Quantcast
Channel: MPEKUZI
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live

James Mbatia achaguliwa tena kuwa mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi

$
0
0
James Mbatia amechaguliwa tena kuwa mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi kwa kipindi cha miaka mitano katika mkutano mkuu wa chama hicho uliofanyika jana jijini Dar es Salaam.

Akizungumza Jumapili Julai 28, 2019 mkuu wa oganaizesheni na utawala wa chama hicho  Florian Mbeo amesema mbali na Mbatia, pia umefanyika uchaguzi wa makamu mwenyekiti Bara na Zanzibar pamoja na wajumbe wa halmashauri kuu.

"Kwa mujibu wa katiba  ya chama chetu ikitokea nafasi mgombea akawa mmoja huwa tunapiga kura za ndio na hapana,” amesema Mbeo akizungumzia uchaguzi huo ambapo nafasi nyingi mgombea alikuwa mmoja.

Amesema nafasi ya mwenyekiti iliwaniwa na Mbatia pekee na kuibuka na ushindi kwa kura 210 za ndio na tisa za hapana.

Mbeo amesema nafasi ya makamu mwenyekiti bara iliwaniwa na Angelina John aliyepata kura 200 za ndio na 19 za hapana.

Waziri Hasunga: Vijana Wakishiriki Ipasavyo Kwenye Kilimo Uchumi Utaimarika

$
0
0
Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Songwe
Mbunge wa Jimbo la Vwawa Mkoani Songwe ambaye ni Waziri wa Kilimo anakusudia kuwakutanisha vijana kwa ajili ya kongamano la kujadili fursa zilizopo katika sekta ya Kilimo.

Waziri Hasunga ameyasema hayo tarehe 28 Julai 2019 wakati akizungumza na vijana wa Jimbo la Vwawa katika kikao kazi kilichofanyika katika ukumbi wa Chama Cha Mapinduzi makao makuu ya Chama hicho Wilayani Mbozi.

Alisema kuwa zaidi ya asilimia 70 ya watanzania wanajihusisha na Kilimo lakini miongoni mwao vijana ni wachache hivyo mkakati huo wa kuwakutanisha vijana ni sehemu ya kueleza kwa viajan fursa zilizopo kwenye sekta ya Kilimo na kuziendeleza.

Alisema kuwa vijana ndio nguvu kazi ya Taifa hivyo kuhusishwa kwenye sekta ya Kilimo ni miongoni mwa mambo msingi yatakayoinua uchumi wa vijana nchini kadhalika kuimarisha uchumi wa Taifa.

Mhe Hasunga amesema kuwa vijana wengi wamekuwa wakijihusisha na mambo yasiyokuwa na tija katika Jamii kama vile kushinda vijiweni badala yake wanatakiwa kufanya kazi kwa bidii ili kuimarisha kipato chao kitakachopelekea vijana kutojihusisha na uovu wa aina yoyote.

Kuhusu kuimarisha masoko ya mazao mbalimbali ikiwemo zao la kahawa, Mhe Hasunga amesema kuwa tayari wizara ya kilimo imeanzisha mkakati kabambe wa kuongeza minada ya kahawa ambapo kwa upande wa Kanda ya ziwa mnada utafanyika mkoani Kagera, Kanda ya Kaskazini utafanyika Manispaa ya Moshi, Kanda ya kusini utafanyika wilayani Mbinga na Kanda ya nyanda za juu kusini mnada wa kahawa utafanyika Wilayani Mbozi.

Ameongeza kuwa kuongeza minada ya uuzaji wa zao la kahawa utatoa fursa kwa wakulima kunufaika na mazao yao kwa kuuza kwa bei nzuri na kulipwa kwa wakati.

Mhe Hasunga amewasihi wakulima mkoani Songwe na Taifa kwa ujumla wake kujishughulisha zaidi na Kilimo kwani ndio sehemu pekee yenye uwezo wa kuwaongezea kipato chao.

Kuhusu kadhia ya mbegu feki kwa wakulima Mhe Hasunga amesema kuwa serikali imejipanga kuimarisha upatikanaji wa viuatilifu kwa wakati na kwa bei nafuu ili wakulima waweze kuvimudu.

"Kumekuwa na mbegu nyingi mtaani ambazo sio sahihi kwa maana hiyo sasa serikali inachukua hatua kali kwa wafanyabiashara wanaojihusisha na biashara hiyo punde watakapobainika" Alikaririwa Mhe Hasunga

MWISHO.

Utomvu Ni Dhahabu Nyingine Inayopatikana Katika Shamba La Sao Hill.

$
0
0
NA FREDY MGUNDA,IRINGA.
Watanzania kuanza kunufaika na zao la miti kutokana na uvunaji wa utomvu kutoka kwenye miti ya kupandwa iliyopo kwenye Shamba la Sao Hill lililopo Mufindi mkoani Iringa kwa kuiliingizia taifa zaidi ya shilingi bilioni mbili kwa kupindi cha miaka miwili ya majaribio.

Hiyo imebainika wakati wa ziara ya baadhi ya viongozi wa wilaya ya Chato,Mkoa wa Geita na viongozi wa vijiji vinavyolizunguka Shamba la Miti la Biharamulo lililopo mkoani Geita baada ya kutembelea Shamba la Miti Sao Hill linalosimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa lengo la kujifunza shughuli mbalimbali za uendeshaji katika shamba hilo.

Akitoa ufafanuzi mkurugenzi wa Rasilimali Misitu na Nyuki TFS, Zawadi Mbwambo alisema kuwa Shamba la Miti Sao Hill wameanziasha mradi mpya wa kuvuna utomvu ambao umekuwa unatengenezewa gundi kwa ajili ya kutumika kwenye bidhaa mbalimbali kulinga na mahitaji ya wahusika.

“Tumeanza kugema utomvu kwenye miti mikubwa kwa kuwa tupo kwenye majaribia lakini wataalamu wamesema kuwa ukianza kugema utomvu mti ukiwa na umri mdogo basi utagemwa kwa muda mrefu na kuleta faida kwa wananchi na taifa kwa ujumla, na kumbukeni kuwa hapa mti haukatwe unaendelea kustawi tu” alisema Mbwambo

Mbwambo alisema kuwa takwimu za dunia zinaonyesha kuwa inawezekana utomvu ukawa unalipa zaidi ya zao la miti hivyo utafiti ukimalizika yawezekana wakulima wa miti wakahamia kwenye uvumaji wa utomvu.

“Kwa takwimu hizo sio muda faida kubwa itakuja kwa wananchi na serikali kwa ujumla maana inaonyesha dhahili kuwa utomvu unalipa sana kuliko mbao hiyo watafiti waliopo hapa katika shamba la Sao Hill ukizaa matunda basi utahamia kwa wakulima wa miti” alisema Mbwambo

Mbwambo alisema kuwa miti milioni tatu kila mwaka ndio inatumika katika uvunaji wa utomvu na hakuna eneo maalum ambao limetengwa kwa ajili ya kuvuna bali wametoa maeneo ambayo yanamiti ambayo inatarajiwa kuvunwa baada ya miaka miwili ijayo

“Shamba hili la Sao Hill ni kubwa sana linakaribia kuwa na hekta laki moja na elfu hamsini na nne hivyo sio rahisi kufanya majaribio shamba lote hiyo tumetoa eneo ambalo miti yake inatarajiwa kuvunwa baada ya miaka miwili” alisema Mbwambo

Mbwambo alisema kuwa soko la utomvu duniani kwa sasa linategemee kutoka nchi China hivyo soko lipo huko na kampuni ya AATY Limited ya kichini inavyovuna hapa katika shamba la Sao Hill na ni kampuni kubwa kuliko zote dunia za uvunaji wa utomvu duniani.

Akizungumza kwenye eneo la tukio mkuu wa msafara huo Mkuu wa Wilaya ya Chato Mhe. Eng. Mtemi Msafiri alisema kuwa wamejifunza kitu kipya ambacho hawakuwahi kukifikiria katika maisha yao kuwa uvunaji au ugemaji wa utomvu unalipa kwa namna hiyo.

“Navyo sema kuwa sasa tumegundua dhahabu ya kijani namaanisha hivi,utomvu unaigiza fedha nyingi tumeana hapa mkurugenzi katueleza hivyo ni lazima tuchukue swala hili kwa umuhimu stahili ili hata kweli kwetu Chato tutalifanya kwa umakini mno” alisema Msafiri

Shamba la Sao Hill lililopo hapa Mufindi lilianzishwa kwa majaribio mnamo mwaka 1939 hadi mwaka 1951 na upandaji kwa kiasi kikubwa ulianza rasmi mwaka 1960 hadi 1980 na shamba hilo linaukubwa wa hekta 135,903 ambazo zimehifadhiwa kwa ajili ya upandaji wa miti na uhifadhi wa mazingira na shamba hilo ni miongoni mwa mashamba 23 ya miti ya kupandwa ya serikali ambayo yanasimamiwa na wizara ya maliasili na utalii kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).

Vijana Mkoani Kagera Wahimizwa Kujitokeza Kugombea Nafasi Mbalimbali Za Uongozi

$
0
0
NA AVITUS BENEDICTO KYARUZI, KAGERA
Mwenyekiti wa umoja wa vijana wa chama cha mapinduzi ccm taifa Kheri James amewataka vijana wenye sifa mkoani Kagera kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbali mbali kuanzia serikali za mitaa  ili waweze kuwatumikia wananchi katika maeneo yao.

Bwana Kheri James ametoa kauli hiyo july 27 mwaka huu katika uzinduzi wa Kagera ya kijani  uliofanyika katika uwanja wa Hamgembe uliopo katika manispaa ya Bukoba mkoani hapa.
 
Mwenyekiti huyo  amesema vijana ni nguzo kubwa katika ujenzi wa taifa hivyo wajitokeze ili kuwatumikia wananchi wao .
 
Ameongeza kuwa muda  wa kukaa vijiweni kwa vijana umeisha ambapo ametumia muda huo kuwahimiza viongozi waliopitia siasa kuwafundisha vijana wanaowania nafasi mbali mbali katika chama hicho kuwa na maadili mema ndani na nje ya chama hicho.
 
Ameongeza kuwa vijana watumie fulsa mbali mbali zitakazo wawezesha kupata mikopo kwani serikali ipo bega kwa bega na makundi muhimu likiwemo la vijana katika uzinduzi huo 

Bwana James amechangisha shilingi milioni kumi  zitakazotumika kuboresha  jengo la mkuu wa mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Elisha Marco Gaguti huku akipongeza juhudi za mkuu huyo wa mkoa katika maendeleo ya Kagera.

THRDC Yawataka Watu Ambao Sauti Zao Zimedukuliwa na Kusambazwa Mitandaoni Wafungue Kesi Mahakamani

$
0
0
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) umewataka watu ambao sauti zao zimedukuliwa na kusambazwa mitandaoni kufungua kesi mahakamani.

Umesema kesi hizo zikifunguliwa, wahusika wanaweza kuwashtaki watu au taasisi wanazodhani kuhusika kwa maelezo kuwa kitendo hicho ni kinyume na katiba ya Tanzania.

Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa, alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ushauri wa hali ya faragha na usalama wa mawasiliano.

"Suala la mawasiliano binafsi limelindwa kikatiba na kisheria kama haki ya faragha, zipo mamlaka ambazo zimeruhusiwa na sheria kuweza kuchukua taarifa binafsi za mtu kwa matumizi maalamu  lakini hazipaswi kubadilika kuwa za umma," alisema Olengurumwa.

Kauli hiyo ya THRDC imekuja zikiwa siku chache baada ya Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saeed Kubenea, kutaka TCRA kuwachukulia hatua wanaohusika na vitendo hivyo vya udukuzi.

Kubenea alisema hayo baada ya kudaiwa kuwa mawasiliano Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye na makatibu wakuu wastaafu wa CCM, Abdulrahman Kinana na Yusuph Makamba, yamedukuliwa na kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii.

Jambo hilo lilibuka baada ya Kinana na Makamba kumwandikia barua Katibu wa Baraza la Ushauri la Viongozi Wakuu Wastaafu wa CCM, Pius Msekwa, wakilalamikia kile walichodai kuwa wamedhalilishwa na mwanaharakati Cyprian Musiba.

Olengurumwa alisema serikali inapaswa kutunga sheria hiyo ili kuepusha ukiukwaji wa haki ya faragha itakayoendana na Katiba ya Tanzania na mikataba mingine ya kimataifa kuhusu haki ya faragha na mawasiliano.

Alisema kifungu cha 16 (1) cha Katiba ya Tanzania kinaeleza kuwa: "Kila mtu anastahili kuheshimiwa na kupata hifadhi kwa nafsi yake, maisha yake binafsi na familia yake na unyumba wake, na pia heshima na hifadhi ya maskani yake na mawasiliano yake ya binafsi."

Pia alisema THRDC inawataka watoa huduma za mawasiliano kuhakikisha wanalinda heshima ya biashara zao kwa kulinda taarifa za faragha za wateja wao na kwamba wananchi ambao haki zao za faragha zimevunjwa wanapaswa kwenda kufungua kesi mahakamani.

"Watu wote ambao haki yao ya faragha imevunjwa, wanahimizwa kufungua kesi katika Mahakama Kuu Kanda yoyote nchini, kuwashtaki watoa huduma au watu binafsi walioingilia kwa namna yoyote kudukua na kutumia mawasiliano hayo bila hati ya ruhusa ya mahakama," alisema Olengurumwa.

Alisema watu hao wanaweza kwenda kufungua kesi na kushtaki watoa huduma za mawasiliano kwa kuwa ni kosa kuvujisha mawasiliano ya mtu bila ya lidhaa.

Akamatwa Kwa Kumhonga Rushwa Mkuu Wa Wilaya

$
0
0
TAKUKURU Mkoa wa Dodoma leo inatarajia kuwafikisha mahakamani watu saba (7) ambao tunawashikilia kwa kujihusisha na vitendo vya kuomba na kupokea rushwa kinyume na kifungu cha 15(1)a na kuahidi na kutoa rushwa kinyume na kifungu cha 15(1)b vyote vya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya mwaka 2007.

Kwanza tunawashikilia wanaume wawili ambao ni Bw. Bahadur Abdalah Hirji (68), Mfanyabiashara na mkazi wa Mtaa wa Tembo Kata ya Madukani Jijini Dodoma na mwanaye Bw. Nahid Bahadur Hirji (33) ambaye ni Mhasibu wa kampuni ya Victory Bookshop Ltd ya Jijini Dodoma kwa kosa la kuahidi na kutoa hongo ya shilingi milioni moja na laki mbili (1,200,000/=) kwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mhe. Petrobas Paschal Katambi ili asifuatilie mapungufu katika utekelezaji wa amri ya Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Dodoma ya kukazia hukumu lililowasilishwa kwake na dada wa Bahadur Hirji.

Baada ya kupata taarifa ya watuhumiwa kuahidi kutoa fedha hiyo kama kishawishi kwa Mkuu wa Wilaya, tulianza kuwafuatilia na kufanikiwa kuwakamata tarehe 27 Julai, 2019 majira ya saa kumi na moja jioni katika Hoteli ya Royal Village, Area D Jijini Dodoma mara baada ya mtuhumiwa Nahid kumkabidhi Mkuu wa Wilaya rushwa hiyo.

Pia tunamshikilia Bw. Omary Said Mtauka ambaye ni Msaidizi wa Mtendaji wa Kata ya Makutupora iliyopo Jijini Dodoma ambaye aliomba na kupokea hongo ya Shilingi laki moja na elfu kumi (110,000/=) kutoka kwa Mzee mwenye umri wa miaka sabini na nane (78) aitwaye Paulo Mawope, mkazi wa Chilungule Kata ya Makutupora ili amalize tuhuma dhidi yake za kugombana na jirani zilizowasilishwa kwa Mtendaji wa Mtaa na baadaye ofisi ya Kata.

Awali, tulipokea taarifa kutoka kwa Mjukuu wa Mzee huyo kwamba alipigiwa simu na ‘Mtendaji wa Kata ya Makutupora’ akitakiwa kutoa fedha hizo ili babu yake aliyekuwa ameshtakiwa katika ofisi ya Kata aachiwe.

Uchunguzi wetu uliweza kuthibitisha uwepo wa suala la Mzee huyo kushtakiwa na jirani yake, kushikiliwa na kutakiwa kutoa fedha ili suala hilo limalizwe na tulifanikiwa kumnasa mtuhumiwa baada ya kupokea hongo hiyo majira ya saa mbili usiku wa tarehe 25 Julai, 2019 katika Bar ya Mama Lili iliyopo Makutupora Jijini Dodoma.

Baada ya kumkamata tulibaini Mtuhumiwa ni Msaidizi wa Mtendaji wa Kata ya Makutupora na alikamilisha uhalifu wake kwa kujifanya ni Mtendaji wa Kata.

Aidha, tunamshikilia Bw. Stanley John Motambi (34) ambaye ni Mtendaji wa Kijiji cha Matumbulu kilichopo Kata ya Matumbulu Jijini Dodoma kwa kosa la kuomba na kupokea hongo ya shilingi elfu sitini na tano (65,000/=), kinyume na taratibu za utendaji, kutoka kwa ndugu za Bw. Wilfred Mnyambwa Mtundu ambaye alikuwa na shauri la mgogoro wa ardhi mbele ya Mtendaji wa Kijiji, kama kishawishi ili asikilize shauri hilo baada ya kutembelea eneo lenye mgogoro.

Baada ya kupata taarifa tulifanya uchunguzi na kuthibitisha kwamba Mtuhumiwa alitenda kosa hilo tarehe 3 Juni, 2019.

Watuhumiwa wengine ni Bw. Venance Msafiri Mayo (34) na Bw. Sulaith Abdul Rusheke (33) ambao ni walimu wa Shule ya Sekondari Viwandani iliyopo Kata ya Viwandani Jijini Dodoma ambao waliomba na kupokea hongo ya shilingi elfu ishirini (20,000/=) ili wampatie cheti cha utambulisho wa kusoma shule (leaving certificate) mtoa taarifa aliyekuwa mwanafunzi wa shule hiyo.

Awali, wakati mwanafunzi huyo alipotaka kuomba nafasi ya kozi fupi katika Taasisi fulani alitakiwa awasilishe cheti hicho hivyo akaenda shuleni hapo na ndipo watuhumiwa wakamtaka, kinyume na utaratibu, atoe rushwa ili wampatie cheti hicho na ndipo akatoa taarifa kwetu.

TAKUKURU ilifuatilia taarifa hiyo na majira ya saa nne na nusu asubuhi tarehe 26 Julai, 2019 kufanikiwa kumkamata Mtuhumiwa Mayo akiwa kwenye Bajaj yenye namba ya usajili MC686BHK iliyoegeshwa nje ya uzio wa shule baada ya kupokea hongo hiyo na kumkabidhi mhusika cheti.

Mtuhumiwa alienda katika eneo hilo akiwa na mhuri wa Mkuu wa Shule na cheti husika na alikigonga mhuri na kumpatia mtoa taarifa wetu baada ya kupokea fedha hiyo. Baada ya hapo tulimkamata pia Mtuhumiwa Rusheke kwani alishiriki katika kushawishi hongo hiyo.  Kiutaratibu vyeti hivyo vinatolewa bila gharama yoyote.

Mwingine ni Bw. Abdulhakim Abbas Kabunga (26) ambaye ni mtumishi wa muda wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) Dodoma ambaye tulimkamata mchana wa tarehe 27 Julai, 2019 baada ya kupata taarifa kwamba amepokea hongo ya shilingi elfu thelathini (30,000/=) kutoka kwa mtu mmoja aliyekuwa na uhitaji wa Kitambulisho cha Taifa ili amsaidie kukipata haraka.

Baada ya kuhojiwa mtuhumiwa amekiri kuhusika na kitendo hicho na atafikishwa mahakamani leo.

Nawakumbusha wote wanaofuatilia vitambulisho vyao NIDA kwamba huduma hiyo ni bure na iwapo watatakiwa kutoa rushwa ili wahudumiwe mapema basi watupe taarifa mara moja.

Pia tunaendelea kuwakumbusha watumishi wote wa umma na wakazi wa Dodoma kwa ujumla kuzingatia maadili ya utumishi na kujiepusha na vitendo vya rushwa kwani sio tu kwamba vinaminya haki za wananchi bali pia havina nafasi kwenye mkoa wetu.

Aidha, tunawashukuru wananchi kwa kuendelea kutupa taarifa na kuwasihi waendelee kuwa washiriki wa dhati katika vita dhidi ya rushwa ikiwa ni pamoja na kushiriki kutoa ushahidi mahakamani.

Imetolewa na:

SOSTHENES KIBWENGO
MKUU WA TAKUKURU (M) DODOMA

Mkataba Ujenzi Daraja la Kigongo Busisi Wasainiwa

$
0
0
Na.Mwandishi Wetu –MAELEZO.
Hatimaye historia imeandikwa nchini Tanzania kwa kusainiwa kwa mkataba wa ujenzi wa daraja la Kigongo Busisi katika Ziwa Victoria mkoani Mwanza lenye urefu wa kilometa 3.2, ambao utagharimu jumla ya fedha za kitanzania Bilioni 592.   

Akizungumza Jijini Dar es Salaam katika hafla ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa daraja hilo, Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isaac Kamwelwe, amesema mradi huo utatekelezwa kwa fedha za walipa kodi wa Tanzania bila kutegemea fedha za wafadhili. 

Waziri Kamwelwe alisema mradi wa Kigongo Busisi kama ilivyo miradi mingine ya kimkakati ulipigwa vita sana na baadhi ya watanzania na hata wahisani, amesema hata baadhi ya wanasiasa waliupinga wakidai ni mradi mkubwa sana kwa taifa na hauna tija kwa wakazi wa maeneo hayo na nchi kwa ujumla.  

“Serikali hii ikiamua jambo inalivalia njuga na inahakikisha linakamilika kwelikweli , huu ni mkonga wetu watanzania na haijawahi hata siku moja mkonga ukamshinda tembo hivyo tunafanya na tutafanikiwa kwa sababu tunatumia fedha zetu wenyewe ili hao waliotukatisha tamaa washangae ” Alisema Waziri Kamwelwe. 

Amesemakuwa ni wakati sasa kwa watanzania kutembea kifua mbele kwani sasa kodi zao zinatumika ipasavyo katika kuwaletea maendeleo, ndio maana mradi huo mkubwa unaanza kutekelezwa, sambamba na miradi mingine kama ya umeme wa mto Rufiji pamoja na kuendelea kununua ndege mpya ili  kuimarisha shirika  la ndege. 

Amesema wahisani wengi walikuwa na masharti kwamba wakikuletea fedha wanakuletea na mkandarasi wao, hivyo amesema kwa Tanzania ya sasa haitakubalika kwani kuna mgawanyo wa majukumu na wataalam wa mikataba, kuna wataalam wa manunuzi na hata washauri katika miradi mbalimbali hivyo serikali iko makini sana hasa katika masuala ya mikataba ili wasiingie mikataba ambayo itakuja kuwa kifungo kwa watanzania.  

Waziri Kamwelwe amesema wakati wa ujenzi wa daraja kutakuwa na ajira za kudumu zaidi ya elfu moja na ajira zisizo za kudumu zaidi ya elfu kumi, kwakua fedha ni za watanzania ni wajibu wa serikali kuhakikisha fedha zinawanufaisha watanzania. 

Hafla ya utiaji saini mkataba wa Ujenzi wa Daraja la Kigongo Busisi ulihudhuriwa pia na Waziri wa  nchi  Ofisi ya Rais TAMISEMI Suleiman Jaffo , wakuu wa mikoa ya Mwanza na Geita, wabunge kutoka katika mikoa hiyo pamoja na baadhi ya wajumbe wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya miundombinu. 

Ujenzi wa daraja hilo unatekelezwa na kampuni ya China Civil Engineering Construction  Cooperation kwa kushirikiana na kampuni ya China Railway 15 Bureau Group , na linatarajiwa kuwa na urefu wa kilometa 3.2 pamoja na barabara zenye urefu wa kilometa 1.66. mkoa wa Mwanza. 

Utiaji saini huo ulifanywa na Mhandisi Patrick Mfugale Mtendaji Mkuu wa Tanroads kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Bw.Zhan Jang kwa niaba ya makampuni ya  China Civil Engineering Cooperation na China Railway 15 Bureau Group. 

Mwisho.

Wataalamu Wa Maabara Wapigwa Msasa Wa Usimamizi Wa Vimelea Hatarishi

$
0
0
Na. OWM, ARUSHA
Wataalam wa maabara nchini kwa kutumia Dhana ya  Afya moja ambao ni wataalam wa maabara kutoka sekta ya Afya ya binadamu, Afya ya wanyamapori na mifugo pamoja na mazingira wameendelea kupewa mafunzo ya Msingi ya  Usimamizi na udhibiti  wa vimelea hatarishi  vya kibailojia kwa kuimarisha ulinzi na usalama wa sampuli za vimelea hivyo.

Vimelea hatarishi  vya kibailojia vinaweza sambaza magonjwa kwa wanyama na binadamu iwapo ulinzi na usalama wake hautaimarishwa wakati wa kuvichukua  kwa wanyama, binadamu na mimea  au  wakati wa kusafirisha vimelea hivyo na  kuvipeleka maabara kwa ajili ya Uchunguzi  pia wakati kuvifanyia uchunguzi pamoja na wakati wa kuviharibu mara baada ya kuvifanyia uchunguzi.

Akiongea wakati wa kufungua mafunzo hayo, leo tarehe 29, Julai, 2019,  Mratibu wa Afya Moja Kitaifa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Harrison Chinyuka amefafanua kuwa Mafunzo hayo ni mwendelezo wa mafunzo ya msingi ambayo wataalam hao tayari walishafundishwa mafunzo ya awali ya Usimamizi  na Usalama wa vimelea hatarishi vya kibailojia mnamo mwezi Machi, mwaka huu.

 “Lengo la mafunzo haya ni kuiwezesha nchi yetu kuwa na wataalamu wa maabara wenye uelewa kuhusu dhana za vihatarishi vya kibaiolojia, ikiwemo wakati wa kusafirisha vimelea hivyo na  kuvipeleka maabara kwa ajili ya Uchunguzi  pia wakati kuvifanyia uchunguzi pamoja na wakati wa kuviharibu mara baada ya kuvifanyia uchunguzi” amesema Chinyuka

Wakiongea kwa nyakati tofauti washiriki wa mafunzo hayo wamebainisha kuwa baada ya mfunzo hayo, mienendo na matendo yao wakiwa  maabara itazingatia usalama wa afya zao na usalama wa jamii inayowazunguka pamoja na Usalama wa watanzania, kwa kusimamia na kudhibiti vihatarishi vya  kiulinzi na usalama vitokanavyo na vimelea hatarishi amabavyo wataalamu hao wamepewa dhamana ya kuvifanyia kazi.

Mafunzo hayo ya siku tano, yameandaliwa na DTRA na Sandia National Laboratories na wawezeshaji wa hapa nchini kutoka wizara ya Afya, maendeleo ya Jamii,Jinsia , Wazee na watoto pamoja na Wizara ya Uvuvi na Mifugo, chini ya Uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu.

Afya Moja ni dhana ni dhana inayojumuisha sekta ya afya ya binadamu , wanyamapori, mifugo na  mazingira katika kujiandaa , kufuatilia  na kukabili magonjwa yanayoathiri binadamu ,wanyamapori na mifugo.

MWISHO.

Mbowe azuiwa kufanya mikutano Kumpisha DC Sabaya

$
0
0
Jeshi la Polisi Wilaya wa Hai limemtaka Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe kusitisha mikutano aliyopanga kuifanya kwa sababu DC Lengai Ole Sabaya anafanya ziara, hivyo mikutano itaingiliana, jambo linaloweza kusababisha uvunjifu wa amani.

 Ziara hiyo ya Mbowe ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema ilitakiwa ianze leo lakini iliahirishwa jana Jumapili Julia 28, 2019 baada ya mbunge huyo kufiwa na kaka yake, Meja Jenerali Alfredy Mbowe.

Leo Jumatatu Julai 29, 2019 barua iliyotolewa na Mkuu wa Polisi wilayani ya Hai, Lwelwe  Mpina yenye kumbukumbu namba MB/JH/27/07/2019  kwenda kwa katibu wa mbunge (Mbowe) imezungumzia kusitishwa kwa ziara hizo za Mbowe.

Zuio hilo litakoma DC akimaliza ziara yake; “Kwa busara, sitisha ziara na mikutano unayotegemea kuifanya  hadi mkuu wa wilaya atakapomaliza ziara yake,” inasomeka barua hiyo

Mhagama Aagiza Maafisa Vijana Wazembe Watimuliwe Mara Moja

$
0
0
Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.
Waziri wa Ofisi ya Waziri  mkuu,sera Bunge kazi vijana ,Ajira na Watu wenye Ulemavu ,Mhe.Jenista Mhagama ametoa agizo kwa  katibu mkuu wa Wizara hiyo kuhakikisha anasimamia na kuwaondoa kazini Maafisa Vijana wanaofanya uzembe wa utekelezaji wa Majukumu yao ndani Ya  Halmashauri husika. 

Mhe.Mhagama ametoa maagizo hayo leo Julai 29,2019  jijini Dodoma Katika uzinduzi wa Mafunzo ya  siku tatu ya  ujasiriamali na Usimamizi wa biashara kwa vijana . 

Mhe.Mhagama amesema pamekuwa na kazi ya mazoea kwa baadhi ya maafisa vijana ngazi ya halmashauri na wamebaki kusubiri fedha za mikopo pekee kutoka serikalini badala ya kuwajibika kutafuta fursa kwa vijana hivyo amesema viongozi wa namna hiyo hawana nafasi kinachotakiwa ni kuwaondoa tu. 

Aidha,Mhe.Mhagama ameziagiza taasisi za kifedha hapa hapa nchini kuwa na masharti nafuu ya mikopo kwa vijana kwani sharti la kigezo cha kuweka dhamana ya nyumba kijana hawezi kumudu kwa sababu asilimia kubwa ya vijana wanaishi nyumba za wazazi wao. 

Katibu mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji kiuchumi Bi.Beng’i Isa amesema   kwa miaka mitano wameweza kuwafikia vijana  elfu kupitia program mbalimbali za mafunzo. 

Katibu mkuu Ofisi ya Waziri mkuu,kazi,vijana,ajira  na wenye ulemavu Bw.Andrew Masawe mafunzo ya kurasimisha ujuzi  na mafunzo  mtambuka ya kilimo cha kisasa cha kitalu nyumba yamefikia halmashauri 87  hadi sasa huku kila halmashauri ikifikia vijana mia moja [100]. 

Manaibu mawaziri Ofisi ya Waziri mkuu,kazi,vijana,Ajira na Wenye Ulemavu,Stella Ikupa amesema  Programu hiyo itakuwa jumuishi kwa vijana wote wakiwemo wenye ulemavu  huku Anthony Mavunde akisema vijana wa kitanzania wanatakiwa kujiamini katika suala la maendeleo.

Mafunzo ya Ujasiriamali na Usimamizi  wa Biashara kwa vijana yanakutanisha kutoka mikoa 26 Tanzania bara huku kaulimbiu ikiwa ni “Wezesha vijana kujiunga na Msingi Endelevu wa ajira”.

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Jumanne July 30

Rais Magufuli Atengua Uteuzi wa Mkurugenzi wa Shirika la Bima la Taifa (NIC)

Waziri Mkuu Akagua Ujezi Wa Ofisi Za Halmashauri Na Hospitali Ya Wilaya Ruangwa

$
0
0
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekagua ujenzi wa ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa na ujenzi wa hospitali ya wilaya hiyo.

Waziri Mkuu ambaye ni mbunge wa jimbo la Ruangwa na yuko jimboni kwake kwa mapumziko mafupi, alikagua ujenzi huo jana jioni (Jumatatu, Julai 29, 2019). Jengo hilo linalojengwa na SUMA JKT, linahitaji sh. bilioni 3.77 hadi kukamilika kwake.

Akiwa kwenye eneo la ofisi hizo, Waziri Mkuu alielezwa kwamba Halmashauri hiyo imepokea shilingi milioni 500 kutoka Serikali Kuu kwa mwaka wa fedha 2018/2019 kwa ajili ya ujenzi wa ofisi mpya ya Halmashauri hiyo.

Ujenzi wa ofisi hiyo ambayo ikikamilika itakuwa na ghorofa moja, ulianza Juni mosi, 2019 na unatarajiwa kukamilika Julai, mwakani. Jengo litakuwa na ofisi 33 za chini, ofisi 26 za ghorofa ya kwanza na kumbi mbili za mikutano.

Kazi ambazo zimeshafanyika hadi sasa ni usafishaji wa eneo kwa ajili ya ujenzi; upimaji wa sampuli ya udongo (Geotech Survey); uingizaji wa maji eneo la ujenzi; uchimbaji wa kisima kikubwa cha kuhifadhia maji  na uvutaji wa umeme eneo la ujenzi.

Kazi zinazoendelea kwa sasa ni ufyatuaji wa tofali ambapo hadi sasa jumla ya matofali 10,000 yamekwishafyatuliwa ambayo ni sawa na asilimia 50 ya mahitaji ya matofali yote. Pia ukusanyaji wa vifaa vya ujenzi eneo la ujenzi unaendelea.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu jana alikagua ujenzi wa hospitali ya wilaya hiyo na kukiri kwamba ameridhishwa na kazi iliyokwishafanyika hadi sasa.

Akiwa hospitalini hapo, Waziri Mkuu alielezwa na Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo, Dkt. Mahela Njile kwamba hadi kukamilika kwake, hospitali hiyo itakuwa na majengo 22 yanayokisiwa kugharimu jumla ya sh. bilioni 7.5 kulingana na maksio ya OR-TAMISEMI.

Dkt. Njile alisema katika awamu ya kwanza Serikali imetoa sh. bilioni 1.5 na kuelekeza yajengwe majengo saba ya kipaumbele ambayo ni jengo la uzazi, la wagonjwa wa nje (OPD), maabara, la X-ray, la utoaji dawa, la kufulia nguo na la utawala.

“Serikali imeelekeza ujenzi huu ufanyike kwa kutumia njia ya manunuzi inayoitwa ‘Force Account’ ambapo Halmashauri inanunua vifaa vya ujenzi na kuajiri mafundi wa kujenga majengo yaliyoelekezwa wakisimamiwa na wataalam wa halmashauri na kamati mbalimbali,” alisema.

Akizungumza na wakazi waliojitokeza kumsikiliza hospitalini hapo, Waziri Mkuu aliwapongeza viongozi wa Halmashauri hiyo kwa kusimamia vizuri ujenzi na kwa kuamua kutumia force account ambayo alisema inapunguza sana gharama za manunuzi.

Aliitaka Halmashauri hiyo isisubiri hadi kazi ya ujenzi ikamilike, na badala yake wahusika wajipange na kuanza kufanya usafi wa eneo linalozunguka hospitali hiyo. “Halmashauri tusikae tu kusubiri ujenzi uishe. Tufanye usafi kuzunguka eneo lote, tupande miti na maua ili mandhari ianze kupendeza,” alisema.

Kuhusu muda wa kukamilisha kazi hiyo, Waziri Mkuu aliwashauri mafundi wazidishiwe muda wa kufanya kazi. “Badala ya kufanya kazi mchana peke yake, bora waongezewe muda wafanye hadi usiku ili kufidia muda uliopotea, na uliobakia ni mfupi mno,” alisema.

Alisema anaamini kazi hiyo itakamilika ndani ya muda mfupi ili huduma zianze kutolewa hapohapo Ruangwa na kuwapunguzia wananchi adha ya kwenda hadi hospitali ya Ndanda.

 (mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,       

Agra Kuimwagia Mamilioni Tanzania Katika Utekelezaji Wa Mpango Wa Pili Wa Maendeleo Ya Sekta Ya Kilimo [ASDP II].

$
0
0
Na.Faustine  Gimu Galafoni ,Dodoma.
Serikali ya Jamhuri ya  Muungano wa Tanzania inatarajia kupokea zaidi ya Ya  Dola za Marekani laki sita kutoka Taasisi ya Mapinduzi ya kijani Barani Afrika ( Alience Green Revelotion in Afrika   AGRA)  Katika utekelezaji wa mradi wa mpango wa Maendeleo  ya  sekta ya kilimo  awamu ya pili[ASDP  II]. 

Hayo yamesemwa Julai 29,2019  jijini Dodoma  na Katibu Mkuu ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI Mhandisi . Joseph Nyamhanga wakati akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya kikao kazi cha Ofisi ya TAMISEMI ,Wizara ya Kilimo pamoja na AGRA Kilicholenga mpango mkakati wa maendeleo ya sekta ya kilimo awamu  ya pili[ASDP II  ambapo  amesema kuwa  kuna hatua kadhaa zitafanywa kabla ya kusaini mkataba huo ikiwa ni pamoja na kupata maoni ya Mwanasheria mkuu wa serikali na kuwasiliana na wizara ya fedha na mipango.

Hivyo,Mhandisi Nyamhanga amesema mradi huo utashirikikisha ngazi mbalimbali za Utawala ikiwa ni pamoja na  vijiji,kata,halmashauri,mikoa huku pia akisema  kuwa fedha hizo  ofisi ya TAMISEMI itasimamia ipasavyo kupitia maafisa kilimo na uongozi serikali za  mitaa. 

Naibu katibu mkuu Wizara ya kilimo Siza Donald Tumbo amesema kuwa mpango wa pili wa maendeleo ya kilimo lengo lake kuu  ni kuongeza uzalishaji pamoja na  kuondoa udumavu  na kuondoa dhana ya kilimo kwa ajili ya kuhimili njaa peke yake bali ni kujikita katika kilimo biashara. 

Malengo mengine ya ASDP II ni kuhakikisha upatikanaji wa pembejeo bora za kilimo kwa bei rahisi huku akibainisha kuwa changamoto ya usafirishaji wa Mazao kwa sasa haipo kwani miundo mbinu ya barabara iko vizuri na kilichobaki ni kuzalisha mazao bora  na upatikanaji wa masoko kwa urahisi zaidi.

Vianey Luendela ambaye ni  Meneja wa AGRA Nchini Tanzania amesema  AGRA imekuwa mdau wa maendeleo ya kilimo kwa miaka 15 nchini Tanzania na AGRA imesha wekeza  Dola Milioni 60 za Tanzania toka imeanzishwa katika eneo la kilimo.

Ikumbukwe kuwa ASDP ni mchakato wa muda mrefu uliobuniwa kutekeleza (ASDS), na ndiyo nyenzo kuu (main tool) ya Serikali katika kuratibu na kufuatilia maendeleo ya kilimo ambapo Programu hii inaoanisha utekelezaji kati ya wizara za sekta ya kilimo na wadau wengine na kuleta ufanisi katika mfumo wa usimamizi.  

Aidha, ASDP inaunganisha mahitaji halisi shambani katika ngazi ya wilaya na kuoanisha ufuatiliaji na uimarishaji wa uwekezaji katika ngazi ya kitaifa na kimataifa katika sekta ya kilimo huku Mtazamo mkuu wa ASDS na ASDP ni kuwapa uwezo wazalishaji wadogo, wa kati na wakubwa wa sekta ya kilimo kupata faida kutokana na kuongeza uzalishaji na tija katika shughuli zao. 

Wasiooga na Kufungua Nguo Wapigwa Marufuku Jijini Dar

$
0
0
Mkuu  wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amepiga marufuku watu wasiooga na kuwa nadhifu kuingia katikati ya jiji hilo wakati wa mkutano wa 39 wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) mwezi ujao.

Tayari vijana 130 wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na mgambo 300 wamesambazwa maeneo mbalimbali ya jiji hilo kusimamia usafi wa mazingira.

Akizungumza jana wakati wa kuzindua kampeni ya usafi wa mazingira kama sehemu ya maandalizi ya mkutano huo, Makonda alisema wamejipanga vyema, hasa katika suala zima la usafi kuepuka kumtia aibu Rais Dk. John Magufuli mbele ya marais wenzake.

“Wakati wa mkutano huu hatutarajii kuona watu wachafu mtaani. Tabia ya kuja mjini hujafua, hujaoga, hujanyoosha nguo ni marufuku, mpumzike tu majumbani kwenu.

“Kwa kipindi hiki tuvumiliane, kama hufui nguo, huogi, pumzika kidogo kuja mjini usitutie aibu, na siyo kwamba tunataka usafi tu wa mazingira hapana, usafi pia wa wananchi wetu, watu wamejaa chawa tu hapa,” alisema Makonda.

Pia aliagiza kuanzia sasa wenye magari binafsi watakaotupa taka ovyo wasitozwe faini badala yake wapewe eneo la kufanya usafi kwani baadhi yao wamekuwa na jeuri ya fedha na kwamba kwao faini si adhabu.

Membe Kakiri Sauti Iliyovuja na Kusambazwa Mitandaoni ni ya Kwake

$
0
0
Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi Bernard Membe, amesema sauti zilizovuja hivi karibuni kupitia mitandao ya kijamii ikihumusisha yeye akifanya mazungumzo na mtu asiyefahamika wakijadili juu ya sintifahamu ndani ya CCM ni ya kwake.

Membe ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na vyombo habari, ambapo amesema ni kweli sauti iliyodukuliwa na kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii ni ya kwake asilimia 100 huku akiomba Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania kuingilia kati suala hilo.
 

"Sauti ni za kwangu, ni mimi 100 kwa 100 na nimeifanyia kazi na ninajua imetoka wapi kwa sababu nina miiko ya kuzingatia sisemi.

"Ni sauti ya kwangu kabisa na ninaelewa kila kilichotokea. Unaweza kuingia ugonjwa wa udukuzi, kama wale wanaotoa taarifa hizi za udukuzi hawachukuliwi hatua, 'hackers' (wadukuzi) wapo duniani, wanataka fedha tu.

"Ni kosa la jinai kudukua mawasiliano ndiyo maana dunia nzima huwasikii wanadukuana waziwazi. Hapa kwetu watu wenye wajibu wa kukataza udukuzi ni TCRA (Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano) mitandao yote ipo chini yao.

"Tuna sheria zipo, sheria mpya ya mwaka 2013, sidhani kama imerekebishwa, inakataza katakata udukuzi na dunia nzima hamuisikii ikifanya hayo ". amesema Membe.

Rais Magufuli afika Nyumbani kwa kina Mbowe kutoa pole ya msiba

$
0
0
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ametoa pole kwa familia, kufuatia kifo cha Meja Jenerali Mstaafu Albert Lameck Mbowe aliyefariki dunia juzi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Jijini Dar es Salaam.

Rais Magufuli amekwenda nyumbani kwa Marehemu Salasala Jijini Dar es Salaam na kukutana na familia ikiongozwa na Freeman Mbowe ambaye ni Mbunge wa Hai na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Pamoja na kutia saini kitabu cha maombolezo, Rais Magufuli ameungana na familia hiyo katika sala ya pamoja ya kumuombea Marehemu Meja Jen. Mstaafu Albert Lameck Mbowe.

Baada ya sala hiyo, Rais Magufuli ameitaka familia hiyo iendelee kuwa na umoja na kumtanguliza Mwenyezi Mungu.

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jen. Venance Salvatory Mabeyo amesema pamoja na kustaafu Meja Jen. Mbowe alikuwa mshauri wa karibu wa Jeshi.

Amesema katika utumishi wake wa miaka 36 na siku 27 Jeshini, Meja Jen. Mstaafu Mbowe alitoa mchango mkubwa katika masuala ya fedha.

Meja Jen. Mstaafu Mbowe alizaliwa Januari 1953, alijiunga na Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) mwaka 1973 na alistaafu utumishi Jeshini mwaka 2009.

Jeshi la Polisi Latoa sababu za kumkamata mwandishi wa habari Erick Kabendera

$
0
0
Polisi kanda maalum ya Dar es salaam imethibitisha kumkamata mwandishi wa kujitegemea, Erick Kabendera kwa kutotii wito alioitwa na jeshi hilo. 

Polisi wamesema kuitwa kwake ni kutaka kutoa utata wa uraia wake na wanaendelea na uchunguzi na kumuhoji kama ni Mtanzania.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne Julai 30, 2019, Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Lazaro Mambosasa amesema walimkamata jana Jumatatu Kabendera baada ya kupelekewa wito wa kufika polisi lakini akakaidi.

"Kuhusu taarifa za Mwanahabari Erick Kabendera ni kwamba July 29 tulimkamata nyumbani kwake baada ya kukataa wito wa Polisi, aliandikiwa barua ya wito kwa ajili ya mahojiano akakaidi, utii wa sheria bila shuruti ni muhimu sana ili kuzuia matokeo ya kukaidi wito halali.

"Sababu ya Erick kuitwa ni kuhusiana na utata wa Uraia wake, Polisi wanaendelea kupeleleza kwa kushirikiana na Uhamiaji ili kuhakikisha lile ambalo anatuhumiwa nalo linawekwa mezani ili athibitishe yeye ni Mtanzania kwa kutoa vielelezo mbalimbali.

"Kama Erick angefika alipoitwa angehojiwa na kuruhusiwa, lakini kwa kuwa ana mashaka ya uraia wake akakataa wito, sasa tuko nae na taratibu za upelelezi zinaendelea, hakutekwa, alikamatwa na wakamataji ni sisi na yuko salama.

"Baada ya kumkamata(Erick), kumezuka taarifa kutoka kwa kada mbalimbali kwenye jamii wengine Wanahabari wakiendelea kusema Mwandishi huyo ametekwa, wala hakutekwa aliitwa lakini kwa ujeuri akawa amekaidi wito huo"- Amesema Mambosasa



Mahakama yasema itaifuta kesi ya Halima Mdee dhidi ya Rais

$
0
0
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imesema itaifuta kesi ya kutoa lugha chafu dhidi ya Rais  Magufuli inayomkabili mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee kwa sababu ya shahidi kushindwa kutoa ushahidi wake kwa zaidi ya mara tatu mfululizo.

Hayo yamesemwa leo Jumanne Julai 30,2019 na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba baada ya Wakili wa Serikali, Silivia Mitato kudai wakili anayeendesha shauri hilo amepangiwa kazi nyingine hivyo anaiomba mahakama impe muda ili apitie jalada hilo.

Baada ya kueleza hayo, Hakimu Simba amesema kumbukumbu zake zinaonyesha shahidi Abdull Chembea amefika mahakamani hapo zaidi ya mara tatu na hajawahi kutoa ushahidi.

"Hili shauri mimi nitalifuta kwa kuwa shauri hili lipo tangu mwaka 2017 kila nikija namuona huyu shahidi anakuja lakini hakuna kinachoendelea, naona upande wa mashitaka mnakwamisha shauri lisiendelee, nawapa sharti mtakapokuja awamu ijayo nataka shauri hili liendelee," amesema.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 28 na Septemba 4, 2019 kwa ajili ya kusikilizwa.

Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga Awasili Mkoani Simiyu, Aridhishwa Na Maandalizi Ya Nanenane Kitaifa

$
0
0
Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Simiyu
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga tarehe 29 Julai 2019 amewasili Mkoani Simiyu kwa ajili ya kujionea maandalizi ya Maadhimisho 26 ya sikukuu ya wakulima maarufu kama (Nane Nane) yenye lengo la kuwatambua na kuwaenzi Wadau Wakuu wa Sekta ya Kilimo ambao ni Wakulima, Wafugaji, Wavuvi, Wanaushirika, Wasindikaji wa mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi na maliasili kwa mchango wao mkubwa wanaoutoa katika kuendeleza uchumi wa nchi yetu.

Mwaka huu wa 2019, sherehe hizi zinafanyika Kitaifa mjini Bariadi katika Viwanja vya maonesho ya kilimo Nyakabindi katika Mkoa wa Simiyu hivyo Mhe Hasunga amepongeza Uongozi wa mikoa ya Simiyu, Shinyanga na Mara kwa juhudi zao za kufanikisha kuingiza uwanjani huduma za msingi ambazo ni maji na umeme.

Alisema kuwa jukumu hilo kwa Serikali na Wadau wa Sekta Binafsi ni kuendeleza viwanja hivyo vya Nyakabindi kwa kujenga mabanda ya maonesho ya kudumu na kuboresha huduma muhimu za kijamii ili kuwe na maonesho endelevu yenye sura ya Kitaifa na Kimataifa.

Alisema kuwa Serikali kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali, imeendelea kuongeza na kuboresha viwanja vya maonesho katika Kanda mbalimbali hapa nchini, kwa sasa kuna viwanja nane (8) vya maonesho ya kilimo ambavyo ni Themi (Arusha) Kanda ya Kaskazini inayohusisha mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara;  Mwl. J.K.Nyerere (Morogoro) Kanda ya Mashariki ambayo mikoa yake ni Dar es Salaam, Pwani, Morogoro na Tanga;na John Mwakangale (Mbeya) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini inayojumuisha mikoa ya Iringa, Mbeya, Ruvuma, Njombe, Katavi, Songwe na Rukwa;

Vingine ni Nzuguni (Dodoma) katika Kanda ya Kati yenye mikoa ya Dodoma na Singida; Nyakabindi (Bariadi) Kanda ya Ziwa Mashariki yenye mikoa ya Simiyu, Shinyanga na Mara; Nyamuhongolo (Mwanza) Kanda ya Ziwa Magharibi yenye mikoa ya Mwanza, Kagera na Geita; Ngongo (Lindi) Kanda ya Kusini inayojumuisha mikoa ya Mtwara na Lindi na Fatma Mwasa (Tabora) Kanda ya Magharibi yenye mikoa ya Tabora na Kigoma.

Akizungumza na mtandao wa Wazo Huru Blog, Waziri huyo wa kilimo ameeleza kuwa Wakati wa sherehe hizo za Nane Nane, Wakulima, Wafugaji, Wavuvi, Wanaushirika na Wadau wengine katika Sekta za Kilimo; watapata fursa nzuri zaidi ya kuona na kujifunza mbinu na teknolojia sahihi za uzalishaji na usindikaji wa mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi, maliasili na bidhaa nyinginezo kupitia Maonyesho ya Kilimo yanayoandaliwa.

Aidha, kwa Wafanyabiashara itakuwa ni fursa nzuri ya kutangaza bidhaa zao hususani pembejeo na zana mbalimbali za uzalishaji na usindikaji wa mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi na maliasili.

Aliitaja Kaulimbiu ya sherehe za Nane Nane Mwaka huu ni kuwa ni “Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa ukuaji wa Uchumi wa Nchi”.  Kaulimbiu hii imechaguliwa baada ya kutafakari kwa undani suala zima la Uchumi wa Viwanda unavyoweza kuchangia katika kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja, pato la Taifa na wakati huo huo kupambana na Umaskini.

"Ni ukweli ulio dhahili kuwa Kilimo ni Sekta kubwa na muhimu kwa maendeleo kutokana na mchango wake katika uchumi wa Taifa. Mfano katika mwaka 2017, Sekta ya Kilimo ilitoa ajira kwa Watanzania kwa asilimia 65.5, ikichangia asilimia 28.7 ya pato la Taifa. Sambamba na hilo Sekta ya Kilimo inachangia asilimia 65 ya malighafi za viwandani. Takwimu zinaonesha kuwa katika robo ya kwanza ya mwaka 2018 ukuaji wa Sekta ya Kilimo ulifikia asilimia 7.1" Alikaririwa Mhe Hasunga

Ameongeza kuwa Kaulimbiu ya mwaka huu inahamasisha Wakulima, Wafugaji, Wavuvi na Wanaushirika kuleta mapinduzi katika Sekta za Kilimo kwa kuzalisha kwa tija ili kukuza uchumi wa Mkulima, Mfugaji, Mvuvi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Kadhalika, ametoa wito kwa Wananchi na Wadau wote kushiriki kikamilifu na kuhudhuria kwa wingi maonesho hayo kuanzia tarehe 1 hadi 8 Agosti, 2019.
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live




Latest Images