Quantcast
Channel: MPEKUZI
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live

Viongozi wa Dini Wazidi Kutofautiana Kuhusu Sakata La Zanzibar.......Sheikh Ponda Issa Ponda Apinga Uchaguzi Kurudiwa Zanzibar

$
0
0

Mgogoro kuhusu kurudiwa kwa uchaguzi viswani Zanzibar unazidi kupasua nchi, sasa viongozi wa Dini ya Kiislam wametofautiana.

Ikiwa ni siku moja baada ya Alhad Mussa Salum ambaye ni Sheikh Mkuu wa Dar es Salaam kuunga mkono Tume ya Uchaguzi wa Zanzibar (ZEC) kutangaza tarehe ya uchaguzi visiwani humo, Jumuiya ya Taasisi za Kiislam Tanzania imepinga.

Sheikh Ponda Issa Ponda, Katibu wa Jumuiya ya Taasisi za Kiislamu nchini katika mkutano wake na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam amesema, kuruhusu kurudiwa kwa uchaguzi visiwani humo ni kupandikiza mbegu za chuki kwa wananchi.

Sheikh Ponda amesema kuwa uchaguzi uliofanyika Oktoba mwaka jana haukuwa na mashaka kwa kuwa, waangalizi wa nje pia walithibitisha hilo.

“Ripoti za waangalizi wa ndani na nje zilithibitisha kuwa uchaguzi haukuwa na dosari. Kuna sababu gani ya kurudia uchaguzi,” amehoji Sheikh Ponda.

Wakati Sheikh Ponda akihoji sababu za ZEC kutaka kurudiwa kwa uchaguzi huo, Sheikh Alhad aliipongeza tume hiyo na kuongeza“tunaiomba ZEC kusimamia kazi hii kwa haki, uadilifu na umakini mkubwa…”

Sheikh Alhad jana alisema kuwa Baraza la Waislam Tanzania (BAKWATA) linaunga mkono uamuzi wa ZEC kurudia uamuzi huku akikitaka Chama cha Wananchi (CUF) ambacho kimesusia uchaguzi huo, kushiriki.

CUF kwenye mkutano wake wa Baraza Kuu uliofanyika tarehe 27 na 28 Januari mwaka huu kilieleza kususia uchaguzi huo uliopangwa kufanyika tarehe 20 Machi mwaka huu na kudai kuwa, hakuna sababu yoyote kwa chama hicho kushiriki. ZEC ilifuta uchaguzi huo tarehe 28 Oktoba mwaka jana.

Hata hivyo, Sheikh Ponda amesema kuwa, ZEC haikuwa na sababu ya kufuta uchaguzi  kwa kuwa, baada ya tume hiyo kutangaza matokeo, haina mamlaka ya kufuta.

Pamoja na kupinga kurudiwa kwa uchaguzi, Sheikh Ponda Sheikh Alhad amepata wapi kauli ya Kiongozi wa Jumuiya za Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (Jumiki), Sheikh Farid Hadi Ahmed kuwa anaunga mkutano marudio ya uchaguzi Zanzibar.

Sheikh Alhad kwenye mkutano wake jana alisema “Hata kiongozi wa Uamsho, Sheikh Farid Ahmad pia anaunga mkono suala la kufanyika uchaguzi wa marudio kwa mujibu wa barua yake aliyonitumia mimi .”

Sheikh Ponda ameeleza kwamba, Sheikh Farid hawezi kutoa kauli hiyo na kwamba kama Sheikh Alhad anayo barua hiyo, aitoe hadharani.

“Sio jambo rahisi kuamini kwamba Sheikh Farid anaweza kutoa kauli hiyo, sio jambo rahisi kabisa na kama ni kweli basi atoe ushahidi wake,” ameeleza Sheikh Ponda.

Pia Sheikh Ponda ameonesha kushangazwa na ZEC kuhalalisha matokeo ya Rais wa Muungano wa Tanzania sambamba na Wabunge wa Bunge la Muungano.

Shekh Ponda amesema kuwa uchaguzi wa Zanzibar na matokeo yake bado ni halali “Sisi kama Tasisi ya Waislamu tunapinga kurudiwa kwa uchaguzi wa Zanzibar.”

Amesema kuwa, taasisi hiyo imeunga mkono hatua za mwanzo zilizochukuliwa na CUF pia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kunusuru hali ya kisiasa visiwani humo na kutaka majadiliano yaendelee.

Shekh Ponda amemshauri Rais John Magufuli kutimiza ahadi yake aliyoitoa bungeni ya kushughulikia mzozo huo kwa kushirikiana na Maalim Seif Shariff Hamad na Dk. Ali Mohammed Shein.

Amesema kuwa, Rais Magufuli hajatoa tamko lolote na kwamba hajaeleza amefikia wapi katika kutatua mzozo huu.

Sheikh Ponda amesema kuwa kuna viashiria vya kuvunjika kwa amani visiwani humo kutokana na watu kuporwa haki zao na kwamba watakapoamua kuitafuata kutazuka vurugu.

LHRC Wamtaka Mwenyekiti wa ZEC Kujiuzulu Mara Moja......Chama cha CCK Chamvua Uanachama Katibu Wake Aliyetangaza Kushiriki Uchaguzi Wa Marudio Zanzibar

$
0
0

Kituo cha sheria na haki za binadamu LHRC kimemtaka Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Zanzibar Jecha Salum Jecha ajiuzulu wadhifa huo kutokana na hatua aliyochukuwa ya kufuta uchaguzi na kutangaza tarehe ya kurudiwa bila kufuata sheria hivyo kumemuondolea sifa ya kusimamia na kuongoza tume hiyo.

Tamko hilo limetolewa jijini Dar esSalaam na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC Bi Imelda Urrio ambapo amesema ukosefu wa taarifa sahihi na rasimi za michakato ya maridhiano toka kufutwa kwa uchaguzi kunaondoa imani ya wananchi juu ya viongozi wao, tume na mchakato mzima wa chaguzi za kidemokrasia Zanzibar.

Amesema kuwa kufutwa na kutangazwa upya kwa uchaguzi wa Zanzibar kunakiuka katiba,sheria,na kanuni za uchaguzi na pia misingi ya demokrasia ya utawala wa  sheria nchini.

Amesema kuwa katiba ya Zanzibar na sheria za uchaguzi hazijampa mamlaka mwenyekiti na hata tume yote kufuta uchaguzi na hivyo kilichotokea Zanzibar kimeaacha watanzania wakiwa hawaelewi ni sheria na katiba ipi imetumika kufuta uchaguzi huo.

Bi Imelda ameongeza kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 123 cha sheria ya uchaguzi Zanzibar mtu akishachaguliwa uchaguzi wake hautohojiwa isipokuwa kwa kupeleka shauri mahakamani,hivyo kwa msingi huo LHRC wanaona kwamba hakuna kifungu chochote cha sheria kinachoipa tume ya uchaguzi au mwenyekiti wake mamlaka ya kufuta uchaguzi na kuamuru marudio isipokuwa kwa amri ya mahakama.

Wakati huohuo chama cha kijamii CCK kimemsimamisha kazi na uanachama naibu katibu mkuu wake wa Zanzibar Ali Khatib Ali ambaye pia alikuwa mgombea urais wa Zanzibar kwenye uchaguzi uliotangazwa kufutwa na ZEC Oktoba 2015.

Mwenyekiti wa CCK Costantine Achitanda amesema chama kimefikia maamuzi hayo ili kupisha uchunguzi dhidi yake kufuatia uamuzi wake binafsi wa kutangazia umma kuwa CCK itashiriki uchaguzi wa marudio huko Zanzibar kinyume na taratibu za chama.

Wakili Hamis Mkindi kutoka LHRC akiongea.Kushoto  ni  kaimu mkutugenzi wa kituo cha sheria na Haki za binadamu Bi Imelda Lulu Urrio
 Waandishi  wa  habari  wakifuatilia  habari hiyo.

IPTL Yakanusha Habari Zilizochapishwa na Gazeti La Jamvi La Habari Kwamba Wanalipwa Milioni 300 Kwa Siku na TANESCO

$
0
0
  1. Makampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) na Pan Africa Power Solutions (T) Limited (PAP), kwa masikitiko makubwa tumesoma taarifa mbali mbali zilizochapishwa na gazeti la kila wiki la Jamvi la Habari hususan toleo namba 90 la tarehe 1 Februari 2016 lenye kichwa cha habari, “Miezi 14 ya sakata la EscrowSethi na IPTL waikamua Tanesco milioni 300 kila siku”; iliyoambatana na dondoo saba zilizosomeka kama ifuatavyo:-
  • Ni malipo ya ‘Capacity Charges’
  • Ni mara mbili zaidi ya kashfa ya Richmond
  • Wanaharakati washangazwa na kimya cha serikali
  • Takukuru yatakiwa kuingilia kati
  • Waziri Muhongo aombwa kuchukua hatua madhubuti
  • Fedha wanazolipwa IPTL zinatosha kurusha ‘Live’ matangazo ya Bunge miaka 36
  • Yaelezwa ni sababu kuu ya gharama za umeme kupanda
  1. Tungependa kukanusha taarifa hizi. Kwanza kabisa, taarifa hizi ni uzushi mtupu wenye lengo la kuichafua IPTL na wamiliki wake akiwemo Mwenyekiti Mtendaji, Bwana Harbinder Singh Sethi. Pili, taarifa hizi ni za kichochezi kwani zinalenga kuwachonganisha wananchi wa Tanzania na serikali yao. Tatu, taarifa hizi zimechongwa na kuchorongwa ili kuwachonganisha wananchi wa Tanzania dhidi ya mwekezaji, IPTL/PAP na mwenyekiti wake mtendaji, Bwana Harbinder Singh Sethi; kwani inakusudia kuwahadaa Watanzania kuwa IPTL inanyonya rasilimali za nchi.
  1. Awali ya yote, tungependa kuutarifu umma wa Watanzania kwamba malipo ya tozo ya uwekezaji (“Capacity Charges”) yamo kwenye mikataba yote ya kufua na kuuziana umeme (Power Purchase Agreement –PPA) duniani kote, baina ya makampuni binafsi ya kufua nishati ya umeme (Independent Power Producers) na mashirika husika ya umma ya ugavi wa nishati ya umeme, kama ilivyo katika mkataba wa kuuziana umeme baina ya IPTL na TANESCO.
  1. Hata hivyo, si kweli kwamba IPTL inalipwa fedha za Kitanzania milioni 300 kwa siku kama “Capacity Charges” kama ilivyodaiwa na gazeti hilo la Jamvi la Habari. Kinacholipwa na TANESCO kwa IPTL kama “capacity charges” haijawahi kuzidi fedha za Kitanzania million 150 kwa siku tokea mradi wa kufua umeme wa IPTL ulipozinduliwa mwaka 2002 hadi leo.
  1. Tunashangaa kuona gazeti linalodai kuwa na waandishi weledi wakiandika taarifa ya upotoshaji zisizofanyiwa utafiti yakinifu kufahamu maana ya “Capacity Charges”; kwanini kampuni inalipwa hiyo “Capacity Charges”; namna gani hiyo “Capacity Charges” inavyokokotolewa; na kiasi gani halisi kinacholipwa kwa kampuni ya IPTL baada ya kuondoa kodi na gharama zingine mbalimbali husika.
  1. Gazeti la Jamvi la Habari pia inaeleza kwenye taarifa yake hiyo kwamba “Capacity Charges” inayolipwa IPTL ndiyo sababu kuu ya gharama za umeme kupanda. Huu ni uzushi mwengine. Jedwali la gharama za “Capacity Charges” zinazotozwa na makampuni mbali mbali binafsi zinazofua na kuiuzia umeme TANESCO (tunalolinukuu hapa chini), inadhihirisha wazi kuwa gharama za “Capacity Charges” inayolipwa kwa IPTL ziko chini ukilinganisha na gharama za “Capacity Charges” zinazolipwa kwa makampuni mengine binafsi zinazofua na kuiuzia umeme TANESCO.
Jedwali: Mlinganisho wa Gharama za Ununuzi na Kuuza kwa Uniti Moja (Kwh)
Tariff for EPPs and IPPs:
Rental Company
Energy Charge / kWh
Capacity Charge / kWh
Total Charge / kWh
Selling Price (USD / kWh)
Difference (USD / kWh)
Aggreko
0.369
0.0577
0.4267
0.1197
(0.307)
Symbion
0.284
0.0565
0.3405
0.1197
(0.2208)
Symbion (natural gas)
0.029
0.0499
0.0789
0.1197
0.0408
IPTL
0.13
0.0106
0.0106
0.1197
(0.1139)
Songas
0.0217
0.0431
0.0648
0.1197
0.0549
  1. Gazeti la Jamvi la Habari pia limehusisha malipo ya Capacity Charges yanayolipwa IPTL na gharama za kurusha matangazo ya moja kwa moja ya bunge katika runinga, likidai kwamba “Fedha wanazolipwa IPTL zinatosha kurusha ‘Live’ matangazo ya Bunge miaka 36”. Gharama za kufua umeme hazina uhusiano wowote na gharama za kurusha ‘Live’ matangazo ya Bunge. Kwa sababu malipo haya yanayolipwa kwa IPTL ni malipo yanayotokana na mkataba wa kufua umeme kati ya IPTL na TANESCO. Kuhusisha gharama hizi za “Capacity Charges” inayolipwa kwa IPTL kwa mujibu wa mkataba wa kufua umeme na gharama za kurusha ‘Live’ matangazo ya Bunge siyo tu ni uchochezi wa wananchi dhidi ya serikali yao bali pia ni uchochezi wa wananchi dhidi ya kampuni ya IPTL/PAP na mwenyekiti wake mtendaji Bwana Harbinder Singh Sethi, ambayo ni uvunjifu wa katiba na sheria husika za nchi.
  1. Mwandishi wa makala husika angeuliza IPTL ama TANESCO bila shaka angeweza kupata taarifa sahihi na ufafanuzi wa kutosha badala ya kukurupuka na kuandika mambo ya kizushi na uchochezi. Tungependa kutumia fursa hii kutoa rai kwa waandishi na vyombo vyote vya habari kuzingatia weledi wa fani zao katika kuandika taarifa sahihi ya mambo mbalimbali wanayoyaandika ikiwemo taarifa za kampuni ya IPTL, PAP na Bwana Harbinder Singh Sethi.
  1. Kwa muhtasari, taarifa zilichochapishwa kwenye makala husika ni uzushi usiokuwa na ukweli wowote. Tungewaomba Watanzania na wote waliosoma au watakaosoma makala husika wazipuuzie taarifa hizo. Pia tunawataka wahariri na wachapishaji wa gazeti la Jamvi la Habari kuomba radhi kwa taarifa hizo za kizushi ndani ya siku kumi na nne (14). Kushindwa kufanya hivyo, hatua za kisheria zitachukuliwa ikiwemo kulifikisha gazeti pamoja na wahariri wake mahakamani.
  1. Tunaomba pia vyombo mbalimbali vinavyohusika na kulinda amani na utengamano wa nchi yetu ikiwemo jeshi la polisi kuwachukulia hatua mwandishi wa makala hiyo na wahariri wa gazeti la Jamvi la Habari kwa kuvunja sheria za nchi kwa kuandika habari za uchochezi.
Ahsanteni sana.
Joseph O. R. Makandege (ADVOCATE)
(Katibu na Mshauri Mkuu wa Sheria)
KAIMU MWENYEKITI MTENDAJI
Independent Power Tanzania Limited / Pan African Power Solutions (T) Limited.

Binti wa Kitanzania Amayesoma India Adhalilishwa Kwa Kupigwa Na Kuvuliwa Nguo

$
0
0

Mtanzania anayesoma India amepigwa, kuvuliwa nguo na kisha kulazimishwa kutembea akiwa uchi na kundi la watu nchini humo.

Mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 21 (jina linahifadhiwa) anayesoma shahada ya biashara, mwaka wa pili katika Chuo Kikuu cha Acharya, Bangalore, alifanyiwa ukatili huo akiwa na Watanzania wengine wanne.

Gazeti la Deccan Chronical la Bangalore, liliripoti kuwa tukio hilo lilitokea Januari 31, baada ya mwanafunzi raia wa Sudan, Ismail Mohammed kugonga gari la raia mmoja wa India, mkazi wa Hesaraghatta aliyekuwa na mkewe na kusababisha kifo cha mama huyo.

Nusu saa baadaye, Watanzania watano akiwamo aliyevuliwa nguo, walifika katika eneo hilo wakiwa kwenye gari ndipo kundi la watu hao lilipoanza kumshambulia binti huyo, kisha kumvua nguo na kumlazimisha atembee uchi.

Baada ya kuchoma gari lililosababisha ajali hiyo, kundi hilo pia liliteketeza gari alilokuwamo Mtanzania huyo.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Mindi Kasiga alisema Balozi wa Tanzania nchini humo, John Kijazi ameshakutana na wanafunzi hao na ameshazungumza na Serikali ya India kuhusu tukio hilo.

Gazeti la Deccan Chronical liliripoti kuwa licha ya polisi waliokuwapo eneo hilo hawakuchukua hatua yoyote hata pale msamaria mwema aliyejitokeza kumsitiri msichana huyo kwa fulana yake ambaye pia alipigwa huku fulana hiyo ikichanwa.

Mshauri wa masuala ya sheria kwa wanafunzi kutoka Afrika wanaosoma Bangalore, Bosco Kaweesi alinukuliwa na gazeti la The Chronical akisema hata dereva wa gari alilokuwa  Mtanzania huyo, Micah Pundugu alipigwa na kujeruhiwa vibaya.

 Alisema hata pale msichana huyo alipojaribu kupanda basi ili kujinusuru na zahama hiyo, abiria walimshusha.

Wabunge Wa CCM Wamgomea Magufuli

$
0
0

Kikao cha siri cha wabunge wa CCM kilichoitishwa juzi usiku kujadili mipango ya Serikali kudhibiti matumizi, kimefanikiwa kukwamisha uamuzi wa kuzitaka halmashauri na mashirika ya umma kuingiza mapato yake yote kwenye mfuko mkuu.

Mpango huo, ambao pia ulipingwa na wabunge kutoka vyama vya upinzani, ulilenga kuondoa utaratibu uliopo wa halmashauri, mashirika na taasisi za Serikali kukusanya mapato yake na kuzitumia na badala yake zilitakiwa ziingize mapato hayo kwenye mfuko mkuu na baadaye Serikali itoe fedha kulingana na bajeti inazopelekewa.

Juzi, katika mjadala wa mwongozo wa Mpango wa Bajeti ya Serikali ya Mwaka 2016/17, wabunge hao walipinga uamuzi huo wakisema utaziua halmashauri na wakataka mashirika ambayo yanamilikiwa na Serikali ndiyo yapeleke fedha kwenye mfuko huo. 

Kutokana na mvutano huo, juzi usiku wabunge wa CCM walikutana katika kikao cha ndani kilichofanyika makao makuu ya chama hicho mjini Dodoma, kujadili jambo hilo na kushauri libadilishwe ili kuziokoa halmashauri nchini.

Jana, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene alisema  kuwa tayari Serikali imetoa maelezo.

“Tumetoa maelezo kuwa hatukumaanisha halmashauri wala mifuko ya hifadhi za jamii. Suala hili litayahusu mashirika ya umma pekee,” alisema Simbachawene.

Habari kutoka ndani ya kikao hicho zinaeleza kuwa wabunge hao walimbana Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango kwamba uamuzi huo utazifanya halmashauri kukosa fedha za kufanya miradi yake mbalimbali ikwame.

“Mkutano ulianza saa mbili usiku na kumalizika saa tano usiku. Tulichokubaliana na kufanyika kwa marekebisho ili halmashauri ziendelee na utaratibu kama wa awali, pia kuitaka Serikali kutoihusisha mifuko ya hifadhi za jamii katika suala hili,” alisema mbunge ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe.

“Fedha zitakazokwenda katika mfuko huo ni za mashirika kama Tanesco na Tanapa.Lengo hapo ni kuweka utaratibu mzuri wa matumizi kwamba shirika linaingiza fedha zake katika mfuko, likihitaji fedha litapelekewa kulingana na utaratibu utakaowekwa.”

Chanzo hicho  kilieleza kuwa mifuko ya hifadhi ya jamii haitaguswa kwa sababu fedha zake ni za wanachama na hutumika kwa ajili ya kuendesha miradi mbalimbali.

“Wabunge pia walihoji kama fedha hizo zitaweza kutoka katika mfuko huo na kuzifikia halmashauri katika kipindi hiki ambacho fedha nyingi zinashindwa kufika kwa wakati kutekeleza miradi ya maendeleo,” alisema mbunge mwingine.

Jana, katika mjadala wa mpango huo hakuna mbunge wa CCM wala wa Ukawa aliyegusia suala hilo, kitendo kinachotafsiriwa kuwa jambo hilo limeondolewa kabisa. 

Wachangia mjadala 
Akichangia mjadala wa mpango huo, Mbunge wa Lulindi (CCM), Jerome Bwanausi aliishauri Serikali kuachana na vyanzo vya mapato vilivyozoeleka, badala yake itafute vyanzo vipya.

Katika mpango huo, Serikali ilitaja baadhi ya vyanzo vyake vya ndani vya mapato kuwa ni kodi katika vinywaji mbalimbali, sigara, muda wa matumizi wa simu za mkononi na kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT). 

Katika eneo hilo imeweka uwekezako wa kukusanya Sh4 trilioni. “Watendaji wa Serikali lazima wajifunze kutoka katika taasisi ambazo zina vyanzo vingi vya mapato. Mapato yako mengi tu hata katika nyumba za kupanga na kuziwezesha halmashauri kukusanya mapato zaidi,” alisema.

Mbunge wa Hanang’(CCM), Dk Mary Nagu alisema uchumi wa viwanda unategemea kilimo, mifugo na uvuvi na kuitaka Serikali kuhakikisha inatilia mkazo sekta hizo kwa maelezo kuwa itasaidia kuinua uchumi wa mwananchi mmoja mmoja.

Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Anatropia Teonist alionyesha wasiwasi juu ya utekelezaji wa mipango huo wa Serikali, kutokana na mawaziri wengi kufanya kazi kwa kutafuta sifa katika vyombo vya habari.

Alimtaja Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, kwamba anahusika katika uporaji wa viwanja vya wananchi. 

“Katika sekta ya ardhi kuna matatizo makubwa. Migogoro ya ardhi inarudisha nyuma maendeleo ya watu kwa kiasi kikubwa. Pale Dar es Salaam sasa mnavunja nyumba za watu wa mabondeni. Kutokana na zoezi hilo, zaidi ya watu 99, 000 watakuwa hawana makazi,” alisema.

Alisema kasi ya Serikali kuwaletea wananchi maendeleo ni ndogo na kwamba kwa kipindi cha miaka 15, Serikali imepunguza umasikini kwa asilimia 14 tu.

Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Alhamisi Ya Februari 4

Mahakama Yawaachia Huru Watoto Wa Vigogo Benki Kuu ya Tanzania (BoT)

$
0
0

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewaachia huru watoto wanane wa vigogo waliokuwa wameshitakiwa wakidaiwa kupatiwa ajira katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kutumia vyeti vya kughushi, baada ya kutowakuta na hatia.

Walioachiwa huru ni Justina Mungai, Christina Ntemi, Siamini Kombakono, Janeth Mahenge, Beatha Massawe, Jacqueline Juma, Philimina Mtagurwa na Amina Mwinchumu. 

Hakimu Mkazi Mkuu, Warialwande Lema, aliwaachia huru washitakiwa hao jana, alipokuwa akisoma hukumu ya kesi hiyo iliyochukua takribani miaka minane.

“Mahakama hii imewaona washitakiwa hawana hatia na kuwaachia huru kutokana na upande wa jamhuri kushindwa kuthibitisha mashitaka dhidi yao pasi na kuacha shaka yoyote,” alisema. 

Alisema wakati wa kusikilizwa kwa kesi hiyo, upande wa jamhuri ulileta mashahidi sita na vielelezo kadhaa na baada ya washitakiwa kuonekana wana kesi ya kujibu walijitetea wenyewe na kuleta vielelezo.

Alisema ni jukumu la upande wa jamhuri kuthibitisha mashitaka pasi na kuacha shaka yoyote na kwamba sio jukumu la mshitakiwa kuthibitisha kosa hilo. 

Hakimu huyo alisema wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo, upande wa jamhuri uliwasilisha nakala za vyeti na kwamba ulishindwa kuwasilisha vyeti halisi kuonesha kipi halali na kipi cha kughushi.

Hakimu huyo alisema pia baada ya kufunga ushahidi pande zote ziliomba kuwasilisha hoja za kisheria iwapo zinaona washitakiwa wana hatia ama la, lakini hadi mahakama inatoa hukumu hakuna upande hata mmoja uliofanya hivyo.

Alisema upande wa jamhuri haukuleta shahidi aliyetengeneza vyeti hivyo badala yake walileta nakala tu za vyeti, hivyo upande wa jamhuri umeshindwa kuthibitisha mashitaka pasi na kuacha shaka yoyote.

Alisema upande wa jamhuri kama walikuwa na nia ya kuthibitisha kesi wangemleta mtaalamu wa maandishi ambaye angethibitisha iwapo vyeti hivyo vilikuwa vya kughushi ama la badala yake imebaki hisia tu.

Hakimu huyo alisema mahakama hiyo imesikiliza ushahidi wa kuhisi, kwa upande wa jamhuri kushindwa kuthibitisha mashitaka, hivyo imewaona washitakiwa hawana hatia na kuwaachia huru. 

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, washitakiwa hao walikuwa wakidaiwa kughushi vyeti vya kuhitimu kidato cha nne na kutoa hati za uongo kwa mwajiri wao ambaye ni BoT.

Mwanasheria Mkuu Akemea Wabunge Kushabikia Vurugu

$
0
0

Mwanasheria  Mkuu wa Serikali, George Masaju amewataka wabunge kusimamia utekelezaji wa sheria wanazotunga na si kuhamasisha uvunjaji wa sheria za nchi.

Alitoa kauli hiyo jana wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Konde, Khatib Said Haji (CUF).

Mbunge huyo alihoji kwa nini serikali haiwachukulii hatua watu wanaofanya uhalifu Zanzibar na kama wameshindwa, wananchi wawaadhibu wahalifu hao kwa kuwapiga mawe.

Pia Mbunge huyo alitaka Waziri wa Mambo ya Ndani atamke kama wameshindwa kudhibiti uhalifu huo, wananchi washughulikie wahalifu hao kwa kuwapiga mawe na magari yao.

Akijibu swali hilo mwanasheria mkuu wa serikali, alisema hoja ya Mbunge huyo sio sahihi na kusisitiza,“Waziri hawezi kutamka watu wavunje sheria, wabunge wanatunga sheria wanatakiwa kusimamia utekelezaji wake”.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Angelah Kairuki alisema kuhusiana na hoja kuwa vyombo vya dola vinakiuka haki za binadamu, endapo mbunge huyo ana malalamiko awasilishe kwenye tume ya haki za binadamu ili yapate kushughulikiwa.

Mbunge wa Rombo, Joseph Selesini (Chadema) katika swali la nyongeza alihoji kwa kuwa matukio ya wananchi kuchukua sheria mkononi yanasababishwa na mambo mawili, ikiwemo polisi kwenda kwenye tukio wakiwa wamechelewa na wahalifu wanapokamatwa baada ya muda wanaachiwa.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuf Masauni alisema Jeshi la polisi linajitahidi kufanya kazi, idadi ya polisi haitoshelezi kutokana na polisi mmoja kuhudumia watu 300 hadi 350.

“Wakati mwingine inatokea baadhi ya polisi wana mapungufu na wamekuwa wakichukuliwa hatua za kisheria na wale wanaotenda makosa ya jinai sheria imekuwa ikifuata mkondo wake,” alisema.

Jaji Mkuu Wa Kenya Ataka Mazungumzo Yaendelee Kumalizo Mzozo Zanzibar

$
0
0

Jaji Mkuu wa Kenya Dk Willy Mutunga ameshauri kuendelea na mazungumzo ya kutafuta suluhu ya kisiasa Zanzibar kwa lengo la kuimarisha Muungano wa Tanzania, huku akionesha hofu kuwa ukivunjika unaweza kuwa na athari kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla.

Jaji Mutunga alitoa ushauri huo jana wakati akizungumza na waandishi wa Habari katika ukumbi wa Mahakama Kuu Dar es Salaam.

“Tanzania ina kila cha kujivunia kwani hakuna ukabila, wanajivunia lugha yao, utamaduni na msimamo wa ujamaa. Sidhani kama mmeingia katika ubepari na ukabaila,’’ alisema Jaji huyo na kuongeza kuwa msimamo wa Mwalimu Julius Nyerere ulijali maslahi ya wengine katika masuala mbalimbali ikiwemo uchumi na siasa.

Aidha, alisema Tanzania inafanya vizuri kuliko Kenya katika masuala ya usikilizaji wa kesi. Alisema watajifunza namna ya kusikiliza kesi haraka ili kumaliza mashauri kwa muda.

“Kenya iliwahi kusikiliza kesi tatu kwa zaidi ya miaka 33 hivyo ni tofauti na wanavyofanya wenzetu Watanzania,’’ alisema Jaji Mutunga na kusisitiza kuwa katika Afrika Mashariki, majaji na mahakimu wengi hawachukui rushwa na kwamba njia nzuri ni kuwatoa wanaopokea rushwa.

Wazanzibari Watakiwa Kuhakiki Simu Zao Haraka Ili Kupeka Kufungiwa Ifikapo Mwezi Wa Saba

$
0
0

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imewataka Wazanzibari kuhakiki simu zao za mkononi ili kuepuka kufungiwa mawasiliano ifikapo Julai, mwaka huu kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo ya kuwapo ambazo ni feki.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Unguja jana, Meneja Mawasiliano wa TCRA, Innocent Mungy alisema ni vyema wananchi wote kuhakiki simu zao ili wakati wa kufungia zisizofaa wasikose mawasiliano.

Mungy alisema TCRA imefikia uamuzi wa kutekeleza matakwa ya sheria kutokana na kuwapo kwa vitendo vya uhalifu na uvunjifu wa maadili kwa kutumia simu.

Alisema kumekuwapo na utumiaji wa simu usio mzuri unaofanywa na baadhi ya wananchi, ikiwamo baadhi yao kuzisajili kwa kutumia majina ya watu ili kuepuka kutambulika wanaposhiriki uhalifu.

“Pamoja na kuwapo kwa baadhi ya watu kusajili simu kwa maji na yasio yao, lakini pia kumekuwapo na vitendo vya wizi wa simu. Hivyo tunaamini wazi kuwa njia hii kwa kiasi kikubwa itasaidia jamii, kwani hata mtu akiiba simu kwa mujibu wa taratibu zetu hataweza kuitumia,” alisema.

Meneja huyo alisema mfumo unaotarajiwa kutumika nchi nzima utamlazimisha mtumiaji wa simu kutumia inayokubalika kisheria, huku usajili wake ukiwa hauna mashaka.

Alizitaja baadhi ya njia ambazo mtumiaji wa simu atahitajika kuzizingatia kabla na baada ya kununua kuwa ni kuhakikisha inalingana na mabadiliko ya kiteknolojia na kupewa muda maalumu wa kutumia usiopungua miezi 12.

Naibu Mkurugenzi wa Masuala ya Matumizi ya Mitandao wa TCRA, Thoday Ringo alisisitiza haja ya wananchi kuwa makini kununua simu zenye ubora.

Alisema baadhi ya watu wamekuwa wepesi kununua simu zinazouzwa kwa bei ya chini bila ya kujua madhara yake.

“Napenda kuwatahadharisha ndugu zangu kuepuka kununua simu ovyo, la msingi ujue kuwa zipo ambazo ni feki,” alisema. 
Naibu Mkurugenzi Masuala ya Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano Thadayo Ringo akionesha mfano wa simu orijino kwa waandishi wa habari wakati wa mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Zanzibar Ocean View Kilimani Zanzibar.
Meneja wa Mawasiliano wa Mamlaka ya TCRA Innocent Mungy, akitowa maelezo kwa waandishi wa habari baada ya kuangalia simu zao baada ya kuingiza namba hizo na kugunduwa kuwa ziko salama na siyo feki. kwa bahati nzuri takribani waandishi wote simu zao zilikuwa  orijino.

Tigo Yawapa Wateja Wake Huduma Ya Whatsapp Bure

$
0
0

Kampuni ya Tigo Tanzania ambayo inaongoza kwa mtindo wa maisha ya kidijitali imetangaza huduma ya bure ya WhatsApp kwa watumiaji wa huduma hiyo ikiwa ni mara ya kwanza kwa kampuni ya simu kutoa ofa ya bure ya mtandao huo wa jamii nchini.

Akitangaza upatikanaji bure wa huduma hiyo kwa vyombo vya habarijijini Dar es Salaam, Meneja Mkuu wa Tigo Diego Gutierrez alisema kuwa wateja wote wa Tigo wanaotumia vifurushi vya intaneti vya kampuni hiyo kwa wiki na mwezi watapata huduma ya WhatsApp bure. Tigo ina wateja zaidi ya milioni 10.

Huduma ya WhatsApp ambayo ni maarufu kwenye kutuma ujumbe kwa njia ya simu, ina watumiaji zaidi ya milioni nane nchini Tanzania na duniani inatumiwa na watu wapatao milioni 900. WhatsApp inawezesha watumiaji kubadilishana habari, ujumbe, video na miito ya sauti.

“Kuanzia sasa na kuendelea wateja wote wa Tigo wanaonunua vifurushi vyetu vya wiki au mwezi watakuwa na fursa ya kufurahia WhatsApp BURE. Hili linawezekana kama mteja ana smartphone. 

"Huduma ya bure ya WhatsApp kwa wateja wetu inaonesha jinsi tulivyojikita katika kuboresha mabadiliko kwenye maisha ya kidijitali na hivyo kuongoza kwenye kutoa teknolojia ya hali ya juu pamoja na ubunifu”, alisema Gutierrez.

Kwa Mujibu wa Gutierrez, ili kufurahia huduma hii, jambo analohitaji mteja wa Tigo ni kuwa na kifurushi cha intaneti cha wiki au mwezi ambacho anaweza kukipata kupitia *148*00# à Tigo-Tigo Xtreme/MiniKabangà Wiki au Mwezi + WHATSAPP YA BURE. Huduma hii inapatikana kwa wanaomiliki simu za aina ya Blackberry, Android na Nokia Symbian60.
 
WhatsApp ni huduma dada na huduma ya Facebook ambayo iliingia makubaliano na Tigo mwaka 2014 na kuwapa fursa wateja wa Tigo huduma ya Facebook bure na kwa lugha ya Kiswahili kupitia simu zao.

Ofisa Elimu Atiwa Mbaroni Katavi Akituhumiwa Kumchoma Kisu Na Kumuua Mgoni Wake Aliyemfumania Akifanya Mapenzi Na Mkewe

$
0
0

Polisi mkoani Katavi inamshikilia Mratibu Elimu Kata ya Katuma wilayani Mpanda, Mohamed Muna (59) kwa tuhuma za kumchoma kisu na kumuua mkazi wa kitongoji cha Misheni, Gidison Vincent (32), anayedaiwa kuwa mgoni wake.

Inadaiwa kuwa mtuhumiwa huyo alimuua Gidison baada ya kumfumania ndani ya nyumba yake akifanya mapenzi na mkewe, Ester Kasansa ‘Chuki’ (36).

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari akithibitisha alisema mkasa huo ulitokea Januari 27, mwaka huu saa 02:30 usiku, katika Kitongoji cha Mashineni, Kata ya Katuma wilayani Mpanda.

“Usiku huo wa tukio, mtuhumiwa alimkuta Gidison (sasa marehemu) akiwa ndani ya nyumba yake akifanya mapenzi na mke wake aitwaye Ester, ndipo alipogonga mlango wa chumbani na mgoni wake (marehemu) kutoka nje na kuanza kupambana naye, ambapo mtuhumiwa alimchoma kisu kifuani na kukimbia,” Kidavashari alisema.

Kwa mujibu wa Kidavashari, chanzo cha mauaji hayo ni wivu wa kimapenzi na mtuhumiwa anatarajiwa kufikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi wa awali kukamilika ili kujibu tuhuma inayomkabili.

Pius Msekwa Asema CCM imepoteza Sifa Ya Kuwa Chama Cha Wanyonge

$
0
0

Wakati kesho CCM ikiadhimisha miaka 39 tangu kuzaliwa kwake, kada mkongwe na muasisi wa chama hicho, Pius Msekwa amechambua uwezo na udhaifu wake, akibainisha kuwa kimepoteza sifa ya asili ya kuwa chama cha wanyonge.

Msekwa amesema   kuwa matukio mbalimbali yanayokikumba chama hicho, ikiwamo migogoro baina ya viongozi wake, makundi na tuhuma za ufisadi, yameathiri taswira yake kwa jamii.

Msekwa  ambaye ni katibu mkuu wa kwanza wa Tanu na makamu mwenyekiti mstaafu (Bara), alibainisha kuwa CCM imepoteza sifa yake ya asili ya kuwa chama kinachojali wanyonge na kubebeshwa mzigo wa kuitwa “chama cha matajiri”.

“Migogoro miongoni mwa viongozi, hususan baina ya makundi yanayozozana au kuhasimiana ndani ya chama na tuhuma za ufisadi, imechangia kuifanya CCM ibebeshwe mzigo wa kuonekana kuwa ni chama kinachokumbatia mafisadi,” alisema.

Aliongeza kuwa CCM pia imeathiriwa na kujipenyeza kwa kasi kubwa kwa wafanyabiashara wasio waadilifu katika baadhi ya vikao vyake vya uamuzi.

Hata hivyo, Msekwa alisema ujio wa Rais John Magufuli umeleta matumaini mapya miongoni mwa wananchi juu ya taswira ya chama hicho.

“Nafarijika kwamba uongozi mpya wa Rais anayetokana na CCM, Dk John Magufuli umeleta matumaini hayo mapya miongoni mwa wananchi walio wengi,” alisema.

Alieleza kuwa CCM kupitia viongozi wake, haina budi kuonyesha kwamba inaweza kuleta mabadiliko yenye tija na yenye kuleta matumaini mapya miongoni mwa wananchi walio wengi.

Alisema ukongwe wa chama hicho kwa maana ya kuwa kimekuwapo na kimekuwa madarakani mfululizo tangu nchi ilipopata uhuru wake mwaka 1961, una faida na hasara zake.

“Faida ni kwamba kwa sababu ya uzoefu wake huo wa miaka mingi, kina (CCM) fursa kubwa ya kuendesha shughuli zake vizuri na kuendelea kupata ushindi katika chaguzi zijazo,”alisema.

Alibainisha pia kuwa kitendo cha CCM kuwapo madarakani muda mrefu kinaweza kusababisha hatari inayotokana na hulka ya binadamu.

Alifafanua kuwa wakati mwingine watu wanaweza kutaka mabadiliko tu ya uongozi wa nchi hata kama chama kilichopo madarakani kinafanya vizuri kiasi gani.

“Hatari iliyopo ni watu wanaweza kuchoka tu kuendelea kuwa chini ya uongozi wa chama kilekile na hatari hiyo inakuwa kubwa zaidi pale matendo ya viongozi wake yatakapokuwa mabaya kiasi cha kuwaudhi watu,”alisema. 

Msekwa alisema katika kipindi hicho cha uhai wa CCM, maadili ya viongozi yameporomoka kwa kiwango kikubwa.

Alitaja sababu za kuporomoka kwa maadili kuwa ni pamoja na kuingia katika mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini na ushindani mkali wa kuwania kushika dola uliojikita katika mfumo huo.

Alisema hali hiyo pia inatokana na hatua ya kusitishwa kwa mafunzo ya viongozi, makada na watendaji wa chama hicho yaliyokuwa yakitolewa kwenye vyuo mbalimbali.

“Hatua hiyo ilichukuliwa kutokana na kusitishwa kwa ruzuku iliyokuwa inatolewa na Serikali kwa chama kwa ajili ya kuendesha mafunzo hayo, katika vyuo vya chama vya Kivukoni na vyuo vyake sita vya kanda vilivyokuwa mikoa mbalimbali,” alisema.

Alisema kutokuwapo kwa msaada wa mafunzo ya maadili na uadilifu kwa viongozi, pia kulichangia kuporomosha maadili ndani ya chama.

“Hapo ilibidi kila kiongozi alazimike kutumia akili zake tu katika shughuli zake za uongozi. Kama wasemavyo Waswahili; akili ni nywele, kila mtu ana zake,” alisema.

Alieleza pia kuwa ushindani katika mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini, umesababisha kukithiri rushwa katika uchaguzi.

Alisema hili hujitokeza wakati wa kura za maoni ndani ya CCM ambako baadhi ya makada wake wameanza tabia ya kuwashawishi wapigakura kwa rushwa ili wachaguliwe katika nafasi wanazozitafuta.

Alisema yapo mambo muhimu ya kuzingatia, wakati wa kutafakari chama hicho kilikotoka na kwamba katika kipindi chote hicho kimekuwa kikipata ushindi unaopanda na kushuka katika chaguzi zote zilizofanyika chini ya mfumo wa vyama vingi vya siasa. 

Credit: Mwananchi

Mahakama Ya Rufaa Kuamua Ugomvi Wa Nyumba Kati Ya Afande Suleiman Kova Na Godfrey Nzowa

$
0
0

Mahakama ya Rufaa wiki ijayo inaanza kusikiliza kesi za rufani 50 za jinai na madai katika Kanda ya Arusha ikiwamo rufaa ya makamishna wawili wa Jeshi wa Polisi wanaogombea nyumba ya serikali iliyopo Uzunguni Arusha.

Maofisa hao, Godfrey Nzowa ambaye ni Mkuu wa Kikosi cha Kupambana na Dawa za Kulevya katika Jeshi hilo amemshitaki mahakamani aliyekuwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova akipinga kuuziwa nyumba hiyo. Kamishna Kova hata hivyo amestaafu rasmi mapema mwaka huu.

Kwa mujibu wa orodha ya kesi zitakazosikilizwa na majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa kwa mwezi mmoja mjini hapa, Nzowa anamlalamikia Kova na wenzake kupinga kuuziwa nyumba hiyo aliyokuwa akiishi alipokuwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (RCO) wa Mkoa wa Arusha.

Nyumba hiyo aliuziwa Kamishna Kova akiwa ameshahama mkoani Arusha na wakati inauzwa Nzowa alikuwa akiishi katika nyumba hiyo, familia yake akiwa RCO kabla ya kuhamishiwa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kuendelea na wadhifa huo, Kova akiwa bosi wake.

Orodha hiyo yenye jumla ya mashauri 50 inaonesha mahakama hiyo itasikiliza rufani ya Wakili maarufu jijini Arusha, Median Mwale ambaye amekata rufaa dhidi ya Jamhuri katika kesi yake ya kudaiwa kutakatisha fedha chafu na kujipatia mabilioni ya fedha kwa njia ya udanganyifu akiwa na wenzake watatu.

Rufani hiyo namba 395 ya mwaka 2013 ya Wakili Mwale dhidi ya Jamhuri imepangwa kusikilizwa na majaji watatu, Mbarouk Salim Mbarouk, Bernard Luanda na Semistocles Kaijage watakaosikiliza pia mashauri mengine kabla ya kutoa uamuzi Machi 5, mwaka huu.

Orodha iliyotolewa na Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufaa, E.Y. Mkwizu inaonesha kesi nyingine yenye mvuto ni ile ya wafanyabiashara Philemon Mang’ehe na Gesso Bajuta iliyodumu kwa miaka 20 sasa.

Katika kesi hiyo, Mang’ehe wa Kampuni ya Bukine anamdai fidia ya mamilioni ya fedha Bajuta baada ya kudai kuharibiwa biashara yake ya kusambaza vifaa vya ofisi katika Mahakama ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) mwaka 1996.

Maalim Seif Shariff Hamad Adai Kikwete Ndiye Aliyevuruga Uchaguzi Zanzibar

$
0
0

Mgombea  urais kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad amemtuhumu Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete kwa kuingilia uchaguzi Zanzibar.

Akizungumza kwenye mkutano wa viongozi wa wilaya na majimbo wa chama hicho uliofanyika kwenye Ukumbi wa Majid, Kiembe Samaki visiwani Zanzibar jana, Maalim Seif ambaye ndiye Katibu Mkuu wa CUF alisema, Rais Kikwete amesababisha kuwepo kwa mgogoro mkubwa wa kisiasa na kikatiba.

Alisema, saa chache kabla ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha kutangaza kufuta uchaguzi huo, kituo kikuu cha kutangazia matokeo kilichokuweko Hoteli ya Bwawani kilizingirwa na vikosi vya jeshi na polisi na kwamba kitendo hicho kuwa ni “Mapinduzi ya Kikatiba”.

“Aliyekuwa Amiri Jeshi Mkuu wakati ule alikuwa Rais Mstaafu Dk. Jakaya Kikwete na ndiye aliyepeleka vikosi vile baada ya kuona chama chake kimeelekea kushindwa kwa upande wa Zanzibar,” alisema Maalim Seif na kuongeza;

“Dkt. Shein wala Balozi Seif (Seif Ali Idd) hawamiliki jeshi wala polisi, vile ni vikosi vya Dk. Kikwete wakati ule na hawezi kukwepa lawama ya kuingilia uchaguzi wa Zanzibar.”

Maalim Seif pia amewashutumu baadhi ya viongozi wakiwemo wa dini wanaojaribu kupotosha ukweli na kuunga mkono uamuzi batili wa kurejewa uchaguzi uliotangazwa na ZEC.

Akizungumzia kuhusu vikao vya kutafuta muafaka wa mkwamo wa kisiasa vilivyokuwa vikifanyika Ikulu ya Zanzibar, Maalim Seif alisema katika vikao hivyo walijadiliana na kukubaliana kuwa ZEC imepoteza sifa ya kusimamia uchaguzi.

Alisema, ameshangazwa na kitendo cha ZEC kutangaza uchaguzi wa marejeo, huku viongozi wa CCM walioshiriki mazungumzo hayo wakiunga mkono.
Akizungumzia hali ya kisiasa Zanzibar, Maalim Seif alisema, siasa za nguvu na kimabavu zinazoendeshwa na CCM hazitoisaidia Zanzibar na badala yake zinaweza kuzidisha mgogoro uliopo.

Kauli ya CUF kugomea uchaguzi uliotangazwa kufanyika tarehe 20 Machi mwaka huu, imeungwa mokono na viongozi hao wa wilaya na majimbo visiwani humo wakiwakilisha wananchi na wafuasi wa chama hicho.

Viongozi hao waliunga mkono hatua hiyo iliyotanguliwa na tamko lililotolewa na Baraza Kuu la Uongozi la chama hicho tarehe 28 Januari mwaka huu.

Kwenye mkutano huo walieleza kuwa uchaguzi halali, huru na wa haki ulifanyika tarehe 25 Oktoba mwaka jana ambapo wananchi walio wengi walimchagua Maalim Seif na uchaguzi huo kufutwa bila sababu za msingi.

Uchaguzi Mameya Kinondoni na Temeke sasa kurudiwa.

$
0
0

Uchaguzi wa kuwapata Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni na Manispaa ya Temeke utalazimika kurudiwa baada ya serikali kutangaza Wilaya mpya sita zikiwemo wilaya mbili zinazozigawa Halmashauri hizo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Simbachawene ameeleza hayo jana wakati akitoa taarifa kuhusu uamuzi wa Rais John Magufuli kuridhia kuanzishwa kwa mkoa wa Songwe pamoja na wilaya hizo.

“Kurudiwa kwa uchaguzi wa wa Kinondoni na Temeke hilo halikwepeki. Serikali inafanya haraka kuanzisha mamlaka na ukishakata utawala lazima uchaguzi utatakiwa kurudiwa, na hilo sio jambo geni,” alisema Waziri Simbachawene.

Alisema kuwa kwa kawaida wilaya hizo mpya zitatakiwa kuwa na viongozi ambao wamewachagua na kwamba madiwani watagawanyika kutoka katika halmashauri za mwanzo. Hivyo, watakata kuwa na viongozi waliowachagua.

Halmashauri hizo za zilishafanya uchaguzi ambapo Boniface Jacob (Chadema) alishinda nafasi ya Umeya wa Kinondoni huku Charles Kuyeko (CCM) akishinda Umeya wa Temeke.

Akizungumzia kurudiwa kwa uchaguzi huo, Meya wa Kinondoni, Boniface Jacob alisema kuwa yeye atahamia katika Wilaya ya Ubungo.

“Nitakwenda kugombea Ubungo,” alisema Meya huyo wa Kinondoni.

“Hata hivyo, Kinondoni pia bado itabaki chini ya Ukawa kwa sababu tuna hazina ya kutosha ya madiwani pamoja na wabunge wa viti maalum,” aliongeza.

Naye katibu wa Chadema Kanda ya Dar es Salaam, Henry Kiwelo alieleza kuwa Ukawa hawana wasiwasi na mgawanyo pamoja na marudio ya chaguzi hizo kwa kuwa wanafahamu kuwa watashinda.

Kwa upande wa CCM, Katibu wa Uendezi wa chama hicho Tawala, Juma Simba alipotafutwa alieleza kuwa alikuwa kwenye kikao na asingeweza kuzungumzia suala hilo.

Mbowe Na Zitto Kabwe Wazika Rasmi Ugomvi Wao Wa Muda Mrefu

$
0
0
Uhasama  uliodumu kwa muda mrefu kati ya Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo) na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe sasa ni wazi unaonekana kumalizika.

Hali hiyo inatokana na viongozi hao kwa nyakati tofauti jana kuweka ujumbe kwenye mitandao yao ya kijamii ya facebook na twitter, ambao unaonyesha kila mmoja akijutia makosa yake na kutaka waungane kwa ajili ya kutetea masilahi ya taifa.

Tangu kuanza kwa mijadala mbalimbali bungeni mjini Dodoma wiki iliyopita, Mbowe na Zitto wameonyesha kukubaliana katika misimamo yao na hivyo kuzua maswali kwamba huenda mbunge huyo wa Kigoma Mjini anataka kujiunga na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Mbowe ambaye pia ni kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni, akiwa na Zitto wiki iliyopita waliwaongoza wabunge wengine wa Ukawa kususia kikao cha Bunge kupinga hatua ya Serikali kusitisha matangazo ya moja kwa moja ya Bunge kupitia Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).

Baadaye viongozi hao pamoja na Mwenyekiti wa Chama cha NCCR Mageuzi, James Mbatia, waliitisha mkutano na waandishi wa habari kueleza umma ambavyo Serikali inarudisha taifa katika zama za udikteta kwa kuzuia haki ya wananchi kupata habari.

Katika kikao hicho cha Bunge, Serikali kupitia kwa Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Nape Nnauye, ilitoa taarifa kuwa wanasitisha matangazo hayo ya moja kwa moja ili kubana matumizi ya Serikali yanayofikia zaidi ya Sh bilioni nne kwa mwaka.

Katika ukurasa wake wa facebook na twitter jana, Zitto alinukuu ujumbe wa Mbowe  ambao ulitafsiriwa kwamba ni hatua ya kiongozi huyo wa upinzani kutaka kumaliza tofauti zake za kisiasa na mbunge huyo.

“Kushirikiana na Zitto si jambo la ajabu kama ambavyo umeona tukifanya. Yapo majeraha mengi ambayo tumeyapitia pande zote (Chadema na Zitto) ambayo huwezi kuyatibu kwa siku moja. Yapo ambayo yatapona kulingana na muda. Unaweza kumfanyia mtu kitu kibaya, lakini baadaye ukatambua kuwa umekosea. Chochote katika siasa kinawezekana,”aliandika Mbowe.

Jana kupitia ukurasa wake wa facebook, Zitto ambaye pia ni Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, alisema nafasi ya chama chake bungeni ni upande wa upinzani hivyo atakuwa pamoja na Ukawa.

“Mbowe siku zote amekuwa kiongozi wangu na siwezi kubeza nafasi yake katika kujenga demokrasia nchini. Tulipishana, tulikoseana, tusameheane.

“Mimi binafsi siwezi kuwa mfungwa wa magomvi yetu ya miaka ya nyuma. Nilishasamehe walionikosea na kuomba radhi niliowakosea.

“Tunaweza kupishana kwenye mkakati wa utekelezaji, hatuwezi kupishana kwenye masilahi ya nchi yetu ya kujenga demokrasia na kukataa udikteta.

“Nafasi ya ACT-Wazalendo bungeni ni upande wa upinzani, na hivyo tutakuwa na wenzetu wa upinzani kwenye kujenga hoja zote za kitaifa.

“Mimi nikiwa mbunge wa ACT-Wazalendo, natekeleza kwa vitendo maelekezo ya chama kwa kushirikiana na wabunge wenzangu wa upinzani bungeni.

“Chama chochote makini huweka tofauti binafsi pembeni kwa masilahi mapana ya taifa. Chama cha ACT-Wazalendo kinaamini katika umoja,”alisema Zitto.

Zitto alifukuzwa Chadema na kujiunga na ACT-Wazalendo Machi 21, 2015 chama ambacho hakina ushirikiano na vyama vinavyounda Ukawa, lakini ameonekana kuwa karibu na umoja huo katika vikao vya Bunge la 11 vinavyoendelea mjini Dodoma.

Mwaka 2013, mwanasiasa huyo machachari pamoja na aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu Chadema, Profesa Kitila Mkumbo na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba walifukuzwa kwenye chama hicho, baada ya mfulululizo wa muda mrefu wa mivutano ya uongozi na baadaye wakaanzisha chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT) mwaka 2014.

Chadema ilichukua uamuzi huo baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kutupilia mbali pingamizi la Zitto dhidi ya Kamati Kuu kutojadili uanachama wake.

Picha: Rais Magufuli Azindua Mwaka Mpya Wa Kimahakama Katika Siku Ya Sheria Duniani Jijini Dar Es Salaam Leo

$
0
0
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akipokewa na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman leo jijini Dar es salaam wakati wa maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini. Rais, Dkt. John Magufuli alikua mgeni rasmi. 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli (katikati) akisalimiana na Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson wakati wa maadhimisho ya Siku ya Sheria leo jijini Dar es salaam.
 Wimbo wa Taifa ukipigwa wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Sheria. Kulia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.     Dkt. John Pombe Magufuli (Kulia) akiwa na Jaji Mkuu wa   Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman 
Baadhi ya Viongozi waliohudhuria Maadhimisho ya Siku ya Sheria wakiwa wamesimama wakati wimbo wa Taifa ukipigwa. Kutoka kulia ni Jaji Mkuu wa Kenya Dkt. Willy Mutunga, Jaji Kiongozi wa Tanzania Mhe. Shaaban Lila (katikati) na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Said Mecki Sadiki.
Baadhi ya Viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama  nchini na wadau muhimu wa Mahakama waliohudhuria Maadhimisho ya Siku ya Sheria wakitoa heshima zao wakati wimbo wa Taifa ukipigwa.
Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Charles Rwechungura akitoa salam na ujumbe wa Chama hicho wakati wa maadhimisho ya Siku ya Sheria leo jijini Dar es salaam.
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue (kulia) akifuatilia hotuba zilizokuwa zikitolewa na viongozi mbalimbali wakati wa maadhimisho ya Siku ya Sheria. Kulia kwake ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama Bw. Hussein Katanga.
 Jaji Mkuu wa  Mkuu wa Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman akiwahutubia viongozi, mabalozi na wageni mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi waliohudhuria maadhimisho ya Siku ya Sheria.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akisisitiza jambo kuhusu utendaji wa Mahakama na Utoaji wa Haki kwa wananchi kwa wakati kwenye maadhimisho ya Siku ya Sheria. Mhe. Rais alikuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo yaliyohudhuriwa na viongozi na wageni mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na Majaji wa Mahakama ya Tanzania leo wakati wa kilele cha Siku ya Sheria nchini.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa dini na baadhi ya wakuu wa vyombo vya ulinzi na Usalama na mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao Tanzania wakati wa kilele cha Siku ya Sheria.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na Mawakili.
Jaji Mkuu wa Kenya Dkt. Willy Mutunga (kulia) akimkabidhi zawadi ya kumbukumbu kutoka nchini Kenya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo jijini Dar es salaam. Jaji Mkuu wa Kenya alikua miongoni mwa wageni mashuhuri walioalikwa na Mahakama ya Tanzania kuhudhuria maadhimisho ya Siku ya Sheria.
Wageni mbalimbali waliohudhuria maadhimisho ya Siku ya Sheria wakifurahia Hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.John Pombe Magufuli aliyokua akiitoa leo jijini Dar es salaam.

AUDIO: Msikilze Hapa Rais John Pombe Magufuli akihutubia wakati wa Maadhimisho ya siku ya Sheria nchini.

$
0
0

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewataka Mahakimu na Majaji wa Mahakama ya Tanzania kufanya kazi kwa kuzingatia weledi wa taaluma ya Sheria katika kushughulikia mashauri  yanayopelekwa Mahakamani.

Aidha amewataka Majaji na Mahakimu kutoa hukumu za mashauri  yanayowasilishwa Mahakamani kwa haraka ili kuwasidia wananchi wanaotafuta haki.

Akizungumza na mamia ya wageni kutoka ndani na nje ya nchi waliohudhuria Maadhimisho ya Siku ya sheria, Dkt. Magufuli amewataka Majaji na Mahakimu hao kutanguliza Uzalendo na maslahi ya taifa mbele pindi wanapotoa maamuzi ya mashauri yaliyoko Mahakamani.

 Mhe. Rais amemtaka Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman  kuchukua hatua kwa watendaji wa Mahakama wanaokiuka maadili kwa kufanya vitendo vinavyochafua taswira ya Mahakama mbele ya macho ya jamii.

Aidha, Katika hotuba yake Mhe. Rais amesema kuwa Serikali ya awamu ya tano itaendelea kuijengea uwezo wa kifedha Mahakama ili iweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

==>Bofya  Hapa  Kumsikiliza  Rais  Magufuli  akihutubia

Jaji Mutungi Atoa Usajili kwa Chama kipya cha CM-TANZANIA.

$
0
0
VYAMA vya Siasa nchini vimeaswa kuepukana na migogoro na kutumia vikao vyao katika kuendeleza shughuli zao za kisiasa.

Hayo yamesemwa leo na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Mhe. Jaji Francis Mutungi wakati akikabidhi Cheti cha Usajili wa muda kwa Chama kipya cha Maadili na Uwajibikaji (CM-TANZANIA).

Aidha, Jaji Mutungi amevitaka Vyama vya siasa nchini kufanya siasa na sio uanaharakati kwaki kwa kufanya hivyo malengo yao yatatimia na kuifanya Tanzania kuwa na amani.

‘’Msipende kukimbilia kwenye vyombo vya habari mnapokuwa na migogoro bali malizeni tofauti zenu ndani ya vikao vyenu kulingana na Katiba ya Vyama vyenu’’, alisema Jaji Mutungi.

Aliongeza kuwa, Tanzania inapaswa kuwa na vyama vya siasa vinavyojitambua na vinavyojua wajibu wao katika kuleta maendeleo ya Taifa kwani siasa sio chuki wala uasama.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Maadili na Uwajibikaji (CM-TANZANIA) Bwana Laban Nkembo amesema kuwa, chama hicho kimeanzishwa kwa lengo la kuiweka Tanzania kimaadili na uwajibikaji kwa kuwa kinabeba mambo makubwa mawili yakiwemo Amani na Upendo.

Ameongeza kuwa, chama chao sio cha Upinzani na kinaheshimu chama kilichopo madarakani hivyo, kinaahidi kushirikiana na Chama Tawala kuenzi mazuri yanayofanywa na chama hicho.

 ‘’Chama chetu sio cha upinzani, tunataka nchi nyingine duniani ziwe zinakuja kujifunza Tanzania kuhusu amani na maendeleo tulionayo’’, alisema Nkembo.

Aidha, amebainisha kuwa, chama chao cha CM-TANZANIA kitatoa ajira za kudumu kwa Wanachama wake na hata kwa wale wasiokuwa wanachama ambapo kimeshaandaa Idara ya usimamizi mzuri wa huduma kwa jamii kama vile Wazee, Wajane, Walemavu pamoja na Yatima.

CM-TANZANIA ni Chama cha 23 kupokea usajili baada ya Vyama vingine vya siasa 22 vyenye usajili wa kudumu.
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live




Latest Images

<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>
<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596344.js" async> </script>