuwa ya Sh. Bilioni 156.24.

Katika bajeti ya mwaka huu kuna ongezeko la Sh. zaidi ya bilioni 92.

Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Boniface Jacob aliwasilisha bajeti hiyo jana jijini Dar es Salaam katika kikao cha Baraza la Madiwani.

Baada ya kuwasilisha bajeti hiyo, Madiwani wote wakiwamo wa upinzani na Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliipitisha kwa kauli moja ili ianze kuwahudumia wananchi.

Akisoma bajeti hiyo, Jacob alitaja ukusanyaji wa mapato ya ndani umeingiza Sh. bilioni 64.28 na kwamba imeongezeka kutoka Sh. bilioni 56.6 za mwaka jana.

Licha ya bajeti ya mwaka huu kulenga kugharamia huduma za matibabu, lakini imelenga kujenga shule ya bweni katika Kata ya Goba kwa gharama ya Sh. milioni 250, ujenzi wa matundu ya vyoo katika shule, kujenga vyumba vya madarasa na ununuzi wa madawati 30,000.

Kazi nyingine zitakazofanyika ni pamoja na ujenzi wa Barabara kuelekea kituo cha daladala cha ya Simu 2000 na Barabara ya Akachube ambazo zimetengewa Sh. bilioni 50.

Kuhusu suala la usafi, Meya Jacob alisema kila Kata itakuwa na gari lake la kuzolea takataka na Manipaa imetenga Sh. 2.2b .
 
Manispaa hiyo ina jumla ya Kata 25 na Sh. bilioni 3.6 zimetengwa kwa ajili ya gharama za kusafirisha takataka.

Aidha, katika bajeti hiyo, Manispaa inatarajia kununua Trekta lenye kijiko kwa ajili ya kutengeneza barabara na zimetengwa Sh. bilioni 1 kwa ajili ya kazi hiyo.

Kazi nyingine za fedha hizo ni kuweka sakafu ngumu katika masoko yote ya manispaa, ili kuondoa adha ya uchafu na matope katika msimu wa mvua na zimetengwa Sh. bilioni 1.65.

Kuhusu vijana na wanawake Manispaa hiyo imetenga Sh. bilioni 4.7 kwa ajili ya kuwakopesha na kila Kata itapata Sh. milioni 200.

Rais Magufuli Aweka jiwe la Msingi ujenzi wa Barabara ya Juu katika makutano ya barabara za Nyerere na Mandela jijini Dar leo

0
0
Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), Eng. Patrick Mfugale akitoa maelezo kwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli, wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la Msingi ujwenzi wa Barabara ya Juu (FlyOver) kwenye makutano ya Barabara ya Mandela na Nyerere, eneo la Tazara, Jijini Dar es salaam leo.

****
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli ameweka jiwe la msingi kwa ajili ya kuanza  rasmi ujenzi wa barabara ya juu kwenye makutano ya barabara za Nyerere na Mandela eneo la Tazara jijini Dar es Salaam leo.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Rais Magufuli amesema ujenzi huo wa barabara ya juu utaanza mara moja kwa ushirikiano na serikali ya Japan  na utagharimu Shilingi 100 bilioni.


Amesema, serikali ya Japan imefadhili mradi huo kwa Sh 93.44 bilioni wakati serikali ya Tanzania imechangia Sh 8.36 bilioni.

Rais amewataka wananchi watakaopata ajira kwenye ujenzi wa mradi huo wawe waaminifu na wasiwe wezi wa mafuta, vifaa vya ujenzi au kuendekeza migomo.

“Pia serikali ya awamu ya tano imetenga Sh 1 trilioni kuanza ujenzi wa reli ya kisasa (standard gauge) kwa reli ya kati. Tutajenga kituo kikubwa Ruvu ili mizigo isafirishwe kwa njia ya reli kutoka bandari ya Dar es Salaam hadi Ruvu na malori yatakuwa yakichukua mizigo pale, jambo hili litasaidia kupunguza foleni hapa Dar es Salaam,” alisema Rais Magufuli.

Aidha ameishukuru serikali ya Japan kwa ufadhili wa miradi ya maendeleo nchini kwa zaidi ya miaka 36. Amesema Japan imekuwa ikiisaidia Tanzania bila masharti kama ilivyo kwa baadhi ya wafadhili wa maendeleo. 


Akionyesha kukerwa na wafadhili wanaotoa misaada yenye masharti na vitisho, Rais Magufuli amesema;“Ni bora kula muhogo wa kujitafutia kuliko kula mkate kwa masimango.”

Mbali na mradi huo, Rais amesema serikali yake pia itajenga barabara ya njia sita kutoka Dar es Salaam hadi Chalinze ambayo itakuwa na barabara za juu tano.

Pia amewataka Mkuu wa Mkoa, Paul Makonda, Wakuu wa Wilaya na Mameya kuhakikisha jiji la Dar es Salaam linakuwa safi muda wote na wachafuzi wa mazingira wachukuliwe hatua za kisheria. 

Wawili washikiliwa Polisi kwa kusafirisha wahamiaji haramu

0
0

Wakazi  wawili wa jijini Dar es Salaam na mmoja wa mkoani Iringa, wanashikiliwa na Polisi mkoani Tanga  kwa tuhuma za kuingiza na kusafirisha wahamiaji haramu 10 kutoka nchini Ethiopia.

Watuhumiwa hao ni Ali Juma (24) ambaye ni dereva wa gari namba T 113 DCV aina ya Toyota Hiace iliyokuwa ikisafirisha watu hao na Joseph John (42), wote wakazi wa Dar es Salaam. Mwingine ni Idi Juma (38), mkazi wa Iringa.

Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Tanga, Leonard Paul alisema watuhumiwa wote walikamatwa saa 8:00 usiku wa kuamkia Aprili 14 mwaka huu, katika eneo la Misajini wakati gari hilo likiendelea na safari.

“Misajini iko katika barabara kuu ya Hedaru - Mombo ambapo baada ya askari wetu kupata taarifa za wasafiri hao, waliwafuatilia na kuwakamata,” alisema.

 Alisema, kumekuwa na matukio ya mara kwa mara ya kukamatwa kwa wahamiaji haramu mkoani kwetu lakini chanzo chake pamoja na mambo mengine ni jiografia ya mkoa yenye njia nyingi za panya.

Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Jumapili ya April 17

Rais Magufuli Awataka Mawaziri Wajiandae Kwa Machungu......Asema Wasioweza Kazi Bila Posho au Safari Wajiondoe Wenyewe

0
0

Viongozi  serikalini wakiwemo mawaziri na makatibu wakuu, wameombwa na Rais John Magufuli, kuvumilia machungu wakati wa uongozi wake, kama ambavyo wananchi walivyovumilia tangu Uhuru.

Amesema hayo jana wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya kwanza ya juu (flyover) nchini Tanzania, inayojengwa katika makutano ya Barabara ya Mandela na Barabara ya Nyerere, eneo la Tazara, kwa ufadhili wa Serikali ya Japan. 

Machungu hayo kwa mujibu wa Rais Magufuli, yataanza kuonekana wakati wa utekelezaji wa Bajeti ya Serikali ya kwanza kwa Awamu ya Tano, ambayo fedha za maendeleo zimeongezeka kutoka asilimia 27 za bajeti iliyopita, hadi kufikia asilimia 40.

Machungu yenyewe 
Ili kufanikisha dhamira hiyo ya Serikali, Rais Magufuli alisema katika bajeti hiyo inayotarajiwa kupelekwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, litakaloanza vikao vyake Dodoma wiki ijayo, machungu hayo yataanza kuonekana kwani fedha za chai, semina na safari, zimekatwa na kujaziwa katika fedha za maendeleo.

Kutokana na makato hayo, Dk Magufuli amesema kutakuwa na machungu hasa kwa watendaji wa Serikali na kuwaomba mawaziri na makatibu wakuu ambao alisema walikuwa wakifaidi matunda ya Uhuru, wavumilie machungu hayo kwani wananchi wa maisha ya chini wamevumilia machungu kwa muda mrefu.

“Wananchi wamechoka kutuona sisi viongozi tunafaidi matunda ya Uhuru wa nchi tangu Uhuru na wao wakiwa wasindikizaji halafu wao tunawaomba kura na wakishatupigia tunawasahau,” alisema na kuongeza kuwa anataka wananchi watoke kwenye machungu na sasa wawe ‘watamu’ kwa maendeleo.

Magufuli alisema lazima viongozi wabadilike na kurudi kwa wananchi wa maisha ya chini na hiyo itakuwa sadaka kwa kuwapa madaraka kwani wananchi wanyonge wameteseka siku nyingi.

Wasiovumilia 
Alisema waliokuwa wamezoea chai, safari na posho za ovyo kama wanaona au wanafikiri hawawezi kufanya kazi bila hizo chai, waache kazi mara moja kwani sasa fedha zinazokusanywa za walipa kodi wanyonge, zitaenda kutatua matatizo yao ya hospitali, barabara na kununua ndege za Serikali.

Pia alionya kuwa katika uongozi wake hakuna mtu atakayekwenda kinyume na utaratibu na kisha ‘akachomoka salama’ na kama kuna anayeona hawezi ajiondoe mwenyewe kwani Watanzania wanaendelea kumuombea.

Dk Magufuli alisema wananchi wote bila kujali vyama vya siasa, wanalilia maendeleo na maendeleo hayana chama, kwani wananchi wamechoka ‘machama chama’, wanataka kwenda mbele, hivyo hakuna sababu ya kubaki nyuma na kubishana kwa mambo ya chama chama, wakati uchaguzi umepita na aliyeshinda ni yeye ambaye ni CCM.

Machungu ya zamani 
Ingawa Rais Magufuli alisema machungu hayo yataanza kuonekana katika Bajeti inayotarajiwa kuanza kujadiliwa na Bunge litakaloanza vikao wiki ijayo, lakini watendaji wa Serikali walianza kuona machungu ya msimamo wake tangu alipoingia madarakani Novemba mwaka jana.

Itakumbukwa kuwa Novemba 7, mwaka jana akiwa Ikulu, Dar es Salaam, katika mkutano wake wa kwanza na watumishi wa ngazi za juu wa Serikali, hasa makatibu wakuu, naibu makatibu wakuu na watendaji wengine wakuu wa Serikali, Rais Magufuli alitangaza kufuta safari zote za nje ya nchi hadi hapo atakapolitolea suala hilo uamuzi mwingine.

Mpaka sasa Rais Magufuli amehakikisha shughuli zote zinazotakiwa kufanywa nje ya nchi zinafanywa na kusimamiwa na mabalozi wa Tanzania wanaowakilisha nchi, ambapo watumishi watasafiri nje iwapo kutatokea jambo la dharura na pamoja na udharura wake, lazima kibali kitolewe na yeye, Katibu Mkuu Kiongozi au Makamu wa Rais.

Katika kile kinachoonekana kuwa hatanii, Rais Magufuli aliagiza kusimamishwa kazi mara moja kwa watumishi waandamizi wanne wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), ambao walikaidi agizo lake la kuwataka watumishi wa umma kutosafiri nje ya nchi.

Watumishi hao ni Mary Mosha, Ekwabi Mujungu, Doreen Kapwani na Rukia Nikitas ambao walisafiri kwenda nje ya nchi, licha ya kutokuwa na kibali cha safari kutoka kwa Rais ama Katibu Mkuu Kiongozi.

Aidha ndani ya siku zake 100 za kwanza tangu alipoingia madarakani, tayari Serikali yake ilikuwa imeshawafukuza kazi vigogo zaidi ya 70 kwa tuhuma mbalimbali ikiwamo za ufisadi.

Novemba 9, mwaka jana, aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Sefue, alitangaza kuwa Rais Magufuli aliamua kufuta shamrashamra za Sikukuu ya Uhuru ambapo fedha zilizookolewa aliagiza zipelekwe katika mradi wa kupanua kipande cha barabara kutoka Morocco mpaka Mwenge katika wilaya ya Kinondoni.

Hatua hiyo ilitanguliwa na kupunguza fedha za sherehe ya kupongezana ya wabunge, ambazo alizielekeza kwenda kununua vitanda, magodoro na mashuka kwa ajili ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Hivi karibuni alipokuwa akiapisha wakuu wa mikoa, aliwataka kwenda kuwasaka watumishi hewa na kutangaza idadi yao, ambapo aliyeteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anne Kilango Malecela, aliposema hajakuta watumishi hewa wakati wapo, Dk Magufuli hakusita kumuondoa mwanzoni mwa wiki hii, ingawa hakuwa amemaliza hata mwezi tangu aripoti kazini.

Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam, Paul Makonda Asema Baadhi ya Ombaomba Wanauza Madawa ya Kulevya

0
0

Mkuu  wa Mkoa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema kwa mujibu wa utafiti alioufanya, ombaomba walioko jijini Dar es Salaam baadhi yao wanajihusisha na uuzaji wa dawa za kulevya.

Akihojiwa katika mahojiano ya moja kwa moja na kituo kimoja cha redio, Makonda alisema wapo watu ambao wanatumia mwanya huo kusambaza dawa za kulevya.

“Wapo wanaotumia fursa hii kusambaza dawa za kulevya kwa sababu anavyopita huwezi kumhisi kwa namna anavyoonekana, lakini watu hawa ni miongoni mwa mawakala wa kusambaza dawa za kulevya,” alisema Makonda.

Makonda aliwataka wakazi wa jiji hilo kushirikiana naye katika kuwaondoa ombaomba hao ambao wengi wanatoka nje ya Da es Salaam na kwamba hakuna tija kuendelea kuwaacha. 

“Watanzania tuna upendo sana lakini tunahitaji kutafakari kama kweli watu walioko barabarani wakiomba kama kweli wanahitaji msaada huo au la,” alisema Makonda.

Alisema kwa kuendelea kuwaacha ombaomba hao pia kutasababisha vijana ambao sasa wanaomba barabarani kuwa watu hatari katika maisha yao ya baadaye kwani wakikosa pesa wataingia katika shughuli za uporaji ili wapate fedha.

“Itafika kipindi ataanza kuangalia kile alichokuwa anakikusanya wakati akiomba na kile anachokipata akifanya kazi, ataona akifanya kazi hapati kiasi kikubwa, ataamua kuwa mporaji,” alisema Makonda.

Makonda alisema kwa mujibu wa utafiti alioufanya, asilimia 80 ya ombaomba wanatoka nje ya Dar es Salaam na kesho operesheni ya kuwaondoa watu hao itaanza rasmi huku wale ambao hawana ulemavu wowote wakikamatwa kwa makosa ya uzururaji.

Trilioni 1 Yatengwa Ili Kuyaondoa Malori ya Mizigo Dar

0
0

Malori  ya kubeba mizigo, ambayo yamekuwa yakichangia msongamano wa magari kwa kiasi kikubwa jijini Dar es Salaam, yanatarajiwa kuondolewa mara tu reli ya kisasa ‘Standard Gauge’, iliyotengewa Sh trilioni moja katika Bajeti ya Serikali, itakapofika Ruvu mkoani Pwani.

Rais John Magufuli amesema hayo jana wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya kwanza ya juu (Flyover) nchini Tanzania, inayojengwa katika makutano ya Barabara ya Mandela na Barabara ya Nyerere eneo la Tazara, kwa ufadhili wa Serikali ya Japan.

Barabara hiyo ya juu kwa mujibu wa taarifa za Wakala wa Barabara (Tanroads), ikikamilika inatarajiwa kupunguza muda wa magari kukatiza katika makutano hayo kwa asilimia 80, kutoka wastani wa dakika 45 hadi dakika 10 tu kwa wanaotoka upande mmoja kwenda mwingine.

Akifafanua zaidi kuhusu reli, Rais Magufuli alisema fedha hizo zimetengwa katika bajeti itakayopelekwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, linalotarajiwa kuanza vikao vyake wiki ijayo, ili ujenzi uanze kwa fedha za ndani wakati wafadhili wa kusaidia kuendeleza wakitafutwa na wakipatikana, wakute reli hiyo imeanza kujengwa.

Kwa mujibu wa Rais Magufuli, reli hiyo itakapofika Ruvu, kutajengwa bandari kavu kubwa ambayo ikikamilika, mizigo yote inayoshuka Bandari ya Dar es Salaam, itasafirishwa kwa reli mpaka katika bandari hiyo na malori yanayochukua na kupeleka mizigo katika bandari hiyo, yataishia katika bandari hiyo kavu.

Ili kuepuka wizi wa mizigo, Rais Magufuli alisema kutafungwa kamera katika njia yote ya reli mpaka Ruvu, ili kontena linaloshushwa katika Bandari ya Dar es Salaam, lifuatiliwe mpaka katika bandari hiyo.

Mbali na reli hiyo ambayo ikikamilika kwa mujibu wa taarifa za Mamlaka ya Bandari (TPA), itapunguza gharama za usafirishaji wa mizigo kwa asilimia 30 na kuongeza kivutio cha bandari hiyo duniani, Rais Magufuli alisema Mfuko wa Barabara utatoa fedha za kujenga barabara za pete, zitakazoongeza kasi ya kupunguza msongamano kama si kuumaliza.

Alionya kuwa fedha za Mfuko wa Barabara si za kulipana posho, bali kutengeneza barabara hizo za pete katika halmashauri na kuagiza makandarasi wanaotoa asilimia 10 kwa ajili ya rushwa, wasipewe zabuni bali watafute makandarasi wazuri.

Alisema kilometa 27 za barabara hizo za pete, zimeanza kujengwa na kwa kuwa wabunge wa Dar es Salaam waliopita walisema sana, waliongezewa kilometa nyingine 86 za barabara hizo za pete, zitakazojengwa kwa lami kwa fedha za mfuko huo.

Malori kutaifishwa 
Pia Rais Magufuli ameagiza halmashauri za Dar es Salaam kuweka sheria itakayokataza kupitisha magari yenye tani zaidi ya 56 katika barabara hizo, yakiwemo malori ili barabara hizo zilizokusudiwa kutumika na magari madogo, zisiharibiwe na magari yenye uzito mkubwa.

“Hakuna kupitisha magari yenye tani zaidi ya 56 na mtu akipitisha kamateni gari na ikiwezekana litaifishwe kabisa ili ajifunze kutopita katika barabara hizo na kuziharibu,“ alisisitiza.

Akizungumzia miradi hiyo ya kupunguza msongamano ikiwemo barabara za juu ikiwemo ya Ubungo, Rais Magufuli alisema zitapunguza hasara iliyokuwa ikitokea kwani katika utafiti wa mwaka 2013, ulionesha kuwa Jiji la Dar es Salaam pekee lilipoteza Sh bilioni 411.3 katika msongamano wa magari.

Mbali na hasara hiyo iliyooneshwa katika utafiti, Rais Magufuli alisema inawezekana kabisa msongamano wa magari Dar es Salaam umesababisha baadhi ya watu kufa kwa kuchelewa kufikishwa hospitalini na baadhi ya ndoa kuvunjika kutokana na kuchelewa kufika nyumbani na kushindwa kujieleza.

Rais alisema msongamano ni tatizo na kama siyo kumaliza basi lazima lipunguzwe kabisa kwa kuwa Dar es Salama ndiyo kioo cha Tanzania, ambapo mizigo inayotoka na kwenda nchi zisizo na bandari inapita hapo.

Alisema barabara ya juu ya Tazara, itatengeneza ajira nyingi na asilimia kubwa ya wanufaika watakuwa Watanzania tena wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, akawaomba vijana watakaopata ajira kwenye mradi huo, kufanya kazi kwa uaminifu wasiibe mafuta, vifaa na wasigome ili umalizike mapema.

Hakuna Muda Wa Kulala, Waziri Mkuu Aiambia DART

0
0

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaambia watendaji na wadau wa mradi Mabasi Yaendayo Haraka wa jijini Dar es Salaam (BRT) kuwa hawana muda wa kulala kupumzika na akawataka wakamilishe haraka vipengele vichache vilivyobakia ili mradi huo uweze kuanza kazi mapema iwezekanavyo.

Ametoa agizo hilo juzi usiku (Ijumaa, Aprili 15, 2016) wakati akizungumza na wakuu wa taaasisi, watendaji wakuu na wadau wa mradi huo kwenye kikao alichokiitisha ofisini kwake Magogoni jijini Dar es Salaam.

“Watu wa DART, UDA-RT hakuna muda wa kulala tena. Nanyi wa eGA, MAXCOM, POLISI NA SUMATRA inabidi mfanye kazi kama timu moja na wenzenu ili maeneo yaliyobakia yaweze kukamilika katika muda mfupi na kikubwa ni kuhakikisha mnatoa elimu ya kutosha,” alisisitiza.

Akielezea utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), Bw. Ronald Rwakatare amesema miundombinu ya mradi huo imekamilika na utoaji huduma unatarajiwa kuanza hivi karibuni kwani hivi sasa wanamalizia ufungaji wa mfumo wa ukusanyaji nauli na uendeshaji wa mabasi hayo.

Pia aliwataka wananchi kutunza miundombinu ya mradi huo na kuwa makini na matumizi ya barabara wakati mradi huo ukiwa kwenye majaribio na hatimaye kuanza kazi rasmi.

Alisema watakuwa na karakana itakayotumika kwa ajili ya hayo mabasi ambayo itakuwepo eneo la Jangwani na kwamba ofisi za mradi pia zitakuwa eneo hilo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa UDA Rapid Transit (UDA-RT), Bw. Robert Kisena amesema mpango wa kuanza kwa mradi huo umekamilika na tayari mabasi yote yamelipiwa kodi pamoja na bima. UDA-RT ni kampuni ya muunganiko wa UDA na wamiliki wa daladala ya kutoa huduma ya usafiri katika miundombinu ya mabasi yaendayo haraka.

Bw. Kisena amesema leo wataanza majaribio ya mradi huo kwa kutumia mabasi 10 na watakuwa wanaongeza mabasi 10 kila siku hadi yafikie 50 hivyo amewataka wananchi kuondoa shaka juu ya mradi huo.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Maxcom Africa, Bw. Juma Rajab amesema mabasi hayo yatakuwa yanatumia kadi za kielektroniki zitakazokuwa zinalipiwa kwa kutumia mitandao mbalimbali ya simu za mkononi.

Bw. Rajab amesema Tanzania inakuwa nchi ya kwanza kuanza kutumia mfumo huo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na kwamba fedha za mteja zitakuwa salama na hata kama atakapopoteza kadi yake.

“Mtu akinunua kadi yake anapaswa atunze namba ya usajili iliyoko kwenye kadi hiyo kwani itatumika kurudishia fedha zake kupitia namba yake ya simu ya mkononi,” alisema.

Amesema Maxcom Africa ndio wakusanyaji wa nauli kwa kushirikiana na UDA-RT ambapo watatumia mawakala wa MaxMalipo hivyo kila mwananchi atapata fursa ya kununua kadi yake kwa urahisi.

Alisema taarifa za kila mtumiaji zitaunganishwa na simu yake ya mkononi ambapo mhusika ataweza kujua kwa urahisi salio la fedha lililomo kwenye kadi yake.

Ofisi ya Bunge Yalivaa Gazeti la Nipashe....Yalitaka Liombe Radhi

0
0

Ofisi ya Bunge imebaini upotoshwaji mkubwa Katika habari iliyochapishwa na Gazeti la Nipashe toleo la Aprili 16, 2016 yenye kichwa cha habari kisemacho “ Bunge sasa laufyata mkataba wa Lugumi”. 

Habari hiyo imeandikwa kufuatia ufafanuzi uliotolewa na Bunge jana kuhusu maagizo yaliyotolewa na Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) dhidi ya utekelezaji wa mkataba wa Jeshi la Polisi na Kampuni ya Lugumi Enterprises Ltd  kuhusu mradi wa utambuzi wa alama za vidole (AFIS) (Automated Fingerprint Identification System.)
 
Ndani ya habari hiyo pia, Gazeti hilo limeeleza kuwa kamati ya PAC iliwahi kuliandikia Jeshi la Polisi kulitaka liwasilishe mkataba huo mbele ya Kamati, jambo ambalo si kweli bali ni upotoshwaji wa makusudi wenye lengo la kujenga hisia mbaya kuhusu mwenendo wa shughuli za Bunge mbele ya Umma.
 
Ukweli ni kwamba PAC haijawahi kuliandikia jeshi la Polisi kama inavyodaiwa na Gazeti hilo. Nukuu ya  maelezo ya PAC katika Hansard kwa Afisa Masuhuli kuhusu jambo hilo inasema kama ifuatavyo:
 
“Kamati inamuagiza Afisa Masuhuli kuwasilisha maelezo ya kina kuhusu utekelezaji wa Mkataba baina ya Jeshi la Polisi na  Kampuni ya Lugumi Enterprises  kuhusu mradi wa AFIS. Maelezo hayo yawasilishwe kwa Ofisi ya  Katibu wa Bunge kabla ya Jumatatu tarehe 11 Aprili, 2016”.
 
Katika agizo hilo PAC haikuwa imeandika kwa maandishi kuhusu agizo lake hilo hadi tarehe 12 Aprili, 2016 ilipo mweleza Katibu wa Bunge aweze kuwasilisha agizo hilo kwa maandishi ili liweze kupata Kinga chini ya Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge ambapo barua iliandikwa na kuwasilishwa kwa Afisa Masuhuli ili kupatiwa maelezo hayo kabla ya tarehe 18 Aprili, 2016.

Aidha, Mwandishi pia amelituhumu Bunge kuwa lina nia ya kuficha ukweli kuhusu jambo hili kwa kusema   taarifa ya ufafanuzi iliyotolewa na Bunge ni “kama kufunika kombe mwanaharamu apite kwa kujaribu kupotosha maagizo ya yaliyotolewa na kamati ya PAC ambayo inataka kuuona mkataba huo”

Ni vyema ikafahamika kuwa si jambo jema kwa mwandishi au chombo chochote cha habari kulituhumu Bunge linapotekeleza majukumu yake kwa kuwa Bunge linafanya kazi zake kwa kwa kuzingatia kanuni zake za Kudumu ikiwa ni pamoja na Sheria.  
 
Ofisi ya Bunge inalisihi Gazeti la Nipashe kuomba radhi kutokana na taarifa yake hiyo iliyojaa upotoshwaji mkubwa kwa uzito ule ule au kurekebisha taarifa yake kulingana na ukweli ulivyo haraka iwezekanavyo.

Imetolewa na;
Ofisi ya Bunge,
Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano,
S.L.P 9133,
DAR ES SALAAM.
16 Aprili, 216.

Makamu Wa Rais Mama Samia Suluhu Amfuta Machozi Millen Magese Mapambano Dhidi Ya Endometriosis ( Kuziba Mirija ya Uzazi )

0
0

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Mama Samia Suluhu amemfuta machozi Mwanadada, Happiness Millen Magese ambaye ni shujaa wa kipekee kutoka Afrika dhidi ya mapambano ya ugonjwa wa Endometriosis.

Mama Samia amechukua hatua hiyo jioni ya 15 Aprili 2016 wakati wa hafla maalum ya kumkabidhi tuzo.

Katika kilio chake hicho, Millen kimemfanya Mama Samia kumfuta machozi na kumpa kitambaa, mwanamitindo huyo huku akimweleza kuwa, Serikali itaendelea kushirikiana naye kwani tatizo hilo si la Millen pekee bali ni kwa wanawake wengi hapa Tanzania.

Mama Samia alimwambia kuwa, tatizo alilonalo la kuziba kwa mirija ya uzazi litapata ufumbuzi na kutaka asilie kwani Serikali inania njema kwa watu wake hivyo wataendeleza juhudi Zaidi huku akifungua milango na mwanadada huyo.

Suluhu alisema kuwa hata yeye tatizo kama hilo lipo katika familia yake, lakini ana amini kwa ushirikiano wa mwanamitindo huyo tatizo hilo linapewa uzito. 

Alisema kuwa ni kitu kilichokuwa kikimuumiza sana kichwa, ana amini kupitia Millen hata binti yake atapata nafuu.

"Nimefurahi kukutana nawe na Serikali haitakuangusha tutakuunga mkono katika kuhakikisha gonjwa hili linapata ufumbuzi na kutoa elimu kwa kila mtanzania kulitambua"alisema.

Akizungumza kwa upande wake Magese alisema amekuwa akifanya semina mbalimbali kwa kushirikiana na madaktari bingwa wa Hospitali ya Taifa, Muhimbili, kuwaelimisha wanawake kuhusu endometriosis.

Alisema Machi 30, mwaka huu Taasisi ya Millen Magese ilikusanya vijana (hususani wa kike) wapatao mia tano kutoka shule za Mugabe, Manzese, Salma Kikwete na Turiani, kuwafundisha, kuwatahadharisha na kuwatanabahi kuhusu Afya, Uenendo, Maisha yao ya kila siku na Changamoto zilizo mbele yao na hususani ikilenga zaidi watoto wa kike ambao wao ndio wahanga wa ugonjwa wa Endometriosis.

Magese alisema watoto hao wakiwafikia hata wenzao 20 tu kila mmoja basi takribani watu elfu kumi watakuwa wamefikiwa.

Alisema ni mwanzo tu angependa kupata ushirikiano na msaada wa Serikali ili afike kila pembe ya nchi yetu hii na kufikia wengi iwezekanavyo.

"Ninaamini -Nikiokoa hata nafsi moja kuna wakati ambao inatosha kwani nafsi hiyo yaweza kuokoa walio wengi zaidi,shabaha yake ni kuona wanawake wenye ugonjwa huo wanapata tiba mapema ili waweze kubaki na uwezo wao wa kushika mimba na kuzaa kwa njia ya kawaida" alisema Magese.

" Mimi nilichelewa na nimejikuta nikipoteza uwezo wa kushika mimba, kwa hiyo siwezi tena kupata mtoto kwa njia ya kawaida, Kibaiolojia.

"Nimeshafanyiwa oparesheni mara 13 kati ya Afrika Kusini na Marekani. Na sasa mirija yangu yote ya uzazi imeziba, vilevile upande mmoja wa ovari haufanyi kazi.

"Naahidi kupambana na ugonjwa huu mpaka mwisho. Pamoja na jitihada zote, lengo langu la juu ni kuhakikisha napata uwezo wa kujenga hospitali kubwa kupitia taasisi yangu ya Millen Magese (Millen Magese Foundation) ambayo itajishughulisha zaidi na utoaji wa tiba ya endometriosis kwa wanawake. Namuomba sana Mungu anisaidie." Alisema Millen

Alisema lengo lake kuu na Taasisi yangu ni kujenga hospitali maalum ya magonjwa ya wanawake hapa nchini.

"Nitashukuru sana iwapo Serikali yako tukufu itatusaidia kupata eneo la kutosha na kutupa muongozo na uwezeshaji mwingine utakaohitajika kadri harakati zitakapokuwa zikiendelea".

Alisema tayari Taasisi ya Millen Magese kwa kushirikiana na ProjectCure ya Marekani imeweza kukusanya vifaa vinavyohusu afya ya mwanamke vyenye thamani ya takribani dola laki moja , ningeomba sana Serikali yako Tukufu kutusaidia kuweza kusafirisha na kuviingiza vifaa hivyo nchini (kwa maana ya taratibu, gharama za usafirishaji na kodi husika).

"Kwa namna moja ama nyingi napenda kuishukuru Wizara ya Afya kupitia kwa Waziri wake Ummy Mwalim na Naibu Waziri Hamis Kingwangwalah, pamoja na Mkuu wa Mkoa Paul Makonda, kwa uhirikiano wao na taasisi yangu ya Millen Magese, katika kuhakikisha tunafanikisha suala la ujenzi wa kituo cha Hospitali.

"Tuko katika maengezi na Hospitali ya Kairuki, ambao wamejitolea kuungana name katika ksaidia tatizo hili, ikiwa ni pamoja na kushirikiana na Hospitali za Serikali katika kusaidia wanawake wenye tatizo hilo.

"Hospitali ya Kairuki imejitolea kusaidia wanawake wenye matatizo hayo, nina amini kwa ushirikiano wake Mhe. Makamu wa Rais, tatizo hili litapewa uzito unaostahili.

"Mheshimiwa Makamu wa Rais,Elimu ya masuala ya uzazi na afya ya mwanamke zifundishwe kwa wadogo zetu, tusichelewe na baadhi yao yakawafika madhla haya yasiyomithilika kama yangu, wakati mwingine huwa nahisi kama visu vinapit tumboni mwangu, natapika, nazimia, nashindwa hata kufanya kazi zangu, ni hivi karibuni tu katika onesho kubwa la mavazi, nilizimia niliporudi nyuma ya jukwaa (Namshukuru Mungu kwa YOTE)

"Naendelea pia na kujitoa katika shughuli za kijamii, kama ambavyo nimeshafanya kama kujenga madarasa na uchangiaji wa madawati, kama ambavyo nimewahi kufanya mkoani Mtwara.

"Nataka pia niwe balozi mzuri wa elimu yetu.

"Mheshimiwa Makamu wa Rais, Sitaki kulia, nimeamua kuwa SAUTI. Sitaki kumuuliza Mungu kwa nini, nimeamua kupokea na kutimiza mapenzi yake. Mheshimiwa Makamu wa Rais, #UpasuajiMara13Umetosha

#TunahitajiUtafitiZaidiKupataTIBA. Daima najivunia nyumbani na popote nilipo duniani ..Tanzania imebaki kuwa tunu ya uwepo na maisha yangu.

"Mwisho nakushukuru mheshimiwa makamu wa rais kwa mkutano huu, nawashukuru wote tuliokutana hapa. Mungu AWABARIKI.

"Naomba unipe ruhusa kama ishara kukukabidhi Tuzo na Tunu mbalimbali nilizozitaja kwa Heshima ya Taifa, Nchi yangu ya Tanzania, Serikali yangu na ndugu zangu Watanzania

#NawapendaSANA.

"Kule kwetu Usukumani kwa heshima huwa tunapiga goti kama Heshima, Mheshimi wa Makamu wa Rais, Mama, nasema Wabeja SANA."

Viewing all 45270 articles
Browse latest View live




Latest Images