Quantcast
Channel: MPEKUZI
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Yatahadharisha Mvua Kubwa za Upepo Mkali

$
0
0

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa tahadhari ya kunyesha mvua kubwa inayozidi milimita 50 wiki hii.

Imesema mvua hizo ambazo zitanyesha katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Morogoro pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba zitakuwa kubwa na kuweza kusababisha madhara.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk Agness Kijazi ilisema mvua hizo zilitarajia kunyesha kuanzia Aprili 13, mwaka huu hadi Jumamosi Aprili 16, mwaka huu.

Dk Kijazi alisema kiwango cha uhakika wa mvua hizo ni kwa asilimia 70 na hali hiyo imetokana na kuimarika kwa ukanda wa mvua sambamba na uwepo wa kimbunga cha Fantala katika Bahari ya Hindi.

Hivyo aliwataka wananchi wanaokaa maeneo yaliyotajwa kuchukua hadhari na kuchukua hatua stahili ili kuepukana na madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na mvua hizo kubwa.

Hivi karibuni, TMA ilisema mvua za masika katika ukanda wa Pwani zilizoanza wiki ya kwanza ya mwezi huu kutakuwa na vipindi vifupi vya mvua kubwa zitakazoweza kusababisha mafuriko.

Aidha, kwa wakati huo hali ya joto kali itaendelea kuwepo nyakati za usiku huku ikipungua nyakati za mchana.


Serikali Yaanza Kulipa Deni La Mifuko Ya Hifadhi Ya Jamii

$
0
0

SERIKALI imeanza kulipa deni la mifuko ya hifadhi ya jamii na hadi kufikia Machi, mwaka huu tayari imeshalipa Sh bilioni 173.11 kwa mfuko wa PSPF huku ikidhamiria kulipa deni lote kufikia Juni, mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) mfuko huo pia umeweza kulipa hundi 49,467 na kati ya hizo 46,000 ni za pensheni za kila mwezi kwa wastaafu na 3,467 za madai mapya.

Aidha, taarifa hiyo inaeleza kuhusu hati fungani, mifuko ambayo ilikuwa bado haijaridhia hati ya makubaliano kwa sasa zimesharidhia.

“Serikali inatarajia kutoa Hati Fungani ya Sh trilioni 2.6 yenye riba ya asilimia 6.5 kwenda PSPF. Hati fungani hizi zitaiva kwa vipindi tofauti, kuna za miaka mitatu, mitano, saba, 10 na kuendelea,” ilieleza taarifa hiyo.

Kwa upande wa miradi ya uwekezaji, Mamlaka hiyo kwa kushirikiana na Benki Kuu (BoT) kwa mujibu wa sheria ilikamilisha ukaguzi wa mifuko kwa mwaka 2015. 

Ukaguzi huo ulisababisha mamlaka kwa kushirikiana na BoT kufanya ukaguzi maalumu kwenye majengo na milki za mifuko yote ya hifadhi ya jamii ukiwemo wa NSSF.

Aidha, ukaguzi huo unatarajiwa kuchukua kati ya miezi hadi tisa kulingana na upatikanaji wa taarifa na kwamba wakati kaguzi hizo zikiendelea mifuko iliyovuka viwango vya uwekezaji imezuiwa kuendelea kuwekeza katika maeneo hayo.

Taarifa hiyo pia ilieleza kuwa mifuko imeonekana kuwa na gharama kubwa ya uendeshaji na kwamba kuwepo kwa gharama hizo kutazorotesha utendaji wa mifuko ya hifadhi ya jamii.

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Ijumaa ya April 15

Waliofunga Mita za Mafuta Bandarini Dar kikaangoni..... Ni wale waliogundulika baada ya ziara ya kushtukiza ya Waziri Mkuu

$
0
0

Kamati ya Miundombinu imeitaka Serikali kuchunguza kwa kina na kuchukua hatua za kisheria kwa yeyote aliyehusika na kufungwa mita za mafuta zilizopo Bandari ya Dar es Salaam, bila kufanya kazi kwa miaka mitano. 

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk Norman Sigala alisema kuna haja ya Serikali kujiridhisha kwa umakini lengo la kufungwa kwa mita hizo na sababu ya kufungwa kwake, kisha ichukue hatua.

“Kamati yetu inatambua wajibu wake ikiwamo kuielekeza Serikali, kuishauri na kuikosoa bila uoga tulitembelea tukaona zile mashine moja ya mafuta ya dizeli tayari ilifungwa na inaendelea kufanya kazi, sasa hiyo nyingine Serikali inapaswa kwenda ndani zaidi kiuchunguzi na kuchukua hatua kali kwa yeyote aliyehusika,” alisema. 

Februari 12, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alifanya ziara ya ghafla kwenye Kitengo cha Upimaji Mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam na kukuta mita zimejaa kutu baada ya kutelekezwa kwa miaka zaidi ya mitano. 

Kutokana na hali hiyo, alimpa saa nne Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo (WMA), Magdalena Chuwa aandike barua ya kujieleza ni kwa nini aliamua kufunga mita hizo zisitumike kwa zaidi ya miaka mitano iliyopita. 

Akizungumzia kiwango cha fedha za bajeti ya Sh4 trilioni iliyotengwa kwa ajili ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, alisema kamati yake inaridhishwa na kiwango hicho. 

Hata hivyo, alisema Serikali inapaswa kuongeza upembuzi katika uteuzi wa watendaji wa idara na taasisi zake, ili kuepusha vitendo vya ufisadi ambavyo vimekuwa vikigharimu fedha nyingi kutafunwa ama kupotea katika mazingira ya kutatanisha, hivyo kukwamisha juhudi za maendeleo. 

“Serikali ifanye uteuzi vyema wa watendaji wake kigezo cha uadilifu na uwezo wa kazi kiangaliwe kwa makini, huwezi kuzuia rushwa mahali ambapo kiongozi si mwadilifu, kamati inaishauri Serikali nafasi hizo zisitolewe kama zawadi,” alisema. 

Alisema wameridhishwa na utendaji wa baadhi ya viongozi wanaokaimu nafasi za ukurugenzi wa taasisi hivyo na wameishauri Serikali pia iwathibitishe watu hao ili waweze kuwa na moyo wa kufanya kazi vizuri zaidi.

Akizungumza kuhusu bajeti, Dk Sigala alisema kamati yake imeridhishwa na mipango ya Serikali iliyoweka kwa mwaka huu wa fedha 2016/17 kwa wizara hiyo inayolenga kuboresha miundombinu muhimu. 

“Serikali imetenga mafungu ya fedha kwa ajili ya kuboresha reli, barabara, viwanja vya ndege pamoja na kununua ndege nne, na kwa kuanzia imetenga Sh250 bilioni kununulia mbili za kuanzia katika mwaka huu wa fedha,” alisema. 

Alisema hata hivyo katika kuboresha utendaji wa Mamlaka ya Bandari wameishauri Serikali kupunguza baadhi ya gharama ambazo zinakuwa zinatozwa na mamlaka hiyo, nia ikiwa ni kuwezesha wavutia wafanyabiashara na kumudu ushindani na bandari za nchi nyingine. 

HakiElimu Yashauri Mambo Matano Muhimu Katika Bajeti ya Elimu 2016/2017

$
0
0

Katika kuelekea bunge la bajeti hivi karibuni, serikali imeshauriwa kuongeza bajeti ya sekta ya elimu kwa mwaka wa fedha 2016/2017 ili kuendana na kauli ya upatikanaji wa elimu bure sambamba na kufidia gharama za uboreshaji na ujenzi wa miundombinu.

Kauli hiyo imetolewa jana Jijini Dar es Salaam na John Kalage Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Hakielimu, wakati alipokuwa akitoa taarifa ya uchambuzi na ushauri wa Shirika la Hakieli juu ya mwelekeo wa bajeti ya elimu2016/2017.

Kalaghe alisema serikali haina budi kuongeza bajeti ya sekta ya elimu kwa mwaka wa fedha 2016/2017 hadi kufikia asilimia 20 ya bajeti ya taifa au asilimia 6 ya pato lote la taiafa.

Aidha alisema kwa mujibu wa uchambuzi walioufanya kama shirika, na kwa kuzingatia takwimu za idadi ya wanafunzi, shule na mahitaji, kila mwaka serikali itapaswa kutenga kiasi cha fedha kisichopungua Tsh. bilioni 1,034.5 nje ya mahitaji mengine ya kisekta ili kugharamia elimu bila malipo.

“Tunafahamu hivi karibuni bunge linatarajiwa kuanza vikao vyake na kama watetezi na mdau wa upatikanaji wa elimu bora nchini, tunapendekeza kwa serikali maeneo ambayo yanahitaji kutiliwa mkazo katika upangaji wa bajeti ya sekta ya elimu yazingatiwe” amesema Kalage.

Akizungumzia maeneo muhimu ambayo serikali inatakiwa kuyazingatia katika upangaji wake wa bajeti kupitia sekta hiyo alisema ni pamoja na eneo la bajeti ya utekelezaji wa elimu bila ada, upangaji wa bajeti ya sekta ya elimu, bajeti ya ukaguzi na uhakiki wa ubora wa elimu, mwongozo wa sera ya mpya ya elimu na makadirio bajeti ya sekta ya elimu 2016/2017.

Alibainisha kuwa eneo la bajeti ya utekelezaji wa elimu bila ada, linapaswa kuanza kutekelezwa kabla ya agizo la elimu bila ada, suala hilo lilikuwa likitekelezwa kupitia michango ya wazazi kwa kuchangia elimu kwa kushirikiana na serikali.

Aidha kuhusu gharama za kufidia ada na ruzuku shuleni kwaajili ya vifaa, gharama za mitihani na gharama za uendeshaji kwa shule za msingi na sekondari alisema, kwa kuwa gharama hizo zilikuwa zikifanikishwa awali kwa ushirikiano wa michango ya wazazi na serikali basi serikali inapaswa kufidia gharama zote kwa kutenga kiasi cha sh.bilioni 161.5 katika maeneo hayo.

Akielezea gharama za kufidia ujenzi na miundombinu ambao nao ulikuwa ukichangiwa na wazazi alisema serikali kufidia gharama hizo kwa kutenga bilioni 1, 438 huku kwa upande wa gharama za kufidia utoaji wa uji katika shule za msingi na awali itenge kiasi cha sh 198.

Vile vile kuhusu upangaji wa bajeti wa sekta ya elimu, alishauri kuwa licha ya changamoto zilizopo katika upangaji wa matumizi katika sekta ya elimu, serikali inatakiwa kuangalia namna ya kuweka uwiano wa bajeti ya matumizi ya kawaida na ya maendeleo.

“Tunaona katika kipindi cha miaka mitano iliyopita wastani wa bajeti ya maendeleo ya sekta ya elimu imekuwa kati ya asilimia 11 hadi 16 tu wakati ile ya matumizi ya kawaida ikifikia asilimia 80 hadi 90, kihalali kiasi kinachotengwa ni kidogosana kulinganisha na changamoto,

“Mathalani bajeti ya mwaka 2015/2016 bajeti nzima ilikuwa sh. Bilioni 3,887 huku bajeti ya maendeleo ikiwa ni asilimia 16 tu” amesema.

Mafaili ya Kampuni ya Lugumi Yatua TAKUKURU

$
0
0

Mkurugenzi Mkuu Takukuru-Valentino Mlowola
Sakata la kampuni ya Lugumi iliyoingia mkataba wa Sh37 bilioni na Jeshi la Polisi wa kufunga mashine za kielektroniki za kuchukua alama za vidole nchi nzima, sasa limetua Takukuru baada ya taasisi ya kupambana na rushwa kuchukua faili lake la usajili.

Kampuni hiyo ilibainika kutotimiza matakwa ya mkataba wake baada ya kufunga mashine 14 tu kati ya 108 ilizotakiwa kufunga, licha ya kulipwa  asilimia 99 ya fedha kwa mujibu wa mkataba.

Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG) ya mwaka 2013/14 ndiyo iliyofichua udhaifu huo.

Wakati Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ikitaka nguvu itumike ili Jeshi la Polisi liwasilishe mkataba huo, utata umeibuka katika umiliki wa kampuni hiyo kutokana na kuwepo tuhuma kuwa baadhi ya vigogo wa Polisi na wanasiasa ni wanahisa wa Lugumi Enterprises.

Jana, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela), Frank Kanyusi alisema kuwa Takukuru inashughulikia suala hilo, huku akibainisha kuwa kwa sasa Brela hawana takwimu za kina za kampuni hiyo.

“Kampuni hii ilisajiliwa kihalali na kupewa cheti cha usajili. Ila ninachoweza kukueleza kwa sasa ni kwamba jalada la usajili la Lugumi lipo Takukuru kwa ajili ya uchunguzi zaidi,” alisema Kinyusi jana.

Kanyusi, ambaye hakutaka kuzungumzia kiundani kuhusu usajili wa kampuni hiyo, alisema: “Waandishi wa habari wamekuwa wakiniuliza maswali mengi kuhusu suala hili ila kwa sasa hali ndiyo hiyo. Jambo hili lipo Takukuru.”

Alisema kwa sasa kampuni zilizosajiliwa na Brela zipo 120,000 na zinakaribia kufika 130,000 na kwamba kampuni lazima zitoe taarifa zake kila mwaka, kinyume na hapo zinaweza kuchukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kufutwa.

Habari za uhakika kutoka ndani ya Brela zilieleza  kuwa taarifa za usajili wa kampuni hiyo zilitoweka takribani miezi miwili iliyopita.

Mwandishi  alipofika katika ofisi za wakala huyo kwa ajili ya kupata ukweli wa usajili, alielezwa na mmoja wa watumishi ambaye hakutaka jina lake kuwekwa wazi kwamba ni vigumu kupata hilo jalada kwa sababu ya mvutano ulioibuka.

Hata baada ya kufuata taratibu za kupewa jalada hilo kwa ajili ya kupitia masuala mbalimbali, alijibiwa kuwa jalada hilo halionekani ingawa baadaye Kanyusi alisema limechukuliwa na Takukuru.

Sakata la Lugumi liliibuka wiki iliyopita wakati PAC ilipokutana na Jeshi la Polisi kupitia taarifa ya hesabu zao za mwaka 2013/14 zilizokaguliwa na CAG.

Katika hesabu hizo ilibainika kuwa mwaka 2011, Polisi iliingia mkataba na Lugumi kwa ajili ya kufunga mashine hizo katika vituo 108 vya polisi kwa gharama ya Sh 37 bilioni.

Hata hivyo, ilibainika kuwa kampuni hiyo imefunga mitambo hiyo kwenye vituo 14 tu, huku ikilipwa asilimia 99 ya fedha hizo.

Kutokana na ukakasi huo, PAC ambayo ilibaini viashiria vya ufisadi katika mkataba huo, iliagiza watendaji wa Polisi kuwasilisha taarifa za mkataba huo pamoja na vielelezo vyake ili kamati hiyo iweze kuupitia na kujiridhisha.

Lakini hadi sasa Jeshi la Polisi halijawasilisha mkataba huo, jambo ambalo huenda likazua mjadala mkali katika mkutano wa Bunge unaoanza Jumanne ijayo.

Anne Kilango Malecela Afunguka Baada ya Rais Magufuli Kumsimamisha Kazi ya Ukuu wa Mkoa wa Shinyanga

$
0
0

Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anne Kilango Malecela, ameibukia kanisani na kutoa ya moyoni, ikiwa siku tano baada ya Rais Dk. John Magufuli kutengua uteuzi wake.

Kilango, Jumatatu wiki hii uteuzi wake ulitenguliwa baada ya Machi 20, mwaka huu, kudai kuwa mkoa wa Shinyanga hauna mtumishi hewa wa serikali hata mmoja.

Hata hivyo, Ikulu ilifanya uchunguzi na kubaini kuwa katika taarifa za awali kuna watumishi hewa 45, huku kazi ya uhakiki ikiendelea katika wilaya za Ushetu na Shinyanga.

Rais Magufuli aliwaagiza wakuu wa mikoa wote, alipokuwa akiwaapisha kuwa wafanya uchunguzi kuhusu uwapo wa watumishi hewa katika mikoa yao na kutoa taarifa.

Kutokana na kutoa taarifa hizo zisizo za kweli, Jumatatu wiki hii, Rais Magufuli alitangaza kutengua uteuzi wake, akiwa amekaa kwenye nafasi hiyo kwa siku 27. Kilango amekuwa mkuu wa mkoa wa 19 tangu kuanzishwa kwa mkoa huo.

Mbali na Kilango, Rais Magufuli pia alimsimamisha kazi Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, Abdul Dachi, kutokana na taarifa hizo za kutokuwapo watumishi hewa katika mkoa.

Alivyosema Kanisani
Akiwasalimia waumini wenzake juzi, katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kusini Mashariki ya Ziwa Victoria, mjini Shinyanga, baada ya kupewa fursa ya kusema neno, Kilango alisema anamshukuru Mungu kwa kila jambo kwa yote yaliyomtokea.

“Ndugu waumini wenzangu, hili ni jambo la kumshukuru Mwenyezi Mungu. Hata mtu unapojifungua mtoto akafariki dunia, unamshukuru Mungu kwani hayo ni mapenzi ya Mungu.

"Ukiona mzazi wako kafariki dunia pia, unamshuruku Mungu. Tunao wajibu wa kumshukuru Mungu kwa kila jambo,” alisema kwa maneno mafupi na kisha kuketi, huku akiacha simanzi miongoni mwa waumini wenzake, wakiwamo viongozi wa kanisa.

Alivyoanza Kazi
Mbele ya kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC), muda mfupi baada ya kuanza kazi, Kilango alisema Shinyanga ni mkoa wenye changamto nyingi ambazo atazishughulikia, lakini atakuwa akilazimika kukimbia Dar es Salaam kumwona mwenzi wake, Mzee John Malecela ambaye ni mgonjwa, na pindi hali yake ikiimarika wataungana naye mjini Shinyanga.

Hayo aliyasema Machi 22, mbele ya wajumbe wa kikao cha kamati hiyo na Ijumaa Machi 25, alisali kanisani hapo.

Sambamba na hayo, aliahidi kupambana na watumishi wazembe na wale wanaoendekeza rushwa na ufisadi na kurejesha hadhi ya mkoa wa Shinyanga kimaendeleo.

Kilango ambaye yuko mjini Shinyanga, akisubiri kukabidhi ofisi kwa mrithi wake kwa mujibu wa utaratibu, bado anaishi hotelini kwa vile aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo, Ally Rufunga, hajaondoka katika nyumba ya serikali iliyoko Ikulu ndogo, eneo la Lubaga.

Takukuru Yalia na Rushwa Mahakama ya Kisutu

$
0
0

Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai ameiomba mahakama iingilie kati kile alichokiita rushwa ya kutisha kwenye taasisi hiyo ya kutoa haki.

Wakili Swai alitoa wito huo baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Kisutu kumuachia huru mkurugenzi mkuu wa zamani wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), William Geofrey Mhando na wenzake wanne akiwamo mkewe Eva Mhando, katika kesi aliyokuwa akiiendesha. 

Katika kesi hiyo, Mhando, mkewe na maofisa wengine watatu wa zamani wa Tanesco; France Lucas Mchalange, Sophia Athanas Misida na Naftali Luhwano Kisinga, walikuwa wakikabiliwa na mashtaka ya matumizi mabaya ya madaraka, kughushi na kuwasilisha nyaraka za uongo kwa mamlaka za Serikali.

Hata hivyo, washtakiwa hao wameibwaga Takukuru baada ya mahakama kuona kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha tuhuma dhidi yao.

“Haki haijatendeka na tunatarajia kukata rufaa,” alisema Wakili Swai alipozungumza na waandishi nje ya mahakama.

“Rushwa iliyopo mahakamani inatisha. Serikali inatakiwa kuingilia kati.”

Hata hivyo, wakili huyo hakueleza rushwa hiyo ilifanyikaje katika kesi hiyo ambayo iliendeshwa na taasisi hiyo iliyopewa dhamana ya kuzuia na kupambana na jinai hiyo.

Awali hukumu hiyo ilipangwa kutolewa Aprili Mosi mwaka huu na Hakimu Mkazi Mkuu, Kwey Rusema aliyekuwa akisiliza kesi hiyo, lakini ikaahirishwa hadi Aprili 6, ambayo pia ilisogezwa mbele hadi jana iliposomwa na Hakimu Mkazi Hellen Riwa.

Akisoma hukumu hiyo kwa niaba ya Hakimu Rusema, Hakimu Riwa alisema kwa mujibu wa ushahidi, suala la msingi lilikuwa ni mkataba kati ya kampuni ya Santa Clara Supply Limited na Tanesco.

Alisema katika mkataba, Mhando, ambaye alikuwa mshtakiwa wa kwanza, alituhumiwa kutumia madaraka yake vibaya kwa kushindwa kutangaza maslahi yake kuwa kampuni ya Santa Clara ni ya Eva Mhando ambaye ni mkewe.

“Suala la msingi la kujiuliza ni vipi mshtakiwa huyo anahusika katika utoaji wa zabuni na nani aliyekuwa na maamuzi ya mwisho,” alisema Hakimu Riwa akisoma hukumu hiyo iliyoandaliwa na Hakimu Rusema.

“Jibu la swali hilo ni kwamba Bodi ya Zabuni ya Tanesco ndiyo iliyohusika na mchakato huo.”

Hakimu Riwa aliongeza kuwa miongoni mwa washtakiwa hao, hakuna hata mmoja aliyekuwa mjumbe katika vikao vilivyoendeshwa na bodi hiyo ya zabuni, wala kuitwa kuhudhuria mkutano wowote wa bodi hiyo.

“Kutokana na sababu hiyo, inawezekana vipi mshtakiwa huyu akatangaza maslahi yake katika mkutano ambao hakuhudhuria?”

Kuhusu suala la mshtakiwa huyo kujua kama Santa Clara inamilikiwa na mkewe na watoto wake, alisema kuwa inawezekana asijue kama wana kampuni.

Alisema kuwa hakuna ushahidi kuwa mshtakiwa huyo aliulizwa swali lolote kuhusu kampuni hiyo.

Katika kusisitiza hoja hiyo, Hakimu Rusema katika hukumu yake hiyo alitoa mfano kuwa mwanamke anaweza kufungua akaunti kwa siri benki na akaweka fedha kisha mumewe asijue.

Kuhusu suala la mshtakiwa wa pili, Eva, kughushi nyaraka na kuziwasilisha Tanesco, alisema hakuna ushahidi wowote unaoonyesha kuwa alifanya kosa hilo na kwamba aliyesaini nyaraka hizo ni mtu mwingine ambaye hata hivyo hakushtakiwa.

Wakati wote Hakimu Riwa alipokuwa akisoma hukumu hiyo, baadhi ya watu ambao wanasadikiwa kuwa ndugu wa washtakiwa hao, walionekana wakifanya ishara ambazo zilionyesha wanamuomba Mungu.

Baada ya hukumu hiyo na kuachiwa huru, Mhando alionekana kutoamini na alipotoka mahakamani, alielekea moja kwa moja kwenye gari lake na kukataa kuongea na mtu yeyote.

Hali hiyo ilionekana kuwatia hofu ndugu zake ambao baadhi walimshauri asiendeshe gari, badala yake aendeshwe kwa kuhofia kuwa kwa hali aliyokuwa nayo angeweza kusababisha ajali.

“Msimuachie aendeshe, Mhando kaa kiti cha nyuma,” alisema mmoja wa ndugu zake. Mhando alikubali na kuhamia kiti cha nyuma kisha mkewe naye aliingia kwenye gari hilo na kuondoka viwanja vya mahakama.

Washtakiwa hao walipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza Mei 26, 2014 na kusomewa mashtaka na Wakili Swai.

Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria Yakataa Kuipokea Taarifa ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF)

$
0
0

Taarifa ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) iliyowasilishwa jana kwenye Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria imekataliwa baada ya kubainika upungufu, ukiwamo udhaifu wa Sera ya Uwekezaji na kiasi cha fedha kilichowekezwa katika miradi iliyopita.

Uamuzi huo umekuja wiki moja baada ya kamati hiyo kuagiza kusimamishwa miradi yote mipya inayotarajiwa kutekelezwa na NSSF hadi Serikali itakapopitia ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na kujiridhisha na utendaji wa mfuko huo.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mohamed Mchengulwa alitoa agizo hilo baada ya kufanya ziara katika ofisi ya Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) ambapo baada ya kupokea ripoti ya SSRA, alisema: “Kamati inaagiza kwamba SSRA isimamie miradi yote mipya inayotarajiwa kutekelezwa hivi sasa isimame haraka, ili iweze kujiridhisha na hesabu ambazo zimefanyika.”

Akizungumza baada ya kikao kati ya kamati hiyo na NSSF jana, Mchengulwa alisema mbali ya mfuko huo kutoonyesha gharama za uwekezaji katika miradi iliyopita, pia alisisitiza taarifa ya mfuko huo haijaonyesha miradi ambayo imeidhinishwa mwaka huu wala miradi ambayo iko kwenye hatua za mwisho za umaliziaji.

Mchengulwa alisema baada ya kubaini upungufu huo wanasubiri kwanza ripoti ya CAG iwasilishwe bungeni, Dodoma, Aprili 25, mwaka huu ili iweze kuijadili kwa kina.

“Baada ya kubaini mapungufu haya, tumeamua kusubiri kwanza Serikali iwasilishe bungeni ripoti ya CAG ili nasi tuanzie hapo.Kwa sasa hatuwezi kupata taarifa ya CAG kwa sababu bado iko kwa Rais,” alisema Mchengulwa.

Mchengulwa, ambaye pia ni mbunge wa Rufiji alisema, “Sisi hatufanyi kazi kwa kusikiliza vyombo vya habari ila tunataka kujiridhisha baada ya kusoma ripoti ya CAG. Baadhi ya wanachama wanajitoa NSSF kwa sababu ya kashfa za ufisadi tunazoziona kwenye mitandao na magazeti.”

Kilichowashtua wabunge hao ni ripoti za vyombo vya habari kuhusu harufu ya ufisadi katika miradi mbalimbali ya mfuko huo; ardhi kuthaminishwa kwa kati ya Sh800 milioni na Sh1.8 bilioni kwa ekari moja; kampuni mbili kulipwa kwa kandarasi moja, mkandarasi kuzidishiwa malipo, na ukiukwaji katika utolewaji wa zabuni.

Miradi iliyoanzishwa na NSSF ambayo vyombo vya habari vimeonyesha kwamba ina harufu ya ufisadi ni wa ujenzi wa mji mpya wa Dege Eco Village, Kigamboni ambao thamani ya ekari moja ni Sh800 milioni; Arumeru ardhi imethaminishwa kwa Sh1.8 bilioni, mkandarasi wa ujenzi wa jengo la Mzizima ameongezewa Sh5 milioni.

Vyombo vya habari vilinukuu ripoti ya ukaguzi wa miradi uliofanywa na CAG pamoja na kampuni ya kimataifa ya Ernst & Young ambayo CAG amewasilisha kwa Rais John Magufuli, ingawa inadaiwa baadhi ya mambo yameondolewa baada ya majibu kupatikana kutoka NSSF.

Mchengulwa alisema baada ya ripoti ya CAG kuwasilishwa bungeni, kamati yake itamwita CAG kueleza ukaguzi wake na itawahoji pia SSRA kwa kushindwa kusimamia mfuko huo.

“Ni wazi kwamba wanachama wengi wa NSSF wameanza kujitoa kwa sababu ya taarifa mbalimbali wanazoziona kwenye mitandao. Sasa hali hiyo ikiendelea mifuko mingi itakufa na wananchi watakosa imani na mifuko hiyo,” alisema.

Aidha, Mchengerwa alisema kamati yake imeitaka serikali na SSRA kuangalia namna wanavyoweza kupunguza mifuko ya hifadhi kwani mingi, inafanya kazi moja na baadhi ya mifu- ko ina hali mbaya kifedha kiasi cha kushindwa kulipa wanachama.

Ofisi ya Makamu wa Rais
Wakati huohuo, kamati hiyo imebaini ukiukwaji wa sheria katika ujenzi wa  jengo la Ofisi ya Makamu wa Rais ambalo tayari lina nyufa kuanzia chini mpaka juu na milango mibovu, jambo linaloashiria kwamba jengo hilo lina matatizo makubwa.

“Kuna baadhi ya kasoro katika kumbi za mikutano iliyopo katika jengo la makamu wa rais, kwa mfano, kumbi za mikutano zina milango midogo ya kutoka mtu mmoja, kama kuna dharura watu wanaweza kupata matatizo,” alisema Mchengulwa baada ya kutembelea jengo hilo.

“Nimeshaagiza Katibu wa Bunge aandike barua kumpa maelekezo CAG kuhusu ukaguzi wa jengo hilo. Wakala wa Majengo (TBA) wamejitetea hapa lakini tunataka kupata taarifa kamili ya value for money kutoka kwa CAG,” alisema.

Mwenyekiti huyo alisema sheria inaruhusu mkandarasi kulipwa asilimia 90 ya gharama zote na baada ya kukabidhi jengo analipwa asilimia 10 ya fedha zilizobaki, lakini alilipwa asilimia 98 ya fedha zote ambazo ni Sh8 bilioni na kubaki na asilimia mbili ambayo ni Sh200 milioni.

Watumishi HEWA Jijini Arusha Waongezeka na Kufikia 300

$
0
0

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Felix Ntibenda amesema idadi ya watumishi hewa mkoani humo imeongezeka baada ya uchunguzi wa awali huku baadhi ya waliokuwa wakifuja fedha za serikali kwa kudanganya wakiomba kuzirejesha.

Aidha, amesema mkoa umepoteza Sh bilioni 1.8 kwa mwaka jana kutokana na kulipa watumishi hewa. 

Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini  Arusha, Ntibenda alisema hivi sasa mkoa huo unafuatilia akaunti za watumishi hao hewa ili fedha hizo zirudishwe serikalini huku watumishi wengine baadhi waliokuwa wakifuja fedha za serikali kwa kudanganya wakiomba kuzirejesha.

Alisema awali wakati timu ya uchunguzi aliyoiunda kuchunguza watumishi hewa ilibaini mkoa huo kuwa na watumishi hewa 270, lakini hadi jana idadi hiyo imeongezeka na kufikia zaidi ya 300.

Alisema wilaya mbili za Karatu na Arumeru ndizo ambazo watumishi hewa wameongezeka. 

“Bado tunaendelea na uchunguzi na naamini wataongezeka lakini hivi sasa hao watumishi hewa wanahaha kurudisha fedha za serikali lakini hata kama wakirudisha watapelekwa mahakamani,” alisema Ntibenda.

Alisema hata kama fedha hizo watazirudisha, lakini watawafikisha mahakamani na pia wanafuatilia kujua ni kwa nini wakuu wa idara zao walifahamu udhaifu huo, lakini walikaa kimya na kuwalipa mishahara huku wakijua kuwa wanaihujumu serikali.

Alisisitiza ni vyema watu wakaacha tabia ya kujipatia fedha nyingi kwa njia isiyo halali kwani watumishi hewa wanasababisha fedha za serikali kushindwa kufanya shughuli nyingine badala yake kupata hasara.

Katikati ya mwezi uliopita, wakati akiwaapisha wakuu wa mikoa wapya, Rais John Magufuli aliagiza waende kufuatilia watumishi hewa katika mikoa yao na hadi sasa wamegundulika watumishi hewa zaidi ya 4,000.

Rais Wa Sudani Kusini, Mhe. Jenerali Salva Kiir Mayardit Awasili Nchini

$
0
0
Rais wa Sudani Kusini, Mhe. Jenerali, Salva Kiir Mayardit (mwenye kofia nyeusi) akishuka katika ndege ya Shirika la Kenya mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius K. Nyerere kwa ajili ya ziara ya kikazi ya siku moja, 15 Aprili, 2016 Jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe. Balozi Augustine Mahiga (kushoto) akisalimiana na Rais wa Sudani Kusini, Mhe. Jenerali, Salva Kiir Mayardit (mwenye fimbo) mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius K. Nyerere kwa ajili ya ziara ya kikazi ya siku moja, 15 Aprili, 2016 Jijini Dar es Salaam.
Rais wa Sudani Kusini, Mhe. Jenerali, Salva Kiir Mayardit (mwenye fimbo) akisalimiana na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Richard Sezibera (wa pili kushoto) mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius K. Nyerere kwa ajili ya ziara ya kikazi ya siku moja, 15 Aprili, 2016 Jijini Dar es Salaam.
Rais wa Sudani Kusini, Mhe. Jenerali, Salva Kiir Mayardit (kulia) akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius K. Nyerere kwa ajili ya ziara ya kikazi ya siku moja, 15 Aprili, 2016 Jijini Dar es Salaam.

Ashikiliwa na Polisi kwa Kumtukana Rais Magufuli

$
0
0

Jeshi la Polisi Mkoani Arusha, limemkamata Isaack Habakuk Emily, kwa kosa la kumtukana Rais John Magufuli kuwa ni bwege na kwamba hawezi fananishwa na Nyerere na kusambaza ujumbe kwenye mitandao ya kijamii.

Akizungumza ofisini kwake, leo jijini Arusha, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, amesema kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa Machi 22 mwaka huu eneo la Hotel ya Anex jijini humo.

Amesema kuwa baada ya kumkamata alifanyiwa upekuzi na kukutwa na simu ya kiganjani aina ya Tecno iliyotumika kutenda kosa la kutuma ujumbe wa kumkashifu Dkt. Magufuli.

Mkumbo amesema kuwa mtuhumiwa huyo alituma ujumbe wa kashfa kwenye Facebook usemao:- “Mnamlinganishaje Magufuli na Nyerere,” na kutuma kwa watu mbalimbali kupitia simu yake ya mkononi.

Mkumbo amesema mtuhumiwa baada ya kusikia hivyo aliandika tena ujumbe kwenye mtandao wake usemao, “Hizi ni siasa za maigizo halafu mnamfananisha huyu bwege na Nyerere wapi Bwana,” amesema.

Amesema baada ya kutuma ujumbe huo uliwaudhi watu wengi waliopokea ujumbe huo na kuwakwaza, hali iliyosababisha kupeleka malalamiko yao Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Mamlaka hiyo ilitoa taarifa polisi na hatua za kisheria zilianza kuchukuliwa.

Aidha amesema baada ya hapo walifanikiwa kumpata mtuhumiwa wa uhalifu kwa njia ya mtandao, kumtia hatiani na jana alifikishwa mahakamani kujibu shitaka lake.

Hata hivyo Jeshi la Polisi limetoa rai wa watu wote kutumia mitandao ya kijamii vizuri kwa kujiletea maendeleo na kubadilishana taarifa zenye tija na siyo zenye kuvunja sheria.

Pia amesema Jeshi hilo limejipanga kuwatia nguvuni wale wote watakaovunja sheria kwa kutumia mitandao ya kijamii.

Mambo Muhimu Ya Kuzingatia Kuhusu Matumizi Ya Daraja La Kigamboni

$
0
0

Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano inapenda kutaarifu Umma kuwa Daraja la kigamboni litaanza kutumika siku ya Jumamosi tarehe 16, Aprili, 2016 kuanzia saa 12:00 asubuhi.

Katika siku za mwanzo, magari yatapita bila kulipia tozo hadi Serikali itakapokamilisha taratibu na kutangaza utaratibu wa kulipia. 

Aidha, watembea kwa miguu na waendesha baiskeli watavuka bure katika Daraja la Kigamboni.  Hata hivyo maguta na mikokoteni haitaruhusiwa kutumia daraja hilo kutokana na sababu za kiusalama.

Magari yatakayoruhusiwa kupita katika Daraja la Kigamboni katika siku hizo za mwanzo ni yale yenye uzito usiozidi tani 10, hatua ambayo itasaidia kufuatilia mwenendo wa upitaji wa magari katika daraja, barabara za juu (Interchange) katika eneo la Kurasini, pamoja na kuhakikisha kwamba magari yanayotoka au kuingia katika daraja hayasababishi msongamano wa magari katika Barabara ya Nelson Mandela, Barabara ya Kilwa na maeneo mengine ya jiji.  

Baada ya utaratibu kukamilika magari ya aina zote yenye uzito unaoruhusiwa kisheria yataruhusiwa kupita katika daraja.
 
Mambo muhimu ambayo madereva na watumiaji wengine wa barabara wanatakiwa kuzingatia ni:-
1) Kuzingatia sheria ya Usalama Barabarani ikiwa ni pamoja na kufuata mwendo kasi unaotakiwa ili kuepuka ajali na kuepuka uharibifu miundombinu ya daraja
2) Kufuata alama za barabarani zilizowekwa katika ‘Interchange’ ya Kurasini ili kwenda kwenye uelekeo sahihi.
3) Kuzingatia alama zilizowekwa kwenye milango (Toll Gates) ya Kituo cha kulipia tozo (Toll Plaza) ili kuepuka uharibifu wa miundombinu ya kituo hicho.
4) Madereva na watumiaji wa barabara wengine watakaosababisha uharibifu wa aina yeyote wa miundombinu ya daraja watatozwa faini au kuchukuliwa hatua nyingine za kisheria.
5) Kutunza mazingira kwa kuepuka kutupa takataka katika eneo la daraja.

Aidha, Wizaraya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano inawataka madereva wa magari ya mizigo wanaoegesha katika barabara ya Nelson Mandela wakisubiri kuingia bandarini watafute eneo stahiki la maegesho na kuyaondoa magari hayo kwani hatua za kisheria zitachukuliwa kwa wale watakaoenda kinyume na agizo hili.

Msongamano wa magari hayo husababisha uharibifu wa barabara na usumbufu mkubwa kwa watumiaji wa barabara katika eneo hilo.

Imetolewa na;
Eng. Joseph M. Nyamhanga
Katibu Mkuu  (Ujenzi)
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
14 Aprili, 2016

Wizara Yakemea Mauaji Ya Wazee Nzega

$
0
0

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto imesikitishwa na kulani viakli matukio ya mauaji ya wazee  kumi (10) yaliyotokea wilaya ya Nzega, mkoani Tabora kwa kipindi cha mwezi Januari hadi Machi, 2016.

Inaelezwa kuwa, miongoni mwa chanzo cha mauaji ya wazee ni imani za kishirikina, uchu wa kumiliki mashamba na visasi mambo ambayo Serikali imekuwa ikiyakemea vikali. Wizara inawataka wananchi kushirikiana na uongozi wa Wilaya ya Nzega, kuhakikisha kuwa watuhumiwa wa mauaji haya wanakamatwa na kuchukuliwa hatua kali ili kuwa fundisho kwa watu wengine. 

Wizara inasisitiza kwamba  wazee ni binadamu, na wanayo haki ya kuishi na kupata hifadhi ya maisha yao kwa mujibu wa Sheria za nchi. 

Vitendo vya mauaji ya kikatili wanavyofanyiwa wazee vinasababisha hofu kubwa kwa wananchi. Mauaji hayo yanawakosesha amani na vinadhohofisha ari ya kufanya shughuli za za maendeleo ya familia na taifa kwa ujumla.

 Familia inayoishi na mzee anayewindwa, itatumia muda mwingi kutekeleza jukumu la ulinzi na hivyo kupunuza tija na uzalishaji wa mwananchi mmoja na familia kawa ujumla. Kwa kutambua hili Wizara inahimiza wadau wote kuunga mkono jitihada za Serikali katika ulinzi wa wazee na kuboresha huduma zao ili kuelekeza nguvukazi katika uzalishaji. 

Wizara inapenda kutoa pole kwa familia ambazo zimeguswa na mauaji ya wazee waliopoteza maisha kwa kuuawa kinyama. 

Wizara inaitaka jamii itambue kuwa wazee wana haki ya kuthaminiwa utu wao, kupata huduma stahiki, na kushiriki haki zote za msingi bila ubaguzi wowote ambao unaweza kuhatarisha maisha yao ikiwemo haki yao ya kuishi. 

Aidha, Jamii ihakikishe kuwa wazee na wananchi wote, wanaishi katika hali ya usalama, amani na utulivu kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa Taifa letu.

Erasto T. Ching’oro (Msemaji)
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto                                                                                         15/4/2016

Ofisi Ya Makamu Wa Rais Yakanusha Taarifa Zinazosambazwa Kwenye Mitandao Ya Kijamii Kwamba Ameyataka Makampuni ya Simu Kuzima Data


Mganga wa Zahanati Kigoma Atiwa Mbaroni kwa Tuhuma za Kumbaka Mgonjwa

$
0
0
Jeshi la Polisi mkoani Kigoma linamshikilia Mganga wa Zahanati ya kijiji cha Kidahwe wilayani Kigoma kwa tuhuma za kumbaka mgonjwa aliyekuwa akimtibu katika zahanati ya kijiji hicho.
 
Kamanda wa Polisi mkoa wa Kigoma Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Ferdinand Mtui amemtaja mganga huyo kuwa ni Ibrahim Bundala (29)na kwamba anatuhumiwa kumbaka binti mwenye umri wa miaka 14 aliyefika katika zahanati hiyo kwa ajili ya kupata matibabu.

Amesema mtuhumiwa huyo ambaye atafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika alitenda kosa hilo baada ya binti huyo kuingia katika chumba cha daktari kwa ajili ya kumueleza ugonjwa anaoumwa.

Katika tukio jingine wahamiaji 55 toka Burundi wamekamatwa katika maeneo mbalimbali baada ya kuingia nchini kinyume cha sheria na wamekabidhiwa idara ya uhamiaji kwa ajili ya taratibu nyingine ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani.

Mwenyekiti wa zamani CHADEMA Mwanza, Adrian Tizeba ahamia CCM

$
0
0

Aliyekuwa Mwenyekiti wa chama cha Demokrsaia  na Maendeleo Chedema mkoa wa Mwanza Andrian Tizeba, leo amejiunga rasmi na CCM wilayani  Sengerema tawi la Lugata.

Tizeba ambaye alitangaza kujivua uanachama wa chadema Machi 29 mwaka huu baada ya kusimamishwa uongozi kwa muda wa mwaka mmoja, na kutangaza kuachana na siasa, amekabidhiwa kadi hiyo  na katibu wa tawi hilo Alfred Mwambala.

Akizungumza kwa njia ya simu, Tizeba amesema uamuzi wake si wa kulazimishwa na mtu bali, ameona ni vema arudi kwenye chama chake cha awali.

Tizeba ambaye ni kaka wa mbunge wa jimbo la Buchosa, Charles Tizeba amesema, nia na dhumuni la kujiunga na chama hicho ni kutokana na utendaji wa Rais John Magufuli anaoufanya.

Mapokezi Ya Rais Wa Sudan Salva Kiir Ikulu Jijini Dar Es Salaam Na Utiaji Wa Saini Kujiunga Na Jumuiya Ya Afrika Mashariki

$
0
0
Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa pamoja na Mhe. Salva Kiir Mayardit, Rais wa Jamhuri ya Sudan Kusini wamesaini Mkataba wa kuiwezesha Jamhuri ya Sudan Kusini kuwa Mwanachama kamili wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Tukio hilo la kihistoria limefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 15 Aprili, 2016.

Akizungumza wakati wa haflya hiyo, Mhe. Dkt. Magufuli aliipongeza nchi hiyo na kusema kuwa anajivunia tukio hili la kihistoria kutokea wakati Tanzania ikiwa ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na kwamba ukurasa mpya wa ushirikiano na mahusiano na nchi hiyo umefunguliwa.

Aliongeza kuwa kihistoria Sudan Kusini, imekuwa na mahusiano ya karibu na nchi za Afrika Mashariki katika nyanja mbalimbali ikiwemo mwingiliano wa tamaduni, ushirikiano wa kibiashara na uchumi na ukaribu wa kijografia. Aidha, alieleza kuwa kujiunga kwa Sudan Kusini kwenye EAC kunaifanya Jumuiya hii kuwa na soko kubwa lenye takriban watu milioni 160.

Vile vile Mhe. Rais Magufuli alisema kuwa ili Jumuiya ya Afrika Mashariki iweze kuwa na maendeleo endelevu suala la kudumisha amani ni la msingi, hivyo aliwahimiza Sudan Kusini kuendeleza juhudi kwenye mazungumzo ya amani.

‘’Dhana ya Mtangamano ni kukuza biashara, uwekezaji na miundombinu ili kujiletea maendeleo endelevu katika Jumuiya yetu, hivyo nahimiza umuhimu wa nchi wanachama kudumisha amani ili kufikia malengo tuliyojiwekea ‘’ alisema Rais Magufuli.

Wakati huohuo, Rais Magufuli alimpongeza Rais Kiir kwa jitihada zake katika kuhakikisha nchi yake inajiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki haraka ambapo miezi minne baada ya nchi hiyo kupata uhuru iliwasilisha maombi ya kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki na miaka mitano imeweza kuwa mwanachama kamili wa Jumuiya hiyo.

Kwa upande wake, Rais Kiir alieleza kufurahishwa kwake na hatua iliyofikiwa na nchi yake ya kuwa mwanachama kamili wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Aidha, alimshukuru Rais Magufuli na Marais wa Nchi zote wanachama kwa kuiunga mkono nchi yake kwa kauli moja.

Mhe. Kiir aliongeza kuwa uamuzi wa nchi yake wa kujiunga na Jumuiya ni wa dhati na kwamba una nia ya kuimarisha ushirikiano kwa manufaa ya wananchi wa Afrika Mashariki kwa ujumla, ambapo nchi yake imeshaanza kufanyia mabadiliko mifumo mbalimbali kwenye Serikali yake ili kuweza kushiriki kikamilifu katika hatua mbalimbali za mtangamano ikiwemo kuunda Wizara inayoshughulikia masuala ya Afrika Mashariki.

‘’Hatimaye Sudan Kusini imerudi nyumbani. Jumuiya ya Afrika Mashariki ni sehemu sahihi kwa nchi yangu kwani Jumuiya ya Afrika Mashariki ni mtangamano unaoheshimika Afrika na Duniani kwa ujumla’’ alisisitiza Rais Kiir.

Pia, Rais Kiir alitangaza kufunguliwa rasmi kwa Ubalozi wa nchi yake hapa nchini na tayari amemteua Balozi Mariano Deng Ngor kuwa Balozi wa Sudan Kusini nchini Tanzania.

Awali akizungumza kabla ya kusainiwa kwa Mkataba huo, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa na Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga alisema kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki itashirikiana kwa karibu na Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha wananchi wa Sudan Kusini waliothirika na migogoro na kuikimbia nchi yao wanarejea kwa ajili ya kuendeleza nchi yao.

Jamhuri ya Sudan Kusini ilipata uhuru wake tarehe 09 Julai, 2011 na iliwasilisha maombi rasmi ya kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki tarehe 10 Novemba, 2011. 


Aidha, Tangazo la kukubaliwa kuwa Mwanachama wa EAC lilitangazwa na Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Mkutano wa 17 wa Wakuu wa Nchi wa EAC uliofanyika jijini Arusha mwezi Machi 2016. 
Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania Dk. John Pombe Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) akiwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzanua Mhe. Samia Suluhu Hassan katikati na Waziri Mkuu Mh. Majaliwa Kassim Majaliwa  wakimsubiri  Rais wa Jamhuri ya Sudan Kusini Mhe. Salva Kiir Mayardit wakati Rais Kiir alipowasili Ikulu na kupokelewa na kwa ajili ya kutia kusani mkataba wa kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki Leo April 15,2016.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzanua Mhe. Samia Suluhu Hassan, akisalimiana na Rais wa Jamhuri ya Sudan Kusini Mhe. Salva Kiir Mayardit wakati Rais Kiir alipowasili Ikulu na kupokelewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania Dk. John Pombe Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa ajili ya kutia kusani mkataba wa kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki Leo April 15,2016
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzanua Mhe. Samia Suluhu Hassan, akisalimiana na Rais wa Jamhuri ya Sudan Kusini Mhe. Salva Kiir Mayardit wakati Rais Kiir alipowasili Ikulu na kupokelewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania Dk. John Pombe Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa ajili ya kutia kusani mkataba wa kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki Leo April 15,2016, Kushoto ni Waziri Mkuu Mh. Majaliwa Kassim Majaliwa.
Rais wa Jamhuri ya Sudan Kusini Mhe. Salva Kiir Mayardit akikagua gwaride la heshima  wakati Rais Kiir   alipowasili Ikulu leo.
Rais wa Jamhuri ya Sudan Kusini Mhe. Salva Kiir Mayardit wakati Rais Kiir akiwapungia mikono viongozi mbalimbali huku akiongozana na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania Dk. John Pombe Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wakati alipowasili Ikulu

Tamko la Ofisi ya Bunge kuhusu mkataba wa Lugumi

$
0
0

Kumekuwa na taarifa zinazoendelea kupotosha umma na baadhi ya vyombo vya Habari kuwa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ilipokuwa ikitekeleza majukumu yake tarehe 5 Aprili, 2016 ililitaka Jeshi la Polisi kuwasilisha Mkataba ulioingiwa Kati ya Jeshi hilo na Kampuni ya Lugumi Enterprises Ltd kuhusu mradi wa Utambuzi wa Alama za Vidole AFIS (Automated Fingerprint Identification System).

Ofisi ya Bunge inapenda kutoa ufafanuzi kuhusu jambo hili kwamba, taarifa hizo si za kweli na zina lengo la kupotosha umma kutokana na kile kilicho amuliwa na kamati hiyo. 

Ukweli kuhusu jambo hili ni kwamba tarehe 5 Aprili, 2016, kamati hiyo ilikutana na kujadili Taarifa ya Ukaguzi wa hesabu zilizokaguliwa za fungu 28, Jeshi la Polisi kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 30, 2014 ambapo kamati pamoja na mambo mengine ilibaini dosari katika utekelezaji wa mkataba huo.

Kutokana na dosari hizo, kamati iliomba Afisa Masuhuli ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuwasilisha maelezo ya kina kwa maandishi kuhusu utekelezaji wa mradi huo kwa Ofisi ya Katibu wa Bunge ili kamati iweze kuchambua na kujadili maelezo hayo kabla ya kupendekeza kwa Bunge hatua zaidi za kuchukua. 

Kufuatia agizo hilo, kamati ilimwandikia pia Katibu wa Bunge taarifa kuhusu agizo hilo tarehe 12 Aprili, 2016 ili kupatiwa maelezo hayo kutoka kwa Afisa Masuhuli.

Aidha, Ofisi ya Bunge ilimwandikia barua Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Ndani tarehe 12 Aprili, 2016 kuwasilsha Taarifa ya utekelezaji wa maagizo ya Kamati Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) iliyotokana na kikao hicho cha tarehe 5 Aprili 2016 kabla ya tarehe 18 Aprili, 2018 kama ilivyoshauriwa na kamati . 

Hivyo ni vyema Umma ukafahamu kuwa kilichoombwa na Kamati ni Maelezo ya utekelezaji wa Mkataba huo na sio Mkataba kama inavyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya Habari ambapo Ofisi ya Bunge iliomba maelezo hayo yawasilishwe kabla ya tarehe 18 Aprili, 2016.

Imetolewa na:
Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano Ofisi ya Bunge
DAR ES SALAAM 15 Aprili, 2016.

Mhasibu Wa Halmashauri Ya Singida Afikishwa Mahakamani Akituhumiwa Kupokea Milioni 29 za Watumishi HEWA

$
0
0

MHASIBU wa Halmashauri ya wilaya ya Singida, Imani Abduli Nyamangaro (44) amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida akikabiliwa na tuhuma za mashitaka 57 ya wizi wa mishahara hewa yenye jumla ya shilingi 29,418,642/=.

Mapema Mwendesha Mashtaka,Wakili wa serikali, Michael Lucas Ng’hoboko alidai kwamba kati ya april , 29  mwaka 2013 na machi, 27 mwaka 2014 mshitakiwa Nyamangaro ambaye ni mkazi wa Mtaa wa Utemini, mjini Singida kwa makusudi aliiba mishahara hewa ya zaidi ya shilingi milioni 29.4 huku akijua wazi kwamba kitendo hicho ni kinyume na sheria.

Mbele ya Hakimu wa Mahakama hiyo, Joyce Minde, Ng’hoboko alidai kwamba mshitakiwa huyo alikuwa akijipatia mishahara hiyo ambayo wahusika waliisha staahafu kazi kwa kipindi cha muda mrefu, kupitia akaunti yake no. 50802503513 iliyopo katika Benki ya NMB Tawi la Singida.

Hata hivyo mshitakiwa Nyamangaro alikana kutenda makosa hayo  yote 57 na hivyo kesi yake imeahirishwa hadi apr, 27 mwaka huu itakapotajwa tena.

Hakimu wa Mahakama hiyo,Minde alisema dhamana ya mshitakiwa ipo wazi na kwamba atapaswa kutoa fedha taslimu shilingi 14,709,321/= Mahakamani au awe na mali isiyohamishika yenye thamani inayolingana na kiasi hicho cha fedha.

Hata hivyo hadi Mwandishi wa Habari hizi anaondoka katika Mahakama  hiyo,mshitakiwa alikuwa bado hajatekeleza masharti ya dhamana hiyo.
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live




Latest Images