Quantcast
Channel: MPEKUZI
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live

Rais Magufuli Apiga Simu Clouds TV Na Kutaja Mshahara Wake Anaolipwa....Asema Akitoka Likizo Ataonyesha Nyaraka za Malipo

0
0

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt. John Pombe Magufuli amempigia simu mtangazaji wa kipindi cha ‪Clouds360‬ cha ‪‎CloudsTv‬, Hudson Kamoga baada ya kusikia watu wanazungumzia kuhusu mshahara wa Rais.

Rais amesema mshahara alioukuta na ambao analipwa  ni milioni 9 na laki 5 (9,500,000)   na  wala  sio milioni 30  kama  wanavyodai wapinzani. Amelazimika kuyasema hayo wakati wa uchambuzi wa magazeti kupitia Clouds360.

Ameahidi akirudi kutoka likizo yupo tayari kuonyesha nyaraka za malipo ya mshahara wake.

Gazeti  la  Nipashe toleo  la leo lilikuwa na habari  iliyowanukuu Tundu Lissu  na  Zitto Kabwe wakitaka Rais Magufuli ataje Mshahara wake na aweke wazi kama anakatwa kodi ili kuondoa sintofahamu iliyopo .
 
Hivi karibuni, Dk. Magufuli ameahidi kupunguza mishahara ya baadhi ya vigogo inayozidi shilingi milioni 15 ili mtumishi anayepata mshahara mkubwa zaidi usizidi kiasi hicho.


Fidia yakwamisha upanuzi wa kiwanja cha ndege Kigoma

0
0

Kiasi cha Sh milioni 473 kinahitajika ili kulipa fidia ya ziada kwa wananchi wanaopaswa kuondoka ili kupisha upanuzi wa uwanja wa ndege wa Kigoma. 

Hatua hiyo ilikuja baada ya wananchi kuweka pingamizi mahakamani wakidai malipo fidia waliyolipwa awali ni madogo.

Akitoa taarifa kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, Meneja wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) mkoani Kigoma, Mohammed Suleiman alisema hatua ya kuongeza fedha hizo za ziada inalenga kumaliza malalamiko ya fidia yanayoukabili mradi huo.

Suleiman alisema katika mpango huo wanatarajia kutoa nyongeza ya Sh 500,000 kwa kila mwananchi anayetakiwa kupisha upanuzi wa uwanja huo, hatua itakayowafanya wananchi waondoe kesi mahakamani na hivyo ujenzi kuanza.

Alisema kiasi cha Sh milioni 650 zilishalipwa kama fidia kwa nyumba, viwanja, mashamba na mazao na kiasi cha Sh milioni 645 zililipwa kama fidia kwa makaburi 2,786. 

Meneja huyo wa TAA alisema kuwa utekelezaji wa mradi wa upanuzi wa njia ya kurukia ndege utawezesha njia hiyo kufikia mita 3,100 na hivyo kuwezesha ndege kubwa ikiwemo Boing 737 kutua na kwamba kwa sasa awamu ya kwanza ya mradi huo imewezesha njia hiyo kufikia mita 1800.

Alisema mradi wa jengo la kisasa la abiria na mnara wa kuongozea ndege unatarajiwa kuanza mwezi Julai mwaka huu na kwamba michakato ya utekelezaji wa mradi huo inaendelea kwa hatua mbalimbali.

Akizungumzia taarifa hiyo, Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, alieleza kusikitishwa kwake na tabia ya baadhi ya wananchi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji kupenda kuzuia miradi ya maendeleo mahakamani kwa kulalamikia fidia.

Wamiliki waliohodhi migodi ya tanzanite kunyang’anywa leseni

0
0

Serikali  imeagiza wamiliki wa migodi ya madini ya tanzanite ambao migodi yao imesimama kwa muda mrefu bila uzalishaji kwa madai ya  kutokuwa na madini, warudishe leseni zao wizarani mara moja.

Kauli hiyo imetolewa mwishoni mwa wiki na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Prosefa James Mdoe, mara baada ya kukagua migodi ya tanzanite ya Kitalu B,D na kitalu C kinachomilikiwa na kampuni ya Tanzanite One, akiwa na wajumbe wa Kamati ya Bunge inayosimamia shughuli za Wizara ya Nishati na Madini.

Profesa Mdoe alisema Sheria ya Madini ya 2010 iko wazi kwa wamiliki wa migodi ambao hawajazalisha kwa muda mrefu, kwa kuwa inataka warudishe leseni ili wapatiwe eneo lingine lenye madini.

 Amesema kuendelea kusimama au kuchimba na kuingia mgodi mwingine ni kinyume na sheria na hatua kali zitachukuliwa.

Katibu Mkuu huyo alisema kuwa migogoro mingi ya wachimbaji wa tanzanite, ni ya ‘mitobozano’ kwa maana ya wachimbaji kuingia katika maeneo ya wenzao na watu kutofuata sheria zilizowekwa na Serikali kwa sasa haitavumilia.

Alisisitiza kila mchimbaji wa madini ya tanzanite wilayani Simanjiro, kuheshimu sheria ya madini iliyowekwa na Serikali badala ya kufanya kazi ya uchimbaji kwa kufuata sheria ambazo si rasmi.

‘’Mgodi wako ukimaliza uzalishaji nirudishie leseni yangu, lakini kuchimba kwa kwenda katika mgodi wa mchimbaji mwingine, ni kinyume na sheria,’’ alisema.

 Naye Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mbunge wa Chumbuni Zanzibar, Ussi Salumu Pondeza, alisema wataishauri Serikali kushughulikia tatizo la mtobozano mapema kabla ya mchimbaji kuingia gharama kubwa.

Alisema pia wamejifunza mambo mengi katika ziara hiyo na wana mengi ya kuishauri Serikali ili madini hayo yanufaishe nchi ya Tanzania na si nchi nyingine.

Hali si Nzuri Bandari ya Dar es Salaam.....Mizigo Yapungua Kwa Asilimia 50

0
0
Hali si shwari kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) baada ya wafanyabiashara wa mataifa yanayotumia Bandari ya Dar es Salaam kutafuta sehemu nyingine kiasi cha kusababisha kiwango cha mizigo kupungua kwa asilimia 50.

Bandari hiyo, ambayo ni maarufu kwa usafirishaji wa mizigo inayokwenda na kutoka nchi za Malawi, Congo, Uganda, Burundi na Rwanda, imekumbwa na kadhia hiyo baada ya wafanyabiashara wa nchi hizo kuamua kutumia bandari nyingine za Beira, Msumbiji na Durban ya Afrika Kusini.

Kaimu Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam, Hebel Mhanga alisema hali ya biashara kwa sasa si nzuri kwa kuwa mtiririko wa shehena za mizigo umepungua ikilinganishwa na miaka iliyopita.

“Miaka yote shehena ya mizigo bandarini ilikuwa ikiongezeka kwa kati ya asilimia 10 mpaka 11, lakini sasa imeshuka mpaka kufikia asilimia 50,” alisema Mhanga kwenye semnina ya wahariri iliyofanyika ofisi za bandari hiyo jana.

Mhanga alitoa mfano wa shehena iliyokuwa ikisafirishwa na wafanyabiashara kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), kuwa imepungua kwa asilimia 50 huku mizigo ya wafanyabiashara wa Zambia ikipungua kwa asilimia 46.

Alitaja sababu zilizochangia kuporomoka kwa biashara hiyo kuwa ni pamoja na wafanyabiashara hao kuanza kukatwa kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).

Alisema tangu sheria ya ulipaji wa VAT ilipopitishwa mwaka jana, wasafirishaji wote wanaotumia bandari hata wale ambao mizigo yao inasafirishwa kwenda nchi jirani, wanalazimika kulipia kodi hiyo.

Sababu nyingine ni utaratibu wa himaya moja ya forodha kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. 

Alisema baada ya kuona mfumo huo unafaa, Tanzania iliamua kuutumia kwa nchi nyingine ambazo hazipo katika jumuiya hiyo.

Alisema katika utaratibu huo, nchi zote zinakuwa na mwakilishi katika ofisi za TPA na masuala ya kodi na mizigo yote inalipiwa ushuru nchini kabla ya kusafirishwa kwenda nchi zao.

“Hili limekuwa mwiba kwa wenzetu wa DRC, kwani nchini mwao mfumo wa ukusanyaji kodi unatoa mianya ya ukwepaji, kwa hiyo kwa kutumia njia hii ni wazi kuwa kila mzigo utalipiwa hapa nchini kabla haujasafirishwa, jambo wanaloona linalowaongezea gharama za uendeshaji,” alisema.

Mhanga alisema kutokana na hali hiyo, kwa sasa wafanyabiashara hao wameamua kutumia bandari za nchi nyingine kupitisha mizigo yao, akizitaja kuwa ni Durban na Beira.

Sababu nyingine aliyoitaja ni kushuka kwa thamani ya Randi dhidi ya Dola ya Marekani, kitu alichosema kinawafanya wasafirishaji kuona kwamba wakipitishia mizigo yao Dar es Salaam wanatumia fedha nyingi kuliko Durban.

“Ulipaji wetu unawalazimisha wafanyabiashara watumie Dola wakati wao wanatumia Randi ya Afrika Kusini na sasa imeshuka, hivyo njia rahisi kwao ni kutumia Bandari ya Durban kwa kuwa watapunguza gharama za usafirishaji,” alisema.

Alisema sababu ya nne ni kukamilika kwa ujenzi wa njia ya reli kutoka Malawi hadi Beira.

Alisema usafirishaji mizigo kwa njia ya reli ni nafuu kwa kuwa unapunguza gharama kwa asilimia 30 na pia hutumia siku chache hivyo wafanyabiashara wengi sasa wanatumia bandari ya Beira badala ya Dar es Salaam. 

 “Kutofanya vizuri kwa reli yetu ni kikwazo kikubwa kwa biashara ya bandari. Mfano hadi Desemba 2015, jumla ya tani 14.8 zilipita bandari yetu, lakini ni asilimia 0.01 pekee ndiyo iliyosafirishwa kwa njia ya reli na asilimia 99.9 ilisafirishwa kwa barabara,” alisema meneja huyo.

Meneja huyo alisema ili kunusuru hali hiyo, busara inahitajika zaidi, ikiwa ni pamoja na kupitia upya sheria hiyo ya VAT.

Alisema kwa upande wao wameshafanya maboresho ili kuvutia wawekezaji kuja nchini, ikiwa ni pamoja na kuimarisha matumizi ya teknolojia tofauti na awali.

Alisema kwa sasa wamezindua mfumo mpya unaojulikana kama ‘Habour View’ unaosaidia kupokea taarifa zote za meli, mizigo na ulipaji hivyo mteja anaweza kulipia kwa njia za benki na simu.

Alisema wamefupisha muda wa kushusha mzigo katika meli hadi kufika siku mbili tofauti na awali ilipokuwa inachukua siku sita.

Alisema kwa upande wa shehena ya magari, mwaka 2010 uwezo ulikuwa ni kushusha magari 200 lakini kwa sasa wana uwezo wa kushusha magari 700.

Awali, Mkurugenzi wa Masoko wa TPA, Fransisca Muhindi alishauri Serikali kuwekeza katika kutangaza bandari hiyo ili kuinusuru.

“Wenzetu hawalali, wanafanya biashara ya ‘door to door market’(nyumba kwa nyumba), wanawekeza kiasi kikubwa. Ni bahati mbaya sana sisi hatuwekezi. Kuna usemi unasema wekeza shilingi ili upate shilingi,” alisema.

Alisema kwa sasa mzigo wa shaba ambao awali ulikuwa asilimia 60 ya mizigo yote bandarini umeshuka hadi kufikia asilimia 15 huku sababu kubwa ikiwa ni reli.

Mtu Mmoja Auawa Kwa Kuchomwa Kisu Jijini Mwanza Kisa Kikiwa ni Wivu wa Mapenzi

0
0

Mtu mmoja amefariki dunia, huku mwingine akijeruhiwa baada ya kuchomwa visu wakati wa ugomvi uliotokana na wivu wa mapenzi wilayani Ilemela mkoani Mwanza.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Justus Kamugisha alimtaja aliyeuawa kuwa ni Makororo Kitota (26) ambaye ni mkazi wa Mtaa wa Iloganzala, alichomwa kisu shingoni na kifuani na kupoteza maisha palepale.

Alisema tukio hilo lilitokea Machi 30, mwaka huu saa nne usiku katika kilabu ya pombe za kienyeji.

Kamugisha alisema mtuhumiwa aliyefanya tukio hilo alikuwa na ugonvi wa muda mrefu na Kitota akimdhania kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mkewe ambaye pia alikuwapo kilabuni hapo wakati wa tukio hilo.

Kwa mujibu wa kamanda huyo, wanandoa hao walikuwa wametengana tangu Agosti 2015 kwa sababu hiyo hiyo kutokana na usaliti katika uhusiano wa kimapenzi.

Aliyejeruhiwa katika tukio hilo ni Nchama Wanda (33), mkazi wa Sabasaba wilayani humo aliyechomwa kisu tumboni na utumbo kutoka nje alipojaribu kuwaamulia wakati wakipigana.

Kamugisha alisema majeruhi huyo amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando kwa matibabu zaidi na kwamba, hali yake siyo nzuri.

Alisema mke wa mtuhumiwa wa mauaji hayo anashikiliwa na polisi baada ya mtuhumiwa na mmiliki wa kilabu hiyo kukimbia kusikojulikana.

Kamanda huyo alisema jeshi hilo linaendelea kuwatafuta watu hao ili kuwafikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Kiwanda cha Mount Meru Millers Chafungwa na Kutozwa Faini ya Milioni 12 Kwa Uharibifu wa Mazingira

0
0

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), limekifunga kiwanda cha Mount Meru Millers Ltd kilichopo wilayani Bunda, mkoani Mara na kukipiga faini ya Sh12 milioni kwa uharibifu wa mazingira kinyume cha Sheria ya Kulinda na Kuhifadhi Mazingira.

Hatua hiyo ya NEMC imekuja baada ya malalamiko  ya muda mrefu  kuhusu kiwanda hicho kutiririsha maji yenye kemikali zenye sumu katika makazi ya watu, vyanzo vya maji na kwenye mashamba ya mpunga.

Mratibu wa NEMC Kanda ya Ziwa, Anna Mdamo alisema uchunguzi uliofanywa na baraza hilo Machi 22, mwaka huu, ulibaini kuwa kiwanda hicho kinaendesha shughuli zake kinyume cha Sheria ya Mazingira ikiwa ni pamoja na kutokutumia mtambo wa kutibu maji kabla ya kuyaachia kuingia mitaani.

Mmoja wa viongozi wa kiwanda hicho aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina alikiri kupokea barua ya kukifunga toka juzi.

Kwa mujibu wa NEMC, kiwanda hicho kinatakiwa kulipa faini ndani ya siku 14, vinginevyo hatua zaidi zitafuata ikiwamo kufikishwa mahakamani.

Mkuu wa Idara ya Mazingira ya Halmashauri ya Mji wa Bunda, Majura Masumbuko aliishukuru NEMC kwa kuchukua hatua dhidi ya kiwanda hicho kilichosababisha mgogoro kati ya mamlaka za Serikali wilayani Bunda.

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Jumapili ya April 3

Vigogo NHC na EWURA Wakana Kulipwa Mhashara wa Milioni 36 kwa Mwezi

0
0

Mabosi  wa mashirika mawili ya Serikali nchini, wanaodaiwa kulipwa mshahara wa Sh milioni 36, wamekanusha madai hayo, huku wakielezea kushangazwa na taarifa hizo wakati hata nusu ya fedha hizo, hawapati.

Akizungumza mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Nehemia Mchechu alisema  halipwi mshahara huo.

Akijibu hoja za wajumbe wa kamati hiyo kuhusu taarifa ya utekelezaji na utendaji wa shirika hilo kwa mwaka 2014/15, Mchechu alisema shirika hilo pamoja na kutekeleza majukumu yake, bado lina changamoto za uhaba wa fedha.

“Katika ujenzi wa nyumba zetu, Serikali haigharamii masuala ya miundombinu kama vile maji, umeme, barabara hilo ni jukumu letu na linatugharimu fedha nyingi. 

“Sasa nashangaa wako watu wanasema mimi nalipwa mshahara mkubwa, sielewi wametoa wapi huo mshahara kwa sababu silipwi mshahara huo, mimi nalipwa chini ya huo walioutaja,” alisema Mchechu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura),Felix Ngamlagosi aliiambia kamati hiyo kwamba mamlaka hiyo ina changamoto nyingi ikiwemo uhaba wa watumishi na maslahi duni. 

Alisema wakati maslahi ya wafanyakazi ni duni, ameshangaa kusikia vyombo vya habari vikisema yeye ni miongoni mwa wakurugenzi wanaolipwa Sh milioni 36 kwa mwezi.

“Jamani hapa tunazungumzia maslahi duni ya watumishi wetu, nashangaa kusikia naambiwa nalipwa milioni 36, mshahara wangu haufiki hata nusu ya hizo fedha,” alisema Ngamlagosi.

 Nyumba nafuu 
Awali wajumbe wa kamati hiyo baada ya kupitia taarifa hiyo ya NHC, waliiomba Serikali kuharakisha kuwepo kwa sera ya nyumba ili kurahisishia mashirika yanayohusika na masuala ya ujenzi wa nyumba kujenga nyumba za bei nafuu kwa wananchi.

“Yapo malalamiko kutoka kwa wananchi kwamba NHC mnauza nyumba kwa bei kubwa, huku mkitoa matangazo kuwa nyumba hizo ni bei nafuu,” alihoji mjumbe wa Kamati hiyo, Mbunge wa Ushetu, Elias Kwandikwa. 

Akijibu hoja hiyo, Mchechu alisema nyumba zinazojengwa na NHC zinauzwa kuanzia Sh milioni 30 hadi 250 kwa fedha taslimu na kwamba mnunuzi atatakiwa kulipa kodi.

Aliongeza kuwa kama mnunuzi hatakuwa na fedha taslimu, benki washirika wanatoa mikopo kwa ajili ya ununuzi wa nyumba hizo, ila wanunuzi watatakiwa kulipa riba za benki husika. 

Baada ya majibu hayo, wajumbe hao walitaka Serikali iangalie jinsi ya kupunguza mzigo kwa shirika hili na ikiwezekana waondolewe kodi ya uingizaji vifaa vya ujenzi ili kusaidia nyumba hizo kuuzwa kwa bei nafuu, kwa lengo la kuwanufaisha wananchi hasa wale wa kima cha chini.

Akizungumzia hoja hizo, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula alisema shirika hilo, linapaswa kuwasiliana na watendaji katika maeneo husika ya ujenzi wa nyumba hizo, ili wawasaidie kubeba gharama ndogondogo.

“Serikali na wizara zinafanya kazi kwa ushirikiano na NHC, na hili la gharama za miundombinu, kila halmashauri nchini ambayo ujenzi wa nyumba hizo unafanywa, inaweza kuangalia jinsi ya kusaidia gharama za miundombinu, ili nyumba hizo ziuzwe kwa bei nafuu zaidi kwa wananchi,” alisema Mabula.

Ndoo Walizobeba Kigogo wa Zamani wa TRA na Miss Tanzania Wakati Wakipelekwa Gerezani Zaibua Utata

0
0
Kitendo cha aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya pamoja na maofisa wawili waandamizi wa zamani wa Benki ya Stanbic, Tawi la Tanzania, Sioi Solomoni na Shose Sinare kubeba ndoo wakati wakitoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuelekea mahabusu, kimezua maswali mengi.

Kitilya na wenzake hao walifikishwa kwenye mahakama hiyo na kusomewa makosa manane likiwamo la kutakatisha fedha kiasi cha Dola milioni sita za Marekani.

Sinare aliyekuwa mrembo wa Tanzania mwaka 1996, anakabiliwa na mashtaka mengine mawili ya kughushi na mengine ya kuwasilisha nyaraka za uongo za Serikali ya Tanzania ilipokopa Dola za Marekani 550 milioni kutoka Benki ya Standard ya Uingereza kati ya mwaka 2012 na 2013.

Mvutano wa kisheria ulioibuka mahakamani hapo juzi ulimfanya Hakimu Elimius Mchauru anayesikiliza kesi hiyo kuamuru washtakiwa wapelekwe mahabusu hadi Aprili 8, mwaka huu atakapotoa uamuzi kama watuhumiwa hao wana haki ya kupewa dhamana au la.

Wakati wakiondoka kwenda kupanda magari tayari kwa kuelekea gerezani, washtakiwa hao walikuwa wamebeba ndoo ndogo za plastiki. Kitilya alionekana akiwa amebeba ndoo moja, Sioi mbili na Sinare moja.

Ndoo hizo zimezua maswali mengi bila majibu ikiwamo sababu ya kuzibeba, muda uliotumika kuziandaa au kama walikwenda nazo mahakamani wakijua watakosa dhamana na kupelekwa mahabusu.

Pia, maswali yameibuka kuwa walikuwa wakienda nazo mahabusu kufanya nini  na je, mahabusi wote huenda na ndoo? Au ni wao tu.

Wakili wa kujitegemea wa kampuni ya uwakili ya Kakamba and Partiners, Mathew Kakamba alisema ameshangaa kuona watuhumiwa wanaelekea mahabusu wakiwa na ndoo.

Alisema hakuna sheria inayoruhusu mtuhumiwa yeyote kwenda na kitu chochote huko na ndiyo maana hufanyiwa upekuzi.

“Ndiyo maana hata mkanda, simu na vifaa vingine wanatakiwa kuviacha mapokezi, sasa sijajua kama hizo ndoo waliruhusiwa kuingia nazo au la,” alisema.

Akizungumzia suala hilo, Ofisa Habari wa Jeshi la Magereza, Lucas Mboje alisema huenda walikuwa wamehifadhia baadhi ya vitu vyao ambavyo wangekwenda navyo mahabusu.

“Labda wamebeba kwa ajili ya kuogea au kuhifadhia baadhi ya vitu vyao lakini kwa Magereza za Dar es Salaam hakuna tatizo la maji,” alisema Mboje.

Rais Magufuli na Waziri Mkuu Mstaafu wa Kenya Raila Odinga Washiriki Misa Takatifu Pamoja Kwenye Kanisa Katoliki Chato

0
0

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ambaye yupo mapumzikoni nyumbani kwake Lubambangwe katika kijijini cha Mlimani, Wilaya ya Chato Mkoani Geita, kwa mara ya kwanza tangu achaguliwe kuwa Rais, ameungana na waumini wenzake wa Kanisa la Bikira Maria Parokia ya Chato, kusali ibada ya Jumapili ya Pili ya Pasaka ambapo pamoja na mambo mengine amewahusia watanzania wote  kuendelea kuliombea Taifa ili liendelee kuwa na amani.

"Niwaombe watanzania wote tuendelee kushirikiana na kushikamana, kwa umoja wetu na siku zote tumtangilize Mungu mbele. 

"Wakati tunaadhimisha wiki moja baada ya kufufuka kwa Bwana wetu Yesu Kristo, Yesu Kristo alikufa kwa sababu ya dhambi zetu, sisi wote tujitahidi kufuata matendo ya Yesu Kristo ya kusameheana, kupendana, kushirikiana na tusibaguane" Amebainisha Rais Magufuli

Pamoja na Rais Magufuli na Mkewe Mama Janeth Magufuli, ibada hiyo imehudhuriwa na Waziri Mkuu Mstaafu wa Kenya Mheshimiwa Raila Amoro Odinga na Mkewe Mama Ida Odinga, ambao ni familia rafiki wa Rais Magufuli, waliowasili hapa Chato jana jioni Tarehe 02 April, 2016 kwa mapumziko wakitokea Nairobi, Kenya.

Katika salamu zake kwa waumini wa Parokia ya Chato, Mheshimiwa Odinga amewashukuru watanzania kwa uhusiano mzuri walionao na wakenya, huku akitoa mfano wa jinsi Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alivyojitoa kupigania uhuru wa mataifa mengi ya Afrika ikiwemo Kenya.

Mheshimiwa Odinga ametoa mfano wake mwenyewe kuwa Mwalimu Nyerere alimpatia pasi ya kusafiria ya Tanzania, aliyoitumia kwa miaka mitatu kwa ajili ya kwenda kusoma nje ya nchi, baada ya utawala wa Kikoloni wa Kenya kukataa kumpa pasi hiyo.

Kuhusu urafiki wake na Rais Magufuli, Mheshimiwa Odinga amesema urafiki huo ulianza tangu Rais Magufuli alipoteuliwa kuwa Waziri wa Ujenzi na yeye kuwa Waziri mwenye dhamana ya ujenzi wa Kenya, ambapo mara kadhaa walibadilishana uzoefu na kushirikiana katika mipango ya miradi ya ujenzi wa barabara, na kwa umuhimu huo ametoa wito kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kuendeleza ushirikiano na mshikamano ulioasisiwa na waasisi Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wa Tanzania, Jalamogi Odinga wa Kenya na Milton Obote wa Uganda.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Chato
03 April, 2016

Rais Magufuli Atoa shilingi Milioni 10 nyumbani kwao Geita leo Kuchangia Upanuzi wa Kanisa

0
0

Rais Magufuli ametoa mchango wa shilingi milioni 10 kwa kanisa la bikira Maria Parokia ya Chato Mkoani Geita kwa ajili kuchagia upanuzi wa kanisa hilo ambapo fedha hizo zimekabidhiwa na kaimu mnikulu Ngusa Samike katika misa ya pili ya ibada ya Jumapili ya pili ya Pasaka, iliyofanyika kanisani hapo leo tarehe 03 April, 2016.

Kabla ya misa hiyo ya pili Rais Magufuli na mkewe Mama Janeth Magufuli wakiwa pamoja na Waziri mkuu mstaafu wa Kenya Raila Odinga na Mkewe Mama Ida Odinga, walisali misa ya kwanza ambapo Rais Magufuli aliahidi kuchangia shilingi milioni 10 kwa ajili ya upanuzi wa kanisa hilo ambao unaendelea.

Taarifa iliyotolewa na Ikulu imesema katika misa hiyo Paroko wa Parokia ya Chato, Padre Henry Mulinganisa alieleza kuwa kanisa hilo linatarajia kuadhimisha miaka 50  tangu kuanzishwa kwake baadaye mwaka huu, na kwamba maadhimisho hayo yanakwenda sambamba na upanuzi wa kanisa ambao unachangiwa na waumini wenyewe.

Padre Mulinganisa amemshukuru Rais Magufuli kwa mchango huo na amemuahidi kuwa utatumika vizuri ili uendeleze upanuzi wa kanisa hilo pamoja na michango ya waumini wengine.

Simbachawene awataka wadau kumaliza changamoto mradi wa Mabasi yaendayo haraka

0
0

Wakala wa mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) na wadau wake wameagizwa kuzimaliza changamoto zinazochelewesha kuanza kwa mradi huo ili huduma ya usafiri iweze kuanza haraka iwezekanavyo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Bw. George Simbachawene alitoa agizo hilo mwishoni mwa juma katika kikao chake na uongozi wa wakala pamoja na  wadau wake.
 
“Kuna baadhi ya changamoto ndogondogo zimebaki...nimetaka wazimalize haraka ili mabasi yaanze kutoa huduma,” Bw. Simbachawene aliwaambia waandishi wa habari mara baada ya kikao hicho. Mradi huo uliosubiriwa kwa muda mrefu unatarajiwa kuanza mwezi huu wa Nne.
 
Aliwataja baadhi ya wadau wanaotakiwa kufanya kazi na wakala huo kuhakikisha kuwa mradi unaanza kuwa ni Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Wakala wa Usafiri wa Majini na Nchi kavu (SUMATRA), Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Wakala wa Serikali  Mtandao (EGA), Msajili wa Hazina, UDA-RT na MAXCOM.
 
Changamoto zinazotakiwa kutatuliwa kwa haraka ni pamoja na kukwama kwa baadhi ya vifaa vya mradi kutokana na kutolipiwa katika Mamlaka ya mapato (TRA), kuweka mifumo ya nauli na kadi zake, umeme, kujenga uzio katika vituo, kuongeza ulinzi na ofisi ya kuongozea mabasi.
 
Aliwataka uongozi wa wakala wa DART kumpatia ripoti ya maendeleo kila baada ya siku mbili kwake ili na yeye aweze kupeleka ripoti kwa Waziri Mkuu kila wiki.
 
“Tutaendelea kuwa na vikao vya kila siku, siku mbili na kila wiki hadi hapo huduma hii itakapoanza kufanya kazi,” alisema.
 
Tayari mabasi mawili yameshaanza kufanya majaribio na idadi inatarajia kuongezeka hivi karibuni.
 
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa DART, Mhandisi  Ronald Lwakatare alisema kikao hicho kilikuwa na mafanikio na ni njia nzuri ya kuharakisha yale yanayotakiwa kukamilishwa haraka ili mradi huo uanze.
 
“Tumejipanga na wadau wote wameitikia wito, tunataraji mradi utaanza kutoa huduma kwa wananchi haraka,”alisema Bw. Lwakatare.
 
Aliwataka wakazi wa jiji kuendelea kuwa watulivu na kuvuta subira kwani mradi wao umeiva na wataanza kuona matunda yake hivi karibuni kwa kuwa yaliyobaki ni mambo madogomadogo.
 
“Pia tunawaomba waendelee kutoa ushirikiano wa kuilinda miundombinu, kwenye vituo kuna vitu vingi vinafungwa, wasiwe chanzo cha uharibifu,” alisema.
 
Alisisitiza kuwa watu wasiwe chanzo cha hujuma kwani kufanya hivyo ni kuhujumu taifa lao wenyewe.

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga amkamua jipu Mhandisi wa manispaa....Amsweka Rumande huku Mkurugenzi wake Akishuhudia

0
0
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro amemsweka rumande Muhandisi wa halmashauri ya manispaa ya Shinyanga Simoni Ngagani, baada ya kupuuza agizo lake la kufanya maandalizi mapema ya kununua kokoto na Saruji kwa ajili ya kusimika mapipa 50 ya kutunzia uchafu kwenye mitaa mbalimbali katika manispaa ya Shinyanga ikiwemo eneo la kituo cha mabasi yaendayo wilayani.

Tukio hilo limetokea juzi asubuhi mjini Shinyanga wakati mkuu huyo wa wilaya akiwa na msafara wake alipowasili katika eneo la stendi ya mabasi yaendayo wilayani kwa lengo la kufanya uzinduzi wa kusimikwa kwa mapipa hayo na kukuta maandalizi hayajakamilika.

Matiro alimuagiza Mhandisi huyo kufanya maandalizi hayo mapema mbele ya mkurugenzi wake wa manispaa ya Shinyanga Kalinjuna Lewis, kuwa ataandaa vifaa hivyo majira ya saa moja asubuhi ili zoezi la  kusimika mapipa hayo likamilike haraka, na baada ya hapo wafanye usafi wa mazingira lakini agizo hilo lilipuuzwa na mhandisi huyo .

Mkuu huyo alipomhoji mhandisi kwanini alipuuzia agizo lake la kufanya maandalizi mapema, mhandisi huyo alisema sababu iliyomkwamisha ni kukosekana kwa pesa za kununua kokoto na saruji kwani mvua kubwa ilinyesha na kushindwa kwenda benki, na alivyoamka asubuhi ndipo atakafuta dhana hizo.

Hata hivyo mkuu huyo hakuridhika na majibu hayo ndipo DC alipochukua uamuzi ya kumsweka rumande kwa kumuagiza mkuu wa kituo cha polisi wilaya ya Shinyanga kumkamata na kumuweka ndani mhandisi huyo wa ujenzi manispaa hiyo Samson Ngagani kwa kosa la kuchelewesha maandalizi ya vifaa vya ujenzi vilivyopangwa kutumika kusimika mapipa ya taka.

“Haiwezekani tukubaliane tuamke mapema ili tufanye kazi hii haraka na pia tuingie Mitaani kufanya usafi, ambapo mimi nimeamka saa 11 nikajiandaa harafu wewe una kuja saa mbili tena bila ya kufanya maandalizi yeyote hii ni kunidharau, hivyo naagiza OCD mkamate akakae Rumande kwanza ili liwe fundisho kwa wengine” ,alisema Matiro.

Katika uzinduzi huo Matiro alisema mapipa hayo ya taka ambayo idadi yake ni zaidi ya 50 yatawekwa katika maeneo mbali mbali ya manispaa ya Shinyanga na wananchi wanatakiwa kuyalinda. 

Awali akiongea katika uzinduzi huo, mkurugenzi wa manispaa ya Shinyanga Lewis Kalinjuna alisema mapipa hayo yamepatikana kutokana na wadau mbali mbali kujitolea kuchangia baada ya kuhamasishwa na mkuu huyo wa wilaya ambapo pipa moja limegharimu shilingi elfu 90.

Naye afisa afya wa manispaa ya shinyanga Elly Nakuzelwa alisema lengo la kuweka mapipa hayo ya taka ni kuhakikisha manispaa ya Shinyanga inakuwa katika hali ya usafi ili kuondoa magonjwa ya miripuko yanayosababishwa na uchafu ikiwemo kipindupindu. 
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akimhoji Mhandisi wa ujenzi wa manispaa ya Shinyanga Simon Ngagani (katikati mwenye kaunda suti)kwa kupuunza agizo lake la kufanya maandalizi mapema ya kununua vifaa vya ujenzi vya kusimikia Mapipa ya uchafu 50 katika mitaa mbalimbali ya Mji wa Shinyanga ,na mwenye traksuti kushoto ni Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Kalinjuna Lewis akishuhudia Mtumishi wake akikamuliwa Jipu na hatimaye kuswekwa rumande kwa kumpuuza DC huyo

Mabenki sasa kupata Taarifa za wadaiwa wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB)

0
0
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) mwishoni mwa wiki imesaini mkataba na Kampuni ya CreditInfo Tanzania Ltd utakaowezesha taarifa za wadaiwa wa mikopo ya elimu ya juu kufikishwa katika Kitengo Uratibu za Taarifa za Mikopo (Credit Reference Bureau) kilichopo katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Kampuni ya CreditInfo Ltd ina leseni iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania kwa ajili ya kufanya kazi hiyo.

Hivyo basi, mnufaika wa mikopo ya elimu ya juu ambaye ataomba mkopo kutoka kwenye taasisi yoyote ya kifedha hapa nchini, taasisi hiyo itakuwa na uwezo wa kuhakiki kama mwombaji huyo ni munufaika wa mkopo wa elimu ya juu na ikiwa ana nidhamu ya kurejesha mikopo.

Kwa mujibu wa mkataba huo, HESLB itawasilisha orodha ya wadaiwa wa mikopo ya elimu ya juu kwa kampuni ya CreditInfo ambayo itahakikisha taarifa za wakopaji zinapatikana kwa taasisi zote za kifedha, yakiwemo mabenki, ili taasisi hizo zijiridhishe kabla ya kutoa mikopo mipya kwa wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu.

“HESLB ina furaha kufanya kazi na CreditInfo kama mdau mpya. Tunawasihi wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu waanze kulipa madeni yao ili wawe na hadhi ya kukopesheka na taasisi za kifedha,” alisema kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Bw. Jerry Sabi wakati wa hafla fupi ya kutia saini mkataba huo katika ofisi za HESLB jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
 
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa CreditInfo Tanzania Ltd Bw. Davith Kahwa amesema lengo la kampuni yake ni kuhakikisha fursa za ukopaji zinazongezeka na wakopaji wanakuwa na nidhamu kwa mikopo waliyopata.

“Wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu ambao wamekuwa wakilipa watapata fursa ya kipekee ya kujadiliana na taasisi za kifedha kuhusu viwango vya riba kwa sababu ya nidhamu wanayoionyesha kwa mikopo yao,” alisema Bw. Kahwa katika hafla hiyo iliyohudhuriwa pia na Meneja wa CreditInfo Tanzania Bw. Van Reynders.

”Tumedhamiria kuiunga mkono HESLB katika kutekeleza majukumu yake hususan yale ya ukusanyaji mikopo iliyoiva,” aliongeza Mtendaji Mkuu huyo wa CreditInfo Tanzania Ltd.

HESLB ni taasisi ya Serikali iliyoanzishwa mwaka 2004 na kuanza kazi rasmi Julai 2005 ili kutoa mikopo kwa watanzania wahitaji na pia kukusanya mikopo iliyoiva ambayo imekuwa ikitolewa na Serikali tangu mwaka 1994.

Hadi sasa, zaidi ya Tshs 2.1 trilioni zimetolewa kwa watanzania na, kati ya hizo, Tshs 258 bilioni zimeiva na hivyo kutakiwa kukusanywa kutoka kwa wanufaika. 

Kiasi kilichobaki kinajumuisha fedha walizopewa wanafunzi ambao bado wanaendelea na masomo na ambao muda wa kuanza kuwadai (miezi 12 baada ya kumaliza masomo) haujafika.

CreditInfo Tanzania Ltd ni sehemu ya Kampuni ya Kimataifa inayofanya kazi kwenye nchi zaidi ya 20 duniai na inayojishughulisha na usimamizi wa taarifa za mikopo. Ilisajiliwa na Benki Kuu ya Tanzania mwaka 2013.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) Bw. Jerry Sabi (kushoto) na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya CreditInfo Tanzania Ltd Bw. Davith Kahwa wakisaini mkataba ambao utaiziwezesha taasisi za kifedha zinazotoa mikopo nchini kuhakiki taarifa za waombaji mikopo, ambao ni wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu, kabla ya kuwapa mikopo mipya. Wengine ni Bw. Frimat Tarimo, Mwanasheria wa HESLB na Bw. Van Reynders, Meneja wa CreditInfo Tanzania. (Picha: HESLB).

Silaha ya kivita SMG na Magazine 2 zenye risasi 21 Yakamatwa ndani ya basi la Nyahunge Ikisafirishwa

0
0

Polisi  mkoani Morogoro inamshikilia Juma George (29) mkazi wa Shinyanga, kwa kukutwa na silaha ya kivita aina ya SMG iliyofutwa namba zake za usajili, magazini mbili, risasi 21 pamoja na panga vikiwa vimehifadhiwa ndani ya begi lake la nguo.

Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei, alisema mtuhumiwa huyo ambaye ni dereva alikamatwa Machi 30, mwaka huu saa mbili usiku maeneo ya stendi kuu ya mabasi ya Msamvu, mjini Morogoro.

Kamanda Matei alisema, askari wakiwa doria katika eneo hilo walipata taarifa kutoka kwa raia mwema kuwa kwenye basi lenye namba za usajili T.141 DEE aina ya Yutong mali ya Kampuni ya Nyahunge likitokea Shinyanga kwenda Morogoro kuna  abiria mmoja amehifadhi silaha.

Alisema baada ya askari kupata taarifa walifika eneo la stendi ya Msamvu na walifanikiwa kumkamata mtu huyo. Ilielezwa kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa akitokea mkoani Shinyanga akielekea Tarafa ya Mngeta, wilaya ya Kilombero.

Kamanda wa Polisi Matei alisema, uchunguzi bado unaendelea na utakapokamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kujibu shitaka linalomkabili.

Katika tukio jingine, Ester Abel (43) mkazi wa Mbumi B Tarafa ya Kilosa, wilayani Kilosa, mkoani Morogoro anashikiliwa na Polisi kwa kukutwa na dawa za kulevya zinazodhaniwa kuwa ni kokeni kete 780 , kilogramu mbili za bangi na misokoto 25 iliyohifadhiwa kwenye mfuko wa nailoni.

Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Morogoro, Matei alisema kuwa mwanamke huyo alikamatwa Machi 30, mwaka huu saa 2:15 usiku katika eneo la Mbumi B , tarafa ya Kilosa Mjini, wilayani humo, mkoani Morogoro .

Kamanda wa Polisi Matei alisema, inadaiwa kuwa mtuhumiwa huyo ni muuzaji wa dawa za kulevya na kwamba uchunguzi unaendelea na atafikishwa mahakamani mara moja baada ya kukamilika kwake.

Kaya 40 Zakosa Makazi baada ya nyumba zao kubomolewa na Mafuriko ya Mvua

0
0

Mvua  kubwa iliyonyesha usiku wa kuamkia juzi imeleta athari kubwa katika Kijiji cha Chenene Kata ya Haneti Tarafa ya Itiso, Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma na kukosesha makazi zaidi ya kaya 40.

Akizungumza jana, Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Farida Mgomi alisema nyumba nyingi zilizobomoka ni zile zilizojengwa kwa matofali ya udongo. Mgomi alisema athari hiyo inaweza kuongezeka kutokana na nyumba kujaa maji na zinaposhindwa kuhimili hudondoka.

“Nyumba nyingi zilijaa maji, kwa hiyo hata chakula, magodoro, nguo vyote vimeharibika,” alisema.

Mgomi alisema tathmini ya awali tayari imefanyika. Na hakuna mtu aliyefariki dunia kufuatia maafa hayo.

“Waathirika wote ambao nyumba zao zimeanguka tayari wamepata sehemu za kujihifadhi kwa msaada mkubwa majirani na kutoka viongozi wa Serikali ngazi ya Kijiji, Kata, Tarafa na Wilaya,” alisema mkuu wa wilaya.

Alisema Kamati ya Maafa ya Wilaya tayari imechukua na inaendelea kuchukua hatua za haraka,kuona namna ya kusaidia familia zilizoathiriwa na maafa hayo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.

Pia alisema hata baadhi ya mashamba (mazao) yamesombwa na maji.

“Baadhi ya wananchi wamepoteza mali zao hifadhi za chakula katika kaya zao, mabati, vyombo vya ndani na mali nyingine za namna hiyo,” alisema.

Naye Ofisa Tarafa wa Itiso, Remidius Emmanuel alisema mvua hiyo imeacha kaya zikiwa hazina makazi.

“Kaya zaidi ya 40 zimeathirika, nyumba nyingi zilizodondoka ni zile zilizojengwa kwa matofali ya udongo,” alisema Emmanuel na kuongeza kuwa nyumba nyingi zilibomoka kutokana na kujaa maji kutoka milimani. 

Pia ujenzi wa barabara ya Kondoa hadi Babati umeonesha kuathiri miundombinu kwani madaraja yaliyojengwa ni madogo yanashindwa kuhimili wingi wa maji kutoka milimani 

“Katika eneo la Chenene ujenzi wa barabara unaonekana kuleta athari kwa makazi ya wananchi kwani madaraja ni madogo, maji yanapofika kwenye barabara yanakosa mwelekeo na kurudi kwenye makazi ya watu hali hiyo ikapelekea nyumba kubomoka,” alisema Ofisa Tarafa huyo.

“Nimetembelea maeneo yote yaliyokumbwa na maafa hayo. Nimekutana na kuzungumza na waathirika wote,” aliongeza.

Watumishi Hewa 14 Kufikishwa Mahakamani

0
0

Halmashauri ya Wilaya ya Muheza mkoani Tanga inatarajia kuwafikisha mahakamani watumishi hewa  14

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Adrian Jungu aliwaambia waandishi wa habari ofisini kwake juzi kuhusiana na hatua iliyochukua baada ya kubainika kuwa halmashauri yake ina watumishi hao hewa.

Jungu alisema mwanasheria wa halmashauri hiyo anaandaa utaratibu wa kuwafikisha mahakamani watumishi hao ambao walikuwa wakipokea mishahara wakati hawapo katika vituo vyao vya kazi.

Alisema watumishi hao ni walimu na hakukuwa na taarifa zozote za sababu za kutokuwapo kwao katika vituo vyao vya kazi.

“Nitawachukulia pia hatua kali wakuu wa idara ambao watabainika walikuwa na watumishi ambao hawakuwa katika vituo vyao vya kazi bila taarifa,” alisema.

Alisema adhabu hiyo itawakumba pia walimu wakuu wa shule kwa kosa la kushindwa kuripoti utoro wa walimu hao kwenye idara husika.

Mkurugenzi huyo aliahidi kuendeleza kazi ya uhakiki watumishi kila baada ya miezi sita ili kukomesha tabia hiyo.

Aliyekuwa Mwenyekiti Chadema Mkoa wa Mwanza Ajivua Uanachama

0
0

Aliyekuwa Mweyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Mwanza, Adrian Tizeba ametangaza kujivua uanchama na kuachana na siasa.

Tizeba aliyesimamishwa uongozi na Baraza la Uongozi la Chadema tangu Mei 4, mwaka jana, alisema hatajiunga na chama chochote cha siasa.

Kwa uamuzi huo, Tizeba amepoteza nyadhifa zake zote ikiwamo ya uenyekiti wa Baraza la uongozi la mkoa na ujumbe wa Baraza la Uongozi Kanda ya Ziwa.

Mei 5, mwaka jana, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, wakati huo, Dk Willibrod Slaa, alimuandikia barua Tizeba yenye Kumb Na C/HO/ADM/KK/08 ,kumsimamisha uongozi wa chama hicho.

Akizungumzia uamuzi wa kiongozi huyo kujivua uanachama na kuachana na siasa, Mratibu wa Chadema Kanda ya Ziwa, Renatus Bujiku alisema chama hicho kimepokea kwa mshtuko taarifa hizo kwa sababu bado suala lake lilikuwa linashughulikiwa.

“Utaratibu wa chama ulikuwa unaendelea kushughulikia suala lake, nadhani kachukua uamuzi wa haraka,” alisema Bujiku.

Tibaijuka Kutanzini Tena Sakata la Escrow.....Bodi ya Rufani ya Kodi Tanzania (TRAB) Yamuamuru Kulipa Kodi ya Shilingi Milioni 586

0
0

Mbunge wa Muleba Kusini (CCM), Profesa Anna Tibaijuka amesema yupo tayari kulipa kodi ya mapato ya Sh586 milioni iwapo Mahakama itaamuru hivyo.

Kodi hiyo inatokana na Sh1.617 bilioni alizopewa  na mfanyabiashara maarufu nchini, James Rugemalira  ambazo zilidaiwa kuchotwa katika akaunti ya Tegeta Escrow.

Profesa Tibaijuka aliyasema hayo jana baada ya taarifa kwamba Bodi ya Rufani ya Kodi Tanzania (TRAB), imeagiza utekelezaji wa suala hilo ili kutimiza matakwa ya sheria kuhusu mapato nchini.

“Ni kweli ninadaiwa kodi ya Sh586 milioni, ila nimeenda mahakamani kutaka ufafanuzi kama ni halali kufanya hivyo kwa fedha zilizotokana na mchango,” alisema Profesa Tibaijuka na kuongeza “Nilipewa fedha kwa ajili ya shule lakini nadaiwa kama ni kipato binafsi, hivyo nataka Mahakama iseme, ikikubali nitalipa bila shida yoyote.”

Mbunge huyo alifafanua kuwa, anatambua kulipa kodi ni suala la kila mwananchi na anachotaka ni ufafanuzi wa uhusiano uliopo kati ya mapato na kodi.

Alisema lengo ni kutaka kujua iwapo mchango ni sehemu ya fedha zinazostahili kutozwa kodi, bila kujali zimepokelewa zikiwa taslimu au kupitia kwenye akaunti benki.

“Nipo msibani hivi sasa. Watu wanakuja kunipa pole, wengine wanatoka Dar na wasioweza wanatuma michango yao na hapa ndipo nisipoelewa dhana ya kodi kwenye michango. Hii nayo inastahili kuingizwa kwenye mkumbo huo?” alihoji.

Msemaji wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Richard Kayombo alithibitisha kutolewa kwa hukumu hiyo kwenye pingamizi la makadirio aliloliweka mbunge huyo na kueleza kuwa bado anaweza akatafuta haki kwenye mamlaka za juu kama hajaridhika.

“Shauri lake liliamriwa Machi 29 na akatakiwa kulipa kiwango hicho alichokadiriwa,” alisema.

Mbunge huyo wa Muleba Kusini, alitakiwa kulipa fedha hizo baada ya TRAB kutupilia mbali rufaa yake ya kupinga kulipa zaidi ya Sh500 milioni.

Profesa Tibaijuka, Waziri wa zamani wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, alikata rufaa hiyo baada ya TRA kumtaka alipe kodi ya mapato Sh586,364,625 kutokana na fedha alizopokea kutoka kwa Mkurugenzi wa Kampuni ya VIP Engineering and Marketing Limited, Rugemalira.

Profesa Tibaijuka ambaye alipokea fedha hizo kupitia akaunti yake iliyopo Benki ya Mkombozi, zilisababisha kuvuliwa uwaziri na Rais mstaafu, Jakaya Kikwete.

Alisema fedha hizo hazikuwa zake binafsi bali zilitolewa msaada kwa Taasisi ya Joha Trust.

Hata hivyo, TRA kupitia kwa Wakili wake, Noah Tito ilisema Tibaijuka anawajibika kulipa kodi hiyo kwani fedha hizo ziliingia katika akaunti yake binafsi.

Mzimu Wazidi Kumuandama Mbunge Wa CCM Suleiman Saddiq Murad.....Baada ya TAKUKURU Kumpandisha Kizimbani, TBS Nao Wavamia Bekari Yake

0
0

Mzimu umeendelea kumwandama Mbunge wa Mvomero, Suleiman Saddiq Murad. 

Baada  ya  TAKUKURU  kumpandisha  mahakamani wiki iliyopita  kwa kuomba rushwa ya milioni 30, shirika la Viwango Tanzania (TBS)  nalo limeifunga Bekari yake( tanuri mikate )   kwa muda usiojulikana kwa kutotimiza masharti  ya viwango vya ubora.

Tanuri mikate hiyo pamoja na zingine 3 za watu wengine zilizopo Mkoani Morogoro, zilikaguliwa kwa mara ya kwanza Julai mwaka jana na wamiliki wake kupewa muda wa miezi sita kurekebisha kasoro zilizokuwepo, lakini hadi Machi 10, mwaka huu katika ukaguzi mwingine walikuwa hawajatekeleza na kutimiza masharti yaliyotolewa na TBS.

Mkaguzi wa TBS, Ashura Katunzi alisema kazi ya kuzifungia tanuri mikate hizo ipo kisheria baada ya wamiliki wake kushindwa kufuata utaratibu walioelekezwa awali wa kurekebisha kasoro kabla ya kuanza kwa uzalishaji tena.

Katunzi ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Udhibiti wa Ubora wa TBS, alisema: “Kabla ya kufunga bekari hizi, wakaguzi wa TBS walizitembelea tena mnamo Machi 10, mwaka huu ili kujiridhisha na iwapo utekelezaji umefanyika katika kipindi cha miezi sita waliopewa, lakini hakuna kilichofanyika,” alisema Katunzi juzi wakati wakifanya ukaguzi na kuchukua uamuzi huo.

Alisema kutokana na kukaidi agizo hilo, TBS imezifungua kwa muda usiojulikana hadi watakaporekebisha kulingana na maelekezo na kuomba upya kufunguliwa baada ya ukaguzi mwingine kufanyika.

Tanuri mikate zilizofungiwa kuanzia juzi ni MS Bakery Magooma Super Market inayomilikiwa na Murad, Baraka Bakery mali ya Salim Nassor, Sifasita Bakery inayomilikiwa na Tanzua Tambi na M&M Bakery mali ya Sarah Sanya.

“Bekari hizi zimekutwa zinafanya kazi katika mazingira hatarishi yasiyo salama na yanatia hofu kwa mlaji, zina ukosefu wa vyoo, zipo kwenye makazi ya watu na ukosefu wa vyumba vya kubadilisha nguo kwa wafanyakazi,” alifafanua Katunzi na kuongeza:

 “Katika ukaguzi wetu tumeona bekari hizi zina ukosefu wa eneo maalumu la kuoshea vyombo, uchakavu wa sakafu, mikate kuwekwa sakafuni na ufinyu wa eneo la kazi.”

Alisema endapo wamiliki hao watarekebisha kasoro na kutimiza viwango vya ubora, wanatakiwa kuwasilisha tena maombi rasmi TBS ili wakaguliwe tena ili kujiridhisha iwapo wametimiza vigezo kabla ya kufunguliwa tena.

“Watakapoharakisha kufanya marekebisho waliyoelelezwa, ndipo watakapoweza kufunguliwa haraka kuendelea na uzalishaji tena,” alifafanua mkaguzi huyo wa shirika la viwango.

Naye Ofisa Uhusiano wa TBS, Roida Andusamile alisema licha ya kuzifungia tanuri mikate hizo, kazi hiyo inaendelea ili kuzifikia nyingine zilizokaguliwa na kushindwa kutekeleza masharti yake.

Hivyo alitoa mwito kwa wazalishaji wa mikate katika Manispaa ya Morogoro na maeneo mengine wafuate utaratibu na kuweka ubora wa mikate kwa kuzingatia viwango vya TBS kabla ya kufikisha sokoni kwa walaji.

Baadhi ya wafanyakazi waliokutwa katika tanuri mikate hizo waliwasihi wakaguzi wa TBS wasiwafungie na badala yake wawapatie muda wa ziada ili warekebishe kasoro hizo wakati wakiendelea na uzalishaji, maombi yaliyogonga mwamba kutokana na kufungwa kwa milango kwa makomeo chini ya ulinzi wa Polisi.
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live




Latest Images