Quantcast
Channel: MPEKUZI
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Jumanne ya March 8


Watumishi 597 Wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa ( NIDA ) Wasimamishwa Kazi

Madaktari wa Hospitali ya Butimba Mwanza Wagoma Baada ya Madaktari Wenzao Kutumbuliwa Majipu

$
0
0

Siku chache baada ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo kuwasimamisha kazi wauguzi watano wa Hospitali ya Butimba wilayani Nyamagana Mkoani Mwanza kufuatia uzembe uliopelekea vifo vya watoto mapacha, madaktari wa hospitali hiyo jana waligoma kwa saa kadhaa.

Madaktari hao waligoma kutoa huduma kwa zaidi ya saa sita na kusababisha usumbufu mkubwa, wakidai kuwa wamekuwa wakinyanyaswa na kutishwa na watu wanaofika hospitalini hapo kupata huduma.Pia  wanadai watumishi wenzao waliosimamishwa kazi hawakupewa nafasi ya kujitetea

Akieleza sababu ya mgomo huo, Bi. Rechungula ambaye ni mmoja kati ya watoa huduma ya afya katika hospitali hiyo alisema kuwa wagonjwa wamekuwa wakikiuka taratibu za kupata huduma huku wakiwatishia na kuwasukuma kufanya kazi zao.

“Wagonjwa wanakuja hawataki kufuata utaratibu, wakifika mlangoni wanataka kuandikiwa kadi mara moja bila kufuata utaratibu. Na wakifika kwa daktari vivyo hivyo."  Alisema Bi. Rechungula

Alisema kuwa wagonjwa wamekuwa wakiwatishia kuwapiga endapo hawatawahudumia kwa muda wanaoutaka.

Kufuatia sakata hilo, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Baraka Konisaga alifika hospitalini hapo na kuwahakikishia usalama wauguzi hao, huku akitahadharisha watu wanaotaka kuhatarisha usalama. 

Alisema kuwa hakutakuwa na sababu ya kuweka ulinzi wa polisi kusimamia huduma hospitalini hapo bali hali ya amani inapaswa kuzingatiwa.

Baada ya kufanya kikao na wauguzi hao pamoja na Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, huduma zilirejea hospitalini hapo majira ya saa saba mchana.

 

==> Ingia Hapa kulisoma sakata zima la madaktari hao

Rais Magufuli Aanza Kuhujumiwa

$
0
0

SERIKALI ya Rais John Magufuli imeanza kuhujumiwa, wanaotajwa kuihujumu ni wafanyabiashara.

Wafanyabiashara wa sukari nchini wameanza kujenga utaratibu wa kuficha sukari ili kuibua malalamiko kutoka kwa wananchi lengo likiwa ni kushinikiza vibabali vya kuingiza sukari kutoka nje vinatolewa.

Hatua hiyo imemwibua Charles Mwijage, Waziri wa Viwanda na Biashara ambaye anakiri kuwepo kwa hujuma hizo na kudai, serikali haitalala.

Amesema, kuna wafanyabiashara wanaficha sukari kwenye maghala yao ili kuchochea mfumko wa bei na kisha waiuze kwa bei ya juu na hatimaye kupata faida kubwa.

Hivi karibuni Rais Magufuli alizuia kutolewa vibali holela vya uingizaji sukari nchini na kumwagiza Kasim Majaliwa, Waziri Mkuu kusimamia hilo.

Taarifa zilizopatikana zinaeleza kwamba, wafanyabiashara waliokuwa wananufaika na uingizaji wa sukari nchini wameanza kuhujumu kwa kushirikiana na wenye maghala ya sukari.

Mwijage amesema, wafanyabiashara hao wamekuwa wakificha sukari ghalani ikiwa pamoja na kufungia maghala yao ili kuzuia mfumuko wa bei na hatimaye kupata faida kubwa.

Amesema hayo katika mkutano na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam ambapo amewataka wananchi kutoa taarifa sahihi za baadhi ya watu wanaoendelea kuficha sukari kwa makusudi.

“Kama kuna taarifa sahihi za baadhi ya watu wanaoficha sukari ghalani kwa makusudi ili kuiaminisha jamii kuwa sukari ya ndani haikidhi na kupandisha bei holela ya sukari kwa masilahi yao binafsi muwataje,” alisema Mwijage.

Mwijage alisema kuwa, kwa dhamana aliyokuwa nayo katika Sekta ya Viwanda na Biashara anauwezo wa kufungia maghala yatakayobainika kuficha sukari kwa makusudi.

“Niwahakikishieni kuwa hakuna mfumuko wa bei ya sukari, mambo ni mazuri na utaratibu uko vizuri, niwasihi wawekezaji wa ndani wajitokeze kuwekeza katika viwanda vya sukari ili kuiendeleza nchi yetu,” alisema.

Alisema, Serikali inampango wa kujenga viwanda vya sukari vidogo na vikubwa ikiwemo ujenzi wa kiwanda kikubwa cha sukari kinachotarajiwa kujengwa hivi karibuni katika mkoa wa Kigoma.

Viwanda vya sukari vinakuja,nchi yetu si ya kupokea bidhaa hafifu, sukari isiyokidhi ubora haitaingia nchini wala kuuzwa na kutumiwa na watanzania,” alisema Mwijage.

Waziri Mkuu Ampa Zawadi Ya Laptop Ya Milionin 1.9 Mwanafunzi Wa Shule Ya Kata

$
0
0

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema shule za sekondari za kata zina fursa ya kufanya vizuri kama zilivyo shule nyingine licha ya kuwa watu wengi wamekuwa wakizidharau.

Ametoa kauli hiyo jana mchana (Jumatatu, Machi 7, 2016) wakati akikabidhi zawadi ya kompyuta mpakato (laptop) kwa mwanafunzi aliyeshinda shindano la kuandika insha katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC ). Kompyuta hiyo ina thamani ya sh. 1,992,000/-.

Mwanafunzi huyo, Jabir Mandando (20),  amehitimu kidato cha nne katika shule ya sekondari ya Mbekenyera iliyoko wilayani Ruangwa mkoani Lindi. Amepata ufaulu wa daraja la pili na sasa anasubiri matokeo ya kujiunga na kidato cha tano. Lakini aliandika insha hiyo mwaka jana wakati akiwa kidato cha nne.

“Huyu ni mtoto wa kijijini tu. Anatoka kijiji cha Namilema wilaya ya Ruangwa mkoa wa Lindi. Shule ya Mbekenyera aliyosoma ni shule ya kata. Ameweza kushinda tuzo na kushika nafasi ya tatu katika shindano lililoshirikisha shule nyingi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.”

“Jabir ameweza kuchomoza kitaifa kwa kushiriki shindano la kimataifa. Nimeamua kumpa zawadi ya laptop pamoja na begi lake ili aweze kujisomea  zaidi na kupata elimu ya masuala mbalimbali kwa kutumia kompyuta hii. Pia nataka iwe ni chachu kwa vijana wengine kushiriki mashindano kama haya,” alisema Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu pia alikabidhi Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Bw. Shanael Nchimbi fedha taslimu sh. 500,000/- zikiwa ni zawadi kwa ajili ya shule hiyo. mwalimu Nchimbi alimsindikiza mwanafunzi huyo Arusha kupokea zawadi hizo kwenye mkutano wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki uliomalizika Arusha wiki iliyopita.

Kwa upande wake, kijana Jabir alisema anashukuru sana kwa zawadi aliyopewa na kuahidi kuwa atajitahidi kusoma kwa bidii masomo ya kidato cha tano na sita ili aweze kutimiza ndoto yake ya kuwa daktari.

Alipoulizwa alipataje taarifa ya uwepo wa shindano hilo, Jabir alisema: “Walimu walipata taarifa wakazileta darasani na kutuambia tushiriki kuandika. Walizikusanya na kuchagua tatu bora, ndipo yangu ikashinda.”

Amesema insha aliyoiandika ilihusu: “The importance of political stability in the East African Integration.”

Alimwonyesha Waziri Mkuu cheti na dola za Marekani 200 ambavyo alipewa zawadi kutokana na ushindi huo. Shule ya Mbekenyera ambayo alikuwa akisoma, pia ilizawadiwa laptop na printer kutokana na ushindi wa kijana Jabir.

Mshindi wa kwanza katika shindano hilo ametoka shule ya Sekondari Mzumbe, mshindi wa pili  alitoka Kenya na wa tatu alitoka shule ya Mbekenyera.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021, 11410 DAR ES SALAAM.
JUMATATU, MACHI 7, 2016.

Paul Makonda Aibuka na Ubunifu Mwingine....Asema Anampango wa Kuanzisha Mtaa Maalumu Kinondoni Kwa Ajili ya Biashara ya Pombe ( Bar)

$
0
0
PAUL Makonda, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, ametangaza mpango mpya wa kuanzisha mtaa maalum utakaokuwa ukihusika na biashara ya uuzaji wa vinywaji vikali na baridi baa (bar).

Makonda ameweka wazi mpango huo jana jijini Dar es Salaam ikiwa pia ndiyo siku ambayo utekelezwa wa mpango wa walimu wa shule za msingi na sekondari kusafiri bure kupitia usafiri wa umma (daladala) ulianza rasmi.

Mkuu huyo wa wilaya alisema mpango huo ni muendelezo wa ubunifu na uthubutu wa mipango ya maendeleo ambao kwa kiasi kikubwa umekuwa ukikosekana miongoni mwa Watanzania na hivyo kufanya kasi ya maendeleo hapa nchini kuwa ndogo tofauti na matarajio ya wananchi.

“Kinondoni nina mpango wa kutengeneza mtaa mmoja maalum wenye bar tu ili watu wakitaka kwenda kunywa pombe waende mtaa huo bila kubugudhiwa. Nasubiri muda tu ufike kwa sababu haiwezekani kila eneo liwe na baa mpaka nyuma ya misikiti na nyuma ya makanisa,” alieleza Makonda.

Wilaya ya Kinondoni ndiyo wilaya yenye watu wengi zaidi hapa nchini ambapo kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 wilaya hiyo ina jumla ya watu milioni 1.7 na kwasasa ikikadiriwa kufikia watu milioni 1.9.

Balozi Ombeni Sefue Amshukuru Rais Magufuli Kwa Heshima Aliyompa......Aahidi Kutoa Ushirikiano kwa Katibu Mkuu Mpya

$
0
0

Baada ya kudumu Ikulu kwa takribani siku 127 zikiwamo 67 tangu aongezewe muda wa mwaka moja akiwa na Serikali ya Awamu ya Tano, Balozi Ombeni Sefue ameshukuru heshima aliyopewa na Rais John Magufuli kwa muda wote aliomsaidia kutekeleza majukumu yake ya ukatibu mkuu kiongozi na kueleza kuwa Serikali ya sasa ni ya mabadiliko. 

Wakati Sefue akiondoka, mhandisi John Kijazi amepokea kijiti cha ukuu wa utumishi serikalini na kuahidi kuwa atafuatilia mazingira ya watumishi wote pamoja na mazingira yao, ili kurekebisha panapohitajika kwa lengo la kuongeza uwajibikaji na tija kwa wananchi.

Akizungumza muda mfupi baada ya kuapishwa kwa mrithi wake, licha ya kumshukuru Rais, Balozi Sefue aliwataka watendaji wote serikalini kumpa ushirikiano wa kutosha Balozi Kijazi ili kuleta ufanisi kwenye huduma za umma.

“Namshukuru Rais kwa kuniamini kwa kipindi chote nilichodumu naye. Ni heshima kubwa kuwatumikia Watanzania pamoja naye. Nitampa ushirikiano wowote atakaouhitaji katibu mkuu kiongozi mpya kwenye utekelezaji wa majukumu yake,” alisema Sefue.

Rais Magufuli, ameahidi na mara zote amekuwa akisisitiza adhma yake ya kutumbua majipu kwa watumishi wote ambao hawaendani na kasi yake.

Tangu taarifa za mabadilio hayo zilipotangazwa jana, kumekuwepo na tetesi nyingi kuwa huenda Sefue naye ni jipu lilikuwepo ikulu, suala ambalo halikupata maelezo ya kutosha kutoka kwa balozi huyo.

Alipoulizwa juu ya tetesi hizo alijibu kwa ufupi: “Hii ni Serikali ya mabadiliko.”

Kwa upande wake Kijazi, alisema atafanya kazi kwa kuzingatia vipaumbele vya Rais huku akimshauri namna sahihi za kuboresha mazingira ya utumishi serikalini.

Akieleza juu ya majukumu yake mapya, alionyesha kuyatambua ipasavyo na kubainisha kuwa atashirikiana na Baraza la Mawaziri kwenye vikao vyao, bila kusahau kuzifuatilia wizara husika na kuona endapo kila kitu kinaenda kama inavyotakiwa.

“Nitakutana na mawaziri kwenye vikao vyao nitakavyoviandaa. Nitawasiliana na kuwafuatilia watendaji wa wizara husika juu ya masuala yatakayokuwa yamejitokeza ndani ya maeneo yao ya uwajibikaji. Kila mmoja atimize wajibu wake ili Taifa lisonge mbele,” alisema Kijazi. 

Ili kuitendea haki hadhi ya utumishi wa umma, Kijazi ameahidi kuhakikisha kila kitu kinasimamiwa kwa ukaribu huku akitoa msisitizo kwenye vipaumbele vya Rais.

 “Kwenye suala la mapato na rushwa, nitafuatilia kwa nguvu ili kuongeza uwajibikaji kwa watumishi wa Serikali,” alisisitiza Kijazi.

Balozi Kijazi aliteuliwa juzi kushika nafasi inayoachwa na Balozi Sefue. Kabla ya uteuzi huo, Kijazi alikuwa mwakilishi wa Tanzania kwa nchi za India, Singapore, Sri Lanka, Bangladesh na Nepal huku makazi yake yakiwa jijini New Delhi, India kuanzia mwaka 2007.

Katika wadhifa huo, alikuwa mkuu wa mabalozi wote wanaowakilisha Tanzania nje ya nchi pamoja na mkuu wa mabalozi wa Afrika nchini India. 

Kabla hajateuliwa kuwa mwakilishi wa nchi, Kijazi amekuwa mtumishi serikalini kwa nafasi mbalimbali ikiwamo Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi kuanzia mwaka 2002 mpaka 2006.

Kabla ya hapo alikuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Miundombinu kati ya mwaka 1996 hadi 2002.

Ndani ya Wizara ya Ujenzi, kabla hajawa katibu mkuu, alikuwa mhandisi mwandamizi wa ujenzi wa barabara kisha kupandishwa cheo na kuwa mkurugenzi wa barabara za mikoa.

Kumbukumbu za taaluma yake zinaonyesha kuwa alipata Sha hada yake ya kwanza ya Sayansi ya Uhandisi wa Umma mwaka 1982 kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na baadaye Shahada ya Uzamili katika Uhandisi wa Barabara kutoka Chuo Kikuu cha Birmingham, Uingereza mwaka 1992.

Jana wakati anaapishwa, saa 4:15 asubuhi, Kijazi alikuwa sambamba na mke wake, Fransiscar Kijazi na kwa pamoja wamejaliwa watoto watatu, David, Emmanuel na Richard. 

Kwa heshima ya familia hiyo, baada ya kukamilisha protokali, Rais Magufuli alipiga picha ya pamoja na familia ya mteule huyo mpya atakayehudumu ikulu kuanzia sasa.

Hata hivyo kwa mara ya mwisho, Sefue aliendelea na kazi yake mpaka jana asubuhi na ndiye aliyemkabidhi Kijazi kitabu kitakatifu cha Biblia, Katiba na kiapo cha uongozi ambacho alisaini. 

Maalim Seif Alazwa Hospitali ya Hindu Mandal jijini Dar es Salaam

$
0
0

Siku tatu baada ya kutoka India alikokwenda kwa ajili ya kupata matibabu, Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad jana alilazwa katika hospitali ya Hindu Mandal jijini Dar es Salaam.

Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Nassoro Mazrui amesema kuwa chanzo cha Maalim Seif kulazwa katika hospitali hiyo jana asubuhi ni uchovu wa safari yake ya India ambayo alienda kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji wa mgongo.

Mazrui alikanusha taarifa zilizokuwa zinaenezwa kwenye mitandao ya kijamii kuwa kiongozi huyo wa CUF alilazwa kutokana na matatizo ya moyo. Alisema kuwa hakuna kumbukumbu yoyote ya ripoti ya daktari inayoonesha kuwa Maalim Seif ana tatizo la moyo.

Naibu Katibu Mkuu huyo wa CUF alisema kuwa kiongozi huyo anaendelea vizuri kiafya na kwamba hayuko katika hali mahututi kama ilivyokuwa ikielezwa.

“Anakula na kufanya kila kitu mwenyewe na hata jioni hii nimeongea naye, anakula kila kitu, hivyo Watanzania wasiwe na wasiwasi juu ya afya ya Maalim Seif,” alisema Mazrui.

Viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa waliwasili katika hospitali hiyo kumjulia hali akiwemo aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba.

Mwanafunzi Aliyeongoza Kitaifa Matokeo Kidato cha Nne Aahidiwa Ajira Na Benki ya CRDB

$
0
0

Benki  ya  CRDB  imemfungulia  Akaunti  ya  Scholarship  na  kumwekea  sh. Milioni 5  mwanafunzi  aliyefanya  vizuri  katika  mtihani  wa  kumaliza  kidato  cha nne  mwaka  2015,  Butogwa Shija  na  kumwahidi  ajira  pindi  amalizapo  masomo.

Hafla  hiyo  ilifanyika  jana  jijini  Dar  es  Salaam  ikiwa  ni  kuelekea   kilele  cha maadhimisho  ya  siku  ya  wanawake  duniani  leo, ambapo Butogwa  alipewa  zawadi  ili  kuwahamasisha  watoto  wa  kike  kwamba  wanaweza.

Pia  Mamlaka  ya  Elimu Tanzania (TEA)  ilimuongezea  mwanafunzi  huyo  kiasi  cha  shilingi 500,000  lengo  likiwa  ni  kuwahamasisha  watoto  wa  kike  ili  kuleta  haki  sawa  kwa  wote.

Naye Butogwa  aliahidi  kutumia  fursa  hiyo  vizuri  kwa  kusoma  kwa  bidii  bila  kubweteka  na  kuwataka  wanafunzi  wengine  kuweka  bidii  kwenye  masomo  yao.

Katika hatua  nyingine, Naibu Mkurugenzi Mtendaji  wa  CRDB, Esther Kitoka  alisema   wametoa  sh. milioni 20  zitakazosaidia  katika  ujenzi  wa  mabweni  kwa  watoto  wa  kike  ili  kuongeza  kasi ya  ufaulu  kwa  wanafunzi


Wanafunzi wa UDOM Ambao ni Wafuasi wa Chadema Watishia Kuandamana

$
0
0

Umoja  wa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chaso), wametishia kufanya maandamano ikiwa Chuo Kikuu Cha Dodoma (UDOM), hakitamrejesha chuoni hapo mwanafunzi wa chuo hicho, Victor Byemelwa, aliyemsimamishwa  kwa kile  wanachodai ni sababu za  kisiasa.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaama jana, Mwenyekiti wa Umoja huo, Jafary Ndege, alisema wanataka chuo hicho kimrejesha masomoni haraka na kwamba ikiwa hawatafanya, hivyo wataandamana kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma kushinikiza arudishwe.

“Tunawataka viongozi wa chuo hicho kumrejesha shuleni mwanafunzi huyo na kama wataendelea kukaa kimya tutafanya maandamano makubwa ya kushinikiza chuo hicho kimrudishe masomoni mwenzetu na yataanzia  Dar es Salaam kwenda Dodoma katika siku ambayo tutatoa taarifa kwenye vyombo vya habari iwapo ombi letu litapuuzwa,” alisema mwenyekiti huyo.

Ndege aliitaka serikali kutoa onyo kwa wanasiasa na kuacha kuingilia utendaji wa vyuo vikuu kama ilivyotokea kwa chuo hicho na kusababisha kufukuzwa mwanafunzi huyo kupitia kwa mshauri wa wanafunzi kwa barua yenye kumbukumu no Re.UDOM/DOS/36 ya Februari 5, 2016.

Kuhusu, suala la kufutiwa usajili kwa vyuo vishiriki vya  St. Joseph Songea na Arusha, na baadhi ya vitivo katika Chuo Kikuu cha Kampala Dar es Salaam, alisema wameshangazwa na hatua hiyo iliyochukuliwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kwa kuwa imechangia kwa kiwango kikubwa kurudisha nyuma maendeleo ya wanafunzi wa vyuo hivyo.

Alisema kama TCU ilikuwa inafahamu kwamba havikuwa vimekidhi vigezo ni vema isingevipa usajili kuliko usumbufu unaotokea kwa wanafunzi hao hivi sasa.

Waziri wa Ardhi, William Lukuvi Akataa Rushwa ya Bilioni 5

$
0
0

Waziri wa  Ardhi, William Lukuvi amesema rushwa imekithiri kwenye sekta ya ardhi kiasi kwamba wafanyabiashara wawili walimuahidi rushwa ya Sh5 bilioni afanikishe mpango wao wa kuiuzia Serikali ardhi kwenye eneo linalotakiwa kujengwa mji wa kisasa wa Kigamboni.

Mji huo kabambe wa Kigamboni unajumuisha kata za Kigamboni, Tungi, Vijibweni, Mjimwema, Kibada, Somangila na eneo lote lina ukubwa wa takribani ekari 6,000.

Awali mradi huo ulitarajiwa kugharimu Sh13 trilioni ambazo zingetolewa na Serikali, lakini ikaamua kushirikisha sekta binafsi ili zishiriki kuujenga na Serikali ishughulikie uwezeshaji wa awali.

Lukuvi, ambaye alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu kwa takriban miaka mitano kabla ya kuhamishiwa Wizara ya Ardhi mapema mwaka jana na kubakizwa wizara hiyo na Rais John Magufuli, alitoa siri hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita.

Mbunge huyo wa miaka mingi wa Isimani mkoani Iringa alisema amegundua kuna mtandao mkubwa wa rushwa unaoanzia ngazi ya halmashauri mpaka wizarani ambao unahusisha maofisa wa Serikali na viongozi wa wizara.

Waziri Lukuvi alisema mtandao huo ni hatari na unaweza kusababisha mtu ashindwe kufanya kazi ya wananchi iwapo ataendekeza rushwa.

“Hapa (Wizara ya Ardhi) fedha ipo,” alisema Lukuvi ambaye amekuwa mbunge wa Isimani tangu mwaka 1995.

“Kama ukiwa na tamaa huwezi fanya kazi uliyotumwa. Kuna wakati walikuja wafanyabiashara wawili wakubwa na kutaka wanipe Sh5 bilioni ili nikubali kupitisha mradi wao wa mabilioni ya shilingi na walitangaza kwa marafiki zangu kuwa wangenipa fedha, lakini hapa hawawezi” alisema Lukuvi.

“Wakati naingia tu wizara hii, nilikuta harakati za kukamilisha mradi wa Kigamboni ukiwa katika hatua za mwisho na kila kitu kilikuwa kimekamilika. Lakini nilipopitia vizuri, nilikataa kuwalipa wafanyabiashara hao. Cha ajabu hazikupita siku mbili wafanyabiashara hao walipata taarifa wakaja mbio kutaka kuniona.”

Kwa mujibu wa Waziri Lukuvi, wafanyabiashara hao walitaka walipwe kiasi cha Sh141 milioni kwa kila ekari wakati wao walinunua ardhi kutoka kwa wananchi kwa Sh5 milioni kwa ekari, jambo ambalo alisema lilishapitishwa awali.

“Niligundua pale kuna udanganyifu na wizi mkubwa. Haiwezekani mwekezaji anunue kutoka kwa wananchi ekari moja kwa Sh5 milioni, kisha Serikali tumlipe Sh141 milioni kwa ekari kwa kuvuka pantoni tu. Ni wizi mkubwa. Kama kweli Serikali ina fedha hizo kwa nini tusimlipe mwananchi moja kwa moja?” alihoji.

Waziri Lukuvi alisema endapo njama hizo zingefanikiwa, Serikali ingetumia zaidi ya Sh84 bilioni kuwalipa wawekezaji hao hewa kwa kuwa mmoja anamiliki takribani ekari 200 na mwingine 400.

“Niliwaambia Serikali haiwezi kuwalipa fedha hizo na badala yake waende kuiendeleza ardhi wenyewe kulingana na mradi unavyotaka. Walitaka kutajirika kwa ujanja ujanja,” alisema Lukuvi.

“Eti walidai wamekopa benki kwa ajili ya mradi huo. Haiingii akilini mtu utumie Sh5 milioni, halafu uje uvune mabilioni ya fedha kwa kuvuka pantoni tu.”

Hata hivyo, Lukuvi alikataa kutaja majina ya wafanyabiashara hao.

Akiongea na gazeti moja la kila wiki mwaka 2013, Profesa Anna Tibaijuka, waziri aliyemtangulia Lukuvi kwenye wizara hiyo, alisema tayari kampuni mbili za Miworld kutoka Dubai na China Hope (China) zilishasaini mkataba wa maridhiano na Serikali wa kujenga nyumba takriban 20,900 kwenye eneo hilo.

Miworld ilisaini mkataba wa kujenga nyumba 5,000 wakati China Hope ilitaka kujenga nyumba 15,900 kwenye eneo hilo la mradi wa mji mpya.

Profesa Tibaijuka aliliambia gazeti hilo wakati huo kuwa wananchi wangefidiwa kwa bei za soko kwa mujibu wa sheria, akisema ekari moja ingefidiwa Sh141 milioni kwa ajili ya kumuwezesha kulipia gharama ya nyumba mpya mbadala.

Akizungumzia migogoro ya ardhi, Waziri Lukuvi alisema amegundua mingi inasababishwa na maofisa na viongozi wa wizara hiyo wasio waaminifu, lakini pia wawekezaji wenye tamaa ya kumiliki kiasi kikubwa cha ardhi hata kama hawana shughuli nayo.

“Nimegundua kuna watu hapa wanataka kumiliki ardhi kila sehemu. (Mtu huyo) Atafanya kila njia ashirikiane na watumishi wasio waaminifu ili wampatie eneo hata kama limeshauzwa,” aliongeza.

Lukuvi alisema wengi wao ni wafanyabiashara wenye asili ya Kiarabu na Asia ambao kwa muda aliokaa wizarani hapo amegundua wamehodhi  mashamba katika miradi yote ya viwanja au mashamba iwe ya halmashauri au wizara.

“Wanasiasa na viongozi wa Serikali wanaohodhi maeneo wapo, lakini siyo wengi ukilinganisha na hawa wafanyabiashara wengi wenye tamaa ambao wakishapata ardhi wanatumia kukopa mabilioni ya fedha ndani na nje ya nchi kisha wanawekeza katika miradi yao mingine ikiwamo kujenga majumba katika nchi za Dubai na Ulaya na kuyatelekeza maeneo hayo kuwa mapori hivyo kusababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi wasio na maeneo."

Akizungumzia matarajio yake, Waziri Lukuvi alisema endapo Rais John Magufuli ataendelea kumuweka katika wizara hiyo anatamani amalize migogoro yote baina ya wananchi katika kipindi cha miaka mitano

Chanzo:  Mwananchi

Stephen Wasira Amng’ang’ania Ester Bulaya......Wapiga Kura Wanne Wanaompigania Wawasilisha Upya Ombi la Kukata Rufaa

$
0
0

Wapigakura wanne wa Jimbo la Bunda Mjini mkoani Mara, wamekamilisha taratibu za kimahakama na kuwasilisha upya maombi ya kukata rufaa katika Mahakama ya Rufaa ya Tanzania kutokana na maombi yao ya awali kutupiliwa mbali Februari 24, mwaka huu.

Maombi hayo yamewasilishwa na wapigakura Magambo Masato, Matwiga Matwiga, Janes Ezekiel na Ascetic Malagila dhidi ya Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya, kuiomba mahakama hiyo kuwapa kibali cha kukata rufaa katika mahakama hiyo.

Wapigakura hao ambao wamekuwa wakimpigania aliyekuwa Waziri wa Chakula, Kilimo na Ushirika na mgombea ubunge wa CCM Jimbo la Bunda Mjini, Stephen Wasira, waliwasilisha maombi ya kufungua shauri katika Mahakama ya Rufaa ya Tanzania ili itoe ufafanuzi kuhusu haki ya mpigakura ya kuhoji matokeo pamoja na vigezo vinavyotakiwa ili aweze kuhoji matokeo ya uchaguzi.

Maombi yao ya awali yalitupiliwa mbali na Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Sirilius Matupa kutokana na kuwasilishwa sura 141 ya sheria ya rufaa na kueleza kuwa yalikuwa yamewasilishwa chini ya kifungu cha 15 (a) (b) badala ya kifungu 15 (c) ambacho ndiyo sahihi kwa ajili ya maombi hayo na kuwaeleza wanaweza kurekebisha na kuyawasilisha upya.

Januari 25, mwaka huu Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Mohamed Gwae, aliitupilia mbali kesi namba moja ya kupinga matokeo ya Uchaguzi Jimbo la Bunda Mjini iliyofunguliwa na wapigakura hao dhidi ya Bulaya.

Wakati huo huo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Sumbawanga, Kakusulo Sambo anayesikiliza kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi Jimbo la Nyamagana, amekutana na mawakili wa pande zote na kuweka mikakati ya namna ya kuiendesha.

Jaji Sambo amekutana jana na mleta maombi (Ezekiel Wenje), mjibu maombi wa kwanza (Stanslaus Mabula) pamoja na mawakili wanaowawakilisha kuweka mikakati ya uendeshwaji wa kesi hiyo ikiwa ni pamoja na kubainisha sehemu zinazobishaniwa.

Akizungumzia hatua hiyo, Wakili Deya Outa anayemwakilisha Wenje, alisema katika kikao hicho wamebainisha sehemu zinazobishaniwa na pande zote katika kesi hiyo pamoja na mashahidi watakaotakiwa kufika mahakamani kutoa ushahidi.

Serikali Yatoa Bei Elekezi ya Sukari..... Kilo moja Kuanzia sasa ni Sh. 1800 Nchi Nzima

$
0
0
HATIMAYE  Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli  imekisikia kilio cha muda mrefu  cha Wananchi ambao  walikuwa wakilalamika kupanda  kwa  bei ya sukari nchini.

Akizungumza na Waandishi wa Habari  mchana huu  jijini Dar es Salaam Mkurugenzi  mkuu wa Bodi ya Sukari nchini,Henry Semwaza amesema kuanzia sasa kilo moja ya  sukari itauzwa sh.  1800 nchi nzima.

"Serikali, kupitia bodi ya Sukari Tanzania, inawaarifu wananchi wote kuwa bei ya rejareja ya sukari sasa itakuwa sh. 1,800 kwa kilo moja
. "Amesema Semwaza na kuongeza;

" Wafanyabiashara wote wanapaswa kuzingatia agizo hili, pamoja na kuhakikisha kuwa sukari inaendelea kusambazwa na kuuzwa kwa wananchi bila kuihodhi.

"Maafisa biashara wa mikoa na wilaya watafuatilia na kusimamia utekelezaji wa agizo kuhusu bei elekezi ya sukari, na hawatasita kuchukua hatua stahiki za kisheria kwa wale watakaobainika kupandisha bei ya bidhaa hiyo. "



Maalim Seif Sharif Hamad azungumzia hali ya afya yake leo

$
0
0
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akizungumza na waandishi wa habari katika hospitali ya Hindu Mandal Jijini Dar es Salaam kuelezea maendeleo ya afya yake.

Amesema anaendelea vyema baada ya jana kuugua ghafla na kulazwa katika hospitali hiyo.

Amewashukuru wananchi ndani na nje ya nchi kwa kuonesha mapenzi na ushirikiano makubwa.

Anatarajiwa kutoka hospitalini hapo leo jioni (Picha na Salmin Said, OMKR)


Waziri mkuu Kassim Majaliwa Asema Tatizo la Rushwa Barani Afrika Limesababisha Bara hilo Lipoteze dola za Bilioni 150 kila Mwaka.

$
0
0

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema tatizo la rushwa barani Afrika limesababisha bara hilo lipoteze dola za Marekani bilioni 150 kila mwaka.

Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumanne, Machi 8, 2016) wakati akihutubia wajumbe wa mkutano wa tano wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) linaloendesha vikao vyake jijini Dar es Salaam. Mkutano huo ulioanza Machi 6, utamalizika Machi 18, mwaka huu.

Akizungumza kwa niaba ya Rais Dk. John Pombe Magufuli, Waziri Mkuu alisema rushwa imechangia kwa kiasi kikubwa kurudisha nyuma maendeleo ya Jumuiya hiyo. "Rushwa yaweza kuwa kwa njia kuhonga fedha, kupata fedha kwa kula njama, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, ama kwa njia za vitisho," alisema.

"Kwa mujibu wa taarifa ya Umoja wa Afrika (AU), rushwa na urasimu vimeainishwa kuwa ni vikwazo vikubwa vinavyochangia kuchelewesha ufanyaji wa biashara kwenye mipaka ya nchi za Jumuiya yetu," alisema.

Amesema sekta binafsi inachukuliwa kama injini ya maendeleo na ukuaji wa uchumi na akatumia fursa hiyo kuipongeza jumuiya ya wafanyabiashara wa Afrika Mashariki kwa kuandaa kanuni za kiutendaji  ambazo zimelenga kuhamasisha uadilifu kwenye ufanyaji biashara unaozingatia haki za binadamu, sheria za kazi, utunzaji mazingira na vita dhidi ya rushwa.

Akizungumzia kuhusu uondoaji wa vikwazo visivyohusisha kodi (non-tariff barriers) kama njia mojawapo ya kuimarisha biashara kwenye jumuiya hiyo, Waziri Mkuu alisema kwa upande wa Tanzania, vizuizi vya barabarani kwenye barabara kuu ya Kaskazini vimepunguzwa kutoka 50 hadi vitano.

Alivitaja vizuizi vitano vilivyobakia kuwa ni vile vilivyopo kwenye mizni ya Mikese (Morogoro), Nala (Dodoma), Njuki (Singida), Mwendakulima (Shinyanga) na Nyakahura (Kagera).

"Sheria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya uondoaji wa vikwazo visivyohusisha kodi ilipitishwa Machi 2015 na sasa hivi inaendelea kusainiwa na Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Pamoja na mambo mengie, nia ya sheria hii ni kuondoa vikwazo vinavyosababisha uagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi na uuzaji wa bidhaa nje ya nchi, kurahisisha sheria za biashara ndani ya Jumuiya yetu," alisema.

Akizungumzia kuhusu miradi ya uwekezaji ya Jumuiya hiyo, Waziri Mkuu alisema miradi ya ujenzi wa barabara inahitaji kiasi cha dola za marekani bilioni 20; ukarabati na upanuzi wa njia za reli unahitaji dola za marekani bilioni 30; uendeshaji wa mashirika ya ndege na viwanja vya ndege unahitaji dola za marekani bilioni 15; uendelezaji bandari na usafiri wa majini unahitaji dola za marekani bilioni 10; utekelezaji wa miundombinu ya nishati inahitaji dola bilioni 5 ambavyo kwa pamoja vinahitaji dola marekani bilioni 80.

Alisema kuwepo kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi ndani ya jumuiya hiyo, kunaifanya Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhesabika kuwa ni jumuiya yenye nguvu kubwa ya kiuchumi barani Afrika.

Mfumuko wa bei wa Taifa kwa mwezi Februari 2016 wapungua kwa asilimia 5.6

$
0
0

Mfumuko wa bei wa Taifa kwa Februari, umepungua kutoka asilimia 6.5 za Januari hadi 5.6 kutokana na kupungua kwa kasi ya upandaji wa bei za bidhaa za vyakula, matunda, mafuta ya dizeli, vinywaji na samaki.

Hata hivyo, akitangaza takwimu hizo jana, Mkurugenzi wa Sensa za Jamii na Takwimu za Uchumi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Ephraim Kwesigabo alisema; “hii inamaanisha kwamba kasi ya upandaji wa bei za bidhaa na ununuzi kwa mwaka ulioishia Februari ndiyo imepungua wala siyo kushuka kwa bei. Naomba lieleweke hapo. Mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa Februari umepungua kutoka asilimia 10.7 ya Januari hadi 9.5 Februari,” alisema.

Kwesigabo alisema kupungua kwa mfumuko huo kumechagizwa na kupungua zaidi kwa bei za baadhi ya bidhaa ya vyakula na zisizo za vyakula kwa kipindi kilichoishia Februari. 
 
Alitaja mwenendo wa baadhi ya bei za bidhaa zilizoonyesha kupungua kuwa ni gesi asilimia 10.3, dizeli asilimia 4.5 na matunda asilimia 7.2.

Maalim Seif Aruhusiwa Kutoka Hospitali.....Asema Afya Yake Kwa Sasa Imeimarika

$
0
0

Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad aliyelazwa juzi katika Hospitali ya Hindul Mandal aliruhusiwa jana akisema amepona na anaweza hata kushiriki mashindano ya mbio hadi Kibaha. 

Maalim Seif juzi alilazwa katika hospitali hiyo baada ya kuugua ghafla akiwa kwenye ndege akitokea Zanzibar kuja Dar es Salaam na aliondoka hospitalini hapo jana saa 12.30 jioni.

Akizungumza wa waandishi wa habari, makamu huyo wa kwanza wa Rais wa Zanzibar alisema madaktari wa hospitali hiyo wamemhudumia vizuri na alianza kupata nafuu baada ya saa tatu, tangu alipofikishwa hospitalini hapo
 
“Kama mnavyoniona niko ‘fit’, nimelala usingizi mzuri leo na hali yangu imerudi kama kawaida, naweza hata kufanya mashindano ya kukimbia,” alisema baada ya kuteremka kutoka ghorofa ya tatu alikolazwa hadi chini kwa lengo la kuwaeleza waandishi wa habari kuhusu afya yake. 

Maalim Seif ambaye alikuwa akitembea kwa ukakamavu, alisema amejisikia faraja baada ya watu wengi kutaka kufahamu maendeleo ya afya yake. 

“Watanzania na Wazanzibari waliopo ndani na nje ya nchi wameonyesha mahaba makubwa kwangu kwa namna wanavyoendelea kufuatilia afya yangu, ninawashukuru sana,” alisema.

 Akisimulia namna alivyougua, Maalim Seif alisema hali yake ilianza kubadilika akiwa katika Uwanja wa Ndege wa Zanzibar akielekea Dar es Salaam. 

“Nilitoka nyumbani jana (juzi) nikiwa mzima wa afya, baada ya kuugua ghafla uwanja wa ndege, niliamua kuendelea na safari kwa kusaidiwa na wasaidizi wangu. Tuliamua kuja Hindu Mandal kwa ajili ya vipimo na matibabu,” alisema. 

Alisema madaktari waliamua alale hospitali hapo ili akupata uangalizi wa karibu. 

Kuhusu safari yake ya India, alisema; “namshukuru Mungu nimerudi salama na Ijumaa iliyopita nikapata mapokezi makubwa Zanzibar. "

Daktari wa Maalim Seif, Dk Omar Suleiman alisema makamu huyo wa Rais, alipata kizunguzungu na madaktari walipomfanyia uchunguzi hawakuona ugonjwa wowote hivyo walisema kizunguzungu hicho kilitokana na uchovu. 

“Kwa hiyo matibabu na kusafiri muda mrefu kutoka India hadi Zanzibar, alihitaji muda mrefu wa kupumzika, nadhani ndiyo maana amepata kizunguzungu,” alisema. 

Kama ilivyo kawaida kwa viongozi mbalimbali kutembelea wenzao wanapokuwa hospitali, jana ilikuwa tofauti kwa Maalim Seif baada ya kutoonekana kiongozi yeyote wa Serikali ya Zanzibar wala wa Muungano.

Viongozi waliomtembea ni wa CUF, akiwamo Naibu Katibu Mkuu, Nassor Ahmed Mazrui na Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano ya Umma, Ismail Jussa.

Wafanyakazi 597 Waliosimamishwa Kazi NIDA Waandamana Kudai Haki Zao

$
0
0

Wafanyakazi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), wameandamana kupinga kitendo cha mamlaka hiyo kuvunja mikataba yao huku wakidai mishahara ya miezi mitatu.

 Wafanyakazi hao walichukua hatua hiyo jana, siku moja baada ya Kaimu Mkurugenzi wa Nida, Dk Modestus Kipilimba kutangaza kuvunja mikataba ya wafanyakazi 597 kwa sababu ya ufinyu wa bajeti na kuongeza ufanisi katika mamlaka hiyo. 

Alipoulizwa kuhusu madai hayo, Dk Kipilimba alikiri wafanyakazi kudai mishahara yao ya miezi mitatu na kuwa ameshapeleka maombi ya fedha serikalini na muda wowote watawalipwa stahiki zao. 

Wafanyakazi hao walisema mkurugenzi huyo amefanya uamuzi huo kwa kukurupuka bila kukaa nao na kuzungumza jinsi gani watalipwa stahiki zao kabla ya kuvunjwa kwa mkataba huo. 

Mtaalamu wa takwimu, Joseph Mtitu alisema alishangazwa na taarifa za kuvunjiwa mkataba wake wakati anadai mishahara ya miezi mitatu. 

Kijana huyo ambaye alikuwa anafanya kazi ya kuingiza taarifa za wananchi kwenye mfumo wa data, alisema mkurugenzi amefanya kazi na vyombo vya habari badala ya kukaa na wafanyakazi wake. 

“Hajafuata taratibu, alitakiwa kutupa taarifa na kuhakikisha kwamba anamaliza madeni yote ndipo avunje mikataba... hatumuelewi,” alisema Mtitu. 

Kijana huyo alisema waathirika wengi kati ya waliovunjiwa mikataba ni vijana ambao wengine wana familia zao akisema kitendo hicho kinaweza kusababisha baadhi yao kujiingiza kwenye vitendo vya ujambazi na ukahaba ili kuendesha maisha yao. 

Mfanyakazi mwingine, Bhoke Mafube alisema Nida imekuwa ikiwakata fedha za mifuko ya jamii ambako walijiandikisha, lakini wakienda kuuliza huko wamekuwa wakiambiwa wao si wanachama na fedha zao hazipo.

Akizungumzia sababu ya ufanisi mdogo, Peter Michael alisema tatizo hilo siyo lao, bali ni ufinyu wa rasilimali uliosababishwa na uongozi wenyewe. 

Hata hivyo, alisema hiyo si sababu ya kukiuka taratibu na haki za wafanyakazi kwa kuvunja mikataba yao kwa kuwa wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu. 

“Tumekuja hapa viongozi hawataki kuzungumza, sijui tutafikiaje muafaka kama wanafanya hivi. 

"Sisi siyo watoto wadogo, madai yetu ni ya msingi. Watulipe mishahara yetu ndiyo tuanze kujadili uhalali wa kuvunja mkataba,” alisema mfanyakazi huyo wa Nida. 

Akifafanua madai hayo, Dk Kipilimba alisema mamlaka yake haina fedha kwa sasa ndiyo maana ameamua kuvunja mikataba ya wafanyakazi hao. Alisema njia pekee ilikuwa ni kuvunja mikataba hiyo ili deni lisiendelee kuongezeka.

 Alisisitiza kwamba haki ya mtu haipotei na kuwa atasimamia kikamilifu suala hilo ili kila mfanyakazi apate haki yake.

 “Ni kweli kwamba wafanyakazi hao hawakulipwa mishahara yao ya miezi mitatu kwa sababu hakuna fedha. Nitahakikisha wanalipwa fedha hizo lakini kwa sasa hakuna kazi. 

"Hebu fikiria, tuna kompyuta 150 tu wakati wafanyakazi hao wako 597, hatuwezi kwenda,” alisema Dk Kipilimba. 

Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa lengo la mamlaka yake ni kutengeneza vitambulisho vya kila mwananchi na siyo kutoa ajira kwa watu hata kama hakuna kazi za kufanya.

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu Ataka Makahaba wanaojiuza Pamoja na Wanaume Wanaowanunua Wakamatwe

$
0
0
WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imetangaza kuiunga mkono Polisi nchini katika operesheni ya kukamata wateja wa makahaba kuhakikisha biashara hiyo inakoma nchini.

Waziri wa wizara hiyo, Ummy Mwalimu alisema takwimu zinaonesha wanawake ndio waathirika wakubwa wa ugonjwa wa Ukimwi, ambapo kati ya Watanzania 10 wanaopimwa, sita ni wanawake na wanaume ni wanne pekee.

Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani Dar es Salaam jana, Ummy alisema si haki kuwakamata wanawake wanaojiuza na kuwaacha wateja wao ambao ni wanaume.

“Ninalipongeza Jeshi la Polisi kwa hatua hiyo kwa sababu imeonesha kutoegemea upande mmoja kwa kuwakamata wanawake makahaba. Wote wanaojiuza na wanaonunua huduma hiyo ni wakosaji wanaostahili kuchukuliwa hatua za kisheria.Tunaungana na Polisi kushiriki operesheni hiyo,” alisema.

Alieleza kuwa, biashara ya ukahaba inayofanywa na wanawake isingekuwepo endapo wateja wasingekuwepo, hivyo, wateja wanastahili kukamatwa pia kwa sababu ndio wanaoichochea.

Ummy alisema familia nyingi zina misukosuko na wanawake wengi wamekuwa wakiteseka na wengine kuambukizwa magonjwa na waume zao wanaoshiriki biashara hiyo.

Katika hatua nyingine, alisema sasa wanataka kuona idadi ya wanaume wateja wa biashara hiyo inatajwa sambamba na ya wanawake wanaokamatwa nao ili ndugu na wake zao wafahamu kuhusu tabia yao hiyo.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadiki, alisema hatua ya kukamata wateja na wauza miili imetokana na makubaliano yaliyofikiwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Dar es Salaam.

Mawaziri Watano Kikaangoni

$
0
0

Siku 87 tangu Rais John Magufuli awaapishe, mawaziri watano  wa Baraza la Mawaziri la Serikali ya Awamu ya Tano wako kwenye msukosuko kutokana na kutajwa, kuhusishwa ama kufanya uamuzi wenye dalili za majipu.

Mawaziri hao, George Simbachawene, Profesa Sospeter Muhongo, Jenister Mhagama, Harison Mwakyembe na January Makamba wamekuwa wakihusishwa na kufanya uamuzi bila ya kufuata kanuni, kufanya mipango ya kuwezesha mgeni kupata zabuni za ujenzi, kufanya uteuzi kinyume na taratibu na kustua watendaji wajiandae kukabiliana na ziara za kustukiza za viongozi wakuu wa Serikali.

Rais John Magufuli, ambaye amekuwa akiwawajibisha watendaji wa umma tangu aapishwe Novemba 5, 2015, alishasema kuwa hataonea aibu yeyote atakayeonekana kutokwenda na kasi yake, msimamo unaowaweka mawaziri hao kwenye hali ngumu wakati huu ambao tuhuma dhidi yao zinashamiri.

Hadi sasa, Serikali haijatoa tamko kuhusu tuhuma zilizoibuliwa dhidi yao, wakati Rais amekuwa hatabiriki katika uamuzi wake na hali hiyo aliizidisha Jumapili alipomuondoa Ombeni Sefue siku 67 baada ya kumteua tena kuendelea na nafasi ya Katibu Mkuu Kiongozi.

 Simbachawene, ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi) amekuwa akitajwa kwenye sakata la ununuzi wa mafuta ya mwezi Septemba, Oktoba na Novemba mwaka 2015 bila ya kushindanisha zabuni na hivyo kusababisha aliyepewa kazi hiyo kupandisha bei kwa Sh40 bilioni.

Mbunge huyo wa Mpwapwa, ambaye alikuwa Waziri wa Nishati na Madini wakati huo, alijitetea kuwa alichukua uamuzi huo kutokana na wasiwasi wa usalama baada ya Uchaguzi Mkuu na sheria inamruhusu kufanya hivyo.

Hata hivyo, Ewura ilisema wakati Waziri Simbachawene anafikia uamuzi huo tayari kulikuwa na zabuni mezani na walitoa ushauri wao.

Ewura ilisema ununuzi huo umesababisha bei ya mafuta kutoshuka kwa kadiri inavyotakiwa na hivyo kuwafanya Watanzania wasinufaike na kuporomoka kwa bei ya nishati hiyo duniani.

Profesa Muhongo anatajwa kuhusika katika sakata la uwashwaji wa mita ya kupimia mafuta kwenye Bandari ya Dar es Salaam siku moja kabla Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kutembelea eneo hilo.

Mita hizo zilikuwa zimezimwa kwa takriban miaka mitano kwa madai kuwa ilikuwa ikipunja wafanyabiashara, lakini iliwashwa kabla ya ziara hiyo baada ya Profesa Muhongo kudaiwa kumtaka bosi wa Wakala wa Vipimo, Magdalena Chuwa kuziwasha siku moja kabla ya ziara ya Majaliwa.

“Mita imeanza kufanya kazi jana kutokana na maagizo yaliyotolewa ngazi za juu, nilitumiwa meseji (ujumbe mfupi) kutoka kwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Muhongo.Aliagiza ianze kazi ndani ya saa 24,” alisema Chuwa alipoulizwa na Majaliwa kuhusu kuwaka kwa mita hizo.

Kwa nyakati tofauti, Profesa Muhongo amelitolea ufafanuzi suala hilo akisema kuwa mita hizo zinamilikiwa na wakala wa vipimo ambao uko chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara.

Waziri mwingine, Mhagama ambaye anaongoza Wizara ya Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, alifanya uteuzi wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Dk Carina Wangwe, lakini saa tano baadaye alilazimika kutengua “kutokana na kutokamilika kwa baadhi ya taratibu”.

Nafasi ya bosi huyo NSSF imezingirwa na mbigiri na hadi sasa haijapata mrithi wala kaimu wake. Dk Wangwe, ambaye ni Mkurugenzi wa Tehama wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Hifadhi ya Jamii (SSRA), aliteuliwa kushika nafasi hiyo Machi 3 saa 11:15 jioni na kutenguliwa siku hiyo hiyo saa 4:15 usiku.

Aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alitolea ufafanuzi suala hilo kwamba uteuzi huo ulikosewa na Dk Wangwe aliteuliwa kuwa mwangalizi tu, siyo kaimu mkurugenzi mkuu.

“Kiswahili cha neno caretaker (mwangalizi) kilikosewa na kuandikwa kaimu mkurugenzi mkuu na hiyo imetokea wakati ambao taratibu za kupata kaimu hazijakamilika.Kutokana na mkanganyiko huo, waziri aliamua kutengua tu,” alisema Balozi Sefue.

Sakata jingine linamuhusisha January, ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais.

Waziri huyo kijana anatajwa kwenye tuhuma zinazomuhusisha dada yake, Mwamvita za mipango ya kumtafutia zabuni raia wa Italia, Vincenzo Cozzolino kwa kutumia nafasi za kisiasa. Zabuni niyo ni ya ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo, ambao umesimamishwa kwa muda kutafuta fedha.

Tuhuma hizo zimetanda kwenye baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya jamii, ingawa wawili hao wamekanusha kuhusika lakini wanakiri kuwapo kwa uhusiano baina ya Mwamvita na Cozzolino uliohusisha kupeana fedha.

January alisema kuwa raia huyo wa Italia alikuwa na urafiki na dada yake, lakini anashangazwa na kitendo cha kutajwa jina lake katika suala hilo.

Cozzolino amenukuliwa katika vyombo vya habari akikanusha January kuhusika katika suala hilo, huku katika mitandao ya kijamii kukiwa na taarifa zinazoonyesha mawasiliano kati ya Mwamvita na raia huyo wa Italia.

Chanzo cha taarifa hizo ni sauti za mazungumzo baina ya Cozzolino na Mwamvita zilizorekodiwa kupitia akaunti ya Instagram ya mmoja wa watu wanaomfahamu Mwamvita, kisha kusambazwa kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii.

January pia yumo kwenye sakata la mawaziri watano walioshindwa kujaza fomu za mali wanazomiliki lililobainika Februari 25, mwaka huu.

Kwa upande wake  Dr Mwakyembe,anatuhumiwa akiwa Waziri wa Uchukuzi katika Serikali ya Rais Mstaafu Jakaya Kikwete, wizara yake iliingiza mabehewa feki 25  na kuisababishia serikali hasara ya mamilioni ya pesa. Sakata hilo la mabehewa  limewafikisha baadhi ya watumishi mahakamani

Viewing all 45270 articles
Browse latest View live




Latest Images