Quantcast
Channel: MPEKUZI
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live

Auawa Kwa Kuchomwa Kisu Akigombea Mwanamke Baa

$
0
0

Watu  wawili wameuawa mkoani Shinyanga katika matukio mawili tofauti, likiwamo la kijana kuchomwa kisu akigombea mwanamke katika baa ya Matunu mjini Shinyanga.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Dismas Kisusi alisema tukio la kwanza ni la juzi saa 6:00 usiku katika eneo la baa hiyo iliyopo mtaa wa Kaunda, kata ya Shinyanga Mjini, ambapo mwendesha bodaboda aliuawa kwa kuchomwa kisu akigombea mwanamke.

Kisusi alimtaja aliyeuawa kuwa ni Jumanne Ramadhani (22) mkazi wa Ndala katika Manispaa ya Shinyanga, ambaye alichomwa kisu kifuani upande wa kushoto na Emmanuel Shombe (20) mkazi wa Majengo na mfanyakazi wa kampuni ya Mobisolar inayojihusisha na uuzaji wa umeme wa jua.

Akielezea zaidi kuhusu tukio hilo, Kaimu Kamanda Kisusi alisema chanzo cha tukio hilo ni Ramadhani kutaka kumchukua kwa nguvu dada wa Shombe, Ester Shombe (18) mkazi wa Majengo mjini hapa.

“Ramadhani alikuwa analazimisha kumchukua kwa nguvu Ester ndipo kaka yake aitwaye Emmanuel akachukua kisu na kumchoma nacho kifuani upande wa kushoto kulikomsababishia kuvuja damu nyingi, alifariki akiwa njiani kupelekwa hospitali”, alieleza Kisusi.

Alisema Polisi inawashikilia watu wanne kwa ajili ya mahojiano zaidi kuhusu tukio. Wanaoshikiliwa ni Shombe, Ester, Joseph Amos na Tausi Mathias.

Katika tukio la pili, mlinzi na mkazi wa kijiji cha Isaka Station, wilayani Kahama, Moshi Saliboko (36) ameuawa kwa kunyongwa huku miguu yake ikiwa imefungwa kamba umbali wa mita 15 kutoka lindoni kwake katika ofisi za kampuni ya simu ya Zantel. Kisusi alisema Saliboko aligundulika kuuawa juzi saa 1:00 asubuhi katika kitongoji cha Majengo, kijijini humo.

Alisema Saliboko aliuawa kwa kunyongwa huku miguu yake ikiwa imefungwa kamba kisha wauaji kupora vipande vinne vya betri, rada aina ya 165AH, betri 1PG na transfoma (3CUWENT). Alisema baada ya tukio wauaji walitokomea kusikojulikana.

Askari wa Zimamoto Wanusurika Kupigwa Baada ya Kuchelewa Kufika Eneo la Tukio

$
0
0
Askari wa Kikosi cha Zimamoto, Manispaa ya Shinyanga wamenusurika kipigo kutoka kwa wananchi wa mtaa wa Banduka, kata ya Ndala mjini hapa, baada ya kuchelewa kufika kwenye tukio la nyumba kuungua moto ikiwa na watoto ndani yake.

Baadhi ya mashuhuda walidai kuwa moto huo ulianza kuwaka kwenye nyumba ya Azizi Abdallah, saa 2:00 asubuhi na uliunguza baadhi ya vitu kwenye nyumba hiyo ambayo wanaishi wapangaji pekee kwa kile kinachosadikiwa kuwa ni hitilafu ya umeme ambayo imekuwa ikijitokeza mara kwa mara.

Mmoja wa walioshuhudia, Onesmo Shija, alisema wapangaji wote walikuwa wamekwenda makazini na kubaki watoto ambapo saa 2:00 aliona moshi ukifuka kwenye madirisha huku watoto wakipiga kelele, ndipo walipokusanyika na kuanza kuuzima na kuwanusuru kifo watoto hao.

Shija alisema baada ya wananchi kutoa taarifa mapema kwa kikosi hicho, walichelewa kufika na walipofika tayari moto ulikuwa umeshazimwa ndipo wananchi walipopandwa hasira na kuanza kuokota mawe na kuwashambulia lakini mwenyekiti wa mtaa aliwazuia.

Mwenyekiti wa mtaa huo, Terege Nyankangara alisikitishwa na kikosi cha Zimamoto kuchelewa kufika eneo la tukio na kueleza uchelewaji huo ulitaka kuhatarisha amani. Hata hivyo, Nyankangara aliwaasa wananchi wake kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi.

Askari wa kikosi cha Zimamoto, Omari Magea alikiri wananchi hao kutaka kuwashambulia kwa mawe na alishukuru Mwenyekiti wa mtaa kuwezesha kurejesha amani. Alisema kilichowachelewesha ni uhaba wa vitendea kazi.

Aidha msimamizi wa nyumba hiyo, Daudi Nyanda alisema nyumba hiyo wanaishi wapangaji 10 na hakuna aliyepata madhara zaidi ya mali zao kuteketea. Alisema thamani bado haijafahamika.

Rais Magufuli Atoa Hati Ya Kiwanja Chenya Ukubwa wa Hekari 5 Kwa Bohari Ya Dawa (MSD)

$
0
0

RAIS Dk. John Magufuli kupitia Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ametoa kiwanja chenye ukubwa wa ekari 5 kwa Bohari ya Dawa (MSD) kilichopo Luguluni nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam, kwa ajili ya ujenzi wa Bohari ya Dawa ili kuondoa upotevu wa fedha kwa maghala ya kukodi.

Ujenzi wa maghala katika kiwanja hicho utaokoa kiasi cha sh. bilioni 4 zilizokuwa zikitumika kila mwaka kwa ajili ya malipo ya maghala ya kukodi yaliyopo Mabibo Ubungo jijini pamoja na kanda mbalimbali nchini.

Akizungumza wakati wa akikabidhi hati hiyo kwa Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu Dar es Salaam jana mchana, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alisema, Rais ametoa ardhi hiyo ili kuepusha gharama zisizo na sababu kwa MSD.

Alisema agizo la rais fedha zilizokuwa zikitumika kwa ajili ya kukodi maghala hayo, zinapaswa kununua dawa ili kila Mtanzania apate huduma bora za kiafya.

“Rais aliniagiza niwape eneo, leo nimetekeleza agizo hilo kilichopo muanze ujenzi kama mlivyoomba kwa ajili ya kujenga ghala la dawa, naamini mtaanza mara moja balada ya kuendelea kukodi maghala na badala yake fedha zote zitumike kwa ajili ya kununulia dawa na vifaa tiba,” alisema Lukuvi na kuongeza;

“Kiwanja hiki ambacho kilikuwa cha Shirika la Taifa la Nyumba (NHC) kilichokuwa na ukubwa wa ekari 200, tumewapa ekari tano kama uhitaji wenu ulivyokuwa, nimewasamehe kodi ya premium na badala yake kiasi cha Sh16.7 hamtalipa na gharama mtakayotakiwa kulipa ni sh. milioni 2 pekee ili muanze ujenzi mara moja.”

Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD) Laurean Bwanakunu alisema tayari wameshazungumza na Bodi ya wadhamini, Wizara ya Afya na wahisani hivyo ujenzi unatarajiwa kuanza mara moja Julai Mosi.

“Tunamshukuru sana Rais kwa sababu ombi hili limefanyiwa kazi kwa haraka sisi kama MSD tulishindwa kuhimili mikiki kutokana na gharama kubwa iliyokuwa ikielekezwa katika malipo ya ghala la kukodi pale ubungo mwaka wa fedha ulioisha tulilipa kiasi cha Sh3.5 bilioni na tukitarajia mwaka huu mpya wa fedha inafikia Sh4 bilioni kwa sababu ya malipo kwa dola,” alisema Bwanakunu.

Alisema katika eneo hilo jipya lililopo Luguluni wanatarajia kujenga zaidi ya maghala matano yenye ukubwa wa sikwea mita mita 5000 yatakayogharimu kiasi cha sh. bilioni 10 kila mojawapo, ujenzi huu utakapokamilika kanda zitakazonufaika ni pamoja na Dar es Salaam, Morogoro na Pwani na kuwa eneo hilo walilopata wanaweza kujenga kiwanda cha maji.

Watu Wanne Watiwa Mbaroni Kwa Tuhuma za Kutumia Jina la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Kutapeli

$
0
0

Watu wanne wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na tuhuma za kujipatia fedha kwa kutumia jina la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Washtakiwa hao walifikishwa katika mahakama hiyo jana kujibu mashtaka 12 yanayowakabili, likiwamo la kughushi barua na kuziwasilisha katika vituo vya mafuta wakirubuni watumiwe kiasi cha fedha ili waweze kupata punguzo la kodi.

Washtakiwa hao ni mwanafunzi, Issa Mohamed Awadhi (27)
maarufu kama Charles Robert au Mwamunyange, mkazi wa Ilala, ambaye hakuwapo mahakamani hapo kutokana na kulazwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) baada ya kuugua.

Wengine ni Hamisi Tembo(37) mkazi wa Ilala, mtengeneza mihuri, Nicolaus Obado(32), mkazi wa Mbagala Kuu na Wakati Mungi (51) mfanyabiashara na mkazi wa Yombo Makangarawe.

Washtakiwa walikana mashtaka na upande wa mashtaka ulidai upelelezi haujakamilika na kukosa dhamana. Kesi itaendelea Aprili 11.

Kamati ya Bunge Yamchokonoa Rais Magufuli Kuhusu Vibali vya Sukari

$
0
0

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, imemwomba Rais John Magufuli kuangalia tatizo la uhaba wa sukari nchini na kuona jinsi ya kufanya kuruhusu kutoa vibali kwa wafanyabiashara kuagiza sukari nje ya nchi.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dk Mary Nagu alisema uhaba wa sukari nchini kwa sasa ni kati ya tani 80,000 hadi 100,000 na kwamba kama hatua za haraka hazitachukuliwa, bidhaa hiyo itahadimika na wananchi watalanguliwa.

“Tumekutana na Bodi ya Sukari, na tumezungumza nao, wametuambia kuna upungufu wa sukari ya matumizi ya nyumbani kati ya tani 80,000 hadi 100,000, tunamuomba Rais na serikali yake kuangalia jambo hili na kuona umuhimu ya kuruhusu kiasi hicho cha sukari kiingizwe,” alisema Dk Nagu.

Alisema kabla ya nchi kubinafsisha viwanda vya sukari ilikuwa inazalishwa kwa mwaka tani 100,000 na baada ya kubinafsishwa viwanda vya ndani vinazalisha tani 320,000 ilhali mahitaji ni tani 420,000.

Hivi karibuni, Rais Magufuli alitangaza kupiga marufuku uingizaji wa sukari kutoka mataifa ya kigeni ili kuvilinda viwanda vya sukari nchini humo ambavyo vimeathiriwa na uingizaji wa sukari ya bei rahisi kutoka nje.

‘’Tuna viwanda nchini ambavyo hununua miwa kutoka kwa wakulima wadogo wadogo. Viwanda hivi huzalisha sukari, ajira na ni chanzo cha mapato ya serikali. Ijapokuwa tuna hifadhi ya kutosha ya sukari kuna watu serikalini wanaotoa vibali vya kuingiza sukari kutoka nje,” alisema Dk Magufuli.

Aidha, Bodi ya Sukari Tanzania ilitangaza kushusha bei ya sukari kwa kutangaza bei elekezi inayoonesha bidhaa hiyo kuanzia sasa inauzwa Sh 1,800 kwa kilo nchini kote, huku ikisema haitasita kuchukua hatua stahiki za kisheria kwa wale watakaobainika kupandisha bei au kuhodhi bidhaa hiyo.

Naye Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwezekezaji, Charles Mwijage alisisitiza kuwa hakuna uhaba wa sukari nchini na kuwataka wafanyabiashara walio na leseni za kuingiza na kuuza bidhaa hiyo, kutoificha.

Hata hivyo, Dk Nagu jana alidai upungufu wa sukari nchini upo na kwamba wapo wafanyabiashara wanaotumia mwanya huo vibaya kwa kuagiza sukari nyingi kuliko ile iliyokubaliwa kwa lengo la wao kunufaika, na kuiomba serikali kuongeza juhudi za kuziba mianya ya uingizaji wa sukari bila vibali.

Alisema ni vyema serikali ikaona haja ya kuondoa tatizo la uhaba wa sukari hivi sasa kwa sababu kama uhaba huo utaendelea, wananchi ndio wataathirika zaidi huku wafanyabiashara akitumia mwanya huo kuongeza bei ya bidhaa hiyo ila iwapo itaagizwa kwa wakati, si rahisi kwa wafanyabiashara hao kupandisha bei.

Mkurugenzi Mkuu wa Kiwanda cha Sukari cha Mtibwa cha mkoani Morogoro, Hamad Yahaya anawasihi wafanyabiashara wasio waaminifu, kuacha kutoa taarifa za uongo kuhusu kiasi cha sukari waliyonayo ili ionekane kuna upungufu na wao wapandishe bei.

Wafanyakazi watatu TANESCO Watiwa Mbaroni Kufuatia Kifo cha Mfanyakazi Mwenzao Aliyenaswa na Umeme Juu ya Nguzo

$
0
0

Wafanyakazi watatu wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) mkoani Morogoro, wanashikiliwa na Polisi wakihojiwa kutokana na kifo cha mfanyakazi mwenzao, Deo Elias (30), mkazi wa Mazimbu, Manispaa ya Morogoro kwa kunaswa na umeme juu ya nguzo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 5.30 asubuhi maeneo ya Mafiga, wakati Elias akiwa na wafanyakazi wenzake katika eneo la kazi.

Kamanda Matei alisema Elias alipokuwa na wenzake katika eneo hilo wakirekebisha umeme, alinaswa na kufa papo hapo.

Meneja wa Tanesco Mkoa wa Morogoro, Mhandisi John Bandiye akizungumzia tukio hilo ofisini kwake jana, alisema Elias alikuwa katika kazi za kawaida kama fundi na tukio hilo limetokea kwa bahati mbaya.

Mhandisi Bandiye alisema mfanyakazi huyo alikuwa akirekebisha njia ya umeme ya Ngazengwa iliyopo eneo la Mafiga na ilikuwa imezimwa, lakini cha kushangazwa ilikuwa na umeme uliosababisha kifo chake.

“Kwa sasa shirika lina wafanyakzi wa muda wanaosaidiana na mafundi wakuu na hupatiwa mafunzo na wanatambulika, tofauti na maneno yaliyozagaa mitaani kuwa marehemu hakuwa mfanyakazi,” alisema.

Alisema mwili wake umesafirishwa kwenda kwao mkoani Mbeya kwa ajili ya maziko.

Diwani wa CHADEMA Apeta Mahakamani, wa CCM Chali baada ya Pingamizi Lake Kutupwa

$
0
0

Mahakama  ya Hakimu Mkazi Arusha imetupilia mbali kesi ya kupinga matokeo ya udiwani katika kata ya Musa wilayani Arumeru Magharibi iliyofunguliwa na mgombea wa CCM, Flora Zelote dhidi ya diwani wa Chadema, Loth Laizer.

Akitoa uamuzi wa hukumu hiyo iliyosomwa jana na Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Mwamkuga Gunta, alisema haoni kama kuna kasoro yoyote katika uchaguzi huo uliompa ushindi Laizer.

Akitoa uamuzi, Gunta alisema licha ya Zelote kudai kudhalilishwa pamoja na kuibiwa kura lakini ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na mashahidi mbalimbali hautoshi kudai kuwa alipokwa ushindi wa kuwa diwani wa kata hiyo.

“Natupilia mbali kesi hii sababu ushahidi uliotolewa mahakamani hapa hautoshi kumvua udiwani diwani wa Chadema, pia mashahidi waliotoa ushahidi mahakamani hapa ushahidi wao umejichanganya hivyo natupilia mbali kesi hii,” alisema Gunta.

Awali kabla ya kuahirishwa kwa kesi hiyo wiki iliyopita, Hakimu Gunta aliomba radhi kwa kutokamilisha hukumu hiyo kwa sababu alikuwa akiuguliwa hivyo aliahidi kutoa hukumu jana, Machi 29.

Kesi hiyo ambayo awali ilisikilizwa kwa siku mbili mfululizo kwa zaidi ya saa nane kila siku, mashahidi wote walikamilisha ushahidi wao akiwamo Laizer aliyekiri mahakamani hapo kuwa aliongozana na kundi kubwa la wafuasi wa chama chake kwenda katika kituo kikuu cha kujumlishia matokeo ya udiwani katika kata hiyo kilichokuwa katika shule ya sekondari ya Musa.

Hata hivyo, akiongozwa na wakili wake Adiel Charles, diwani huyo alishindwa kukanusha lugha ya matusi iliyotolewa na wafuasi wake aliyokuwa ameongozana nao Oktoba 25 mwaka jana, wakiwa na silaha za jadi ambazo ni sime na fimbo pamoja na kutishia usalama wa maisha ya mgombea wa CCM, Zelote.

Wengine waliotoa ushahidi wa upande wa mlalamikiwa ni pamoja na msimamizi msaidizi wa uchaguzi kata ya Musa, Tuwati Leondoya. 

Wengine ni Lomito Robert na Ally Mollel. Kwa upande wa mlalamikaji, mashahidi watano walitoa ushahidi akiwamo Zelote, Meimoite Kivuyo, Lekisongo Singa, Edson Lesikari na Alex Lukumay.

Kesi hiyo ya uchaguzi namba sita ya mwaka 2015 ilifunguliwa mahakamani hapo na Zelote aliyekuwa mgombea wa udiwani katika kata hiyo kwa tiketi ya CCM dhidi ya Laizer wa Chadema.

Zelote alifungua kesi hiyo baada ya kubaini kuwapo kwa ukiukwaji mkubwa wa taratibu za kampeni pamoja na uchaguzi zilizotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC). Laizer alitangazwa mshindi katika uchaguzi huo.

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Jumatano ya March 30


Waliompiga Daktari Mkoani Mtwara Wakamatwa Wakijiandaa Kutoroka Kwenda Nje ya Nchi

$
0
0

Kufuatia tukio la ndugu wa mgonjwa  kumpiga Daktari Mkoani Mtwara, tayari jeshi la Polisi Mkoani humo linawashikilia watu kadhaa kwa kitendo hicho cha kumpiga Daktari wakati akiwa katika majukumu yake ya kikazi.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Mtwara,Henry Mwaibambe (Pichani) amesema hadi sasa watu 2 wanaotuhumiwa kumpiga daktari hospitali ya Mkoa wamekamatwa usiku wa kuamkia jana wakitoroka nchini huku wengine 3 wakiendelea kusakwa.

Awali wauguzi na Madaktari wa Hospitali hiyo waligoma kufanya kazi hadi hapo watakapohakikishiwa usalama wao ndipo wafanye kazi

Jana, Waziri wa Afya Ummy Mwalimu aliweza kufika Hospitalini hapo na kusuluhisha mgogoro huo huku akiomba Jeshi la Polisi kuongeza usalama kwa watumishi hao wa Afya.

Waziri wa Mambo ya nje, Balozi Mahiga Asema Serikali imesikitishwa na Kusitishwa kwa Msaada wa Mabilioni ya Marekani

$
0
0

Serikali imeeleza kusikitishwa na uamuzi wa Marekani kusitisha uhusiano katika Shirika la Changamoto za Milenia (MCC), bila kuishirikisha wala kuisikiliza.

Kadhalika, imesema hakuna umuhimu wa misaada ya afya na elimu inayofadhiliwa na Marekani kwa dola za Marekani milioni 700 (Sh. trilioni 1.5), kama imejitoa katika kusaidia miradi ya umeme ambayo ni muhimu katika utekelezaji wa miradi inayofadhili, kwa kuwa ni sawa na kutoa kwa mkono wa kulia na kupora kwa mkono wa kushoto.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, baada ya kupokea taarifa ya uamuzi wa MCC, Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Augustine Mahiga, alisema uhusiano na Marekani utaendelea katika maeneo mengine, lakini kwa fedha hizo hakuna la kufanya ingawa milango iko wazi iwapo watafikiria upya.

“Fedha ni zao, uamuzi ni wao wameutoa Washington. Hatuwezi kulia kwa ajili ya hili, tutaendeleza ushirikiano katika maeneo mengine, lakini tunawaomba wafanye uchambuzi wa kigezo cha demokrasia kwa asilimia 100 kinachotumika katika misaada hiyo,” alibainisha na kuongeza:

“Wametusaidia kwa miaka mitano kwa vile tulikidhi vigezo, ila sasa tumeshindwa kimoja inafuta imani na uelewano ambao ulikuwapo kati yetu. Nishati ndiyo nyenzo ya maendeleo kwa Tanzania. Kwa sasa tunaelekeza umeme vijijini ili vijana wanaosoma bure wajisomee na hospitali zitoe huduma muda wote.”

Waziri Mahiga alisema Tanzania imetia saini mkataba wa malengo ya milenia ambayo yanakwenda sambamba na MCC, hivyo kufuta fedha hizo kwa sasa ni sawa na kuumiza mahali panapouma zaidi huku ikiwa (Marekani) kiongozi wa utawala bora, demokrasia na soko huria duniani.

Alifananisha kunyimwa fedha hizo sawa na kutoa adhabu kwa mkosaji bila kujali kuwa alipaswa kumwelimisha na kumwonya kabla ya adhabu kubwa.

“Ukichukua mizani na kuweka nyama upande huu na jiwe upande mwingine, ukapima mazuri ambayo Tanzania imekuwa ikifanya na kuonekana mtoto mzuri machoni mwa dunia, lakini upungufu wa sasa waliouona, utaona tuna mazuri mengi, hivyo  hatukustahili adhabu hii,” alisisitiza.

“Uamuzi wao hatuwezi kuwaingilia, nasi tukiamua yetu wasituingilie. Tumejitahidi tuwezavyo kulinda demokrasia na hatutarudi nyuma kwani katika uchaguzi wa Zanzibar vyama vilishirikishwa. Waelewe na kutambua mazuri yetu tunayofanya na tutaendelea kufanya,” afafanua.

Aidha, alisema suala la Zanzibar liliendeshwa vizuri kwa kuwa lilitoa nafasi ya mazunguzo kwa pande zote na kwamba hakuna mwenye uwezo wa kuingilia masuala ya uchaguzi, serikali na mambo ya ndani ya visiwa hivyo kwa kuwa wana katiba na sheria zao bali mambo machache tunashirikiana na hata Rais Dk. John Magufuli, alikuwa mwangalizi tu.

Balozi Mahiga aliishangaa Marekani kwa kueleza kuwa uamuzi wa sasa unapingana na tamko la hivi karibuni lililosisitiza mazungumzo baada ya serikali mpya kuingia madarakani, kwa kuwa kabla ya utekelezaji, imetoa uamuzi wa kuvunja uhusiano na Tanzania katika MCC.

“Kitu kinachoitwa demokrasia kingekuwa kinafugwa kwenye bomba na kuona kinamiminika ingekuwa rahisi sana, lakini ni kitu cha kulea na kutengeneza. Tanzania imejulikana duniani kama mlezi na mjenzi wa demokrasia tangu kipindi cha chama kimoja hadi vyama vingi,” alisema.

Aidha, alisema kutokana na hali hiyo, serikali itafanya marekebisho katika bajeti yake na mpango wa maendeleo ambao ulijumuisha fedha hizo na kwamba kinachopaswa kufanyika kwa sasa ni kujikita kwenye ukusanyaji wa kodi kikamilifu.

“Ndani ya vikao vya Bunge la Marekani tuna marafiki zetu ambao tunaamini wataendelea kuihoji serikali yao juu ya uamuzi huu na hasa wakizingatia historia yetu katika kukuza na kuendeleza demokrasia nchini,” alibainisha.

Waziri wa Ujenzi Prof. Mbarawa afanya ziara ya kushtukiza KOJ Kurasini

$
0
0

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amemuagiza Kaimu Meneja Msaidizi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) Nelson Mlali kufanya uhakiki wa kampuni zinazotoa huduma mbalimbali bandarini ili kuboresha utendaji kazi na kuepuka mgongano wa maslahi binafsi minongoni wa watumishi wa bandari.

Profesa Mbarawa alitoa kauli hiyo baada ya kufanya ziara ya kushtukiza jana jioni(29/03/2016) kwenye ofisi za Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) eneo la kupakulia mafuta yanayoingia nchini (KOJ) Kurasini.

“Mtafanyaje kazi na mtu ambaye ni mfanyakazi na huku kampuni yake inatoa huduma bandarini, hamuoni kutakuwa na mgongano wa kimaslahi binafsi,” alihoji Profesa Mbarawa.

Aidha, Prof. Mbarawa amemtaka Kaimu Meneja Msaidizi Mlali azingatie umiliki wa makampuni kulingana na taarifa za Wakala wa Usajili wa Biashara na Kampuni nchini (BRELA) katika zoezi la kuhakiki kampuni hizo.

Akiwa eneo la (KOJ) Kurasini, Prof. Mbarawa amewataka wafanyakazi wa TPA  wabadilike na kufanya kazi kwa juhudi na maarifa badala ya kufanya kazi kwa mazoea ili kuboresha kuongeza ufanisi na kuliongezea taifa mapato kwa manufaa ya wananchi.

Prof. Mbarawa amewaagiza pia Mamlaka ya Bandari wanaponunua vipuri na vifaa mbalimbali vinavyohitajika bandarini hapo wazingatie vipimo sahihi kulingana na vifaa vinavyohitajika kuendeshea mitambo mbalimbali ili kulipunguzia taifa gharama zisizohitajika.

Mamlaka ya Bandari nchini ina bandari mbalimbali zilizopo katika ukanda wa bahari ya Hindi na maziwa yaliyopo nchini.

Ukanda wa Bahari ya Hindi una bandari ya kuu za Dar es salaam, Tanga na Mtwara pamoja na Bandari ndogo zilizopo Lindi, Kilwa Masoko, Mafia, Bagamoyo, Pangani na Kwale.

Bandari nyingine ziliozo katika maziwa mbalimbali nchini ni pamoja na Ziwa Victoria lenye bandari ya Mwanza, Bukoba, Kemondo, Musoma na Nansio, Ziwa Tanganyika likihusisha bandari ya Kigoma na Kasanga wakati Ziwa Nyasa kuna bandari ya  Itungi, Manda, Liuli na Mbaba Bay.

Tanzania yapokea msaada wa shilingi bilioni 116.4 kutoka Japan.

$
0
0
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesaini hati mbili za makubaliano na Serikali ya Japan itakayoiwezesha Tanzania kupata kiasi Yen Bilioni 6 ambazo ni sawa na Sh. Bilioni 116.4 za Kitanzania.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kusaini hati hizo, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Servacius Likwelile alisema mkataba wa kwanza utasaidia katika kukamilisha bajeti ya Serikali ya mwaka 2016/17.

Dkt. Likwelile alisema kuwa msaada huo unalenga kuweka mazingira rafiki ya kwa wafanyabiashara, kuboresha masoko na kuwezesha mazingira ya ushindani katika utengenezaji wa ajira nchini.

Mkataba wa pili  unahusu masuala ya kiufundi  yatakayotumika katika kufanya marekebisho ya mkataba uliosainiwa  Octoba 20, 1966, kwa kuzingatia sheria nyingi zimebadilika, kusainiwa kwa hati hiyo ya makubaliano itasaidia kutabadilisha baadhi ya vifungu vyenye jina Tanzania na kuweka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kujumuisha pande zote mbili za Muungano katika kutekeleza miradi ya maendeleo nchini.

Aidha, makubaliano hayo yatasaidia kubadilisha baadhi ya vipengele vya mkataba uliopita ikiwemo kipengele cha usambazaji wa madawa ili kuweza kukidhi mahitaji ya sasa ya wataalamu kutoka nchini Japan kuweza kuja kufanya kazi za kujitolea hapa nchini Tanzania.

Katibu Mkuu Dkt. Likwelile ameishukuru Serikali ya Japan na kusisitiza kuwa fedha hizo zitatumika kama ilivyopangwa ili kuweza kuwa na tija na kuwaletea maendeleo Watanzania.

Naye Balozi wa Japan nchini Tanzania Bw. Masaharu Yoshida amesema kuwa Serikali ya Japan ina imani kuwa ushirikiano uliopo baina ya nchi hizi mbili utasaidia kukuza maendeleo ya uchumi na kijamii.

Balozi Yoshida amesema kuwa Serikali ya Japani inaunga mkono juhudi za Serikali inayo ongozwa na Rais Dkt. John Magufuli katika masuala ya viwanda na mazingira mazuri yanayovutia wawekezaji  kuwekeza nchini Tanzania.

Adha Balozi Yoshida amesema kuwa Japan itaendelea kuwaleta vijana wanaojitolea katika sekta ya uchumii na ya kijamii jambo limekuwa likitekelezwa tangu mwaka 1969 ambapo hadi sasa idadi ya vijana hao wa kujitolea imefikia zaidi ya 1500.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Servacius Likwelile (kushoto) akikisaini hati ya makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Japan leo jijini Dar es salaam ambao utaiwezesha Tanzania kupata kiasi Yen Bilioni 6 ambazo ni sawa na Sh. Bilioni 116.4 za Kitanzania. Kulia ni Balozi wa Japan nchini Tanzania Bw. Masaharu Yoshida.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Servacius Likwelile akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) mara baada ya kusaini hati ya makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Japan leo jijini Dar es salaam ambao utaiwezesha Tanzania kupata kiasi Yen Bilioni 6 ambazo ni sawa na Sh. Bilioni 116.4 za Kitanzania.

Makamu Wa Pili Wa Rais Wa Zanzibar Aapishwa

$
0
0
Balozi Seif Ali Iddi akielekea sehemu ya kula kiapo kuwa Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar alipoapishwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein katika hafla iliyofanyika leo Ikulu Mjini Zanzibar.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akimuapisha Balozi Seif Ali Iddi kuwa Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar katika hafla iliyofanyika leo Ikulu Mjini Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kushoto) akibadilishana mawazo na Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi baada ya kumuapisha rasmi leo katika ukumbi wa Ikulu Mjini Unguja.

TAKUKURU Yabuni Mbinu Mpya ya Kupambana na Rushwa

$
0
0

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa wa Kinondoni imebuni mbinu mpya ya kushirikiana na wananchi kwa urahisi zaidi katika mapambano dhidi ya rushwa kwa kusogeza huduma zake za kiofisi kwa kuwafuata wananchi na kuweka ofisi katika eneo lililowazi ili Wananchi waweze kutoa kero zao na kupatiwa ufumbuzi papo hapo.

Njia hii ya ofisi inayotembea (mobile office) ilizinduliwa rasmi na Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa kinondoni Bw. Benn Lincolin siku ya tarehe 23/03/2016 eneo la Bakhresa Manzese kwa kauli mbiu ‘Mwananchi ulipo TAKUKURU tupo kutatua kero yako ya Rushwa kwa wakati’ inayoenda sambamba na kauli mbiu ya Serikali ya awamu ya tano ya ‘ Hapa Kazi Tu’ kwa lengo la kutoa huduma kwa kuwafuata wananchi mahali walipo na sio kwa kusubiri wao kuleta malalamiko yao katika ofisi za TAKUKURU.

Imeonekana kwamba njia hii itasaidia kutoa elimu kuhusu mapambano dhidi ya rushwa na kurahisisha ufuatiliaji wa fedha za miradi zinazotolewa kwenye Manispaa. Pia itakuwa fursa nzuri ya kuwaelewesha wananchi kuhusiana na sheria katika upatikanaji wa dhamana mahakamani na polisi.

Wito unatolewa kwa wananchi kujitokeza kwa wingi katika maeneo ambayo ofisi hii inayotembea ya TAKUKURU Kinondoni itakapokua ili waweze kupata elimu na kutatuliwa kero zao. Zawadi zitatolewa kwa mwananchi ambae atakua akijibu vizuri maswali ya Chemsha Bongo kwani zoezi hili ni endelevu.

IMETOLEWA NA
MKUU WA TAKUKURU (M) KINONDONI
BENN LINCOLIN
30/03/2016.

Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) Yasema Imejipanga kukusanya Bilioni 8 kwa mwezi...... Kamati ya Bunge yataka orodha ya wadaiwa

$
0
0

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imesema imeanza kutekeleza mikakati mipya ya ukusanyaji wa mikopo ya elimu ya juu kutoka kwa wadaiwa ambayo itaongeza wastani wa ukusanyaji wa Tshs 2.6 bilioni za sasa hadi kufikia Tshs 8 bilioni ifikapo mwezi Julai mwaka huu.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Bw. Jerry Sabi ameyasema hayo jana (Jumatano, Machi 30, 2016) jijini Dar es Salaam alipokuwa akiongea mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii iliyotembelea ofisi za Bodi hiyo zilizopo Mwenge.

“Hadi mwezi uliopita (Februari, 2016) tulikuwa tunakusanya wastani wa shilingi bilioni 2.6 kwa mwezi, lakini sasa tumeongeza kasi na mikakati mipya ambayo itawezesha kukusanya shilingi bilioni 6 mwezi Aprili na shilingi bilioni 8 ifikapo mwezi Juni mwaka huu,” alisema Bw. Sabi aliyeteuliwa kushika nafasi hiyo na miezi miwili iliyopita.

HESLB ilianzishwa ilianza kazi mwaka 2005 ili kutoa mikopo kwa wanafunzi wahitaji na pia kukusanya mikopo kwa wanufaika.

Hadi sasa, zaidi ya shilingi 2.1 trilioni zimetolewa kwa wanufaika na kati ya fedha hizi, mikopo iliyoiva na inayopaswa kukusanywa ni shilingi 258 bilioni ambazo wanufaika wake wamemaliza au kusitisha masomo yao na vilevile kumaliza muda wa kujipanga kuanza kulipa (grace period).

Kwa mujibu wa Bw. Sabi, hadi sasa, HESLB imekusanya shilingi 91 bilioni kati ya shilingi 258 bilioni zilizoiva na hivyo kupaswa kukusanya. 

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji huyo alikuwa akijibu hoja zilizotolewa na Wajumbe wa Kamati hiyo waliokutana na watendaji wa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi na HESLB wakiongozwa na Waziri Prof. Joyce Ndalichako na Naibu wake Mhandisi Stella Manyanya.

Bw. Sabi alitaja mikakati mipya iliyobuniwa na HESLB kuwa ni pamoja na kuimarisha mtandao baina ya Bodi na waajiri kutoka sekta binafsi na umma ambao unalenga kubaini na kukusanya kiasi cha shilingi 7.02 bilioni kwa mwaka kutoka kwa wanufaika 136,252.

“Tunapata ushirikiano mkubwa kutoka kwa taasisi za Serikali na sasa tumejipanga kupitia upya mitandao ya waajiri kwa kushirikiana na taasisi kama Chama cha Waajiri (ATE), Mfuko wa Sekta Binafsi (TPSF) na Shirikisho la Asasi zisizo za Kiserikali (TANGO) ili kuhuisha takwimu zetu kuhusu waajiri ili kukusanya taarifa za wadaiwa wapya kwa haraka,” alifafanua Bw. Sabi.

Mikakati mingine ni kutoa elimu na kuimarisha ushirikiano na wadau mahsusi kama Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Usimamizi wa Mashirika ya Hifadhi za Jamii (SSRA), Wakala wa Usajili wa Makampuni (BRELA), Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) na vyama vya kitaaluma.

Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini Bw. Peter Serukamba ameitaka HESLB kuongeza kasi ya kudai mikopo iliyoiva na kuutaka uongozi wa HESLB kuandaa orodha ya wadaiwa wote na kuiwasilisha kwa kamati ili ifanyiwe kazi.
 
“Ni lazima kuwe na fedha ili kuwezesha kutoa mikopo kwa wahitaji wengine ...haiwezekani mtu anapata mkopo halafu halipi...andaeni orodha ya wote walionufaika na mikopo ambayo itaonyesha nani halipi, nani analipa na nani amemaliza na tutaamua tufanye nini,” alisema Sekukamba.

HESLB ilianzishwa mwaka 2004 na kuanza kazi rasmi mwezi Julai mwaka 2005 kwa lengo la kutoa mikopo kwa watanzania wahitaji waliopata nafasi za masomo katika vyuo vya elimu ya juu na kukusanya mikopo iliyoiva kutoka kwa wadaiwa walionufaika na mikopo tangu mwaka 1994.
Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii wakibadilishana mawazo na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi Prof. Joyce Ndalichako (katikati) wakati Kamati hiyo ilipotembelea ofisi za Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) jijini Dar es Salaam
 Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi Bi. Maimuna Tarishi akisalimiana na Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii Dkt. Ely Macha (kulia) wakati Kamati hiyo ilipotembelea ofisi za Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) jijini Dar es Salaam jana (Jumatano, Machi 30, 2016). Katikati mwenye suti ya kijivu ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Bw. Jerry Sabi. (Picha: HESLB)

Mkuu wa Wilaya Aagiza kushushwa Vyeo Wakuu wa shule za Msingi na Sekondari Zilizofanya Vibaya Katika Matokea ya Mtihani

$
0
0

Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, Chande Nalicho ameagiza kushushwa vyeo wakuu wa shule zote za msingi na sekondari katika wilaya hiyo, ambao shule zao zimefanya vibaya katika matokeo ya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi na sekondari mwaka 2015/2016.

Aidha amewataka wenyeviti na wajumbe wa bodi za shule kujipima uhalali wao kama wana sifa ya kuendelea kuwemo katika nyadhifa zao, kutokana na matokeo mabaya yaliyopata shule wanazozisimamia ambayo yameitia aibu wilaya hiyo.

Alisema wenyeviti na wajumbe wa bodi ni lazima waachie ngazi kwani shule zao zimefanya vibaya na imeonekana sababu mojawapo ya kufanya vibaya kwa shule hizo ni walimu kutowajibika.

Alisema wameshindwa kuwafuatilia na kushindwa kushirikiana na wazazi kutatua changamoto mbalimbali zinazozikabili shule zao.

Nalicho alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na wakuu wa shule nne za sekondari, wajumbe na wenyeviti wa bodi za shule hizo zilizofanya vibaya katika matokeo ya kumaliza elimu ya sekondari mwaka uliopita.

Alikutana nao katika kikao maalumu cha kazi na baadhi ya watumishi wa kata ya Lusewa kilicholenga kutafuta majawabu juu ya kero zinazowakabili wakazi wa kata hiyo.

 Shule zilizofanya vibaya katika matokeo hayo ni Lusewa, Msisima, Kwizombe na Matepwende.

Aliwataka walimu na wakuu wa shule hizo kuongeza juhudi katika kuwasaidia watoto madarasani ili waweze kufanya vizuri katika masomo yao.

“Sitakubali mwaka ujao kuona shule zenu zinaendelea kushika mkia, ninyi ndiyo chanzo cha wilaya yetu kushika nafasi ya pili kutoka mwisho katika matokeo ya mitihani ya mwaka jana. Nataka muongeze juhudi katika kazi zenu, tumieni muda mwingi kuwafundisha hawa watoto madarasani, badala ya kutumia muda wenu kwa ajili ya kufanya anasa,” alisema Nalicho.

Alisema suala la elimu ni muhimu katika maisha ya binadamu kwani hakuna anayeweza kufanikiwa katika maisha yake kama hajakwenda shule.

Aliwasisitiza kuwa muda umefika kwa wakazi wa kata hiyo kuona aibu na matokeo hayo, badala yake wahimize watoto wao kupenda shule kwa kuwa elimu ndiyo urithi bora kwa mtoto.

Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Alhamisi ya March 31

Meya Wa Jiji La Dar Es Salaam, Isaya Mwita Aapishwa

$
0
0

Meya Wa Jiji La Dar Es Salaam, Isaya Mwita amesema kati ya Aprili 10 na 11 ataitisha kikao cha kwanza cha Baraza la Jiji, kwa ajili ya kumpata naibu meya.

Mwita aliyasema hayo jana  muda mfupi baada ya kuapishwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Sokoine.

Machi 22, Mwita alichaguliwa kuwa meya wa Jiji la Dar es Salaam baada ya kupata kura 84 dhidi mpinzani wake, Yusuf Yenga (CCM) aliyeambulia 67.

Mwita alisema kinachoendelea hivi sasa ni taratibu za kuwapata wajumbe watakaoingia katika baraza hilo, ambalo lipo tofauti na lililomchagua yeye.

“Ningeweza kuitisha baraza hili hata Ijumaa, lakini sheria inanitaka nikishateuliwa, niitishe baada ya siku saba,” alisema Mwita ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Vijibweni (Chadema).

Machi 23, Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Wilson Kabwe alisema kuwa naibu meya atapatikana katika Baraza la Jiji litakaloongozwa na meya akishirikiana na yeye.

Hata hivyo, Kabwe alisema jana kuwa wanaendelea na maandalizi ya baraza hilo, ikiwamo kusubiri kuwasilishwa kwa akidi ya wajumbe watakaoshiriki kikao hicho.

Baada ya kuapishwa, Mwita aliwaambia wanahabari kuwa anadhamiria kuwa kiongozi muunganishi bila kujali tofauti za kiitikadi.

Alisema hatarajii kipindi chake cha uongozi kiwe na vurugu au machafuko katika Jiji la Dar es Salaam.

‘’Viongozi wangu wa chini wajisikie amani, kwani mimi nitakuwa kiongozi bora kwa watu wote. Wala sikuja kwa ajili ya kuleta machafuko na ugomvi, bali nahitaji amani ili tutafute maendeleo,’’ amesema.

Mwita alisisitiza ushirikiano kwa viongozi wote ili washughulikie changamoto za muda mrefu katika jiji hilo – usafiri, miundombinu, afya, elimu, na huduma nyingine za jamii.

Watu 580 Wajitokeza Kuhakiki Silaha Dar es Salaam

$
0
0

Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, imesema watu 574 wamejitokeza kuhakiki wa silaha zao.

Mkuu wa mkoa huo, Paul Makonda alitoa siku 90 kwa wakazi wa Dar es Salaam wawe wamehakiki silaha zao ifikapo Julai mosi, ikiwa ni miongoni mwa mikakati yake ya kupambana na uhalifu uliokithiri.

Hivi karibuni, Rais John Magufuli alihakiki silaha zake anazomiliki.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro alisema wanaendelea kuwahimiza wananchi waendelee kujitokeza kuhakiki silaha zao kwa muda uliotolewa.

“Hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wote waliokaidi kujitokeza kuhakiki silaha zao, baada ya siku 90 zilizopangwa kumalizika” alisema.

Wakati huohuo, Siro alisema wafanyabishara wanaouza vipuri vya magari vilivyotumika maeneo ya Kariakoo, wengi wanauza vilivyoibwa sehemu mbalimbali nchini.

 “Nimeshapata mtandao mzima wasipoacha kununua vitu vya wizi tutawakamata na wale wanaojifanya madalali wao, wanashirikiana na majambazi hivyo nataka waache mara moja,” alisema.

Wananchi Waanza Kugombania Kiti Alichokikalia Rais Magufuli Kwenye Mgahawa Jijini Mwanza

$
0
0

Mgahawa aliotumia Rais John Magufuli kupata mlo wa mchana na msafara wake juzi kwenye Uwanja wa Ndege wa Mwanza, umekuwa kivutio kwa wateja wengi wakinunua chakula na kutaka kukalia kiti na meza alivyotumia kiongozi huyo.

Meneja wa mghahawa huo wa Victoria, Elizabeth Maneno (pichani) alisema jana kwamba hali hiyo ilijitokeza mara baada ya Rais kuondoka hapo.

“Hata leo tumepokea wateja wengi kulinganisha na siku nyingine, baadhi yao wanaagiza chakula kwa sharti la kutaka kukikalia kiti na meza aliyotumia Rais Magufuli,” alisema Elizabeth.

Akizungumzia hali ilivyokuwa juzi kabla na wakati wa ugeni huo meneja huyo alisema: “Ilikuwa ni hofu na woga uliochanganyika na furaha kumwona Rais akiingia kwenye mgahawa wetu wa chai ya rangi ya Sh200 na ya maziwa Sh300.

“Mshtuko wetu uligeuka furaha baada ya kubaini kuwa oda ya sahani 28 za kubeba (takeaway), tulizoagizwa mapema asubuhi bila kuelezwa zinakoenda zilikuwa za ujumbe wa Rais,” alisema na kuongeza:

“Kabla Rais Magufuli hajaingia kwenye mgahawa wetu, alikuja mtu mmoja tusiyemfahamu na kuagiza sahani 28 za chakula kwa gharama ya Sh5,000 kila moja,”

Alisema baada ya kumtaarifu mteja wake kuwa chakula kiko tayari, alielekezwa kuandaa meza na viti kwa sababu wageni wake (wa mteja), sasa wameamua kula palepale mgahawani.

“Ghafla tulimwona Rais anaingia ndani ya mghahawa wetu; kwanza tulishikwa hofu, woga na kihoro tusijue tufanye nini hadi tulipogutushwa na aliyetoa oda kwa kutuagiza tugawe chakula alichoagiza,” alisema meneja huyo;“hapo ndipo tulipobaini kumbe chakula kile kilikuwa cha ugeni wa Rais.”

Pamoja na chai ya rangi na ya maziwa, mghahawa huo pia unauza vyakula vya aina mbalimbali kwa bei kati ya Sh1,500 hadi Sh5,000 kwa vyakula vya kubeba, huku soda ikiuzwa kwa Sh500 kwa chupa.
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live




Latest Images