Quantcast
Channel: MPEKUZI
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live

Majambazi Yaua Polisi Tanga

0
0

Askari wa jeshi la polisi Koplo George Braiton aliyepigwa risasi na majambazi wakati akikabiliana nao katika tukio la ujambazi lililotokea barabara ya sita na saba jijini Tanga amefariki dunia.

Koplo Braiton amefariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya Mkoa wa Tanga,Bombo, akiwa na watu wengine wawili waliopigwa risasi katika tukio hilo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga ACP.Mihayo Msikhela amesema kuwa bastola ilitumika kupoteza uhai wa Koplo George Braiton wa kituo cha polisi Chumbageni na kujeruhi raia wengine wawili ambao bado wanaendelea na matibabu katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Tanga.

Polisi wamesema walifanikiwa kuwakamata majambazi hao wakiwa na bastola waliyoitumia kwenye tukio hilo pamoja na visu wanavyovitumia kwenye matukio ya kihalifu.

Majirani waliokuwa wakiishi na Koplo Braitoni wamesema tukio hilo limewagusa,lakini wakaiomba jamii kuwafichua wahalifu kwa lengo la kukabiliana na vitendo hivyo.

Kolpo Braitoni anatarajiwa kusafirishwa kupelekwa mkoani Mara Februari 16 kwa ajili ya mazishi.

Museveni: Nimeandaa Mrithi wa Mashamba Yangu Lakini Sio Mrithi wa Uganda.....Hakuna Chama Cha Kutuondoa Madarakani

0
0

Rais wa Uganda Yoweri Museveni amesema kwamba ameandaa mrithi wa shamba lake lakini sio mrithi wa Uganda na Waganda watachagua mtu wa kuwaongoza pale ambapo yeye atastaafu wadhifa huo.

Museveni ameyasema hayo kipindi ambapo kampeni za lala salama zinaendelea nchini Uganda na uchaguzi wa kumpata Rais wa nchi hiyo unafanyika siku ya Alhamisi ya wiki hii.

Rais Museveni ambaye amedumu madarakani kwa muda wa miaka 30 anatetea tena nafasi yake hiyo huku akitamba kuwa hakuna chama chenye uwezo wa kuweza kushinda chama chake cha National Resistance Movement (NRM)

“Sidhani vyama vya upinzani vitashinda NRM. Kwa sababu tunajua nguvu yetu. Tunajua tutashinda, lakini kama itakuwa tumeshindwa basi tutawaachia wale ambao wameshinda. Lakini sidhani kuna chama kinaweza kushinda NRM wakati huu,” amesema

Aidha kwa sasa katiba inaeleza umri wa juu zaidi wa Rais kuwa madarakani ni miaka 75. Kwa sasa Rais Museveni anakaribia kutimiza umri wa miaka 72 ikimaanisha kwamba katika mwaka wake wa mwisho wa muhula ujao iwapo ataingia madarakani, atakuwa na umri wa miaka 76.

Chanzo BBC

Magufuli Ataka Bandari Zilindwe Na Jeshi La Polisi Kama Ilivyokuwa Hapo Awali

0
0

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amelitaka jeshi la polisi nchini kurejesha kitengo cha ulinzi bandarini na pia eneo ambalo linafungwa mita za mafuta.

Taarifa ya Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue, imesema Rais Magufuli ametaka jeshi la polisi nchini kurejesha ulinzi kama ilivyokuwa nyakati za nyuma kabla mamlaka ya bandari haijaamua kubandilisha mfumo wa kuweka walinzi wake.

Balozi Ombeni Sefue ameongeza kuwa katika eneo ambalo linafungwa mita za mafuta (Flowmeters), ambalo waziri mkuu alitembelea na kumsimamisha mkurugenzi wa wakala wa vipimo sasa ni lazima lilindwe na jeshi la polisi.

Waziri wa Elimu Amfuta Kazi Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi Ya Mikopo ya Wanafunzi Pamoja na Wakurugenzi Wengine Watatu

0
0
Waziri wa Elimu Sayansi, Teknolojia na ufundi, Prof Joyce Ndalichako amesitisha mkataba wa kazi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo  George Nyatenga (Pichani  chini). 

Pia amewasimamisha kazi wakurugezi watatu wa Bodi hiyo ambao ni Mkurugenzi wa Fedha na Utawala Yusufu Kisare, Mkurugenzi wa Urejeshaji Mikopo Juma Chagonja na Mkurugenzi wa Upangaji na Utoaji Mikopo. 

Prof Ndalichako  amemwagiza Mkaguzi wa ndani Mkuu wa Serikali ahakiki maelezo na Nyaraka zilizowasiliwa na Bodi ya Mikopo pamoja na kufanya ukaguzi maalum kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2013 hadi sasa.

Bomba Kubwa La Kusambazia Maji Kutoka Chanzo Cha Maji Cha Ruvu Chini Lafika Jijini Dar Es Salaam

0
0
Juu na Chini - Mafundi wakiendelea na kazi ya kulaza mabomba ya Maji eneo la Mbezi Beach jijini Dar es salaam. Mabomba hayo ambayo sasa yamekamilika kwa urefu wa kilometa 54.8 kati ya 55.9 yatatumika kusafirisha maji kutoka mtambo wa kuzalisha maji wa Ruvu Chini, Bagamoyo mkoani Pwani.


( Na. Aron Msigwa - Dar es salaam)
Huduma ya Usambazaji wa Maji Safi katika jiji la Dar es salaam inatarajiwa kuimarika kwa kuwafikia wananchi wengi zaidi mwishoni mwa mwezi Februari mwaka huu kufuatia kukamilika kwa kilometa 54.8 za mradi wa Ujenzi wa Bomba kubwa la kusambazia Maji kutoka chanzo cha Maji cha Ruvu Chini.

Mradi huo unajengwa na Kampuni ya JBG Gauff Ingenieure kwa gharama ya shilingi Bilioni 141 ambazo zimetolewa na Serikali ya Tanzania una jumla ya urefu wa kilometa 55.9.

Akizungumzia mradi huo leo jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa Usimamizi na Ufundi wa DAWASA, Romanus Mwang’ingo amesema kuwa mpaka sasa ujenzi wa bomba hilo kuelekea matangi ya kuhifadhia maji ya Chuo Kikuu cha Ardhi umefika eneo la Mbezi Beach jijini Dar es salaam na huku ikiwa imebakiza kilometa 1.1.

 Amesema ujenzi wa mradi huo kutoka mtambo wa Ruvu Chini ndiyo utakuwa suluhisho la tatizo la maji katika jiji la Dar es Salaam na maeneo ya mkoa wa Pwani na kuongeza kuwa utakapokamilika utazalisha lita milioni 270 kwa siku kutoka lita milioni 182 ambazo zote zitasukumwa kuja jijini Dar es salaam.

 Aidha, amesema kasi ya mkandarasi ya kulaza bomba hilo inaridhisha licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali zinazochelewesha kazi hiyo zikiwemo za ufinyu wa eneo linapojengwa bomba hilo kuwezesha mitambo kufanya kazi vizuri katika eneo la mbezi Beach, mvua zinazoendelea kunyesha ,changamoto ya makazi ya watu kuwa ndani ya mradi ambapo kulikuwa na kesi 17 Mahakamani zikihusisha madai mbalimbali ya wananchi katika maeneo hayo.

“Ni kweli zipo changamoto zilizosababisha mradi kukawia kumalizika zikiwemo za wananchi kufungua kesi 17  Mahakama ya Ardhi, hadi sasa DAWASA tumeshinda kesi 14  ndiyo maana tumepata haki ya kutumia njia hii kukamilisha upanuzi wa mradi” Amesema Mwang’ingo.

Ameongeza kuwa lengo la mradi huu nikuongeza uzalishaji wa maji na kuboresha huduma kwa wakazi wa maeneo ya uwekezaji (EPZ) Bagamoyo, Chasimba, Buma, Zinga, Kerege na Mpiji mkoa wa Pwani.

Maeneo mengine yatakayonufaika na mradi huo kwa Mkoa wa Dar es Salaam ni Bunju, Wazo, Salasala, Madale na Kinzudi Mbezi Juu, Goba, Kawe, Makongo, Mwenge, Msasani, Mikocheni, Mlalakua, Masaki, Sinza, Kijitonyama, Manzese, Konondoni, Magomeni, Kigogo na Vingunguti.

Kwa upande wake Meneja Mradi wa Kampuni inajenga bomba hilo nchini Muhandisi Eric Omuruli akizungumzia mradi huo amesema kuwa yeye kama Meneja mradi atahakikisha anashughulikia changamoto zilizopo ili kukamilisha kwa wakati.

Amesema kuwa licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali katika eneo la mradi hasa eneo la Mbezi Beach jijini Dar es salaam kampuni ya JBG Gauff Ingenieure inafanya kila linalowezekana ili mradi huo ukamilike mwishoni mwa mwezi Februari mwaka huu.

“Tumejipanga kufanya kazi hadi usiku kupunguza muda,kazi iliyobaki ni ndogo, tunawahakikishia DAWASA tutaimaliza kazi hii mwishoni mwa mwezi huu” Amesisitiza.

Mkurugenzi wa Usimamizi na Ufundi wa DAWASA, Romanus Mwang’ingo (katikati) akitoa ufafanuzi kuhusu maendeleo ya Mradi wa ujenzi  wa bomba hilo la kusafirishia Maji kutoka Ruvu Chini  kuelekea matangi ya kuhifadhia maji ya Chuo Kikuu cha Ardhi ambao umefika eneo la Mbezi Beach jijini Dar es salaam

IGP Mangu Awaapisha Makamishna Wa Polisi Waliopandishwa Vyeo Na Mheshimiwa Rais

0
0
Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP Ernest Mangu akimuapisha Kamishna wa Polisi, CP Simon Sirro baada ya kupandishwa cheo na Mheshimiwa Rais ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, kutoka Naibu Kamishna wa Polisi na kuwa Kamishna wa Polisi ambapo pia amemteua kuwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam.

Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP Ernest Mangu akimuapisha Kamishna wa Polisi, CP Albert Nyamuhanga baada ya kupandishwa cheo na Mheshimiwa Rais ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, kutoka Naibu Kamishna wa Polisi na kuwa Kamishna wa Polisi ambapo pia amemteua kuwa Kamishna wa Fedha na Logostiki wa Jeshi la Polisi.
Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP Ernest Mangu akimuapisha Kamishna wa Polisi, CP Robert Boaz baada ya kupandishwa cheo na Mheshimiwa Rais ya Jamuhuri wa Muungano ya Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, kutoka Naibu Kamishna wa Polisi na kuwa Kamishna wa Polisi ambapo pia amemteua kuwa Kamishna wa Intelijensia wa Jeshi la Polisi.
Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP Ernest Mangu akimuapisha Kamishna wa Polisi, CP Nsato Marijani baada ya kupandishwa cheo na Mheshimiwa Rais ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, kutoka Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi na kuwa Kamishna wa Polisi ambapo pia amemteua kuwa Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi.
Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP Ernest Mangu (kushoto) akimpongeza Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, CP Nsato Marijani baada ya kumuapisha jana Makao makuu ya Jeshi la Polisi. CP Nsato Marijani amepandishwa cheo na Mheshimiwa Rais ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, kutoka Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi na kuwa Kamishna wa Polisi ambapo pia amemteua kuwa Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi. Picha na Hassan Mndeme-Jeshi la Polisi.

Gazeti La Mawio Lamponza Tundu Lissu

0
0

TUNDU Lissu, Mwanasheria wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) pia Mbunge wa Singida Magharibi leo jijini Dar es Salaam amehojiwa na Jeshi la Polisi kuhusu hoja alizozitoa kwenye Gazeti la MAWIO.

Lissu amehojiwa kwa zaidi ya saa moja Makao Makuu ya Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam baada ya kuhitajika kutoa maelezo kwa madai ya kutoa kauli za uchoelezwa zilizoandikwa kwenye Gazeti la MAWIO zilizohusu mgogoro wa kisiasa visiwani Zanzibar.

Habari iliyoandikwa na gazeti hilo iliyobeba kichwa cha habari ‘Machafuko yaja Zanzibar’ inaelezwa kuwa sababu ya serikali kulifungia gazeti hilo tarehe 15 Januari mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumaliza kutoa maelezo Lissu amesema, serikali inajaribu kumziba mdomo asizungumzie kuhusu suluhu ya mgogoro wa kisiasa unaoendelea visiwani Zanzibar wakati wahusika hawazingatii misingi ya demokrasia.

“Wale waliobebwa kwenye uchaguzi leo wanataka kutufumba midomo tusizungumzie masula ya uchaguzi wa Zanzibar kwani machafuko yanaweza kutokea visiwani humo kwa tahadhari hiyo wanatuita wachochezi,” amesema Lissu.

Amesema kuwa, wao wametoa tahadhari ili yasitokee machafuko na umwagikaji wa damu na kwamba, Rais John Magufuli atawajibika kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) kama alivyowajibishwa Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya.

Amesema, mahojiano yake na Gazeti la Mawio ndio yaliyosababisha yeye kuitwa na kuhojiwa na polisi na kwamba, mtazamo wake ulioandikwa kwenye gazeti hilo ndio umechangia kufutwa kwa gazeti hilo.

Amesema kuwa hatokubali kuzibwa mdomo hata kama watatumia nguvu ya polisi.

Amesema, hatua ya Rais Magufuli kukakataa kujihusisha na mgogoro wa Zanzibar haikubaliki kwa kuwa ndiye ndiye atakayepeleka jeshi pale vurugu zitakapotokea.

Lissu amefika polisi hapo akiwa na mawakili wa watatu wa Chadema ambao ni Peter Kibatala, Fedrick Kiwelo na Hekima Mwasibu.

Amesema, baada ya mahojiano hayo polisi watapeleka jalada lake kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kwa hatua zaidi.

Taarifa Muhimu Kuhusu Matokeo Ya Kidato Cha Nne 2015 (CSEE) 2015

0
0

Baraza la Mitihani la Tanzania limekuwa likipigiwa simu na watu mbalimbali wakiomba ufafanuzi kuhusu taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuwa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi imetangaza kuwa matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Nne (CSEE) 2015 yamezuiwa kwa muda hadi tarehe 08/03/2016.

Baraza la Mitihani la Tanzania linapenda kuwajulisha watahiniwa na umma kwa ujumla kuwa taarifa hizo ni za UONGO na zinalenga kupotosha umma na kuleta taharuki.

Hivyo, Baraza linaomba umma kuzipuuza taarifa hizo kwa kuwa Wizara haijasitisha utoaji wa matokeo hayo. Matokeo yatatangazwa mara tu mchakato utakapokamilika.

Imetolewa na,
AFISA HABARI NA UHUSIANO

Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Jumatano Ya Februari 17

Waziri Mahiga Amtetea Rais Magufuli Kwa Kutohudhuria Sherehe Ya Mwaka Ya Mabalozi

0
0

Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dk Augustine Mahiga amemtetea Rais John Magufuli kwa kutohudhuria hafla ya mwaka ya mabalozi akisema alikuwa Singida kwenye maadhimisho ya miaka 39 ya CCM.

Balozi Mahiga alikuwa mgeni rasmi kwenye hafla hiyo iliyofanyika Ikulu ya kukaribisha mwaka mpya wa mabalozi ambayo kwa kawaida mwenyeji huwa ni Rais.

Dk Mahiga alitoa ufafanuzi huo kwa waandishi wa habari jana baada ya kuulizwa sababu za Rais kushindwa kuhudhuria hafla hiyo, lakini maelezo hayo yalichanganya zaidi, kwa kuwa hafla hiyo ya mabalozi ilifanyika Februari 8 wakati kilele cha sherehe za CCM kilikuwa Februari 6.

Kuhusu tofauti hiyo ya siku, Dk Mahiga alisema baada ya sherehe ya Singida, Rais alipitia kwenye ziara ambayo hata hivyo hakuifafanua.

Wakati huohuo, Waziri Mahiga alisema licha ya Dk Magufuli kuwakilishwa kwenye mikutano katika nchi mbalimbali, nchi hizo zinafahamu anachokifanya na bado nchi inaheshimika.

Akitoa mfano, katika mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika ulioandaliwa na China ambao ulifanyika Afrika Kusini, alisema licha ya Tanzania kuwakilishwa na makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, ilikuwa miongoni mwa nchi nne kati ya 54 za Afrika zilizopewa kipaumbele na kuwekeza katika sekta ya viwanda. Nchi nyingine zilizopewa kipaumbele ni Kenya, Ethiopia na Afrika Kusini.

“Utaona namna tunavyokubalika kimataifa kati ya nchi 54 za Afrika tunakuwa miongoni wa nchi nne zitakazopewa kipaumbele,” alisema.

Alisema wizara yake itaendelea kubana matumizi kwa kuziwezesha balozi za nje ili ziwe na uwakilishi imara.

Akitoa mfano, Dk Mahiga alisema juzi alirejea kutoka Angola ambako alimwakilisha Rais Magufuli kwenye mkutano wa Maziwa Makuu, akiongozana na watu watatu tofauti na zamani ambako angekuwa na msururu wa watu.

Alisema hata Makamu wa Rais alipokwenda Ethiopia kwenye mkutano wa Umoja wa Afrika (AU) alisafiri na watu 14 wakati zamani angesafiri na zaidi ya watu 30.

Mawakala wa Forodha Wapinga Makampuni 210 Kufungiwa Bandarini.........Wasimulia Jinsi Wafanyakazi wa Bandari Wanavyoshirikiana na Benki Kuiba Kodi

0
0

Sakata la upotevu wa makontena katika bandari ya Dar es Salaam na kufungiwa kwa makampuni 210 ya forodha limechukua sura mpyabaada ya Chama cha Mawakala wa Forodha (Taffa) kueleza kuwa kuna ushirikiano kati ya wafanyakazi wa taasisi hiyo na benki kuiba tozo za bandari.

Taffa, Wasafirishaji wa Nchi Kavu Wenye Magari (Tatoa), Mawakala wa Usafiri wa Majini (Tasaa) na Wamiliki wa Bandari Kavu (Cidat) wamesema hawahusiki na ukwepaji wa kodi.

Kwa muda sasa, kampuni za uwakala wa upakuaji na upakiaji wa mizigo zimekuwa zikituhumiwa kusaidia kukwepa kodi na kufikia hatua ambayo 210 zilitangazwa kufutiwa uwakala hivi karibuni.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika mkutano uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mwalimu Nyerere jijini Dar jana, mawakala hao walitaka uchunguzi ufanyike na endapo moja ya kampuni hizo itabainika kuhusika, hatua za kisheria zichukuliwe.

Mmoja wa wamiliki wa kampuni ya uwakala wa forodha, Ratish Kamanoor alisema alitoa mzigo bandarini 2013 na kulipa Sh40 milioni kupitia Benki ya CRDB Tawi la Water Front, lakini taarifa za TPA zilionyesha mzigo haujalipiwa. Baada ya kufanyika kwa utafiti ilibainika hundi yake imelipia kampuni nyingine 21.

Tony Swai wa Kampuni ya Wakala wa Forodha ya Transnotic alisema alifanya malipo ya Sh33 milioni kwa ankara yenye namba 11013092014, mwaka 2012, lakini malipo hayo hayakuonekana katika mfumo wa TPA licha ya kuwa na vielelezo vya benki na TPA vikionyesha kontena limeruhusiwa kutoka.

Mkurugenzi wa CRDB wa tawi hilo, Donath Shirima alipotafutwa kuhusiana na tuhuma hizo, alisema hawezi kuzungumza kwa kuwa siyo msemaji wa benki.

Mwenyekiti wa Taffa, Stephen Ngatunga alisema wamemwandikia barua Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa kumweleza jinsi wizi unavyofanywa na TPA pamoja na kumpa ushahidi. 

“Tulimpelekea waziri sampuli ya kampuni 29 zinavyolipa tozo za bandari na kumweleza kuwa TPA wamechana ushahidi,” alisema.

Ngatunga aliilalamikia Serikali kutangaza kuwa kampuni 284 zinakwepa kodi na kuwa, kitendo hicho kinachafua taswira ya Tanzania kimataifa na utendaji wa bandari. 

Tume yaundwa 
Baada ya Taffa kukutana na Waziri Mbarawa iliundwa tume huru kuchunguza wizi huo iliyopewa siku 10 kutoa taarifa za uchunguzi. 

Jinsi wizi unavyofanyika
Kwa maelezo ya wamiliki wa kampuni za uwakala wa forodha, wizi huo hufanyika kati ya wafanyakazi wa benki, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na TPA.

Mfumo wa malipo kwa njia ya benki ulianzishwa baada ya ule wa kawaida kuonekana unachangia wizi huo bandarini.

Taffa, Tatoa, Tasaa na Cidat walieleza kuwa wizi huo hufanyika kwa njia ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kupitia mfumo wa malipo wa IePS. Walielezwa kuwa baada ya mawakala kulipa, mfanyakazi wa TPA huingiza taarifa za malipo kama utaratibu unavyotaka.

Vyama hivyo vilisema baada ya TPA kumpa wakala risiti ya kuonyesha kuwa amelipa na kutoa mzigo wake, mtu wa kitengo cha Ieps cha TPA husubiri wakala anapotoa mzigo bandarini huwasiliana tena na mtu wa benki ambaye hurudisha malipo hayo.

Kuanzia hapo mfumo huonyesha kuwa mzigo huo haukulipiwa. Inaeleza kuwa mchezo huo huchezwa kati ya mtu wa benki kitengo cha Ieps cha TPA na anayeingiza taarifa za malipo kwenye mfumo.

Meya wa Manispaa ya Kionondoni, Boniface Jacob Atema Cheche Kuhusu Wakwepa Kodi....Atoa Siku 7 Kwa Wadaiwa Wote Kulipa Madeni Yao

0
0

Kampuni 12 zinazomiliki mabango makubwa ya matangazo ya barabarani katika Manispaa ya Kinondoni, zinadaiwa kukwepa kodi ya zaidi ya Sh10 bilioni na kusababisha manispaa hiyo kukosa mapato.

Meya wa manispaa hiyo, Boniface Jacob alisema jana kuwa kwa mwaka wa fedha wa 2015/16, Kinondoni imeazimia kukusanya zaidi ya Sh40 bilioni kutoka katika vyanzo mbalimbali vikiwamo vikuu sita ambavyo vitakusanya zaidi ya Sh35 bilioni.

Alisema miongoni mwa nyanzo hivyo ni ushuru wa mabango ambao walitarajia kupata Sh13 bilioni, lakini hali ni tofauti kwani hivi sasa kampuni hizo zimeilipa manispaa hiyo Sh2.5 bilioni badala ya kiasi walichokusudia.

“Mkiona Kinondoni inalalamika haina fedha, mambo yenyewe ndiyo kama haya. Wamiliki hawa wa mabango wanashirikiana na baadhi watendaji kitengo cha matangazo kufanya uhuni huu,” alisema Jacob.

Alisema mchezo huu umebainika baada ya manispaa hiyo kuunda timu tatu kutoka kampuni binafsi ambazo zilifanya uchunguzi wa mabango yaliyopo maeneo mbalimbali ya manispaa hiyo, na kwamba baadhi ya watumishi waliohusika na mchezo huo wameshachukuliwa hatua. 

Alisema timu hizo tatu zimegundua udanganyifu wa aina mbalimbali unaofanywa na wamiliki wa mabango hayo, ikiwamo vipimo, ukubwa na idadi ya mabango hayo yaliyowekwa barabarani kuwa tofauti na vielelezo vilivyowasilishwa na kampuni hizo.

“Tungewatumia watumishi wa ndani kufanya uchunguzi huu ingekula kwetu.Lakini hizi timu tatu zimefanya kazi kubwa, kwa sababu hawa wamiliki wa mabango wanapiga fedha nyingi, ukiwa na bango moja Kinondoni unalipia Sh30 milioni tena kwa dola,” alisema Jacob.

Jacob ambaye pia ni Diwani wa Ubungo (Chadema), aliwapa siku saba wamiliki hao kulipa fedha hizo, kila mmoja kulingana na anavyodaiwa na baada ya hapo, hatua madhubuti zitachukuliwa dhidi yao, ikiwamo kushusha mabango wanayoyamiliki.

“Tunahitaji hizi fedha walizokwepa kulipa haraka iwezekanavyo ili tuzipeleke kwenye sekta ya elimu. Najua kuna wengine watazunguka mlango wa nyuma na kwenda ngazi za juu kutafuta huruma, lakini nawaambia huko wanajisumbua bora waje hapa ofisini tena wakiwa na fedha zetu,” alisema Jacob.

Alisema amechoshwa na hali hiyo ya udanganyifu inayofanywa na kampuni hizo, huku akitolea mfano moja ya kampuni iliyotakiwa kulipa Sh2 bilioni kama kodi, lakini imelipa Sh500 milioni tu.

Mhasibu wa manispaa hiyo, Maximilian Tabonwa alisema lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha mapato yanakuwa kwa kasi katika manispaa hiyo na walianza kwenye mabango madogo kisha kuhamia kwenye makubwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Platnum Media, aliyejitambulisha kwa jina la Martin, alisema hawezi kuzungumza chochote kwa kitu kilichoandikwa au tetesi zilizosemwa na mtu fulani.

Hata hivyo, Jacob alisema hadi kufikia saa 10 jioni jana, wamiliki na wawakilishi wa kampuni sita walikwenda kujisalimisha katika ofisi yake juu ya sakata hilo.

Serikali Ya Tanzania Yasema Haitajitoa katika Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC)

0
0

SERIKALI imesema Tanzania haitajitoa katika Mahakama ya Kimataifa yaMakosa ya Jinai (ICC). Hata hivyo, imesema tabia ya ubaguzi dhidi ya viongozi wa Bara la Afrika inayooneshwa na mahakama hiyo inaweza kurekebishwa.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Dk Agustine Mahiga wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya Siku 100 za Rais John Magufuli tangu aingie madarakani.

“Sisi ni miongoni mwa nchi ambazo zimesaini mkataba wa Roma ambao ulianzisha Mahakama ya ICC… Tunataka kuona baadhi ya mambo yakirekebishwa ili kuondoa kile kinachoonekana kuwa ni ubaguzi kwa viongozi wa Afrika,” alisema Balozi Mahiga.

Waziri huyo alisema, katika Siku 100 za Serikali ya Awamu ya Tano Tanzania imeweza kufanikiwa katika mambo mengi kupitia Wizara hiyo ikiwa ni pamoja na kushughulikia masuala ya uhusiano na migogoro mbalimbali.

Alisema tangu alipoapishwa kuwa Waziri ameshughulikia baadhi ya migogoro ukiwemo wa Burundi ambapo Rais Magufuli alimuagiza kwenda nchini humo ili kuzungumza na Rais wa nchi hiyo, Pierre Nkurunziza ili akubali kufanya mazungumzo ya kutafuta mwafaka wa mgogoro unaoendelea nchini mwake.

Balozi Mahiga alisema, hatua ya Rais kuzuia safari za nje kwa watumishi imesaidia kupunguza gharama ambazo wakati mwingine zilikuwa si za lazima, hivyo ni jambo ambalo linapaswa kupongezwa.

“Si kwamba Rais hatasafiri, hapana ila kwa sasa tunajua bado ana jukumu kubwa la kujenga serikali yake. Serikali si kwa maana ya Mawaziri tu ila watendaji wote kwa ujumla. Mambo yakishatulia nadhani hata yeye sasa ataweza kusafiri kwa safari atakazohitajika,” alisema.

Serikali Yaitaka Kampuni Ya Halotel Kuzingatia Mkataba

0
0
Serikali imesema itachukua hatua kali kwa kampuni ya Halotel kama itashindwa kutekeleza makubaliano ya mkataba wa kusambaza huduma za simu na mtandao katika ofisi za Serikali katika kila Wilaya nchini kote.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa wilayani Maswa wakati akizungumza na watendaji wa sekta ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mkoani Simiyu na kusisitiza kutoa ushirikiano unaostahili kwa kampuni hiyo.
 
“Makubaliano yetu kati ya Serikali na Halotel ni kuunganisha ofisi za Umma kwa mtandao zikiwemo shule tatu katika kila Wilaya, Hospitali, Mahakama na Ofisi za Polisi ili kuwezesha mkakati wa mawasiliano vijijini kutekelezeka”, amesema Prof. Mbarawa.
 
Waziri Prof. Mbarawa ameeleza kuwa ifikapo mwaka 2017 kila eneo hapa nchini litakuwa na huduma ya mawasiliano ya mtandao na kuwezesha wananchi wote kunufaika na huduma hizo.
 
Katika hatua nyingine Prof. Mbarawa amekagua Ujenzi wa Barabara ya Lamadi-Bariadi KM 71.8 na Bariadi-Maswa KM 49.7 na kuwapongeza makandarasi wanaojenga barabara hizo kwa kazi nzuri wanayofanya.
 
“Nawapongeza kwa kazi nzuri mnayoifanya, hakikisheni kazi yenu inauwiana na thamani ya fedha na kuhakikisheni wafanyakazi wazawa wanapewa kipaumbele katika kazi wanazoziweza na kupewa mikataba stahiki ya kazi wanazozifanya”, amesititiza Prof. Mbarawa.
 
Aidha, Waziri Prof. Mbarawa amemuagiza mkandarasi anaejenga barabara ya Maswa-Mwigumbi KM 50.3 kuhakikisha nyumba zinazojengwa kwa ajili ya mkandarasi zinajengwa kwa ubora ili zitumike kwa muda mrefu.
 
“Nakuagiza Meneja wa TANROADS, hakikisha nyumba hizi baada ya mradi wa barabara kukamilika unazikabidhi kwa jeshi la polisi ili waweze kuzitumia kwa ajili ya makazi na ofisi”, amesema Prof. Mbarawa.
 
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Bw. Eraston Mbwilo amemwomba Waziri Prof. Mbarawa kuelekeza nguvu za ujenzi wa ofisi na nyumba za watumishi katika mkoa huo.
 
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Wilaya ya Maswa Bi. Rosemary Kirigini amemuomba Waziri Prof. Mbarawa kuwawezesha Wakala wa Majengo nchini (TBA) kukamilisha mradi wa Ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya hiyo unaojengwa sasa kwa miaka mitano ili kuipunguzia Wilaya hiyo adha ya kutumia jengo chakavu ambalo si salama hasa kipindi cha mvua.
 
Waziri Prof. Mbarawa pia amekagua Kiwanja wa Ndege kilichopo Mkoa wa Shinyanga na ofisi za Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) kiwanjani hapo na kusisitiza kuwa Serikali iko katika hatua za kuboresha uwanja huo kuwa wa kisasa ili kuvutia mashirika mengi ya ndege kutumiwa kiwanja hicho.
 
Waziri Prof. Mbarawa yupo kwenye ziara ya kukagua miradi ya ujenzi kwenye sekta za barabara, nyumba, viwanja vya ndege na mkongo wa taifa wa mawasiliano katika mikoa ya kanda ya ziwa ambapo ametembelea Wilaya za Busega, Bariadi na Maswa mkoani Simiyu.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (aliyevaa koti la bluu), akisikiliza maelezo ya mkandarasi kuhusu ujenzi wa mtambo (hauonekani pichani) wa kusaga kokoto kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Maswa-Mwigumbi Km 50.3.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa, akiongea na vibarua wanaofanya kazi kwenye mradi wa barabara ya Maswa-Mwigumbi Km 50.3, mkoani Simiyu.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akiongea na wafanyakazi wa sekta za Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kuhusiana na mkakati wa Wizara wa kuongeza mapato mkoani Simiyu.

Mfanyakazi Wa Kihindi Afukuzwa Kazi Nchini Kwa Kuwaita Watanzania Nyani

0
0

Raia wa India, Dennis Smith ameachishwa kazi katika Hoteli ya Ramada kwa madai ya kuwatukana wafanyakazi wa ngazi za chini akiwaita nyani.

Smith, ambaye ni meneja wa chakula na vinywaji wa hoteli hiyo, aliwatukana na kuwadhalilisha wafanyakazi hao siku ya Sikukuu ya Wapendanao akiwatuhumu kushindwa kuandaa meza vizuri.

Kutokana na udhalilishaji huo, wafanyakazi wa hoteli hiyo jana waligoma wakishinikiza meneja huyo asimamishwe kazi au wao waache kazi.

Wakizungumza jana, baadhi ya wafanyakazi ambao waliomba majina yao yahifadhiwe walisema tabia ya meneja huyo imekuwa sugu na tukio la juzi lilikuwa halivumiliki. Walisema raia huyo wa India amekuwa mwenye majivuno na kutoa lugha chafu dhidi yao.

“Tumechoshwa, anatuitaje sisi nyani, hii tabia ni ya muda mrefu na sasa hatuwezi kuivumilia,” alisema mmoja wa wafanyakazi hao.

Mwakilishi wa wafanyakazi hao, Mathew Misalaba alisema bosi huyo amekuwa akiwarushia maneno ya kuwadhalilisha kila wanapofanya makosa hata kidogo.

Alisema licha ya uongozi wa hoteli kuahidi kumsimamisha kazi Smith, wamelipeleka suala hilo polisi ili hatua stahiki zichukuliwe.

Meneja Rasilimaliwatu wa hoteli hiyo, Sebastian Nchimbi alisema tayari Smith ameachishwa kazi kutokana na tukio hilo.

“Tulizungumza na wafanyakazi wakatuambia kuwa hawataki Smith awepo kazini na sisi tukafanya uamuzi ili kuwalinda wafanyakazi wetu,” alisema.

Alisema waliamua kumwachisha kazi Smith baada ya kupata malalamiko mengi kutoka kwa wafanyakazi hao.

“Si tukio la mara ya kwanza na ndiyo maana tulipoona yamezidi tuliamua kuchukua hatua,” alisema.

Hata hivyo, Nchimbi alimsifu Smith akisema ni mtendaji mzuri na alikuwa na tija kwa hoteli hiyo ya kitalii lakini hakuwa na kauli nzuri kwa wafanyakazi Waafrika.

“Kiutendaji ni mzuri mno… yaani kwetu sisi tunapoteza mtu hasa, tatizo ni mdomo tu,”
alisema.

Mimba ya Wema Sepetu 'Yatoweka Ghafla'........., Idris aandika ya moyoni kuhusu kupoteza mapacha wake

0
0

Mpenzi wa Wema Sepetu, Idris Sultan usiku wa kuamkia Jumatano hii amepost picha ya watoto mapacha huku akiandika ujumbe unao onyesha mimba ya mpenzi wake (Wema Sepetu)  imearibika.

Kupitia instagram idris ameandika

To my unborn twins,
    So quickly you came into our lives,
    So quickly torn away.
    Never got the chance to meet you,
   There’s so much I want to say. 
 
All these thoughts running  through my head,
    It’s enough to drive me insane.
    Though you lived only 13 short weeks,
    You were loved so very much.
    I wish that I could hold you,
    I long to feel your touch.

I pray that in another life, We get the chance to meet. God brings and takes as he plans and we cannot complain but only pray that all that was for a better reason and a better plan in store for us. 

We have learnt lessons painfully but wont stop trying again and again and do swear by the time your brothers and sisters are made to come to this world we will be more than ready for them.
    
Sincerely Your Dad. 
-----------
 
==>Hivi ndivyo unavyosomeka ujumbe wa Idris kwa lugha ya Kiswahili

Kwa mapacha wangu ambao walikuwa bado hawajazaliwa

“Ni haraka sana mmeingia katika mfumo wa maisha yetu, lakini ni haraka pia mmetuacha, sikuwahi kupata nafasi ya kukutana na nyinyi, nina vingi nataka niseme ninavyofikiria ndani ya kichwa changu vinatosha kunifanya mwendawazimu, ukizingatia mmeishi kwa wiki sita pekee, tuliwapenda sana na natamani ningepata nafasi ya kuwashika, mungu ametoa na mungu ametwa kama ambavyo amepanga na hatuwezi kulalamika huenda ametuandalia mengine mazuri zaidi” 

Walimu Watatu Wakatwakatwa Mapanga Huko Musoma, Mara

0
0
Walimu watatu wa shule ya Secondary Mara iliyopo katika manispaa ya mji wa Musoma Mkoani Mara,Vedastus Rwechungula ,Juma Amos Na Maccelo Ndege, Wamekatwa Mapanga sehemu mbali mbali ya miili yao walipokuwa wakirejea shuleni hapo Usiku wa Saa Nne toka matembezini.

Wakizungumza wakiwa wamelazwa katika hospital ya Rufaa ya Musoma,Walimu hao wamesema kuwa Vitendo vya Uhalifu jirani na Shule hiyo vimekuwa vikijitokeza mara kwa mara kutokana na vibaka waliopo katika eneo hilo kuwakata watu kwa mapanga.

Barua aliyoiandika Mtanzania Jackline Cliff kutoka gerezani China

0
0

Ikiwa ni miaka miwili toka video vixen Jackie Cliff akamatwe kwenye uwanja wa ndege na kufungwa gerezani huko Macao China kwa kosa la kujaribu kuingiza dawa za kulevya, ameandika barua ya wazi kwa watanzania ambapo amezungumzia mambo mbalimbali kuhusu maisha yake.


Barua hiyo imesomwa kwa mara ya kwanza na kipindi cha Amplifaya cha Clouds FM Jumanne hii na mtangazaji wa kipindi hicho Millard Ayo.
 

Sikiiza hapa.

Mwanasheria Wa Serikali na Askari Magereza Washikiliwa kwa Kumtorosha Mtuhumiwa Gerezani

0
0

Mwanasheria wa Serikali Mkoa wa Katavi pamoja na askari magereza wawili wanashikiliwa na jeshi la polisi mkoani humo kwa tuhuza za kula njama na kisha kumtorosha kwa siku 124 mtuhumiwa wa kesi ya kujaribu kumuua mlemavu wa ngozi (Albino) baada ya kupokea rushwa ya jumla ya Sh3 milioni.

Tukio la kutoroshwa kwa mtuhumiwa huyo linadaiwa kufanyika Oktoba 12 mwaka jana, baada ya kupokea fedha kiasi hicho ambapo Mwanasheria wa serikali mkoani Katavi, Falhati Seif Khatibu(45) alipokea kiasi cha Sh2 milioni na askari Magareza A.287 S/SGT- John Masagula(50) pamoja na A. 5385 SGT Deogratius Katani(50) wakigawana kiasi cha Sh milioni moja.

Kamanda wa polisi Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari alisema kuwa kukamatwa kwa watuhumiwa hao kulifanikiwa kutokana na taarifa za siri kutoka kwa raia wema ambao walidai kuwa kuna mtuhumiwa aliyekuwa anashikiliwa ametoroka kutoka katika gereza la mahabusu la Mpanda lililopo mkoani humo.

Alisema baada ya taarifa hizo ndipo uchunguzi ulipofanyika Januari 19 mwaka huu, na kubaini kuwa mtuhumiwa Alex Manyanza(27) ambaye alikuwa anashikiliwa kwa tuhuza za kujaribu kumuua kwa kumkata kiganja cha mkono mlemavu wa ngozi Limi Luchoma(30), mwanzoni mwa mwaka na kufunguliwa shitaka namba MTO/IR/76/2015 alikuwa ametoroka mahabusu.

Baada ya upelelezi ilibainika kuwa ndugu wa mtuhumiwa huyo ndio waliotekeleza mpango huo na kisha kumtorosha mtuhumiwa na kwenda kumficha katika kijiji cha Kipande kilichopo mkoani Rukwa, na ndipo walipompa fedha hizo mwanasheria mkuu wa serikali ili amuondelee shitaka linalomkabili mtuhumiwa huyo baada ya kufanikiwa kutoroka gerezani.

Alisema mtuhumiwa ni mzoefu kwa vitendo vya kutoroka gerezani kwani kabla ya kufanya tukio hilo alikuwa ametoroka katika gereza la Kalila Nkulunkulu lililopo mkoani humo, ambapo alikuwa anatumikia kifungo cha miaka mitano jela baada ya mahakama kumtia hatiani kwa kosa la wizi wa mifugo.

Kamishna wa Elimu Awavua Madaraka Wakuu Watatu wa Vituo vya Elimu ya Watu Wazima Dar, Dodoma na Mwanza

0
0

Kamishna  wa Elimu, Teknolojia, Sayansi na Ufundi, Profesa Eustella Balamsesa amemuagiza Mkurugenzi wa Elimu ya Watu Wazima, Fedelis Mafumiko kuwavua madaraka Wakuu Watatu (3) wa vituo vya  Elimu ya Watu Wazima kutokana na kukiuka utaratibu wa kuchagua wanafunzi wanaojiunga kidato cha kwanza kuwaingiza katika Mfumo wa Elimu ya Watu Wazima.

Profesa Eustella ameyasema hayo leo wakati alipokutana na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam .

Amesema kuwa wakufunzi hao wamekuwa wakishirikiana na Halmashauri baada ya kuchagua wanafunzi wa kidato cha kwanza ambao wamefanya vizuri wao huchukua wanafunzi waliofeli na kuwapeleka katika shule za serikali wakidai kuwa wanafunzi wamechaguliwa katika chaguo la pili.

Baada ya kuchaguliwa wanafunzi hao wakifika shule wanadaiwa ada wakati serikali imesema elimu  ni  bure, hali inayowachanganya  wazazi.

Wakuu wa vituo waliovuliwa madaraka ni Wotugu Mganda (Dar es Salaam), Senorina Kateule (Dodoma),Steward Ndandu Geita na (Mwanza).

Profesa Eustella amesema kuwa wakufunzi hao wamekuwa wakidandia matokeo ya kidato cha kwanza kwa kufanya upotoshaji kwa wazazi wakati wanafunzi wanaosoma katika elimu ya watu wazima ni hiari kutokana  na sera ya elimu.

Wanafunzi ambao wamechaguliwa kwa mwaka huu wamekuwa wakidai ada ya sh. 80,000 hadi 250,000 na ndipo malalamiko yakaanza kwa wazazi baada ya kudaiwa ada hiyo.

Profesa Eustella, amesema kuwa mmoja wanafunzi katika Mkoa wa Dar es Salaam aliambiwa amefaulu katika chaguo la pili katika shule ya sekondari ya Oasterbay .Baada ya kufika shuleni, mwanafunzi huyo alikuta mambo tofauti kwa kudaiwa ada na kuambiwa awasiliane na Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima.
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live




Latest Images