Quantcast
Channel: MPEKUZI
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live

Korea Kaskazini Yafyatua Makombora Mawili

$
0
0
Korea Kaskazini imerusha kombora la masafa mafupi baharini kulingana na mkuu wa wafanyikazi wa umma nchini Korea Kusini.


Makombora hayo yalizinduliwa mapema siku ya Alhamisi , yakisafiri umbali wa kilomita 430 na kupaa angani umbali wa kilomita 50 kabla ya kuanguka katika bahari ya Japan , ambayo pia inajulikana kama bahari ya mashariki.

Hatua hiyo inajiri baada ya taifa hilo kukasirishwa na mipango ya zoezi la pamoja la kijeshi kati ya Marekeni na Korea Kusini linalotarajiwa kufanyika mwezi ujao.

Korea Kaskazini imeonya kwamba mazoezi hayo yatarudisha nyuma mazungumzo ya taifa hilo kutojihami na silaha za kinyuklia.

Kombora la kwanza lilirushwa mwendo wa saa 05.34 mapema alfajiri na la pili mwendo wa 5.57 kulingana na Korea Kusini.

Makombora hayo yalirushwa karibu na mji wa Wonsan. Haijulikani iwapo kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong un alisimamisha uzinduzi huo.

Mtaalam wa silaha nchini Korea Kaskazini Jeffrey Lewis alisema katika ujumbe wake wa twitter kwamba silaha hizo zilifanana kama zile za makombora ya KN-23s.

Kulingana na Lewis wa Taasisi ya masomo ya kimataifa ya Middlebury , makombora ya Kn-23s yanaweza kubeba kichwa cha kombora la nyuklia na kuruka umbali wa kuweza kulenga vikosi vya Marekani nchini Korea Kusini.

Wizara ya ulinzi nchini Korea Kusini imeambia Pyonyang kusitisha vitendo ambavyo ilisema havisaidii kupunguza hali ya wasiwasi , kulingana na chombo cha habari cha reuters.

Waziri wa ulinzi nchini Japan alisema kuwa kombora hilo halikufika katika maji ya Japan na halikuwa na madhara yoyote kwa usalama wa taifa hilo.

Baada ya kumualika kupitia mtandao wa twitter mnamo mwezi Juni, rais Trump na mwenzake wa Korea Kaskazini walifanya kikao katika eneo linalolindwa sana ambalo linagawanya Korea zote mbili ambapo walikubaliana kuanza upya mazungumzo ya kutojihami na silaha za nyuklia .

Baada ya kikao hicho waziri wa ulinzi nchini Marekani Mike Pompeo alisema kuwa mikutano ya kufanyia kazi mpango huo itaanza mwezi Julai lakini kufikia sasa hakujakua na mikutano yoyote kati ya Marekani na maafisa wa Korea kaskazini.

Lakini Korea Kaskazini imeshutumu mpango wa zoezi la kijeshi la pamoja kati ya Marekani na Korea Kusini mwezi ujao , ikiutaja kuwa ukiukaji wa taarifa ya pamoja iliotiwa saini na rais Trump na bwana Kim katika mazungumzo hayo ya ana kwa ana nchini Singapore mwaka uliopita.

''Korea Kaskazini imekasirishwa kwamba Marekani inafanya zoezi la kijeshi la pamoja na Korea Kusini'', alisema Harry Kazianis wa kituo cha Washington cha Maslahi ya kitaifa ambaye alikuwa akizunguma na reuters.

Mwaka uliopita Bwana Kim alisema kwamba Korea Kaskazini itasitisha majaribio yake ya kinyuklia mbali na majaribio yake ya makombora ya masafa marefu.

Vitendo vya Kinyuklia vinaonekana kuendelea na picha za Setlaiti katika kituo kikubwa cha Korea Kaskazini zilionyesha vitendo fulani , madai ambayo huenda taifa hilo likawa na mpango wa kukusanya vifaa vya kutengeza mafuta ya bomu.

Pyongyang pia inaendelea kuonyesha uwezo wake wa kutengeza silaha mpya licha ya vikwazo vyenye masharti makali.

Mapema wiki hii bwana Kim aliikagua manowari yenye muundo mpya , viliripoti vyombo vya habari vya taifa hilo ambayo inaweza kuimarishwa kubeba kombora la masafa marefu kulingana na wachanganuzi.

Pyongayang pia ilifanya jaribio kama hilo la silaha ya masafa mafupi manmo mwezi Mei.

Ni jaribio lake la kwanza kama hilo tangu ifanyie majaribio kombora lake la masafa marefu mwaka 2017.

Bwana Trump alijibu wakati huo kwa kusema anaamini kwamba Kim hawezi kufanya kitu kinachoweza kuathiri mpango wa kuafikia maaamuzi ya uhusiano mwema.

Alituma ujumbe wa twitter kwamba bwana Kim anajua kwamba niko naye na kwamba hataki kuvunja ahadi yake.

-BBC

Mangula Atoa ONYO Kwa Wanachama wa CCM Walioanza kuusaka ubunge, Udiwani

$
0
0
Makamu  Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Philip Mangula, ameonya wanachama wa chama hicho wanaojipenyeza kuwania ubunge na udiwani wakati viti hivyo bado vina watu.

Alitoa onyo hilo Wilaya ya Ikungi mkoani Singida wakati wa mkutano kuwapongeza wanaCCM wa Jimbo la Singida Mashariki kbaada ya Miraji Mtaturu kutangazwa kuwa mbunge akimrithi Tundu Lissu.

“Natoa maelekezo kuwa mtu yeyote atakayebainika kuanza kujipenyeza kwenye majimbo kuanza kufanya kampeni ya kuwania nafasi hizo za uongozi hatutamwonea huruma, tunamchukulia hatua za kinidhamu,” alisema Mangula.

Alisema katika majimbo kuna wawakilishi ambao muda wao wa miaka mitano bado haujaisha, hivyo waachwe watekeleze ilani ya chama hicho kwa kuwapelekea wananchi maendeleo.

Alisema mwanaCCM mwenye nia ya kutaka nafasi hizo, anatakiwa kusubiri muda utakapofika na wanachotakiwa sasa ni kwenda kwa wananchi kutangaza kazi za maendeleo zilizofanywa na viongozi waliopo madarakani.

Alitoa maagizo kwa wanaCCM kuwa pindi watakapomwona mtu yeyote ameanza kujipenyeza katika majimbo hayo, watoe taarifa ili aweze kuchukuliwa hatua kupitia kamati ya maadili.

Rais Magufuli asafiri kwa treni kutoka Dar kwenda Morogoro

$
0
0
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli  amesafiri kwa treni ya TAZARA kutoka Jijini DSM kuelekea Kisaki Mkoani Morogoro na baadaye atakwenda Rufiji Mkoani Pwani ambako kesho atakuwa Mgeni Rasmi katika sherehe ya kuweka jiwe la msingi mradi wa kuzalisha umeme katika mto Rufiji.

Kabla ya kupanda treni, Rais Magufuli ambaye ameongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli amezungumza na viongozi wa TAZARA na kuwataka kuwasilisha mapendekezo yao juu ya hatua zinazopaswa kuchukuliwa kuboresha usafirishaji wa mizigo na abiria kupitia TAZARA.

Rais Magufuli amesema Serikali inatambua umuhimu wa TAZARA na haiwezi kuiacha ikifanya kazi kwa ufanisi mdogo usiowaleta manufaa Watanzania kama ilivyokusudiwa.

TAZARA iliyojengwa kwa msaada kutoka China, ilianza kutoa huduma mwaka 1975 na inamilikiwa kwa ubia wa asilimia 50 kwa 50 wa nchi ya Tanzania na Zambia.

Reli ya TAZARA yenye urefu wa kilometa 1,860 ina uwezo wa kusafirisha tani Milioni 5 za mizigo kwa mwaka lakini kutokana na uwekezaji mdogo uliosababisha upungufu mkubwa wa injini na mabehewa inasafirisha chini ya tani laki 3 kwa mwaka.

Mkurugenzi Mkuu wa TAZARA Bw. Bruno Chingandu na Meneja Mkuu wa TAZARA Tanzania Fuad Abdallah wamemueleza Rais Magufuli kuwa tayari mapendekezo ya mabadiliko ya sheria yamewasilishwa Serikalini ili kuwezesha kila nchi kuwekeza katika TAZARA kwa lengo la kuboresha usafirishaji wa abiria na mizigo.

Rais Magufuli ameagiza mchakato wa kufanya marekebisho ya sheria hiyo uharakishwe ili juhudi za kununua injini na mabehewa zifanyike haraka.

DC Lengai Ole Sabaya Akana Tuhuma za Kuomba Rushwa kwa Mfanyabiashara

$
0
0
Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya, ametoa ufafanuzi kuhusu kipande cha video kinachosambaa kwenye mitandao ya kijamii, akituhumiwa kuomba rushwa kwa mfanyabiashara na mmiliki wa Hoteli ya Kitalii ya Weruweru River wilayani huko.

Akizungumzia video hiyo katika mkutano wake na waandishi wa habari jana, Ole Sabaya alisema kiini cha kusambazwa kwake ni uamuzi wake wa kumwondoa mfanyabiashara huyo kwenye eneo la ardhi analodaiwa kumpoka mjane, Mary Diriwa (86).

Kipande cha video hiyo kilianza kusambaa juzi kikimwonyesha mfanyabiashara Curthebert Swai, akidai kuombwa rushwa na kiongozi huyo wa wilaya.

Akijibu tuhuma hizo jana akiwa kwenye ardhi ya mjane anayedaiwa kupokwa eneo la ekari moja na robo na mwekezaji huyo, Ole Sabaya alisema: "Na ninyi waandishi wa habari mnanipigia simu kuniuliza juu ya hiyo 'clip' (kipande cha video), mkitaka maelezo yake chanzo chake ndiyo hiki.

"Kwenye taarifa yake, mliyoiona hiyo clip inayozunguka huko, inazungumzia mtu aliyemwomba pesa ya rushwa mara nne, mara ya kwanza, mara ya pili, mara ya tatu na mara ya nne na akisema kwenye hiyo clip kwamba huyu mtu najua siyo, Rais amemtuma.

"Lakini kuna vyombo vya dola hapa, kuna Takukuru (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa) Wilaya, kuna Takukuru Mkoa na unajua huyo mtu anafanya kwa matakwa yake na toka mwezi wa 11, 2018, leo ndiyo unakuja kuchukua hatua uliyoombwa rushwa, baada ya kuchukua mali za hawa kina bibi.

"Kuna 'clip' mnaipeleka huko duniani, anasema kwa mazingira hayo ametishiwa usalama, usalama umetishiwa kwa sababu na yeye ametishia usalama wa wanyonge, kwa hiyo OCD (Mkuu wa Polisi wa Wilaya-Lwelwe Mpina), nakuelekeza kwa sababu na yeye ametoa tuhuma zake hizo akijua kabisa leo (jana) nilikuwa nakuja kufanya uamuzi hapa na ana taarifa hiyo na hata taarifa ya mkutano huu anayo kwamba nitakuja leo tarehe hii."

Akiwa katika mkutano wa hadhara na wananchi wa Kijiji cha Kimashuku, Kata ya Mnadani, Wilayani Hai, Mkuu huyo wa Wilaya amemwagiza Mkuu wa Polisi wa Hai, Lwelwe Mpina, kumhakikishia usalama mfanyabiashara huyo ili haki yake naye itendeke wakati vyombo vya dola vikifuatilia ukweli wa madai yake.

"Kwa hiyo kwanza OCD, fanya hivi mhakikishie Curthebert Swai usalama wake mwenyewe na kwa kuwa wewe ndiyo chombo cha kuhakikisha usalama wake na wewe ili wawe salama," alisema.

"Bibi (mjane aliyedai kunyang'anywa eneo lake), kuanzia tarehe ya leo, tutakuandikia barua, eneo hili ni la kwako na mtu yeyote haruhusiwi kuingilia.

"Zile fedha Sh. milioni 16.3 mlizopatiwa na upinzani kwa ajili ya kusaidia kuandikisha wapigakura wao mngezitumia kuwasaidia watu wanyonge badala ya kuzitumia kuzitumia kunyanyasa wanyonge kama bibi huyu mjane."

Swai akizungumza katika mkutano na TRA, alidai mkuu huyo wa wilaya amekuwa ni kikwazo kwa wawekezaji na wafanyabiashara.

Alisema licha ya kulipa kodi serikalini, kiasi cha Sh milioni 148 kwa mwaka, lakini amekuwa akipokea vitisho na manyanyaso kutoka kwa mkuu huyo wa wilaya na kumlazimisha kumpa fedha.

Alidai mara kwa mara Sabaya amekuwa akivamia katika hoteli yake ya kitalii ya Weruweru River Lodge usiku kwa madai kuwa anakusanya kodi.

Swai alisema Sabaya akiwakuta wafanyakazi na wakashindwa kumpa majibu, huwachukua na kuwaweka mahabusu bila sababu za msingi.

“Amekuwa akija usiku hotelini na ile ni hoteli ya kitalii na alipomkuta meneja na akimuuliza maswali akashindwa kumjibu maana siyo kazi yake, alimchukua na kumweka ndani na kumtoa asubuhi, nilipomfuata kufahamu shida nini, alisema anataka Sh milioni tano, ametumwa na anafanya kazi ya Serikali,” alidai.

Swai alidai kuwa Sabaya alimweleza kwamba anaweza kuitafsiri kauli hiyo kama ni sawa na ya mkuu mmoja wa mkoa nchini ama rushwa.


“Alisema anahitaji hiyo fedha na anaripoti moja kwa moja juu.
Nilimpa milioni mbili, lakini bado alininyanyasa, na nilimfuata mfanyabiashara mwenzangu kuomba ushauri, alinishauri nimpe tu hizo fedha na kuniambia nikicheza na mjinga atanipasua jicho,” alidai.

Alidai baada ya kumpa fedha hizo, alikuja tena na kumpa milioni mbili kwa mara ya pili na mara ya tatu milioni mbili na akarudi tena kuvamia hoteli hiyo na kufanya fujo huku akiambatana na walinzi wake wawili.

“Nimesema haya nikiwa sijui hatima yangu itakuwaje, lakini mpaka sasa nimeshampa Sh milioni 10 na alikuja na kufanya fujo ambapo nilikuwa na mteja wangu mwenye wafuasi zaidi ya elfu 30,000, alimsumbua sana,” alidai.

Alidai mbali na hilo, alikuwa akiwachukua wasanii wa kucheza na nyoka kutoka Kanda ya Ziwa na kuwaleta hotelini hapo na kuwalipa, lakini Sabaya alikwenda na kuwafukuza huku wakiwa wameingia makubaliano ya kufungua bustani ya nyoka (snake park).

“Sijui hatima yangu itakuwa nini lakini nimeamua kuzungumza kwamba tunanyanyaswa tena sana, hatuna amani na kitakachonipata ni yeye, lakini sifikirii kama hata Rais anaweza kukubaliana na jambo kama hili, sisi tunalipa kodi ya Serikali na hatudaiwi kwanini tuteseke?” alisema.

Magufuli aeleza sababu za kumrejesha kazini mkurugenzi TPDC

$
0
0
Rais  Magufuli ameeleza sababu za kumrejesha kazini Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Dk. James Mataragio, aliyesimamishwa kazi mwaka 2016.
 
Akizungumza Ikulu jijini Dar es Salaam jana wakati wa kupokea vipande 22 vya dhahabu vyenye uzito wa kilo 35.34 na fedha zilizodaiwa kuibwa nchini mwaka 2004 katika Benki ya NBC Moshi mkoani Kilimanjaro, Rais Magufuli alifichua mchezo mchafu uliofanywa dhidi ya kigogo huyo.

Alisema mkurugenzi huyo alisimamishwa kazi baada ya kupinga kuuzwa kwa vitalu vyote vya gesi na Tanzania kubaki bila kitalu hata kimoja inachomiliki.

"Huyu mkurugenzi alisimamishwa kazi baada ya kukataa rushwa ya kampuni fulani iliyokuwa inataka vitalu baharini. Alipigania tubaki na vitalu viwili, tuwekeze fedha kidogo kidogo na kuchimba wenyewe kuliko kuwapa vyote wawekezaji," alibainisha Rais Magufuli.

Jumatatu wiki hii, Ikulu ilitoa taarifa kwa umma ikieleza kuwa Rais Magufuli ameagiza kurejeshwa kazini kwa mkurugenzi huyo mara moja.

Mkurugenzi huyo alisimamishwa kazi na Bodi ya Wakurugenzi wa TPDC Agosti 20, mwaka 2016 na Rais amebatilisha uamuzi huo na kumwagiza Waziri wa Nishati kumrejesha kazini haraka.

Chama cha TLP chamteua Rais Magufuli kuwa mgombea wa Urais 2020

$
0
0
Mwenyekiti wa Chama Cha TLP, Augustine Mrema amesema kuwa chama chake kimefikia uamuzi kuhusu uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 hususan nafasi ya urais na wameamua kuwa ‘mgombea wao’ atakuwa Rais John Magufuli.

Mrema ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Parole, amesema kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho ilifikia uamuzi huo hivi karibuni.

Ameeleza kuwa baada ya kutathmini kazi aliyoifanya Rais Magufuli, wameona hakuna haja ya kuweka mgombea mwingine wa urais katika uchaguzi huo bali wamuunge mkono.

“Tulitafakari kwa makini kazi anayoifanya Rais wetu… anafanya mambo makubwa ambayo yamewahi kutendeka ndani ya nchi yetu ukiondoa utawala wa Mwalimu Nyerere ambaye ametuletea uhuru,” alisema Mrema.

“Tukaangalia Rais huyu pia anajaribu kupaisha uchumi wa nchi ulingane na dunia ya kisasa, ametengeneza Reli ya Kisasa, anatengeneza Bwawa la Kuzalisha Umeme Rufiji. Tuliona kwanini tushindane naye, kwanini tupoteze rasilimali za nchi… sisi tukasema tutamuunga mkono Dkt. John Pombe Magufuli, hatutaweka mgombea na tukataka iwe ni message (ujumbe) hata kwa wanasiasa wengine ambao amedai hawana fadhila,” aliongeza.

Aidha, Mwanasiasa huyo mkongwe alieleza kuwa atagombea tena Ubunge wa jimbo la Vunjo na anaamini ataungwa mkono na Rais Magufuli. 

Amesema anarudi kugombea katika jimbo hilo ambalo aliwahi kuwa mbunge wake kwakuwa ameambiwa na wananchi kuwa wanamhitaji tena.

Waziri Mpina awatangazia vita wavuvi haramu

$
0
0
Waziri wa Mifugo na Uvuvi nchini Tanzania, Luhanga Mpina ametangaza vita dhidi ya wavuvi haramu huku akisema hata  akitokea akauawa atateuliwa waziri mwingine atakayeendelea mapambano hayo.

Kauli hiyo ya Waziri Mpina ameitoa kufuatia tukio la mauaji ya watu wanne katika mapambano kati ya wakazi wa Kisiwa cha Siza wilayani Ukerewe na maofisa wa kikosi cha kupambana na uvuvi haramu wa kanda hiyo.

Waliofariki ni pamoja na ofisa mfawidhi wa rasilimali za uvuvi kanda ya Ukerewe, Ibrahim Nyangali (38). Wengine ni Damian Joseph (18), Malanja Malima (18) na Chrisant Christian (47).

Tafrani hiyo ilitokea baada ya maofisa hao waliofika wakitokea Kisiwa cha Ghana kwa ajili ya operesheni hiyo ya kusaka nyavu zinazotumika katika uvuvi haramu.

Jana Jumatano, Julai 24, 2019, Waziri Mpina aliwaongoza waombolezaji kuaga mwili wa ofisa huyo visiwani Ukerewe mkoani Mwanza ambapo alitumia fursa hiyo kutangaza mapambano dhidi ya wavuvi haramu.

“Nawapa pole sana wote katika hili tukio lililotokea. Hamuwezi kushindana na Serikali na hapa natangaza kwamba suala la uvuvi haramu ndio linaanza leo (jana),” alisema Waziri Mpina

“Damu ya hawa, damu ya maofisa iliyomwagika na wananchi watatu iliyomwagwa itaendelea kuwalilia wavuvi haramu wa Tanzania.”

Akizungumza kwa msisitizo, Waziri Mpina alisema, “Na leo (jana) natangaza vita haramu, vita mpya  na tutawasaka kila mahali, tutaimarisha sekta zote kuhakikisha uvuvi haramu unakomeshwa na hata mkiniua leo atateuliwa waziri mwingine, hamuwezi kupona kwa kutumia nguvu.”

TECNO Na TIGO Watambulisha Rasmi Phantom 9

$
0
0
Dar es Salaam, Tanzania, 25/7/2019- Kampuni  maarufu ya simu nchini TECNO ikishirikiana na TIGO imezindua rasmi simu yao kubwa ya  TECNO Phantom 9 ikiwa ni mwendelezo katika matoleo ya Phantom ikiambatanishwa na ofa ya GB 18. TECNO Phantom 9 ni simu ya kwanza katika upande wa TECNO Phantom series kuja na kamera tatu za teknolojia ya AI (AI triple)  zenye 16MP+8MP+2MP. 

Akizungumza na vyombo vya habari Meneja  wa Uhusiano wa kampuni ya TECNO, Bwana Eric Mkomoye alisema kwamba “Katika ulimwengu wa sasa wa smartphone, kamera  zinapata ushindani mkubwa toka kwa kamera za simu  kwani kila mpiga picha  anatambua umuhimu wa kutumia simu yenye kupiga picha vizuri ili kuepuka usumbufu wa kujibebesha mizigo, na TECNO tumelifanyia kazi kupitia Phantom 9 kwani ina kila sifa zenye kukidhi haja ya wateja wetu  wanaopenda kuchukua matukio kupitia kamera za simu zao. 
 
Bwana Mkomoye aliongeza, “TECNO phantom 9 ikiwa kama “flag ship” ya kampuni kwa mwaka huu, TECNO imehakikisha ujuzi si katika upande wa kamera tu bali hata uwezo wa kuhifadhi files na speed ni mkubwa ikipewa uwezo na memory yenye GB 128Rom + 6Ram pamoja na Operating system ya Android Pie (P). lakini vile vile phantom 9 ina AMOLED Screen ya nch 6.4 FHD yenye kupiga picha  zenye rangi halisi na upana zaidi”.
 
Katika uzinduzi huo, Meneja Mawasiliano wa TIGO Tanzania, Bi. Woinde Shisael alizungumza machache kuhusiana na ushirika uliopo baina ya kampuni hizo mbili na namna ambavyo wateja wa Tigo watakaonunua simu hii ya Phantom 9 katika maduka ya Tigo au katika maduka ya wabia wetu watakavyonufaika na ofa ya mpaka GB 96 kutoka TIGO.
 
“TECNO na TIGO tukiwa kampuni pendwa na zenye kujali wateja wetu  tunafahamu ni kwa namna gani wateja wetu wanatamani kwenda sambamba na mfumo wa maisha ya kidigital na kwa kuzingatia hilo tumeileta rasmi Phantom 9  ikiwa na ofa ya mpaka  GB 98 kwa mwaka mzima ili wateja wetu waendelee kufurahia mtandao bora wakiperuzi mitandaoni”.  
 
Wateja wote wanaotaka kununua Phantom 9 wanaweza kuweka oda za awali (pre-order) katika maduka ya TECNO smart hubs yaliyoko Dar es salaam ,mtaa wa samora, kariakoo katika jingo la china plaza na pia mlimani city, kiasi cha shilingi 50,000 kitapokelewa na  siku ya kuja kuchukua simu mteja atamalizia pamoja  na kupewa zawadi maalumu.

TAZARA: Tuko Tayari Kupokea Nakusafirisha Mizigo Na Vifaa Vya Ujenzi Mradi Wa Umeme Rufuji.

$
0
0
Shirika la Reli la Tanzania na Zambia (TAZARA) limekamilisha ujenzi na ukarabati wa Stesheni ya Treni Fuga uliohusisha Stendi kubwa ya kupokea mizigo na vifaa vya ujenzi wa bwawa la kufua Umeme Mto Rufuji.

Akizungumza katika ziara ya kutembelea ujenzi wa huo, Meneja wa Shirika hilo nchini Tanzania, Fuad Abdallah amasema kuwa Serikali ya jamuhuri ya Tanzania imewapa dhamana kubwa ya kutekeleza ujenzi wa stendi hiyo ya kutunzia vifaa vya ujenzi kwa hiyo ni historia kubwa kwa shirika hilo kushiriki katika mageuzi ya kwenda uchumi wa kati wenye viwanda.

 Fuad Abdallah amesema kuwa reli ya TAZARA ipo bega kwa bega katika kutekelezaji wa agizo la Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli katika kushiriki ujenzi wa mradi mkubwa wa kuzalisha umeme na kazi ambayo ilitakiwa kutekelezwa tayari imemalizika kwa sasa stesheni hiyo iko tayari kupokea mizigo kwa matumizi ya ujenzi wa mradi mkubwa wa kufua umeme mto Rufiji.

“TAZARA inajukumu kubwa sana la kuhakikisha mizigo yote mizito inayotakiwa kujenga mradi huu mkubwa wa Serikali, inafika kwa usalama na kwa wakati katika stesheni yetu lakini pia mahali ambapo mradi unajengwa, kwa matumizi ya reli inamaana kuwa kuna mizigo mingine haiwezi kupita barabarani hivyo TAZARA ni jukumu letu kuhakikisha atucheleweshi mradi huu kwa kufikisha malighafi za ujenzi kwa wakati” alisema Fuad Abdallah.

Fuad alisema kuwa Serikali imeimarisha miundombinu ya umeme, maji, vyumba vya kulala na kituo cha kufikia mizigo,kuhifadhi na kusafiriha mizigo, na itajikita zaifdi katika kuboresha miundombinu ya Reli hiyo ambayo inategemewa zaidi katika usafirishaji wa mizigo ya ujenzi wa mradi wa kufua umeme Mto Rufiji.

Kwa upande wake msimamizi wa mradi wa ukarabati wa fuga stesheni, Gideon Mubepi, alisema kuwa kituo hicho cha fuga Stesheni pamoja na Reli  ya kushushia mizigo kimekamilika kwa asilimia mia moja, na kwa wakati mbali na changamoto zilizokuwepo wakati wa ujenzi.

Naye Kamanda wa Polisi TAZARA, ACP Debora Magiligimba alisema kuwa Jeshi la Polisi TAZARA wamejipanga kimamilifu kuhakikisha mizigo inayotakiwa kufika katika mradi huo mkubwa itakuwa salama na kuwezesha mradi huo wa kufua umeme kukamilika kwa wakati.

“Jeshi la Polisi TAZARA, tumejipanga kuhakikisha ulinzi wa vifaa vyote vinavyoshushwa hapa, na ata pale vinavyochukuliwa kwa ajili ya kupelekwa kwenye mradi husika” ACP Debora Magiligimba

Naye  Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Dkt. Tito Mwinuka alisema kuwa  utekelzaji huo wa ujenzi wa bwawa la  kufua umeme utarahisika kwa sababu ya kituo hicho cha  kupokea na kusafirisha,  mizigo na vifaa vya ujenzi, kimefanyiwa ukarabati mkubwa na sasa kipo tayari,hasa uwepo wa stendi ya kuifadhi malighafi za ujenzi katika stesheni ya Fuga.

“TAZARA wamefanya kazi nzuri sana, wameandaa kituo hiki cha Fuga na  wamekijenga vizuri sana na tayari kinauwezo wa kupakua,kuhifadhi  na kuisafirisha malighafi za ujenzi kwenda kwenye mradi huu mkubwa wa kufua  umeme katika bonde la Mto Rufiji na sasa tuna uhakika kabisa hakuna mzigo utakao shindwa kufika eneo husika sababu miundombinu yote ipo salama” Dkt. Tito Mwinuka.
 
MWISHO

Rais Magufuli Waziri Biteko waongea “kitakwimu” sekta ya Madini

$
0
0
Na Issa Mtuwa “WM”– Ikulu DSM
Tukio kubwa la kihistoria lililofanyika Ikulu jijini Dar es salaam tarehe 24/07/2019 la kupokea na kukabidhiana dhahabu yenye uzito wa Kg. 35 iliyokamatwa Kenya ikitokea Tanzania ndio lililo wafanya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na Waziri wa Madini Doto Biteko kuongelea sekta ya madini kwa lugha ya “kitakwimu” (Namba).
 
Katika tukio hilo  Rais Dkt. John Pombe Magufuli alipokea na kukabidhiwa dhahabu hiyo iliyokamatwa Kenya baada ya kutoroshwa kutoka Tanzania siku ya tarehe 15/02/2018 baada ya kuvuka mipaka ya Tanzania na kukamatwa Kenya. Dhahabu hiyo ililetwa Tanzania na mjumbe maalum ambae pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya Monica Juma alie tumwa na Rais Uhuru Kenyata kuja kukabidhi dhahabu hiyo.
 
Akizungumzia mafanikio katika  sekta ya madini mara baada ya kupokea na kukabidhiwa dhahabu hiyo, Rais Magufuli alisema, tangu afanye mageuzi makubwa katika sekta ya madini sambamba na marekebisho ya sheria kumekuwa na mafanikio makubwa katika sekta hiyo. 
 
Alisema kuanzishwa kwa wizara maalum ya kusimamia madini, ujenzi wa ukuta huko Mirerani, uanzishwaji wa masoko ya madini na marekebisho ya sheria vimekuwa chachu ya mafanikio katika sekta hiyo.
 
Rais Magufuli aliyataja baadhi tuu ya mafanikio hayo kuwa ni  kupunguza kodi nyingi kwa wachimbaji wadogo, pia  tangu mwezi Machi 2019 jumla ya masoko 28 ya madini yameanzishwa nchini kote, ongezeko la mapato kutoka sekta ya madini ambapo mwaka 2017/2018 malengo ya makusanyo yalikuwa bilioni 191 lakini wizara ilikusanya bilioni 301 sawa na ongezeko la bilioni 110, mwaka 2018/2019 malengo yalikuwa kukusanya bilioni 310 lakini ikakusanywa bilioni 335 sawa na ongezeko la bilioni 25 na mwaka wa fedha 2019/2020 imekadiriwa kukusanya bilioni 470.35.
 
Kwa upande wa udhibiti wa matukio ya utoroshwaji wa madini, Rais Magufuli alisema, katika kipindi cha miaka mitatu jumla ya matukio 102 yaliripotiwa ambayo yalihusisha madini yenye uzito wa gramu 163, 566,416.45 na Carat 6826.68 huku thamani ya madini yote ikikadiriwa kuwa na zaidi ya bilioni 45.
 
Kwa upande wake Waziri wa Madini Doto Biteko akitoa maelezo kwa Mhe. Rais Magufuli, alisema takwimu za mauzo kwenye masoko ya madini kumekuwa na mafanikio makubwa. Alisema mpaka sasa zaidi madini yenye thamani ya bilioni 136.7 yameuzwa kwenye masoko yote nchini na serikali imepata mrabaha na clearance fee ya jumla ya bilioni 7.7. Aliongeza kuwa dhahabu iliyokuwa inakusanywa kwa mwaka sasa wanakusanya kwa siku moja kutokana na uwepo wa masoko hayo.
 
“Mhe. Rais pale Chunya kwa mwaka tulikuwa tunakusanya Kg. 12 lakini tunavyo zungumza tangu kuanzishwa kwa soko lile tarehe 21/03/2019 mpaka leo tarehe 24/07/2019 jumla ya Kg. 270 zimeuzwa kwenye soko hilo”. Alisema Biteko.
 
Kwa upande wa utoaji wa leseni za uchimbaji, Biteko alisema tangu mwaka 2010 wizara haijawahi kutoa leseni kubwa zenye gharama ya USD 100, lakini mwaka huu wanakwenda kutoa leseni mbili kubwa ambapo mchakato wake umekamilika. Aliongeza kuwa leseni 2673 za wachimbaji wadogo zimetolewa huku leseni za uchimbaji wa kati 32 na leseni 105 za utafiti wa madini zimetolewa.  Biteko aliongeza kuwa mwaka huu pia watatoa leseni 2 ya Refinery kwa ajili ya dhahabu na 1 ya Smelter.
 
Kuhusu wanao hujumu masoko ya madini alisema teyari wamesha ukamata mtandao wa wanaohujumu masoko hayo na mpaka sasa watu 12 wamekamtwa wanaendelea “kupatiwa elimu” polepole na vyombo vya dola.
 
Akimalizia maelezo yake ya kitakwimu kwa Mhe. Rais, Biteko alimwambia Rais kuwa wizara yake inakabiliwa na upungufu mkubwa wa watumishi na kwa upande wa Tume ya Madini pekee inahitaji watumishi 220 hivyo anaomba kibali chake waweze kuajiri watumishi hao ili kuongeza ufanisi wa wizara yake. 

Waziri Mkuu Ataka Ruvuma Iondoe Vikwazo Vya Uwekezaji

$
0
0
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameutaka uongozi wa mkoa wa Ruvuma uendelee kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo na kuondoa vikwazo vyote ili kuvutia wawekezaji zaidi.

“Mkoa wa Ruvuma kama ilivyo mikoa mingine, unazo fursa ambazo zikiendelezwa, zitaleta tija na kusaidia kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wa Taifa letu. Nitoe rai kwa mkoa uendelee kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo sambamba na kuondoa vikwazo vyovyote vya uwekezaji na biashara ili kuvutia zaidi wawekezaji wa ndani na nje,” amesema.

Ametoa wito huo leo mchana (Alhamisi, Julai 25, 2019) wakati akifungua Kongamano la Biashara na Uwekezaji mkoani Ruvuma linaloendelea kwenye uwanja wa Majimaji, Manispaa ya Songea. Pia amezindua Mwongozo wa Uwekezaji wa mkoa huo.

Amesema katika ustawi wa uchumi, nchi nyingi hapa duniani zimeweza kukuza uchumi wao kupitia ujenzi wa viwanda na zikafanikiwa kupunguza umasikini katika jamii zao. Amezitaja nchi hizo kuwa ni Marekani, China, Japani, Korea ya Kusini na Ujerumani.

“Tunapaswa kuiga kutoka wa wenzetu. Ndiyo maana Tanzania pia tunahamasisha ujenzi wa viwanda kuanzia ngazi ya vijiji mpaka mikoa ili tulete mageuzi ya kiuchumi yatakayowezesha upatikanaji wa ajira na hatimaye kuondoa umaskini,” amesema Waziri Mkuu na kuongeza:

“Kongamano hili ambalo kaulimbiu yake ni “Ruvuma itavuma kwa uchumi wa viwanda, wekeza sasa,” imelenga kutangaza fursa za uwekezaji na biashara zilizopo mkoani humu, na  inajipambanua vema na kuendana na azma ya Serikali ya awamu ya tano ya kujenga uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda ifikapo 2025.”

Amesema mchango wa sekta ya viwanda kiuchumi na kijamii nchini ni pamoja na kuongeza pato la Taifa na kupandisha hali ya maisha ya wananchi; kusaidia nchi isiyumbe kiuchumi ikizingatiwa kuwa viwanda vingi havitegemei hali ya hewa kama kilimo; kuboresha urari wa biashara (improve balance of trade) kwa sababu tija yake ni kubwa na hasa zikiuzwa bidhaa nyingi nje ya nchi na kupunguza uagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi.

Amezitaja faida nyingine kuwa ni kuchangia maendeleo ya sekta nyingine kama za kilimo, uvuvi, elimu na madini; kutengeneza ajira kwa wananchi; kuchagiza na kuharakisha maendeleo ya teknolojia na rasilimali watu na kuwezesha matumizi mazuri ya maliasili zilizopo kwa faida zaidi.

Nyingine ni kuleta uhakika wa soko la mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi, misitu na madini kwa sababu hutumika kama malighafi na kuwepo kwa uhakika wa kuingiza fedha za kigeni nchini kupitia mauzo ya bidhaa nje ambapo husaidia kuagiza mitambo, malighafi na bidhaa nyingine ambazo hazizalishwi nchini.

Mapema, akitoa salamu kwa niaba mabalozi wengine, Mwakilishi wa Balozi wa China, Bw. Xian Bing alisema ana uhakika kuwa kongamano hilo litafanikiwa kuleta mabadiliko mkoani humo kwa sababu wana bidii ya kazi.

“Ninaahidi kuleta wawekezaji kutoka China kwa sababu tunataka waje kuleta teknolojia mpya, wafanye kazi pamoja na Watanzania na wawafundishe teknolojia hizo mpya. Tunataka hapa Ruvuma iwe model (mfano) kwa mikoa mingine,” alisema.

Akielezea kwa kifupi kuhusu mwongozo uliozinduliwa na Waziri Mkuu, mtafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Kijamii (ESRF), Dkt. Hoseana Lunogelo alisema walitumia mfumo shirikishi ili kupata mwongozo unahusisha wawekezaji wa ndani.

“Mwongozo huu umezingatia Dira ya Taifa ya 2025 katika kutimiza azma ya Serikali ya kuwa nchi ya uchumi na viwanda, tumeshirikisha wananchi wa mkoa wa Ruvuma ili wasibakie kuwa watazamaji,” alisema.

(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU, 

DC Mpya Wa Ikungi Aapishwa Rasmi Leo Jijini Dodoma.

$
0
0
Na.Faustine  Gimu Galafoni,Dodoma.
Mkuu mpya wa Wilaya ya Ikungi Mkoani Singida   Edward Mpogolo aliyeteuliwa jana usiku na Rais Magufuli ameapishwa leo Julai 25,2019 zoezi lililofanyika   katika makao Makuu ya nchi,Dodoma.
 
Akizungumza wakati akimwapisha mkuu huyo mpya wa Wilaya  ya Ikungi ,Mkuu wa Mkoa Wa SINGIDA Rehema Nchimbi amesema  amesema amempongeza Mkuu Mpya wa Wilaya ya Ikungi Edward  Mpogolo ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa katibu tawala wilaya ya Dodoma Mjini.
 
Hivyo, Mhe.Nchimbi amemtaka mkuu huyo mpya wa wilaya kutekeleza  majukumu yake katika miradi mbalimbali ya wilaya ya Ikungi ili kuwaletea  Maendeleo ya Wananchi.
 
“Singida ni makao makuu mwenza   ya Tanzania ,sasa  wewe mkuu wa wilaya Edward  Mpogolo ni kuwahakikishia watanzania kuwa Singida sio kame,Singida sio masikini,Singida sio njaa.Singida imekuwa ikipokea fedha  nyingi kama mikoa mingine kwani kwa ndani ya miaka minne imepokea zaidi ya Tsh.bilioni mia saba kwa ajili   ya Maendeleo “alisema Nchimbi.
 
Aidha ,Mkuu huyo wa Mkoa Wa Singida amemtaka   mkuu mpya wa Wilaya ya Ikungi kwenda kusimamia mkakati kabambe wa Mkoa Wa Singida ambao umeanzishwa kwa lengo la kupunguza kero za mishahara kwa watumishi ujulikanao kama”Mshahara wangu Uko wapi “huku pia akimtaka kwenda kutatua na kusimamia suala la kilimo hususan kilimo cha Alizeti na korosho Pamoja na Sekta ya kilimo.
 
Kwa  upande wake  Mkuu mpya wa wilaya ya Ikungi Edward  Mpogolo ameahidi kuwa ataenda kushirikiana na halmashauri ya Ikungi katika kusimamia miradi mbalimbali na kuongeza makusanyo ya halmashauri   ili kwa ajili ya Maendeleo ya nchi katika utekelezaji wa Ilani ya  Uchaguzi ya Mwaka 2015.
 
Kabla ya uteuzi huo, Bw. Mpogolo alikuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Dodoma, nafasi ya Katibu Tawala wa Wilaya ya Dodoma itajazwa baadaye.

Ikumbukwe kuwa  hapo jana Julai 24,2019 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli alimteua Bw. Edward Mpogolo kuwa Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Mkoani Singida ambapo Mpogolo anachukua nafasi ya Bw. Miraji Mtaturu ambaye amechaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki lililokuwa linaongozwa na Tundu Lisu [CHADEMA ]ambapo umbunge wake ulifutwa.

Rais wa Tunisia Caid Essebsi afariki dunia

$
0
0
Rais wa Tunisia, Beji Caid Essebsi amefariki dunia leo Alhamisi Julai 25, katika hospitali  ya  kijeshi mjini  Tunis akiwa na umri wa miaka 92, baada ya kuugua kwa kipindi kirefu.

Taarifa zinasema Essebsi alipelekwa  hospitalini hapo jana jioni kwa  mara ya pili  ndani ya mwezi mmoja.

Rais huyo alikuwa kiongozi mkongwe zaidi duniani baada ya Malkia Elizabeth II wa Uingereza na amekuwa  madarakani  tangu  mwishoni mwa mwaka 2014 baada ya kushinda uchaguzi huru wa kwanza kufuatia vuguvugu la maandamano katika mataifa ya kiarabu.

Mapema mwaka huu, Essebsi alitangaza kwamba hatogombea katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa Novemba mwaka huu alisema kwamba muda umewadia kwa kijana kushika nafasi hiyo ya uongozi.

Makamu Wa Rais Kufungua Maonesho Ya Nanenane Kitaifa 2019 Mkoani Simiyu

$
0
0
Na Stella Kalinga, Simiyu
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan anatarajia kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa Maonesho ya Nanenane Kitaifa mwaka 2019, yatakayofanyika Kanda ya Ziwa Mashariki katika Viwanja vya Nyakabindi Mjini Bariadi kuanzia tarehe 29/07/2019 hadi 08/08/2019.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka wakati akizungumza na waandishi wa habari  katika mkutano maalum wa kutoa taarifa kwa Umma uliofanyika  Mjini Bariadi, Julai 24, 2019.

Mtaka amesema Mhe Makamu wa Rais atafungua rasmi maonesho hayo Agosti Mosi, 2019 na waoneshaji mbalimbali zikiwemo Taasisi, Mashirika mbalimbali na wajasiriamali wataanza kuonesha teknolojia, huduma na bidhaa zao Julai 29, 2019 ikiwa ni maandalizi ya ufunguzi rasmi utakaofanywa na Mhe. Makamu wa Rais.

“Shughuli ya ufunguzi itafanywa tarehe 01/08/2019 na Mhe. Makamu wa Rai, haya ni maonesho ambayo yatakaribisha viongozi wa Kitaifa, Agosti 03, 2019 tutakuwa na Mhe. Waziri Mkuu, Agosti 06, 2019 tutakuwa na Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda na Kilele tunatarajia kuwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli” alisema.

Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Omary Mgumba amesema ameridhishwa na maandalizi ya Maonesho ya nanenane yanayoendelea mkoani Simiyu na kutoa wito kwa wakulima na wananchi wote kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kushiriki katika maonesho haya ili kuja kujionea teknolojia mbalimbali zitakazojibu changamoto za wakulima, wafugaji na wavuvi.

Aidha, Mhe. Mgumba ametoa wito kwa waoneshaji kuwa wabunifu katika teknolojia, huduma na bidhaa watakazoonesha ili maonesho haya yawe  chachu ya kuwasaidia wakulima, wavuvi na wafugaji  kuongeza tija katika uzalishaji

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mhe. Adam Malima amesema matarajio ya mikoa ya Simiyu, Mara na Shinyanga inayounda Kanda ya Ziwa Mashariki ni kuwa na maonesho ya tofauti na mwaka jana, lengo likiwa ni kuifanya kanda hiyo kuwa ni mahali pa kudumu pa wakulima, wafugaji na wavuvi kuwa na maonesho ya kilimo biashara.

Maonesho ya Nanenane Kitaifa yanafanyika kwa mara ya pili sasa mkoani Simiyu tangu Kanda ya Ziwa ilipogawanywa katika kanda mbili yaani, Kanda ya Ziwa Mashariki(Simiyu, Mara na Shinyanga) na Kanda ya Ziwa Magharibi(Mwanza, Geita na Kagera) ambapo mwaka huu yanaadhimishwa chini ya kauli Mbiu:-“KILIMO, MIFUGO NA UVUVI KATIKA UKUAJI WA UCHUMI WA NCHI”

MWISHO

Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Ijumaa 26 July


Sampuli ya Mabaki ya Aliyechomwa moto na mumewe kufanyiwa uchunguzi

$
0
0
Mabaki ya mwili wa Naomi Marijani anayedaiwa kuuwawa na mume wake, kisha mwili wake kuchomwa moto na mabaki kufukiwa shambani, yamefikishwa kwenye Ofisi ya Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa lengo la kufanyia uchunguzi wa sampuli za mabaki hayo.

Mkemia Mkuu wa Serikali Dkt. Fidelice Mafumiko, amesema wameyapokea mabaki ya mwili huo na kwamba uchunguzi wa vinasaba katika sampuli hizo imeanza Julai 24.

Dkt. Mafumiko ameongeza kuwa, uchunguzi wa namna hiyo huchukua takribani siku 21, lakini watazifanyia kazi sampuli hizo ndani ya muda mfupi na kwa weledi mkubwa, na kwamba sampuli zinazohusisha mahakama na mauaji majibu yake hutoka haraka ili taratibu zingine ziendelee.

Tangu taarifa za kuuawa kwa Naomi zijulikane, ndugu wa marehemu imewabidi kusubiri majibu rasmi ya vinasaba yatakayothibitisha kama ni kweli yale ni mabaki ya ndugu yao ili waweze kuendelea na taratibu za msiba.

Inadaiwa kuwa Naomi aliuwawa Mei 15, 2019 na mume wake Khamis Luwongo kisha kumchoma na moto wa magunia mawili ya mkaa na kwenda kuyafukia mabaki hayo shambani kwake Mkuranga, ambapo hadi sasa Jeshi la Polisi linaendelea kumshikilia mwanaume huyo kwa upelelezi zaidi.

Serikali Ya China Na Tanzania Kuendeleza Ushirikiano Katika Mapambano Dhidi Ya Malaria

$
0
0
Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China imeahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali ya Tanzania katika mapambano dhidi ya Malaria ili kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi salama isiyo ya maambukizi ya Ugonjwa huo.

Hayo yamesemwa jana na Naibu Waziri wa Afya kutoka Uchina Mhe. Lin Bin alipotembelea Ikwiriri, Rufiji Mkoa wa Pwani katika mradi wa ushirikiano wa pamoja baina ya China na Tanzania katika kudhibiti ugonjwa wa malaria huku akiongozana na mwenyeji wake Waziri wa Afya,M aendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu.

“China kuwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa kimatafa tutaendeleak ushirikiana kwa pamoja katika kusaidia Tanzania inafikia malengo ya kutokomeza ugonjwa wa malaria” amesema Mhe. Lin Bin na kuendelea kusema Ugonjwa wa malaria unatibika na kuzuilikaW aziri Lin Bin amesema kuwa ushirikiano baina ya Tanzania na China umeleta manufaa katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria kwa kupunguza kiwango cha maambukizi ya ugonjwa huo Wilayani Rufiji kutoka asilimia 25 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 4.9 mwaka 2019.

“Kwa muda wa miaka 60 tumekuwa tukipambana dhidi ya ugonjwa wa malaria ambao umeathiri zaidi ya watu milioni 30, na tangia mwaka 2017 hakuna taarifa zilizolipotiwa kuhusu ugonjwa wa malaria nchini China” amesema Mhe. Lin Bin huku akiipongeza Tanzania kwa mikakati mizuri yenye lengo la kuhakikisha inatokomeza ugonjwa wa malaria.

Kwa upande wake Waziri wa Afya Tanzania, Mhe. Ummy Mwalimu ameishuruku Serikali ya China inayoongozwa na Rais Xi Jinping kwa kuendeleza ushirikiano wa enzi uliopo wa baina ya nchi hizo.

Waziri Ummy amesema kuwa ugonjwa wa malaria bado ni tatizo kubwa sana nchini Tanzania, huku takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO)z ikionyesha kuwa asilimia 55 ya vifo vitokanavyo na malaria vinatoka katika nchini saba za Bara la Afrika ikiwemo Tanzania.

“Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli tumechukua hatu ambali mbali kwa kushirikiana na wadau wakiwemo China kupambana na malaria na yapo mafanikio makubwa ambayo tumeyapata” Amesema Waziri Ummy Mwalimu na kuendelea;
“Tumeweza kupunguza kiwango cha maambukizi ya malaria kutoka asilimia 14.7 mwaka 2015 hadi 7.3 mwaka 2018”.

Amesema kuwa wagonjwa wapya wa malaria wamepungua kwa asilimia 26 kutoka watu 161 katika kila watu 1000 mwaka 2014 hadi kufikia 119k atika kila watu 1000 mwaka 2018 huku vifo vitokanavyo na malaria vimepungua kwa asilimia 55, kutoka vifo 20 katika watu 1000 mwaka 2014 hadi kufikia vifo 9 kati ya watu 1000 mwaka 2018.

“Serikali ya Tanzania itaendela kuchukua hatua kwa kushirikiana na wadau wetu wakiwemo Serikali ya China kuhakikisha tunapunguza kiwango cha maambukizi ya maralia hadi kufikia asilimia 1 ifikapo mwaka 2020” alisema Waziri Ummy Mwalimu.

Polisi Watatu Akiwemo Staff Officer I Mkoa Wa Kipolisi Rufiji Wafariki Dunia

$
0
0
NA MWAMVUA MWINYI,MKURANGA
ASKARI wawili wa kanda maalum Rufiji, pamoja na staff officer I mkoa wa kipolisi Rufiji (ACP) ,Issah Bukuku ,wanadaiwa kufariki dunia katika ajali ya gari baada ya kupasuka gurudumu la nyuma na kupinduka na kusababisha majeruhi wawili.

Taarifa za awali kuhusu ajali hiyo zinaeleza,imetokea Julai 25 mwaka huu, huko kijiji cha Kilimahewa barabara ya Kilwa wilaya ya Mkuranga na mkoa wa kipolisi Rufiji ambapo gari namba PT. 3822 Toyota land cruiser mali ya jeshi la polisi mkoa wa kipolisi Rufiji likiendeshwa na askari namba F7167 PC Ibrahim likitokea polisi Ikwiriri kuelekea kijiji cha Mwalusembe wilaya ya Mkuranga .

Waliofariki dunia katika ajali hiyo ni staff officer I mkoa wa kipolisi Rufiji (ACP) ,Issah Bukuku ,inspector Esteria wa ofisi ya RCO Rufiji na G 1132 PC Lameck wa FFU Rufiji.

Majeruhi katika ajali ni dereva wa gari hiyo F 7167 PC Ibrahim wa ofisi ya RCO Rufiji ambaye ameumia sehemu mbalimbali za mwili wake na G7651 PC Mgusi wa ofisi ya RPC Rufiji ambaye ameumia sehemu mbalimbali za mwili wake.

Chanzo cha ajali ni kupasuka gurudumu la nyuma kulia na kusababisha gari hilo kupinduka.

Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilaya ya Mkuranga, Filberto Sanga alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na taarifa kamili za kipolisi kanda maalum Rufiji zinaendelea na uchunguzi na itatoa habari kamili .

Tanzania kuiuzia mahindi Tani Milioni Moja nchi ya Kenya

$
0
0
Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amesema, Serikali itaiuzia nchi ya Kenya mahindi tani milioni moja katika kipindi cha mwaka mmoja, baada ya msimu wa mvua kugoma nchini humo hali inayotishia kuwepo kwa upungufu wa chakula.

Bashe ameyabainisha hayo jana Julai 25,  katika kikao kilichokutanisha idara zilizo chini yake na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo wa Kenya Hamad Boga pamoja na Balozi wa Kenya nchini Tanzania Dan Kazungu.

Ambapo wamekubaliana kwa wiki ijayo watakutana na kufanya kikao kitakachozikutanisha idara zote za mapato na  masuala ya viwango na ubora wa bidhaa kutoka nchi ya Kenya na Tanzania pamoja na sekta zote zinazohusika na mauzo ya chakula.

''Tumekubaliana na wenzetu kwamba mahitaji yao kwa sasa ni Tani milioni moja, sasa hivi NFRA na Bodi ya mazao mchanganyiko wametuthibitishia kuwa wana uwezo wa kuhudumia hilo hitaji la tani milioni moja''

Hatua hiyo imekuja baada ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo ya Kenya, Profesa Fred Segor, kusema mwaka huu wana changamoto ya hali ya hewa, kwa kuwa mvua haikunyesha ipasavyo.
 
Julai 24, 2019, Rais John Magufuli katika mazungumzo yake na Rais Uhuru Kenyatta, alisema alipomtembelea nyumbani kwake Chato, alizungumzia hitaji la kununua mahindi kutoka Tanzania.

Wizara ya Kilimo: Tumeamua Kufanya Mabadiliko Makubwa Ya Kuwatambua Wakulima Wote Nchini

$
0
0
Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Songwe
Wizara ya Kilimo inaendelea na mkakati madhubuti wa kuwatambua wakulima wote nchini ili kuwa na ufahamu wa watu wanaopaswa kuhudumiwa kwa ajili ya pembejeo za kilimo.

Mkakati huo wa wizara wa kuwatambua wakulima nchini unahusisha usajili wa wakulima ili kubaini mahali wanapoishi, ukubwa wa mashamba yao na mazo wanayolima.

Hayo yamebainishwa  jana tarehe 25 Julai 2019 na Mbunge la Jimbo la Vwawa Mkoani Songwe Mhe Japhet Hasunga ambaye ni Waziri wa Kilimo wakati akizungumza kwenye mikutano ya hadhara katika kijiji cha Chizumbi, Ukwile, Chimbuya katika kata ya Isandula pamoja na Kijiji cha Ikomela, Isandula na Kilimampimbi vilivyopo kata ya Kilimampimbi wakati wa ziara yake ya ukaguzi wa shughuli za maendeleo jimboni humo.

Alisema kuwa asilimia kubwa ya waTanzania wanawategemea wakulima katika kukamilisha mahitaji yao lakini wakulima hao hawatambuliki, hivyo mkakati wa utambuzi wa wakulima utaimarisha uwezekano wa kuwahudumia ili kuongeza tija na uzalishaji wa mazao mbalimbali.

Mhe Hasunga pia amewaeleza wananchi hao lengo la serikali kuanzisha mradi mkubwa wa ujenzi wa treni ya kisasa itakayorahisisha huduma za kijamii ikiwemo usafirishaji wa mizigo yakiwemo mazao ya wakulima.

Pia amesema kuwa serikali inaendelea na mchakato wa kuwafikishia wananchi huduma bora ikiwemo upatikanaji wa umeme katika maeneo yote vijijini.

Kuhusu sekta ya Kilimo Mhe Hasunga amesema kuwa katika kipindi cha muda mrefu wakulima wamekuwa wakilima lakini matokeo yake wanapata hasara au kipato cha kujikimu hivyo ili kupata faida na tija ni wazi kuwa wakulima lazima wabadilishe mtazamo ili waweze kuwa na Kilimo chenye tija na kibiashara.

Alisema wizara yake imejipanga kutoa elimu bora kwa wakulima juu ya Kilimo ili kufuata taratibu za Kilimo bora zinazotolewa na wataalamu mbalimbali wa Kilimo katika vijiji.

Kadhalika Mhe Hasunga amesikitishwa na wananchi kutokula vizuri ilihali wao ndio wazalishaji wakubwa wa mazao ya mbogamboga na matunda.

"Ukienda mahospitalini watu wengi wanaoumwa ni wakulima, kwahiyo nawasihi wakulima mkizalisha chakula muwe wa kwanza kula vizuri halafu ziada ndio mkauze" Alisisitiza Mhe Hasunga

MWISHO
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live




Latest Images